T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 19 Jul 2026 12:40:33

Fedha za kilimo zinufaishe wakulima wa mashamba madogo

MASHIRIKA ya kifedha yamehimizwa kubuni upya huduma za ufadhili wa kilimo ili ziambatane na hali halisi ya wakulima, vijana, wanawake wajasiriamali na masoko ya chakula badala ya kuzingatia utoaji wa mikopo pekee. Wito huo ulitolewa wakati wa mkutano wa Financing Agri-Food Systems Sustainably (FINAS) 2026 uliofanyika Nairobi chini ya kaulimbiu "Towards Sustainable Financial Architecture for Africa's Food Systems." Mkutano huo ulileta pamoja serikali, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo na wadau wa kilimo kujadili mbinu za kuwekeza katika mifumo imara ya chakula. Mkurugenzi Mkuu wa Heifer International Kenya, Wairimu Munyinyi-Wahome, alisema huduma za kifedha zinapaswa kuzingatia misimu ya uzalishaji, uwezo wa biashara, fursa za masoko na hatari zinazowakabili wakulima. [caption id="attachment_190271" align="aligncenter" width="300"] Mkurugenzi Mkuu wa Heifer International Kenya, Wairimu Munyinyi-Wahome akizungumza jijini Nairobi. Picha|Sammy Waweru[/caption] "Kwa muda mrefu tumekuwa tukihoji kama wakulima wanafaa kupewa mikopo. Swali muhimu ni kama mifumo yetu ya kifedha iliundwa kuambatana na uhalisia wa kilimo," alisema. Aliongeza kuwa mfumo bora wa kifedha unapaswa kuendana na kilimo, badala ya kulazimisha wakulima kufuata masharti magumu kama dhamana, ratiba zisizobadilika za malipo ya mikopo na historia rasmi ya mikopo. Kwenye kongamano na FINAS 2026, Heifer ilieleza kuwa imejikita katika kuunganisha ufadhili na ujuzi, kuongeza uzalishaji, kuimarisha usawa wa kijinsia katika huduma za kifedha na kusaidia vijana pamoja na wakulima wadogo kupata uwekezaji wa kibiashara. Mkurugenzi Mkuu wa Heifer Rwanda, Verena Ruzibuka, alisema ubunifu mwingi unaoanzishwa na vijana unahitaji msaada zaidi ili kukua na kuwa biashara zinazowanufaisha wakulima. "Mpango wa AYuTe Africa NextGen unaowapa wabunifu wa teknolojia za kilimo ufadhili, mafunzo, ushauri na masoko, umeonyesha jinsi ya kufadhili wakulima," alitaja. [caption id="attachment_190274" align="aligncenter" width="300"] Baadhi ya wakulima walionufaika mwaka huu 2026 kupitia mpango wa AYuTE wa Heifer Kenya ambao hulenga kupiga jeki vijana wenye bunifu mbalimbali za kilimo. Picha|Sammy Waweru[/caption] Mkurugenzi wa Ubunifu wa Fedha wa Heifer Afrika, Wangui Muna, alisema matumizi ya teknolojia na takwimu sahihi yatapunguza hatari za utoaji wa mikopo na kuongeza upatikanaji wa bidhaa za kifedha zinazofaa sekta ya kilimo. Mkutano huo pia ulitumika kuzindua Agricultural Finance Technical Working Group, kundi la kiufundi la fedha litakalosaidia kuimarisha sera na kanuni za ufadhili wa kilimo kwa kutumia ushahidi wa kisayansi. Aidha, kundi hilo linaongozwa na Kenya Bankers Association kwa ushirikiano na GIZ, FSD Kenya, Africa Guarantee Fund, Heifer International na Aceli Africa. Mkurugenzi wa Sera wa Aceli Africa, Titianne Donde, alisema taarifa na takwimu zilizopo zinapaswa kutafsiriwa kuwa sera zitakazochochea uwekezaji katika kilimo. [caption id="attachment_190275" align="aligncenter" width="300"] Heifer Interntanional inahimiza mashirika ya kifedha kubuni upya huduma za ufadhili wa kilimo ili ziambatane na hali halisi ya wakulima, vijana, wanawake wajasiriamali na masoko ya chakula badala ya kuzingatia utoaji wa mikopo pekee. Wengi wa wanaokuza kabichi ni wakulima wa mashamba madogo hivyo basi wanahitaji kupigwa jeki kifedha. Picha|Sammy Waweru[/caption] Kulingana na Wairimu Munyinyi-Wahome, Heifer itaendelea kushirikiana na wadau kubuni mifumo ya kifedha itakayowawezesha wakulima, vyama vya ushirika, wanawake na vijana kujenga biashara imara na endelevu.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Demu anataka nimnunulie simu kabla nionje asali, inafaa hivyo kweli? Nishauri

Kuna msichana tunayependana na anataka nimnunulie simu ya bei ghali kisha anionjeshe asali. Nifanyeje? Mapenzi hayafunguliwi kwa simu bali kwa moyo. Ukianza kununua ili upendwe, utamalizia kuwa na madeni. Kaa mbali na penzi la biashara. Nilimsaidia rafiki yangu wa kike baada ya mume wake kufariki. Nilianza kumlipia ada mtoto wake kwa miaka kadhaa na nikawa karibu naye kiasi kwamba mtoto huyo alianza kuniita "Baba".  Sasa mama yake ameolewa tena na mume wake mpya amekataa mtoto huyo kuendelea kuwasiliana nami. Anasema mimi si baba yake na anataka niondoke kabisa katika maisha yao. Mtoto huyo hunipigia simu kwa siri na kuniuliza kwa nini nimemtelekeza. Mimi sijawahi kutaka kuchukua nafasi ya baba yake, lakini nimekuwa sehemu ya maisha yake kwa miaka mingi. Je, nina haki ya kuendelea kumsaidia au ni lazima nikubali kuondoka? Ulifanya jambo nzuri kwa kumsaidia mtoto, lakini msaada wa muda mrefu unaweza kujenga uhusiano wa kihisia ambao hauwezi kufutwa kwa siku moja. Hata hivyo, unapaswa kuheshimu mipaka ya familia hiyo mpya. Usimlazimishe mtoto kukutana nawe kwa siri kwa sababu hilo linaweza kumweka katika mgogoro na mama yake na baba wa kambo. Jaribu kuzungumza na mama yake kwa utulivu na kumweleza kuwa lengo lako si kuingilia ndoa yake, bali kuhakikisha mtoto huyo anaendelea vizuri. Kama mawasiliano yataendelea, yawe ya wazi na yenye heshima. Kijana wa 'Gym' sasa animezea mate Nimependa mhudumu wa gym ninakofanya mazoezi. Kila siku ananisifu na kweli naona tamaa machoni mwake. Hata ananiambia nikuje mafunzo ya kipekee. Nimechanganyikiwa. Baadhi yao hufanya kazi ya kusifu wateja ili warudi kesho. Usichukue maneno yake kama ishara ya mapenzi. Kaa macho. Ataka nimlipe kodi sababu nyumba ni yake Shangazi, niliolewa miaka mitano iliyopita. Kabla ya ndoa, mume wangu alikuwa amenunua nyumba kwa mkopo. Sasa hivi kila tunapogombana, huniambia nyumba ni yake na ninapaswa kumshukuru kwa kuniruhusu kuishi humo. Mimi pia hufanya kazi na huchangia chakula, ada za watoto na bili zote za nyumbani. Juzi aliniambia kama sitaki kuitwa mpangaji, nianze kumlipa kodi kila mwezi. Maneno hayo yameniumiza sana. Nipe ushauri. Umiliki wa mali na heshima ndani ya ndoa ni mambo mawili tofauti. Inawezekana nyumba iko kwa jina la mume wako, lakini hilo halimpi haki ya kukudhalilisha au kutumia makazi kama silaha wakati wa ugomvi. Mnapaswa kuzungumza kuhusu michango ya kila mmoja na namna mnavyotaka kusimamia mali na fedha zenu. Usijenge maisha yako kwa kutegemea maneno ya "hii ni yangu" kila mnapokosana. Pia, usikubali kutishwa bila kuelewa haki na wajibu wako.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 57 minutes ago

