T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 09 Sep 2026 15:07:35

Wagonjwa wapumua sasa baada ya wauguzi kusitisha mgomo wa siku 44

MUUNGANO wa Kitaifa wa Wauguzi na Wakunga Kenya (KNUNM) jana ulisitisha mgomo wake wa kitaifa uliodumu kwa siku 41 baada ya kufikiana na Baraza la Magavana Nchini (CoG). Uamuzi huo ulitangazwa baada ya mkutano wa siku nzima wa faragha kati ya viongozi wa KNUNM na CoG. Katibu Mkuu wa KNUNM Seth Panyako alisema mgomo huo ulioanza Julai 29, 2026, umesitishwa mara moja. "Kwa mamlaka niliyopewa na Katiba ya Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi Kenya na Katiba ya Kenya, natangaza kwamba mgomo ulioanza tarehe 29 Julai 2026 umesitishwa," akasema Bw Panyako. Aliwataka wauguzi kurejea kazini mara moja au ndani ya saa 24 ili kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kutolewa katika hospitali. "Ninawasihi wanachama kurejea kazini mara moja na kwa vyovyote vile si zaidi ya saa 24 kuanzia sasa," akaongeza. Kusitishwa kwa mgomo huo kumaliza kusambaratika kwa huduma za afya katika hospitali za umma kote nchini kwa karibu wiki sita. Wauguzi walikuwa wakishinikiza kuboreshwa kwa malipo na marupurupu, hali iliyosababisha baadhi ya wagonjwa kukosa huduma muhimu. Mapema wiki hii, wauguzi walikuwa wameandamana hadi katika afisi za CoG na kuahidi kuendelea kuwa hapo kila siku hadi malalamishi yao yasikilizwe. Jumanne, CoG ilionyesha dalili za kusuluhisha mzozo huo baada ya kufichua kuwa ilikuwa imewasilisha ofa kwa wauguzi. Mwenyekiti wa CoG Ahmed Abdullahi alisema wauguzi wangepata nyongeza ya Sh8,000 katika marupurupu ya mazingira hatari ya kufanya kazi na Sh5,000 ya marupurupu ya sare, jumla ya Sh13,000. "Kupitia juhudi za kamati yetu ya afya, ninaweza kuripoti kwamba hatimaye tumefikia makubaliano ikiwa hawatabadilisha msimamo wao hadi wakati mkataba utakapotiwa saini. Tumewapa nyongeza ya marupurupu ya mazingira hatari ya kazi hadi Sh8,000 na pia tumewapa nyongeza ya Sh5,000 ya marupurupu ya sare," akasema Bw Abdullahi katika mkutano uliofanyika Ikulu. Suluhu hiyo pia imezuia mgomo ambao ulikuwa unatishia kuanzishwa na madaktari. Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno Kenya (KMPDU) ulikuwa umetoa ilani ya siku saba ukitaka mzozo wa wauguzi usuluhishwe, na kuonya kuwa madaktari wangeingia mgomoni iwapo suala hilo halingetatuliwa. KMPDU ilikuwa imesema kuvurugika kwa huduma katika hospitali za umma kwa muda mrefu kulikuwa kumeongeza mzigo wa kazi kwa madaktari na wahudumu wengine wa afya. Kusitishwa kwa mgomo huo sasa kunatarajiwa kurejesha huduma za afya kama kawaida, huku utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa ukitarajiwa kuwa hatua muhimu ya kuzuia migogoro mingine kati ya wauguzi na serikali.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 12 hours ago

T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Wakazi walalamika mamia ya ng'ombe wakiuawa kwenye msako wa majangili

WAKAZI wa Samburu wameibua malalamishi baada ya mamia ya ng'ombe, mbuzi na punda kuripotiwa kuuawa wakati wa operesheni ya usalama iliyolenga majangili na kurejesha mifugo iliyoibwa. Operesheni hiyo ilianzishwa kufuatia mashambulizi yaliyotekelezwa na majangili katika mpaka wa Samburu na Isiolo, ambapo maafisa wawili wa Kitengo cha Kupambana na Wizi wa Mifugo (ASTU), polisi mmoja wa akiba na raia wawili waliuawa walipokuwa wakifuatilia mifugo iliyoibwa. Hata hivyo, viongozi na wakazi wa Samburu Mashariki sasa wanasema operesheni hiyo imesababisha hasara kubwa kwa familia zinazotegemea ufugaji kama chanzo kikuu cha maisha.Gavana wa Samburu, Lati Lelelit, alisema ingawa kaunti yake iliunga mkono juhudi za kuimarisha usalama, jinsi operesheni hiyo ilivyotekelezwa ilisababisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na uharibifu wa mali ya wananchi. "Matokeo yamekuwa mabaya sana, yakisababisha ukatili na mauaji ya kiholela ya mifugo ya wananchi," alisema.Idadi kamili ya mifugo iliyouawa bado inapingwa. Takwimu zilizowasilishwa katika Seneti zinaonyesha kuwa mbuzi 415 na ng'ombe 102 waliuawa katika Wadi ya Waso ndani ya siku tatu. Hata hivyo, Mbunge wa Samburu Mashariki Jackson Lekumontare alisema tathmini yake inaonyesha zaidi ya mbuzi 700, ng'ombe 500 na punda kadhaa waliangamia wakati wa operesheni hiyo. Kwa upande wake, Chama cha Wataalamu wa Samburu kimesema kimeorodhesha angalau wanyama 717 waliouawa, wakiwemo mbuzi 415, ng'ombe 352 na punda 50, huku uchunguzi ukiendelea. Chama hicho kinasema hasara hiyo haihusiani tu na mali bali pia maisha ya familia nyingi zinazotegemea mifugo kwa chakula, elimu ya watoto, huduma za afya na mapato ya kila siku. Tukio hilo lilichochea maandamano katika maeneo ya Samburu Mashariki huku wakazi wakitaka uchunguzi huru ufanywe na familia zilizoathirika zilipwe fidia.Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na mwenzake wa Samburu Lelegwe Ltumbesi pia wameitaka serikali kueleza mazingira yaliyosababisha mauaji hayo ya mifugo. Katibu Mkuu wa Chama cha Wanafunzi wa Vyuo Vikuu cha Samburu, Meshack Ramati, alitaka uchunguzi wa kina ufanywe kubaini idadi ya mifugo iliyouawa, maafisa waliohusika na walioidhinisha operesheni hiyo. "Serikali ina wajibu wa kulinda raia, mali yao na heshima yao. Tunataka uwazi, haki na fidia kwa familia zilizopoteza mifugo yao," alisema.Wakazi wanasema juhudi za kupambana na ujangili ni muhimu, lakini hazipaswi kufanywa kwa njia inayohatarisha maisha na uchumi wa wananchi wasio na hatia.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

