T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 03 Sep 2026 03:55:28

Ruto aagiza sheria ipitishwe kuzuia wageni kufanya uchuuzi Kenya

RAIS William Ruto amesema kwamba haikubaliki kwa raia wa kigeni kuja nchini kufanya uchuuzi na biashara ndogo ndogo. Anasema wageni wana ruhusa ya kuwa wawekezaji pekee, sio kushindana na wenyeji katika biashara ndogo kama uchuuzi na maduka madogo madogo. Akizungumza baada ya kukutana na sehemu ya wafanyabiashara waliofanya maandamano wiki jana kulalamikia ushuru mpya wa KRA kuhusu shehena ya bidhaa za kutoka nje katika Ikulu ya Nairobi Jumatano, Rais aliagiza mawaziri husika kuharakisha mswada bungeni unaoharamisha aina fulani ya biashara kufanywa na raia wa kigeni. "Tuko na wafanyabiashara kutoka nchi zingine, wacha nisiseme nchi gani, wamekuja hapa na kuwa wachuuzi, wanauza duvets. Bw Mukwana na Lee Kinyanjui, tayari tuko na mswada bungeni kuhusu mambo ya biashara. Katika hiyo bill, tumesema kuna biashara mgeni hawezi kufanya hapa Kenya by law. Nataka mketi chini na hawa wafanyabiashara muangalie na tuzibe mianya yote. Isitokee kwamba mtu ametoka China na amekuja kuwa hawker au kuuza duka kidogo hapo. Ichungwa, you don't need any further instructions. Monday muamkie hiyo biashara. Hao wachuuzi wote wanafanya hii biashara kidogo kidogo wafunge na wasipofunga (ashangiliwa) tutafunga. Hatujajenga Investor Confidence ndio watu wakuje kuwa wachuuzi. Tumejenga Investor Confidence ndio watu wakuje kuwekeza," akasema Bw Ruto. Katika maandamano ya Agosti 28, 2026, waandamanaji walikusanyika katika eneo la Archives kabla ya kuelekea makao makuu ya KRA katika jengo la Times Tower katikati mwa jiji. Wafanyabiashara hao walisema mabadiliko ya kiwango kinachotumiwa kukadiria thamani ya bidhaa za uagizaji yameongeza gharama za biashara na kupunguza faida zao. Kwa mujibu wao, KRA imepandisha kiwango cha ukadiriaji kutoka 2.5m hadi 3.2m, hatua wanayodai imeongeza kwa kiasi kikubwa kodi inayolipwa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, hususan kutoka China. Walisema mabadiliko hayo yamesababisha ongezeko la takriban asilimia 28, huku thamani ya bidhaa kwa madhumuni ya kodi ikiongezeka kutoka Sh2.5 milioni hadi Sh3.2 milioni.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 25 minutes ago

Hivi ndivyo maisha ya Obado yatakuwa gerezani kwa miaka 25

Aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado aliingia katika chumba cha mahakama jijini Nairobi Ijumaa saa mbili na dakika arobaini na tano asubuhi akiwa amevalia suti ya buluu, shati jeupe, tai na viatu vyeusi vilivyong'arishwa. Wafuasi wake waliokuwa wamemsubiri walimkaribisha kwa jina Sibuor (Simba). Aliwajibu kwa kuinua mikono yote miwili akiwa amefungwa pingu. Lakini saa tano asubuhi, Jaji Cecilia Githua alipoanza kusoma hukumu, ukumbi ulitulia. Kwa takriban dakika 40, Obado alisikiliza bila kuonyesha hisia huku mahakama ikieleza nafasi yake katika mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno. Jaji alimweleza kuwa alikuwa mpangaji mkuu, mfadhili na mtekelezaji wa mpango wa kumuua Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26 na ujauzito wa miezi saba. Mahakama ilipohitimisha na kumhukumu miaka 25 jela, baadhi ya wafuasi wake walilia, huku wengine wakizungumza kwa lugha ya Dholuo wakionyesha kutoamini hukumu hiyo. Hata hivyo, baadhi walipiga makofi baada ya mawakili wake kutangaza kuwa watakata rufaa. Obado, ambaye sasa yuko katika miaka ya sitini, anaweza kuwa na zaidi ya miaka 90 atakapomaliza kifungo chake mwaka 2051, iwapo hukumu haitabadilishwa. Kwa siku 123 tangu apatikane na hatia, alikuwa amezuiliwa rumande akisubiri hukumu. Akiwa gerezani Kamiti, alikuwa akiruhusiwa kupokea wageni kwa muda maalumu na kuhudhuria ibada Jumamosi. Sasa maisha yake yamebadilika rasmi. Yeye pamoja na washtakiwa wenzake Michael Oyamo, aliyekuwa msaidizi wake, na Caspal Ojang Obiero, aliyekuwa mfanyakazi wa Kaunti ya Migori, wataanza kutumikia vifungo vyao. Mlinzi mmoja wa gereza la Kamiti aliambia Taifa Leo kuwa baada ya kuhukumiwa, watatu hao watafuata taratibu za wafungwa waliopatikana na hatia. Watavua nguo zao za kawaida na kupewa sare za gerezani zinazojulikana kama "zebra". Pia watasajiliwa, kunyolewa, kupewa nambari za wafungwa na kupangiwa seli. Vilevile, watapewa majukumu ya kufanya gerezani kama wafungwa wengine. Idara ya Magereza inaweza kuwahamishia vituo vingine kama Naivasha, Manyani, Kisumu au Shimo la Tewa. Kwa sasa, maisha ya aliyekuwa gavana hayatatawaliwa tena na ratiba za ofisi ya kisiasa, bali sheria za gereza, kazi atakazopangiwa na muda wa kifungo. Hata hivyo, mawakili wake wamesema watakata rufaa, hivyo bado kuna uwezekano wa mahakama ya rufaa kubadilisha hukumu hiyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Huu ndio ushahidi uliomfanya Obado kusukumwa jela miaka 25

