taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 09 Jul 2026 08:35:33
Trump aapa kuipiga Iran mpaka isalimu amri
WASHINGTON, Amerika: JESHI la Amerika limesema lilianzisha uvamizi dhidi ya Iran ili kuhakikisha Mkondo-bahari wa Hormuz unafunguliwa kwa usafirishaji wa mafuta na bidhaa nyingine muhimu duniani. Hatua hiyo imesababisha Iran nayo kulipiza kisasi kwa kushambulia kambi za kijeshi za Amerika nchini Kuwait na Bahrain. Vita kati ya mataifa hayo mawili vimechipuka upya huku mazungumzo ya kusitisha vita kati yao yakionekana kutozaa matunda yoyote hivi karibuni. Amerika ilishambulia Iran baada ya nchi hiyo kushambulia meli za kusafirisha mizigo. Rais wa Amerika, Donald Trump tayari amesema kuwa mazungumzo ya kusaka amani na Iran yamekufa na sasa ni wakati wa kurejelea vita. "Wanajeshi wa Amerika wameanza kuendeleza mashambulizi zaidi dhidi ya Iran ili kuwalemaza wasiwe na nguvu tena ya kuzuia usafirishaji wa mafuta na mali kwenye Mlango-bahari wa Hormuz," akasema Kamanda wa jeshi la Amerika katika Ukanda wa Mashariki maarufu kama CENTOM kupitia X. "Amerika inalaumu Iran kwa kushambulia meli ambazo zilikuwa zikipitia mkondo wa Hormuz na kuhatarisha maisha ya manahodha wake," ikaongeza. Mashambulizi ya Amerika yalivuruga miji mingi Kusini mwa Pwani ya Iran huku baadhi ikikosa umeme. Iran nayo ilijibu kwa kushambulia Kuwait na Bahrain ambazo zina makao ya wanajeshi wa Amerika. Wizara ya Ulinzi ya Kuwait ilisema kuwa ilikuwa ikitungua droni na makombora kutoka Iran lakini Qatar nayo ilitoa onyo la kiusalama. Afisa mmoja wa usalama wa Amerika alisema kuwa mashambulizi dhidi ya Iran yataongezeka na kuonya kuwa mara hii wanalenga kulemaza taifa hilo kabisa kijeshi.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 13 hours ago
Ruto afufua mbinu za Moi kujenga mtandao wa ushawishi mashinani kuelekea uchaguzi mkuu
RAIS William Ruto anaonekana kufufua baadhi ya mikakati iliyotumiwa na mlezi wake wa siasa hayati rais Daniel arap Moi ya kuimarisha utawala wa mashinani, baada ya kuwatambua rasmi wazee wa vijiji na kuwaingiza katika mfumo wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAO). Hatua hiyo imezua mjadala mpya kuhusu iwapo serikali inalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi au inajenga upya mtandao wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Kwa miaka mingi, machifu, manaibu wao na makamishna wa mikoa walikuwa nguzo kuu ya serikali za Moi. Mbali na kusimamia usalama na utekelezaji wa sera za serikali, walitumiwa pia kuhamasisha wananchi kuunga mkono chama tawala cha Kanu. Lakini mfumo huo ulikosolewa vikali wakati wa harakati za kurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa miaka ya 1990, huku viongozi wa upinzani wakidai ulitumiwa kuwanyanyasa wakosoaji wa serikali na kuvuruga shughuli za kisiasa. Ingawa Katiba ya mwaka 2010 na ugatuzi ulipunguza mamlaka ya utawala huo, serikali zilizofuata ziliendelea kuuhifadhi kwa kuubadilisha na kuuita Utawala wa Serikali ya Kitaifa. Sasa, miaka 16 baadaye, Rais Ruto ameupanua zaidi kwa kuwaingiza rasmi wazee wa vijiji katika mfumo huo. Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi mbele ya zaidi ya wazee wa vijiji 10,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini, Rais alisema wazee 106,000 wameingizwa rasmi katika utawala wa mikoa. Alitangaza kuwa kila mmoja wao ataanza kupokea posho ya Sh3,000 kila mwezi, baada ya kuhudumu kwa miaka mingi bila malipo. Aidha, alisema serikali italipia bima yao ya afya kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), kuwapatia simu za kisasa za kurahisisha kazi zao na kuongeza maafisa wa Polisi wa Utawala katika maeneo yao. Pia alimwagiza Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi, kutenga fedha katika bajeti ya ziada ili serikali ilipie michango ya SHA kwa wazee hao, wake au waume wao pamoja na watoto wao kuanzia Januari 2027. Rais alisema lengo ni kuwapa wazee wa vijiji nafasi rasmi katika utawala wa serikali na kuimarisha ushirikiano wao na machifu, manaibu wa machifu na maafisa wengine wa serikali. Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Raymond Omollo, alisema huo ni uamuzi wa kihistoria kwa sababu ni mara ya kwanza wazee wa vijiji kutambuliwa rasmi na kupewa malipo ya kila mwezi. Alisema hatua hiyo itaimarisha uongozi mashinani, kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Hata hivyo, mkutano huo uligeuka wa kisiasa baada ya Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Kimani Ichung'wah kuwataka wazee hao kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027. "Mmengoja kutambuliwa kwa miaka mingi. Rais Ruto ametimiza ahadi hiyo. Mkumbukeni na wakati ukifika, muungeni pia," alisema Bw Ichung'wah. Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, pia alitaka Rais aungwe kwa muhula wa pili, akisema ametambua mchango wa wazee wa vijiji kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Mkuu wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi, alisema serikali itaendelea kuwaunga mkono wazee hao ili kuimarisha usalama na huduma kwa wananchi, huku akieleza kuwa uongozi wa Rais Ruto umeifanya Kenya kuwa na ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika. Lakini viongozi wa upinzani walikosoa mpango huo. Kiongozi wa chama cha DCP, Bw Rigathi Gachagua, alisema serikali imekuwa ikitoa ahadi nyingi ambazo hazijatekelezwa. "Aliahidi machifu vipakatalishi lakini mpaka leo hawajazipata. Sasa anawaahidi wazee wa vijiji simu za kisasa. Kwa nini wamwamini?" alihoji. Pia alisema baadhi ya wazee wa vijiji wamemweleza kuwa posho ya Sh3,000 haitoshi kukabiliana na gharama ya maisha. Wachambuzi wa siasa wanasema hatua ya serikali kuimarisha mtandao wa utawala mashinani inaweza kuboresha huduma kwa wananchi, lakini pia inaweza kupatia utawala huo uzito mkubwa wa kisiasa huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 12 hours ago
