T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 18 Jul 2026 12:00:23

AI yatarajiwa kubadili kilimo COMESA ikihamasisha huduma za nyanjani za kidijitali kwa wakulima

AKILI Mnemba (AI) inazidi kujitokeza kama teknolojia itakayobadilisha sekta ya kilimo barani Afrika huku Soko la Pamoja la Eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) likiendesha juhudi za kuunganisha sera za kidijitali ili kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji, kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kupata huduma za nyanjani kwa urahisi. Akizungumza jijini Nairobi wakati wa mafunzo ya uhamasishaji kuhusu matumizi ya AI na teknolojia zinazoibuka, Afisa wa Mawasiliano wa Sekretarieti ya COMESA, Leonard Chitunda, alisema AI tayari inaleta mageuzi katika kilimo kupitia utoaji wa taarifa muhimu kwa wakati ufaao. Afisa huyo alisema teknolojia hiyo inasaidia wakulima kupata utabiri wa hali ya hewa, taarifa za afya ya udongo, pembejeo zinazofaa, pamoja na mwenendo wa masoko ili kufanya maamuzi bora. "AI ni teknolojia inayogusa sekta nyingi. Inaongeza uzalishaji wa kilimo, inaboresha ufuatiliaji wa tabianchi na kuongeza ufanisi katika huduma mbalimbali," alisema Chitunda. COMESA inatekeleza mpango wa Inclusive Digitalisation for Eastern and Southern Africa unaofadhiliwa na Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola 2.5 bilioni (Ksh323.7 bilioni). Kati ya fedha hizo, Dola 10 milioni (Ksh1.3 bilioni) zimetengwa kwa COMESA kuandaa sera za pamoja, viwango na kujenga uwezo wa AI na mageuzi ya kidijitali. [caption id="attachment_190224" align="aligncenter" width="300"] Afisa wa Mawasiliano wa Sekretarieti ya COMESA, Leonard Chitunda. Picha|Sammy Waweru[/caption] Kiwango kikubwa cha fedha hizo kitaelekezwa kwa nchi wanachama kuboresha miundombinu ya kidijitali na huduma za intaneti ili wakulima, hasa wa maeneo ya vijijini, waweze kupata huduma za kilimo mtandaoni. Chitunda alisema AI inasaidia kuziba pengo lililosababishwa na upungufu wa maafisa wa nyanjani kwa kuwawezesha wakulima kupata ushauri wa kitaalamu kupitia simu na majukwaa ya kidijitali. "Wakulima wanaweza kupata ushauri kuhusu mbegu bora, matumizi ya pembejeo, hali ya hewa na mifugo inayofaa kwa maeneo yao bila kumwona afisa wa nyanjani ana kwa ana," alisema. Aliongeza kuwa COMESA inaendesha utafiti wa kikanda kubaini maeneo yatakayofaidika zaidi na AI, matokeo ambayo yatatumika kuandaa mkakati wa pamoja wa matumizi ya teknolojia hiyo. Mkurugenzi wa ICT katika Idara ya Serikali ya Biashara nchini Kenya, Timothy Were, alisema AI tayari inatumika katika sekta mbalimbali ikiwemo benki, afya, usafirishaji na sasa kilimo. [caption id="attachment_190223" align="aligncenter" width="300"] Mkurugenzi wa ICT katika Idara ya Serikali ya Biashara nchini Kenya, Timothy Were. Picha|Sammy Waweru[/caption] "AI inasaidia wakulima kupata taarifa za masoko, utabiri wa hali ya hewa, tahadhari za milipuko ya wadudu na magonjwa, pamoja na ushauri wa kitaalamu unaowasaidia kupunguza hasara na kuongeza uzalishaji," alielezea. Hata hivyo, Were alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sheria na sera zinazofanana katika nchi za COMESA ili kuhakikisha usalama wa mifumo ya kidijitali na kuzuia uhalifu wa mtandaoni. Wadau wanaamini kuwa utekelezaji wa mkakati wa AI wa COMESA utaifanya teknolojia hiyo kuwa nguzo muhimu ya mageuzi katika kilimo, kwa kuboresha upatikanaji wa taarifa, kuimarisha huduma za nyanjani na kusaidia wakulima kuhimili changamoto za tabianchi huku wakifikia masoko kwa urahisi zaidi.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 57 minutes ago

Omtatah apinga kinga ya IMF na Benki ya Dunia inayowazuia kushtakiwa nchini

SENETA wa Busia Okiya Omtatah akishirikiana na wanaharakati Bernard Muchiri na Naomi Misati, wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu wakitaka sheria inayoyapa mashirika ya kifedha ya IMF na Benki ya Dunia, kinga dhidi ya mashtaka, ushuru na kufichua taarifa kuwa kinyume cha Katiba. Walalamishi wanapinga Kifungu cha Sheria ya Bretton Woods ya 1963, wakisema kimepitwa na wakati wala hakiendani na Katiba ya 2010. Kwa mujibu wa kesi hiyo, sheria hiyo inaipa serikali mamlaka makubwa ya kuingia mikataba ya kimataifa ya kifedha, kukopa fedha na kutumia hazina ya umma bila usimamizi wa kutosha wa Bunge. Aidha, sheria hiyo inalinda IMF na Benki ya Dunia dhidi ya kuwajibishwa katika mahakama za Kenya. Wanadai kuwa Kifungu cha tano cha sheria hiyo kinazipa taasisi hizo kinga dhidi ya kushauri mahakama, ushuru, ukaguzi, kutwaliwa kwa mali, jambo ambalo linawanyima Wakenya haki ya kupata haki, kusikilizwa kwa usawa na kupata taarifa. Aidha, wanasema sheria hiyo inaruhusu serikali kutekeleza mikataba ya kimataifa bila idhini ya Bunge na kutoa fedha kutoka Hazina Kuu ya Fedha moja kwa moja kwa IMF na Benki ya Dunia bila kuidhinishwa kila mwaka na wabunge. Bw Omtatah na wenzake wanaeleza kuwa hali hiyo inadhoofisha mamlaka ya Bunge na Mahakama katika kusimamia matumizi ya fedha za umma. Pia inakiuka masharti mbalimbali ya Katiba, pamoja na sura inayohusu usimamizi wa fedha za umma. Mahakama Kuu imewaagiza washtakiwa na wahusika wengine kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 14. Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 29, 2026, kwa mwelekeo zaidi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