Makosa yaliyozoeleka katika kutumia 'vivumishi safi', 'hodari' na 'nadhifu'

KIVUMISHI ni neno linalotoa habari zaidi kuhusu nomino inayozungumziwa. Kuna aina mbalimbali kama vile: vivumishi vya pekee, vivumishi vya sifa, vivumishi viashiria, vivumishi vimilikishi, vivumishi vya idadi na vivumishi viulizi. Maneno safi, hodari na nadhifu ni vivumishi vya sifa ambavyo ni kapa au tasa. Vivumishi hivyo vinapotumiwa katika sentensi huwa havichukui viambishi vya nomino au vya ngeli yoyote. Kwa hivyo havibadiliki katika kuzungumzia nomino yoyote katika umoja au wingi. Ingawa vivumishi safi, hodari na nadhifu havifai kubadilika katika wingi au kuchukua viambishi vyovyote vya nomino, kuna mazoea ya wanafunzi kutunga sentensi kama vile: *Mwanafunzi mhodari katika somo la Kiswahili alituzwa jana. *Wakulima wahodari walipata mavuno mengi. Sentensi hizi si sahihi. Isitoshe, katika matumizi ya neno safi utakumbana na sentensi kama vile: *Vikombe visafi vimetumiwa kunywea chai. *Mwanafunzi msafi anavutia. Vilevile, kivumishi nadhifu hutumiwa isivyofaa kwa kutunga sentensi kama vile: *Wanafunzi wanadhifu walisifiwa na mwalimu.Mifano hii ya sentensi ina kosa la kuvipa vivumishi kapa safi, hodari na nadhifu viambishi. Ili kuzisahihisha tunafaa kusema: Mwanafunzi hodari katika somo la Kiswahili alituzwa jana. Wakulima hodari walipata mavuno mengi. Vikombe safi vimetumiwa kunywea chai. Mwanafunzi safi anavutia. Wanafunzi nadhifu walisifiwa na mwalimu. Mwanafunzi mwenye changamoto ya kutumia vivumishi safi, hodari na nadhifu kwa usahihi katika sentensi, anafaa kufanya mazoezi ya kutunga sentensi mbalimbali akitumia viumishi hivyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

KAULI YA MATUNDURA: Ni kwa nini imani ya wananchi kwa Rais inadorora kila uchao?

JUZI, Naibu Rais Kithure Kindiki aliwakosoa viongozi wanaoshindwa kutimiza ahadi wanazotoa kwa raia. Kindiki alisema, mienendo ya kuwadanganya wananchi, na baadaye kurudi kwao (kuwaomba kura?) lazima ikomeshwe mara moja. Alisisitiza kuwa viongozi watoapo ahadi, ni sharti wahakikishe zimetimizwa kwa vitendo. Kauli ya Kindiki inasadifiana matamshi ya Rais Ruto kuhusu ufadhili wa elimu nchini. "Kuanzia sasa, mwanafunzi yeyote, mradi tu amefaulu mtihani na kuteuliwa kujiunga na taasisi au chuo kikuu, atafadhiliwa kuafikia elimu ya juu […] sasa tuna mfumo utakaomlipia kila mwanafunzi," akasema Dkt Ruto. Mpaka sasa, Wakenya wengi wanatilia shaka kauli hii ya rais kwa misingi kwamba, ahadi nyingi alizowahi kutoa mbeleni hazijawahi kutimizwa mpaka sasa. Hali hii imesababisha kupungua kwa imani ya wananchi katika serikali. Data kutokana na asasi za Utafiti ya TIFA inadokeza kwamba, Wakenya wengi hawamwamini Rais Ruto. Kwa nini? Kwanza, tathmini inaonesha katika mamia ya ahadi alizotoa wakati wa kampeni kutangulia uchaguzi mkuu 2022, ni chache tu zilizokwisha kutimizwa. Hali hii imewatamausha wananchi. Pili, serikali inawatoza wananchi kiasi kikubwa cha ushuru. Hatua hii inakera kwa sababu Rais alipokuwa akisaka urais, alijisawiri kama mtetezi wa wanyonge na watu wa kipato cha chini. Alijinasibisha sana na mahasla, na kushabikiwa sana kwa mfumo wa kiuchumi wa Bottom – Up. Alivunja ahadi hii pindi alipotwaa mamlaka. Rais anatoa ahadi za kufadhili kikamilifu wanafunzi wa vyuo vikuu katika kipindi ambapo Taasisi ya Utoaji wa Mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu (HELB) ina nakisi ya takriban Sh57.65 bilioni. Kosa jingine ambalo yamkini analifanya Rais Ruto ni kujinaki kwamba kwa vyovyote vile, atashinda kwenye uchaguzi mkuu wa 2027. Huenda hajagundua, umaarufu aliokuwa nao 2022 unapungua kila uchao kwa sababu anasema sana kuliko anavyotenda. Katika kughairi misimamo yake mikali kuhusu sera zilizowaumiza wananchi zikiwemo kukubali kubadilisha mfumo wa ufadhili wa wanafunzi katika vyuo vikuu, yaelekea Rais Ruto anatumia mbinu ya Saikolojia kinyume (Reverse psychology). Hii ni mbinu ya kiushawishi ambapo mtu hutetea jambo lililo kinyume kabisa na kile anachokitaka, akitarajia mtu au watu wengine kupinga pendekezo lake, na badala yake kufanya jambo unalolitaka hasa. Kwa mfano: Ni kweli kwamba serikali haijui magenge au wahuni wanashirikiana na polisi kuhangaisha wananchi? Itakuwa hatari kwa Rais Ruto kuendelea kutoa ahadi hewa kwenye kampeni kutangualia 2027. Utekelezaji utafaa zaidi. Bitugi Matundura ni mhadhiri