Chuo Kikuu cha Rongo kilipokuwa kikifanya mahafali yake ya 11 mjini Migori Ijumaa, aliyekuwa gavana wa kwanza wa kaunti hiyo, Okoth Obado, alikuwa akihukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa mauaji ya mwanafunzi wa zamani wa chuo hicho, Sharon Otieno. Baada ya kuhudumu kwa miaka tisa akiwa na mamlaka makubwa kisiasa, Obado sasa anaanza maisha ya gerezani pamoja na aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa serikali ya kaunti ya Migori, Caspal Obiero. Obado na Oyamo walihukumiwa kifungo cha miaka 25 kila mmoja, huku Obiero akipewa miaka 18 kwa kuhusika katika njama ya kumuua Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26. Hukumu hiyo ilifunga rasmi kesi iliyokuwa ikifuatiliwa kwa karibu nchini kwa miaka minane.Usiku wa Septemba 3, 2018, Sharon, ambaye alikuwa na watoto watatu na ujauzito wa miezi saba, alitekwa nyara pamoja na mwandishi wa habari wa Nation Media Group, Barack Odour. Odour aliweza kutoroka kwa kuruka kutoka kwenye gari lililokuwa likienda kasi. Sharon hakubahatika. Baadaye mwili wake ulipatikana ukiwa na majeraha saba ya visu tumboni. Alifariki pamoja na mtoto aliyekuwa tumboni mwake. Mauaji hayo yalizua hasira kubwa nchini huku wananchi wakitaka haki itendeke. Katika uamuzi wake wa Julai 23, Jaji Cecilia Githua alisema kuwa ingawa hakukuwa na mtu aliyeshuhudia washtakiwa wakimuua Sharon, ushahidi uliowasilishwa mahakamani uliunganisha matukio yote na kuonyesha jinsi mauaji yalivyopangwa. "Ushahidi uliowasilishwa ulipounganishwa uliunda msururu kamili kiasi kwamba hapakuwa na njia nyingine ya kufikia hitimisho isipokuwa kwamba washtakiwa, kwa pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani, walitenda kosa hilo," alisema jaji. Kiini cha kesi ya upande wa mashtaka kilikuwa mzozo kuhusu ujauzito wa Sharon. Obado alitajwa kuwa baba wa mtoto huyo, lakini inadaiwa alitaka Sharon aiavye mimba huku yeye akisisitiza kuutunza ujauzito. Mama yake Sharon, Melinda Auma, aliambia mahakama kuwa binti yake alimweleza kuhusu mabadiliko ya ghafla katika tabia ya Obado. Alisema gavana huyo alianza kuepuka simu za Sharon, akasitisha msaada wa kifedha na kumpa Sh30,000 ili atoe mimba, lakini Sharon alikataa. Ushahidi wa mawasiliano kati ya wawili hao pia uliwasilishwa. Katika baadhi ya jumbe, Sharon alikuwa akimuuliza Obado kuhusu nyumba ya vyumba vitatu aliyokuwa ameahidi kununua Kisumu. Mahakama pia iliona picha za uchunguzi wa mtoto aliyekuwa tumboni mwa Sharon. Obado alipoonyeshwa picha hizo, alijibu, "Sawa sawa. Nakutakia kila la heri."Mwanahabari Odour aliambia mahakama kuwa Sharon alikuwa amemchezea rekodi za mazungumzo yake na Obado kwa lugha ya mama. Katika mazungumzo hayo, gavana huyo alidaiwa kumshinikiza atoe mimba na kuahidi kumpa pesa.Odour pia alieleza jinsi alivyovutwa katika mtego wa kukutana na Sharon na Oyamo katika Hoteli ya Graca mjini Rongo. Baadaye waliambiwa waingie kwenye gari aina ya Toyota Fielder. Gari lilipoanza kuondoka, Oyamo alishuka na wanaume wawili wakaingia nyuma, wakimzingira Sharon na Odour. Watekaji waliwaamuru watoe simu zao.Odour alitoroka kwa kuruka kutoka kwenye gari hilo, lakini Sharon akabaki mikononi mwa watekaji.Ushahidi wa simu na mawasiliano ya WhatsApp uliwasaidia wachunguzi kuunganisha watatu hao. Rekodi zilionyesha mawasiliano kati ya Obado, Oyamo na Obiero katika kipindi cha kabla na baada ya mauaji.Wachunguzi pia walifuatilia gari lililotumiwa katika utekaji nyara. Kampuni iliyokuwa imeweka kifaa cha kufuatilia gari hilo iliambia mahakama kuwa kifaa hicho kilizimwa siku ya tukio na kuwashwa tena siku iliyofuata. Gari hilo lilikuwa likitumika kama teksi na lilimilikiwa na Olivia Oloo, mke wa Obiero. Dereva wake, Jackson Otieno Gombe, alitoa ushahidi mahakamani. Oyamo alijisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Uriri siku iliyofuata, akidai kuwa alikuwa ametekwa na kuibiwa Sh270,000 za gavana. Hata hivyo, Odour alikuwa tayari ameripoti kutekwa kwake katika vituo vya polisi.Polisi walipopokea taarifa kuhusu Oyamo, alikamatwa akiandika taarifa yake na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Homa Bay. Baadaye mwili wa Sharon ulipatikana kichakani karibu na Mto Owade na Moses Onditi Oguta. Ugunduzi huo uliimarisha uchunguzi uliofanywa na kitengo cha mauaji cha DCI. Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 42 na vielelezo 81. Ushahidi huo ulijumuisha rekodi za simu, jumbe, taarifa za mashahidi na maelezo kuhusu gari lililotumiwa katika utekaji nyara. Obado alijitetea akisema alikuwa Nairobi wakati Sharon alipouawa. Hata hivyo, jaji alikataa maelezo hayo baada ya kuchunguza ushahidi uliounganisha washtakiwa na mpango huo. Katika kesi hiyo, aliyekuwa MCA wa Kanyadoto, Lawrence Obonyo Owour almaarufu Mulla, pia alitoa ushahidi. Alifariki Mei 2024 baada ya kuanguka mjini Homa Bay na kufikishwa hospitalini akiwa tayari amefariki. Familia yake ilisema alikuwa ameonekana mzima kabla ya kifo chake cha ghafla, na polisi wakaanzisha uchunguzi kuhusu kilichosababisha kifo chake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Masaibu ya Mackenzie yazidi, apatikana na hatia ya kuua watu 123 kwa kuwanyima chakula

Kiongozi wa dhehebu la Good News International, Paul Mackenzie, amepatikana na hatia ya kuua watu 123 kwa kuwashawishi kufunga hadi kufa katika Msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi. Hata hivyo, Mahakama Kuu ilimwachilia huru katika mashtaka mengine 115 yaliyohusisha vifo vya waathiriwa wengine, ikisema upande wa mashtaka haukuthibitisha chanzo cha vifo hivyo bila shaka yoyote. Jaji Alex Ithuku alisema Mackenzie ndiye aliyepanga mpango wa kufunga, akatoa maagizo kuhusu nani angekufa kwanza na kuelekeza wafuasi wake kwenda maeneo yaliyofichwa ili wasifuatiliwe. Mahakama ilisikiliza ushahidi wa mashahidi waliosema Mackenzie mwenyewe alitangaza maagizo ya kufunga na mpangilio wa vifo. Aliwaambia wafuasi kuwa angekuwa wa mwisho kufa, lakini yeye aliendelea kula huku wengine wakiteseka kwa njaa. Pia alikataza wafuasi kuomba chakula kutoka kwa majirani. Watoto waliotoroka maeneo ya kufungia walirudishwa kwake, huku mmoja akipigwa kwa kujaribu kutoroka. Jaji alisema Mackenzie pia aliamuru miili ihamishwe polisi walipokaribia makazi hayo, na alikataa kuruhusu mwili wa mwanamke aliyefariki upelekwe nyumbani kwao kwa mazishi. Mahakama ilikataa madai kuwa vifo vilitokana na ukame, umaskini au uamuzi wa watu kufunga kwa hiari. Ilibainika kuwa chakula kilikuwepo katika baadhi ya nyumba, huku bwawa la maji likiwa na maji. "Watu hawafi kwa njaa kando ya bwawa lililojaa maji na ghala lenye chakula kwa bahati mbaya," alisema Jaji Ithuku. Hata hivyo, jaji alisisitiza kuwa kupatikana kwa mwili msituni hakumaanishi moja kwa moja kuwa mtu huyo alikufa kwa njaa. Kila kifo kilihitaji ushahidi wake. Alisema kuwa mshiriki wa dhehebu hilo, kuishi Shakahola au kuhudhuria mikutano ya Mackenzie si kosa la jinai. Kila mshtakiwa lazima ahukumiwe kutokana na vitendo vyake binafsi. Mahakama ilisema waliozuia watu kutoroka, kuwanyima chakula au kuwazuia waokoaji wanaweza kuwajibishwa. Wazazi waliowanyima watoto chakula wakijua wanakufa kwa njaa pia wanaweza kuwajibika kwa vifo vyao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Obado kula maharagwe jela miaka 25 kwa mauaji ya Sharon Otieno

Aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado amehukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno na mtoto wake ambaye hakuwa amezaliwa mwaka 2018. Mahakama Kuu ya Milimani pia ilimhukumu aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi Michael Juma Oyamo kifungo cha miaka 25, huku aliyekuwa mfanyakazi wa serikali ya kaunti ya Migori Caspal Ojwang Obiero akifungwa miaka 18. Hukumu hizo zilitolewa na Jaji Cecilia Githua jana. Sharon alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Rongo akisomea stashahada ya afya ya tiba. Alikuwa na ujauzito wa miezi saba alipopatikana ameuawa Septemba 2018. Pia alikuwa na watoto watatu kutokana na uhusiano wake wa awali. Mamake Sharon, Melinda Auma Rangili, aliambia mahakama kuwa bintiye alikuwa amemweleza kuwa Obado ndiye aliyempa mimba. Uchunguzi wa DNA ulithibitisha kuwa Obado ndiye baba wa mtoto huyo, jambo ambalo alikubali mahakamani. Alisema alikuwa na uhusiano na Sharon na kwamba mtoto aliyekuwa amebeba tumboni alikuwa wake. Katika uamuzi uliotolewa Julai 23, mahakama iliwapata wanaume hao watatu na hatia ya mauaji baada ya kusikiliza mashahidi 42 wa upande wa mashtaka na kupokea vielelezo 81. Jaji Githua alikubaliana na ushahidi wa upande wa mashtaka kuwa Obado ndiye aliyekuwa na sababu ya kupanga mauaji hayo na kutoa fedha, Oyamo alisaidia kutekeleza mpango huo, huku Obiero akitoa msaada wa usafirishaji na kuficha uhalifu huo. "Nimeridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha bila shaka yoyote kuwa washtakiwa, kwa pamoja na watu wengine ambao hawako mbele ya mahakama, walisababisha kifo cha marehemu Sharon Belyne Otieno kwa nia ya kutekeleza uhalifu huo," alisema Jaji Githua katika uamuzi wake wa kuwapata na hatia. Mahakama ilikataa hoja za utetezi kuwa tofauti katika maelezo ya mashahidi zilidhoofisha kesi ya upande wa mashtaka. Ilisema tofauti hizo hazikuathiri ushahidi mkuu uliowaunganisha washtakiwa na kutekwa nyara na kuuawa kwa Sharon. Kulingana na ushahidi uliowasilishwa, Sharon alikuwa ametafuta msaada wa Obado kwa miezi kadhaa. Alikuwa ametumia mwandishi wa habari na mtu wa kati kuwasiliana naye, huku mikutano ikipangwa Nairobi na Homa Bay. Hata hivyo, mahakama ilisema mkutano uliopangwa Septemba 3, 2018 ulitumika kuwezesha kutekwa kwake. Mwandishi wa habari aliyekuwa ameandamana na Sharon kwenye mkutano huo alifanikiwa kutoroka kwa kutoka kwenye gari  likiendeshwa. Aliripoti tukio hilo, na maelezo yake yaliungwa mkono na mashahidi waliomuona akiwa amejeruhiwa na kumsaidia baada ya kutoroka. Wazazi wa Sharon waliomba mahakama impe Obado adhabu isiyohusisha kifungo gerezani, wakisema familia yake ilikuwa imeomba msamaha na kwamba walikuwa wamemsamehe. Mamake Sharon alisema watoto watatu wa marehemu wanahitaji msaada na kuwa Obado angeweza kusaidia kuwalea iwapo angepewa adhabu ya nje ya gereza. Alisema kifungo cha maisha au hukumu ya kifo kingekuwa sawa na kupoteza mtu mwingine katika familia yao. Babake Sharon, Douglas Zakaria Otieno, pia alisema familia yake ilikubali maridhiano na familia ya Obado, lakini akatoa hasira zake dhidi ya Oyamo na Obiero. Akizungumza kupitia mkalimani wa lugha ya Dholuo, aliwashutumu wawili hao kuwa miongoni mwa watu wa mwisho kukutana na bintiye kabla ya kuuawa. Alizidiwa na hisia na kulazimika kusitisha hotuba yake kwa muda. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulisema maoni ya wazazi hayapaswi kuwa msingi pekee wa kuamua adhabu. Wakili wa serikali Wangui Gichuhi alisema maoni ya familia yanapaswa kuzingatiwa, lakini kosa hilo lilikuwa dhidi ya Serikali na jamii kwa jumla. Alisema adhabu inapaswa kuzuia uhalifu kama huo na kudumisha imani ya umma katika mfumo wa haki. Upande wa mashtaka pia ulisema hukumu ya kifo bado inaruhusiwa kisheria katika kesi zinazostahili, licha ya uamuzi wa Mahakama ya Juu uliopinga utoaji wa hukumu hiyo moja kwa moja bila kuzingatia mazingira ya kesi. Mawakili wa Obado waliomba mahakama izingatie, hali yake ya kiafya, muda aliokaa kizuizini na jinsi alivyofuata masharti ya dhamana wakati wa kesi. Pia walitaja maridhiano kati ya familia hizo na kuomba apewe adhabu ya nje ya gereza chini ya usimamizi. Mawakili hao walisema wazazi wa Sharon walikuwa wamekubali kuwa Obado aliwasaidia watoto na familia baada ya kifo cha binti yao. Waliomba mahakama iamuru utaratibu maalumu wa fidia ili kusaidia mahitaji ya watoto hao. Wakili wa Oyamo naye aliomba mteja wake apewe adhabu ya nje ya gereza, akisema ripoti iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha kuwa alikuwa anaheshimiwa katika jamii yake. Alisema familia yake ya watoto wanane inamtegemea na kuwa alikuwa ameonyesha majuto kupitia jamaa zake waliowasiliana na familia ya Sharon. Kwa upande wake, wakili wa Obiero aliomba mahakama imhurumie mteja wake na kumpa adhabu isiyohusisha kifungo gerezani, akitaja misiba na changamoto ambazo familia yake imepitia.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Ruto apewa miezi sita kurekebisha idara 7 alizoanzisha, ambazo sasa zimefutwa na korti

