taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 03 Sep 2026 10:39:42
WHO yataka juhudi za kukabiliana na Ebola DRC ziharakishwe
WHO imesema Ebola bado ni changamoto na inahitaji rasilimali nyingi. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus,alisema Jumatano kwamba hadi kila maambukizi yatakapobainika na kukatizwa, ugonjwa huo utaendelea kuwa hatari DRC, nchi jirani na eneo lote. Idadi ya waliofariki kutokana na mkurupuko huo imevuka 3,000, kwa mujibu wa takwimu za serikali, huku ugonjwa huo ukiendelea kuenea kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo. Mkurupuko huo, unaosababishwa na aina ya kirusi cha Ebola cha bundibugyo, sasa ndio mkubwa na wenye vifo vingi zaidi katika historia ya DRC na imezidi mkurupuko uliotokea mnamo na 2018–2020. Tedros alisema vifo vingi vimetokea miongoni mwa watu ambao hawakuwa kwenye orodha ya waliokuwa wamewasiliana na wagonjwa, hali inayoashiria kuwepo kwa maambukizi mengi ambayo hayajulikani. Alisema mazishi yasiyofanywa kwa njia salama pia yanaendelea kuchangia kuenea kwa virusi hivyo. WHO imeomba kuongezwa kwa fedha za mpango wa kukabiliana na Ebola unaoongozwa na serikali ya Congo, unaohitaji dola bilioni 1.3 (Sh168 bilioni). WHO imetuma tani 320 za vifaa na kuongeza uwezo wa vipimo hadi 3,000 kwa siku, lakini inahitaji fedha zaidi kuongeza vitanda katika vituo vya matibabu.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
Ziara ya Ruto Nyanza yaacha makovu ODM
ZIARA ya siku tano ya Rais William Ruto Luo Nyanza wiki iliyopita iliacha makovu ya uhasama na mgawanyiko wa kisiasa kati ya baadhi ya viongozi wa eneo hilo hasa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2027 zinavyoendelea kunoga. Rais Ruto alifanya ziara ambayo ilionekana ilifana katika kaunti za Kisumu, Siaya, Migori na Homa Bay ambako alipigia debe azma yake ya kuwahi muhula wa pili. Hata hivyo, baada tu kuondoka, ziara hiyo imezua uhasama kati ya viongozi wa ODM ambao wanalumbana kuhusu siasa za eneo hilo. Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo Mabono alimchemkia Gavana Glady Wanga akidai ndiye alihusika na masaibu yake mbele ya Rais. Bi Odhiambo wiki hii alimfokea Gavana Wanga akidai alihusika na kuzomewa kwake katika mkutano ambao viongozi wa Luo Nyanza walikutana na Rais Ruto katika ikulu ndogo ya Kisumu. "Gladys Wanga nakuheshimu kama dadangu mdogo na mwenyekiti wa ODM lakini usichukulie hilo kama jambo la kawaida. Unawatuma watu waje wanidharau na kunishambulia katika eneobunge langu kisha unaketi kitako na kujifanya mzuri," akasema Bi Odhiambo. Mbunge huyo alitishia kuwa huenda akaendesha kampeni kali dhidi ya Bi Wanga iwapo ataendelea kuvamiwa kwenye mikutano anayoandaa sehemu mbalimbali ya Nyanza. "Nitakukabili, na pia nitawaambia watu hawa wasikupigie kura. Najua unajishasha kwa sababu Rais aliwaambia watu hawa wakupigie kura lakini Rais huwa hapigi kura hapa, "Mimi sijui vita vyovyote vya kujificha na ukiendelea nitaendeleza vita vikali dhidi yako," akaongeza Odhiambo. Mbunge huyo na Bi Wanga wamekuwa na uhusiano vuguvugu hasa kuhusu uongozi wa kaunti na siasa za kitaifa. Bi Odhiambo ni kati ya wabunge Luo Nyanza ambao wamekuwa vuguvugu akionekana kutounga mkono mrengo wa ODM unaoongozwa na Dkt Oburu Oginga au vuguvugu la Linda Mwananchi chini ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Katika mkutano wa Ikulu ndogo ya Kisumu, Bi Odhiambo alikuwa na wakati mgumu kuhutubu huku akipigiwa kelele na umati. "Alituma watu Kisumu wanizomee, akatuma watu pia katika eneobunge langu wanipigie kelele. Sitaendelea kumvumilia," akasema. Juhudi za kumtaka Gavana Wanga azungumzie madai hayo hazikufaulu ila gavana huyo amekuwa akionekana kuhepa kujibizana na mbunge huyo anayehudumu muhula wake wa nne. Kinaya ni kwamba majibizano hayo yanapoendelea kama Mwenyekiti wa ODM, Bi Wanga ndiye atatia saini cheti cha chama iwapo Bi Odhiambo atapewa tikiti ya kutetea kiti chake kupitia chungwa. Katika Kaunti ya Homa Bay, kuna ushindani mkali wa kiti cha ugavana mnamo 2027 huku Bi Wanga akikabiliwa na kivumbi dhidi ya aliyekuwa Naibu Gavana Oyugi Magwanga. Wawili hao walikosana mwaka jana, Bw Magwanga akajiuzulu na itakumbukwa mnamo 2022, marehemu Raila Odinga alitekeleza jukumu muhimu la kuwapatanisha. Kupitia kupatanishwa na Bw Odinga, Bi Wanga aliishia kugombea ugavana naye Bw Magwanga akikubali kuwa mgombeaji mwenza wake. Katika kaunti jirani ya Migori, ziara ya Rais Ruto imeacha uhasama mkali kati ya Mbunge wa Uriri Mark Nyamita na Gavana Ochilo Ayacko. Bw Nyamita ambaye anahudumu muhula wa pili kupitia ODM analenga ugavana 2027 kupitia chama hicho. Bw Ayacko naye analenga kutetea kiti chake pia kupitia ODM na wawili hao watakabiliana katika mchujo wa chama. "Kazi ya Bw Ayacko ilikuwa kununua vuvuzela kwa vijana ili wazipulize katika mikutano yake ndipo waone kuwa yeye ni maarufu. Baada ya mkutano wa Kisumu, hakuenda Siaya bali alirudi hapa Migori kuhakikisha kuwa vijana wanapewa malori matatu ya vuvuzela," akasema Bw Nyamita.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Ruto asema upinzani 'unampigia debe' kwa kukosoa miradi yake ya maendeleo
RAIS William Ruto amewajibu viongozi wa upinzani wanaokosoa rekodi yake ya maendeleo akisema kwa kufanya hivyo wanasaidia kuitangaza miradi yake kwa wananchi bila malipo. Akizungumza mjini Wundanyi, Kaunti ya Taita Taveta, Jumamosi, Rais Ruto alisema ataendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kote nchini licha ya madai kuwa baadhi ya miradi hiyo inafaidi maeneo yanayohusishwa naye kisiasa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Uchumba wa Rigathi, Sifuna kisiasa utautikisa upinzani
