T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 21:55:27

Kunanyesha pesa na miradi Ol Kalou uchaguzi mdogo ukiweka historia kuwa ghali zaidi

HUKU zikiwa zimesalia siku nane kabla ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ol Kalou utakaofanyika Julai 16, eneo hilo linashuhudia kampeni zinazotajwa kuwa miongoni mwa ghali zaidi katika historia ya Kaunti ya Nyandarua. Vyama vya United Democratic Alliance (UDA) na Democracy for the Citizens Party (DCP) vinaongoza kampeni hizo kwa kutumia mikakati mbalimbali ya kuwashawishi wapigakura. Mbali na mikutano ya kisiasa, wagombeaji na wafuasi wao wamekuwa wakigawa fedha, zawadi na kuandaa mikutano ya uhamasishaji huku serikali ikiendelea kuzindua miradi ya maendeleo katika eneo hilo. Kiti hicho kilibaki wazi baada ya kifo cha Mbunge Njuguna Kiaraho wa chama cha Jubilee, Machi 29, 2026. Wanaowania kiti hicho ni Kamau Ngotho wa DCP, Muchina Nyaga wa UDA, Wilson Kigwa wa Jubilee, Rachel Wangui wa People's Democratic Party, Mathenge Mwaniki wa Kenya Moja Movement, Abdifatah Hussein wa Federal Party of Kenya, Timothy Kamau wa People's Renaissance Party, Stephen Wanyoike wa National Liberal Party na Edwin Muchiri wa Party of National Unity. Kwa mujibu wa walio karibu na kampeni za DCP, makazi ya Seneta wa Nyandarua John Methu katika eneo la Mugumo yamegeuzwa kuwa kituo kikuu cha uratibu wa shughuli za chama hicho. [caption id="attachment_189921" align="alignnone" width="720"] Wakazi waliohudhuria mkutano wa kisiasa wapewa magodoro. Picha|Hisani[/caption] Kila asubuhi, makundi mbalimbali hukusanyika hapo kabla ya kutumwa katika maeneo tofauti kufanya kampeni. Washiriki hupewa kifungua kinywa na fedha za kujikimu zinazokadiriwa kuwa kati ya Sh500 na Sh1,000 kabla ya kuanza shughuli za siku. Akizungumza jana, kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua aliwataka wakazi wa Ol Kalou kutodanganywa na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali wakati huu wa kampeni. "Serikali inaweza kuleta hata boti, transfoma, treni za kasi, matangi ya maji pamoja na miradi mingine ambayo haijawahi kufikishwa Ol Kalou tangu 1963. Msikubali kuuza haki yenu ya kupiga kura kwa sababu ya zawadi za dakika za mwisho," alisema Bw Gachagua. Kwa upande wa UDA, kampeni zinaonekana kuwa na mtandao mpana zaidi. Chama hicho kimeunda timu mbalimbali zinazolenga makundi tofauti ya wapigakura huku washiriki wakipewa fedha za kujikimu kulingana na aina ya shughuli wanazoshiriki. Baadhi ya timu hizo husafirishwa hadi miji jirani kama Gilgil kwa mikutano ya kupanga mikakati, ambapo kila mshiriki hudaiwa kulipwa kati ya Sh1,000 na Sh2,000. Duru zenye ufahamu kuhusu kampeni hizo zinaeleza kuwa UDA huandaa wastani wa mikutano sita kila siku, huku viongozi wa serikali na waliochaguliwa wakihusika moja kwa moja katika shughuli hizo. Mbali na mikutano ya hadhara, chama hicho pia kimekuwa kikifanya mikutano na viongozi wa dini, wazee wa makanisa na waumini wenye ushawishi mkubwa, mikutano ambayo huwasilishwa kama warsha za amani na elimu ya uraia. Kiongozi mmoja wa kidini aliyeshiriki katika baadhi ya mikutano hiyo alisema kiwango cha fedha kinachotolewa hutegemea hadhi ya mkutano. Alidai kuwa mikutano ya kiwango cha kaunti washiriki hupokea takriban Sh5,000 kila mmoja huku mikutano ya ngazi ya mashinani wakipata karibu Sh3,000, bila kujumuisha fedha zinazotolewa kwa makanisa na viongozi wa dini wanaoratibu shughuli hizo. Kwa mujibu wa watu wanaofahamu mipango ya kampeni, mikutano mingi ya ndani huvutia takriban watu 500 wanaopewa kati ya Sh1,000 na Sh2,000 kila mmoja. Wanaoongoza kampeni pia hulipwa kati ya Sh5,000 na Sh10,000. Makadirio yanaonyesha kuwa UDA inaweza kutumia zaidi ya Sh3 milioni kwa siku kugharamia mikutano ya ndani pekee, bila kujumuisha gharama za usafiri, malazi, chakula na shughuli nyingine za kampeni. Baada ya mikutano ya hadhara, washiriki wengi huripotiwa kupanga foleni katika makundi ya watu kumi, utaratibu unaojulikana kama "ikumi ikumi", ambapo kila mmoja hupokea kati ya Sh300 na Sh500. Kutumiwa kwa fedha kumeibua biashara mpya kwa baadhi ya vijana wa eneo hilo. Makundi ya vijana hukodisha pikipiki kwa siku nzima na kuhama kutoka mkutano mmoja wa kampeni hadi mwingine ili kuongeza kiwango cha fedha wanachopata. Mwendesha bodaboda James Kanja alisema vijana watatu au wanne huchangia takriban Sh3,000 kukodisha pikipiki kwa siku pamoja na gharama ya mafuta. "Ni biashara nzuri kuliko kusubiri abiria mjini. Tunaweza kuhudhuria zaidi ya mikutano mitano kwa siku na kila mmoja akaondoka na kati ya Sh2,500 na Sh4,000," alisema. Mwendesha bodaboda mwingine, Robert Kiambati, alisema vijana hufuatilia ratiba za kampeni ili kujua mikutano inayotarajiwa kutoa fedha nyingi zaidi. Huku kampeni zikiendelea, serikali nayo imeongeza kasi ya kuzindua miradi ya maendeleo katika eneo hilo. Miradi hiyo ni pamoja na usambazaji wa mitungi 20,000 ya gesi, matangi ya maji, godoro, vyakula, vifaa vya kidijitali kwa shule za sekondari msingi, pamoja na boti mbili za thamani ya Sh5 milioni kwa Bwawa la Gwa Kiongo. Mawaziri na Makatibu mbalimbali wamekuwa wakizuru eneo hilo mara kwa mara kuzindua miradi ya barabara, umeme, nyumba za bei nafuu, masoko ya kisasa, reli na huduma za kidijitali. Kwa upande wa DCP, uchaguzi huo pia umegeuka kuwa uwanja wa kujitambulisha kwa wanasiasa wanaojiandaa kugombea viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Baadhi ya wanaotaka ugavana, ubunge na uwakilishi wa wadi wamekuwa wakifanya kampeni za nyumba kwa nyumba kwa gharama zao wenyewe ili kuongeza nafasi za mgombeaji wa DCP, Kamau Ngotho.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Lojini za bei nafuu Eldoret zageuka 'mitego ya kifo' baada ya wanawake wawili kuuawa

