taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 30 Jul 2026 07:52:35
Wiper yakanusha Kalonzo alikula ugali na Ruto, yasema madai ni propaganda tupu
CHAMA cha Wiper Patriotic Front (WPF) kimekanusha vikali madai kuwa kinara wake Kalonzo Musyoka amekuwa na mazungumzo ya kisiasa na Rais William Ruto, kikisema taarifa hizo ni propaganda zinazolenga kuvuruga umoja wa upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027. Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti ambaye pia ni Seneta wa Kitui, Enock Wambua, alisema madai yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Kalonzo alikutana na Rais Ruto hivi majuzi hayana ukweli wowote. Alisisitiza kuwa hakujakuwa na mkutano kati ya viongozi hao wawili wala mazungumzo yoyote kuhusu kushirikiana kisiasa kabla ya uchaguzi ujao. "Ukweli ndio huu, kiongozi wetu hajawahi kukutana na Rais Ruto kwa mazungumzo hayo. Pia hakujakuwa na mazungumzo yoyote kuhusu kushirikiana katika uchaguzi mkuu ujao," alisema Bw Wambua. Alitaja taarifa hizo kuwa "habari za uongo, taarifa potovu na propaganda" zilizobuniwa ili kuleta mgawanyiko ndani ya upinzani unaojiandaa kumenyana na serikali ya Kenya Kwanza mwaka 2027. Bw Wambua alisema wanaosambaza uvumi huo wanajaribu kwa kila njia kudhoofisha kile alichokitaja kuwa serikali mbadala inayoundwa na vyama vya upinzani. Ili kuondoa utata, seneta huyo alieleza ratiba ya Kalonzo siku ambayo inadaiwa alikutana na Rais Ruto. Alisema alikuwa na Kalonzo siku nzima na kwamba kwanza walihudhuria mkutano na wahariri wakuu wa vyombo vya habari katika hoteli moja jijini Nairobi kabla ya kuelekea mkutano mwingine nyumbani kwa kiongozi huyo. "Ikiwa Rais Ruto alikutana na mtu anayeitwa Kalonzo siku hiyo, basi hakuwa kiongozi wa Wiper," alisema. Wambua alisisitiza kuwa Kalonzo bado ameweka nguvu zake katika juhudi za kuunganisha viongozi wa upinzani ili kuunda muungano mmoja utakaokuwa na mgombea mmoja wa urais dhidi ya Rais Ruto mwaka 2027. Aliongeza kuwa mkutano mkuu wa wajumbe wa Wiper uliofanyika Oktoba 10, 2025 katika Bustani ya Uhuru ulimuidhinisha Kalonzo kuwa mgombea wa urais wa chama hicho na pia kumpa mamlaka ya kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vingine kwa lengo la kuunda muungano mpana wa upinzani. Seneta huyo pia alipuuza video inayosambazwa mtandaoni ikidaiwa kuonyesha mkutano kati ya Kalonzo na Rais Ruto. Alisema video hiyo ilirekodiwa Machi 4, 2024 wakati Kalonzo, akiwa mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO), alipowasilisha ripoti ya kamati hiyo kwa Rais Ruto pamoja na wajumbe wengine. Kauli hiyo imejiri wakati uvumi kuhusu miungano mipya ya kisiasa ukiendelea kushamiri, huku Wiper ikisisitiza kuwa mashauriano yanayoendelea yanalenga kuimarisha umoja wa upinzani badala ya kuanzisha ushirikiano na serikali ya Kenya Kwanza.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 13 hours ago
Matumaini tele mbegu za kiume zikiundwa katika maabara
KWA miaka mingi, wanaume waliogunduliwa kuwa gumba kabisa wamekuwa wakikabiliwa na ukweli mchungu kwamba huenda wasiweze kupata watoto. Hata hivyo, utafiti mpya umeibua matumaini mapya baada ya wanasayansi kufanikiwa kutengeneza seli za awali za mbegu za uzazi za kiume katika maabara kwa kutumia seli zilizotokana na damu ya binadamu. Utafiti huo, uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Cell Stem Cell na watafiti wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania nchini Amerika, unaonyesha hatua kubwa katika juhudi za kutengeneza mbegu za uzazi nje ya mwili wa binadamu. Ingawa mbegu hizo hazikufikia ukomavu kamili wa kurutubisha yai, watafiti wanasema wamefikia hatua ambayo haijawahi kufikiwa katika tafiti za binadamu. Wataalamu walitumia seli zilizobadilishwa kutoka kwenye damu na kuzielekeza kuwa seli za mwanzo zinazoweza kukua na kuwa mbegu za uzazi. Baadaye waliziweka katika mazingira yanayofanana na korodani ndogo maabarani, ambako ziliendelea kukua na kuonyesha shughuli za vinasaba zinazofanana kwa asilimia 97 na ukuaji wa kawaida wa mbegu za uzazi kwa binadamu. Iwapo teknolojia hii itafanikiwa kukamilishwa, inaweza kuwapa matumaini wanaume wanaokabiliwa na ugumba usiotibika kupata watoto wao kuzaa kwa kutumia mbegu zilizotengenezwa maabarani. Ugumba wa wanaume ni tatizo kubwa duniani lakini mara nyingi huzungumziwa kwa kiwango kidogo. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu mmoja kati ya sita hukumbwa na changamoto hili katika kipindi cha maisha yake ya uzazi. Takriban asilimia 20 hadi 30 ya visa hivyo husababishwa na matatizo ya mwanaume pekee, huku katika asilimia 30 hadi 40 matatizo ya mwanaume na mwanamke yakichangia kwa pamoja. Nchini Kenya, Chama cha Madaktari wataalamu wa Mfumo wa Mkojo kinasema kati ya asilimia 10 na 15 ya wanandoa hushindwa kupata watoto, na katika asilimia 60 ya visa hivyo tatizo huwa linahusu mwanaume kwa kiwango fulani au kikamilifu. Mojawapo ya hali ngumu zaidi ni ile ambapo mwanaume hukosa mbegu za uzazi. Kuna aina mbili za hali hiyo. Ya kwanza hutokana na kuziba kwa njia za kupitisha mbegu na mara nyingi inaweza kutibiwa kwa upasuaji na ya pili hutokea pale korodani zinaposhindwa kabisa kuzalisha mbegu za uzazi, jambo ambalo lina tiba chache na ndilo lililolengwa na watafiti katika utafiti huu. Kwa sasa, wanaume wengi wenye tatizo hilo hulazimika kufanyiwa upasuaji wa kutafuta mbegu za uzazi moja kwa moja kwenye korodani. Hata hivyo, katika baadhi ya wagonjwa nafasi ya kupata hata mbegu moja inayoweza kutumika ni karibu asilimia 40 pekee. Zaidi ya hayo, matibabu hayo pamoja hugharimu kati ya Sh150,000 na zaidi ya Sh500,000 kwa mzunguko mmoja nchini Kenya. Gharama hizi hazifadhiliwi na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Katika utafiti huo, seli hizo ziliendelea kukua hadi hatua ambayo ni seli za mwanzo kabisa zinazozalisha mbegu za uzazi. Hata hivyo, hazikufikia hatua ya mwisho ya kuwa mbegu kamili zinazoweza kurutubisha yai. Kiongozi wa utafiti huo, Dkt Kotaro Sasaki wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania, alisema tofauti kati ya seli za binadamu na zile za panya zilizotumika kusaidia ukuaji huenda ndiyo iliyozuia kukamilika kwa mchakato huo. Hatua inayofuata ni kutumia seli zinazotokana na binadamu badala ya panya ili kuona kama mbegu kamili zinaweza kutengenezwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 12 hours ago
