T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 16 Jul 2026 02:29:39

TAHARIRI: Amani na uwazi ni muhimu katika kura ya Ol Kalou

UCHAGUZI mdogo wa ubunge wa Ol Kalou leo ni zaidi ya mashindano ya kisiasa kati ya vyama na wagombea wa vyama vikuu nchini. Ni fursa ya kuonyesha kwamba, Kenya imejifunza kutokana na makosa ya chaguzi zilizopita na kwamba, taasisi zake zina uwezo wa kusimamia uchaguzi ulio huru, wa haki na wa kuaminika. Hii ndiyo maana Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) ina wajibu leo wa kuhakikisha kuwa kuna viwango vya juu vya uwazi. Mshindi wa uchaguzi wa leo anastahili kuamuliwa kwa haki wala kusiwe na visa ambavyo vitasababisha kura yenyewe kuzua ghasia au kutiliwa shaka. Maafisa wa IEBC wanapaswa kusimamia zoezi hilo kwa uwazi, uadilifu na kutii sheria. Kila kura itakayoopigwa lazima ihesabiwe kwa uwazi, matokeo ya kila kituo yatangazwe wazi na fomu zote za matokeo zitolewe kwa maajenti na kuwekwa hadharani ili kuondoa mashaka. Wapigakura nao wana jukumu la kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani. Hawapaswi kuruhusu kushawishiwa kwa pesa, vitisho, propaganda au misimamo ya kisiasa inayochochea chuki. Baada ya kupiga kura hakuna haja ya kumiminika vituoni, bali kila mtu aende nyumbani na kuachia IEBC jukumu la kuhesabu kura. Kukusanyika vituoni na kituo cha kujumuisha kura kutazua tu ghasia na makabiliano kati ya wanasiasa pinzani. Aidha, polisi wana wajibu wa kuhakikisha usalama wa kila mtu bila upendeleo. Maafisa wa usalama wanapaswa kuwalinda wapigakura, maajenti wa vyama, maafisa wa uchaguzi na waangalizi wa uchaguzi. Polisi hawapaswi kuegemea upande wowote wala kutumiwa kuvuruga matokeo ya uchaguzi wenyewe. Hatua yoyote ya kukabiliana na ukiukaji wa sheria inapaswa kufanywa kwa kuzingatia sheria. Ni muhimu pia vyama vya kisiasa na wagombea wakubali kuwa ushindi na kushindwa ni sehemu ya demokrasia. Badala ya kutoa matamshi ya uchochezi au kuhamasisha wafuasi wao kufanya vurugu, wanapaswa kutumia njia za kisheria iwapo watakuwa na malalamishi kuhusu matokeo. Ol Kalou imevutia macho ya taifa kwa sababu uchaguzi huu unatazamwa kama kipimo cha nguvu za kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Hata hivyo, umuhimu wake haupaswi kuwa sababu ya kuvuruga amani au kukiuka sheria. Wakenya wanatarajia kuona uchaguzi unaoendeshwa kwa uwazi, usawa na uaminifu.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Sifuna sasa alenga kusajili Linda Mwananchi

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna ameanza mchakato wa kusajili Linda Mwananchi kuwa chama cha kisiasa atakachotumia kuwania urais mnamo 2027. Washirika wa Bw Sifuna wamethibitisha kuwa tayari wameweka mikakati mbadala iwapo juhudi hizo zitakumbana na vikwazo vya kisheria au kisiasa. Viongozi wa mrengo wa Linda Mwananchi, ambao ni mrengo wa waasi ndani ya ODM, walisema wamepanga kukutana na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) leo ili kuendeleza mchakato wa kusajiliwa kwa chama hicho. Baadhi yao walidai kuwa tayari wamehifadhi jina hilo, ingawa haikubainika iwapo liliidhinishwa kama lilivyo au kufanyiwa marekebisho. Hatua ya sasa inafuatia ombi la awali la kusajili chama kwa jina Linda Mwananchi Party of Kenya (LMPK) kukataliwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa, John Cox Lorionokou. Katika barua yake kwa Charles Wanyonyi aliyewasilisha ombi hilo, msajili alisema jina hilo linafanana na kaulimbiu nyingine zilizohifadhiwa, ikiwemo Linda Mkenya na Boresha Kenya, hivyo haliwezi kuidhinishwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Kisiasa. Hata hivyo, viongozi wa Linda Mwananchi wanasema hawajakata tamaa. Seneta wa Kisii Richard Onyonka alisema wameandaa majina mengine mawili mbadala iwapo usajili wa jina hilo utakwama. "Jumatatu tunakutana na Msajili wa Vyama vya Kisiasa. Tayari tumeshahifadhi jina hilo, lakini katika siasa za Kenya ni lazima uwe na mpango B na C. Tumejipanga kwa sababu tunaamini ODM imekufa kisiasa," akasema Bw Onyonka. Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema hakuna mtu anayeweza kuwazuia kusajili chama hicho kwa jina la Linda Mwananchi kwa kuwa tayari limejulikana kitaifa kama utambulisho wa mrengo wao. "Linda Mwananchi ni yetu. Ndilo jina ambalo wananchi wanalitambua, na hakuna atakayetuzuia kulitumia," akasema Bw Osotsi. Aliongeza kuwa tayari wameunda jopo la wataalamu litakalotayarisha katiba, sera na ilani ya chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027. Ingawa mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi analiwakilisha kundi hilo katika Baraza la Azimio, Bw Osotsi alisema kipaumbele chao kwa sasa ni kusajili chama na kukijenga nchini kote kabla ya kuingia katika mazungumzo ya miungano ya kisiasa.  "Hatua ya kwanza ni kuwa na chama na kukieneza katika kaunti zote 47. Baada ya hapo tutaanza mazungumzo ya kuunda muungano mkubwa wa upinzani," alisema. Hatua hiyo inajiri wakati Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ameanza kuweka juhudi mpya za kuunganisha vyama vya upinzani ili viweze kumenyana na Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027. Bw Onyonka na Bw Osotsi walisisitiza kuwa Bw Sifuna ndiye mgombea wao wa urais na watashawishi vyama vingine vya upinzani kumuunga mkono. Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Anthony Kibagendi naye amesema Linda Mwananchi itaungana na vyama vingine katika muungano mkubwa wa upinzani.  "Njia pekee ya kumshinda Rais Ruto ni vyama vya upinzani kuungana na kumsimamisha mgombeaji mmoja," akasema Bw Kibagendi. Mkutano wa Azimio unatarajiwa kujadili mfumo wa kuwasimamisha wagombea wa pamoja huku ukihusisha vyama vya Wiper, Jubilee, Kanu na vingine pamoja na makundi mapya kama Linda Mwananchi, DCP ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na People's Liberation Party (PLP) ya Martha Karua. Wachanganuzi wa siasa wanasema historia imeonyesha kuwa mgawanyiko wa upinzani umekuwa ukiwanufaisha walio madarakani. Mnamo 1992 na 1997, upinzani ulishindwa kumwondoa aliyekuwa Rais Daniel arap Moi kutokana na kusimamisha wagombea wengi wa urais. Hali kama hiyo ilijitokeza mnamo 2007, ambapo mgawanyiko kati ya Raila Odinga na Kalonzo Musyoka uliigawa kambi ya ODM na kumwezesha Rais Mwai Kibaki kutangazwa mshindi katika uchaguzi uliosababisha machafuko makubwa baada ya matokeo kutangazwa. Kwa sasa, viongozi wa Linda Mwananchi wanaamini kuwa chama kipya kitakuwa msingi wa kuunganisha upinzani na kumpa Bw Sifuna jukwaa la kuwania urais 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 8 hours ago

