taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 16 Aug 2026 04:55:31
Ripoti yaonyesha KTDA ilikopa kuwafurahisha wakulima na bonasi
KWA miaka mingi, bonasi ya chai imekuwa ikichukuliwa na wakulima wadogo kama kipimo cha mafanikio yao shambani. Malipo makubwa ya mwisho wa mwaka yamekuwa yakitafsiriwa kuwa ushahidi wa uzalishaji mzuri, bei nzuri za chai na usimamizi bora wa viwanda. Hata hivyo, ukaguzi uliofanywa na Bodi ya Chai Kenya umefichua ukweli tofauti. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika baadhi ya viwanda, sehemu ya bonasi iliyolipwa wakulima haikutokana na mapato ya mauzo ya chai bali ilitokana na mikopo kutoka benki za kibiashara. Kwa maneno mengine, baadhi ya wakulima walilipwa kile kilichoonekana kuwa bonasi ilhali fedha hizo zilikuwa mikopo ambayo baadaye ilibaki kama deni la kiwanda. Madeni hayo sasa yanapaswa kulipwa kutoka kwa mapato ya baadaye ya wakulima hao hao. Ripoti ya Machi 2026 iliyoandaliwa baada ya agizo la Wizara ya Kilimo inaonyesha kuwa kufikia Desemba 31, 2025, viwanda 69 vya chai vilikuwa na madeni ya jumla ya Sh34.05 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh30.36 bilioni zilikuwa mikopo iliyochukuliwa kwa jina la kufadhili shughuli za chai na bonasi za wakulima. Sekta ya chai ni muhimu sana nchini Kenya. Viwanda 71 vya wakulima wadogo vinamilikiwa na zaidi ya wakulima 650,000 na huzalisha zaidi ya nusu ya chai yote nchini. Mwaka 2025, sekta hiyo ilileta zaidi ya Sh215 bilioni. Lakini sasa baadhi ya viwanda vinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni. Ripoti ya ukaguzi imeonya kuwa uwezo wa baadhi ya viwanda kuendelea kufanya kazi uko mashakani kutokana na kiwango kikubwa cha madeni. Kiwanda cha Kapkoros kiliongoza kwa kuwa na deni la Sh2.77 bilioni, kikifuatiwa na Litein na deni la Sh1.88 bilioni, Mogogosiek Sh1.60 bilioni na Kapset Sh1.48 bilioni. Wakaguzi walibaini kuwa katika kipindi cha miezi sita hadi Desemba 2025, kampuni ya KTDA Management Services iliratibu mikopo ya mabilioni ya fedha kupitia benki mbalimbali kwa viwanda 55 ili kufadhili malipo ya pili ya wakulima. Jumla ya Sh30.47 bilioni zilichukuliwa kutoka benki mbalimbali. Hata hivyo, mahitaji halisi ya viwanda kwa ajili ya bonasi na malipo mengine yalikuwa Sh25.29 bilioni pekee. Hivyo, wakaguzi hawakuweza kueleza sababu ya kukopa Sh5 bilioni zaidi. Ripoti hiyo pia imeibua maswali kuhusu jinsi fedha hizo zilivyotumiwa. Imebainika kwamba sehemu ya mikopo iliyochukuliwa kwa jina la bonasi ilitumika pia kulipa madeni ya zamani gharama za uendeshaji wa viwanda na mikopo mingine iliyokuwepo awali. Matokeo yake ni kwamba baadhi ya wakulima waliamini walikuwa wanapokea faida kutokana na mauzo ya chai ilhali fedha walizopokea zilikuwa sehemu ya mikopo. Ukaguzi huo pia umebaini udhaifu mkubwa katika usimamizi wa mikopo. Katika baadhi ya viwanda, bodi za wakurugenzi ziliidhinisha mikopo bila kutaja kiwango kinachopaswa kukopwa. Katika visa vingine, viwanda vilikopa zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa. Tatizo jingine lilihusisha tathmini ya thamani ya chai iliyokuwa bado haijauzwa. Wakaguzi waligundua kuwa baadhi ya viwanda viliongeza thamani ya chai hiyo kwa kiwango kikubwa kuliko bei halisi ya soko. Hatua hiyo iliviwezesha kukopa fedha nyingi zaidi na kutangaza bonasi kubwa kuliko uwezo wao wa kifedha. Bodi ya Chai sasa inapendekeza kuwa malipo ya bonasi yajayo yawe yanategemea mapato halisi na fedha zilizopo, badala ya mikopo na makadirio yaliyopandishwa ya thamani ya chai. Kwa wakulima, funzo kuu kutoka kwa ripoti hiyo ni kwamba bonasi kubwa si lazima iwe ishara ya mwaka mzuri wa biashara. Wakati mwingine inaweza kuwa fedha za mkopo ambazo baadaye hulipwa kupitia mapato yao ya siku zijazo.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
Ruto asuta upinzani akidai ni wabinafsi
RAIS William Ruto amewashambulia viongozi wa upinzani akiwalaumu kwa kujali maslahi yao binafsi badala ya masuala yanayowahusu Wakenya. Akiwa katika ziara ya maendeleo kaunti za Busia na Bungoma jana, Rais alisema wapinzani wamekuwa wakitumia muda mwingi kuzozana kuhusu nani atawania urais mwaka 2027 badala ya kuandaa mipango ya maendeleo. Alisema serikali yake inaendelea kutekeleza miradi huku wapinzani wakihangaika na siasa za urithi. "Hawa wamekaa zaidi ya mwaka mmoja wakibishana kuhusu mgombea wao wa urais. Ikiwa hawawezi kukubaliana kuhusu mtu mmoja, watafikiriaje ajenda ya Wakenya wa kawaida?" akauliza. Ruto alitetea rekodi ya serikali yake akisema imewekeza katika barabara, masoko, elimu na afya. Alisema Sh21 bilioni zimetengwa kujenga kilomita 210 za barabara na Sh75 milioni kwa soko la kisasa la Misikhu. Alisema serikali imefufua kiwanda cha sukari cha Nzoia na kwamba atatembelea Mumias Jumatatu kutoa bonasi kwa wakulima wa miwa. Katika elimu, alisema serikali imeajiri walimu zaidi ya 100,000 na itawapa walioajiriwa na bodi za shule kazi za kudumu. Pia alisema asilimia 55 ya wakazi wa Bungoma wamejiandikisha katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Rais alizindua ujenzi wa barabara ya Butula-Amukura yenye urefu wa kilomita 55. Pia alizindua soko la kisasa la Bumala lililogharimu Sh230 milioni na linalotarajiwa kuwahudumia wafanyabiashara zaidi ya 300. Alisema serikali itaunganisha familia 16,000 Busia na umeme kwa gharama ya Sh2 bilioni. Akihutubia wakazi wa Misikhu, Ruto aliwaomba kumuunga mkono kwa muhula wa pili akisema miradi yake inapaswa kuendelea. Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge Moses Wetang'ula pia waliwataka wakazi kumuunga mkono Ruto, wakisema ametekeleza ahadi zake kwa eneo hilo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
Mawaziri, maafisa wa ikulu kujiuzulu ili kuwania viti 2027
TAMAA ya kuwania nyadhifa za kisiasa imeanza kutikisa serikali ya Rais William Ruto, huku mawaziri, makatibu wa wizara na maafisa wakuu wa Ikulu wakijiandaa kujiuzulu ili kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 2027. Miongoni mwa wanaotajwa ni Mdhibiti wa Ikulu Katoo Ole Metito, msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed na Mawaziri Lee Kinyanjui na Geoffrey Ruku. Wengine ni mawaziri Alice Wahome na Alfred Mutua pamoja na mshauri wa Rais Charles Keter. Makataa ya kisheria ya Februari 10, 2027, yanakaribia na huenda yakasababisha mabadiliko makubwa katika serikali, ikiwa maafisa hao wataamua kuondoka ili kujipigia debe kwa wapigakura. Metito anamezea mate kiti cha ugavana Kajiado, ambako anatarajiwa kukabiliana na Gavana Joseph Ole Lenku, ambaye anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho. Utafiti wa TIFA uliochapishwa Novemba 24 ulimweka Metito mbele kwa asilimia 59 dhidi ya Kanar Seki Lenku aliyepata asilimia 21. Hata hivyo, matokeo hayo ni picha ya awali ya umaarufu wa wagombeaji. Metito, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Kajiado Kusini na Waziri wa Usalama wa Ndani, alishindwa na Lenku katika uchaguzi wa 2022 kwa kura 111,725 dhidi ya 117,600. Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed naye analenga ubunge Kamukunji. Chanzo kilicho karibu na Ikulu kimesema azma yake tayari imekubaliwa na Rais Ruto. Mohamed amekuwa akishiriki shughuli za kijamii katika eneo hilo na amepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Kamukunji waliokutana na Rais Ikulu. Alizaliwa Moi Airbase, Eastleigh, na ana mizizi katika eneo hilo. Hata hivyo, atakabiliana na Mbunge wa sasa Yusuf Hassan, ambaye amewakilisha eneo hilo tangu 2011. Hassan amejiunga na chama cha DCP cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na anatarajiwa kutetea kiti chake kupitia chama hicho. Aliambia NTV atajiuzulu Katika Baraza la Mawaziri, Waziri wa Biashara na Viwanda Lee Kinyanjui ameweka wazi mipango yake. Mnamo Novemba 26 aliambia NTV kuwa atajiuzulu kabla ya Februari ili kuwania ugavana Nakuru. Kinyanjui anasema anataka kukamilisha miradi aliyoanzisha alipokuwa gavana kati ya 2017 na 2022. Atakabiliana na Gavana Susan Kihika pamoja na wagombea wengine akiwemo aliyekuwa gavana Kinuthia Mbugua, Seneta Tabitha Karanja na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti Joel Kairu. Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku naye amezindua azma ya kuwania ugavana Nairobi kupitia UDA. Hatua yake imezua ushindani wa mapema na Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri, ambaye pia anataka tiketi ya chama hicho baada ya Gavana Johnson Sakaja kuhamia ODM. Maafisa wengine wanaotajwa kuwa na mipango ya kuingia siasa ni Waziri wa Ardhi Alice Wahome, anayehusishwa na ugavana Murang'a, na Waziri wa Kazi Alfred Mutua, anayetajwa kutaka kiti cha Seneti Machakos. Mshauri wa Rais kuhusu Masuala ya Eneo la Maziwa Makuu Charles Keter anataka ugavana Kericho. Aliyekuwa Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi, ambaye sasa ni mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), pia ametangaza kurejea siasani kuwania kiti hicho. Katibu wa Wizara ya Usafiri wa Anga Triza Mbaika amethibitisha kuwa atawania ubunge wa Kaiti, Kaunti ya Makueni. Aliyekuwa Gavana wa Turkana Josephat Nanok anasemekana kufikiria kuwania useneta, huku mipango ya Waziri wa ICT William Kabogo kuhusu ugavana Kiambu ikiwa haijabainika. Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema makataa hayo yatamlazimu Rais kusawazisha uaminifu wa kisiasa, uwakilishi wa maeneo na mwendelezo wa shughuli za serikali anapoteua viongozi wapya. Kwa upande wake, wakili Chris Omore anasema sheria inalenga kuhakikisha maafisa wa serikali hawatumii mamlaka yao kuathiri ushindani wa uchaguzi kwa kuwataka wajiuzulu miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu. Kwa wanaotaka kuwania, Februari itakuwa wakati wa kufanya uamuzi mgumu: kujiuzulu na kukabiliana na hatari ya kukosa tiketi za vyama, au kubaki serikalini na kuahirisha ndoto zao za kisiasa za 2027.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
Kinachofanya wanawake kuvutiwa na wanaume wanaowakwaza
WAPO vipusa wanaovutiwa zaidi na wanaume wanaowapa wakati mgumu, huku wanaume wenye upendo, heshima na msimamo wakiachwa pembeni. Lakini je, ni kweli mwanamke humkataa mwanaume mwema na baadaye kujuta? Katika ulimwengu wa mapenzi, kuna swali ambalo limezua mijadala mingi: Je, vidosho wanapendelea wanaume wanaowatesa kihisia kuliko wale wanaowapa upendo wa kweli, heshima na usalama? Hoja inayozua mjadala ni kwamba baadhi ya mademu huvutiwa zaidi na wanaume wanaowafanya wajitahidi kupata mapenzi yao, huku wakikosa kuvutiwa na wanaume wanaoonyesha nia ya dhati tangu mwanzo. Kwa mtazamo huu, mwanaume mwaminifu, mwenye msimamo, anayejali na asiyecheza na hisia za mwanamke anaweza kuonekana kama mtu asiye na msisimko. Kinyume chake, mwanaume ambaye ni mgumu kueleweka, anayepotea bila maelezo na kumfanya mwanamke apiganie nafasi katika maisha yake anaweza kuonekana kuwa na mvuto mkubwa. Wanaounga mkono hoja hii wanasema kuwa baadhi ya watu huchanganya mapenzi yenye afya na kuchoshana, huku wakitafsiri mahusiano yenye migogoro na kutokuwa na uhakika kuwa yenye msisimko. Hoja nyingine ni kwamba baadhi ya vipusa huvutiwa na wanaume wanaotamaniwa na wanawake wengine. Mwanaume aliye kwenye uhusiano mwingine au anayehusishwa na wanawake wengi anaweza kuonekana kuwa na thamani kubwa kutokana na ushindani unaomzunguka. Katika hali hiyo, mwanamke anaweza kujikuta akishindania upendo na uangalizi wa mwanaume ambaye hana nia ya kujitoa kikamilifu katika uhusiano mmoja. Hata hivyo, mvuto wa aina hiyo unaweza kuwa na gharama kubwa kihisia, hasa pale mtu anapoanza kupima thamani yake kwa kiwango cha uangalizi na uthibitisho anaopata kutoka kwa mwenzi wake. Moja ya hoja zinazotolewa ni kwamba baadhi ya watu huingia katika mahusiano wakitafuta hisia walizozoea tangu utotoni, hata kama hazikuwa chanya. Mtu aliyekulia katika mazingira ya kukosa upendo, kutengwa au kutokuwa na uhakika wa kupata uangalizi anaweza, akiwa mtu mzima, kuvutiwa na mwenzi anayempa hisia zinazofanana na alizopitia. Hivyo, mwanaume mwenye upendo thabiti na anayewasiliana vizuri anaweza kuonekana kutokuwa na msisimko kwa mtu aliyezoea mahusiano yenye misukosuko. Wanaume wanaozingatia uaminifu, mawasiliano ya wazi na heshima wanaweza pia kujikuta wakishindana na wale wanaotumia mbinu za kuchezea hisia za wenzi wao. Hata hivyo, si sahihi kuhitimisha kuwa vipusa wote wanapendelea wanaume wasiokuwa waaminifu au kwamba wanaume wote wanaojiita wazuri wanakataliwa kwa sababu ya tabia zao nzuri. Mvuto wa kimapenzi hutegemea mambo mengi, yakiwemo utu, mawasiliano, malengo ya maisha na matarajio ya kila mtu. Swali muhimu ni iwapo mwanamke anayemkataa mwanaume aliyekuwa tayari kumpa upendo wa dhati hujikuta akijuta baadaye. Katika baadhi ya mahusiano, mtu anaweza kutambua thamani ya mwenzi aliyemkataa baada ya kupitia mahusiano yaliyomuumiza au kumkatisha tamaa. Anaweza kukumbuka mwanaume aliyekuwa tayari kumsikiliza, kumheshimu na kujenga naye maisha, lakini ambaye wakati huo hakuvutiwa naye. Hata hivyo, majuto si lazima yawe matokeo ya kila uamuzi wa kumkataa mtu. Mwanamke ana haki ya kukataa uhusiano ambao haumvutii, hata kama mwanaume anayehusika ana sifa nzuri. Vivyo hivyo, kuwa mwema hakumpi mtu haki ya kupendwa au kuchaguliwa kimapenzi. Wanaume wazuri hawajakosa nafasi Hoja hii pia inazua mjadala kuhusu wanaume wanaohisi kwamba uaminifu na tabia njema hazithaminiwi katika ulimwengu wa sasa wa uchumba. Baadhi yao hujiuliza kwa nini wanapata shida kupata wanawake wanaotaka mahusiano ya dhati ilhali wanaume wanaochezea hisia za wengine wanaonekana kuwa na mafanikio zaidi. Hata hivyo, changamoto si kwamba wanaume wazuri wamehukumiwa kubaki waseja. Badala yake, huenda baadhi yao wanakutana na watu ambao hawalingani nao katika matarajio na namna wanavyoelewa mapenzi. Uhusiano wenye afya haujengwi kwa ushindani wa nani atakayemtesa mwenzake zaidi, bali kwa watu wawili wanaochagua kuheshimiana, kuaminiana na kujitolea. Kwa hivyo, swali si tu kama wanawake hujuta kuwakataa wanaume wazuri, bali pia kwa nini baadhi ya watu huvutiwa na mahusiano yanayowapa maumivu badala ya utulivu. Mwanaume mwema hapaswi kubadilika na kuwa mtu anayewachezea wanawake ili apate kupendwa. Vivyo hivyo, mwanamke hapaswi kukubali uhusiano kwa sababu tu mwanaume anamchukulia vizuri. Mapenzi ya kweli yanahitaji mvuto, heshima, uaminifu na juhudi kutoka pande zote mbili. Na pengine, majuto makubwa zaidi si kumkataa mtu mwema, bali kushindwa kutambua mapema aina ya uhusiano ambao mtu anahitaji kujenga.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
SHERIA: Ndoa ya wengi hubadilishwa kwa hiari ya wanandoa kuwa ya mke mmoja