Yafichuka daktari aliyeuawa kwa risasi asubuhi jijini aliwahi kuripoti kupokea vitisho
MAUAJI ya mwanasaikolojia Dkt Victoria Nthunya Mutiso kwa kupigwa risasi katika Barabara ya Mbagathi Link, Nairobi, Jumatano asubuhi, yamezua maswali mapya baada ya kubainika alikuwa ameripoti matukio mawili ya kutishiwa maisha miezi michache kabla ya kuuawa. Sasa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wanachunguza iwapo matukio hayo yanahusiana na mauaji yake. Kwa mujibu wa taarifa za awali za polisi, Dkt Mutiso alikuwa akisafiri kuelekea kazini ndani ya teksi, gari la rangi nyeusi lilipoziba njia katika eneo la Mbagathi. Mtu aliyekuwa na bunduki alikaribia gari lao na kumpiga risasi kabla ya kutoroka. Wapelelezi wanaamini huenda alifuatwa alipoondoka nyumbani kwake. Mkurugenzi wa Mawasiliano katika DCI, John Marete, alisema maafisa wa kitengo cha mauaji wanaendelea kukusanya ushahidi wa kisayansi na kurekodi taarifa za mashahidi. Alisema watu wawili wanaochunguzwa, mwanamume na mwanamke, wanazuiliwa huku uchunguzi ukiendelea. Mnamo Februari mwaka huu, Dkt Mutiso aliripoti katika Kituo cha Polisi cha Mlolongo kuwa kundi la watu, akiwemo aliowatambua kuwa maafisa wa polisi, walivamia nyumba yake, kuharibu mali na kujaribu kuwaondoa kwa nguvu waliokuwa ndani. Alidai operesheni hiyo iliongozwa na afisa mmoja mkuu wa polisi. Baadaye alilalamika kuwa hakupatiwa mara moja nambari ya kuripoti tukio hilo (OB), ingawa aliipokea baadaye mwezi Mei. Kisha Julai 7, aliripoti tukio jingine baada ya mtu aliyekuwa ameabiri pikipiki kushuka akiwa na kitu kilichoonekana kama bunduki na kuelekea kwenye gari lake akiwa amesimama kwenye msongamano wa magari jijini Nairobi. Aliondoka haraka na kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kilimani. Wiki tatu baadaye, alipigwa risasi na kuuawa. Wapelelezi pia wanachunguza iwapo mauaji hayo yanahusiana na mzozo wa muda mrefu kuhusu nyumba aliyokuwa akiishi, ambao ulihusisha kesi kuhusu umiliki na ndoa zilizodumu kwa zaidi ya miaka 20 na hatimaye kusababisha kufurushwa kwa wakazi. DCI imesema uchunguzi unaendelea kubaini iwapo mizozo hiyo au matukio ya awali yalichangia mauaji hayo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Njuguna Ndung'u aanika Ruto, asema hulazimu mawaziri kufanya anachokitaka kwa woga
ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Prof Njuguna Ndung'u, amemshutumu Rais William Ruto kwa kuingilia utendakazi wa taasisi huru, akisema mtindo huu umezorotesha uwezo wa kutekeleza majukumu ipasavyo. Akizungumza katika mkutano kuhusu misaada nchini Uswizi, Prof Ndung'u alisema taasisi nyingi zina uwezo wa kufanya maamuzi sahihi lakini zinalemazwa na kile alichokitaja kuwa tabia ya mtu mmoja kutaka kudhibiti kila kitu. "Hivi sasa Rais wa sasa anaingilia utendakazi wa taasisi zote. Nendeni mkaninukuu," alisema Prof Ndung'u, akiongeza kuwa maafisa wengi hulazimika kufuata maagizo kwa hofu. Alisema akiwa Waziri wa Fedha alikataa kushiriki mikataba au mipango ambayo haikuwa sahihi. Hii ni mara ya kwanza Prof Ndung'u kuzungumzia hadharani changamoto alizokumbana nazo akiwa serikalini kabla ya kuondolewa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofuatia maandamano ya Gen Z dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka 2024. Kauli zake zimeibua tena mjadala kuhusu mtindo wa uongozi wa Rais Ruto. Wakosoaji wanasema anapenda kusimamia karibu kila uamuzi wa serikali, huku wafuasi wake wakimtetea wakisema ni kiongozi anayefuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya serikali. Prof Ndung'u pia alikosoa sera ya kuongeza ushuru ili kuimarisha mapato ya serikali, akisema ushuru mkubwa mara nyingi hupunguza mapato badala ya kuyaongeza. Alisema tofauti za kisiasa ndani ya serikali pia zilichangia ugumu wa kusimamia uchumi alipokuwa Waziri wa Fedha.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 14 hours ago
Matangazo ya mazishi kwa vipaza sauti yazua hisia mseto Kisii
SAA nne na nusu asubuhi, sauti nzito ya kipaza sauti hupenya vilima na mabonde ya South Mugirango, Kaunti ya Kisii, ikitangaza kifo na safari ya mwisho ya marehemu mwili ukipelekwa nyumbani kwa mazishi. Kwa wakazi wengi wa maeneo ya South Mugirango, Bomachoge Borabu na Bomachoge Chache, huu ni utamaduni uliodumu kwa miaka mingi na ambao bado unatumika licha ya kuenea kwa simu za kisasa, WhatsApp na mitandao ya kijamii. Gari dogo lililofungwa vipaza sauti hutangulia gari la kubeba mwili kutoka mochari ya Kisii, huku watangazaji wawili wakitoa taarifa kuhusu marehemu na mahali atakapozikwa. Tangazo la kwanza hutolewa kati ya saa nne na saa sita mchana familia ikielekea kuchukua mwili. La pili, kati ya saa saba na saa tisa alasiri, hutolewa mwili unaporejeshwa nyumbani na ndilo linalovutia watu wengi zaidi. Bw Jared Mobisa, mmoja wa watangazaji maarufu wa mazishi eneo hilo, anasema kazi yao ni kuhakikisha jamii inajiandaa mapema kumpokea marehemu. "Tunatangaza tukielekea mochari na tunaporudi na mwili. Kufikia wakati msafara unafika nyumbani, wanakijiji wote tayari huwa wamekusanyika," anasema. Familia hulipa kati ya Sh3,000 na Sh5,000 kwa huduma hiyo, gharama inayojumuisha mafuta na umeme wa kuendesha mfumo wa sauti. Kabla ya safari, mtangazaji hupewa maandishi yenye taarifa za marehemu. Huyasoma mara kwa mara hadi ayakariri, kisha hutangaza kutoka kijiji kimoja hadi kingine. Kwa wakazi wengi, mfumo huo bado una umuhimu mkubwa. Bi Alice Moraa wa Ogembo anasema bila matangazo hayo wengi wasingejua mwili unarejeshwa nyumbani kwa mazishi. Hata hivyo, kizazi kipya kinaanza kuhoji iwapo desturi hiyo bado inafaa katika zama za kidijitali. Bi Sharon Kemunto, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Moi, anasema kelele za vipaza sauti humvurugia masomo kila kunapokuwa na mazishi. "Wiki iliyopita kulikuwa na mazishi maeneo matatu. Nilishindwa kusoma hadi nikalazimika kwenda Suneka kutafuta sehemu tulivu," anasema. Ingawa