T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 21 Sep 2026 03:55:17

Viongozi wa DCP wawaka kuhusu kutawazwa kwa Kindiki Mlimani

VIONGOZI wa DCP wamepinga kutawazwa kwa Naibu Rais Prof Kithure Kindiki kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya, wakisisitiza kuwa uongozi wa kisiasa huamuliwa na wananchi wala si wazee. Wakiongozwa na Seneta wa Nyandarua, John Methu, viongozi hao walifika Embu na kusema Kiongozi wa DCP, Rigathi Gachagua, ndiye anayetambuliwa na wananchi wa eneo hilo kama kinara wao. "Ni wakazi wa eneo hili wanaoamua nani awe kinara wao, wala si wazee. "Kindiki anapaswa kuacha kufikiria kuwa yeye ndiye kinara wetu," akasema Bw Methu akiwa Kianjokoma, Manyatta. Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji alidai kuwa Sh60 bilioni zinatumika kugawanya Mlima Kenya kisiasa ili kura za eneo hilo zisiende 'kapu' moja kuelekea uchaguzi wa 2027.  "Hatutaruhusu hili lifanyike. Eneo letu litaendelea kuwa kitu kimoja, iwe serikali ya Kenya Kwanza inapenda au la," akasema Bw Mukunji. Kauli zao zilijiri baada ya wazee kutoka jamii za Kikuyu, Embu, Mbeere na Meru kumuidhinisha Prof Kindiki kuwa msemaji wa eneo hilo katika hafla iliyofanyika Kirigiti, Kiambu mnamo Jumamosi. Wazee hao walimkabidhi Prof Kindiki mamlaka ya kuwakilisha maslahi ya jamii zote za Mlima Kenya na wakasisitiza umuhimu wa umoja wa eneo hilo. Prof Kindiki aliwashukuru kwa kumuamini na kuahidi kutumikia jamii zote bila ubaguzi, huku akisema hataruhusu tofauti za kisiasa kugawanya eneo hilo. Viongozi wa DCP pia walikosoa serikali kuhusu kuuawa kwa vijana wawili katika uwanja wa Nembure, Embu, wakati wa mkutano wa kisiasa uliohudhuriwa na Prof Kindiki na Gavana Cecily Mbarire.  Bw Methu alitaka waliohusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Shahbal njiapanda kuhusu ugavana, akumbushwa 'ana dili nyingi za kibiashara na serikali'

MWEKEZAJI na mwanasiasa Suleiman Shahbal anakabiliwa na changamoto ya kutenganisha mikataba yake ya mabilioni ya pesa katika miradi ya serikali na azma yake ya ugavana Mombasa, huku shinikizo ikizidi kwake ajiondoe kwenye kinyang'anyiro cha 2027. Shinikizo hizo zimezidi kujitokeza wiki chache baada ya kutia saini mkataba wa kuanzisha Eneo Maalum la Kiuchumi (SEZ) jijini Mombasa na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji bandarini ya DP World katika Ikulu ya Nairobi. Rais William Ruto awali alikuwa amemshauri Bw Shahbal kuachana na siasa, lakini mfanyabiashara huyo akakataa. Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Omar Hassan, ambaye pia analenga kumng'oa Gavana Abdulswamad Nassir kitini, sasa amesema kuna hatari ya kutokea mgongano wa maslahi iwapo Bw Shahbal atakuwa gavana wa Mombasa huku akiendelea kuwa mshirika mkubwa katika sekta ya biashara ya kaunti hiyo. Mkataba huo wa Sh12 bilioni kati ya kampuni yake ya GulfCap Group na DP World unalenga kujenga Eneo Maalum la Kiuchumi (SEZ) lenye ukubwa wa ekari 535 Jomvu. Ardhi hiyo inamilikiwa na Serikali ya Kaunti ya Mombasa na hapo awali ilikodishwa kwa shirika la Kenya Meat Commission. Mbali na mradi wa SEZ, GulfCap pia inahusika katika ujenzi wa mradi wa nyumba za bei nafuu kwa ushirikiano na serikali ya kaunti mtaani Buxton. Mradi huo wa Sh6 bilioni ulianzishwa wakati wa utawala wa zamani wa kaunti chini ya gavana wa zamani Hassan Joho, ambaye sasa ni Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, baada ya kubomolewa kwa nyumba za zamani za kaunti. Vilevile, GulfCap ina mradi mwingine kama huo jijini Nairobi. "Ukiwa mfanyabiashara, shikilia biashara na uwaachie wasimamizi wa serikali jukumu la kuweka mifumo na taratibu zinazostahili, kwa sababu una mgongano wa maslahi," Bw Omar alisema. Huku akijipigia debe, Bw Omar alitaja uzoefu wake kama mwanaharakati wa haki za binadamu, seneta wa zamani wa Mombasa na Katibu Mkuu wa UDA kama sehemu ya sifa zake katika kinyang'anyiro cha ugavana. Alisema azma yake ya kisiasa imechochewa na hitaji la kuboresha utawala na kurejesha heshima, hadhi na uzingatiaji wa Katiba Mombasa. Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, pia alimkosoa Bw Shahbal kwa kumpinga Gavana Nassir katika uchaguzi wa 2027, licha ya serikali ya kaunti kumuunga mkono katika mpango wake wa kuendeleza SEZ. "Wale wanaomiliki SEZ wameanza kumpiga vita gavana hata kabla mradi haujaanza. Lakini leo tunawaambia kwamba gavana ataweka siasa kando. Huu sasa ni wakati wa maendeleo. Mtu mnayempiga vita ndiye huyo huyo atakayewanyooshea mkono na kuunga mkono mradi ili maendeleo yaje na watu wapate ajira," alisema. Wakati wa kusainiwa kwa mkataba wa SEZ Septemba 8, Rais Ruto alisema Kenya inahitaji wawekezaji wakubwa, wawekezaji na wajasiriamali makini wenye uwezo wa kutekeleza miradi itakayochangia ukuaji wa uchumi. Hata hivyo, Bw Shahbal alikataa wito wa kuachana na siasa na ameendelea kusisitiza kuwa atawania kiti cha ugavana wa Mombasa mwaka 2027. Hivi majuzi, mbunge huyo wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) alieleza wasiwasi kwamba siasa za ugavana zinaweza kuathiri mradi wake na kuwataka wapinzani wake kuweka tofauti zao kando ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa. Bw Shahbal, ambaye ametangaza kuwa hatatafuta tiketi ya ODM kugombea mwaka wa 2027, alimuonya Rais Ruto dhidi ya mipango ya kisiasa ya kugawana maeneo kati ya ODM na UDA, almaarufu kama 'zoning'. "Upuuzi huu wote wa kugawana maeneo umeandaliwa na watu wanaoogopa kuenda mashinani kukutana na watu. Ikiwa una imani na uongozi wako, nenda kwa wananchi uwaambie ulichofanya nao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