Serikali yasema imepata shamba la kuzipa makao familia 21,000 zilizofurushwa Mau

SERIKALI inakaribia kutatua moja ya migogoro ya muda mrefu katika Bonde la Ufa baada ya kuthibitisha kuwa imepata mashamba makubwa katika Kaunti ya Narok ili kuzipa makazi mapya familia zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau pamoja na watu wengine wasio na ardhi. Hatua hiyo inalenga kumaliza mateso ya zaidi ya familia 21,000 zilizofurushwa katika oparesheni mbalimbali za serikali ndani ya kipindi cha miaka 21 iliyopita. Tangazo hilo linajiri huku Rais William Ruto akitarajiwa kuzuru Kusini mwa Bonde la Ufa mwezi ujao. Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alisema serikali iko katika hatua za mwisho za kuwafidia waathiriwa wa Mau na kuwapa makazi mapya waliokosa ardhi katika Kaunti ya Narok. Akizungumza Kapkwen, Kaunti ya Bomet, alisema Wizara ya Ardhi inakamilisha taratibu za mwisho na kwamba orodha ya walionufaika itatangazwa hivi karibuni. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dkt Paul Kipronoh Ronoh, pia alisema maagizo ya Rais Ruto ya kuwahamisha waathiriwa hao tayari yanatekelezwa. "Serikali imefanikiwa kupata ardhi ya kuhamishia familia zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau katika maeneo ya Narok Kusini na Narok Magharibi pamoja na watu wasio na ardhi Angata Barikoi, eneobunge la Kilgoris," akasema. Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, alisema serikali tayari imelipia baadhi ya mashamba hayo na hatimiliki zimekabidhiwa Wizara ya Ardhi. Pia alisema serikali iko katika hatua za mwisho za kununua zaidi ya ekari 5,000 zinazomilikiwa na familia ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, marehemu Isaiah Cheluget, katika eneo la Tendwet, Narok Magharibi. Kwa mujibu wa Seneta huyo, uhakiki wa majina ya waathiriwa umekamilika na serikali sasa inakamilisha utaratibu wa kugawa fidia na ardhi. Suala la kufurushwa kwa wakazi wa Mau limekuwa ajenda ya kisiasa kwa zaidi ya miongo miwili. Tangu 2005, marais na wagombea mbalimbali wameahidi kuwafidia na kuwapa makazi mapya walioathiriwa, lakini ahadi hizo zimekuwa zikicheleweshwa. Katika muhula wa pili wa Rais Uhuru Kenyatta, maelfu ya familia zilifurushwa tena kutoka maeneo yanayopakana na msitu, huku nyumba, mashamba na mali nyingine zikiharibiwa katika operesheni iliyoongozwa na aliyekuwa Kamishina Ukanda wa Bonde la Ufa George Natembeya. Rais Ruto amesema serikali yake tayari imelipa familia 2,000 fidia ya Sh300,000 kila moja na imeahidi kuwahamisha jumla ya familia 12,000 ili ziishi maisha ya kibinadamu. Hata hivyo, baadhi ya viongozi na wakazi wanasema kiwango hicho cha fedha hakitoshi kununua ardhi wala kujenga nyumba. "Kiasi cha Sh300,000 hakitoshi hata kununua kiwanja, sembuse kujenga nyumba. Watu walipoteza mashamba, mifugo, mazao na mali nyingine. Wanastahili fidia ya haki," alisema kiongozi wa eneo hilo Johnstone Kiptanui. Seneta wa Narok Ledama Ole Kina, ambaye hapo awali aliunga mkono kufurushwa kwa wakazi hao ili kulinda msitu, sasa anasema wakati umefika serikali iwape makazi mapya na fidia kwa kuwa lengo la kuhifadhi Msitu wa Mau. Hatua ya serikali ya kuharakisha mpango huo inachukuliwa kuwa jaribio la kumaliza mgogoro ambao umeathiri maelfu ya familia na umekuwa ukitumiwa kama ajenda ya kisiasa katika kila uchaguzi mkuu tangu 2007.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Mawaziri wa Ruto wazozana Wahome akimponda Duale, Kindiki naye akimkemea Ruku

