taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
KCPE, KCSE zafufua kumbukumbu za shule kwa Wakenya wanaoishi Uingereza
KWA Wakenya wengi, kumbukumbu za mitihani ya KCPE na KCSE huibua picha za usiku wa kukesha wakisoma, wasimamizi wakali wa mitihani na shinikizo kubwa la kufaulu. Lakini sasa, kile kilichokuwa chanzo cha hofu kimegeuzwa kuwa burudani inayowaleta pamoja Wakenya nchini na ughaibuni. Nchini Uingereza, jamii ya Wakenya imeanzisha usiku maalum wa maswali na majibu unaotumia maswali ya KCPE na KCSE kama njia ya kuburudika, kukumbushana maisha ya shule na kuimarisha urafiki. Miongoni mwa walioanzisha shughuli hiyo ni Nicholas Njomo Kamau, mtaalamu wa afya anayefanya kazi katika Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza (NHS). Alivutiwa na hafla kama hizo zilizoandaliwa Nairobi na jumuiya ya ubunifu ya Qwani. "Niliona zinafanyika Kenya nikafikiria kwa nini tusizilete hapa, ambako kuna Wakenya wengi. Nimefurahishwa na zilivyopokolewa," alisema. Hafla hizo sasa zimefanyika mara tatu katika ukumbi wa Vaha Lounge mjini Northampton. Washiriki huwekwa katika makundi na kujibu maswali ya Hisabati, Kiingereza, Kiswahili, Sayansi na Masomo ya Jamii bila presha ya kufaulu. Kwa Njomo, uzuri wa wazo hilo ni kwamba karibu kila Mkenya amepitia mfumo wa elimu wa 8-4-4. "Sote tumewahi kupitia mitihani hiyo," alisema. Kilichoanza kama mkutano wa kujiburudisha sasa kimekuwa jukwaa la kujenga urafiki. Washiriki wameunda makundi ya WhatsApp na huendelea kuwasiliana hata baada ya hafla kuisha. Ingawa washindi hupata zawadi kama vile chupa za pombe, wengi husema zawadi kubwa ni kurejea kumbukumbu za utotoni, walimu waliowapenda, ushindani wa shule na maswali magumu yaliyowasumbua. Njomo alisema jambo lililomshangaza zaidi ni kuona hata Wakenya wa umri mkubwa wakijiunga na kufurahia hafla hizo. "Pia tumewaona watu wasiokuwa Wakenya wakija kudadisi. Huondoka wakifurahia muziki, ushindani na mazingira ya Kikenya," alisema huku akicheka. Baada ya maswali na majibu, hafla hubadilika kuwa sherehe ya nyimbo za zamani za Kenya. Wageni hufurahia ugali, nyama choma, pilau na mboga za kienyeji huku nyimbo za Gengetone na nyimbo za zamani zikichezwa. "Tunawaleta ma-DJ wa Kenya kucheza nyimbo zinazotukumbusha enzi za shule," alisema. Mwanafunzi wa uuguzi nchini Uingereza, Lynn Saina, alisema hafla hizo huwasaidia Wakenya kupunguza hamu ya nyumbani. "Kinachonivutia zaidi ni furaha na vicheko. Chumba kilichojaa wageni hubadilika haraka na kuwa familia moja kubwa," alisema. Aliongeza kuwa kati ya vipengele vinavyovutia zaidi ni maswali ya methali za Kiswahili, ambapo washiriki hujaribu kukamilisha methali lakini mara nyingi huishia kubuni methali mpya zinazochekesha kila mtu. Siku ya kwanza, hafla hiyo ilivutia zaidi ya watu 150 uliwathibitishia kuwa Wakenya walikuwa na hamu kubwa ya kumbukumbu zao za shule.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
Mwanamume apigwa risasi Siaya wakazi wakipinga kiwanda cha nyuklia
MTU mmoja amelazwa hospitalini baada ya kupigwa risasi mguuni vurugu zilizozuka katika mkutano wa uhamasishaji kuhusu mradi wa kujenga kiwanda cha nyuklia cha thamani ya Sh1 trilioni katika eneo la Central Sakwa, Bondo, Kaunti ya Siaya, Ijumaa alasiri. Mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Biashara cha Ka'John ulihudhuriwa na maafisa wa KenGen, Shirika la Nishati na Umeme wa Nyuklia na Mbunge Gideon Ochanda. Waliokuwa wakielezea mradi huo kwa wakazi kabla ya vurugu kuzuka. David Otieno Mboya, mchimbaji mdogo wa madini kutoka kijiji cha Lenya, alisema hakuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo bali alikuwa akirejea nyumbani kutoka kazini alipopigwa risasi. "Nilikuwa napita karibu na eneo la mkutano vurugu zilipoanza. Wakazi walikuwa wakirusha mawe huku polisi wakifyatua risasi. Ghafla nilihisi maumivu makali kwenye mguu wa kushoto na nikagundua nimepigwa risasi," alisema. Alisema hajui iwapo alipigwa risasi na walinzi wa Mbunge Ochanda au maafisa wa polisi waliokuwa eneo hilo. Wasamaria wema walimkimbiza katika Hospitali ya Nango kabla ya kuhamishwa hadi Hospitali ya Bondo. Otieno alisema wakazi wengi wanapinga mradi huo kwa sababu utawalazimu kuhamishwa kutoka makazi yao ya muda mrefu. Mkazi mwingine, Otieno Ombok, alisema NuPEA imepuuza maswali ya jamii kuhusu usalama, fidia na uhamishaji wa wakazi, jambo lililosababisha hasira. Kamanda wa Polisi wa Bondo Peter Leparsare, alisema hakuna aliyekuwa ameripoti rasmi kupigwa risasi kufikia Ijumaa usiku, lakini alithibitisha kuwa polisi walifyatua risasi angani kutawanya umati baada ya mzozo kati ya wakazi na walinzi wa mbunge. Mradi huo ulihamishwa kutoka Kilifi hadi Siaya baada ya kupingwa na wakazi wa Kilifi. Serikali inapanga kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kwa kati ya megawati 3,000 na 6,000 kupitia mradi huo. Gavana wa Siaya James Orengo amesisitiza kuwa mafanikio yake yatategemea ushirikishaji wa wananchi, uwazi na ridhaa kamili ya jamii itakayoathirika.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
Mtego wa kutoka jadi unaovunja upinzani ufikapo uchaguzi mkuu
KUGAWANYIKA kwa upinzani si jambo geni katika siasa za Kenya. Mwaka 1992, chama cha FORD kilichokuwa kimeibuka kama tishio kubwa kwa utawala wa KANU kilisambaratika baada ya viongozi wake Kenneth Matiba na Jaramogi Oginga Odinga kutofautiana kuhusu nani angewania urais. Kutoka kwa mgawanyiko huo vilizaliwa vyama vya FORD-Asili chini ya Matiba na FORD-Kenya chini ya Jaramogi. Badala ya kupambana na Rais Daniel arap Moi, viongozi hao waligeukiana, kila mmoja akidai ndiye aliyekuwa na haki ya kupeperusha bendera ya upinzani. Zaidi ya miaka 30 baadaye, hali kama hiyo inaonekana kujitokeza tena. Viongozi wa upinzani wanakubaliana kuwa Rais William Ruto anapaswa kukabiliwa na mgombea mmoja mwaka 2027. Hata hivyo, bado hawajakubaliana ni nani atakayebeba bendera hiyo. Muungano unaowaleta pamoja Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Fred Matiang'i, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Justin