WANAHARAKATI wa haki za binadamu na wanaotetea wafanyabiashara wa ngono wameonya kuhusu ongezeko la mauaji ya wanawake Eldoret baada ya wanawake wawili kuuawa katika visa viwili tofauti ndani ya siku tano. Visa hivyo vimeibua wasiwasi kuhusu usalama katika nyumba za kulala ambazo wakazi wanasema zimegeuka kuwa maeneo hatari kwa uhalifu. Kisa cha hivi majuzi kilitokea Alhamisi asubuhi katika mtaa wa Kipkaren ambapo mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 26 ulipatikana umefungwa kwenye gunia na kutupwa katika nyumba ya kupanga baada ya waliokuwa wakiishi humo kutoroka. Siku chache kabla ya hapo, mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 38, aliyetambuliwa na wenzake kwa jina la Zeddy, ulipatikana katika nyumba ya gesti eneo la Juakali, kando ya barabara kuu ya Eldoret-Webuye. Mauaji hayo yameongeza hofu miongoni mwa wanawake wanaofanya biashara ya ngono, huku mashirika ya haki yakisema yanaweza kuwa sehemu ya mtindo unaoibuka wa mauaji yanayowalenga wanawake walio katika mazingira hatari. Wakazi wanasema baadhi ya nyumba hizo za kulala wageni hazina rejista za wageni, kamera za usalama wala mifumo madhubuti ya kudhibiti wanaoingia na kutoka. Kiongozi wa Nyumba Kumi eneo hilo, Solomon Musumi, alisema Zeddy alikuwa akiishi katika mojawapo ya vyumba hivyo. Alisema Jumatatu usiku alipokea mwanaume aliyedhaniwa kuwa mteja, kabla ya wanawake waliokuwa katika vyumba vya jirani kugundua mwili wake asubuhi iliyofuata. "Eneo hili haliwezi kuendelea kuwa maficho ya wauaji. Nyumba hizi hazina rejista za wageni wala kamera za usalama, na hivyo kuwa mitego ya kifo," alisema Musumi. Polisi wamethibitisha wameanzisha uchunguzi kuhusu visa hivyo. Kamanda wa Polisi kaunti ndogo ya Kapseret Zaphaniah Kamren alisema washukiwa wawili wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Kipkaren. "Tunaahidi umma kuwa hatutakoma hadi waliohusika na vitendo hivi vya kinyama wakabiliwe na sheria," alisema. Kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi wa Turbo Patrick Wekesa alisema uchunguzi kuhusu kifo cha Zeddy unaendelea.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

DCI imefichua kuwa maafisa walilipwa kumuuwa Dkt Mutiso

WAPELELEZI wametaja Konstebo wa Polisi Elijah Kibelion Kimoi kuwa ndiye aliyempiga risasi na kumuua Daktari Victoria Mutiso katika shambulizi la kikatili lililotokea wiki iliyopita. Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) ilisema Ijumaa kuwa Kimoi, ambaye tayari amekamatwa, alitumia bastola ya polisi kumuua Dkt Mutiso. DCI pia ilimtaja raia Daniel Mwangi Njoroge kuwa mmoja wa waliopanga mauaji hayo. Kulingana na DCI, Njoroge aliajiriwa na mwanasiasa Rose Mbithe Mulwa na mwanawe Christopher Mulwa kwa lengo la kumuua Dkt Mutiso. Inadaiwa mauaji hayo yalitokana na mzozo wa muda mrefu wa kifamilia kuhusu ardhi ya ukubwa wa ekari 20 huko Mlolongo, Machakos. Bi Mulwa amekuwa akizozania ardhi hiyo na aliyekuwa mumewe, Dkt David Musyimi Ndetei, pamoja na mkewe Dkt Mutiso tangu 2001. Mkuu wa DCI Mohamed Amin alisema Njoroge alikodi magari mawili aina ya Toyota Prado kutekeleza mauaji hayo. Alisema Njoroge pia alishirikiana na mhudumu wa bodaboda Kelvin Ngugi Kinuthia, ambaye anadaiwa kumsafirisha Kimoi hadi eneo la tukio na baadaye kumtorosha. Dkt Mutiso alikuwa akisafiri katika teksi ya Uber iliyokuwa ikiendeshwa na Victor Job Chunguli mnamo Julai 29. Walipofika eneo la Mawensi, Upper Hill, Nairobi, Toyota Prado nyeusi ilizuia teksi hiyo.Pikipiki pia ilisimama karibu nao. Mtu aliyekuwa ameketi kiti cha nyuma cha pikipiki alifyatua risasi kadhaa kuelekea Dkt Mutiso kabla ya pikipiki na Prado kutoroka. Bw Chunguli alimpeleka Dkt Mutiso katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, lakini akatangazwa kuwa amefariki alipowasili. Bw Amin alisema baada ya kuwahoji Njoroge na Kinuthia, wawili hao waliwapeleka wapelelezi kwa maafisa watatu wa polisi. Walitajwa kuwa Inspekta Kenneth Kipkemboi Sang, Konstebo Elijah Kibelion Kimoi na Konstebo Collins Kiplangat Bett. Kimoi amekamatwa huku Sang na Bett wakitoroka na wanaendelea kusakwa na polisi . "Kushiriki kwa maafisa hawa ni usaliti mkubwa kwa sare ya polisi na imani ambayo umma umeweka kwao. Lazima wachukuliwe hatua," alisema Bw Amin. Bw Amin pia alisema bastola iliyotumiwa kumuua Dkt Mutiso ilikuwa ya polisi na ilikuwa imewekwa katika kituo kidogo cha polisi cha Nderi, chini ya Kituo cha Polisi cha Kikuyu. Wapelelezi walipokagua sanduku la kuhifadhia silaha katika kituo hicho, walipata bastola aina ya Mini Jericho yenye nambari KP47302127 pamoja na magazini iliyokuwa na risasi 12 za milimita tisa. Ukaguzi wa rejista ya utoaji wa silaha ulionyesha kuwa bastola hiyo ilikuwa imetolewa kwa Inspekta Sang. Silaha hiyo ilipelekwa katika maabara ya uchunguzi wa kisayansi ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa uchunguzi wa risasi. Kulingana na DCI, uchunguzi ulithibitisha kuwa bastola hiyo ndiyo iliyotumiwa katika kumuua Dkt Mutiso. Maganda ya risasi yaliyopatikana eneo la tukio na kichwa cha risasi kilichopatikana mwilini mwa marehemu wakati wa uchunguzi wa mwili vililingana na risasi kutoka kwa bastola hiyo. Bastola hiyo pamoja na pikipiki ya Kinuthia zimechukuliwa na polisi kama ushahidi. Uchunguzi wa mauaji hayo ulihusisha pia kuangalia picha za kamera za usalama, ushahidi wa kisayansi na taarifa nyingine za kijasusi. DCI ilisema ushahidi uliopatikana unaonyesha kuwa baadhi ya washukiwa wa mauaji ya Dkt Mutiso huenda pia walihusika katika mauaji ya wakili Kyalo Mbobu mnamo Septemba 9, 2025. Mbobu alipigwa risasi na mtu aliyekuwa nyuma ya pikipiki akiendesha gari kuelekea nyumbani kando ya Barabara ya Magadi. Mauaji hayo yalifanana na yaliyompata Dkt Mutiso kwa kuwa mshambuliaji alitumia pikipiki. Bw Amin pia alidai kuwa matamshi ya Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kuhusu uchunguzi huo huenda yalifikia Sang na Bett na kuwafanya kutoroka. Alimtaka Bw Gachagua kuwasilisha kwa DCI taarifa yoyote aliyo nayo ambayo inaweza kusaidia uchunguzi wa mauaji hayo. Bw Gachagua alikuwa amedai kuwa maafisa wawili wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Kikuyu walihusika katika mauaji ya Dkt Mutiso. Alisema madai yake yalitokana na "taarifa za kuaminika". "Maafisa hawa wawili katika Kituo cha Polisi cha Kikuyu ndio waliomuua wakili Kyalo Mbobu na pia Dkt Victoria Mutiso," Bw Gachagua alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Umoja: Kalonzo ateua washirika wa Gachagua katika uongozi wa Wiper