UHASAMA mkali unaendelea kulikumba Baraza la Mawaziri la Rais William Ruto huku mawaziri wake wakijibizana hadharani na kuibua maswali kuhusu uwezekano wa kutekeleza mabadiliko kuelekea kura ya 2027. Licha ya Rais Ruto kusema akiwa kituo cha kibiashara cha Amagoro, Teso, Busia kuwa hajaanza siasa, mawaziri wake wanaendelea kuzozana huku malumbano yao yakichukua mkondo wa siasa za kikabila. Uhasama wa ndani kwa ndani umeibua maswali kuhusu uwezo wa baraza hilo la mawaziri kuwajibikia Wakenya ipasavyo, miezi 12 kabla ya kura kuwadia. Tukio la hivi punde ni majibizano makali kati ya Waziri wa Afya Aden Duale na Waziri wa Ardhi Alice Wahome kuhusu matamshi ambayo Bw Duale anadaiwa kutoa dhidi ya jamii ya Mlima Kenya. Aidha, Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki ametofautiana vikali na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku kuhusu Mlima Kenya Mashariki kutengana na Magharibi na kujiamulia kivyake mustakabali wake wa kisiasa. Kwenye video ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii, Bw Duale akiongea kwa lugha ya mama, anadaiwa kulinganisha jamii ya Agikuyu na ya Wasomali kwa kutumia idadi yao nchini huku akidai jamii yake ya Wasomali imekuwa ikibaguliwa na tawala zilizopita za marais Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta wote huku nyingine zikinufaika. Akiongea katika Kaunti ya Mandera, Bw Duale alilinganisha jamii ya Agikuyu na fisi ambaye hutaka kula kila kitu isitake jamii nyingine zinufaike kwa miradi ya serikali. Katika video hiyo, Bw Duale alimshukuru Rais Ruto kwa kumaliza kile alichosema ni uongozi ambao umekuwa ukipendelea jamii moja na kubagua jamii nyingine. Waziri wa Ardhi, Alice Wahome ni kati ya viongozi kutoka Ukanda wa Mlima Kenya ambao sasa wanataka Bw Duale aombe msamaha kwa kauli yake. Waziri huyo tayari amesema hawezi kuomba msamaha kwa sababu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amewahi kuyatoa matamshi yanayoweza kufasiriwa kama ya kikabila lakini hajawahi kuchukuliwa hatua zozote. Vilevile Bw Duale amesema kuwa hatafika mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) iwapo Bw Gachagua hatafanya hivyo kwanza. "Makosa mawili hayafanyi jambo liwe sawa na ni mpumbavu tu ndiye asiyebadilisha fikra zake," akaandika Bi Wahome kwenye mtandao wa X. Bi Wahome ambaye alihudumu kama mbunge wa Kandara kabla ya kuteuliwa waziri, ni wa kwanza kwenye baraza la mawaziri kumshambulia Bw Duale na kumtaka aombe msamaha. Mbali na waziri huyo baadhi ya viongozi kutoka Mlima Kenya akiwemo Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba wamemshambulia Bw Duale kutokana na matamshi yake hayo. Waziri huyo naye amejitetea kuwa matamshi yake, 'Waraabe la-tagis bartay, ka-ridis waa ku dhib', ni methali ya Kisomali wala haikulenga jamii fulani. "Ujumbe wangu ulilenga kuhakikisha kuna umoja jinsi ambavyo serikali imekuwa ikifanya bila kujali dini au kabila," akasema Bw Duale. "Nilenga kuonyesha ugumu wa kumalizwa kwa mtindo ambao upande mmoja umekuwa ukinufaika kwa kipindi kirefu. Sikulenga jamii yoyote au kumdunisha yeyote. Kuna jaribio la kufasiri matamshi yangu visivyo," akasema. Uhasama mwingine ulioonekana wazi katika baraza la mawaziri ni ule kati ya Prof Kindiki na Bw Ruku kuhusu Mlima Kenya Mashariki kuwa na mwelekeo wa kisiasa 2027. Mlima Kenya Mashariki una kaunti za Embu, Tharaka-Nithi, Meru na sehemu ya kaunti za Kirinyaga na inakadiriwa itakuwa na karibu kura milioni mbili mnamo 2027. Eneo hili limekuwa likipiga kura kwenye kapu moja na wenzao wa Nyandarua, Murangá, Nyeri, Kiambu, Laikipia na Nakuru. Bw Ruku anasema mtindo huu umefanya wabaguliwe na hata sasa wanaonewa gere kwa kushikilia wadhifa wa Naibu Rais. "Mimi siwachukii Wakikuyu lakini lazima tufurahie utambulisho wetu. Tulikuwa na majenerali waliopigania uhuru wa nchi kutoka Mlima Kenya Mashariki ndiyo maana tuliwaunga Jomo Kenyatta, Kibaki na Uhuru," akasema mnamo Juni 30 katika ibada ya Kanisa Kaunti ya Kiambu. "Haiwezekani kuwa mwana wa kiume kutoka Mlima Kenya Mashariki akifanya kazi na Rais Ruto basi viongozi wa Mlima Kenya Magharibi wanatuambia serikali ni mbaya na tunafaa kutoka. Hatutatoka," akaongeza Bw Ruku. Hata hivyo, Naibu wa Rais alionekana kumkemea siku chache baadaye akisema eneo hilo limeungana kwa kipindi kirefu na linastahili kuendelea kufanya hivyo. "Sitaki watu wazungumze lugha tofauti kwa sababu tumefanya mambo mengi pamoja, tuna historia pevu na hakuna kitu ambacho kitatutenganisha," akasema Prof Kindiki mnamo Julai 19 wakati wa ibada katika Kaunti ya Embu. Aidha, Prof Kindiki alikiri kuwa anajikuna kichwa kuhusu unaibu rais ambao unamezewa mate na viongozi wengine kama Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya lakini akasisitiza hawabanduki serikalini. "Najua tumeongezeka akina Oparanya wamekuja lakini hatuondoki, tutang'ang'ana hapa ndani," akasema Kindiki. Wikendi iliyopita, Prof Kindiki aliwachemkia viongozi ambao wanamezea mate wadhifa wake na kumsawiri kama asiyefaa kushikilia wadhifa huo. "Serikali haiwezi kuwa mzuri wakati naibu rais akitoka upande wao na ni mbaya akitoka hapa. Wakati Uhuru alikuwa rais tulimuunga mkono na hatuwezi kubali jamii ya eneo hilo liongee lugha tofauti," akasema Profesa Kindiki. "Ni haki yao kuenda mahali wameenda lakini upande wao wamepangana na namba zote zimeenda na tuko namba 20. Rais Ruto akimaliza muhula wake urais utakuja pande hii," akasema. Wikendi viongozi wa ODM kutoka Nyanza na Magharibi walisisitiza kuwa UDA ikiwahi urais naye mgombeaji mwenza anastahili kutoka chama hicho cha chungwa. "Watu wakuje pole pole na wajue kwamba huwezi kuruka laini. UDA ikipata urais, sisi lazima tupate naibu rais na huyo ni Oparanya," akasema Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed wikendi akiwa Kakamega. Kwa mujibu wa Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Profesa Lumala Masibo ni wazi kuwa baraza la mawaziri lina vita vya ndani kwa ndani hasa baada ya Profesa Kindiki kuonekana kuanza kuridhiana na Bw Gachagua. "Baadhi sasa wanamwona kama anayejipanga kivyake na hata alivyoongea wikendi, anaonekana kama mtu ambaye si mtiifu sana kwa Rais tena. Anaweza aje kudai unaibu rais utasalia kwake ilhali si anayeteua mshikilizi wa nafasi hiyo," akasema Profesa Masibo. Kauli yake inatokana na hatua ya Bw Gachagua kuwaamrisha viongozi wanaoumuunga mkono wasimshambulie Profesa Kindiki bali wamlenge Rais Ruto moja kwa moja. "Baada ya Ol Kalou ni dhahiri kuwa Rais amepoteza Mlima Kenya na shida sasa ni kupambania nafasi ya mgombeaji mwenza. Pia baadhi ya mawaziri kutoka Mlima Kenya sasa wanajificha nyuma ya kauli ya Bw Duale kumridhisha Gachagua kwa sababu ya umaarufu wake mlimani," akaongeza.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