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Mume amlaghai mkewe mwanatenisi mabilioni ya pesa

ALIYEKUWA nyota wa tenisi nchini Uhispania, Arantxa Sanchez Vicario, amemlaumu mume wake wa zamani baada ya kupoteza utajiri wake wa Sh5.4 bilioni. Bingwa huyo mara nne wa Grand Slam mwenye umri wa miaka 54, aliolewa na mjasiriamali Josep Santacana kati ya 2008 na 2019. Arantxa na Santacana walikuwa na mtoto wa kiume na wa kike pamoja. Kupitia kipindi cha televisheni cha Universo Callejo nchini Uhispania, Arantxa alisema hivi kuhusu mumewe wa zamani: "Nilimwamini kwa sababu alikuwa baba wa watoto wangu. Nilimpenda kipofu na sikudhania ni mtu mbaya sampuli hiyo. Kumbe alikuwa laghai, mdanganyifu na tapeli." Arantxa na Santacana walifikishwa mahakamani mwaka wa 2023 wakituhumiwa kuficha mali ili kuepuka kulipa deni wanalodaiwa na Benki ya Luxembourg. Mwanatenisi huyo mstaafu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na kuamriwa kulipa deni la thamani ya Sh957 milioni. Alipoulizwa kuhusu jinsi alivyopoteza mapato yake ya kazi, ya takriban Sh5.4 bilioni, Arantxa aliongeza: "Ni kweli, hicho ndicho kiasi kilichoonekana na vyombo vya habari. Nilizingatia sana kucheza tenisi na sikuwahi kushughulikia masuala yangu ya kifedha kwa sababu nilimwamini sana mume wangu. Ndiye aliyetoweka na mabilioni yangu yote huku nikiachwa na mzigo mkubwa." Kuhusu namna alivyofaulu kuepuka kifungo, aliongeza: "Sikuenda jela kwa sababu ninalipa asilimia 50 ya mapato yangu kama sehemu ya mkopo wa benki. Kumbe nilikuwa na mume laghai. Ilinibidi kwenda kwenye matibabu kwa sababu sikuamini alichonifanyia. Kwa wakati fulani niliona tukio hilo likiwa kama ndoto." Arantxa alishinda mataji matatu ya French Open na ndiye mchezaji wa kwanza kuwahi kufanya hivyo akiwa na umri wa miaka 17 pekee. Mhispania huyo pia alishinda US Open mnamo 1994, pamoja na kufika fainali nyingi za Australian Open na Wimbledon. Aliorodheshwa nambari moja duniani mnamo 1995, na pia aliwakilisha nchi yake kwenye makala matano ya Olimpiki. Nyota huyo mzaliwa wa Barcelona alistaafu mnamo 2002. Sanchez Vicario pia alijaribu mkono wake katika ukocha na aliwahi kumnoa mwanatenisi Caroline Wozniacki aliyewahi kushikilia nambari ya kwanza duniani mnamo 2015.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 8 hours ago

Vijana waingizwa katika biashara za ngono ajira ikiadimika nchini

UKOSEFU wa ajira unaozidi kushuhudiwa nchini umeanza kuwasukuma vijana wengi kuingia katika biashara haramu huku baadhi wakitumbukia kwenye mitandao ya utengenezaji wa filamu za ngono zinazouzwa kwa wateja wa mataifa ya kigeni. Katika mwezi mmoja uliopita pekee, maafisa wa polisi wamevamia nyumba kadhaa katika kaunti za Kiambu, Nairobi, Kajiado na Nakuru na kuwaokoa zaidi ya wanawake 50 waliokuwa wakidaiwa kulazimishwa kutengeneza filamu za ngono. Hii ni baada ya kudanganywa kwa ahadi za ajira zenye mishahara minono. Wiki nne zilizopita, polisi walivamia nyumba moja eneo la Ngoigwa, Thika, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wakazi. Vijana kadhaa wenye umri wa kati ya miaka 18 na 30 walikamatwa wakishukiwa kutengeneza filamu za ngono zilizokusudiwa kuuzwa katika masoko ya nje ya nchi. Polisi walinasa kompyuta, kamera na vifaa vingine vilivyokuwa vikitumiwa kurekodi filamu hizo. Miezi michache kabla ya hapo, maafisa wa Idara ya Upelelezi (DCI) walivunja mtandao mwingine jijini Nakuru baada ya kuvamia sherehe ya ngono katika eneo la Naka Estate. Mfanyabiashara mmoja alikamatwa akishukiwa kuwavutia vijana, wakiwemo wasichana wa shule wenye umri wa miaka 13 hadi 17, kushiriki katika kurekodi filamu ya ngono zilizokuwa zikununuliwa barani Ulaya. Mnamo Julai 21, DCI iliwaokoa wanawake watano waliokuwa wakizuiliwa katika nyumba moja eneo la Mihang'o, Embakasi Mashariki, Nairobi. Uchunguzi ulionyesha kuwa walikuwa wameahidiwa kazi zenye mishahara mizuri lakini badala yake wakalazimishwa kutengeneza filamu ya ngono kwa ajili ya biashara ya mtandaoni. "Waathiriwa walidanganywa kwa ahadi za ajira zenye mapato mazuri lakini wakageuzwa watumwa wa kutengeneza filamu ya ngono kwa manufaa ya biashara," akasema Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin. Siku tatu baadaye, polisi waliwaokoa wanawake wengine 48 katika maeneo ya Ongata Rongai na Kiserian, Kaunti ya Kajiado, walikokuwa wakishikiliwa na magenge mawili yanayoshukiwa kujihusisha na biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu na unyanyasaji wa kingono. Moja ya nyumba hizo ilikuwa imegeuzwa studio ya kisasa ya kamera za mtandaoni yenye kompyuta, kamera na vifaa vya kurusha matangazo ya moja kwa moja kwa wateja wa ng'ambo. Kwa mujibu wa wachunguzi, magenge hayo huwavutia vijana wasiokuwa na ajira kwa matangazo ya kazi kama watayarishaji wa filamu, wapiga picha, wanamitindo, wasaidizi wa masoko ya kidijitali au wafanyakazi wa nyumbani. Wakishakubali kazi hizo, huzuiliwa katika nyumba za kupanga na kulazimishwa kushiriki katika biashara hiyo haramu. "Magenge haya yanatumia ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha kama silaha. Vijana huahidiwa mishahara mikubwa, safari za nje ya nchi na nafasi za kazi, lakini baadaye hulazimishwa kutengeneza filamu za ngono," akasema afisa mmoja mkuu wa DCI aliyeomba kutotajwa. Maafisa wa upelelezi pia wamebaini kuwa baadhi ya washukiwa hutuma fedha kupitia simu au zawadi za thamani ili kujenga uaminifu kwa waathiriwa kabla ya kuwalazimisha kutuma picha na video za ngono. DCI imesema mitandao hiyo sasa inaendesha shughuli zake katika miji ya Nairobi, Nakuru, Kisumu, Eldoret na Thika. Imetoa wito kwa vijana kuwa waangalifu wanapotafuta ajira na kuhakikisha wanathibitisha waajiri kabla ya kukubali ofa yoyote.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Hofu tele mauaji ya usiku yakitanda vijijini Kwale