KIONGOZI wa Wiper Patriotic Front , Kalonzo Musyoka Ijumaa alitangaza mabadiliko katika uongozi wa chama hicho kwa kuwateua washirika wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, huku akilenga kuonyesha umoja wa upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Bw Musyoka alimteua aliyekuwa waziri, Jamleck Kamau kuwa mwenyekiti wa chama, Mbunge wa Nyali, Mohamed Ali kuwa naibu kiongozi wa chama, na wakili wa masuala ya Katiba Ndegwa Njiru kuwa msemaji wa chama. Uteuzi huo ulianza kutekelezwa mara moja na unaashiria upanuzi mkubwa wa uongozi wa Wiper vyama vya upinzani vinapoendelea na mashauriano kuhusu muungano w kukabiliana na Rais William Ruto mwaka 2027. Bw Kamau, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Kigumo, amewahi kuhusishwa kisiasa na Bw Gachagua, huku Bw Njiru akiwa mmoja wa mawakili mashuhuri waliowahi kumtetea kiongozi huyo wa DCP. Bw Musyoka alisema uteuzi huo ulitokana na jukumu alilopewa na wajumbe wa chama wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe la Oktoba 10 mwaka jana. "Jukumu la kwanza nililopewa na wajumbe lilikuwa kutafuta urais wa Jamhuri ya Kenya mnamo Agosti 2027. Jukumu la pili lilikuwa kupanua na kujenga uongozi wa chama hiki hadi kiwe sura ya Kenya," alisema. Alisema mabadiliko hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha Wiper pamoja na muungano mpana wa upinzani kuelekea uchaguzi wa 2027. Bw Musyoka alisema mashauriano yanaendelea kuunganisha vyama vinavyopinga utawala wa Rais Ruto chini ya mwavuli mmoja wa kisiasa. "Huu si uteuzi wa kujipendekeza, bali ni uteuzi wa imani. Kila mmoja wao anafaa kikamilifu katika chama ambacho ajenda yake pekee ni 'Komboa Kenya'," alisema. Kando na mabadiliko hayo ya uongozi, Bw Musyoka alisema hataruhusu tofauti kati ya viongozi wa upinzani kuvuruga juhudi za kuunda muungano mmoja dhidi ya Rais Ruto. Alisema viongozi wa upinzani wanaendelea na mashauriano ya kuleta pamoja Wakenya na akaonya kuwa mgawanyiko utawanufaisha viongozi wa Kenya Kwanza. "Tunapoendelea na kazi hii, mashauriano yanaendelea ili kuleta upinzani chini ya mwavuli mmoja wa kuaminika. Tumekubaliana kuwa mgawanyiko ndiyo mkakati pekee wa utawala huu," alisema. Bw Musyoka pia aliwataka Wakenya kutotafsiri tofauti zinazojitokeza kati ya viongozi wa upinzani kama ishara kwamba mchakato wa kuunda muungano umevunjika. "Hata mkiona tofauti kati ya viongozi wa vyama ndani ya muungano, tafadhali msizichukulie kwa uzito sana. Tumeungana kwa sababu tukigawanya upinzani, William Ruto atapata muhula wa pili," alisema. Alisema mashauriano yataendelea hadi vyama na viongozi wote wanaopinga serikali waungane. "Mashauriano hayo yanaendelea na hayatasitishwa hadi kila chama na kila kiongozi anayepinga serikali awe chini ya paa moja, tayari kuunda serikali moja inayosubiri kuchukua uongozi," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Hofu virusi vya ukimwi vikizidi kukosa kusikia dawa muhimu

WANASAYANSI wamegundua hali mpya ya kutisha ya virusi vya Ukimwi kuanza kustahimili dawa muhimu inayotumika katika matibabu ya ugonjwa huo katika nchi nne za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Utafiti uliowasilishwa katika mkutano wa International Aids Society (IAS) mjini Rio de Janeiro, Brazil, umeonyesha hali hiyo miongoni mwa watu wanaoishi na Ukimwi nchini Kenya, Tanzania, Msumbiji na Lesotho. Watafiti wameonya kuwa hali hiyo ikiendelea, maambukizi mapya ya Ukimwi yanaweza kuongezeka. Kinga ya mwili ya wagonjwa ambao virusi vyao vitakuwa vimekuwa sugu kwa dawa hiyo inaweza pia kudhoofika na kuwa katika hatari ya kupata magonjwa mengine ambayo yanaweza kusababisha kifo. Dawa inayohusika ni dolutegravir, inayojulikana kwa kifupi kama DTG. Tangu 2018, dawa hiyo imekuwa chaguo la kwanza na la pili katika matibabu ya Ukimwi. Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema DTG ina ufanisi mkubwa, ni rahisi kutumia na husababisha madhara machache ikilinganishwa na baadhi ya dawa nyingine zinazotumika. Dawa hiyo pia inajulikana kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia virusi vya Ukimwi kuzoea na kustahimili matibabu. Daktari Loice Ombajo, mtafiti mkuu wa utafiti huo na mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, alisema sampuli za kwanza za utafiti zilikusanywa kutoka kwa watu 2,994 katika vituo 131 nchini Kenya. Washiriki hao walikuwa wametumia matibabu yenye DTG kwa angalau miezi sita.  Baadhi ya washiriki waliopatikana kuwa na mabadiliko ya virusi yanayohusishwa na usugu wa DTG waliingizwa katika utafiti maalumu ili kupata ushahidi wa kusaidia kuboresha matibabu ya wagonjwa ambao dawa hiyo imeshindwa kuwasaidia. "Bado kuna ushahidi mdogo kuhusu namna ya kuwahudumia watu wanaoishi na Ukimwi ambao virusi vyao vimekuwa sugu kwa dolutegravir," alisema Dkt Ombajo. Alisema utafiti huo unalenga kutoa ushahidi utakaosaidia wataalamu kufanya maamuzi bora kuhusu matibabu ya wagonjwa hao. Takriban watu tisa kati ya 10 wanaotumia DTG hufikia kiwango ambacho virusi vya HIV havionekani kwa wingi katika damu. Hata hivyo, baadhi yao hushindwa kufikia kiwango hicho. Dkt Ombajo alisema sababu kubwa ni kutotumia dawa ipasavyo. Alisema baadhi ya wagonjwa huchoka kutumia dawa kila siku, wengine husahau, huku wengine wakikosa hamu ya kuendelea na matibabu kutokana na hali yao.  "Usipotumia dawa au ukaitumia mara kwa mara bila kufuata ratiba, virusi vinaweza kubadilika na kuwa sugu kwa dawa hiyo," alisema. Katika utafiti huo, watafiti walifanya kazi na washiriki waliokuwa hawatumii dawa ipasavyo ili kuwasaidia kuendelea na matibabu. Takriban asilimia 70 walifikia kiwango cha kudhibiti virusi, huku asilimia 30 wakishindwa. Watafiti walilenga kundi hilo kubaini iwapo kiwango kikubwa cha virusi kilisababishwa na kuzoea dawa. Waligundua kuwa watatu kati ya kila washiriki 10 katika kundi hilo virusi vilikuwa sugu kwa DTG. Dkt Ombajo alisema hali hiyo ni ya kutia wasiwasi kwa sababu dawa hiyo inaweza kushindwa kufanya kazi hata mgonjwa akiendelea kuitumia. Tatizo jingine ni gharama kubwa ya vipimo vya kubaini hali ya dawa kwa virusi, huku nchi nyingi zikikosa rasilimali za kutosha kufanya vipimo hivyo mara kwa mara. Utafiti pia ulibaini baadhi ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanakumbwa na hali hiyo. Alisema hali hiyo inaweza kuongeza hatari ya mama mwenye kiwango kikubwa cha virusi kumwambukiza mtoto au mwenzi wake wa ngono.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Wantam, tutam: Uchaguzi wa urais ulifaa kufanyika Agosti 2026 mahakama yasema

