T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 15 Aug 2026 12:02:06

Watengenezaji wa chakula cha mifugo wahamasisha kilimo cha mahindi ya manjano kuziba pengo la malighafi

MABADILIKO ya tabianchi, ukame wa muda mrefu na mvua zisizotabirika vinaendelea kuathiri uzalishaji wa mazao nchini Kenya, hali inayowasukuma watengenezaji wa chakula cha mifugo kuhimiza kilimo cha mahindi ya manjano ili kupunguza utegemezi wa malighafi kutoka nje na gharama za uzalishaji. Chama cha Watengenezaji wa Chakula cha Mifugo Kenya (AKEFEMA) kinaitaka serikali, watafiti na wakulima kuhamasisha uzalishaji wa mahindi ya manjano kwa ajili ya chakula cha mifugo, huku mahindi meupe yakitengwa zaidi kwa matumizi ya binadamu. "Malighafi huchangia kati ya asilimia 70 na 80 ya gharama ya kutengeneza chakula cha mifugo. Kenya bado inaagiza malighafi nyingi kutoka nje, licha ya kuwa na uwezo wa kuzalisha sehemu kubwa humu nchini," alisema Mwenyekiti wa AKEFEMA Joseph Karuri. [caption id="attachment_191153" align="aligncenter" width="300"] Mahindi shambani yakiendelea kukua. Picha|Sammy Waweru[/caption] Karuri alisema mahindi ndiyo chanzo kikuu cha virutubisho vya wanga (carbohydrates) katika chakula cha mifugo, lakini uhaba wa mahindi kwa matumizi ya binadamu unalazimisha wafugaji kushindana na watu kwa nafaka hiyo. Chama hicho pia kinataka kuongezwa kwa uzalishaji wa alizeti, soya, pamba na canola, ambazo mabaki yake baada ya kukamua mafuta hutumika kama chanzo muhimu cha protini katika chakula cha mifugo. Karibu asilimia 80 ya malighafi hizo za protini huagizwa kutoka Tanzania, Uganda, Malawi na Zambia. Kenya hutumia takriban magunia milioni saba ya mahindi ya kilo 90 kila mwaka kutengeneza chakula cha mifugo, sawa na tani 630,000. Ingawa uwezo wa viwanda vya kutengeneza chakula cha mifugo ni karibu tani milioni nne kwa mwaka, uzalishaji halisi ni tani milioni 2.5 pekee kutokana na uhaba wa malighafi. [caption id="attachment_191155" align="aligncenter" width="300"] Mkulima akikagua shamba lake la mahindi katika kaunti ya Kiambu. Picha|Sammy Waweru[/caption] Karuri alisema kuboresha lishe ya mifugo ni muhimu kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na mayai. Kenya huzalisha karibu lita bilioni tano za maziwa kwa mwaka, lakini ng'ombe mmoja hutoa wastani wa lita saba hadi nane kwa siku. Aidha, AKEFEMA pia inahimiza matumizi ya teknolojia ya Near Infrared (NIR), inayowezesha kuchanganua ubora wa malighafi ndani ya dakika tano hadi 10 na kusaidia wataalamu kutengeneza mchanganyiko sahihi wa chakula. Makamu Mwenyekiti wa AKEFEMA, Dkt David Murumba, alisema teknolojia hiyo inaweza kupunguza upotevu wa malighafi wakati wa uundaji wa malisho, kuongeza ufanisi na kuboresha afya ya mifugo. [caption id="attachment_191156" align="aligncenter" width="300"] Chama cha Watengenezaji wa Chakula cha Mifugo Kenya (AKEFEMA) kinaitaka serikali, watafiti na wakulima kuhamasisha uzalishaji wa mahindi ya manjano kwa ajili ya chakula cha mifugo. Picha|Sammy Waweru[/caption] Katibu Mkuu wa AKEFEMA, Dkt Wilfred Kamau, alisema uwekezaji katika mashine za kisasa, wataalamu na mikopo nafuu ni muhimu kupunguza gharama za uzalishaji na hatimaye bei ya maziwa, mayai na nyama ya nguruwe kwa walaji pia itashuka.  

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Kenya yapewa leseni ya kuunda dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi

KENYA imepewa leseni ya kutengeneza dawa mpya ya kumeza ya kuzuia maambukizi ya ukimwi, hatua inayoiweka miongoni mwa nchi tatu Afrika zitakazozalisha dawa hiyo kwa ajili ya masoko ya Afrika. Kampuni ya dawa ya Merck imetoa leseni ya kuzalisha toleo la bei nafuu la Alimatravir, dawa inayotarajiwa kumezwa mara moja kwa mwezi. Nchini Kenya, dawa hiyo itatengenezwa na Kampuni ya Universal Corporation. Hatua hiyo inatajwa kuwa ya kihistoria kwani watengenezaji wa dawa barani Afrika wamehusishwa katika mchakato wa uzalishaji wa dawa ya HIV tangu mwanzo. Utafiti wa awamu ya tatu unaoendelea Kenya, Uganda na Afrika Kusini unahusisha wanawake vijana na unatarajiwa kukamilika mwaka ujao. "Afrika inabeba robo ya mzigo wa magonjwa duniani. Tunatengeneza chini ya asilimia sita ya vifaa vya matibabu tunavyohitaji na asilimia moja ya chanjo tunazotumia." akasema Rais William Ruto, katika hotuba iliyosomwa na Waziri wa Afya Aden Duale katika mkutano wa pembeni wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Alisema janga la Covid-19 lilionyesha madhara ya kutegemea minyororo ya usambazaji kutoka nje. "Watu wetu walilipa gharama ya minyororo ya usambazaji ambayo hatukuimiliki. Hatutapitia hali hiyo tena," akasema. Rais Ruto pia alisema Afrika sasa ina fursa ya kutengeneza dawa zake badala ya kusubiri kuzinunua kutoka nje. "Kiwanda kisichokuwa na wanunuzi si sekta ya viwanda. Ni jengo la gharama kubwa," alisema. Merck inasema dawa hiyo inaweza kugharimu dola tano (Sh650) kwa mtu kwa mwaka. Dkt Nicholas Muraguri alisema ushirikiano huo utasaidia Afrika kuimarisha uzalishaji wa dawa, ajira na usambazaji. "Ushirikiano huu si wa kusambaza dawa pekee, unahusu kubadilisha mfumo wa usawa katika afya duniani," akasema. Alisema tatizo la kuzuia maambukizi ya ukimwi si ukosefu wa sayansi, bali gharama na kupungua kwa ufadhili wa programu za afya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 6 hours ago

