taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 13 Sep 2026 06:55:12
Gachagua afichua sababu kutotaja mwaniaji urais wa upinzani mapema
KINARA wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, amesema upinzani umeamua kuchelewesha kuunda afisi ya pamoja kwa sababu ya hofu ya kuingiliwa na serikali, huku akisisitiza kuwa lengo lao kuu ni kumng'oa Rais William Ruto mamlakani katika uchaguzi mkuu mwaka ujao. Akizungumza Ijumaa jioni mbele ya wafuasi wake mjini Portland, Oregon, Amerika anakozuru, Bw Gachagua alidai Rais William Ruto atashindwa kwa tofauti ya kura zaidi ya milioni saba. Alisema anatarajia kupokea simu kutoka kwa Rais Ruto usiku wa manane wa Agosti 10, 2027, akikubali kushindwa na kuomba kulindwa baada ya kuondoka madarakani. Gachagua pia alidai Rais amepenyeza watu wake ndani ya baadhi ya makundi ya upinzani ili kupata taarifa za siri kuhusu mikakati yao. "Majuzi tulikuwa katika kikao cha mkakati katika hoteli moja Nairobi. Kulikuwa na mmoja wa viongozi wa upinzani aliyekuwa amejiunga na muungano wetu akiwa na wanawake wawili. Hatukuwa hata tumemaliza kikao nilipoona taarifa ya kile tulichokuwa tunajadili ikiibuka kwenye simu yangu," alisema. Hata hivyo, alionya kuwa serikali ya upinzani haitawalinda wale watakaopatikana na makosa ya ufisadi, mauaji au utekaji nyara wa vijana waliokuwa wakishiriki maandamano. "Nataka iwe wazi kuwa serikali ya upinzani haitawalinda wezi wa rasilimali za umma, wauaji au waliotekeleza utekaji nyara. Wote watawajibishwa kwa mujibu wa sheria," alisema. Gachagua pia alikanusha madai kwamba anapanga kukutana na Rais Ruto wakati wa ziara zao nchini Amerika. "Puuzeni propaganda zinazoenezwa kwamba nina nia ya kukutana na Rais Ruto hapa Amerika. Hilo halipo kabisa katika mipango yangu," alisema. Alieleza sababu ya kucheleweshwa kwa sekretarieti ya pamoja ya upinzani, Gachagua akisema ni rahisi kuvurugwa na serikali.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
Wakenya 49 miongoni mwa maelfu wanaosubiri kutimuliwa na Trump kutoka Amerika
Raia 49 wa Kenya ni miongoni mwa maelfu ya watu walio katika orodha mpya ya wanaosubiri taratibu za kufurushwa kutoka Amerika. Majina na picha za Wakenya hao zimechapishwa hadharani kama sehemu ya msako mpana wa maafisa wa Amerika dhidi ya wahamiaji wanaokiuka sheria za uhamiaji. Idara ya Usalama wa Taifa ya Amerika (DHS) imechapisha hifadhidata maarufu inayoorodhesha raia 125 kutoka Afrika wanaosubiri kuondolewa nchini humo katika siku zijazo, huku Wakenya 49 wakiongoza orodha hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi kutoka taifa moja. DHS imepanua hifadhidata yake inayojulikana kama "Wabaya zaidi", inayolenga watu wasiokuwa raia wa Amerika walio na rekodi za uhalifu na wanaotafutwa kuzuiliwa na kufurushwa kutoka nchi hiyo. Ingawa orodha ya awali au utekelezaji wa mpango huo katika maeneo tofauti ilikuwa na idadi ndogo ya Wakenya, kama vile watu 15 au 45, ripoti za hivi majuzi zinaonyesha kuwa Wakenya 49 sasa wako katika kampeni mpya ya utekelezaji wa sheria za uhamiaji. Kulingana na takwimu za Shirika la Uhamiaji na Utekelezaji wa Sheria za Forodha la Amerika (ICE), raia 1,282 wa Kenya wako kwenye orodha ya watu ambao wana maagizo ya mwisho ya kuondolewa nchini lakini hawajazuiliwa. Wakenya hao ni sehemu ya orodha inayojumuisha zaidi ya watu milioni 1.4 wasio raia wa Amerika kutoka mataifa 187 duniani. Takwimu hizo zinaonyesha kuimarishwa kwa hatua za utekelezaji wa sheria za uhamiaji nchini Amerika, hali ambayo imezua wasiwasi mkubwa na changamoto za kisheria miongoni mwa jamii ya Wakenya wanaoishi nchini humo. Mbali na kundi hilo la watu ambao hawajazuiliwa, kuna idadi ndogo ya Wakenya waliohukumiwa kwa makosa makubwa ya jinai ambao wamewekwa katika orodha maalum za DHS za watu wanaopewa kipaumbele katika hatua za kufurushwa. Wakenya wanaongoza orodha hiyo kwa watu 49, wakifuatwa na raia 44 wa Ghana. Aidha, taarifa nyingine ya DHS inaonyesha kuwa raia 112 wa Nigeria 112 pia wanasubiri kufurushwa kutoka Amerika. Mauritania ina watu 12 kwenye orodha hiyo, Morocco 11 huku Afrika Kusini ikiwa na watu tisa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Viongozi watuzwa kwa uongozi bora
AFISA Mkuu Mtendaji wa Shirika la Usambazaji Umeme Maeneo ya Mashambani (REREC) ni miongoni mwa viongozi wa kampuni na mashirika ya umma na ya kibinafsi waliotambuliwa kwa uongozi bora na mchango wao katika mageuzi ya kijamii na kiuchumi nchini Kenya. Dkt Rose Mkalama alituzwa Afisa Mkuu Mtendaji bora wa mwaka wakati wa makala ya pili ya East Africa Leadership Awards, kwa uongozi wake katika kupanua upatikanaji wa umeme nchini kupitia Mpango wa Last Mile Connectivity. Chini ya juhudi za kitaifa za kusambaza umeme, kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini Kenya kimeongezeka hadi zaidi ya asilimia 76, kutoka karibu asilimia 27 mwaka 2013. Kulingana na Dkt Mkalama, tuzo hiyo si mafanikio yake binafsi pekee, bali ni utambuzi wa kazi inayofanywa na REREC kuhakikisha umeme unawafikia maelfu ya Wakenya katika maeneo ya vijijini na mashambani. "Nina furaha kuwa REREC imeweza kufikia maelfu ya Wakenya katika karibu kila kijiji nchini kupitia Mpango wa Last Mile Connectivity," alisema. REREC ilipoanzishwa, kiwango cha kuunganishwa kwa umeme nchini kilikuwa takriban asilimia 8. Afisa Mkuu Mtendaji huyo wa shirika hilo alisema ongezeko hilo limechangiwa na ufadhili wa serikali, ushirikiano na wabunge pamoja na utekelezaji endelevu wa miradi ya usambazaji umeme katika maeneobunge yote 290 nchini. [caption id="attachment_192455" align="aligncenter" width="300"] Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Usambazaji Umeme Maeneo ya Mashambani (REREC), Dkt Rose Mkalama akizungumza awali. Picha|Hisani[/caption] Anasema manufaa ya umeme yameendelea kuyapa maboma mwangaza, ikizingatiwa yamesaidia kufanikisha elimu, afya, kilimo na biashara, na hivyo kuwezesha jamii kushiriki zaidi katika