Muturi unasema unataka mgombea mmoja. Lakini kila upande unaonekana kutaka mgombea huyo atoke katika kambi yake. Wakati huo huo, kiongozi wa Safina Jimi Wanjigi ameendelea na mkakati wake tofauti. Kama alivyofanya Mwai Kibaki mwaka 1992, Wanjigi amesema atazingatia ajenda ya uchumi badala ya kujiingiza katika mvutano kuhusu nani anafaa kuongoza muungano. Kwa sasa, wafuasi wa upinzani hawaonekani tu kumpinga Rais Ruto, bali pia wanapambana wao kwa wao. Kila kambi inatumia matokeo ya kura za maoni na nguvu za maeneo yao kama ushahidi wa kwa nini mgombea wao anastahili kupewa tiketi. Historia ya FORD inaonyesha hatari iliyopo. Kwanza, KANU haikuiangusha FORD. FORD ilianguka kwa sababu ya migawanyiko yake yenyewe. Katika harakati za kutafuta mgombea bora, upinzani wa sasa unaweza kujikuta ukijenga migawanyiko itakayompa Ruto nafasi ya kushinda. Wakati FORD ilipoanzishwa, ilionekana kama serikali inayosubiri kuingia madarakani. Mikutano yake ilivutia umati mkubwa na viongozi wake waliheshimiwa kwa mchango wao katika mapambano ya kurejesha mfumo wa vyama vingi. Lakini chama hicho hakikuwahi kuafikiana kuhusu namna ya kumpata mgombea wake wa urais. Matokeo yake yalionekana wazi katika uchaguzi wa mwaka 1992. Upinzani uliingia uchaguzini ukiwa umegawanyika kati ya Matiba, Jaramogi na Kibaki. Moi aliibuka mshindi huku kura za upinzani zikigawanyika. Hilo lilichelewesha kuondolewa kwa KANU madarakani kwa takriban muongo mmoja. Leo, viongozi wa upinzani wanakabiliwa na mtihani kama huo. Gachagua amesema mgombeaji anaweza kutangazwa hata Mei 2027, ilhali Muturi ametaka uamuzi ufanywe mapema na tayari ameonyesha kumuunga mkono Kalonzo. Martha Karua pia amehoji mfumo unaopendekezwa wa kumpata mgombeaji. Wachambuzi wanasema miungano mingi haisambaratiki siku ya uchaguzi. Huvunjika mapema kila upande unapoanza kujijengea mtandao wake, kukusanya fedha na kuwashawishi wafuasi kuwa hakuna mgombeaji mwingine anayefaa. Hapo ndipo kinachoitwa athari ya Matiba huanza. Kila mwanasiasa anakubali umuhimu wa umoja, lakini kwa sharti kwamba umoja huo umuunge mkono yeye. Somo jingine muhimu ni kwamba sheria na taratibu zinapaswa kuwekwa kabla ya majina ya wagombeaji. FORD haikuwahi kukubaliana kuhusu mfumo wa kumpata mgombeaji wake, jambo lililochochea mzozo ulioigawa. Kwa upinzani wa sasa, bado hakuna makubaliano kuhusu sifa za mgombeaji, ratiba ya uteuzi wala mfumo wa kutatua migogoro. Historia pia inaonyesha kuwa umati mkubwa wa watu kwenye mikutano si lazima uwe ishara ya ushindi. Matiba aliporejea nchini mwaka 1992 na kupokelewa na maelfu ya watu, wengi waliamini alikuwa tayari ameshinda. Lakini mvutano kuhusu mgombeaji ndio uliovunja FORD. Aidha, muungano wowote unaotegemea tu kumpinga aliye madarakani huwa katika hatari ya kusambaratika. Swali ambalo Safina amekuwa ikiuliza ni: Baada ya Ruto, nini kitafuata? Kwa mujibu wa Wanjigi, upinzani unapaswa kueleza sera zake kuhusu ushuru, deni la taifa, ukosefu wa ajira, ufisadi, afya, elimu na gharama ya maisha badala ya kutegemea kaulimbiu ya "Wantam" pekee. Somo la mwisho ni kwamba umoja wa kweli huhitaji viongozi wengine kujinyima kwa manufaa ya lengo la pamoja. Hilo lilitokea mwaka 2002, Raila Odinga alipomuunga mkono Mwai Kibaki kwa kauli maarufu ya "Kibaki tosha", hatua iliyosaidia kuondoa KANU madarakani. Historia ya FORD si simulizi ya zamani tu. Ni onyo kwamba upinzani unaweza kuwa na uungwaji mkono mkubwa wa wananchi, lakini ukashindwa ikiwa viongozi wake watashindwa kuweka maslahi ya taifa mbele ya tamaa zao binafsi. Tatizo jingine ambalo lilichangia kusambaratika kwa FORD ni kwamba kila kiongozi aliamini historia yake ya kisiasa ilimpa haki ya kuwania urais. Jaramogi alijiona ndiye aliyekuwa amepigania demokrasia kwa miongo mingi dhidi ya tawala za Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi. Kwa upande wake, Matiba aliamini mateso aliyopitia, ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa bila kesi na kuugua kiharusi akiwa kizuizini, yalikuwa yamemjengea uhalali wa kuongoza upinzani. Kila mmoja alitumia historia yake kama msingi wa kudai tiketi ya urais. Hali kama hiyo inaonekana kujitokeza katika upinzani wa sasa. Baadhi ya viongozi wanategemea ukongwe wao kisiasa, wengine wanajivunia idadi ya wapiga kura kutoka maeneo yao, huku wengine wakisisitiza tajriba yao serikalini, uadilifu wao au mateso wanayodai kuyapata kutokana na kupambana na utawala uliopo. Ingawa hoja hizo zinaweza kuwapa nguvu kisiasa, hazitoshi kuwapa haki ya moja kwa moja ya kupeperusha bendera ya muungano. Kwa mujibu wa historia ya FORD, umoja wa kisiasa haujengwi kwa hoja za nani ameteseka zaidi au nani anaungwa mkono na watu wengi zaidi, bali kwa kuweka utaratibu unaokubalika na wote. Bila makubaliano ya wazi kuhusu namna ya kumpata mgombeaji na jinsi ya kushughulikia malalamishi yatakayojitokeza, tofauti za viongozi zinaweza kugeuka chanzo cha mgawanyiko na kuudhoofisha upinzani kabla hata ya kampeni rasmi kuanza.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 2 hours ago
Ruto, Sifuna walumbana kuhusu 'uwezo wa kuku kupanda orofa ya 12' ya Affordable Housing
RAIS William Ruto na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wamezua mjadala mkali kuhusu ujenzi wa nyumba za ghorofa chini ya Mpango wa Nyumba za Gharama Nafuu, baada ya kutofautiana kuhusu iwapo nyumba hizo zinafaa kwa maisha ya wakazi wa Magharibi mwa Kenya. Mzozo huo ulianza baada ya Sifuna kuhoji ujenzi wa nyumba za orofa 12 katika eneo la Funyula, akisema hazilingani na mtindo wa maisha wa jamii za eneo hilo. Akizungumza kwenye mahojiano katika kituo cha redio cha Mulembe FM Jumatano, Julai 22, 2026, Sifuna alitumia mfano wa kufuga kuku kukosoa mpango huo. "Wamejenga nyumba za orofa 12 za gharama nafuu Funyula. Sisi Waluhya hatuwezi kuishi mahali ambapo kuku wetu hawawezi kuishi. Niambie, kuku wako atafikaje kwenye orofa ya 12?" alihoji. Rais Ruto alimjibu Alhamisi, Julai 23, wakati wa katika Ikulu ya Nairobi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Wataalam watetea kiwanda cha mafuta cha Dangote Lamu
