T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Walimu wakataa nyongeza ya Sh8.4 bilioni, wasema nyongeza nzima inamezwa na ushuru

WALIMU nchini wamekataa nyongeza ya mishahara ya awamu ya pili ya Mkataba wa Pamoja wa Ajira (CBA) wa miaka ya 2025–2029, wakisema ni ndogo mno wala haiendani na gharama ya maisha inayozidi kupanda. Malalamishi hayo yameibuka baada ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kutoa barua inaoyoelekeza utekelezaji wa awamu ya pili ya mkataba huo kuanzia Julai 1, 2026. Walimu wengi waligundua kuwa nyongeza yao halisi ni kati ya Sh693 na Sh2,055 pekee kulingana na cheo na kiwango cha mshahara. Ingawa serikali ilitenga Sh8.4 bilioni kutekeleza awamu hiyo, walimu wanasema kiasi kinachoingia katika akaunti zao baada ya makato ya kisheria hakina tofauti kubwa na mshahara wa awali. "Mwalimu wa daraja ya C3 alitarajiwa kuongezewa Sh2,055, lakini hiyo ni kabla ya makato ya PAYE, SHA, Ushuru wa Nyumba na NSSF. Kinachobaki ni kidogo sana na hakiwezi hata kusaidia kulipa mkopo wa SACCO," alisema mwalimu mmoja wa Nairobi. Mkataba huo wa miaka minne una thamani ya Sh33.75 bilioni, ukihusisha nyongeza ya mishahara na masuala ya ustawi wa walimu. Hata hivyo, walimu wengi sasa wanasema matarajio yaliyotolewa na vyama vyao hayalingani na hali halisi. Katibu wa KUPPET tawi la Vihiga, Sabala Inyeni, alisema nyongeza hiyo haijazingatia mfumuko wa bei wala kupanda kwa gharama za usafiri. "Marupurupu ya usafiri hayajabadilishwa kwa zaidi ya miaka 15 ilhali bei ya mafuta imeendelea kupanda. Ongezeko hili haliendani na hali halisi ya maisha," alisema. Walimu wanaofanya kazi katika maeneo magumu na kame pia wameeleza kutoridhishwa kwao baada ya marupurupu ya mazingira magumu kukosa kuongezwa. Katibu wa chama cha walimu wanaohudumu katika maeneo hayo Ndung'u Wangenye, alisema baadhi ya walimu wameongezewa chini ya Sh500 huku wakifanya kazi katika mazingira magumu. "Walimu wa maeneo kame wanahisi wamesalitiwa. Marupurupu ya mazingira magumu ndiyo yanayowatia moyo kuendelea kufanya kazi huko, lakini hayajaguswa kabisa," alisema. Naibu Katibu Mkuu wa KUPPET Moses Nthurima, alisema walimu wengi hawajaridhishwa na matokeo ya mazungumzo ya CBA. "Serikali imechukua fedha nyingi kupitia makato ya SHA, ushuru wa nyumba, NSSF na kodi kuliko ilivyorejesha kupitia nyongeza ya mishahara. Ndiyo maana walimu hawaoni faida ya ongezeko hili," alisema.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Wanaume wawili wakanusha kusafirisha kokeni ya Sh4 milioni

WASHUKIWA wawili wameshtakiwa katika Mahakama ya Mombasa kwa madai ya kula njama ya kusafirisha kokeini yenye thamani ya karibu Sh4 milioni. Hilton Gocho Chopeta na Mohamed Jabir Ali walifikishwa mahakamani kuhusiana na makosa yanayodaiwa kutendeka kati ya Julai 15 na 16, 2026, katika Kaunti ya Mombasa. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wawili hao wanadaiwa kula njama kwa pamoja na watu wengine ambao bado hawajakamatwa ili kusafirisha kokeini, kinyume na sheria. Mbali na shtaka la kula njama, wawili hao wanakabiliwa na mashtaka tofauti ya kusafirisha dawa za kulevya. Bw Chopeta anadaiwa kusafirisha gramu 734.9528 za kokeini zenye thamani ya Sh2,939,811. Kwa upande mwingine, Bw Ali anadaiwa kuhifadhi gramu 256.478 za kokeini zenye thamani ya karibu Sh1,025,912. Jumla ya kokeini iliyopatikana katika operesheni hiyo ilikuwa gramu 991.4308, yenye thamani ya pamoja ya Sh3,965,723. Washukiwa hao walikanusha mashtaka. Katika hati ya kiapo iliyopinga kuachiliwa kwao kwa dhamana, wapelelezi waliiambia mahakama kuwa washukiwa hao huenda wangetoroka iwapo wangeachiliwa kabla kesi hiyo kusikilizwa na kuamuliwa. Konstebo Gershom Wachitsa, mpelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) mjini Mombasa na afisa anayechunguza kesi hiyo, alisema uchunguzi bado unaendelea, kwa hivyo ni muhimu kuwaweka washukiwa hao kizuizini. Polisi walisema Bw Chopeta alikamatwa Julai 15 ikiaminika alikuwa akielekea kupanda ndege kwenda Dubai. Alisindikizwa hadi katika ofisi za DCI, ambako wapelelezi walisema alitoa kwa njia ya haja kubwa vidonge 15 vilivyoshukiwa kuwa na kokeini kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Port Reitz, ambako alitoa vidonge vingine 29, na kufikisha jumla ya vidonge vilivyopatikana mwilini mwake hadi 44. Siku iliyofuata, Bw Ali alikamatwa alipokuwa akivuka Kivuko cha Likoni kuelekea Kisiwa cha Mombasa. Wapelelezi walisema baadaye aliwaongoza maafisa hadi nyumbani kwake Bombolulu kuchukua funguo kabla ya kuwaelekeza kwenye nyumba nyingine katika eneo la Bamburi Fisheries, ambako vidonge 16 zaidi vilivyoshukiwa kuwa na kokeini vilipatikana. Afisa mpelelezi aliiambia mahakama kuwa Bw Ali tayari ana kesi nyingine ya uhalifu inayosubiri kusikilizwa mahakamani. Upande wa mashtaka uliiomba mahakama iwanyime wawili hao dhamana hadi kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa kwa maslahi ya haki. Hata hivyo, washukiwa hao walipinga ombi la upande wa mashtaka, wakisema kuwa Serikali imeshindwa kutoa sababu za msingi za kuwanyima dhamana. Kupitia wakili wao, waliiambia mahakama kuwa haki zao za kikatiba tayari zilikuwa zimekiukwa baada ya kufikishwa mahakamani nje ya muda uliowekwa kisheria baada ya kukamatwa. Walisema pia kuwa upande wa mashtaka haujaonyesha jinsi kuwaachilia kwa dhamana kungeingilia uchunguzi au utekelezaji wa haki. Kwa mujibu wa muhtasari wa uchunguzi, mshukiwa alitoa vidonge 15 mara ya kwanza, akifuatiwa na vingine vitatu siku aliyolazwa. Katika saa za mapema za siku iliyofuata, alitoa vidonge vingine vitano asubuhi, kufuatiwa na kidonge kimoja, na vingine vitatu. Mnamo Julai 17, alitoa vidonge viwili vya mwisho, na kufikisha jumla ya vidonge vilivyopatikana hadi 44. Uchunguzi wa eksrei ulithibitisha vidonge vyote vilitoka.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Waasi wa Houthi sasa wafungia Saudia bahari katika mbinu ya kuunga mkono Iran