WAKAZI wa vijiji vinavyopakana na misitu iliyo Mangawani, Kaunti ya Kwale, wanaishi kwa hofu ya mashambulio ya kihalifu ambayo yametanda kwa miaka kadha. Wakazi hao wameeleza hofu kutokana na mfululizo wa mauaji ya kikatili na wizi unaodaiwa kufanywa na genge la wahalifu ambalo hufanya mashambulio usiku na kutoweka katika misitu inayozunguka vijiji hivyo. Kulingana nao, washambuliaji hao hujitokeza kati ya saa mbili na saa tatu usiku, wakiwavamia watu wanaorejea nyumbani kutoka shughuli zao za kila siku. Wakiwa wamejihami kwa mapanga, washambuliaji hao hudaiwa kuwajeruhi au kuwaua waathiriwa kwa haraka kabla ya kutoweka ghafla. Bw Kisilu Mbai, 86, alisema kutokujulikana kwa wahusika wala nia yao ni jambo la kutisha sawa na mauaji yenyewe. "Inashangaza kuwa wahusika hawawezi kupatikana. Tumekuwa tukisihi serikali itusaidie kuwapata, ili angalau tujue ni kina nani," anasema. Katika vijiji 17 vya Mangawani na maeneo jirani, baadhi ya wakazi wanaamini wahalifu hao hujificha katika misitu, huku wengine wakishuku kuwa ni watu kutoka maeneo ya nje wanaoingia vijijini kupanga mashambulizi kabla ya kutoroka. Mauaji hayo pia yamehusishwa na migogoro ya kifamilia, mizozo ya urithi na uhasama wa muda mrefu wa kijamii, ingawa madai hayo hayajathibitishwa. Bw Jacob Mwanzia anasema familia yake ilivunjika moyo baada ya nyanya yake kupatikana ameuawa. "Hatuelewi nia ya washambulizi. Inaonekana wao hunuia tu kuua," akasema. Kulingana na wazee wa vijiji, mashambulizi hayo hujitokeza kwa vipindi vya miezi kadha. Wakati huo, wazazi huwazuia watoto kutoka nje baada ya giza kuingia, makanisa hupunguza shughuli za usiku na waendesha bodaboda hufunga kazi mapema. Mauaji hayo yameambatana na wizi wa mara kwa mara. Makanisa yameripotiwa kuvamiwa na kuibiwa vifaa vya matangazo, vyombo vya muziki, vifaa vya umeme na sadaka. Pia, pikipiki, vifaa vya nyumbani na zana za kilimo zimeibwa. Chifu Msaidizi wa Mangawani, Bw Salim Nzala anasema wamepokea ripoti za mauaji matatu tangu Desemba 2025, huku uchunguzi ukiashiria zaidi migogoro ya kifamilia. "Visa vingi tulivyopokea viliwasilishwa kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu. Kilichosalia kwetu ni kuhakikisha kuna ushirikiano. Kwa hivyo wakazi wasilalamike kwamba serikali haijali, kwa sababu masuala yao yanashughulikiwa," akasema. Serikali imeanzisha kituo cha polisi Mangawani, imeongeza doria na kuandaa mikutano ya umma ili kuwahimiza wakazi kutoa taarifa. Hata hivyo, wakazi wanataka hatua zaidi, wakisema misitu na barabara duni huwapa wahalifu nafasi ya kutoroka. Kamanda wa Polisi wa eneo la Pwani, Bw Ali Nuno anasema hali ya usalama katika eneo zima kwa jumla imeimarika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Ker Odungi Randa atetea uamuzi wa Baraza la Waluo kuimba 'Tutam'

