T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Hali inazidi kuwa mbaya nchini, Kanisa laonya

KANISA la Anglican Church of Kenya (ACK), limekosoa vikali serikali, likionya kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha, ongezeko la ushuru, visa vya kutoweka kwa watu, ukiukaji wa haki za kibinadamu, ghasia za kisiasa na ufisadi. Katika taarifa iliyotolewa baada ya kikao cha Kamati ya Kudumu ya Kanisa hilo kilichofanyika katika Kanisa la All Saints' Cathedral jijini Nairobi, Askofu Mkuu wa ACK, Jackson Ole Sapit, alisema Kenya inakabiliwa na mazingira ya kisiasa yanayozidi kuwa hatari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027. Kanisa hilo lilionya dhidi ya kurejea kwa siasa za ukabila, uchochezi, vitisho, kuhadaa wapigakura na vurugu zinazoweza kuhatarisha amani ya taifa. "Kuongezeka kwa uhuni wa kisiasa, matamshi ya uchochezi, mgawanyiko wa kikabila na kuvurugwa kwa shughuli za kisiasa kunapaswa kuwatia wasiwasi Wakenya wote wenye nia njema," alisema Askofu Ole Sapit. Alisema jambo linalotia hofu zaidi ni matumizi ya vijana wasio na ajira kama zana za mizozo ya kisiasa. "Maisha ya vijana yanatolewa kafara kwa ajili ya tamaa za kisiasa. Tunasema wazi kuwa hali hiyo ni mbaya na haikubaliki. Tunaomboleza wale waliopoteza maisha katika makabiliano ya kisiasa. Hakuna cheo kinachostahili damu ya Mkenya kumwagika," alisema. ACK iliwataka viongozi wa kisiasa kupunguza joto la kisiasa na kuepuka kauli za uchochezi, huku ikihimiza idara za usalama kutekeleza sheria bila upendeleo. Kanisa hilo pia liliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuanza maandalizi ya mapema ya uchaguzi huru, wa haki, unaoaminika na unaoweza kuthibitishwa. "Uchaguzi wa amani haujengwi siku ya kupiga kura. Hujengwa kupitia haki, kuaminiana na maandalizi ya muda mrefu kabla ya uchaguzi kufanyika," alisema.  Kuhusu ufisadi, ACK ilieleza kuwa rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma ndiyo kidonda kikubwa zaidi kinacholikabili taifa. Kanisa linataka mashirika ya kupambana na ufisadi, vyombo vya uchunguzi na Idara ya Mahakama kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika bila kujali hadhi zao. "Wakenya wamechoshwa na uchunguzi usiozaa matunda na kashfa zisizo na matokeo. Haki haipaswi kuzingatia mamlaka, utajiri au ushawishi wa mtu," alisema Askofu Ole Sapit.  Kanisa pia lilielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya huduma za afya nchini, likitaja mgomo wa muda mrefu wa wauguzi na changamoto nyingine zinazokumba sekta hiyo. "Huduma za afya si anasa ya matajiri. Serikali za kitaifa na kaunti zinapaswa kushirikiana kwa haraka na wahudumu wa afya kutatua migogoro iliyopo," alisema. Aidha, ACK ilipinga baadhi ya mapendekezo katika Mswada wa Elimu ya Msingi, ikisema masuala yanayohusu mamilioni ya watoto hayawezi kuamuliwa bila mashauriano ya kutosha na wadau mbalimbali. Kanisa hilo lilionya kuwa Wakenya wengi wanateseka kutokana na ukosefu wa ajira, kupanda kwa gharama ya maisha, kufungwa kwa biashara na mzigo mkubwa wa ushuru. "Ushuru ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, lakini ushuru unaowaumiza wananchi huku rasilimali za umma zikifujwa unakuwa chombo cha ukosefu wa haki," ilisema taarifa hiyo. ACK ilihitimisha kwa kusema kuwa Kenya ipo katika kipindi muhimu cha kihistoria na kwamba changamoto zinazolikabili taifa si za kisiasa na kiuchumi pekee bali pia za kimaadili na kiroho. Kanisa liliwataka viongozi na wananchi kukumbatia uwajibikaji, uadilifu na toba ili kunusuru taifa dhidi ya migawanyiko na migogoro inayoweza kujitokeza kabla ya uchaguzi wa mwaka 2027.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 minutes ago

Maseneta walalamikia Ruto kuandamana na kikosi cha mawaziri saba ziarani Amerika

Uamuzi wa Rais William Ruto kusafiri  New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) akiandamana na Mawaziri saba umeibua mvutano mpya katika Seneti, ambapo baadhi ya maseneta wanahoji iwapo ukubwa wa ujumbe huo una sababu za msingi wakati Bunge linaendelea kutafuta majibu kutoka kwa serikali kuhusu masuala yanayowakabili Wakenya. Mjadala huo uliibuka Jumatano wakati wa vikao vya Seneti Mashinani vilivyofanyika Kaunti ya Kilifi. Maseneta wa upinzani walilalamikia kutokuwepo kwa baadhi ya mawaziri wakisema hali hiyo imechelewesha mijadala kuhusu matatizo yanayowakumba wananchi pamoja na utekelezaji wa miradi ya serikali. Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, alihoji sababu ya mawaziri saba kuandamana na Rais katika mkutano huo wa kimataifa. "Kenya si taifa lililoshindwa kiasi kwamba mawaziri saba waandamane na Rais kwenda UNGA ilhali jukumu lao ni kuketi nyuma yake anaposoma hotuba," alisema Khalwale. Alisema hatua hiyo inaathiri utendaji wa serikali na pia inaongeza mzigo kwa walipa ushuru kutokana na gharama za tiketi za ndege, usalama na matumizi mengine ya safari. Lawama hizo ziliongezeka baada ya kubainika kuwa baadhi ya mawaziri waliokuwa wakihitajika kujibu maswali ya Seneti hawakuwapo nchini. Miongoni mwao ni Waziri wa Madini Hassan Joho, Waziri wa Elimu Julius Migos na Waziri wa Teknolojia ya Habari William Kabogo. Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alisema kutokuwepo kwa Bw Joho kulitatiza mijadala kuhusu kituo cha samaki cha Kilifi Central ambacho maseneta walikuwa wametembelea. Kwa mujibu wa Sifuna, wavuvi, vijana na wakazi wa eneo hilo walieleza hofu kuhusu mustakabali wa mradi huo na nafasi za ajira zitakazotokana nao. "Wananchi wana wasiwasi mkubwa, hasa vijana ambao hawajapewa hakikisho kwamba wao watapewa kipaumbele cha ajira katika eneo hilo," alisema. Aidha alisema wakazi wana hofu kuwa mradi huo huenda ukaendeshwa kupitia ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi, hali inayozua maswali kuhusu nani atanufaika. Sifuna pia alikosoa viongozi wa serikali kwa kutumia muda mwingi nje ya nchi huku wananchi wakikumbwa na changamoto mbalimbali nyumbani. Hata hivyo, Seneta wa Tana River Danson Mungatana alitetea uamuzi wa mawaziri kuandamana na Rais akisema safari kama hizo huwapa nafasi ya kufanya mikutano ya pembeni, kujadiliana na mataifa mengine na kutia saini mikataba ya maendeleo. "Katika safari moja, mawaziri wanaweza kufanya shughuli nyingi muhimu za serikali badala ya kusafiri mara kwa mara kwa gharama kubwa zaidi," alisema. Mvutano huo unaonyesha changamoto iliyopo kati ya shughuli za kimataifa za serikali na hitaji la mawaziri kuwajibika kwa wananchi na Bunge.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Sifuna, Kalonzo wapigania jina 'Ukombozi'