Majengo ya kisasa yanavyoharibu utamu wa uswahili wa Mombasa

KWA miongo mingi, nyumba za jadi za muundo wa Waswahili zimekuwa alama muhimu ya utambulisho wa Mombasa. Hata hivyo, mandhari hiyo sasa inabadilika kwa kasi huku majengo marefu ya kisasa yakizidi kujengwa katika maeneo mbalimbali ya jiji. Katika mitaa ya Majengo, Kisauni, Old Town, Tudor na Ganjoni, nyumba za zamani za Waswahili zinabomolewa ili kupisha majengo ya ghorofa yanayolenga kukidhi ongezeko la mahitaji ya makazi. Mzee Abubakar Mohamed, mwenye umri wa miaka 90, anasema nyumba hizo zilijengwa kwa kuzingatia mazingira ya pwani yenye joto na unyevunyevu mwingi."Muundo wake uliwezesha hewa kupita kwa urahisi na kutoa hali ya baridi ndani ya nyumba. Pia uliakisi historia na utamaduni wa watu wa pwani," anasema. Kwa mujibu wa wakazi, ongezeko la thamani ya ardhi na mahitaji makubwa ya nyumba limewavutia wawekezaji wengi wanaotaka kujenga majengo ya kisasa katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa na nyumba za familia moja. Mkazi wa Majengo, Mohamed Hussein, ni mmoja wa walioamua kushirikiana na mwekezaji badala ya kuuza mali yake.Nyumba yake ilibomolewa na sasa jengo la ghorofa linaendelea kujengwa katika eneo hilo. Kupitia makubaliano yao, Hussein atamiliki nyumba sita ndani ya jengo hilo pindi mradi utakapokamilika. "Mwekezaji alinipa chaguo la kuuza au kushirikiana naye. Nilichagua ushirikiano kwa sababu nilitaka kuendelea kuwa na sehemu ya umiliki wa ardhi hiyo," alisema.Wakazi wengine wamechagua kuuza nyumba zao na kuhamia maeneo mengine, huku baadhi wakitumia fedha walizopata kuanza maisha mapya nje ya jiji.Lakini pamoja na faida za kiuchumi zinazotokana na miradi hiyo, wataalamu wanatahadharisha kuhusu hatari ya Mombasa kupoteza urithi wake wa kihistoria na usanifu wa kipekee. Mwenyekiti wa Chama cha Wasanifu Majengo Kenya (AAK) tawi la Pwani, Dancan Odhiambo, anasema ubomoaji wa nyumba za Kiswahili unafuta urithi ambao huenda usirejeshwe kamwe."Usasa haupaswi kuja kwa gharama ya utambulisho wa usanifu wa jiji. Vipengele vya nyumba za Kiswahili vinaweza kuingizwa katika majengo mapya ili kulinda utamaduni huo," anasema. Wataalamu pia wanaeleza kuwa ongezeko la majengo marefu linaweka shinikizo kwa miundombinu kama maji, mabomba ya maji taka, barabara, maegesho na mfumo wa ukusanyaji taka.Mbunifu Abdulnassir Mohamed anasema maendeleo hayawezi kuzuiwa, lakini yanahitaji mipango bora ili kuhakikisha ukuaji wa jiji unaendana na uwezo wa miundombinu iliyopo. "Mombasa inaweza kukua bila kupoteza utambulisho wake, lakini tunahitaji kueleza maana ya usanifu wa Mombasa katika majengo ya kisasa," anasema.Kadiri paa za nyumba za Kiswahili zinavyozidi kutoweka na majengo marefu kuchukua nafasi yake, Mombasa inakabiliwa na changamoto ya kusawazisha maendeleo ya kisasa na uhifadhi wa urithi wake wa kitamaduni,

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Kalonzo naye kutua Nyanza kuwinda ngome ya ODM baada ya Ruto

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, wikendi hii anatarajiwa kufanya ziara ya kisiasa katika maeneo ya Nyanza na Magharibi mwa Kenya katika juhudi za kuimarisha azma yake ya kuwania urais mwaka 2027, huku Rais William Ruto akiendelea kuongeza ushawishi wake katika ngome ambazo kwa muda mrefu zilijulikana kuwa za upinzani. Bw Musyoka ataanza ziara hiyo kwa kuzuru Bumala na Nambale katika Kaunti ya Busia leo kabla ya kuelekea Bondo, Kaunti ya Siaya, Jumapili. Akiwa Bondo, atahudhuria ibada katika Kanisa Kuu la St Michael's All Angels Cathedral na baadaye kufanya mikutano ya kukutana na wananchi. Ziara hiyo inampeleka moja kwa moja katika maeneo ambayo kwa miaka mingi yalikuwa msingi mkuu wa siasa za marehemu Raila Odinga. Pia inafanyika siku chache baada ya Rais Ruto kukamilisha ziara ya siku tano katika eneo la Nyanza, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kujijengea msingi mpya wa kisiasa katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa ngome za ODM na upinzani kwa jumla. Kwa wachanganuzi wa siasa, ziara ya Kalonzo ina umuhimu mkubwa katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Kiongozi huyo wa Wiper analenga kujenga uhusiano wa moja kwa moja na wapigakura wa Nyanza na Magharibi ambao kwa muda mrefu walimuunga mkono Raila katika kila uchaguzi. Kalonzo alikuwa mshirika wa karibu wa Raila kwa zaidi ya muongo mmoja. Mwaka 2013 alikubali kuweka kando azma yake ya urais na kuwa mgombea mwenza wa Raila kupitia muungano wa Coalition for Reforms and Democracy (CORD). Mwaka 2017 waligombea pamoja tena chini ya muungano wa National Super Alliance (NASA). Katika uchaguzi wa mwaka 2022, Kalonzo alibaki kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa kampeni za Azimio la Umoja One Kenya licha ya Raila kumteua Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake. Uhusiano huo wa muda mrefu ulimfanya Kalonzo kuwa sura inayofahamika sana katika kampeni za Nyanza. Hata hivyo, changamoto kubwa sasa ni jinsi ya kubadilisha urafiki huo wa kisiasa kuwa uungwaji mkono binafsi kutoka kwa wapigakura wa eneo hilo. Changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi kufuatia kifo cha Raila Odinga na mabadiliko ya kisiasa yaliyojitokeza baada yake. Baadhi ya washirika wa zamani wa Raila wameanza kushirikiana kwa karibu na serikali ya Kenya Kwanza huku wengine wakijaribu kuunda sura mpya ya upinzani. Kwa mujibu wa duru za kisiasa, Kalonzo anategemea ushirikiano wa Gavana wa Siaya James Orengo katika kuimarisha kampeni zake Nyanza. Orengo amebaki mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika eneo hilo licha ya kuhusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Ziara za Kalonzo katika Kaunti ya Busia nazo zina umuhimu wa kisiasa. Busia imekuwa sehemu ya maeneo ambayo kwa kawaida huunga mkono vyama vya upinzani. Hata hivyo, katika miezi ya hivi majuzi Rais Ruto ameongeza shughuli zake za kisiasa na maendeleo katika eneo hilo, akiwavutia baadhi ya viongozi wa eneo hilo kuunga mkono ajenda ya serikali. Ziara ya Rais katika kaunti za Kisumu, Siaya, Migori na Homa Bay ilijikita katika miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, huduma za maji, masoko, afya na elimu. Wachanganuzi wanasema mkakati huo umemsaidia kujenga taswira ya kiongozi anayelenga maendeleo badala ya siasa za mgawanyiko. Hali hiyo imeweka shinikizo jipya kwa viongozi wa upinzani ambao sasa wanapaswa kushindana si tu na ushawishi wa kisiasa wa Rais Ruto bali pia na mvuto wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali. Kwa upande mwingine, Kalonzo anaonekana kuwekeza zaidi katika siasa za mashinani na kujenga muungano mpya wa upinzani. Hatua hizi zinajiri baada ya muungano wa Azimio la Umoja kubadilishwa jina na kuitwa Ukombozi Alliance. Kalonzo amesema mabadiliko hayo ni sehemu ya mkakati wa kujiandaa mapema kwa uchaguzi wa mwaka 2027. Pia amekuwa akifanya mazungumzo na viongozi wengine wa upinzani akiwemo Justin Muturi, Eugene Wamalwa na Lenny Kivuti kuhusu mfumo bora wa kuunganisha upinzani. Hata hivyo, hesabu za kisiasa ndani ya upinzani zimeendelea kuwa tata kutokana na azma ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuwania urais kupitia chama chake cha Democracy for the Citizens Party (DCP). Kauli za viongozi wa DCP zimeonyesha kuwa bado kuna tofauti kuhusu jinsi muungano mpana wa upinzani utakavyoundwa. Kwa sasa, Kalonzo anakabiliwa na jukumu la kuthibitisha kuwa mvuto wake wa kisiasa unaweza kuvuka mipaka ya Ukambani na kupata uungwaji mkono katika maeneo yaliyokuwa ngome za Raila. Ziara yake ya Bondo inachukuliwa kuwa moja ya majaribio muhimu zaidi ya kupima uwezo wake wa kuvutia wapigakura wa Nyanza.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