MJADALA kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027 umechukua mkondo mpya baada ya kauli za viongozi wa kisiasa kuashiria uwezekano wa kuibuka kwa muungano wa kisiasa kati ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Huku baadhi ya wadau wakichukulia ushirikiano huo kama silaha ya kumenyana na Rais William Ruto, wengine wanahisi unaweza kuwa chanzo cha migawanyiko mipya ndani ya upinzani. Aliyekuwa Seneta wa kuteuliwa Gloria Orwoba ni mmoja wa waliozua mjadala huo baada ya kusema Wakenya wasipuuzilie mbali uwezekano wa Gachagua na Sifuna kujitokeza pamoja kwenye tiketi ya urais mwaka 2027. Kwa mujibu wa Orwoba, Sifuna si mwanasiasa wa kawaida bali ni kiongozi anayeweza kuwa mgombea mkuu wa kiti hicho. Kauli hiyo imeongeza uzito kwa mjadala unaoendelea kuhusu nafasi ya Sifuna katika siasa za kitaifa huku uchaguzi ukikaribia. Nyota ya Sifuna anayehusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi imekuwa iking'aa na kujijenga kama nguvu mpya ya kisiasa kuelekea 2027. Hata hivyo, changamoto kubwa imekuwa ni chombo cha kisiasa atakachotumia kwa azma yake. Orwoba anadai kuwa Sifuna tayari ana chama lakini anatafuta namna ya kukipa sura mpya ili kivutie wafuasi wengi zaidi. Ndani ya vuguvugu la Linda Mwananchi, mjadala kuhusu chama bado unaendelea. Lakini licha ya mjadala kuhusu vyama, Orwoba anaamini chama hakitakuwa kigezo kikuu kwa wapigakura. Kwa mtazamo wake, Wakenya wataangalia zaidi mgombea kuliko nembo ya chama. Kauli hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu uwezekano wa kuundwa kwa tiketi ya Gachagua na Sifuna. Kwa mara ya kwanza, viongozi wa upinzani wameanza kuzungumzia waziwazi uwezekano wa wawili hao kushirikiana katika kinyang'anyiro cha urais. Kinachofanya mjadala huo kuwa wa kipekee ni kwamba Gachagua mwenyewe amewahi kusema hadharani kwamba yuko tayari kuwa mgombea mwenza wa Sifuna iwapo viongozi wa upinzani wataafikiana kuwa seneta huyo ndiye anayefaa kuongoza muungano huo. Aidha, amesema pia kwamba mpangilio wa kinyume unaweza kutokea ambapo yeye akiongoza tiketi na Sifuna kuwa mgombea mwenza. Kauli hizo zimezua hisia mseto ndani ya upinzani. Wapo wanaoamini kuwa ushirikiano kati ya mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika Mlima Kenya na kiongozi anayevutia vijana na wakazi wa mijini unaweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za taifa. Hata hivyo, wengine wanatahadharisha kuwa hatua hiyo inaweza kuibua malumbano mapya kuhusu nani anafaa kupeperusha bendera ya upinzani. Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ni mmoja wa watetezi wakuu wa muungano huo. Malala anaamini kwamba kuunganisha nguvu za Gachagua na Sifuna kutaunda kambi imara yenye uwezo wa kumpa Rais Ruto ushindani mkubwa. Kwa mujibu wa Malala, hesabu za kisiasa zinaonyesha kwamba kuunganisha Mlima Kenya, Magharibi na jamii za Maa kunaweza kuunda msingi mkubwa wa kura. Ndiyo sababu ametangaza mpango wa kuanzisha vuguvugu la "Triple M" linalolenga kuleta pamoja watu wa Mrima, Mulembe na Maa. Malala amekuwa akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Mlima Kenya na Magharibi mwa Kenya unaweza kuamua matokeo ya uchaguzi mkuu ujao. Hata hivyo, siasa za upinzani bado zinaonekana kuwa katika hatua ya mazungumzo. Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kimeweka wazi kwamba kwa sasa hakitajiunga na Muungano wa Ukombozi (TUA). Badala yake, kina nia ya kushirikiana kwanza na vuguvugu la Linda Mwananchi kabla ya kuingia katika mazungumzo ya kuunda muungano mpana wa upinzani. Msimamo huo unaonyesha kuwa bado kuna tofauti za kimkakati kati ya vikundi mbalimbali vinavyolenga kumng'oa Rais Ruto mamlakani mwaka 2027. Wakati Kalonzo Musyoka na washirika wake wakisisitiza umuhimu wa muungano mmoja wa upinzani, makundi mengine yanaonekana kutaka kujijenga kwanza kabla ya kuamua namna ya kushirikiana. Kwa sasa, tiketi ya Gachagua na Sifuna bado ni wazo linalojadiliwa kisiasa na si makubaliano rasmi. Hata hivyo, kauli za Orwoba, Malala na Gachagua mwenyewe zimeifanya kuwa mojawapo ya mada zinazovutia zaidi katika siasa za 2027. Iwapo "ndoa" hiyo ya kisiasa itafungwa rasmi, inaweza kuimarisha upinzani au kuibua mvutano mpya ikizingatiwa kuwa Gachagua ni mmoja waliosuka muungano wa upinzani unaohusisha Kalonzo, Martha Karua, Eugene Wamalwa, Fred Matiang'i, Justin Muturi miongoni mwa wengine ambao awali walionekana kuungana dhidi ya Rais Ruto. Lakini jambo moja liko wazi: mjadala kuhusu Gachagua na Sifuna umeanza kuvuruga hesabu za upinzani na kufungua sura mpya ya siasa za uchaguzi
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Aliyebuni Azimio La Umoja asikitika Raila anasahaulika haraka
MFANYABIASHARA Ronny Raburu, anayesema ndiye aliyependekeza jina Azimio la Umoja kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga mwaka 2021, amesema amesikitishwa na uamuzi wa viongozi wa upinzani kuacha kutumia jina hilo na kulibadilisha kuwa Ukombozi Alliance. Raburu, Mkenya ambaye amekuwa akiishi Tanzania kwa takriban miaka 25, anasema jina la Azimio halikuwa tu kauli ya kisiasa bali lilikuwa na msingi wa kihistoria na kiitikadi uliotokana na Azimio la Arusha la mwaka 1967 lililoasisiwa na rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere. Akizungumza kuhusu mabadiliko hayo, Raburu alisema anahisi urithi wa kisiasa wa Raila Odinga unasahaulika kwa haraka mno. "Nimevunjika moyo. Baba alikuwa akifanya siasa zenye misingi na falsafa maalum. Kila jambo alilofanya lilikuwa na maana yake. Inanishangaza kuona urithi wake ukiondolewa haraka hivi," alisema. Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ulitangaza wiki hii kuwa umeamua kubadili jina kuitwa Ukombozi Alliance kama sehemu ya kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Raburu alieleza kwamba wazo la Azimio lilizaliwa baada ya mahakama kubatilisha mpango wa Maridhiano ya Kitaifa (BBI) uliokuwa ukisukumwa na Raila Odinga na Rais( sasa mstaafu) Uhuru Kenyatta kufuatia maridhiano yao ya mwaka 2018. Kwa mujibu wake, Raila alimtafuta akihitaji jina la Kiswahili ambalo lingeendeleza roho ya BBI ya kuunganisha taifa lakini kwa lugha ambayo wananchi wengi wangetambua na kuielewa. "Alinipigia simu na kuniambia BBI imekwama na angependa jina la Kiswahili ambalo lingeendeleza lengo la umoja wa kitaifa. Alinitaka kushauriana na marafiki zangu Tanzania ili tupate jina mwafaka," alisema. Raburu anasema alifanya mazungumzo na marafiki, wazee na watu waliokuwa na uelewa mkubwa wa historia ya Tanzania kabla ya kuwasilisha mapendekezo kadhaa kwa Raila. Miongoni mwa majina aliyopendekeza ni Azimio la Umoja, ambalo lilivutiwa na Azimio la Arusha lililotumika kama nguzo ya siasa za ujamaa na ujenzi wa taifa nchini Tanzania. "Nilihisi kwamba kwa kuwa BBI ilikuwa imeanguka, kulikuwa na haja ya kupata jina ambalo lingeendelea kuakisi wazo la kujenga madaraja ya umoja," alisema. Siku chache baadaye, alishuhudia