SANAA, Yemen: WAASI wa Houthi nchini Yemen wamezitaka kampuni za usafirishaji wa mizigo kwa njia ya bahari kutopakia wala kushusha mizigo katika bandari za Saudi Arabia. Houthi imeonya kuwa meli zitakazokiuka agizo hilo zitashambuliwa mahali popote ndani ya maeneo yanayofikiwa na vikosi vyao. Onyo hilo lilitolewa kupitia baruapepe iliyoandikwa Julai 20 na kutumwa kwa kampuni kadhaa za usafirishaji mizigo. Mnamo Jumatatu, Houthi walitangaza kuwa wamezingira bahari isitumiwe na Saudi Arabia. Hii ni hatua inayoweza kuzidisha vita kati ya Amerika na Iran huku biashara ya ulimwengu ikivurugika na bei ya mafuta kupanda hata zaidi. "Meli zote zimepigwa marufuku kupakia au kushusha mizigo katika bandari yoyote ya Saudi Arabia," ikasema barua hiyo ya Houthis. Waasi hao wamewashauri manohadha wa meli wachukue tahadhari kubwa kabla ya kushiriki shughuli zozote zinazohusisha bandari za Saudi Arabia. Kwa mujibu wa barua hiyo, masharti hayo mapya yalianza kutekelezwa Julai 20 na kundi hilo limesisitiza litahakikisha yanatiliwa manani. "Meli zitakazokiuka agizo hili zitakabiliwa na vikwazo. Aidha, zitashambuliwa mahali popote zilipo ndani ya maeneo yanayofikiwa na uwezo wa vikosi vyetu hapa Yemen," ikasema taarifa hiyo iliyotumwa na Kituo cha Kuratibu Oparesheni za Kibinadamu cha Houthi (HOCC), chenye makao yake jijini Sana'a. Iwapo njia ya kusini ya Bahari ya Shamu itafungwa, Saudi Arabia itapoteza njia muhimu mbadala ya kufikia Mlango wa Hormuz. Hali hii inaweza kuongeza hofu ya kupungua kwa mafuta na bidhaa katika soko la dunia. Usafiri wa meli katika Bahari ya Shamu bado haujarejea kawaida tangu Houthi waanze kushambulia meli za kibiashara mnamo Novemba 2023. Walitekeleza mashambulizi hayo wakisema walikuwa wanaunga mkono Wapalestina katika vita vya Gaza dhidi ya Israel. HOCC ndiyo kitengo kilichotumiwa na Houthi kutoa onyo kadhaa kwa sekta ya usafirishaji wa baharini wakati wa mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara kati ya 2023 na 2025. Walikomesha kushambulia meli baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza mnamo Oktoba mwaka jana kufikiwa. Duru kutoka mojawapo ya kampuni zilizopokea barua hiyo zilisema ujumbe huo unaonyesha kuwa Houthi bado wanataka kudhihirisha kuwa wana uwezo wa kuathiri usafiri wa baharini katika eneo hilo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Ujuzi wake wa uchinjaji kuku kwa ubora wa juu umemdumishia soko tangu enzi za Corona