WATAALAMU wa miundomsingi, viwanda na maendeleo ya kimaeneo wameutetea mradi wa Sh2.2 trillioni wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi Lamu. Kiwanda hicho kitafadhiliwa na kampuni ya Dangote Group kutoka nchini Nigeria inayomilikiwa na tajiri wa Afrika, Bw Aliko Dangote. Licha ya kiwanda hicho kutajwa kuwa na manufaa tele endapo kitawekezwa Lamu, Kenya, wenyeji wanasema kwamba lazima watambuliwe, kushirikishwa na matakwa yao kuzingatiwa kwanza kabla ya hatua zozote za kutekeleza mradi huo kuendelezwa maeneo yao. Katika mahojiano na Taifa Jumapili, wataalamu, ikiwemo wafanyakazi wa idara za serikali, waliutaja mradi huo wa kiwanda cha mafuta kuwa suluhu ya pekee itakayobadilisha eneo la Lamu kwa uzuri. Kamishna wa Petroli kwenye Wizara ya Kawi na Petroli nchini, Bw Joseph Otieno, alisema mradi huo utabadilisha eneo hilo kuwa jungu la kiviwanda na maendeleo. Bw Otieno alisema Kenya imekuwa ikinunua na kusafirisha bidhaa za petroli kwa bei ghali kutoka nje, hasa mataifa ya Mashariki ya Kati kupitia bandari ya Mombasa. "Watu wa Lamu waondoe shaka. Mradi utatekelezwa kwa kuwazingatia. Kutakuwa na mikutano na makongamano ya kuwaelimisha wenyeji na umma kwa jumla ili wauelewe vyema mradi. Kutakuwa na vikao vya wadau wa serikali, mwekezaji na wakazi wa mashinani Lamu ambao ndio wenyeji wa mradi," akasema Bw Otieno. Aliongeza, "Lamu itapanuka kimaendeleo. Barabara zitaboreshwa, biashara zitanoga na sekta zote kunufaika. Hata utendakazi wa bandari ya Lamu pia utaboreka na kufanyika kwa njia ya haraka endapo kutakuwepo na kiwanda cha mafuta." Afisa Mtendaji na Mkurugenzi Mkuu wa Zamani wa Mradi wa Bandari ya Lamu, Uchukuzi na Miundomsingi ya Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia (LAPSSET), Dkt Silvester Kasuku alisema kuwekezwa kwa kiwanda cha Sh2.2 trilioni cha kusafisha mafuta kutaleta mwamko na taswira mpya ya Lamu kama eneo ambalo kihistoria lilikuwa limetelekezwa. Dkt Kasuku aliwahakikishia wakazi kwamba serikali itafanya kazi na kushirikiana nao kwa karibu wakati wa kutekelezwa kwa mradi huo. "Tushafanya kazi kwa karibu na jamii ya Lamu wakati tukitekeleza mradi wa Bandari ya Lamu na tukafaulu. Wananchi wa Lamu watambue kuwa tunawazingatia. Masuala ya ajira, utunzi wa mazingira, ufadhili wa kimasomo na mambo mengine, yote tutayajadili kwa pamoja na kuyakidhi katika kila hatua tutakazopiga wakati mradi utakapokuwa ukitekelezwa eneo hilo," akasema Dkt Kasuku. Mwenyekiti wa Zamani wa Muungano wa Save Lamu, Bw Mohamed Athman alitisha kuwa endapo vilio vyao kama jamii kuuhusu mradi vitakaidiwa basi hawatakuwa na budi ila kuelekea mahakamani kuuzuia mradi usifanyike eneo lao. Afisa Mtendaji wa Muungano wa Wanawake wa Lamu, Bi Raya Famau alishikilia haja ya jamii kuhusishwa kwenye vikao mbalimbali vya umma kutoa maoni kuhuuhusu mradi. Alisema wao hawapingi mradi ila furaha yao ni kuona haki zao za kijamii zikiheshimiwa. Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Shee Mbwana alimuomba mwekezaji, Bw Dangote kuweka kikao cha moja kwa moja na wanajamii ili waweze kutoa maoni na vilio vyao kuuhusu mradi. "Hatuna imani na serikali. Imekuwa ikitudhulumu ardhi zetu kila kunapowekezwa miradi mikuu eneo letu. Sasa tunamsihi Dangote afanye kikao cha moja kwa moja na sisi wanajamii ili tumpe vilio na mapendekezo yetu kabla mradi uendelee," akasema Bw Mbwana. Utakapokamilika, mradi huo utakuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku. Kiwanda hicho ambacho ni kikubwa zaidi Afrika Mashariki kinatarajiwa kujengwa kwa muda wa miaka mitatu. Kitasambaza bidhaa za petroli iliyosafishwa Kenya na pia nchi jirani, hivyo kupunguza hali ya ukanda wa Afrika Mashariki kutegemea mafuta yanayonunuliwa kutoka nje. Kiwanda hicho kinalengwa kujengwa eneo la Magogoni karibu na mradi wa Bandari ya Lamu ulioko Kililana, Lamu Magharibi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
Salasya sasa adai Sifuna hana umaarufu kisiasa
HUKU viongozi vijana wakichangamkia kuimarika kwa umaarufu wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya amepuuzilia mbali matokeo ya kura ya maoni uliofanywa na kampuni ya TIFA ambao kinara huyo wa Linda Mwananchi aling'aa. Akizungumza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii Julai 24, 2026, mbunge huyo alidai kuwa utafiti huo ulifadhiliwa na Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) kwa lengo la kuzua mgawanyiko ndani ya muungano wa upinzani. Salasya alidai kuwa madhumuni ya utafiti huo yalikuwa kuonyesha kuwa vuguvugu la Linda Mwananchi linaungwa mkono zaidi kuliko muungano wa upinzani, jambo alilosema lilinuia kudhoofisha ushawishi wa viongozi wa upinzani kama kvile Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua. Pia aliubeza utafiti huo kwa kejeli, akisema iwapo mwelekeo huo utaendelea, basi Sifuna atakuwa na asilimia 80 ya umaarufu katika utafiti ujao. Alisisitiza kuwa matokeo hayo hayana uhalali. "NIS wanafanya kazi ya punda kugawanya upinzani kwa kuonyesha Linda Mwananchi inaungwa mkono zaidi kuliko Muungano wa Upinzani. Tiketi ya Sifuna/Matiang'i sasa ndiyo inaongoza, na hivyo kumfanya Kalonzo na Rigathi waonekane si lolote kisiasa. Kwa kweli, wiki ijayo Sifuna atakuwa na asilimia 80 katika kura za maoni kama mgombeaji bora wa urais," alisema Salasya. Kauli za Salasya zilijiri muda mfupi baada ya TIFA kutoa matokeo ya utafiti wake wa hivi punde kuhusu wanaopendelewa kuwania urais, uliomweka Rais William Ruto kileleni kwa asilimia 24 ya uungwaji mkono. Kwa mujibu wa utafiti huo, Sifuna alishika nafasi ya pili kitaifa kwa kupata asilimia 15, na hivyo kuwa mwanasiasa wa upinzani aliyeongoza kwa umaarufu. Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i alifuatia kwa asilimia 14, huku kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akishika nafasi ya nne kwa asilimia 13.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Ndoa kati ya Ruto na Oburu ni ya kulazimisha- TIFA
