taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 16 Sep 2026 04:55:52
NI HISTORIA: Sababu za Kenya kutuzwa uandalizi wa mbio kubwa zaidi duniani
HISTORIA pevu ya Kenya katika riadha, ongezeko kubwa la mashabiki wa mchezo huo, ukarabati kabambe wa miundomsingi ya michezo na ufadhili thabiti wa serikali umeiwezesha Nairobi kushinda zabuni ya kuandaa Riadha za Dunia za mwaka 2029. Tunu hiyo pia imetokana na mafunzo muhimu yaliyopatikana baada ya Nairobi kushindwa katika zabuni ya kuandaa Riadha za Dunia za 2025, ambazo zilipewa Tokyo, Japan. Nairobi ilirekebisha kasoro zilizojitokeza katika uwaniaji huo na kuboresha mipango yake ili kulishawishi Baraza la Riadha Duniani mara hii. Rais wa Riadha Duniani, Sebastian Coe, alisema Nairobi iliweka rekodi nzuri zaidi baada ya kurejea na pendekezo imara la kuandaa mashindano ya 2029, ikitumia tajriba ya karibu muongo mmoja ya kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa ya riadha. Coe alisema Nairobi ilianza kujijengea sifa kwa kuandaa Riadha za Dunia za Wasiozidi miaka 18 (Under-18) mnamo 2017, Under-20 mwaka 2021 na Kip Keino Classic, mashindano ya World Athletics Continental Tour Gold yaliyoanzishwa mwaka wa 2020. "Riadha za Under-18 ya 2017 zilidhihirisha hamu kubwa ya Wakenya katika riadha, huku umati mkubwa ukijaza uwanja wa Kasarani katika kipindi chote cha mashindano. "Tangu wakati huo, Nairobi imeifanya Kip Keino Classic kuwa mojawapo ya mashindano makubwa ya siku moja barani Afrika, huku mashindano hayo yakiwa sehemu ya World Athletics Continental Tour Gold," alisema Coe. Aliongeza kuwa tajriba hiyo iliweka msingi imara wa zabuni ya 2029 iliyojumuisha mipango madhubuti ya uendeshaji pamoja na dhamana za kifedha. Uwanja wa Kasarani, ambao unafanyiwa ukarabati mkubwa kabla ya kuandaa Kombe la Afrika (AFCON) 2027, miaka miwili kabla ya Riadha za Dunia, ni sehemu muhimu ya maono ya kuandaa Riadha za Dunia kwa mara ya kwanza barani Afrika. Kiongozi huyo wa riadha duniani alisema Nairobi imeonyesha wazi kuwa wakati umefika wa kuharakisha maendeleo ya riadha nchini Kenya na barani Afrika, huku ikiweka urithi utakaolihamasisha bara hilo na dunia nzima. Nguvu ya uhusiano wa Kenya na riadha pia imeonekana katika utafiti wa World Athletics kuhusu mashabiki, ambao umeonyesha kiwango cha kipekee cha ushiriki wao. Asilimia 68 ya Wakenya waliohojiwa walisema wana hamu kubwa ya kufuatilia riadha, ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa asilimia 39. Hii inaifanya Kenya kuwa soko lenye hamu kubwa zaidi ya riadha miongoni mwa masoko yaliyofanyiwa utafiti. "Kenya ina alama ya juu zaidi ya net promoter score kuliko soko lolote, na riadha ndiyo mchezo wa pili unaofuatiliwa zaidi nchini, baada ya soka pekee," alisema Coe. Aliongeza kuwa Kenya ni nchi ya nne duniani kwa idadi ya wafuasi wa kurasa za Riadha Duniani katika mitandao ya kijamii. Kenya ni nchi ya pili yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Mashindano ya Dunia ya Riadha, ikiwa nyuma ya Marekani katika orodha ya medali. Kenya imeshinda jumla ya medali 182 — dhahabu 72, fedha 60 na shaba 50 — tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mjini Helsinki, Finland, mwaka 1983. Marekani ina medali 649, zikiwemo dhahabu 211, fedha 139 na shaba 119. Katika Mashindano ya Dunia ya Riadha yaliyofanyika Tokyo mwaka uliopita, Kenya ilishinda medali saba za dhahabu na 11 kwa jumla. Wanariadha wa Kenya walinyakua mataji yote ya wanawake katika mbio za masafa ya kati hadi marefu uwanjani na mbio za marathoni. Coe alisema Nairobi iliwasilisha zabuni iliyokuwa na ushindani mkubwa na iliyogusa hisia, akieleza jiji hilo kuwa kitovu kinachokua kwa kasi, chenye nguvu na cha kisasa katika huduma, uchumi, utamaduni na siasa za Afrika Mashariki. "Kupeleka Mashindano ya Dunia ya Riadha barani Afrika kwa mara ya kwanza kutakuwa jambo la kihistoria. Ilikuwa muhimu mashindano hayo yaje Afrika wakati tunapokuwa na mwenyeji anayefaa, zabuni inayofaa na mazingira yanayofaa. Nairobi imeonyesha wazi kuwa wakati wake umefika," alisema Coe. Alisema riadha imejikita katika maisha ya Wakenya na imekuwa chimbuko la wanariadha waliounda historia ya mchezo huo duniani, wakiwemo mabingwa wa dunia Faith Kipyegon, Vivian Cheruiyot, Eliud Kipchoge, Hellen Obiri na David Rudisha. Wengine ni bingwa wa Olimpiki mara mbili Kip Keino, bingwa mara kadhaa wa dunia wa mbio za nyika Paul Tergat na bingwa mara kadhaa wa dunia wa nusu marathoni Tegla Loroupe.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 47 minutes ago
Kioni ajiuzulu, 'amwachia' Matiang'i Jubilee akigusia kujiundia chama chake
CHAMA cha Jubilee kimepata mabadiliko mapya baada ya naibu kiongozi wake Jeremiah Kioni kujiuzulu, akihitimisha uhusiano wake wa kisiasa wa miaka 11 na chama hicho kinachojiandaa kufanya mkutano maalumu wa wajumbe wiki ijayo. Bw Kioni, aliyewahi kuwa Mbunge wa Ndaragwa na katibu mkuu wa zamani wa Jubilee, alitangaza kuondoka Alhamisi, siku moja baada ya chama kutoa notisi ya kuitisha Mkutano Maalumu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) Desemba 3 katika Jockey Club, barabara ya Ngong, Nairobi. Mkutano huo unatarajiwa kujadili ripoti za vitengo mbalimbali vya chama, kuchagua na kuidhinisha viongozi wa kitaifa, pamoja na mapendekezo ya mabadiliko ya katiba ya Jubilee. Hatua hiyo inajiri huku chama hicho kikiendelea na mabadiliko ya uongozi chini ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang'i, ambaye anajiandaa kuwania urais katika uchaguzi wa 2027. Katika barua yake ya kujiuzulu, Bw Kioni alisema uamuzi wake umetokana na kutafakari safari yake ya miaka 11 ndani ya Jubilee, akieleza kuwa chama hicho kilikuwa kama nyumbani kwake na kilimpa nafasi ya kuwatumikia Wakenya. "Imekuwa miaka 11, safari ndefu na muhimu katika maisha yangu, ambayo naweza kuwa tayari kuipitia tena," alisema. Alimshukuru Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa uongozi na urafiki wao, akisema uhusiano wao ulivuka mipaka ya siasa. Pia aliwashukuru wanachama wa Jubilee kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuwa katibu mkuu kwa miaka minne na naibu kiongozi wa chama kwa karibu mwaka mmoja. Alisema nyadhifa hizo zilimfundisha unyenyekevu, subira na umuhimu wa kuheshimu taasisi. Bw Kioni pia alimtakia Dkt Matiang'i mafanikio katika kuongoza chama hicho na kampeni zake za kuwania urais. Kuondoka kwake kunafuatia mabadiliko ya uongozi yaliyoanza Januari mwaka huu, alipohamishwa kutoka wadhifa wa katibu mkuu na kuwa naibu kiongozi wa chama. Aliyekuwa Mbunge wa Narok Kaskazini, Moitalel Ole Kenta, aliteuliwa kuchukua nafasi ya katibu mkuu. Mabadiliko hayo yaliendelea Septemba baada ya Bw Kenyatta kuacha uongozi wa Jubilee na kumkabidhi Dkt Matiang'i, akisalia mwanachama na mshauri wa chama. Bw Kioni alikuwa ametangaza nia ya kumrithi Bw Kenyatta, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuchaguliwa kidemokrasia na wajumbe badala ya kukabidhiwa mamlaka. Wiki iliyopita, alidokeza uwezekano wa kuondoka Jubilee, akisema hakuwa akishirikishwa katika shughuli za kisiasa za Dkt Matiang'i wala kupewa majukumu maalumu licha ya kuwa naibu kiongozi. Alisema awali alitarajia kushirikiana na Dkt Matiang'i, ambapo waziri huyo wa zamani angejikita katika azma ya urais huku yeye akijenga chama. Katika barua yake, Bw Kioni alifafanua kuwa kuondoka Jubilee hakumaanishi mwisho wa safari yake ya kisiasa. "Kuondoka kwangu si kuaga maisha ya umma wala mwisho wa safari yangu ya kisiasa. Ninapojiandaa kuzindua jukwaa jingine, ninachukua mafunzo na urafiki wa miaka hii 11 katika hatua inayofuata," alisema. Mkutano wa Desemba 3 unatarajiwa kurasimisha mabadiliko ya uongozi na kuweka msingi wa Jubilee kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