Tutaenda wapi: Wakazi wa Nairobi walalamikia onyo kuhusu mafuriko ya El Nino

Wakazi wa maeneo yanayokumbwa na hatari ya mafuriko jijini Nairobi wanakabiliwa na changamoto kubwa huku serikali ikiendelea kuwaonya kuondoka katika maeneo hayo kabla ya mvua ya El Niño inayotarajiwa kuanza kunyesha mwishoni mwa mwaka. Kwa wengi wao, swali kuu si kama wanapaswa kuhama, bali watahamia wapi. Esther Makhokha, mkazi wa Mukuru Kayaba, bado anakumbuka mafuriko ya Machi mwaka huu. Anasema jioni moja mvua iliponyesha kwa nguvu, maji yalianza kuingia katika nyumba yake huku yeye na dada zake wawili wakitayarisha chakula. Kwa kukosa muda wa kufanya maamuzi, walichukua watoto na kuwapeleka katika baa iliyokuwa karibu ambayo haikuwa imezingirwa na maji. Baadaye, yeye na dada yake walilala kwa jirani wakisubiri maji yapungue. "Nililazimika kukimbia na watoto na kulala sakafuni kwa jirani. Sitaki kupitia hali hiyo tena," alisema. Makhokha, ambaye amekulia Mukuru Kayaba tangu utotoni, anasema hana mahali pengine pa kwenda iwapo mafuriko yatatokea tena. "Hata wakiniambia nihame, sina mahali pa kwenda. Sina pesa za kuhamia sehemu nyingine. Hapa ndipo nimeishi maisha yangu yote," alisema. Anasema wakati wa mafuriko yaliyopita hakupata usaidizi kutoka kwa serikali ya kaunti. Badala yake, waandishi wa habari walioenda kuripoti tukio hilo walimsaidia kwa chakula, mavazi, godoro na nepi za watoto. Mkazi mwingine wa Mukuru Kayaba, Immaculate Wavinya, anakabiliwa na changamoto sawa. Mama huyo anayelea mtoto peke yake amesema amehudhuria mikutano kadhaa ambapo wakazi wamehimizwa kuhama kutoka maeneo yanayokumbwa na mafuriko. Hata hivyo, anasema ushauri huo haujatiwa nguvu na msaada wa kuwawezesha wananchi kuhamia maeneo salama. "Familia yangu iko hapa. Biashara yangu iko hapa. Nimemlea mtoto wangu hapa tangu mwaka 2015. Nikiambiwa nihame, niende wapi na kwa pesa gani?" alihoji. Kulingana naye, wakazi wengi hawajaona juhudi za kutosha za serikali kuwasaidia kuhama. Katika eneo la Nairobi Dam karibu na Highrise, Ruth Mwikali pia anahofia mvua inayotarajiwa. Anasema amesikia onyo kuhusu El Niño lakini hajapewa mwongozo wa wazi kuhusu mahali pa kwenda iwapo makazi yao yatazingirwa na maji. Wasiwasi wa wakazi hawa unajiri huku serikali ya Kaunti ya Nairobi ikisema imeongeza maandalizi ya kukabiliana na mafuriko. Gavana Johnson Sakaja amesema maeneo kama Mukuru, Kibra, Mathare na sehemu za Ruaraka ni miongoni mwa maeneo ambayo huathiriwa mara kwa mara wakati mvua kubwa inapozidi uwezo wa mitaro ya kuondoa maji. Kaunti imesema inaendelea kusafisha, kupanua na kuchimba zaidi mitaro ya maji katika zaidi ya maeneo 36 yanayokumbwa na mafuriko. Pia imeanzisha vituo 27 vya uokoaji na makazi ya muda kwa watu watakaolazimika kuhama. Hata hivyo, kwa wakazi wengi wa mitaa ya mabanda, maandalizi hayo hayajibu swali lao kuu. "Hauwezi kuwaambia watu wahame bila kuwaonyesha mahali pa kwenda," alisema Mzee Francis Kaviti wa Mukuru Kayaba.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 18 hours ago