Wakenya wengi wanapinga ushirikiano wa kisiasa kati ya ODM na UDA, hali inayozua maswali kuhusu mustakabali wa mpango huo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Haya ni kwa mujibu wa utafiti mpya wa kampuni ya Trends and Insights for Africa (TIFA) uliofanywa kati ya Juni 13 na 22, 2026, ukihusisha watu 2,048 kutoka kaunti zote 47 nchini na ambao matokeo yake yalitolewa Ijumaa. Utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 52 ya Wakenya wanapinga Serikali Jumuishi, huku asilimia 30 pekee wakiunga mkono mpango huo. Asilimia 15 hawakuwa na maoni huku asilimia nne wakisema hawaufahamu ushirikiano huo. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa licha ya ushirikiano wa karibu miaka miwili kati ya Rais William Ruto na ODM kufuatia maandamano ya Gen Z ya mwaka 2024, bado umma haujaukubalika kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa TIFA, kiwango cha uungwaji mkono kwa ndoa ya vyama hivyo kimeendelea kubaki karibu kilekile kwa mwaka mmoja uliopita. Kilikuwa asilimia 22 Mei 2025, kikaongezeka hadi asilimia 44 Agosti mwaka huo kabla ya kushuka hadi asilimia 30 Novemba 2025. Katika utafiti wa sasa, kimeendelea kusalia asilimia 30. Ripoti hiyo inasema mgawanyiko unaoendelea ndani ya ODM kuhusu iwapo chama hicho kinafaa kuunga mkono azma ya Rais Ruto ya kutetea urais mwaka 2027 umefunga kiwango ambacho ushirikiano huo unaweza kupata uungwaji mkono. Hakuna eneo lolote kati ya kanda tisa za utafiti lililoonyesha wengi wanaounga mkono ushirikiano huo. Eneo la kati la Bonde la Ufa linaongoza kwa asilimia 47 ya wanaounga ushirikiano huo, likifuatiwa na Kaskazini mwa Kenya kwa asilimia 43 na Nyanza kwa asilimia 35. Magharibi ina asilimia 29, Pwani asilimia 31, Kusini mwa Rift Valley asilimia 25, Nairobi asilimia 22, Kusini Mashariki asilimia 30 na Mlima Kenya asilimia 13. TIFA pia imebaini kuwa uungwaji mkono umeshuka kwa kasi zaidi Magharibi mwa Kenya, kutoka asilimia 62 Novemba 2025 hadi asilimia 29 sasa. Nyanza pia imeshuka kutoka asilimia 59 hadi 35, huku Mlima Kenya na Kaskazini mwa Kenya zikisajili kupungua kwa uungwaji mkono. Ripoti hiyo inahusisha hali hiyo na mvutano unaoendelea ndani ya ODM kati ya makundi ya Linda Mwananchi na Linda Ground kuhusu mustakabali wa chama na ushirikiano wake na Kenya Kwanza. Viongozi kama Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi wameendelea kupinga ushirikiano wa karibu na serikali. Wapigakura ambao hawajaamua Wakati huo huo, utafiti huo unaonyesha kuwa uchaguzi wa urais wa 2027 huenda ukaamuliwa katika maeneo yenye wapigakura wengi ambao bado hawajaamua upande wa kuunga mkono. Mlima Kenya, wenye takriban wapiga kura milioni 5.7, umejitokeza kuwa uwanja mkubwa wa kisiasa. Asilimia 25 ya wakazi wa eneo hilo bado hawajaamua mgombea watakayemuunga mkono. Nairobi pia imejitokeza kuwa uwanja muhimu wa kisiasa. Kalonzo anaongoza kwa asilimia 23, akifuatiwa kwa karibu na Sifuna kwa asilimia 22 na Matiang'i kwa asilimia 17. Rais Ruto anaungwa mkono na asilimia sita huku Gachagua akiwa na asilimia nane. Asilimia 21 ya wakazi wa jiji bado hawajaamua. Pwani pia imeonekana kuwa eneo la ushindani mkali. Sifuna anaongoza kwa asilimia 27, Rais Ruto asilimia 21, Kalonzo asilimia 10 na Matiang'i asilimia tisa. Asilimia 21 ya wakazi bado hawajafanya uamuzi. Katika eneo la Kusini Mashariki, Kalonzo ameendelea kutawala ngome yake kwa asilimia 58 dhidi ya asilimia 15 za Rais Ruto. Ni asilimia tisa pekee ambao hawajaamua. Magharibi mwa Kenya pia inaonekana kuwa eneo litakaloamua matokeo ya uchaguzi. Sifuna anaongoza kwa asilimia 28, Rais Ruto asilimia 14 na Matiang'i asilimia 12. Hata hivyo, asilimia 31 ya wakazi bado hawajafanya uamuzi. Kwa upande mwingine, Rais Ruto anaendelea kutawala Kaskazini mwa Kenya kwa asilimia 61 ya uungwaji mkono na bado ana nguvu katika baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa. Nyanza nayo inaendelea kuwa ngome ya upinzani, ingawa ushindani unaongezeka huku Matiang'i akipata asilimia 29 na Rais Ruto asilimia 30. Kwa mujibu wa Katiba, mgombea wa urais lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura halali pamoja na angalau asilimia 25 ya kura katika zaidi ya nusu ya kaunti zote nchini. Kutokana na hali hiyo, TIFA inaeleza kuwa ushindi wa mwaka 2027 hautategemea tu ngome za kisiasa bali pia uwezo wa vyama kuwashawishi mamilioni ya wapiga kura ambao bado hawajaamua katika maeneo kama Mlima Kenya, Nairobi, Magharibi na Pwani. Utafiti huo unatarajiwa kuathiri mikakati ya kampeni za kisiasa, huku Kenya Kwanza na viongozi wa upinzani wakiongeza juhudi za kuvutia wapigakura katika maeneo hayo muhimu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Wanawake pia hutumika kueneza uhuni wa kisiasa-Utafiti
WANAWAKE wanazidi kuwa sehemu muhimu lakini isiyoonekana ya mitandao ya wahuni wa kisiasa nchini, huku wakitumika kuhamasisha vijana, kusafirisha silaha kwa siri na kukusanya taarifa za kisiri, utafiti mpya umebaini. Kwa miaka mingi, macho ya umma yamekuwa yakielekezwa kwa vijana wanaume wanaovamia mikutano ya kisiasa na maandamano wakiwa na rungu na mawe. Hata hivyo, ripoti mpya inaonyesha kuwa nyuma ya vurugu hizo kuna mtandao uliopangwa vyema unaowahusisha pia wanawake. Kijana mmoja kutoka Mathare, Nairobi, aliyekubali kuzungumza na Taifa Jumapili kwa masharti ya kutotajwa jina kwa hofu ya usalama wake, alisema wanawake wamekuwa sehemu ya mfumo huo. "Bila shaka wapo. Huenda wasiwe mstari wa mbele, lakini wanashiriki kikamilifu," alisema. Kijana huyo, anayejitambulisha kama mmoja wa "vigogo" wa eneo hilo wanaotafutwa na wanasiasa na wafanyabiashara kuwasaka vijana kwa shughuli za kisiasa, alisema hawabagui wanawake wanapofanya uajiri. "Sisi ndio viongozi wanaotafutwa na wanasiasa wanapohitaji watu. Hatujali jinsia. Tunawaajiri wanawake, nao pia huleta wengine," alisema. Kwa mujibu wake, wanawake mara nyingi hawashiriki moja kwa moja katika mashambulizi, bali hujichanganya na umati ili mikutano ionekane kuwa na watu wengi kuliko ilivyo. Pia hukusanya taarifa, huwatetea wenzao wanapokamatwa na wakati mwingine husafirisha mawe au silaha ndogo wanazofichwa kwenye mikoba yao. "Kama hujui utakula nini mchana au jioni, huwezi kuanza kuuliza kama mwanamke anafaa kujiunga na kundi au la," alisema. Hata hivyo, alisema hajawahi kuona mwanamke akifikia kiwango cha kuwa kiongozi mkuu wa mtandao huo, ingawa wengi hutumiwa kuajiri wengine. Ripoti inayoitwa Goonland: Looking Beyond the Money and Violence in the Political Exploitation of Young Men, iliyoandaliwa na shirika la OdipoDev, inaeleza kuwa magenge ya kisiasa si mkusanyiko wa vijana wasio na ajira pekee, bali ni mtandao wenye viongozi, waajiri, wajumbe na waratibu wanaofanya kazi kwa mpangilio maalumu. Utafiti huo ulifanywa kupitia mahojiano na wanachama 40 wa magenge ya wahuni, waajiri watano na maafisa watano wa usalama kutoka Nairobi, Mombasa na Kiambu. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mawasiliano hufanywa kupitia makundi ya WhatsApp na vituo vya mitaani, huku fedha na silaha zikisafirishwa kwa siri kupitia watu wanaoaminika. Wanawake ni miongoni mwa watu hao wanaoaminiwa kusafirisha na kuficha silaha kwa kuwa hawashukiwi kirahisi wakati wa ukaguzi kuhusu usalama. Mzee wa kijiji cha Mathare, Joseph Ouna, alisema akina mama wachanga wanazidi kuvutwa katika shughuli hizo kutokana na ugumu wa maisha. "Akina mama hawa wana watoto, na vijana hawa ni marafiki wao. Wanawapa pesa na kuwasaidia kwa mahitaji mbalimbali, hivyo huwa rahisi kuwashawishi wakubali kazi za kisiasa," alisema. Aidha, alisema baadhi ya wanawake hujitokeza kuwatetea vijana hao wanapokamatwa kwa kuwasawiri kama waathiriwa badala ya wahusika wa vurugu. Mratibu mmoja wa kisiasa kutoka Kayole ambaye hakutaka kutajwa jina alisema aliwahi kuombwa na mwanamke mwenzake amtafutie vijana kwa shughuli za kisiasa lakini alikataa kwa kuhofia kukamatwa au kushambuliwa. Alidai pia kuwa rafiki yake mmoja alipelekwa Ol Kalou kuvuruga uchaguzi mdogo uliofanyika eneo hilo. "Nilimshawishi asiende lakini alikataa. Hadi leo sijui alilipwa kiasi gani," alisema. Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Nyandarua Central, Kenneth Kiprop, alisema hakuna mwanamke aliyekamatwa kufuatia vurugu za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, wala uchunguzi haukubaini wanawake walioshiriki moja kwa moja katika mashambulizi hayo. Utafiti huo unaonyesha kuwa fedha ndizo kichocheo kikuu cha vijana kujiunga na magenge hayo. Kuvuruga mikutano ya kisiasa hulipwa kati ya Sh500 na Sh1,500, shughuli za kuvuruga maandamano hulipa Sh500 hadi Sh2,500, huku migogoro ya ardhi ikilipa kati ya Sh500 na Sh2,000. Hata hivyo, watafiti wanasema si pesa pekee zinazowafanya vijana wabaki kwenye mitandao hiyo. Wengi walieleza kuwa hupata wanatambuliwa, kupata ulinzi, hadhi na hisia ya kuwa sehemu ya kundi. Ripoti hiyo inaonya kuwa kuanzisha nafasi za ajira pekee hakutamaliza tatizo la magenge ya kisiasa, kwa sababu wanaojiunga nayo hujengewa uhusiano unaotokana na hofu na mshikamano wa kijamii ambao si rahisi kuuvunja.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Wantam: Sifuna aoshewa lami, apokelewa kishujaa Bungoma
KIFO cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kimebadilisha kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa siasa za Kenya, huku Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna akiibuka kama mmoja wa viongozi wanaotikisa hesabu za uchaguzi mkuu wa 2027. Baada ya kuondolewa kama Katibu Mkuu na msemaji wa ODM, Sifuna sasa anaongoza vuguvugu la Linda Mwananchi, ambalo wachambuzi wanasema linaweza kubadili kabisa sura ya siasa za nchi na kutatiza mipango ya serikali pamoja na upinzani. Ndani ya ODM, baadhi ya viongozi wanakiri kuwa kumuondoa Sifuna kutoka uongozi wa chama kulikuwa kosa kubwa. Hata hivyo, sasa anaongoza vuguvugu linalovutia wafuasi wengi, hasa vijana, na ambazo zinazidi kupata nguvu kote nchini. Umaarufu wake umewatia wasiwasi viongozi wa kisiasa wa Magharibi kama Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambao wamekuwa wakijitambulisha kama vinara wa eneo hilo. Jana, Sifuna aliongoza mikutano mikubwa ya kisiasa katika Kaunti ya Trans Nzoia na kutangaza kuwa yuko tayari kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2027. Akizungumza katika mkutano wa mwisho mjini Kitale, Sifuna alimshukuru Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kwa kumuunga mkono na kumhimiza azunguke nchi nzima kutafuta uungwaji mkono. "Nimekubali jukumu hilo. Niko tayari kuzunguka Kenya nzima kutafuta kura na sitawaangusha Wakenya," alisema. Sifuna alidai kuwa upinzani utaungana na kumteua mgombeaji mmoja wa urais atakayemenyana na Rais William Ruto katika uchaguzi ujao. Baada ya mikutano hiyo, msafara wa viongozi hao ulipitia Kaplamai na kusimama katika soko la Sibanga, Cherang'any, kabla ya kurejea Kitale kwa mkutano wa mwisho. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni wa TIFA uliotolewa Ijumaa, Sifuna amempiku kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika umaarufu wa urais kwa mara ya kwanza. Katika utafiti huo, Sifuna alipata asilimia 15 ya uungwaji mkono, akifuatiwa na Naibu Kiongozi wa Jubilee Fred Matiang'i kwa asilimia 14, Kalonzo Musyoka asilimia 13, kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua asilimia saba na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino asilimia mbili. Kwa jumla, viongozi wa upinzani wanaungwa mkono na asilimia 51 ya Wakenya, huku Rais William Ruto akiongoza kivyake kwa asilimia 24. Hata hivyo, kiwango hicho bado hakitoshi kumwezesha kushinda uchaguzi katika duru ya kwanza. Kinachowashangaza wengi si tu umaarufu wa Sifuna bali kasi aliyopanda nayo. Miezi miwili iliyopita hakuwa hata akitajwa katika mazungumzo ya wagombeaji urais. Sasa ameibuka kama mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini. Katika uchaguzi wa Seneti wa Nairobi mwaka 2022, Sifuna alimshinda Askofu Margaret Wanjiru kwa kura 716,876. Leo, umaarufu wake unatajwa kuwa unaweza kubadili mazungumzo ya muungano wa upinzani kuhusu mgombeaji mmoja wa urais. Hata baada ya kuondolewa katika uongozi