USTAHIMILIVU, ujuzi wa kuchinja na ukwasi wa kutambua hitaji la soko zimekuwa silaha kibindoni iliyomwezesha Douglas Sobera, 34, kubadili changamoto ya janga la Corona kuwa biashara ya mamilioni ya pesa mjini Kisii. Sobera ni mmiliki wa Maa Chicken, buchari inayochinja na kusambaza kuku kwa zaidi ya asilimia 80 ya hoteli kubwa na mikahawa mjini Kisii na viunga vyake. Yeye si mgeni kwenye tasnia ya nyama ya kuku. Alipata uzoefu wa miaka mitano kama mfanyakazi wa Quality Meat Packers (QMP) — kampuni ya kibinafsi humu nchini ya kuchinja na kusaga nyama. Akiishi Kajiado, mwaka 2019 alianzisha mradi mdogo wa kununua kuku kutoka kwa wafugaji na kuwauza kwa QMP. Wakati huo biashara ilikuwa ikinawiri. Lakini mwaka 2020 janga la Covid-19 lilipoteka ulimwengu mzima hoteli nyingi zilifungwa, QMP ikapunguza ununuzi kwa asilimia 70, na Sobero akalia na kuku zaidi ya 400 asijue la kufanya. Baada ya kutafiti soko alirejea nyumbani Kisii mwisho wa 2021. Aliona fursa na akaidandia, kama anavyoeleza: "Wakazi wa Kisii wanapenda sherehe kila wikendi. Hoteli zinajaa, lakini hakuna msambazaji wa kuku aliye na viwango vya ubora kama vya QMP. Niliona pengo na nikaja kulijaza." Februari 2022 alifungua buchari yake ya Maa Chicken katika soko la Marikiti mjini Kisii. Duka hilo liko katika kiingilio cha nyuma cha jumba la Uhuru Plaza ambalo ni maarufu sana katika mji huo. Maa ni jina la Kimaasai. Kwa kuwa Sobera alianza kazi yake ya uuzaji nyama ya kuku katika himaya ya jamii ya Maasai huko Kajiado, aliamua kuita biashara yake jina hilo kama njia ya kuweka kumbukizi alikoanzia. Leo hii Maa Chicken ni kitovu cha kuku Kisii. Mauzo ya wastani ni kuku 100 kwa siku, sawa na kilo 180-200 ambapo bei ni Sh420 kwa kilo. Haya ni mapato ya takriban Sh 75,600 kwa siku au Sh 2.2 milioni kwa mwezi. Maa Chicken huuza aina zote za nyama ya kuku: waliofugwa mahususi kwa nyama yao maarufu broila, ambao huuzia hoteli za bei nafuu; kienyeji walioimarishwa, ambao huuzia wateja wa kati; na kienyeji halisi, ambao huuzia hoteli za kifahari na kwa mteja anayetaka kwa ajili ya kupika kitoweo. Huduma ni kulingana na mteja: kuku mzima, au vipande vyake — paja, mbawa, kidari, maini, firigisi na sehemu zinginezo. Kila kitu hupimwa kutumia mizani ya kidijitali mbele ya mteja. "Hatuuzi kwa kubahatisha. Hoteli ikitaka nyama ya broila isiyo na mfupa kilo 20 saa kumi na mbili asubuhi, ni lazima zifike. Kuchelewa ni kupoteza mteja!"anasisitiza Sobera. Ili kuhakikisha hakosi kuku amejenga ushirikiano na wafugaji zaidi ya 30 wa kudumu kutoka Bonchari, Kitutu Chache, na Nyaribari. Anawalipa kwa bei nzuri papo hapo. "Uaminifu ni mtaji. Mfugaji akijua analipwa leo, hata mvua ikinyesha ataleta kuku," Sobera aongeza. Biashara yake imeajiri vijana 10 moja kwa moja: kuna wachinjaji, wasafirishaji wanaotumia pikipiki ili kufikia wateja chapchap, wauzaji na wasimamizi. Kwa kutumia ujuzi na desturi za ubora za QMP, Maa Chicken imeweka viwango vya juu vya usafi. Kuku huchinjwa na kusafirishwa hadi kwa mteja wakiwa freshi. Wafanyakazi huvalia magwanda na kofia spesheli zinazotumika ndani ya chumba cha kichinjio pekee. Nazo sakafu, meza na vifaa vingine vya matumizi husafishwa kila saa. Ana majokufu makubwa matatu ambayo humsaidia kuhifadhi nyama kwa nyuzi hasi 18 (yaani -18°C) ikisubiri wanunuzi. "Afisa wa afya akipita hapa hawezi kutufungia duka. Ndio maana hoteli za Daraja Mbili, Mwembe, Getare zinatuamini," anadeka Sobera. Kama wafugaji wengine wa kuku Sobera analia kuhusu gharama ya juu ya lishe ambayo imefanya wakuzaji wasizalishe mifugo hao kwa wingi. "Bei ya chakula cha kuku imepanda kwa asilimia 22 mwaka huu na kutupunguzia faida. Barabara duni za mashambani pia ni tatizo wakati wa masika," aliongeza. Sobera analenga kufungua matawi katika miji ya Nyamira na Migori kabla ya 2028, na kuweka bidhaa zake za Maa Chicken kwenye maduka ya jumla. "Corona ilinifukuza Kajiado, lakini Kisii imenipa ufalme. Kijana usiseme hakuna kazi - tafuta ujuzi, tafuta pengo, kisha ingia kwa hatua moja na uendelee kupiga ingine kwa ingine," anahitimisha.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Stroberi za 'chandler' ni tamu pia kwa upande wa hela