WANANDOA wana uhuru wa kubadilisha aina ya ndoa yao kutoka ile inayoweza kuwa ya wake wengi na kuwa ya mke mmoja, lakini sheria inataka uamuzi huo ufanywe kwa hiari na kwa makubaliano ya wote wawili. Kifungu cha nane kuhusu ubadilishaji wa ndoa kinaeleza kuwa wanandoa wanaweza kutangaza rasmi nia yao ya kubadili ndoa yao na kuifanya iwe ya mke mmoja badala ya ile inayoweza kuwa ya wake wengi. Hata hivyo, sheria inaweka masharti maalumu kwa wanandoa wanaotaka kufanya mabadiliko hayo. Kwanza, kila mmoja lazima akubali kwa hiari bila kulazimishwa na mwenzake. Hii ina maana kuwa mume au mke hawezi kufanya uamuzi huo peke yake bila kupata ridhaa ya mwenzake. Kwa upande wa ndoa ambayo tayari ina wake wengi, sheria inaweka kizuizi zaidi. Ndoa ya aina hiyo haiwezi kubadilishwa kuwa ya mke mmoja ikiwa mume ana zaidi ya mke mmoja wakati wa kutaka kufanya mabadiliko hayo. Hivyo, mume mwenye wake wawili au zaidi hawezi kutumia utaratibu huu kubadilisha ndoa yake kuwa ya mke mmoja. Sharti hilo linaonyesha kuwa sheria inatambua tofauti kati ya ndoa inayoweza kuwa ya wake wengi na ile ambayo tayari ina wake wengi. Ili mabadiliko hayo yatambulike rasmi, wanandoa wanapaswa kutoa tangazo lao mbele ya afisa wa ndoa. Tangazo hilo lazima liandikwe na kutiwa saini na kila mmoja wao kuthibitisha kuwa wamekubaliana kufanya mabadiliko hayo. Hii inamaanisha ni kubadilisha ndoa kuwa ya mke mmoja ni lazima kufanyike kupitia harusi, iwe kanisani au katika afisi ya msajili wa ndoa, yaani ndoa ya kiraia. Afisa wa ndoa anayepokea tangazo hilo anatakiwa kutuma nakala yake kwa Msajili wa Ndoa mara moja ili kuwezesha hatua zinazofuata za usajili. Baada ya kupokea tangazo hilo, msajili atachukua cheti cha awali kilichosajili ndoa hiyo kama inayoweza kuwa ya wake wengi na kutoa cheti kipya kinachoonyesha kuwa sasa ni ndoa ya mke mmoja. Sheria pia inamtaka msajili kurekodi maelezo ya ndoa zilizobadilishwa katika daftari maalumu linalotunzwa kwa madhumuni hayo. Utaratibu huu unahakikisha kuwa mabadiliko ya aina ya ndoa yanafanywa kwa ridhaa ya wanandoa wote na kutambuliwa rasmi na mamlaka husika. Kwa hivyo, wanandoa hawawezi kubadilisha aina ya ndoa yao kwa makubaliano ya mdomo pekee. Lazima wafuate utaratibu uliowekwa, huku kila mmoja akipewa nafasi ya kuamua kwa hiari yake bila kushinikizwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Mke wa Mackenzie alivyosaidia kueneza maovu ya mumewe
SIMULIZI ya mauaji ya Shakahola mara nyingi humwangazia kiongozi wa dhehebu la Good News International, Paul Mackenzie, aliyewashawishi mamia ya wafuasi wake kufunga kula hadi kufa wakiamini wangepata wokovu. Lakini nyuma ya mhubiri huyo aliyekuwa akieneza mafundisho hayo hatari, kulikuwa na mwanamke aliyesaidia kuyadumisha — mkewe, Rhoda Mumbua Maweu. Mwanzoni mwa uchunguzi, Maweu alionekana kama mwanamke aliyenaswa kwenye mkasa huo kwa sababu tu ya ndoa yake na Mackenzie. Mahakama hata ilimwachilia kwa dhamana ya Sh300,000, ikisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha dhidi yake isipokuwa uhusiano wake na mhubiri huyo. Hata hivyo, uchunguzi ulipoendelea na mashahidi kueleza maisha ndani ya kanisa hilo, picha tofauti ilianza kujitokeza. Ushahidi mahakamani ulimuonyesha Maweu kama mtu mwenye ushawishi mkubwa, aliyeshiriki kufundisha na kudhibiti wafuasi. Alihifadhi vitabu na machapisho ya kidini yaliyotumiwa kuimarisha mafundisho ya kanisa hilo. Pia alikuwa akiongoza wanawake na watoto, akiwaelekeza kufuata mafundisho ya mumewe. Mahakama ilimpata na hatia ya kushiriki uhalifu wa kupangwa na kueneza itikadi kali. Ilisema alishiriki shughuli za kundi hilo kwa kuhifadhi machapisho ya kidini na kuwaongoza wanawake na watoto katika masuala ya kiroho. Hata hivyo, mahakama ilisema upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kutosha kumhusisha moja kwa moja na utengenezaji au usambazaji wa CD, DVD na vijitabu vilivyopatikana nyumbani kwa Mackenzie. Ushahidi mwingine uliomhusisha ulitokana na kifo cha Joseph Juma Buyuka akiwa mikononi mwa polisi Watamu. Maweu alidaiwa kumhimiza kuendelea kufunga kula licha ya hali yake ya kiafya kuzorota. Ijumaa iliyopita, mahakama ya Mombasa ilimpata na hatia ya kosa moja la kuua bila kukusudia kuhusiana na kifo cha Buyuka akiwa rumande. Jaji Alex Ithuku alisema Maweu ana hatia katika shtaka hilo. Anakabiliwa na hukumu, huku kosa la kuua bila kukusudia likiwa na adhabu ya juu ya kifungo cha maisha. Maweu alizaliwa mwaka 1998 Kibwezi, Kaunti ya Makueni, katika familia ya wakulima wadogo. Alikuwa mtoto wa pili kati ya wanne. Alisoma Shule ya Upili ya St Joseph's Kibwezi na kupata alama ya B katika mtihani wa KCSE mwaka 2016. Alipata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha JKUAT, lakini familia yake ilikosa karo. Baadaye alihamia Nairobi na kupata kazi ya vibarua kama mhudumu katika hoteli. Huko ndiko alikokutana na Mackenzie. Walifunga ndoa ya kitamaduni mwaka 2019. Wakati huo Mackenzie tayari alikuwa mhubiri na alikuwa na watoto wanne kutoka mahusiano ya awali. Baadaye wawili hao walipata mtoto wa kike. Kwa sasa, mtoto huyo anaishi chini ya uangalizi wa shangazi yake wa upande wa baba Malindi. Safari ya Maweu kutoka kwa mwanafunzi aliyefanya vizuri hadi kuwa miongoni mwa watu waliopatikana na hatia katika mkasa wa Shakahola inaonyesha jinsi alivyohusika katika mojawapo ya visa vikubwa vya itikadi kali za kidini nchini.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Sababu za Ruto kupondwa zaidi kuliko marais waliomtangulia
WAKENYA wanaomkosoa Rais William Ruto huenda wakasahau kuwa marais wanne waliomtangulia pia walikumbwa na tuhuma za ufisadi, mauaji ya kiholela, matumizi mabaya ya mamlaka na upendeleo wa kisiasa. Tangu enzi za Rais wa kwanza Jomo Kenyatta hadi utawala wa Uhuru Kenyatta, masuala hayo yamekuwa sehemu ya historia ya uongozi wa Kenya. Wakati wa utawala wa Jomo Kenyatta, suala la ardhi lilikuwa mojawapo ya changamoto kubwa. Wakosoaji wanasema rais huyo na watu wake wa karibu walitumia mamlaka ya serikali kujinyakulia maeneo makubwa ya ardhi katika Bonde la Ufa na Pwani. Wapinzani wa serikali yake pia walikabiliwa na ukandamizaji, huku mauaji ya wanasiasa kama Pio Gama Pinto, Tom Mboya na JM Kariuki yakitia doa utawala wake. Mrithi wake, Daniel arap Moi, aliongoza kwa miaka 24 iliyokumbukwa kwa ukandamizaji wa wapinzani. Mwaka 1982 alibadilisha Katiba na kufanya Kenya kuwa nchi ya mfumo wa chama kimoja, huku wakosoaji wakikamatwa na kuzuiliwa bila kufikishwa mahakamani. Mauaji ya Wagalla mwaka 1984 na mauaji ambayo hayajatatuliwa ya Waziri wa Masuala ya Kigeni Robert Ouko mwaka 1990 yalizidisha wasiwasi kuhusu matumizi mabaya ya mamlaka. Pia, kashfa ya Goldenberg ilitajwa kuwa mojawapo ya visa vikubwa vya ufisadi nchini. Mwai Kibaki aliingia madarakani akiwa na matumaini ya mageuzi, lakini utawala wake pia ulikumbwa na changamoto. Kashfa ya Anglo-Leasing iliharibu sifa ya serikali yake katika muhula wa kwanza. Uchaguzi wa 2007 uliopingwa ulisababisha ghasia zilizoua zaidi ya watu 1,000 na kuwafanya mamia ya maelfu kutoroka makazi yao. Baadhi ya viongozi walifikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Pia, operesheni dhidi ya kundi la Mungiki ilisababisha vifo au kutoweka kwa zaidi ya watu 500, kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu Kenya. Utawala wa Uhuru Kenyatta nao ulikosolewa kwa kukopa fedha nyingi za kufadhili miradi kama reli ya kisasa ya SGR, hali iliyoongeza deni la taifa. Kulikuwa pia na mikataba iliyodaiwa kuwa ya bei ya juu, maswali kuhusu matumizi ya fedha za Eurobond na kashfa ya ufisadi katika Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS). Kwa nini basi ukosoaji dhidi ya Dkt Ruto unaonekana kuwa mkali zaidi? Mtaalamu wa siasa Gasper Odhiambo anasema ufisadi pekee hauwezi kueleza hasira za baadhi ya Wakenya dhidi ya serikali ya sasa, kwa kuwa nchi imekuwa ikikumbwa na serikali zinazokabiliwa na tuhuma za ufisadi kwa miaka 60. Anasema tofauti ni kwamba marais waliomtangulia hawakuahidi mabadiliko makubwa kama Ruto. "Wanamchukia huyu kwa sababu aliahidi kuwa tofauti lakini akathibitisha kuwa ni kama wengine. Kibaki hakuahidi kuwa mtakatifu, Moi hakuahidi kuwa mwanamageuzi na Uhuru hakuahidi kuwa hustler," alisema. Odhiambo anasema Ruto aliinua matarajio ya wananchi kupitia kaulimbiu kama Bottom Up, Hustler Nation, kukomesha utekaji nyara na kuondoa udhibiti wa serikali na watu wachache katika uchumi. Lakini kwa maoni yake, rais ameshindwa kutimiza matarajio hayo. Alisema marais waliomtangulia walielewa umuhimu wa kutotangaza kila hatua ya serikali hadharani, lakini Ruto amekuwa akitoa matamshi makali mbele ya kamera. Hata