wa ODM, utafiti unaonyesha karibu nusu ya wafuasi wa chama hicho wangependa awe mgombeaji wao wa urais. Matokeo hayo yanaendana na utafiti wa awali wa Infotrak uliomuonyesha Sifuna akipunguza pengo kati yake na viongozi waliokuwa wakitajwa kama vigogo wa upinzani, jambo linaloashiria kuwa kupanda kwake si bahati bali ni mwelekeo mpya wa kisiasa. Akizungumza baada ya matokeo ya utafiti huo kutolewa, Sifuna alisema jambo muhimu si asilimia aliyopata, bali ni kwamba Rais Ruto anaendelea kushuka chini ya kiwango kinachohitajika kushinda uchaguzi kwa urahisi. Alisema iwapo upinzani utaungana nyuma ya mgombeaji mmoja, utaweza kumshinda Rais Ruto. "Tukijumlisha asilimia za Sifuna, Kalonzo, Matiang'i na viongozi wengine wa upinzani, ziko juu zaidi ya za Rais Ruto. Tunahitaji umoja ili kuwasikiliza Wakenya wanaotaka mabadiliko," alisema. Mchambuzi wa siasa Arnold Maliba alisema wengi wanakosea kuchukulia Linda Mwananchi kama muungano wa kawaida wa kisiasa. Kwa mujibu wake, vuguvugu hilo linalenga kubadili mjadala wa kisiasa kutoka ukabila na makubaliano ya viongozi kuelekea masuala ya utawala bora, uwajibikaji, Katiba na ushiriki wa wananchi. "Linda Mwananchi si chama cha kawaida. Ni vuguvugu linaloweka shinikizo kwa serikali na pia kwa upinzani uliopo," alisema. Kwa Rais Ruto, kupanda kwa Sifuna kunamaanisha hatari ya kupoteza kura za eneo la Magharibi, ambazo ni muhimu katika azma yake ya kutetea urais, hasa baada ya kupoteza uungwaji mkono mkubwa katika Mlima Kenya. Ndani ya upinzani, kuibuka kwa Sifuna kumebadili hesabu zilizoweka Kalonzo Musyoka na Fred Matiang'i kama wagombeaji wakuu wa urais.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Gachagua aapa kuzima njama za kuleta mgawanyiko Mlimani
KIONGOZI wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, ameapa kupinga kile alichokitaja kama njama za Rais William Ruto kugawanya eneo la Mlima Kenya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Akizungumza katika mikutano ya hadhara mjini Embu, Kathangariri, Karurumo, Gategi na Siakago Jumamosi, Gachagua alimshutumu Rais Ruto kwa kutumia Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku kuendeleza mpango wa kugawanya eneo hilo kuwa Mlima Kenya Mashariki na Magharibi. "Lazima nimzuie Ruto kugawanya Mlima Kenya. Tunataka tubaki pamoja ili tumpeleke nyumbani katika uchaguzi ujao," alisema Gachagua katika soko la Kathangariri, Embu. Alidai Rais Ruto amewasaliti wakazi wa Mlima Kenya waliomuunga mkono kwa wingi 2022 kwa kuwaita wakabila. Pia alimshutumu Rais kwa madai ya kuruhusu makundi ya wahuni kuwashambulia wakazi wa Mlima Kenya na kuharibu mali yao. "Nitahakikisha Ruto anakuwa rais wa muhula mmoja. Kilichotokea Ol Kalou kitajirudia katika Mlima Kenya mzima," alisema. Gachagua pia alimkosoa Waziri wa Afya Aden Duale kwa madai ya kutoa matamshi ya kuwadhalilisha wakazi wa Mlima Kenya, akisema atawajibishwa kisiasa katika uchaguzi ujao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 20 hours ago
Kavulani amwonya Asefa, aapa kumlaza mapema kwenye pambano Ndondi
Bondia wa Kenya Jane Kavulani ametuma onyo kali kwa mpinzani wake Roman Asefa Abate wa Ethiopia akiahidi kumwangusha kwa kushinda kwa 'Knockout' yaani KO katika raundi za kwanza, watakapokutana katika mashindano ya ndondi yatakayofanyika Jumamosi hii kwenye ukumbi wa Edge Convention Centre jijini Nairobi. Kavulani, anayefanya mazoezi katika ukumbi wa Pal Pal Gymnasium uliopo Gikomba jijini Nairobi, alisema amejiandaa vya kutosha na hana shaka ya kuibuka mshindi dhidi ya Methiopia huyo ambaye atakuwa akicheza pambano lake la kwanza la kulipwa. "Nimefanya maandalizi ya kutosha. Lengo langu ni kumaliza pambano mapema kwa KO na kuwapa mashabiki ushindi wa kujivunia," alisema Kavulani. Hata hivyo, Asefa naye ameonyesha kujiamini akisema ananuia kuanza maisha yake ya ndondi za kulipwa kwa ushindi na kurejea Ethiopia akiwa ameshinda pambano lake la kwanza. Zaidi ya mapambano hayo ya wanawake uzani wa featherweight, mashabiki watashuhudia jumla ya mapambano 11 kwenye usiku huo wa ngumi uliofadhiliwa na SportPesa na kuandaliwa na promota Maurice Odera kupitia kampuni ya UFS BXNG. Pambano kuu la usiku litamshuhudia bingwa wa Kenya na Afrika Mashariki Javan Buyu akipambana na Ramadhani Idd wa Tanzania kuwania taji la Universal Boxing Organisation (UBO) Inter-Continental Lightweight katika pambano la raundi 10. Buyu anatarajiwa kutumia uzoefu wake mbele ya mashabiki wa nyumbani huku Idd akinuia kuvuruga mipango ya Mkenya huyo kwa kutwaa taji hilo na kuliondoka nalo Tanzania. Buyu, ambaye ni bingwa wa Kenya na Afrika Mashariki, ana nafasi ya kutwaa taji lake la tatu la kulipwa na kuwa miongoni mwa mabondia wachache wa Kenya kushinda mkanda wa ngazi ya mabara. Bondia huyo amesema yuko tayari kwa mtihani huo baada ya kufanya maandalizi ya miezi mitatu bila kuacha jambo lolote kwa bahati. "Nimekuwa nikifanya mazoezi na kumuomba Mungu kwa ajili ya taji hili. Mimi na timu yangu tumefanya kazi kubwa kujiandaa kwa Julai 25 na tuko tayari. Tumeimarisha kila eneo muhimu litakalotupa ushindi," alisema Buyu. Buyu alitwaa ubingwa wa Kenya Oktoba mwaka jana baada ya kumshinda Christopher Osicho kabla ya kuongeza mkanda wa PST kwa kumcharaza Mtanzania Nasoro Madimba kwa Technical Knockout katika raundi ya tatu mapema mwaka huu. Amesema tayari amemchunguza Ramadhani kupitia video zake. "Ni bondia mzuri, ningempa alama saba kati ya 10, lakini nina kila kitu kinachohitajika kumlazimisha akate tamaa. Namwahidi pambano zuri, lakini aandae moyo wa kukubali kushindwa," alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 23 hours ago
Wetang'ula: Ukabila hauna nafasi katika siasa za Kenya