Jinsi ya kutambua walaghai wa mapenzi wanakunyemelea mtandaoni

Kadri watu wengi wanavyotumia mitandao na apu za kutafuta wachumba, ndivyo matapeli wa kimapenzi wanavyozidi kuwanasa waathiriwa wao. Utafiti wa TransUnion unaonyesha kuwa karibu Wakenya watatu kati ya kumi wanaotumia apu za uchumba mtandaoni wamewahi kukumbana na jaribio la ulaghai. Zaidi ya asilimia 80 ya Wakenya pia wanasema wamewahi kulengwa na walaghai wa kidijitali kupitia simu zao. Mtaalamu wa usalama wa mitandao na mshirika wa kampuni ya Techrise, Polycap Oliver Oluoch Ochieng, anasema ishara ya kwanza ya tahadhari ni mtu kuharakisha mapenzi. "Ikiwa mtu anaanza kukutamkia mapenzi ndani ya siku chache kabla hata ya mawasiliano ya kawaida kama simu ya video, hilo ni jambo la kutiliwa shaka," anasema. Pia anaonya kuhusu watu wanaokwepa mawasiliano ya video au mikutano ya ana kwa ana kwa kutoa visingizio mbalimbali kama kamera kuharibika au kuwa mbali kikazi. Kwa mujibu wake, matapeli mara nyingi hutumia picha za kuvutia zilizoibwa mitandaoni na hujenga wasifu unaoonekana mkamilifu kupita kiasi. "Mfano ni mtu  kuchapisha picha za kitaalamu pekee bila picha za kawaida akiwa na marafiki au familia. Hiyo ni ishara ya tahadhari," anasema. Anashauri watumiaji kufanya uchunguzi wa picha mtandaoni ili kubaini iwapo zimeibwa kutoka kwa wanamitindo au watu maarufu. Mtaalamu huyo pia anatahadharisha kuhusu watu wanaoharakisha kuhamisha mazungumzo kutoka apu za uchumba hadi WhatsApp au Telegram ambako ni vigumu kufuatilia ulaghai. Kwa kawaida, matapeli huanza kwa kuomba kiasi kidogo cha pesa kama vocha ya simu au mkopo mdogo. Baada ya kuona mwathiriwa yuko tayari kusaidia, huanza kuomba fedha nyingi zaidi kwa madai ya dharura za hospitali, usafiri au uwekezaji. "Ikiwa mtu anaomba pesa kwa sababu yoyote ile, huo ni wakati wa kusitisha mawasiliano," anasema Oluoch. Mshauri wa masuala ya mahusiano Benjamin Zulu anasema watu wanaotafuta mapenzi mtandaoni hawapaswi kutegemea mawasiliano ya mtandaoni pekee. "Mtandao unaweza kuwa sehemu ya kukutana, lakini uhusiano wa kweli hujengwa kupitia mawasiliano ya ana kwa ana," anasema. Zulu anaongeza kuwa mtu anayekwepa kukutana ana kwa ana huenda ana jambo la kuficha. Pia anawahimiza watu kutotoa taarifa za kibinafsi kama anwani ya nyumbani, nambari ya kitambulisho au hali zao za kifedha kabla ya kuwa na imani kamili kwa mtu huyo. Anashauri watu kuwa waangalifu hasa wanapopitia maumivu ya moyo au upweke, kwani hali hiyo huwafanya kuwa rahisi kudanganywa. Kwa maoni yake, mapenzi ya kweli hayapaswi kuhusisha maombi ya pesa. "Usichukue mkopo wala kutumia akiba yako kumsaidia mtu uliyekutana naye mtandaoni," anasema. Wataalamu wanashauri watu kufanya simu za video kabla ya kuwekeza hisia zao, kuchagua maeneo ya wazi wanapokutana kwa mara ya kwanza na kuwafahamisha marafiki au jamaa kuhusu mahali walipo. Aidha, yeyote anayeshuku ulaghai anaweza kuripoti kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kupitia nambari ya bure 0800 722 203 au kwa simu za dharura za polisi 999, 911 au 112.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Kaa chonjo: Maeneo hatari kwa ghasia za kisiasa 2027 yamulikwa

HUKU Kenya ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 10, 2027, wasiwasi unazidi kuongezeka kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa ghasia za kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini. Wiki za hivi majuzi zimeshuhudia visa vya vurugu katika mikutano ya kisiasa huko Homa Bay, Embu na Garissa, hali ambayo imeibua hofu kuwa siasa za ushindani huenda zikachochea ukosefu wa usalama kama ilivyoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita. Mashambulizi dhidi ya viongozi wa muungano wa Linda Mwananchi mjini Homa Bay na vurugu zilizoripotiwa katika mkutano wa kisiasa Nembure, Embu, ni baadhi ya matukio ambayo yamefanya hali ya kisiasa nchini kuwa katika hali ya taharuki. Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, na washirika wake pia walilazimika kuondoka haraka Garissa baada ya kukumbana na mazingira yaliyotishia usalama wao. Kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR), watu wasiopungua 11 wamepoteza maisha tangu Februari mwaka huu kutokana na matukio yanayohusishwa na mikutano ya kisiasa nchini. Tume hiyo imeonya kuwa mivutano inayoshuhudiwa katika maeneo kama mpaka wa Turkana na West Pokot, Isiolo, Embu na kaunti nyingine ni ishara ya hatari inayopaswa kushughulikiwa mapema kabla ya uchaguzi. "Tunahitaji kulinda haki za msingi kabla hazijakiukwa, si baada ya madhara kutokea," ilisema KNCHR ikitaka uchunguzi wa kina kufanywa kuhusu visa vyote vya vurugu. Kwa upande wake, Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imezidi kuwaonya wanasiasa dhidi ya matumizi ya lugha za uchochezi na kuajiri vijana kutekeleza mashambulizi dhidi ya wapinzani wao. Mwenyekiti wa NCIC, Kepha Nyamweya Omae, alisema vijana wanapaswa kushirikishwa katika demokrasia kwa njia halali badala ya kutumiwa kama silaha za kisiasa. Wataalamu wa masuala ya usalama wanasema maeneo hatari ya ghasia za uchaguzi nchini yamebakia karibu yale yale kwa miaka mingi. Mtaalamu George Musamali anasema Nairobi, sehemu za Bonde la Ufa, Mombasa, Homa Bay, Migori, Kisii na Kiambu zinaendelea kuonekana kuwa maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kushuhudia vurugu. Maeneo yaliyotajwa mara kwa mara kama yenye uwezekano mkubwa wa kushuhudia ghasia za kisiasa ni Nairobi, Nakuru, Kericho, Kisumu, Uasin Gishu, Mombasa, Homa Bay, Migori, Kisii, Kiambu, sehemu za Bonde la Ufa, Turkana-West Pokot, Isiolo, Embu, Kitengela, Bungoma, Kakamega, Nandi na Marsabit. Haya ni maeneo yaliyotambuliwa kutokana na historia ya vurugu za uchaguzi, mivutano ya kisiasa, migogoro ya ardhi, tofauti za kikabila na ushindani wa kisiasa. "Kila uchaguzi tangu mfumo wa vyama vingi urejee mwaka 1992 umeshuhudia aina fulani ya ghasia. Mara nyingi maeneo hayo hubakia yale yale kwa sababu siasa zetu zimejengwa kwenye misingi ya kikabila," alisema Bw Musamali. Aidha, ameonya kuhusu kuibuka kwa makundi ya vijana wanaotumiwa na wanasiasa kuvuruga mikutano ya wapinzani na kuzua hofu miongoni mwa wapiga kura. Ripoti mbalimbali zimeonyesha kuwa ghasia za uchaguzi nchini mara nyingi huchochewa na mchanganyiko wa siasa za kikabila, migogoro ya ardhi, malalamishi ya kihistoria na ukosefu wa usawa katika ugavi wa rasilimali za umma. Mwanaharakati wa haki za binadamu Ernest Cornel anaeleza kuwa vurugu zinaweza kutokea kati ya jamii tofauti au hata ndani ya jamii moja kulingana na maslahi ya kisiasa na kijamii yanayokinzana. "Kuna maeneo ambapo migogoro ya ardhi na mipaka imeendelea kwa muda mrefu. Siasa zinapoingilia kati, baadhi ya watu huona kama fursa ya kulipiza kisasi," alisema. Takwimu zinaonyesha kuwa ghasia za uchaguzi wa 2007/2008 zilisababisha vifo vya takriban watu 1,300 na kuwafanya zaidi ya watu 650,000 kuhama makazi yao. Ingawa Kenya imepiga hatua kubwa tangu wakati huo, wataalamu wanaonya kuwa dalili zinazoonekana sasa zinafanana na zile zilizotangulia migogoro ya zamani. Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga pia ameonya kuhusu umuhimu wa kuwa na Idara za usalama ambazo haziegemei upande wowote, akisema upendeleo wa kisiasa ndani ya taasisi za usalama unaweza kutumbukiza nchi katika machafuko. Kampeni za uchaguzi zinapoanza kushika kasi, wadau wa kisiasa, asasi za kiraia na idara za usalama wanahimizwa kushirikiana ili kuzuia kurejea kwa historia ya vurugu. Swali kuu sasa ni iwapo Kenya itazingatia ishara hizi za tahadhari au itasubiri hadi madhara yatokee tena.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 15:45:17