Raila akilizindua jina hilo hadharani mjini Nakuru. Baadaye lilikuwa msingi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya uliowaleta pamoja ODM, Jubilee, Wiper, Kanu na vyama vingine katika kampeni za urais za mwaka 2022. Hata hivyo, baada ya upinzani kuamua kujiita Ukombozi Alliance, Raburu anaamini siasa zimeondoka kwenye misingi ya itikadi na kuelekea katika misemo ya muda mfupi ya kisiasa. "Haya sasa ni maneno ya kampeni tu. Inaonekana watu wanatafuta jina litakalofaa wakati huo na kusaidia kushinda uchaguzi. Sioni falsafa iliyo nyuma yake," alisema. Raburu, ambaye anatoka Kaunti ya Kisumu lakini ameishi Tanzania kwa muda mrefu, anasema urafiki wake na Raila ulijengwa kutokana na mapenzi yao ya pamoja kwa historia ya ukombozi wa Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika harakati hizo. Anamkumbuka Raila kama mwanasiasa aliyependa sana historia ya Tanzania, urithi wa Nyerere na mchango wa nchi hiyo katika kupigania uhuru wa mataifa mbalimbali ya Afrika. Kifo cha Raila, anasema, kilimuumiza sana kiasi kwamba hadi leo hajafuta nambari yake ya simu. "Mara nyingi narejelea jumbe tulizowasiliana. Wakati mwingine ninapoona siasa za sasa na watu wakidai Baba aliwaambia jambo fulani, natamani kuchapisha baadhi ya jumbe zake kuthibitisha ukweli, lakini naambiwa ni mawasiliano ya kibinafsi," alisema. Kwa mujibu wa Raburu, si Azimio pekee linalopaswa kukumbukwa, bali pia mchango wa Raila katika siasa za Kenya. "Tunamsahau haraka sana. Hilo ndilo linaloniumiza zaidi," alisema. Aidha, alisisitiza kuwa Kenya inapaswa kuendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania kwa kuwa nchi hizo mbili zimekuwa washirika wa karibu katika biashara, utalii na diplomasia kwa miaka mingi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Serikali inavyolipa mabilioni kutokana na blanda za maafisa wake
WALIPA ushuru nchini wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa kifedha kutokana na maamuzi ya serikali ambayo baadaye yanabainika kuwa yalikiuka sheria, yalitekelezwa vibaya au yalikiuka haki za raia. Uchunguzi wa kesi mbalimbali mahakamani unaonyesha kuwa serikali, kaunti, polisi na mashirika ya umma yameamriwa kulipa mabilioni ya pesa kama fidia, marupurupu, mishahara iliyocheleweshwa na mikataba iliyovunjwa. Kesi hizo zinahusu kukamatwa kwa watu kinyume cha sheria, mateso, mauaji ya kiholela, kufutwa kazi visivyo halali, migogoro ya ardhi, zabuni za umma na mikataba iliyokiukwa. Moja ya kesi zilizotikisa serikali ni ile ya kiongozi wa kampeni ya Nigeria, Nnamdi Kanu. Mahakama Kuu iliamua mwaka 2025 kuwa Kanu alitekwa nyara, kuwekwa kizuizini kwa siri na kuteswa kabla ya kupelekwa Nigeria. Serikali iliamriwa kumlipa Sh10 milioni kama fidia pamoja na gharama ya kesi. Katika kesi nyingine, Mahakama Kuu iliagiza polisi na Mwanasheria Mkuu kulipa Sh35.4 milioni kwa familia na waathiriwa 28 wa operesheni za polisi wakati wa maandamano ya Azimio mwaka 2023 katika maeneo ya Kisumu, Migori na Ahero. Mahakama ilibaini kuwa baadhi yao waliuawa, kujeruhiwa au kuteswa kinyume cha sheria. Mwanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha JKUAT, Allan Omondi, pia alitunukiwa Sh8 milioni baada ya mahakama kubaini kuwa polisi walimpiga na kumweka kizuizini kinyume cha sheria wakati wa machafuko ya wanafunzi mwaka 2019. Wiki hii, mtaalamu wa teknolojia ya habari Ndiang'ui Kinyagia alishinda fidia ya Sh5 milioni baada ya mahakama kuamua kuwa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai walivamia nyumba yake huko Kinoo bila kibali cha mahakama na kutwaa mali yake kinyume cha sheria. Mbali na amri za mahakama, serikali imeanza kutekeleza mpango wa kufidia waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa maandamano yaliyofanyika kati ya 2013 na 2025. Serikali tayari imetenga Sh2 bilioni kwa mpango huo ambao unahusisha fidia kwa waliouawa, waliojeruhiwa na wale waliokumbwa na ukiukaji wa haki zao. Seneti pia inapambana mahakamani kupinga agizo la kulipa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Sh50 milioni baada ya mahakama kubaini kuwa baadhi ya haki zake za kikatiba zilikiukwa wakati wa mchakato wa kumbandua madarakani. Kesi nyingine kubwa zinahusisha ukiukaji wa haki za binadamu uliotokea katika miaka ya nyuma. Michael Rubia alitunukiwa Sh17 milioni baada ya kubainika kuwa alizuiliwa kinyume cha sheria na kuteswa katika utawala wa zamani. Serikali pia ililazimika kugharamia matibabu yake nchini Uingereza. Mahakama ya Juu pia iliidhinisha malipo ya Sh2.5 milioni kwa kila mmoja wa wafungwa sita wa kisiasa waliokamatwa mwaka 1992 wakati wa maandamano Freedom Corner. Ilibainika serikali ilikiuka haki zao kwa kuwa walikamatwa na kuteswa. Katika kesi ya maafisa wa zamani wa Jeshi la Anga walioathiriwa baada ya jaribio la mapinduzi la mwaka 1982, Mahakama ya Rufaa iliidhinisha malipo ya jumla ya Sh6.25 bilioni kwa maafisa 284 walioteswa, kufungwa na kufutwa kazi kwa njia isiyofaa. Serikali pia imebeba gharama kutokana na mauaji yanayohusishwa na polisi. Familia ya mwandishi wa habari wa Pakistan, Arshad Sharif, ilitunukiwa Sh10 milioni baada ya mahakama kuamua kuwa alipigwa risasi visivyo halali katika eneo la Kajiado mwaka 2022. Katika sekta ya ardhi, Mahakama ya Mazingira na Ardhi ilitunuku Johannes Akello Omboto Sh5 milioni baada ya ukuta wa mali yake kubomolewa na maafisa waliokuwa wakitekeleza shughuli za Shirika la Reli Kenya bila kufuata taratibu. Mashirika ya umma pia yamejikuta yakilipa mamilioni kutokana na kuvunja mikataba. Hazina ya Taifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) iliamriwa kulipa zaidi ya Sh112 milioni kwa kampuni ya Micro-City Computers baada ya kujiondoa katika mkataba wa mfumo wa CCTV ikitaja ukosefu wa fedha. Aidha, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) kiliamriwa kulipa Sh39.9 milioni kwa mkandarasi baada ya kufuta zabuni ya mradi wa Sh799 milioni bila uwazi wa kutosha. Kesi hizi zinaonyesha jinsi maamuzi ya serikali yanavyoweza kuwa na gharama kubwa kwa walipa ushuru. Japo maafisa wanaohusika mara nyingi hawaathiriki binafsi, mzigo wa kulipa fidia na madeni hayo huishia kwa wananchi kupitia fedha za umma.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 12 hours ago
Vita vyazidi mrengo wa upinzani vinara waking'ang'ania vyama