BARAZA la Wazee la Waluo limetetea uamuzi wake wa kushiriki masuala ya kisiasa, likisema hali ya sasa inalazimu wazee kutoa mwongozo kwa jamii badala ya kusalia kimya. Akizungumza katika Ukumbi wa Ofafa jijini Kisumu, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Ker Odungi Randa, alisema wazee walifikia uamuzi huo baada ya mashauriano ya ndani na kubaini kuwa hawawezi tena kunyamaza kuhusu masuala yanayoathiri jamii ya Waluo. "Sisi kama wazee ni alama ya mwongozo. Tunapoona mambo hayaendi sawa, tuna wajibu wa kutoa mwelekeo," akasema huku akisisitiza kuwa baraza linaendelea kuunga mkono Serikali Jumuishi ya Rais William Ruto. Bw Randa pia aliwataka viongozi wa Luo kukoma kushambuliana hadharani akisema migawanyiko ya ndani hupunguza nguvu ya jamii katika majadiliano ya kisiasa na kuwapa nafasi watu wa nje kutumia tofauti hizo kwa manufaa yao. Kauli yake ndiyo utetezi mkubwa zaidi ambao baraza hilo limewahi kutoa kuhusu kuhusika kwake katika siasa. Kwa miaka mingi, baraza lilikuwa likisisitiza kuwa jukumu lake ni kuhifadhi utamaduni wa Waluo, lakini msimamo huo umebadilika kufuatia mabadiliko ya kisiasa ndani ya jamii. Mnamo Julai 2024, baraza liliwahimiza viongozi wa upinzani kufanya mazungumzo yaliyofanikisha kuundwa kwa Serikali Jumuishi. Baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga mnamo 2025, Ker Randa aliwahimiza Waluo kuendeleza mkondo wa kisiasa ulioanzishwa na marehemu. Mnamo Mei mwaka huu, baraza lilimuunga mkono hadharani Rais Ruto kuwania muhula wa pili katika mkutano uliofanyika Kisumu na kuhudhuriwa na viongozi wa ODM. Tamko hilo linakuja wakati ODM inakabiliwa na migawanyiko kufuatia kifo cha Raila. Mrengo unaoongozwa na Seneta wa Siaya Oburu Oginga unaunga mkono ushirikiano na Rais Ruto, huku ule unaoongozwa na Gavana wa Siaya James Orengo ukipinga ushirikiano huo na kudai serikali inaingilia shughuli za chama. Hapo awali, Orengo amesema Baraza la Wazee wa Waluo haliwezi kuwa mpatanishi huru kwa kuwa tayari limeegemea upande mmoja kisiasa. Hata hivyo, baraza limekataa madai kwamba limeacha wajibu wake wa kitamaduni, likisema kutoa mwongozo nyakati za sintofahamu ni sehemu ya jukumu lake kama mlezi wa mila na maadili ya Waluo. Wazee hao pia walidokeza kuwa hivi karibuni watamtangaza mlezi mpya wa baraza hilo baada ya kifo cha Raila Odinga, huku wakithibitisha kuwa tamasha la kitamaduni la Piny Luo litafanyika Kisumu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 10 hours ago

Aladwa: Nitakuwa debeni na ODM lazima iungwe mkono kiti cha ugavana Nairobi

BAADHI ya viongozi wa ODM jijini Nairobi wamekataa wazo la kugawana nyadhifa za kisiasa na UDA kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, wakisisitiza kuwa ODM ndiyo inafaa kutoa mgombeaji wa ugavana wa Nairobi. Wakiongozwa na Mwenyekiti wa ODM Nairobi ambaye pia ni Mbunge wa Makadara, George Aladwa, viongozi hao walisema chama hicho kimekubaliana kumuunga mkono Rais William Ruto na Naibu wake Profesa Kithure Kindiki katika azma yao ya kutetea viti vyao mnamo 2027. Kwa hivyo ODM inastahili kupewa nafasi ya kuwania ugavana wa Nairobi na iungwe mkono na wanasiasa wa vyama vingine tanzu ndani ya Kenya Kwanza. "Kiti cha ugavana wa Nairobi lazima kibaki ODM na hakuna njia ya mkato kuhusu hilo. Tumesema tutamuunga mkono Rais Ruto na Naibu wake katika uchaguzi ujao. Hatutaki siasa za ugavi wa nyadhifa katika ngome za ODM," alisema Bw Aladwa. Mbunge huyo pia alitangaza rasmi nia yake ya kuwania ugavana wa Nairobi. "Nimeijenga na kuihudumia ODM kwa miaka mingi pamoja na marehemu Raila Odinga. Wale wanaopanga kujiunga na chama wawe tayari kwa mchujo. Madiwani na wajumbe wengi wako nyuma yangu, na mchujo utakuwa wa haki na uwazi," akaongeza. Bw Aladwa pia alimtetea Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, akimtuhumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuwashambulia viongozi ambao anajua hawatajibu matamshi yake hadharani. "Kanja alipitia taratibu zote za kuajiriwa na akathibitishwa kisheria. Gachagua aache kusambaza propaganda na amruhusu afanye kazi yake bila kuingiliwa," alisema. Viongozi hao walimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen kuchukua hatua dhidi ya Bw Gachagua wakidai matamshi yake yanayolenga jamii fulani yanaweza kuchochea mvutano wa kisiasa. "Akihitaji kutofautiana na Rais afanye hivyo bila kuwahusisha wananchi wengine. Anapaswa kuheshimu Rais ambaye alichaguliwa na Wakenya," akasema. Aidha, walimtetea Waziri wa Afya Aden Duale, wakisema kauli tata anazodaiwa kutoa zilifasiriwa vibaya na baadhi ya viongozi kwa ajili ya maslahi ya kisiasa. "Hakuna jamii iliyo bora kuliko nyingine nchini Kenya. Wanaomshambulia Duale wanapaswa kwanza kumkosoa Gachagua kwa matamshi yake," akasema Bw Aladwa. Bw Aladwa ndiye mgombeaji pekee wa ODM kutoka mrengo unaoongozwa na Dkt Oburu Oginga ambaye ametangaza analenga ugavana wa Nairobi. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino pia anataka ugavana ila kuna uwezekano finyu atatumia ODM kwa sababu anaegemea mrengo wa Linda Mwananchi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Ruto amwaga miradi ya mamilioni Magharibi, Oparanya akipigiwa debe 2027