hivyo, mtaalamu mwingine wa siasa John Okumu anasema utawala wa Ruto umefanya baadhi ya mafanikio ambayo hayapaswi kupuuzwa. Anasema Ruto alipoingia madarakani Septemba 2022, mfumuko wa bei ulikuwa takriban asilimia tisa, shilingi ilikuwa imefika Sh167 dhidi ya dola moja na Kenya ilikuwa katika hatari ya kushindwa kulipa madeni yake. Kwa mujibu wake, mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 3.8 wakati mmoja, akiba ya fedha za kigeni ikaongezeka kutoka kati ya dola bilioni tano na sita hadi dola bilioni 10.3, huku shilingi ikitulia. Hata hivyo, mfumuko wa bei ulipanda tena hadi asilimia 6.8 Septemba 2026. Okumu pia anasema bei ya mbolea ilipungua kutoka Sh7,000 hadi Sh2,000 kwa gunia, huku bei ya mbegu zilizoidhinishwa ikipunguzwa kwa nusu. Bei za kahawa na maziwa pia zilipanda. Katika elimu, anasema serikali imeajiri karibu walimu 100,000 na kujenga madarasa 23,000. Hata hivyo, Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri anasema Ruto anakosolewa kwa sababu ya kufanya kazi katika mazingira ambako wapinzani wake wanatumia siasa za chuki. Anasema marais waliomtangulia walikuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti taarifa zilizowafikia wananchi, tofauti na sasa ambapo simu za mkononi na mitandao ya kijamii husambaza matukio kwa haraka. "Ruto anahukumiwa wakati mambo yanatokea, ilhali waliomtangulia walihukumiwa miaka mingi baadaye, wakati hasira za wananchi zilikuwa zimepungua," alisema. Lakini Seneta wa Murang'a Joe Nyutu anasema rais ndiye adui wake mkubwa wa kisiasa. Anasema Ruto alijiwasilisha kama mtu wa nje ya mfumo wa kisiasa mwaka 2022, akiahidi kukomesha ufisadi, mauaji ya kiholela na utawala wa familia zenye nguvu. "Alisema alikuwa hustler na angevunja mfumo wa watu wachache kudhibiti serikali. Lakini alipoingia madarakani alifanya mambo kama mfumo uleule," alisema Nyutu. Mchambuzi wa siasa Gitile Naituri anasema Ruto huzungumza kama mwanasiasa anayefanya kampeni hata akiwa rais, jambo linalofanya mamlaka yake ionekane ya kutisha. Joseph Kaguthi, ambaye alihudumu kwa muda mrefu katika utawala wa umma, anasema Ruto ameingia katika migogoro na karibu kila kituo cha ushawishi. Anataja mgogoro wake na Uhuru, kuondolewa kwa Rigathi Gachagua, mivutano na wafanyabiashara kuhusu ushuru na maandamano ya Gen Z mwaka 2024. Anasema kuondolewa kwa Gachagua kuliumiza kisiasa eneo la Mlima Kenya, ambalo lilimsaidia Ruto kushinda urais mwaka 2022. Kwa upande mwingine, Waziri wa Afya Aden Duale anamtetea rais akisema alirithi uchumi uliokuwa katika hali mbaya, ukiwa na deni la zaidi ya Sh10 trilioni na shinikizo za taasisi za kimataifa kuongeza ushuru. Anasema Ruto alilazimika kufanya maamuzi magumu ili kuzuia nchi kushindwa kulipa madeni yake. Hata hivyo, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro anasema Ruto alidhani kushinda uchaguzi ndilo lilikuwa jambo gumu zaidi, bila kuelewa kuwa kuongoza nchi ni kazi ngumu kuliko kufanya kampeni.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
Mzozo wa ardhi ya Mau warejea Gideon Moi akilaumu serikali
MZOZO kuhusu umiliki wa ardhi inayozunguka Msitu wa Mau umekuwa zaidi ya suala la uhifadhi wa mazingira. Kwa miaka mingi, umekuwa chanzo cha migawanyiko ya kisiasa, kuvunjika kwa urafiki na kubadilisha miungano ya uchaguzi katika eneo la Bonde la Ufa. Sasa, huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi ameibua tena suala hilo, akionya kuwa Kenya inaweza kuingia katika uchaguzi mwingine bila kutatua dhuluma za kihistoria zilizokumba maelfu ya familia zilizofurushwa. Akizungumza nyumbani kwake Kabarak alipokutana na ujumbe kutoka Ololung'a, Kaunti ya Narok, Bw Moi alihoji ikiwa serikali inaweza kuomba muhula mwingine bila kutoa suluhu kwa wakazi hao. "Tusipotatua suala la Mau katika utawala huu, tukiingia katika uchaguzi mwingine, je, suala hili litawahi kutatuliwa?" aliuliza. Mzozo huo ulizua mgawanyiko mkubwa katika serikali ya muungano ya Rais Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wakati wa operesheni za kufurusha wakazi msituni mwaka 2008 na 2009. Serikali ilikabiliwa na changamoto ya kusawazisha uhifadhi wa mojawapo ya vyanzo muhimu vya maji nchini na madai ya familia zilizosema zilinunua au kupewa ardhi kihalali. Ripoti ya Tume ya Ndung'u ya mwaka 2004 ilifichua ugawaji wa ardhi uliotiliwa shaka katika mfumo wa ikolojia wa Mau na kupendekeza kufutwa kwa hati zilizotolewa kinyume cha sheria. Mnamo Julai 2008, Raila alianzisha mpango wa kurejesha msitu, huku jopo kazi likipewa jukumu la kupendekeza namna ya kuwahamisha wakazi na kurekebisha maeneo yaliyoharibiwa. Ripoti yake ya 2009 ilibainisha pia haki za jamii ya Ogiek, ambayo ina uhusiano wa kihistoria na msitu huo.Waziri wa Mazingira wakati huo, John Michuki, alisisitiza kuwa msitu ulipaswa kusafishwa. Hata hivyo, wanasiasa wa Bonde la Ufa, akiwemo William Ruto aliyekuwa Waziri wa Kilimo, walipinga kufurushwa kwa familia bila fidia au ardhi mbadala. Mnamo Julai 2009, wabunge 18 wakiongozwa na Ruto, Franklin Bett na Hellen Sambili walipinga msimamo wa Michuki. Mazungumzo kati ya Raila na wabunge 22 wa eneo hilo yalijadili uwezekano wa kuwahamisha wakazi kwa fidia, huku gharama iliyopendekezwa ikifikia Sh38 bilioni. Mzozo huo ulimpa Ruto nafasi ya kujitokeza kama mtetezi wa familia zilizoathirika. Alishutumu serikali ya Raila kwa kuongoza operesheni bila kuhakikisha wakazi wanapata makao mapya. Mnamo Desemba 2009, Ruto alitangaza kuwa serikali ingetumia Sh1 bilioni kununua ardhi mbadala. Alisema ekari 4,000 zilikuwa zimepatikana na nyingine 3,000 zilikuwa zikitafutwa. Suala hilo baadaye likawa sehemu ya kampeni za uchaguzi wa 2013. Ruto na Uhuru Kenyatta walilitumia kukumbusha wapiga kura kuhusu mgawanyiko uliokuwepo katika serikali ya Kibaki na Raila. Hata hivyo, baada ya kuingia madarakani, serikali ya Jubilee ilikabiliwa na jukumu la kutimiza ahadi ya kuwapa makao waliofurushwa. Baadhi ya familia zililipwa Sh400,000 kwa kila mkuu wa familia, lakini madai yote hayakutatuliwa. Hadi sasa, familia katika Maasai Mau zinataka ufafanuzi kuhusu wanaostahili fidia na makao mapya. Wakazi wa Kuresoi pia wanataka vizuizi vilivyowekwa kwenye ardhi nje ya msitu rasmi viondolewe. Katika Ang'ata Barikoi, mzozo unahusu ekari 8,500. Wakazi wanadai kuwa ni ekari 1,500 pekee zilizotolewa kwa wenyeji na wanataka kujua kilichotokea kwa ekari 7,000 zilizosalia. Kwa Bw Moi, serikali inapaswa kuweka wazi vigezo vya wanaostahili fidia, kukamilisha utoaji wa hati na kutatua madai yanayohusu ardhi hizo. Kwa familia zilizoathirika, mabadiliko ya serikali na miungano ya kisiasa hayana maana bila kupata ardhi salama, fidia au makao ya kudumu. Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, swali kuu ni iwapo mzozo wa Mau utatatuliwa au utaendelea kutumiwa kama silaha ya kampeni.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Makosa ya Rais Uhuru yaliyojengea Ruto jina Mlimani kura iliyopita