Vyeti feki vyanoga miongoni mwa wanaoajiriwa serikalini

WAKENYA wanaotumia vyeti ghushi vya masomo kupata ajira, vyeo na mishahara mikubwa sasa wanaandamwa huku hukumu za hivi majuzi zikifichua jinsi barua hizo zimekuwa zikitumiwa kuingia na kupanda ngazi katika utumishi wa umma. Mnamo Jumatatu, mahakama moja jijini Nairobi ilimpiga faini ya Sh80,000 aliyekuwa afisa msaidizi wa uchaguzi katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), George Kipyatich Kibor, baada ya kupatikana na hatia ya kuwasilisha cheti ghushi cha shahada. Bw Kibor aliwasilisha cheti ghushi cha Shahada ya Usimamizi wa Biashara (Fedha na Benki) alichodai kilitolewa na Chuo Kikuu cha Moi. Hukumu yake ilitolewa siku chache baada ya aliyekuwa afisa wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme nchini (KenGen), David Mogire Nyabuti, kuhukumiwa kifungo cha miaka 11 kwa kutumia barua ghushi za masomo kupata ajira na kujipatia karibu Sh15 milioni. Bw Nyabuti alitumia cheti ghushi cha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne(KCSE) na hati ya matokeo kupata nafasi ya kujiunga na Chuo cha Mafunzo cha Kampuni ya Umeme Nchini (KPC) kabla ya kupata ajira KenGen. Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilibaini kuwa aliwasilisha barua hizo kama vyeti halali vilivyotolewa na Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC). Kati ya Agosti 2003 na Septemba 2018, alipokea Sh14.94 milioni kama mishahara na marupurupu kutokana na udanganyifu huo. Mahakama ilimpata na hatia ya kujipatia mali ya umma kwa njia ya udanganyifu na kumuamuru kurejesha fedha hizo au kutumikia kifungo cha miaka mitano. Pia alipigwa faini ya Sh900,000, huku akikabiliwa na kifungo cha miaka miwili iwapo angeshindwa kulipa. Kesi hizo ni sehemu ya tatizo kubwa la vyeti ghushi katika taasisi za umma. EACC inasema imefikisha mahakamani kesi 90 zinazohusu vyeti ghushi vya masomo. Kati ya hizo, 43 zimeishia wahusika kuhukumiwa, 39 bado zinasubiri kuamuliwa, washukiwa saba waliachiliwa huru na kesi moja iliondolewa. Katika mwaka wa kifedha wa 2025/26 pekee, EACC ilirejesha Sh18.5 milioni zilizolipwa kwa njia ya udanganyifu kwa maafisa wa umma kupitia mishahara iliyotokana na vyeti ghushi na ajira mbili. Miongoni mwa waliopatikana na hatia ni Martin Maigua Maina, aliyedanganya kwa kutumia cheti cha Shahada ya Sanaa katika Sayansi ya Siasa ili kupata cheo IEBC. Jecinter Hezron Adoyo alishtakiwa kwa kughushi barua za masomo kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi ili kupata ajira katika Tume ya Ugavi wa Mapato kama mdadisi mkuu na msaidizi wa kibinafsi wa mwenyekiti. Katika Kampuni ya Maji ya Nairobi, Stacy Mwikali alitumia cheti ghushi cha Shahada ya Teknolojia ya Habari alichodai kimetolewa na Chuo Kikuu cha JKUAT kupata cheo cha kaimu meneja kampuni hiyo. Aliyekuwa mfanyakazi wa Kaunti ya Nairobi Gabriel Bukachi Chapia alihukumiwa mwaka jana kifungo cha miaka miwili na nusu, huku akipewa chaguo la kulipa faini ya Sh150,000, baada ya kukiri kughushi vyeti vya masomo. Pia aliamriwa kurejesha Sh3.9 milioni alizopata alipokuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 21 Sep 2026 07:55:25

Kituo kikuu cha kujumuisha kura chazidi kuleta utata kuelekea uchaguzi 2027

ZIKIWA zimesalia miezi 11 kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027, vita vya kisheria kuhusu kuwepo kwa Kituo cha Kitaifa cha Kuhesabu Kura za Urais (NTC) vimeanza kushika kasi, huku macho yakielekezwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Mahakama Kuu inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu uhalali wa kikatiba wa NTC Septemba 22, 2026, kufuatia kesi zilizowasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah pamoja na viongozi wa upinzani wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa DCP Rigathi Gachagua. Walalamishi wanataka mahakama itangaze kuwa kuanzishwa na kuendesha NTC kwa ajili ya kuthibitisha tena matokeo ya urais ni kinyume cha Katiba, na hivyo kubatilishwe. Wanadai kuwa katiba inaweka eneobunge kuwa kituo cha msingi na cha mwisho cha kuhesabu, kuthibitisha na kutangaza matokeo ya urais. Wanaopinga NTC pia wanataka IEBC izuiwe kuhesabu tena au kubadilisha matokeo yaliyotangazwa na maafisa wasimamizi wa uchaguzi wa maeneobunge. Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga ameunga mkono wito wa kuondolewa kwa NTC. "Katiba haitoi nafasi kwa kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura. Jukumu la IEBC ni kutangaza matokeo, wala si kuhesabu kura tena," akasema Maraga. Hata hivyo, msimamo huo unatofautiana na uamuzi wa Mahakama ya Juu katika kesi ya uchaguzi wa urais wa 2017. Mahakama hiyo ilisema IEBC ina jukumu la kujumuisha na kuthibitisha kura kabla ya kutangaza mshindi, huku mchakato huo ukiendelea kutoka kituo cha kupigia kura hadi eneobunge na hatimaye NTC. Katika kesi ya 2022, Mahakama ya Juu ilifafanua kuwa jukumu la kuhesabu na kuthibitisha matokeo katika NTC ni la IEBC kama taasisi, huku mamlaka ya kutangaza mshindi yakiwa ya mwenyekiti wa tume. Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na aliyekuwa rais wa Chama cha Mawakili (LSK) Nelson Havi pia wameunga mkono kuondolewa kwa NTC, wakisema matokeo yaliyohesabiwa na kutangazwa katika maeneobunge 290 yanapaswa kuwa ya mwisho. Kwa upande mwingine, aliyekuwa kamishIna wa IEBC Paul Kurgat anasema Katiba haijaweka jengo maalumu kuwa kituo cha kuhesabia kura, bali inasimamia mchakato. Anasema Kanuni za Uchaguzi zinahitaji kuhesabiwa kwa kura kikamilike katika kituo kilichotangazwa rasmi na IEBC. Mzozo huo sasa unahusu zaidi ya eneo la Bomas, kwani kesi hizo zinahoji iwapo IEBC ina mamlaka ya kikatiba na kisheria kuthibitisha matokeo ya urais katika ngazi ya kitaifa baada ya kutangazwa katika maeneo bunge. Kwa kuzingatia uwezekano wa suala hilo kufikishwa Mahakama ya Juu, uamuzi wa Mahakama Kuu unaweza kuwa hatua ya kwanza katika vita virefu vya kisheria kuhusu mfumo wa kuhesabu na kuthibitisha matokeo ya urais kuelekea uchaguzi wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 21 Sep 2026 06:55:28