ODM mambo ni matatu tu kuhusu 2027
CHAMA cha ODM kinakabiliwa na chaguo tatu: kumuunga mkono Rais William Ruto kuwania muhula wa pili, kuungana na viongozi wa upinzani au kushiriki kivyake katika uchaguzi wa 2027. Uongozi wa ODM umeweka Januari 31, 2027 kuwa tarehe ya mwisho ya kukamilisha mazungumzo na UDA kuhusu uwezekano wa kuunda muungano rasmi. Uamuzi huo ulitangazwa Jumatano baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Usimamizi ya chama hicho, huku viongozi wakisema wanataka mazungumzo hayo yakamilike mapema ili kutoa nafasi ya kupanga mikakati ya uchaguzi. Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohamed, alisema timu inayoshughulikia sera na manifesto za vyama hivyo itaharakisha kazi ili kutoa ripoti ifikapo Januari 31. Alisema ripoti hiyo itafafanua masuala na sera zitakazotumika kuunda muungano na UDA. Hatua hiyo inajiri huku baadhi ya viongozi wa ODM wakilalamikia kutoheshimiwa na kutotambuliwa kwa mchango wa chama hicho katika serikali jumuishi. Rais Ruto na kiongozi wa ODM Oburu Oginga tayari wameunda kamati ya kiufundi inayolenga kuunganisha manifesto za vyama hivyo kabla ya kutia saini makubaliano rasmi. Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Nyanza wanataka Rais Ruto akutane nao haraka ili kujadili masharti ya kumuunga mkono, ikiwemo ugavi wa maeneo ya kisiasa na nafasi ambazo ODM itanufaika nazo. Mbunge mmoja aliambia Taifa Leo kuwa chama hicho kina wasiwasi kuwa kinaendelea kuunga mkono serikali huku baadhi ya maafisa wakifanya kazi ya kukidhoofisha kisiasa. Alisema ODM inataka uhakika kuhusu manufaa ya kumuunga mkono Rais Ruto, badala ya kuonekana kuwa kinaiunga mkono bila kupata chochote. Hata hivyo, alisema chama hakitishwi na wimbi la chama cha MDG, akisema Dkt Oburu ameahidi uteuzi wa haki ambapo wagombea wenye nguvu watapata nafasi na uamuzi wa wananchi kuheshimiwa. Oburu tayari ametangaza kuwa ODM haitakuwa na mgombea wa urais mwaka 2027 na badala yake itamuunga mkono Ruto. Mnamo Julai 12, 2026, alisema chama hicho kitashiriki katika uchaguzi nyuma ya Rais Ruto ili kumwezesha kuhudumu kwa muhula wa pili. Hata hivyo, alisisitiza kuwa ushirikiano huo lazima uwe na muundo unaohakikisha ODM inapata nafasi serikalini na sera zake kuingizwa katika ajenda ya serikali. Mchambuzi wa siasa Profesa Masibo Lumala anaamini ODM haina nafasi kubwa ya kubadili msimamo na kusimamisha mgombea urais. Alisema migawanyiko ya ndani na ukosefu wa viongozi wenye ushawishi wa kutosha vimedhoofisha uwezo wa chama kujadiliana na UDA. Alitaja kuondoka kwa James Orengo, Babu Owino na Edwin Sifuna na kujitenga kwa Profesa Anyang' Nyong'o na siasa za kila siku, kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia pengo la uongozi. Lakini Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi, anasema ODM haina njia nyingine isipokuwa kuendelea kushirikiana na Ruto. Alisema chama hicho hakiwezi kuungana na makundi hasimu ya kisiasa yanayoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Wakati huohuo, Seneta wa Narok Ledama Ole Kina amewataka viongozi wa ODM kuketi pamoja na kukubaliana kuhusu mwelekeo wa chama. Alisema wakati umefika wa kuacha kujificha nyuma ya makundi ya kisiasa na badala yake kufanya mazungumzo ya wazi kuhusu umoja na mustakabali wa chama. Ndani ya ngome ya Nyanza, baadhi ya viongozi, akiwemo Waziri wa Hazina John Mbadi, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, wanataka ODM ipate mgao wa 50-50 katika ushirikiano huo. Pia, chama hicho kinataka wadhifa wa Naibu Rais uwe sehemu ya makubaliano ya kugawana mamlaka. Hata hivyo, Atandi amewataka viongozi kutofanya kiti hicho kuwa sharti la kumuunga mkono Ruto, akisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuchagua mgombea mwenza wake. Mbadi ana matumaini kuwa makubaliano rasmi yatatiwa saini Februari mwaka ujao. Mchambuzi wa siasa Javas Bigambo anasema migawanyiko hiyo inatokana pia na tamaa za uongozi na hofu ya ushindani katika kipindi cha baada ya kifo cha Raila Odinga. Alisema baadhi ya wanasiasa wanajaribu kujitwalia nafasi ya Raila, huku wengine wakitumia kutokuwepo kwake kupinga maamuzi ya chama. Bw Bigambo aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wanatumia MDG kama kisingizio cha hofu yao kuhusu uteuzi, huku ODM ikijaribu kulinda ushawishi wake Nyanza baada ya Raila.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
Linda Mwananchi yapigwa na baridi bila Sifuna aliye ziarani Amerika
SAFARI ya Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna nchini Amerika imevuruga kwa muda mikakati ya mrengo wa Linda Mwananchi, ambao ulikuwa umeanza kupata umaarufu kupitia mikutano ya hadhara na shughuli za kujijenga mashinani. Kutokuwepo kwa Seneta Sifuna, ambaye ndiye sura kuu ya vuguvugu hilo, sasa kunatoa mtihani wa kwanza kuhusu uwezo wa viongozi wake kuendeleza hamasa kwa wafuasi bila yeye kuwepo. Hali hii inajiri huku Rais William Ruto akizidisha kampeni zake katika eneo la Magharibi mwa Kenya, ambako anaanza ziara ya siku nne kesho. Sifuna alianza ziara yake Amerika Novemba 20, akikutana na Wakenya wanaoishi ughaibuni kwa lengo la kuchangisha fedha za kufadhili shughuli za kisiasa za Linda Mwananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Ziara hiyo inatarajiwa kukamilika Desemba 7. Alisafiri na ujumbe wa viongozi kadhaa, akiwemo Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na mkuu wa mawasiliano wa vuguvugu hilo Pauline Njoroge. Hata hivyo, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka, Mbunge wa Funyula Oundo Mudenyo na aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo waliachwa nchini. Mkutano mkubwa wa mwisho wa Linda Mwananchi ulifanyika Ukunda, Kaunti ya Kwale, Oktoba 31. Tangu wakati huo, shughuli nyingi za vuguvugu hilo zimeonekana kupungua, huku viongozi wake wakisubiri kurejea kwa Sifuna. Baadhi ya viongozi walioonekana kuwa washirika wake wa karibu wameendelea na shughuli zao binafsi za kisiasa. Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino amekuwa akifanya mikutano yake jijini Nairobi, huku Gavana wa Siaya James Orengo akijiunga na mrengo wa unaohusishwa na Fred Matiang'i, Ndindi Nyoro na Martha Karua, akipigia debe chama chake cha Liberal Democratic Party (LDP). Wakati huo, viongozi wengine wa upinzani wameendelea na mikutano ya kutafuta uungwaji mkono kivyao. Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua mnamo Alhamisi alifanya mikutano Kamukunji, Mathare na maeneo mengine ya Eastlands jijini Nairobi, akitangaza chama chake cha DCP. Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka naye alifanya mikutano katika eneo bunge la Mwala mwishoni mwa wiki, akiendeleza kampeni za kuwania urais katika ngome yake ya Ukambani. Katika eneo la Magharibi, Natembeya, ambaye ndiye mwakilishi mkuu wa Sifuna, amekuwa akijikita zaidi katika shughuli za kisiasa za Kaunti ya Trans Nzoia. Akizungumza na Taifa Leo, gavana huyo alisema mikutano ya Linda Mwananchi itarejea Sifuna atakaporejea kutoka Amerika. Alisema kwa sasa vuguvugu hilo linaangazia kupata uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya wanaoishi ughaibuni, lakini akasisitiza kuwa shughuli za kisiasa haziishii katika mikutano ya hadhara. Alisema dhamira yao bado ni kushiriki katika uongozi wa nchi baada ya uchaguzi wa 2027 na kwamba ujumbe wa Sifuna Amerika umepokelewa vyema. Hata hivyo, kutokuwepo kwa Sifuna kumeambatana na kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa kati ya viongozi wa upinzani Magharibi. Mnamo Alhamisi, kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa alitangaza kumwondoa Natembeya katika nafasi ya naibu kiongozi wa chama, pamoja na Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula, ambaye ameonyesha kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi ujao. Wamalwa alisema Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya amependekezwa kuchukua nafasi ya Natembeya na atathibitishwa katika kikao cha Baraza Kuu la Kitaifa la chama (NEC) wiki ijayo. Wamalwa na Natembeya wamekuwa na uhusiano wenye misukosuko kutokana na mvutano kuhusu nani anayepaswa kuwakilisha Magharibi katika meza ya mazungumzo ya upinzani. Natembeya amekuwa akimshutumu Wamalwa kwa kufanya njama kumdhoofisha Sifuna na kuzuia azma yake ya kuwania urais kupitia upinzani. Gavana huyo amemtaka Wamalwa kuacha kuwa kikwazo kwa Sifuna na badala yake ajitokeze kuwania ugavana wa Trans Nzoia. Hata hivyo, Wamalwa amepuuzilia mbali madai hayo, akisema hana pingamizi kwa Sifuna kuzingatiwa kama mgombea wa urais wa upinzani. Alisema upinzani unapaswa kuimarisha ushirikiano na kutafuta washirika katika maeneo mengine ya nchi badala ya kutegemea eneo moja pekee. Kwa upande wake, Natembeya alielezea kuondolewa kwake katika uongozi wa DAP-Kenya kuwa uamuzi bora zaidi ambao Wamalwa amewahi kufanya kisiasa. Alisema hajawahi kumuomba Wamalwa kumpa nafasi ya uongozi na kumtaka aendelee na shughuli zake za chama bila kumzuia.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 2 hours ago
Ngumi na mateke yatamba baina ya madiwani Kisumu katika jaribio la kung'oa Spika Oraro
VURUGU zilitokea katika Bunge la Kaunti ya Kisumu Alhamisi baada ya kundi la madiwani kuanzisha mchakato wa kumuondoa ofisini Spika Elisha Oraro, huku wenzake waliopinga wakijaribu kumlinda. Mzozo huo uligeuka mapigano ya mateke na makonde, huku Oraro akiondolewa kwa nguvu kutoka kwenye kiti chake. Tukio hilo lilianza baada ya madiwani kuuliza kwa nini hoja ya kumuondoa spika haikuwa kwenye ratiba ya shughuli za bunge iliyowasilishwa. MCA wa South West Nyakach Gard Olima na mwenzake wa East Kano Wawidhi Moses Ochele walitaka kujua kwa nini Oraro hakuwa akiongoza kikao kwa kutumia ratiba ya ziada iliyokuwa na hoja hiyo. Oraro alisema baada ya kushauriana na karani wa bunge, hakuwa amepokea ratiba hiyo ya ziada. Alisema ataheshimu uamuzi wa madiwani iwapo mchakato wa kumuondoa madarakani utafuata sheria na kanuni za bunge. Hata hivyo, jibu lake lilizua hasira na kundi la madiwani kuvamia kiti chake na kumtoa kwa nguvu. Baadhi ya waliopinga walijaribu kumkinga, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na mapigano yakazuka. Maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Kisumu Central walifika kujaribu kurejesha utulivu. Oraro aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi huku baadhi ya wananchi waliokuwa nje ya bunge wakimzomea na kumtishia. Jaribio lake la kurejea bungeni akiwa ameandamana na polisi lilizimwa na madiwani. Ochele aliteuliwa kuwa Kaimu Spika na kuongoza kikao kilichofanyika bila karani wala ratiba rasmi ya shughuli za bunge.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 13 hours ago
Wadau wataka kasi iongezwe katika juhudi za kukomesha ndoa za watoto
ULIMWENGU unapoadhimisha leo Siku ya Kukomesha Ndoa za Watoto, kwa mara ya kwanza baada ya kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa, washikadau wanataka kasi ya juhudi hizo iimarishwe ili kufikia malengo. Wadau tofauti wakiongozwa na shirika la Femnet, walisema kuwa kwa muda mrefu wameangazia juhudi za kibinafsi, lakini sasa kuna haja ya kuja pamoja na kuelekeza mikakati yao kwa wahusika ili kupata matokeo yatakayosaidia kuzima ndoa za watoto. Walishiriki warsha hiyo Novemba 26, 2026 katika hoteli ya Park In Radisson, Nairobi. Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban wasichana 12 milioni huozwa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18. Kusini mwa Asia ndiko kuna asilimia kubwa ya 44 ya watoto wasichana wanaoozwa mapema, huku Kusini mwa Jangwa la Sahara ikifuata na asilimia 18. Ingawaje, kulingana na Malengo Endelevu (SDGs), hatua ilikuwa kutimiza lengo hilo kufikia 2030, juhudi hizo zimeonekana kwenda pole pole, na sababu ya wito wa kasi hiyo kuongezwa. Akiongea katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Femnet Dkt Carole Agengo alisisitiza haja ya mashirika na wadau husika kuungana na kuleta fikra na juhudi zao pamoja ili kuweza kufanikisha lengo hilo. Mkurugenzi wa Wanawake, Jinsia, na Vijana katika Umoja wa Afrika, Bi Prudence Nonkululeko Ngwenya, pia alishikilia msimamo huo wa kuimarisha juhudi hizo, na watu kuelekea mashinani ambapo matukio hayo yanafanyika na kutafuta suluhu za kudumu. "Tunalazamika sasa kuondoka kutoka kwa ahadi za kuchukua hatua, na twende kwenye utekelezaji. Lazima tuwekeze kwa wasichana hawa kwa kuhakikisha kuwa wanasalia shuleni na kuimarisha uwajibikaji," alisema. Mwakilishi wa Idara ya Jinsia, Bi Verity Mghanga, alifafanua juhudi za serikali huku akisema kuwa kuna mengi ambayo bado yanastahili kufanywa. Alieleza kuwa licha ya juhudi hizo, mambo mengi bado yanafanywa kwa siri kubwa na kuhusisha jamii, kumaanisha kuwa jamii inakubali au kuvumilia desturi kama hiyo ya kuoza watoto. "Utapata katika baadhi ya jamii, msichana hata wa miaka saba anatumwa kuishi na familia fulani. Kisha anapotimiza umri fulani, anaelezwa kuwa alipelekwa hapo kwa kuwa yeye ni mke wa mzee wa boma," anasema akiongeza kuwa baadhi ya watoto hao pia hupitia maisha magumu kwa kuwa huenda katika familia walizoozwa kuna wake wengine wakubwa ambao wanawatumisha kazi nyingi za nyumbani bila kuzingatia umri wao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 16 hours ago