CHAMA cha Wiper Patriotic Movement kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka kimeeleza kwa mara ya kwanza jinsi kilivyotwaa jina The Ukombozi Alliance (TUA), huku mzozo kuhusu jina hilo ukizidi kupamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Kupitia kampuni ya mawakili ya LAK Advocates, chama hicho kimesema kilianza kutafuta na kuhifadhi majina ya vyama tangu Machi 2025, wakati kilipokuwa kikijiandaa kuunda muungano wa kisiasa. Kwa mujibu wa nyaraka zilizopatikana na Taifa Dijitali, chama hicho kilihifadhi majina tisa, yakiwemo The Ukombozi Alliance, kabla ya kuchagua kuwa jina lake. Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa mchakato ulianza Machi 18, 2025, wakati jina Chama Cha Ukombozi lilipohifadhiwa. Wiki moja baadaye, likafuata jina Ukombozi Freedom Party. Mnamo Aprili 6, 2025, chama kilihifadhi Ukombozi Freedom Front, huku majina mengine yakihifadhiwa baadaye mwaka huo na mwaka 2026. Mnamo Julai 20, 2026, jina The Ukombozi Alliance lilihifadhiwa rasmi. Muungano huo unasema mchakato huo uliodumu zaidi ya mwaka mmoja ulifikia kilele Agosti 3, 2026, wakati jina hilo lilipochaguliwa na Azimio La Umoja One Kenya Coalition na kuwasilishwa kushughulikiwa. Mzozo huo uliibuka baada ya washirika wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna pia kujaribu kutumia jina Ukombozi kwa chama cha kisiasa. Katika barua ya Septemba 8, 2026, Msajili wa Vyama vya Kisiasa, John Cox Lorionokou, alikataa ombi la upande wa Bw Sifuna kubadilisha jina la United Democratic Party (UDP) kuwa Ukombozi People's Party (UPP). Msajili alisema jina hilo lilifanana kwa kiwango kikubwa na The Ukombozi Alliance. Hata hivyo, nyaraka zinaonyesha kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP), ilikuwa imeidhinisha awali uhifadhi wa jina Ukombozi People's Party mnamo Machi 13, 2025, baada ya ombi la wakili Allan Akivanga. ORPP ilisema uhifadhi huo ungekuwa wa muda usiozidi siku 90. Baadaye, Julai 9, waanzilishi wa UPP waliandikia ORPP wakitaka kusitisha mchakato wa usajili. Bw Akivanga alisema walikuwa wameomba kusitisha usajili baada ya kuombwa na UDP, iliyotaka kubadilisha jina lake kuwa UPP. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya alihusishwa na mpango wa kubadilisha jina la UDP, chama kilichowahi kuhusishwa na aliyekuwa mbunge wa Lugari, marehemu Cyrus Jirongo. Lakini Septemba 21, Bw Akivanga alibadilisha msimamo na kueleza ORPP kuwa UPP sasa itaendelea na mchakato wa usajili. Alisema hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na kucheleweshwa kwa mchakato wa usajili. Upande wa Bw Musyoka unasema Bw Akivanga hakuongeza muda wa kuhifadhi jina hilo na kwa hivyo alipoteza haki ya kulidai. Kwa mujibu wa LAK Advocates, uhifadhi wa jina la chama huwa wa muda usiozidi siku 90 na muombaji anapaswa kuomba kuongezewa muda ili kuendelea kulilinda. Kampuni hiyo inasema uhifadhi wa jina UPP ulimalizika Juni 13, 2025 bila Bw Akivanga kuchukua hatua za kuuongeza. LAK pia inasema haikuwa na taarifa kuhusu mpango wa UDP kubadilisha jina lake kuwa UPP hadi ilipoona tangazo la gazeti. Mzozo huo ulizidi baada ya UDP kuchapisha tangazo Agosti ikialika maoni kuhusu pendekezo la kubadilisha jina lake. LAK ilisema iliwasilisha pingamizi Agosti 10, 2026, ikieleza kuwa matumizi ya jina Ukombozi yanaweza kusababisha mkanganyiko miongoni mwa wananchi kutokana na kufanana kwa majina hayo. Mzozo huo sasa umeangazia mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kukataa majina yanayoweza kuwachanganya wapiga kura. LAK inasema sheria inampa Msajili mamlaka ya kukataa jina, kaulimbiu au nembo ya chama kipya ikiwa inafanana kwa karibu na chama au taasisi nyingine iliyosajiliwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

Serikali yaandaa Nairobi tayari kwa mafuriko El Niño

Serikali imeanza maandalizi ya kuwaondoa wakazi katika maeneo hatari kwa mafuriko Nairobi huku mvua kubwa inayotarajiwa kuanza wiki ya pili au ya tatu ya Oktoba ikikaribia. Naibu Rais Kithure Kindiki alisema maeneo yanayoweza kuathiriwa yametambuliwa na vituo vya muda vya kuwahifadhi watu wanaoweza kuhamishwa vimeandaliwa. Takriban watu 100,000 Nairobi wanatarajiwa kuathiriwa, huku Mukuru, Mathare, Kibra, Embakasi, Dagoretti South, Makadara na Westlands yakitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyo hatarini. Barabara kuu kama Uhuru Highway, Jogoo Road, Bunyala Road na Mombasa Road pia zinatarajiwa kukumbwa na mafuriko. Prof Kindiki alisema serikali imejiandaa kutoa chakula, dawa na misaada mingine kwa watu watakaohamishwa. Alisema maagizo ya kuondoka yatatolewa wakati utakapofika na serikali itahakikisha wananchi wanaondolewa kwa utu na kupewa taarifa mapema. "Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha uwezekano wa mvua nyingi Nairobi, na inatarajiwa kuwa wiki ya pili na ya tatu ya Oktoba ndipo mvua itaanza," alisema. Idara ya kukabiliana na majanga ya Kaunti ya Nairobi imeanza kusafisha mabomba na njia za maji ya mvua ili kupunguza hatari ya mafuriko. Prof Kindiki alisema maeneo yote yanayozuia maji yametambuliwa na kazi ya kuyafungua na kuondolea uchafu inaendelea. Kaunti inashirikiana na Tume ya Mto Nairobi, huku vijana wa Green Army na Climate Works wakishiriki katika zoezi hilo. Wakati huo huo, Waziri wa Maji Erick Mugaa amewataka wanaoishi kando ya mito kuwa waangalifu kutokana na uwezekano wa viwango vya maji kupanda. Akizungumza wakati wa sherehe za Mara Day huko Bomet, Bw Mugaa alisema wataalamu wa hali ya hewa wanatarajia mvua nyingi kuliko kawaida. Alisema serikali inashirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki na Tume ya Bonde la Ziwa Victoria katika maandalizi. Kamishna wa Wilaya ya Tarime nchini Tanzania, Meja Edward Golowe, alisema tope linalosababishwa na shughuli za binadamu sehemu za juu za Mto Mara limebadilisha mkondo wa mto huo na kuongeza hatari kwa familia zinazoishi kando yake. Serikali pia imeanza kukagua njia za umeme ili kupunguza kukatika kwa umeme wakati wa mvua. Bw Mugaa alisema vituo vya kupima viwango vya maji vinaendelea kutoa taarifa za wakati halisi ili kusaidia kutoa tahadhari na kuhamisha watu hadi maeneo salama. Kituo cha Kitaifa cha Kushughulikia Majanga (NDOC) kinaratibu maandalizi hayo kote nchini. Maafisa wa serikali za kaunti wamepewa jukumu la kutambua maeneo hatari kwa mafuriko na maporomoko ya ardhi, njia za uokoaji na vituo vya kuwahamishia waathiriwa. Tahadhari pia itatolewa kupitia mikutano ya hadhara, makanisa, misikiti na vituo vya redio vya kimaeneo. Serikali imesema makundi yaliyo katika hatari zaidi, wakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, watapewa kipaumbele wakati wa uokoaji. Wakati huo huo, viongozi wa dini kupitia Association of Religious Practitioners Professionals (AREPP) wamejiunga na maandalizi hayo. Mkurugenzi wake, Dkt Ezekiel Muendo, alisema waumini 470 na wajitolea 940 wamehamasishwa kusaidia katika maandalizi na shughuli za uokoaji. Alisema maeneo ya ibada yako tayari kutumika kama vituo vya uokoaji na shughuli za dharura kuanzia Oktoba 2026 hadi Machi 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Kituo kipya cha huduma za uwekezaji Nyali kufaidi Pwani