RAIS William Ruto amepewa miezi sita kurekebisha mchakato wa kuanzisha idara saba mpya za serikali baada ya Mahakama Kuu kutangaza kuwa uamuzi wa kuziunda ulikiuka Katiba na sheria. Jaji Roselyne Aburili alibatilisha uamuzi wa Rais wa Machi 2025 ulioongeza idara za serikali kutoka 51 hadi 57, katika kipindi cha kuundwa kwa serikali jumuishi kufuatia makubaliano ya kisiasa kati yake na aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga. Hata hivyo, jaji huyo alisimamisha utekelezaji wa uamuzi huo kwa miezi sita kuanzia Novemba 26, ili serikali iweze kufuata utaratibu unaotakiwa. Isipofanya hivyo, agizo la kubatilisha kuundwa kwa idara hizo litaanza kutekelezwa moja kwa moja. Idara hizo ni Usimamizi wa Uwekezaji na Mali za Umma, Uratibu wa Serikali ya Kitaifa, Haki na Masuala ya Katiba, Sayansi na Utafiti, Usafiri wa Anga, Mipango Maalum na Huduma za Ustawi wa Watoto. Kesi hiyo iliwasilishwa na Francis Njoroge Machi 22, 2025, akisema serikali haikushirikisha wananchi kabla ya kuanzisha idara hizo, kama inavyotakiwa na Katiba. Jaji Aburili alisema Rais ana mamlaka ya kupanga muundo wa serikali, lakini lazima afuate masharti ya kisheria, yakiwemo kushirikisha Tume ya Utumishi wa Umma (PSC). Mahakama ilisema serikali haikutoa ushahidi kuwa tume hiyo ilihusika katika mchakato huo au kuwa wananchi walipata nafasi ya kutoa maoni kabla ya idara kuundwa. Jaji alisema kuhusishwa kwa wananchi wakati wa Bunge kuidhinisha walioteuliwa makatibu wakuu hakukutosheleza hitaji la kushirikisha umma kuhusu kuanzishwa kwa ofisi hizo. Mahakama ilisema serikali lazima ionyeshe mahitaji ya kuunda idara hizo, majukumu yake na gharama zake kabla ya kuanzishwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Obado ataangushiwa hukumu ipi? Wazazi wa Sharon wawasili Nairobi kusikiza uamuzi

WAKAZI wa kaunti za Migori na Homa Bay wanatazamia kwa hamu hukumu itakayotolewa leo, dhidi ya aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado na washirika wake wawili waliopatikana na hatia ya mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno. Obado, aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa kaunti hiyo Caspal Obiero, walipatikana na hatia Julai 23, 2026, baada ya kesi iliyodumu kwa miaka minane. Katika Kaunti ya Migori, ambako watatu hao walikuwa na ushawishi mkubwa, wakazi wana maoni tofauti kuhusu adhabu wanayostahili. Baadhi wanataka hukumu kali huku wengine wakitaka mahakama iwaonee huruma. Hali ni hiyo hiyo Homa Bay, nyumbani kwa Sharon, ambako wazazi na jamaa zake wanasubiri haki itendeke kwa binti yao. Wazazi wa Sharon wamewasili Nairobi kuhudhuria kikao cha hukumu hiyo. Baba yake, Douglas Otieno, alisema familia itakubali uamuzi wowote wa mahakama. "Tulianza safari usiku na kufika asubuhi ili tuweze kufika mahakamani kwa wakati. Kesi hii imedumu miaka minane, ambayo imekuwa mateso kwangu," alisema. Mama yake Sharon, Melida Auma, aliomba mahakama Septemba 16 impatie Obado adhabu isiyohusisha kifungo gerezani. Alisema familia imemsamehe na haitaki ahukumiwe kifo au kifungo cha maisha. Alisema Sharon aliacha watoto watatu na kumtaka Obado kutimiza ahadi zake za kuwasaidia kupata makazi na mahitaji. Hata hivyo, wazazi hao walitaka Oyamo na Obiero waadhibiwe kwa mujibu wa sheria. Katika hukumu yake, Jaji Cecilia Githua alisema Obado alitoa sababu na fedha zilizowezesha mauaji hayo, Oyamo alisaidia kutekeleza mpango huo huku Obiero akitoa usaidizi wa vifaa na kuficha uhalifu. Obado aliomba msamaha akitaja umri, afya na kuwa hajawahi kupatikana na hatia awali. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga familia kuamua adhabu, ukisema uzito wa kosa lazima uzingatiwe. Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26 na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, alitekwa Septemba 3, 2018. Mwili wake ulipatikana siku iliyofuata katika msitu wa Kodera, Homa Bay. Alikuwa na ujauzito wa miezi saba. Uchunguzi ulionyesha uwezekano wa asilimia 99.99 kuwa Obado alikuwa baba wa mtoto huyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Magenge yenye mapanga yatia hofu wakazi Pwani yakipiga na kuibia boda pikipiki

WAKAZI wa maeneo mbalimbali ya Pwani wameingiwa na hofu kutokana na ongezeko la mashambulizi ya magenge yanayotumia mapanga, wizi wa pikipiki na uporaji, hasa nyakati za usiku. Mjini Mombasa, waendesha bodaboda katika maeneo ya Kisauni na Likoni wanasema wahalifu huwarai hadi maeneo yaliyotengwa, kisha kuwashambulia na kuwaibia pikipiki, simu na vitu vingine vya thamani. Shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa limeonya kuwa maeneo ya Likoni na Kisauni yamekuwa hatari kutokana na mashambulizi yanayotokea hata mchana. Shirika hilo limehusisha hali hiyo na ukosefu wa taa za barabarani na kamera za CCTV, likisema giza huwapa wahalifu nafasi ya kushambulia na kutoroka bila kutambuliwa. Ndani ya wiki moja, angalau waendesha bodaboda wanane waliripotiwa kushambuliwa na kujeruhiwa Kisauni, hasa Mshomoroni, Barsheba na Bakarani. Septemba 15, Said Faiz Khamis alishambuliwa na kundi la zaidi ya watu 10 waliokuwa na silaha eneo la Barsheba saa tano usiku. Alijeruhiwa kichwani na vidoleni huku pikipiki yake ikipatikana baadaye katika kituo cha polisi cha Kiembeni. Alisema awali alikuwa ameibiwa pikipiki nyingine na simu karibu na Kongowea. Siku iliyofuata, mwendesha bodaboda Chai Chivatsi alishambuliwa Bakarani na kujeruhiwa vidole, huku pikipiki yake ikiibwa. Hali hiyo imewalazimu baadhi ya waendesha bodaboda kusita kufanya kazi usiku, wakihofia kupoteza maisha na mali yao. Wakazi pia wamelalamikia wahalifu wanaotumia tuk-tuk kuwavizia abiria. Inadaiwa washukiwa hujifanya abiria wa kawaida kabla ya kumzingira mtu, kumuibia na wakati mwingine kumlewesha kwa dawa za kulevya. Hofu iliongezeka Oktoba 26 baada ya kundi la vijana wapatao 40 waliokuwa na silaha kuvamia kituo cha ukusanyaji ushuru cha Kaunti ya Mombasa, Likoni, na kumuua afisa wa kaunti Omari Mzerera. Walijeruhi pia afisa mmoja wa Polisi wa Utawala na maafisa wawili wa kaunti, kisha wakatoroka na bunduki aina ya AK-47. Mbunge wa Likoni Mishi Mboko alitaka uchunguzi wa kina, akisema washambuliaji hawakuiba kompyuta wala simu, bali walichukua bunduki pekee. Utafiti wa Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu wa mwaka 2025 ulitaja Mombasa kuwa na magenge mengi zaidi kati ya kaunti 11 zilizochunguzwa, ikiwa na 73. Nairobi ilikuwa na 56 na Kilifi 47. Hata hivyo, takwimu za Shirika la Kitaifa la Takwimu zinaonyesha kuwa makosa yaliyoripotiwa polisi Mombasa yalipungua kutoka 2,689 mwaka 2024 hadi 2,541 mwaka 2025. Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Mohamed Nur alisema karibu washukiwa 200 wamekamatwa katika operesheni za usalama. Alisema baadhi ya wafungwa wanaomaliza vifungo hurudia uhalifu na akataka vijana hao wapewe mafunzo ya ujuzi ili kuwasaidia kujikimu. Alisema polisi wanaendelea kuchunguza mauaji ya afisa huyo na wanachunguza vidokezo kadhaa, huku akiomba wakazi kutoa taarifa zitakazosaidia kuwakamata wahusika. Kwa waendesha bodaboda na wakazi wanaotegemea kusafiri usiku, swali kuu ni iwapo wataweza kuendelea na shughuli zao bila kuhatarisha maisha yao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 27 Nov 2026 04:55:20