MAHAKAMA Kuu imesema uchaguzi ujao wa urais nchini ulifaa kufanyika Agosti 2026, badala ya 2027, lakini imekataa kuamuru uchaguzi huo uandaliwe mara moja ikisema hatua hiyo inaweza kutumbukiza nchi katika vurugu. Jaji wa Mahakama Kuu ya Malindi Mugure Thande alisema Katiba inahitaji uchaguzi wa urais ufanyike Jumanne ya pili ya Agosti katika mwaka wa tano baada ya uchaguzi mkuu uliopita. Jaji huyo alisema Ibara ya 136(2)(a) ya Katiba inataka uchaguzi huo ufanyike katika mwaka wa tano na si baada ya mwaka huo kukamilika. Alisema mwaka wa tano baada ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022 ulianza Agosti 9, 2026. "Kufanya uchaguzi ujao wa urais katika tarehe nyingine yoyote isipokuwa Jumanne ya pili ya Agosti 2026 kutakiuka Katiba," Jaji Thande alisema. Hata hivyo, mahakama ilisimamisha utekelezaji wa uamuzi huo hadi baada ya uchaguzi mkuu ujao. Hatua hiyo inamaanisha kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haijaamrishwa kuandaa uchaguzi wa urais mwezi huu wa Agosti. Walalamishi katika kesi hiyo, Dkt Owiso Owiso, Khelef Khalifa na Ashioya Biko, walitaka mahakama itoe uamuzi kuhusu tarehe sahihi ya uchaguzi na pia iamuru IEBC kufanya uchaguzi huo Agosti 11, 2026. Jaji Thande alikataa ombi la kuamuru uchaguzi ufanyike mara moja. Alisema kesi hiyo iliwasilishwa Oktoba 2025 wakati maandalizi ya uchaguzi wa 2027 yalikuwa tayari yameanza. Alisema IEBC, wagombea watarajiwa na Wakenya kwa ujumla walikuwa tayari wamejiandaa kwa uchaguzi wa Agosti 2027. "Kuamuru tume ya uchaguzi kuandaa uchaguzi wa urais Agosti 2026 kutakuwa kutoa amri ambayo haiwezekani kutekelezwa kwa njia ya kiutendaji," alisema. Jaji huyo aliongeza kuwa hatua kama hiyo inaweza kuingiza nchi katika machafuko. Mahakama ilisema ililazimika kusawazisha utekelezaji wa Katiba na tahadhari ya kimahakama ili kuepuka kusababisha "vurugu kubwa kitaifa ambazo haziwezi kudhibitiwa". Mzozo huo ulitokana na tafsiri ya Ibara ya 136(2)(a), inayoweka wakati wa kufanyika kwa uchaguzi wa urais. Walalamishi walidai kuwa mwaka wa tano baada ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022 ulianza Agosti 9, 2026 na kumalizika Agosti 8, 2027. Kwa hesabu hiyo, walisema Jumanne ya pili ya Agosti 2026, ambayo ni Agosti 11, ndiyo tarehe iliyowekwa na Katiba kwa uchaguzi. Walitegemea pia Ibara ya 259(5)(c), inayoweka namna vipindi vinavyotajwa kwa miaka vinavyopaswa kuhesabiwa. Walalamishi walitaja uchaguzi wa 2013 na 2017 kama mifano ya kuonyesha kuwa Katiba haimpi rais haki ya lazima ya kutawala kwa miaka mitano kamili iwapo kufanya hivyo kutapingana na tarehe iliyowekwa kikatiba ya uchaguzi. Jaji Thande pia alisema ratiba ya uchaguzi iliyowekwa na Katiba ina uzito kuliko dhana kwamba rais lazima atumikie miaka mitano kamili. Alisema IEBC inaposhindwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, mahakama inaweza kuingilia kati. Hata hivyo, mahakama ilisitisha utekelezaji wa uamuzi kwamba uchaguzi utakaofanyika nje ya Agosti 2026 utakuwa batili hadi baada ya uchaguzi mkuu ujao. Hii ina maana kuwa ingawa mahakama imesema tarehe inayofaa kikatiba ilikuwa Agosti 2026, haijaamuru Kenya kufanya uchaguzi wa urais mwezi huo. Mahakama pia ilisema muhula wa rais si miaka mitano chini ya Ibara ya 136(2)(a), na kwamba, Ibara ya 142 au kifungu kingine chochote cha Katiba hakimpi rais muhula wa miaka mitano. Kesi hiyo iliwasilishwa kupitia kampuni ya mawakili ya Otieno Ogola Company Advocates na Osundwa Company Advocates. Miongoni mwa waliotajwa kuwa wahusika wenye maslahi katika kesi hiyo ni Chama cha Wanasheria Kenya (LSK), Katiba Institute, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, UDA, aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, mwanaharakati Okiya Omtatah, mwanasiasa Jimi Wanjigi, aliyekuwa Waziri Fred Matiang'i na Kenya Human Rights Commission.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 21:55:35

Ruto afufua mbinu za Moi kujenga mtandao wa ushawishi mashinani kuelekea uchaguzi mkuu

RAIS William Ruto anaonekana kufufua baadhi ya mikakati iliyotumiwa na mlezi wake wa siasa hayati rais Daniel arap Moi ya kuimarisha utawala wa mashinani, baada ya kuwatambua rasmi wazee wa vijiji na kuwaingiza katika mfumo wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAO). Hatua hiyo imezua mjadala mpya kuhusu iwapo serikali inalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi au inajenga upya mtandao wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Kwa miaka mingi, machifu, manaibu wao na makamishna wa mikoa walikuwa nguzo kuu ya serikali za Moi. Mbali na kusimamia usalama na utekelezaji wa sera za serikali, walitumiwa pia kuhamasisha wananchi kuunga mkono chama tawala cha Kanu. Lakini mfumo huo ulikosolewa vikali wakati wa harakati za kurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa miaka ya 1990, huku viongozi wa upinzani wakidai ulitumiwa kuwanyanyasa wakosoaji wa serikali na kuvuruga shughuli za kisiasa. Ingawa Katiba ya mwaka 2010 na ugatuzi ulipunguza mamlaka ya utawala huo, serikali zilizofuata ziliendelea kuuhifadhi kwa kuubadilisha na kuuita Utawala wa Serikali ya Kitaifa. Sasa, miaka 16 baadaye, Rais Ruto ameupanua zaidi kwa kuwaingiza rasmi wazee wa vijiji katika mfumo huo. Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi mbele ya zaidi ya wazee wa vijiji 10,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini, Rais alisema wazee 106,000 wameingizwa rasmi katika utawala wa mikoa. Alitangaza kuwa kila mmoja wao ataanza kupokea posho ya Sh3,000 kila mwezi, baada ya kuhudumu kwa miaka mingi bila malipo. Aidha, alisema serikali italipia bima yao ya afya kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), kuwapatia simu za kisasa za kurahisisha kazi zao na kuongeza maafisa wa Polisi wa Utawala katika maeneo yao. Pia alimwagiza Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi, kutenga fedha katika bajeti ya ziada ili serikali ilipie michango ya SHA kwa wazee hao, wake au waume wao pamoja na watoto wao kuanzia Januari 2027. Rais alisema lengo ni kuwapa wazee wa vijiji nafasi rasmi katika utawala wa serikali na kuimarisha ushirikiano wao na machifu, manaibu wa machifu na maafisa wengine wa serikali. Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Raymond Omollo, alisema huo ni uamuzi wa kihistoria kwa sababu ni mara ya kwanza wazee wa vijiji kutambuliwa rasmi na kupewa malipo ya kila mwezi. Alisema hatua hiyo itaimarisha uongozi mashinani, kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Hata hivyo, mkutano huo uligeuka wa kisiasa baada ya Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Kimani Ichung'wah kuwataka wazee hao kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027. "Mmengoja kutambuliwa kwa miaka mingi. Rais Ruto ametimiza ahadi hiyo. Mkumbukeni na wakati ukifika, muungeni pia," alisema Bw Ichung'wah. Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, pia alitaka Rais aungwe kwa muhula wa pili, akisema ametambua mchango wa wazee wa vijiji kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Mkuu wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi, alisema serikali itaendelea kuwaunga mkono wazee hao ili kuimarisha usalama na huduma kwa wananchi, huku akieleza kuwa uongozi wa Rais Ruto umeifanya Kenya kuwa na ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika. Lakini viongozi wa upinzani walikosoa mpango huo. Kiongozi wa chama cha DCP, Bw Rigathi Gachagua, alisema serikali imekuwa ikitoa ahadi nyingi ambazo hazijatekelezwa. "Aliahidi machifu vipakatalishi lakini mpaka leo hawajazipata. Sasa anawaahidi wazee wa vijiji simu za kisasa. Kwa nini wamwamini?" alihoji. Pia alisema baadhi ya wazee wa vijiji wamemweleza kuwa posho ya Sh3,000 haitoshi kukabiliana na gharama ya maisha. Wachambuzi wa siasa wanasema hatua ya serikali kuimarisha mtandao wa utawala mashinani inaweza kuboresha huduma kwa wananchi, lakini pia inaweza kupatia utawala huo uzito mkubwa wa kisiasa huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 22:55:40