Ni kaunti 10 pekee ndizo zilitumia asilima 70 ya fedha kwa maendeleo-Ripoti

KAUNTI 10 zinaongoza katika matumizi ya fedha za maendeleo katika mwaka wa kifedha wa 2025/2026, huku kila moja ikitumia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti iliyotengewa miradi ya maendeleo. Ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakang'o iliyotolewa wiki iliyopita inaonyesha Kilifi, Wajir, Mandera, Meru, Trans Nzoia, Kirinyaga, Marsabit, Samburu, Kericho na Vihiga ziliongoza katika matumizi hayo. Kilifi iliongoza kwa asilimia 84.52, ikifuatwa na Wajir kwa asilimia 83.03 na Mandera kwa asilimia 80. Meru ilitumia asilimia 79.04, Trans Nzoia (asilimia 73.94), Kirinyaga (asilimia 73.89), Marsabit (asilimia 73.79) na Samburu ( asilimia 73.24). Kericho na Vihiga zilitumia asilimia 71.70 na 70.16 mtawalia. Kaunti hizo 10 zilitumia jumla ya Sh34 bilioni kati ya Sh126.69 bilioni zilizotumiwa na kaunti zote 47 katika miradi ya maendeleo. "Katika mwaka wa kifedha wa 2025/2026, serikali zote 47 za kaunti zilitumia Sh126.69 bilioni katika shughuli za maendeleo, sawa na kiwango cha matumizi cha asilimia 54 ya bajeti ya maendeleo ya Sh233.69 bilioni," inasema ripoti hiyo. Hata hivyo, matumizi ya kawaida yalichukua sehemu kubwa ya bajeti, huku kaunti zikitumia Sh369.89 bilioni, sawa na asilimia 89.23 ya matumizi yote ya Sh496.58 bilioni. Matumizi ya maendeleo yalikuwa Sh126.69 bilioni, sawa na asilimia 25.51 ya matumizi yote. Meru na Wajir pia ziliongoza katika matumizi ya kawaida, kwa asilimia 91.85 na 90.23 mtawalia. Matumizi ya maendeleo yaliongezeka kwa Sh3 bilioni ikilinganishwa na 2024/2025, ambapo kaunti zilitumia Sh123.76 bilioni. Kilifi ilitumia Sh6.3 bilioni kati ya Sh7.4 bilioni zilizotengewa maendeleo, Wajir Sh4 bilioni kati ya Sh4.9 bilioni, huku Mandera ikitumia Sh4.3 bilioni kati ya Sh5.4 bilioni. Kwa upande mwingine, kaunti 13 zilitajwa kwa kuwa na kiwango cha chini cha matumizi ya fedha za maendeleo. Kaunti hizo ni Nakuru (asilimia 48.97), Kajiado (asilimia 48.05), Baringo (asilimia 47.76), Mombasa (asilimia 45.75), Laikipia (asilimia 45.49), Kiambu (asilimia 43.10), Kisii (asilimia 41.01), Uasin Gishu (asilimia 40.10), Narok (asilimia 34.42), Elgeyo-Marakwet (asilimia 34.17), Nairobi (asilimia 28.47), Siaya (asilimia 26.53) na Kisumu (asilimia 25.92). Utawala wa Gavana Johnson Sakaja, kwa mfano, ulitumia Sh3.8 bilioni kati ya Sh13.4 bilioni zilizotengewa maendeleo Nairobi. Siaya ilitumia Sh1.6 bilioni kati ya Sh6 bilioni, huku Kisumu ikitumia Sh1.7 bilioni kati ya Sh6.7 bilioni. Ripoti pia ilieleza wasiwasi kuhusu kaunti kutumia fedha nyingi katika mishahara na shughuli za kawaida badala ya maendeleo. Kaunti zilitumia Sh235.96 bilioni kulipa mishahara, mishahara midogo na marupurupu, huku Sh133.92 bilioni zikitumika katika shughuli za ukarabati. Kaunti pia zilikusanya Sh96.08 bilioni kutokana na mapato ya ndani, sawa na asilimia 89.99 ya lengo lao la mwaka. Hii ilikuwa ongezeko kutoka Sh67.3 bilioni zilizokusanywa mwaka wa 2024/2025. Aidha, kaunti zilipokea Sh415 bilioni kama mgao wa kitaifa. Mdhibiti wa Bajeti amezitaka kaunti kudhibiti matumizi ya mishahara na kuzingatia sheria inayowataka kuweka matumizi hayo katika viwango endelevu. Ripoti inaonyesha miradi 189 yenye thamani ya Sh10.51 bilioni imekwama katika kaunti mbalimbali. Pia, kaunti ziliripoti madeni ambayo hayajalipwa yenye thamani ya Sh172.53 bilioni kufikia Juni 30, 2026. Nairobi ilikuwa na deni kubwa zaidi la Sh86.9 bilioni, sawa na asilimia 50.35 ya jumla hiyo. Bi Nyakang'o alisema baadhi ya kaunti hutumia hadi asilimia 70 ya fedha zao kulipa mishahara na kuacha asilimia 30 pekee kwa maendeleo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Viongozi wa Samburu, Meru wakosoa oparesheni ya usalama unaoendeshwa na kikosi maalum cha polisi

VIONGOZI kutoka kaunti za Meru na Samburu wamegawanyika kuhusu oparesheni ya usalama inayoendelea katika Kaunti ya Samburu kulenga majangili wanaodaiwa kuvamia maeneo ya Meru na Isiolo. Oparesheni hiyo ilianzishwa baada ya mashambulizi ya mara kwa mara ya majangili katika maeneo hayo na kuuawa kwa maafisa wawili wa polisi, polisi wa akiba na raia wawili Isiolo wiki iliyopita. Bunduki za maafisa hao pia ziliibwa wakati wa shambulizi hilo huko Gotu. Hata hivyo, oparesheni hiyo inayotekelezwa na kikosi maalumu cha polisi imekosolewa baada ya mamia ya mifugo kuuawa katika Wadi ya Waso, Samburu. Gavana wa Samburu Lati Lelelit na Mbunge wa Samburu Mashariki Jackson Lekumontare wameitaka serikali kusitisha oparesheni hiyo. "Watu wasio na hatia wamepoteza mifugo 700, wakiwemo ng'ombe, mbuzi na punda, katika muda wa siku nne na maafisa wa polisi wamekuwa wakifyatua risasi bila kujali. Ni jambo la kusikitisha kwamba wahalifu wachache waliwaua watu watano Isiolo, lakini hilo haliwezi kuhalalisha mauaji ya kiholela ya mifugo," akasema Bw Lelelit. Bw Lekumontare alisema wakazi walioathiriwa wanapaswa kufidiwa na oparesheni hiyo isimamishwe ili wazee wa jamii washirikishwe katika kuwatambua majangili. Kamanda wa Polisi wa Samburu David Nkoroi alisema wakazi kadhaa wameripoti kupoteza mifugo, lakini bado hawajabaini idadi kamili ya mifugo hiyo Wabunge John Mutunga (Tigania Magharibi), Dan Kiili (Igembe ya Kati), Julius Taitumu (Igembe Kaskazini), Mugambi Rindikiri (Buuri) na Mpuru Aburi (Tigania Mashariki) nao wameitaka serikali kuimarisha oparesheni dhidi ya majangili. Wakizungumza mjini Meru Jumamosi, wabunge hao walisema wafugaji wa Meru wamepoteza karibu ng'ombe 20,000 huku watu 300 wakiuawa au kujeruhiwa na majangili wanaoendesha shughuli zao kutoka Isiolo na Samburu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Mnamo Machi, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alitangaza baadhi ya maeneo ya Laikipia, Meru, Samburu na Isiolo kuwa hatari. Bw Murkome aliidhinisha oparesheni iendelezwe kutwaa silaha haramu mikononi mwa raia. Naibu Rais Kithure Kindiki aliunga mkono oparesheni hiyo, akisema serikali itaongeza nguvu dhidi ya majangili wenye silaha katika Isiolo na Samburu. Wakati huo huo, Bw Murkomen alijutia kuuawa kwa mifugo Samburu, lakini akasema serikali haitasitisha juhudi za kurejesha usalama katika Isiolo, Samburu, Turkana na Pokot Magharibi. Alisema oparesheni hizo zinalenga kurejesha silaha haramu na mifugo iliyoibwa, kuvunja mitandao ya uhalifu na kurejesha amani ya kudumu. Waziri huyo alisema vyombo vya usalama vimeagizwa kuchukua tahadhari zaidi ili kupunguza madhara kwa raia na mali wakati wa oparesheni. Aliongeza kuwa zaidi ya silaha 3,000 haramu na risasi 8,000 zimepatikana katika oparesheni za usalama Kaskazini mwa Bonde la Ufa na Kaskazini mwa Kenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 8 hours ago