Pombe haramu yaua watatu Kitengela, wawili mahututi

Huzuni imetanda katika kijiji cha Noonkpoir, Kitengela, Kaunti ya Kajiado, baada ya watu watatu kufariki dunia na wengine wawili kulazwa hospitali wakiwa mahututi kutokana na kile kinachoshukiwa kuwa pombe haramu. Mnamo Ijumaa asubuhi, Christine na jamaa zake waliomboleza kifo cha mumewe, James Maina Nguru, aliyefariki Jumatatu usiku baada ya kunywa pombe hiyo. Kwa mujibu wa wakazi, waathiriwa hao walikunywa pombe hiyo katika eneo la Migingo jioni ya Jumatatu kabla ya kufariki nyakati tofauti karibu na makazi yao. Migingo, eneo lililoko Kitengela, limekuwa likihusishwa kwa miaka kadhaa na biashara ya pombe haramu, dawa za kulevya na uhalifu. Bi Mukeira alisema mumewe, aliyekuwa fundi na baba wa watoto watatu, alirejea nyumbani akiwa katika hali mbaya baada ya kutoka kwenye baa maarufu eneo hilo. "Alikuwa akilalamika maumivu makali ya tumbo na hakuweza kusimama vizuri. Muda mfupi baadaye alianza kutapika damu na akafariki mbele yetu," alisema kwa huzuni. Sasa mjane huyo anasema amelazimika kulea watoto wao peke yake. Familia hiyo imeamua kutofanya uchunguzi wa maiti kutokana na hali ngumu ya kifedha na imani kuwa pombe ndiyo iliyosababisha kifo chake. Mama yake Nguru, Mary Muthoni, ameitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaosambaza pombe hatari. Alisema mara nyingi alimuonya mwanawe kuhusu madhara ya pombe lakini hakumsikiliza. Katika eneo hilo hilo, Lynette Sirengo pia anaomboleza kifo cha mumewe, Godfrey Simiyu Kiliswa, aliyefariki baada ya kupatikana akiwa hajitambui karibu na baa inayojulikana kama "Kwa Omosh". Alifariki siku iliyofuata nyumbani kwake. Mwanaume mwingine, Elisha Okello, naye alifariki baada ya kurejea nyumbani akiwa amelewa. Mwili wake ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Kitengela. Wakati huo huo, ndugu wa mmoja wa manusura amesema mgonjwa amelazwa katika hospitali moja jijini Nairobi akiwa katika hali mahututi, huku viungo vya ndani vikidaiwa kuathiriwa vibaya. Wakazi wamewalaumu maafisa wa usalama kwa kushindwa kudhibiti uuzaji wa pombe haramu, madai ambayo polisi wamekanusha wakisema wameimarisha msako dhidi ya wauzaji wa vileo haramu na dawa za kulevya. Serikali pia imeagiza operesheni kali kote nchini kukabiliana na biashara hiyo inayozidi kuhatarisha maisha ya wananchi

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 15:06:49

Ushindi kwa serikali Mahakama ya Rufaa ikiunga ushuru wa nyumba

Mpango wa Rais William Ruto wa nyumba za bei nafuu umepata nguvu kubwa baada ya Mahakama ya Rufaa kuidhinisha sheria ya makazi nafuu na ushuru wa nyumba, huku ikitupilia mbali kesi 42 zilizopinga sheria hiyo. Katika uamuzi wake, jopo la majaji watano lilisema Sheria ya Makazi Nafuu ilitungwa ili kutekeleza haki ya kila Mkenya kupata makazi bora na ya kutosha kama ilivyo katika Katiba. Mahakama ilikataa hoja za waliowasilisha kesi wakitaka sheria hiyo itangazwe kuwa batili na serikali iamriwe kurejesha mabilioni ya pesa ilizokusanywa kupitia ushuru huo kutoka kwa waajiri na wafanyakazi. Kwa mujibu wa sheria hiyo, mwajiri na mfanyakazi huchangia kila mmoja asilimia 1.5 ya mshahara  wa mfanyakazi kila mwezi kwa Hazina ya Makazi Nafuu. Waliopinga sheria hiyo, akiwemo daktari wa upasuaji kutoka Nakuru, Magare Gikenyi, walidai ushuru huo unawalazimisha Wakenya kugharamia nyumba ambazo huenda wasinufaike nazo kamwe. Pia walidai kuwa jukumu la makazi ni la serikali za kaunti na kwamba serikali kuu ilikiuka Katiba kwa kulitwaa. Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa ilisema makazi ni jukumu kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti, hivyo sheria hiyo haikiuki mfumo wa ugatuzi. Majaji waliongeza kuwa ushuru huo hauwezi kutajwa kama ubaguzi au unyakuzi haramu wa mali kwa kuwa serikali ina mamlaka ya kuweka kodi ili kutekeleza majukumu yake ya kikatiba. Hata hivyo, mahakama ilionya kuwa mpango huo unapaswa kuhakikisha pia unawanufaisha Wakenya maskini zaidi na usitumike kuwanufaisha washirika wa kisiasa au watu wenye ushawishi pekee. Uamuzi huo unaimarisha moja ya miradi mikuu ya Rais Ruto inayolenga kuongeza upatikanaji wa nyumba nafuu nchini.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 15:10:21