Jinsi ya kusafisha korodani na makosa yanayofanywa na wanaume

WANAUME wengi hawazingatii sana jinsi wanavyosafisha sehemu zao za siri. Wengi huamini kwamba kuoga kila siku kunatosha, lakini madaktari wa mfumo wa mkojo wanasema si kila wakati. Kutumia sabuni kali, kukaa muda mrefu na chupi zenye jasho au kupuuza usafi wa sehemu za siri kunaweza kusababisha mwasho, fangasi, harufu mbaya na matatizo mengine yanayoweza kuzuiliwa. Daktari mtaalamu wa mfumo wa mkojo, Dkt Victor Albert Okoth, anasema usafi wa korodani ni sehemu muhimu ya afya ya uzazi wa mwanaume. "Usafi mzuri ni kusafisha sehemu hizo bila kupita kiasi. Ngozi ya sehemu za siri ni nyepesi na kuisugua sana kunaweza kusababisha majeraha na mwasho," anasema. Anashauri wanaume waoge sehemu za siri angalau mara moja kila siku kwa kutumia maji ya uvuguvugu. Wakati wa kuoga, mwanaume anapaswa kuosha uume, korodani, kinena na eneo lililo kati ya korodani na njia ya haja kubwa. Kwa wanaume ambao hawajatahiriwa, anashauri wavute govi nyuma, waoshe sehemu iliyo chini yake vizuri, wasuuze kwa maji kisha warudishe govi mahali pake. "Hakuna haja ya kusugua korodani kwa nguvu. Tumia mikono. Kusudi ni kuondoa uchafu, si kuua kila kimelea," anasema. Dkt Okoth anaongeza kuwa wanaume wanaofanya mazoezi mara kwa mara, wanaofanya kazi nje au wanaokaa katika mazingira yenye joto wanapaswa kuoga tena baada ya kutoa jasho. Anasema jasho hutengeneza mazingira yenye unyevunyevu yanayochochea ukuaji wa fangasi na bakteria. "Hali ya hewa ya Kenya huwa na joto katika maeneo mengi. Kuoga baada ya mazoezi na kubadilisha chupi yenye jasho ni tabia muhimu ya kujikinga na maambukizi," anasema. Hata hivyo, anaonya kuwa kuosha sehemu hizo mara nyingi kupita kiasi kunaweza kuharibu kinga ya ngozi na kusababisha ukavu, mwasho na uvimbe. Dkt Okoth anashauri matumizi ya maji pekee au sabuni laini isiyo na manukato makali. Anasema wanaume wengi huamini sabuni zenye povu nyingi au harufu kali husafisha vizuri zaidi, jambo ambalo si kweli. Bidhaa kama dawa za kuondoa harufu vinaweza kusababisha mwasho isipokuwa kwa ushauri wa daktari. Baada ya kuoga, sehemu za siri zinapaswa kukaushwa vizuri kwa taulo safi. Anasema unyevunyevu unaobaki kwenye ngozi huchochea ukuaji wa fangasi. Kwa wanaume ambao hawajatahiriwa, sehemu iliyo chini ya govi inapaswa kukaushwa vizuri kabla ya kuirudisha. Pia anashauri wanaume kuvaa chupi zinazopitisha hewa na kuzibadilisha kila siku au mara moja zinapolowa na jasho. Dkt Okoth anasema makosa yanayofanywa mara nyingi ni kutosafisha chini ya govi, kutumia sabuni kali au manukato kwenye sehemu za siri, kuvaa chupi yenye jasho kwa muda mrefu na kunyoa nywele za sehemu za siri kwa ukali kiasi cha kujeruhi ngozi. Anasema kosa kubwa zaidi ni kudhani kila tatizo la sehemu za siri husababishwa na uchafu. "Harufu, vipele, uvimbe au usaha si lazima vitokane na ukosefu wa usafi. Magonjwa ya zinaa kama kisonono huenezwa kupitia ngono na yanahitaji uchunguzi na matibabu ya kitaalamu," anasema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 23:55:52

Linda Mwananchi yalenga ngome za Raila ambazo ODM inapambana kuzihifadhi kwa ajili ya Ruto

BAADA ya kufanya mikutano iliyofanikiwa katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia wiki mbili zilizopita, viongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi sasa wamehamishia kampeni zao katika ngome za kisiasa za aliyekuwa kinara wa ODM, Raila Odinga, wakilenga kuimarisha ushawishi wao huku wakipanua mtandao wao nchini. Vuguvugu hilo linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, linatarajia kufanya mikutano Busia Ijumaa kabla ya kuelekea Kakamega Jumamosi na Jumapili. Viongozi hao wananuia kuvutia wafuasi wa ODM katika eneo la Magharibi huku chama hicho kikijitahidi kulinda ngome zake za jadi. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, ambaye ameahidi kuunga mkono azma ya Bw Sifuna ya kuwania urais mwaka 2027, anatarajiwa kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuunganisha kura za jamii ya Mulembe kabla ya kampeni hizo kusambazwa kote nchini. Ziara ya Kakamega pia inalenga ngome ya viongozi wanaounga mkono Rais William Ruto akiwemo Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, Gavana Fernandes Barasa, Naibu Gavana Ayub Savula pamoja na zaidi ya wabunge wanane wanaounga mkono serikali jumuishi. Ziara hiyo inafanyika wiki chache baada ya Bw Oparanya kufanya mkutano Malava ambapo alipendekezwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto na kuahidi kuongoza juhudi za kuunganisha eneo la Magharibi kumuunga mkono Rais huku akiimarisha ODM. Mnamo Agosti 16, msafara wa Linda Mwananchi utaelekea Homa Bay, mojawapo ya ngome kuu za ODM, ukiongozwa na Gavana Orengo. Hii itakuwa mara ya pili kwa kundi hilo kuingia eneo la Luo Nyanza baada ya kufanya mkutano Kisumu. Bw Orengo pia analenga kuimarisha nafasi yake kama msemaji wa kisiasa wa jamii ya Waluo kupitia mikutano Homa Bay, Kisumu na Siaya, huku mipango ikisukwa kupeleka kampeni hizo Migori. Hata hivyo, maandalizi ya mkutano wa Homa Bay yamekumbwa na misukosuko baada ya kuripotiwa visa vya vurugu. Mratibu wa muda wa Linda Mwananchi katika eneo hilo, Samuel Nyauke, alishambuliwa na kundi la vijana waliomshutumu kwa kupuuza uongozi wa kisiasa wa eneo hilo. Mali iliharibiwa baada ya mawe kurushwa katika ofisi yake, huku vijana sita wakikamatwa na baadaye kuachiliwa. 'Kwa wanaotumia vurugu kulinda maeneo yao ya kisiasa, Kenya ni ya Wakenya wote. Hakuna vitisho vitakavyotuzuia. Tutakuwa Homa Bay kama ilivyopangwa,' alisema Bw Orengo. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa ODM ambaye pia ni Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga, aliwataka wakazi kudumisha amani na kuruhusu kila chama kufanya siasa kwa uhuru. 'ODM ilipigania uhuru wa kila Mkenya. Kila mtu ana haki ya kufika sehemu yoyote ya nchi na kuuza sera zake. Wanaotaka kuja Homa Bay wanakaribishwa,' alisema Bi Wanga. Aliwahimiza vijana kutoruhusu kutumiwa kuzua vurugu za kisiasa, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuvuruga amani. Bi Wanga alisisitiza kuwa Homa Bay bado ni ngome ya ODM, huku akifichua kuwa chama hicho kina mpango wa kuongeza wanachama wake na kuimarisha mtandao wake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Pia alithibitisha kuwa ODM itaendelea kushirikiana na serikali jumuishi na iko tayari kuanza mazungumzo na UDA kuhusu ushirikiano wa kisiasa kabla ya uchaguzi ujao. 'ODM inaamini katika ushirikishaji wa wote na kuheshimiana kati ya jamii mbalimbali. Tuko tayari kwa uchaguzi wa 2027 na hatuna hofu ya kukabiliana na yeyote,' alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 07 Aug 2026 00:55:27