Viongozi wa ODM wampa Aladwa 'kibali' kupambana na Sakaja 2027

MBUNGE wa Makadara, George Aladwa, amepata uungwaji mkono mkubwa katika azma yake ya kuwania ugavana wa Nairobi baada ya wajumbe na wenyekiti wa matawi ya ODM kumuunga mkono katika uchaguzi wa 2027. Katika hafla iliyofanyika katika eneobunge lake wikendi, Bw Aladwa aliidhinishwa kwa kauli moja na wajumbe wa matawi ya ODM, hatua iliyompa nafasi rasmi ya kutafuta tiketi ya chama katika uchaguzi huo. Bw Aladwa, ambaye pia ni mwenyekiti wa tawi la ODM, alisema yuko tayari kushindana na wagombea wengine ambao wametangaza nia ya kuwania kiti hicho. Katika hotuba yake, mbunge huyo alisema yeye ni miongoni mwa wanachama wa muda mrefu wa ODM ambao wamekiunga mkono wakati wa mazuri na magumu, hivyo anastahili kupewa tiketi. "ODM ina mgombea na nimejisajili. Nimewahudumia Wakenya kupitia chama hiki na niko tayari kuwa gavana wa Nairobi," akasema Bw Aladwa. Pia alifichua kuwa baadhi ya viongozi wanapanga kuondoka katika vyama vyao na kujiunga na ODM kwa matumaini ya kupewa tiketi ya kuwania kiti hicho. "Kwa wale wanaotoa pesa wakitarajia kumng'oa Aladwa, nataka kuwaambia kwamba mimi si mtu wa kusukumwa pembeni na nyinyi nyote mnajua hilo. Kutakuwa na ushindani. ODM ni chama cha kidemokrasia chini ya kiongozi wetu wa chama, Dkt Oburu Oginga," akasema Bw Aladwa. Kuhusu mpango wa mafuta wa ununuzi wa mafuta wa serikali kwa serikali (G-to-G, mbunge huyo alisema ulilenga kutatua tatizo la awali kwa kuruhusu bidhaa za petroli kuagizwa kwa masharti ya mkopo yaliyoongezwa hadi siku 180. Alisema hatua hiyo ilipunguza shinikizo la haraka katika soko la fedha za kigeni na kuipa nchi nafasi zaidi ya kudhibiti mahitaji yake ya dola. "Ikiwa mpango wa G-to-G unaelezwa kuwa wa gharama kubwa au usio wa kawaida, basi wanaotoa madai hayo wanapaswa kuwasilisha mikataba, bei za uagizaji, ada za ziada, gharama za usafirishaji na ushahidi mwingine," akasema. "Ikiwa kuna ushahidi wa ufisadi au ukiukaji wa sheria, uwasilishwe Bungeni, kwa mashirika ya uchunguzi na taasisi nyingine zinazohusika. Madai mazito yanahitaji ushahidi mzito." akaongeza. Mbali na Bw Aladwa, wagombea wengine ambao wametangaza nia ya kuwania kiti hicho ni pamoja na Askofu Margaret Wanjiru, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya na Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri. Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja pia anatarajiwa kuwania muhula mwingine katika juhudi za kuwa gavana wa kwanza wa Nairobi kuchaguliwa tena tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi mwaka 2013.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Kauli tata ya Kalonzo kuhusu 'uwezekano wa kufanya handisheki na Ruto' yazua gumzo

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amezua mjadala kuhusu msimamo wake wa kisiasa baada ya kuonyesha dalili ya kuwa atashiriki handisheki na Rais William Ruto upinzani ukishindwa uchaguzi wa 2027. Bw Musyoka amesisitiza kuwa siasa za ushindani kati ya Rais Ruto na vinara wa upinzani inastahili kuzingatia masuala yanayohusisha maslahi ya nchi badala ya uhasama wa kisiasa. "Ukitushinda, tunaweza kutathmini ukiwa na tabia nzuri. Tukikushinda, tutaangalia masuala haya yote. Tuangaliane kwa sababu tuna nchi na Mungu haheshimu binadamu licha ya hadhi yake," akasema Bw Musyoka. Bw Musyoka alikuwa akizungumza jana katika Kaunti ya Siaya ambayo ni ngome ya kisiasa ya marehemu kigogo wa siasa za upinzani Raila Odinga. Hatua ya kinara huyo wa Wiper kumsifu Rais Ruto imeibua mjadala kuhusu mahali ambapo uaminifu wake wa kisiasa upo. Siku tatu zilizopita alimsifu Rais kwa kujenga barabara inayoelekewa kwake Tseikuru. "Bw Ruto kwa sababu ya kuogopa sisi ameweka bidii barabara ifike Tseikuru na namwambia awekee bidii imechelewa kwa sababu barabara hiyo ingekuwa imefika Maua. Bw Ruto anatumiwa na Mungu kwa njia spesheli. Kuweka hiyo bidii si Ruto ni Mungu. Kufikia Agosti mwaka tukikuja nyumbani itakuwa imekaribia sana," akasema Bw Musyoka wakati wa Ukumbusho wa miaka 20 tangu mauti ya mamake.  "Sasa tuna chuo cha kitaifa cha kiufundi baada ya kuongea na Ruto. Tunakubali kuwa hii inafaa kuwa chuo cha kitaifa cha kiufundi," akaongeza. Kauli ya Bw Musyoka imekuja wakati ambapo kuna kutoaminiana ndani ya upinzani huku Rais Ruto akitumia kauli za kiongozi huyo wa Wiper kumkejeli na kusema kuwa ni kati ya viongozi wanayemtambua kazi yake. Aidha Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki miezi ya nyuma amekuwa akimsifu Bw Musyoka na kumrejelea kama kiongozi muungana ambaye anastahili kuungana na serikali ili kuwafanyia Wakenya kazi. Jana Bw Musyoka pia aliitaka serikali kuelekeza nguvu kwa wapinzani watakaokuwa kwenye debe badala ya kumlenga Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 10 hours ago

Wantam! Sifuna aidhinishwa na Linda Mwananchi kupambana na Ruto 2027

HATUA ya Linda Mwananchi kumuidhinisha rasmi Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwa mgombea wake wa urais, inaonekana kufunga mlango kwa azma ya Gavana wa Siaya James Orengo kuwania uongozi wa nchi kupitia vuguvugu hilo. Katika mkutano huo wa Jumamosi, viongozi wakuu wa vuguvugu hilo waliamua kumuunga Seneta Sifuna huku wakisaka muungano mkubwa wa upinzani kuelekea kwa Uchaguzi Mkuu wa 2027.  "Leo (Jumamosi), tulikutana kama uongozi wa Linda Mwananchi na kuamua kusonga mbele pamoja, tukiwa tumeunganishwa na lengo moja la kujibu wito wa Wakenya wanaotafuta utawala bora na kuikomboa nchi. "Pia tuliamua kwamba Edwin Watenya Sifuna ndiye kiongozi wetu na mgombea wetu wa urais," ikasema taarifa ya vuguvugu hilo. Mkutano huo ulihudhuriwa na Bw Sifuna, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi. Wengine waliohudhuria ni Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo, Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini), Clive Gisairo (Kitutu Masaba), Gavana wa zamani wa Meru Kawira Mwangaza na aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Faith Odhiambo. "Orengo alituma udhuru lakini sote tulikubaliana kwamba ni Sifuna pekee atakayeungwa kuwania urais. Hana nafasi sasa kwa sababu wote waliokuwepo walikubaliana kuhusu uwanizi wa Sifuna," akasema Dkt Khalwale. Dkt Khalwale alisema wanachama walijaribu kumshawishi Bw Owino kuwania ugavana wa Nairobi kwa kutumia chama kimoja na Bw Sifuna katika juhudi za kuunganisha ngome zao za kisiasa. "Wengi walimpinga lakini sasa suala hilo ni uamuzi wake kwa sababu yeye alisimama kidete na msimamo wake," akasema Dkt Khalwale. Bw Owino tayari amesajili The Mwananchi Party (TMP), ambayo anakusudia kutumia kuwania ugavana wa Nairobi. Mipango yake ya kisiasa imekuwa ikipingana na juhudi za kupata chama kimoja cha kisiasa, huku Bw Natembeya akisukuma Bw Sifuna kuwania kwa kutumia UDP. Bw Natembeya alisema wiki iliyopita kuwa Bw Sifuna alikuwa tayari kutangaza UDP kuwa chama atakachotumia kuwania urais. Jaribio la awali la kubadilisha jina la UDP kuwa Ukombozi People's Party (UPP) lilikwama baada ya Kiongozi wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka kusajili The Ukombozi Alliance (TUA), hatua iliyotatiza mipango ya vuguvugu hilo kuhusu jina hilo. Linda Mwananchi imetangaza mipango ya kuzindua chama cha Bw Sifuna cha kuwania urais Oktoba 3.  Mmoja wa viongozi wakuu waliohudhuria mkutano wa Jumamosi lakini akakataa kutajwa jina alisema kutokuwepo kwa Bw Orengo hakupaswi kuchukuliwa kama ishara ya mgawanyiko ndani ya vuguvugu hilo. "Alisema hangeweza kuhudhuria mkutano lakini tutamuunga mkono Sifuna kama kila mtu alivyokubaliana. Hakuna mgawanyiko kama inavyodaiwa na tunaamini Orengo yuko pamoja nasi katika kumuunga mkono Sifuna," akasema kiongozi huyo. Aliongeza kuwa maandalizi ya uzinduzi wa chama cha Bw Sifuna yalikuwa yamepiga hatua kubwa lakini akakataa kutoa maelezo zaidi. Bw Owino, katika taarifa baada ya mkutano huo, pia alisisitiza umoja ndani ya vuguvugu hilo, akisema lengo la upinzani kushinda serikali linaweza kufikiwa tu kupitia umoja wao. Bw Orengo hakuhudhuria mkutano wa faragha wa Jumamosi ambako uamuzi huo ulifanywa, licha ya kuwa ametangaza hadharani nia yake ya kuwania urais. Viongozi waliohudhuria kikao hicho walisema Bw Orengo alituma udhuru kwa sababu alikuwa na mwanafamilia mgonjwa, na kusisitiza kuwa kutokuwepo kwake hakupaswi kufasiriwa kama ishara ya mgawanyiko. Bw Orengo amekuwa akisisitiza kuwa umoja wa upinzani haupaswi kuzima azma za wagombea wengine na amekuwa akitaka uteuzi huru wa kumpata mgombeaji wa urais wa Linda Mwananchi. "Hakuna tatizo kushindana ndani ya Linda Mwananchi au upinzani. Muhimu ni kuwasilisha wagombea wote kwenye mchakato wa kuaminika wa uteuzi na, mwishowe, tupate mgombea mmoja wa kukabiliana na Rais William Ruto," akasema gavana huyo hapo awali. Jana Taifa Dijitali ilijaribu kubaini sababu ya Bw Orengo kukosa mkutano huo na ikiwa anaunga mkono kuidhinishwa kwa Bw Sifuna, lakini hakujibu jumbe wala kupokea simu. Gavana huyo alitarajiwa Jumapili kuungana na kiongozi wa Jubilee Fred Matiang'i na Kiongozi wa People's Party of Kenya Ndindi Nyoro kwa ibada katika Kanisa la Dominion Olerai kabla ya mkutano wa hadhara mjini Narok.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 18 hours ago