KWA miaka mingi Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alikuwa na ushawishi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya. Lakini katika uchaguzi wa 2022 alishuhudia wafuasi wake wengi wwa Mlimani wakipuuza chaguo lake la urithi wa kisiasa, Raila Odinga, wakamuunga mkono aliyekuwa naibu wake, William Ruto. Sasa, Seneta wa Murang'a Joe Nyutu anasema uamuzi huo haukutokana tu na umaarufu wa Ruto, bali pia makosa ya kisiasa aliyofanya Uhuru katika muhula wake wa pili. Makosa hayo ndiyo yaliumba nafasi kwa naibu wake kujijenga kisiasa neo hilo. Akizungumza katika mahojiano na kituo cha redio Jumanne, Nyutu alisema Uhuru alishindwa kudumisha uhusiano wa karibu na viongozi waliochaguliwa Mlima Kenya, na hivyo kumpa Ruto fursa ya kujenga mtandao wake. "Rais Uhuru Muigai Kenyatta hakuwahi kuwapa viongozi waliochaguliwa Mlima Kenya nafasi ya kukutana naye katika muhula wake wa pili. Unaweza kuthibitisha hilo. Miaka yote mitano," alisema Nyutu. Alidai kuwa hata viongozi walipokutana na Uhuru mara nyingi waliondoka wamekerwa na jinsi aliwahudumia.Ruto akatambua pengo hilo na kulitumia kuimarisha uhusiano wake na viongozi na wakazi wa eneo hilo. "Rais Ruto, ambaye wakati huo alikuwa naibu rais, alitambua kulikuwa na pengo. Viongozi wa Mlima Kenya hawakuwa wakipata nafasi ya kuzungumza na rais (uhuru). Aliona pengo, akalijaza. Aliwakumbatia viongozi hao na alikuwa akipatikana," akaeleza. Kauli za Nyutu zinagusia mojawapo ya masuala yaliyotikisa Jubilee katika muhula wa pili wa Uhuru: uhusiano uliokuwa ukizorota kati yake na naibu wake, na mgawanyiko chamani. Dalili za kutoridhika zilionekana hata kabla ya uchaguzi wa 2022. Mnamo Januari 2021 baadhi ya wabunge wa Mlimani waliandika barua kwa Uhuru wakilalamikia kutopata mwaliko wa mkutano wa Sagana na kukosa nafasi ya kuwasilisha matatizo ya wakazi. Walilalamikia kile walichosema ni kutofikiwa kwa rais na kutokuwepo kwa utekelezaji wa masuala yaliyojadiliwa katika mikutano ya awali. Hali hiyo ilimpa Ruto nafasi ya kuendeleza ziara zake Mlimani ikiwemo kuhudhuria ibada za kanisa na kuwasiliana na viongozi na wakazi. Utafiti wa kitaaluma kuhusu uchaguzi wa 2022 ulionyesha kuwa ziara za mara kwa mara za Ruto, michango yake kwa makanisa na kampeni yake ya kujenga uungwaji mkono mashinani zilichangia kuimarisha umaarufu wake. Uhuru na Ruto walijenga ushirikiano wa kisiasa uliowapa ushindi katika kura ya 2013 na 2017. Ushirikiano huo ulijulikana kupitia kauli maarufu ya "Kumi yangu, kumi ya Ruto". Hata hivyo, baada ya 2017 uhusiano wao ulianza kudhoofika, hasa baada ya Uhuru kuanzisha ushirikiano na aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitia 'handisheki' mwaka 2018. Ruto alijitenga na mrengo wa raiss na kuanza kujijenga kama mpinzani ndani ya serikali aliyokuwa akihudumu. Alitumia ujumbe wa "hasla" dhidi ya "dynasty", akijiwasilisha kama mtetezi wa watu wa kawaida waliokabiliana na changamoto za kiuchumi. Uchambuzi wa kitaaluma kuhusu uchaguzi wa 2022 unaonyesha kuwa ujumbe huo ulivutia wapiga kura mbalimbali wakiwemo vijana, huku kampeni ya Ruto ikijikita katika ziara za maeneo mengi na kujenga miungano ya mashinani. Mnamo Februari 23, 2022, Uhuru alitumia mkutano wa Sagana kumtangaza Raila kuwa mgombea aliyemtaka amrithi katika Ikulu. Aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kumuunga mkono, akisema alikuwa na maslahi ya taifa moyoni. Pia alimkosoa Ruto, akidai kuwa naibu wake alikuwa akidhoofisha serikali aliyokuwa akihudumu. Lakini kwa mujibu wa Nyutu, wakati huo ulikuwa umechelewa kwa sababu Ruto alikuwa tayari amejenga uhusiano wa karibu na wakazi wa eneo hilo. Alisema Uhuru alitarajia wakazi wa Mlima Kenya wamwache mwanasiasa waliyekuwa wakimwona mara kwa mara na kumuunga mkono Raila bila kuwapa sababu zilizowashawishi. Nyutu pia alidai kuwa taswira ya Ruto kama mwanasiasa aliyekuwa akidhulumiwa na aliyekuwa bosi wake ilimshindia huruma miongoni mwa wapiga kura. Katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022, Ruto alipata kura 7,176,141 sawa na asilimia 50.49, huku Raila akipata kura 6,942,930, sawa na asilimia 48.85. Nyutu anasema wakazi wa eneo hilo walifanya kosa kwa kupuuza onyo la Uhuru dhidi ya kumchagua Ruto. "Ndipo tulipoingia kwenye mtego. Mtego hatari zaidi ambao eneo hili limewahi kuingia. Mtego wa kumchagua Rais Ruto," alisema. Hata hivyo, uchaguzi huo pia ulionyesha kuwa wapiga kura hawakufuata moja kwa moja msimamo wa rais aliyekuwa madarakani, bali walifanya uamuzi wao wenyewe. Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, mjadala kuhusu ushawishi wa Uhuru katika Mlima Kenya unaendelea. Makosa anayotajwa kufanya sasa yanajadiliwa wakati eneo hilo linakabiliwa na ushindani wa viongozi wanaotaka kuongoza maamuzi yake ya kisiasa. Kwa Nyutu, funzo kuu ni kuwa kiongozi hawezi kudhani kuwa uungwaji mkono wa wananchi ni wa kudumu bila kudumisha mawasiliano na kushughulikia malalamishi yao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
ODM yaanza kujipenyeza ngome ya UDA
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinatanua ushawishi wake katika Bonde la Ufa, eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa ngome ya kisiasa ya Rais William Ruto na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA). Kuvutiwa kwa wanasiasa wanaotaka kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa 2027 nkupitia tiketi ya ODM kunaashiria mabadiliko katika hesabu za kisiasa katika eneo hilo. Hali hii inajiri huku UDA na ODM zikiwa zimeingia katika ushirikiano wa kisiasa unaolenga kumuunga mkono Rais Ruto kuwania muhula wa pili kupitia serikali jumuishi. Hata hivyo, Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga amesisitiza kuwa ushirikiano huo hautamaanisha chama chake kukabidhi ngome zake za kisiasa kwa UDA. "Makubaliano ya kisiasa na UDA ni kuhakikisha Rais Ruto anachaguliwa tena na hayatahusisha kukabidhi maeneo ambayo ni ngome za ODM," alisema Wanga wakati viongozi wa chama hicho walipotembelea Bonde la Ufa hivi majuzi. Miongoni mwa wanasiasa walioamua kujiunga na ODM ni aliyekuwa Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio, ambaye alihama chama cha Kanu pamoja na baadhi ya viongozi wa eneo hilo wakiwemo madiwani. "Nimeondoka rasmi Kanu na kujiunga na ODM. Nitaelekeza nguvu na rasilimali zangu katika kukieneza chama hiki," alisema Poghisio. Hatua hiyo inatarajiwa kuzidisha ushindani wa kisiasa Pokot Magharibi, ambako Poghisio ana nia ya kuwania ugavana dhidi ya wapinzani wake wa muda mrefu. Kwa ODM, kuhama kwa Poghisio ni ushindi mkubwa katika juhudi za kupanua ushawishi wake katika eneo ambako Kanu na UDA zimekuwa na wafuasi wengi. Naibu kiongozi wa ODM, ambaye pia ni Gavana wa Kisii, Simba Arati alisema chama hicho kinaandaa mikutano mikubwa ya kisiasa Pokot Magharibi na maeneo mengine nchini kuelekea uchaguzi wa 2027. Alisema ODM itaendelea kumuunga mkono Rais Ruto katika azma yake ya kuchaguliwa tena, huku ikijenga nguvu zake za kisiasa. Arati pia alidai kuwa wabunge 11 walio mamlakani kutoka vyama vingine wanatarajiwa kujiunga na ODM. "Chama chetu bado kina nguvu na tutapigania usawa chini ya kaulimbiu ya Usawa ni Sawa," alisema. Kuingia kwa ODM katika Bonde la Ufa kunakipatia fursa ya kupanua ushawishi wake nje ya maeneo yake ya jadi na kujijenga kama chama chenye uwezo wa kushindana katika eneo ambalo kwa miaka mingi limekuwa gumu kwake kisiasa. Kwa upande mwingine, umaarufu mkubwa wa UDA katika eneo hilo umevutia wanasiasa wengi wanaotaka tiketi ya chama hicho kuwania nyadhifa mbalimbali. Hali hiyo imeongeza ushindani wa mchujo wa chama, na baadhi ya wanasiasa wanaweza kutafuta vyama mbadala ili kulinda nafasi zao za kisiasa. Mchambuzi wa siasa Wilson Saina kutoka Eldoret anasema tiketi ya UDA Bonde la Ufa inachukuliwa kama njia rahisi ya kushinda uchaguzi mkuu kutokana na nguvu ya chama hicho eneo hilo. "Kupata tiketi ya UDA katika mchujo wa chama Bonde la Ufa ni sawa na kushinda uchaguzi mkuu. Ndio maana upenyo wa ODM unatoa njia mbadala kwa wanasiasa wengi wanaowinda nyadhifa 2027," aeleza. Kulingana naye ODM inaweza kuwa kimbilio la wanasiasa wanaotaka kubaki ndani ya serikali jumuishi lakini hawana uhakika wa kupata tiketi ya UDA. Saina anasema ushirikiano kati ya UDA na ODM umebadilisha siasa za kawaida ambapo vyama vilikuwa vikijulikana wazi kuunga serikali au upinzani. Chini ya mpangilio huo, wanasiasa wa ODM wanaweza kuunga mkono serikali huku wakihifadhi utambulisho wa chama chao na kuendelea kukitafutia wafuasi katika maeneo ambayo awali kilikuwa na ushawishi mdogo. Wanga amesema lengo la