Jinsi ya kusafisha korodani na makosa yanayofanywa na wanaume
WANAUME wengi hawazingatii sana jinsi wanavyosafisha sehemu zao za siri. Wengi huamini kwamba kuoga kila siku kunatosha, lakini madaktari wa mfumo wa mkojo wanasema si kila wakati. Kutumia sabuni kali, kukaa muda mrefu na chupi zenye jasho au kupuuza usafi wa sehemu za siri kunaweza kusababisha mwasho, fangasi, harufu mbaya na matatizo mengine yanayoweza kuzuiliwa. Daktari mtaalamu wa mfumo wa mkojo, Dkt Victor Albert Okoth, anasema usafi wa korodani ni sehemu muhimu ya afya ya uzazi wa mwanaume. "Usafi mzuri ni kusafisha sehemu hizo bila kupita kiasi. Ngozi ya sehemu za siri ni nyepesi na kuisugua sana kunaweza kusababisha majeraha na mwasho," anasema. Anashauri wanaume waoge sehemu za siri angalau mara moja kila siku kwa kutumia maji ya uvuguvugu. Wakati wa kuoga, mwanaume anapaswa kuosha uume, korodani, kinena na eneo lililo kati ya korodani na njia ya haja kubwa. Kwa wanaume ambao hawajatahiriwa, anashauri wavute govi nyuma, waoshe sehemu iliyo chini yake vizuri, wasuuze kwa maji kisha warudishe govi mahali pake. "Hakuna haja ya kusugua korodani kwa nguvu. Tumia mikono. Kusudi ni kuondoa uchafu, si kuua kila kimelea," anasema. Dkt Okoth anaongeza kuwa wanaume wanaofanya mazoezi mara kwa mara, wanaofanya kazi nje au wanaokaa katika mazingira yenye joto wanapaswa kuoga tena baada ya kutoa jasho. Anasema jasho hutengeneza mazingira yenye unyevunyevu yanayochochea ukuaji wa fangasi na bakteria. "Hali ya hewa ya Kenya huwa na joto katika maeneo mengi. Kuoga baada ya mazoezi na kubadilisha chupi yenye jasho ni tabia muhimu ya kujikinga na maambukizi," anasema. Hata hivyo, anaonya kuwa kuosha sehemu hizo mara nyingi kupita kiasi kunaweza kuharibu kinga ya ngozi na kusababisha ukavu, mwasho na uvimbe. Dkt Okoth anashauri matumizi ya maji pekee au sabuni laini isiyo na manukato makali. Anasema wanaume wengi huamini sabuni zenye povu nyingi au harufu kali husafisha vizuri zaidi, jambo ambalo si kweli. Bidhaa kama dawa za kuondoa harufu vinaweza kusababisha mwasho isipokuwa kwa ushauri wa daktari. Baada ya kuoga, sehemu za siri zinapaswa kukaushwa vizuri kwa taulo safi. Anasema unyevunyevu unaobaki kwenye ngozi huchochea ukuaji wa fangasi. Kwa wanaume ambao hawajatahiriwa, sehemu iliyo chini ya govi inapaswa kukaushwa vizuri kabla ya kuirudisha. Pia anashauri wanaume kuvaa chupi zinazopitisha hewa na kuzibadilisha kila siku au mara moja zinapolowa na jasho. Dkt Okoth anasema makosa yanayofanywa mara nyingi ni kutosafisha chini ya govi, kutumia sabuni kali au manukato kwenye sehemu za siri, kuvaa chupi yenye jasho kwa muda mrefu na kunyoa nywele za sehemu za siri kwa ukali kiasi cha kujeruhi ngozi. Anasema kosa kubwa zaidi ni kudhani kila tatizo la sehemu za siri husababishwa na uchafu. "Harufu, vipele, uvimbe au usaha si lazima vitokane na ukosefu wa usafi. Magonjwa ya zinaa kama kisonono huenezwa kupitia ngono na yanahitaji uchunguzi na matibabu ya kitaalamu," anasema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Linda Mwananchi yalenga ngome za Raila ambazo ODM inapambana kuzihifadhi kwa ajili ya Ruto
BAADA ya kufanya mikutano iliyofanikiwa katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia wiki mbili zilizopita, viongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi sasa wamehamishia kampeni zao katika ngome za kisiasa za aliyekuwa kinara wa ODM, Raila Odinga, wakilenga kuimarisha ushawishi wao huku wakipanua mtandao wao nchini. Vuguvugu hilo linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, linatarajia kufanya mikutano Busia Ijumaa kabla ya kuelekea Kakamega Jumamosi na Jumapili. Viongozi hao wananuia kuvutia wafuasi wa ODM katika eneo la Magharibi huku chama hicho kikijitahidi kulinda ngome zake za jadi. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, ambaye ameahidi kuunga mkono azma ya Bw Sifuna ya kuwania urais mwaka 2027, anatarajiwa kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuunganisha kura za jamii ya Mulembe kabla ya kampeni hizo kusambazwa kote nchini. Ziara ya Kakamega pia inalenga ngome ya viongozi wanaounga mkono Rais William Ruto akiwemo Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, Gavana Fernandes Barasa, Naibu Gavana Ayub Savula pamoja na zaidi ya wabunge wanane wanaounga mkono serikali jumuishi. Ziara hiyo inafanyika wiki chache baada ya Bw Oparanya kufanya mkutano Malava ambapo alipendekezwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto na kuahidi kuongoza juhudi za kuunganisha eneo la Magharibi kumuunga mkono Rais huku akiimarisha ODM. Mnamo Agosti 16, msafara wa Linda Mwananchi utaelekea Homa Bay, mojawapo ya ngome kuu za ODM, ukiongozwa na Gavana Orengo. Hii itakuwa mara ya pili kwa kundi hilo kuingia eneo la Luo Nyanza baada ya kufanya mkutano Kisumu. Bw Orengo pia analenga kuimarisha nafasi yake kama msemaji wa kisiasa wa jamii ya Waluo kupitia mikutano Homa Bay, Kisumu na Siaya, huku mipango ikisukwa kupeleka kampeni hizo Migori. Hata hivyo, maandalizi ya mkutano wa Homa Bay yamekumbwa na misukosuko baada ya kuripotiwa visa vya vurugu. Mratibu wa muda wa Linda Mwananchi katika eneo hilo, Samuel Nyauke, alishambuliwa na kundi la vijana waliomshutumu kwa kupuuza uongozi wa kisiasa wa eneo hilo. Mali iliharibiwa baada ya mawe kurushwa katika ofisi yake, huku vijana sita wakikamatwa na baadaye kuachiliwa. 'Kwa wanaotumia vurugu kulinda maeneo yao ya kisiasa, Kenya ni ya Wakenya wote. Hakuna vitisho vitakavyotuzuia. Tutakuwa Homa Bay kama ilivyopangwa,' alisema Bw Orengo. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa ODM ambaye pia ni Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga, aliwataka wakazi kudumisha amani na kuruhusu kila chama kufanya siasa kwa uhuru. 'ODM ilipigania uhuru wa kila Mkenya. Kila mtu ana haki ya kufika sehemu yoyote ya nchi na kuuza sera zake. Wanaotaka kuja Homa Bay wanakaribishwa,' alisema Bi Wanga. Aliwahimiza vijana kutoruhusu kutumiwa kuzua vurugu za kisiasa, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuvuruga amani. Bi Wanga alisisitiza kuwa Homa Bay bado ni ngome ya ODM, huku akifichua kuwa chama hicho kina mpango wa kuongeza wanachama wake na kuimarisha mtandao wake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Pia alithibitisha kuwa ODM itaendelea kushirikiana na serikali jumuishi na iko tayari kuanza mazungumzo na UDA kuhusu ushirikiano wa kisiasa kabla ya uchaguzi ujao. 'ODM inaamini katika ushirikishaji wa wote na kuheshimiana kati ya jamii mbalimbali. Tuko tayari kwa uchaguzi wa 2027 na hatuna hofu ya kukabiliana na yeyote,' alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Wanamazingira wajaa hofu baada ya kunguru hatari kutoka India kutua jijini