Ruto kupigia uwekezaji nchini Kenya debe katika kongamano la UNGA

RAIS William Ruto aliondoka Nairobi kuelekea New York, Amerika, Jumamosi usiku ambako anatarajiwa kutumia Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa (UNGA) kutangaza Kenya kama kitovu cha uwekezaji, teknolojia na fedha Afrika. Ziara yake ya siku tano itajikita katika kuvutia uwekezaji katika sekta za kawi, miundomsingi, kilimo, viwanda, afya, teknolojia na Akili-Unde (AI). Mradi unaotarajiwa kupewa uzito ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Sh2.2 trilioni ($17 bilioni) mjini Lamu. Serikali inasema kiwanda hicho chenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku kinaweza kuunda zaidi ya nafasi 60,000 za ajira na kusababisha Kenya na mataifa ya karibu kujitosheleza kwa kawi. Kulingana na Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed, Rais Ruto atashirikiana na mfanyabiashara wa Nigeria, Aliko Dangote kuongoza mikutano ya uwekezaji iliyoandaliwa na kampuni za Africa Finance Corporation na Global Africa Business Initiative. Ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kuanza Septemba 30. Katika hotuba yake UNGA, Rais Ruto pia anatarajiwa kutetea mpango wa Afrika kujifadhili, maarufu kama "Africa-financing-Africa", unaolenga kutumia zaidi akiba na mitaji ya Waafrika kufadhili maendeleo ya bara. Rais atatoa wito wa mageuzi na dhamana za kimataifa zitakazowezesha mtaji huu kutumika katika miundomsingi, biashara na vipaumbele vingine vya maendeleo," alisema Bw Mohamed. Rais pia atatangaza Hazina ya Kitaifa ya Miundomsingi inayolenga kukusanya hadi $40 bilioni (Sh5.7 trilioni) kupitia wawekezaji binafsi na taasisi bila kuongeza deni la serikali. Teknolojia na Akiliunde pia zitakuwa sehemu muhimu ya ziara hiyo. Rais Ruto na Rais wa Finland Alexander Stubb wataongoza AI Middle Powers Initiative, inayolenga kuunganisha rasilimali za kompyuta, data na wataalamu ili mataifa yaendeleze uwezo wao wa AI.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 21 Sep 2026 05:55:44

Oparanya apinga Arati, Oburu kuhusu suala la kugawana maeneo na UDA

MJADALA kuhusu mpango wa kugawana maeneo ya kisiasa unaendelea kuibua tofauti ndani ya ODM, huku Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya akipinga pendekezo hilo na kuunga mkono ushindani wa kirafiki kati ya ODM na UDA katika uchaguzi wa 2027. Mpango huo, ambao unalenga vyama washirika kukubaliana kutowasilisha wagombea dhidi ya wenzao katika maeneo fulani, ni miongoni mwa masuala tata katika mazungumzo ya makubaliano ya kabla ya uchaguzi kati ya ODM na UDA. Bw Oparanya, anayesemekana kuwa miongoni mwa wanaoweza kuchaguliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais William Ruto, alisema ODM na UDA zinapaswa kuruhusu ushindani katika maeneo ya uchaguzi badala ya kuyagawana. "Tunataka vyama hivi viwili vikubwa viunde serikali imara mwaka ujao kwa sababu kila kimoja kinapaswa kuwa na nguvu. Tumekubaliana kuhusu kiongozi na tunataka ODM na UDA ziwe na nguvu hapa na kule tushindane kwa urafiki," akasema Bw Oparanya katika uwanja wa Mayuba, Kaunti ya Bungoma mnamo Jumamosi. "Hatutaki ugawaji wa maeneo bali tushindane kwa urafiki kwa sababu sasa tuna baba mmoja. Mshindane huku mkijua kwamba tuna baba mmoja," akaongeza. Msimamo wake unatofautiana na ule wa kiongozi wa ODM, Oburu Oginga, ambaye amekuwa akitaka maeneo yanayochukuliwa kuwa ngome za chama yalindwe katika makubaliano na UDA. "Baadhi ya watu wanasema hatutaki maeneo yatengwe. Ikiwa hamtaki, mnataka nini? Tunataka yatengwe kwa sababu Homa Bay ni eneo letu. Hatutaki UDA Homa Bay," akasema Dkt Oginga. Amependekeza maeneo ambako chama kina magavana, wabunge na madiwani wake yahesabiwe kuwa ngome zake moja kwa moja. Msimamo huo umeungwa mkono na baadhi ya viongozi wa ODM, akiwemo Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga na Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa ODM wamepinga mpango huo wakisema unaweza kuzuia ushindani wa kisiasa na kupunguza nafasi ya wapiga kura kuchagua viongozi wanaowataka.  Mnamo Aprili, wabunge Millie Odhiambo, Jared Okello, Onyango Koyoo, Phelix Jalang'o na Elisha Odhiambo walipinga ugawaji wa maeneo na kutaka uteuzi wa wagombea ufanywe kwa njia huru na ya haki. "Tunaihimiza chama chetu kufanya mchujo wa kuaminika kwa sababu tukifanya hivyo hatutahitaji kuwa na wasiwasi kuhusu ugawaji wa maeneo. ODM bado itashinda viti," akasema Bw Odhiambo. Mjadala huo pia umeenea Magharibi, ambako Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula amepinga mpango wa kuzuia vyama kuwasilisha wagombea katika maeneo fulani. Alisema makubaliano ya serikali pana hayapaswi kutumiwa kuzuia ushindani wa uchaguzi. "Makubaliano ya Serikali Jumuishi hayapaswi kutafsiriwa kuwa makubaliano ya kunyima vyama vya kisiasa nafasi ya kuwasilisha wagombea. Vyama vinapaswa kushindana" akasema Bw Savula. Katika ziara ya Rais Ruto Nyanza, suala hilo pia liliibua hisia tofauti. Mbunge wa Uriri Mark Nyamita alisema viongozi wa ODM wanapaswa kuruhusiwa kushindana katika viti vyao bila kuingiliwa na makubaliano ya vyama. Kwa upande mwingine, Naibu Kiongozi wa ODM Simba Arati alitaka UDA kuachwa nje ya Nyanza, akisema eneo hilo ni ngome ya ODM.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 21 Sep 2026 04:55:28