Benki ya Standard Chartered imefungua kituo kipya cha huduma za kifedha cha Priority Centre katika eneo la Nyali, Mombasa, hatua inayolenga kuwahudumia wateja wenye uwezo mkubwa wa kifedha katika eneo la Pwani.   Kituo hicho kitatoa huduma maalumu za ushauri kuhusu uwekezaji, upangaji wa mali, ufadhili, uhifadhi wa utajiri na mipango ya kurithisha mali  vizazi vijavyo. Benki hiyo imesema hatua hiyo inalenga kuwaleta karibu wananchi wa Pwani na fursa za uwekezaji wa kimataifa kupitia mtandao wake mkubwa duniani. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo,Birju Sanghrajka, Mkurugenzi Mkuu wa Standard Chartered Kenya, alisema Mombasa imeendelea kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi nchini kutokana na ukuaji wa biashara, utalii, usafirishaji na viwanda. Alibainisha kuwa uchumi wa kaunti hiyo una thamani ya zaidi ya Sh700 bilioni, jambo linaloongeza mahitaji ya huduma za kifedha za hali ya juu. Kwa upande wake,  Edith Chumba,  Mkuu wa Huduma za Utajiri wa Standard Chartered Kenya na Afrika Mashariki, alisema wateja wengi wanahitaji ushauri unaovuka mipaka ya uwekezaji wa kawaida ili kuwasaidia kujenga, kuhifadhi na kuhamisha utajiri wao kwa vizazi vijavyo. Kauli  hiyo pia ilionyesha kuwa Mombasa inaendelea kuimarika kama kitovu cha biashara na uwekezaji. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, Bandari ya Mombasa ilihudumia tani milioni 22.3 za mizigo, huku tani 566,400 zikisafirishwa kwa reli. Aidha, zaidi ya wageni wa kimataifa 96,700 waliwasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mombasa katika miezi minne ya kwanza ya mwaka huo. Kituo kipya cha Nyali kinaongeza uwepo wa huduma za Priority Banking za Standard Chartered nchini Kenya, huku benki hiyo ikilenga kupanua huduma zake kwa wateja wenye utajiri mkubwa nje ya Nairobi na kuwapa fursa za kifedha kutoka shirika la kimataifa

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Sifuna ngangari licha ya misukosuko ya kupata chama

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anakabiliwa na shinikizo la kupata chama atakachotumia kuwania urais katika uchaguzi wa 2027, huku pia akishughulikia tofauti za kisiasa ndani ya vuguvugu la Linda Mwananchi. Timu yake iko katika Mahakama ya Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT), ikipinga uamuzi wa kuhifadhi jina la "Linda" kwa mtu mwingine. Wakati huo huo, baadhi ya viongozi wa upinzani wanamtaka Bw Sifuna awe mgombea mwenza wa kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, katika uchaguzi huo. Hata hivyo, ndani ya Linda Mwananchi kuna viongozi wenye mipango tofauti ya kisiasa, hali inayotishia umoja wa vuguvugu hilo. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesajili The Mwananchi Party (TMP), huku Mbunge wa Saboti Caleb Amisi akiondoka na kuunda People's Renaissance Movement (PRM). Bw Sifuna pia ameingia kwenye mzozo na Bw Musyoka baada ya kiongozi huyo kuhifadhi jina la The Ukombozi Alliance (TUA) kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP). ORPP ilikataa ombi la upande wa Bw Sifuna kubadili jina la United Democratic Party (UDP) kuwa Ukombozi People's Party (UPP), ikisema jina hilo linafanana na TUA. Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema suala la tarehe ya Oktoba 15 iliyowekwa na IEBC halimaanishi Bw Sifuna lazima awe tayari na chama kufikia siku hiyo. Alisema tarehe muhimu kisheria ni Februari 2027, wakati wagombea watapaswa kuwa wanachama wa chama kwa angalau miezi sita kabla ya uchaguzi. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya alisema timu hiyo tayari imekubaliana kuhusu chama kitakachotumiwa na Bw Sifuna na kwamba kitazinduliwa Oktoba 3. Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka alisema maandalizi ya uzinduzi yanaendelea na akakanusha madai kwamba Bw Sifuna atakuwa mgombea mwenza wa Bw Musyoka. Alisema mazungumzo pia yanaendelea na chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachohusishwa na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kuhusu uwezekano wa ushirikiano. Mbunge wa Funyula Oundo Midenyo alisema licha ya kushindwa kupata jina la Ukombozi, Linda Mwananchi itaendelea na mipango yake na Bw Sifuna atasalia kuwa mgombea wake wa urais. Alisema chama kipya kitazinduliwa kikiwa na nembo na rangi zinazohusishwa na Linda Mwananchi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Tunataka hivi: Wadau wa elimu wapendekeza mabadiliko makubwa katika Mswada wa elimu 2026

WADAU wa elimu wanataka mabadiliko makubwa katika Mswada wa Elimu ya Msingi wa 2026, ikiwemo kuimarishwa kwa ushiriki wa wazazi, mfumo wa elimu wa 2-6-3-3 kukitwa katika sheria na serikali kubeba kikamilifu gharama ya elimu ya msingi. Mswada huo unapendekeza kuchukua nafasi ya sheria iliyopo kuhusu elimu ya msingi na unahusu usimamizi wa shule, ufadhili, ustawi wa wanafunzi, walimu, ubora wa elimu na data za elimu. Katika mapendekezo yao kwa Bunge kuhusu miswada ya Elimu ya Msingi na Elimu ya Juu, Uteuzi na Ufadhili wa Wanafunzi ya 2026, wadau pia wanataka wazazi wapewe mamlaka zaidi kisheria na mfumo wa usimamizi wa vifaa vya kufunza ufanyiwe mabadiliko. Kundi la Elimu Bora Working Group (EBWG) limehoji sababu za kuwasilisha  miswada hiyo kabla ya sera mpya ya kitaifa ya elimu kuidhinishwa. Kundi hilo linataka mfumo wa 2-6-3-3 — miaka miwili ya elimu ya chekechea, sita ya msingi, mitatu ya sekondari msingi na mitatu ya sekondari pevu — uwekwe wazi kwenye sheria. Linasema kuacha mfumo huo uamuliwe kupitia kanuni kunaweza kupatia serikali ijayo nafasi ya kubadilisha mfumo wa elimu bila kuhitaji sheria mpya. EBWG pia inataka vigezo vya kuwaweka wanafunzi katika mikondo ya shule ya upili viwekwe wazi, ikiwemo matokeo, maslahi, uwezo na hatua za kuwasaidia wanafunzi kutoka makundi yaliyotengwa. Kuhusu ufadhili, kundi hilo linataka serikali iwajibike kikamilifu kugharamia miundomsingi, vifaa vya kufunza, chakula, usafi na mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu. Linasema mianya inayoruhusu shule kutoza "ada za ziada" inaweza kutumiwa kurejesha ada kwa jina jingine. Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA) nacho kinataka kitambuliwe kikamilifu kisheria na kupewa uwezo wa kumiliki mali, kuajiri wafanyakazi, kuendesha akaunti na kushtaki au kushtakiwa kwa jina lake. NPA pia kinataka miundo yake ya uwakilishi kuanzia shuleni hadi kitaifa ihifadhiwe na neno PTA libadilishwe kuwa Parents Associations. Shirika la Education Stakeholders Association of Kenya (ESAK) limependekeza pia lipewe nafasi ya kuteua mwakilishi katika kila Bodi kati ya 47 za Elimu za Kaunti. ESAK linasema wadau wengi wa elimu wameachwa nje ya bodi hizo licha ya kuwa na mchango muhimu katika usimamizi wa elimu ya msingi. Kuhusu elimu ya juu, EBWG inataka serikali iwafadhili kikamilifu wanafunzi na wanafunzi wa mafunzo ya ufundi, huku ufadhili huo ukijumuisha karo, malazi, chakula, vifaa, usafiri, afya na utafiti. Pia linataka mikopo, ruzuku, ufadhili wa masomo na basari zitofautishwe wazi na wanafunzi waendelee kupata ufadhili hadi watakapokamilisha masomo yao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 24 Sep 2026 06:00:58