KUNGURU wavamizi kutoka India, wanaojulikana kwa kuharibu mazingira na kuangamiza ndege wa asili, wameonekana kwa mara ya kwanza jijini Nairobi, hali iliyozua hofu miongoni mwa wataalamu wa uhifadhi wa mazingira. Ndege hao walionekana awali katika Soko la Burma na mfanyabiashara mmoja aliyewaona akawafukuza bila kujua hatari wanayoweza kusababisha. Hata hivyo, picha yao ilipofikia wataalamu wa uhifadhi, ilithibitisha hofu ambayo wamekuwa nayo kwa miaka mingi. Kunguru hao, wanaojulikana kama Indian house crow, wamekuwa wakisambaa kutoka ukanda wa Pwani na sasa wameingia Nairobi, zaidi ya kilomita 400 kutoka Mombasa. Kwa miaka mingi, wengi walidhani tatizo hilo lilikuwa la Mombasa pekee. Historia inaonyesha kuwa ndege hao waliletwa Zanzibar miaka ya 1890 kusaidia kusafisha taka za chakula bandarini. Walipoongezeka, walivuka hadi Mombasa mwishoni mwa miaka ya 1940 na kuenea haraka katika ukanda wa Pwani kutoka Diani hadi Lamu. Mtafiti wa Makavazi ya Kitaifa ya Kenya, Bw John Musina, alisema kuongezeka kwa idadi yao kuliwaruhusu kusonga kuelekea maeneo ya bara. "Wamekuwa wakifuata miundombinu kama barabara. Walivuka eneo Tsavo, wakafika Makindu na sasa wameingia Nairobi,' alisema. Alisema kunguru hao ni miongoni mwa viumbe hatari zaidi kwa sababu hushindana na ndege wa asili kwa makazi na chakula huku wakivamia viota vyao na kula mayai pamoja na vifaranga. "Wanazaana kwa kasi kubwa kuliko ndege wa hapa, hivyo kuwafanya kupungua," alisema. Kwa mujibu wa Bw Musina, taka zinazotupwa ovyo katika majaa zimekuwa chanzo kikubwa cha chakula kinachowafanya kuongezeka kwa kasi. "Majaa yanawapa chakula kingi. Hiyo huwafanya wazaane kuliko ilivyo kawaida. Ukifika Mombasa utaona jinsi walivyo waharibifu," alisema. Wataalamu sasa wana hofu kuwa iwapo kunguru hao wataenea Nairobi, wataathiri ndege wanaopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Nairobi, ambayo ni miongoni mwa hifadhi chache duniani zilizo ndani ya jiji kuu. Pia kuna wasiwasi kuwa idadi yao inaweza kuongeza hatari ya ndege kugongana na ndege za abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na Uwanja wa Wilson. Kwa sasa, Makavazi ya Kitaifa ya Kenya kwa ushirikiano na Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS) zimeanza kufanya uchunguzi kubaini idadi ya ndege hao na maeneo waliyotua. Hadi sasa wameonekana katika eneo la Shauri Moyo na Soko la Burma pekee.Musina alisema hatua za mapema zinaweza kuzuia kuenea kwao. "Tunataka kutumia mbinu zilizofanikiwa Mombasa ili kudhibiti idadi yao kabla hawajaongezeka Nairobi," alisema. Kenya pia inachunguza mbinu zilizotumiwa nchini Afrika Kusini na Sri Lanka kudhibiti ndege hao. Hata hivyo, Bw Musina alionya kuwa juhudi hizo haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa nchi jirani. "Tukiwadhibiti hapa lakini wasidhibitiwe Tanzania, watarejea tena. Lazima tushirikiane kikanda," alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Aliacha kazi ya udaktari serikalini, sasa analenga kubadilisha sekta ya afya
MIAKA kadhaa iliyopita, Dkt Godfrey Macharia Kiruhi alipokuwa akifanya kazi katika hospitali ya umma, alikumbana kila siku na changamoto kadhaa. Wagonjwa walikuwa wengi, lakini madaktari na wauguzi walikuwa wachache. Aligundua kuwa uhaba wa wataalamu wa afya ulikuwa ukisababisha msongamano mkubwa hospitalini huku wagonjwa wengi wakikosa huduma wanazohitaji kwa wakati ufaao. Kutokana na hali hiyo, Dkt Kiruhi aliamua kuacha ajira serikalini na kuanzisha zahanati ndogo ya kibinafsi ili kuwahudumia wakazi wa eneo lake. Kadiri mahitaji ya huduma za afya yalivyoongezeka, zahanati hiyo ilikua na hatimaye ikabadilika kuwa Hospitali ya Outspan, mojawapo ya hospitali zinazotambulika zaidi mjini Nyeri. Hata hivyo, ukuaji wa hospitali haukuondoa changamoto zote. Ingawa wahitimu wapya wa tiba walikuwa na maarifa ya kitaaluma, wengi wao walikosa huruma na uelewa wa mahitaji ya kihisia ya wagonjwa. Dkt Kiruhi alitambua kuwa mageuzi ya sekta ya afya yasingewezekana bila kubadilisha mfumo wa mafunzo ya wataalamu wa tiba. Mwaka wa 2009, alishirikiana na wadau wengine kuanzisha Chuo cha Tiba cha Outspan. [caption id="attachment_190893" align="alignnone" width="1500"] Hospitali ya Outspan iliyoanzishwa mnamo 2009. Kwa sasa hospitali hiyo imetoa fursa za ajira kwa wengi na kutoa matibabu kwa jamii. PICHA|MAKTABA[/caption] Mbali na masomo ya uuguzi na tiba, wanafunzi walilazimika kusoma saikolojia ili kuelewa hisia za wagonjwa, stadi za kidijitali za kutumia teknolojia za kisasa hospitalini pamoja na maadili ya kazi. Mwanzoni mwa mwaka huu, taasisi hiyo ilipata kibali cha muda kutoka Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) na kupandishwa hadhi kuwa Chuo Kikuu cha Outspan Global. Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Paul Mungai Mbugua, anasema mahitaji ya kozi za afya yameongezeka kwa kiwango kikubwa. Mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi yanafanyika katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Outspan iliyoko Nyeri. Chuo hicho pia kinawekeza katika huduma za afya ya akili, eneo ambalo bado halijapewa uzito unaostahili nchini. Naibu Makamu Mkuu anayeshughulikia mipango, utawala na fedha, Bw David Macharia, anasema wahitimu wa saikolojia kutoka chuo hicho hupata ajira kwa urahisi, ingawa bado jamii nyingi hazitambui umuhimu wa afya ya akili. Kupitia Kituo cha Serenity kilichopo Nyeri, chuo hicho huendesha kampeni za uhamasishaji kuhusu matatizo ya akili na kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza namna ya kuwasaidia waathiriwa wa uraibu wa dawa za kulevya na msongo wa mawazo. Pamoja na mafanikio hayo, taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uhaba wa madaktari bingwa katika nyanja kama saratani, magonjwa ya moyo na afya ya akili. Naibu Makamu Mkuu wa masuala ya kitaaluma, Dkt Lydia Muthoni, anasema chuo hicho kimejenga ushirikiano na vyuo vikuu vya kimataifa ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kunufaika na utaalamu wa kimataifa. Kwa sasa, chuo hicho kina wanafunzi 1,500 na kina ndoto ya kupanua huduma zake kote nchini na baadaye katika ukanda wa Afrika Mashariki. "Kila mwaka Wakenya wengi husafiri kwenda India kutafuta matibabu. Tunataka kubadilisha hali hiyo kwa kuimarisha huduma za afya hapa nyumbani ili wagonjwa kutoka mataifa mengine waanze kuja Kenya kutafuta matibabu," Bw Macharia aliambia Taifa Dijitali.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Makazi ya gavana Turkana yafyonza Sh300 milioni na bado hayajakamilika
ZAIDI ya miaka 10 tangu ujenzi wake uanze na karibu Sh300 milioni za walipa ushuru kutumika, makazi rasmi ya Gavana wa Turkana bado hayajakamilika huku mkandarasi wa pili akiondoka kwenye mradi huo. Kutokana na hali hiyo, gavana wa kaunti hiyo anaendelea kuishi katika makazi yake binafsi huku mradi uliotarajiwa kuwa moja ya mikubwa ya kaunti ukibaki kuwa ndoto. Ujenzi wa makazi hayo ulianzishwa mwaka wa 2015 wakati wa utawala wa gavana wa kwanza wa Turkana, Josphat Nanok. Hata hivyo, mradi huo umecheleweshwa mara kwa mara baada ya kampuni ya Landmark Holdings Limited, iliyopewa kandarasi mwaka wa fedha wa 2019/2020, kusitisha kazi ikidai haijalipwa fedha zake kwa wakati. Afisa Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa Kaunti ya Turkana, Winston Ebei, alisema serikali ya kaunti imeanza rasmi mchakato wa kuvunja mkataba na kampuni hiyo baada ya kuomba kujiondoa kwenye mradi. "Kwa kushirikiana na Ofisi ya Gavana na Timu ya Utekelezaji wa Miradi ya Kaunti, tulikagua eneo la ujenzi kubaini kazi iliyokamilika na ile ambayo bado haijafanywa," alisema. Kulingana na rekodi zilizowasilishwa mbele ya Kamati ya Seneti ya Hesabu za Serikali za Kaunti, mkandarasi wa kwanza alilipwa Sh206 milioni kwa kazi ya msingi na sehemu ya majengo. Baadaye mkandarasi mwingine alipewa kandarasi ya Sh90.5 milioni kukamilisha kazi iliyobaki. Hata hivyo, naye alisimamisha ujenzi akidai malipo ya Sh28 milioni ambayo hayakuwa yametolewa. Mwaka wa 2023, Kamati ya Seneti ya Hesabu za Serikali za Kaunti ilipotembelea eneo hilo, ilieleza wasiwasi kuhusu kiwango kikubwa cha fedha kilichotumika ikilinganishwa na kazi iliyofanywa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Wakulima wa mahindi wazongwa na madeni kutokana na mavuno duni msimu huu
MAMIA ya wakulima wa mahindi katika Bonde la Ufa wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni baada ya ukame, uhaba wa mbolea na mashambulizi ya viwavi jeshi kuharibu mazao yao. Hii inaweza kufanya wakulima wengi kupoteza mashamba yao yakipigwa mnada na madalali. Kwa miaka mingi, wakulima wamekuwa wakitegemea mikopo kutoka taasisi za kifedha kufadhili kilimo wakiamini mavuno mazuri yatawasaidia kulipa madeni na kujiandaa kwa msimu unaofuata. Lakini msimu huu hali imebadilika. Mahindi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa yamekauka kabla ya kukomaa, jambo ambalo limefanya wakulima kuhofia kushindwa kulipa mikopo waliyochukua kutoka Shirika la Fedha za Kilimo (AFC), Benki ya KCB na Equity Bank. Hofu sasa ni kuwa baadhi yao wanaweza kupokonywa mashamba na mali nyingine ikiwa watashindwa kulipa madeni yao. Bw Samuel Macharia wa Moi's Bridge, Kaunti ya Uasin Gishu, alisema anahangaika kutafuta namna ya kulipa mkopo wa Sh1.5 milioni aliouchukua kutoka KCB kufadhili kilimo katika shamba lake la mahindi la ekari 70. Alisema kila mwaka amekuwa akikopa, kuvuna na kulipa mkopo bila matatizo. Hata hivyo, ukame wa msimu huu umeharibu mazao wakati muhimu wa ukuaji. "Kwa kawaida huwa nakopa kila mwaka na kulipa baada ya kuuza mahindi. Lakini mwaka huu mavuno yatakuwa mabaya sana na sijui nitapata wapi fedha za kulipa deni," alisema. Alikuwa akitarajia kuvuna zaidi ya magunia 1,500 ya mahindi na kupata zaidi ya Sh6 milioni. Fedha hizo zingelipa mkopo na kugharimia msimu mwingine wa kilimo. Tatizo lake limeongezeka baada ya mkewe pia kuchukua mkopo wa Sh1.2 milioni kutoka Equity Bank kununua tinga tinga. "Tuliamini tungelipa madeni hayo kwa mapato kutoka mavuno. Lakini ukame na magonjwa ya mazao yameharibu kila kitu," alisema. Katika eneo la Ziwa, mkulima Michael Kosgei alisema huenda akashindwa kulipa mkopo wa Sh500,000 kutoka AFC baada ya mahindi yake ya ekari 10 kunyauka. "Sitarajii kupata mavuno ya kutosha, hata kwa matumizi ya nyumbani. Hilo lina maana nitapata ugumu mkubwa kulipa mkopo," alisema. Kwa kawaida yeye huvuna kati ya magunia 25 na 30 kwa ekari lakini mwaka huu anatarajia mavuno duni sana. Alisema wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo walitembelea shamba lake kutathmini kiwango cha uharibifu na kukadiria mavuno yanayotarajiwa. Wakulima wengine wanasema serikali inapaswa kuingilia kati ili kuzuia taasisi za kifedha kupiga mnada mashamba yao. "Serikali inafaa kuwakinga wakulima dhidi ya kupoteza mashamba yao kutokana na hasara iliyosababishwa na ukame," alisema Amos Kipchirchir wa Moiben. Wakulima wengi Kaskazini mwa Bonde la Ufa hutegemea mikopo kununua mbegu bora, mbolea na kugharimia shughuli nyingine za kilimo. Hata hivyo, mgogoro wa sasa umeonyesha umuhimu wa kuimarisha ufadhili wa sekta ya kilimo. Wanamtaka Rais William Ruto kutimiza ahadi yake ya kuongezea AFC pesa kutoka Sh5 bilioni hadi Sh20 bilioni kila mwaka na kupunguza riba ya mikopo. "Kuna mengi yanayohitajika zaidi ya mbolea ya bei nafuu. Wakulima wanahitaji mikopo ya kutosha na mabohari bora ya kuhifadhi mazao," alisema Isaac Kosgei wa Sergoit. Mkurugenzi Mkuu wa AFC George Kubai alisema mahitaji ya mikopo ni makubwa kuliko fedha zinazopatikana. Alisema shirika hupokea maombi ya mikopo ya thamani ya zaidi ya Sh15 bilioni kila mwaka lakini linaweza kutoa takriban Sh4 bilioni pekee.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 09:22:44