Prof Okumu ateuliwa mkuu mpya wa Chuo Kikuu cha Kenyatta

BARAZA la Chuo Kikuu cha Kenyatta jana lilimteua Profesa John Okumu kuwa Naibu Chansela wa chuo hicho baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa kuajiri ulioendeshwa na Tume ya Utumishi kwa Umma (PSC). Uteuzi huo ulitangazwa Jumatatu kupitia taarifa iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Profesa Clara S. Momanyi, ambaye alisema uamuzi huo ulifanywa kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu na kwa idhini ya Waziri wa Elimu. Profesa Okumu anafahamu vyema Chuo Kikuu cha Kenyatta kutokana na kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi kwa miaka mingi. Aliwahi kuwa Naibu Chansela anayesimamia Masuala ya Kitaaluma kwa miaka 10, pamoja na kushikilia nyadhifa nyingine za juu za usimamizi. Baraza lilimsifu kama msomi na msimamizi mwenye tajriba kubwa katika uongozi wa elimu ya juu, utafiti na maendeleo ya taasisi. Prof Momanyi alisema ana imani kuwa tajriba na uwezo wa Profesa Okumu katika kupanga mikakati, kusimamia taasisi na kushirikiana na wadau utasaidia kuimarisha maendeleo ya chuo hicho. "Tunamkaribisha Profesa Okumu katika nafasi hii muhimu na tunatoa wito kwa wanajamii wote wa chuo na wadau kumpa ushirikiano anaohitaji ili atekeleze wajibu wake na afanikiwe," akasema. Profesa Okumu alikuwa akishikilia wadhifa huo kwa muda tangu mwishoni mwa Januari 2026 baada ya kumrithi Profesa Paul Wainaina, aliyestaafu baada ya kuhudumu kwa miaka minane. Katika mahojiano yaliyofanywa na PSC, Profesa Okumu alipata alama 84.5, akiwashinda Profesa Stephen Odebero na Profesa Godfrey Mse. Hata hivyo, uteuzi huo ulikumbwa na changamoto za kisheria baada ya Profesa Waceke Wanjohi, Naibu Chansela wa Masuala ya Kitaaluma na mmoja wa waliowania wadhifa huo, kufikisha kesi Mahakama Kuu akidai ndiye aliyepata alama za juu zaidi na kwamba aliondolewa isivyo haki. Mnamo Aprili, Jaji Njoki Mwangi alitoa amri za muda zilizokizuia chuo kujaza nafasi hiyo hadi kesi hiyo isikizwe, huku pia akiamuru mkataba wa Profesa Wanjohi uongezwe. Mvutano huo uliibua sintofahamu kuhusu hatima ya nafasi hiyo kwa miezi kadhaa kabla ya Baraza la Chuo kuthibitisha rasmi uteuzi wa Profesa Okumu. Uteuzi huo unatarajiwa kuleta utulivu katika uongozi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta na kuweka msingi wa utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Demu anataka nimnunulie simu kabla nionje asali, inafaa hivyo kweli? Nishauri

Kuna msichana tunayependana na anataka nimnunulie simu ya bei ghali kisha anionjeshe asali. Nifanyeje? Mapenzi hayafunguliwi kwa simu bali kwa moyo. Ukianza kununua ili upendwe, utamalizia kuwa na madeni. Kaa mbali na penzi la biashara. Nilimsaidia rafiki yangu wa kike baada ya mume wake kufariki. Nilianza kumlipia ada mtoto wake kwa miaka kadhaa na nikawa karibu naye kiasi kwamba mtoto huyo alianza kuniita "Baba".  Sasa mama yake ameolewa tena na mume wake mpya amekataa mtoto huyo kuendelea kuwasiliana nami. Anasema mimi si baba yake na anataka niondoke kabisa katika maisha yao. Mtoto huyo hunipigia simu kwa siri na kuniuliza kwa nini nimemtelekeza. Mimi sijawahi kutaka kuchukua nafasi ya baba yake, lakini nimekuwa sehemu ya maisha yake kwa miaka mingi. Je, nina haki ya kuendelea kumsaidia au ni lazima nikubali kuondoka? Ulifanya jambo nzuri kwa kumsaidia mtoto, lakini msaada wa muda mrefu unaweza kujenga uhusiano wa kihisia ambao hauwezi kufutwa kwa siku moja. Hata hivyo, unapaswa kuheshimu mipaka ya familia hiyo mpya. Usimlazimishe mtoto kukutana nawe kwa siri kwa sababu hilo linaweza kumweka katika mgogoro na mama yake na baba wa kambo. Jaribu kuzungumza na mama yake kwa utulivu na kumweleza kuwa lengo lako si kuingilia ndoa yake, bali kuhakikisha mtoto huyo anaendelea vizuri. Kama mawasiliano yataendelea, yawe ya wazi na yenye heshima. Kijana wa 'Gym' sasa animezea mate Nimependa mhudumu wa gym ninakofanya mazoezi. Kila siku ananisifu na kweli naona tamaa machoni mwake. Hata ananiambia nikuje mafunzo ya kipekee. Nimechanganyikiwa. Baadhi yao hufanya kazi ya kusifu wateja ili warudi kesho. Usichukue maneno yake kama ishara ya mapenzi. Kaa macho. Ataka nimlipe kodi sababu nyumba ni yake Shangazi, niliolewa miaka mitano iliyopita. Kabla ya ndoa, mume wangu alikuwa amenunua nyumba kwa mkopo. Sasa hivi kila tunapogombana, huniambia nyumba ni yake na ninapaswa kumshukuru kwa kuniruhusu kuishi humo. Mimi pia hufanya kazi na huchangia chakula, ada za watoto na bili zote za nyumbani. Juzi aliniambia kama sitaki kuitwa mpangaji, nianze kumlipa kodi kila mwezi. Maneno hayo yameniumiza sana. Nipe ushauri. Umiliki wa mali na heshima ndani ya ndoa ni mambo mawili tofauti. Inawezekana nyumba iko kwa jina la mume wako, lakini hilo halimpi haki ya kukudhalilisha au kutumia makazi kama silaha wakati wa ugomvi. Mnapaswa kuzungumza kuhusu michango ya kila mmoja na namna mnavyotaka kusimamia mali na fedha zenu. Usijenge maisha yako kwa kutegemea maneno ya "hii ni yangu" kila mnapokosana. Pia, usikubali kutishwa bila kuelewa haki na wajibu wako.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Makosa yaliyozoeleka katika kutumia 'vivumishi safi', 'hodari' na 'nadhifu'