UCHAGUZI Mkuu wa mwaka 2027 unapokaribia, ushindani wa kumng'oa Rais William Ruto unaonekana kugeuka kuwa vita vya ndani ya upinzani huku vinara wakuu wakisaka vyama vya kisiasa na majukwaa yatakayowawezesha kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania urais. Ingawa viongozi wa upinzani wanakubaliana kwamba serikali ya sasa inapaswa kubadilishwa kupitia kura, bado hawajakubaliana kuhusu nani anayefaa kupeperusha bendera ya muungano wao katika kinyang'anyiro hicho. Miongoni mwa wanaotajwa kuwania uongozi wa upinzani ni aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua wa People's Liberation Party, Fred Matiang'i wa Jubilee, Eugene Wamalwa wa DAP-Kenya, Justin Muturi wa Democratic Party, Peter Munya wa PNU na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Kinachoibuka sasa ni ushindani wa kisiasa unaoonyesha kila mmoja wa viongozi hao akitaka kuwa na chama au jukwaa lake kabla ya mazungumzo ya kuunda muungano wa mwisho kufanyika. Huku Kalonzo akijaribu kuimarisha muungano wa Ukombozi Alliance, Sifuna kupitia vuguvugu la Linda Mwananchi anatafuta chombo chake cha kisiasa. Naye Gachagua anaendelea kujenga chama chake cha Democracy for Citizens Party (DCP) huku akiacha mlango wazi kwa mazungumzo na makundi mengine ya upinzani. Katibu Mkuu wa DCP Cleophas Malala amesema wazi kuwa chama hicho hakiko tayari kujiunga na Ukombozi Alliance kwa sasa. Badala yake, amependekeza DCP ishirikiane kwanza na Sifuna kabla ya kuanza mazungumzo na vyama vingine vya upinzani. Kauli hiyo imeonyesha kiwango cha kutoaminiana miongoni mwa viongozi wa upinzani, ambapo wengi wao wanaonekana kutaka kuhifadhi vyama vyao ili kuongeza uzito wao katika mazungumzo yatakayofuata. Wakati huo huo, Martha Karua na Fred Matiang'i wameendelea kusisitiza kwamba mgombea wa urais wa upinzani hafai kuteuliwa kupitia makubaliano ya viongozi wachache. Badala yake, wanataka kuwepo kwa mchakato ulio wazi, wa haki na unaokubalika kwa washirika wote. Kwa upande wake, Kalonzo ameonekana kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha muundo wa upinzani. Baada ya kugeuza Azimio kuwa Ukombozi Alliance, amekuwa akifanya mikutano ya kisiasa katika maeneo yaliyokuwa ngome za aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Wikiendi hii Kalonzo, Muturi na Wamalwa wamekuwa wakifanya kampeni za pamoja Busia na Siaya. Lakini huku Kalonzo akiimarisha Ukombozi Alliance, kambi ya Sifuna imekuwa ikisaka njia yake ya kisiasa. Hata mvutano uliojitokeza kuhusu matumizi ya jina "Ukombozi" umeonyesha tofauti zinazozidi kujitokeza kati ya makundi hayo mawili. Washirika wa Sifuna sasa wanatazamia kutumia chama cha United Democratic Party (UDP), kilichowahi kuhusishwa na mwanasiasa marehemu Cyrus Jirongo, kama chombo chake cha kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027. Katika mazingira hayo, nafasi ya Gachagua imeendelea kuwa muhimu. Kiongozi huyo amekuwa akisisitiza kuwa yuko tayari kumuunga mkono mwanasiasa yeyote atakayeonyesha uwezo mkubwa wa kumshinda Rais Ruto, hata kama si yeye mwenyewe. Kauli hiyo imebadili kwa kiasi kikubwa mjadala wa kisiasa ndani ya upinzani. Badala ya kusisitiza kuwa lazima aongoze muungano huo, Gachagua amesema mgombea anapaswa kuamuliwa kwa kuzingatia nguvu za kisiasa na uungwaji mkono wa kitaifa. Hata hivyo, msimamo huo haujaondoa ushindani uliopo. Malala ameendelea kusukuma wazo la ushirikiano kati ya Mlima Kenya na eneo la Mulembe, akisema maeneo hayo yana kura za kutosha kuathiri matokeo ya uchaguzi wa urais. Baadhi ya viongozi kutoka Magharibi mwa Kenya, akiwemo Mbunge wa Bumula Jack Wamboka, wamependekeza Sifuna awe mgombea wa urais huku mgombea mwenza akitoka Mlima Kenya. Hata hivyo, pendekezo hilo linapingana na msimamo wa wafuasi wa Kalonzo ambao wanataka kiongozi huyo wa Wiper apewe tiketi ya urais huku Sifuna akichukua nafasi ya mgombea mwenza. Aidha, aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta amewahimiza wanachama wa Jubilee kuanza maandalizi ya uchaguzi wa 2027 mapema na kushirikiana na viongozi vijana ili kuunda muungano mpana wa kisiasa. Wachambuzi wa siasa wanasema changamoto kubwa inayokabili upinzani si kuwakutanisha viongozi wake, bali ni kupata utaratibu wa haki wa kumteua mgombea mmoja anayekubalika kwa wote. Wanasema historia ya siasa za Kenya imeonyesha mara nyingi kuwa miungano mingi huvunjika kutokana na mizozo kuhusu mgombea wa urais, mgombea mwenza na ugavi wa mamlaka. Kwa sasa, upinzani unaonekana kuunganishwa na lengo moja la kumng'oa Rais Ruto. Hata hivyo, ushindani wa ndani kuhusu vyama, miungano na nafasi za uongozi unaendelea kutishia umoja huo huku saa ya uchaguzi wa 2027 ikiendelea kuyoyoma.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 26 Sep 2026 09:55:38
Julius Kyazze atambuliwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi Afrika
MWANABIASHARA wa sekta ya ubunifu na burudani kutoka Uganda, Julius Kyazze, ametambuliwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa barani Afrika. Kyazze, ambaye ni mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa LIVE54+, alitunukiwa tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika Kigali, Rwanda, Septemba 25, 2026. Alikuwa mwakilishi pekee wa sekta ya ubunifu miongoni mwa viongozi waliotambuliwa katika nyanja mbalimbali. Kutambuliwa kwake kunafuatia zaidi ya miongo miwili ya shughuli za ujasiriamali katika sekta za ubunifu, burudani, vyombo vya habari na michezo barani Afrika. Kyazze amehusika katika kujenga na kuendesha biashara Uganda, Kenya, Tanzania, Ghana na Rwanda, huku akishirikisha wataalamu na wadau kutoka masoko mbalimbali. Kupitia LIVE54+, amekuwa akihusishwa na shughuli zinazohusu vyombo vya habari, ubunifu, uzoefu wa chapa, maudhui, vipaji na uzalishaji wa kazi za burudani. Katika taarifa yake, LIVE54+ ilisema kutambuliwa kwa Kyazze kunaangazia mchango wa wafanyabiashara katika kukuza sekta ya ubunifu barani Afrika. "Kyazze amejikita katika kujenga biashara," ilisema taarifa hiyo. Taarifa hiyo iliongeza kuwa kutambuliwa kwake pamoja na viongozi kutoka sekta nyingine kunaweka biashara za ubunifu katika mjadala mpana kuhusu ushawishi na maendeleo ya bara. LIVE54+ ni kundi la biashara za Kiafrika zinazofanya kazi katika sekta za vyombo vya habari, ubunifu, maudhui, vipaji na uzalishaji.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 26 Sep 2026 07:50:33