Gachagua akivutia umati mkubwa Bonde la Ufa, asidhanie hizo ni kura – Cheruiyot

WASHIRIKA wa Rais William Ruto sasa wanasema aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua yuko huru kuzuru Bonde la Ufa Kusini, lakini wakamwonya asichukulie mapokezi atakayopata kama ishara ya uungwaji mkono katika uchaguzi mkuu wa 2027. Akizungumza katika Taasisi ya Mafunzo ya Ufundi ya Chepalungu, Kaunti ya Bomet, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot alisema wakazi wa Bonde la Ufa huwapokea viongozi wote bila ubaguzi, lakini bado wanaunga mkono Rais Ruto na chama cha UDA. "Bw Gachagua anakaribishwa kama kiongozi mwingine yeyote. Sisi ni watu wenye ukarimu, lakini asidhani umati utakaompokea ni kura. Ukarimu wetu usichukuliwe kuwa uungwaji mkono wa kisiasa," akasema Seneta Cheruiyot. Alimkumbusha Bw Gachagua kuwa mnamo 2017 muungano wa NASA ulikusanya umati mkubwa Bomet wakati wa kampeni, lakini Rais wa zamani Uhuru Kenyatta ndiye aliyeshinda kwa kura nyingi katika eneo hilo. Kauli hiyo inajiri huku Bw Gachagua akitangaza mipango ya kuzuru Bonde la Ufa Kusini, akidai wakazi wamekata tamaa kutokana na kile alichosema ni ukosefu wa maendeleo licha ya kumuunga mkono Rais Ruto 2022. Hata hivyo, Bw Cheruiyot alikanusha madai hayo akisema eneo hilo linaendelea kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo barabara, hospitali, miradi ya maji, taasisi za elimu ya juu na viwanja vya ndege. Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo walisisitiza kuwa jamii ya Kipsigis itaendelea kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027 na kuwataka wakazi kujisajili kama wapigakura mapema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Siasa sasa zapelekwa WhatsApp uchaguzi wa 2027 ukikaribia

KATIKA siasa za Kenya za sasa, mapambano makali hayafanyiki tena kwenye mikutano ya hadhara, Bunge au runinga pekee. Sasa vita hivyo vimechacha kwenye makundi ya WhatsApp. Makundi yaliyoundwa awali kwa ajili ya kuratibu shughuli na kuhamasisha wafuasi sasa yamegeuka kuwa uwanja wa kupimana nguvu, kujenga au kuvunja ushirikiano na kuonyesha uaminifu wa kisiasa. Kuongezwa, kuondolewa au hata kuzimwa kwenye kundi sasa ni ujumbe wa kisiasa unaoweza kuzua mjadala mkubwa. Hapo awali, wanaoasi walikuwa wakifukuzwa kutoka afisi za vyama au kuzuiwa kuhudhuria mikutano. Leo, hatua hiyo hufanyika kwa kubofya kitufe cha kuwaondoa kwenye kundi la WhatsApp. Aidha, makundi hayo yamekuwa mahali pa mijadala mikali kuhusu misimamo ya vyama. Baadhi ya mapendekezo huzimwa humo kabla hata hayajafika bungeni, huku mengine yakianza kama mjadala wa WhatsApp na baadaye kuibuka kwenye mijadala ya Seneti na Bunge la Kitaifa. Mvutano unaoendelea ndani ya ODM kati ya viongozi wa mrengo wa Linda Mwananchi na uongozi wa chama unaendelezwa kwa kiasi kikubwa kupitia makundi hayo. Wiki iliyopita, wabunge wanaohusishwa na mrengo huo waliondolewa kwenye kundi la WhatsApp la Kundi la Wabunge wa ODM, ambalo hutumika kupanga ajenda za chama na kuelekeza wabunge jinsi ya kupiga kura au kujadili miswada. Walioondolewa ni pamoja na Maseneta Edwin Sifuna wa Nairobi, Godfrey Osotsi wa Vihiga na Richard Onyonka wa Kisii. Wabunge Babu Owino, Caroli Omondi, Caleb Amisi, Anthony Kibagendi, Clive Gisairo na Wilberforce Oundo pia walitimuliwa kwenye kundi hilo. Bw Sifuna alisema baada ya mkutano wa kisiasa Kitale waligundua wameondolewa kwenye kundi hilo, hatua aliyofasiriwa kama ishara kwamba uongozi wa ODM hauwataki tena. Kwa upande wake, Seneta Osotsi alisema hii si mara ya kwanza kwao kufutwa kwenye makundi ya chama. Alikumbuka kuwa mapema mwaka huu baadhi yao waliondolewa kwenye kundi la Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) kabla ya kupokonywa nyadhifa za chama. Alisema hatua hiyo inaonyesha kuwa wameonekana kama watu wasiostahili kuwa ndani ya ODM na sasa wanatafakari kusitisha michango yao ya kila mwezi kwa chama. Mivutano hiyo pia ilijitokeza wakati wa kuondolewa kwa Bw Sifuna kama Naibu Kiranja wa Wachache katika Seneti. Taarifa ya mkutano ilitumwa kupitia WhatsApp, jambo lililosababisha mabishano makali kabla ya mkutano huo kugeuka vurugu. Hata hivyo, tukio lililovuta hisia zaidi lilikuwa kuondolewa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwenye kundi la WhatsApp la Ikulu wakati wa tofauti zake na Rais William Ruto. Bw Gachagua alisema yeye, katibu wake binafsi na mkuu wa wafanyakazi wake waliondolewa kwenye kundi hilo, hatua iliyowafanya washindwe kupata taarifa kuhusu ratiba ya Rais na shughuli rasmi za Ikulu. Muda mfupi baadaye aling'olewa mamlakani kupitia mchakato wa kumbandua. Mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiru, maarufu kama Mejja Donk, alisema wabunge wengi wanaoonekana kumuunga mkono Bw Gachagua pia wameondolewa kwenye makundi ya Kenya Kwanza na UDA. Anasema hatua hiyo imewanyima taarifa za mikutano ya chama na shughuli nyingine za kisiasa. Kwa sababu hiyo, amesema alipunguza mchango wake wa kila mwezi kwa chama kutoka Sh20,000 hadi Sh500. Kwa mujibu wa wanasiasa mbalimbali, makundi ya WhatsApp sasa ni nyenzo muhimu katika kampeni za uchaguzi. Hutumika kupanga mikutano ya kisiasa, kuajiri wahudumu wa kujitolea, kusambaza ratiba za kampeni na kueneza ujumbe kwa wafuasi. Lakini pamoja na manufaa hayo, makundi hayo pia yamegeuka njia ya ujasusi wa kisiasa. Wapinzani hujiingiza kwenye makundi hayo na kutoa mikakati ya siri kwa hasimu wao. Katika kitabu chake Unwritten Political Rules, Cathy Irungu anaeleza jinsi watu waliodaiwa kuwa vibaraka walivyopenya kwenye timu ya kampeni ya Raila Odinga mwaka 2022 na kupata taarifa muhimu kupitia makundi ya WhatsApp. Na kadiri uchaguzi mkuu wa 2027 unavyokaribia, WhatsApp inatarajiwa kuendelea kuwa silaha muhimu ya kisiasa. Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa jukwaa hilo pia linaongeza kasi ya kusambaa kwa habari za uongo, kauli za kughushi na video zilizohaririwa ambazo zinaweza kupotosha umma. Wachambuzi wa siasa wanasema matumizi ya WhatsApp yamebadili kabisa namna vyama vya kisiasa vinavyofanya maamuzi. Tofauti na zamani ambapo viongozi walilazimika kukutana ana kwa ana ili kujadili masuala muhimu, sasa maamuzi mengi hufanyika kupitia simu za mkononi. Mikutano ya dharura hupangwa ndani ya dakika chache, huku taarifa zikisambazwa kwa mamia ya wanachama kwa wakati mmoja. Hata hivyo, kasi hiyo imeambatana na changamoto nyingi. Ujumbe unaovuja kutoka kwenye makundi ya viongozi mara nyingi huzua mizozo ya kisiasa na kuwapa wapinzani nafasi ya kufahamu mikakati ya vyama. Wakati mwingine picha za mazungumzo ya siri husambazwa mitandaoni na kusababisha viongozi kulaumiana kwa usaliti au kuvuja kwa taarifa. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya vyama sasa vimeweka masharti makali kuhusu matumizi ya makundi ya WhatsApp. Wanachama wanaotuhumiwa kuvuja siri au kupinga maamuzi ya chama huondolewa kwenye makundi hayo au kunyamazishwa wasichangie mijadala. Hatua hizo zimegeuza WhatsApp kuwa chombo chenye ushawishi mkubwa katika siasa za kisasa, ambapo kubaki au kuondolewa kwenye kundi kunaweza kufasiriwa kama ishara ya kupanda au kushuka kwa ushawishi wa mwanasiasa ndani ya chama chake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Kamati yapinga mswada wa kudhibiti nauli za matatu