Ruto ataka walinzi wa kibinafsi na polisi kushirikiana katika ujasusi
RAIS William Ruto ametangaza kuwa serikali itaanza kutumia taarifa za kijasusi zinazokusanywa na walinzi wa kampuni za kibinafsi ili kuimarisha vita dhidi ya uhalifu na kuimarisha usalama nchini. Akizungumza Alhamisi katika Ikulu ya Nairobi alipokutana na mamia ya walinzi hao, Rais alisema mchango wao katika kulinda mali na maisha ya Wakenya ni muhimu na unapaswa kuunganishwa na juhudi za idara za usalama za serikali. Aliagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Mamlaka ya Kudhibiti Kampuni za Kibinafsi za Ulinzi (PSRA) na Afisi ya Rais kuandaa mfumo wa ushirikiano kati ya polisi na walinzi hao. 'Mnafanya kazi muhimu ya kuhakikisha usalama. Pia mnakusanya taarifa nyingi kuhusu wahalifu. Ushirikiano huu utasaidia kuimarisha usalama nchini,' alisema Rais Ruto. Rais pia alisema sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo zitarekebishwa ili kutoa nafasi ya kupandishwa vyeo kwa wanaofanya kazi kwa ufanisi. Aidha, aliagiza taasisi za mafunzo ya walinda usalama kuoanisha mitaala yao ili kuwe na mfumo mmoja wa maendeleo ya taaluma. Kuhusu mishahara, Dkt Ruto alisisitiza kuwa agizo la serikali la kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kwa asilimia 15 bado linafaa kutekelezwa. Alionya kampuni zinazowalipa walinzi chini ya kiwango cha chini cha mshahara, akisema baadhi hulipa wafanyakazi wao kiasi cha Sh6,000 pekee kwa mwezi. Pia alizitaka kampuni zote kuhakikisha wafanyakazi wao wamejiandikisha kikamilifu katika Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA). Katika hotuba yake, Rais pia alitetea rekodi ya serikali yake na kusema wapinzani wake hawana ajenda ya maendeleo isipokuwa kampeni ya kutaka ahudumu muhula mmoja.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 06:47:36
Kisii yageukia mfumo mbadala kutatua mauaji yaletwayo na migogoro ya mashamba
KAUNTI ya Kisii imezindua rasmi Mfumo Mbadala wa Haki wa mazungumzo maarufu kama Alternative Justice System (AJS) katika juhudi za kukomesha mauaji yanayosababishwa na migogoro ya ardhi ambayo imegharimu maisha ya mamia ya watu katika miaka ya hivi karibuni. Jaji Mkuu Martha Koome Jumanne alizindua Kituo cha AJS eneo la Mashauri pamoja na Mahakama ya Manispaa mjini Kisii. Aliandamana na Gavana wa gatuzi hilo Simba Arati, majaji na maafisa wakuu kutoka kwa Idara ya Mahakama. Akizungumza na wazee, mawakili na wakazi wa Kisii, Koome alisema mahakama za kawaida zimelemewa na idadi kubwa ya kesi na haziwezi tena kumaliza migogoro ya ardhi inayochochea mauaji kwa haraka. "Hatuezi kuendelea kuzika wazazi na watoto wetu kwa sababu ya ardhi. Mahakama zimejaa, kesi zinachukua miaka, na familia zinavunjika kabla ya hukumu kutolewa. Ndiyo maana tunawasihi wakazi kuzungumza kwanza kunapotokea migogoro kama hiyo," Koome alisema. Takwimu za vyombo vya usalama zinaonyesha angalau watu saba huuawa kila mwezi Kisii kutokana na migogoro ya mashamba. Kati ya Januari 2021 na Mei 2022, watu zaidi ya 126 walipoteza maisha, kulingana na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kisii kwa wakati huo Francis Kooli. Mahakama ya Kisii pia inasema zaidi ya asilimia 80 ya kesi zilizoko mbele yake ni za mauaji yanayotokana na migogoro ya ardhi. Kituo hicho cha AJS kitatumia Baraza la Wazee waliothibitishwa pamoja na wapatanishi wa mahakama kutatua migogoro ya mipaka, ardhi na ugomvi wa kifamilia. Kesi zitachunguzwa ndani ya siku 14. Ikiwa pande zote zitakubaliana, makubaliano yatasajiliwa mahakamani na kuwa na nguvu za kisheria. Ikiwa mazungumzo yatafeli, kesi itarudi mahakamani. Takwimu kutoka kaunti zilizozindua mfumo huo mbadala zinaonyesha kuwa AJS inamaliza baadhi ya ugomvi ndani ya miezi mitatu ikilinganishwa na miaka mitatu mahakamani. Jaji Mkuu alimwomba Gavana Arati kuwasaidia kifedha wazee hao kwa kuwa watakuwa na jukumu kubwa katika kusikiza kesi. Pamoja na AJS, Koome pia alizindua Mahakama ya Manispaa itakayoshughulikia makosa madogo kama kama vile utupaji taka kiholela, kelele na ukiukaji wa sheria za trafiki. Gavana Arati alisema mahakama hiyo itarejesha nidhamu mjini Kisii. "Kwa muda mrefu mji wetu umeteseka na uchafu. Watu wanatupa taka ovyo. Sasa tutakuwa na mahali pa kuwafikisha watupaji hao wa kiholela mara moja," alisema. Arati alidokeza kuwa tayari amezindua timu ya vijana wa kusafisha na kusimamia sheria za mazingira mjini Kisii, ingawa wakazi wamelalamika kuwa timu hiyo "imekuwa ikiwanyasa". "Tukikukamata ukitupa takataka ovyo, hatutakupa onyo. Tutakupeleka mahakamani," alionya. Ugomvi wa ardhi Kisii ni dondasugu. Watoto hawasubiri hata wazazi wao kufa. Baba akiwa mgonjwa tu, ugomvi wa hati ya ardhi unaanza.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 02:55:54
Maafisa wa kaunti watumia mfumo wa malipo kupora mamilioni ya pesa za umma