anatambua umuhimu wa mila hiyo, anahoji kwa nini familia zisitumie makundi ya WhatsApp au matangazo mengine ya kisasa kuwafahamisha watu. Hata hivyo anakiri kuwa familia yao ilipofiwa na mjomba wake, tangazo kupitia kipaza sauti ndilo lililowakusanya watu wengi. Kwa Mzee Abel Ombongi wa Etago, huo ndio ushahidi kuwa utamaduni huo bado una nafasi yake. Anasema ujumbe wa WhatsApp huhitaji simu za kisasa na mtandao, ilhali tangazo la kipaza sauti humfikia kila mtu bila gharama za ziada. "Katika safari mbili tu kati ya Kisii na Ogembo, maelfu ya watu huwa wamepata taarifa," anasema. Bi Dorcas Kemunto, mzee wa kanisa, anaamini matangazo hayo ni ishara ya heshima kwa marehemu. "Ukisikia kipaza sauti unajua marehemu anarudishwa nyumbani kwa mara ya mwisho. Watu husitisha shughuli zao na kujiandaa kumpokea," anasema. Anasema wazee wengi vijijini hawana simu za kisasa, hivyo hutegemea matangazo hayo kupata habari. Mzee Joseph Menge, 78, anaongeza kuwa huduma hiyo ni nafuu kuliko matangazo ya redio, ambayo yanaweza kugharimu kati ya Sh5,000 na Sh15,000. Lakini si kila mtu anaunga mkono desturi hiyo. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Gusii, Bw James Matundura, anasema vipaza sauti hivyo vimepitwa na wakati na sasa vinachangia kelele. "Leo tuna simu za mkononi na WhatsApp. Hatuna sababu ya kuwasumbua wagonjwa, wanafunzi na watu wanaofanya kazi kwa kelele hizi," anasema. Mjadala huo unaendelea huku baadhi ya wakazi wakisisitiza kuwa matangazo hayo ni sehemu ya utamaduni wao, ilhali wengine wakitaka mbinu za kisasa zitumike bila kuvuruga maisha ya kila siku.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 30 Jul 2026 00:55:43
Kibarua Upinzani kuamua gani kali kati ya Kalonzo-Matiang'i, Kalonzo-Sifuna, Sifuna-Kalonzo
UPINZANI sasa unakabiliwa na mtihani mkubwa zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Baada ya kuonekana kukubaliana kuhusu haja ya kuungana dhidi ya Rais William Ruto, sasa viongozi wake wanapaswa kuamua nani atapeperusha bendera ya urais na nani atakuwa mgombea mwenza. Baada ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuondolewa rasmi katika kinyang'anyiro cha urais kufuatia kutimuliwa afisini, mjadala umehamia kwa miungano minne inayoweza kuundwa. Wachambuzi wa kisiasa na viongozi wa upinzani sasa wanazungumzia uwezekano wa tiketi za Kalonzo-Matiang'i, Matiang'i-Kalonzo, Kalonzo-Sifuna au Sifuna-Kalonzo. Hadi majuzi, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i walionekana kuwa wagombeaji wakuu wa kuwania urais kupitia muungano huo. Hata hivyo, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ametikisa hesabu hizo baada ya kura ya maoni ya TIFA kumweka mbele ya Kalonzo na Matiang'i kwa mara ya kwanza. Licha ya mabadiliko hayo, jambo moja linaonekana wazi katika mazungumzo yote ya upinzani; Kalonzo bado anaonekana kuwa nguzo muhimu, iwe kama mgombea wa urais au mgombea mwenza. Wachambuzi wanasema kuibuka kwa Sifuna na vuguvugu la Linda Mwananchi kumebadilisha kabisa mizani ya kisiasa ndani ya upinzani. Ingawa viongozi wote wanakubaliana kuwa umoja ndio njia pekee ya kumng'oa Rais Ruto mwaka 2027, bado hawajakubaliana nani anafaa kuongoza tiketi hiyo. Kwa mujibu wa wachambuzi, uchaguzi nchini Kenya hauamuliwi na umaarufu pekee. Mchanganyiko wa maeneo, makabila, usimamizi wa miungano na hisia za ushirikishwaji huwa na uzito mkubwa sawa na umaarufu wa mgombeaji. Kalonzo anaungwa mkono kwa hoja kwamba ana tajriba ya kisiasa ya miongo kadhaa, aliwahi kuwa Makamu wa Rais na amekuwa akisubiri nafasi ya kuwania urais kwa muda mrefu. Kwa upande mwingine, Matiang'i anaonekana kuwa na taswira ya kiongozi mwenye uwezo wa kiutawala na anayekubalika na wapigakura wanaotaka mageuzi. Naye Sifuna anaonekana kuwa sura mpya inayovutia zaidi vijana na Wakenya wanaotaka kizazi kipya cha uongozi. Kura ya maoni ya Infotrak ilionyesha kuwa tiketi ya Kalonzo-Sifuna ndiyo inayopendelewa zaidi na wapigakura kwa asilimia 23. Kwa upande mwingine, kura ya TIFA ilimpa Sifuna asilimia 15 ya uungwaji mkono kugombea urais, akifuatiwa na Matiang'i kwa asilimia 14 huku Kalonzo akipata asilimia 13. Wachambuzi wanasema matokeo hayo yanaibua maswali magumu. Iwapo Sifuna ndiye anayependwa zaidi, je, atakubali kuwa mgombea mwenza? Na ikiwa Kalonzo ataacha tena azma baada ya kusubiri kwa miaka mingi, je, wafuasi wake watamuunga mkono mgombeaji mwingine? Seneta wa Kitui Enoch Wambua amesema muungano wa upinzani na Linda Mwananchi utaendelea kushirikiana licha ya changamoto zozote. "Makundi hayo mawili yana lengo moja; kuhakikisha Rais Ruto anahudumu muhula mmoja tu, na yatafanya kazi pamoja," alisema. Matiang'i pia amesisitiza kuwa mgombea wa urais anapaswa kupatikana kupitia mchakato wa wazi na unaokubalika na wote. Kwa upande wake, msemaji wa muungano wa upinzani Dkt Mukhisa Kituyi amesema kuibuka kwa Linda Mwananchi kunamaanisha Sifuna sasa ni sehemu muhimu ya hesabu ya upinzani. "Yupo mtoto mpya kwenye ulingo, Sifuna na timu yake. Lazima tuzungumze nao na tuone hatua wanazopanga kuchukua," alisema. Hata hivyo, changamoto nyingine kubwa ni eneo la Mlima Kenya. Wachambuzi wanaonya kuwa kuacha eneo hilo nje ya tiketi ya urais kunaweza kupunguza ari ya wapigakura wake. Ingawa Gachagua alitimuliwa afisini, wengi wanaamini bado ana ushawishi mkubwa wa kisiasa katika eneo hilo. Wakili Nelson Osiemo anasema upinzani utapata wakati mgumu kuwashawishi wakazi wa Mlima Kenya kuunga mkono tiketi ambayo haina mmoja wao. Kwa sasa, viongozi pekee kutoka eneo hilo waliotangaza nia ya kuwania urais ni kiongozi wa Safina Jimi Wanjigi na kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua. Kwa upande mwingine, Naibu Rais Kithure Kindiki ameendelea kuimarisha kampeni za Kenya Kwanza Mlima Kenya akisisitiza kuwa mustakabali wa eneo hilo uko ndani ya serikali ya Rais Ruto. Sifuna amesema yuko tayari kushirikiana na Gachagua licha ya kuwa miongoni mwa maseneta waliopiga kura ya kumtimua afisini. "Tutafanya kazi na yeyote anayeamini katika Katiba, utawala wa sheria na kwamba Rais Ruto hastahili kuongezewa hata siku moja madarakani," alisema. Viongozi wa upinzani wanasema bado hawajafikia uamuzi wa mwisho kuhusu mgombea wao wa urais na mgombea mwenza. Wanatarajia kutangaza tiketi yao na mfumo wa kugawana madaraka kufikia Machi mwaka ujao. Hadi wakati huo, mazungumzo yanatarajiwa kuendelea huku maslahi ya kikanda, kura za maoni na matarajio ya viongozi mbalimbali yakizidi kuathiri hesabu za kisiasa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 30 Jul 2026 01:55:59