Wakazi walalamika mamia ya ng'ombe wakiuawa kwenye msako wa majangili
WAKAZI wa Samburu wameibua malalamishi baada ya mamia ya ng'ombe, mbuzi na punda kuripotiwa kuuawa wakati wa operesheni ya usalama iliyolenga majangili na kurejesha mifugo iliyoibwa. Operesheni hiyo ilianzishwa kufuatia mashambulizi yaliyotekelezwa na majangili katika mpaka wa Samburu na Isiolo, ambapo maafisa wawili wa Kitengo cha Kupambana na Wizi wa Mifugo (ASTU), polisi mmoja wa akiba na raia wawili waliuawa walipokuwa wakifuatilia mifugo iliyoibwa. Hata hivyo, viongozi na wakazi wa Samburu Mashariki sasa wanasema operesheni hiyo imesababisha hasara kubwa kwa familia zinazotegemea ufugaji kama chanzo kikuu cha maisha.Gavana wa Samburu, Lati Lelelit, alisema ingawa kaunti yake iliunga mkono juhudi za kuimarisha usalama, jinsi operesheni hiyo ilivyotekelezwa ilisababisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na uharibifu wa mali ya wananchi. "Matokeo yamekuwa mabaya sana, yakisababisha ukatili na mauaji ya kiholela ya mifugo ya wananchi," alisema.Idadi kamili ya mifugo iliyouawa bado inapingwa. Takwimu zilizowasilishwa katika Seneti zinaonyesha kuwa mbuzi 415 na ng'ombe 102 waliuawa katika Wadi ya Waso ndani ya siku tatu. Hata hivyo, Mbunge wa Samburu Mashariki Jackson Lekumontare alisema tathmini yake inaonyesha zaidi ya mbuzi 700, ng'ombe 500 na punda kadhaa waliangamia wakati wa operesheni hiyo. Kwa upande wake, Chama cha Wataalamu wa Samburu kimesema kimeorodhesha angalau wanyama 717 waliouawa, wakiwemo mbuzi 415, ng'ombe 352 na punda 50, huku uchunguzi ukiendelea. Chama hicho kinasema hasara hiyo haihusiani tu na mali bali pia maisha ya familia nyingi zinazotegemea mifugo kwa chakula, elimu ya watoto, huduma za afya na mapato ya kila siku. Tukio hilo lilichochea maandamano katika maeneo ya Samburu Mashariki huku wakazi wakitaka uchunguzi huru ufanywe na familia zilizoathirika zilipwe fidia.Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na mwenzake wa Samburu Lelegwe Ltumbesi pia wameitaka serikali kueleza mazingira yaliyosababisha mauaji hayo ya mifugo. Katibu Mkuu wa Chama cha Wanafunzi wa Vyuo Vikuu cha Samburu, Meshack Ramati, alitaka uchunguzi wa kina ufanywe kubaini idadi ya mifugo iliyouawa, maafisa waliohusika na walioidhinisha operesheni hiyo. "Serikali ina wajibu wa kulinda raia, mali yao na heshima yao. Tunataka uwazi, haki na fidia kwa familia zilizopoteza mifugo yao," alisema.Wakazi wanasema juhudi za kupambana na ujangili ni muhimu, lakini hazipaswi kufanywa kwa njia inayohatarisha maisha na uchumi wa wananchi wasio na hatia.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 26 Sep 2026 06:55:48
Majengo ya kisasa yanavyoharibu utamu wa uswahili wa Mombasa
KWA miongo mingi, nyumba za jadi za muundo wa Waswahili zimekuwa alama muhimu ya utambulisho wa Mombasa. Hata hivyo, mandhari hiyo sasa inabadilika kwa kasi huku majengo marefu ya kisasa yakizidi kujengwa katika maeneo mbalimbali ya jiji. Katika mitaa ya Majengo, Kisauni, Old Town, Tudor na Ganjoni, nyumba za zamani za Waswahili zinabomolewa ili kupisha majengo ya ghorofa yanayolenga kukidhi ongezeko la mahitaji ya makazi. Mzee Abubakar Mohamed, mwenye umri wa miaka 90, anasema nyumba hizo zilijengwa kwa kuzingatia mazingira ya pwani yenye joto na unyevunyevu mwingi."Muundo wake uliwezesha hewa kupita kwa urahisi na kutoa hali ya baridi ndani ya nyumba. Pia uliakisi historia na utamaduni wa watu wa pwani," anasema. Kwa mujibu wa wakazi, ongezeko la thamani ya ardhi na mahitaji makubwa ya nyumba limewavutia wawekezaji wengi wanaotaka kujenga majengo ya kisasa katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa na nyumba za familia moja. Mkazi wa Majengo, Mohamed Hussein, ni mmoja wa walioamua kushirikiana na mwekezaji badala ya kuuza mali yake.Nyumba yake ilibomolewa na sasa jengo la ghorofa linaendelea kujengwa katika eneo hilo. Kupitia makubaliano yao, Hussein atamiliki nyumba sita ndani ya jengo hilo pindi mradi utakapokamilika. "Mwekezaji alinipa chaguo la kuuza au kushirikiana naye. Nilichagua ushirikiano kwa sababu nilitaka kuendelea kuwa na sehemu ya umiliki wa ardhi hiyo," alisema.Wakazi wengine wamechagua kuuza nyumba zao na kuhamia maeneo mengine, huku baadhi wakitumia fedha walizopata kuanza maisha mapya nje ya jiji.Lakini pamoja na faida za kiuchumi zinazotokana na miradi hiyo, wataalamu wanatahadharisha kuhusu hatari ya Mombasa kupoteza urithi wake wa kihistoria na usanifu wa kipekee. Mwenyekiti wa Chama cha Wasanifu Majengo Kenya (AAK) tawi la Pwani, Dancan Odhiambo, anasema ubomoaji wa nyumba za Kiswahili unafuta urithi ambao huenda usirejeshwe kamwe."Usasa haupaswi kuja kwa gharama ya utambulisho wa usanifu wa jiji. Vipengele vya nyumba za Kiswahili vinaweza kuingizwa katika majengo mapya ili kulinda utamaduni huo," anasema. Wataalamu pia wanaeleza kuwa ongezeko la majengo marefu linaweka shinikizo kwa miundombinu kama maji, mabomba ya maji taka, barabara, maegesho na mfumo wa ukusanyaji taka.Mbunifu Abdulnassir Mohamed anasema maendeleo hayawezi kuzuiwa, lakini yanahitaji mipango bora ili kuhakikisha ukuaji wa jiji unaendana na uwezo wa miundombinu iliyopo. "Mombasa inaweza kukua bila kupoteza utambulisho wake, lakini tunahitaji kueleza maana ya usanifu wa Mombasa katika majengo ya kisasa," anasema.Kadiri paa za nyumba za Kiswahili zinavyozidi kutoweka na majengo marefu kuchukua nafasi yake, Mombasa inakabiliwa na changamoto ya kusawazisha maendeleo ya kisasa na uhifadhi wa urithi wake wa kitamaduni,
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 26 Sep 2026 05:55:23
Kalonzo naye kutua Nyanza kuwinda ngome ya ODM baada ya Ruto
KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, wikendi hii anatarajiwa kufanya ziara ya kisiasa katika maeneo ya Nyanza na Magharibi mwa Kenya katika juhudi za kuimarisha azma yake ya kuwania urais mwaka 2027, huku Rais William Ruto akiendelea kuongeza ushawishi wake katika ngome ambazo kwa muda mrefu zilijulikana kuwa za upinzani. Bw Musyoka ataanza ziara hiyo kwa kuzuru Bumala na Nambale katika Kaunti ya Busia leo kabla ya kuelekea Bondo, Kaunti ya Siaya, Jumapili. Akiwa Bondo, atahudhuria ibada katika Kanisa Kuu la St Michael's All Angels Cathedral na baadaye kufanya mikutano ya kukutana na wananchi. Ziara hiyo inampeleka moja kwa moja katika maeneo ambayo kwa miaka mingi yalikuwa msingi mkuu wa siasa za marehemu Raila Odinga. Pia inafanyika siku chache baada ya Rais Ruto kukamilisha ziara ya siku tano katika eneo la Nyanza, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kujijengea msingi mpya wa kisiasa katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa ngome za ODM na upinzani kwa jumla. Kwa wachanganuzi wa siasa, ziara ya Kalonzo ina umuhimu mkubwa katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Kiongozi huyo wa Wiper analenga kujenga uhusiano wa moja kwa moja na wapigakura wa Nyanza na Magharibi ambao kwa muda mrefu walimuunga mkono Raila katika kila uchaguzi. Kalonzo alikuwa mshirika wa karibu wa Raila kwa zaidi ya muongo mmoja. Mwaka 2013 alikubali kuweka kando azma yake ya urais na kuwa mgombea mwenza wa Raila kupitia muungano wa Coalition for Reforms and Democracy (CORD). Mwaka 2017 waligombea pamoja tena chini ya muungano wa National Super Alliance (NASA). Katika uchaguzi wa mwaka 2022, Kalonzo alibaki kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa kampeni za Azimio la Umoja One Kenya licha ya Raila kumteua Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake. Uhusiano huo wa muda mrefu ulimfanya Kalonzo kuwa sura inayofahamika sana katika kampeni za Nyanza. Hata hivyo, changamoto kubwa sasa ni jinsi ya kubadilisha urafiki huo wa kisiasa kuwa uungwaji mkono binafsi kutoka kwa wapigakura wa eneo hilo. Changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi kufuatia kifo cha Raila Odinga na mabadiliko ya kisiasa yaliyojitokeza baada yake. Baadhi ya washirika wa zamani wa Raila wameanza kushirikiana kwa karibu na serikali ya Kenya Kwanza huku wengine wakijaribu kuunda sura mpya ya upinzani. Kwa mujibu wa duru za kisiasa, Kalonzo anategemea ushirikiano wa Gavana wa Siaya James Orengo katika kuimarisha kampeni zake Nyanza. Orengo amebaki mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika eneo hilo licha ya kuhusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Ziara za Kalonzo katika Kaunti ya Busia nazo zina umuhimu wa kisiasa. Busia imekuwa sehemu ya maeneo ambayo kwa kawaida huunga mkono vyama vya upinzani. Hata hivyo, katika miezi ya hivi majuzi Rais Ruto ameongeza shughuli zake za kisiasa na maendeleo katika eneo hilo, akiwavutia baadhi ya viongozi wa eneo hilo kuunga mkono ajenda ya serikali. Ziara ya Rais katika kaunti za Kisumu, Siaya, Migori na Homa Bay ilijikita katika miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, huduma za maji, masoko, afya na elimu. Wachanganuzi wanasema mkakati huo umemsaidia kujenga taswira ya kiongozi anayelenga maendeleo badala ya siasa za mgawanyiko. Hali hiyo imeweka shinikizo jipya kwa viongozi wa upinzani ambao sasa wanapaswa kushindana si tu na ushawishi wa kisiasa wa Rais Ruto bali pia na mvuto wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali. Kwa upande mwingine, Kalonzo anaonekana kuwekeza zaidi katika siasa za mashinani na kujenga muungano mpya wa upinzani. Hatua hizi zinajiri baada ya muungano wa Azimio la Umoja kubadilishwa jina na kuitwa Ukombozi Alliance. Kalonzo amesema mabadiliko hayo ni sehemu ya mkakati wa kujiandaa mapema kwa uchaguzi wa mwaka 2027. Pia amekuwa akifanya mazungumzo na viongozi wengine wa upinzani akiwemo Justin Muturi, Eugene Wamalwa na Lenny Kivuti kuhusu mfumo bora wa kuunganisha upinzani. Hata hivyo, hesabu za kisiasa ndani ya upinzani zimeendelea kuwa tata kutokana na azma ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuwania urais kupitia chama chake cha Democracy for the Citizens Party (DCP). Kauli za viongozi wa DCP zimeonyesha kuwa bado kuna tofauti kuhusu jinsi muungano mpana wa upinzani utakavyoundwa. Kwa sasa, Kalonzo anakabiliwa na jukumu la kuthibitisha kuwa mvuto wake wa kisiasa unaweza kuvuka mipaka ya Ukambani na kupata uungwaji mkono katika maeneo yaliyokuwa ngome za Raila. Ziara yake ya Bondo inachukuliwa kuwa moja ya majaribio muhimu zaidi ya kupima uwezo wake wa kuvutia wapigakura wa Nyanza.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 26 Sep 2026 04:55:07
Tutaenda wapi: Wakazi wa Nairobi walalamikia onyo kuhusu mafuriko ya El Nino
Wakazi wa maeneo yanayokumbwa na hatari ya mafuriko jijini Nairobi wanakabiliwa na changamoto kubwa huku serikali ikiendelea kuwaonya kuondoka katika maeneo hayo kabla ya mvua ya El Niño inayotarajiwa kuanza kunyesha mwishoni mwa mwaka. Kwa wengi wao, swali kuu si kama wanapaswa kuhama, bali watahamia wapi. Esther Makhokha, mkazi wa Mukuru Kayaba, bado anakumbuka mafuriko ya Machi mwaka huu. Anasema jioni moja mvua iliponyesha kwa nguvu, maji yalianza kuingia katika nyumba yake huku yeye na dada zake wawili wakitayarisha chakula. Kwa kukosa muda wa kufanya maamuzi, walichukua watoto na kuwapeleka katika baa iliyokuwa karibu ambayo haikuwa imezingirwa na maji. Baadaye, yeye na dada yake walilala kwa jirani wakisubiri maji yapungue. "Nililazimika kukimbia na watoto na kulala sakafuni kwa jirani. Sitaki kupitia hali hiyo tena," alisema. Makhokha, ambaye amekulia Mukuru Kayaba tangu utotoni, anasema hana mahali pengine pa kwenda iwapo mafuriko yatatokea tena. "Hata wakiniambia nihame, sina mahali pa kwenda. Sina pesa za kuhamia sehemu nyingine. Hapa ndipo nimeishi maisha yangu yote," alisema. Anasema wakati wa mafuriko yaliyopita hakupata usaidizi kutoka kwa serikali ya kaunti. Badala yake, waandishi wa habari walioenda kuripoti tukio hilo walimsaidia kwa chakula, mavazi, godoro na nepi za watoto. Mkazi mwingine wa Mukuru Kayaba, Immaculate Wavinya, anakabiliwa na changamoto sawa. Mama huyo anayelea mtoto peke yake amesema amehudhuria mikutano kadhaa ambapo wakazi wamehimizwa kuhama kutoka maeneo yanayokumbwa na mafuriko. Hata hivyo, anasema ushauri huo haujatiwa nguvu na msaada wa kuwawezesha wananchi kuhamia maeneo salama. "Familia yangu iko hapa. Biashara yangu iko hapa. Nimemlea mtoto wangu hapa tangu mwaka 2015. Nikiambiwa nihame, niende wapi na kwa pesa gani?" alihoji. Kulingana naye, wakazi wengi hawajaona juhudi za kutosha za serikali kuwasaidia kuhama. Katika eneo la Nairobi Dam karibu na Highrise, Ruth Mwikali pia anahofia mvua inayotarajiwa. Anasema amesikia onyo kuhusu El Niño lakini hajapewa mwongozo wa wazi kuhusu mahali pa kwenda iwapo makazi yao yatazingirwa na maji. Wasiwasi wa wakazi hawa unajiri huku serikali ya Kaunti ya Nairobi ikisema imeongeza maandalizi ya kukabiliana na mafuriko. Gavana Johnson Sakaja amesema maeneo kama Mukuru, Kibra, Mathare na sehemu za Ruaraka ni miongoni mwa maeneo ambayo huathiriwa mara kwa mara wakati mvua kubwa inapozidi uwezo wa mitaro ya kuondoa maji. Kaunti imesema inaendelea kusafisha, kupanua na kuchimba zaidi mitaro ya maji katika zaidi ya maeneo 36 yanayokumbwa na mafuriko. Pia imeanzisha vituo 27 vya uokoaji na makazi ya muda kwa watu watakaolazimika kuhama. Hata hivyo, kwa wakazi wengi wa mitaa ya mabanda, maandalizi hayo hayajibu swali lao kuu. "Hauwezi kuwaambia watu wahame bila kuwaonyesha mahali pa kwenda," alisema Mzee Francis Kaviti wa Mukuru Kayaba.