maendeleo ya kiuchumi. "Kwa sasa, tunatekeleza miradi inayolenga kuunganisha taasisi za umma na jamii kwenye huduma za umeme, huku mipango ya usambazaji umeme kupitia gridi ikilenga kufikia mamia ya maelfu ya wateja," Dkt Mkalama akadokeza. Viongozi wengine waliotuzwa ni pamoja na Dkt Lilian Nyawada, Kamishna wa Forodha na Udhibiti wa Mipaka katika Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA), na Dkt David Okeyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Nutrition and Dieticians Institute. Kabla ya kutawazwa viongozi bora, huduma za mashirika na kampuni zao zilipigwa msasa na jopo la majaji mashuhuri kutoka World Human Resource Congress, wasimamizi wa huduma za wafanyakazi kutoka India na viongozi tajika wa kijamii. Akizungumza wakati wa kuwatuza, Mkuu wa Kitengo cha Bionuwai, Ujumuishaji na Haki za Watu wenye Mahitaji Maalum (Head of the Office of Diversity, Inclusion and Disability Rights in the Executive Office of the President) katika Afisi ya Rais, Isaac Mwaura, aliwataka viongozi wa taasisi za umma na kibinafsi kuhamasisha wafanyakazi wao kujitahidi kutoa huduma bora. "Uongozi haupaswi kupimwa kwa cheo pekee, bali pia kwa urithi ambao viongozi wanaacha katika taasisi na jamii," Mwaura akasema. Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mt Kenya Prof Bindu Madhavi, pia alitambuliwa kwa tuzo ya Profesa mwenye ushawishi mkubwa kutokana na mchango wake katika elimu, utafiti, kunoa wanafunzi makali na masuala ya dawa na sayansi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Maoni mseto Rais akimpa mzee wa Waluo gari ya mamilioni kama zawadi
ZAWADI ya gari jipya aina ya Toyota Prado TX lililotolewa na Rais William Ruto kwa mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Luo, Ker Odungi Randa, imeibua mjadala mkali wa kisiasa katika eneo la Nyanza. Gari hilo la thamani ya mamilioni lilifikishwa nyumbani kwa Bw Randa katika eneo la Boya na maafisa kutoka afisi ya Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, siku chache baada ya kiongozi huyo wa kitamaduni kumuomba Rais msaada wa usafiri wakati wa ziara yake katika eneo hilo. Kwa mujibu wa taarifa, ombi hilo lilitolewa wakati wa mkutano uliofanyika Homa Bay, ambapo Rais aliahidi kulitekeleza. Afisa kutoka afisi ya Dkt Omollo, Bw Charles Osako, alisema Rais alitimiza ahadi yake kwa Baraza la Wazee wa Luo na kwamba gari hilo litasaidia shughuli na majukumu ya wazee hao. "Gari hili linaonyesha kutambuliwa kwa mchango muhimu wa wazee na viongozi wa kitamaduni katika kuhifadhi maadili, mila na utambulisho wetu," alisema Bw Osako. Mbunge wa Lang'ata, Phelix Jalango Odiwuor, ambaye alishuhudia mazungumzo hayo, alisema baada ya mkutano wa mwisho wa hadhara Migori, Dkt Omollo alimwalika kuhudhuria kikao kati ya Rais na viongozi wa Baraza la Wazee wa Luo. Alisema mwishoni mwa mkutano huo, Bw Randa alimuomba Rais amsaidie kupata gari la kurahisisha shughuli zake za kila siku. "Kwa utulivu, Rais alimwambia angepata gari Ijumaa. Leo asubuhi timu ya Dkt Omollo imekabidhi gari hilo jipya aina ya Toyota Prado," alisema Bw Odiwuor baada ya gari kuwasilishwa. Bw Randa alipokea funguo za gari hilo na kulijaribu kabla ya kurejea nyumbani kwake. "Nashukuru Rais Ruto kwa zawadi hii. Itanisaidia kusafiri na kukutana na Waluo walioko Nairobi, Mombasa, Uganda, Tanzania na maeneo mengine mengi," alisema. Hata hivyo, zawadi hiyo imezua maswali kuhusu uhuru wa Baraza la Wazee wa Luo, ambalo kwa kawaida halifai kuzingatia siasa za vyama na linatarajiwa kuwa sauti ya maridhiano katika jamii. Wakosoaji wanasema kupokea gari kutoka kwa Rais kunaweza kuathiri msimamo wa baraza hilo, hasa wakati ushindani wa kisiasa kati ya vyama vya UDA na ODM unaendelea kushika kasi Nyanza. Mkazi wa Kisumu, Bw Martin Oria, alihoji jinsi baraza hilo litakavyodumisha kutopendelea upande wowote wakati litakapohitajika kutatua mizozo ya kisiasa. Lakini wengine wametetea zawadi hiyo, wakisema viongozi mbalimbali wa kitaifa wamekuwa wakiwasaidia wazee wa jamii kwa miaka mingi. Kwa mujibu wa David Dimba Jakobuya, Bw Randa ni mmoja wa wazee wachache waliosalia ambao walishiriki katika harakati za ukombozi wa kwanza na wa pili nchini Kenya. Alisema amekuwa akikabiliwa na changamoto za usafiri tangu gari lake la awali lilipoibwa miaka kadhaa iliyopita. Akijibu ukosoaji huo, Bw Randa alisema wale wanaopinga zawadi hiyo hawakuwahi kujitokeza alipokuwa akikosa usafiri. "Sikusikia mtu yeyote akilalamika kwa niaba yangu wakati sikuwa na gari. Sasa nimepewa gari, kila mtu ana maoni. Marais wengine pia wamekuwa wakitoa zawadi kwa watu wengi nchini," alisema. Wakati huo huo, baadhi ya wakazi wamehoji iwapo gari hilo ni mali ya Bw Randa binafsi au ya Baraza la Wazee wa Luo. Hata hivyo, kiongozi huyo amesisitiza kuwa ni zawadi ya kibinafsi aliyopewa na Rais kufuatia ombi lake. Mjadala huo umechukua sura ya kisiasa zaidi baada ya Bw Randa kutoa wito kwa jamii ya Waluo kumuunga mkono Rais Ruto katika azma yake ya kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu ujao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Karua ashtaki Uganda kwa kumtimua asiwakilishe Besigye