Wasichana wengi wanaobalehe Tana River ni wajawazito – Utafiti
ZAIDI ya msichana mmoja kati ya wanne aliyefikia umri wa kubalehe katika Kaunti ya Tana River alikuwa mjamzito kati ya Januari na Juni mwaka huu, utafiti mpya umebaini. Utafiti huo uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Utafiti kuhusu Wanawake Afrika (ICRW Africa) kwa ushirikiano na Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu Kenya (KNBS), umeonyesha kuwa asilimia 27.5 ya wasichana wanaobalehe katika kaunti hiyo walikuwa wajawazito wakati wa utafiti huo. Matokeo hayo pia yanaonyesha hali ya kutatanisha katika kaunti za Garissa, Homa Bay, Samburu na Pokot Magharibi, ambako wasichana wengi wanakosa taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi kufanya maamuzi yanayofaa. Utafiti huo uliandaliwa kabla ya kuanza kwa mpango wa miaka mitano unaoitwa Her Health Initiative, unaolenga kuboresha afya ya uzazi kwa wasichana katika kaunti hizo tano. Ripoti hiyo iliyoidhinishwa Nairobi Ijumaa iliyopita ilibaini kuwa ni asilimia 53 pekee ya wasichana wa Tana River ambao wamewahi kuhudhuria shule, huku asilimia 51 wakiwa hawajui kusoma wala kuandika. Aidha, wastani wa umri wa wasichana kuanza kushiriki ngono ni miaka 15.8. Kati ya wasichana wanaoshiriki ngono, asilimia 81.3 wamewahi kupata ujauzito, huku asilimia 27.5 ya wote waliohojiwa wakiwa wajawazito wakati wa utafiti. Mkurugenzi wa Reproductive Health Network Kenya (RHNK), Bi Nelly Munyasia, alisema viwango vya chini vya elimu na maarifa vinachangia ongezeko la mimba za mapema. "Wasichana wasiohudhuria shule hukosa elimu. Kukosa elimu kunawanyima taarifa sahihi. Kukosa taarifa kunapunguza matumizi ya njia za kupanga uzazi, na mimba huwafanya wengine kuacha shule. Mzunguko huo unaendelea kujirudia," alisema. Ripoti hiyo pia ilibaini kuwa ni asilimia 41.3 pekee ya shule za Tana River zinazotoa elimu kuhusu afya ya uzazi, kiwango cha chini zaidi kati ya kaunti zote zilizoshirikishwa. Hata hivyo, watafiti walisema sababu za hali hiyo zinatofautiana kati ya kaunti hizo, hivyo suluhu pia zinapaswa kuwa tofauti. Katika Samburu, wasichana huanza kushiriki ngono wakiwa na wastani wa miaka 15.5, kiwango cha chini zaidi kati ya kaunti zote. Ingawa zaidi ya asilimia 89 wanafahamu kuhusu sindano kupanga uzazi na asilimia 92 wanajua kuhusu kondomu, zaidi ya asilimia 82 walisema wanahitaji elimu zaidi kuhusu afya ya uzazi. Kwa upande wa Homa Bay, utafiti ulionyesha hali tofauti. Kaunti hiyo ina kiwango cha juu zaidi cha mahudhurio shuleni cha asilimia 99.1 na asilimia 98.7 ya wasichana wanajua kusoma na kuandika. Hata hivyo, asilimia 36.4 ya wasichana wanaoshiriki ngono wamewahi kupata ujauzito, huku asilimia 7.5 wakiwa wajawazito wakati wa utafiti. Garissa ndiyo kaunti iliyorekodi kiwango cha chini zaidi cha wasichana waliowahi kushiriki ngono, asilimia 1.3 pekee, na hakuna aliyekuwa mjamzito wakati wa utafiti. Hata hivyo, utafiti ulionyesha kuwa maarifa kuhusu matumizi ya kondomu katika kaunti hiyo ni ya chini zaidi, yakifikia asilimia 27.2 pekee. Ripoti hiyo ilibaini kuwa katika kaunti zote tano, walimu ndio chanzo kikuu cha taarifa kuhusu afya ya uzazi kwa wasichana wa balehe, huku akina mama wakishika nafasi ya pili. Bi Munyasia alisema matokeo hayo yanaonyesha umuhimu wa kuwawezesha walimu na wazazi kwa mafunzo na nyenzo zinazohitajika ili kuwapa vijana taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 30 Jul 2026 02:55:54
Serikali yashtakiwa kwa kukosa kufidia walimu, polisi wanaofariki
SERIKALI imeshtakiwa kwa madai ya kukosa kulipa bima ya zaidi ya Sh20 bilioni familia za watumishi wa umma waliofariki au kujeruhiwa kazini, wakiwemo walimu na maafisa wa polisi. Kesi hiyo iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu Nairobi na John Gitonga inadai kuwa serikali imekuwa ikikiuka sheria kwa kushindwa kutoa bima ya lazima na kulipa fidia kwa vifo, ulemavu na majeraha ya kazini kwa mamia ya maelfu ya watumishi wa umma. Bw Gitonga anasema hali hiyo imeacha familia za marehemu na watumishi waliopata ulemavu bila fidia wanazohakikishiwa na sheria. Walioshtakiwa ni Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Mamlaka ya Kudhibiti Bima (IRA), Hazina ya Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSSF), Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC), Tume ya Utumishi wa Mahakama (JSC), Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi, Mwanasheria Mkuu, Bunge la Kitaifa pamoja na kampuni kadhaa za bima. Kesi hiyo inadai kumekuwa na dosari katika usimamizi wa mipango ya bima ya watumishi wa umma. Bw Gitonga anakadiria kuwa serikali inadaiwa Sh8.4 bilioni kwa watumishi wa umma, Sh3 bilioni kwa polisi na magereza, na angalau Sh10 bilioni kwa walimu. Anasema madai hayo yanatokana na usimamizi wa bima za ajali kazini, fidia chini ya Sheria ya Fidia kwa Majeraha Kazini (WIBA), bima ya maisha ya kikundi na bima ya gharama za mazishi. Anataka mahakama itangaze mpango huo kuwa ni kinyume cha Katiba, iamuru malipo ya madai yote yaliyosalia, ukaguzi ufanywe kwa kina wa fedha na kuagiza mageuzi katika usimamizi wa bima za watumishi wa umma. Katika hati yake ya kiapo, Bw Gitonga anasema aliamua kwenda mahakamani baada ya dadake aliyekuwa mfanyakazi wa TSC kufariki akiwa kazini huku watoto wake wakikosa kulipwa mafao ya bima licha ya kufuatilia kwa muda mrefu.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 30 Jul 2026 06:46:45
Besigye mahututi ICU, mkewe Winnie Byanyima athibitisha