KAMATI ya Bunge kuhusu Uchukuzi na Miundombinu imependekeza wabunge wakatae kabisa Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA), ikisema kudhibiti nauli za magari ya uchukuzi wa umma kunaweza kusababisha matatizo makubwa kuliko manufaa. Katika ripoti iliyowasilishwa bungeni, kamati ilisema Kenya inaendeshwa kwa mfumo wa uchumi wa soko huru, na hivyo serikali haipaswi kuingilia nauli za matatu kwa njia ya sheria. Kamati ilionya kuwa utekelezaji wa sheria hiyo utakumbwa na changamoto za kiutawala na ufuatiliaji, huku ukikinzana na baadhi ya makubaliano ya kikanda na kimataifa ambayo Kenya imetekeleza. Kamati ilieleza kuwa sekta ya uchukuzi wa umma inaendeshwa zaidi na wawekezaji wa kibinafsi kupitia vyama vya akiba na mikopo (Sacco), kampuni na watu binafsi. Kwa sababu hiyo, kudhibiti nauli kutahitaji mashauriano ya kina kutokana na gharama zinazobadilika mara kwa mara, ikiwemo bei ya vipuri vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi. Mswada huo wa mwaka 2023 unalenga kurekebisha Sheria ya NTSA ya mwaka 2012 ili kuweka mwongozo wa serikali kuhusu nauli zinazotozwa abiria wa magari ya uchukuzi wa umma. Mswada huo, unaodhaminiwa na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, unapendekeza kukomesha uhuru ambao wamiliki wa matatu wamekuwa nao wa kuamua nauli wanavyotaka, hasa wakati wa sikukuu, mvua au misimu ya shughuli nyingi. Iwapo utapitishwa, Kenya itaungana na mataifa kama Ghana, Rwanda, Tanzania, Cameroon na Ujerumani ambako serikali hushiriki katika kuweka kiwango cha chini cha nauli za usafiri wa umma. Hata hivyo, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alipinga mswada huo alipofika mbele ya kamati mwaka 2023. Alisema Kenya iliondoa sera za kudhibiti bei kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1980 hadi 1990 baada ya mageuzi ya kiuchumi yaliyolenga kupatia nguvu zaidi soko huru kuliko serikali. Kwa upande wake, Shirikisho la Sekta ya Uchukuzi wa Umma pia limepinga mswada huo likisema kabla ya serikali kuanza kuamua nauli, ni lazima iweke sera, sheria na taasisi madhubuti zitakazowezesha mfumo huo kufanya kazi. Shirikisho hilo lilibainisha kuwa gharama kubwa zinazowakabili waendeshaji wa matatu tayari zinadhibitiwa na sheria. Mafuta hudhibitiwa na Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA), bima husimamiwa na Mamlaka ya Kudhibiti Bima (IRA), huku waendeshaji wakitakiwa kutii sheria za ajira, kujiunga na Sacco au kampuni, kulipa ada za kaunti, kufanya ukaguzi wa magari kila mwaka na kuwa na vifaa vya usalama. Kwa mujibu wa shirikisho hilo, masharti hayo yote huongeza gharama za uendeshaji na kufanya biashara ya matatu kuwa ngumu, huku kampuni nyingi zikifungwa baada ya miaka michache. Lilisema sekta hiyo inapaswa kuendelea kufanya kazi katika mazingira ya ushindani wa soko huru kama ilivyo kwa mashirika ya ndege, ambayo hubadilisha nauli kulingana na msimu, likizo za shule, Pasaka na Krismasi. Licha ya mapendekezo ya kamati, Bw Barasa alisema hatarudi nyuma. Alisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho utatolewa na Bunge. "Nimeona ripoti ya kamati ikitaka mswada ukataliwe, lakini ni Bunge litakaloamua hatima yake," alisema. Mjadala kuhusu mswada huo ulianza wiki hii na unatarajiwa kuendelea wiki ijayo, huku wabunge wengi wakionekana kuunga mkono hatua ya kuweka utaratibu wa kudhibiti ongezeko la ghafla la nauli za matatu. Si mara ya kwanza pendekezo kama hilo kujitokeza. Mwaka 2018, Bunge lilikataa mpango wa Wizara ya Uchukuzi uliolenga kumpa waziri mamlaka ya kuweka nauli za magari ya uchukuzi wa umma. Vilevile mwaka 2020, Chama cha Wamiliki wa Matatu kilipinga pendekezo kama hilo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Je, Ruto anajaribu 'kumpanga' Mudavadi kumrithi 2032?

JE, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ndiye mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika serikali ya Rais William Ruto kwa sasa? Swali hilo limeibuka kufuatia madai kwamba baadhi ya majukumu muhimu ya uratibu wa shughuli za serikali yaliyokuwa yakisimamiwa na afisi ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki sasa yamehamishiwa na kuwekwa chini ya himaya ya Bw Mudavadi. Hatua hiyo imezua mjadala mpya kuhusu iwapo mwanasiasa huyo ndiye anaaminiwa zaidi na Rais Ruto katika utawala wa Kenya Kwanza. Bw Mudavadi amekuwa mwenyeji wa Rais Ruto katika ziara zake Magharibi mwa Kenya huku Profesa Kindiki akikosa ziara hizo. Wikendi iliyopita alimkaribisha Rais Ruto katika Kaunti ya Busia wakati wa kutawazwa kwa Askofu wa Dayosisi ya Katakwa ya Kanisa la Anglikana, Vitalis Job Ekuru, na baadaye akamkaribisha kuhutubia waumini pamoja na mkutano wa hadhara mjini Amagoro. Awali, Juni 13, Bw Mudavadi pia alikuwa mwenyeji wa Rais katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro wakati wa uzinduzi wa Chama cha Ushirika cha Shirikiana. Katika hafla mbalimbali za umma, Rais Ruto amekuwa akimtaja Bw Mudavadi kwa jina lake la heshima la kitamaduni, "Omwami", jambo ambalo linaonyesha ukuruba wa kisiasa kati ya wawili hao. Ushawishi wa Bw Mudavadi uliongezeka zaidi Oktoba 5, 2024 baada ya Rais kumkabidhi Wizara ya Masuala ya Nje kutoka kwa Waziri Alfred Mutua. Tangu wakati huo, amekuwa akiongoza shughuli za kidiplomasia za Kenya na ameandamana na Rais katika karibu kila ziara muhimu ya nje. Wakati mwingine amekuwa akisafiri mapema kuandaa mikutano mataifa ya nje kabla ya ujio wa rais. Mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba alipuuza madai kuwa kinara huyo wa mawaziri kuongezwa majukumu kunaashiria Rais anapanga kumpiga kumbo Profesa Kindiki. "Hata Profesa Kindiki alisema haya ni mabadiliko ya kawaida ya kiutawala. Mudavadi ni mmoja wa nguzo kuu za serikali hii na kupewa majukumu zaidi hakufai kuzua maswali," akasema Bw Milemba. Mbunge huyo alisema uamuzi wa Bw Mudavadi kutowania wadhifa wowote wa 2027 unampa nafasi ya kujikita kikamilifu katika kuratibu shughuli za serikali na kusukuma mbele ajenda ya Rais Ruto. Hatua imefufua kumbukumbu Kuongezwa kwa majukumu ya Bw Mudavadi pia kumefufua kumbukumbu za utawala wa mwisho wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambapo aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i alipewa mamlaka ya kusimamia shughuli za serikali huku aliyekuwa Naibu Rais William Ruto akionekana kutengwa kuelekea uchaguzi wa 2022. Mbunge wa Khwisero Christopher Aseka naye anasema Rais Ruto anamtegemea Bw Mudavadi katika kuratibu wa shughuli za serikali, utekelezaji wa sera na masuala ya kiutawala, huku akimtegemea Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang'ula kuimarisha ushawishi wake kisiasa Magharibi. Hata hivyo, Bw Aseka amemwonya Bw Mudavadi asidhani kuwa nafasi yake ya sasa itamhakikishia moja kwa moja uungwaji mkono wa kisiasa 2032. Kwa mujibu wa Bw Aseka, kuongezwa kwa idara chini ya usimamizi wa Bw Mudavadi ni ishara ya imani kubwa ambayo Rais Ruto anayo kwake. Bw Mudavadi tayari ametangaza kuwa hatawania urais wala nafasi ya naibu rais 2027, akisema lengo lake ni kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2032. "Mimi silengi wadhifa wa nambari mbili, nalenga kuwa namba moja kwa sababu nimewahi kuwa makamu wa rais. Mimi nalenga uongozi wa nchi mnamo 2032," akasema Bw Mudavadi mwezi uliopita akiwa katika ziara kwenye Kaunti ya Trans Nzoia. wa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Lumala Masibo, Rais Ruto analenga kutumia Bw Mudavadi kutuliza joto kali kati ya mirengo ya ODM na UDA kuhusu nafasi ya naibu rais.  "Ukiangalia vizuri kwa sasa Profesa Kindiki anafanya kila awezalo kuhakikisha kwamba anamdhihirishia rais eneo la Mlima Kenya Mashariki lipo nyuma yake. Kwa upande mwingine mrengo wa ODM nao unasaka nafasi hiyo,  "Hii ina maana kuwa Bw Mudavadi ndiye anaweza kumakinikia mengi ya majukumu ya serikali kwa sababu naye hawanii wadhifa wowote wa kisiasa 2027," akasema Profesa Masibo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Huzuni tele watu 21 wafariki katika ajali barabarani ndani ya saa 24