Kindiki asihi mlima kumwamini aupeleke 'canaan'

NAIBU wa Rais Kithure Kindiki amewaomba wapiga kura wa Mlima Kenya wamwamini kuwaongoza katika mazungumzo ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Prof Kindiki alisema eneo hilo linahitaji umoja na ajenda ya maendeleo ili kupata manufaa zaidi kisiasa na kiuchumi. Akizungumza Maragua alipokagua ujenzi wa barabara ya Gwathamaki-Mbombo yenye urefu wa kilomita 16 kwa thamani ya Sh1 bilioni, Prof Kindiki alisema Mlima Kenya unapaswa kuingia katika uchaguzi wa 2027 ukiwa umeungana. "Mlima ni mmoja. Ajenda ni maendeleo. Thamani ni mazungumzo ya pamoja yanayolenga mwananchi bila kupoteza mwelekeo wa miradi ya maendeleo. Niaminini niwafanyie mazungumzo. Nia yangu ni ustawi wa watu wetu na utulivu wa taifa," alisema. Alisema wakosoaji wa Rais William Ruto wanaodai kuwa aliahidi mengi hawatafanikiwa, akisisitiza kuwa serikali itaonyesha matokeo kupitia miradi ya maendeleo. Prof Kindiki alizungumza siku nne baada ya kundi la wazee wa Mlima Kenya kumteua kuwa msemaji mkuu wa eneo hilo kuelekea uchaguzi wa 2027. Hata hivyo, uteuzi huo umezua mgawanyiko miongoni mwa wazee, hasa upande wa magharibi wa Mlima Kenya. Mlezi wa Kiama Kia Ma, Kung'u Muigai, na mwenyekiti wa Baraza la  Wazee la Kikuyu, Wachira Kiago, wamekataa kutambua mkutano wa Kirigiti Stadium, Kiambu, wakisema haukuwa na uhalali wala ushawishi unaodaiwa. Profesa Kindiki aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kuepuka siasa za hisia na badala yake kuzingatia utawala na maendeleo. Alisema pia eneo hilo halipaswi kujitenga kisiasa, bali linapaswa kushirikiana na Wakenya wengine katika kutafuta mustakabali bora wa nchi. Naibu Rais alisema serikali imetenga Sh56 bilioni kujenga takriban kilomita 1,200 za barabara za lami katika Kaunti ya Murang'a. Alisema wakulima pia wananufaika kutokana na ongezeko la bei za mazao, akitaja kahawa ambayo bei yake imeongezeka kutoka Sh50 hadi Sh130 kwa kilo na maziwa kutoka Sh35 hadi Sh50 kwa lita. Alisema bei ya mbolea imeshuka kutoka Sh7,000 hadi Sh2,000 kwa gunia, huku mbegu ya mahindi iliyothibitishwa ikishuka kutoka Sh300 hadi Sh150 kwa kilo. Prof Kindiki pia alitaja miradi ya umeme, masoko ya mazao, nyumba za gharama nafuu, mabweni ya wanafunzi na vituo vya ICT miongoni mwa miradi inayoendelea Murang'a.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 24 Sep 2026 05:00:48

Mbunge afichua ODM ilivyozima nyota ya PAA ya Kingi

AFISA wa zamani wa ngazi ya juu katika chama cha Spika wa Seneti Amason Kingi, Pamoja African Alliance (PAA), amefichua matukio yaliyopelekea chama hicho kuamua hakitakuwa na wagombeaji katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Mbunge wa Ganze, Bw Kenneth Tungule, ambaye alikuwa katibu mkuu wa chama hicho, amelaumu siasa za ushirikiano wa ODM na UDA kwa kudhoofisha PAA. Kulingana naye, baadhi ya viongozi wa Pwani walimshinikiza Rais William Ruto kukivunja chama hicho baada ya kuhisi wangekumbwa na ushindani mkali kwa vile PAA ilikuwa imeanza kuvutia wanasiasa wenye ushawishi. Chama hicho kilitangaza uamuzi wake usio wa kawaida Machi, huku Bw Kingi akisisitiza kuwa chama hicho hakikuvunjwa, bali hakitawasilisha wagombea katika uchaguzi ujao. "Rais Ruto hakushinikiza kuvunjwa kwa PAA, kama watu wengi wanavyodai. Rais alikuwa akipokea shinikizo kubwa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa eneo hili, hasa viongozi waliohisi kuwa PAA ilikuwa ikiingia katika ngome yao. Unajua ni chama gani ninachomaanisha. Kwa sababu Pwani imekuwa ngome ya chama fulani kwa miongo kadhaa," alisema Bw Tungule katika mahojiano ya redio. Baadhi ya maafisa wake waliondoka na kuunda chama kingine kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Leba, Bw Kazungu Kambi. Wanasiasa kadha waliojiunga na chama hicho, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa, walilazimika kujipanga upya. Bi Jumwa, ambaye ana azma ya kuwania ugavana, alikuwa ameondoka UDA baada ya kubaini kuwa viongozi wa chama hicho Kilifi walikuwa wakimpigia debe Gavana Gideon Mung'aro wa ODM. Baadaye alirejea UDA kabla ya kuhama tena kutafuta chama kingine upande wa upinzani. Katika mwaka wa 2022, PAA ilishinda viti vitatu vya ubunge, kupitia kwa Bw Tungule, Bw Gonzi Rai wa Kinango na Anthony Kenga wa Rabai, pamoja na viti kadhaa vya udiwani. Pwani imekuwa ngome ya ODM kwa muda mrefu, ambapo aliyekuwa kiongozi wa chama hicho, hayati Raila Odinga, alikuwa na ushawishi mkubwa. Chama hicho kinashinikiza ugawaji wa maeneo ya kisiasa kama sehemu ya makubaliano ya kabla ya uchaguzi na UDA, na uwepo wa vyama vidogo vya Kenya Kwanza vinavyowasilisha wagombea katika maeneo yanayochukuliwa kuwa ngome zake ungeathiri nia hiyo. Mbunge wa Ganze alisema maafisa wa PAA walisafiri hadi Nairobi kukutana na Rais na kutoa hoja dhidi ya kuvunjwa kwa chama hicho. "Tulipokutana naye, tulimweleza jinsi tulivyohisi kuhusu kuvunjwa kwa chama. Tulimwambia kuwa hatua hiyo ingeenda kinyume na maslahi yake. Lakini msukumo kutoka upande mwingine ulikuwa mkubwa zaidi," alisema mbunge huyo wa muhula wa kwanza. Bw Tungule alisema aliendelea kupinga kuvunjwa kwa chama hicho akiwa katibu mkuu, lakini akatambua kuwa maafisa wengine wa chama walikuwa tayari wamekubali uamuzi huo. "Rais angepata kura nyingi zaidi kitaifa. Watu wengi wangetoka kuunga mkono wagombea wao, na mwishowe, tungekusanya kura nyingi zaidi kwa urais," alisema. Mbali na Bi Jumwa, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo pia alikuwa amejiunga na PAA. Bw Mbogo, ambaye anapanga kuwania ugavana wa Mombasa, sasa amejiunga na chama cha Jubilee kilicho upande wa upinzani. Awali, Bw Kingi aisema Rais Ruto alikuwa amehisi mgawanyiko wa vyama ndani ya Kenya Kwanza unaweza kuathiri uwezo wa kushinda viti vingi uchaguzini.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 24 Sep 2026 04:00:58