MURAYA Mburu alipoacha kufanya kazi katika Kampuni ya Huduma za Maji na Usafi ya Nakuru (NAWASSCO) mwaka 2012 alijitosa katika kilimo shambani mwake Nyakiambi mjini Elburgon, Kaunti ya Nakuru. Tulipomtembelea majuzi tulimpata katika pilkapilka za kuvuna na kupakia mavuno ya matunda ya stroberi kwa ajili ya kuyauza. "Baada ya kuzalisha mahindi kwa miaka mitano nilififia kwani kilimo hicho hakikuwa kikienda vizuri. Baada ya kuuza mahindi makavu niliyokuwa nayo nilinunua kondoo dume 12 kwa kati ya Sh3,000 na Sh 5,000 kila mmoja kulingana na saizi. Nikawalea kwa mwaka mmoja kabla kuwauza Sh9,000 kila moja," alitanguliza Muraya kuhusu safari yake ndefu ya kilimo na ufugaji. Akapata ugumu kulea kondoo zaidi kutokana na uhaba wa malisho. [caption id="attachment_190380" align="alignnone" width="2560"] Muraya Mburu aonyesha stroberi alizopakia katika vikontena tayari kuuzwa, katika shamba Nyakiambi mjini Elburgon, Nakuru, wiki chache zilizopita. PICHA| JOHN NJOROGE[/caption] Ni wakati akikuna kichwa alipokumbuka makala katika chapisho la awali la Akili Mali, jinsi wakulima walikuwa wakistawi kwa kuuza bidhaa zao mtandaoni. Pitapita zake zikampeleka kwa kilimo cha stroberi. Akabaini ni rahisi kuanzisha, hakikuwa na kazi nyingi, na matunda yalichukua miezi michache kukomaa, tofauti na mahindi ambayo huchukua karibu mwaka mzima. Pia aligundua mauzo ya stroberi yalikuwa mazuri hata katika soko la mashinani. Muraya akafuatilia wakulima wa matunda hayo na kutembelea baadhi waliochapisha bidhaa zao mtandaoni. Ni kutoka kwa mmoja alijifunza kuhusu aina za stroberi zilizofaa maeneo mbalimbali. "Mnamo 2019 nilitembelea mkulima mjini Nyahururu, Kaunti ya Laikipia, nikanunua miche 800 kabla baadaye kuongeza 800 zaidi, kila moja ikiwa Sh30, kutoka kwa mtaji wa Sh120,000 niliokuwa nao," asema na kuongeza kuwa alihakikishiwa miche hiyo ilikuwa bora na ingenawiri eneo lake. Alitumia pesa zilizobaki kununua matangi ya maji, mabomba, kutayarish shamba, na nyavu ili kuepusha ndege wasifikie matunda shambani. Baada ya kukuza miche kwa mwezi mmoja aliipandikiza katika shamba lake la nusu robo. "Kwa kuwa sikuwa na mbolea ya kinyesi cha kondoo, ambayo ilikuwa bora kuchanganya na udongo wakati wa kupanda, niliweka ile ya kutokana na kinyesi cha ng'ombe baada ya wiki tatu," aeleza. Aliendelea kumwaga maji kwa miche hiyo kila asubuhi na jioni hasa wakati hakuna mvua, lakini baada ya miezi miwili alikuwa akitia maji mara mbili pekee kila wiki. Muraya anasema spishi ya chandler ambayo ndiyo anakuza katika shamba lake hustahimili hali ya anga ya eneo la Elburgon na Molo, ambayo mara nyingi ni baridi na mvua. Hata hivyo, atahadharisha kuwa mvua nyingi ni tatizo kwani matunda hupenda kiangazi wakati wa kukomaa. "Ningeomba serikali ya kaunti iimarishe mafunzo kwa wakulima kuhusu upanzi na soko la stroberi ili wapate mapato mazuri. Matunda haya ni matamu na utamu huo umefanya wateja kuongezeka, ikiwemo wakulima wanaonunua miche kwa upanzi," aeleza. Ni ombi ambalo Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Nakuru Leonard Bor, amelisikia kwani anasema maafisa wa kilimo nyanjani wako tayari kufika kokote katika kaunti ili kuhamasisha wakulima kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo mifumo faafu ya kilimo, maradhi ya mimea, kudhibiti wadudu waharibifu na kadhalika. "Kama serikali ya kaunti tutaimarisha mipango ya kuhamasisha na kuwafikia wakulima wengi hususan siku za kilimo au kuwatembelea mashambani mwao ili kuendelea kufanikisha kilimo," alisema Bor na kuongeza kuwa wakulima pia huarifiwa wakati wa siku za kilimo kupitia ofisi za chifu katika maeneo yao. Muraya anahoji kwamba soko la matunda limeongezeka pakubwa katika maeneo ya Molo, Elburgon na Kuresoi tangu janga la corona kutokana na himizo la wataalamu wa afya kwamba matunda yana virutubishi ambavyo huimarisha kingamwili, na hivyo kusaidia kupambana na homa hiyo. Mavuno yake ya kwanza yalikuwa ya kuridhisha, lakini mwanzoni alipata changamoto kuyauza katika soko la mashinani kwani stroberi bado zilikuwa hazijachangamkiwa sana. Akaanza kupakia katika vikontena vidogo vya plastiki vya kuweka vyakula kavu [punnets kwa Kimombo] kwa wateja wa mijini na baadaye maduka makubwa ya jumla. Hata hivyo, aliendelea kuuza matunda yake reja reja kwa kutembea kutoka sehemu moja hadi nyingine kutokana kwamba baadhi ya wateja na maduka hayakuwa na friji za kuhifadhi matunda hayo katika vikontena. Sasa anafurahia matunda ya bidii yake kwani soko lake limeendelea kunawiri katika mji wa Elburgon na viunga vyake. Mkulima huyu hana majuto tangu alipozamia kilimo cha stroberi miaka saba iliyopita kwani amefanikiwa kumudu karo ya shule ya watoto wake na kukidhi mahitaji mengine ya kimsingi nyumbani. "Msimu mzuri ninavuna mara mbili kwa wiki, kati ya paneti 40 na 60 na kuuza kila kifurushi Sh150," alisema Muraya na kuongeza kuwa mpango wake ni kufuga kondoo ambao watamsaidia kupata mbolea asilia, ambayo ndiyo yeye hutumia shambani. Aidha, maono yake katika siku zijazo ni kupanua shamba hadi ekari tano akitumai soko la stroberi litaendelea kunawiri eneo hilo na kote nchini.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Mwanamume aliyepatwa amemeza mihadarati alazimishwa kuitema