WATU 21 wamepoteza maisha katika ajali tofauti za barabarani nchini ndani ya kipindi cha chini ya saa 24, hali inayozua wasiwasi kuhusu ongezeko la vifo vinavyotokana na ajali katika barabara kuu na maeneo hatari. Ajali ya hivi punde ilitokea saa kumi na mbili alfajiri Jumamosi kwenye barabara ya Kimbimbi-Ngurubani, Kaunti ya Kirinyaga, ambapo watu wanane walifariki baada ya tuk-tuk kugongana na lori la kusafirisha mizigo. Wengi wa waliofariki walikuwa vibarua waliokuwa wakielekea mashambani Mwea kupanda mpunga. Ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Murubara, eneobunge la Mwea Mashariki. Nguvu ya mgongano iliharibu kabisa tuk-tuk hiyo na kuwanasa waliokuwa ndani. Waokoaji walitumia mashine maalumu kukata mabaki ya chuma ili kutoa miili huku jamaa na wakazi wakitazama kwa huzuni. Kamanda wa Polisi wa Mwea Mashariki, Stephen Okal, alisema dereva wa lori alikuwa akielekea Embu kutoka Ngurubani alipojaribu kukwepa shimo na kuingia njia ya magari yaliyokuwa yakitoka upande wa pili, kabla ya kugongana na tuk-tuk hiyo. Watu watano walifariki papo hapo, wawili wakafariki hospitalini baada ya kupelekwa Hospitali ya Kimbimbi Level Four. Lori hilo pia liligonga watembea kwa miguu wawili waliokufa papo hapo. Dereva wa tuk-tuk alikuwa miongoni mwa walioaga dunia. Dereva wa lori, ambaye alipata majeraha madogo, alikamatwa na atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika. Miili ya marehemu ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kerugoya Level Five huku magari yaliyoharibika yakipelekwa Kituo cha Polisi cha Wang'uru. Mapema usiku wa kuamkia Jumamosi, mwanamke mmoja alifariki na watu wengine wanne kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha magari kadhaa eneo la Mlima Nugu kwenye barabara ya Narok-Mai Mahiu. Polisi walisema lori lililokuwa likielekea Narok lilipoteza mwelekeo na kuanguka mtaroni. Basi lililokuwa nyuma yake likaligonga kabla ya kugongana na gari aina ya Toyota Probox lililokuwa likitoka upande wa pili. Majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok huku uchunguzi ukiendelea. Ajali hizo zimetokea saa chache baada ya watu wengine 12 kufariki katika ajali mbili tofauti Alhamisi usiku. Katika eneo maarufu la Mlima Punda kwenye barabara ya Eldoret-Nakuru, watu saba, akiwemo wanafunzi wawili waliokuwa wakirejea nyumbani kwa likizo, walifariki baada ya lori lililokuwa likipita magari mengine kugongana na matatu mbili. Kamanda wa Polisi wa Uasin Gishu Wilberforce Sicharani alisema dereva wa lori alipoteza udhibiti alipokuwa akiteremka mlima na kugonga matatu zilizokuwa zikielekea Nakuru. Kaunti ya Marsabit pia ilirekodi vifo vya watu watano baada ya trela moja kugonga nyingine katika Kargi Junction kwenye barabara ya Isiolo-Moyale. Wanne walifariki papo hapo huku mmoja akifariki hospitalini. Visa hivyo vinafuatia ajali nyingine ya basi la shule katika Kaunti ya Meru wiki hii ambapo wanafunzi wawili walifariki na wengine 49, pamoja na walimu wanne na dereva, kujeruhiwa walipokuwa wakirejea kutoka ziara ya masomo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 01 Aug 2026 22:55:25