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 26 Sep 2026 03:55:49
Jinsi ya kutambua walaghai wa mapenzi wanakunyemelea mtandaoni
Kadri watu wengi wanavyotumia mitandao na apu za kutafuta wachumba, ndivyo matapeli wa kimapenzi wanavyozidi kuwanasa waathiriwa wao. Utafiti wa TransUnion unaonyesha kuwa karibu Wakenya watatu kati ya kumi wanaotumia apu za uchumba mtandaoni wamewahi kukumbana na jaribio la ulaghai. Zaidi ya asilimia 80 ya Wakenya pia wanasema wamewahi kulengwa na walaghai wa kidijitali kupitia simu zao. Mtaalamu wa usalama wa mitandao na mshirika wa kampuni ya Techrise, Polycap Oliver Oluoch Ochieng, anasema ishara ya kwanza ya tahadhari ni mtu kuharakisha mapenzi. "Ikiwa mtu anaanza kukutamkia mapenzi ndani ya siku chache kabla hata ya mawasiliano ya kawaida kama simu ya video, hilo ni jambo la kutiliwa shaka," anasema. Pia anaonya kuhusu watu wanaokwepa mawasiliano ya video au mikutano ya ana kwa ana kwa kutoa visingizio mbalimbali kama kamera kuharibika au kuwa mbali kikazi. Kwa mujibu wake, matapeli mara nyingi hutumia picha za kuvutia zilizoibwa mitandaoni na hujenga wasifu unaoonekana mkamilifu kupita kiasi. "Mfano ni mtu kuchapisha picha za kitaalamu pekee bila picha za kawaida akiwa na marafiki au familia. Hiyo ni ishara ya tahadhari," anasema. Anashauri watumiaji kufanya uchunguzi wa picha mtandaoni ili kubaini iwapo zimeibwa kutoka kwa wanamitindo au watu maarufu. Mtaalamu huyo pia anatahadharisha kuhusu watu wanaoharakisha kuhamisha mazungumzo kutoka apu za uchumba hadi WhatsApp au Telegram ambako ni vigumu kufuatilia ulaghai. Kwa kawaida, matapeli huanza kwa kuomba kiasi kidogo cha pesa kama vocha ya simu au mkopo mdogo. Baada ya kuona mwathiriwa yuko tayari kusaidia, huanza kuomba fedha nyingi zaidi kwa madai ya dharura za hospitali, usafiri au uwekezaji. "Ikiwa mtu anaomba pesa kwa sababu yoyote ile, huo ni wakati wa kusitisha mawasiliano," anasema Oluoch. Mshauri wa masuala ya mahusiano Benjamin Zulu anasema watu wanaotafuta mapenzi mtandaoni hawapaswi kutegemea mawasiliano ya mtandaoni pekee. "Mtandao unaweza kuwa sehemu ya kukutana, lakini uhusiano wa kweli hujengwa kupitia mawasiliano ya ana kwa ana," anasema. Zulu anaongeza kuwa mtu anayekwepa kukutana ana kwa ana huenda ana jambo la kuficha. Pia anawahimiza watu kutotoa taarifa za kibinafsi kama anwani ya nyumbani, nambari ya kitambulisho au hali zao za kifedha kabla ya kuwa na imani kamili kwa mtu huyo. Anashauri watu kuwa waangalifu hasa wanapopitia maumivu ya moyo au upweke, kwani hali hiyo huwafanya kuwa rahisi kudanganywa. Kwa maoni yake, mapenzi ya kweli hayapaswi kuhusisha maombi ya pesa. "Usichukue mkopo wala kutumia akiba yako kumsaidia mtu uliyekutana naye mtandaoni," anasema. Wataalamu wanashauri watu kufanya simu za video kabla ya kuwekeza hisia zao, kuchagua maeneo ya wazi wanapokutana kwa mara ya kwanza na kuwafahamisha marafiki au jamaa kuhusu mahali walipo. Aidha, yeyote anayeshuku ulaghai anaweza kuripoti kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kupitia nambari ya bure 0800 722 203 au kwa simu za dharura za polisi 999, 911 au 112.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 26 Sep 2026 02:55:26
Kaa chonjo: Maeneo hatari kwa ghasia za kisiasa 2027 yamulikwa
HUKU Kenya ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 10, 2027, wasiwasi unazidi kuongezeka kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa ghasia za kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini. Wiki za hivi majuzi zimeshuhudia visa vya vurugu katika mikutano ya kisiasa huko Homa Bay, Embu na Garissa, hali ambayo imeibua hofu kuwa siasa za ushindani huenda zikachochea ukosefu wa usalama kama ilivyoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita. Mashambulizi dhidi ya viongozi wa muungano wa Linda Mwananchi mjini Homa Bay na vurugu zilizoripotiwa katika mkutano wa kisiasa Nembure, Embu, ni baadhi ya matukio ambayo yamefanya hali ya kisiasa nchini kuwa katika hali ya taharuki. Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, na washirika wake pia walilazimika kuondoka haraka Garissa baada ya kukumbana na mazingira yaliyotishia usalama wao. Kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR), watu wasiopungua 11 wamepoteza maisha tangu Februari mwaka huu kutokana na matukio yanayohusishwa na mikutano ya kisiasa nchini. Tume hiyo imeonya kuwa mivutano inayoshuhudiwa katika maeneo kama mpaka wa Turkana na West Pokot, Isiolo, Embu na kaunti nyingine ni ishara ya hatari inayopaswa kushughulikiwa mapema kabla ya uchaguzi. "Tunahitaji kulinda haki za msingi kabla hazijakiukwa, si baada ya madhara kutokea," ilisema KNCHR ikitaka uchunguzi wa kina kufanywa kuhusu visa vyote vya vurugu. Kwa upande wake, Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imezidi kuwaonya wanasiasa dhidi ya matumizi ya lugha za uchochezi na kuajiri vijana kutekeleza mashambulizi dhidi ya wapinzani wao. Mwenyekiti wa NCIC, Kepha Nyamweya Omae, alisema vijana wanapaswa kushirikishwa katika demokrasia kwa njia halali badala ya kutumiwa kama silaha za kisiasa. Wataalamu wa masuala ya usalama wanasema maeneo hatari ya ghasia za uchaguzi nchini yamebakia karibu yale yale kwa miaka mingi. Mtaalamu George Musamali anasema Nairobi, sehemu za Bonde la Ufa, Mombasa, Homa Bay, Migori, Kisii na Kiambu zinaendelea kuonekana kuwa maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kushuhudia vurugu. Maeneo yaliyotajwa mara kwa mara kama yenye uwezekano mkubwa wa kushuhudia ghasia za kisiasa ni Nairobi, Nakuru, Kericho, Kisumu, Uasin Gishu, Mombasa, Homa Bay, Migori, Kisii, Kiambu, sehemu za Bonde la Ufa, Turkana-West Pokot, Isiolo, Embu, Kitengela, Bungoma, Kakamega, Nandi na Marsabit. Haya ni maeneo yaliyotambuliwa kutokana na historia ya vurugu za uchaguzi, mivutano ya kisiasa, migogoro ya ardhi, tofauti za kikabila na ushindani wa kisiasa. "Kila uchaguzi tangu mfumo wa vyama vingi urejee mwaka 1992 umeshuhudia aina fulani ya ghasia. Mara nyingi maeneo hayo hubakia yale yale kwa sababu siasa zetu zimejengwa kwenye misingi ya kikabila," alisema Bw Musamali. Aidha, ameonya kuhusu kuibuka kwa makundi ya vijana wanaotumiwa na wanasiasa kuvuruga mikutano ya wapinzani na kuzua hofu miongoni mwa wapiga kura. Ripoti mbalimbali zimeonyesha kuwa ghasia za uchaguzi nchini mara nyingi huchochewa na mchanganyiko wa siasa za kikabila, migogoro ya ardhi, malalamishi ya kihistoria na ukosefu wa usawa katika ugavi wa rasilimali za umma. Mwanaharakati wa haki za binadamu Ernest Cornel anaeleza kuwa vurugu zinaweza kutokea kati ya jamii tofauti au hata ndani ya jamii moja kulingana na maslahi ya kisiasa na kijamii yanayokinzana. "Kuna maeneo ambapo migogoro ya ardhi na mipaka imeendelea kwa muda mrefu. Siasa zinapoingilia kati, baadhi ya watu huona kama fursa ya kulipiza kisasi," alisema. Takwimu zinaonyesha kuwa ghasia za uchaguzi wa 2007/2008 zilisababisha vifo vya takriban watu 1,300 na kuwafanya zaidi ya watu 650,000 kuhama makazi yao. Ingawa Kenya imepiga hatua kubwa tangu wakati huo, wataalamu wanaonya kuwa dalili zinazoonekana sasa zinafanana na zile zilizotangulia migogoro ya zamani. Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga pia ameonya kuhusu umuhimu wa kuwa na Idara za usalama ambazo haziegemei upande wowote, akisema upendeleo wa kisiasa ndani ya taasisi za usalama unaweza kutumbukiza nchi katika machafuko. Kampeni za uchaguzi zinapoanza kushika kasi, wadau wa kisiasa, asasi za kiraia na idara za usalama wanahimizwa kushirikiana ili kuzuia kurejea kwa historia ya vurugu. Swali kuu sasa ni iwapo Kenya itazingatia ishara hizi za tahadhari au itasubiri hadi madhara yatokee tena.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 11:55:18
Diwani asema Sakaja hafai kupewa 'tutam' sababu ameshindwa kuwahudumia wakazi ipasavyo
DIWANI wa Wadi ya Nairobi South, Waithera Chege, amesema rekodi ya maendeleo ya Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja haimruhusu kuwania muhula wa pili 2027. Akizungumza katika mkutano wa kisiasa eneo la South B, Bi Chege alidai kuwa uongozi wa Gavana Sakaja umeshindwa kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2022. Alisema baadhi ya maeneo ya Nairobi hayajanufaika kikamilifu na miradi ya maendeleo, akidai kuwa hali hiyo imeathiri zaidi wadi zinazowakilishwa na madiwani wanaokosoa utawala wa Gavana Sakaja. "Uongozi wa Sakaja umeshindwa kutumikia wananchi. Nairobi imekosa baadhi ya huduma muhimu za ugatuzi, hali ambayo imelazimu Serikali ya Kitaifa kuingilia kati na kutekeleza miradi ambayo inapaswa kufanywa na Serikali ya Kaunti," alisema Bi Chege. Alitoa wito kwa chama cha UDA kutafuta mgombea mwingine wa ugavana wa Nairobi iwapo kinataka kuhifadhi kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa 2027. Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Alex Wachira, pia aliwataka wakazi kumuunga mkono Rais William Ruto kwa muhula wa pili. Bw Wachira alisema Rais anafaa kupewa nafasi ya kukamilisha miradi aliyoanzisha katika muhula wake wa kwanza. Alitaja marais wa zamani Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, ambao walihudumu kwa mihula miwili, akisema Rais Ruto pia anapaswa kupewa nafasi kama hiyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 15:45:17
Pombe haramu yaua watatu Kitengela, wawili mahututi
Huzuni imetanda katika kijiji cha Noonkpoir, Kitengela, Kaunti ya Kajiado, baada ya watu watatu kufariki dunia na wengine wawili kulazwa hospitali wakiwa mahututi kutokana na kile kinachoshukiwa kuwa pombe haramu. Mnamo Ijumaa asubuhi, Christine na jamaa zake waliomboleza kifo cha mumewe, James Maina Nguru, aliyefariki Jumatatu usiku baada ya kunywa pombe hiyo. Kwa mujibu wa wakazi, waathiriwa hao walikunywa pombe hiyo katika eneo la Migingo jioni ya Jumatatu kabla ya kufariki nyakati tofauti karibu na makazi yao. Migingo, eneo lililoko Kitengela, limekuwa likihusishwa kwa miaka kadhaa na biashara ya pombe haramu, dawa za kulevya na uhalifu. Bi Mukeira alisema mumewe, aliyekuwa fundi na baba wa watoto watatu, alirejea nyumbani akiwa katika hali mbaya baada ya kutoka kwenye baa maarufu eneo hilo. "Alikuwa akilalamika maumivu makali ya tumbo na hakuweza kusimama vizuri. Muda mfupi baadaye alianza kutapika damu na akafariki mbele yetu," alisema kwa huzuni. Sasa mjane huyo anasema amelazimika kulea watoto wao peke yake. Familia hiyo imeamua kutofanya uchunguzi wa maiti kutokana na hali ngumu ya kifedha na imani kuwa pombe ndiyo iliyosababisha kifo chake. Mama yake Nguru, Mary Muthoni, ameitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaosambaza pombe hatari. Alisema mara nyingi alimuonya mwanawe kuhusu madhara ya pombe lakini hakumsikiliza. Katika eneo hilo hilo, Lynette Sirengo pia anaomboleza kifo cha mumewe, Godfrey Simiyu Kiliswa, aliyefariki baada ya kupatikana akiwa hajitambui karibu na baa inayojulikana kama "Kwa Omosh". Alifariki siku iliyofuata nyumbani kwake. Mwanaume mwingine, Elisha Okello, naye alifariki baada ya kurejea nyumbani akiwa amelewa. Mwili wake ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Kitengela. Wakati huo huo, ndugu wa mmoja wa manusura amesema mgonjwa amelazwa katika hospitali moja jijini Nairobi akiwa katika hali mahututi, huku viungo vya ndani vikidaiwa kuathiriwa vibaya. Wakazi wamewalaumu maafisa wa usalama kwa kushindwa kudhibiti uuzaji wa pombe haramu, madai ambayo polisi wamekanusha wakisema wameimarisha msako dhidi ya wauzaji wa vileo haramu na dawa za kulevya. Serikali pia imeagiza operesheni kali kote nchini kukabiliana na biashara hiyo inayozidi kuhatarisha maisha ya wananchi
read moreRight Column Content