Kutawazwa kwa Kindiki kwazua mvutano Mlimani

Washirika wa Rais William Ruto wanaonekana kuwa na nafasi muhimu katika juhudi za kumuinua Naibu Rais Kithure Kindiki kuwa msemaji wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya. Hafla ya Jumamosi katika Uwanja wa Kirigiti, Kiambu, ilifichua vita vipya vya kutafuta ushawishi wa kisiasa katika eneo hilo kuelekea uchaguzi wa 2027. Hafla hiyo iliyohudhuriwa na wazee kutoka jamii za Agikuyu, Embu na Meru ilimshuhudia Profesa Kindiki akivishwa mavazi ya kitamaduni na kutangazwa kuwa msemaji wa kisiasa wa Mlima Kenya. Wawakilishi wa mashirika sita ya wazee kutoka Mlima Kenya waliidhinisha uungaji mkono kwa Rais Ruto na Profesa Kindiki, huku wakipinga juhudi za kugawanya Mlima Kenya kisiasa. Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika mjadala kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo, alitetea hafla hiyo. Bw Ruku aliitaja kama tamko rasmi la wazee wa Mlima Kenya kumtambua Profesa Kindiki kuwa msemaji na anayeshikilia mustakabali za kisiasa za eneo hilo. Hafla hiyo pia ilionekana kufunga mjadala wa Bw Ruku wa kugawanya Mlima Kenya Mashariki na Magharibi. Kwa wiki kadhaa, waziri huyo alikuwa akitumia shoka na msumeno kuashiria wazo la kugawanya maeneo hayo kisiasa. Hata hivyo, hafla hiyo ilizua upinzani kutoka kwa baadhi ya wazee na wanasiasa ambao walipinga uhalali wake. Mlezi wa Kiama Kia Ma, Kung'u Muigai, alipinga kutawazwa kwa Profesa Kindiki huku mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu, Wachira Kiago, akisema kundi lake halikushiriki hafla hiyo. "Wakati mwingine inafikia mahali ambapo unapaswa kujiondoa na kuwa shahidi wa yanayotokea. Nadhani hiyo ilikuwa hafla ya Kiama Kia Ma na sisi hatukuhusika," akasema Bw Muigai. Bw Muigai alisema baadhi ya wazee waliohudhuria hafla hiyo waliwahi kumtembelea aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro na kumtambua kama kiongozi wa kisiasa wa Mlima Kenya. Alisema ushiriki wao katika hafla ya Profesa Kindiki ulizua maswali iwapo walikuwa wakiendeleza maslahi ya kibinafsi. Bw Gachagua, ambaye sasa anaongoza chama cha DCP , alijitenga na hafla hiyo na kukana kuhusishwa na wazee walioiandaa. Alidai baadhi ya waliohudhuria walilipwa Sh3,000 kila mmoja, ingawa madai hayajidhibitishwa. "Hizi ni njama za kisiasa zinazolenga kuwapatia nafasi salama mawakala wawili wa kugawanya mlima ambao ni Profesa Kindiki na Bw Ruku, kwa niaba ya Rais Ruto. Lakini kwa pamoja wanapaswa kujua kuwa kura ya 2027 itakuwa wakati wa kuwawajibisha," akasema akiwa Kansas, Amerika. Profesa Kindiki aliteuliwa kuwa Naibu Rais Novemba 1, 2024 baada ya Bw Gachagua kuondolewa mamlakani. Tangu wakati huo, amekuwa akijitokeza kama kiungo kati ya serikali ya Kenya Kwanza na jamii za Mlima Kenya, huku akisisitiza kuwa atakuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto 2027. Hata hivyo, uongozi wake wa kisiasa katika eneo hilo unapingwa na Bw Gachagua, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Martha Karua na viongozi wengine wa kisiasa. Mbunge wa Juja, George Koimburi na mwenzake wa Ndia, George Kariuki, pia walizua maswali kuhusu kutawazwa kwa Profesa Kindiki, wakisema hafla hiyo haikuwa halali.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 21 Sep 2026 02:55:18

Sifuna ajiandaa kuzindua chama cha Ukombozi People's Party (UPP)

