taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 12 Jul 2026 02:55:17
Kinaya serikali ikigeuka adui wa kutunza misitu
SERIKALI inaendelea kusukuma mpango wake wa kupanda miti bilioni 15 ifikapo 2032 kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kurejesha mazingira yaliyoharibiwa. Hata hivyo, wanaharakati wa mazingira wanaonya kuwa mafanikio ya mpango huo yanaweza kutatizwa na ongezeko la miradi ya maendeleo inayopendekezwa ndani ya misitu asili. Kwa mujibu wa wanamazingira, hali ya sasa inaibua kinaya. Wanasema huku serikali ikihamasisha wananchi kupanda mabilioni ya miche ya miti, sehemu nyingine za misitu inaendelea kukatwa ili kupisha ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege, nyumba za serikali na miradi mingine ya miundombinu. Rais William Ruto, ambaye kabla ya kuingia katika siasa alisomea Botania, Zoolojia na Ikolojia ya Mimea katika Chuo Kikuu cha Nairobi, amefanya uhifadhi wa mazingira kuwa mojawapo ya nguzo kuu za utawala wake. Serikali yake imeweka lengo la kupanda miti bilioni 15 ndani ya miaka kumi ili kuongeza kiwango cha misitu nchini na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, tangu alipoingia madarakani mwaka 2022, serikali imelaumiwa kwa kuruhusu miradi mbalimbali inayopangwa ndani ya misitu. Hali hiyo imezua maswali kuhusu iwapo juhudi za kurejesha mazingira zinaenda sambamba na kulinda misitu ya asili ambayo imekuwepo kwa miongo mingi. Takwimu za ripoti ya hali ya uchumi zinaonyesha kuwa eneo la mashamba ya miti ya serikali liliongezeka kutoka hekari 143,900 mwaka 2021 hadi hekari 148,600 mwaka 2025. Pia kasi ya upanzi wa miti iliongezeka baada ya kuzinduliwa kwa mpango wa kitaifa, huku maelfu ya hekari zikipandwa miche mipya kila mwaka. Lakini wakati huo huo, ukataji wa miti katika mashamba ya serikali ulirejelewa baada ya kuondolewa kwa marufuku ya miaka sita, ingawa baadaye mahakama ilisimamisha uamuzi huo. Kwa wanaharakati wa mazingira, changamoto kubwa si uvunaji wa miti pekee bali kutumiwa kwa misitu asili kwa miradi ya maendeleo. Wanasema kila barabara, njia ya umeme au jengo linalojengwa ndani ya msitu hupunguza uwezo wa mfumo wa ikolojia kuendelea kufanya kazi ipasavyo. Wasiwasi huo uliongezeka baada ya Bunge kupitisha Sheria ya Marekebisho ya Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu ya mwaka 2025, ambayo inaruhusu Huduma ya Misitu Kenya (KFS) kutoa nafasi kwa ujenzi wa barabara, njia za umeme na miundombinu mingine ndani ya misitu ya umma. Mojawapo ya miradi iliyozua mjadala mkubwa ni barabara ya Ihithe-Ndunyu Njeru inayopangwa kupita ndani ya Msitu wa Aberdare. Ripoti za tathmini ya mazingira zinaonyesha kuwa ujenzi huo utahitaji kukatwa kwa sehemu ya msitu wa mianzi, msitu wa milimani na maeneo ya nyasi. Wanaharakati wanaonya kuwa Aberdare ni mojawapo ya vyanzo muhimu vya maji nchini, ikihudumia mabwawa ya Sasumua na Ndakaini pamoja na kuchangia uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji. Kwa sababu hiyo, Mahakama ya Mazingira ilisimamisha mradi huo kwa muda huku kesi ikiendelea kusikilizwa. Katika Jiji la Nairobi, hofu kama hiyo imejitokeza kuhusu Msitu wa Ngong Road, ambapo sehemu ya ardhi imetengwa kwa miradi inayohusiana na Uwanja wa Talanta. Wanaharakati wanasema ujenzi wa barabara ya kuingia, eneo la wakandarasi na miundombinu mingine unaweza kuendelea kugawa msitu huo katika vipande vidogo. Kadhalika, katika Msitu wa Karura, ukataji wa baadhi ya miti mapema mwaka huu uliibua maswali kutoka kwa wanaharakati. Serikali ilieleza kuwa eneo hilo linatayarishwa kwa vitalu vya miche ya miti na makazi ya muda ya vijana wa Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS) wanaoshiriki katika mpango wa kupanda miti. Katibu wa Maendeleo ya Misitu, George Tarus, amesisitiza kuwa serikali haina mpango wa kuharibu misitu asili. Alisema tayari miti takriban1.9 bilioni imepandwa chini ya mpango wa kitaifa na kwamba miradi yote inayopendekezwa ndani ya misitu lazima ifanyiwe tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuidhinishwa. Kwa mujibu wake, lengo ni kurejesha mazingira yaliyoharibiwa katika misitu, maeneo ya malisho, mashamba na sehemu za kijani mijini, huku maendeleo muhimu yakiendelea kwa kuzingatia sheria za mazingira. Hata hivyo, wanaharakati wanasisitiza kuwa mafanikio ya mpango wa kupanda miti hayatapimwa kwa idadi ya miche iliyopandwa pekee. Wanasema kipimo kikubwa kitakuwa uwezo wa Kenya kulinda misitu yake ya kale na mifumo yake ya ikolojia dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na miradi ya maendeleo, ili juhudi za kurejesha mazingira zisiwe zinafutwa na uharibifu unaoendelea katika misitu asili.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 2 hours ago
Ruto ataka walinzi wa kibinafsi na polisi kushirikiana katika ujasusi
RAIS William Ruto ametangaza kuwa serikali itaanza kutumia taarifa za kijasusi zinazokusanywa na walinzi wa kampuni za kibinafsi ili kuimarisha vita dhidi ya uhalifu na kuimarisha usalama nchini. Akizungumza Alhamisi katika Ikulu ya Nairobi alipokutana na mamia ya walinzi hao, Rais alisema mchango wao katika kulinda mali na maisha ya Wakenya ni muhimu na unapaswa kuunganishwa na juhudi za idara za usalama za serikali. Aliagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Mamlaka ya Kudhibiti Kampuni za Kibinafsi za Ulinzi (PSRA) na Afisi ya Rais kuandaa mfumo wa ushirikiano kati ya polisi na walinzi hao. 'Mnafanya kazi muhimu ya kuhakikisha usalama. Pia mnakusanya taarifa nyingi kuhusu wahalifu. Ushirikiano huu utasaidia kuimarisha usalama nchini,' alisema Rais Ruto. Rais pia alisema sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo zitarekebishwa ili kutoa nafasi ya kupandishwa vyeo kwa wanaofanya kazi kwa ufanisi. Aidha, aliagiza taasisi za mafunzo ya walinda usalama kuoanisha mitaala yao ili kuwe na mfumo mmoja wa maendeleo ya taaluma. Kuhusu mishahara, Dkt Ruto alisisitiza kuwa agizo la serikali la kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kwa asilimia 15 bado linafaa kutekelezwa. Alionya kampuni zinazowalipa walinzi chini ya kiwango cha chini cha mshahara, akisema baadhi hulipa wafanyakazi wao kiasi cha Sh6,000 pekee kwa mwezi. Pia alizitaka kampuni zote kuhakikisha wafanyakazi wao wamejiandikisha kikamilifu katika Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA). Katika hotuba yake, Rais pia alitetea rekodi ya serikali yake na kusema wapinzani wake hawana ajenda ya maendeleo isipokuwa kampeni ya kutaka ahudumu muhula mmoja.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