Amisi ampigia debe Matiang'i, asema kiti cha chini anachoweza kupata ni unaibu wa rais

MBUNGE wa Saboti, Caleb Amisi, amesema kiti cha chini kabisa ambacho kiongozi wa Jubilee, Dkt Fred Matiang'i, anaweza kukubali katika muungano wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 ni Unaibu Rais, kama si tiketi ya kuwania urais yenyewe. Amisi alisema hayo alipozuru kaunti ya Kisii mnamo Alhamisi, Septemba 24, kuwa ni kudhalilisha kumzungumzia Matiang'i kwa vyeo vya chini kama Uwaziri, akisema aliyekuwa Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ameshavuka kiwango hicho. "Mtu kama Fred Matiang'i, kiti cha chini kabisa anachoweza kupewa ni Unaibu wa Rais. Kama si hivyo, basi apewe tiketi ya Urais. Hatuwezi kumzungumzia tena kama mtu wa kupewa Wizara. Amepita hapo," Amisi alisema. Mbunge huyo alikuwa Kisii kukipigia debe chama chake kipya cha People's Renaissance Movement (PRM) na kujenga uungwaji mkono wa Dkt Matiang'i katika eneo la Gusii. Kwenye ziara yake, Amisi alikutana na makundi ya vijana na kina mama katika mikutano ya hoteli na ya barabarani maeneo ya Keumbu na Kisii Mjini, ambako alielezea dira ya chama chake na msimamo wake kuhusu mustakabala wa upinzani. Alisema upinzani unapojipanga kumkabili Rais William Ruto, lazima uonyeshe heshima kwa viongozi wenye uzito wa kitaifa kama Dkt Matiang'i. "Kuna tabia ndani ya upinzani ya kutaka kumpunguza Matiang'i hadi nafasi ya uwaziri. Hiyo ni dharau kubwa. Mtu aliyesimamia wizara kubwa kama Mambo ya Ndani na Elimu, akaonyesha uwezo wa kipekee, si mtu wa kupewa tena nafasi ya waziri. Ameshavuka hapo," alisema Amisi. Aliongeza kuwa Matiang'i ndiye kiongozi anayefaa zaidi kuongoza muungano wa upinzani kutokana na uzoefu wake serikalini na mtindo wake wa uongozi unaoaminika. "Ukizungumzia viongozi ambao wamewahi kuendesha serikali kwa msimamo na nidhamu, Matiang'i yuko juu. Ndiyo maana tunasema kama hatutampatia urais, basi angalau tumpatie unaibu. Chini ya hapo ni kumkosea heshima jamii nzima ya Gusii na Wakenya wanaomuamini," alisisitiza. Amisi alisema chama chake cha PRM kimejipanga kuzunguka maeneo mbalimbali nchini kuimarisha umoja wa vijana na kina mama ambao ndio wamekuwa wakisahaulika licha ya kuwa na kura nyingi. Alisema jamii ya Gusii imekuwa na mchango mkubwa katika siasa za taifa lakini imekuwa ikipata nafasi ndogo katika uongozi wa juu, na wakati huu inastahili kupata nafasi kubwa kupitia Matiang'i. "Gusii imekuwa na kura, imekuwa na viongozi wazuri, lakini haijawahi kupata nafasi ya juu. Wakati huu msikubali makombo. Lazima muwe mezani, na njia ya kuwa mezani ni kumpa Matiang'i tiketi ya juu," alisema. Kauli ya Amisi inakuja wakati viongozi wa upinzani wakiendelea na mazungumzo ya kuunda umoja mpana wa kumkabili Rais Ruto, huku mgawanyo wa nafasi ukiwa kitovu cha mvutano.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 10:13:16

Wakenya 49 miongoni mwa maelfu wanaosubiri kutimuliwa na Trump kutoka Amerika

Raia 49 wa Kenya ni miongoni mwa maelfu ya watu walio katika orodha mpya ya wanaosubiri taratibu za kufurushwa kutoka Amerika. Majina na picha za Wakenya hao zimechapishwa hadharani kama sehemu ya msako mpana wa maafisa wa Amerika dhidi ya wahamiaji wanaokiuka sheria za uhamiaji. Idara ya Usalama wa Taifa ya Amerika (DHS) imechapisha hifadhidata maarufu inayoorodhesha raia 125 kutoka Afrika wanaosubiri kuondolewa nchini humo katika siku zijazo, huku Wakenya 49 wakiongoza orodha hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi kutoka taifa moja. DHS imepanua hifadhidata yake inayojulikana kama "Wabaya zaidi", inayolenga watu wasiokuwa raia wa Amerika walio na rekodi za uhalifu na wanaotafutwa kuzuiliwa na kufurushwa kutoka nchi hiyo. Ingawa orodha ya awali au utekelezaji wa mpango huo katika maeneo tofauti ilikuwa na idadi ndogo ya Wakenya, kama vile watu 15 au 45, ripoti za hivi majuzi zinaonyesha kuwa Wakenya 49 sasa wako katika kampeni mpya ya utekelezaji wa sheria za uhamiaji. Kulingana na takwimu za Shirika la Uhamiaji na Utekelezaji wa Sheria za Forodha la Amerika (ICE), raia 1,282 wa Kenya wako kwenye orodha ya watu ambao wana maagizo ya mwisho ya kuondolewa nchini lakini hawajazuiliwa. Wakenya hao ni sehemu ya orodha inayojumuisha zaidi ya watu milioni 1.4 wasio raia wa Amerika kutoka mataifa 187 duniani. Takwimu hizo zinaonyesha kuimarishwa kwa hatua za utekelezaji wa sheria za uhamiaji nchini Amerika, hali ambayo imezua wasiwasi mkubwa na changamoto za kisheria miongoni mwa jamii ya Wakenya wanaoishi nchini humo. Mbali na kundi hilo la watu ambao hawajazuiliwa, kuna idadi ndogo ya Wakenya waliohukumiwa kwa makosa makubwa ya jinai ambao wamewekwa katika orodha maalum za DHS za watu wanaopewa kipaumbele katika hatua za kufurushwa. Wakenya wanaongoza orodha hiyo kwa watu 49, wakifuatwa na raia 44 wa Ghana. Aidha, taarifa nyingine ya DHS inaonyesha kuwa raia 112 wa Nigeria 112 pia wanasubiri kufurushwa kutoka Amerika. Mauritania ina watu 12 kwenye orodha hiyo, Morocco 11 huku Afrika Kusini ikiwa na watu tisa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 08:34:43