Jubilee hakukaliki Kioni na Matiang'i waking'ang'ania kiti cha Kenyatta

Mabadiliko ya uongozi katika Chama cha Jubilee yamezua vita vipya vya kuwania usukani wa chama hicho, huku uteuzi wa Dkt Fred Matiang'i kushika hatamu ukishindwa kuzima mjadala kuhusu nani anafaa kukiongoza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Sasa mchuano huo unaelekea  Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC), ambapo aliyekuwa mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu, amesema wajumbe ndio wanaopaswa kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo Dkt Matiang'i ataendelea kuwa kiongozi wa chama au nafasi hiyo ichukuliwe na Naibu Kiongozi wa Chama, Jeremiah Kioni. Bw Kioni Jumatano alikataa kueleza wazi msimamo wake kuhusu iwapo atampinga Dkt Matiang'i katika mkutano huo. "Tunahitaji mahojiano maalum," alisema Bw Kioni alipohojiwa kuhusu hatua yake ya kukosa kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu  la Jubilee (NEC) kilichofanyika Jumanne na iwapo atachuana na Dkt Matiang'i kwenye NDC. Kimya chake kilijiri siku moja baada ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kukabidhi uongozi wa chama kwa Dkt Matiang'i, hatua ambayo bado inasubiri kuidhinishwa rasmi na wajumbe katika NDC. Kwa mujibu wa maafisa wa chama, ni Dkt Matiang'i na Beatrice Gambo pekee, ambaye ni Naibu Kiongozi wa Chama anayesimamia mikakati, waliohudhuria hafla hiyo kutoka makundi mawili ya manaibu viongozi wa chama. Kutokuwepo kwa Bw Kioni kulivutia hisia, hasa kwa kuzingatia kwamba amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa kiongozi wa Jubilee anafaa kuchaguliwa na wajumbe badala ya kuteuliwa kupitia makubaliano ya viongozi wa juu. Mrengo wake sasa unatarajiwa kuongeza juhudi za kushawishi wajumbe kabla ya NDC inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba. Hali hiyo imezua mapambano ya  kipekee ya kisiasa ambapo Dkt Matiang'i ni mgombea wa urais wa Jubilee na wakati huohuo kiongozi wa muda wa chama, huku Bw Kioni akiendelea kuhudumu kama naibu kiongozi mwenye ushawishi ndani ya chama. Na Bw Wambugu ameweka wazi msimamo wake. "Matiang'i hakuwa chaguo langu la kwanza kuwa kiongozi wa chama, ingawa ndiye mgombea wangu ninayempendelea  wa  urais. Mimi nilimpendelea Kioni. Lakini ninaweza kukubali uamuzi huu hadi NDC ambayo Uhuru amesema itafanyika karibuni, halafu tuone wajumbe watasema nini," alisema. Msimamo huo unatenganisha nafasi mbili ambazo zimeonekana kufungamana ndani ya Jubilee: uongozi wa chama na uteuzi wa mgombea wa urais. Jubilee ilimuidhinisha Dkt Matiang'i kuwa mgombea wake wa urais mnamo Oktoba mwaka jana, wakati ambao Bw Kioni alikuwa Katibu Mkuu wa chama. Dkt Matiang'i pia aliteuliwa kuwa Naibu Kiongozi wa Chama. Hatua hiyo ilionekana kumweka Dkt Matiang'i katikati ya juhudi za kufufua chama hicho. Hata hivyo, azma ya Bw Kioni kutwaa uongozi wa chama imeibua kitovu kingine cha mamlaka. Katibu mkuu huyo wa zamani wa chama amekuwa akisisitiza kuwa kiongozi wa Jubilee anapaswa kuibuka kupitia mchakato wa NDC badala ya kukabidhiwa madaraka moja kwa moja. Kutokana na hali hiyo, Jubilee sasa inakabiliwa na swali gumu: Je, mgombea wa urais wa chama anapaswa kuwa kiongozi wa chama moja kwa moja, au wajumbe ndio wanafaa kuamua ni nani atakayeshikilia nafasi hiyo? Bw Wambugu, ambaye amehusika katika migogoro kadhaa ya ndani ya Jubilee, ameibuka kama mmoja wa watu wanaopinga vikali dhana kwamba Dkt Matiang'i anapaswa kurithi moja kwa moja nafasi ya Bw Kenyatta. Katika barua yake ya wazi kwa Dkt Matiang'i Jumanne, alimpongeza kwa kuaminiwa kushika usukani wa chama, lakini akasisitiza kuwa uamuzi huo bado unategemea idhini ya NDC. Aliwataka viongozi wapya wa chama kutoa ratiba wazi ya mkutano huo na hatua zitakazofuatwa kabla yake, ishara kwamba vita vya kuwania ushawishi ndani ya chama vinaweza kuwa vikali. "NDC inatoa fursa ya kutatua masuala yaliyosalia kuhusu uongozi, kurekebisha miundo ya chama panapohitajika, kufanya upya mamlaka ya viongozi wa kitaifa na kuwapa wanachama nafasi ya kuamua mwelekeo wa chama chao kupitia wajumbe wao," alisema. Aidha, alionya dhidi ya maamuzi yasiyofuata taratibu rasmi za chama, akisema masuala yanayowahusu wanachama na wanaotaka kugombea yanafaa kushughulikiwa kupitia vyombo vinavyotambulika kikatiba. Msimamo huo unaendana na hoja ya awali ya Bw Kioni kwamba Jubilee ni chama cha kitaifa na viongozi wake wanapaswa kuchaguliwa na wajumbe. NDC sasa imeibuka kuwa uwanja mkuu wa mapambano ya kisiasa ndani ya Jubilee wakati chama hicho kinajaribu kurekebisha miundo yake kufuatia miezi kadhaa ya migogoro ya ndani na kesi mahakamani. Jaribio kubwa la kwanza kwa Dkt Matiang'i linaweza kuwa mgogoro ambao haujatatuliwa kuhusu nafasi ya Katibu Mkuu wa chama. Hivi majuzi, Mahakama ya Migogoro ya Vyama vya Kisiasa ilibatilisha uteuzi wa Moitalel Ole Kenta kama Katibu Mkuu wa Jubilee, ikisema hakutimiza masharti ya uanachama wakati wa uteuzi wake. Ingawa Jubilee imepinga uamuzi huo na kuahidi kutumia njia za kisheria kuupinga, Bw Wambugu amesema chama kinafaa kurekebisha utaratibu uliotumika badala ya kuendeleza mzozo huo. "Suala lililo mbele yetu si Kenta kama mtu binafsi. Ni mchakato wa kujaza nafasi ya Katibu Mkuu," alisema. Kwa Dkt Matiang'i, mgogoro huo ni mtihani wa mapema wa uwezo wake wa kurejesha imani ya wanachama katika taasisi za chama akijiandaa kwa NDC na uchaguzi wa 2027. Katika hafla ya Jumanne, Bw Kenyatta na Dkt Matiang'i walisisitiza umuhimu wa umoja ndani ya chama na kuwataka wanachama kuacha kutegemea mahakama kutatua migogoro ya ndani. "Tusiendelee kurudisha chama nyuma kupitia kesi za mahakamani. Tuungane na vyama vyenye malengo sawa," alisema Bw Kenyatta. Dkt Matiang'i naye alitoa wito wa kutatua migogoro kupitia miundo ya chama. "Tafadhali tusikimbilie mahakamani. Tuna mifumo ya kutatua matatizo yetu ndani ya chama," alisema. Hata hivyo, vita vya Jubilee si kuhusu nyadhifa pekee. Chama hicho bado kina mtandao wa kitaifa wa kisiasa, chapa inayotambulika na ufadhili wa umma. Kwa mwaka wa kifedha wa 2026/27, Jubilee imetengewa Sh128.86 milioni kutoka Hazina ya Vyama vya Kisiasa. Ingawa kiwango hicho kimeshuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ambayo Jubilee ilikuwa mojawapo ya vyama vikuu nchini, udhibiti wa chama bado una umuhimu mkubwa. Udhibiti huo huamua nani atasimamia miundo ya chama, wanachama, michakato ya uteuzi wa wagombea na nafasi ya chama katika mazungumzo ya miungano kuelekea uchaguzi wa 2027. Ndiyo maana ushindani kati ya Dkt Matiang'i na Bw Kioni unaweza kuwa muhimu zaidi kadri NDC inavyokaribia. Ingawa Bw Kenyatta ameachia rasmi uongozi wa chama, amesema ataendelea kuwa mwanachama na mshauri mwandamizi. Hata hivyo, uwepo wake una maana kwamba mabadiliko hayo hayawezi kuonekana tu kama kubadilishwa kwa viongozi. Bado ana ushawishi mkubwa ndani ya historia na mtandao wa kisiasa wa Jubilee.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 24 Sep 2026 03:00:14