Kisii yageukia mfumo mbadala kutatua mauaji yaletwayo na migogoro ya mashamba
KAUNTI ya Kisii imezindua rasmi Mfumo Mbadala wa Haki wa mazungumzo maarufu kama Alternative Justice System (AJS) katika juhudi za kukomesha mauaji yanayosababishwa na migogoro ya ardhi ambayo imegharimu maisha ya mamia ya watu katika miaka ya hivi karibuni. Jaji Mkuu Martha Koome Jumanne alizindua Kituo cha AJS eneo la Mashauri pamoja na Mahakama ya Manispaa mjini Kisii. Aliandamana na Gavana wa gatuzi hilo Simba Arati, majaji na maafisa wakuu kutoka kwa Idara ya Mahakama. Akizungumza na wazee, mawakili na wakazi wa Kisii, Koome alisema mahakama za kawaida zimelemewa na idadi kubwa ya kesi na haziwezi tena kumaliza migogoro ya ardhi inayochochea mauaji kwa haraka. "Hatuezi kuendelea kuzika wazazi na watoto wetu kwa sababu ya ardhi. Mahakama zimejaa, kesi zinachukua miaka, na familia zinavunjika kabla ya hukumu kutolewa. Ndiyo maana tunawasihi wakazi kuzungumza kwanza kunapotokea migogoro kama hiyo," Koome alisema. Takwimu za vyombo vya usalama zinaonyesha angalau watu saba huuawa kila mwezi Kisii kutokana na migogoro ya mashamba. Kati ya Januari 2021 na Mei 2022, watu zaidi ya 126 walipoteza maisha, kulingana na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kisii kwa wakati huo Francis Kooli. Mahakama ya Kisii pia inasema zaidi ya asilimia 80 ya kesi zilizoko mbele yake ni za mauaji yanayotokana na migogoro ya ardhi. Kituo hicho cha AJS kitatumia Baraza la Wazee waliothibitishwa pamoja na wapatanishi wa mahakama kutatua migogoro ya mipaka, ardhi na ugomvi wa kifamilia. Kesi zitachunguzwa ndani ya siku 14. Ikiwa pande zote zitakubaliana, makubaliano yatasajiliwa mahakamani na kuwa na nguvu za kisheria. Ikiwa mazungumzo yatafeli, kesi itarudi mahakamani. Takwimu kutoka kaunti zilizozindua mfumo huo mbadala zinaonyesha kuwa AJS inamaliza baadhi ya ugomvi ndani ya miezi mitatu ikilinganishwa na miaka mitatu mahakamani. Jaji Mkuu alimwomba Gavana Arati kuwasaidia kifedha wazee hao kwa kuwa watakuwa na jukumu kubwa katika kusikiza kesi. Pamoja na AJS, Koome pia alizindua Mahakama ya Manispaa itakayoshughulikia makosa madogo kama kama vile utupaji taka kiholela, kelele na ukiukaji wa sheria za trafiki. Gavana Arati alisema mahakama hiyo itarejesha nidhamu mjini Kisii. "Kwa muda mrefu mji wetu umeteseka na uchafu. Watu wanatupa taka ovyo. Sasa tutakuwa na mahali pa kuwafikisha watupaji hao wa kiholela mara moja," alisema. Arati alidokeza kuwa tayari amezindua timu ya vijana wa kusafisha na kusimamia sheria za mazingira mjini Kisii, ingawa wakazi wamelalamika kuwa timu hiyo "imekuwa ikiwanyasa". "Tukikukamata ukitupa takataka ovyo, hatutakupa onyo. Tutakupeleka mahakamani," alionya. Ugomvi wa ardhi Kisii ni dondasugu. Watoto hawasubiri hata wazazi wao kufa. Baba akiwa mgonjwa tu, ugomvi wa hati ya ardhi unaanza.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Maafisa wa kaunti watumia mfumo wa malipo kupora mamilioni ya pesa za umma
KAUNTI nyingi nchini zimegeuza mfumo wa malipo ya dharura maarufu kuwa njia mpya ya kupora pesa za umma kupitia madai ya matumizi yasiyo na msingi, ripoti mpya za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) zinaonyesha. Mfumo huu wa malipo ulianzishwa mwaka wa 2013 baada ya ugatuzi kuanza, ukiwa na lengo la kurahisisha malipo ya haraka ya matumizi madogo yasiyopangwa ambayo hayawezi kuzidi Sh2 milioni. Lakini miaka kadhaa baadaye, mfumo huo umegeuzwa kuwa chanzo cha ufisadi huku maafisa wa kaunti wakidai fedha kwa shughuli ambazo hazikufanyika au kushindwa kuwasilisha hesabu za matumizi hayo. Ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, na EACC zinaonyesha kuwa matumizi mabaya ya mfumo huo sasa ni mojawapo ya mbinu mpya zinazotumiwa kupora mamilioni ya pesa za walipa ushuru. Ukaguzi wa miaka ya kifedha ya 2023/2024 na 2024/2025 umebaini kuwa kaunti huenda zilipoteza zaidi ya Sh500 milioni kupitia mfumo huo. Katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024 pekee, kaunti 12 zilishindwa kueleza matumizi ya zaidi ya Sh230 milioni zilizotolewa kwa malipo ya dharura. Ripoti hiyo inaonyesha baadhi ya maafisa walipewa pesa zaidi ya mara moja, kinyume cha sheria za usimamizi wa fedha za serikali za kaunti zinazowataka kurejesha au kuwasilisha hesabu za fedha hizo ndani ya siku saba baada ya kurejea kazini. Sheria hizo pia zinakataza afisa kupewa pesa upya kabla ya kuwasilisha hesabu ya ile ya awali au fedha hizo kukatwa kwenye mshahara wake. Kaunti ya Turkana ndiyo inaongoza kwa fedha ambazo hazijaelezwa matumizi yake ikiwa na Sh85 milioni. Samburu inafuata kwa Sh39.3 milioni, Mombasa Sh25.8 milioni, Bungoma Sh21.6 milioni, Tana River Sh19.8 milioni na Embu Sh12.8 milioni. Siaya na Nandi kila moja ina Sh6.3, Kisumu Sh5.1 milioni, Nyandarua Sh3 milioni, Busia Sh1.3 milioni huku Kiambu ikiwa na zaidi ya Sh801,000. Mkaguzi Mkuu alisema baadhi ya serikali za kaunti hazikuwa na sajili sahihi