POLISI katika Kaunti ya Mombasa wanamzuilia mwanamume aliyepatikana amemeza madonge ya dawa za kulevya, akilenga kuyasafirisha hadi Dubai yakiwa ndani ya mwili wake. Mnamo Julai 15, wakati wasafiri wakisubiri kuabiri ndege ya saa saba mchana kutoka Mombasa kuelekea Dubai, wapelelezi katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi jijini Mombasa walikuwa wakimfuatilia mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 67. Taarifa za kijasusi zilikuwa zimemhusisha na mtandao wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya, huku wachunguzi wakishuku kwamba alikuwa ameficha kokeini ndani ya mwili wake. Wapelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), wakishirikiana na maafisa wa usalama wa uwanja huo wa ndege, walimkamata kabla ya kuabiri ndege. Operesheni hiyo baadaye ilihusishwa na mtandao wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya ambao umekuwa ukichunguzwa kwa miezi kadhaa. [caption id="attachment_190364" align="alignnone" width="2560"] Polisi wapata mihadarati kutoka kwa msafiri mmoja aliyekuwa anaelekea Dubai Picha|Kevin Odit[/caption] Walanguzi hao wa kimataifa hutumia Mombasa kama kituo cha kupitisha dawa za kulevya kuelekea nchi nyingine za nje. Mshukiwa alikamatwa na kupelekwa katika kituo maalumu cha kutengwa kwa ajili ya uangalizi wa kimatibabu. Baadaye alipelekwa katika Hospitali ya Port Reitz, ambapo madaktari na wahudumu wa afya walimweka chini ya uangalizi wa karibu ili kusaidia kutoa dawa hizo alizokuwa amemeza kwa njia salama. Polisi walisema wataalamu wa matibabu walifanikiwa kutoa vidonge 44 vilivyofunikwa kutoka tumboni mwake kwa njia iliyolenga kuvizuia kupasuka. "Dawa hizo za kulevya zitatumika kama vielelezo mahakamani," alisema Kamanda wa Polisi wa eneo la Pwani Ali Nuno. Kulingana na wachunguzi, kumeza dawa za kulevya ili kukwepa ukaguzi wa usalama ni mojawapo ya njia hatari zaidi za kusafirisha dawa hizo, kwa sababu vikipasuka ndani ya mwili vinaweza kusababisha maafa. Polisi walifichua kwamba kukamatwa kwa mwanamume huyo kulitokana na operesheni inayoendelea ambayo hadi sasa imesababisha kukamatwa kwa washukiwa wengine kadhaa, wakiwemo wanaodaiwa kuwa walanguzi wakuu wa dawa za kulevya. Kwa jumla, dawa za kulevya zenye thamani ya karibu Sh151 milioni zimepatikana na polisi katika kipindi cha karibu miezi minne iliyopita. Operesheni hiyo pia ilifanikisha kukamatwa kwa mshukiwa mwingine ambaye wapelelezi wanaamini alikuwa kinara wa biashara hiyo haramu. Wakati wakiendeleza uchunguzi, maafisa walivamia nyumba iliyoshukiwa kutumiwa kama maficho na kituo cha muda cha kuwahifadhi wasafirishaji wa dawa za kulevya. Upekuzi huo ulisababisha kupatikana kwa vipande vingine 16 vinavyodhaniwa kuwa na kokeini. Uchunguzi unaendelea kubaini ukubwa kamili wa mtandao huo na kuwatambua washukiwa wengine. Takwimu zilizotolewa na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha DCI zinaonyesha kwamba wapelelezi wamekamata kilo 37 za heroini zenye thamani ya takriban Sh111.846 milioni katika miezi minne iliyopita. Pia wamekamata gramu 1,336 za kokeini zenye thamani ya takriban Sh5.344 milioni. "Jumla ya watu tuliowakamata kuhusiana na dawa za kulevya ni washukiwa 27. Kati yao, watano ni wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya bila shaka yoyote, 10 ni wasafirishaji na 12 ni wauzaji," alisema Bw Nuno. Ripoti hiyo pia inaonyesha kwamba maafisa walikamata gramu 204 za methamphetamine, inayofahamika zaidi kama meth, yenye thamani ya takriban Sh1.632 milioni katika operesheni zilizofanywa katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Bangi bado ndiyo dawa ya kulevya inayokamatwa zaidi katika eneo hilo, polisi wakiripoti kukamata kilo 10,747.84 zenye thamani ya takriban Sh32.243 milioni katika kipindi hicho. Kwa jumla, thamani ya dawa zote za kulevya zilizokamatwa katika operesheni za kupambana na biashara hiyo katika eneo la Pwani ni takriban Sh151.065 milioni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Serikali yakubali ukosoaji wa ufadhili elimu ya juu; yaweka mpango wa 'kufaidi wote'