Vita vyazuka ndani ya Bunge la Kaunti ya Kisumu wakati wa jaribio la kutimua Spika Oraro
Vurugu zilitokea katika Bunge la Kaunti ya Kisumu Alhamisi baada ya kundi la madiwani kuanzisha mchakato wa kumuondoa ofisini Spika Elisha Oraro, huku wenzake waliopinga wakijaribu kumlinda. Mzozo huo uligeuka mapigano ya mateke na makonde, huku Oraro akiondolewa kwa nguvu kutoka kwenye kiti chake. Tukio hilo lilianza baada ya madiwani kuuliza kwa nini hoja ya kumuondoa spika haikuwa kwenye ratiba ya shughuli za bunge iliyowasilishwa. MCA wa South West Nyakach Gard Olima na mwenzake wa East Kano Wawidhi Moses Ochele walitaka kujua kwa nini Oraro hakuwa akiongoza kikao kwa kutumia ratiba ya ziada iliyokuwa na hoja hiyo. Oraro alisema baada ya kushauriana na karani wa bunge, hakuwa amepokea ratiba hiyo ya ziada. Alisema ataheshimu uamuzi wa madiwani iwapo mchakato wa kumuondoa madarakani utafuata sheria na kanuni za bunge. Hata hivyo, jibu lake lilizua hasira na kundi la madiwani kuvamia kiti chake na kumtoa kwa nguvu. Baadhi ya waliopinga walijaribu kumkinga, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na mapigano yakazuka. Maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Kisumu Central walifika kujaribu kurejesha utulivu. Oraro aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi huku baadhi ya wananchi waliokuwa nje ya bunge wakimzomea na kumtishia. Jaribio lake la kurejea bungeni akiwa ameandamana na polisi lilizimwa na madiwani. Ochele aliteuliwa kuwa Kaimu Spika na kuongoza kikao kilichofanyika bila karani wala ratiba rasmi ya shughuli za bunge. MCA wa Muhoroni Koru Vincent K'Omudho aliwasilisha hoja ya kumwondoa Oraro, akitaja sababu tano, zikiwemo usimamizi mbaya wa shughuli za bunge, ukosefu wa uongozi na kupuuza maslahi ya madiwani na wafanyakazi. Madiwani pia walimshutumu kwa kukosa uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za bunge. Aidha, walidai alishindwa kushughulikia malalamishi kuhusu marupurupu na mazingira ya kazi ya madiwani na wafanyakazi. MCA wa Kolwa Central Kelvin Oraro, aliyeunga mkono hoja hiyo, alidai Spika alihusika na kupandisha gharama ya miradi kutoka bajeti zilizoidhinishwa na bunge. Mzozo huo umeibua kumbukumbu za namna Oraro mwenyewe alivyopata wadhifa huo baada ya kuondolewa kwa mtangulizi wake, Onyango Oloo, katika mazingira ya vurugu na migawanyiko ya kisiasa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 14 hours ago
EACC kushirikiana na wanahabari kuchunguza wagombeaji 2027
TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) itaanzisha mfumo wa kuwapa wanahabari taarifa zitakazowawezesha kuchunguza uadilifu na sifa za wanaotaka nyadhifa za uchaguzi na uteuzi kabla ya uchaguzi wa 2027. Mwenyekiti wa EACC David Oginde alisema mpango huo utasaidia wanahabari kuchunguza historia, mwenendo na rekodi za wagombea badala ya kutegemea ahadi za kampeni na miungano ya kisiasa. Akizungumza katika mkutano wa tisa wa wahariri nchini, uliofanyika Travelers Beach Hotel, Mombasa, Alhamisi, Dkt Oginde alitaja vyeti ghushi, hongo ya wapiga kura, matumizi mabaya ya rasilimali za umma na ghasia za kisiasa kuwa baadhi ya maovu yanayohitaji uchunguzi zaidi. Alisema EACC itaimarisha ufuatiliaji na uchunguzi wa hongo ya wapiga kura, akiwataka wanahabari kuelimisha wananchi kuhusu madhara yake kwa demokrasia. "Hongo ya wapiga kura inadhoofisha uhuru wa wananchi kuchagua viongozi wao. Inageuza uamuzi muhimu wa kidemokrasia kuwa biashara," alisema. Pia aliwaonya maafisa wa umma dhidi ya kutumia magari, fedha, wafanyakazi na shughuli za serikali kujinufaisha kisiasa, akisisitiza kuwa wanaotaka kugombea lazima wajiuzulu angalau miezi sita kabla ya uchaguzi. Dkt Oginde alilaani matumizi ya vijana kuchochea ghasia na vitisho wakati wa kampeni, akisema wanaopanga na kufadhili vurugu lazima wawajibishwe. Rais wa Kenya Editors Guild Zubeida Kananu aliwataka wanahabari kuchunguza jinsi wagombea walivyoishi, walivyohudumu na wanavyofadhili kampeni zao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 15 hours ago
Pigo kwa Netanyahu bunge likiidhisha achunguzwe kuhusiana na shambulio la Hamas
JERUSALEM, Israel: BUNGE la Israel limepiga hatua ya kwanza kuidhinisha mswada wa kuanzisha tume huru ya kuchunguza kushindwa kwa vyombo vya usalama kuzuia shambulizi la Hamas la Oktoba 7, 2023, ambalo lilikuwa baya zaidi katika historia ya taifa hilo. Hatua hiyo ni pigo kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambaye anapinga uchunguzi huru na badala yake anataka serikali ipewe mamlaka ya kuunda tume na kuteua wajumbe wake. Mswada huo ulipata uungwaji mkono wa wabunge 65 dhidi ya 50, huku ukiungwa mkono na kambi ya upinzani inayoongozwa na Gadi Eisenkot pamoja na vyama vinavyowakilisha jamii ya Waarabu. Hata hivyo, mswada huo unahitaji kupitishwa katika hatua nyingine tatu kabla ya kuwa sheria. Eisenkot, ambaye anajaribu kuunda serikali mpya baada ya muungano wa Netanyahu kupoteza wingi wa wabunge katika uchaguzi wa Oktoba 27, alisema ukweli lazima ujulikane ili kuzuia maafa kama hayo siku zijazo. "Kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, manusura wa utumwani na wale ambao hawakurejea wakiwa hai, tutafichua ukweli na kuchukua kila hatua kuzuia janga jingine," akasema katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii. Netanyahu anapinga tume huru akitaka uchunguzi utakaoongozwa na serikali, huku wapinzani wake wakidai hatua hiyo inalenga kuficha ukweli kuhusu uzembe uliosababisha shambulizi hilo. "Mswada huu utawachunguza wanajeshi wetu jasiri na mashujaa badala ya kumakinikia masuala ya kimsingi," akasema Waziri wa Uchukuzi Miri Regev, mshirika wa karibu wa Netanyahu, akikosoa mswada huo. Katika shambulizi hilo, wapiganaji wa Hamas waliwaua watu 1,200 na kuwateka nyara zaidi ya 250. Israel ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza, yaliyosababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 74,000 na kuwahamisha karibu wakazi wote milioni mbili wa eneo hilo. Wakati huo huo, Eisenkot anakabiliwa na changamoto ya kuunda serikali kabla ya Disemba 6, baada ya kambi yake kupata viti 48 dhidi ya 53 vya muungano wa Netanyahu katika bunge lenye viti 120. Iwapo atashindwa, Netanyahu anaweza kupewa nafasi nyingine ya kuunda serikali, la sivyo uchaguzi mwingine utafanyika.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 19 hours ago
KINAYA: ODM Hawajui Kutongoza!