Harambee Stars yatoka nyuma kulazimisha sare dhidi ya Eritrea

Harambee Stars ilitoka nyuma na kunyakua alama moja dhidi ya Eritrea, katika mechi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027. Mechi hiyo ya Kundi D iliyochezwa jana Uwanja wa Nyayo, Nairobi, iliisha kwa sare ya 1-1. Wageni walitangulia kwa bao la dakika ya 36 kupitia kwa Girmai Netabay Kabaka, kabla ya mshambuliaji Ryan Ogam kusawazisha dakika ya 87. Stars itasafiri hadi Conakry, Guinea, kwa mechi dhidi ya wenyeji Oktoba 1 katika Uwanja wa Stade du 28 Septembre, kabla ya dirisha la kimataifa la mapumziko kufungwa. Ingawa Stars tayari imefuzu moja kwa moja kwa fainali za AFCON 2027 kama mwenyeji pamoja na Uganda na Tanzania, kocha Bennie McCarthy amesisitiza kuwa bado analenga kumaliza miongoni mwa timu mbili bora kundini. Stars, chini ya kocha McCarthy, iliingia kambini Jumanne lakini maandalizi yake yalitatizwa na mgomo wa wachezaji waliokuwa wakidai malipo ya posho. Wachezaji walifanya mazoezi yao ya kwanza Ijumaa tu Uwanja wa Nyayo, na kuingia uwandani moja kwa moja Jumamosi baada ya mgomo. Katika kipindi cha pili, wachezaji watatu wa Stars walianguka uwandani kwa wakati mmoja, ishara kuwa ukosefu wa mazoezi umeanza kuwaathiri. Kocha McCarthy alianza na Bryne Omondi langoni , akilindwa na Hannif Wesonga, nahodha Abud Omar na Frank Onyango. Kiungoni aliwaweka Duke Abuya, Timothy Ouma na Job Ochieng, huku safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Ryan Ogam na Micah Obonyo. Kati ya wachezaji 11 walioanza, ni watatu pekee wanaocheza ligi ya Kenya ikilinganishwa na Eritrea ambao Wachezaji wake wanacheza soka ya kulipwa Ulaya. Wachezaji chipukizi Shariff Musa na Amos Wanjala walipewa nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza. Kwa upande wa Eritrea, ni mchezaji mmoja tu kati ya 11 walioanza ndiye anayecheza ligi ya nyumbani. Golini alianza kipa anayeishi Australia, Yonathan Abiel wa Green Gully SC, akilindwa na Jonas Idris Ibrahim anayecheza Norway katika klabu ya BK Fremad, Jemal Mahmoud wa Preston Lions, Australia na Victor Stefan wa Kongsvinger, Norway. Kiungoni nahodha Ablelom Teklezghi wa RSFC ya Eritrea aliongoza safu iliyojumuisha Tesfaldet Simon wa Al Masry ya Misri, Esrom Mussie wa SAIT Trojans ya Canada na Namrud Embaye wa Wurzburger Kickers ya Ujerumani. Katika safu ya ushambuliaji waliwamo Filmon Rezene wa SV Elversberg ya Ujerumani, Ali Suleiman wa Al Masry ya Misri na Esrom Mussie wa Degerfors ya Sweden. Eritrea, inayofunzwa na Mmisri Hesham Yakan na kushika nafasi ya 184 ikilinganishwa na Kenya iliyonafasi ya 104. Wanaofahamika kama Red Sea Camels wamekuwa na mechi chache za ushindani miaka ya hivi karibuni, hali inayowafanya kuwa wagumu kutathminiwa kwa kukosekana kwa video za kutosha kwa benchi la ufundi la Kenya. Mechi hii ilikuwa ya 10 kati ya mataifa hayo mawili, Kenya ikiwa na rekodi bora zaidi ya na sasa imepata ushindi Mara tano , sare mbili na kupoteza mechi tatu. Katika mechi nyingine ya Kundi D, Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana ilipata ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Guinea jana.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Enez Mango sasa ni mali ya Politehnica Timișoara Feminina ya Romania

BEKI wa Harambee Starlets, Enez Mango, amejiunga na klabu ya Politehnica Timișoara Feminina ya Romania baada ya kuitumikia Farul Constanța ya Romania kwa miaka minne. Mango, ambaye ni beki wa kushoto, amesaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo inayoshiriki Ligi ya Divisheni ya Pili ya Wanawake nchini Romania, ukiwa na kipengele cha kuongeza muda wake. Akizungumza kipekee na Taifa Spoti, Mango hakuficha furaha yake kujiunga na klabu hiyo, akisema atapata fursa ya kucheza tena pamoja na kiungo Laura Rus, ambaye anamtaja kuwa mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea katika soka ya Romania. "Nina furaha kubwa kwa sababu Laura Rus, ambaye ni mmoja wa wachezaji bora katika historia ya soka la Romania, yupo hapo. Nilicheza naye Farul, lakini aliondoka mapema. Kucheza naye tena ni jambo la kufurahisha kwa sababu tulikuwa na maelewano mazuri sana uwanjani," alisema Mango. Aliongeza: "Politehnica ni klabu kubwa, na pia ninapenda jiji hilo pamoja na mazingira na hali za timu." Mango anatarajiwa kujiunga na wenzake pindi atakapopata visa ya kwenda Romania. Beki huyo mwenye uzoefu pia alikuwa akivutia vilabu vingine viwili vya Romania, Gloria na Timișoara, kabla ya kuamua kujiunga na Politehnica. Klabu hiyo yenye makao yake katika jiji la Timișoara, magharibi mwa Romania, ilianzishwa mwaka 1921 na Chuo Kikuu cha Ufundi cha Timișoara. Kwa sasa inapigania kupanda daraja na kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini humo msimu ujao. Uhamisho huo unamfungulia Mango ukurasa mpya katika soka ya kulipwa barani Ulaya, baada ya kipindi chenye mafanikio akiwa na Farul Constanța, ambako pia ni nyumbani kwa mlinda lango wa Starlets, Lilian Awuor. Mango alijiunga na Farul mwaka 2022 akitokea Vihiga Queens, ambapo alikuwa nahodha na mmoja wa wachezaji tegemeo wa timu hiyo. Akiwa Farul, alishinda mataji mawili ya ligi na kuhudumu kama nahodha. Pia alishiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya kwa Wanawake (UEFA ), ambako alicheza pamoja na Awuor. Kabla ya kuhamia Romania, Mango alikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Vihiga Queens, akiiongoza kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF-WPL). Pia aliiongoza Vihiga Queens kutwaa ubingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa ya Wanawake ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) mwaka 2021. Ushindi huo uliiwezesha timu hiyo kufuzu kwa mara ya kwanza kwa Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake. Mango, 33, amekuwa mchezaji wa Starlets tangu mwaka 2015, akishiriki katika mechi mbalimbali za kimataifa, zikiwemo kuwakilisha Kenya katika Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON). Alikuwa sehemu ya kikosi cha Kenya kilichoshiriki fainali za WAFCON nchini Morocco mwaka huu, ambapo Starlets ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji Morocco, Algeria na Senegal lakini Kenya ikabanduliwa mapema baada ya kupoteza mechi zote za hatua ya makundi. Uzoefu wake wa soka ya ndani na kimataifa unatarajiwa kuwa muhimu anapoanza safari mpya na Politehnica Timișoara, huku akilenga kusaidia klabu hiyo kupanda daraja na kufikia malengo yake ya kushiriki michuano ya UEFA.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Kenya na Tanzania kumenyana katika vita vya kufuzu AFCON 23