KAMPALA, Uganda: MWANASIASA mashuhuri wa upinzani Uganda, Kizza Besigye, anaendelea kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Mulago baada ya kuzimia akiwa mahakamani jijini Kampala mnamo Jumatano. Mkewe, Winnie Byanyima, alithibitisha taarifa hiyo kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X mapema Alhamisi, akisema mwanasiasa huyo, 70, alikuwa amepoteza fahamu na hali yake ya afya ilikuwa mbaya. "Amepoteza fahamu, hawezi kuzungumza na hata maumivu yakimlemea hagutuki," akasema Byanyima, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS). Besigye alizimia alipofika mahakamani jijini Kampala, ambako anakabiliwa na mashtaka ya uhaini. Baadaye aliondolewa mahakamani kwa gari la wagonjwa na kukimbizwa hospitalini. Msemaji wa serikali ya Uganda, Alan Kasujja, hakujibu jumbe au simu ili kutoa maoni kuhusu tukio hilo. Kiongozi huyo mkongwe wa upinzani amekuwa rumande tangu Novemba 2024 baada yake na msaidizi wake, Obeid Lutale, kukamatwa Kenya kabla ya kurejeshwa Uganda, ambako baadaye walishtakiwa kwa kosa la uhaini. Mawakili wake, wafuasi na wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakipinga mashtaka hayo wakisema yana msukumo wa kisiasa. Wanasema kuendelea kuzuiliwa kwake ni mbinu ya serikali ya kuwazima wakosoaji wa utawala wa Rais Yoweri Museveni. Rais Museveni, 81, alitangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Uganda uliofanyika Januari. Matokeo hayo yalikataliwa na mpinzani wake mkuu Bobi Wine, ambaye tangu wakati huo ameishi uhamishoni Amerika. Kuzuiliwa kwa Besigye kumezua wasiwasi mkubwa katika mataifa mbalimbali duniani. Ingawaje, anafahamika kama mmoja wa viongozi wachache waliothubutu kumpinga Rais Museveni katika utawala wake wa miongo kadhaa Uganda.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 30 Jul 2026 07:40:25
Demu ashtuka kujua kalameni aliyeshuku ni mwizi aliomoka
MAKIMA, Embu: POLO mmoja amezua gumzo mtaani hapa baada ya kusimulia jinsi kipusa aliyekuwa akimmezea mate alivyokataa kupanda gari lake akidai ni la kukodisha. Mwanadada huyo aliamini kijana huyo hakuwa na uwezo wa kumiliki gari kwa sababu anatoka familia maskini.Jamaa alisema hakubishana naye wala kujitetea. Badala yake, alimwacha aamini alichotaka. Miezi kadhaa baadaye, demu alibaini kuwa gari hilo lilikuwa mali yake halali na alikuwa amejiendeleza kimya kimya kupitia biashara zake. Baada ya ukweli kufichuka, msichana huyo alianza kutaka kufufua mawasiliano, lakini jamaa hakutaka uhusiano naye tena akidai alimdharau. Kisa hicho kimezua mjadala mkubwa hapa, wengi wakisema si busara kumhukumu mtu kwa asili ya familia yake au mali anayoonekana kuwa nayo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 30 Jul 2026 09:18:57
Kiir atimua Gavana wa Benki Kuu, arejesha aliyemfuta kwa wadhifa huo mwaka jana
JUBA, Sudan Kusini RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir Alhamisi alimfuta kazi Gavana wa Benki Kuu Johnny Ohisa, kiongozi huyo akionekana kukumbatia mbinu ya kutekeleza mabadiliko ya mara kwa mara katika serikali yake. Kiir alitangaza kuondolewa kwa Ohisa kupitia amri iliyosomwa kwenye runinga ya serikali, lakini hakutoa sababu ya uamuzi huo. Nafasi ya Ohisa imechukuliwa na Addis Ababa Othow, ambaye aliwahi kuhudumu kama gavana wa Benki Kuu kati ya Juni na Novemba mwaka jana. Rais Kiir amekuwa akitekeleza mabadiliko makubwa katika uongozi wa serikali yake. Wadadisi wa siasa wanasema hatua hizo zinaashiria juhudi za kuimarisha ushawishi wake huku kukiwa na hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu atakayemrithi. Ohisa, ambaye ni mwanauchumi, amewahi kuhudumu mara kadhaa kama gavana wa Benki Kuu ya Sudan Kusini. Alirejeshwa katika wadhifa huo mapema mwaka huu baada ya kushikilia nafasi hiyo katika vipindi viwili tofauti hapo awali. Uchumi wa Sudan Kusini kwa sasa unakabiliwa na changamoto kubwa, zikiwemo kupungua kwa mapato yanayotokana na mafuta, uhaba wa fedha, mfumuko wa bei unaoendelea kupanda na kushuka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 17 hours ago
Ruto halali akitupangia lakini hatupati ng'o, wasema viongozi wa Upinzani
VIONGOZI wa upinzani wameanza mikakati ya kuunda muungano mkubwa wa kisiasa unaofanana na ule wa National Rainbow Coalition (NARC) uliomwingiza madarakani Rais mstaafu Mwai Kibaki mwaka wa 2002. Mipango hiyo ilibainika jana baada ya kiongozi wa Wiper Patriotic Front (WPF), Kalonzo Musyoka kufanya kikao cha faragha na viongozi wa mrengo wa Linda Mwananchi, ukiongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Katika muungano wa Narc, vyama vya upinzani na waliokuwa wamehama Kanu waliungana na kumuidhinisha Kibaki kuwania urais kupitia kauli - mbiu maarufu ya Kibaki Tosha iliyobuniwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Kwa mujibu wa duru zilizohudhuria mkutano huo, Bw Sifuna alisema mrengo wa Linda Mwananchi uko katika hatua za mwisho za kusajili chama kipya cha kisiasa. Viongozi hao walikubaliana kuwa kila upande uendelee kuimarisha ngome zake kisiasa kabla ya kukubaliana kuhusu mgombeaji mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kumkabili Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027. Aidha, imebainika kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ameita kikao cha Baraza la Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kitakachofanyika Jumatatu kujadili mikakati ya uchaguzi huo. Kiongozi wa Kanu Gideon Moi pia anatarajiwa kuhudhuria kikao hicho, huku aliyekuwa mgombea ugavana wa Nairobi kupitia Kanu, Tony Gachoka, akiwakilisha chama hicho katika mkutano wa Alhamisi. Kiongozi mmoja wa Linda Mwananchi alisema muungano huo unalenga kuwaleta pamoja viongozi wote wanaotaka Rais Ruto ahudumu muhula mmoja pekee. "Tutashirikisha makundi yote yanayounga mkono ajenda ya muhula mmoja. Hatimaye kutakuwa na mkutano mkubwa wa vyama vyote vya upinzani na tutaunda muungano mmoja mkubwa kama Narc ya mwaka 2002," alisema. Mkutano huo umefanyika wiki moja baada ya viongozi wa Linda Mwananchi kufanya mazungumzo kama hayo na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang'i. Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi alisema kundi hilo pia linapanga kukutana na kiongozi wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua pamoja na Martha Karua wa People's Liberation Party (PLP). Baada ya mkutano huo, Bw Kalonzo alikanusha madai kwamba anafanya mazungumzo ya siri na Rais Ruto kuhusu kujiunga na serikali. Alisema uvumi huo unalenga kudhoofisha umoja wa upinzani lakini hautafanikiwa. "Ninataka kumwambia William Ruto aache kudhani kwamba Stephen Kalonzo Musyoka anaweza kujiunga naye. Tutakutana naye kwenye sanduku la kura mwaka wa 2027," alisema. "Nasi viongozi wa upinzani, Sifuna, Gachagua au mimi, yeyote atakayekubali kuungana na Ruto, atapata adhabu kali kutoka kwa raia." Kalonzo alisisitiza kuwa ataendelea kushirikiana na vyama vingine vinavyotaka kuondoa Kenya Kwanza mamlakani kupitia uchaguzi. Kwa upande wake, Seneta Sifuna alisema Wakenya wanataka kuona upinzani ulioungana na wenye uwezo wa kutoa uongozi mbadala. "Tutazungumza na viongozi wote wa upinzani ili kujenga mwafaka. Hatutaki kuwaangusha Wakenya ambao wanatarajia kuona viongozi wakifanya kazi pamoja," alisema. Awali, Sifuna aliwahi kusema Linda Mwananchi iko tayari kushirikiana na yeyote anayepinga muhula wa pili wa Rais Ruto, akiwemo Bw Gachagua. Hata hivyo, licha ya kauli za umoja, kuna hofu kuwa maslahi ya kisiasa yanaweza kuvuruga mipango hiyo. Kalonzo, Gachagua, Sifuna, Dkt Matiang'i, Martha Karua na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa wote wameonyesha nia ya kuwania urais. Wachambuzi wa siasa wanasema changamoto kubwa haitakuwa kuunda muungano bali kukubaliana kuhusu mgombea wa urais na mgombea mwenza, huku masuala ya ushawishi wa kikanda na usawa wa kisiasa yakitarajiwa kuwa muhimu. Historia inaonyesha migawanyiko imeigharimu upinzani mara kadhaa. Mwaka 1992, vyama vya upinzani vilishindwa kuafikiana kuhusu mgombea mmoja na hivyo kumpa aliyekuwa Rais Daniel arap Moi ushindi mwingine. Hali kama hiyo ilijirudia mwaka wa 1997 na tena mwaka wa 2007, ambapo mgawanyiko kati ya Raila Odinga na Kalonzo Musyoka uliwanufaisha wapinzani wao na kuchangia mvutano mkubwa baada ya uchaguzi. Kutokana na historia hiyo, viongozi wa sasa wa upinzani wanajaribu kuepuka makosa yaliyopita kwa kuanza mazungumzo mapema ili kuunda muungano mmoja wenye uwezo wa kumpa Rais Ruto ushindani mkali katika uchaguzi wa 2027. Jana, Bw Musyoka alisema kinara yeyote wa upinzani atakayezungumza na Rais Ruto atatengwa na wenzake akisema hakuna aliye tayari kusaliti Wakenya. "Hatutasaliti hisia za taifa, atakayesikika alikutana na Ruto, awe ni Sifuna au rafiki yangu Rigathi Gachagua, huo utakuwa mwisho wa kushirikiana nasi," alisema msimamo ambao Sifuna alikubaliana nao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 16 hours ago
Jumwa atema UDA kwa mara ya pili: 'Ruto nimevumilia nimechoka, niache salama usinidhuru'
ALIYEKUWA Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa, ambaye analenga kuwania ugavana Kilifi, ametangaza kujiondoa katika chama cha United Democratic Alliance (UDA). Hii ni mara ya pili kwa Bi Jumwa kujiondoa UDA. Mnamo Desemba mwaka jana, mwenyekiti huyo wa Bodi ya Barabara nchini (KRB) alitangaza kuondoka UDA na kujiunga na chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa na Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi. Hata hivyo, baada ya PAA kutangaza kuwa hakitawasimamisha wagombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 bali kitaiunga mkono UDA, Bi Jumwa alijikuta njia panda. Baadaye aliendelea na kampeni zake za mashinani chini ya bendera ya UDA akitarajia kupata tiketi ya ugavana, lakini alikumbana na upinzani kutoka kwa viongozi wa chama katika kaunti hiyo ambao waliweka wazi msimamo wao kumuunga mkono Gavana Gideon Mung'aro wa ODM. Akizungumza katika kikao na wanahabari Alhamisi, Bi Jumwa alitangaza kuwa yeye si mwanachama tena wa chama cha Rais William Ruto, akitaja kile alichodai kuwa ni vitendo visivyo vya kidemokrasia vinavyodhoofisha matakwa ya wananchi wa Kilifi. Mbunge huyo wa zamani wa Malindi alisema amefikia uamuzi huo baada ya mashauriano na wakazi wa Kilifi, kutafakari na kufanya maombi. Bi Jumwa, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa UDA, alisema kuondoka katika chama hicho halikuwa jambo rahisi kwa kuwa alitumia nguvu na kujitolea kukijenga chama hicho. "Kama wengi wenu mnavyojua, mimi ni mmoja wa waanzilishi wa United Democratic Alliance. Kuondoka katika chama ulichosaidia kukijenga si uamuzi mwepesi," alisema. Hata hivyo, alisisitiza kuwa uongozi ni wa wananchi na si wa vyama vya kisiasa au watu binafsi, akisema demokrasia inapaswa kulinda haki ya wananchi kuchagua viongozi wao kwa uhuru. "Uaminifu wangu kwa watu wa Kilifi utakuwa mkubwa siku zote kuliko uaminifu wangu kwa chama chochote cha kisiasa. Sauti ya watu wa Kilifi ni kubwa kuliko sauti ya UDA," alisema. Bi Jumwa alidai kuwa kumekuwa na juhudi za kuzima matarajio na uchaguzi wa wananchi wa Kilifi. Kulingana naye, vitendo hivyo vinakwenda kinyume na misingi ya demokrasia. Aidha, alifichua kuwa aliwasilisha malalamishi yake kwa Rais Ruto, akieleza matumaini yake kuwa haki, usawa na heshima kwa matakwa ya wananchi zitazingatiwa. Bi Jumwa alisema hivi karibuni atazindua chombo kipya cha kisiasa kitakachoendeleza kile alichokitaja kuwa ni ndoto ya pamoja ya kuijenga Kilifi iliyo bora. Aliwahimiza wakazi wa Kilifi kudumisha amani na umoja, akisema harakati hiyo mpya inalenga kuboresha huduma za afya, kuunda nafasi za ajira, kupanua fursa kwa wakulima, kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na kuimarisha uongozi wenye uwajibikaji. Tangazo hilo linaashiria mabadiliko ya kisiasa kwa mwanasiasa huyo mashuhuri wa Pwani huku mipangilio mipya ya kisiasa ikianza kujitokeza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2027. Mapema wiki hii, kulikuwa na taarifa kuwa alikuwa akifikiria kujiunga na vuguvugu la Linda Mwananchi. Kujiondoa kwake kulipokewa vyema na wanasiasa wa Linda Mwananchi ambao wamemkaribisha katika upinzani. Bi Jumwa alisema yuko tayari kumenyana na Bw Mung'aro katika uchaguzi wa ugavana wa Kilifi mwaka wa 2027. Kaunti ya Kilifi imeendelea kuwa ngome ya ODM tangu mwaka 2007.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 15 hours ago
UCHANGANUZI: Si rahisi vile kwa Ruto kumtema Kindiki uchaguzi wa 2027