Linda Mwananchi yazidi kuvutia wawaniaji mbalimbali uchaguzi ukikaribia

VUGUVUGU la Linda Mwananchi linazidi kubadili sura ya siasa nchini huku likiwavutia wanaowania ugavana kutoka maeneo mbalimbali ya Kenya. Kilichoanza kama jukwaa la viongozi waliopinga uamuzi wa ODM kuunga mkono azma ya Rais William Ruto kutafuta muhula wa pili, sasa kinaibuka kuwa nguvu mpya ya kisiasa inayojipanga kushindana katika uchaguzi wa 2027. Chini ya uongozi wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, vuguvugu la Linda Mwananchi limekuwa kivutio kikuu kwa viongozi wanaotafuta ugavana, huku wengi wakisubiri kutangazwa kwa chama ambacho litatumia katika uchaguzi mkuu ujao. Katika Kaunti ya Vihiga, Seneta Godfrey Osotsi tayari amejiunga na mkondo huo huku akijiandaa kuwania ugavana baada ya muhula wa Gavana Wilber Ottichilo kumalizika. Kaunti ya Bungoma nayo imekuwa kitovu cha vuguvugu hilo baada ya Mbunge wa Westlands, Tim Wanyonyi kuhamishia azma yake ya kisiasa huko. Bw Sifuna tayari amemtangaza kuwa mmoja wa viongozi anaoamini na hata kutabiri kuwa gavana ajaye wa Bungoma atatoka Linda Mwananchi. "Nimekutana na Tim Wanyonyi na viongozi wengine wengi. Ninachoamini ni kwamba gavana wa Bungoma mwaka 2027 atatoka Linda Mwananchi," alisema Bw Sifuna katika moja ya mikutano yake. Jijini Nairobi, Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa kundi hilo, ameweka wazi kuwa atamenyana na Gavana Johnson Sakaja katika uchaguzi ujao. Bw Owino amekuwa akitumia mikutano ya Linda Mwananchi kuimarisha mtandao wake wa kisiasa huku akipata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa vuguvugu hilo. Seneta wa Kisii, Richard Onyonka pia amejiunga na kundi la wanaotafuta ugavana kupitia Linda Mwananchi. Bw Sifuna tayari amemuidhinisha akisema ana uwezo wa kuongoza Kaunti ya Kisii. Katika Kaunti ya Kakamega, Seneta Boni Khalwale ameanza kujihusisha zaidi na Linda Mwananchi licha ya hapo awali kuhusishwa na chama chake cha United Patriotic Movement (UPM). Hatua hiyo imezua hisia kuwa huenda akakitumia chama kitakachozaliwa na vuguguvu hilo kuwania ugavana. Machakos pia haijaachwa nyuma. Mbunge wa Mavoko, Patrick Makau ameibuka kuwa mmoja wa washirika wakuu wa Linda Mwananchi na tayari ameweka wazi nia yake ya kuwania ugavana wa Machakos mwaka 2027. Bw Makau ni miongoni mwa viongozi ambao kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka alisema aliwaruhusu kushirikiana na Bw Sifuna katika juhudi za kujenga umoja wa upinzani. Katika Taita Taveta, Mbunge wa Wundanyi, Danson Mwashako pia ametangaza azma ya kuwania ugavana. Katika mkutano wa hivi majuzi wa Linda Mwananchi, Babu Owino aliwaongoza viongozi wengine kumuidhinisha Bw Mwashako na kuwataka wakazi wa kaunti hiyo kumuunga mkono. Aliyekuwa Naibu Katibu wa Uratibu wa Jubilee, Pauline Njoroge naye ameweka kando ndoto yake ya kuwania ugavana wa Nairobi na badala yake akaamua kumuunga mkono Babu Owino. Hata amedokeza kuwa yuko tayari kuwa mgombea mwenza wake iwapo mazungumzo ya kisiasa yatazaa makubaliano hayo. Aliyekuwa Gavana wa Bungoma, Wycliffe Wangamati pia ameanza kujitenga na chama chake cha DAP-K na kutangaza kuwa yuko tayari kutumia chama kitakachozinduliwa na Linda Mwananchi ili kurejea katika kinyang'anyiro cha ugavana wa Bungoma. Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, naye amesema atatetea kiti chake kupitia chama kitakachozaliwa na vuguvugu hilo. Bw Sifuna tayari amemtangaza kuwa anayefaa kuendelea kuongoza kaunti hiyo. Kwa upande mwingine, Gavana wa Siaya, James Orengo, mmoja wa vinara wa vuguvugu hilo ameendelea kutoa ishara zinazochanganya kuhusu mustakabali wake wa kisiasa huku kukiwa na tetesi kuwa huenda akagombea urais au akatetea kiti chake cha ugavana. Huku viongozi zaidi wakiendelea kuhamia Linda Mwananchi, wachambuzi wanabashiri litakuwa nguvu mpya ya kisiasa itakayoathiri uchaguzi wa ugavana 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Gachagua atoa makataa kwa wanaohamia DCP

KIONGOZI wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, ameongeza kwa siku 10 mkutano wake wa kisiasa unaoendelea katika makazi yake ya Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri, huku akitoa onyo kwa viongozi wanaotaka kuhamia chama hicho kwamba muda wa kufanya uamuzi unakaribia kuisha. Bw Gachagua alisema aliongeza muda huo kufidia siku alizotumia kusherehekea ushindi wa DCP katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou ambao mgombea wa chama hicho, Kamau Ngotho, alishinda mgombea wa UDA. Pia alisema alitumia muda kuzuru kaunti za Embu, Meru na Tharaka Nithi kupinga juhudi za kutenganisha kisiasa eneo la Mlima Kenya Mashariki. Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na mchambuzi wa siasa Herman Manyora, Bw Gachagua alisema masuala mawili makuu yanayojadiliwa katika mkutano huo ni nani anayefaa kuungwa mkono kuwania urais mwaka wa 2027 na masharti ambayo Mlima Kenya utaweka iwapo haitatoa mgombea wa urais. "Kuna upungufu mkubwa wa imani katika siasa. Wananchi wengi wanasema wanatamani niwaongoze, lakini pia ninaelewa kuwa Mlima Kenya hauwezi kushinda urais peke yake. Tutahitaji kushirikiana na maeneo mengine," alisema. Alisisitiza kuwa yuko tayari kuacha azma yake ya kuwania urais ikiwa hatua hiyo itasaidia kuondoa serikali ya Rais William Ruto kupitia uchaguzi. "Hata hivyo, kura za Mlima Kenya hazitatolewa bure. Tutataka kujua wananchi wetu watanufaika vipi kutokana na ushirikiano huo," alisema. Kwa mujibu wake, mazungumzo hayo hayatakuwa kuhusu ugavi wa nyadhifa za kisiasa pekee bali pia masuala ya uchumi yanayowagusa wananchi wa eneo hilo. "Tutazungumzia kodi, mazingira bora ya biashara, usalama wa wafanyabiashara, bei ya uhakika ya mazao na mikopo nafuu. Hayo ndiyo mambo tunayopigania," alisema. Bw Gachagua pia alitangaza kuwa ameongeza hadi katikati ya Agosti muda aliowapa viongozi wanaotaka kuhamia DCP. Alisema anahitaji kujua idadi ya wagombeaji watakaotumia tiketi ya chama hicho ili kupanga bajeti ya kampeni, ambayo anakadiria kufikia Sh4 bilioni. Aidha, alidai kuwa baadhi ya Mawaziri na Makatibu wamekuwa wakimtafuta kwa siri wakitaka kujiunga na DCP, lakini akawataka watangaze hadharani uamuzi huo. "Wengine wanakuja usiku. Nimewaambia kama kweli wanataka kuhamia DCP wafike mchana mbele ya kamera ili bosi wao aone wakihama," alisema. Kauli hizo zimezua mjadala ndani ya chama hicho. Seneta wa Murang'a, Joe Nyutu alipinga viongozi waliokuwa waaminifu kwa serikali kupewa nafasi katika DCP, akisema wanachama waliobaki na Bw Gachagua wakati wa kipindi kigumu hawapaswi kusukumwa pembeni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 01 Aug 2026 21:55:47