KIVUMISHI ni neno linalotoa habari zaidi kuhusu nomino inayozungumziwa. Kuna aina mbalimbali kama vile: vivumishi vya pekee, vivumishi vya sifa, vivumishi viashiria, vivumishi vimilikishi, vivumishi vya idadi na vivumishi viulizi. Maneno safi, hodari na nadhifu ni vivumishi vya sifa ambavyo ni kapa au tasa. Vivumishi hivyo vinapotumiwa katika sentensi huwa havichukui viambishi vya nomino au vya ngeli yoyote. Kwa hivyo havibadiliki katika kuzungumzia nomino yoyote katika umoja au wingi. Ingawa vivumishi safi, hodari na nadhifu havifai kubadilika katika wingi au kuchukua viambishi vyovyote vya nomino, kuna mazoea ya wanafunzi kutunga sentensi kama vile: *Mwanafunzi mhodari katika somo la Kiswahili alituzwa jana. *Wakulima wahodari walipata mavuno mengi. Sentensi hizi si sahihi. Isitoshe, katika matumizi ya neno safi utakumbana na sentensi kama vile: *Vikombe visafi vimetumiwa kunywea chai. *Mwanafunzi msafi anavutia. Vilevile, kivumishi nadhifu hutumiwa isivyofaa kwa kutunga sentensi kama vile: *Wanafunzi wanadhifu walisifiwa na mwalimu.Mifano hii ya sentensi ina kosa la kuvipa vivumishi kapa safi, hodari na nadhifu viambishi. Ili kuzisahihisha tunafaa kusema: Mwanafunzi hodari katika somo la Kiswahili alituzwa jana. Wakulima hodari walipata mavuno mengi. Vikombe safi vimetumiwa kunywea chai. Mwanafunzi safi anavutia. Wanafunzi nadhifu walisifiwa na mwalimu. Mwanafunzi mwenye changamoto ya kutumia vivumishi safi, hodari na nadhifu kwa usahihi katika sentensi, anafaa kufanya mazoezi ya kutunga sentensi mbalimbali akitumia viumishi hivyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

KAULI YA MATUNDURA: Ni kwa nini imani ya wananchi kwa Rais inadorora kila uchao?

JUZI, Naibu Rais Kithure Kindiki aliwakosoa viongozi wanaoshindwa kutimiza ahadi wanazotoa kwa raia. Kindiki alisema, mienendo ya kuwadanganya wananchi, na baadaye kurudi kwao (kuwaomba kura?) lazima ikomeshwe mara moja. Alisisitiza kuwa viongozi watoapo ahadi, ni sharti wahakikishe zimetimizwa kwa vitendo. Kauli ya Kindiki inasadifiana matamshi ya Rais Ruto kuhusu ufadhili wa elimu nchini. "Kuanzia sasa, mwanafunzi yeyote, mradi tu amefaulu mtihani na kuteuliwa kujiunga na taasisi au chuo kikuu, atafadhiliwa kuafikia elimu ya juu […] sasa tuna mfumo utakaomlipia kila mwanafunzi," akasema Dkt Ruto. Mpaka sasa, Wakenya wengi wanatilia shaka kauli hii ya rais kwa misingi kwamba, ahadi nyingi alizowahi kutoa mbeleni hazijawahi kutimizwa mpaka sasa. Hali hii imesababisha kupungua kwa imani ya wananchi katika serikali. Data kutokana na asasi za Utafiti ya TIFA inadokeza kwamba, Wakenya wengi hawamwamini Rais Ruto. Kwa nini? Kwanza, tathmini inaonesha katika mamia ya ahadi alizotoa wakati wa kampeni kutangulia uchaguzi mkuu 2022, ni chache tu zilizokwisha kutimizwa. Hali hii imewatamausha wananchi. Pili, serikali inawatoza wananchi kiasi kikubwa cha ushuru. Hatua hii inakera kwa sababu Rais alipokuwa akisaka urais, alijisawiri kama mtetezi wa wanyonge na watu wa kipato cha chini. Alijinasibisha sana na mahasla, na kushabikiwa sana kwa mfumo wa kiuchumi wa Bottom – Up. Alivunja ahadi hii pindi alipotwaa mamlaka. Rais anatoa ahadi za kufadhili kikamilifu wanafunzi wa vyuo vikuu katika kipindi ambapo Taasisi ya Utoaji wa Mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu (HELB) ina nakisi ya takriban Sh57.65 bilioni. Kosa jingine ambalo yamkini analifanya Rais Ruto ni kujinaki kwamba kwa vyovyote vile, atashinda kwenye uchaguzi mkuu wa 2027. Huenda hajagundua, umaarufu aliokuwa nao 2022 unapungua kila uchao kwa sababu anasema sana kuliko anavyotenda. Katika kughairi misimamo yake mikali kuhusu sera zilizowaumiza wananchi zikiwemo kukubali kubadilisha mfumo wa ufadhili wa wanafunzi katika vyuo vikuu, yaelekea Rais Ruto anatumia mbinu ya Saikolojia kinyume (Reverse psychology). Hii ni mbinu ya kiushawishi ambapo mtu hutetea jambo lililo kinyume kabisa na kile anachokitaka, akitarajia mtu au watu wengine kupinga pendekezo lake, na badala yake kufanya jambo unalolitaka hasa. Kwa mfano: Ni kweli kwamba serikali haijui magenge au wahuni wanashirikiana na polisi kuhangaisha wananchi? Itakuwa hatari kwa Rais Ruto kuendelea kutoa ahadi hewa kwenye kampeni kutangualia 2027. Utekelezaji utafaa zaidi. Bitugi Matundura ni mhadhiri