Wanamazingira wajaa hofu baada ya kunguru hatari kutoka India kutua jijini

KUNGURU wavamizi kutoka India, wanaojulikana kwa kuharibu mazingira na kuangamiza ndege wa asili, wameonekana kwa mara ya kwanza jijini Nairobi, hali iliyozua hofu miongoni mwa wataalamu wa uhifadhi wa mazingira. Ndege hao walionekana awali katika Soko la Burma na mfanyabiashara mmoja aliyewaona akawafukuza bila kujua hatari wanayoweza kusababisha. Hata hivyo, picha yao ilipofikia wataalamu wa uhifadhi, ilithibitisha hofu ambayo wamekuwa nayo kwa miaka mingi. Kunguru hao, wanaojulikana kama Indian house crow, wamekuwa wakisambaa kutoka ukanda wa Pwani na sasa wameingia Nairobi, zaidi ya kilomita 400 kutoka Mombasa. Kwa miaka mingi, wengi walidhani tatizo hilo lilikuwa la Mombasa pekee. Historia inaonyesha kuwa ndege hao waliletwa Zanzibar miaka ya 1890 kusaidia kusafisha taka za chakula bandarini. Walipoongezeka, walivuka hadi Mombasa mwishoni mwa miaka ya 1940 na kuenea haraka katika ukanda wa Pwani kutoka Diani hadi Lamu. Mtafiti wa Makavazi ya Kitaifa ya Kenya, Bw John Musina, alisema kuongezeka kwa idadi yao kuliwaruhusu kusonga kuelekea maeneo ya bara. "Wamekuwa wakifuata miundombinu kama barabara. Walivuka eneo Tsavo, wakafika Makindu na sasa wameingia Nairobi,' alisema. Alisema kunguru hao ni miongoni mwa viumbe hatari zaidi kwa sababu hushindana na ndege wa asili kwa makazi na chakula huku wakivamia viota vyao na kula mayai pamoja na vifaranga. "Wanazaana kwa kasi kubwa kuliko ndege wa hapa, hivyo kuwafanya kupungua," alisema. Kwa mujibu wa Bw Musina, taka zinazotupwa ovyo katika majaa zimekuwa chanzo kikubwa cha chakula kinachowafanya kuongezeka kwa kasi. "Majaa yanawapa chakula kingi. Hiyo huwafanya wazaane kuliko ilivyo kawaida. Ukifika Mombasa utaona jinsi walivyo waharibifu," alisema. Wataalamu sasa wana hofu kuwa iwapo kunguru hao wataenea Nairobi, wataathiri ndege wanaopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Nairobi, ambayo ni miongoni mwa hifadhi chache duniani zilizo ndani ya jiji kuu. Pia kuna wasiwasi kuwa idadi yao inaweza kuongeza hatari ya ndege kugongana na ndege za abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na Uwanja wa Wilson. Kwa sasa, Makavazi ya Kitaifa ya Kenya kwa ushirikiano na Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS) zimeanza kufanya uchunguzi kubaini idadi ya ndege hao na maeneo waliyotua. Hadi sasa wameonekana katika eneo la Shauri Moyo na Soko la Burma pekee.Musina alisema hatua za mapema zinaweza kuzuia kuenea kwao. "Tunataka kutumia mbinu zilizofanikiwa Mombasa ili kudhibiti idadi yao kabla hawajaongezeka Nairobi," alisema. Kenya pia inachunguza mbinu zilizotumiwa nchini Afrika Kusini na Sri Lanka kudhibiti ndege hao. Hata hivyo, Bw Musina alionya kuwa juhudi hizo haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa nchi jirani. "Tukiwadhibiti hapa lakini wasidhibitiwe Tanzania, watarejea tena. Lazima tushirikiane kikanda," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 07 Aug 2026 01:30:13

Aliacha kazi ya udaktari serikalini, sasa analenga kubadilisha sekta ya afya

MIAKA kadhaa iliyopita, Dkt Godfrey Macharia Kiruhi alipokuwa akifanya kazi katika hospitali ya umma, alikumbana kila siku na changamoto kadhaa. Wagonjwa walikuwa wengi, lakini madaktari na wauguzi walikuwa wachache. Aligundua kuwa uhaba wa wataalamu wa afya ulikuwa ukisababisha msongamano mkubwa hospitalini huku wagonjwa wengi wakikosa huduma wanazohitaji kwa wakati ufaao. Kutokana na hali hiyo, Dkt Kiruhi aliamua kuacha ajira serikalini na kuanzisha zahanati ndogo ya kibinafsi ili kuwahudumia wakazi wa eneo lake. Kadiri mahitaji ya huduma za afya yalivyoongezeka, zahanati hiyo ilikua na hatimaye ikabadilika kuwa Hospitali ya Outspan, mojawapo ya hospitali zinazotambulika zaidi mjini Nyeri. Hata hivyo, ukuaji wa hospitali haukuondoa changamoto zote. Ingawa wahitimu wapya wa tiba walikuwa na maarifa ya kitaaluma, wengi wao walikosa huruma na uelewa wa mahitaji ya kihisia ya wagonjwa. Dkt Kiruhi alitambua kuwa mageuzi ya sekta ya afya yasingewezekana bila kubadilisha mfumo wa mafunzo ya wataalamu wa tiba. Mwaka wa 2009, alishirikiana na wadau wengine kuanzisha Chuo cha Tiba cha Outspan. [caption id="attachment_190893" align="alignnone" width="1500"] Hospitali ya Outspan iliyoanzishwa mnamo 2009. Kwa sasa hospitali hiyo imetoa fursa za ajira kwa wengi na kutoa matibabu kwa jamii. PICHA|MAKTABA[/caption] Mbali na masomo ya uuguzi na tiba, wanafunzi walilazimika kusoma saikolojia ili kuelewa hisia za wagonjwa, stadi za kidijitali za kutumia teknolojia za kisasa hospitalini pamoja na maadili ya kazi. Mwanzoni mwa mwaka huu, taasisi hiyo ilipata kibali cha muda kutoka Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) na kupandishwa hadhi kuwa Chuo Kikuu cha Outspan Global. Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Paul Mungai Mbugua, anasema mahitaji ya kozi za afya yameongezeka kwa kiwango kikubwa. Mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi yanafanyika katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Outspan iliyoko Nyeri. Chuo hicho pia kinawekeza katika huduma za afya ya akili, eneo ambalo bado halijapewa uzito unaostahili nchini. Naibu Makamu Mkuu anayeshughulikia mipango, utawala na fedha, Bw David Macharia, anasema wahitimu wa saikolojia kutoka chuo hicho hupata ajira kwa urahisi, ingawa bado jamii nyingi hazitambui umuhimu wa afya ya akili. Kupitia Kituo cha Serenity kilichopo Nyeri, chuo hicho huendesha kampeni za uhamasishaji kuhusu matatizo ya akili na kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza namna ya kuwasaidia waathiriwa wa uraibu wa dawa za kulevya na msongo wa mawazo. Pamoja na mafanikio hayo, taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uhaba wa madaktari bingwa katika nyanja kama saratani, magonjwa ya moyo na afya ya akili. Naibu Makamu Mkuu wa masuala ya kitaaluma, Dkt Lydia Muthoni, anasema chuo hicho kimejenga ushirikiano na vyuo vikuu vya kimataifa ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kunufaika na utaalamu wa kimataifa. Kwa sasa, chuo hicho kina wanafunzi 1,500 na kina ndoto ya kupanua huduma zake kote nchini na baadaye katika ukanda wa Afrika Mashariki. "Kila mwaka Wakenya wengi husafiri kwenda India kutafuta matibabu. Tunataka kubadilisha hali hiyo kwa kuimarisha huduma za afya hapa nyumbani ili wagonjwa kutoka mataifa mengine waanze kuja Kenya kutafuta matibabu," Bw Macharia aliambia Taifa Dijitali.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 07 Aug 2026 01:55:32

Makazi ya gavana Turkana yafyonza Sh300 milioni na bado hayajakamilika

ZAIDI ya miaka 10 tangu ujenzi wake uanze na karibu Sh300 milioni za walipa ushuru kutumika, makazi rasmi ya Gavana wa Turkana bado hayajakamilika huku mkandarasi wa pili akiondoka kwenye mradi huo. Kutokana na hali hiyo, gavana wa kaunti hiyo anaendelea kuishi katika makazi yake binafsi huku mradi uliotarajiwa kuwa moja ya mikubwa ya kaunti ukibaki kuwa ndoto. Ujenzi wa makazi hayo ulianzishwa mwaka wa 2015 wakati wa utawala wa gavana wa kwanza wa Turkana, Josphat Nanok. Hata hivyo, mradi huo umecheleweshwa mara kwa mara baada ya kampuni ya Landmark Holdings Limited, iliyopewa kandarasi mwaka wa fedha wa 2019/2020, kusitisha kazi ikidai haijalipwa fedha zake kwa wakati. Afisa Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa Kaunti ya Turkana, Winston Ebei, alisema serikali ya kaunti imeanza rasmi mchakato wa kuvunja mkataba na kampuni hiyo baada ya kuomba kujiondoa kwenye mradi. "Kwa kushirikiana na Ofisi ya Gavana na Timu ya Utekelezaji wa Miradi ya Kaunti, tulikagua eneo la ujenzi kubaini kazi iliyokamilika na ile ambayo bado haijafanywa," alisema. Kulingana na rekodi zilizowasilishwa mbele ya Kamati ya Seneti ya Hesabu za Serikali za Kaunti, mkandarasi wa kwanza alilipwa Sh206 milioni kwa kazi ya msingi na sehemu ya majengo. Baadaye mkandarasi mwingine alipewa kandarasi ya Sh90.5 milioni kukamilisha kazi iliyobaki. Hata hivyo, naye alisimamisha ujenzi akidai malipo ya Sh28 milioni ambayo hayakuwa yametolewa. Mwaka wa 2023, Kamati ya Seneti ya Hesabu za Serikali za Kaunti ilipotembelea eneo hilo, ilieleza wasiwasi kuhusu kiwango kikubwa cha fedha kilichotumika ikilinganishwa na kazi iliyofanywa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 07 Aug 2026 02:55:34