KAUNTI nyingi nchini zimegeuza mfumo wa malipo ya dharura maarufu kuwa njia mpya ya kupora pesa za umma kupitia madai ya matumizi yasiyo na msingi, ripoti mpya za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) zinaonyesha. Mfumo huu wa malipo ulianzishwa mwaka wa 2013 baada ya ugatuzi kuanza, ukiwa na lengo la kurahisisha malipo ya haraka ya matumizi madogo yasiyopangwa ambayo hayawezi kuzidi Sh2 milioni. Lakini miaka kadhaa baadaye, mfumo huo umegeuzwa kuwa chanzo cha ufisadi huku maafisa wa kaunti wakidai fedha kwa shughuli ambazo hazikufanyika au kushindwa kuwasilisha hesabu za matumizi hayo. Ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, na EACC zinaonyesha kuwa matumizi mabaya ya mfumo huo sasa ni mojawapo ya mbinu mpya zinazotumiwa kupora mamilioni ya pesa za walipa ushuru. Ukaguzi wa miaka ya kifedha ya 2023/2024 na 2024/2025 umebaini kuwa kaunti huenda zilipoteza zaidi ya Sh500 milioni kupitia mfumo huo. Katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024 pekee, kaunti 12 zilishindwa kueleza matumizi ya zaidi ya Sh230 milioni zilizotolewa kwa malipo ya dharura. Ripoti hiyo inaonyesha baadhi ya maafisa walipewa pesa zaidi ya mara moja, kinyume cha sheria za usimamizi wa fedha za serikali za kaunti zinazowataka kurejesha au kuwasilisha hesabu za fedha hizo ndani ya siku saba baada ya kurejea kazini. Sheria hizo pia zinakataza afisa kupewa pesa upya kabla ya kuwasilisha hesabu ya ile ya awali au fedha hizo kukatwa kwenye mshahara wake. Kaunti ya Turkana ndiyo inaongoza kwa fedha ambazo hazijaelezwa matumizi yake ikiwa na Sh85 milioni. Samburu inafuata kwa Sh39.3 milioni, Mombasa Sh25.8 milioni, Bungoma Sh21.6 milioni, Tana River Sh19.8 milioni na Embu Sh12.8 milioni. Siaya na Nandi kila moja ina Sh6.3, Kisumu Sh5.1 milioni, Nyandarua Sh3 milioni, Busia Sh1.3 milioni huku Kiambu ikiwa na zaidi ya Sh801,000. Mkaguzi Mkuu alisema baadhi ya serikali za kaunti hazikuwa na sajili sahihi ya pesa chini ya mfumo huu kama inavyotakiwa na sheria. Kutokana na hali hiyo, imekuwa vigumu kufuatilia nani alipokea fedha hizo, kiasi alichopewa, tarehe ya kutolewa na iwapo fedha hizo zilirejeshwa au matumizi yake kuelezwa. Katika Kaunti ya Isiolo, ukaguzi ulibaini maafisa wawili walipewa jumla ya Sh8.4 milioni kabla ya kuwasilisha hesabu za fedha walizopewa awali. Aidha, kaunti hiyo ilitoa Sh4 milioni kupitia kwa shughuli ya upangaji wa ardhi Garbatulla na utoaji wa hati za ugavi wa ardhi, hatua ambayo wakaguzi wanasema haikufuata utaratibu unaostahili. Katika Kaunti ya Wajir, zaidi ya Sh149 milioni zilihamishwa kutoka akaunti za Benki Kuu ya Kenya hadi akaunti za benki ya kibiashara zilizokuwa zikitumika kwa mfumo huu na baadaye kutumiwa kwa malipo ya kawaida ya shughuli za kaunti. Kaunti ya Embu ilikuwa na zaidi ya Sh21.8 milioni ambazo hazikuelezwa matumizi yake kufikia Juni 30, 2025. Machakos ilikuwa na zaidi ya Sh3.6 milioni ambazo hazikuwa zimerejeshwa kwa wakati, huku Samburu ikiwa na zaidi ya Sh1.3 milioni ambazo zilikuwa zimechelewa kurejeshwa bila hatua zozote kuchukuliwa. Katika Kaunti ya Kakamega, kulikuwa na zaidi ya Sh18.3 milioni ambazo hazikuwa zimeelezwa, huku Nandi, Uasin Gishu na Siaya zikitajwa kwa kushindwa kuweka rekodi sahihi za utoaji na urejeshaji wa fedha hizo. Kwa upande wake, EACC ilisema imekuwa ikichunguza visa vingi ambapo mfumo huu umegeuzwa chanzo cha kujinufaisha na fedha za umma. Mwenyekiti wa EACC, Bw Abdi Mohamud, alisema baadhi ya maafisa wamekuwa wakichukua mfumo huu kana kwamba ni pesa zao binafsi. Ripoti hizo sasa zimeibua wasiwasi kuhusu udhaifu wa usimamizi wa fedha za umma katika kaunti na kuibua wito wa hatua kali dhidi ya maafisa wanaotumia mianya hiyo kujinufaisha kwa gharama ya walipa ushuru.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 01:55:47
Wakazi waanza kuvuna shughuli zikiongezeka bandarini Lamu, Dangote akikaribia kuja
WAKAZI wa Kaunti ya Lamu wana sababu ya kutabasamu huku Bandari ya Lamu ikiendelea kuvutia meli nyingi zaidi, hali inayotarajiwa kuleta nafasi za ajira na kukuza biashara katika eneo hilo. Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) imesema bandari hiyo imepokea meli 167 tangu Januari mwaka huu na idadi hiyo inatarajiwa kufikia karibu meli 200 kufikia Septemba. Mwaka jana, bandari hiyo ilikuwa imehudumia chini ya meli 50 katika kipindi kama hicho. Ongezeko hilo limechangiwa na mabadiliko ya njia za usafirishaji wa baharini kufuatia mvutano wa Mashariki ya Kati, ambapo baadhi ya kampuni za usafirishaji zimehamishia shughuli zao Lamu. [caption id="attachment_190868" align="alignnone" width="2000"] Wafanyakazi wakiendelea na shughuli za ujenzi katika bandari ya Lamu katika picha hii ya Agosti 27, 2019. Picha|Maktaba[/caption] Kwa wakazi wa Lamu, ongezeko la shughuli bandarini linamaanisha ajira zaidi kwa madereva, wapakiaji, mawakala wa forodha, wafanyabiashara wa chakulana wamiliki wa nyumba za kupanga na watoa huduma mbalimbali. Meneja Mkuu wa Bandari ya Lamu Abdulaziz Mzee, alisema mwaka 2026 unaonekana kuwa bora zaidi tangu bandari hiyo izinduliwe mwaka wa 2021. "Tunaendelea kushuhudia ongezeko la meli zinazoingia bandarini. Pia tunawekeza katika korongo mpya za kupakia na kupakua mizigo pamoja na vifaa vingine ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka," alisema. Aidha, maelfu ya magari yaliyogeuzwa kutoka Bandari ya Dubai kuelekea Lamu yameongeza shughuli za usafirishaji na kuhifadhi mizigo, hatua iliyowanufaisha wafanyabiashara wa eneo hilo. Wataalamu wa uchukuzi wa baharini wanasema ikiwa Serikali itaharakisha ujenzi wa barabara na miundombinu ya mradi wa LAPSSET, Bandari ya Lamu itakuwa kitovu kikuu cha biashara Afrika Mashariki na kufungua fursa zaidi za ajira na maendeleo kwa wakazi wa eneo hilo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 06 Aug 2026 00:55:09
Mateso hospitalini wauguzi wakikaa ngumu mgomoni