ODM ni kupata viti vingi vya ubunge na nyadhifa nyingine ili kuwa na nguvu katika mazungumzo ya kugawana mamlaka baada ya uchaguzi. "Serikali ijayo itaundwa na UDA na ODM. Tunataka kushinda viti vingi ili tuwe na nafasi ya kujadiliana kwa usawa wa asilimia 50 kwa 50 kuhusu nyadhifa za juu serikalini, zikiwemo za makatibu wa wizara," alisema. Aliahidi kuwa mchujo wa ODM utakuwa huru na wa haki. Bonde la Ufa ni eneo muhimu katika siasa za Kenya, huku mifumo ya upigaji kura ikiathiriwa kwa kiasi kikubwa na miungano ya kikabila na nguvu za vyama vinavyohusishwa na viongozi wa eneo hilo. UDA iliimarisha ngome yake baada ya uchaguzi wa 2022, ambapo Rais Ruto alipata uungwaji mkono mkubwa katika kaunti za Uasin Gishu, Nandi, Elgeyo Marakwet na maeneo mengine ya Bonde la Ufa. Hata hivyo, uchaguzi wa 2027 unaanza kufichua migawanyiko mipya. Katika Uasin Gishu, kwa mfano, tayari kuna makundi mawili yanayowania ushawishi katika kinyang'anyiro cha ugavana. Kundi moja linaunga mkono Gavana Jonathan Bii kutetea kiti chake na linahusishwa na Mbunge wa Kapsaret Oscar Sudi. Kundi la pili linaongozwa na Seneta Jackson Mandago, ambaye anamuunga mkono Katibu katika Wizara ya Elimu, Julius Bitok, kuwania ugavana. Pia kuna mfanyabiashara Bundotich Zedekiah Kiprop, maarufu kama Buzeki, aliyejiunga na UDA na anatarajiwa kujaribu kwa mara ya tatu kuwania ugavana. Kwa wanasiasa wanaohisi hawana nafasi nzuri ya kupata tiketi ya UDA, ODM inaweza kuwa njia mbadala bila kuwalazimisha kujiondoa katika ushirikiano wa serikali jumuishi. Kupanuka kwa ODM katika Bonde la Ufa sasa kunakuwa mtihani kwa Rais Ruto, ambaye atalazimika kusawazisha maslahi ya kisiasa yanayokinzana katika ngome yake huku akijaribu kuimarisha uungwaji mkono kuelekea uchaguzi wa 2027.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Gachagua sasa amfunika Uhuru Mlimani wimbi la DCP likizoa wengi
CHAMA cha Jubilee kilichomuingiza madarakani Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kilichowahi kutawala siasa za Mlima Kenya, sasa kinakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Democracy for Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake Mei 2025, DCP imevutia viongozi waliokuwa wanachama wa Jubilee, na hivyo kuzidisha vita vya kisiasa kuhusu nani atatawala eneo hilo kuelekea uchaguzi wa 2027. Baada ya Gachagua kung'olewa mamlakani Oktoba 2024, Jubilee ilianza juhudi za kurejesha ushawishi wake. Uhuru alitangaza kuwa chama hicho kingerejea chini ya uongozi wa Dkt Fred Matiang'i, aliyekuwa akitajwa kuwa mgombeaji wake wa urais. Lakini Gachagua alipozindua DCP, ushindani wa kisiasa ulizidi. Alisema chama chake ndicho kingekuwa chombo pekee cha kisiasa cha Mlima Kenya, huku vingine vikijivuta. Miongoni mwa viongozi waliohama kutoka UDA na kujiunga na DCP ni magavana Irungu Kang'ata wa Murang'a na Kiarie Badilisha wa Nyandarua, pamoja na wabunge Wachira Karani, Muchangi Karemba, Rahab Mukami na Martha Wangari. Aliyekuwa Mbunge wa EALA Kanini Kega, ambaye alikuwa mmoja wa washirika wa karibu wa Uhuru, pia alihamia DCP mwaka 2025. Alisema Jubilee ilikosa uongozi na kwamba wanachama walikuwa wakiondoka kwa wingi. Huko Nairobi, wabunge wote watatu waliochaguliwa kwa tiketi ya Jubilee—Yusuf Hassan wa Kamukunji, Mark Mwenje wa Embakasi Central na Amos Mwago wa Starehe—wametangaza kuwa watatetea viti vyao kupitia DCP. Chama hicho pia kimepokea madiwani wa Jubilee jijini Nairobi. Pigo jingine lilitokea katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, ambapo DCP ilipata asilimia 86 ya kura, ikilinganishwa na asilimia 13 za UDA. Jubilee ilipata kura 128 pekee. Mnamo Septemba 22, Uhuru alimkabidhi Matiang'i uongozi wa Jubilee. Hata hivyo, viongozi wa DCP walianza kueneza ujumbe kuwa chama hicho kilikuwa kimeelekezwa zaidi eneo la Gusii, huku DCP ikijikita Mlima Kenya. Baadaye, Uhuru alipohudhuria mazishi ya babake Martha Karua Kirinyaga Oktoba 3, alitoa wito kwa viongozi wa upinzani kuungana na kumteua mgombeaji mmoja wa urais dhidi ya Rais William Ruto mwaka 2027. Kauli hiyo ilitafsiriwa na baadhi ya wanachama wa Jubilee kama ishara kuwa hakuwa na nia ya kufufua chama hicho. Aliyekuwa Mbunge wa Mwea Kabinga wa Thayu alisema alihama kwa sababu Jubilee ilikuwa ikijaribu kujifufua huku mwanzilishi wake akionyesha kutopendezwa na siasa za vyama. Matiang'i, hata hivyo, amepuuzilia mbali madai ya mgawanyiko, akisema taarifa kuhusu mvutano kati ya viongozi wa upinzani zinalenga kuwatenganisha. Gachagua naye anasema hahusiki moja kwa moja na uhamaji huo, akidai viongozi wanashinikizwa na wafuasi wao kujiunga na DCP. Anasema kazi yake ni kuwapokea na kuratibu mikutano yao katika makao yake Wamunyoro. Hata hivyo, aliyekuwa Naibu Kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alijiuzulu Novemba 25, 2026 akisema anajiandaa kuanzisha jukwaa jingine la kisiasa. Jubilee, chama cha PPK cha Ndindi Nyoro, PLP cha Karua na PNU cha Peter Munya sasa vinafanya kampeni zao tofauti katika Mlima Kenya. Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Zack Kinuthia amesema chama hicho kitarejea kwa nguvu na kuendelea kutetea demokrasia ya vyama vingi. Amesema hali ya sasa ni ya muda tu na hakuna eneo la nchi linalopaswa kutawaliwa na chama kimoja pekee.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 21 hours ago
Kifungo cha Obado miaka 25 jela chazua hisia mseto
Je, haki imetendeka hatimaye katika mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno, au adhabu iliyotolewa ni hafifu ikilinganishwa na uzito wa kosa? Hili ndilo swali linaloibua mjadala baada ya aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado kuhukumiwa kifungo cha miaka 25 jela. Baadhi ya Wakenya na mashirika ya kutetea haki za binadamu wamesema adhabu hiyo ni ndogo, wakiamini Obado na washirika wake walistahili vifungo vikali zaidi kutokana na mauaji ya Sharon aliyekuwa mjamzito. Hata hivyo, familia ya Sharon imesema itakata rufaa ikitaka Obado aachiliwe huru. Wakili wake, Antony Opondo, alithibitisha hatua hiyo. Kikosi cha mawakili wake pia imesema itakata rufaa kupinga uamuzi huo. Obado alihukumiwa Ijumaa kifungo cha miaka 25 kwa mauaji ya Sharon, aliyekuwa mpenzi wake. Aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi, Michael Oyamo, naye alipata miaka 25, huku aliyekuwa karani wa Kaunti ya Migori, Caspal Obiero, akihukumiwa miaka 18. Shirikisho la Wanasheria Wanawake nchini (FIDA-Kenya) lilipongeza uamuzi huo, likisema ni hatua muhimu katika kuwawajibisha wahusika na kuhakikisha waathiriwa wanapata haki. Mwenyekiti wa FIDA Christine Kungu alisema hukumu hiyo imehitimisha hatua muhimu katika harakati za miaka karibu minane za familia ya Sharon kutafuta haki. Alisema hakuna hukumu inayoweza kurejesha maisha ya Sharon na mtoto wake ambaye hajazaliwa, wala kuondoa maumivu ambayo familia imepitia. Gavana wa sasa wa Migori Ochilo Ayacko alisema amefuatilia kwa wasiwasi hukumu dhidi ya mtangulizi wake na washtakiwa wenzake. Alituma salamu za pole na faraja kwa watatu hao na familia zao. Mwanasiasa na mwanaharakati Tony Gachoka alielezea mauaji ya Sharon kuwa ya kikatili, akisema hakuelewa sababu iliyomfanya Obado kumuua mpenzi wake na mama wa mtoto aliyekuwa tumboni. Nchini Homa Bay, wanaharakati wa masuala ya jinsia walipongeza hukumu hiyo, ingawa walitofautiana kuhusu uzito wa adhabu. Julius Omuga wa shirika la Zana Africa alisema Obado alistahili kifungo cha maisha kwa kuwa mauaji hayo yalihusisha Sharon na mtoto wake ambaye hajazaliwa. Alisema adhabu kali ingetuma ujumbe kwa wanaume wanaowaua wanawake, hasa wakati huu wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, Hellen Oromo, mratibu wa mipango katika shirika la Lake Region Community Development, alisema kifungo cha miaka 25 ni hatua muhimu baada ya familia kusubiri miaka minane. Alisema hukumu hiyo inaonyesha kuwa hakuna mtu aliye na mamlaka makubwa kiasi cha kukwepa mkono wa sheria, licha ya madai kwamba Obado alikuwa na watu wenye ushawishi ambao wangemsaidia kukwepa haki.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 28 Nov 2026 06:55:18