Viongozi watuzwa kwa uongozi bora

AFISA Mkuu Mtendaji wa Shirika la Usambazaji Umeme Maeneo ya Mashambani (REREC) ni miongoni mwa viongozi wa kampuni na mashirika ya umma na ya kibinafsi waliotambuliwa kwa uongozi bora na mchango wao katika mageuzi ya kijamii na kiuchumi nchini Kenya. Dkt Rose Mkalama alituzwa Afisa Mkuu Mtendaji bora wa mwaka wakati wa makala ya pili ya East Africa Leadership Awards, kwa uongozi wake katika kupanua upatikanaji wa umeme nchini kupitia Mpango wa Last Mile Connectivity. Chini ya juhudi za kitaifa za kusambaza umeme, kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini Kenya kimeongezeka hadi zaidi ya asilimia 76, kutoka karibu asilimia 27 mwaka 2013. Kulingana na Dkt Mkalama, tuzo hiyo si mafanikio yake binafsi pekee, bali ni utambuzi wa kazi inayofanywa na REREC kuhakikisha umeme unawafikia maelfu ya Wakenya katika maeneo ya vijijini na mashambani. "Nina furaha kuwa REREC imeweza kufikia maelfu ya Wakenya katika karibu kila kijiji nchini kupitia Mpango wa Last Mile Connectivity," alisema. REREC ilipoanzishwa, kiwango cha kuunganishwa kwa umeme nchini kilikuwa takriban asilimia 8. Afisa Mkuu Mtendaji huyo wa shirika hilo alisema ongezeko hilo limechangiwa na ufadhili wa serikali, ushirikiano na wabunge pamoja na utekelezaji endelevu wa miradi ya usambazaji umeme katika maeneobunge yote 290 nchini. [caption id="attachment_192455" align="aligncenter" width="300"] Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Usambazaji Umeme Maeneo ya Mashambani (REREC), Dkt Rose Mkalama akizungumza awali. Picha|Hisani[/caption] Anasema manufaa ya umeme yameendelea kuyapa maboma mwangaza, ikizingatiwa yamesaidia kufanikisha elimu, afya, kilimo na biashara, na hivyo kuwezesha jamii kushiriki zaidi katika maendeleo ya kiuchumi. "Kwa sasa, tunatekeleza miradi inayolenga kuunganisha taasisi za umma na jamii kwenye huduma za umeme, huku mipango ya usambazaji umeme kupitia gridi ikilenga kufikia mamia ya maelfu ya wateja," Dkt Mkalama akadokeza. Viongozi wengine waliotuzwa ni pamoja na Dkt Lilian Nyawada, Kamishna wa Forodha na Udhibiti wa Mipaka katika Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA), na Dkt David Okeyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Nutrition and Dieticians Institute. Kabla ya kutawazwa viongozi bora, huduma za mashirika na kampuni zao zilipigwa msasa na jopo la majaji mashuhuri kutoka World Human Resource Congress, wasimamizi wa huduma za wafanyakazi kutoka India na viongozi tajika wa kijamii. Akizungumza wakati wa kuwatuza, Mkuu wa Kitengo cha Bionuwai, Ujumuishaji na Haki za Watu wenye Mahitaji Maalum (Head of the Office of Diversity, Inclusion and Disability Rights in the Executive Office of the President) katika Afisi ya Rais, Isaac Mwaura, aliwataka viongozi wa taasisi za umma na kibinafsi kuhamasisha wafanyakazi wao kujitahidi kutoa huduma bora. "Uongozi haupaswi kupimwa kwa cheo pekee, bali pia kwa urithi ambao viongozi wanaacha katika taasisi na jamii," Mwaura akasema. Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mt Kenya Prof Bindu Madhavi, pia alitambuliwa kwa tuzo ya Profesa mwenye ushawishi mkubwa kutokana na mchango wake katika elimu, utafiti, kunoa wanafunzi makali na masuala ya dawa na sayansi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 08:55:51

Maoni mseto Rais akimpa mzee wa Waluo gari ya mamilioni kama zawadi

ZAWADI ya gari jipya aina ya Toyota Prado TX lililotolewa na Rais William Ruto kwa mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Luo, Ker Odungi Randa, imeibua mjadala mkali wa kisiasa katika eneo la Nyanza. Gari hilo la thamani ya mamilioni lilifikishwa nyumbani kwa Bw Randa katika eneo la Boya na maafisa kutoka afisi ya Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, siku chache baada ya kiongozi huyo wa kitamaduni kumuomba Rais msaada wa usafiri wakati wa ziara yake katika eneo hilo. Kwa mujibu wa taarifa, ombi hilo lilitolewa wakati wa mkutano uliofanyika Homa Bay, ambapo Rais aliahidi kulitekeleza. Afisa kutoka afisi ya Dkt Omollo, Bw Charles Osako, alisema Rais alitimiza ahadi yake kwa Baraza la Wazee wa Luo na kwamba gari hilo litasaidia shughuli na majukumu ya wazee hao. "Gari hili linaonyesha kutambuliwa kwa mchango muhimu wa wazee na viongozi wa kitamaduni katika kuhifadhi maadili, mila na utambulisho wetu," alisema Bw Osako. Mbunge wa Lang'ata, Phelix Jalango Odiwuor, ambaye alishuhudia mazungumzo hayo, alisema baada ya mkutano wa mwisho wa hadhara Migori, Dkt Omollo alimwalika kuhudhuria kikao kati ya Rais na viongozi wa Baraza la Wazee wa Luo. Alisema mwishoni mwa mkutano huo, Bw Randa alimuomba Rais amsaidie kupata gari la kurahisisha shughuli zake za kila siku. "Kwa utulivu, Rais alimwambia angepata gari Ijumaa. Leo asubuhi timu ya Dkt Omollo imekabidhi gari hilo jipya aina ya Toyota Prado," alisema Bw Odiwuor baada ya gari kuwasilishwa. Bw Randa alipokea funguo za gari hilo na kulijaribu kabla ya kurejea nyumbani kwake. "Nashukuru Rais Ruto kwa zawadi hii. Itanisaidia kusafiri na kukutana na Waluo walioko Nairobi, Mombasa, Uganda, Tanzania na maeneo mengine mengi," alisema. Hata hivyo, zawadi hiyo imezua maswali kuhusu uhuru wa Baraza la Wazee wa Luo, ambalo kwa kawaida halifai kuzingatia siasa za vyama na linatarajiwa kuwa sauti ya maridhiano katika jamii. Wakosoaji wanasema kupokea gari kutoka kwa Rais kunaweza kuathiri msimamo wa baraza hilo, hasa wakati ushindani wa kisiasa kati ya vyama vya UDA na ODM unaendelea kushika kasi Nyanza. Mkazi wa Kisumu, Bw Martin Oria, alihoji jinsi baraza hilo litakavyodumisha kutopendelea upande wowote wakati litakapohitajika kutatua mizozo ya kisiasa. Lakini wengine wametetea zawadi hiyo, wakisema viongozi mbalimbali wa kitaifa wamekuwa wakiwasaidia wazee wa jamii kwa miaka mingi. Kwa mujibu wa David Dimba Jakobuya, Bw Randa ni mmoja wa wazee wachache waliosalia ambao walishiriki katika harakati za ukombozi wa kwanza na wa pili nchini Kenya. Alisema amekuwa akikabiliwa na changamoto za usafiri tangu gari lake la awali lilipoibwa miaka kadhaa iliyopita. Akijibu ukosoaji huo, Bw Randa alisema wale wanaopinga zawadi hiyo hawakuwahi kujitokeza alipokuwa akikosa usafiri.  "Sikusikia mtu yeyote akilalamika kwa niaba yangu wakati sikuwa na gari. Sasa nimepewa gari, kila mtu ana maoni. Marais wengine pia wamekuwa wakitoa zawadi kwa watu wengi nchini," alisema. Wakati huo huo, baadhi ya wakazi wamehoji iwapo gari hilo ni mali ya Bw Randa binafsi au ya Baraza la Wazee wa Luo. Hata hivyo, kiongozi huyo amesisitiza kuwa ni zawadi ya kibinafsi aliyopewa na Rais kufuatia ombi lake. Mjadala huo umechukua sura ya kisiasa zaidi baada ya Bw Randa kutoa wito kwa jamii ya Waluo kumuunga mkono Rais Ruto katika azma yake ya kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu ujao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 08:57:46