RAIS William Ruto anakabiliwa na uamuzi mgumu wa kisiasa na kikatiba kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 kufuatia kufurushwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua madarakani Oktoba 2024. Ingawa Bw Gachagua aliondolewa afisini kupitia mchakato wa bunge, hatua hiyo haikufifisha ushawishi wake kisiasa. Badala yake, ameibuka kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani kupitia chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), ambacho kinaendelea kujijengea ngome katika eneo la Mlima Kenya. Hali hiyo imeongeza shinikizo kwa Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kuthibitisha kuwa anaweza kudumisha uungwaji mkono wa Rais Ruto katika eneo hilo kabla ya uchaguzi wa 2027. Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata, amesema Rais atalazimika kufanya uamuzi kuhusu mgombea mwenza wake, akisema nafasi hiyo ni muhimu katika kuvutia kura za Mlima Kenya. "Tatizo kubwa ni kwamba Mlima Kenya unaonekana kuelekea upande wa Gachagua na DCP. Swali ni iwapo Prof Kindiki anaweza kurejesha kura hizo," alisema. Kauli hiyo imejiri huku kukiwa na mjadala kuhusu uwezo wa Prof Kindiki kuimarisha ushawishi wa Kenya Kwanza katika eneo hilo baada ya Bw Gachagua kugeuka mkosoaji mkubwa wa serikali. Hata hivyo, wataalamu wa sheria wanasema Rais hawezi kumuondoa Naibu Rais kwa uamuzi wake binafsi. Wakili Geoffrey Kahuthu, alisema Katiba imeweka utaratibu maalumu wa kumuondoa Naibu Rais kupitia mchakato wa kuondolewa madarakani au kwa misingi ya kutokuwa na uwezo wa kimwili au kiakili. Kwa upande wake, Prof Kindiki amesema hana mpango wa kujiuzulu. "Wanaoniambia nijiuzulu wamekosea. Siwezi kujenga nyumba, niweke samani halafu niende kuishi msituni. Sitajiuzulu," alisema. Kauli hiyo imezua maswali kuhusu hatua ambayo Rais angechukua ikiwa ataamua kuwa anahitaji mgombea mwenza mwingine ili kuongeza nafasi ya kushinda mwaka 2027. Wakili Timothy Kariuki, alisema jaribio jingine la kumuondoa Naibu Rais ndani ya muhula mmoja lingeleta athari kubwa kisiasa. Alisema hatua hiyo ingeonyesha kuwa tatizo si manaibu rais bali ni Rais mwenyewe. Mchambuzi wa siasa Peter Kagwanja, anaamini Rais anaweza kutafuta njia nyingine za kuwapa nafasi viongozi wenye ushawishi badala ya kubadilisha mgombea mwenza. Alisema huenda akaimarisha nyadhifa nyingine serikalini ili kuwavutia viongozi wa kisiasa na kuongeza uungwaji mkono wa muungano wake. Wakati huo huo, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, anaendelea kushinikiza kuundwa kwa muungano wa kisiasa wa "Mlima Kenya Mashariki" unaojumuisha kaunti za Embu, Meru, Tharaka Nithi, Kirinyaga na Isiolo ili kumuunga mkono Rais Ruto na Prof Kindiki. Lakini matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, ambako mgombea aliyeungwa mkono na serikali alipata kura chache, yamezua maswali kuhusu kiwango ambacho serikali inaungwa mkono katika eneo hilo. Mwanasiasa na mchambuzi Gasper Odhiambo, alisema hali ya Prof Kindiki inaonyesha changamoto kubwa ndani ya Kenya Kwanza. Naye Bw Gachagua alisema hali anayopitia Prof Kindiki inafanana na aliyopitia kabla ya kuondolewa madarakani. Alidai kuwa Rais Ruto alimchagua Prof Kindiki ili kuziba pengo lililoachwa alipoondolewa lakini akasema Naibu Rais huyo ameshindwa kurejesha uungwaji mkono Mlima Kenya. Kwa mujibu wa Gavana Kang'ata, Rais anakabiliwa na uchaguzi mgumu. "Akimdumisha Kindiki anaweza kupoteza kura. Asipomchagua, kura chache alizonazo Mlima Kenya zinaweza kutoweka. Akimuondoa, anaweza kuzua mgogoro mpya kuhusu mrithi wake," alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 29 Jul 2026 21:55:56
Bunge lakaribia kupatia NTSA nguvu kudhibiti nauli za matatu
BUNGE linakaribia kupitisha mswada utakaopatia Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) mamlaka ya kudhibiti na kuidhinisha nauli zinazotozwa na magari ya uchukuzi wa umma nchini. Mswada huo wa Marekebisho ya Sheria ya NTSA wa mwaka 2023, unaodhaminiwa na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, unalenga kurekebisha Sheria ya NTSA ya mwaka 2012 ili kuweka mwongozo wa kupanga na kudhibiti nauli zinazolipwa na abiria wa magari ya uchukuzi wa umma. Iwapo utapitishwa, utamaliza uhuru ambao wamiliki wa matatu wamekuwa nao kwa miaka mingi wa kupanga na kubadilisha nauli watakavyo. Kwa sasa, nauli huamuliwa na nguvu za soko, jambo ambalo limekuwa likisababisha ongezeko la bei bila utaratibu maalumu. Mswada huo unapendekeza NTSA iwe na mamlaka ya kuidhinisha nauli zinazotozwa na magari ya uchukuzi wa umma na kuwapa abiria njia rasmi ya kuwasilisha malalamiko dhidi ya wanaotoza nauli kupita kiasi. Kenya itajiunga na nchi kama Ghana, Rwanda, Tanzania, Cameroon, Ivory Coast, Fiji na Ujerumani ambazo serikali hudhibiti kiwango cha chini cha nauli za usafiri wa umma. Wakati wa mjadala wa mswada huo, wabunge wengi waliunga mkono pendekezo hilo wakisema ni wakati wa kuleta utaratibu katika sekta ya matatu na kukomesha unyonyaji wa abiria kupitia nauli zisizotabirika. Bw Barasa alisema haiwezekani Kenya kuendelea kuwa nchi ambayo nauli hubadilishwa kulingana na hali ya hewa au idadi ya abiria waliopo katika vituo. "Hatuwezi kuwa na nchi ambayo leo ubao unaonyesha nauli ya Sh300, halafu mvua ikinyesha unawekwa mwingine unaosomeka Sh500. Hatuwezi kuwaacha Wakenya mikononi mwa magenge ya matatu," alisema. Aliongeza kuwa kama serikali inavyodhibiti bei ya miwa, mafuta na bidhaa nyingine muhimu, pia inapaswa kuwalinda wananchi dhidi ya sekta ya uchukuzi. "Mkenya anapotoka nyumbani akiwa na Sh100 ya nauli hajui atatozwa kiasi gani jioni. Mswada huu utaleta usawa na kuwasaidia wananchi kupanga matumizi yao," alisema. Mbunge wa Kesses Julius Ruto alisema kudhibiti sekta ya uchukuzi ni suala la maslahi ya umma ambalo Bunge haliwezi kulipuuza. Kwa upande wake, Mbunge wa Tigania West John Mutunga alisema imekuwa kawaida nauli kupanda bei ya mafuta inapoongezeka lakini zinakosa kushuka mafuta yanapopungua. "Hatuwezi kuruhusu matatu kubadilisha nauli watakavyo. Lazima kuwe na mfumo wa kupitia upya nauli kulingana na hali halisi," alisema. Mbunge wa Dagoretti North Beatrice Elachi alisema kizazi kijacho kinastahili mfumo wa uchukuzi ulio na utaratibu. "Lazima tuweke sheria zitakazoongoza sekta hii hata kama wahudumu wa matatu ni wapiga kura wetu. Tunahitaji mfumo wenye nidhamu," alisema. Pia alipendekeza kanuni hizo ziwahusu makanga wanaowanyanyasa abiria. Mbunge Maalum Sabina Chege alisema ni wajibu wa Bunge kuwalinda watumiaji wa huduma za uchukuzi dhidi ya kutozwa nauli kiholela. Hata hivyo, mswada huo umepingwa na Kamati ya Bunge ya Uchukuzi na pia aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen. Murkomen aliambia kamati ya Bunge mwaka 2023 kuwa kabla ya serikali kuanza kudhibiti nauli, lazima ifanye utafiti wa kina na mashauriano na wadau wote ili kubaini iwapo mfumo huo unaweza kutekelezwa bila kukiuka sheria na mikataba ya kimataifa. Mwaka 2018, Bunge lilikataa pendekezo kama hilo la Wizara ya Uchukuzi la kumpa Waziri mamlaka ya kudhibiti nauli za matatu. Pia Chama cha Wamiliki wa Matatu kilipinga pendekezo hilo mwaka 2020.