WANAFUNZI wote watakaofuzu kujiunga na vyuo vikuu nchini watapata ufadhili kamili wa masomo kutoka kwa serikali iwapo pendekezo jipya la ufadhili wa elimu ya juu litapitishwa na Bunge. Rais William Ruto alitangaza hatua hiyo Jumanne katika Ikulu, akisema serikali imewasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria yatakayowezesha kila mwanafunzi anayefaulu mtihani wa kitaifa na kupata nafasi katika chuo kikuu au taasisi ya elimu ya juu kufadhiliwa kikamilifu bila kujali hali ya kifedha ya wazazi wake. "Kwa sasa tuna pendekezo bungeni litakalowezesha elimu ya juu kuwa ya wote. Haitajali mtoto anatoka katika familia gani, bali uwezo wake kitaaluma. Mwanafunzi yeyote anayefaulu na kupata nafasi chuoni atapata ufadhili kamili," alisema Rais Ruto. Aliwahimiza wabunge kuharakisha kupitisha marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) ili wanafunzi watakaoanza masomo Septemba mwaka huu wanufaike kwa mfumo huo mpya. Tangazo hilo linaashiria kuwa serikali inaweza kuachana na mfumo wa sasa wa ufadhili wa elimu ya juu ulioanzishwa mwaka wa 2023 ambao umekoselewa na wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu. Rais alisema mfumo wa awali haukufaulu kwani ulisababisha vyuo vikuu vingi kukumbwa na matatizo ya kifedha baada ya serikali kushindwa kutoa kiwango cha fedha ilichoahidi. "Baadaye tukaanzisha mfumo wa usawa ambapo wazazi walichangia sehemu ya karo, serikali ikatoa sehemu kupitia ufadhili na sehemu nyingine kupitia mkopo. Tulidhani ungeleta usawa lakini umeonekana kutotosha," alisema. Aliongeza kuwa chini ya mfumo mpya, wazazi watakuwa na hiari ya kuchangia karo za watoto wao, lakini iwapo hawataweza kufanya hivyo, serikali itagharimia masomo yote. "Hatutaki mwanafunzi yeyote ashindwe kuendelea na masomo kwa sababu ya ukosefu wa fedha," alisema Rais. Hata hivyo, maelezo ya kina kuhusu mfumo huo bado hayajatolewa. Katibu wa Elimu ya Juu, Dkt Beatrice Inyangala, alisema pendekezo hilo bado linashughulikiwa kabla ya kuwasilishwa rasmi kwa wadau na Bunge. "Bado tunalifafanua na kulikamilisha. Ni mchakato unaohitaji muda," alisema. Mwenyekiti wa Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Umma, Prof Daniel Mugendi, pia alisema bado hajapokea maelezo kamili ya mfumo huo. "Hatujapata maelezo ya kina. Yakikamilika tutashirikishwa kwa majadiliano zaidi," alisema. Changamoto ya ufadhili wa elimu ya juu imekuwa ikisumbua serikali kwa miaka kadhaa. Madeni ya vyuo vikuu vya umma yameongezeka kutoka takriban Sh60 bilioni mwaka wa 2022 hadi zaidi ya Sh85 bilioni sasa. Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa HELB Geoffrey Monari amependekeza taasisi hiyo ipate fedha kupitia masoko ya kifedha kwa kutoa dhamana ya kijamii ya thamani ya Sh500 milioni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata ufadhili kwa wakati. Kwa sasa, takriban 450,000 wanaonufaika na mikopo ya HELB wanaendelea kulipa mikopo yao, hali inayowezesha bodi hiyo kukusanya karibu Sh700 milioni kila mwezi. Mbali na mikopo, HELB hutenga Sh237 milioni kila mwaka kama ufadhili kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ambapo Sh137 milioni huenda kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na Sh100 milioni kwa wanafunzi wa vyuo vya TVET.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Gachagua akemewa kwa kauli yake kwamba watalii wasije Kenya sababu ya wahuni

KAULI ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ya kuwataka watalii na wawekezaji wa kigeni kusubiri hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 kabla ya kuja Kenya imesolewa vikali serikalini, sekta ya utalii na hata baadhi ya washirika wake wa kisiasa. Akizungumza katika ibada ya kanisani mwishoni mwa wiki, Bw Gachagua alisema hali ya usalama nchini imezorota kutokana na ongezeko la ghasia za kisiasa na shughuli za makundi ya wahuni, akidai kuwa watalii na wawekezaji hawako salama. Kauli hiyo ilipingwa na Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura, ambaye alisema utalii ni nguzo muhimu ya uchumi. Wakati huo huo, Rais William Ruto amekosoa Mahakama kwa kile alichosema ni kuwapa dhamana nafuu washukiwa wa uhalifu wanaotuhumiwa kuvuruga mikutano ya kisiasa, akisema hatua hiyo imechangia ongezeko la wahuni nchini. Akizungumza Ikulu, Nairobi, Jumanne, Rais alisema washukiwa wanaokamatwa kwa makosa ya jinai huachiliwa kwa dhamana ndogo na kurejea mitaani kuendelea na vitendo vyao. "Vijana wanaokamatwa kwa uhalifu hupelekwa mahakamani, wanapewa dhamana ya Sh200 na kuachiliwa kwa sababu ni watoto wetu. Kisha wanarudi katika mikutano ya kisiasa na kuendelea na vitendo vya kihuni," alisema Rais Ruto. Alisema Kenya lazima iwe na mjadala wa dhati kuhusu ongezeko la wahuni huku joto la kisiasa likizidi kupanda kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amesema uchunguzi unaendelea kubaini waliohusika na vurugu hizo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 21 Jul 2026 21:55:42