Kioni ajiuzulu, 'amwachia' Matiang'i Jubilee akigusia kujiundia chama chake

CHAMA cha Jubilee kimepata mabadiliko mapya baada ya naibu kiongozi wake Jeremiah Kioni kujiuzulu, akihitimisha uhusiano wake wa kisiasa wa miaka 11 na chama hicho kinachojiandaa kufanya mkutano maalumu wa wajumbe wiki ijayo. Bw Kioni, aliyewahi kuwa Mbunge wa Ndaragwa na katibu mkuu wa zamani wa Jubilee, alitangaza kuondoka Alhamisi, siku moja baada ya chama kutoa notisi ya kuitisha Mkutano Maalumu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) Desemba 3 katika Jockey Club, barabara ya Ngong, Nairobi. Mkutano huo unatarajiwa kujadili ripoti za vitengo mbalimbali vya chama, kuchagua na kuidhinisha viongozi wa kitaifa, pamoja na mapendekezo ya mabadiliko ya katiba ya Jubilee. Hatua hiyo inajiri huku chama hicho kikiendelea na mabadiliko ya uongozi chini ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang'i, ambaye anajiandaa kuwania urais katika uchaguzi wa 2027. Katika barua yake ya kujiuzulu, Bw Kioni alisema uamuzi wake umetokana na kutafakari safari yake ya miaka 11 ndani ya Jubilee, akieleza kuwa chama hicho kilikuwa kama nyumbani kwake na kilimpa nafasi ya kuwatumikia Wakenya. "Imekuwa miaka 11, safari ndefu na muhimu katika maisha yangu, ambayo naweza kuwa tayari kuipitia tena," alisema. Alimshukuru Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa uongozi na urafiki wao, akisema uhusiano wao ulivuka mipaka ya siasa. Pia aliwashukuru wanachama wa Jubilee kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuwa katibu mkuu kwa miaka minne na naibu kiongozi wa chama kwa karibu mwaka mmoja. Alisema nyadhifa hizo zilimfundisha unyenyekevu, subira na umuhimu wa kuheshimu taasisi. Bw Kioni pia alimtakia Dkt Matiang'i mafanikio katika kuongoza chama hicho na kampeni zake za kuwania urais. Kuondoka kwake kunafuatia mabadiliko ya uongozi yaliyoanza Januari mwaka huu, alipohamishwa kutoka wadhifa wa katibu mkuu na kuwa naibu kiongozi wa chama. Aliyekuwa Mbunge wa Narok Kaskazini, Moitalel Ole Kenta, aliteuliwa kuchukua nafasi ya katibu mkuu. Mabadiliko hayo yaliendelea Septemba baada ya Bw Kenyatta kuacha uongozi wa Jubilee na kumkabidhi Dkt Matiang'i, akisalia mwanachama na mshauri wa chama. Bw Kioni alikuwa ametangaza nia ya kumrithi Bw Kenyatta, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuchaguliwa kidemokrasia na wajumbe badala ya kukabidhiwa mamlaka. Wiki iliyopita, alidokeza uwezekano wa kuondoka Jubilee, akisema hakuwa akishirikishwa katika shughuli za kisiasa za Dkt Matiang'i wala kupewa majukumu maalumu licha ya kuwa naibu kiongozi. Alisema awali alitarajia kushirikiana na Dkt Matiang'i, ambapo waziri huyo wa zamani angejikita katika azma ya urais huku yeye akijenga chama. Katika barua yake, Bw Kioni alifafanua kuwa kuondoka Jubilee hakumaanishi mwisho wa safari yake ya kisiasa. "Kuondoka kwangu si kuaga maisha ya umma wala mwisho wa safari yangu ya kisiasa. Ninapojiandaa kuzindua jukwaa jingine, ninachukua mafunzo na urafiki wa miaka hii 11 katika hatua inayofuata," alisema. Mkutano wa Desemba 3 unatarajiwa kurasimisha mabadiliko ya uongozi na kuweka msingi wa Jubilee kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 27 Nov 2026 04:25:49