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula amewataka viongozi wa kisiasa kuachana na siasa za ukabila na kuhubiri umoja wa kitaifa, akionya kuwa matamshi ya chuki yanaweza kugawanya taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Akizungumza Jumamosi katika eneo la Oloiborsoito, Kilgoris, Kaunti ya Narok, wakati wa hafla ya kuchangia fedha Shirika la Wanawake la Olerai, Wetang'ula alisema tofauti za kisiasa hazipaswi kugeuka kuwa chuki, vurugu au uhasama wa kikabila. "Mtu yeyote anayehubiri ukabila ana fikra za zamani. Tunaweza kutofautiana kisiasa, lakini hiyo si sababu ya kutukanana au kuumizana," alisema. Aliwataka wanasiasa kuepuka matamshi ya uchochezi yanayoweza kuwashawishi vijana kuingia katika vurugu, akisisitiza kuwa viongozi wana wajibu wa kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa. "Siasa hazipaswi kuwa sababu ya umwagaji damu. Vijana ni mustakabali wa taifa na hawapaswi kutumiwa katika migogoro ya kisiasa," alisema. Wetang'ula alisema kuwawezesha wanawake na vijana kupitia ujuzi na fursa za kiuchumi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Pia alisifu jamii ya Wamaasai kwa kuhifadhi utamaduni wao, akisema umechangia kukuza utalii nchini. Spika huyo alimkosoa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa madai ya kutoa matamshi yanayoweza kudhoofisha sekta ya utalii, huku akitoa wito wa kutungwa kwa sheria zitakazolinda wachimbaji madini na kuwawezesha kunufaika na rasilimali za taifa. Katika hafla hiyo, mshauri wa Rais William Ruto, Farouk Kibet, aliwataka wakazi wa Kilgoris kuishi kwa amani, huku Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot akilaani siasa za ukabila na kuitaka Wizara ya Usalama kuchukua hatua dhidi ya viongozi wanaotoa matamshi ya uchochezi. Mbunge wa Kitutu Chache North Japheth Nyakundi aliwataka viongozi kuzingatia sera za maendeleo badala ya siasa za kikabila, huku Mbunge wa Kibwezi West Mwengi Mutuse akitetea rekodi ya maendeleo ya serikali ya Rais William Ruto.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 25 Jul 2026 03:55:09
Waziri Duale motoni kwa kauli tata ya kueneza ukabila
WAZIRI wa Afya, Aden Duale analaumiwa kufuatia matamshi yake kuhusu jamii za Kenya kuzua mjadala mkubwa nchini, huku Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ikianzisha uchunguzi kubaini iwapo kauli hizo zilichochea mgawanyiko wa kikabila. Video iliyosambaa kwa kasi mitandaoni ilimuonyesha Bw Duale akizungumza kwa lugha ya Kisomali katika mkutano uliofanyika eneo la Lafey, Kaunti ya Mandera, Julai 20, 2026. Katika hotuba hiyo, alisema utawala wa Rais William Ruto umefanya maendeleo makubwa zaidi katika eneo la Kaskazini Mashariki kuliko tawala za marais waliotangulia, akiwemo Hayati Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta. Pia alieleza kuwa jamii ya Wasomali ina watu takriban milioni 41 duniani na kudai kuwa kwa muda mrefu baadhi ya jamii zimekuwa zikitawala siasa na nafasi muhimu serikalini huku maeneo mengine yakisalia nyuma. Hata hivyo, matamshi hayo yamekosolewa vikali na viongozi wa kisiasa na wananchi walioyataja kuwa ya uchochezi na yanayoweza kuvuruga mshikamano wa kitaifa. Mnamo Ijumaa, NCIC ilisema imeanza uchunguzi kuhusu matamshi hayo. "Timu ya uchunguzi ya Tume inaendelea kufanya uchunguzi bila upendeleo kuhusu matamshi hayo. Tunawahimiza viongozi kujiepusha na kauli zinazoweza kuchochea chuki za kikabila na kuwakumbusha kuwa Kenya ni ya Wakenya wote," alisema mwenyekiti wa NCIC, Askofu Kepha Omae. Aliongeza kuwa tume itaendelea kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mtu yeyote atakayehatarisha umoja wa taifa, hasa wakati nchi inaelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru alisema kauli za Duale zilikuwa za kusikitisha na hatari. "Ni jambo hatari na la kupotosha kueleza changamoto za kisiasa kwa misingi ya ukabila. Kauli kama hizo hazikubaliki kutoka kwa kiongozi mwenye hadhi ya Waziri wa Baraza la Mawaziri," alisema. Suala hilo pia liliibuliwa katika Seneti ambapo Maseneta Enoch Wambua (Kitui), Ledama Ole Kina (Narok) na Abdul Haji (Garissa) walitaka viongozi kuwa waangalifu wanapozungumza kuhusu masuala ya kikabila. Seneta Ole Kina alisema viongozi wana jukumu la kuwaunganisha Wakenya. "Nilimsikia Waziri akilinganisha jamii na kuacha taswira kwamba jamii moja ni bora kuliko nyingine. Kauli kama hizi zinaweza kurudisha taifa kwenye siasa za migawanyiko," alisema. Seneta Wambua alionya kuwa matamshi hayo yanawakumbusha Wakenya hali ilivyokuwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2007. "Tuliona kilichotokea mwaka 2007 baada ya viongozi kuanza kutumia lugha ya chuki. Tunapoelekea uchaguzi wa 2027, viongozi wanapaswa kuhubiri amani badala ya kuwagawa wananchi," alisema. Seneta Abdul Haji alisema iwapo Duale alitoa matamshi hayo kama yalivyosikika kwenye video, basi ilikuwa makosa. Aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando pia alimkosoa Duale, akidai kauli zake zinaakisi msimamo wa utawala wa sasa. Akijibu lawama hizo, Duale alisema kauli zake zilitokana na methali ya jadi ya Kisomali ambayo imetafsiriwa vibaya na kutumiwa kisiasa. Alisema methali hiyo inamrejelea mnyama mwenye tabia ya kujinufaisha na inalenga watu au makundi yaliyozoea kunufaika na mamlaka na rasilimali kiasi kwamba inakuwa ugumu kukubali kugawa nafasi kwa jamii nyingine. Kwa mujibu wa Duale, alichomaanisha ni kwamba tangu uhuru, eneo la Mlima Kenya limekuwa likishikilia nafasi za juu serikalini, ikiwemo urais au makamu wa rais, na kwamba Rais Ruto amejaribu kupanua ushirikishaji kwa kuwapa nafasi Wakenya kutoka jamii mbalimbali. Pia alimshutumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa madai ya kutoa matamshi yaliyolenga Wasomali, ikiwemo kuita Kaskazini Mashariki eneo la ugaidi, kupinga kuondolewa kwa mfumo wa ukaguzi wa vitambulisho kwa Wasomali na kuhoji uteuzi wa Wasomali katika nyadhifa za serikali. Alipoulizwa iwapo angeomba msamaha, Duale alisema taarifa aliyotoa tayari ilifafanua alichomaanisha. "Maneno yangu yanajieleza yenyewe," alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 25 Jul 2026 02:55:02
Kaunti zadaiwa Sh50b, michango ya pensheni ya wafanyakazi