Wakulima wa mahindi wazongwa na madeni kutokana na mavuno duni msimu huu

MAMIA ya wakulima wa mahindi katika Bonde la Ufa wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni baada ya ukame, uhaba wa mbolea na mashambulizi ya viwavi jeshi kuharibu mazao yao. Hii inaweza kufanya wakulima wengi kupoteza mashamba yao yakipigwa mnada na madalali. Kwa miaka mingi, wakulima wamekuwa wakitegemea mikopo kutoka taasisi za kifedha kufadhili kilimo wakiamini mavuno mazuri yatawasaidia kulipa madeni na kujiandaa kwa msimu unaofuata. Lakini msimu huu hali imebadilika. Mahindi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa  yamekauka kabla ya kukomaa, jambo ambalo limefanya wakulima kuhofia kushindwa kulipa mikopo waliyochukua kutoka Shirika la Fedha za Kilimo (AFC), Benki ya KCB na Equity Bank. Hofu sasa ni kuwa baadhi yao wanaweza kupokonywa mashamba na mali nyingine ikiwa watashindwa kulipa madeni yao. Bw Samuel Macharia wa Moi's Bridge, Kaunti ya Uasin Gishu, alisema anahangaika kutafuta namna ya kulipa mkopo wa Sh1.5 milioni aliouchukua kutoka KCB kufadhili kilimo katika shamba lake la mahindi la ekari 70. Alisema kila mwaka amekuwa akikopa, kuvuna na kulipa mkopo bila matatizo. Hata hivyo, ukame wa msimu huu umeharibu mazao wakati muhimu wa ukuaji. "Kwa kawaida huwa nakopa kila mwaka na kulipa baada ya kuuza mahindi. Lakini mwaka huu mavuno yatakuwa mabaya sana na sijui nitapata wapi fedha za kulipa deni," alisema. Alikuwa akitarajia kuvuna zaidi ya magunia 1,500 ya mahindi na kupata zaidi ya Sh6 milioni. Fedha hizo zingelipa mkopo na kugharimia msimu mwingine wa kilimo. Tatizo lake limeongezeka baada ya mkewe pia kuchukua mkopo wa Sh1.2 milioni kutoka Equity Bank kununua tinga tinga. "Tuliamini tungelipa madeni hayo kwa mapato kutoka mavuno. Lakini ukame na magonjwa ya mazao yameharibu kila kitu," alisema. Katika eneo la Ziwa, mkulima Michael Kosgei alisema huenda akashindwa kulipa mkopo wa Sh500,000  kutoka AFC baada ya mahindi yake ya ekari 10 kunyauka. "Sitarajii kupata mavuno ya kutosha, hata kwa matumizi ya nyumbani. Hilo lina maana nitapata ugumu mkubwa kulipa mkopo," alisema. Kwa kawaida yeye huvuna kati ya magunia 25 na 30 kwa ekari lakini mwaka huu anatarajia mavuno duni sana. Alisema wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo walitembelea shamba lake kutathmini kiwango cha uharibifu na kukadiria mavuno yanayotarajiwa. Wakulima wengine wanasema serikali inapaswa kuingilia kati ili kuzuia taasisi za kifedha kupiga mnada mashamba yao. "Serikali inafaa kuwakinga wakulima dhidi ya kupoteza mashamba yao kutokana na hasara iliyosababishwa na ukame," alisema Amos Kipchirchir wa Moiben. Wakulima wengi  Kaskazini mwa Bonde la Ufa hutegemea mikopo kununua mbegu bora, mbolea na kugharimia shughuli nyingine za kilimo. Hata hivyo, mgogoro wa sasa umeonyesha umuhimu wa kuimarisha ufadhili wa sekta ya kilimo. Wanamtaka Rais William Ruto kutimiza ahadi yake ya kuongezea AFC pesa kutoka Sh5 bilioni hadi Sh20 bilioni kila mwaka na kupunguza riba ya mikopo. "Kuna mengi yanayohitajika zaidi ya mbolea ya bei nafuu. Wakulima wanahitaji mikopo ya kutosha na mabohari bora ya kuhifadhi mazao," alisema Isaac Kosgei wa Sergoit. Mkurugenzi Mkuu wa AFC George Kubai alisema mahitaji ya mikopo ni makubwa kuliko fedha zinazopatikana. Alisema shirika hupokea maombi ya mikopo ya thamani ya zaidi ya Sh15 bilioni kila mwaka lakini linaweza kutoa takriban Sh4 bilioni pekee.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 09:22:44

Ruto ataka walinzi wa kibinafsi na polisi kushirikiana katika ujasusi

RAIS William Ruto ametangaza kuwa serikali itaanza kutumia taarifa za kijasusi zinazokusanywa na walinzi wa kampuni za kibinafsi ili kuimarisha vita dhidi ya uhalifu na kuimarisha usalama nchini. Akizungumza Alhamisi katika Ikulu ya Nairobi alipokutana na mamia ya walinzi hao, Rais alisema mchango wao katika kulinda mali na maisha ya Wakenya ni muhimu na unapaswa kuunganishwa na juhudi za idara za usalama za serikali. Aliagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Mamlaka ya Kudhibiti Kampuni za Kibinafsi za Ulinzi (PSRA) na Afisi ya Rais kuandaa mfumo wa ushirikiano kati ya polisi na walinzi hao. 'Mnafanya kazi muhimu ya kuhakikisha usalama. Pia mnakusanya taarifa nyingi kuhusu wahalifu. Ushirikiano huu utasaidia kuimarisha usalama nchini,' alisema Rais Ruto. Rais pia alisema sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo zitarekebishwa ili kutoa nafasi ya kupandishwa vyeo kwa wanaofanya kazi kwa ufanisi. Aidha, aliagiza taasisi za mafunzo ya walinda usalama kuoanisha mitaala yao ili kuwe na mfumo mmoja wa maendeleo ya taaluma. Kuhusu mishahara, Dkt Ruto alisisitiza kuwa agizo la serikali la kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kwa asilimia 15 bado linafaa kutekelezwa. Alionya kampuni zinazowalipa walinzi chini ya kiwango cha chini cha mshahara, akisema baadhi hulipa wafanyakazi wao kiasi cha Sh6,000 pekee kwa mwezi. Pia alizitaka kampuni zote kuhakikisha wafanyakazi wao wamejiandikisha kikamilifu katika Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA). Katika hotuba yake, Rais pia alitetea rekodi ya serikali yake na kusema wapinzani wake hawana ajenda ya maendeleo isipokuwa kampeni ya kutaka ahudumu muhula mmoja.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 06:47:36