TIMU ya taifa ya soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23, Emerging Stars, leo itaanza kampeni yake ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana (U23 AFCON) 2027 itakapokutana na Tanzania leo, katika mechi ya raundi ya kwanza katika uwanja wa Kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi kuanzia saa tisa mchana. Tiketi za mechi zilikuwa zikiuzwa kwa Sh 200 kwa watu kawaida na Sh 500 kwa watu mashuhuri. Kocha wa Kenya Antony Kimani, Jumapili alitangaza kikosi cha mwisho cha wachezaji 27 kwa ajili ya mechi hiyo, huku timu hiyo ikilenga kuanza kampeni kwa matokeo mazuri dhidi ya watani wake wa Afrika Mashariki. Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa Kenya na Tanzania kukutana katika kiwango hiki, huku timu hizo zikitafuta tiketi ya kushiriki fainali za U23 AFCON zitakazofanyika Misri mwakani. Kenya bado haijawahi kufuzu kwa fainali za mashindano hayo, huku Tanzania pia ikiwa haijawahi kufikia hatua hiyo. Kenya iliingia uwanjani mara ya mwisho mwaka 2021 wakati wa michuano ya CECAFA, ambapo ilipoteza 1-0 dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya mchujo. Tangu ianze kushiriki katika kiwango cha U23 mwaka huo, Kenya imecheza mechi saba katika mashindano mbalimbali, ikishinda mbili, kutoka sare mbili na kupoteza tatu. Tanzania, kwa upande wake, mara ya mwisho ilishiriki mechi za kufuzu U23 AFCON mwaka 2022, ilipoondolewa na Nigeria 3-1 kwa jumla ya mabao. Kwa jumla, Tanzania imecheza mechi nane tangu ilipoanza kushiriki katika kiwango hiki mwaka 2021, ikishinda tatu, kutoka sare nne na kupoteza moja. Kabla ya mechi hiyo, Kenya imekumbwa na pigo baada ya mshambuliaji Humphrey Aroko kuachwa nje ya kikosi kutokana na jeraha alilopata akiwa katika majukumu ya klabu yake, Rosengård ya Uswidi. Kiungo Aldrine Kibet anayeipigia RC Celta ya Uhispania naye hakusafiri kwa ajili ya mechi hiyo kutokana na suala la kibali chake cha kazi, ambacho muda wake wa matumizi unakaribia kumalizika na kwa sasa anashughulikia. Mshindi wa jumla kati ya Kenya na Tanzania atakutana na Ivory Coast katika raundi ya pili ya mchujo. Raundi ya kwanza inashirikisha timu 28 katika mikondo 14 ya mechi mbili, huku mechi za kwanza zikichezwa Septemba 20 na marudiano Oktoba 6, 2026. Mechi za raundi ya pili zimepangwa kuchezwa Novemba 9 na 17, kabla ya raundi ya tatu na ya mwisho kufanyika Machi 2027. Mshindi wa jumla katika kila mchujo saba ya raundi ya tatu atafuzu kwa fainali za U23 AFCON nchini Misri pamoja na wenyeji ambao wamepata tiketi moja kwa moja. Mashindano hayo yana umuhimu wa ziada kwa sababu yatatumika kama njia ya Afrika kupata wawakilishi katika Mashindano ya Soka ya Olimpiki ya Los Angeles 2028. Timu za Afrika zina historia nzuri katika soka ya wanaume la Olimpiki. Nigeria ilitwaa dhahabu Atlanta mwaka 1996 na kuwa taifa la kwanza la Afrika kushinda medali hiyo, kabla ya Cameroon kutwaa dhahabu Sydney mwaka 2000. Nigeria pia ilishinda fedha Beijing 2008 na shaba Rio 2016, na kuwa taifa la Afrika lililopata mafanikio mengi zaidi katika mashindano hayo. Ghana iliweka historia Barcelona mwaka 1992 kwa kuwa taifa la kwanza la Afrika kushinda medali katika soka la wanaume la Olimpiki baada ya kutwaa shaba. Kikosi cha Mwisho Walinda lango Caleb Kramer (Ado Den Haag, Uholanzi) Mateo Ochieng (Providence College, Uingereza) Collins Omondi (Kariobangi Sharks) Mabeki Ian Onyango (Mathare United) Collins Ochieng (Tusker FC) Francis Okoth (Kenya Police) Baron Ochieng (Unattached) Wycliffe Omondi (Tusker FC) Joseph Bate (Nairobi United) Price Omenda (Murang'a Seal) Viungo wa Kati Omar Ateek (Mathare United) Kevin Wangaya (Nairobi United) Kelly Madada (Afc Leopards) Oliver Machaka (Kenya Police) Andreas Odhiambo (Enkopings SK, Uswidi) Jack Onganya (Cadiz, Uhispania) Irad Mshindi (Leipja, Latvia) Washambuliaji Dancan Oluoch (Nairobi United) Lawrence Okoth (Bandari FC) Syphas Owuor (Nairobi United) Collins Okello Jeremy Bisau (Sd Huesca, Uhispania) Telena Ochieng (Tusker FC) Brooklyn Kazungu (MK Dons, Uingereza) Paul Osama (Enkopings SK, Uswidi) Henry Omollo (Mufurila Wanderers, Zambia) Hassan Beja (Red Castleue SC, UAE)