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Mume amlaghai mkewe mwanatenisi mabilioni ya pesa

ALIYEKUWA nyota wa tenisi nchini Uhispania, Arantxa Sanchez Vicario, amemlaumu mume wake wa zamani baada ya kupoteza utajiri wake wa Sh5.4 bilioni. Bingwa huyo mara nne wa Grand Slam mwenye umri wa miaka 54, aliolewa na mjasiriamali Josep Santacana kati ya 2008 na 2019. Arantxa na Santacana walikuwa na mtoto wa kiume na wa kike pamoja. Kupitia kipindi cha televisheni cha Universo Callejo nchini Uhispania, Arantxa alisema hivi kuhusu mumewe wa zamani: "Nilimwamini kwa sababu alikuwa baba wa watoto wangu. Nilimpenda kipofu na sikudhania ni mtu mbaya sampuli hiyo. Kumbe alikuwa laghai, mdanganyifu na tapeli." Arantxa na Santacana walifikishwa mahakamani mwaka wa 2023 wakituhumiwa kuficha mali ili kuepuka kulipa deni wanalodaiwa na Benki ya Luxembourg. Mwanatenisi huyo mstaafu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na kuamriwa kulipa deni la thamani ya Sh957 milioni. Alipoulizwa kuhusu jinsi alivyopoteza mapato yake ya kazi, ya takriban Sh5.4 bilioni, Arantxa aliongeza: "Ni kweli, hicho ndicho kiasi kilichoonekana na vyombo vya habari. Nilizingatia sana kucheza tenisi na sikuwahi kushughulikia masuala yangu ya kifedha kwa sababu nilimwamini sana mume wangu. Ndiye aliyetoweka na mabilioni yangu yote huku nikiachwa na mzigo mkubwa." Kuhusu namna alivyofaulu kuepuka kifungo, aliongeza: "Sikuenda jela kwa sababu ninalipa asilimia 50 ya mapato yangu kama sehemu ya mkopo wa benki. Kumbe nilikuwa na mume laghai. Ilinibidi kwenda kwenye matibabu kwa sababu sikuamini alichonifanyia. Kwa wakati fulani niliona tukio hilo likiwa kama ndoto." Arantxa alishinda mataji matatu ya French Open na ndiye mchezaji wa kwanza kuwahi kufanya hivyo akiwa na umri wa miaka 17 pekee. Mhispania huyo pia alishinda US Open mnamo 1994, pamoja na kufika fainali nyingi za Australian Open na Wimbledon. Aliorodheshwa nambari moja duniani mnamo 1995, na pia aliwakilisha nchi yake kwenye makala matano ya Olimpiki. Nyota huyo mzaliwa wa Barcelona alistaafu mnamo 2002. Sanchez Vicario pia alijaribu mkono wake katika ukocha na aliwahi kumnoa mwanatenisi Caroline Wozniacki aliyewahi kushikilia nambari ya kwanza duniani mnamo 2015.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Vijana waingizwa katika biashara za ngono ajira ikiadimika nchini

UKOSEFU wa ajira unaozidi kushuhudiwa nchini umeanza kuwasukuma vijana wengi kuingia katika biashara haramu huku baadhi wakitumbukia kwenye mitandao ya utengenezaji wa filamu za ngono zinazouzwa kwa wateja wa mataifa ya kigeni. Katika mwezi mmoja uliopita pekee, maafisa wa polisi wamevamia nyumba kadhaa katika kaunti za Kiambu, Nairobi, Kajiado na Nakuru na kuwaokoa zaidi ya wanawake 50 waliokuwa wakidaiwa kulazimishwa kutengeneza filamu za ngono. Hii ni baada ya kudanganywa kwa ahadi za ajira zenye mishahara minono. Wiki nne zilizopita, polisi walivamia nyumba moja eneo la Ngoigwa, Thika, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wakazi. Vijana kadhaa wenye umri wa kati ya miaka 18 na 30 walikamatwa wakishukiwa kutengeneza filamu za ngono zilizokusudiwa kuuzwa katika masoko ya nje ya nchi. Polisi walinasa kompyuta, kamera na vifaa vingine vilivyokuwa vikitumiwa kurekodi filamu hizo. Miezi michache kabla ya hapo, maafisa wa Idara ya Upelelezi (DCI) walivunja mtandao mwingine jijini Nakuru baada ya kuvamia sherehe ya ngono katika eneo la Naka Estate. Mfanyabiashara mmoja alikamatwa akishukiwa kuwavutia vijana, wakiwemo wasichana wa shule wenye umri wa miaka 13 hadi 17, kushiriki katika kurekodi filamu ya ngono zilizokuwa zikununuliwa barani Ulaya. Mnamo Julai 21, DCI iliwaokoa wanawake watano waliokuwa wakizuiliwa katika nyumba moja eneo la Mihang'o, Embakasi Mashariki, Nairobi. Uchunguzi ulionyesha kuwa walikuwa wameahidiwa kazi zenye mishahara mizuri lakini badala yake wakalazimishwa kutengeneza filamu ya ngono kwa ajili ya biashara ya mtandaoni. "Waathiriwa walidanganywa kwa ahadi za ajira zenye mapato mazuri lakini wakageuzwa watumwa wa kutengeneza filamu ya ngono kwa manufaa ya biashara," akasema Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin. Siku tatu baadaye, polisi waliwaokoa wanawake wengine 48 katika maeneo ya Ongata Rongai na Kiserian, Kaunti ya Kajiado, walikokuwa wakishikiliwa na magenge mawili yanayoshukiwa kujihusisha na biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu na unyanyasaji wa kingono. Moja ya nyumba hizo ilikuwa imegeuzwa studio ya kisasa ya kamera za mtandaoni yenye kompyuta, kamera na vifaa vya kurusha matangazo ya moja kwa moja kwa wateja wa ng'ambo. Kwa mujibu wa wachunguzi, magenge hayo huwavutia vijana wasiokuwa na ajira kwa matangazo ya kazi kama watayarishaji wa filamu, wapiga picha, wanamitindo, wasaidizi wa masoko ya kidijitali au wafanyakazi wa nyumbani. Wakishakubali kazi hizo, huzuiliwa katika nyumba za kupanga na kulazimishwa kushiriki katika biashara hiyo haramu. "Magenge haya yanatumia ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha kama silaha. Vijana huahidiwa mishahara mikubwa, safari za nje ya nchi na nafasi za kazi, lakini baadaye hulazimishwa kutengeneza filamu za ngono," akasema afisa mmoja mkuu wa DCI aliyeomba kutotajwa. Maafisa wa upelelezi pia wamebaini kuwa baadhi ya washukiwa hutuma fedha kupitia simu au zawadi za thamani ili kujenga uaminifu kwa waathiriwa kabla ya kuwalazimisha kutuma picha na video za ngono. DCI imesema mitandao hiyo sasa inaendesha shughuli zake katika miji ya Nairobi, Nakuru, Kisumu, Eldoret na Thika. Imetoa wito kwa vijana kuwa waangalifu wanapotafuta ajira na kuhakikisha wanathibitisha waajiri kabla ya kukubali ofa yoyote.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Hofu tele mauaji ya usiku yakitanda vijijini Kwale