MIPANGO ya kuzindua Ukombozi People's Party (UPP), chama kinachotarajiwa kutumiwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna katika azma yake ya kuwania urais mwakani, imeanza kushika kasi huku uzinduzi ukitarajiwa kufanyika mapema Oktoba. Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya na Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi walisema wikendi kuwa chama hicho kitazinduliwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo, huku Oktoba 3 ikitajwa kuwa tarehe inayopendekezwa kwa uzinduzi huo. Hata hivyo, viongozi hao walikataa kutoa maelezo kuhusu mahali ambapo hafla hiyo itafanyika na maafisa watakaoshikilia nyadhifa katika chama hicho kipya. Bw Osotsi aliishutumu serikali kwa kuzuia juhudi za vuguvugu la Linda Mwananchi kusajili jina la kisiasa lililopendekezwa, akisema changamoto hizo hazijawazuia viongozi wake kutafuta chama mbadala. "Mmekuwa mkiuliza chama chetu ni kipi. Wamejaribu kuchukua jina la chama chetu na kuwaweka watu wao, lakini kesi hiyo itaamuliwa Septemba 30. Tulijaribu kupata chama lakini wakaweka vikwazo," akasema Bw Osotsi. "Hata hivyo, sisi ni wajanja na tumepata chama. Ndani ya wiki mbili tutatangaza chama ambacho Edwin Sifuna atatumia kuwania urais," akaongeza akiwa Vihiga. Mahakama ya Migogoro ya Vyama vya Kisiasa inatarajiwa kutoa uamuzi Septemba 30 kuhusu mzozo unaohusu jina la Linda Mwananchi. Bw Natembeya pia aliwaambia wafuasi wa Bw Sifuna kuwa muda wa kusubiri chombo cha kisiasa unaelekea ukingoni. "Katika wiki tatu zijazo, tarajieni moshi mweupe na hakuna mtu atakayetuchezea tena," akasema. Uzinduzi huo unatarajiwa kuwakutanisha viongozi wa upinzani huku vuguvugu hilo likijaribu kujenga jukwaa imara kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Viongozi kadhaa waliozungumza na Taifa Leo walikataa kutoa maelezo kuhusu hafla hiyo na badala yake wakamtaka mwandishi awasiliane na Bw Sifuna. "Sina maelezo kuhusu mahali hafla hiyo itafanyika, lakini kuna bajeti na mambo mengine yanayohusika. Wasiliana na Sifuna mwenyewe," akasema Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga. Duru ndani ya kambi ya upinzani zilisema waandalizi wanapanga kuwaalika wageni mashuhuri, wakiwemo baadhi kutoka nje ya Kenya. Mipango ya uzinduzi huo inafanyika wakati kukiwa na tofauti ndani ya Linda Mwananchi kuhusu chama cha kisiasa kitakachotumika katika uchaguzi wa 2027. Bw Natembeya ameunga mkono Ukombozi kutumiwa na Bw Sifuna, huku Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino akisisitiza atatumia chama chake cha Mwananchi Party na kupendekeza muungano wa vyama hivyo. Akizungumza katika mazishi yaliyofanyika Nyakach, Kaunti ya Kisumu, Ijumaa, Bw Owino alisema ataendelea kuunga mkono azma ya Bw Sifuna ya kuwania urais licha ya tofauti hizo.  "Tutamsimamisha Sifuna kuwa mgombea wa urais na kuunda muungano, huku Sifuna akiwa kiongozi wa Chama cha Ukombozi na Babu akiwa kiongozi wa Chama cha Mwananchi," akasema. Hata hivyo, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi ameonya kuwa Linda Mwananchi huenda ikasambaratika kabla ya uchaguzi wa 2027 iwapo viongozi wake hawatamaliza tofauti zao. Bw Amisi, ambaye ameondoka katika vuguvugu hilo, aliwashutumu baadhi ya viongozi kwa kufuata maslahi yao binafsi na kudhoofisha azma ya Bw Sifuna ya kujijenga kitaifa.  "Babu Owino ana mapungufu yake kama binadamu, lakini bado ni kiongozi. Na kwa kuwa tunamhitaji Sifuna ashinde, lazima umpe nafasi kwa njia bora iwezekanavyo," alisema akizungumzia tofauti kati ya Bw Owino na Bw Sifuna kuhusu chama cha kutumika katika uchaguzi wa mwaka ujao. Bw Amisi pia alijitolea kutoa chama chake cha People's Renaissance Movement (PRM) kiwe chombo mbadala cha Seneta Sifuna, akisema yuko tayari kurejea Linda Mwananchi iwapo waanzilishi wa awali wa vuguvugu hilo watakutana na kutatua tofauti zao. "Ninaweza kurejea Linda Mwananchi, lakini kwanza tukutane kama waanzilishi wa awali na tutafute tulikosea wapi. Sifuna bado ni kiongozi wetu na chama kiko tayari. Suala la kutafuta chama halipaswi kuwepo kwa sababu chama hiki kilianzishwa hata kabla ya Linda Mwananchi," akasema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 19 Sep 2026 16:45:14

Wito Kenya iweke mikakati kukuza mastaa chipukizi

Kocha wa Rising Stars Gilbert Selebwa ameitaka Kenya kuwa mikakati ya muda mrefu ya kukuza chipukizi,  utakaowezesha taifa kuwa na wachezaji wanaopanda kutoka timu za wadogo hadi wakubwa. Selebwa alitoa ombi hilo baada ya matumaini ya Kenya kufuzu kwa fainali za mwakani za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa wachezaji wasiozidi miaka za 20, kufifia kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Sudan Kusini katika mechi yao ya mwisho ya kufuzu Kundi 'C' Jumamosi jijini Dar es Salaam. "Watu wanapaswa kuelewa kwamba kujenga timu ina utaratibu wake. Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kunoa timu ya taifa na asilimia 70 ya wachezaji walikuwa wakicheza katika kiwango hiki kwa mara ya kwanza. Matarajio yalikuwa makubwa kutoka kwetu," alisema Selebwa. Alisema pia muundo wa kikosi hicho ulidhihirisha pengo lililopo katika mfumo wa Kenya wa kukuza vipaji vya vijana. "Ukiangalia jinsi tulivyounda kikosi, asilimia 90 ya wachezaji hawakuwa wamecheza katika AFCON ya mwaka jana, huku wengi wao wakiwa wamepandishwa hadi timu za U20 na U23," alisema. Selebwa anaamini Kenya inahitaji kuwa na kundi thabiti la wachezaji wanaopitia hatua timu za chipukizi za timu za taifa za vijana badala ya kuunda vikosi wakati mashindano yanapokaribia. "Tunapaswa kuwa na kundi maalum la wachezaji wanaopanda kutoka U15 hadi U17 na kisha U20 kwa sababu hilo ndilo tunalokosa," alisema kocha huyo wa zamani wa AFC Leopards, Shabana FC na Muhoroni Youth. Pia aliitaka Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuhakikisha makocha waliohitimu na wenye uwezo wanawekwa katika ngazi za chini ili kutambua na kukuza vipaji. "FKF inahitaji kuwa na makocha sahihi wanaoshuka chini kuwanoa wachezaji. Hii itasaidia kuimarisha timu zetu za vijana," aliongeza Selebwa. Kenya ilimaliza kampeni yake ya kufuzu kwa AFCON bila ushindi baada ya kupoteza 2-0 dhidi ya Burundi katika mechi yake ya kwanza kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Sudan Kusini. Brighton Nancheri aliokoa pointi moja kwa Rising Stars kwa kusawazisha dakika ya 93 baada ya Sudan Kusini kupata bao kupitia Jonathan Ajoung dakika ya 26. Matokeo hayo yaliiacha Kenya katika nafasi ya pili Kundi C ikiwa na pointi moja, sawa na Sudan Kusini lakini ikiwa mbele kwa tofauti ya mabao. Burundi iliongoza kundi hilo kwa pointi sita na kufuzu kwa nusu-fainali. Kufuatia kutolewa huko, Kenya itakosa AFCON za mwaka ujao nchini Ghana.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 16:14:13