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 27 Sep 2026 07:55:59

Ziara ya Ruto Nyanza yaacha makovu ODM 

ZIARA ya siku tano ya Rais William Ruto Luo Nyanza wiki iliyopita iliacha makovu ya uhasama na mgawanyiko wa kisiasa kati ya baadhi ya viongozi wa eneo hilo hasa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2027 zinavyoendelea kunoga. Rais Ruto alifanya ziara ambayo ilionekana ilifana katika kaunti za Kisumu, Siaya, Migori na Homa Bay ambako alipigia debe azma yake ya kuwahi muhula wa pili. Hata hivyo, baada tu kuondoka, ziara hiyo imezua uhasama kati ya viongozi wa ODM ambao wanalumbana kuhusu siasa za eneo hilo.  Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo Mabono alimchemkia Gavana Glady Wanga akidai ndiye alihusika na masaibu yake mbele ya Rais. Bi Odhiambo wiki hii alimfokea Gavana Wanga akidai alihusika na kuzomewa kwake katika mkutano ambao viongozi wa Luo Nyanza walikutana na Rais Ruto katika ikulu ndogo ya Kisumu. "Gladys Wanga nakuheshimu kama dadangu mdogo na mwenyekiti wa ODM lakini usichukulie hilo kama jambo la kawaida. Unawatuma watu waje wanidharau na kunishambulia katika eneobunge langu kisha unaketi kitako na kujifanya mzuri," akasema Bi Odhiambo. Mbunge huyo alitishia kuwa huenda akaendesha kampeni kali dhidi ya Bi Wanga iwapo ataendelea kuvamiwa kwenye mikutano anayoandaa sehemu mbalimbali ya Nyanza.  "Nitakukabili, na pia nitawaambia watu hawa wasikupigie kura. Najua unajishasha kwa sababu Rais aliwaambia watu hawa wakupigie kura lakini Rais huwa hapigi kura hapa, "Mimi sijui vita vyovyote vya kujificha na ukiendelea nitaendeleza vita vikali dhidi yako," akaongeza Odhiambo. Mbunge huyo na Bi Wanga wamekuwa na uhusiano vuguvugu hasa kuhusu uongozi wa kaunti na siasa za kitaifa. Bi Odhiambo ni kati ya wabunge Luo Nyanza ambao wamekuwa vuguvugu akionekana kutounga mkono mrengo wa ODM unaoongozwa na Dkt Oburu Oginga au vuguvugu la Linda Mwananchi chini ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Katika mkutano wa Ikulu ndogo ya Kisumu, Bi Odhiambo alikuwa na wakati mgumu kuhutubu huku akipigiwa kelele na umati.  "Alituma watu Kisumu wanizomee, akatuma watu pia katika eneobunge langu wanipigie kelele. Sitaendelea kumvumilia," akasema. Juhudi za kumtaka Gavana Wanga azungumzie madai hayo hazikufaulu ila gavana huyo amekuwa akionekana kuhepa kujibizana na mbunge huyo anayehudumu muhula wake wa nne. Kinaya ni kwamba majibizano hayo yanapoendelea kama Mwenyekiti wa ODM, Bi Wanga ndiye atatia saini cheti cha chama iwapo Bi Odhiambo atapewa tikiti ya kutetea kiti chake kupitia chungwa. Katika Kaunti ya Homa Bay, kuna ushindani mkali wa kiti cha ugavana mnamo 2027 huku Bi Wanga akikabiliwa na kivumbi dhidi ya aliyekuwa Naibu Gavana Oyugi Magwanga. Wawili hao walikosana mwaka jana, Bw Magwanga akajiuzulu na itakumbukwa mnamo 2022, marehemu Raila Odinga alitekeleza jukumu muhimu la kuwapatanisha. Kupitia kupatanishwa na Bw Odinga, Bi Wanga aliishia kugombea ugavana naye Bw Magwanga akikubali kuwa mgombeaji mwenza wake. Katika kaunti jirani ya Migori, ziara ya Rais Ruto imeacha uhasama mkali kati ya Mbunge wa Uriri Mark Nyamita na Gavana Ochilo Ayacko. Bw Nyamita ambaye anahudumu muhula wa pili kupitia ODM analenga ugavana 2027 kupitia chama hicho. Bw Ayacko naye analenga kutetea kiti chake pia kupitia ODM na wawili hao watakabiliana katika mchujo wa chama. "Kazi ya Bw Ayacko ilikuwa kununua vuvuzela kwa vijana ili wazipulize katika mikutano yake ndipo waone kuwa yeye ni maarufu. Baada ya mkutano wa Kisumu, hakuenda Siaya bali alirudi hapa Migori kuhakikisha kuwa vijana wanapewa malori matatu ya vuvuzela," akasema Bw Nyamita.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 27 Sep 2026 05:55:37

Uchumba wa Rigathi, Sifuna kisiasa utautikisa upinzani

MJADALA kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027 umechukua mkondo mpya baada ya kauli za viongozi wa kisiasa kuashiria uwezekano wa kuibuka kwa muungano wa kisiasa kati ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Huku baadhi ya wadau wakichukulia ushirikiano huo kama silaha ya kumenyana na Rais William Ruto, wengine wanahisi unaweza kuwa chanzo cha migawanyiko mipya ndani ya upinzani. Aliyekuwa Seneta wa kuteuliwa Gloria Orwoba ni mmoja wa waliozua mjadala huo baada ya kusema Wakenya wasipuuzilie mbali uwezekano wa Gachagua na Sifuna kujitokeza pamoja kwenye tiketi ya urais mwaka 2027. Kwa mujibu wa Orwoba, Sifuna si mwanasiasa wa kawaida bali ni kiongozi anayeweza kuwa mgombea mkuu wa kiti hicho. Kauli hiyo imeongeza uzito kwa mjadala unaoendelea kuhusu nafasi ya Sifuna katika siasa za kitaifa huku uchaguzi ukikaribia. Nyota ya Sifuna anayehusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi imekuwa iking'aa na kujijenga kama nguvu mpya ya kisiasa kuelekea 2027. Hata hivyo, changamoto kubwa imekuwa ni chombo cha kisiasa atakachotumia kwa azma yake. Orwoba anadai kuwa Sifuna tayari ana chama lakini anatafuta namna ya kukipa sura mpya ili kivutie wafuasi wengi zaidi. Ndani ya vuguvugu la Linda Mwananchi, mjadala kuhusu chama bado unaendelea. Lakini licha ya mjadala kuhusu vyama, Orwoba anaamini chama hakitakuwa kigezo kikuu kwa wapigakura. Kwa mtazamo wake, Wakenya wataangalia zaidi mgombea kuliko nembo ya chama. Kauli hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu uwezekano wa kuundwa kwa tiketi ya Gachagua na Sifuna. Kwa mara ya kwanza, viongozi wa upinzani wameanza kuzungumzia waziwazi uwezekano wa wawili hao kushirikiana katika kinyang'anyiro cha urais. Kinachofanya mjadala huo kuwa wa kipekee ni kwamba Gachagua mwenyewe amewahi kusema hadharani kwamba yuko tayari kuwa mgombea mwenza wa Sifuna iwapo viongozi wa upinzani wataafikiana kuwa seneta huyo ndiye anayefaa kuongoza muungano huo. Aidha, amesema pia kwamba mpangilio wa kinyume unaweza kutokea ambapo yeye akiongoza tiketi na Sifuna kuwa mgombea mwenza. Kauli hizo zimezua hisia mseto ndani ya upinzani. Wapo wanaoamini kuwa ushirikiano kati ya mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika Mlima Kenya na kiongozi anayevutia vijana na wakazi wa mijini unaweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za taifa. Hata hivyo, wengine wanatahadharisha kuwa hatua hiyo inaweza kuibua malumbano mapya kuhusu nani anafaa kupeperusha bendera ya upinzani. Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ni mmoja wa watetezi wakuu wa muungano huo. Malala anaamini kwamba kuunganisha nguvu za Gachagua na Sifuna kutaunda kambi imara yenye uwezo wa kumpa Rais Ruto ushindani mkubwa. Kwa mujibu wa Malala, hesabu za kisiasa zinaonyesha kwamba kuunganisha Mlima Kenya, Magharibi na jamii za Maa kunaweza kuunda msingi mkubwa wa kura. Ndiyo sababu ametangaza mpango wa kuanzisha vuguvugu la "Triple M" linalolenga kuleta pamoja watu wa Mrima, Mulembe na Maa. Malala amekuwa akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Mlima Kenya na Magharibi mwa Kenya unaweza kuamua matokeo ya uchaguzi mkuu ujao. Hata hivyo, siasa za upinzani bado zinaonekana kuwa katika hatua ya mazungumzo. Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kimeweka wazi kwamba kwa sasa hakitajiunga na Muungano wa Ukombozi (TUA). Badala yake, kina nia ya kushirikiana kwanza na vuguvugu la Linda Mwananchi kabla ya kuingia katika mazungumzo ya kuunda muungano mpana wa upinzani.  Msimamo huo unaonyesha kuwa bado kuna tofauti za kimkakati kati ya vikundi mbalimbali vinavyolenga kumng'oa Rais Ruto mamlakani mwaka 2027. Wakati Kalonzo Musyoka na washirika wake wakisisitiza umuhimu wa muungano mmoja wa upinzani, makundi mengine yanaonekana kutaka kujijenga kwanza kabla ya kuamua namna ya kushirikiana. Kwa sasa, tiketi ya Gachagua na Sifuna bado ni wazo linalojadiliwa kisiasa na si makubaliano rasmi. Hata hivyo, kauli za Orwoba, Malala na Gachagua mwenyewe zimeifanya kuwa mojawapo ya mada zinazovutia zaidi katika siasa za 2027.  Iwapo "ndoa" hiyo ya kisiasa itafungwa rasmi, inaweza kuimarisha upinzani au kuibua mvutano mpya ikizingatiwa kuwa Gachagua ni mmoja waliosuka muungano wa upinzani unaohusisha Kalonzo, Martha Karua, Eugene Wamalwa, Fred Matiang'i, Justin Muturi miongoni mwa wengine ambao awali walionekana kuungana dhidi ya Rais Ruto. Lakini jambo moja liko wazi: mjadala kuhusu Gachagua na Sifuna umeanza kuvuruga hesabu za upinzani na kufungua sura mpya ya siasa za uchaguzi