WAKAZI wa vijiji vinavyopakana na misitu iliyo Mangawani, Kaunti ya Kwale, wanaishi kwa hofu ya mashambulio ya kihalifu ambayo yametanda kwa miaka kadha. Wakazi hao wameeleza hofu kutokana na mfululizo wa mauaji ya kikatili na wizi unaodaiwa kufanywa na genge la wahalifu ambalo hufanya mashambulio usiku na kutoweka katika misitu inayozunguka vijiji hivyo. Kulingana nao, washambuliaji hao hujitokeza kati ya saa mbili na saa tatu usiku, wakiwavamia watu wanaorejea nyumbani kutoka shughuli zao za kila siku. Wakiwa wamejihami kwa mapanga, washambuliaji hao hudaiwa kuwajeruhi au kuwaua waathiriwa kwa haraka kabla ya kutoweka ghafla. Bw Kisilu Mbai, 86, alisema kutokujulikana kwa wahusika wala nia yao ni jambo la kutisha sawa na mauaji yenyewe. "Inashangaza kuwa wahusika hawawezi kupatikana. Tumekuwa tukisihi serikali itusaidie kuwapata, ili angalau tujue ni kina nani," anasema. Katika vijiji 17 vya Mangawani na maeneo jirani, baadhi ya wakazi wanaamini wahalifu hao hujificha katika misitu, huku wengine wakishuku kuwa ni watu kutoka maeneo ya nje wanaoingia vijijini kupanga mashambulizi kabla ya kutoroka. Mauaji hayo pia yamehusishwa na migogoro ya kifamilia, mizozo ya urithi na uhasama wa muda mrefu wa kijamii, ingawa madai hayo hayajathibitishwa. Bw Jacob Mwanzia anasema familia yake ilivunjika moyo baada ya nyanya yake kupatikana ameuawa. "Hatuelewi nia ya washambulizi. Inaonekana wao hunuia tu kuua," akasema. Kulingana na wazee wa vijiji, mashambulizi hayo hujitokeza kwa vipindi vya miezi kadha. Wakati huo, wazazi huwazuia watoto kutoka nje baada ya giza kuingia, makanisa hupunguza shughuli za usiku na waendesha bodaboda hufunga kazi mapema. Mauaji hayo yameambatana na wizi wa mara kwa mara. Makanisa yameripotiwa kuvamiwa na kuibiwa vifaa vya matangazo, vyombo vya muziki, vifaa vya umeme na sadaka. Pia, pikipiki, vifaa vya nyumbani na zana za kilimo zimeibwa. Chifu Msaidizi wa Mangawani, Bw Salim Nzala anasema wamepokea ripoti za mauaji matatu tangu Desemba 2025, huku uchunguzi ukiashiria zaidi migogoro ya kifamilia. "Visa vingi tulivyopokea viliwasilishwa kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu. Kilichosalia kwetu ni kuhakikisha kuna ushirikiano. Kwa hivyo wakazi wasilalamike kwamba serikali haijali, kwa sababu masuala yao yanashughulikiwa," akasema. Serikali imeanzisha kituo cha polisi Mangawani, imeongeza doria na kuandaa mikutano ya umma ili kuwahimiza wakazi kutoa taarifa. Hata hivyo, wakazi wanataka hatua zaidi, wakisema misitu na barabara duni huwapa wahalifu nafasi ya kutoroka. Kamanda wa Polisi wa eneo la Pwani, Bw Ali Nuno anasema hali ya usalama katika eneo zima kwa jumla imeimarika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 27 Jul 2026 00:55:58

Ker Odungi Randa atetea uamuzi wa Baraza la Waluo kuimba 'Tutam'