RAIS William Ruto jana alisema serikali yake itaendelea kutekeleza miradi ya mabilioni ya pesa Magharibi mwa nchi huku wabunge wanaounga serikali yake wakiahidi kuwa eneo hilo litaendelea kuunga serikali katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Kiongozi wa nchi jana alikuwa katika Kaunti ya Busia ambapo alipigia debe miradi ambayo serikali yake imetekeleza na inaendelea kutekeleza kuinua eneo hilo kimaendeleo. Kwa upande mwingine, Kiongozi wa Wachache katika Bunge, Junet Mohamed, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na wabunge wa ODM na UDA nao walishiriki mchango eneobunge la Malava ambapo walipuuza umaarufu wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Huku Rais akiwa Busia, kundi la wabunge wa chama cha ODM likiwa Magharibi nalo lilisema kuwa Bw Oparanya ndiye atakuwa mgombeaji mwenza wa Rais 2027. "Watu wakuje polepole na wajue huwezi kuruka laini na wajue kuna watu walikaa na Raila miaka na mikaka. Oparanya ndiye anatosha kutuongoza hapa Magharibi kama kiongozi wa ODM baada ya Oburu Oginga. UDA wakipata rais, sisi ODM lazima tupate naibu rais na huyo ni Oparanya," akasema Bw Mohamed. "Hii pesa yote ambayo inataka kugawanya ODM ni pesa ya Uhuru Kenyatta na ndiyo anatumia kugawa chama chetu lakini hatafaulu. Kama Uhuru alishindwa kufanya baba kuwa rais 2022 sasa ndiye atasaidia mtu yeyote, sisi hatuwezi kuelekea barabara hiyo," akaongeza mbunge huyo wa Suna Mashariki. Mbunge huyo alisisitiza kuwa ODM haitarejelea siasa za maasi na nguvu zao zote sasa ni kuhakikisha kuwa chama kitaendelea kuwa imara. Bw Oparanya alisema amekuwa na uzoefu wa siasa na hatikiswi na wimbi la Bw Sifuna huku akisema kuwa hawezi kusaliti ndoto ya marehemu Raila Odinga. "Mimi mpaka watu wamekuja kuniambia nitengeneze chama kipya lakini nikakataa. Hakuna kiongozi ambaye alikuwa na ufuasi kuliko Raila na wakati huu kama Magharibi tunaingia moja kwa moja kwa serikali ya Rais Ruto," akasema Bw Oparanya. Rais Ruto alisema eneo la Magharibi ni sehemu ya nchi wala haliwezi kuachwa nyuma huku maeneo mengine yakiendelea kupiga hatua kimaendeleo. Alitaja baadhi ya miradi ambayo serikali yake imetekeleza huku akijizuia kuzungumzia suala la umaarufu wa Sifuna. "Tulianzisha barabara ya Mundere kule Seo Port, Matayos na Funyula. Mliniuliza barabara kutoka Butula-Nambale-Amukura-Kocholia, na mwezi ujao nitakuja hapa kuanzisha barabara hiyo ya kilomita 58 kwa sababu nimepata mwanakandarasi," akasema Rais. Alikuwa akihutubu wakati wa kutawazwa kwa Askofu wa nne wa Kanisa la ACK Vitalis Job Ekuru, hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Uganda Jesca Alupe.  "Tuna reli kutoka Narok na tumesema itakuja ifike hapa Malaba ili kurahisisha usafiri. Mimi na Rais wa Uganda Yoweri Museveni tulikubaliana huu ni mradi ambao tufanya pamoja kurahisisha usafiri na kusaidia nchi zetu kuimarisha uchumi," akaongeza Rais Ruto "Kuna barabara itakayofika hapa Malaba kutoka Mau Summit. Nitakuja kuzindua barabara ya Malava-Kimaeti-Bungoma. Barabara nyingine ambazo ziko hapa Busia ambazo ni kilomita 225 zimetengewa Sh5 bilioni na serikali," akasema Rais Ruto. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Gavana Paul Otuoma, mwenzake wa Kakamega Fernandes Barasa na Kenneth Lusaka wa Bungoma miongoni mwa wabunge wengine kutoka Magharibi mwa Nchi. "Tumeweka Sh1.2 bilioni za kuongezea miradi ya stima hapa Busia. Nilikuja kuzindua soko Amagoro na tunaendelea kuwajengea masoko mengine 19 mapya kwa sababu tunataka wafanyabiashara wetu waendelee kufanya biashara mahali safi na kuna umeme," akasema "Tumetoa Sh3.6 bilioni kuwajenga wanafunzi nyumba kupitia mradi wa nyumba ili wasome mahali ambao kuna usafi na panatoshana," "Nimeona wengine wananiambia eti niondoke kwa serikali niunge mtu mwengine mkono (Sifuna) eti ataunda serikali nisiyoijua. Hao viongozi hawajui wanaenda wapi na wao watuheshimu badala ya kututusi ndipo tuwaunge mkono kwa lazima," akaongeza Bw Oparanya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 12 hours ago

Sifuna apokelewa kishujaa Magharibi, Wantam ikitanda hewani

ENEO la Magharibi limegeuka uwanja mkuu wa mapambano ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku Rais William Ruto na viongozi wa upinzani wakilenga zaidi ya milioni 3.3. Magharibi kwa sasa ina jumla ya wapigakura waliosajiliwa milioni 2.92 katika kaunti tano, na inachukuliwa kuwa ngome muhimu inayoweza kuamua mshindi wa urais. Kufikia 2027, eneo hilo lenye kaunti za Bungoma, Kakamega, Trans Nzoia, Vihiga na Busia litakuwa na zaidi ya kura milioni 3.3. Katika uchaguzi wa 2022, Rais Ruto alipata ushindi mkubwa katika Kaunti ya Bungoma kwa kura 255,906, dhidi ya kura 145,280 za aliyekuwa mpinzani wake Raila Odinga. Matokeo hayo yalimsaidia kuingia Ikulu kwa tofauti ndogo ya kura. Sasa, ikiwa zimesalia chini ya miezi 12 kabla ya uchaguzi mkuu, vita vya kuhifadhi au kurejesha kura hizo vimeanza rasmi. umapili, Kiongozi wa kundi la Linda Mwananchi na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alikamilisha ziara ya siku mbili katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia huku Rais Ruto akiwa katika Kaunti ya Busia akizindua na kukagua miradi ya maendeleo. Pande zote mbili zilijitokeza zikisisitiza kuwa zinaungwa mkono na wakazi wa Magharibi. Katika mikutano yake, Bw Sifuna aliendelea kujisawiri kama mgombeaji anayetarajia kupeperusha bendera ya upinzani katika uchaguzi wa urais wa 2027, huku akiwataka wakazi wa Magharibi wasimwache njiani. "Watu wengi wanasema mnanipigia debe tu. Mmenihimiza niende hadi kwenye debe? Msije mkaniacha njiani. Simameni nami ili nikabiliane na Rais William Ruto uso kwa macho," akasema Alisema kundi la Linda Mwananchi limezunguka maeneo mengi nchini na kupokea ahadi za kuungwa mkono. "Nimeunda kikosi imara kutoka Pwani, Mlima Kenya, Nyanza, Magharibi na maeneo mengine. Kwa mapenzi ya Mungu, ndani ya miezi 12 tutakuwa tumekamilisha safari yetu kuelekea Ikulu," akaongeza. Bw Sifuna alisema safari yake ya kisiasa ilianzia Magharibi alipojaribu kuwania ubunge wa Kanduyi kabla ya marehemu Raila Odinga kumlea kisiasa na kumwezesha kuwa Seneta wa Nairobi, Katibu Mkuu wa ODM na Kiranja wa Wachache katika Seneti. Aidha, alidai kuwa viongozi wanaomuunga mkono Rais Ruto wanampotosha kwa kumwambia anaungwa mkono Bungoma. "Kuna watu wanamdanganya Rais kuwa ana kura Bungoma. Ukweli ni kwamba hana kura hapa. Safari ya mabadiliko tayari imeanza," akasema. Ziara hiyo ilihudhuriwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na Waziri wa zamani Musikari Kombo ambaye alihudumu katika utawala wa marehemu Rais Mwai Kibaki. Tangu asubuhi, mamia ya wafuasi walifurika mjini Bungoma wakiwa na mabango yenye picha ya Bw Sifuna huku wakiimba nyimbo za jadi za Bukusu na nyimbo zilizokuwa zikitumika katika kampeni za marehemu Raila Odinga. Msafara huo ulianza kwa ibada katika Kanisa Kuu la St Immaculate mjini Kitale kabla ya kupitia Kiminini, Sikhendu, Kamukuywa, Kimilili, Chwele na Kanduyi. Katika ishara ya kumuunga mkono, wakazi walichangia kati ya Sh50 na Sh1,000 kufanikisha kampeni zake za urais. "Afadhali nidaiwe Sh10 na kila mwananchi wa Bungoma kuliko kudaiwa na tajiri mmoja ambaye baadaye atanitaka nimlipe kwa zabuni nikichaguliwa," akasema Bw Sifuna. Aliahidi kuwa serikali ya upinzani itafuta Ushuru wa Nyumba, ushuru wa mafuta na kodi nyingine alizosema zimekuwa mzigo kwa wananchi. Kwa upande wake, Gavana Natembeya alisema Magharibi imekuwa ikikosa nafasi za kisiasa kutokana na migawanyiko ya viongozi wake, akitoa wito wa kuungwa mkono kwa mgombeaji mmoja wa urais. "Historia yetu imejaa migawanyiko. Watu walidhani mimi na Sifuna tungepambana, lakini tuliketi na kukubaliana. Wenzangu wa upinzani wawe jasiri na waseme wazi, 'Sifuna tosha'," akasema Bw Natembeya. Aliwataka pia viongozi wa Nyanza kuunga mkono mgombeaji kutoka jamii ya Mulembe kama walivyofanya kwa Raila Odinga kwa miaka mingi. Viongozi hao pia waliwashambulia Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, kwa kumpotosha Rais Ruto kuwa Bw Natembeya alisema serikali ya upinzani itafuta Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Ushuru wa Nyumba, Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC) na kodi nyingine alizodai zinawaumiza raia. Gavana Orengo alisema safari ya upinzani kuelekea Ikulu haiwezi kuzuiwa isipokuwa kupitia wizi wa kura, huku Seneta Osotsi akitaka kizazi kipya cha viongozi kupewa nafasi Magharibi. Naye Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alisema Linda Mwananchi tayari imefanya ziara katika kaunti 16 na inalenga kufika kaunti zote 47 kabla ya 2027. Alisema baada ya Magharibi, kundi hilo litaelekea Nyanza, Kisii, Mlima Kenya na Ukambani kukutana na viongozi wa upinzani akiwemo Fred Matiang'i, Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka ili kuunda muungano mmoja utakaompinga Rais Ruto mwakani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 26 Jul 2026 08:51:50