INAONEKANA chama cha Orange Democratic Movement (ODM) hakijui siri ya utongozaji. Ni siri ya wanaume wengi hasa, na hakuna uamuzi wowote wa mahakama unaomkataza mtu kuifichua. Nitakutobolea. Nakusihi ujongee nikudokezee kwa matao ya chini. Sharti langu ni kwamba usiwaambie watu wa 'pawa' kule ODM. Hatuwezi kuwafunza kila kitu. Acha kiwarambe kidogo. Tangu hapo wajinga ndio waliwao. Na hawa wataliwa na Ulliam kwa raha zake, awatengezee mishikaki au kaimati. Sijali, nitaketi kitako na kujionea sinema yenyewe. Siri ya utongozaji ni kwamba, kabla hujapewa 'mechi' hufai kumuuliza mwenzako iwapo ana mtu au la. Unamtaka yeye, au mtu wake? Tumia akili nanii… Pia, usimwonyeshe kwamba umesalitika kwake kishenzi, yaani huna chaguo, akitaka akumalize. Kisa na maana, huenda ukapewa jawabu usilopenda, likukatishe tamaa, janja zote ulizotembeza ziwe mbio za sakafuni ambazo kawaida huishia ukingoni. Kumbuka kukataliwa kubaya. Kuna safari ambazo hazifai kuvunjikia njiani kabla ya wino na karatasi kukutana. Mtu akishaingia 'boksi', kisha umuulize iwapo ana 'mtu', hata akitoa jawabu lisilokupendeza, hatakuwa na sababu ya kutomuacha 'mtu' wake au kutoendelea na uhusiano huo na kukufuata kwa kuwa tayari amevuka 'mshororo mwekundu'. Hata akitaka kuondoka, unamkumbusha mmetembea pamoja safari ndefu sana, kwake kutaka kurejea alikotoka, au kuketi hapo tu kizembe, ni kufanya maamuzi ya kijinga, kitoto, au yote mawili. Aghalabu atakufuata shingo upande. Ni upungufu wa hekima kwa ODM kujaribu kumpa Ulliam masharti kabla ya kuamua iwapo watamuunga mkono au la katika uchaguzi utakaofanyika mwakani. Tayari wanajiita 'sirkal', wanaturingia eti wamo ndani jikoni, kunakopakuliwa na kuliwa hasa, nasi wengine sote ni watazamaji tunaokula kwa macho. Ulliam na ujanja wake anawaangalia na kujiambia kimoyomoyo 'akili za hawa wote ama zimelala usingizi usiojua wakati wa kuamka, zimekwenda likizoni, wanashindwa kuzitumia, au wamesema zilale tutumie zangu kali'. ODM mnampa Ulliam masharti gani ya kumtishia ilhali tayari mnaramba viatu vyake na kujilaza chini ili awakanyage migongo yenu asipate vumbi tena? Na akiwakanyaga kisha awaambie mfanye mnavyotaka, hatowapa mkate nusu mnaomezea mate? Na akiwaambia tayari amegawa serikali, kazi zinazosalia ni za utarishi na usafishaji vyoo, mtatorokea wapi? Tena, mna muda wa kutoroka kweli, uchaguzi mkuu ujao ukisalia miezi tisa pekee? Hata mkikosa soni na muamue kutoroka, mtakuwa wageni wa nani? Hamna uwezo wala mbinu za kuushawishi upinzani uwape chochote. Mtafungiwa nje pamoja na majibwa, msage meno kisawasawa chambilecho Biblia takatifu. Utongozaji, hata wa kisiasa, unamhitaji mja amakinike, lau sivyo ageuzwe jamvi la wageni. Mtatia akili mara hii. Ulliam, kanyaga shingo kabisa, bado wanapumua! - Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya aliyeishi Amerika kwa muda mrefu (mutua_muema@yahoo.com)
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 21 hours ago
Matabibu watishia kugoma tena wakidai ahadi walizopewa na serikali zimepuuzwa
BAADA ya takriban miaka tisa ya mazungumzo, maafisa wa utabibu hatimaye walipata makubaliano ya pamoja (CBA) kuhusu masuala waliyoibua, lakini sasa wanatishia kugoma wakidai serikali za kaunti hazijatekeleza makubaliano hayo. Katibu Mkuu wa Muungano wa Maafisa wa Utabibu nchini (Kuco) George Gibore, amesema chama hicho kimetoa notisi ya siku saba kwa Baraza la Magavana, Wizara ya Utumishi wa Umma, serikali za kaunti na Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), wakitaka utekelezaji wa makubaliano hayo uanze mara moja. Alisema kucheleweshwa zaidi kwa utekelezaji kutawalazimu wanachama kurejea kwenye mgomo. Mazungumzo kuhusu CBA yalianza mwaka 2017 na makubaliano yalifikiwa mwaka jana. Kaunti zote zilialikwa kutia saini mkataba huo pamoja na makubaliano ya kurejea kazini baada ya mgomo. Hata hivyo, baadhi hazikutia saini. "Tumekuwa tukikabiliwa na uhasama katika kaunti nyingi," alisema Bw Gibore. Maafisa hao waligoma Julai mwaka huu, na kaunti nyingi zikakubali kutia saini makubaliano hayo. Hata hivyo, Nairobi, Vihiga, Kakamega, Turkana na Uasin Gishu bado hazijatia saini. Kwa mujibu wa Bw Gibore, baadhi ya wanachama katika kaunti hizo wameendelea kugoma kwa zaidi ya siku 100. Alilitaka Baraza la Magavana kuhakikisha kaunti zote zinatia saini mikataba hiyo na kuitekeleza. Miongoni mwa masuala yaliyokubaliwa ni kuongezwa kwa marupurupu ya hatari kazini, kupitiwa upya kwa mishahara na kuboreshwa kwa mwongozo wa kupandishwa vyeo. Mwenyekiti wa Kuco, Peterson Wachira, alisema marupurupu ya hatari kazini yalipaswa kuongezwa kwa Sh4,000 kutoka Sh3,000 za sasa. Pia, malipo hayo yalipaswa kuanza kuhesabiwa kuanzia Julai mwaka jana, lakini hakuna utekelezaji uliofanyika. Alisema malimbikizi ya malipo hayo yanaendelea kuongezeka huku maafisa hao wakikosa uhakika wa lini watalipwa. "Tumekuwa tukipewa visingizio na kuzungushwa katika taratibu za kiutawala. Ndiyo maana tumetoa notisi ya madai," alisema Bw Wachira. Aliongeza kuwa maafisa hao hawataki kugoma tena, lakini wanaweza kulazimika kufanya hivyo kwa kuwa serikali haionekani kusikiliza malalamishi yao. Muungano huo pia unalaumu Baraza la Magavana kwa kutowasilisha kwa kaunti zote maelezo yanayohitajika kutekeleza CBA, hasa kuhusu marupurupu yaliyoongezwa. Barua iliyotumwa kwa idara ya mishahara ya Tume ya Utumishi wa Umma ilitaja kaunti 17 pekee zilizokuwa zimetii makubaliano wakati huo. Bw Gibore alisema hatua hiyo inawaacha maafisa wengine nyuma, ilhali muda wa utekelezaji wa CBA ni miaka minne na tayari muda mwingi umepita. Pia, muungano huo unasema kaunti nyingi hazijatekeleza mapitio ya mishahara yaliyofanywa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) tangu 2019. Kwa mujibu wa Bw Gibore, ni kaunti chache zilizotekeleza mapitio hayo katika awamu mbili, ilhali sasa yanaingia awamu ya tano. Aidha, maafisa hao wanalalamikia kutopandishwa vyeo kwa mujibu wa mwongozo mpya. Afisa wa utabibu anayeanza kazi anapaswa kuajiriwa katika daraja la J, lakini wengi wanawekwa daraja la H, ambalo halipo katika muundo rasmi wa utumishi. Kuco pia imesema baadhi ya kaunti hazijatoa barua za ajira kwa wafanyakazi wa afya wa mpango wa huduma ya afya kwa wote na wale waliofanya kazi chini ya Global Fund, licha ya fedha kutolewa kwa ajili yao. Muungano huo umeunga mkono wafanyakazi wa KNH wanaogoma kupinga kucheleweshwa kwa mishahara na kutowasilishwa kwa makato ya wafanyakazi kwa taasisi husika. Viongozi hao wamesema wako tayari kutafuta suluhu kwa mazungumzo, lakini wakatahadharisha kuwa amani kazini haiwezi kupatikana ikiwa makubaliano yanapuuzwa na ahadi hazitekelezwi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 21 hours ago
Nina maradhi ya zinaa lakini sielewi nimeyaokota wapi na nimuelezeje mume wangu!