Kiongozi wa Chama cha People's Liberation Party (PLP) na aliyekuwa Waziri wa Haki nchini Kenya, Martha Karua, amewasilisha kesi katika mahakama ya Uganda akitaka kubatilishwa kwa uamuzi wa kufurushwa kwake nchini humo na kuruhusiwa kurejea ili kumwakilisha kiongozi wa upinzani, Dkt Kizza Besigye, na mshtakiwa mwenzake. Besigye aliyekamatwa akiwa Nairobi Nairobi mwaka 2024 anakabiliwa na kesi ya uhaini. Bi Karua, kwa ushirikiano na Chama cha Wanasheria cha Uganda (Uganda Law Society), wanapinga uamuzi uliotolewa Juni 22 na Afisa Mkuu wa Uhamiaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe wa kumzuia kuingia nchini Uganda na kutangaza kuwa mtu asiyehitajika nchini humo. Wanasema uamuzi huo ulikuwa kinyume cha sheria na ulifanywa bila kumpa nafasi ya kujitetea au kusikilizwa. Kupitia Kitengo cha Malalamishi cha Mahakama Kuu mjini Kampala, Karua anataka mahakama ibatilishe uamuzi huo na kuzuia maafisa wa uhamiaji kuingilia haki yake ya kuingia Uganda ili kutekeleza majukumu yake ya kitaaluma kama wakili. Katika hati zake za kesi, Karua anaeleza kuwa alisafiri kwenda Uganda Juni 22 ili kuwakilisha Dkt Besigye na Hajj Obeid Lutale baada ya kupata Cheti Maalum cha Uwakili kilichomruhusu kufanya kazi katika mahakama za Uganda. Anasema maafisa wa uhamiaji walimzuia kuingia nchini humo, wakachukua simu zake na baadaye wakampatia notisi ya kumtaka arejee Kenya. Dkt Besigye na Bw Lutale walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini na makosa mawili ya kuficha taarifa kuhusu uhaini. Upande wa mashtaka unadai walihusika katika njama za kupindua serikali ya Uganda. Mashtaka hayo yalitokana na kukamatwa kwa wawili hao jijini Nairobi mnamo Novemba 2024. Awali walifikishwa mbele ya Mahakama ya Kijeshi ya Uganda kabla ya kuhamishiwa mahakama za kiraia kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu uliosema kuwa raia hawawezi kushtakiwa katika mahakama za kijeshi. Baadaye walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkuu ya Nakawa mnamo Februari 21, 2025. Hatua ya Karua kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Uganda kutokana na vitendo vya maafisa wa uhamiaji imefuatia ombi la awali lililowasilishwa na Dkt Besigye na Bw Lutale kuhusu suala hilo hilo. Mahakama Kuu ilikataa kuamua iwapo uamuzi wa uhamiaji ulikuwa halali, ikisema kuwa changamoto hiyo ilipaswa kuwasilishwa kupitia mchakato wa mapitio ya mahakama, na hivyo ikatupilia mbali ombi hilo. Karua na Chama cha Wanasheria cha Uganda wanataka mahakama itangaze kuwa uamuzi huo ulikuwa haramu, wa kiholela, usio na sababu za msingi na uliofanywa kinyume cha taratibu zinazotakiwa kisheria. Pia wanataka mahakama iubatilishe, kuagiza mamlaka za uhamiaji kutathmini upya suala hilo, na kutoa amri ya kudumu ya kutomzuia kuingia Uganda kwa madhumuni ya kitaaluma. "Uamuzi huo ni haramu, hauna mantiki na ulifanywa kinyume cha taratibu zinazotakiwa na sheria," walisema. Katika kiapo chake cha kuunga mkono kesi hiyo, makamu wa rais wa Chama cha Wanasheria cha Uganda, Anthony Asiimwe, alisema Karua ni Wakili Mkuu na anamiliki Cheti Maalum cha Uwakili kilichotolewa chini ya Kifungu cha 18 cha Sheria ya Mawakili. Alisema cheti hicho kilimruhusu kuongoza timu ya utetezi katika kesi inayowahusu Besigye na Lutale. Asiimwe alieleza kuwa alisafiri hadi Entebbe kumpokea Karua baada ya kuwasili kutoka Kenya, lakini akakuta maafisa wa uhamiaji tayari wamemzuia kuingia nchini. Walalamishi hao wanasisitiza kwamba Karua hakupatiwa nafasi ya kusikilizwa wala sababu zinazokidhi kanuni za haki za asili kabla ya uamuzi huo kufanywa. Wanasema hatua hiyo ilikiuka Katiba ya Uganda, Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pamoja na misingi inayolinda uhuru wa taaluma ya sheria. Kwa mujibu wao, Karua amepata hasara kitaaluma na kifedha kwa sababu hawezi kurejea Uganda kutekeleza majukumu yake. "Mlalamishi wa pili ameendelea kupata madhara makubwa ya kitaaluma na jina lake kuharibiwa baada ya kutangazwa hadharani kuwa ' mtu asiyetakiwa' bila msingi wowote wa kisheria," alisema Asiimwe. Kabla ya kuwasilisha kesi hiyo, Chama cha Wanasheria cha Uganda kilijaribu kutafuta suluhu kupitia njia za kiutawala. Barua zilizoambatishwa katika kesi zinaonyesha kuwa chama hicho kiliwaomba maafisa wa Uganda kufuta uamuzi huo na kumruhusu Karua kuingia nchini. Hadi sasa, Mwanasheria Mkuu wa Uganda hajawasilisha majibu kuhusu madai yaliyomo katika kesi hiyo mpya.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Shughuli zakwama Mombasa mihadarati ya thamani ya Sh8.2 bilioni ikiteketezwa
SHUGHULI za kawaida zilisitishwa kwa muda Mombasa Alhamisi asubuhi wakati msafara wenye ulinzi mkali ulipokuwa ukielekea katika kiwanda cha simiti cha Bamburi kutoka kambi ya jeshi la wanamaji iliyo Mtongwe. Msafara huo uliojumuisha walinzi wa usalama wenye silaha ulikuwa ukienda kwa shughuli ya kuteketeza dawa za kulevya aina ya methamphetamine zilizokadiriwa kuwa za Sh8.2 bilioni. Operesheni hiyo ilihusisha maafisa kutoka Jeshi la Wanamaji, Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Idara ya Huduma ya Polisi, Polisi wa Kimataifa (Interpol) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP). Tanuri za Bamburi Cement zimeidhinishwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) kwa ajili ya uharibifu salama na uchakataji wa taka hatari na zisizo hatari. Kupitia Geocycle Kenya, kiwanda hicho pia hutumia taka zinazochomwa kama chanzo mbadala cha nishati ya joto katika uzalishaji wa simiti. Dawa hizo haramu kwanza zilipimwa uzani na kuthibitishwa kuwa zile halisi zilizokamatwa, kabla ya mahakama kutoa amri ya mwisho kuruhusu mchakato uliofuata. Hakimu Mkuu Anthony Mwicigi alisimamia shughuli hiyo na kuamrisha kwamba dawa hizo ziharibiwe, baada ya mahakama kuridhika kwamba zilikuwa zile zile ambazo zilipatikana kwa washukiwa. Washukiwa hao ambao ni raia wa Iran ni Jaseem Darzadeh Nia, Nadeem Jadgal, Hassan Baloch, Raheem Baksh, Imran Baloch na Imtiyaz Daryay. Wanadaiwa kusafirisha kilo 1,036.044 za methamphetamine zenye thamani ya takriban Sh8.2 bilioni, na kesi yao bado inaendelea katika Mahakama ya Shanzu. Upande wa mashtaka unadai kuwa dawa hizo zilisafirishwa ndani ya meli MV Mashaallah, ambayo inadaiwa haikusajiliwa na haikuwa na uraia wa nchi yoyote. Meli hiyo ilikamatwa katika bahari kuu, huku kosa linalodaiwa kutendeka kati ya Oktoba 17 na 20, 2025. Washukiwa hao sasa wataanza kuwasilisha utetezi wao mmoja baada ya mwingine huku kesi hiyo ikiendelea. Tanuri ya Bamburi Cement imewahi kutumiwa kwa shughuli kama hiyo awali. Katika mwaka wa 2025, mihadarati aina ya heroin na kokeni za Sh400 milioni ziliharibiwa hapo baada ya washukiwa kupatikana na hatia au kupoteza maisha kwa njia zisizoeleweka. Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen, alisema shughuli hiyo ya Alhamisi ilithibitisha nia ya serikali kukatiza mitandao ya ulanguzi wa dawa za kulevya kimataifa. "Leo tunatuma ujumbe sio tu kwa watumizi bali pia walanguzi wakubwa wa mihadarati. Tumeweka wazi kwamba serikali itatwaa mali za walanguzi wote na kuzitumia kurekebisha tabia za waraibu na shughuli nyingine za kukabiliana na biashara hiyo haramu," akasema. Shughuli nzima ilifanywa kwa utaratibu na kushirikisha pande zote husika za kesi, ili kuepusha changamoto kama zile zilizoibuka baada ya serikali kulipua meli iliyodaiwa kuwa na mihadarati baharini mwaka wa 2014 chini ya aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta. Hatua hiyo ilizua utata na kutatiza kesi iliyokua ikiendelea, hadi baadhi ya washukiwa wakaachiliwa huru mwaka wa 2025 wakati mahakama ilipoamua kulikuwa na udhaifu wa kisheria, ikiwemo uharibifu wa meli husika kabla ushahidi muhimu kukusanywa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
Kauli ya Uhuru yafufua kidonda cha uchaguzi wa 2022
KAULI ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kwamba bado anaamini marehemu Raila Odinga ndiye aliyeshinda uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka 2022 imezua mjadala mkali wa kisiasa, huku ikifungua upya majeraha ya uchaguzi huo na kuibua maswali mapya kuhusu yaliyojiri baada ya kura za Agosti 9, 2022. Akizungumza katika makao makuu ya chama cha Jubilee jijini Nairobi, Bw Kenyatta alisema hana shaka kuwa Raila Odinga alipata kura za kutosha kushinda urais, lakini mambo yalienda kwa njia ambayo hakutaka yajirudie tena. "Tulifanya kila kitu kuhakikisha Baba anakuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya. Alipata kura na hadi leo ninaamini ndiye aliyeshinda kura hizo. Tunajua yaliyotokea na hatutaki yatokee tena kwa njia hiyo," alisema. Kauli hiyo imezua mvutano mpya kati ya viongozi wa chama tawala cha UDA, viongozi wa ODM na hata baadhi ya wanafamilia wa marehemu Raila Odinga. Mjadala huo umefufua kumbukumbu za uchaguzi wa 2022 wakati Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimtangaza William Ruto mshindi kwa kura 7,176,141 sawa na asilimia 50.49 dhidi ya kura 6,942,930 za Raila Odinga zilizokuwa asilimia 48.85. Baadaye Mahakama ya Juu ilitupilia mbali kesi zote zilizopinga ushindi wa Dkt Ruto na kuthibitisha matokeo hayo mnamo Septemba 5, 2022. Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga, alisema kauli ya Uhuru inathibitisha kile ambacho chama chake kiliamini wakati huo, lakini imezua maswali mapya. "Ikiwa alikuwa na hakika Raila alishinda, kwa nini serikali yake ilikabidhi madaraka kwa mtu ambaye aliamini hakushinda uchaguzi?" alihoji. Dkt Oginga alisema ODM ilitumia njia zote za kikatiba kupinga matokeo ya uchaguzi lakini baada ya kushindwa mahakamani iliamua kuacha suala hilo na kuendelea mbele kwa manufaa ya taifa. "Baada ya kutumia njia zote za kikatiba zilizokuwapo, tuliamua kulimaliza suala hilo na kusonga mbele kama nchi," alisema. Aidha alionya dhidi ya kutumia uchaguzi wa 2022 na mchango wa Raila Odinga kama silaha ya kampeni za kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027. Kwa upande wake, Bw Kenyatta alitetea nafasi yake katika kampeni za Raila mwaka 2022 na kupinga madai kwamba hakufanya vya kutosha kumuunga mkono. "Wanaposema walinishinda, je ni mimi niliyekuwa kwenye kura au alikuwa Raila Odinga? Niliwezaje kushindwa ilhali nilikuwa nasaidia Raila?" aliuliza. Rais William Ruto naye aliwahi kumjibu Bw Kenyatta katika mkutano huko Siaya, akisema ikiwa hakumshinda alipokuwa rais, itakuwa vigumu zaidi kumshinda sasa akiwa amestaafu. "Uhuru Kenyatta hakunishinda alipokuwa Rais, sasa mimi ndiye Rais na yeye amestaafu. Atawezaje kunishinda?" alihoji Dkt Ruto. Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar alikataa madai ya Bw Kenyatta na kusisitiza kuwa Dkt Ruto alishinda uchaguzi huo kwa njia halali. "Rais William Ruto alishinda uchaguzi wa mwaka 2022 kwa uwazi na kwa uhalali kamili," alisema Omar. Naye kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ameongeza uzito wa mjadala huo kwa kudai kuwa upande wa Raila Odinga uliibiwa ushindi sio tu mwaka 2022 bali pia katika uchaguzi wa 2013 na 2017. Akizungumza Kitui, Kalonzo alisema anaamini muungano wao ulishinda mara zote tatu lakini haukutangazwa mshindi. Kauli za Bw Kenyatta pia zimegawanya maoni ndani ya familia ya Odinga. Ndugu yake Raila, Omondi Oginga, alimkosoa kwa kufufua suala hilo miaka kadhaa baada ya uchaguzi na baada ya kifo cha kiongozi huyo wa ODM. "Uhuru hapaswi kucheza mchezo huu nasi. Raila ameondoka na hatufurahii suala hili kufufuliwa tena. Alikuwa madarakani na alikuwa na uwezo wote, kwa nini hakuchukua hatua wakati huo?" alihoji. Seneta wa Narok Ledama Ole Kina naye alihoji kwa nini Bw Kenyatta anatoa madai hayo sasa ilhali alikuwa Rais, Amiri Jeshi Mkuu na ndiye aliyekabidhi mamlaka kwa Dkt Ruto. Mjadala huo umefufua historia ya uchaguzi tata nchini Kenya, hasa uchaguzi wa 2007 uliosababisha machafuko makubwa ya baada ya uchaguzi, pamoja na ule wa 2017 ambao Mahakama ya Juu ilibatilisha na kuagiza urudiwe. Sasa, huku maandalizi ya uchaguzi wa 2027 yakianza kushika kasi, kauli ya Uhuru imefanya uchaguzi wa 2022 kurejea tena katikati ya siasa za taifa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Maseneta walalamikia Ruto kuandamana na kikosi cha mawaziri saba ziarani Amerika