BARAZA la Wazee la Waluo limetetea uamuzi wake wa kushiriki masuala ya kisiasa, likisema hali ya sasa inalazimu wazee kutoa mwongozo kwa jamii badala ya kusalia kimya. Akizungumza katika Ukumbi wa Ofafa jijini Kisumu, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Ker Odungi Randa, alisema wazee walifikia uamuzi huo baada ya mashauriano ya ndani na kubaini kuwa hawawezi tena kunyamaza kuhusu masuala yanayoathiri jamii ya Waluo. "Sisi kama wazee ni alama ya mwongozo. Tunapoona mambo hayaendi sawa, tuna wajibu wa kutoa mwelekeo," akasema huku akisisitiza kuwa baraza linaendelea kuunga mkono Serikali Jumuishi ya Rais William Ruto. Bw Randa pia aliwataka viongozi wa Luo kukoma kushambuliana hadharani akisema migawanyiko ya ndani hupunguza nguvu ya jamii katika majadiliano ya kisiasa na kuwapa nafasi watu wa nje kutumia tofauti hizo kwa manufaa yao. Kauli yake ndiyo utetezi mkubwa zaidi ambao baraza hilo limewahi kutoa kuhusu kuhusika kwake katika siasa. Kwa miaka mingi, baraza lilikuwa likisisitiza kuwa jukumu lake ni kuhifadhi utamaduni wa Waluo, lakini msimamo huo umebadilika kufuatia mabadiliko ya kisiasa ndani ya jamii. Mnamo Julai 2024, baraza liliwahimiza viongozi wa upinzani kufanya mazungumzo yaliyofanikisha kuundwa kwa Serikali Jumuishi. Baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga mnamo 2025, Ker Randa aliwahimiza Waluo kuendeleza mkondo wa kisiasa ulioanzishwa na marehemu. Mnamo Mei mwaka huu, baraza lilimuunga mkono hadharani Rais Ruto kuwania muhula wa pili katika mkutano uliofanyika Kisumu na kuhudhuriwa na viongozi wa ODM. Tamko hilo linakuja wakati ODM inakabiliwa na migawanyiko kufuatia kifo cha Raila. Mrengo unaoongozwa na Seneta wa Siaya Oburu Oginga unaunga mkono ushirikiano na Rais Ruto, huku ule unaoongozwa na Gavana wa Siaya James Orengo ukipinga ushirikiano huo na kudai serikali inaingilia shughuli za chama. Hapo awali, Orengo amesema Baraza la Wazee wa Waluo haliwezi kuwa mpatanishi huru kwa kuwa tayari limeegemea upande mmoja kisiasa. Hata hivyo, baraza limekataa madai kwamba limeacha wajibu wake wa kitamaduni, likisema kutoa mwongozo nyakati za sintofahamu ni sehemu ya jukumu lake kama mlezi wa mila na maadili ya Waluo. Wazee hao pia walidokeza kuwa hivi karibuni watamtangaza mlezi mpya wa baraza hilo baada ya kifo cha Raila Odinga, huku wakithibitisha kuwa tamasha la kitamaduni la Piny Luo litafanyika Kisumu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 26 Jul 2026 23:55:41

Aladwa: Nitakuwa debeni na ODM lazima iungwe mkono kiti cha ugavana Nairobi

BAADHI ya viongozi wa ODM jijini Nairobi wamekataa wazo la kugawana nyadhifa za kisiasa na UDA kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, wakisisitiza kuwa ODM ndiyo inafaa kutoa mgombeaji wa ugavana wa Nairobi. Wakiongozwa na Mwenyekiti wa ODM Nairobi ambaye pia ni Mbunge wa Makadara, George Aladwa, viongozi hao walisema chama hicho kimekubaliana kumuunga mkono Rais William Ruto na Naibu wake Profesa Kithure Kindiki katika azma yao ya kutetea viti vyao mnamo 2027. Kwa hivyo ODM inastahili kupewa nafasi ya kuwania ugavana wa Nairobi na iungwe mkono na wanasiasa wa vyama vingine tanzu ndani ya Kenya Kwanza. "Kiti cha ugavana wa Nairobi lazima kibaki ODM na hakuna njia ya mkato kuhusu hilo. Tumesema tutamuunga mkono Rais Ruto na Naibu wake katika uchaguzi ujao. Hatutaki siasa za ugavi wa nyadhifa katika ngome za ODM," alisema Bw Aladwa. Mbunge huyo pia alitangaza rasmi nia yake ya kuwania ugavana wa Nairobi. "Nimeijenga na kuihudumia ODM kwa miaka mingi pamoja na marehemu Raila Odinga. Wale wanaopanga kujiunga na chama wawe tayari kwa mchujo. Madiwani na wajumbe wengi wako nyuma yangu, na mchujo utakuwa wa haki na uwazi," akaongeza. Bw Aladwa pia alimtetea Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, akimtuhumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuwashambulia viongozi ambao anajua hawatajibu matamshi yake hadharani. "Kanja alipitia taratibu zote za kuajiriwa na akathibitishwa kisheria. Gachagua aache kusambaza propaganda na amruhusu afanye kazi yake bila kuingiliwa," alisema. Viongozi hao walimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen kuchukua hatua dhidi ya Bw Gachagua wakidai matamshi yake yanayolenga jamii fulani yanaweza kuchochea mvutano wa kisiasa. "Akihitaji kutofautiana na Rais afanye hivyo bila kuwahusisha wananchi wengine. Anapaswa kuheshimu Rais ambaye alichaguliwa na Wakenya," akasema. Aidha, walimtetea Waziri wa Afya Aden Duale, wakisema kauli tata anazodaiwa kutoa zilifasiriwa vibaya na baadhi ya viongozi kwa ajili ya maslahi ya kisiasa. "Hakuna jamii iliyo bora kuliko nyingine nchini Kenya. Wanaomshambulia Duale wanapaswa kwanza kumkosoa Gachagua kwa matamshi yake," akasema Bw Aladwa. Bw Aladwa ndiye mgombeaji pekee wa ODM kutoka mrengo unaoongozwa na Dkt Oburu Oginga ambaye ametangaza analenga ugavana wa Nairobi. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino pia anataka ugavana ila kuna uwezekano finyu atatumia ODM kwa sababu anaegemea mrengo wa Linda Mwananchi.

read more