BARAZA la Magavana (CoG) limetaka maafisa wa kaunti wanaoshindwa kuwasilisha michango ya pensheni iliyokatwa kutoka mishahara ya wafanyakazi wachukuliwe hatua za jinai, huku madeni hayo yakifikia zaidi ya Sh50 bilioni. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Hazina ya Pensheni (RBA), Charles Machira alisema mashirika ya umma, yakiwemo serikali za kaunti, yanadaiwa zaidi ya Sh71.4 bilioni za michango ambayo ilikatwa lakini haikuwasilishwa. Ingawa CPF Group, inayosimamia pensheni za wafanyakazi wa kaunti, imeendelea kuongeza wanachama na mali zake, kutowasilishwa kwa michango hiyo kumetajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa ukuaji wa hazina hiyo. Akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa CPF Group, Mkurugenzi Mkuu, Hosea Kili alisema taasisi hiyo inaendelea na mazungumzo na serikali za kaunti, Baraza la Magavana na Wizara ya Fedha ili kutafuta suluhu ya madeni hayo. "Hazina ilipata faida ya asilimia 10 mwaka huu, jambo linaloonyesha uthabiti wa uwekezaji wa muda mrefu. Hata hivyo, kutowasilishwa kwa michango na waajiri ni changamoto kubwa. Sielewi kwa nini mshahara unalipwa pamoja na makato ya kisheria lakini fedha hizo haziwasilishwi kwenye hazina husika," alisema Kili. Alisema ukuaji wa mali umeathiriwa na madeni ya zaidi ya Sh50 bilioni ya michango ambayo haijawasilishwa. Naye Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Ahmed Abdullahi alisema kutowasilisha michango iliyokatwa kutoka mishahara ya wafanyakazi ni kosa la jinai. "Ni uhalifu kukata fedha za mfanyakazi halafu ukose kuziwasilisha. Inasikitisha kuwa maafisa wanaohusika, wakiwemo maafisa wa mishahara, wakaguzi wa hesabu, mabunge ya kaunti na Seneti, wameshindwa kuhakikisha sheria inafuatwa. Maafisa wanaosimamia mishahara lakini hawawasilishi makato wanapaswa kukamatwa," alisema. Aliongeza kuwa madeni yanapodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja huwa vigumu kulipwa kutokana na vikwazo vya bajeti. "Wasimamizi wa hazina ya pensheni wahakikishe serikali za sasa za kaunti hazimalizi muhula wao zikiwa na madeni mapya. Madeni ya zamani yashughulikiwe kivyake kupitia mpango maalumu wa malipo," alisema. Wadau pia wamependekeza hatua mbalimbali za kumaliza tatizo hilo, ikiwemo kubadilishana madeni na mali na kukata michango moja kwa moja kabla fedha hazijafika kwa kaunti. Bw Kili alilitaka Baraza la Magavana kushawishi wizara ya fedha kutoa hati za dhamana kwa niaba ya kaunti zote 47 ili kuharakisha ulipaji wa madeni hayo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 25 Jul 2026 01:55:34
Ushahidi muhimu uliomwangusha Obado
KESI ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado, aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na Caspal Obiero ilidumu kwa miaka saba na miezi 10, huku upande wa mashtaka ukiwasilisha mashahidi 42 kueleza jinsi mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno alivyouawa. Hata hivyo, hukumu ilitegemea ushahidi wa watu wachache muhimu waliowahusisha washtakiwa hao na mauaji hayo. Miongoni mwao alikuwa shahidi aliyelindwa, aliyetambulishwa kama XYZ, ambaye ni mwanahabari aliyekuwa akichunguza uhusiano kati ya Sharon na Obado. Ushahidi wake uliungwa mkono na dereva wa teksi Jackson Otieno Gombe, aliyewasafirisha Sharon, XYZ na watu waliomteka siku ya mauaji. Jaji Cecilia Githua alisema ushahidi ulionyesha kuwa mkutano uliofanyika katika Hoteli ya Graca mnamo Septemba 3, 2018 haukuwa wa kuwasilisha ujumbe kutoka kwa Obado kwa Sharon kama Oyamo alivyodai, bali ulikuwa hatua ya kumkabidhi Sharon kwa wauaji wake. "Ninaamini mkutano wa Hoteli ya Graca haukuwa wa kuwasilisha ujumbe bali ulikuwa wa kuwakabidhi Sharon na XYZ kwa wauaji wa Sharon," alisema jaji. Jaji Githua alisema Sharon na mwanahabari XYZ walikuwa tishio kwa hadhi ya Obado kwani tayari walikuwa wameanza kufikisha suala hilo kwa vyombo vya habari.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 25 Jul 2026 00:55:50
Ruto aendeleza juhudi za kuvutia vijana akitafuta Tutam
RAIS William Ruto ameongeza juhudi za kuwavutia vijana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 baada ya kuzindua mpango wa Sh2 bilioni wa kuwawezesha kupata ajira kupitia mafunzo kazini, nafasi za kazi za kidijitali na ushirikiano na sekta ya kibinafsi. Mpango huo wa NextGen Youth Empowerment Programme, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali, Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) na sekta ya kibinafsi, unalenga kuwapa vijana ujuzi na uzoefu unaohitajika katika soko la ajira. Hatua hiyo inajiri huku serikali ya Kenya Kwanza ikijaribu kurejesha imani ya vijana baada ya miezi kadhaa ya malalamiko kuhusu ukosefu wa ajira, ushuru mkubwa na gharama ya juu ya maisha. Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), zaidi ya Wakenya milioni 22.1 walikuwa wamejisajili kupiga kura mwaka 2022, huku walio na umri wa kati ya miaka 18 na 34 wakiwa zaidi ya nusu ya wapigakura wote. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Rais Ruto alisema serikali imeamua kuwekeza katika mipango inayounganisha elimu na ajira. "Mafunzo kazini si kazi za muda tu. Ni daraja kati ya kujifunza na kujipatia kipato, kati ya uwezo na utendaji, na kati ya ndoto na mafanikio. Leo tunajenga daraja hilo kwa vijana wa Kenya kupitia mpango wa NextGen," alisema. Rais alikiri kuwa wahitimu wengi hukumbwa na changamoto ya kupata ajira kwa sababu waajiri wanahitaji uzoefu wa kazi kuliko vyeti vya kitaaluma. "Waajiri wanatafuta uzoefu wa vitendo, nidhamu kazini na ujuzi unaohitajika na sekta mbalimbali. Vipaji vinapokosa nafasi, ndoto huchelewa kutimia na taifa hupoteza uwezo wake wa uzalishaji," alisema. Alisema vijana 100,000 walioajiriwa kama walimu chini ya serikali yake walipitia mafunzo kazini kabla ya kuajiriwa rasmi. Aidha, wahitimu 5,600 wanapata mafunzo chini ya Mpango wa Makazi Nafuu, huku zaidi ya mafundi 2,000 wakipata vyeti kupitia mpango wa kutambua ujuzi. Rais pia alisema zaidi ya vijana 1.9 milioni wamefunzwa ujuzi wa kidijitali, hatua iliyochangia kuundwa kwa nafasi za kazi 350,000 katika sekta hiyo. Aliongeza kuwa zaidi ya Wakenya 580,000 kwa sasa wanafanya kazi nje ya nchi kupitia mpango wa serikali wa ajira majuu.
read moreRight Column Content