Mwanamume apigwa risasi Siaya wakazi wakipinga kiwanda cha nyuklia

MTU mmoja amelazwa hospitalini baada ya kupigwa risasi mguuni vurugu zilizozuka katika mkutano wa uhamasishaji kuhusu mradi wa kujenga kiwanda cha nyuklia cha thamani ya Sh1 trilioni katika eneo la Central Sakwa, Bondo, Kaunti ya Siaya, Ijumaa alasiri. Mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Biashara cha Ka'John ulihudhuriwa na maafisa wa KenGen, Shirika la Nishati na Umeme wa Nyuklia na Mbunge Gideon Ochanda. Waliokuwa wakielezea mradi huo kwa wakazi kabla ya vurugu kuzuka. David Otieno Mboya, mchimbaji mdogo wa madini kutoka kijiji cha Lenya, alisema hakuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo bali alikuwa akirejea nyumbani kutoka kazini alipopigwa risasi. "Nilikuwa napita karibu na eneo la mkutano vurugu zilipoanza. Wakazi walikuwa wakirusha mawe huku polisi wakifyatua risasi. Ghafla nilihisi maumivu makali kwenye mguu wa kushoto na nikagundua nimepigwa risasi," alisema. Alisema hajui iwapo alipigwa risasi na walinzi wa Mbunge Ochanda au maafisa wa polisi waliokuwa eneo hilo. Wasamaria wema walimkimbiza katika Hospitali ya Nango kabla ya kuhamishwa hadi Hospitali ya Bondo. Otieno alisema wakazi wengi wanapinga mradi huo kwa sababu utawalazimu kuhamishwa kutoka makazi yao ya muda mrefu. Mkazi mwingine, Otieno Ombok, alisema NuPEA imepuuza maswali ya jamii kuhusu usalama, fidia na uhamishaji wa wakazi, jambo lililosababisha hasira. Kamanda wa Polisi wa Bondo Peter Leparsare, alisema hakuna aliyekuwa ameripoti rasmi kupigwa risasi kufikia Ijumaa usiku, lakini alithibitisha kuwa polisi walifyatua risasi angani kutawanya umati baada ya mzozo kati ya wakazi na walinzi wa mbunge. Mradi huo ulihamishwa kutoka Kilifi hadi Siaya baada ya kupingwa na wakazi wa Kilifi. Serikali inapanga kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kwa kati ya megawati 3,000 na 6,000 kupitia mradi huo. Gavana wa Siaya James Orengo amesisitiza kuwa mafanikio yake yatategemea ushirikishaji wa wananchi, uwazi na ridhaa kamili ya jamii itakayoathirika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 26 Jul 2026 08:19:07