ya pesa chini ya mfumo huu kama inavyotakiwa na sheria. Kutokana na hali hiyo, imekuwa vigumu kufuatilia nani alipokea fedha hizo, kiasi alichopewa, tarehe ya kutolewa na iwapo fedha hizo zilirejeshwa au matumizi yake kuelezwa. Katika Kaunti ya Isiolo, ukaguzi ulibaini maafisa wawili walipewa jumla ya Sh8.4 milioni kabla ya kuwasilisha hesabu za fedha walizopewa awali. Aidha, kaunti hiyo ilitoa Sh4 milioni kupitia kwa shughuli ya upangaji wa ardhi Garbatulla na utoaji wa hati za ugavi wa ardhi, hatua ambayo wakaguzi wanasema haikufuata utaratibu unaostahili. Katika Kaunti ya Wajir, zaidi ya Sh149 milioni zilihamishwa kutoka akaunti za Benki Kuu ya Kenya hadi akaunti za benki ya kibiashara zilizokuwa zikitumika kwa mfumo huu na baadaye kutumiwa kwa malipo ya kawaida ya shughuli za kaunti. Kaunti ya Embu ilikuwa na zaidi ya Sh21.8 milioni ambazo hazikuelezwa matumizi yake kufikia Juni 30, 2025. Machakos ilikuwa na zaidi ya Sh3.6 milioni ambazo hazikuwa zimerejeshwa kwa wakati, huku Samburu ikiwa na zaidi ya Sh1.3 milioni ambazo zilikuwa zimechelewa kurejeshwa bila hatua zozote kuchukuliwa. Katika Kaunti ya Kakamega, kulikuwa na zaidi ya Sh18.3 milioni ambazo hazikuwa zimeelezwa, huku Nandi, Uasin Gishu na Siaya zikitajwa kwa kushindwa kuweka rekodi sahihi za utoaji na urejeshaji wa fedha hizo. Kwa upande wake, EACC ilisema imekuwa ikichunguza visa vingi ambapo mfumo huu umegeuzwa chanzo cha kujinufaisha na fedha za umma. Mwenyekiti wa EACC, Bw Abdi Mohamud, alisema baadhi ya maafisa wamekuwa wakichukua mfumo huu kana kwamba ni pesa zao binafsi. Ripoti hizo sasa zimeibua wasiwasi kuhusu udhaifu wa usimamizi wa fedha za umma katika kaunti na kuibua wito wa hatua kali dhidi ya maafisa wanaotumia mianya hiyo kujinufaisha kwa gharama ya walipa ushuru.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Wakazi waanza kuvuna shughuli zikiongezeka bandarini Lamu, Dangote akikaribia kuja
WAKAZI wa Kaunti ya Lamu wana sababu ya kutabasamu huku Bandari ya Lamu ikiendelea kuvutia meli nyingi zaidi, hali inayotarajiwa kuleta nafasi za ajira na kukuza biashara katika eneo hilo. Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) imesema bandari hiyo imepokea meli 167 tangu Januari mwaka huu na idadi hiyo inatarajiwa kufikia karibu meli 200 kufikia Septemba. Mwaka jana, bandari hiyo ilikuwa imehudumia chini ya meli 50 katika kipindi kama hicho. Ongezeko hilo limechangiwa na mabadiliko ya njia za usafirishaji wa baharini kufuatia mvutano wa Mashariki ya Kati, ambapo baadhi ya kampuni za usafirishaji zimehamishia shughuli zao Lamu. [caption id="attachment_190868" align="alignnone" width="2000"] Wafanyakazi wakiendelea na shughuli za ujenzi katika bandari ya Lamu katika picha hii ya Agosti 27, 2019. Picha|Maktaba[/caption] Kwa wakazi wa Lamu, ongezeko la shughuli bandarini linamaanisha ajira zaidi kwa madereva, wapakiaji, mawakala wa forodha, wafanyabiashara wa chakulana wamiliki wa nyumba za kupanga na watoa huduma mbalimbali. Meneja Mkuu wa Bandari ya Lamu Abdulaziz Mzee, alisema mwaka 2026 unaonekana kuwa bora zaidi tangu bandari hiyo izinduliwe mwaka wa 2021. "Tunaendelea kushuhudia ongezeko la meli zinazoingia bandarini. Pia tunawekeza katika korongo mpya za kupakia na kupakua mizigo pamoja na vifaa vingine ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka," alisema. Aidha, maelfu ya magari yaliyogeuzwa kutoka Bandari ya Dubai kuelekea Lamu yameongeza shughuli za usafirishaji na kuhifadhi mizigo, hatua iliyowanufaisha wafanyabiashara wa eneo hilo. Wataalamu wa uchukuzi wa baharini wanasema ikiwa Serikali itaharakisha ujenzi wa barabara na miundombinu ya mradi wa LAPSSET, Bandari ya Lamu itakuwa kitovu kikuu cha biashara Afrika Mashariki na kufungua fursa zaidi za ajira na maendeleo kwa wakazi wa eneo hilo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Mateso hospitalini wauguzi wakikaa ngumu mgomoni
HUDUMA za afya nchini zimeendelea kutatizika huku mgomo wa wauguzi ukiingia siku ya sita, hali iliyosababisha wagonjwa wengi, hasa wajawazito na watoto wachanga, kukosa huduma muhimu katika hospitali za umma. Chama cha Madaktari wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake nchini (KOGS) kimetoa wito kwa serikali kutatua mgogoro huo haraka, kikionya kuwa kucheleweshwa kwa suluhu kunaongeza hatari ya vifo vinavyoweza kuzuiliwa kwa akina mama na watoto wachanga. Rais wa chama hicho, Dkt Kireki Omanwa, amesema huduma za uzazi zimeathirika pakubwa huku wodi za wazazi na watoto wachanga zikifurika kutokana na wagonjwa kuhamishwa kutoka hospitali ambazo hazifanyi kazi. Alionya kuwa mgomo huo unaweza kudhoofisha juhudi za serikali kufanikisha mpango unaolenga kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga kufikia mwaka 2028. Hata hivyo, hali imeanza kubadilika katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) baada ya wauguzi kurejea kazini kufuatia makubaliano kati ya uongozi wa hospitali hiyo na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC). Makubaliano hayo yaliongeza marupurupu ya sare kutoka Sh15,000 hadi Sh25,000 kwa mwaka, ya huduma za uuguzi kutoka Sh20,000 hadi Sh30,000, pamoja na kuboresha yale ya likizo kulingana na daraja la kazi. Licha ya muafaka huo, wauguzi katika hospitali nyingi za kaunti bado hawajarejea kazini. Katibu Mkuu Msaidizi wa Muungano wa Wauguzi Kenya (KNUN), Lucy Mburu, amesema mazungumzo kati ya viongozi wa chama hicho, Baraza la Magavana na maafisa wa wizara za Afya na Kazi yalikuwa yakiendelea lakini hayakuwa yamezaa matunda. Katika Kaunti ya Isiolo, hali imezidi kuwa mbaya kwani hata madaktari wamekuwa mgomoni kwa siku 66. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari (KMPDU), Dkt Dennis Miskellah, alisema madaktari walikosa mishahara kwa miezi mitatu, huku makato ya kodi, SHA na mikopo yakikosa kuwasilishwa kwa taasisi husika. Kaunti za Homa Bay na Siaya pia zinakabiliwa na tishio la migomo ya madaktari kutokana na migogoro ya ajira na bima ya afya. Katika kaunti ya Homa Bay, viongozi wa wauguzi wamemtaka Gavana Gladys Wanga kutumia nafasi yake kama mwenyekiti wa Kamati ya Wafanyakazi ya Baraza la Magavana kushinikiza suluhu ya mgogoro huo. Katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii, wagonjwa wengi wameelekea hospitali za kibinafsi baada ya huduma nyingi kukwama. Hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) mjini Kisumu nayo imeelemewa baada ya kupokea wagonjwa wengi kutoka kaunti jirani. Mkurugenzi wa huduma za uuguzi Teresa Okiri alisema hospitali hiyo sasa inapokea wastani wa wagonjwa 50 mahututi kila siku, huku wodi za wazazi, watoto wachanga na dharura zikifurika. Katika Hospitali ya Rufaa ya Kitui, mamia ya wagonjwa walionekana wakisubiri huduma bila mafanikio. "Tunaomba serikali isikilize malalamishi ya wahudumu wa afya ili huduma zirudi kawaida," alisema Mary Mutua, mmoja wa wagonjwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Wanasiasa mashakani mali ikipigwa mnada kwa kulemewa na madeni
WANASIASA wengi nchini huchora taswira ya watu wasioweza kutikiswa kutokana na mamlaka wanayoshikilia, misafara ya magari, walinzi na bajeti kubwa wanazosimamia. Lakini hali hubadilika. Matatizo ya kifedha sasa yameanza kuwakumba baadhi ya viongozi wakuu huku benki zikielekeza madalali kuuza mali yao ili kufidia madeni. Aliyekuwa Gavana wa Murang'a na sasa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Mwangi wa Iria, ndiye mwathiriwa wa hivi punde. Shirika la Dalali Traders Auctioneers limetangaza kuwa mnamo Agosti 25 litauza nyumba yake ya Karen pamoja na Hospitali ya Edinburgh Mountain na Chuo cha Edinburgh vilivyoko Murang'a kutokana na deni ambalo halijafichuliwa. Aliyekuwa Waziri Raphael Tuju ndiye mwanasiasa aliyepoteza mali nyingi zaidi mwaka huu. Mnamo Machi, alipoteza Dari Business Park iliyoko Karen baada ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) kuiuza kufidia mkopo wa dola milioni 9.3 (zaidi ya Sh1.2 bilioni) aliouchukua 2015. Deni hilo sasa limeongezeka hadi Sh4.5 bilioni. Wiki hii, kampuni ya Garam Investments ilitangaza pia mnada wa Entim Sidai Wellness Sanctuary, mali nyingine ya kifahari ya Tuju iliyoko Karen. Mfanyabiashara Mary Wambui Mungai, ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi ya Athi Water Works Development Agency, alipoteza hoteli yake ya Glee mwezi uliopita. Aliyekuwa Waziri Moses Kuria alinusurika kwa muda baada ya mkewe Joyce Njambi kupinga mpango wa Benki ya Equity kuuza majengo yao ya vyumba vya kupangisha yaliyoko Ruaka na Juja kufidia mkopo wa Sh54 milioni. Mkewe alidai mali hiyo ni ya ndoa na haikupaswa kutumika kama dhamana bila idhini yake. Kesi bado inaendelea mahakamani. Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu pia amekuwa akipambana na wakopeshaji.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 12 hours ago
Hivi ndivyo msanii wa Bongo Matonya aliponyoka kesi ya ubakaji na mwanamke Mkenya
MSANII wa Bongo Flava kutoka Tanzania, Sefu Ramadan almaarufu Matonya, aliponyoka kesi ya ubakaji iliyokuwa ikimuandama kufuatia ombi lililotolewa na mamake kwa mwanamke aliyekuwa amemshtaki. Jambo hilo lilifanya Mahakama ya Shanzu, Mombasa kumuondolea kesi hiyo. Imebainika kuwa mamake Matonya alimtafuta mfanyabiashara huyo wa Kenya na kumsihi amsamehe mwanawe. Mwanamke huyo baadaye aliambia mahakama kuwa aliamua kuondoa kesi hiyo baada ya ombi la mama huyo pamoja na msongo wa mawazo alioupata kutokana na mchakato mzima wa kesi. "Nimeamua kumsamehe mtuhumiwa kwa sababu kesi imeniletea msongo wa mawazo. Mamake mshukiwa ambaye ni mgonjwa alinifikia na kuniomba nimsamehe mwanawe," alisema mwanamke huyo katika Mahakama ya Shanzu. Stakabadhi za Mahakama zinaonyesha kuwa ombi hilo halikupingwa na upande wa mashtaka ambao uliiambia mahakama kuwa ulikuwa na maagizo ya kuondoa kesi hiyo. "Kwa kuwa ombi la kuondoa mashtaka limeungwa mkono na upande wa mashtaka, kesi hii imeondolewa. Mtuhumiwa yuko huru," iliamua mahakama, na kuamuru pia pasipoti ya Matonya irejeshwe, ilani iliyowekwa iondolewe na mdhamini wake kuachiliwa. Kwa upande wake, Matonya, alitoa shukrani tu. "Nashukuru. Naomba pasipoti yangu irejeshwe," alisemaKatika kiapo chake, mlalamishi huyo alisisitiza kuwa uamuzi wake ulikuwa wa hiari bila kulazimishwa, kutishwa, kushawishiwa au kuahidiwa chochote. "Ni uamuzi wangu binafsi kufuta kesi na najua nikishaifuta siwezi kuirudisha tena," alisema. Alieleza mahakama kuwa amepatana na mtuhumiwa na kuchagua kumsamehe. Pia alitaja majukumu ya safari za mara kwa mara ambayo yangemzuia kuendelea kufika mahakamani. Mwanamke huyo aliongeza kuwa kesi hiyo imemsababishia msongo wa mawazo, kuathiri maisha yake binafsi na mahusiano ya kijamii, na kumweka katika hali ya aibu na unyanyapaa wa kijamii. "Kwa kuzingatia yote haya, sitaki tena kushiriki katika kesi hii. Ningependa kuendelea na maisha yangu na kuzingatia mambo yangu binafsi na majukumu ya baadaye," alisema. Aliongeza kuwa uamuzi wake ulitokana na maridhiano na mtuhumiwa, majukumu ya safari na athari za kihisia na kijamii za kesi, akisisitiza kuwa hakukuwa na masharti yoyote na ulikuwa ni tendo la msamaha pekee. Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa Matonya alikana mashtaka Aprili 9, na kesi ikapangwa kusikizwa. Jaribio la kwanza la kuondoa kesi lilifanyika Juni 11, lakini mahakama ilimtaka mlalamishi kuwasilisha kiapo cha kina kwa kuwa kesi ilihusisha tuhuma za ubakaji na ilikuwa ya maslahi ya umma. Baada ya kiapo kuwasilishwa, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ilipeleka faili kwa maafisa wa ngazi ya juu kwa idhini. Julai 1, upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa umepata idhini na ukaomba rasmi kuondoa mashtaka. Mlalamishi aliapishwa, akathibitisha yaliyomo kwenye kiapo chake na kurudia sababu zake kabla ya mahakama kuruhusu ombi hilo, na hivyo kumaliza rasmi kesi ya jinai dhidi ya mwanamuziki huyo wa Tanzania. Aprili 9, Matonya alishtakiwa kwa kosa la ubakaji na alikana mashtaka mawili ya unyanyasaji wa kijinsia. Msanii huyo alishtakiwa kwa kosa kinyume na Kifungu cha 3(1)(a) kinachosomwa pamoja na Kifungu cha 3(3) cha Sheria ya Makosa ya Kingono. Upande wa mashtaka ulidai kuwa Aprili 7, 2026, katika nyumba ya kifahari eneo la Nyali, Mombasa, mtuhumiwa alimbaka mlalamishi J.G. kwa kutumia nguvu. Alikabiliwa pia na shtaka mbadala la kutenda kitendo kisicho cha heshima kwa mtu mzima, ambapo mahakama iliambiwa kuwa mtuhumiwa alimgusa sehemu za siri za mwanamke huyo bila ridhaa yake.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 13 hours ago
Hamtaingia DCP kienyeji, asema Gachagua akiunda kamati ya kupekua wanaohama serikali
CHAMA cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Rigathi Gachagua kimeunda kamati maalumu ya watu saba kuchuja viongozi wanaotaka kuhama kutoka chama cha United Democratic Alliance (UDA) kabla ya kupokelewa rasmi. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kutokea mvutano mkali kati ya Bw Gachagua na baadhi ya washirika wake waliochaguliwa kuhusu iwapo wahamiaji kutoka UDA wanapaswa kupokelewa bila masharti. Kamati hiyo itaongozwa na Kaimu Katibu Mkuu wa DCP, Seneta wa Nyandarua John Methu. Wanachama wengine ni Seneta wa Murang'a Joe Nyutu, Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang'wa, Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Njeri Maina, Mbunge wa Naivasha Jayne Kihara, Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiru. Bw Methu alisema uamuzi wa kuunda kamati hiyo ulifikiwa baada ya vikao 19 vya mashauriano vilivyoanza Juni 16, 2026, katika makazi ya Bw Gachagua, Wamunyoro, na baadaye kuendelea katika Hoteli ya Outspan, Nyeri. Alisema DCP imepokea maombi 816 kutoka kwa viongozi wanaotaka kuhama kutoka upande wa serikali. Kwa mujibu wake, miongoni mwao ni mawaziri watano, makatibu wanane wa wizara, wabunge 83, maseneta watano, magavana wanne pamoja na madiwani na maafisa wa mashirika ya serikali. Bw Methu alisema kila anayetaka kujiunga na DCP atalazimika kutangaza hadharani kuwa hatagombea uchaguzi wa 2027 kupitia chama chochote kinachomuunga mkono Rais William Ruto. Aidha, alisema hakuna mwanasiasa atakayeruhusiwa kumfikia moja kwa moja Bw Gachagua ili kuomba kujiunga na chama. Alidai baadhi ya wanaotaka kuhamia DCP wamekuwa wakipiga picha na Bw Gachagua kisha kusambaza taarifa kuwa walitoa hongo ili wapate tiketi za moja kwa moja katika uchaguzi mkuu ujao. Pia aliwashutumu baadhi yao kwa kurekodi kwa siri mazungumzo yao na kiongozi huyo na kuyapeleka kwa serikali. Bw Methu alisema wafuasi wengi wa DCP bado hawajawasamehe viongozi waliomuunga mkono Rais Ruto kumng'oa Bw Gachagua kutoka wadhifa wa Naibu Rais mnamo 2024. Kwa upande wake, Mbunge wa Ol Kalou Kamau Ngotho alisema Bw Gachagua amewaambia viongozi wa chama kuwa amewasamehe wote waliopiga kura ya kumuondoa madarakani. Alisema hatua hiyo ilitokana na ushauri wa viongozi wa kidini na wazee waliomtaka aunganishe viongozi badala ya kuendeleza tofauti za kisiasa. Hata hivyo, Mbunge wa Mwea Mary Maingi alikosoa hatua ya kuchuja wanaotaka kuhamia DCP, akisema hakuna mwanasiasa anayepaswa kuamua hatima ya wengine kisiasa. Naye Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri alisema viongozi hawapaswi kulazimishwa kujiunga na chama kimoja kwa kuwa wananchi ndio huamua watakaochagua. Mbunge wa Naivasha Jayne Kihara alisema suala hilo limegawanya chama kwa sababu baadhi ya wanachama wanaamini waliowatesa kisiasa hawawezi kupokelewa bila kuchunguzwa. Aliongeza kuwa viongozi wanaohusishwa na makundi ya wahuni waliovuruga mikutano ya DCP au waliohusishwa na vurugu za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou hawatapokelewa kirahisi. Kwa upande wake, Seneta Karungo wa Thang'wa alisema mchakato wa uchunguzi ni muhimu ili kuzuia wanaoweza kuhujumu chama kutoka ndani. Naye Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Njeri Maina alisema kamati hiyo haitakuwa ya kujinufaisha kwani wanachama hawatalipwa posho yoyote. Alisema kazi yake ni kusikiliza maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo ya iwapo mwombaji anafaa kupokelewa au la, bila kutoza ada wala kutoa adhabu yoyote.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 10:55:38
Mvutano wazuka kuhusu usajili wa Linda Mwananchi
MVUTANO kuhusu usajili wa chama kipya cha kisiasa cha Linda Mwananchi Party umechukua mwelekeo mpya baada ya mawakili wa Charles Wanyonyi, aliyekuwa wa kwanza kujaribu kukisajili kushtumu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kwa kutaka kupitia upya uamuzi wa awali bila kumshirikisha muombaji wa kwanza. Hatua hiyo imejiri siku moja baada ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na viongozi wanaohusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi kukutana kwa faragha na Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou. Baada ya mkutano huo, viongozi hao walitangaza kuwa msajili alikubali kupitia upya uamuzi wa kukataa kuhifadhi jina la chama hicho. Hata hivyo, mawakili wa Bw Wanyonyi wanasema hatua hiyo ni kinyume cha Katiba na haki ya kila mtu kusikilizwa iwapo mteja wao hatahusishwa katika mchakato huo. Katika barua iliyowasilishwa kwa msajili Agosti 5, mawakili wa kampuni ya Wanzau, Odhiambo and Associates walisema Bw Wanyonyi ndiye aliyekuwa wa kwanza kuomba kuhifadhi jina la "Linda Mwananchi Party of Kenya" mnamo Februari 24, 2026. Kwa mujibu wa mawakili hao, maombi ya kuhifadhi majina ya vyama yanapaswa kushughulikiwa kwa kufuata utaratibu wa aliyewasilisha kwanza.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 10:22:10