Wahalifu waanika taarifa za Wakenya milioni 32 walizoiba eCitizen
WAHALIFU wa mtandaoni waliovamia na kudukua tovuti ya eCitizen wameanza kusambaza taarifa za kibinafsi za Wakenya zaidi ya 32 milioni katika mtandao fiche wa Dark Web, hatua inayowaweka mamilioni ya watu katika hatari ya utapeli. Taarifa zilizopatikana na 'Taifa Leo' zinaonyesha kuwa wadukuzi hao waliiba rekodi za Wakenya 32,128,394, zikiwemo nakala za pasipoti, picha za pasipoti, nambari za vitambulisho vya kitaifa na tarehe za kuzaliwa. Pia waliiba nambari za usajili za Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA), alama za vidole na nambari za kidijitali za afya zinazotumiwa na wanachama wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).Baadhi ya vitambulisho vya kikazi vya maafisa wa serikali pia vimesambazwa, hali inayozua hofu kuwa taarifa hizo zinaweza kutumiwa kuomba mikopo kwa majina yao au kuwatapeli. Kikundi cha wahalifu wa mtandaoni kinachojulikana kama ByteToBreach kimekiri kuhusika na shambulizi hilo.Kikundi hicho kinadai kuwa kiliingia katika mifumo ya eCitizen na kuiba gigabaiti 600 za stakabadhi za kuthibitisha utambulisho wa wateja, gigabaiti 100 za taarifa za data na gigabaiti 40 za msimbo unaoendesha mifumo hiyo.Taarifa hizo ziligunduliwa Jumatatu na kampuni ya Amerika ya usalama wa mtandao, Vecert, inayofuatilia vitisho na shughuli za wahalifu katika mitandao fiche. Wachunguzi wa kampuni hiyo walikagua rekodi za wahalifu hao na kubaini kuwa huenda walipata nafasi ya kuingia katika mitambo ya eCitizen Novemba 15 kwa kutumia udhaifu katika data inayotumika kuthibitisha utambulisho wa watumiaji.Dark Web ni sehemu fiche ya mtandao ambayo haipatikani kupitia injini za kawaida za kutafuta taarifa kama Google. Mara nyingi hutumiwa na wahalifu kuuza taarifa zilizoibwa na huduma za udukuzi.Wataalamu wanaonya kuwa taarifa zilizoibwa zinaweza kutumiwa kutuma jumbe za ulaghai zinazodaiwa kutoka kwa serikali, benki au taasisi za afya ili kuwashawishi wananchi kutoa nywila na taarifa zao za siri. Pia wahalifu wanaweza kutumia taarifa hizo kufungua akaunti za kifedha, kuomba mikopo kwa majina ya waathiriwa au kuwatishia kusambaza taarifa zao za faragha wasipolipa pesa.Hatari ni kubwa zaidi kwa sababu baadhi ya taarifa zilizoibwa ni za kibayometriki na afya. Tofauti na nywila, alama za vidole haziwezi kubadilishwa kirahisi zinapovuja.Mtafiti wa usalama wa mtandao na Mkurugenzi Mkuu wa Cyber Guard Africa, Dkt Bright Gameli, alisema kuvamiwa kwa mfumo mmoja wa utambulisho kunaweza kuhatarisha huduma nyingine zinazotegemea mfumo huo. "Ukiukaji wa usalama wa mfumo mkuu wa uthibitishaji wa utambulisho unaweza kutoa njia ya kuingia katika huduma nyingine zilizounganishwa nao, kutegemea jinsi mifumo hiyo ilivyoundwa na kiwango cha kupenya alichopata mvamizi," alisema. ByteToBreach ilitaja SHA, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Huduma ya Kitaifa ya Polisi miongoni mwa taasisi zinazoweza kuathiriwa kupitia mfumo huo. Hata hivyo, hakuna ushahidi uliotolewa kuthibitisha kuwa mifumo ya taasisi hizo ilivamiwa.Mnamo Jumanne, Wizara ya Masuala ya Ndani ilikiri kupokea taarifa kuhusu kuingia bila idhini katika data za eCitizen na kusema timu za kiufundi na usalama zilikuwa zikichunguza ukubwa wa tukio hilo. Wizara hiyo ilisema huduma za eCitizen zinaendelea kupatikana na wananchi wanaweza kuendelea kuzitumia kama kawaida.eCitizen ni jukwaa kuu la serikali linalowawezesha wananchi na wakazi kupata huduma zaidi ya 22,000, ikiwemo maombi ya pasipoti, leseni za udereva, vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa na ndoa, vyeti vya tabia njema na usajili wa biashara. Wizara haijatoa taarifa nyingine kuhusu matokeo ya uchunguzi huo. Mamlaka ya Mawasiliano nchini nayo ilielekeza maswali kuhusu tukio hilo kwa Shirika la Kitaifa la Usalama wa Mtandao, ambalo halikuwa limejibu maswali kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hii.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 28 Nov 2026 06:55:55
Mpango wa TSC kutoa vyeti kwa walimu vya kuendelea kufundisha wazua hisia mseto
PENDEKEZO la Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuanza kutoa vyeti maalumu kuruhusu walimu kuendelea kufundisha limezua mjadala mkali, huku wadau wa elimu wakitofautiana kuhusu mamlaka ya tume hiyo kusimamia ajira na pia kudhibiti taaluma ya ualimu. Pendekezo hilo limo katika Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya TSC wa 2026, unaolenga kufanya mafunzo ya mara kwa mara ya kuwaongezea walimu ujuzi kuwa ya lazima. Walimu watakaokosa kushiriki mafunzo hayo wanaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Hata hivyo, wadau wanatofautiana kuhusu mpango huo. Baadhi wanataka kuundwa kwa chombo huru kitakachosimamia mafunzo na utoaji wa vyeti vya kitaaluma, huku wengine wakitaka serikali ihakikishe walimu hawalazimishwi kulipia mafunzo hayo. Kifungu cha 28 cha mswada huo kinapendekeza kubadilishwa kwa Kifungu cha 35 cha Sheria ya TSC ili kuipa tume jukumu la kuhakikisha walimu wote wanazingatia viwango vya taaluma ya ualimu.Mswada huo unapendekeza tume iwalazimishe walimu wote waliosajiliwa kushiriki mafunzo ya kuendeleza ujuzi wao na kisha kuwapa vyeti vya kuwaruhusu kuendelea kufundisha. Mwalimu atakayekosa kutimiza masharti hayo atakabiliwa na hatua za kiutawala zitakazofafanuliwa katika kanuni.Pendekezo hilo lina maana kwamba hata walimu ambao wamesajiliwa na TSC na wamehudumu kwa miaka mingi watalazimika kutimiza masharti mapya ili kupata vyeti hivyo.Ingawa usajili wa TSC unatambua mwalimu kuwa amekidhi masharti ya kujiunga na taaluma, cheti kipya kitategemea ushiriki wake katika mafunzo ya mara kwa mara. Hata hivyo, mswada haujaeleza vyeti hivyo vitakuwa halali kwa muda gani, vitafanywa upya baada ya kipindi gani, au kama walimu watalazimika kuvilipia. Pia haujaweka wazi muda wa mafunzo hayo wala atakayeyagharamia. Chama cha Wadau wa Elimu nchini kimepinga pendekezo hilo, kikisema TSC haipaswi kuwa mwajiri na wakati huo huo kuwa msimamizi wa leseni za taaluma.Katibu Mkuu wa kitaifa wa chama hicho, Ndung'u Wangenye, alisema Bunge linapaswa kupitisha sheria ya kuunda chombo huru kitakachosimamia mafunzo na kutoa vyeti vya kitaaluma kwa walimu. Alisema jukumu la TSC linapaswa kubaki kuwa kuajiri walimu, kama vile serikali za kaunti, shule za kibinafsi na bodi za usimamizi wa shule zinavyoajiri.Kwa upande mwingine, Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kati (Kuppet), kimeunga mkono pendekezo hilo, kikisema mafunzo ya mara kwa mara yatawasaidia walimu kutambua udhaifu wao na kuboresha maarifa na ujuzi. Naibu Katibu Mkuu wa Kuppet, Moses Nthurima, alisema mafunzo yatakayofanyika mtandaoni yatawapa walimu nafasi ya kuchagua maeneo wanayohitaji kuimarisha na kujifunza kwa wakati unaowafaa.A lisema mfumo huo unatumika katika taaluma nyingine duniani, akitaja mawakili, wahandisi na masoroveya ambao hulazimika kuhudhuria mafunzo ili kudumisha leseni zao za kazi.Aliongeza kuwa vyeti hivyo vinaweza kuwasaidia walimu wa Kenya kupata nafasi za ajira nje ya nchi kwa kuwa vitatoa ushahidi wa ziada kuhusu uwezo wao wa kitaaluma. Hata hivyo, Kuppet inakiri kuwa kuna changamoto ya TSC kuwa mwajiri na mdhibiti wa taaluma kwa wakati mmoja. Bw Nthurima alisema hali hiyo imetokana na mfumo uliowekwa na Katiba na kwamba walimu wanapaswa kukubali mfumo uliopo hadi mabadiliko yatakapofanywa. Naye Bw Boaz Waruku wa kundi la Elimu Bora Working Group, alisema anaunga mkono mafunzo ya mara kwa mara kwa sababu yanaweza kuinua viwango vya ufundishaji.Hata hivyo, alionya kuwa walimu hawapaswi kubebeshwa gharama za mafunzo hayo. Alisema kama TSC inawataka walimu kujiendeleza kitaaluma, basi kama mwajiri ina wajibu wa kugharamia mafunzo yao. "Utekelezaji wa mpango huu haupaswi kuwa kwa gharama ya mwalimu," alisema. Bw Waruku pia aliunga mkono wazo la kutenganisha majukumu ya TSC kama mwajiri na mdhibiti wa taaluma, akisema chombo maalumu kinaweza kuundwa ndani ya mfumo wa sasa wa kikatiba kusimamia udhibiti wa taaluma. Alisema utaratibu huo utasaidia kuimarisha uwajibikaji na kuondoa mgongano wa maslahi unaoweza kujitokeza pale taasisi moja inapokuwa mwajiri na mdhibiti wa wafanyakazi wake ."Kuendeleza ujuzi ni jambo la kawaida katika taaluma ya sheria, udaktari na uhandisi. Kinachopaswa kujadiliwa ni nani atakayelipia mafunzo hayo," alisema.Aliongeza kuwa mwajiri ana wajibu wa kuendelea kuwapa wafanyakazi wake mafunzo, hivyo TSC inapaswa kugharimia mpango huo badala ya kuwatwika walimu mzigo wa ziada.