Kenya yageuzwa ngome ya wahuni sasa wakitumiwa kutwaa ardhi, biashara na mali

KENYA inaendelea kugeuka kuwa paradiso ya wahuni wanaotumiwa kutwaa ardhi, nyumba, biashara na mali nyingine huku amri za mahakama zikipuuzwa na mamlaka zikionekana kushindwa kuwalinda waathiriwa. Katika miaka ya hivi karibuni, makundi ya vijana wenye silaha yamekuwa yakihusishwa na uvamizi wa hospitali, kufurusha familia kutoka nyumba zao, kutwaa majengo ya biashara na kuzuia utekelezaji wa amri halali za mahakama. Mojawapo ya visa vinavyoibua wasiwasi ni kile cha Hospitali ya Nakuru War Memorial, ambayo imefungwa kwa zaidi ya miaka miwili licha ya mahakama kuagiza ifunguliwe tena. Msimamizi mkuu wa wauguzi wa hospitali hiyo, Patricia Musale, anasema mgogoro ulianza Oktoba 2023 alipopigiwa simu akiarifiwa kuwa kundi la watu lilikuwa limevamia hospitali likidai limechukua usimamizi wake. Alipofika, lango kuu lilikuwa limefungwa na akalazimika kuruka ua kuingia ndani. "Muda mfupi baadaye, maafisa wa kaunti walichukua udhibiti wa hospitali na wagonjwa wote wakaanza kuhamishwa. Kabla ya usiku wa manane, kila mgonjwa alikuwa ameondolewa, wakiwemo watoto waliokuwa kwenye mashine za kuwasaidia kupumua," alisema. Hospitali ilipata amri za mahakama za kufunguliwa tena lakini kabla ya kutekelezwa, kundi jingine la zaidi ya vijana 200 lilivamia eneo hilo Januari 2024 na kuzuia mtu yeyote kuingia. "Tulipata amri kadhaa za mahakama lakini kila tunapofika tunawakuta wahuni wamezingira lango. Hata polisi wakifuatana nasi hakuna kinachofanyika," alisema Bi Musale. Kwa zaidi ya miaka miwili sasa, vifaa vya matibabu vya thamani ya mamilioni ya pesa vimekaa bila kutumika huku wafanyakazi wengi wakipoteza ajira na wagonjwa waliokuwa wakitegemea huduma kama za figo na matibabu ya Virusi vya Ukimwi wakiteseka. Mzozo huo unatokana na mgogoro wa umiliki wa ardhi kati ya hospitali na Serikali ya Kaunti ya Nakuru. Mnamo Februari 2024, Jaji Mkuu Martha Koome alieleza wasiwasi kuhusu uvamizi huo na ukaidi wa amri za mahakama, lakini hadi leo hospitali haijafunguliwa. Kisa kingine kinachoonyesha jinsi wahuni wanavyotumiwa kutwaa mali ni cha mfanyabiashara Avan Shah wa Nairobi. Bi Shah anasema Novemba 2022 dalali aliwasili nyumbani kwake akiwa ameandamana na takriban watu 30 waliokuwa na mapanga na marungu. "Walidai wanatekeleza amri ya mahakama. Kabla hatujathibitisha stakabadhi walikuwa tayari wameanza kubomoa nyumba. Polisi walifika lakini hawakutusaidia," alisema. Familia hiyo ilifurushwa kutoka nyumba waliyoishi kwa karibu miaka 50 na hadi sasa haijarejea huku kesi ikiendelea mahakamani. Kamati ya Ardhi ya Bunge la Kaunti ya Nairobi baadaye ilibaini kuwa kulikuwa na dosari katika usimamizi wa rekodi za ardhi hiyo na kupendekeza hatua zichukuliwe dhidi ya maafisa waliohusika. Visa hivi vinaonyesha mwenendo unaozidi kushika kasi ambapo migogoro ya ardhi, biashara na mali haiamuliwi tena mahakamani pekee bali pia kwa nguvu za makundi ya wahuni. Katika maeneo mengi nchini, wahuni hutumiwa kuwafurusha wapangaji, kufunga njia za kuingia katika majengo yanayobishaniwa, kutwaa biashara na hata kuzuia utekelezaji wa amri za mahakama. Hata madalali wanasema mara nyingi hulazimika kufanya kazi katika mazingira ya vitisho na ghasia. Wakenya wengi wanaishi kwa hofu kwamba siku moja wanaweza kupokonywa nyumba, biashara au ardhi yao kwa nguvu licha ya kuwa na haki kisheria. Kwa wengi, hali hiyo inaashiria hatari kubwa kwa utawala wa sheria, ambapo nguvu za makundi ya wahuni zinaanza kushinda mamlaka ya mahakama katika kuamua nani anamiliki mali nchini.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 21 Jul 2026 11:13:32