Jiandaeni vya kutosha El Nino huja na magonjwa, kaunti zaonywa

Katika maeneo mbalimbali nchini, Wakenya wanaangalia anga kwa hofu na matumaini, kama walivyofanya wakati wa misimu mikubwa ya El Niño ya 1997, 2015 na 2023. Hata hivyo, mwaka huu tahadhari imeongezeka baada ya Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya (KMD) kutangaza kuwa kuna uwezekano wa asilimia 81 wa kutokea kwa El Niño kali, huku kukiwa na asilimia 97 ya mvua  kuendelea hadi miezi ya kwanza ya mwaka 2027. Kwa Wizara ya Afya, utabiri huo si jambo la kupuuzwa. Katibu wa Afya ya Umma, Mary Muthoni, amewaandikia magavana wote wa kaunti akiwatahadharisha kujiandaa kukabiliana na magonjwa kama kipindupindu, homa ya matumbo, malaria na homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever), ambayo huongezeka wakati wa mafuriko. Wizara hiyo ilikumbusha kuwa katika msimu wa El Niño wa 2023-2024, watu 175 walifariki dunia, 40 wakatoweka na 242 kujeruhiwa. Zaidi ya watu 384,000 walihamishwa makwao na kuwekwa katika kambi 170 za muda. Aidha, vituo 64 vya afya viliathiriwa na kushindwa kutoa huduma kutokana na mafuriko. Bi Muthoni alisema kaunti zote zinapaswa kuwa tayari kwa kiwango cha chini, huku zile zinazokabiliwa na hatari kubwa ya mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa na utapiamlo zikichukua hatua za haraka zaidi. Kaunti zilizotajwa kuwa na hatari kubwa ya mafuriko ni pamoja na Mandera, Wajir, Marsabit, Garissa, Kitui, Makueni, Machakos, Lamu, Kilifi, Kwale, Tana River, Taita Taveta na Mombasa. Maeneo mengine yaliyo katika hatari ni Budalang'i, Kano na Tana Delta. Ripoti hiyo pia imeonya kuhusu hatari ya homa ya Bonde la Ufa katika kaunti za Marsabit, Wajir, Isiolo, Mandera na Garissa, hasa maeneo yaliyo karibu na mito na mabwawa yanayofurika. Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Utabiri wa Hali ya Hewa, David Koros, alisema mvua ya Oktoba hadi Desemba itachochewa na mchanganyiko wa El Niño na hali ya joto katika Bahari ya Hindi, jambo linalotarajiwa kuongeza kiwango cha mvua nchini. Wakati huohuo, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limesema linajiandaa kwa hali ambayo huenda ikawa mbaya zaidi kuliko misimu iliyoshuhudiwa katika miongo miwili iliyopita. Mkurugenzi wa Afya ya Umma, Dkt Stephen Muleshe, alisema changamoto kubwa inayotarajiwa ni milipuko ya magonjwa yanayoenezwa kupitia maji machafu, majeraha yatokanayo na mafuriko na kuvurugika kwa huduma za lishe na afya. Msimu mbaya zaidi wa El Niño nchini Kenya unasalia ule wa 1997-1998, uliosababisha vifo vya takriban watu 2,000, kuathiri zaidi ya watu milioni 1.5 na kusababisha hasara ya mabilioni ya shilingi kutokana na uharibifu wa barabara, madaraja, mifugo na miundombinu mingine. Wataalamu sasa wanaonya kwamba ikiwa maandalizi hayatatiwa maanani, mvua inayotarajiwa zinaweza kuathiri afya, usafiri, kilimo na uchumi kwa kiwango kikubwa katika miezi ijayo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 24 Sep 2026 02:00:17