Unganisheni Wakenya badala ya kujitokeza tu wakati wa uchaguzi, Wetang'ula ahimiza NCIC
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang'ula, amehimiza Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) kurejesha imani ya Wakenya na kuwa mstari wa mbele kuimarisha umoja wa taifa wakati wote, badala ya kujitokeza tu kipindi cha uchaguzi. Wetang'ula alisema tume hiyo ilianzishwa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ili kuponya migawanyiko ya kisiasa, lakini imeendelea kukumbwa na changamoto ya kutokuaminiwa na wananchi. "NCIC ina tatizo kubwa la kuaminiwa. Haipaswi kuonekana kama taasisi inayofanya kazi wakati wa uchaguzi pekee," alisema alipokutana na viongozi wa tume hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wake, Askofu Kepha Omae, katika majengo ya Bunge. Alisisitiza kuwa elimu endelevu kwa wananchi ndiyo njia bora ya kubadili mitazamo na kujenga mshikamano wa kudumu. "Hakuna tatizo mtu kuwa wa jamii fulani. Tatizo ni pale utambulisho huo unapotumiwa kuwabagua au kuwanyanyasa wengine," alisema. Wetang'ula pia aliitaka NCIC kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Elimu ili kukuza utamaduni wa umoja miongoni mwa wanafunzi na vijana. Aidha, alihimiza tume hiyo kuimarisha ushirikiano na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Mahakama na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili kuongeza ufanisi wake. "Mnayo mamlaka ya kuchunguza, lakini mashtaka yanaendeshwa na DPP. NCIC inapaswa kujijengea heshima kwa kufanya kazi kwa weledi. Bunge litaendelea kuunga mkono kwa mujibu wa sheria," alisema. Spika huyo aliongeza kuwa uchaguzi ni mchakato unaoendelea na si tukio la siku moja, hivyo NCIC ina jukumu muhimu la kukabiliana na matamshi ya chuki na viongozi wanaochochea migawanyiko. Kwa upande wake, Askofu Kepha Omae alisema tume tayari imeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 kupitia mpango unaolenga kuzuia migogoro, kuimarisha ushirikiano na kushirikisha wadau mbalimbali. "Tumeandaa ramani ya utekelezaji. Tunataka kushirikiana na taasisi nyingine na viongozi wa kisiasa ili kupunguza ubaguzi na ukabila," alisema. Aliongeza kuwa NCIC itafanya kazi kwa karibu na wazee wa jamii, viongozi wa dini, shule na taasisi nyingine za elimu ili kuhamasisha siasa za amani na kuwataka viongozi kupunguza matamshi ya uchochezi. Kamishna wa NCIC Jerusha Mwaathime alitaka Bunge kupatia tume mamlaka makubwa zaidi ya uchunguzi ili iweze kushughulikia kwa ufanisi visa vinavyochochea chuki na migawanyiko nchini.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 09:47:11
Biya afanya mabadiliko ya kijeshi bila kuonekana
DOUALA, Cameroon: RAIS wa Cameroon Paul Biya Jumanne alifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa jeshi huku kukiwa na mjadala mkali kuhusu kutokuwepo kwake hadharani kwa muda wa miezi miwili. Kupitia amri tatu za rais zilizotiwa saini Jumatatu na kutangazwa kupitia redio ya taifa, Biya alipandisha cheo mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Rais kutoka kanali hadi brigedia jenerali. Pia aliwateua makamanda wapya katika maeneo manne kati ya matano ya kijeshi nchini humo na kufanya mabadiliko mengine katika uongozi wa vikosi vya jeshi. Mabadiliko hayo pia yalihusisha kuteuliwa kwa kamanda mpya wa Rapid Intervention Brigade (BIR), kikosi maalum kinachohusika na operesheni za kukabiliana na ugaidi na makundi yenye silaha. Aidha, Meja Jenerali Ebaka Hippolyte alipandishwa kuwa afisa mwandamizi katika Makao Makuu ya Jeshi, huku makanali kadhaa wakipandishwa cheo kuwa mabrigedia jenerali. Hatua hiyo imejiri wakati Biya hajaonekana hadharani tangu Juni 7, alipoondoka Cameroon kuelekea Ulaya kwa kile serikali ilichokitaja kuwa "ziara fupi ya kibinafsi". Hata hivyo, hajarejea nchini, jambo lililozua wasiwasi na uvumi kuhusu afya yake na uwezo wake wa kuendelea kuongoza taifa hilo. Msemaji wa serikali, Rene Emmanuel Sadi, alisema Biya yuko hai na anatarajiwa kurejea nchini humo hivi karibuni, lakini hakutoa tarehe rasmi ya kurejea kwake. Kutokuwepo kwa Biya kulisababisha chama tawala cha Cameroon People's Democratic Movement (CPDM) kuitisha kikao kisicho cha kawaida mwezi uliopita ili kujadili hali ya kisiasa nchini humo. Kikao hicho kilifanyika huku shinikizo likiongezeka kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na sehemu ya umma wanaotaka ufafanuzi kuhusu uongozi wa nchi. Biya, 93, ndiye kiongozi mzee zaidi duniani anayehudumu madarakani. Ameiongoza Cameroon tangu 1982 baada ya kumrithi Ahmadou Ahidjo. Katika kipindi hicho, alishinda chaguzi kadhaa ambazo mara nyingi zilikosolewa na wapinzani pamoja na waangalizi wa kimataifa kwa madai ya kukosa uwazi na usawa. Kwa miaka mingi, Cameroon imekabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo uasi wa waasi wa Boko Haram kaskazini, mzozo wa kujitenga katika maeneo ya wanaozungumza Kiingereza ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi, pamoja na malalamishi ya ukosefu wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Biya amekuwa akitumia muda mrefu nje ya ya nchi, hasa Uswisi, kwa mapumziko au ziara binafsi. Hata hivyo, safari yake ya sasa ndiyo ndefu zaidi kuwahi kushuhudiwa, hali ambayo imeongeza mijadala kuhusu mrithi wake na mustakabali wa uongozi wa Cameroon kuelekea uchaguzi ujao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 08:24:03
Hivi ni sahihi kutumia neno 'nyanja' kwa maana ya umoja na wingi?