MAONI: Ushindi wa DCP Ol Kalou si picha halisi ya kura za 2027

MATOKEO ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ol Kalou yanapaswa kudadisiwa kwa jicho la pili. Ushindi wa mgombea wa chama cha Democracy for Citizen Party (DCP) dhidi ya mgombea wa UDA unaibua mengi. Matokeo ya uchaguzi huo yamefasiriwa kama ishara ya talaka kati ya eneo la Mlima Kenya na chama cha UDA. Picha hiyo huenda si ya kuaminika kama taswira kamili ya uchaguzi mkuu ujao katika taifa zima. Msisimko na hisia za kudhulumiwa kwa aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua kisiasa yalichangia pakubwa katika matokeo hayo kwani wapigakura walihisi kutengwa na kuamua kuiadhibu serikali kwa maamuzi ya kumbandua Rigathi Gachagua serikalini. Ikichunguzwa kwa makini, ngome hiyo imeegemea upande wa upinzani bila sera maalum isipokuwa msukumo wa wimbi la ghadhabu. Wapigakura Ol Kalou waliiona fursa hiyo kama ya kipekee ya kumfuta machozi mmoja wao ambaye ni kinara wa DCP hasa baada ya upinzani kushindwa katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Malava, Mbeere Kaskazini na Emurua Dikirr. Upinzani umepata ushindi katika ngome yake wala si maeneo mengine nchini. Kwa hivyo hauwakilishi hali halisi ya uchaguzi mkuu ambao utashirikisha wananchi kutoka taifa zima. Ingawa wananchi wengi katika eneobunge la Ol Kalou walijitokeza kupiga kura, kuna uwezekano wa baadhi ya wapigakura kutoka ngome ya DCP kukosa mvuto wa kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao. Ni wazi kuwa upinzani ukikosa kuwa na mwaniaji wa urais kutoka eneo hilo - ambaye mara nyingi huwa kichocheo cha wengi kujituma kupiga, kura nyingi hazitapigwa. Waziri Wycliffe Oparanya kuazimia kuwa mgombea mwenza wa urais katika serikali ya muungano, ni hesabu tata ya kuangamiza juhudi za Linda Mwananchi kumnadi Edwin Sifuna katika eneo la Magharibi. Katibu mkuu Francis Atwoli pamoja na viongozi wakongwe kisiasa katika eneo la Magharibi wameonyesha dalili za kuitetea hatamu ya pili ya rais William Ruto. Hili ni pigo kwake Sifuna ambaye anafanya jaribio la kutanua mbawa zake kisiasa kwa mara ya kwanza. Mbinu hizo za serikali zitayeyusha nguvu za upinzani ikizingatiwa kuwa Linda Mwananchi inapigiwa upatu na wanasiasa walio katika upinzani ambao bado haujafanya maamuzi ya ni nani atawania nafasi ya urais. Eneo la Mlima Kenya bado linakumbwa na siasa za mpasuko wa Mlima Kenya Magharibi na Mlima Kenya Mashariki. Hii itadhoofisha nguvu za chama cha DCP katika ukanda huo wa nchi. Uchaguzi ujao utashindwa na yule atakayeweza kunasa nyoyo za wananchi kwa sera madhubuti za kuipa nchi mkondo mpya kiuchumi. Iwapo serikali itatekeleza miradi iliyoahidi katika kila eneo nchini na kurahisisha gharama ya maisha, basi upinzani utakuwa na kibarua kigumu kujinadi. Hongera OlKalau kwa kuwafunza Wakenya kuwa pesa na zawadi za kuwafumba macho wapigakura hazina thamani katika kumchagua kiongozi. Mlivipokea vingi lakini mkafanya uamuzi bila kupofushwa na misaada ya kuchumbiwa ya muda mfupi. Rekodi hii ikihifadhiwa katika kumbukumbu za wapigakura basi hongo na ulaghai wa kisiasa zitafika kikomo na demokrasia kunawiri humu nchini.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 21 Jul 2026 02:55:28

DPP: Upo ushahidi kifo cha Ojwang kilipangwa mikononi mwa polisi

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga ameambia Mahakama Kuu kuwa upande wa mashtaka utawasilisha ushahidi kuonyesha kuwa kifo cha mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang kilipangwa. Bw Ingonga anasema mauaji hayo yalipangwa Bw Ojwang akiwa mikononi mwa polisi, wala si ajali kama ilivyodaiwa awali. Akitoa hoja wakati wa kuanza kwa kesi katika Mahakama Kuu ya Kibera jana, mwendesha mashtaka mkuu msaidizi Gikui Gichuhi alisema ushahidi utaonyesha jinsi maafisa wa polisi walipanga kipigo kilichosababisha kifo cha Ojwang kisha wakajaribu kuficha ukweli. Aliyekuwa Kamanda wa Kituo cha Polisi cha Central, Samson Tallam, anakabiliwa na mashtaka ya mauaji pamoja na maafisa wa polisi James Mukhwana na Peter Kimani. Wengine walioshtakiwa ni raia watatu, John Ngige Gitau, Jim Ambao na Brian Njue, waliokuwa wakizuiliwa katika seli moja na Bw Ojwang. Bw Gichuhi alisema ushahidi wa kimatibabu utaonyesha kuwa Ojwang alipata majeraha mengi mwilini yaliyosababishwa na kupigwa, kinyume na madai ya awali ya polisi kwamba alijijeruhi kwa kujigonga ukutani. Upande wa mashtaka pia ulisema utawasilisha ushahidi unaodaiwa kuonyesha kulikuwa na juhudi za kuharibu uchunguzi, ikiwemo kufutwa kwa picha za kamera za usalama (CCTV) katika kituo cha polisi. Bw Ojwang alikamatwa nyumbani kwake Kakoth, Kaunti ya Homa Bay, Juni 7, 2025 na maafisa wa DCI kufuatia malalamishi kuhusu chapisho la mitandaoni lililomlenga na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Langat. Baadaye alihamishwa hadi Kituo cha Polisi cha Central, Nairobi, ambako alifariki akiwa rumande. Ripoti ya uchunguzi wa maiti ilibaini alikuwa na majeraha mabaya kichwani, shingoni na sehemu nyingine za mwili, huku wataalamu wakihitimisha kuwa yalitokana na kushambuliwa na si kujidhuru. DPP anasisitiza kuwa washtakiwa wote sita walihusika katika mauaji hayo, huku uchunguzi ukiendelea chini ya Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA).

read more