NILIPOENDA hospitalini kwa uchunguzi wa kawaida, niligundua nina ugonjwa wa zinaa. Daktari aliniambia kuna matibabu na kwamba mwenzangu anapaswa pia kuchunguzwa. Nimekuwa nikilia kwa siri kwa sababu sijui ugonjwa huo ulianzia wapi. Mume wangu anaweza kunishutumu kuwa nimekuwa na uhusiano mwingine, ingawa mimi mwenyewe sijui hali yake ya kiafya. Tuna mtoto mdogo na sitaki jambo hili ligeuke kuwa vita nyumbani. Nifanyeje? Pole kwa wasiwasi unaopitia. Ugonjwa wa zinaa unaweza kuleta hofu, lakini matokeo ya kipimo pekee hayawezi kila mara kuonyesha lini au kutoka kwa nani maambukizi yalipatikana. Fuata matibabu uliyopewa na muulize mtaalamu wa afya jinsi mwenzako anavyoweza kupimwa na kutibiwa. Ni muhimu kuzungumza naye kwa uwazi kuhusu afya yenu, lakini ikiwa unaogopa kwamba anaweza kukudhuru, tafuta ushauri wa mhudumu wa afya kuhusu namna salama ya kumjulisha. Epuka kujitibu au kuacha dawa bila maelekezo. Shemeji huchukua nguo zangu bila idhini SHANGAZI, shemeji yangu huja nyumbani na kuchukua nguo zangu bila kuniomba ruhusa. Nikimkabili, hunisema nina roho mbaya na sitaki kushirikiana na familia. Nimeanza kufungia nguo zangu chumbani. Je, nimekosea? Hujakosea kutaka kuheshimiwa. Kushirikiana si kuruhusu kila mtu kuvuka mipaka yako. Mwambie kwa utulivu kuwa anapaswa kukuomba kabla ya kutumia mali yako. Weka mipaka bila matusi wala ugomvi. Mke alijifungua na sasa mambo ya chumbani hana hamu nayo tena, tutasaidiana vipi? SHANGAZI, tangu mke wangu ajifungue miezi minane iliyopita, hana hamu ya tendo la ndoa. Nikimkaribia husema amechoka. Nimeanza kuhisi hanipendi tena. Je, hali hii ni ya kawaida? Baada ya kujifungua, mabadiliko ya homoni, uchovu, kunyonyesha na changamoto za kihisia yanaweza kuathiri hamu ya tendo la ndoa. Mpe muda na umsaidie katika malezi. Zungumzeni bila kumshinikiza na mhimize kupata ushauri wa daktari ikiwa hali inamsumbua. Ninaishi na mtu anayenikosoa kila siku, amefanya maisha yawe magumu na bado sina uwezo wa kujisimamia, nitasaidika? NINAISHI na binamu yangu kwa sababu ya kazi mjini. Kila ninaponunua kitu, kuvaa vizuri au kutoka na marafiki, hunikosoa. Hata mshahara wangu huulizia. Sina uwezo wa kupanga nyumba yangu kwa sasa. Nitawezaje kuvumilia? Kusaidiwa kuishi mahali fulani hakumaanishi kupoteza uhuru wako. Epuka kumweleza kila jambo kuhusu maisha yako na weka mipaka kwa heshima. Anza kuweka akiba kidogo kidogo ili uweze kujitegemea. Amani yako pia ni muhimu.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 22 hours ago
MASHAIRI: Charlene Arusi Ilifana
La leo hili natunga, Charlene kumpongezaKwa yake ndoa kufunga, pasipo cha kutatizaKama mola livopanga, ahadi wakatimizaMwanako Ruto arusi, kule Mwanza ilifana Mwanako Ruto arusi, ilifana kwelikweliBintiyo yani rais, kafunga yake halaliMungu bila wasiwasi, liwabariki JalaliMwanako Ruto arusi, kule Mwanza ilifana Babake pia mamake, mlikuwa kando yakeKumzawadi manake, yeye na kipenzi chake Naye kweli mama yake, ni mfano bora kwakeMwanako Ruto arusi, kule Mwanza ilifana Wachache lohudhuria, sana walifurahiaMavazi ya kuvutia, wote waliyavaliaViusasa lionea, yote liyoendeleaMwanako Ruto arusi, kule Mwanza ilifana La maua lako koti, nalo chonjo kakuweka Nzuri nzuri yako suti, mfalme kaonekaRachel naye kwa hakika, malkia lipendekaMwanako Ruto arusi, kule Mwanza ilifana Ingawaje sikuweza, kufika niliwaonaKaramu ilipendeza, mkafurahia sanaHata densi mlicheza, na Sudi nilimuonaMwanako Ruto arusi, kule Mwanza ilifana Mwanzo wao kule Mwanza, ninaomba mshairiMaisha wanapoanza, ya ndoa wawe tayari Beti hizi nawatunza, kuwatakia la heriMwanako Ruto arusi, kule Mwanza ilifana JADIEL MWENDA"MACHO KUBWA MUONA MBALI"MAUA, MERU Sijaumbiwa mbwembwe Ningaling'aa gizani, palipo mwanga hafifu,Wengineo watamani, kufikia yangu kifu,Jambo moja asilani, nalipinga maradufu,Majigambo na shauo, sijaumbiwa Mirumbe.Ningaandika vitabu, nivijaze kwenye safu,Mashairi niratibu, na riwaya timilifu, Sikubali majaribu, kwangu mja nijisifu,Majigambo na shauo, sijaumbiwa Mirumbe.Ningazichangia mada, kwa magazeti tukufu,Nichangie ya ziada, makala mengi lufufu,Hino kwangu kawaida, Rabana kaniakifu, Majigambo na shauo, sijaumbiwa Mirumbe.Ningalishika hatamu, hatamu kikamilifu,Kujinadi kwa kaumu, siyo wangu udhaifu,Mbele yote majukumu, nisiwaze kujisifu,Majigambo na shauo, sijaumbiwa Mirumbe.Ningamiliki magari, ya kupofua vipofu,Unigande utajiri, waniheshimu turufu,Kwa Rabana n'nakiri, nitadumisha insafu,Majigambo na shauo, sijaumbiwa Mirumbe.Ningalifikia mwisho, wa shairi bila hofu,Wino ubaki apisho, niloupa wadilifu,Na udumu hadi kesho, sini siwezi jisifu,Majigambo na shauo, sijaumbiwa Mirumbe. MIRUMBE P. NICKSON'USTADHI BABU KIJANA'SHULE YA UPILI YA EMMANUEL Magazeti tusomeni Magazeti naguzia, ninakwea kwa kilili,Magazeti chombo murua, hili jambo najadili,Magazeti mefidia, lipovuka dijitali,Magazeti tusomeni, mubadala wa runinga,Magazeti huchapisha, makala yanovutia,Magazeti yatupasha, matukio tunajua,Magazeti chombo tosha, kurasa kizipitia,Magazeti tusomeni, mubadala wa runinga,Magazeti burudani, mitima hutuliwaza,Magazeti kote nchini, kila siku wasambaza,Magazeti bei chini, mifuko kutoumia,Magazeti tusomeni, mubadala wa runinga,Magazeti kwayo kina, habari tunapatani,Magazeti tena sana, yanafika mashinani,Magazeti hata wana, wanayasoma shuleni,Magazeti tusomeni, mubadala wa runinga,Magazeti tayapata, kila siku kwa maduka,Magazeti kwa kompyuta, utasoma kwayo bwaka,Magazeti utakuta, lugha zote waandika,Magazeti tusomeni, mubadala wa runinga,Magazeti kusomeka, hatuhitaji sitima,Magazeti kwa hakika, hayana kubwa gharama,Magazeti kuyandika, yanachangia kusoma,Magazeti