ODM mambo ni matatu tu kuhusu 2027

CHAMA cha ODM kinakabiliwa na chaguo tatu: kumuunga mkono Rais William Ruto kuwania muhula wa pili, kuungana na viongozi wa upinzani au kushiriki kivyake katika uchaguzi wa 2027. Uongozi wa ODM umeweka Januari 31, 2027 kuwa tarehe ya mwisho ya kukamilisha mazungumzo na UDA kuhusu uwezekano wa kuunda muungano rasmi. Uamuzi huo ulitangazwa Jumatano baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Usimamizi ya chama hicho, huku viongozi wakisema wanataka mazungumzo hayo yakamilike mapema ili kutoa nafasi ya kupanga mikakati ya uchaguzi. Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohamed, alisema timu inayoshughulikia sera na manifesto za vyama hivyo itaharakisha kazi ili kutoa ripoti ifikapo Januari 31. Alisema ripoti hiyo itafafanua masuala na sera zitakazotumika kuunda muungano na UDA. Hatua hiyo inajiri huku baadhi ya viongozi wa ODM wakilalamikia kutoheshimiwa na kutotambuliwa kwa mchango wa chama hicho katika serikali jumuishi. Rais Ruto na kiongozi wa ODM Oburu Oginga tayari wameunda kamati ya kiufundi inayolenga kuunganisha manifesto za vyama hivyo kabla ya kutia saini makubaliano rasmi. Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Nyanza wanataka Rais Ruto akutane nao haraka ili kujadili masharti ya kumuunga mkono, ikiwemo ugavi wa maeneo ya kisiasa na nafasi ambazo ODM itanufaika nazo. Mbunge mmoja aliambia Taifa Leo kuwa chama hicho kina wasiwasi kuwa kinaendelea kuunga mkono serikali huku baadhi ya maafisa wakifanya kazi ya kukidhoofisha kisiasa. Alisema ODM inataka uhakika kuhusu manufaa ya kumuunga mkono Rais Ruto, badala ya kuonekana kuwa kinaiunga mkono bila kupata chochote. Hata hivyo, alisema chama hakitishwi na wimbi la chama cha MDG, akisema Dkt Oburu ameahidi uteuzi wa haki ambapo wagombea wenye nguvu watapata nafasi na uamuzi wa wananchi kuheshimiwa. Oburu tayari ametangaza kuwa ODM haitakuwa na mgombea wa urais mwaka 2027 na badala yake itamuunga mkono Ruto. Mnamo Julai 12, 2026, alisema chama hicho kitashiriki katika uchaguzi nyuma ya Rais Ruto ili kumwezesha kuhudumu kwa muhula wa pili. Hata hivyo, alisisitiza kuwa ushirikiano huo lazima uwe na muundo unaohakikisha ODM inapata nafasi serikalini na sera zake kuingizwa katika ajenda ya serikali. Mchambuzi wa siasa Profesa Masibo Lumala anaamini ODM haina nafasi kubwa ya kubadili msimamo na kusimamisha mgombea urais. Alisema migawanyiko ya ndani na ukosefu wa viongozi wenye ushawishi wa kutosha vimedhoofisha uwezo wa chama kujadiliana na UDA. Alitaja kuondoka kwa James Orengo, Babu Owino na Edwin Sifuna na kujitenga kwa Profesa Anyang' Nyong'o na siasa za kila siku, kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia pengo la uongozi. Lakini Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi, anasema ODM haina njia nyingine isipokuwa kuendelea kushirikiana na Ruto. Alisema chama hicho hakiwezi kuungana na makundi hasimu ya kisiasa yanayoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Wakati huohuo, Seneta wa Narok Ledama Ole Kina amewataka viongozi wa ODM kuketi pamoja na kukubaliana kuhusu mwelekeo wa chama. Alisema wakati umefika wa kuacha kujificha nyuma ya makundi ya kisiasa na badala yake kufanya mazungumzo ya wazi kuhusu umoja na mustakabali wa chama. Ndani ya ngome ya Nyanza, baadhi ya viongozi, akiwemo Waziri wa Hazina John Mbadi, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, wanataka ODM ipate mgao wa 50-50 katika ushirikiano huo. Pia, chama hicho kinataka wadhifa wa Naibu Rais uwe sehemu ya makubaliano ya kugawana mamlaka. Hata hivyo, Atandi amewataka viongozi kutofanya kiti hicho kuwa sharti la kumuunga mkono Ruto, akisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuchagua mgombea mwenza wake. Mbadi ana matumaini kuwa makubaliano rasmi yatatiwa saini Februari mwaka ujao. Mchambuzi wa siasa Javas Bigambo anasema migawanyiko hiyo inatokana pia na tamaa za uongozi na hofu ya ushindani katika kipindi cha baada ya kifo cha Raila Odinga. Alisema baadhi ya wanasiasa wanajaribu kujitwalia nafasi ya Raila, huku wengine wakitumia kutokuwepo kwake kupinga maamuzi ya chama. Bw Bigambo aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wanatumia MDG kama kisingizio cha hofu yao kuhusu uteuzi, huku ODM ikijaribu kulinda ushawishi wake Nyanza baada ya Raila.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 27 Nov 2026 03:55:22

Linda Mwananchi yapigwa na baridi bila Sifuna aliye ziarani Amerika

SAFARI ya Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna nchini Amerika imevuruga kwa muda mikakati ya mrengo wa Linda Mwananchi, ambao ulikuwa umeanza kupata umaarufu kupitia mikutano ya hadhara na shughuli za kujijenga mashinani. Kutokuwepo kwa Seneta Sifuna, ambaye ndiye sura kuu ya vuguvugu hilo, sasa kunatoa mtihani wa kwanza kuhusu uwezo wa viongozi wake kuendeleza hamasa kwa wafuasi bila yeye kuwepo. Hali hii inajiri huku Rais William Ruto akizidisha kampeni zake katika eneo la Magharibi mwa Kenya, ambako anaanza ziara ya siku nne kesho. Sifuna alianza ziara yake Amerika Novemba 20, akikutana na Wakenya wanaoishi ughaibuni kwa lengo la kuchangisha fedha za kufadhili shughuli za kisiasa za Linda Mwananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Ziara hiyo inatarajiwa kukamilika Desemba 7. Alisafiri na ujumbe wa viongozi kadhaa, akiwemo Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na mkuu wa mawasiliano wa vuguvugu hilo Pauline Njoroge. Hata hivyo, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka, Mbunge wa Funyula Oundo Mudenyo na aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo waliachwa nchini. Mkutano mkubwa wa mwisho wa Linda Mwananchi ulifanyika Ukunda, Kaunti ya Kwale, Oktoba 31. Tangu wakati huo, shughuli nyingi za vuguvugu hilo zimeonekana kupungua, huku viongozi wake wakisubiri kurejea kwa Sifuna. Baadhi ya viongozi walioonekana kuwa washirika wake wa karibu wameendelea na shughuli zao binafsi za kisiasa. Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino amekuwa akifanya mikutano yake jijini Nairobi, huku Gavana wa Siaya James Orengo akijiunga na mrengo wa unaohusishwa na Fred Matiang'i, Ndindi Nyoro na Martha Karua, akipigia debe chama chake cha Liberal Democratic Party (LDP). Wakati huo, viongozi wengine wa upinzani wameendelea na mikutano ya kutafuta uungwaji mkono kivyao. Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua mnamo Alhamisi alifanya mikutano Kamukunji, Mathare na maeneo mengine ya Eastlands jijini Nairobi, akitangaza chama chake cha DCP. Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka naye alifanya mikutano katika eneo bunge la Mwala mwishoni mwa wiki, akiendeleza kampeni za kuwania urais katika ngome yake ya Ukambani. Katika eneo la Magharibi, Natembeya, ambaye ndiye mwakilishi mkuu wa Sifuna, amekuwa akijikita zaidi katika shughuli za kisiasa za Kaunti ya Trans Nzoia. Akizungumza na Taifa Leo, gavana huyo alisema mikutano ya Linda Mwananchi itarejea Sifuna atakaporejea kutoka Amerika. Alisema kwa sasa vuguvugu hilo linaangazia kupata uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya wanaoishi ughaibuni, lakini akasisitiza kuwa shughuli za kisiasa haziishii katika mikutano ya hadhara. Alisema dhamira yao bado ni kushiriki katika uongozi wa nchi baada ya uchaguzi wa 2027 na kwamba ujumbe wa Sifuna Amerika umepokelewa vyema. Hata hivyo, kutokuwepo kwa Sifuna kumeambatana na kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa kati ya viongozi wa upinzani Magharibi. Mnamo Alhamisi, kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa alitangaza kumwondoa Natembeya katika nafasi ya naibu kiongozi wa chama, pamoja na Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula, ambaye ameonyesha kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi ujao. Wamalwa alisema Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya amependekezwa kuchukua nafasi ya Natembeya na atathibitishwa katika kikao cha Baraza Kuu la Kitaifa la chama (NEC) wiki ijayo. Wamalwa na Natembeya wamekuwa na uhusiano wenye misukosuko kutokana na mvutano kuhusu nani anayepaswa kuwakilisha Magharibi katika meza ya mazungumzo ya upinzani. Natembeya amekuwa akimshutumu Wamalwa kwa kufanya njama kumdhoofisha Sifuna na kuzuia azma yake ya kuwania urais kupitia upinzani. Gavana huyo amemtaka Wamalwa kuacha kuwa kikwazo kwa Sifuna na badala yake ajitokeze kuwania ugavana wa Trans Nzoia. Hata hivyo, Wamalwa amepuuzilia mbali madai hayo, akisema hana pingamizi kwa Sifuna kuzingatiwa kama mgombea wa urais wa upinzani. Alisema upinzani unapaswa kuimarisha ushirikiano na kutafuta washirika katika maeneo mengine ya nchi badala ya kutegemea eneo moja pekee. Kwa upande wake, Natembeya alielezea kuondolewa kwake katika uongozi wa DAP-Kenya kuwa uamuzi bora zaidi ambao Wamalwa amewahi kufanya kisiasa. Alisema hajawahi kumuomba Wamalwa kumpa nafasi ya uongozi na kumtaka aendelee na shughuli zake za chama bila kumzuia.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 27 Nov 2026 02:55:28