HUDUMA za afya nchini zimeendelea kutatizika huku mgomo wa wauguzi ukiingia siku ya sita, hali iliyosababisha wagonjwa wengi, hasa wajawazito na watoto wachanga, kukosa huduma muhimu katika hospitali za umma. Chama cha Madaktari wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake nchini (KOGS) kimetoa wito kwa serikali kutatua mgogoro huo haraka, kikionya kuwa kucheleweshwa kwa suluhu kunaongeza hatari ya vifo vinavyoweza kuzuiliwa kwa akina mama na watoto wachanga. Rais wa chama hicho, Dkt Kireki Omanwa, amesema huduma za uzazi zimeathirika pakubwa huku wodi za wazazi na watoto wachanga zikifurika kutokana na wagonjwa kuhamishwa kutoka hospitali ambazo hazifanyi kazi. Alionya kuwa mgomo huo unaweza kudhoofisha juhudi za serikali kufanikisha mpango unaolenga kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga kufikia mwaka 2028. Hata hivyo, hali imeanza kubadilika katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) baada ya wauguzi kurejea kazini kufuatia makubaliano kati ya uongozi wa hospitali hiyo na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC). Makubaliano hayo yaliongeza marupurupu ya sare kutoka Sh15,000 hadi Sh25,000 kwa mwaka, ya huduma za uuguzi kutoka Sh20,000 hadi Sh30,000, pamoja na kuboresha yale ya likizo kulingana na daraja la kazi. Licha ya muafaka huo, wauguzi katika hospitali nyingi za kaunti bado hawajarejea kazini. Katibu Mkuu Msaidizi wa Muungano wa Wauguzi Kenya (KNUN), Lucy Mburu, amesema mazungumzo kati ya viongozi wa chama hicho, Baraza la Magavana na maafisa wa wizara za Afya na Kazi yalikuwa yakiendelea lakini hayakuwa yamezaa matunda. Katika Kaunti ya Isiolo, hali imezidi kuwa mbaya kwani hata madaktari wamekuwa mgomoni kwa siku 66. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari (KMPDU), Dkt Dennis Miskellah, alisema madaktari walikosa mishahara kwa miezi mitatu, huku makato ya kodi, SHA na mikopo yakikosa kuwasilishwa kwa taasisi husika. Kaunti za Homa Bay na Siaya pia zinakabiliwa na tishio la migomo ya madaktari kutokana na migogoro ya ajira na bima ya afya. Katika kaunti ya Homa Bay, viongozi wa wauguzi wamemtaka Gavana Gladys Wanga kutumia nafasi yake kama mwenyekiti wa Kamati ya Wafanyakazi ya Baraza la Magavana kushinikiza suluhu ya mgogoro huo. Katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii, wagonjwa wengi wameelekea hospitali za kibinafsi baada ya huduma nyingi kukwama. Hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) mjini Kisumu nayo imeelemewa baada ya kupokea wagonjwa wengi kutoka kaunti jirani. Mkurugenzi wa huduma za uuguzi Teresa Okiri alisema hospitali hiyo sasa inapokea wastani wa wagonjwa 50 mahututi kila siku, huku wodi za wazazi, watoto wachanga na dharura zikifurika. Katika Hospitali ya Rufaa ya Kitui, mamia ya wagonjwa walionekana wakisubiri huduma bila mafanikio. "Tunaomba serikali isikilize malalamishi ya wahudumu wa afya ili huduma zirudi kawaida," alisema Mary Mutua, mmoja wa wagonjwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 23:55:05
Wanasiasa mashakani mali ikipigwa mnada kwa kulemewa na madeni
WANASIASA wengi nchini huchora taswira ya watu wasioweza kutikiswa kutokana na mamlaka wanayoshikilia, misafara ya magari, walinzi na bajeti kubwa wanazosimamia. Lakini hali hubadilika. Matatizo ya kifedha sasa yameanza kuwakumba baadhi ya viongozi wakuu huku benki zikielekeza madalali kuuza mali yao ili kufidia madeni. Aliyekuwa Gavana wa Murang'a na sasa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Mwangi wa Iria, ndiye mwathiriwa wa hivi punde. Shirika la Dalali Traders Auctioneers limetangaza kuwa mnamo Agosti 25 litauza nyumba yake ya Karen pamoja na Hospitali ya Edinburgh Mountain na Chuo cha Edinburgh vilivyoko Murang'a kutokana na deni ambalo halijafichuliwa. Aliyekuwa Waziri Raphael Tuju ndiye mwanasiasa aliyepoteza mali nyingi zaidi mwaka huu. Mnamo Machi, alipoteza Dari Business Park iliyoko Karen baada ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) kuiuza kufidia mkopo wa dola milioni 9.3 (zaidi ya Sh1.2 bilioni) aliouchukua 2015. Deni hilo sasa limeongezeka hadi Sh4.5 bilioni. Wiki hii, kampuni ya Garam Investments ilitangaza pia mnada wa Entim Sidai Wellness Sanctuary, mali nyingine ya kifahari ya Tuju iliyoko Karen. Mfanyabiashara Mary Wambui Mungai, ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi ya Athi Water Works Development Agency, alipoteza hoteli yake ya Glee mwezi uliopita. Aliyekuwa Waziri Moses Kuria alinusurika kwa muda baada ya mkewe Joyce Njambi kupinga mpango wa Benki ya Equity kuuza majengo yao ya vyumba vya kupangisha yaliyoko Ruaka na Juja kufidia mkopo wa Sh54 milioni. Mkewe alidai mali hiyo ni ya ndoa na haikupaswa kutumika kama dhamana bila idhini yake. Kesi bado inaendelea mahakamani. Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu pia amekuwa akipambana na wakopeshaji.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 22:55:05
Hivi ndivyo msanii wa Bongo Matonya aliponyoka kesi ya ubakaji na mwanamke Mkenya
MSANII wa Bongo Flava kutoka Tanzania, Sefu Ramadan almaarufu Matonya, aliponyoka kesi ya ubakaji iliyokuwa ikimuandama kufuatia ombi lililotolewa na mamake kwa mwanamke aliyekuwa amemshtaki. Jambo hilo lilifanya Mahakama ya Shanzu, Mombasa kumuondolea kesi hiyo. Imebainika kuwa mamake Matonya alimtafuta mfanyabiashara huyo wa Kenya na kumsihi amsamehe mwanawe. Mwanamke huyo baadaye aliambia mahakama kuwa aliamua kuondoa kesi hiyo baada ya ombi la mama huyo pamoja na msongo wa mawazo alioupata kutokana na mchakato mzima wa kesi. "Nimeamua kumsamehe mtuhumiwa kwa sababu kesi imeniletea msongo wa mawazo. Mamake mshukiwa ambaye ni mgonjwa alinifikia na kuniomba nimsamehe mwanawe," alisema mwanamke huyo katika Mahakama ya Shanzu. Stakabadhi za Mahakama zinaonyesha kuwa ombi hilo halikupingwa na upande wa mashtaka ambao uliiambia mahakama kuwa ulikuwa na maagizo ya kuondoa kesi hiyo. "Kwa kuwa ombi la kuondoa mashtaka limeungwa mkono na upande wa mashtaka, kesi hii imeondolewa. Mtuhumiwa yuko huru," iliamua mahakama, na kuamuru pia pasipoti ya Matonya irejeshwe, ilani iliyowekwa iondolewe na mdhamini wake kuachiliwa. Kwa upande wake, Matonya, alitoa shukrani tu. "Nashukuru. Naomba pasipoti yangu irejeshwe," alisemaKatika kiapo chake, mlalamishi huyo alisisitiza kuwa uamuzi wake ulikuwa wa hiari bila kulazimishwa, kutishwa, kushawishiwa au kuahidiwa chochote. "Ni uamuzi wangu binafsi kufuta kesi na najua nikishaifuta siwezi kuirudisha tena," alisema. Alieleza mahakama kuwa amepatana na mtuhumiwa na kuchagua kumsamehe. Pia alitaja majukumu ya safari za mara kwa mara ambayo yangemzuia kuendelea kufika mahakamani. Mwanamke huyo aliongeza kuwa kesi hiyo imemsababishia msongo wa mawazo, kuathiri maisha yake binafsi na mahusiano ya kijamii, na kumweka katika hali ya aibu na unyanyapaa wa kijamii. "Kwa kuzingatia yote haya, sitaki tena kushiriki katika kesi hii. Ningependa kuendelea na maisha yangu na kuzingatia mambo yangu binafsi na majukumu ya baadaye," alisema. Aliongeza kuwa uamuzi wake ulitokana na maridhiano na mtuhumiwa, majukumu ya safari na athari za kihisia na kijamii za kesi, akisisitiza kuwa hakukuwa na masharti yoyote na ulikuwa ni tendo la msamaha pekee. Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa Matonya alikana mashtaka Aprili 9, na kesi ikapangwa kusikizwa. Jaribio la kwanza la kuondoa kesi lilifanyika Juni 11, lakini mahakama ilimtaka mlalamishi kuwasilisha kiapo cha kina kwa kuwa kesi ilihusisha tuhuma za ubakaji na ilikuwa ya maslahi ya umma. Baada ya kiapo kuwasilishwa, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ilipeleka faili kwa maafisa wa ngazi ya juu kwa idhini. Julai 1, upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa umepata idhini na ukaomba rasmi kuondoa mashtaka. Mlalamishi aliapishwa, akathibitisha yaliyomo kwenye kiapo chake na kurudia sababu zake kabla ya mahakama kuruhusu ombi hilo, na hivyo kumaliza rasmi kesi ya jinai dhidi ya mwanamuziki huyo wa Tanzania. Aprili 9, Matonya alishtakiwa kwa kosa la ubakaji na alikana mashtaka mawili ya unyanyasaji wa kijinsia. Msanii huyo alishtakiwa kwa kosa kinyume na Kifungu cha 3(1)(a) kinachosomwa pamoja na Kifungu cha 3(3) cha Sheria ya Makosa ya Kingono. Upande wa mashtaka ulidai kuwa Aprili 7, 2026, katika nyumba ya kifahari eneo la Nyali, Mombasa, mtuhumiwa alimbaka mlalamishi J.G. kwa kutumia nguvu. Alikabiliwa pia na shtaka mbadala la kutenda kitendo kisicho cha heshima kwa mtu mzima, ambapo mahakama iliambiwa kuwa mtuhumiwa alimgusa sehemu za siri za mwanamke huyo bila ridhaa yake.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 21:55:55
Hamtaingia DCP kienyeji, asema Gachagua akiunda kamati ya kupekua wanaohama serikali
CHAMA cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Rigathi Gachagua kimeunda kamati maalumu ya watu saba kuchuja viongozi wanaotaka kuhama kutoka chama cha United Democratic Alliance (UDA) kabla ya kupokelewa rasmi. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kutokea mvutano mkali kati ya Bw Gachagua na baadhi ya washirika wake waliochaguliwa kuhusu iwapo wahamiaji kutoka UDA wanapaswa kupokelewa bila masharti. Kamati hiyo itaongozwa na Kaimu Katibu Mkuu wa DCP, Seneta wa Nyandarua John Methu. Wanachama wengine ni Seneta wa Murang'a Joe Nyutu, Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang'wa, Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Njeri Maina, Mbunge wa Naivasha Jayne Kihara, Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiru. Bw Methu alisema uamuzi wa kuunda kamati hiyo ulifikiwa baada ya vikao 19 vya mashauriano vilivyoanza Juni 16, 2026, katika makazi ya Bw Gachagua, Wamunyoro, na baadaye kuendelea katika Hoteli ya Outspan, Nyeri. Alisema DCP imepokea maombi 816 kutoka kwa viongozi wanaotaka kuhama kutoka upande wa serikali. Kwa mujibu wake, miongoni mwao ni mawaziri watano, makatibu wanane wa wizara, wabunge 83, maseneta watano, magavana wanne pamoja na madiwani na maafisa wa mashirika ya serikali. Bw Methu alisema kila anayetaka kujiunga na DCP atalazimika kutangaza hadharani kuwa hatagombea uchaguzi wa 2027 kupitia chama chochote kinachomuunga mkono Rais William Ruto. Aidha, alisema hakuna mwanasiasa atakayeruhusiwa kumfikia moja kwa moja Bw Gachagua ili kuomba kujiunga na chama. Alidai baadhi ya wanaotaka kuhamia DCP wamekuwa wakipiga picha na Bw Gachagua kisha kusambaza taarifa kuwa walitoa hongo ili wapate tiketi za moja kwa moja katika uchaguzi mkuu ujao. Pia aliwashutumu baadhi yao kwa kurekodi kwa siri mazungumzo yao na kiongozi huyo na kuyapeleka kwa serikali. Bw Methu alisema wafuasi wengi wa DCP bado hawajawasamehe viongozi waliomuunga mkono Rais Ruto kumng'oa Bw Gachagua kutoka wadhifa wa Naibu Rais mnamo 2024. Kwa upande wake, Mbunge wa Ol Kalou Kamau Ngotho alisema Bw Gachagua amewaambia viongozi wa chama kuwa amewasamehe wote waliopiga kura ya kumuondoa madarakani. Alisema hatua hiyo ilitokana na ushauri wa viongozi wa kidini na wazee waliomtaka aunganishe viongozi badala ya kuendeleza tofauti za kisiasa. Hata hivyo, Mbunge wa Mwea Mary Maingi alikosoa hatua ya kuchuja wanaotaka kuhamia DCP, akisema hakuna mwanasiasa anayepaswa kuamua hatima ya wengine kisiasa. Naye Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri alisema viongozi hawapaswi kulazimishwa kujiunga na chama kimoja kwa kuwa wananchi ndio huamua watakaochagua. Mbunge wa Naivasha Jayne Kihara alisema suala hilo limegawanya chama kwa sababu baadhi ya wanachama wanaamini waliowatesa kisiasa hawawezi kupokelewa bila kuchunguzwa. Aliongeza kuwa viongozi wanaohusishwa na makundi ya wahuni waliovuruga mikutano ya DCP au waliohusishwa na vurugu za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou hawatapokelewa kirahisi. Kwa upande wake, Seneta Karungo wa Thang'wa alisema mchakato wa uchunguzi ni muhimu ili kuzuia wanaoweza kuhujumu chama kutoka ndani. Naye Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Njeri Maina alisema kamati hiyo haitakuwa ya kujinufaisha kwani wanachama hawatalipwa posho yoyote. Alisema kazi yake ni kusikiliza maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo ya iwapo mwombaji anafaa kupokelewa au la, bila kutoza ada wala kutoa adhabu yoyote.
read moreRight Column Content