Wantam! Uhuru aanza kupanga majenerali kukabili Ruto 2027

RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuongoza mkutano muhimu wa Baraza la Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Jumatatu, hatua inayotafsiriwa kama kurejea kwake katika siasa za upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Mkutano huo unafanyika huku viongozi wa upinzani wakiharakisha juhudi za kuunda muungano mpana utakaoweza kukabiliana na Rais William Ruto, ambaye washirika wake wanaonekana kuwa mbele katika kujipanga kisiasa. Ajenda kuu itakuwa mustakabali wa Azimio, muungano aliotumia Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022. Baada ya kifo cha Raila mwaka jana, Uhuru alimkabidhi kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka jukumu la kusimamia muungano huo. Kalonzo amekuwa akipigia debe muundo unaofanana na ule wa Narc uliomuingiza Mwai Kibaki mamlakani mwaka 2002, ambapo vyama vilihifadhi utambulisho wao lakini vikaungana nyuma ya mgombea mmoja wa urais. Hata hivyo, juhudi hizo zimekumbwa na pingamizi kutoka kwa kiongozi wa Democracy for Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, ambaye amesema hakuna chama kitakachopewa tiketi ya urais kwa makubaliano ya viongozi pekee. "Kila chama kijipigie debe kwa wananchi. Tusifikirie kuwa watu watakaa mahali wagawane nafasi. Hilo halitafanyika," alisema Gachagua. Kwa miezi kadhaa, viongozi wa upinzani wamekuwa wakizungumzia mkutano mkubwa wa kuunganisha makundi yote yanayompinga Rais Ruto, lakini mkutano huo bado haujafanyika kutokana na ushindani wa ndani wa wanaotamani kuwania urais. Seneta wa Makueni Dan Maanzo alisema Uhuru ataongoza mkutano wa Jumatatu ambao utajadili jinsi ya kupanga upya na kupatia Azimio sura mpya kabla ya uchaguzi wa 2027. Anasema vyama kama Wiper, Jubilee, Kanu na washirika wengine vitashiriki, huku pia kukiwa na mazungumzo ya kuingiza makundi mapya kama Linda Mwananchi ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, DCP ya Gachagua na People's Liberation Party (PLP) ya Martha Karua. Wadadisi wa siasa wanasema upinzani unahofia kuchelewa kujipanga Kenya Kwanza ikijiiimarisha kupitia ushirikiano kati ya UDA na ODM. Maanzo alisema lengo ni kuunda muungano utakaowapa nafasi viongozi wapya bila kulazimisha vyama kuvunjwa. "Tunataka muundo mpya unaoweza kuwaleta pamoja wote wanaotaka mabadiliko," alisema. Mchambuzi wa siasa Dismas Mokua alisema uwezekano wa viongozi kuvunja vyama vyao na kuunda chama kimoja ni mdogo sana. "Kilicho rahisi ni muungano mkubwa ambapo kila chama kitabaki kivyake lakini kishirikiane kumpata mgombea mmoja wa urais," alisema. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Multimedia, Profesa Gitile Naituli, alisema changamoto kubwa si jina la muungano bali uwezo wa viongozi kukubaliana kuhusu ajenda ya pamoja. Wakati huo huo, vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Sifuna linazidi kupata nguvu baada ya kufanya mazungumzo na Kalonzo, mgombea wa Jubilee Dkt Fred Matiang'i na viongozi wengine wa upinzani. Vyanzo vinaeleza kuwa vuguvugu hilo linajisajili kuwa chama cha kisiasa ili kushiriki kikamilifu katika mazungumzo ya kuunda muungano mpya. Kulingana na kura ya maoni ya TIFA, Sifuna anaungwa mkono kwa asilimia 15 katika kuwania urais, akimzidi Kalonzo ambaye ana asilimia 13, huku Dkt Matiang'i akiwa na asilimia 14. Kwa pamoja, wagombea wa upinzani wana uungwaji mkono mkubwa kuliko Rais Ruto. Hata hivyo, swali kubwa ni iwapo DCP ya Gachagua itajiunga na muungano huo. Mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiru, maarufu Mejja Donk, alisema DCP iko tayari kushirikiana lakini haitaki kumezwa na Azimio. "Tunataka ushirikiano unaozingatia nguvu za kila upande. Si majina makubwa pekee bali pia idadi ya wafuasi," alisema. Naibu kiongozi wa DCP Cleophas Malala pia alisema chama kiko tayari kushirikiana na kundi lolote linalotaka Rais Ruto ahudumu kwa muhula mmoja pekee. Kwa upande wake, Martha Karua alipinga wazo la kuunda chama kimoja cha upinzani. "Hatutarudi katika mfumo wa chama kimoja. Katiba yetu inatambua siasa za vyama vingi na hilo halitabadilika," alisema. Ndani ya Jubilee, baadhi ya viongozi wana wasiwasi kuwa kumpa Kalonzo uongozi wa Azimio kunaweza kudhoofisha mgombea wao Dkt Matiang'i. Hata hivyo, Naibu Kiongozi Mwenza Jeremiah Kioni alisema Kalonzo aliteuliwa kwa sababu ndiye alikuwa kiongozi mkuu zaidi aliyesalia ndani ya Azimio. Mkutano wa Jumatatu unatarajiwa kuwa kipimo muhimu cha uwezo wa viongozi wa upinzani kuweka kando tofauti zao na kujenga muungano utakaoweza kutoa ushindani mkubwa dhidi ya Rais Ruto katika uchaguzi wa mwaka 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 01 Aug 2026 01:55:36

China yakana madai ya kuuzia Iran silaha

SERIKALI ya China imekanusha vikali madai kwamba imekubali kuiuzia Iran mamia ya mifumo ya ulinzi wa angani, wakati mapigano kati ya Iran na Amerika yakiendelea kushika kasi na kuzua hofu ya kusambaa kwa vita katika eneo lote la Mashariki ya Kati. Wizara ya Ulinzi ya China mnamo Alhamisi ilisema ripoti zilizodai kuwa Beijing inapanga kuipatia Tehran kati ya mifumo 300 na 400 ya ulinzi wa anga ni 'za uongo na zisizo na msingi wowote.' Msemaji wa wizara hiyo, Jiang Bin, alisema China haijahusika katika makubaliano yoyote ya aina hiyo. Kauli hiyo imejiri siku moja baada ya shirika la habari la Reuters kuripoti, ikinukuu durukutoka sehemu tatu zinazofahamu suala hilo, kwamba Iran ilikuwa inatarajiwa kupokea mifumo ya makombora ya QW-12 na FN-16 yenye thamani ya kati ya Sh7.7 bilioni na Sh9 bilioni. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makubaliano hayo yalidaiwa kuhusisha kampuni moja yenye makao yake Hong Kong iliyokuwa ikifanya kazi kama mpatanishi kati ya Iran na China. Duru hizo zilidai kuwa shehena za kwanza zilitarajiwa kusafirishwa kutoka mji wa Urumqi, magharibi mwa China, kupitia Pakistan kuelekea Iran. Hata hivyo, jeshi la Pakistan limekanusha madai hayo, likisema kuwa taarifa zinazodai nchi hiyo inahusika katika usafirishaji huo ni za kubuni. Mvutano huo umeongezeka wakati Amerika ikiendelea na mashambulizi dhidi ya jeshi la Iran. Mnamo Jumatano, ndege za kivita za Amerika zilifanya mashambulizi mapya dhidi ya vituo vya kijeshi vya Iran, huku mapigano yakisambaa hadi maeneo ya pwani ya Misri baada ya shambulizi dhidi ya bandari moja muhimu katika Bahari ya Shamu. Mashambulizi hayo yamezidisha hofu ya kuvurugika kwa biashara ya kimataifa, hasa usafirishaji wa mafuta kupitia Mkondo wa Hormuz na Bahari ya Shamu. Wataalamu wa masuala ya usalama wanaonya kuwa kuongezeka kwa mapigano kunaweza kuathiri usafirishaji wa bidhaa muhimu na kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani. Wakati huo huo, Iran imeendelea kusisitiza kuwa ina haki ya kujilinda dhidi ya kile inachokiita uchokozi wa Amerika na washirika wake. Serikali ya Tehran imeonya kuwa mashambulizi yoyote mapya yatachochea hatua kali za kulipiza kisasi. China, ambayo ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Iran, imeendelea kutaka pande zote kurejea kwenye meza ya mazungumzo badala ya kutumia nguvu za kijeshi. Beijing imeonya kuwa vita hivyo vinaweza kuhatarisha uthabiti wa uchumi wa dunia na kuzidisha migogoro ya kisiasa katika eneo hilo. Licha ya mazungumzo ya kidiplomasia yanayoendelea kupitia Qatar, Oman na Umoja wa Mataifa, hakuna dalili za haraka kwamba mapigano hayo yatamalizika hivi karibuni. Wachambuzi wanaonya kuwa iwapo vita vitaendelea, mataifa mengi zaidi yanaweza kujikuta yakivutwa katika mzozo huo unaotikisa Mashariki ya Kati.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 01 Aug 2026 02:55:15