Wanafunzi wafunzwa namna ya kuzoa na kuchakata upya taka kiuchumi

KARATASI zilizotumika, chupa za plastiki, makopo na vifungashio vingine vinavyotupwa kwa pamoja mara nyingi huonekana kama taka zisizo na thamani. Lakini yamkini usilojua ni kwamba iwapo taka hizo zitatenganishwa kwa usahihi, zinaweza kubadilika zikawa vifaa vipya kabisa kwa mwanadamu huku vikitoa fursa za kipato kwa maelfu ya watu wanaoshiriki katika sekta ya uchakataji upya wa vifaa vilivyotumika (recycling). Ni kwa msingi huo ambapo mpango mpya unaolenga kuwafundisha wanafunzi kutenganisha taka kisha kuiunda taka hiyo kuwa vifaa muhimu, ulibuniwa, ukiwalenga watoto kama washiriki muhimu katika kubadilisha namna taka zinavyokusanywa na kushughulikiwa nchini. Mpango huo unalenga kuifanya shule kuwa mahali ambapo tabia ya kutenganisha taka, kutambua vifaa vinavyoweza kuchakataliwa upya/kurejelewa na kuelewa thamani ya rasilimali zilizotumika inaanza mapema. Kupitia mpango huo, unaojulikana kama Tuwezeshe, kampuni ya PAKPRO (Packaging Producer Responsibility Organisation) na Kenya Scouts Association (KSA) zinalenga kuwapa wanafunzi maarifa na ujuzi wa vitendo kuhusu usimamiaji wa taka za vifaa vya kufungia bidhaa, kama vile plastiki, karatasi, makopo na vifaa vingine vinavyoweza kuchakatwa tena. Ushirikiano huo ulizinduliwa katika Kambi ya Maskauti ya Rowallan, Nairobi, ukiwalenga watoto wenye umri wa kati ya miaka sita na 24. Sehemu muhimu ya mpango huo ni usambazaji wa mapipa 600 katika shule 150, ambapo wanafunzi watafundishwa kutenganisha taka badala ya kuzichanganya zote katika pipa moja. Lengo ni kuhakikisha kuwa vifaa vinavyoweza kurejelewa vinakusanywa kwa njia inayowezesha kupelekwa kwa wakusanyaji, vituo vya ununuzi wa taka na wachakataji walio katika sekta rasmi ya urejeleaji. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa PAKPRO, Joyce Gachugi-Waweru, alisema mabadiliko ya kweli katika usimamizi wa taka yanahitaji kuanza na elimu na tabia zinazojengwa mapema. Alisema watoto wa leo ndio watakaokuwa viongozi na wafanyaji wa maamuzi katika kipindi cha miaka 20 ijayo, hivyo ni muhimu kuwafunza namna taka zinavyoweza kuwa rasilimali badala ya mzigo. "Tunataka kizazi kitakachoelewa kuwa taka si kitu cha kutupwa tu. Kuna vifaa vinavyoweza kurejelewa na kuendelea kuwa na thamani katika uchumi, ikiwa vitatenganishwa na kushughulikiwa ipasavyo," alisema. Kwa mujibu wa PAKPRO, uchanganyaji wa taka bado ni changamoto kubwa inayopunguza ufanisi wa urejeleaji. Vifaa vinavyoweza kuchakatwa vinapochanganywa na mabaki ya chakula na taka nyingine, huwa vigumu zaidi kutenganishwa na mara nyingi hupoteza thamani yake. Mpango wa Tuwezeshe unalenga kushughulikia changamoto hiyo kuanzia katika chanzo cha taka - shuleni- kwa kuwapa wanafunzi uwezo wa kutambua, kutenganisha na kuhifadhi vifaa vinavyoweza kurejelewa. Kamishna Mkuu wa KSA, Victor Radido, alisema ushirikiano huo utawezesha maskauti kutumia mtandao wao wa shule na vikundi vya vijana kueneza maarifa kuhusu usimamizi bora wa taka. Alisema elimu hiyo haitakiwi kubaki darasani pekee, bali inapaswa kuwafikia wazazi na jamii kupitia tabia ambazo wanafunzi wataendelea nazo wakiwa nyumbani. "Tunataka watoto wetu waelewe kwamba usimamiaji taka unaanza na hatua rahisi kama kuweka karatasi, plastiki na taka nyingine katika mapipa yanayofaa. Hii ni tabia watakayoweza kuendeleza shuleni, nyumbani na katika jamii," alisema. Washirika hao wanasema mpango huo hautahusu kuweka mapipa pekee, bali pia kuwasaidia wanafunzi kuelewa kinachotokea baada ya taka kuwekwa kwenye pipa. Hii ni pamoja na kufahamu safari ya chupa ya plastiki, karatasi au makopo kutoka shuleni hadi kwa mkusanyaji na hatimaye kwa mchakataji anayezigeuza kuwa malighafi au bidhaa mpya. Walimu pia watapewa nafasi ya kuongoza shughuli za vitendo, ikiwemo mashindano ya usafi, mafunzo ya ubunifu wa kutumia tena vifaa na ufuatiliaji wa kiasi cha taka kinachokusanywa. Hatua hizi zitasaidia shule kupima maendeleo na kudumisha mpango kwa muda mrefu zaidi. PAKPRO imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na urejeleaji wa taka za vifungashio. Shirika hilo linasema zaidi ya chupa bilioni moja za plastiki zimekusanywa kupitia mifumo ya urejeleaji inayohusishwa na juhudi zake, huku zaidi ya Sh100 milioni zikiwa zimeelekezwa katika kukuza shughuli za urejeleaji na kuwawezesha wahusika katika sekta hiyo. Sekta ya urejeleaji inahusisha maelfu ya watu, wakiwemo wakusanyaji taka, waendeshaji wa vituo vya ununuzi wa taka, wasafirishaji, waunganishaji na wachakataji. Kwao, taka zilizotenganishwa vizuri ni malighafi yenye thamani. Kwa kuwafundisha wanafunzi kutenganisha taka, mpango huo unalenga pia kuwaonyesha uhusiano kati ya tabia za kila siku na fursa za kiuchumi zinazotokana na urejeleaji. Wanafunzi watakapojifunza kutenganisha taka shuleni, wanatarajiwa kupeleka maarifa hayo nyumbani na kuwahamasisha familia zao kufuata utaratibu huo. Ushirikiano huo unatekelezwa wakati Kenya ikiendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi endelevu wa taka chini ya sheria na kanuni zinazosisitiza kupunguza taka, kutumia tena na kurejeleza vifaa vinavyoweza kurejeshwa. PAKPRO na KSA zinasema mpango wa Tuwezeshe ni hatua ya kujenga kizazi kitakachotambua kuwa thamani ya taka haimaliziki zinapotumiwa mara ya kwanza. Badala yake, kupitia utenganishaji sahihi, vifaa hivyo vinaweza kurejea katika uzalishaji, kusaidia biashara za urejeleaji na kupunguza kiasi cha taka kinachoishia kwenye jalala kama Dandora, Kayole na vingenevyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 07:55:20