JUMA hili nimesisimshwa na Makala yaliyoandikwa na mweledi mashuhuri wa lugha ya Kiswahili Ustadh Abdilatif Abdalla. Japo yeye daima hunyenyekea kwamba si msomi wa Kiswahili, mimi humuona kama mmoja kati ya wabobezi wachache wa Kiswahili, Uswahili na fasihi yake. Daima mimi huchukizwa na matumizi ya *nyimbo hii (na ninafikiri niliona Prof. F. E. M. K. Senkoro pia akitaja hilo) na kwa sababu hiyo maelezo ya Ustadh yalinichangamsha mno! Kwa kuwa Ustadh aliyaandika maelezo yake katika kumbi za umma kwa kusudi la kuelimisha, naomba niyanukuu neno kwa neno. "… neno nyanja ni wingi wa uwanja. Kwa hivyo, kwa maoni yangu mimi mzungumzaji wa Kiswahili wa kawaida tu (ambaye si mtaalamu wala si msomi), si sawa, wala si Kiswahili fasaha, wala si Kiswahili Sanifu, kulitumia neno nyanja kama kwamba umoja wake na wingi wake ni huo huo.Kuna na maneno mengine (ambayo nitayaorodhesha hapa chini) yaliyotiwa katika mkumbo huo wa matumizi ya makosa, kama hilo nyanja, kiasi cha kwamba wale wasioujua usuli wa maneno hayo haiwapitikii kamwe kuwa wafanyayo ni makosa! Na baadhi yayo yamekuwa yakitumiwa kwa makosa kwa muda mrefu (hata na wale wanaoshughulika na kukisanifu Kiswahili!) mpaka leo imekuwa ukimtanabahisha mtu kuwa hayo ni makosa, wewe mtanabahishaji ndiye utakayeonekana kuwa unakosea. Nimewahi kuambiwa na baadhi ya wataalamu wetu wa Sarufi na Isimu kwamba makosa yafanyikayo katika/kwenye lugha, na yakazowewa na baadhi ya watu na yakaendelea kufanywa kwa muda mrefu, makosa hayo huweza kukubaliwa kuwa sahihi. Kama nilivyotangulia kueleza, mimi si mtaalamu wala si msomi wa lolote. Kwa hivyo, napata tabu kuikubali hoja (huja) hii. Mtaniwia radhi wataalamu na wasomi. Huenda nisingekuwa na shida hiyo kama nami ningekuwa nimejaaliwa kuwamo katika/kwenye matengo hayo. Na linipalo tabu zaidi ni kuona jinsi baadhi yetu tulivyojipa leseni ya kuyafanya makosa kama haya kwa wepesi mno na (pengine) bila kujali, na kwa sababu hiyo niliyoieleza. Lakini huwa twalifanya hilo humu Kiswahilini tu. Hatuthubutu kulifanya hilo kwenye lugha za kigeni tujifunzazo. Huko huwa tuna hadhari sana, na hufanya juhudi kubwa, tusionekane tumefanya makosa. Na mtu huwa haachiliwi kuendelea kuyafanya makosa, hata kama makosa hayo yamekuwa yakitumiwa na baadhi ya watu kwa muda mrefu. Kwa nini, basi, makosa kama hayo yawe yanakubalika katika/kwenye hiki tukiitacho Kiswahili Sanifu? Naelewa, na ninakubali, kwamba nje ya Kiswahili fasaha na sanifu watu watakitumia Kiswahili vile watakavyo wao wenyewe, maadamu watakuwa wanaelewana wenyewe kwa wenyewe. Lakini tushughulikapo na Kiswahili fasaha na sanifu, yatubidi tuweke mipaka. Tusikifanye Kiswahili kama kwamba ni ng'ombe asiyekuwa na mchunga. Haya yafuatayo ni baadhi tu ya maneno ambayo wengine wetu tumekuwa tukitumia wingi wake kuwa ni umoja. Maneno yaliyoko kushoto yamo katika hali ya umoja, na yaliyo kulia ni wingi wayo:Wenzo (huu) - nyenzo (hizi) Usimulizi (huu) - simulizi (hizi) Utanzu (huu) - tanzu (hizi) Utungo (huu) - tungo (hizi) Ubeti (huu) - beti (hizi) Uga (huu) - nyuga (hizi) Uchango (huu) - chango (hizi) Waraka (huu) - nyaraka (hizi) Utumbuizo (huu) - tumbuizo (hizi) Wimbo (huu) - nyimbo (hizi)Juma lijalo nitaendeleza makala haya kwa kutoa hoja zilizotolewa na Prof Kineene wa Mutiso wakati akitoa jibu kuhusu makala haya.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 07:37:42
Mali ya Champions: Bruno Guimaraes aacha unahodha Newcastle kuja kuwa kiungo wa Arsenal
MABINGWA wa Ligi Kuu Uingereza (EPL) Arsenal, wamekubaliana na Newcastle United kuhusu uhamisho wa nahodha wao Bruno Guimaraes kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Uingereza zilizochapishwa Jumatano. Kwa mujibu wa Sky Sports, ofa ya kwanza ya Arsenal kwa kiungo huyo wa Brazil ilikataliwa mapema wiki hii. Hata hivyo, klabu hiyo ya London ilirejea na ofa iliyoboreshwa na kufikia makubaliano na Newcastle. Guimaraes sasa ameuzwa kwa Arsenal kwa ada ya pauni milioni 75 (Sh13.2 bilioni). Ripoti zinasema Guimaraes, 28, alikuwa ameiambia Newcastle kwamba angependa kujiunga na Arsenal iwapo ofa inayofaa ingewasilishwa. Newcastle ilikuwa ikitaka kusalia na nahodha huyo, ambaye bado ana miaka miwili katika mkataba wake, pamoja na mwanya wa kuongeza mwaka mmoja zaidi. Guimaraes alijiunga na Newcastle akitokea Olympique Lyon ya Ufaransa mnamo Januari 2022 na tangu wakati huo amekuwa nguzo muhimu ya klabu hiyo. Amecheza mechi 195 katika mashindano yote, akifunga mabao 31, na aliiongoza Newcastle kutwaa League Cup (Carabao 2025) taji lao la kwanza baada ya kipindi kirefu. Iwapo uhamisho huo utakamilika, Guimaraes ataongeza ubora na uzoefu katika safu ya kati ya kocha Mikel Arteta