Karua ashtaki Uganda kwa kumtimua asiwakilishe Besigye

Kiongozi wa Chama cha People's Liberation Party (PLP) na aliyekuwa Waziri wa Haki nchini Kenya, Martha Karua, amewasilisha kesi katika mahakama ya Uganda akitaka kubatilishwa kwa uamuzi wa kufurushwa kwake nchini humo na kuruhusiwa kurejea ili kumwakilisha kiongozi wa upinzani, Dkt Kizza Besigye, na mshtakiwa mwenzake. Besigye aliyekamatwa akiwa Nairobi Nairobi mwaka 2024 anakabiliwa na kesi ya uhaini. Bi Karua, kwa ushirikiano na Chama cha Wanasheria cha Uganda (Uganda Law Society), wanapinga uamuzi uliotolewa Juni 22 na Afisa Mkuu wa Uhamiaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe wa kumzuia kuingia nchini Uganda na kutangaza kuwa  mtu asiyehitajika nchini humo. Wanasema uamuzi huo ulikuwa kinyume cha sheria na ulifanywa bila kumpa nafasi ya kujitetea au kusikilizwa. Kupitia Kitengo cha Malalamishi cha Mahakama Kuu mjini Kampala, Karua anataka mahakama ibatilishe uamuzi huo na kuzuia maafisa wa uhamiaji kuingilia haki yake ya kuingia Uganda ili kutekeleza majukumu yake ya kitaaluma kama wakili. Katika hati zake za kesi, Karua anaeleza kuwa alisafiri kwenda Uganda Juni 22 ili kuwakilisha Dkt Besigye na Hajj Obeid Lutale baada ya kupata Cheti Maalum cha Uwakili kilichomruhusu kufanya kazi katika mahakama za Uganda. Anasema maafisa wa uhamiaji walimzuia kuingia nchini humo, wakachukua simu zake na baadaye wakampatia notisi ya kumtaka arejee Kenya. Dkt Besigye na Bw Lutale walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini na makosa mawili ya kuficha taarifa kuhusu uhaini. Upande wa mashtaka unadai walihusika katika njama za kupindua serikali ya Uganda. Mashtaka hayo yalitokana na kukamatwa kwa wawili hao jijini Nairobi mnamo Novemba 2024. Awali walifikishwa mbele ya Mahakama ya Kijeshi ya Uganda kabla ya kuhamishiwa mahakama za kiraia kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu uliosema kuwa raia hawawezi kushtakiwa katika mahakama za kijeshi. Baadaye walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkuu ya Nakawa mnamo Februari 21, 2025. Hatua ya Karua kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Uganda kutokana na vitendo vya maafisa wa uhamiaji imefuatia ombi la awali lililowasilishwa na Dkt Besigye na Bw Lutale kuhusu suala hilo hilo. Mahakama Kuu ilikataa kuamua iwapo uamuzi wa uhamiaji ulikuwa halali, ikisema kuwa changamoto hiyo ilipaswa kuwasilishwa kupitia mchakato wa mapitio ya mahakama, na hivyo ikatupilia mbali ombi hilo. Karua na Chama cha Wanasheria cha Uganda wanataka mahakama itangaze kuwa uamuzi huo ulikuwa haramu, wa kiholela, usio na sababu za msingi na uliofanywa kinyume cha taratibu zinazotakiwa kisheria. Pia wanataka mahakama iubatilishe, kuagiza mamlaka za uhamiaji kutathmini upya suala hilo, na kutoa amri ya kudumu ya kutomzuia kuingia Uganda kwa madhumuni ya kitaaluma. "Uamuzi huo ni haramu, hauna mantiki na ulifanywa kinyume cha taratibu zinazotakiwa na sheria," walisema. Katika kiapo chake cha kuunga mkono kesi hiyo, makamu wa rais wa Chama cha Wanasheria cha Uganda, Anthony Asiimwe, alisema Karua ni Wakili Mkuu na anamiliki Cheti Maalum cha Uwakili kilichotolewa chini ya Kifungu cha 18 cha Sheria ya Mawakili. Alisema cheti hicho kilimruhusu kuongoza timu ya utetezi katika kesi  inayowahusu Besigye na Lutale. Asiimwe alieleza kuwa alisafiri hadi Entebbe kumpokea Karua baada ya kuwasili kutoka Kenya, lakini akakuta maafisa wa uhamiaji tayari wamemzuia kuingia nchini. Walalamishi hao wanasisitiza kwamba Karua hakupatiwa nafasi ya kusikilizwa wala sababu zinazokidhi kanuni za haki za asili kabla ya uamuzi huo kufanywa. Wanasema hatua hiyo ilikiuka Katiba ya Uganda, Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pamoja na misingi inayolinda uhuru wa taaluma ya sheria. Kwa mujibu wao, Karua amepata hasara kitaaluma na kifedha kwa sababu hawezi kurejea Uganda kutekeleza majukumu yake. "Mlalamishi wa pili ameendelea kupata madhara makubwa ya kitaaluma na jina lake kuharibiwa baada ya kutangazwa hadharani kuwa ' mtu asiyetakiwa' bila msingi wowote wa kisheria," alisema Asiimwe. Kabla ya kuwasilisha kesi hiyo, Chama cha Wanasheria cha Uganda kilijaribu kutafuta suluhu kupitia njia za kiutawala. Barua zilizoambatishwa katika kesi zinaonyesha kuwa chama hicho kiliwaomba maafisa wa Uganda kufuta uamuzi huo na kumruhusu Karua kuingia nchini. Hadi sasa, Mwanasheria Mkuu wa Uganda hajawasilisha majibu kuhusu madai yaliyomo katika kesi hiyo mpya.

read more