Watu 49 wafariki Nigeria baada ya kunywa pombe yenye sumu

TAKRIBAN watu 49 wamefariki na wengine 182 wamelazwa hospitalini baada ya kushukiwa kuathiriwa na sumu kwenye pombe katika jimbo la Ondo, kusini-magharibi mwa Nigeria, Waziri wa Afya wa jimbo hilo alisema Ijumaa. Suala hilo liliripotiwa kwa mara ya kwanza Septemba 5, wakati maafisa walisema watu 29 walikuwa wamefariki ndani ya wiki ya kwanza baada ya kunywa pombe hiyo. Waziri wa Afya wa Ondo, Banji Ajaka, alisema idadi ya waliofariki ilikuwa imeongezeka hadi 49 kufikia Ijumaa. Mamlaka za Ondo zinashuku kuwa vifo hivyo vilisababishwa na sumu ya methanol iliyokuwa kwenye pombe ya kienyeji inayotengenezwa kwa njia isiyodhibitiwa na inayojulikana kwa jina la "Monkey Tail". Tukio hilo limeangazia hatari za pombe zisizodhibitiwa ambazo bado hutumiwa kwa wingi katika baadhi ya maeneo ya Nigeria kutokana na bei yake ya chini na kupatikana kwa urahisi. Bw Ajaka alisema tukio hilo lilifuatiliwa hadi kwenye sherehe mbili za kitamaduni katika eneo la Odigbo, ambapo wageni walikunywa pombe iliyotengenezwa nchini humo. "Dalili za ugonjwa na taarifa kuhusu walichokunywa zimeibua tuhuma kubwa za kitabibu kwamba huenda waliathiriwa na pombe yenye sumu. Hata hivyo, bado hatujapata ushahidi wa maabara," alisema Bw Ajaka katika taarifa. Waathiriwa waliripoti dalili mbalimbali zikiwemo maumivu ya kichwa, maumivu ya mwili, matatizo ya kupumua, kupoteza fahamu. Bw Ajaka alisema madhara hayo yalijitokeza kwa kasi baada ya watu kutumia pombe hiyo. "Jambo hili lilitokea haraka. Unapokunywa, kutegemea kiwango ulichotumia, figo zinaweza kushindwa kufanya kazi, macho kupoteza uwezo wa kuona na ubongo kuharibika," alisema. Methanol ni aina ya sumu ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa mwilini inapomezwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 06:55:43

Hofu tele wasichana 36 wa shule moja ya Upili wakipata mimba

WADAU wa elimu pamoja na viongozi wa utawala katika Kaunti Ndogo ya Webuye Mashariki, Kaunti ya Bungoma, juzi walifanya mkutano wa dharura kufuatia ongezeko kubwa la mimba za mapema katika shule moja ya eneo hilo. Wanafunzi wasiopungua 36 wa Shule ya Sekondari ya Bakisa wamekuwa wajawazito au wameacha masomo mwaka huu baada ya kupata watoto. Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa na uongozi wa shule hiyo, wanafunzi 10 kwa sasa ni wajawazito na bado wanaendelea na masomo yao huku wakikabiliana na changamoto za ujauzito. Wengine 13 walijifungua majuzi, huku wanafunzi 13 zaidi wakiacha shule kabisa baada ya kupata mimba. Mkutano huo uliofanyika Ndivisi uliwaleta pamoja maafisa wa usalama, viongozi wa elimu, wazazi, viongozi wa kidini na wanasiasa ili kutafuta suluhu za haraka za kukabili tatizo hilo. Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Kamishna wa Kaunti wa Ndivisi, Emmanuel Kenga, alisema umaskini uliokithiri na uzembe wa baadhi ya wazazi ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia kuongezeka kwa mimba za mapema. Alisema kuna wanaume wanaowalenga wasichana wadogo kwa kuwapa chakula, zawadi ndogo na fedha ili kushawishi kushiriki ngono. "Umaskini unachangia sana tatizo hili. Baadhi ya wanaume wanatumia udhaifu wa wasichana wetu kwa kuwavutia kwa pesa na mahitaji ya msingi," alisema Kenga. Aidha, alitaja matumizi yasiyodhibitiwa ya simu za mkononi na teknolojia kama sababu nyingine inayowafanya watoto kukumbana na maudhui yasiyofaa katika umri mdogo. Baadhi ya wazazi waliodhuria mkutano huo walidai kwamba wasichana wengi hushawishiwa na wanaume wanapokuwa njiani kuelekea au wakitoka shuleni. Wengine walilaumu hali ya watoto kulelewa na babu na nyanya huku wazazi wao wakitafuta ajira mijini. Viongozi wa utawala walifichua kuwa baadhi ya familia hukubali fidia kutoka kwa wanaodaiwa kuwapa mimba watoto wao badala ya kuripoti kesi hizo ili hatua za kisheria zichukuliwe. Inadaiwa kwamba kesi nyingi hutatuliwa kupitia mikutano ya kijamii au baraza za wazee kwa makubaliano ya kifedha. Mwalimu Margaret Muindi aliwataka wazazi kukoma kupokea zawadi au fedha kutoka kwa wahusika wa vitendo hivyo kwa kuwa hatua hiyo huathiri juhudi za kupata haki kwa waathiriwa. Naye Nancy Chibeu, alionyesha masikitiko yake akisema kuwa licha ya wanafunzi 36 kuathiriwa, ni kesi moja pekee ambayo imeripotiwa rasmi. Alitoa wito kwa wananchi kuwafichua wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria na wasichana walindwe dhidi ya unyanyasaji wa kingono.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 05:55:59