Amerika yamezea mate madini ya Kenya bila kuficha

Amerika imeongeza hamu yake katika madini muhimu ya Kenya wakati ambapo serikali ya Rais William Ruto inataka kuendeleza uwezo wa kuchakata madini ndani ya nchi badala ya kuyauza nje yakiwa ghafi. Suala hilo lilijitokeza kwa uzito wakati wa mkutano kati ya Rais Ruto na Waziri wa Masuala ya Kigeni  wa Amerika, Marco Rubio, Septemba 21, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, viongozi hao wawili walijadili diplomasia ya biashara pamoja na amani na usalama wa kikanda, huku madini muhimu yakitajwa kama eneo kuu la ushirikiano wa kiuchumi. Waziri huyo alitafutia kampuni za Amerika nafasi ya kushiriki katika sekta hiyo. "Walizungumza kuhusu jinsi fursa zilizopo katika madini muhimu nchini Kenya zinavyoweza kuweka nchi kama mhusika muhimu katika sekta hiyo huku zikifungua nafasi kwa kampuni za Amerika kuongeza thamani ya bidhaa hizo," alisema msemaji wa Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, Tommy Pigott. Majadiliano hayo yamejiri chini ya wiki mbili baada ya afisa mkuu wa Amerika kusema kuwa Washington iko tayari kusaidia Kenya kuendeleza viwanda vinavyohusiana na migodi ya madini muhimu. Hatua hizi zinaashiria kuongezeka kwa maslahi ya kibiashara ya Amerika katika madini ya Kenya na Afrika kwa jumla huku ikitafuta kupunguza uwezo wa China. Mapema mwezi huu, Naibu Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika anayeshughulikia masuala ya Afrika, Frank Garcia, alisema wanataka kampuni za Amerika kuwekeza katika uchakataji wa madini, mafunzo kwa wafanyakazi, uhamishaji wa teknolojia na viwanda vinavyoweza kuibuka kutokana na hazina za madini nchini Kenya. Bw Garcia alisema utawala wa Rais Donald Trump uko tayari kusaidia Kenya kujenga mitambo ya usindikaji wa madini na kusisitiza kuwa kampuni za Amerika zinataka kushiriki katika kuongeza thamani ya madini badala ya kuyachimba na kuyasafirisha nje moja kwa moja. Mwelekeo huo mpya umefanya madini ya Kenya kuwa na mvuto mkubwa kimataifa. Katika eneo la Pwani, madini adimu kama niobium yaliyopo katika Kilima cha Mrima, Kaunti ya Kwale, yamevutia kampuni kadhaa za kimataifa huku Kenya ikitafakari jinsi ya kuendeleza rasilimali hiyo. Madini mengine kama titanium, chromite, coltan na manganese pia yamegunduliwa katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa Pwani, ikiwemo kaunti za Tana River na Kilifi. Madini ya adimu hutumika katika utengenezaji wa bidhaa nyingi za teknolojia ya hali ya juu, huku niobium ikitumika kutengeneza vifaa vinavyotumika katika sekta za anga, silaha na matumizi mengine ya viwandani. Mbali na Amerika, kampuni za Australia pia zimeonyesha nia ya kufanya utafiti wa madini katika Kilima cha Mrima. Eneo hilo linakadiriwa kuwa na akiba ya madini adimu yenye thamani ya takriban Sh8 trilioni na niobium yenye thamani ya takriban Sh4.5 trilioni. Waziri wa Madini Hassan Joho, ambaye ni sehemu ya ujumbe wa Kenya mjini New York, alisisitiza msimamo wa serikali wakati wa mkutano wa ngazi ya juu wa Africa Minerals Strategy Group kuhusu maendeleo ya madini muhimu barani Afrika. "Msimamo wa Kenya uko wazi. Hatuwezi kukubali kuondolewa kwa madini yetu bila kuongeza thamani hapa nchini. Madini yetu, lithiamu, shaba na niobium lazima yasafishwe na kuchakatwa nchini kabla ya kusafirishwa nje ili manufaa yaongezeke, teknolojia ihamishwe na ajira za kitaalamu zibaki Afrika," alisema Joho. Aliongeza kuwa ongezeko la mahitaji ya madini muhimu limeweka Afrika katika nafasi ya kipekee ndani ya uchumi wa kimataifa wa madini na kupatia fursa ya kuwa mhusika mkuu katika mifumo ya usambazaji duniani. Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika ilisema mjadala kuhusu madini muhimu ni sehemu ya uhusiano mpana wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili, ikitaja Kenya kama mshirika muhimu asiye mwanachama wa NATO na wa biashara anayekua kwa kasi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 11:22:17

Wachezaji wa Harambee Stars wagoma kufanya mazoezi kulalamikia kutolipwa posho

Wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, wamesusia mazoezi kuelekea mechi yao ya kwanza ya Kundi D ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 dhidi ya Eritrea, iliyopangwa kuchezwa Jumamosi katika Uwanja wa Nyayo. Taarifa zinaonyesha kuwa kikosi hicho kiliripoti kambini jijini Nairobi Jumanne, lakini wachezaji walikataa kufanya mazoezi wakidai kulipwa marupurupu yao pamoja na kuboreshwa kwa maslahi wakichezea timu ya taifa. Mkuu wa Miradi na Timu za Taifa katika Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Athanus Obango, alisema Jumatano kuwa wachezaji wanadai posho za mechi za Senegal na Lesotho ambazo bado hawajalipwa. "Suala ni kwamba posho za mechi ya Senegal zimechelewa sana kulipwa, na pia wanataka posho za mechi ya Lesotho. Kila mchezaji anadaiwa takriban Sh80,000," alisema Obango. Aliongeza kuwa jukumu la kulipa posho za wachezaji ni la serikali na si FKF, huku akielezea matumaini kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi haraka. "Baadhi ya wanaogoma kwa sasa hawakuwa hata kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Lesotho na Senegal. Wanasema wanaonyesha mshikamano na wenzao," alisema. Mchezaji mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina alisema ni wachache tu katika kikosi cha sasa walioshiriki mechi hizo mbili na wana haki ya kulipwa posho zao. "Hata hivyo, ninavyojua, baadhi yao wanachochewa na watu wa nje wanaotaka kudhoofisha timu ya taifa katika vita vyao dhidi ya uongozi wa FKF. Mimi si sehemu ya mgomo huo," alisema mchezaji huyo. Kenya ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Lesotho Juni 4 na Juni 27 mwaka huu katika Uwanja wa Lukas Moripe mjini Johannesburg, Afrika Kusini, ikitoka sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza kabla ya kupokea kichapo cha 4-1 katika pambano la pili. Mnamo Novemba 8, 2025, Harambee Stars pia ilipokea kichapo cha mabao 8-0 kutoka kwa Senegal katika mechi nyingine ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mardan Sports Complex mjini Antalya, Uturuki. Kocha wa Harambee Stars, Benni McCarthy wa Afrika Kusini, anatarajiwa kuzungumza na wanahabari baadaye Jumatano kuhusu mgomo huo wa wachezaji. Wiki iliyopita McCarthy alitangaza kikosi cha wachezaji 24, wengi wao wakicheza soka ya kulipwa nje ya nchi, kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Eritrea. Baada ya mechi ya Eritrea, Kenya itasafiri kucheza dhidi ya Guinea mjini Conakry Oktoba 1. Timu nyingine katika kundi hilo ni Afrika Kusini. Wakati huo huo, Eritrea iliwasili nchini Jumanne na imekuwa ikifanya mazoezi katika Uwanja wa Police Sacco. Kenya, ambayo ni mwenyeji mwenza wa Afcon 2027, tayari imejihakikishia nafasi ya kushiriki fainali hizo na inashiriki mchujo huo ili kudumisha kiwango cha ushindani na utimamu wa wachezaji wake. Si mara ya kwanza kwa wachezaji wa Harambee Stars kugoma kutokana na malipo ya posho. Tukio maarufu lilitokea mwaka 2005 wakati timu hiyo iligoma kusafiri kwenda Kigali, Rwanda, kwa michuano ya Kombe la Cecafa Senior Challenge kutokana na kutolipwa marupurupu yao. Ingawa suala hilo lilitatuliwa baadaye, timu iliondolewa katika mashindano hayo baada ya kuchelewa kuwasili.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 08:51:28

Wawili wafariki, sita wajeruhiwa basi likigonga lori Kwale

Watu wawili wamethibitishwa kufariki dunia huku wengine sita wakijeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Mghalani kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Tarafa Ndogo ya Samburu, Lydia Mambo, basi la Dreamline lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi kuelekea Mombasa liligonga lori lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara kati ya Mackinnon na Taru, Kaunti ya Kwale. Bi Mambo alithibitisha kuwa mmoja wa waliofariki alikuwa abiria aliyekwama ndani ya basi hilo. "Lori hilo lilikuwa limeharibika barabarani na dereva wake hakuwa ameweka alama zozote za tahadhari, jambo ambalo huenda lilichangia ajali hiyo kulingana na matokeo yetu ya awali ya uchunguzi," alisema. Maafisa wa polisi walifika haraka eneo la tukio na kuwaokoa abiria, huku majeruhi wakipelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi. Kwa mujibu wa Bi Mambo, eneo la tukio tayari limeshughulikiwa na magari hayo mawili kuvutwa hadi Kituo cha Polisi cha Taru huku uchunguzi ukianza. Afisa wa Utekelezaji wa Sheria za Trafiki katika Ukanda wa Pwani, Asha Wario, amewatahadharisha madereva wanaotumia barabara kuu yenye shughuli nyingi ya Mombasa-Nairobi kuwa waangalifu na kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni za trafiki. "Ningependa kuwasihi madereva wawe waangalifu kwa sababu nyingi ya ajali hizi hutokea asubuhi. Hii ina maana kuwa hutokea kutokana na mwonekano hafifu unaosababishwa na manyunyu ya mvua za asubuhi," alisema Bi Wario. Alisisitiza kuwa madereva watakaopatikana wakikiuka sheria za trafiki watafikishwa mahakamani, akiongeza kuwa juhudi pia zinaendelea za kuelimisha madereva wa mabasi na malori kuhusu usalama barabarani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 09:00:46