huku Arsenal ikisaka kutetea ubingwa wa EPL na pia kutamba katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Guimaraes pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil katika Kombe la Dunia 2026. Kuondoka kwake kutakuwa pigo jingine kwa Newcastle, ambayo tayari imewapoteza Anthony Gordon, Sandro Tonali na kocha Eddie Howe. Wakati huo huo, Kocha Mfaransa Herve Renard naye amerejea kuinoa Ivory Coast, miaka 11 baada ya kuiongoza kutwaa Kombe la Afrika 2015. Shirikisho la Soka la Ivory Coast lilitangaza Jumanne kuwa Renard, 57, atamrithi Emerse Fae, ambaye mkataba wake haukuongezwa baada ya Kombe la Dunia 2026. Fae alifikisha Ivory Coast hatua ya mchujo kwa mara ya kwanza katika kombe la dunia ambao walishiriki kwa mara ya nne. Renard aliinoa Tunisia kwa muda katika Kombe la Dunia baada ya kuanza vibaya kwa kipigo cha 5-1 dhidi ya Uswidi. Alishindwa kubadili mambo huku wakipoteza pia dhidi ya Japan na Uholanzi. Kocha huyo pia amewahi kuzinoa Angola, Morocco, Saudi Arabia na Zambia, aliyoiongoza kutwaa taji la AFCON 2012. Sasa atalenga kutwaa ubingwa wake wa tatu wa AFCON mwaka ujao katika mashindano yatakayoandaliwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 05:51:41
Utafiti: Waamerika hawaamini Rais Trump ataimarisha uchumi
WASHINGTON, Amerika: UTAFITI mpya wa Reuters/Ipsos unaonyesha kuwa kwa mara ya kwanza katika karibu mwongo mmoja, raia wengi wa Amerika wanaamini Democrat ina uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia uchumi kuliko Republican. Utafiti huo pia umebaini kuwa utendakazi wa Rais Donald Trump umeshuka hadi asilimia 35 na raia wengi wanaelekea kukosa imani naye kutokana na uchumi mgumu. Asilimia 37 ya wapigakura waliosajiliwa walisema Democrats wana sera bora za uchumi ikilinganishwa na asilimia 36 waliounga mkono Republicans, huku asilimia 27 wakisema hawakuwa na msimamo kuhusu Trump na utawala wake. Matokeo hayo yanakuja huku raia wa Amerika wakikabiliwa na kupanda kwa gharama ya maisha, wengi wakilalamikia pia mapato kidogo. La mno zaidi kwa raia wa Amerika ni kupanda kwa bei ya mafuta kutokana na vita kati ya Iran na Israel vinavyoungwa mkono na Amerika. Tangu vita hivyo vianze, bei ya petroli imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 25, jambo limeathiri pakubwa bajeti za familia nyingi na sekta za utengenezaji bidhaa. Kwa mujibu wa kura hiyo, asilimia 42 ya wapigakura wangewaunga wagombea wa Democratic iwapo uchaguzi wa Bunge ungefanyika sasa. Kwa upande mwingine asilimia 37 walisema wangewapigia kura Republicans. Wapigakura huru pia walionyesha kuwapendelea Democrats kwa tofauti ya asilimia 12 kuliko Republicans. Mwelekeo huo unaonyesha kuwa chama cha Republican kinachotarajia kutetea wingi wa wakilishi wake katika Bunge la Congress kwenye uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika Novemba, kina kibarua kudumisha umaarufu wake. Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wameonya kuwa matokeo ya kura za maoni za kitaifa hayawezi kutabiri moja kwa moja matokeo ya uchaguzi kwa sababu ushindani mkali unatarajiwa katika idadi ndogo ya maeneo ya uchaguzi na si taifa lote. Rais Trump naye amepuuzilia mbali matokeo ya tafiti hizo, akidai kupitia mtandao wake wa Truth Social umaarufu wake upo juu zaidi kuwahi kushuhudiwa, na kwamba tafiti zinazochapishwa na vyombo vya habari hazionyeshi hali halisi. Amedai kuwa raia wengi wanachangamkia utawala wake na wana matarajio mengi kuwa serikali yake itaipaza Amerika kimaendeleo. Uungwaji mkono wa Republican kuhusu usimamizi wa uchumi umeendelea kupungua katika muhula wa sasa wa Rais Donald Trump, hasa baada ya bei ya mafuta kupanda kufuatia mashambulizi ya Amerika na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari na vita vinavyoendelea.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 05 Aug 2026 05:30:34
Buda azusha kupewa ngombe waliokonda kama mahari ya bintiye na kuagiza warudishwe
KULISHUHUDIWA kioja cha mwaka kijijini hapa baba wa msichana alipodinda kupokea ng'ombe wawili kama mahari, akidai ni dharau kwa bintiye. Badala yake baba huyo aliamuru ng'ombe hao warudishwe walikotolewa mara moja. Waliofika kikao hicho cha mahari walijaribu kumbembeleza akubali mifugo hao kama sehemu ya mahari, bila mafanikio kwani baba alikaa ngumu. "Yaani wewe unanichukuliaje? Mimi nimemtunza binti yangu vyema kiasi kwamba kijana wako amependezwa naye na yuko tayari kumuoa, halafu waniletea ng'ombe mifupa mitupu? alifoka buda huyo. "Utarudi nao. Sitachukua kamwe ng'ombe waliokonda!" akasisitiza. Ilibidi kikao hicho cha mahari kisitishwe watu wakafumkana huku aliyeleta ng'ombe akilazimika kurudi nao.
read moreRight Column Content