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 28 Nov 2026 05:55:05
IEBC yahitaji Sh10bn kununua vifaa vipya vya uchaguzi 2027
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) huenda ikalazimika kununua vifaa vipya vya teknolojia ya uchaguzi kila baada ya miaka mitano, hali inayoweza kuongeza mzigo wa matumizi kwa walipa ushuru. Naibu mwenyekiti wa IEBC Fahima Abdalla aliambia Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria ya Bunge la Kitaifa kuwa ukaguzi wa kiufundi uliofanywa na Mamlaka ya ICT (ICTA) ulibaini kuwa vifaa vya usimamizi za uchaguzi Kenya (Kiems) vilivyonunuliwa mwaka 2021 kwa uchaguzi wa 2022 vimefikia mwisho wa muda wake wa matumizi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vifaa 15,000 vilivyonunuliwa wakati huo haviwezi kutegemewa katika uchaguzi mkuu wa 2027. Hali hii ina maana kuwa IEBC italazimika kutafuta angalau Sh10 bilioni kununua vifaa vipya 60,000 ili kuendesha uchaguzi ujao. "Wataalamu wa Mamlaka ya ICT walikuja kukagua vifaa vya Kiems na kutuambia kuwa teknolojia hiyo ina muda wa matumizi wa miaka mitano. Walitueleza kuwa vifaa hivyo havitafanya kazi ipasavyo katika uchaguzi mkuu wa 2027," alisema Bi Abdalla. Kauli yake ilijiri baada ya Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo kutaka kujua ni vifaa vingapi vilivyonunuliwa kwa uchaguzi wa 2022 ambavyo vinaweza kutumika tena mwaka 2027. Hata hivyo, uamuzi huo unazua wasiwasi kuhusu matumizi ya mabilioni ya fedha za umma kila baada ya miaka mitano, huku serikali ikikabiliwa na mahitaji mengine kama afya, miundombinu na malimbikizo ya madeni. IEBC pia inakabiliwa na changamoto ya jinsi ya kutupa vifaa vya zamani. Hapo awali, tume hiyo ilipendekeza kuvifuta taarifa na kuvitoa kwa shule au taasisi nyingine za serikali. Hata hivyo, vifaa hivyo vina teknolojia maalumu za utambuzi wa wapigakura na baadhi ya taarifa zake huhitajika kuhifadhiwa kama ushahidi iwapo kutakuwa na kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi. Mtaalamu wa utawala bora Barasa Nyukuri alisema kununua vifaa vipya kila baada ya miaka mitano kunaweza kuilazimisha IEBC kufanya ununuzi kwa haraka, hali inayoweza kuongeza gharama na kuzua migogoro ya zabuni. Mwanasheria na mtaalamu wa uchaguzi David Ochami alisema mfumo huo utaifanya Kenya kuendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazotumia fedha nyingi kuendesha uchaguzi. Kenya hutumia takriban Sh2,000 hadi Sh2,500 kwa kila mpigakura, ikilinganishwa na wastani wa dola nne hadi tano katika demokrasia zilizoimarika. "Vifaa vya thamani ya mabilioni ya fedha vinapochukuliwa kama vitu vya kutumika kwa miaka mitano pekee, gharama kubwa ya kuvinunua inaingizwa kwenye kila bajeti ya kitaifa," alisema. Kiems ni mfumo wa vifaa vya kielektroniki vinavyotumia mfumo wa Android, vikiwa na mashine za kusoma alama za vidole. Vinatumika kusajili wapigakura, kuwatambua na kutuma matokeo ya uchaguzi. Wataalamu wa ICTA wanasema betri za vifaa hivyo hupoteza uwezo kadri miaka inavyopita, hata kama havitumiki mara kwa mara. Pia programu za zamani za Android huacha kupata usalama baada ya miaka mitatu hadi mitano. Walisema kutumia vifaa ambavyo havipati tena hakikisho la usalama kunaweza kuhatarisha uchaguzi na kuzua maswali kuhusu uaminifu wa matokeo. Kenya ilianza kutumia mfumo jumuishi wa Kiems mwaka 2017, wakati iliponunua vifaa 45,000 kutoka kampuni ya Ufaransa ya Safran, ambayo baadaye ilibadilishwa jina kuwa Idemia, kwa takriban Sh4.3 bilioni. Katika uchaguzi wa 2022, IEBC ilitumia tena takriban vifaa 41,000 vilivyonunuliwa 2017 na kununua vingine 14,100 kutoka kampuni ya Smartmatic ya Venezuela kwa Sh3.2 bilioni. Smartmatic pia iliboresha programu za vifaa vya zamani ili viweze kutumika katika vituo 46,229 vya kupigia kura. Tofauti na uchaguzi wa 2013, ambao ulitumia mifumo tofauti kutoka kwa kampuni mbalimbali, chaguzi za 2017, 2022 na 2027 zinategemea mfumo jumuishi wa teknolojia. Hata hivyo, Kenya bado hulazimika kutumia karatasi za kupigia kura, sajili za wapigakura na zaidi ya makarani 600,000 wa muda, sambamba na teknolojia hiyo, hali inayoongeza gharama ya uchaguzi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 28 Nov 2026 05:04:48
Hivi ndivyo maisha ya Obado yatakuwa gerezani kwa miaka 25
Aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado aliingia katika chumba cha mahakama jijini Nairobi Ijumaa saa mbili na dakika arobaini na tano asubuhi akiwa amevalia suti ya buluu, shati jeupe, tai na viatu vyeusi vilivyong'arishwa. Wafuasi wake waliokuwa wamemsubiri walimkaribisha kwa jina Sibuor (Simba). Aliwajibu kwa kuinua mikono yote miwili akiwa amefungwa pingu. Lakini saa tano asubuhi, Jaji Cecilia Githua alipoanza kusoma hukumu, ukumbi ulitulia. Kwa takriban dakika 40, Obado alisikiliza bila kuonyesha hisia huku mahakama ikieleza nafasi yake katika mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno. Jaji alimweleza kuwa alikuwa mpangaji mkuu, mfadhili na mtekelezaji wa mpango wa kumuua Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26 na ujauzito wa miezi saba. Mahakama ilipohitimisha na kumhukumu miaka 25 jela, baadhi ya wafuasi wake walilia, huku wengine wakizungumza kwa lugha ya Dholuo wakionyesha kutoamini hukumu hiyo. Hata hivyo, baadhi walipiga makofi baada ya mawakili wake kutangaza kuwa watakata rufaa. Obado, ambaye sasa yuko katika miaka ya sitini, anaweza kuwa na zaidi ya miaka 90 atakapomaliza kifungo chake mwaka 2051, iwapo hukumu haitabadilishwa. Kwa siku 123 tangu apatikane na hatia, alikuwa amezuiliwa rumande akisubiri hukumu. Akiwa gerezani Kamiti, alikuwa akiruhusiwa kupokea wageni kwa muda maalumu na kuhudhuria ibada Jumamosi. Sasa maisha yake yamebadilika rasmi. Yeye pamoja na washtakiwa wenzake Michael Oyamo, aliyekuwa msaidizi wake, na Caspal Ojang Obiero, aliyekuwa mfanyakazi wa Kaunti ya Migori, wataanza kutumikia vifungo vyao. Mlinzi mmoja wa gereza la Kamiti aliambia Taifa Leo kuwa baada ya kuhukumiwa, watatu hao watafuata taratibu za wafungwa waliopatikana na hatia. Watavua nguo zao za kawaida na kupewa sare za gerezani zinazojulikana kama "zebra". Pia watasajiliwa, kunyolewa, kupewa nambari za wafungwa na kupangiwa seli. Vilevile, watapewa majukumu ya kufanya gerezani kama wafungwa wengine. Idara ya Magereza inaweza kuwahamishia vituo vingine kama Naivasha, Manyani, Kisumu au Shimo la Tewa. Kwa sasa, maisha ya aliyekuwa gavana hayatatawaliwa tena na ratiba za ofisi ya kisiasa, bali sheria za gereza, kazi atakazopangiwa na muda wa kifungo. Hata hivyo, mawakili wake wamesema watakata rufaa, hivyo bado kuna uwezekano wa mahakama ya rufaa kubadilisha hukumu hiyo.
read moreRight Column Content