Mpango wa Gachagua kuwachuja wafuasi wa Ruto ulivyofeli

BAADA ya chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Rigathi Gachagua kushinda uchaguzi mdogo wa Ol Kalou mnamo Julai 2026, viongozi wengi waliokuwa wakimuunga mkono Rais William Ruto walianza kuonyesha nia ya kuhamia upande wa Gachagua. Katika uchaguzi huo, mgombea wa DCP Kamau Ngotho alipata kura 35,440 dhidi ya kura 5,450 za mgombea wa UDA Muchina Nyagah. Ushindi huo mkubwa ulitafsiriwa kama ishara kwamba eneo la Mlima Kenya lilikuwa likibadili msimamo wake wa kisiasa. Kutokana na wimbi hilo la viongozi waliotaka kuhamia DCP, Gachagua alitangaza kuwa chama chake kingepokea wanachama wapya lakini wale waliokuwa washirika wa karibu wa Rais Ruto wangepitia mchujo mkali kabla ya kukubaliwa. Hatua hiyo ilifuatia shinikizo kutoka kwa viongozi wa DCP waliokuwa na wasiwasi kuwa baadhi ya wanasiasa hao walitaka kuingia chamani ili kukidhoofisha kutoka ndani. Viongozi hao walikumbushwa jinsi baadhi yao walivyoshiriki kampeni dhidi ya Gachagua na DCP. Mnamo Agosti 2, 2026, Gachagua alitangaza kuundwa kwa kamati ya watu saba kuchunguza maombi ya viongozi waliotaka kuhama kutoka UDA kwenda DCP. Kamati hiyo ilijumuisha Maseneta John Methu, Joe Nyutu na Karungo Thang'wa pamoja na wabunge na viongozi wengine wa chama. Hata hivyo, mpango huo haukudumu. Wanachama wa DCP waliibua malalamiko wakitaka wanaotaka kujiunga na chama wapimwe hadharani katika mikutano ya kisiasa badala ya kuhojiwa kwa siri. Hali hiyo ilifanya kamati ya uchunguzi ishindwe kuanza kazi rasmi. Mbunge wa Gatundu Kusini Gabriel Kagombe alikuwa miongoni mwa walioathiriwa na mfumo huo mpya. Alimuomba Gachagua msamaha hadharani na kutangaza kwamba amechoka na Rais Ruto. Lakini aliporuhusiwa kuhutubia mikutano ya DCP katika maeneo mbalimbali, wananchi walimzomea na kukataa kumpokea. Kilichompata Kagombe kilituma ujumbe kwa viongozi wengine waliotaka kuhama. Wengi waliogopa aibu ya kukataliwa mbele ya umma na hivyo wakaamua kubaki katika UDA au kutafuta vyama vingine. Aliyekuwa mwenyekiti wa Kampuni ya Mbegu Kenya, Wangui Ngirichi, pia alikabiliwa na hali ngumu alipojaribu kujiunga na DCP. Mikutano aliyohudhuria iligeuka kuwa ya vurugu huku wafuasi wake wakikabiliana na wale wa DCP, hali iliyosababisha majeraha na kifo cha mtu mmoja. Kwa sasa, viongozi wa DCP wanasema kanuni za uchunguzi bado zipo, lakini hakuna aliyewasilisha rasmi ombi la kuchunguzwa. Hivyo basi, kamati iliyoundwa na Gachagua imebaki bila kazi. Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa mpango wa kuwachuja wafuasi wa Rais Ruto uliporomoka kutokana na upinzani wa wanachama wa DCP wenyewe. Badala ya mchakato rasmi wa uchunguzi, wanachama waliamua kuwa wapiga kura katika mikutano ya hadhara ndio wawe waamuzi wa mwisho kuhusu nani anafaa kupokelewa katika chama hicho. Matokeo yake ni kwamba viongozi wengi waliokuwa wakipanga kuhamia DCP wameendelea kusalia katika UDA au wanasaka majukwaa mengine ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 04:55:42

Oburu angali Uingereza, asubiri madaktari wampe idhini kurejea

KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Dkt Oburu Oginga, bado yuko nchini Uingereza akipokea matibabu huku familia yake ikisema hali yake imeimarika lakini bado hajaruhusiwa na madaktari kurejea nchini. Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kisumu, Ruth Odinga, ambaye ni dadake mdogo, alisema mwanasiasa huyo mkongwe anaendelea kufuatiliwa na madaktari na familia haijafanya mipango yoyote ya haraka ya kumrejesha nyumbani. Kwa mujibu wa Bi Odinga, jambo la msingi kwa sasa ni kuruhusu madaktari kukamilisha kukagua afya yake kabla ya uamuzi wowote kufanywa kuhusu safari yake ya kurejea Kenya. "Ameimarika sana, lakini hatujapanga kurejea kwake Kenya kwa sasa," alisema Bi Odinga akiwa Uingereza. Aliongeza kuwa familia haina haraka ya kumrejesha nchini kwa kuwa bado ana miadi kadhaa ya matabibu ambayo lazima ahudhurie. Bi Odinga alifafanua kuwa Dkt Oginga hajalazwa hospitalini kwa sasa. Badala yake, anaishi karibu na hospitali anayohudumiwa ili iwe rahisi kuhudhuria ukaguzi na miadi ya madaktari. "Hajalazwa. Tunaishi karibu na hospitali, kwa hivyo ni rahisi kwake kuonana na madaktari wakati wowote anapohitajika," alisema. Familia hiyo imesisitiza kuwa afya ya mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 83 ni muhimu zaidi kuliko majukumu yake ya kisiasa. Kwa sababu hiyo, hawataki kuharakisha kurejea kwake kabla madaktari kuthibitisha kuwa yuko katika hali nzuri. Habari hizo zinajiri huku Dkt Oginga akiendelea kushiriki shughuli mbalimbali kwa njia ya mtandao akiwa Uingereza. Wiki hii alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akieleza kuwa yeye na mkewe, Mama Judy, walimpokea Balozi wa Kenya nchini Uingereza, Maurice Makoloo, katika makazi yao.  Alisema walijadili jinsi ya kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na Uingereza, kusaidia Wakenya wanaoishi ughaibuni pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji na ujuzi wao.

read more