Uamuzi wa Rais William Ruto kusafiri New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) akiandamana na Mawaziri saba umeibua mvutano mpya katika Seneti, ambapo baadhi ya maseneta wanahoji iwapo ukubwa wa ujumbe huo una sababu za msingi wakati Bunge linaendelea kutafuta majibu kutoka kwa serikali kuhusu masuala yanayowakabili Wakenya. Mjadala huo uliibuka Jumatano wakati wa vikao vya Seneti Mashinani vilivyofanyika Kaunti ya Kilifi. Maseneta wa upinzani walilalamikia kutokuwepo kwa baadhi ya mawaziri wakisema hali hiyo imechelewesha mijadala kuhusu matatizo yanayowakumba wananchi pamoja na utekelezaji wa miradi ya serikali. Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, alihoji sababu ya mawaziri saba kuandamana na Rais katika mkutano huo wa kimataifa. "Kenya si taifa lililoshindwa kiasi kwamba mawaziri saba waandamane na Rais kwenda UNGA ilhali jukumu lao ni kuketi nyuma yake anaposoma hotuba," alisema Khalwale. Alisema hatua hiyo inaathiri utendaji wa serikali na pia inaongeza mzigo kwa walipa ushuru kutokana na gharama za tiketi za ndege, usalama na matumizi mengine ya safari. Lawama hizo ziliongezeka baada ya kubainika kuwa baadhi ya mawaziri waliokuwa wakihitajika kujibu maswali ya Seneti hawakuwapo nchini. Miongoni mwao ni Waziri wa Madini Hassan Joho, Waziri wa Elimu Julius Migos na Waziri wa Teknolojia ya Habari William Kabogo. Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alisema kutokuwepo kwa Bw Joho kulitatiza mijadala kuhusu kituo cha samaki cha Kilifi Central ambacho maseneta walikuwa wametembelea. Kwa mujibu wa Sifuna, wavuvi, vijana na wakazi wa eneo hilo walieleza hofu kuhusu mustakabali wa mradi huo na nafasi za ajira zitakazotokana nao. "Wananchi wana wasiwasi mkubwa, hasa vijana ambao hawajapewa hakikisho kwamba wao watapewa kipaumbele cha ajira katika eneo hilo," alisema. Aidha alisema wakazi wana hofu kuwa mradi huo huenda ukaendeshwa kupitia ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi, hali inayozua maswali kuhusu nani atanufaika. Sifuna pia alikosoa viongozi wa serikali kwa kutumia muda mwingi nje ya nchi huku wananchi wakikumbwa na changamoto mbalimbali nyumbani. Hata hivyo, Seneta wa Tana River Danson Mungatana alitetea uamuzi wa mawaziri kuandamana na Rais akisema safari kama hizo huwapa nafasi ya kufanya mikutano ya pembeni, kujadiliana na mataifa mengine na kutia saini mikataba ya maendeleo. "Katika safari moja, mawaziri wanaweza kufanya shughuli nyingi muhimu za serikali badala ya kusafiri mara kwa mara kwa gharama kubwa zaidi," alisema. Mvutano huo unaonyesha changamoto iliyopo kati ya shughuli za kimataifa za serikali na hitaji la mawaziri kuwajibika kwa wananchi na Bunge.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Hali inazidi kuwa mbaya nchini, Kanisa laonya
KANISA la Anglican Church of Kenya (ACK), limekosoa vikali serikali, likionya kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha, ongezeko la ushuru, visa vya kutoweka kwa watu, ukiukaji wa haki za kibinadamu, ghasia za kisiasa na ufisadi. Katika taarifa iliyotolewa baada ya kikao cha Kamati ya Kudumu ya Kanisa hilo kilichofanyika katika Kanisa la All Saints' Cathedral jijini Nairobi, Askofu Mkuu wa ACK, Jackson Ole Sapit, alisema Kenya inakabiliwa na mazingira ya kisiasa yanayozidi kuwa hatari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027. Kanisa hilo lilionya dhidi ya kurejea kwa siasa za ukabila, uchochezi, vitisho, kuhadaa wapigakura na vurugu zinazoweza kuhatarisha amani ya taifa. "Kuongezeka kwa uhuni wa kisiasa, matamshi ya uchochezi, mgawanyiko wa kikabila na kuvurugwa kwa shughuli za kisiasa kunapaswa kuwatia wasiwasi Wakenya wote wenye nia njema," alisema Askofu Ole Sapit. Alisema jambo linalotia hofu zaidi ni matumizi ya vijana wasio na ajira kama zana za mizozo ya kisiasa. "Maisha ya vijana yanatolewa kafara kwa ajili ya tamaa za kisiasa. Tunasema wazi kuwa hali hiyo ni mbaya na haikubaliki. Tunaomboleza wale waliopoteza maisha katika makabiliano ya kisiasa. Hakuna cheo kinachostahili damu ya Mkenya kumwagika," alisema. ACK iliwataka viongozi wa kisiasa kupunguza joto la kisiasa na kuepuka kauli za uchochezi, huku ikihimiza idara za usalama kutekeleza sheria bila upendeleo. Kanisa hilo pia liliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuanza maandalizi ya mapema ya uchaguzi huru, wa haki, unaoaminika na unaoweza kuthibitishwa. "Uchaguzi wa amani haujengwi siku ya kupiga kura. Hujengwa kupitia haki, kuaminiana na maandalizi ya muda mrefu kabla ya uchaguzi kufanyika," alisema. Kuhusu ufisadi, ACK ilieleza kuwa rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma ndiyo kidonda kikubwa zaidi kinacholikabili taifa. Kanisa linataka mashirika ya kupambana na ufisadi, vyombo vya uchunguzi na Idara ya Mahakama kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika bila kujali hadhi zao. "Wakenya wamechoshwa na uchunguzi usiozaa matunda na kashfa zisizo na matokeo. Haki haipaswi kuzingatia mamlaka, utajiri au ushawishi wa mtu," alisema Askofu Ole Sapit. Kanisa pia lilielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya huduma za afya nchini, likitaja mgomo wa muda mrefu wa wauguzi na changamoto nyingine zinazokumba sekta hiyo. "Huduma za afya si anasa ya matajiri. Serikali za kitaifa na kaunti zinapaswa kushirikiana kwa haraka na wahudumu wa afya kutatua migogoro iliyopo," alisema. Aidha, ACK ilipinga baadhi ya mapendekezo katika Mswada wa Elimu ya Msingi, ikisema masuala yanayohusu mamilioni ya watoto hayawezi kuamuliwa bila mashauriano ya kutosha na wadau mbalimbali. Kanisa hilo lilionya kuwa Wakenya wengi wanateseka kutokana na ukosefu wa ajira, kupanda kwa gharama ya maisha, kufungwa kwa biashara na mzigo mkubwa wa ushuru. "Ushuru ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, lakini ushuru unaowaumiza wananchi huku rasilimali za umma zikifujwa unakuwa chombo cha ukosefu wa haki," ilisema taarifa hiyo. ACK ilihitimisha kwa kusema kuwa Kenya ipo katika kipindi muhimu cha kihistoria na kwamba changamoto zinazolikabili taifa si za kisiasa na kiuchumi pekee bali pia za kimaadili na kiroho. Kanisa liliwataka viongozi na wananchi kukumbatia uwajibikaji, uadilifu na toba ili kunusuru taifa dhidi ya migawanyiko na migogoro inayoweza kujitokeza kabla ya uchaguzi wa mwaka 2027.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
NCIC kutumia Sh962m kuzuia ghasia za uchaguzi