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 27 Sep 2026 04:55:12

Aliyebuni Azimio La Umoja asikitika Raila anasahaulika haraka

MFANYABIASHARA Ronny Raburu, anayesema ndiye aliyependekeza jina Azimio la Umoja kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga mwaka 2021, amesema amesikitishwa na uamuzi wa viongozi wa upinzani kuacha kutumia jina hilo na kulibadilisha kuwa Ukombozi Alliance. Raburu, Mkenya ambaye amekuwa akiishi Tanzania kwa takriban miaka 25, anasema jina la Azimio halikuwa tu kauli ya kisiasa bali lilikuwa na msingi wa kihistoria na kiitikadi uliotokana na Azimio la Arusha la mwaka 1967 lililoasisiwa na rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere. Akizungumza kuhusu mabadiliko hayo, Raburu alisema anahisi urithi wa kisiasa wa Raila Odinga unasahaulika kwa haraka mno. "Nimevunjika moyo. Baba alikuwa akifanya siasa zenye misingi na falsafa maalum. Kila jambo alilofanya lilikuwa na maana yake. Inanishangaza kuona urithi wake ukiondolewa haraka hivi," alisema. Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ulitangaza wiki hii kuwa umeamua kubadili jina kuitwa Ukombozi Alliance kama sehemu ya kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Raburu alieleza kwamba wazo la Azimio lilizaliwa baada ya mahakama kubatilisha mpango wa Maridhiano ya Kitaifa (BBI) uliokuwa ukisukumwa na Raila Odinga na Rais( sasa mstaafu) Uhuru Kenyatta kufuatia maridhiano yao ya mwaka 2018. Kwa mujibu wake, Raila alimtafuta akihitaji jina la Kiswahili ambalo lingeendeleza roho ya BBI ya kuunganisha taifa lakini kwa lugha ambayo wananchi wengi wangetambua na kuielewa. "Alinipigia simu na kuniambia BBI imekwama na angependa jina la Kiswahili ambalo lingeendeleza lengo la umoja wa kitaifa. Alinitaka kushauriana na marafiki zangu Tanzania ili tupate jina mwafaka," alisema. Raburu anasema alifanya mazungumzo na marafiki, wazee na watu waliokuwa na uelewa mkubwa wa historia ya Tanzania kabla ya kuwasilisha mapendekezo kadhaa kwa Raila. Miongoni mwa majina aliyopendekeza ni Azimio la Umoja, ambalo lilivutiwa na Azimio la Arusha lililotumika kama nguzo ya siasa za ujamaa na ujenzi wa taifa nchini Tanzania. "Nilihisi kwamba kwa kuwa BBI ilikuwa imeanguka, kulikuwa na haja ya kupata jina ambalo lingeendelea kuakisi wazo la kujenga madaraja ya umoja," alisema. Siku chache baadaye, alishuhudia Raila akilizindua jina hilo hadharani mjini Nakuru. Baadaye lilikuwa msingi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya uliowaleta pamoja ODM, Jubilee, Wiper, Kanu na vyama vingine katika kampeni za urais za mwaka 2022. Hata hivyo, baada ya upinzani kuamua kujiita Ukombozi Alliance, Raburu anaamini siasa zimeondoka kwenye misingi ya itikadi na kuelekea katika misemo ya muda mfupi ya kisiasa. "Haya sasa ni maneno ya kampeni tu. Inaonekana watu wanatafuta jina litakalofaa wakati huo na kusaidia kushinda uchaguzi. Sioni falsafa iliyo nyuma yake," alisema. Raburu, ambaye anatoka Kaunti ya Kisumu lakini ameishi Tanzania kwa muda mrefu, anasema urafiki wake na Raila ulijengwa kutokana na mapenzi yao ya pamoja kwa historia ya ukombozi wa Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika harakati hizo. Anamkumbuka Raila kama mwanasiasa aliyependa sana historia ya Tanzania, urithi wa Nyerere na mchango wa nchi hiyo katika kupigania uhuru wa mataifa mbalimbali ya Afrika. Kifo cha Raila, anasema, kilimuumiza sana kiasi kwamba hadi leo hajafuta nambari yake ya simu. "Mara nyingi narejelea jumbe tulizowasiliana. Wakati mwingine ninapoona siasa za sasa na watu wakidai Baba aliwaambia jambo fulani, natamani kuchapisha baadhi ya jumbe zake kuthibitisha ukweli, lakini naambiwa ni mawasiliano ya kibinafsi," alisema. Kwa mujibu wa Raburu, si Azimio pekee linalopaswa kukumbukwa, bali pia mchango wa Raila katika siasa za Kenya. "Tunamsahau haraka sana. Hilo ndilo linaloniumiza zaidi," alisema. Aidha, alisisitiza kuwa Kenya inapaswa kuendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania kwa kuwa nchi hizo mbili zimekuwa washirika wa karibu katika biashara, utalii na diplomasia kwa miaka mingi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 27 Sep 2026 03:55:14

Serikali inavyolipa mabilioni kutokana na blanda za maafisa wake

WALIPA ushuru nchini wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa kifedha kutokana na maamuzi ya serikali ambayo baadaye yanabainika kuwa yalikiuka sheria, yalitekelezwa vibaya au yalikiuka haki za raia. Uchunguzi wa kesi mbalimbali mahakamani unaonyesha kuwa serikali, kaunti, polisi na mashirika ya umma yameamriwa kulipa mabilioni ya pesa kama fidia, marupurupu, mishahara iliyocheleweshwa na mikataba iliyovunjwa. Kesi hizo zinahusu kukamatwa kwa watu kinyume cha sheria, mateso, mauaji ya kiholela, kufutwa kazi visivyo halali, migogoro ya ardhi, zabuni za umma na mikataba iliyokiukwa. Moja ya kesi zilizotikisa serikali ni ile ya kiongozi wa kampeni ya Nigeria, Nnamdi Kanu. Mahakama Kuu iliamua mwaka 2025 kuwa Kanu alitekwa nyara, kuwekwa kizuizini kwa siri na kuteswa kabla ya kupelekwa Nigeria. Serikali iliamriwa kumlipa Sh10 milioni kama fidia pamoja na gharama ya kesi. Katika kesi nyingine, Mahakama Kuu iliagiza polisi na Mwanasheria Mkuu kulipa Sh35.4 milioni kwa familia na waathiriwa 28 wa operesheni za polisi wakati wa maandamano ya Azimio mwaka 2023 katika maeneo ya Kisumu, Migori na Ahero. Mahakama ilibaini kuwa baadhi yao waliuawa, kujeruhiwa au kuteswa kinyume cha sheria. Mwanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha JKUAT, Allan Omondi, pia alitunukiwa Sh8 milioni baada ya mahakama kubaini kuwa polisi walimpiga na kumweka kizuizini kinyume cha sheria wakati wa machafuko ya wanafunzi mwaka 2019. Wiki hii, mtaalamu wa teknolojia ya habari Ndiang'ui Kinyagia alishinda fidia ya Sh5 milioni baada ya mahakama kuamua kuwa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai walivamia nyumba yake huko Kinoo bila kibali cha mahakama na kutwaa mali yake kinyume cha sheria. Mbali na amri za mahakama, serikali imeanza kutekeleza mpango wa kufidia waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa maandamano yaliyofanyika kati ya 2013 na 2025. Serikali tayari imetenga Sh2 bilioni kwa mpango huo ambao unahusisha fidia kwa waliouawa, waliojeruhiwa na wale waliokumbwa na ukiukaji wa haki zao. Seneti pia inapambana mahakamani kupinga agizo la kulipa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Sh50 milioni baada ya mahakama kubaini kuwa baadhi ya haki zake za kikatiba zilikiukwa wakati wa mchakato wa kumbandua madarakani. Kesi nyingine kubwa zinahusisha ukiukaji wa haki za binadamu uliotokea katika miaka ya nyuma. Michael Rubia alitunukiwa Sh17 milioni baada ya kubainika kuwa alizuiliwa kinyume cha sheria na kuteswa katika utawala wa zamani. Serikali pia ililazimika kugharamia matibabu yake nchini Uingereza. Mahakama ya Juu pia iliidhinisha malipo ya Sh2.5 milioni kwa kila mmoja wa wafungwa sita wa kisiasa waliokamatwa mwaka 1992 wakati wa maandamano Freedom Corner. Ilibainika serikali ilikiuka haki zao kwa kuwa walikamatwa na kuteswa. Katika kesi ya maafisa wa zamani wa Jeshi la Anga walioathiriwa baada ya jaribio la mapinduzi la mwaka 1982, Mahakama ya Rufaa iliidhinisha malipo ya jumla ya Sh6.25 bilioni kwa maafisa 284 walioteswa, kufungwa na kufutwa kazi kwa njia isiyofaa. Serikali pia imebeba gharama kutokana na mauaji yanayohusishwa na polisi. Familia ya mwandishi wa habari wa Pakistan, Arshad Sharif, ilitunukiwa Sh10 milioni baada ya mahakama kuamua kuwa alipigwa risasi visivyo halali katika eneo la Kajiado mwaka 2022. Katika sekta ya ardhi, Mahakama ya Mazingira na Ardhi ilitunuku Johannes Akello Omboto Sh5 milioni baada ya ukuta wa mali yake kubomolewa na maafisa waliokuwa wakitekeleza shughuli za Shirika la Reli Kenya bila kufuata taratibu. Mashirika ya umma pia yamejikuta yakilipa mamilioni kutokana na kuvunja mikataba. Hazina ya Taifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) iliamriwa kulipa zaidi ya Sh112 milioni kwa kampuni ya Micro-City Computers baada ya kujiondoa katika mkataba wa mfumo wa CCTV ikitaja ukosefu wa fedha. Aidha, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) kiliamriwa kulipa Sh39.9 milioni kwa mkandarasi baada ya kufuta zabuni ya mradi wa Sh799 milioni bila uwazi wa kutosha. Kesi hizi zinaonyesha jinsi maamuzi ya serikali yanavyoweza kuwa na gharama kubwa kwa walipa ushuru. Japo maafisa wanaohusika mara nyingi hawaathiriki binafsi, mzigo wa kulipa fidia na madeni hayo huishia kwa wananchi kupitia fedha za umma.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 27 Sep 2026 02:55:21