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 29 Jul 2026 22:55:47
Jinsi kuvuliwa mamlaka Seneti kwa Sifuna na Osotsi kunawapunguzia malipo kwa Sh240,000
MABADILIKO kwenye kamati za Seneti yamemvua Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na mwenzake wa Vihiga Godfrey Osotsi baadhi ya nyadhifa zenye ushawishi mkubwa bungeni, hatua inayopunguza ushawishi wao wa kusimamia matumizi ya fedha za umma na kupunguza marupurupu yao kwa hadi Sh240,000 kwa mwezi. Mabadiliko hayo yaliyoidhinishwa Jumanne iliyopita yalimuondoa Bw Osotsi kama mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Uwekezaji wa Kaunti na Hazina Maalum, wadhifa aliokuwa ameshikilia kwa miaka minne. Sasa atahudumu kama mwanachama wa kawaida wa Kamati ya Biashara, Ustawi wa Viwanda na Utalii. Kwa upande mwingine, Bw Sifuna, ambaye amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa utawala wa Rais William Ruto ndani ya Seneti, aliondolewa kutoka Kamati ya Hesabu za Serikali za Kaunti (CPAC) na kuhamishiwa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Hatua hiyo imejiri siku chache baada ya kuvuliwa wadhifa wake wa Naibu Kiranja wa Wachache katika Seneti. Mbali na athari za kisiasa, mabadiliko hayo pia yanagusa maslahi ya kifedha ya wawili hao. Akiwa mwenyekiti wa kamati, Bw Osotsi alikuwa akipokea posho ya Sh15,000 kwa kila kikao cha kamati, kiwango ambacho kilikuwa kinaweza kufikia Sh240,000 kwa mwezi, mbali na mshahara na marupurupu mengine ya ubunge. Sasa, akiwa mwanachama wa kawaida wa kamati marupurupu yake yatashuka hadi Sh7,500 kwa kikao, huku kiwango cha juu kwa mwezi kikibaki Sh120,000. Pia atapoteza baadhi ya manufaa yanayotokana na kuongoza kamati yenye jukumu la kusimamia matumizi ya fedha za umma. Maseneta pia hulipwa gharama za safari moja ya kwenda na kurudi kutoka Bunge hadi kaunti wanazowakilisha kila wiki kwa kiwango kilichoidhinishwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), kulingana na umbali kutoka Nairobi. Hata hivyo, wanaohudumu katika kamati zenye majukumu makubwa ya usimamizi hupata nafasi nyingi zaidi za safari za kikazi, ukaguzi wa miradi na shughuli nyingine za uangalizi. Kwa kuondolewa katika kamati hizo muhimu, ushawishi wa Bw Sifuna na Bw Osotsi katika masuala ya uwajibikaji wa serikali za kaunti unatarajiwa kupungua. Kwa miaka minne, Bw Osotsi aliongoza moja ya kamati zenye nguvu zaidi Seneti, iliyokuwa ikichunguza matumizi ya fedha katika mashirika ya kaunti, kampuni za maji, hazina maalum na taasisi nyingine zinazotumia mabilioni ya fedha za umma. Kamati hiyo mara kwa mara huwaita magavana, maafisa wakuu wa kaunti na maafisa wa uhasibu kujibu hoja za ukaguzi zilizotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kama mwenyekiti, Bw Osotsi alikuwa akiongoza shughuli za kamati, kuelekeza uchunguzi na kuidhinisha ripoti ambazo mara nyingi zilikuwa msingi wa mapendekezo ya Seneti kuhusu ufisadi, matumizi mabaya ya fedha na urejeshaji wa pesa za umma. Akizungumza katika kikao cha Seneti Alhamisi, Bw Osotsi alishutumu uongozi wa ODM kwa kile alichokiita mienendo ya kidikteta. "Ikiwa kuna mtu anataka kumwondoa mwanachama katika kamati yoyote ya Bunge, afuate utaratibu wa kuwasilisha hoja rasmi badala ya kuwatisha wabunge kutia saini ombi la kumuondoa mwanachama ambalo sasa linasambazwa," alisema. Nafasi yake sasa imechukuliwa na Seneta wa Taita Taveta Johnnes Mwaruma, ambaye amehamishwa kutoka Kamati ya Hesabu za Serikali za Kaunti. Kuondolewa kwa Bw Sifuna kutoka Kamati ya Hesabu za Serikali za Kaunti nako kunaonekana kuwa pigo kubwa. Kamati hiyo ndiyo huchunguza ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kuhusu serikali za kaunti na huwa mstari wa mbele katika kuhoji magavana kuhusu matumizi ya fedha, zabuni, miradi iliyokwama na madeni yanayosubiri kulipwa. Kwa miaka ya hivi karibuni, Bw Sifuna alijijengea sifa kama mmoja wa wanachama waliokuwa wakitoa maswali makali kwa magavana na maafisa wa kaunti kuhusu hoja za ukaguzi. Maswali yake ya moja kwa moja, msisitizo wa kutaka ushahidi wa stakabadhi na ukosoaji wake wa matumizi yenye utata ulimfanya kuwa mmoja wa sauti kuu za upinzani katika kamati hiyo. Kuhamishwa kwake kwenda Kamati ya Kilimo kunamuondoa katika mstari wa mbele wa usimamizi wa fedha za kaunti na kumpokonya jukwaa ambalo amekuwa akilitumia kuikosoa serikali kupitia vikao vya kamati. Mabadiliko hayo pia yamemwingiza Kiongozi wa Wachache Seneti Stewart Madzayo katika Kamati ya Hesabu za Serikali za Kaunti kuchukua nafasi ya Bw Sifuna. Hatua hiyo imezua mjadala iwapo serikali jumuishi inaondoa kwa makusudi wakosoaji wake kutoka kamati muhimu za uwajibikaji ili kuimarisha ushawishi wake ndani ya Bunge. Hata hivyo, Bw Madzayo ametetea mabadiliko hayo akisema ni ya kawaida na yanalenga kuwapa maseneta nafasi ya kuhudumu katika kamati tofauti kwa ufanisi zaidi. "Tumefanya mabadiliko haya kama sehemu ya utaratibu wa kawaida. Yamekuja wakati ambapo hali ya kisiasa imepamba moto, lakini lengo ni kuwapa wanachama nafasi ya kuhudumu katika kamati mbalimbali ili kuboresha utendakazi," alisema. Wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kudhoofisha uwezo wa Seneti kusimamia matumizi ya fedha za umma kwa kupunguza idadi ya sauti huru katika kamati muhimu za uwajibikaji.
read moreRight Column Content