tusomeni, mubadala wa runinga,Magazeti ninakoma, mutazamo uwe chanya,Magazeti tukisoma, mambo mengi tutamanya, Magazeti kwayo umma, twayatamani kupenya,Magazeti tusomeni, mubadala wa runinga, FRANKLIN MUKEMBU'MAWIMBI YA NCHI KAVU'KAJUKI, NITHI Picha yangu Picha yangu kitazama, utaona mengi ndaniSi rahisi kuisoma, ina siri ya moyoniTabasamu lisohama, limebeba shukuraniNi hadithi ya maisha, iloandikwa moyoniMacho yana nyingi ndoto, zatafuta muangazaNdoto kubwa shinda moto, uchomao kushangazaSio ndoto za kitoto, ndio yangu kiolezaNi hadithi ya maisha, iloandikwa moyoni Picha yangu mjarari, wa maisha usukaniYasukuma yangu ari, kubadili ya usoniNi kivuli cha safari, iloanza kule chini Ni hadithi ya maisha, iloandikwa moyoni Siitupi yangu picha, naiweka ukutaniSitowahi kuificha, naiweka hadharaniUshuhuda wa galacha, usomwe mtandaoniNi hadithi ya maisha, iloandikwa moyoniBado nina ilhamu, kusema mangi ya pichaIla imeganda damu, tamatini kuwaachaNdilo jambo la muhimu, muelewe hii pichaNi hadithi ya maisha, iloandikwa moyoni SYLVIA SISANYA 'WARIDI LA MCHONGOMA'PHARO SCHOOL NAIROBI Mche mwema Mti mwema mche wake, tayari nimeupata,Msimu sihadaike, nahofu nisijejuta,Shamba heri lilimike, gugu sumu sijeota,Mche huu wa thamani, kiunga chanitatiza!Kiunga chanitatiza, magugu apanda nani?Nataka pawe pakuza, matunda yenye amani,Jua kali lachomoza, wapita kando ndaluni,Wapate penye amani, tulizo ya nyoyo zao.Tulizo ya nyoyo zao, mchana ulio hari,Wengine bila makao, watuame hali shwari, Mti uwe ni kigao, kinga yao wasafiri, Changia yao furaha, mti wangu wa amani.Mti wangu wa amani, bayana nauvumbua, Ulionenwa kwa uneni, fahari nimetambua,Wa konde uwe kondeni, macho nimeyafumbua,Limbuko nitalimbua, mche wa matumaini. JUMA OKAL,'MALENGA USTADH'NAIROBI Jugwe Mcheza jugwe hachoki, kwa nguvu kamba avuta,Kwake jugwe sio chuki, 'ngawa lina iga vita,Vuta vuta nikuvute, ndo' utamu wa mchezo.Abadan hatetereki, sana ameshika kamba,Zinamsakama dhiki, vitanga tele sagamba,Vuta vuta nikuvute, ndo' utamu wa mchezo.Jasho halikadiriki, si kidogo amelowa,Anatafuta riziki, apate sima kwa chewa,Vuta vuta nikuvute, ndo' utamu wa mchezo.Haichoki halaiki, sana 'nawashangilia,Ili wasiweke breki, au kamba kwachilia,Vuta vuta nikuvute, ndo' utamu wa mchezo.Wanavuta kwa hamaki, ghafla kamba 'nakatika,Matope yanawasaki, matopeni waanguka,Vuta vuta nikuvute, ndo' utamu wa mchezo.Papo hapo hawatoki, wanangoja yao tuzo,Mfawidhi kwa mikiki, waanze upya mchezo,Vuta vuta nikuvute, ndo' utamu wa mchezo. AUSTINE O. ONYANGO'MALENGA WA MTO NILE'CHUO KIKUU CHA JARAMOGI (JOOUST) Kosawo Shule yetu yapendeza, mandhari yanavutia,Talanta tunazikuza, nazo randa kupigia,Hivi leo naeleza, natunga kuwasifia,Kosawo yetu daima, siku zote tuko mbele,,Michezoni tunavuma, handiboli inatesa,Timu zote twazilima, uwanjani kijitosa,Wachezaji hujituma, kwazo mbinu za kisasa,Kosawo yetu daima, siku zote tuko mbele,Mkuu wa shule hongera, Amilo kutuongoza,Hakika hatuja tara, na mbele kutusogeza,Pia wewe ndiye bora, vyema kutuelekeza,Kosawo yetu daima, siku zote tuko mbele,Twakienzi Kiswahili, lugha yetu ashirafu,Vitenzi pia methali, hakika twafua dafu,Twazidisha na akili,maarifa ni sufufu,Kosawo yetu daima, siku zote tuko mbele,Maadili ndiyo dira, yatuongoza kufika,Tunazidisha ubora, bila yoyote mashaka,Hulka hazija charara, ni chanda chema hakika,Kosawo yetu daima, siku zote tuko mbele,Wanagenzi ni bashasha, Taifa Leo Makala,Gazeti lawashibisha, li lazima kama sala,Sokomoko ikibisha, mithili ya zilizala,Kosawo yetu daima, siku zote tuko mbele, MUSTAPHA MADETEKISUMU Pendo hubakishani? Wa usiku ja manane, usingizi waugura,Moyo kusomba mengine, tabia za kuchakura,Fichua yalo manene, ndwele mlimo hasara,Chupa ishara mafuta, je pendo hubakishani?Nataka nijue haki, i wapi pa kufidia, Wa kupenda bila chuki, dau hakudhamiria, Kwa bima wala bunduki, pendo kinga kufanyia,Chupa ishara mafuta, je pendo hubakishani?Maimamu ibadani, waadhini kuswalia,Wachungaji Kanisani, ndoa pendo apishia, Watunzi mle hewani, malenga wa kughania,Chupa ishara mafuta, je pendo hubakishani?Hapa naweka komeo, uso wengi kubania,Niende tua machweo, jibu mkitafutia,Nyinyi ndinyi tegemeo, baruwa kunifikia,Chupa ishara mafuta, je pendo hubakishani?Nalingoja hilo jibu, mizani sio pungufu,Wachungaji kwa vitabu, Imamu wa misahafu,Pangeni bila ya tabu, vina mimi nitasifu,Chupa ishara mafuta, je pendo hubakishani? JUMA OKAL, 'MALENGA USTADH' NAIROBI Dhahabu Uliingia moyoni, furaha ukanijaza, Ikawa ni tumaini, lilojaa miujiza, Ulinijaza imani, na upendo kunangaza, Wewe dhahabu ya kweli, ung'ae moyoni mwangu. Urembo wako wa kweli, kama wake jua mwanga, Hujajaa ufedheli, kazi yako ni kujenga, Kwangu wewe ni aali, kama njugu karanga, Wewe dhahabu ya kweli, ung'ae moyoni mwangu. Wa kwako uchangamfu, hunijaza tabasamu, Wewe ni binti faafu, na tena mja adhimu, Nitazidi kukusifu, kwangu wewe ni alimu, Wewe dhahabu ya kweli, ung'ae moyoni mwangu. Wewe ni mwenye kujali, Olgah wangu mpenzi, Sifa zako bulibuli, wangu wa huba mlinzi, Upendo wako asali, huba mfanowe kanzi, Wewe dhahabu ya kweli, ung'ae moyoni mwangu. Wako uwepo lazizi, kwangu ni wenye amana, Najihisi sijiwezi, habibu furaha sina, Nalimisi lako pozi, ewe liye wangu nana, Wewe dhahabu ya kweli, ung'ae moyoni mwangu. Wenye kupendwa wako, ila sio wa kudumu, Popote wewe uliko, kwangu una umuhimu, Olgah nakupa heko, kama wewe ni adimu, Wewe dhahabu ya kweli, ung'ae moyoni mwangu. Kulinde Mungu Jalia, na kukupa afya nzuri, Upendo wako famia, ni upendo wenye heri, Uzidi kulitunzia, penzi letu kwa hiari, Wewe dhahabu ya kweli, ung'ae moyoni mwangu. Yako iliyo thamani, nitaitunza daima, Sitaiacha asilani, taniongoza Karima, Itanijaa amani, ya penzi letu hatima, Wewe dhahabu ya kweli, ung'ae moyoni mwangu. MALENGA OKWETSO,SHULE YA UPILI YA SAWAGONGO