Ngumi na mateke yatamba baina ya madiwani Kisumu katika jaribio la kung'oa Spika Oraro

VURUGU zilitokea katika Bunge la Kaunti ya Kisumu Alhamisi baada ya kundi la madiwani kuanzisha mchakato wa kumuondoa ofisini Spika Elisha Oraro, huku wenzake waliopinga wakijaribu kumlinda. Mzozo huo uligeuka mapigano ya mateke na makonde, huku Oraro akiondolewa kwa nguvu kutoka kwenye kiti chake. Tukio hilo lilianza baada ya madiwani kuuliza kwa nini hoja ya kumuondoa spika haikuwa kwenye ratiba ya shughuli za bunge iliyowasilishwa. MCA wa South West Nyakach Gard Olima na mwenzake wa East Kano Wawidhi Moses Ochele walitaka kujua kwa nini Oraro hakuwa akiongoza kikao kwa kutumia ratiba ya ziada iliyokuwa na hoja hiyo. Oraro alisema baada ya kushauriana na karani wa bunge, hakuwa amepokea ratiba hiyo ya ziada. Alisema ataheshimu uamuzi wa madiwani iwapo mchakato wa kumuondoa madarakani utafuata sheria na kanuni za bunge. Hata hivyo, jibu lake lilizua hasira na kundi la madiwani kuvamia kiti chake na kumtoa kwa nguvu. Baadhi ya waliopinga walijaribu kumkinga, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na mapigano yakazuka. Maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Kisumu Central walifika kujaribu kurejesha utulivu. Oraro aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi huku baadhi ya wananchi waliokuwa nje ya bunge wakimzomea na kumtishia. Jaribio lake la kurejea bungeni akiwa ameandamana na polisi lilizimwa na madiwani. Ochele aliteuliwa kuwa Kaimu Spika na kuongoza kikao kilichofanyika bila karani wala ratiba rasmi ya shughuli za bunge.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 26 Nov 2026 16:28:18

Wadau wataka kasi iongezwe katika juhudi za kukomesha ndoa za watoto

ULIMWENGU unapoadhimisha leo Siku ya Kukomesha Ndoa za Watoto, kwa mara ya kwanza baada ya kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa, washikadau wanataka kasi ya juhudi hizo iimarishwe ili kufikia malengo. Wadau tofauti wakiongozwa na shirika la Femnet, walisema kuwa kwa muda mrefu wameangazia juhudi za kibinafsi, lakini sasa kuna haja ya kuja pamoja na kuelekeza mikakati yao kwa wahusika ili kupata matokeo yatakayosaidia kuzima ndoa za watoto. Walishiriki warsha hiyo Novemba 26, 2026 katika hoteli ya Park In Radisson, Nairobi. Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban wasichana 12 milioni huozwa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18. Kusini mwa Asia ndiko kuna asilimia kubwa ya 44 ya watoto wasichana wanaoozwa mapema, huku Kusini mwa Jangwa la Sahara ikifuata na asilimia 18. Ingawaje, kulingana na Malengo Endelevu (SDGs), hatua ilikuwa kutimiza lengo hilo kufikia 2030, juhudi hizo zimeonekana kwenda pole pole, na sababu ya wito wa kasi hiyo kuongezwa. Akiongea katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Femnet Dkt Carole Agengo alisisitiza haja ya mashirika na wadau husika kuungana na kuleta fikra na juhudi zao pamoja ili kuweza kufanikisha lengo hilo. Mkurugenzi wa Wanawake, Jinsia, na Vijana katika Umoja wa Afrika, Bi Prudence Nonkululeko Ngwenya, pia alishikilia msimamo huo wa kuimarisha juhudi hizo, na watu kuelekea mashinani ambapo matukio hayo yanafanyika na kutafuta suluhu za kudumu. "Tunalazamika sasa kuondoka kutoka kwa ahadi za kuchukua hatua, na twende kwenye utekelezaji. Lazima tuwekeze kwa wasichana hawa kwa kuhakikisha kuwa wanasalia shuleni na kuimarisha uwajibikaji," alisema. Mwakilishi wa Idara ya Jinsia, Bi Verity Mghanga, alifafanua juhudi za serikali huku akisema kuwa kuna mengi ambayo bado yanastahili kufanywa. Alieleza kuwa licha ya juhudi hizo, mambo mengi bado yanafanywa kwa siri kubwa na kuhusisha jamii, kumaanisha kuwa jamii inakubali au kuvumilia desturi kama hiyo ya kuoza watoto. "Utapata katika baadhi ya jamii, msichana hata wa miaka saba anatumwa kuishi na familia fulani. Kisha anapotimiza umri fulani, anaelezwa kuwa alipelekwa hapo kwa kuwa yeye ni mke wa mzee wa boma," anasema akiongeza kuwa baadhi ya watoto hao pia hupitia maisha magumu kwa kuwa huenda katika familia walizoozwa kuna wake wengine wakubwa ambao wanawatumisha kazi nyingi za nyumbani bila kuzingatia umri wao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 26 Nov 2026 12:45:21

Vita vyazuka ndani ya Bunge la Kaunti ya Kisumu wakati wa jaribio la kutimua Spika Oraro