TUME ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) inapanga kutumia Sh962.6 milioni kudhibiti matamshi ya chuki, ukabila na ghasia za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Mpango huo, unaojulikana kama Salama 2027, unalenga kutambua mapema maeneo yenye mivutano, kukabiliana na matamshi ya chuki mitandaoni, kuwahusisha vijana na kurejesha imani ya wananchi katika taasisi. Mwenyekiti wa NCIC, Askofu Kepha Omae, alisema Sh250 milioni zinatarajiwa kutoka kwa Serikali kupitia bajeti za ziada, huku fedha zilizosalia zikitarajiwa kutoka kwa wafadhili. "Uchaguzi wa 2027 lazima uchukuliwe kama mchakato na wala si tukio la siku moja. Ni lazima tujenge upya imani, tuwahusishe vijana na kutambua mivutano mapema," alisema. NCIC inapanga kuanzisha mifumo ya kisasa ya kutambua matamshi hatari mtandaoni, kutuma vikosi vya upatanishi katika maeneo hatari, kuendesha misafara ya amani na kutoa elimu ya uraia. Mpango huo pia utahusisha kutambua maeneo yenye uwezekano wa mizozo katika kaunti zote 47.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Sifuna, Kalonzo wapigania jina 'Ukombozi'
CHAMA cha Wiper Patriotic Movement kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka kimeeleza kwa mara ya kwanza jinsi kilivyotwaa jina The Ukombozi Alliance (TUA), huku mzozo kuhusu jina hilo ukizidi kupamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Kupitia kampuni ya mawakili ya LAK Advocates, chama hicho kimesema kilianza kutafuta na kuhifadhi majina ya vyama tangu Machi 2025, wakati kilipokuwa kikijiandaa kuunda muungano wa kisiasa. Kwa mujibu wa nyaraka zilizopatikana na Taifa Dijitali, chama hicho kilihifadhi majina tisa, yakiwemo The Ukombozi Alliance, kabla ya kuchagua kuwa jina lake. Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa mchakato ulianza Machi 18, 2025, wakati jina Chama Cha Ukombozi lilipohifadhiwa. Wiki moja baadaye, likafuata jina Ukombozi Freedom Party. Mnamo Aprili 6, 2025, chama kilihifadhi Ukombozi Freedom Front, huku majina mengine yakihifadhiwa baadaye mwaka huo na mwaka 2026. Mnamo Julai 20, 2026, jina The Ukombozi Alliance lilihifadhiwa rasmi. Muungano huo unasema mchakato huo uliodumu zaidi ya mwaka mmoja ulifikia kilele Agosti 3, 2026, wakati jina hilo lilipochaguliwa na Azimio La Umoja One Kenya Coalition na kuwasilishwa kushughulikiwa. Mzozo huo uliibuka baada ya washirika wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna pia kujaribu kutumia jina Ukombozi kwa chama cha kisiasa. Katika barua ya Septemba 8, 2026, Msajili wa Vyama vya Kisiasa, John Cox Lorionokou, alikataa ombi la upande wa Bw Sifuna kubadilisha jina la United Democratic Party (UDP) kuwa Ukombozi People's Party (UPP). Msajili alisema jina hilo lilifanana kwa kiwango kikubwa na The Ukombozi Alliance. Hata hivyo, nyaraka zinaonyesha kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP), ilikuwa imeidhinisha awali uhifadhi wa jina Ukombozi People's Party mnamo Machi 13, 2025, baada ya ombi la wakili Allan Akivanga. ORPP ilisema uhifadhi huo ungekuwa wa muda usiozidi siku 90. Baadaye, Julai 9, waanzilishi wa UPP waliandikia ORPP wakitaka kusitisha mchakato wa usajili. Bw Akivanga alisema walikuwa wameomba kusitisha usajili baada ya kuombwa na UDP, iliyotaka kubadilisha jina lake kuwa UPP. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya alihusishwa na mpango wa kubadilisha jina la UDP, chama kilichowahi kuhusishwa na aliyekuwa mbunge wa Lugari, marehemu Cyrus Jirongo. Lakini Septemba 21, Bw Akivanga alibadilisha msimamo na kueleza ORPP kuwa UPP sasa itaendelea na mchakato wa usajili. Alisema hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na kucheleweshwa kwa mchakato wa usajili. Upande wa Bw Musyoka unasema Bw Akivanga hakuongeza muda wa kuhifadhi jina hilo na kwa hivyo alipoteza haki ya kulidai. Kwa mujibu wa LAK Advocates, uhifadhi wa jina la chama huwa wa muda usiozidi siku 90 na muombaji anapaswa kuomba kuongezewa muda ili kuendelea kulilinda. Kampuni hiyo inasema uhifadhi wa jina UPP ulimalizika Juni 13, 2025 bila Bw Akivanga kuchukua hatua za kuuongeza. LAK pia inasema haikuwa na taarifa kuhusu mpango wa UDP kubadilisha jina lake kuwa UPP hadi ilipoona tangazo la gazeti. Mzozo huo ulizidi baada ya UDP kuchapisha tangazo Agosti ikialika maoni kuhusu pendekezo la kubadilisha jina lake. LAK ilisema iliwasilisha pingamizi Agosti 10, 2026, ikieleza kuwa matumizi ya jina Ukombozi yanaweza kusababisha mkanganyiko miongoni mwa wananchi kutokana na kufanana kwa majina hayo. Mzozo huo sasa umeangazia mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kukataa majina yanayoweza kuwachanganya wapiga kura. LAK inasema sheria inampa Msajili mamlaka ya kukataa jina, kaulimbiu au nembo ya chama kipya ikiwa inafanana kwa karibu na chama au taasisi nyingine iliyosajiliwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 23 hours ago
Serikali yaandaa Nairobi tayari kwa mafuriko El Niño
Serikali imeanza maandalizi ya kuwaondoa wakazi katika maeneo hatari kwa mafuriko Nairobi huku mvua kubwa inayotarajiwa kuanza wiki ya pili au ya tatu ya Oktoba ikikaribia. Naibu Rais Kithure Kindiki alisema maeneo yanayoweza kuathiriwa yametambuliwa na vituo vya muda vya kuwahifadhi watu wanaoweza kuhamishwa vimeandaliwa. Takriban watu 100,000 Nairobi wanatarajiwa kuathiriwa, huku Mukuru, Mathare, Kibra, Embakasi, Dagoretti South, Makadara na Westlands yakitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyo hatarini. Barabara kuu kama Uhuru Highway, Jogoo Road, Bunyala Road na Mombasa Road pia zinatarajiwa kukumbwa na mafuriko. Prof Kindiki alisema serikali imejiandaa kutoa chakula, dawa na misaada mingine kwa watu watakaohamishwa. Alisema maagizo ya kuondoka yatatolewa wakati utakapofika na serikali itahakikisha wananchi wanaondolewa kwa utu na kupewa taarifa mapema. "Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha uwezekano wa mvua nyingi Nairobi, na inatarajiwa kuwa wiki ya pili na ya tatu ya Oktoba ndipo mvua itaanza," alisema. Idara