T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 28 Sep 2026 16:52:55

Alinihadaa nitamuoa, raia wa Uholanzi amshtaki mwanamke Mkenya, adai Sh2.2 milioni

UHUSIANO wa kimapenzi uliodumu miaka minne kati ya mwanamume raia wa Uholanzi na mwanamke Mkenya umeishia kortini kuhusiana na zawadi ikiwemo Sh2.2 milioni anazosema alituma kujenga boma walilopaswa kuishi pamoja baada ya kufunga ndoa. Hata hivyo, mwanamke  huyo Bi SL anasema pesa hizo alipewa kwa hiari kama zawadi walipokuwa wakichumbiana na kukanusha kuahidi kuolewa na raia huyo wa kigeni, Bw BD, wala kujenga boma naye. Kiini cha mvutano huo kinadaiwa kuwa ahadi ya ndoa ambayo haikutimizwa, mwanamume mwingine kuishi katika nyumba husika, polisi kuhongwa na kupigania kurejeshewa hela. Mgogoro huo umebadilika kutoka uhusiano wa kimapenzi uliotibuka kuwa kesi ya uhalifu ambapo Bi SL anashutumiwa kudanganya na kupata hela kupitia ujanja katika kesi ambapo Bw BD anaitisha kulipwa Sh2.4 milioni kwa jumba la ghorofa tatu kutoka kwa SL eneo la Vikwathani, Bamburi, Mombasa. Mahakama Kuu Ijumaa ilipuuzilia mbali jaribio la SL kusimamisha kesi ya uhalifu, ikiacha mashtaka ya uhusiano, hela na mali kushughulikiwa katika kesi iliyowasilishw mbele ya korti za hakimu. Kulingana na Bi SL, uhusiano ulianza baada ya Bw BD kumfuata kupitia jamaa wa familia kuanzia 2019. Alimwelezea kama raia wa Uholanzi anayezuru Kenya mara moja kwa mwaka. Kuanzia mwishoni mwa 2020 hadi 2023 katikati, alisema BD alimtumia kupitia M-Pesa, aghalabu Sh100, Sh200 au Sh1,000 kwa kadi ya simu au chamcha kama "mpenzi wake mtarajiwa." Alisema Sh70,000 zilitumwa kwa mazishi ya baba yake BD huku fedha nyingine zikitumika kuweka paa nyumba yake Likoni. Alisema walikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza mwishoni mwa 2022. "Korti hii haiwezi kuchukua hatua kwa ushahidi ambapo upande mmoja unasema upo lakini umeamua kutowasilisha," alisema Jaji Ngaah Jairus. Jaji alikanusha hoja kuwa mzozo huo unahusu tu uhusiano uliotibuka au suala la mali. "Iwe pesa zilikuwa zawadi au zilipatikana kupitia ulaghai ndiyo aina ya suala halisi, ambalo ni sharti korti itoe uamuzi kulihusu baada ya kusikiza ushahidi utakaopigwa msasa kupitia kuhoji," alisema jaji.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Mamia kunufaika na mradi wa kiwanda cha Bamburi