Mtego wa kutoka jadi unaovunja upinzani ufikapo uchaguzi mkuu

KUGAWANYIKA kwa upinzani si jambo geni katika siasa za Kenya. Mwaka 1992, chama cha FORD kilichokuwa kimeibuka kama tishio kubwa kwa utawala wa KANU kilisambaratika baada ya viongozi wake Kenneth Matiba na Jaramogi Oginga Odinga kutofautiana kuhusu nani angewania urais. Kutoka kwa mgawanyiko huo vilizaliwa vyama vya FORD-Asili chini ya Matiba na FORD-Kenya chini ya Jaramogi. Badala ya kupambana na Rais Daniel arap Moi, viongozi hao waligeukiana, kila mmoja akidai ndiye aliyekuwa na haki ya kupeperusha bendera ya upinzani. Zaidi ya miaka 30 baadaye, hali kama hiyo inaonekana kujitokeza tena. Viongozi wa upinzani wanakubaliana kuwa Rais William Ruto anapaswa kukabiliwa na mgombea mmoja mwaka 2027. Hata hivyo, bado hawajakubaliana ni nani atakayebeba bendera hiyo. Muungano unaowaleta pamoja Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Fred Matiang'i, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Justin Muturi unasema unataka mgombea mmoja. Lakini kila upande unaonekana kutaka mgombea huyo atoke katika kambi yake. Wakati huo huo, kiongozi wa Safina Jimi Wanjigi ameendelea na mkakati wake tofauti. Kama alivyofanya Mwai Kibaki mwaka 1992, Wanjigi amesema atazingatia ajenda ya uchumi badala ya kujiingiza katika mvutano kuhusu nani anafaa kuongoza muungano. Kwa sasa, wafuasi wa upinzani hawaonekani tu kumpinga Rais Ruto, bali pia wanapambana wao kwa wao. Kila kambi inatumia matokeo ya kura za maoni na nguvu za maeneo yao kama ushahidi wa kwa nini mgombea wao anastahili kupewa tiketi. Historia ya FORD inaonyesha hatari iliyopo. Kwanza, KANU haikuiangusha FORD. FORD ilianguka kwa sababu ya migawanyiko yake yenyewe. Katika harakati za kutafuta mgombea bora, upinzani wa sasa unaweza kujikuta ukijenga migawanyiko itakayompa Ruto nafasi ya kushinda. Wakati FORD ilipoanzishwa, ilionekana kama serikali inayosubiri kuingia madarakani. Mikutano yake ilivutia umati mkubwa na viongozi wake waliheshimiwa kwa mchango wao katika mapambano ya kurejesha mfumo wa vyama vingi. Lakini chama hicho hakikuwahi kuafikiana kuhusu namna ya kumpata mgombea wake wa urais. Matokeo yake yalionekana wazi katika uchaguzi wa mwaka 1992. Upinzani uliingia uchaguzini ukiwa umegawanyika kati ya Matiba, Jaramogi na Kibaki. Moi aliibuka mshindi huku kura za upinzani zikigawanyika. Hilo lilichelewesha kuondolewa kwa KANU madarakani kwa takriban muongo mmoja. Leo, viongozi wa upinzani wanakabiliwa na mtihani kama huo. Gachagua amesema mgombeaji anaweza kutangazwa hata Mei 2027, ilhali Muturi ametaka uamuzi ufanywe mapema na tayari ameonyesha kumuunga mkono Kalonzo. Martha Karua pia amehoji mfumo unaopendekezwa wa kumpata mgombeaji. Wachambuzi wanasema miungano mingi haisambaratiki siku ya uchaguzi. Huvunjika mapema kila upande unapoanza kujijengea mtandao wake, kukusanya fedha na kuwashawishi wafuasi kuwa hakuna mgombeaji mwingine anayefaa. Hapo ndipo kinachoitwa athari ya Matiba huanza. Kila mwanasiasa anakubali umuhimu wa umoja, lakini kwa sharti kwamba umoja huo umuunge mkono yeye. Somo jingine muhimu ni kwamba sheria na taratibu zinapaswa kuwekwa kabla ya majina ya wagombeaji. FORD haikuwahi kukubaliana kuhusu mfumo wa kumpata mgombeaji wake, jambo lililochochea mzozo ulioigawa. Kwa upinzani wa sasa, bado hakuna makubaliano kuhusu sifa za mgombeaji, ratiba ya uteuzi wala mfumo wa kutatua migogoro. Historia pia inaonyesha kuwa umati mkubwa wa watu kwenye mikutano si lazima uwe ishara ya ushindi. Matiba aliporejea nchini mwaka 1992 na kupokelewa na maelfu ya watu, wengi waliamini alikuwa tayari ameshinda. Lakini mvutano kuhusu mgombeaji ndio uliovunja FORD. Aidha, muungano wowote unaotegemea tu kumpinga aliye madarakani huwa katika hatari ya kusambaratika. Swali ambalo Safina amekuwa ikiuliza ni: Baada ya Ruto, nini kitafuata? Kwa mujibu wa Wanjigi, upinzani unapaswa kueleza sera zake kuhusu ushuru, deni la taifa, ukosefu wa ajira, ufisadi, afya, elimu na gharama ya maisha badala ya kutegemea kaulimbiu ya "Wantam" pekee. Somo la mwisho ni kwamba umoja wa kweli huhitaji viongozi wengine kujinyima kwa manufaa ya lengo la pamoja. Hilo lilitokea mwaka 2002, Raila Odinga alipomuunga mkono Mwai Kibaki kwa kauli maarufu ya "Kibaki tosha", hatua iliyosaidia kuondoa KANU madarakani. Historia ya FORD si simulizi ya zamani tu. Ni onyo kwamba upinzani unaweza kuwa na uungwaji mkono mkubwa wa wananchi, lakini ukashindwa ikiwa viongozi wake watashindwa kuweka maslahi ya taifa mbele ya tamaa zao binafsi. Tatizo jingine ambalo lilichangia kusambaratika kwa FORD ni kwamba kila kiongozi aliamini historia yake ya kisiasa ilimpa haki ya kuwania urais. Jaramogi alijiona ndiye aliyekuwa amepigania demokrasia kwa miongo mingi dhidi ya tawala za Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi. Kwa upande wake, Matiba aliamini mateso aliyopitia, ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa bila kesi na kuugua kiharusi akiwa kizuizini, yalikuwa yamemjengea uhalali wa kuongoza upinzani. Kila mmoja alitumia historia yake kama msingi wa kudai tiketi ya urais. Hali kama hiyo inaonekana kujitokeza katika upinzani wa sasa. Baadhi ya viongozi wanategemea ukongwe wao kisiasa, wengine wanajivunia idadi ya wapiga kura kutoka maeneo yao, huku wengine wakisisitiza tajriba yao serikalini, uadilifu wao au mateso wanayodai kuyapata kutokana na kupambana na utawala uliopo. Ingawa hoja hizo zinaweza kuwapa nguvu kisiasa, hazitoshi kuwapa haki ya moja kwa moja ya kupeperusha bendera ya muungano. Kwa mujibu wa historia ya FORD, umoja wa kisiasa haujengwi kwa hoja za nani ameteseka zaidi au nani anaungwa mkono na watu wengi zaidi, bali kwa kuweka utaratibu unaokubalika na wote. Bila makubaliano ya wazi kuhusu namna ya kumpata mgombeaji na jinsi ya kushughulikia malalamishi yatakayojitokeza, tofauti za viongozi zinaweza kugeuka chanzo cha mgawanyiko na kuudhoofisha upinzani kabla hata ya kampeni rasmi kuanza.

read more