ya kukabiliana na majanga ya Kaunti ya Nairobi imeanza kusafisha mabomba na njia za maji ya mvua ili kupunguza hatari ya mafuriko. Prof Kindiki alisema maeneo yote yanayozuia maji yametambuliwa na kazi ya kuyafungua na kuondolea uchafu inaendelea. Kaunti inashirikiana na Tume ya Mto Nairobi, huku vijana wa Green Army na Climate Works wakishiriki katika zoezi hilo. Wakati huo huo, Waziri wa Maji Erick Mugaa amewataka wanaoishi kando ya mito kuwa waangalifu kutokana na uwezekano wa viwango vya maji kupanda. Akizungumza wakati wa sherehe za Mara Day huko Bomet, Bw Mugaa alisema wataalamu wa hali ya hewa wanatarajia mvua nyingi kuliko kawaida. Alisema serikali inashirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki na Tume ya Bonde la Ziwa Victoria katika maandalizi. Kamishna wa Wilaya ya Tarime nchini Tanzania, Meja Edward Golowe, alisema tope linalosababishwa na shughuli za binadamu sehemu za juu za Mto Mara limebadilisha mkondo wa mto huo na kuongeza hatari kwa familia zinazoishi kando yake. Serikali pia imeanza kukagua njia za umeme ili kupunguza kukatika kwa umeme wakati wa mvua. Bw Mugaa alisema vituo vya kupima viwango vya maji vinaendelea kutoa taarifa za wakati halisi ili kusaidia kutoa tahadhari na kuhamisha watu hadi maeneo salama. Kituo cha Kitaifa cha Kushughulikia Majanga (NDOC) kinaratibu maandalizi hayo kote nchini. Maafisa wa serikali za kaunti wamepewa jukumu la kutambua maeneo hatari kwa mafuriko na maporomoko ya ardhi, njia za uokoaji na vituo vya kuwahamishia waathiriwa. Tahadhari pia itatolewa kupitia mikutano ya hadhara, makanisa, misikiti na vituo vya redio vya kimaeneo. Serikali imesema makundi yaliyo katika hatari zaidi, wakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, watapewa kipaumbele wakati wa uokoaji. Wakati huo huo, viongozi wa dini kupitia Association of Religious Practitioners Professionals (AREPP) wamejiunga na maandalizi hayo. Mkurugenzi wake, Dkt Ezekiel Muendo, alisema waumini 470 na wajitolea 940 wamehamasishwa kusaidia katika maandalizi na shughuli za uokoaji. Alisema maeneo ya ibada yako tayari kutumika kama vituo vya uokoaji na shughuli za dharura kuanzia Oktoba 2026 hadi Machi 2027.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 24 Sep 2026 09:54:48
Kituo kipya cha huduma za uwekezaji Nyali kufaidi Pwani
Benki ya Standard Chartered imefungua kituo kipya cha huduma za kifedha cha Priority Centre katika eneo la Nyali, Mombasa, hatua inayolenga kuwahudumia wateja wenye uwezo mkubwa wa kifedha katika eneo la Pwani. Kituo hicho kitatoa huduma maalumu za ushauri kuhusu uwekezaji, upangaji wa mali, ufadhili, uhifadhi wa utajiri na mipango ya kurithisha mali vizazi vijavyo. Benki hiyo imesema hatua hiyo inalenga kuwaleta karibu wananchi wa Pwani na fursa za uwekezaji wa kimataifa kupitia mtandao wake mkubwa duniani. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo,Birju Sanghrajka, Mkurugenzi Mkuu wa Standard Chartered Kenya, alisema Mombasa imeendelea kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi nchini kutokana na ukuaji wa biashara, utalii, usafirishaji na viwanda. Alibainisha kuwa uchumi wa kaunti hiyo una thamani ya zaidi ya Sh700 bilioni, jambo linaloongeza mahitaji ya huduma za kifedha za hali ya juu. Kwa upande wake, Edith Chumba, Mkuu wa Huduma za Utajiri wa Standard Chartered Kenya na Afrika Mashariki, alisema wateja wengi wanahitaji ushauri unaovuka mipaka ya uwekezaji wa kawaida ili kuwasaidia kujenga, kuhifadhi na kuhamisha utajiri wao kwa vizazi vijavyo. Kauli hiyo pia ilionyesha kuwa Mombasa inaendelea kuimarika kama kitovu cha biashara na uwekezaji. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, Bandari ya Mombasa ilihudumia tani milioni 22.3 za mizigo, huku tani 566,400 zikisafirishwa kwa reli. Aidha, zaidi ya wageni wa kimataifa 96,700 waliwasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mombasa katika miezi minne ya kwanza ya mwaka huo. Kituo kipya cha Nyali kinaongeza uwepo wa huduma za Priority Banking za Standard Chartered nchini Kenya, huku benki hiyo ikilenga kupanua huduma zake kwa wateja wenye utajiri mkubwa nje ya Nairobi na kuwapa fursa za kifedha kutoka shirika la kimataifa
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 24 Sep 2026 08:00:54
Sifuna ngangari licha ya misukosuko ya kupata chama
SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anakabiliwa na shinikizo la kupata chama atakachotumia kuwania urais katika uchaguzi wa 2027, huku pia akishughulikia tofauti za kisiasa ndani ya vuguvugu la Linda Mwananchi. Timu yake iko katika Mahakama ya Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT), ikipinga uamuzi wa kuhifadhi jina la "Linda" kwa mtu mwingine. Wakati huo huo, baadhi ya viongozi wa upinzani wanamtaka Bw Sifuna awe mgombea mwenza wa kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, katika uchaguzi huo. Hata hivyo, ndani ya Linda Mwananchi kuna viongozi wenye mipango tofauti ya kisiasa, hali inayotishia umoja wa vuguvugu hilo. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesajili The Mwananchi Party (TMP), huku Mbunge wa Saboti Caleb Amisi akiondoka na kuunda People's Renaissance Movement (PRM). Bw Sifuna pia ameingia kwenye mzozo na Bw Musyoka baada ya kiongozi huyo kuhifadhi jina la The Ukombozi Alliance (TUA) kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP). ORPP ilikataa ombi la upande wa Bw Sifuna kubadili jina la United Democratic Party (UDP) kuwa Ukombozi People's Party (UPP), ikisema jina hilo linafanana na TUA. Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema suala la tarehe ya Oktoba 15 iliyowekwa na IEBC halimaanishi Bw Sifuna lazima awe tayari na chama kufikia siku hiyo. Alisema tarehe muhimu kisheria ni Februari 2027, wakati wagombea watapaswa kuwa wanachama wa chama kwa angalau miezi sita kabla ya uchaguzi. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya alisema timu hiyo tayari imekubaliana kuhusu chama kitakachotumiwa na Bw Sifuna na kwamba kitazinduliwa Oktoba 3. Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka alisema maandalizi ya uzinduzi yanaendelea na akakanusha madai kwamba Bw Sifuna atakuwa mgombea mwenza wa Bw Musyoka. Alisema mazungumzo pia yanaendelea na chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachohusishwa na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kuhusu uwezekano wa ushirikiano. Mbunge wa Funyula Oundo Midenyo alisema licha ya kushindwa kupata jina la Ukombozi, Linda Mwananchi itaendelea na mipango yake na Bw Sifuna atasalia kuwa mgombea wake wa urais. Alisema chama kipya kitazinduliwa kikiwa na nembo na rangi zinazohusishwa na Linda Mwananchi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 24 Sep 2026 07:00:18