Hesabu za Gachagua zinavyozidi kuwa ngumu mlimani

Hesabu za kisiasa za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 zinazidi kuwa ngumu kutokana na swali moja muhimu - iwapo ataruhusiwa kugombea au atalazimika kusalia nje ya debe na kujadiliana kisiasa kutoka pembeni. Hatima yake kisiasa inahusishwa moja kwa moja na mapambano yake ya kisheria kufuatia kutimuliwa kwake afisini  Oktoba 2024. Ingawa Mahakama Kuu ilikataa kufutilia mbali uamuzi wa Seneti wa kuidhinisha kuondolewa kwake madarakani, iliamua kuwa baadhi ya haki zake za kikatiba zilikiukwa. Gachagua amekata rufaa. Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, suala hilo si kuhusu uwezo wake wa kugombea tu, bali pia kuhusu ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya, ambako amekuwa akijijenga kama kinara mkuu wa upinzani dhidi ya Rais William Ruto. Iwapo mahakama haitafungua njia yake ya kugombea, Gachagua atakabiliwa na uamuzi mgumu. Mchambuzi wa siasa Steve Ngari anasema kumuunga mkono mgombea wa upinzani ambaye hana mizizi ya Mlima Kenya kunaweza kupunguza uwezo wake wa kushawishi eneo hilo kuunga mkono muungano huo na pia kudhoofisha nafasi yake ya kujadiliana ndani ya muungano unaoongozwa na viongozi kutoka maeneo mengine. Kwa upande mwingine, akimuunga mkono mwanasiasa mwingine kutoka Mlima Kenya kuwania urais, huenda akasaidia kuibua mpinzani mpya ambaye baadaye atachukua nafasi yake ya ushawishi katika eneo hilo. Mambo yanazidi kuwa magumu kutokana na uwezekano mkubwa wa Naibu Rais Kithure Kindiki kubaki katika tiketi ya Kenya Kwanza kama mgombea mwenza wa Rais Ruto mwaka 2027. Wafuasi wa serikali mlimani wamekuwa wakitumia uwepo wa Profesa Kindiki kama hoja kwamba eneo hilo bado  linawakilishwa katika kazi ya juu serikalini na hivyo halijatengwa kisiasa. Kindiki mwenyewe ameonya kuwa eneo hilo linaweza kushushwa hadhi katika upinzani. Akizungumza katika mikutano ya kisiasa, amesema kuwa baada ya Ruto, nafasi inayofuata ya uongozi wa taifa inaweza kwenda kwa Mlima Kenya, ilhali katika upinzani eneo hilo linaweza kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kupata nafasi kama hiyo. Rais Ruto pia ameonyesha hadharani kumuunga mkono naibu wake, hali inayowapa wapinzani changamoto ya kueleza kwa nini Mlima Kenya unapaswa kujitenga na tiketi ya Ruto-Kindiki. Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema vita vya kisiasa vinavyoibuka si kuhusu nani atakuwa mgombea wa upinzani pekee, bali nani atawakilisha na kujadiliana kwa niaba ya maslahi ya Mlima Kenya. Swali hilo limezidi kuwa tata kutokana na kuibuka kwa wanasiasa kadhaa kutoka eneo hilo wanaotajwa kuwa na uwezo wa kuathiri hesabu za kisiasa za Gachagua. Miongoni mwao ni Seneta wa Nyandarua John Methu, ambaye ni mmoja wa washirika wake wa karibu na Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP). Tangu Gachagua aanze safari yake za kisiasa nje ya nchi, Methu ameonekana kuchukua jukumu kubwa katika shughuli za chama hicho. Kuna minong'ono kwamba Gachagua anaweza kumteua Methu kama sura ya Mlima Kenya katika tiketi ya upinzani iwapo yeye mwenyewe hataidhinishwa kugombea. Hata hivyo, wakili Chris Omore anaonya kuwa kumpandisha hadhi mwanasiasa mwingine kunaweza kuunda kituo kipya cha nguvu za kisiasa ambacho baadaye kinaweza kumpokonya Gachagua ushawishi wake. Mjadala huo pia unaeleza umuhimu wa kiongozi wa chama cha Safina Jimi Wanjigi, ambaye tayari ametangaza nia ya kuwania urais na amekutana mara kadhaa na Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro. Kwa mujibu wa wakili Nelson Osiemo, Wanjigi ni tofauti na Methu kwa sababu tayari anajitokeza kama mgombea wa urais mwenye mtandao wake wa kisiasa wa kitaifa. Ikiwa upinzani hatimaye utachagua mgombea kutoka nje ya Mlima Kenya, Wanjigi anaweza kuwa mgombeaji kutoka eneo hilo. Hilo linaibua swali iwapo Gachagua atamuunga mkono, atashirikiana naye kisiasa au ataendelea kusukuma DCP kama chombo kikuu cha upinzani  Mlima Kenya. Gachagua mwenyewe amesema yuko tayari kumuunga mkono yeyote atakayeshinda mchakato wa uteuzi wa mgombeaji wa upinzani. Lakini si rahis hata. Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ameanzisha chama cha People's Party of Kenya (PPK) na ameanza kampeni ya kitaifa ya kujenga chama hicho. Hatua hiyo imeibua kituo kingine cha ushawishi katika Mlima Kenya. Aidha, juhudi za Gachagua kutaka vyama vya kisiasa vya eneo hilo viungane chini ya DCP zimepata upinzani kutoka kwa viongozi kama Peter Munya, Justin Muturi na Lenny Kivuti, ambao wanasisitiza kuwa vyama vinaweza kushirikiana bila kuvunjwa. Kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua naye anaendelea kuwa moja ya sauti muhimu za kisiasa kutoka Mlima Kenya, huku mgombea wa Jubilee Fred Matiang'i akionekana kuongeza ushindani ndani ya upinzani. Huku viongozi kama Kalonzo Musyoka na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wakitajwa katika tiketi ya  upinzani, swali kuu linasalia jinsi muungano huo utakavyovutia kura za Mlima Kenya bila kumpa mmoja wa viongozi wa eneo hilo nafasi ya juu kwenye tiketi. Kwa Gachagua, huo ndio mtihani mkubwa. Akiidhinishwa kugombea, atawaomba wapigakura wa Mlima Kenya wamuunge mkono moja kwa moja. Lakini akizuiwa, atalazimika kuamua ni nani atakayebeba matarajio ya kisiasa ya eneo hilo. Wachambuzi wanasema ikiwa ataweza kuunganisha maslahi ya Methu, Wanjigi, Nyoro, Karua, Munya na Muturi chini ya mradi mmoja wa upinzani, bado atabaki na ushawishi mkubwa hata bila kuwapo kwenye karatasi ya kura.

read more