Kisii yageukia mfumo mbadala kutatua mauaji yaletwayo na migogoro ya mashamba

KAUNTI ya Kisii imezindua rasmi Mfumo Mbadala wa Haki wa mazungumzo maarufu kama Alternative Justice System (AJS) katika juhudi za kukomesha mauaji yanayosababishwa na migogoro ya ardhi ambayo imegharimu maisha ya mamia ya watu katika miaka ya hivi karibuni. Jaji Mkuu Martha Koome Jumanne alizindua Kituo cha AJS eneo la Mashauri pamoja na Mahakama ya Manispaa mjini Kisii. Aliandamana na Gavana wa gatuzi hilo Simba Arati, majaji na maafisa wakuu kutoka kwa Idara ya Mahakama. Akizungumza na wazee, mawakili na wakazi wa Kisii, Koome alisema mahakama za kawaida zimelemewa na idadi kubwa ya kesi na haziwezi tena kumaliza migogoro ya ardhi inayochochea mauaji kwa haraka. "Hatuezi kuendelea kuzika wazazi na watoto wetu kwa sababu ya ardhi. Mahakama zimejaa, kesi zinachukua miaka, na familia zinavunjika kabla ya hukumu kutolewa. Ndiyo maana tunawasihi wakazi kuzungumza kwanza kunapotokea migogoro kama hiyo," Koome alisema. Takwimu za vyombo vya usalama zinaonyesha angalau watu saba huuawa kila mwezi Kisii kutokana na migogoro ya mashamba. Kati ya Januari 2021 na Mei 2022, watu zaidi ya 126 walipoteza maisha, kulingana na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kisii kwa wakati huo Francis Kooli. Mahakama ya Kisii pia inasema zaidi ya asilimia 80 ya kesi zilizoko mbele yake ni za mauaji yanayotokana na migogoro ya ardhi. Kituo hicho cha AJS kitatumia Baraza la Wazee waliothibitishwa pamoja na wapatanishi wa mahakama kutatua migogoro ya mipaka, ardhi na ugomvi wa kifamilia. Kesi zitachunguzwa ndani ya siku 14. Ikiwa pande zote zitakubaliana, makubaliano yatasajiliwa mahakamani na kuwa na nguvu za kisheria. Ikiwa mazungumzo yatafeli, kesi itarudi mahakamani. Takwimu kutoka kaunti zilizozindua mfumo huo mbadala zinaonyesha kuwa AJS inamaliza baadhi ya ugomvi ndani ya miezi mitatu ikilinganishwa na miaka mitatu mahakamani. Jaji Mkuu alimwomba Gavana Arati kuwasaidia kifedha wazee hao kwa kuwa watakuwa na jukumu kubwa katika kusikiza kesi. Pamoja na AJS, Koome pia alizindua Mahakama ya Manispaa itakayoshughulikia makosa madogo kama kama vile utupaji taka kiholela, kelele na ukiukaji wa sheria za trafiki. Gavana Arati alisema mahakama hiyo itarejesha nidhamu mjini Kisii. "Kwa muda mrefu mji wetu umeteseka na uchafu. Watu wanatupa taka ovyo. Sasa tutakuwa na mahali pa kuwafikisha watupaji hao wa kiholela mara moja," alisema. Arati alidokeza kuwa tayari amezindua timu ya vijana wa kusafisha na kusimamia sheria za mazingira mjini Kisii, ingawa wakazi wamelalamika kuwa timu hiyo "imekuwa ikiwanyasa". "Tukikukamata ukitupa takataka ovyo, hatutakupa onyo. Tutakupeleka mahakamani," alionya. Ugomvi wa ardhi Kisii ni dondasugu. Watoto hawasubiri hata wazazi wao kufa. Baba akiwa mgonjwa tu, ugomvi wa hati ya ardhi unaanza.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 02:55:54

Maafisa wa kaunti watumia mfumo wa malipo kupora mamilioni ya pesa za umma

KAUNTI nyingi nchini zimegeuza mfumo wa malipo ya dharura maarufu kuwa njia mpya ya kupora pesa za umma kupitia madai ya matumizi yasiyo na msingi, ripoti mpya za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) zinaonyesha. Mfumo huu wa malipo ulianzishwa mwaka wa 2013 baada ya ugatuzi kuanza, ukiwa na lengo la kurahisisha malipo ya haraka ya matumizi madogo yasiyopangwa ambayo hayawezi kuzidi Sh2 milioni. Lakini miaka kadhaa baadaye, mfumo huo umegeuzwa kuwa chanzo cha ufisadi huku maafisa wa kaunti wakidai fedha kwa shughuli ambazo hazikufanyika au kushindwa kuwasilisha hesabu za matumizi hayo. Ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, na EACC zinaonyesha kuwa matumizi mabaya ya mfumo huo sasa ni mojawapo ya mbinu mpya zinazotumiwa kupora mamilioni ya pesa za walipa ushuru. Ukaguzi wa miaka ya kifedha ya 2023/2024 na 2024/2025 umebaini kuwa kaunti huenda zilipoteza zaidi ya Sh500 milioni kupitia mfumo huo. Katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024 pekee, kaunti 12 zilishindwa kueleza matumizi ya zaidi ya Sh230 milioni zilizotolewa kwa malipo ya dharura. Ripoti hiyo inaonyesha baadhi ya maafisa walipewa pesa zaidi ya mara moja, kinyume cha sheria za usimamizi wa fedha za serikali za kaunti zinazowataka kurejesha au kuwasilisha hesabu za fedha hizo ndani ya siku saba baada ya kurejea kazini. Sheria hizo pia zinakataza afisa kupewa pesa upya kabla ya kuwasilisha hesabu ya ile ya awali au fedha hizo kukatwa kwenye mshahara wake. Kaunti ya Turkana ndiyo inaongoza kwa fedha ambazo hazijaelezwa matumizi yake ikiwa na Sh85 milioni. Samburu inafuata kwa Sh39.3 milioni, Mombasa Sh25.8 milioni, Bungoma Sh21.6 milioni, Tana River Sh19.8 milioni na Embu Sh12.8 milioni. Siaya na Nandi kila moja ina Sh6.3, Kisumu Sh5.1 milioni, Nyandarua Sh3 milioni, Busia Sh1.3 milioni huku Kiambu ikiwa na zaidi ya Sh801,000. Mkaguzi Mkuu alisema baadhi ya serikali za kaunti hazikuwa na sajili sahihi ya pesa chini ya mfumo huu kama inavyotakiwa na sheria. Kutokana na hali hiyo, imekuwa vigumu kufuatilia nani alipokea fedha hizo, kiasi alichopewa, tarehe ya kutolewa na iwapo fedha hizo zilirejeshwa au matumizi yake kuelezwa. Katika Kaunti ya Isiolo, ukaguzi ulibaini maafisa wawili walipewa jumla ya Sh8.4 milioni kabla ya kuwasilisha hesabu za fedha walizopewa awali. Aidha, kaunti hiyo ilitoa Sh4 milioni kupitia kwa shughuli ya upangaji wa ardhi Garbatulla na utoaji wa hati za ugavi wa ardhi, hatua ambayo wakaguzi wanasema haikufuata utaratibu unaostahili. Katika Kaunti ya Wajir, zaidi ya Sh149 milioni zilihamishwa kutoka akaunti za Benki Kuu ya Kenya hadi akaunti za benki ya kibiashara zilizokuwa zikitumika kwa mfumo huu na baadaye kutumiwa kwa malipo ya kawaida ya shughuli za kaunti. Kaunti ya Embu ilikuwa na zaidi ya Sh21.8 milioni ambazo hazikuelezwa matumizi yake kufikia Juni 30, 2025. Machakos ilikuwa na zaidi ya Sh3.6 milioni ambazo hazikuwa zimerejeshwa kwa wakati, huku Samburu ikiwa na zaidi ya Sh1.3 milioni ambazo zilikuwa zimechelewa kurejeshwa bila hatua zozote kuchukuliwa. Katika Kaunti ya Kakamega, kulikuwa na zaidi ya Sh18.3 milioni ambazo hazikuwa zimeelezwa, huku Nandi, Uasin Gishu na Siaya zikitajwa kwa kushindwa kuweka rekodi sahihi za utoaji na urejeshaji wa fedha hizo. Kwa upande wake, EACC ilisema imekuwa ikichunguza visa vingi ambapo mfumo huu umegeuzwa chanzo cha kujinufaisha na fedha za umma. Mwenyekiti wa EACC, Bw Abdi Mohamud, alisema baadhi ya maafisa wamekuwa wakichukua mfumo huu kana kwamba ni pesa zao binafsi. Ripoti hizo sasa zimeibua wasiwasi kuhusu udhaifu wa usimamizi wa fedha za umma katika kaunti na kuibua wito wa hatua kali dhidi ya maafisa wanaotumia mianya hiyo kujinufaisha kwa gharama ya walipa ushuru.

read more