Vita vyazidi mrengo wa upinzani vinara waking'ang'ania vyama

UCHAGUZI Mkuu wa mwaka 2027 unapokaribia, ushindani wa kumng'oa Rais William Ruto unaonekana kugeuka kuwa vita vya ndani ya upinzani huku vinara wakuu wakisaka vyama vya kisiasa na majukwaa yatakayowawezesha kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania urais. Ingawa viongozi wa upinzani wanakubaliana kwamba serikali ya sasa inapaswa kubadilishwa kupitia kura, bado hawajakubaliana kuhusu nani anayefaa kupeperusha bendera ya muungano wao katika kinyang'anyiro hicho. Miongoni mwa wanaotajwa kuwania uongozi wa upinzani ni aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua wa People's Liberation Party, Fred Matiang'i wa Jubilee, Eugene Wamalwa wa DAP-Kenya, Justin Muturi wa Democratic Party, Peter Munya wa PNU na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Kinachoibuka sasa ni ushindani wa kisiasa unaoonyesha kila mmoja wa viongozi hao akitaka kuwa na chama au jukwaa lake kabla ya mazungumzo ya kuunda muungano wa mwisho kufanyika. Huku Kalonzo akijaribu kuimarisha muungano wa Ukombozi Alliance, Sifuna kupitia vuguvugu la Linda Mwananchi anatafuta chombo chake cha kisiasa. Naye Gachagua anaendelea kujenga chama chake cha Democracy for Citizens Party (DCP) huku akiacha mlango wazi kwa mazungumzo na makundi mengine ya upinzani. Katibu Mkuu wa DCP Cleophas Malala amesema wazi kuwa chama hicho hakiko tayari kujiunga na Ukombozi Alliance kwa sasa. Badala yake, amependekeza DCP ishirikiane kwanza na Sifuna kabla ya kuanza mazungumzo na vyama vingine vya upinzani. Kauli hiyo imeonyesha kiwango cha kutoaminiana miongoni mwa viongozi wa upinzani, ambapo wengi wao wanaonekana kutaka kuhifadhi vyama vyao ili kuongeza uzito wao katika mazungumzo yatakayofuata. Wakati huo huo, Martha Karua na Fred Matiang'i wameendelea kusisitiza kwamba mgombea wa urais wa upinzani hafai kuteuliwa kupitia makubaliano ya viongozi wachache. Badala yake, wanataka kuwepo kwa mchakato ulio wazi, wa haki na unaokubalika kwa washirika wote. Kwa upande wake, Kalonzo ameonekana kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha muundo wa upinzani. Baada ya kugeuza Azimio kuwa Ukombozi Alliance, amekuwa akifanya mikutano ya kisiasa katika maeneo yaliyokuwa ngome za aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Wikiendi hii Kalonzo, Muturi na Wamalwa wamekuwa wakifanya kampeni za pamoja Busia na Siaya. Lakini huku Kalonzo akiimarisha Ukombozi Alliance, kambi ya Sifuna imekuwa ikisaka njia yake ya kisiasa. Hata mvutano uliojitokeza kuhusu matumizi ya jina "Ukombozi" umeonyesha tofauti zinazozidi kujitokeza kati ya makundi hayo mawili. Washirika wa Sifuna sasa wanatazamia kutumia chama cha United Democratic Party (UDP), kilichowahi kuhusishwa na mwanasiasa marehemu Cyrus Jirongo, kama chombo chake cha kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027. Katika mazingira hayo, nafasi ya Gachagua imeendelea kuwa muhimu. Kiongozi huyo amekuwa akisisitiza kuwa yuko tayari kumuunga mkono mwanasiasa yeyote atakayeonyesha uwezo mkubwa wa kumshinda Rais Ruto, hata kama si yeye mwenyewe. Kauli hiyo imebadili kwa kiasi kikubwa mjadala wa kisiasa ndani ya upinzani. Badala ya kusisitiza kuwa lazima aongoze muungano huo, Gachagua amesema mgombea anapaswa kuamuliwa kwa kuzingatia nguvu za kisiasa na uungwaji mkono wa kitaifa. Hata hivyo, msimamo huo haujaondoa ushindani uliopo. Malala ameendelea kusukuma wazo la ushirikiano kati ya Mlima Kenya na eneo la Mulembe, akisema maeneo hayo yana kura za kutosha kuathiri matokeo ya uchaguzi wa urais. Baadhi ya viongozi kutoka Magharibi mwa Kenya, akiwemo Mbunge wa Bumula Jack Wamboka, wamependekeza Sifuna awe mgombea wa urais huku mgombea mwenza akitoka Mlima Kenya. Hata hivyo, pendekezo hilo linapingana na msimamo wa wafuasi wa Kalonzo ambao wanataka kiongozi huyo wa Wiper apewe tiketi ya urais huku Sifuna akichukua nafasi ya mgombea mwenza. Aidha, aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta amewahimiza wanachama wa Jubilee kuanza maandalizi ya uchaguzi wa 2027 mapema na kushirikiana na viongozi vijana ili kuunda muungano mpana wa kisiasa. Wachambuzi wa siasa wanasema changamoto kubwa inayokabili upinzani si kuwakutanisha viongozi wake, bali ni kupata utaratibu wa haki wa kumteua mgombea mmoja anayekubalika kwa wote. Wanasema historia ya siasa za Kenya imeonyesha mara nyingi kuwa miungano mingi huvunjika kutokana na mizozo kuhusu mgombea wa urais, mgombea mwenza na ugavi wa mamlaka. Kwa sasa, upinzani unaonekana kuunganishwa na lengo moja la kumng'oa Rais Ruto. Hata hivyo, ushindani wa ndani kuhusu vyama, miungano na nafasi za uongozi unaendelea kutishia umoja huo huku saa ya uchaguzi wa 2027 ikiendelea kuyoyoma.

read more