Tunataka hivi: Wadau wa elimu wapendekeza mabadiliko makubwa katika Mswada wa elimu 2026
WADAU wa elimu wanataka mabadiliko makubwa katika Mswada wa Elimu ya Msingi wa 2026, ikiwemo kuimarishwa kwa ushiriki wa wazazi, mfumo wa elimu wa 2-6-3-3 kukitwa katika sheria na serikali kubeba kikamilifu gharama ya elimu ya msingi. Mswada huo unapendekeza kuchukua nafasi ya sheria iliyopo kuhusu elimu ya msingi na unahusu usimamizi wa shule, ufadhili, ustawi wa wanafunzi, walimu, ubora wa elimu na data za elimu. Katika mapendekezo yao kwa Bunge kuhusu miswada ya Elimu ya Msingi na Elimu ya Juu, Uteuzi na Ufadhili wa Wanafunzi ya 2026, wadau pia wanataka wazazi wapewe mamlaka zaidi kisheria na mfumo wa usimamizi wa vifaa vya kufunza ufanyiwe mabadiliko. Kundi la Elimu Bora Working Group (EBWG) limehoji sababu za kuwasilisha miswada hiyo kabla ya sera mpya ya kitaifa ya elimu kuidhinishwa. Kundi hilo linataka mfumo wa 2-6-3-3 — miaka miwili ya elimu ya chekechea, sita ya msingi, mitatu ya sekondari msingi na mitatu ya sekondari pevu — uwekwe wazi kwenye sheria. Linasema kuacha mfumo huo uamuliwe kupitia kanuni kunaweza kupatia serikali ijayo nafasi ya kubadilisha mfumo wa elimu bila kuhitaji sheria mpya. EBWG pia inataka vigezo vya kuwaweka wanafunzi katika mikondo ya shule ya upili viwekwe wazi, ikiwemo matokeo, maslahi, uwezo na hatua za kuwasaidia wanafunzi kutoka makundi yaliyotengwa. Kuhusu ufadhili, kundi hilo linataka serikali iwajibike kikamilifu kugharamia miundomsingi, vifaa vya kufunza, chakula, usafi na mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu. Linasema mianya inayoruhusu shule kutoza "ada za ziada" inaweza kutumiwa kurejesha ada kwa jina jingine. Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA) nacho kinataka kitambuliwe kikamilifu kisheria na kupewa uwezo wa kumiliki mali, kuajiri wafanyakazi, kuendesha akaunti na kushtaki au kushtakiwa kwa jina lake. NPA pia kinataka miundo yake ya uwakilishi kuanzia shuleni hadi kitaifa ihifadhiwe na neno PTA libadilishwe kuwa Parents Associations. Shirika la Education Stakeholders Association of Kenya (ESAK) limependekeza pia lipewe nafasi ya kuteua mwakilishi katika kila Bodi kati ya 47 za Elimu za Kaunti. ESAK linasema wadau wengi wa elimu wameachwa nje ya bodi hizo licha ya kuwa na mchango muhimu katika usimamizi wa elimu ya msingi. Kuhusu elimu ya juu, EBWG inataka serikali iwafadhili kikamilifu wanafunzi na wanafunzi wa mafunzo ya ufundi, huku ufadhili huo ukijumuisha karo, malazi, chakula, vifaa, usafiri, afya na utafiti. Pia linataka mikopo, ruzuku, ufadhili wa masomo na basari zitofautishwe wazi na wanafunzi waendelee kupata ufadhili hadi watakapokamilisha masomo yao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Thu, 24 Sep 2026 06:00:58
Kindiki asihi mlima kumwamini aupeleke 'canaan'
NAIBU wa Rais Kithure Kindiki amewaomba wapiga kura wa Mlima Kenya wamwamini kuwaongoza katika mazungumzo ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Prof Kindiki alisema eneo hilo linahitaji umoja na ajenda ya maendeleo ili kupata manufaa zaidi kisiasa na kiuchumi. Akizungumza Maragua alipokagua ujenzi wa barabara ya Gwathamaki-Mbombo yenye urefu wa kilomita 16 kwa thamani ya Sh1 bilioni, Prof Kindiki alisema Mlima Kenya unapaswa kuingia katika uchaguzi wa 2027 ukiwa umeungana. "Mlima ni mmoja. Ajenda ni maendeleo. Thamani ni mazungumzo ya pamoja yanayolenga mwananchi bila kupoteza mwelekeo wa miradi ya maendeleo. Niaminini niwafanyie mazungumzo. Nia yangu ni ustawi wa watu wetu na utulivu wa taifa," alisema. Alisema wakosoaji wa Rais William Ruto wanaodai kuwa aliahidi mengi hawatafanikiwa, akisisitiza kuwa serikali itaonyesha matokeo kupitia miradi ya maendeleo. Prof Kindiki alizungumza siku nne baada ya kundi la wazee wa Mlima Kenya kumteua kuwa msemaji mkuu wa eneo hilo kuelekea uchaguzi wa 2027. Hata hivyo, uteuzi huo umezua mgawanyiko miongoni mwa wazee, hasa upande wa magharibi wa Mlima Kenya. Mlezi wa Kiama Kia Ma, Kung'u Muigai, na mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Kikuyu, Wachira Kiago, wamekataa kutambua mkutano wa Kirigiti Stadium, Kiambu, wakisema haukuwa na uhalali wala ushawishi unaodaiwa. Profesa Kindiki aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kuepuka siasa za hisia na badala yake kuzingatia utawala na maendeleo. Alisema pia eneo hilo halipaswi kujitenga kisiasa, bali linapaswa kushirikiana na Wakenya wengine katika kutafuta mustakabali bora wa nchi. Naibu Rais alisema serikali imetenga Sh56 bilioni kujenga takriban kilomita 1,200 za barabara za lami katika Kaunti ya Murang'a. Alisema wakulima pia wananufaika kutokana na ongezeko la bei za mazao, akitaja kahawa ambayo bei yake imeongezeka kutoka Sh50 hadi Sh130 kwa kilo na maziwa kutoka Sh35 hadi Sh50 kwa lita. Alisema bei ya mbolea imeshuka kutoka Sh7,000 hadi Sh2,000 kwa gunia, huku mbegu ya mahindi iliyothibitishwa ikishuka kutoka Sh300 hadi Sh150 kwa kilo. Prof Kindiki pia alitaja miradi ya umeme, masoko ya mazao, nyumba za gharama nafuu, mabweni ya wanafunzi na vituo vya ICT miongoni mwa miradi inayoendelea Murang'a.
read moreRight Column Content