Ugatuzi: Kilichozima kabisa jumuiya za kiuchumi za kaunti

MIAKA 13 baada ya ugatuzi kuanza, ndoto ya kuanzishwa kwa jumuiya za kiuchumi za kaunti ili kuimarisha maendeleo imekwama kutokana na ukosefu wa fedha, mvutano wa kisiasa na kukosekana kwa sheria zinazozitambua rasmi. Magavana walipoanzisha ushirikiano huo mwaka wa 2013, waliahidi kwamba ungechochea ukuaji wa uchumi, kuvutia wawekezaji na kuboresha maisha ya wakazi kupitia miradi ya pamoja. Kaunti mbalimbali ziliunda miungano kama Jumuiya ya Kaunti za Pwani, Jumuiya ya Kiuchumi ya kaunti za eneo la Ziwa (LREB), Jumuiya ya Kiuchumi ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa (Noreb), Jumuiya ya Kiuchumi ya Eneo la Kati(Cereb), Jumuiya ya Kiuchumi ya Kusini Mashariki Kenya na na Baraza la Ustawi la Kaunti za Kaskazini Mashariki. Hata hivyo, matumaini hayo yamefifia. Miradi mingi imekwama huku baadhi ya kanda zikigeuka kuwa majukwaa ya mikutano bila matokeo yanayoonekana. Baadhi ya changamoto zinazotajwa ni ukosefu wa fedha, ushindani wa kisiasa, mabadiliko ya uongozi wa kaunti na kukosekana kwa sheria inayoruhusu kaunti kuchangisha na kutumia fedha kwa pamoja. Mfano ni LREB, iliyopanga kuanzisha benki ya maendeleo ya Sh2 bilioni ili kutoa mikopo nafuu kwa wafanyabiashara. Mpango huo ulisitishwa mwaka wa 2023 baada ya Afisi ya Mdhibiti wa Bajeti kukataa kuidhinisha mradi huo kwa sababu haukuwa na msingi wa kisheria. Kila kaunti mwanachama ilitarajiwa kuchangia Sh200 milioni, lakini hilo halikufanyika. Mkurugenzi wa Kamati na Mipango katika Baraza la Magavana (CoG), Bw Kizito Osore Wangalwa, amesema ukosefu wa sheria ndio kikwazo kikubwa. Alisema sheria itapatia kanda hizo uhalali, kurahisisha upatikanaji wa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo na kuhakikisha zinaendelea hata baada ya mabadiliko ya kisiasa. Mswada wa Rasilmali za Kaunti unaolenga kutambua rasmi kanda hizo na kuruhusu kaunti kuunganisha rasilimali, bado umekwama Seneti. Wataalamu wa utawala pia wanasema kuchelewa kwa sheria hiyo kumedhoofisha utekelezaji wa miradi mingi. Mtaalamu wa utawala Dkt Peter Mbae alisema mabunge mengi ya kaunti hayajapitisha sheria zinazowezesha matumizi ya fedha kwa shughuli za kanda hizo, hali inayozua maswali ya ukaguzi wa hesabu. Katika Jumuiya ya Kaunti za Pwani, mwenyekiti wake ambaye pia ni Gavana wa Tana River, Dhado Godana, amesema baadhi ya kaunti hazijawasilisha michango yao ya kila mwaka ya Sh2.5 milioni, jambo linalotatiza shughuli. Licha ya changamoto hizo, wataalamu wanaamini kuwa ikiwa zitawekewa msingi wa kisheria na kufadhiliwa ipasavyo, miungano ya kiuchumi ya kanda inaweza kuimarisha kilimo, utalii, biashara, viwanda na kuongeza ajira kupitia miradi ya pamoja inayovuka mipaka ya kaunti.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 01 Aug 2026 00:55:38

Ripoti ya polisi yafichua ukatili wa wanajeshi wa Uingereza Laikipia

RIPOTI ya siri ya polisi imefichua madai mazito ya ubakaji, ulawiti wa watoto na ukiukaji wa haki za kibinadamu unaodaiwa kutekelezwa na wanajeshi wa kikosi cha Uingereza wanaopata mafunzo Kenya (BATUK) katika Kaunti ya Laikipia. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Mei 19, 2026, iliyotiwa saini na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na kuwasilishwa bungeni, baadhi ya wanajeshi walivuka kutoka eneo lao la mazoezi ya kijeshi hadi vijiji vya jirani na kuwashambulia wakazi. Katika kijiji cha Lekiji, Kaunti Ndogo ya Laikipia Kaskazini, msichana mwenye umri wa miaka 12 anaripotiwa kubakwa mara kadhaa na wanajeshi hao baada ya kushawishiwa kwa peremendepipi alipokuwa akivua samaki karibu na mto. Ripoti hiyo inadai kuwa baadaye alipata ujauzito na kujifungua mtoto mwenye asili mchanganyiko. Watoto wengine, kwa mujibu wa uchunguzi huo, walinaswa kwa kupewa biskuti, chokoleti na vinywaji kabla ya kudhulumiwa kingono. Ripoti hiyo inaeleza kuwa manusura wengi walitelekezwa wakiwa wamepoteza fahamu na kuokolewa baadaye na jamaa, majirani au wachungaji wa mifugo waliovutiwa na vilio vyao. Katika Kaunti ya Laikipia pekee, polisi walirekodi visa vya watu 37 waliodaiwa kubakwa na genge, watu 20 kubakwa na wengine wawili kujeruhiwa walipokuwa wakijaribu kutoroka mashambulizi hayo. Waathiriwa walieleza kuwa washambuliaji walikuwa wamevalia sare za kijeshi na mara nyingi waliwashambulia katika maeneo yaliyotengwa kama vichakani, njia za porini na kandokando ya mito walipokuwa wakichota maji, kukusanya kuni, kuogelea au kuchunga mifugo. Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa manusura wengi hawakupata matibabu hospitalini kutokana na hofu, unyanyapaa, mila za jamii na ukosefu wa huduma za afya. Badala yake, baadhi yao walifanyiwa matambiko ya jadi na kupewa dawa za mitishamba. Baadhi ya wanawake walidai walipoteza mimba baada ya mashambulizi hayo huku wengine wakisema hawakuweza tena kupata ujauzito. Wachunguzi walichukua taarifa kutoka kwa manusura 40 wenye umri kati ya miaka 48 na 90 waliotoa ushahidi kuhusu ukatili huo pamoja na madhara ya muda mrefu ya kimwili na kisaikolojia. Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa watoto waliozaliwa kutokana na visa hivyo wanakabiliwa na ubaguzi, unyanyapaa na kukosa msaada kutoka kwa wanaodaiwa kuwa baba zao. Polisi walitambua mtoto mmoja mwenye asili mchanganyiko Laikipia, huku ikielezwa kuwa sampuli za DNA za baadhi ya waathiriwa zilipelekwa Uingereza kwa uchunguzi kubaini baba mzazi. Kutokana na matokeo hayo, polisi wanapendekeza serikali ichukue hatua za kisheria kupitia mikataba ya kimataifa ya usaidizi wa kisheria na pia kuendelea na uchunguzi wa DNA kwa idhini ya waathiriwa ili kuwabaini wanaodaiwa kuwa baba wa watoto hao. Ripoti hiyo ilifuatia agizo la Bunge mwaka jana kwa polisi kufanya uchunguzi huru baada ya Kamati ya Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni kubaini madai ya unyanyasaji wa kingono, matumizi mabaya ya mamlaka na ukiukaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na wanajeshi hao. Wakati huo huo, licha ya serikali kutangaza kurejelewa kwa mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Kenya na Uingereza, wabunge wanataka makubaliano hayo yafanyiwe marekebisho ili kosa la mauaji lisikilizwe katika mahakama za Kenya na BATUK iwajibike zaidi kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 31 Jul 2026 23:55:01