Vurugu zilitokea katika Bunge la Kaunti ya Kisumu Alhamisi baada ya kundi la madiwani kuanzisha mchakato wa kumuondoa ofisini Spika Elisha Oraro, huku wenzake waliopinga wakijaribu kumlinda. Mzozo huo uligeuka mapigano ya mateke na makonde, huku Oraro akiondolewa kwa nguvu kutoka kwenye kiti chake. Tukio hilo lilianza baada ya madiwani kuuliza kwa nini hoja ya kumuondoa spika haikuwa kwenye ratiba ya shughuli za bunge iliyowasilishwa. MCA wa South West Nyakach Gard Olima na mwenzake wa East Kano Wawidhi Moses Ochele walitaka kujua kwa nini Oraro hakuwa akiongoza kikao kwa kutumia ratiba ya ziada iliyokuwa na hoja hiyo. Oraro alisema baada ya kushauriana na karani wa bunge, hakuwa amepokea ratiba hiyo ya ziada. Alisema ataheshimu uamuzi wa madiwani iwapo mchakato wa kumuondoa madarakani utafuata sheria na kanuni za bunge. Hata hivyo, jibu lake lilizua hasira na kundi la madiwani kuvamia kiti chake na kumtoa kwa nguvu. Baadhi ya waliopinga walijaribu kumkinga, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na mapigano yakazuka. Maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Kisumu Central walifika kujaribu kurejesha utulivu. Oraro aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi huku baadhi ya wananchi waliokuwa nje ya bunge wakimzomea na kumtishia. Jaribio lake la kurejea bungeni akiwa ameandamana na polisi lilizimwa na madiwani. Ochele aliteuliwa kuwa Kaimu Spika na kuongoza kikao kilichofanyika bila karani wala ratiba rasmi ya shughuli za bunge. MCA wa Muhoroni Koru Vincent K'Omudho aliwasilisha hoja ya kumwondoa Oraro, akitaja sababu tano, zikiwemo usimamizi mbaya wa shughuli za bunge, ukosefu wa uongozi na kupuuza maslahi ya madiwani na wafanyakazi. Madiwani pia walimshutumu kwa kukosa uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za bunge. Aidha, walidai alishindwa kushughulikia malalamishi kuhusu marupurupu na mazingira ya kazi ya madiwani na wafanyakazi. MCA wa Kolwa Central Kelvin Oraro, aliyeunga mkono hoja hiyo, alidai Spika alihusika na kupandisha gharama ya miradi kutoka bajeti zilizoidhinishwa na bunge. Mzozo huo umeibua kumbukumbu za namna Oraro mwenyewe alivyopata wadhifa huo baada ya kuondolewa kwa mtangulizi wake, Onyango Oloo, katika mazingira ya vurugu na migawanyiko ya kisiasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 26 Nov 2026 15:07:15

EACC kushirikiana na wanahabari kuchunguza wagombeaji 2027

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) itaanzisha mfumo wa kuwapa wanahabari taarifa zitakazowawezesha kuchunguza uadilifu na sifa za wanaotaka nyadhifa za uchaguzi na uteuzi kabla ya uchaguzi wa 2027. Mwenyekiti wa EACC David Oginde alisema mpango huo utasaidia wanahabari kuchunguza historia, mwenendo na rekodi za wagombea badala ya kutegemea ahadi za kampeni na miungano ya kisiasa. Akizungumza katika mkutano wa tisa wa wahariri nchini, uliofanyika Travelers Beach Hotel, Mombasa, Alhamisi, Dkt Oginde alitaja vyeti ghushi, hongo ya wapiga kura, matumizi mabaya ya rasilimali za umma na ghasia za kisiasa kuwa baadhi ya maovu yanayohitaji uchunguzi zaidi. Alisema EACC itaimarisha ufuatiliaji na uchunguzi wa hongo ya wapiga kura, akiwataka wanahabari kuelimisha wananchi kuhusu madhara yake kwa demokrasia. "Hongo ya wapiga kura inadhoofisha uhuru wa wananchi kuchagua viongozi wao. Inageuza uamuzi muhimu wa kidemokrasia kuwa biashara," alisema. Pia aliwaonya maafisa wa umma dhidi ya kutumia magari, fedha, wafanyakazi na shughuli za serikali kujinufaisha kisiasa, akisisitiza kuwa wanaotaka kugombea lazima wajiuzulu angalau miezi sita kabla ya uchaguzi. Dkt Oginde alilaani matumizi ya vijana kuchochea ghasia na vitisho wakati wa kampeni, akisema wanaopanga na kufadhili vurugu lazima wawajibishwe. Rais wa Kenya Editors Guild Zubeida Kananu aliwataka wanahabari kuchunguza jinsi wagombea walivyoishi, walivyohudumu na wanavyofadhili kampeni zao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 26 Nov 2026 13:57:54

Pigo kwa Netanyahu bunge likiidhisha achunguzwe kuhusiana na shambulio la Hamas

JERUSALEM, Israel:  BUNGE la Israel limepiga hatua ya kwanza kuidhinisha mswada wa kuanzisha tume huru ya kuchunguza kushindwa kwa vyombo vya usalama kuzuia shambulizi la Hamas la Oktoba 7, 2023, ambalo lilikuwa baya zaidi katika historia ya taifa hilo. Hatua hiyo ni pigo kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambaye anapinga uchunguzi huru na badala yake anataka serikali ipewe mamlaka ya kuunda tume na kuteua wajumbe wake. Mswada huo ulipata uungwaji mkono wa wabunge 65 dhidi ya 50, huku ukiungwa mkono na kambi ya upinzani inayoongozwa na Gadi Eisenkot pamoja na vyama vinavyowakilisha jamii ya Waarabu. Hata hivyo, mswada huo unahitaji kupitishwa katika hatua nyingine tatu kabla ya kuwa sheria. Eisenkot, ambaye anajaribu kuunda serikali mpya baada ya muungano wa Netanyahu kupoteza wingi wa wabunge katika uchaguzi wa Oktoba 27, alisema ukweli lazima ujulikane ili kuzuia maafa kama hayo siku zijazo. "Kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, manusura wa utumwani na wale ambao hawakurejea wakiwa hai, tutafichua ukweli na kuchukua kila hatua kuzuia janga jingine," akasema katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii. Netanyahu anapinga tume huru akitaka uchunguzi utakaoongozwa na serikali, huku wapinzani wake wakidai hatua hiyo inalenga kuficha ukweli kuhusu uzembe uliosababisha shambulizi hilo. "Mswada huu utawachunguza wanajeshi wetu jasiri na mashujaa badala ya kumakinikia masuala ya kimsingi," akasema Waziri wa Uchukuzi Miri Regev, mshirika wa karibu wa Netanyahu, akikosoa mswada huo. Katika shambulizi hilo, wapiganaji wa Hamas waliwaua watu 1,200 na kuwateka nyara zaidi ya 250. Israel ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza, yaliyosababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 74,000 na kuwahamisha karibu wakazi wote milioni mbili wa eneo hilo. Wakati huo huo, Eisenkot anakabiliwa na changamoto ya kuunda serikali kabla ya Disemba 6, baada ya kambi yake kupata viti 48 dhidi ya 53 vya muungano wa Netanyahu katika bunge lenye viti 120. Iwapo atashindwa, Netanyahu anaweza kupewa nafasi nyingine ya kuunda serikali, la sivyo uchaguzi mwingine utafanyika.

read more