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 23 hours ago
Kilichofanya Mackenzie kupatikana na hatia ya kutesa watoto
WAJIBU wa wazazi katika kuwalinda watoto ulikuwa kiini cha hukumu iliyotolewa Jumanne na Mahakama ya Watoto Mombasa dhidi ya mhubiri mtatanishi Paul Mackenzie na wafuasi wake kuhusu ukatili dhidi ya watoto katika msitu wa Shakahola kati ya 2020 na 2023. Hakimu Mkuu Nelly Chepchirchir alisema ushawishi wa Mackenzie kwa wafuasi wake haukumfanya moja kwa moja kuwajibika kwa kila ukiukaji wa haki za watoto, akisisitiza kuwa kila mshtakiwa alipaswa kuhusishwa na kosa mahususi. "Ushahidi dhidi ya kila mshtakiwa ulizingatiwa kivyake. Ukubwa wa matukio au umaarufu wake hauwezi kuchukua nafasi ya kuthibitisha hatia," alisema hakimu. Mahakama ilisema wazazi waliowapeleka watoto wao msituni walikuwa na wajibu wa kuwalinda, huku upande wa mashtaka ukishindwa kuthibitisha kuwa Mackenzie alikuwa na wajibu wa moja kwa moja wa malezi ya watoto hao. Hata hivyo, hakimu alikataa hoja za utetezi kwamba vitendo vilivyofanyika vilichochewa na imani za kidini au vilikuwa njia ya kuwaadhibu watoto. Alisema uhuru wa kuabudu hauwezi kutumiwa kuhalalisha vitendo vinavyodhuru watoto. Mackenzie alipatikana na hatia ya kushambulia kulikosababisha madhara ya mwili na makosa matano ya kuwafanyia watoto ukatili. Washtakiwa wengine kadhaa walipatikana na hatia ya ukatili na kuwanyima watoto haki ya elimu. Washitakiwa wengine 24 waliachiliwa huru baada ya mahakama kubaini kuwa mashtaka hayakuthibitisha wajibu wao binafsi. Mackenzie na washitakiwa wenzake wanatarajiwa pia kusikiliza hukumu katika kesi ya itikadi kali katika Mahakama ya Shanzu Alhamisi, Novemba 26.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 23 hours ago
Vyama 94 vya kisiasa hatarini kukosa kushiriki uchaguzi wa 2027
Vyama 94 vya kisiasa nchini vimepewa hadi Desemba 7, 2026 kurekebisha kanuni zao za uteuzi wa wagombeaji, la sivyo vikose kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema ni vyama 11 pekee vilivyotimiza masharti ya kisheria kuhusu kanuni za uteuzi, huku vingine 94 vikihitajika kufanya marekebisho. Miongoni mwa vyama vikuu vilivyotakiwa kurekebisha kanuni hizo ni United Democratic Alliance (UDA) ya Rais William Ruto, Orange Democratic Movement (ODM), Democracy for the Citizens Party (DCP) ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Linda Mwananchi Movement, iliyokuwa ikijulikana kama The Equitable Party. Hata hivyo, Wiper Patriotic Front ya Kalonzo Musyoka, Jubilee Party na The Mwananchi Party ya Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ni miongoni mwa vyama 11 vilivyotimiza masharti. Vyama vingine vilivyofaulu ni Kenya Moja Movement, Safina, Liberal Democratic Party, Grand Dream Development, Democratic National Alliance, Chama ya Mapatano of Kenya, Vision for Development Alliance na Forward Kenya. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alisema tume ilikagua kanuni zilizowasilishwa na vyama ili kuhakikisha zinafuata Katiba, Sheria ya Uchaguzi na kanuni husika. Alisema tathmini hiyo ilichunguza muundo na mamlaka ya kamati za uchaguzi za vyama, taratibu za kutambua na kuteua wagombeaji, masharti ya wanaotaka kuwania nafasi za uongozi na jinsi kura za mchujo zinavyopaswa kuendeshwa. Pia, tume ilikagua jinsi vyama vinavyoshughulikia malalamishi ya ndani, ukiukaji wa kanuni za uchaguzi na masuala yanayohusu maadili ya uchaguzi. Bw Ethekon alisema vyama vilivyopatikana na kasoro vimearifiwa maeneo yanayohitaji kurekebishwa na vinapaswa kuwasilisha kanuni mpya kabla ya tarehe ya mwisho. Hata hivyo, alifafanua kuwa kutotimiza masharti katika tathmini ya kwanza hakumaanishi moja kwa moja kuwa chama kimeondolewa kwenye uchaguzi wa 2027. Alisema hatua hiyo inalenga kuvipatia vyama nafasi ya kurekebisha dosari huku tume ikihakikisha uteuzi unafanyika kwa uwazi, haki na kufuata sheria. IEBC ilitangaza ratiba muhimu za uchaguzi Agosti 25. Vyama vilitakiwa kuwasilisha majina ya maafisa walioidhinishwa na sampuli za sahihi zao kufikia Oktoba 15, huku kanuni za uteuzi zikitarajiwa kuthibitishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa kufikia Oktoba 30 na kuwasilishwa kwa tume kufikia Novemba 6. Vyama pia vinapaswa kuwasilisha orodha za wanachama na majina ya wagombeaji wa kura za mchujo kufikia Machi 16, 2027, pamoja na tarehe na maeneo ya uchaguzi huo. Kura zote za mchujo zinapaswa kukamilika na mizozo ya ndani kutatuliwa kufikia Mei 8, 2027. Uteuzi wa wagombeaji unatarajiwa kuwa mtihani mkubwa kwa vyama vikuu kutokana na ushindani wa kisiasa na maslahi yanayokinzana ndani yake. ODM, chini ya Oburu Oginga, inakabiliwa na changamoto ya kudumisha ushawishi wake Nyanza katika kipindi cha baada ya kifo cha Raila Odinga. Wanasiasa wenye uzoefu wanawania nafasi mbalimbali huku baadhi wakipinga mapendekezo ya chama kugawana maeneo ya kisiasa kwa misingi ya kanda. Chama hicho pia kinakabiliwa na ushindani kutoka kwa vyama vingine, vikiwemo Movement for Democracy and Growth na Peoples' Prosperity Party ya aliyekuwa Waziri Eliud Owalo. Kwa upande wake, Bw Gachagua anajaribu kuimarisha DCP katika eneo la Mlima Kenya, ambako wanasiasa waliokuwa wameegemea UDA wanazidi kuelekea makazi yake ya kisiasa Wamunyoro kutafuta ushirikiano mpya. Hivyo, mbali na kurekebisha kanuni, vyama hivyo vinakabiliwa na jukumu la kuhakikisha kura zao za mchujo hazitazua migawanyiko inayoweza kudhoofisha nafasi zao katika uchaguzi ujao
read moreRight Column Content