Wantam: Upinzani wakosoa ndoto mpya ya Ruto ya ustawi

VIONGOZI wakuu wa upinzani wamekosoa vikali pendekezo la Rais William Ruto la kuanzisha mwongozo mpya wa maendeleo ya taifa utakaofuata Ruwaza ya 2030, wakisema serikali inajaribu kubadilisha mjadala kutoka kwa matatizo yanayowakumba Wakenya kwa sasa. Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, kinara wa vuguvugu la Linda Mwananchi Seneta Edwin Sifuna, aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga na viongozi wengine walisema taifa halihitaji mpango mpya kabla ya serikali kutekeleza ahadi ilizotoa na kushughulikia changamoto za gharama ya maisha, ufisadi na utawala. Rais Ruto alitangaza kuwa kuanzia Agosti 12 ataanzisha mazungumzo ya kitaifa yatakayowaleta pamoja wataalamu, viongozi wa kisiasa, wanavyuo, wafanyabiashara, viongozi wa dini, vijana na wadau wengine ili kuandaa mwongozo mpya wa maendeleo utakaoongoza taifa hadi mwaka wa 2060. Kulingana na rais, mwongozo huo utajengwa juu ya mafanikio ya Ruwaza ya 2030 lakini pia utazingatia mabadiliko ya uchumi wa dunia, teknolojia na fursa mpya za maendeleo. Alisema lengo ni kuhakikisha Kenya inakuwa taifa lenye uchumi wa juu na viwanda imara katika miongo ijayo. Lakini Bw Gachagua alisema pendekezo hilo ni mbinu ya kisiasa inayolenga kuwafanya Wakenya wasahau matatizo ya sasa. "Si jambo la kujadiliwa kwamba rais ambaye amezamisha nchi kwenye mzigo wa madeni na anayeshuhudia uchumi ukidorora sasa anataka kutupeleka mwaka 2060. Huu ni udanganyifu wa kiuchumi unaolenga kufufua siasa zake zilizokwama," alisema. "Amekubali kuwa mfumo wake wa ufadhili wa elimu umefeli. Anapaswa pia kukubali kuwa SHA imefeli na ushuru wa nyumba umewaumiza Wakenya. Hata ruwaza hii mpya imezaliwa ikiwa imekufa," alisema. Kwa upande wake, Bw Maraga alisema hotuba ya rais haikugusia suala ambalo, kwa maoni yake, ndilo linazorotesha maendeleo nchini. "Rais hakutaja hata mara moja neno ufisadi. Kenya inapoteza mabilioni ya fedha kila siku kutokana na ufisadi. Zaidi ya Sh1 trilioni hupotea kila mwaka na pesa hizo zinaweza kubadilisha maisha ya Wakenya," alisema. Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang'i naye alipinga mpango huo akisema serikali haijatekeleza hata mapendekezo yaliyopo, yakiwemo yale ya Kamati ya NADCO. Seneta Sifuna alisema rais hawezi kutenganisha maendeleo na misingi ya Katiba.  "Katiba inaanza kwa kusisitiza demokrasia, haki za binadamu, uhuru, usawa, utawala wa sheria na haki ya kijamii. Hauwezi kuzungumzia maendeleo bila kuheshimu misingi hiyo kwanza," alisema. Kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi alisema Rais Ruto anapaswa kwanza kutoa tathmini ya utekelezaji wa Ajenda ya Mabadiliko ya Uchumi kuanzia mashiani (BETA) kabla ya kuanzisha mjadala mwingine wa maendeleo. "Wakenya bado wanasubiri kuona matokeo ya ahadi za mwaka 2022. Serikali ichapishe ripoti ya mafanikio yake badala ya kubadilisha mjadala," alisema. Aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Amerika Elkanah Odembo alisema Kenya haina uhaba wa sera za maendeleo bali tatizo kuu ni utawala mbaya. Kwa mujibu wake, Ruwaza ya 2030 tayari ina mapendekezo mengi mazuri ambayo hayajatekelezwa ipasavyo kutokana na changamoto za uongozi. Naye Mweka Hazina wa ODM Timothy Bosire alisema ufisadi umeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya taifa. Alisema iwapo serikali itadhibiti ufisadi na kuhakikisha taasisi za umma zinafanya kazi kwa uhuru, Kenya inaweza kufikia maendeleo bila kuhitaji mwongozo mwingine mpya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 31 Jul 2026 22:55:56

Orengo amrai Jumwa aingie wantam baada ya kumtema Ruto

KIONGOZI wa vuguvugu la Linda Mwananchi, Bw James Orengo, amemkaribisha rasmi aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Jinsia, Bi Aisha Jumwa, kujiunga na upinzani katika juhudi za kumuondoa Rais William Ruto mamlakani kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2027. Bw Orengo alisema kujiunga kwa Bi Jumwa kutaimarisha ushawishi wa vuguvugu hilo katika eneo la Pwani kutokana na tajriba na ushawishi wake wa kisiasa. Bw Orengo alisema anaheshimu uamuzi wa Bi Jumwa wa kuendelea na mashauriano kabla ya kutangaza msimamo wake wa kisiasa, lakini akasisitiza kuwa milango ya Linda Mwananchi iko wazi kwake. Hata hivyo, aliongeza kuwa iwapo Bi Jumwa ataamua kujiunga na vuguvugu hilo, atapewa nafasi ya juu ya uongozi, huku akidai kuwa viongozi wengi wa Pwani wako tayari kuondoka UDA na kujiunga na upinzani kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027. Hatua hiyo inajiri siku moja baada ya Bi Jumwa kutangaza kujiondoa katika chama cha Rais William Ruto, akitaja kile alichodai kuwa ni vitendo visivyo vya kidemokrasia vinavyodhoofisha matakwa ya wananchi wa Kilifi. Mbunge huyo wa zamani wa Malindi alisema alifikia uamuzi huo baada ya mashauriano na wakazi wa Kilifi, kutafakari na kufanya maombi. Bi Jumwa, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa UDA, alisema kuondoka katika chama hicho halikuwa jambo rahisi kwa kuwa alitumia nguvu na kujitolea kukijenga chama hicho. Hata hivyo, kwenye mkutano na Bw Orengo, Bi Jumwa alisema bado anaendelea na mashauriano na vyama mbalimbali vya kisiasa kabla ya kutangaza msimamo wake kuhusu chama atakachotumia kuwania ugavana wa kaunti ya Kilifi mwaka 2027. "Leo nimetembelewa na Gavana James Orengo na tumekuwa na mazungumzo yenye manufaa. Nilipotoa taarifa ya kujiondoa UDA nilisema niko tayari kuzungumza na watu wenye mawazo yanayofanana na yangu kwa manufaa ya watu wa Kilifi, pwani na taifa kwa ujumla. Bado naendelea kushauriana na wananchi wa Kilifi na pwani kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, lakini ninaamini siku zijazo zitakuwa njema," alisema Bi Jumwa. Bw Orengo, ambaye pia ni Gavana wa Siaya, alisema mara tu alipopata taarifa za kujiondoa kwa Bi Jumwa kutoka UDA, aliamua kumtafuta haraka na kumshawishi kujiunga na Linda Mwananchi. "Kama kiongozi wa Linda Mwananchi, sikuona sababu ya kupoteza muda. Bi Jumwa alikuwa mmoja wa washirika wa karibu wa kinara wa ODM Raila Odinga. Kila alipokuwa akifanya mikutano ya kisiasa, Bi Jumwa alikuwa mstari wa mbele. Baba alimpa jina la Mekatilili wa Menza kutokana na ujasiri wake. Ninaamini alipo Bw Odinga anafurahia kuona tukishirikiana tena," alisema Bw Orengo. Aliwataka wakazi wa Mombasa, Kilifi, Kwale, Lamu, Tana River na Taita Taveta kumuunga mkono Bi Jumwa, akimtaja kuwa mwanasiasa shupavu, mzungumzaji mahiri na mwenye uwezo wa kuongoza. "Pwani sasa imepata kiongozi ambaye anaweza kutetea maslahi ya wananchi wake. Wapwani wengi wanaunga mkono ajenda ya mabadiliko, lakini baadhi ya viongozi wamekuwa na hofu ya kujitokeza hadharani. Uamuzi wa Bi Jumwa utawapa wengine ujasiri wa kujiunga nasi," alisema. Aliongeza kuwa Linda Mwananchi tayari imeanza kujipanga kwa uchaguzi wa 2027 na ina imani kuwa itashinda. "Tutasimama kidete kumlinda mtoto wetu wa Pwani. Bi Jumwa ni kiongozi ambaye amepitia changamoto nyingi za kisiasa lakini ameendelea kusimama imara. Tunahitaji Pwani iungane na vuguvugu letu," alisema.

read more