KIWANDA kipya cha kuzalisha kemikali ya kuunda saruji kinachojengwa Matuga, Kaunti ya Kwale, kinatarajiwa kuongeza uwezo wa Bamburi Cement kuzalisha kemikali ya Clinker kutoka tani milioni moja hadi milioni 2.6 kwa mwaka. Mradi huo wa Sh250 milioni pia utaongeza uwezo wa kampuni hiyo kuzalisha saruji kutoka tani milioni 1.8 hadi milioni nne kila mwaka, hatua inayolenga kuimarisha sekta ya ujenzi nchini na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa hiyo. Rais William Ruto aliweka jiwe la msingi la mradi huo, uliohudhuriwa na viongozi wa serikali, wawekezaji na viongozi wa eneo hilo. Miongoni mwa waliohudhuria ni Mawaziri Hassan Joho na Salim Mvurya, Mkurugenzi Mkuu wa Amsons Group Edha Nahdi, Gavana wa Kwale Fatuma Achani, Spika wa Seneti Amason Kingi na Mwenyekiti wa Bodi ya Bamburi Cement Dkt John Simba. Akizungumza katika hafla hiyo, Nahdi alisema uwekezaji huo unaonyesha dhamira ya muda mrefu ya Amsons Group katika kukuza uchumi wa Kenya na kuimarisha uzalishaji wa bidhaa nchini. Kwa upande wake, Dkt Simba alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha jamii zinazoishi karibu na mradi zinanufaika na uwekezaji huo. Alitaja mpango wa kuhamisha wakazi wa Kijiji cha Mwachome, ambao ulihusisha pia mafunzo ya usimamizi wa fedha ili kuwasaidia wakazi walioathiriwa kutumia vizuri rasilimali walizopokea. Gavana Achani alitoa wito kwa wakazi wa Matuga na wafanyabiashara wa eneo hilo kushirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo ili wanufaike na fursa za kiuchumi. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuunda zaidi ya nafasi 10,000 za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hususan katika sekta za usafirishaji, uchimbaji wa mawe. Mkurugenzi Mkuu wa Wave 360 Africa, Zedd Mukoya, alisema mradi huo ni fursa kwa vijana wa Kwale kushiriki katika maendeleo ya viwanda katika kaunti yao. "Matumaini yangu ni kwamba siku moja kijana kutoka Kwale ataweza kuutazama kiwanda hicho na kusema, 'Nilisaidia kukijenga na kimenipa mustakabali mzuri katika eneo langu,'" alisema Mukoya Kampuni ya Wave 360 Africa ilihusika na maandalizi na uratibu wa hafla hiyo, ikisimamia miundombinu, uwekaji chapa, itifaki na shughuli za uwanjani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Askofu Wanjiru aishinikiza IEBC ihakikishe uwazi kwenye kura

UPINZANI  nchini umeitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kushughulikia wasiwasi ulioibuliwa na wadau kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027. Mwaniaji wa Ugavana Nairobi Askofu Margaret Wanjiru amesema imani ya wananchi kwa tume hiyo inapungua huku wapigakura wakijiuliza iwapo iko tayari kuendesha uchaguzi, mfumo utakaotumiwa na usahihi wa sajili ya wapigakura. Akizungumza Jumanne baada ya kuzindua makao makuu ya chama cha Kenya Moja Movement Party (KMMP)  katika Barabara ya Kiambu, Bi Wanjiru, ambaye ni kiongozi wa chama hicho, alisema IEBC inapaswa kuwahakikishia Wakenya kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru, wa haki na uwazi. "Tunaitaka IEBC kuonyesha uhuru, kutopendelea upande wowote na kuwa tayari kusimamia uchaguzi mkuu huru, wa haki, wa kuaminika na ulio wazi. Uaminifu wa demokrasia yetu unategemea mchakato wa uchaguzi ambao Wakenya wanaweza kuutegemea," akasema Bi Wanjiru. "Kwa sasa kuna upungufu wa imani nchini. IEBC lazima irejeshe imani hiyo kwa Wakenya," akasema. Alisema tume hiyo inaweza kurejesha imani ya wananchi kwa kuhakikisha kila kura inahesabiwa, wagombeaji wanatendewa kwa usawa na matakwa ya wananchi yanaheshimiwa. Aliongeza kuwa IEBC inapaswa kushughulikia mapema masuala yanayohusu maandalizi ya uchaguzi, uwazi na uadilifu wa mchakato mzima. Matamshi yake yalijiri siku mbili baada ya kiongozi DCP, Rigathi Gachagua, kuipa IEBC hadi Januari 2027 kutatua malalamishi ya upinzani au ikabiliwe na maandamano ya kitaifa. Wakati wa hafla hiyo, Bi Wanjiru alitangaza kuwa chama chake kitahakikisha mchujo unaendeshwa kwa uwazi kinapojitayarisha kushindania viti mbalimbali vya uchaguzi nchini. Pia alimkosoa Gavana Johnson Sakaja, akidai utawala wake haujafanya juhudi za kutosha kuboresha maisha ya wakazi. Alisema akichaguliwa atashughulikia mgao wa maji, mifumo mibovu ya mifereji ya maji, taka zinazotapakaa jijini, msongamano wa magari na hali mbaya ya barabara. "Sisi akina mama ni watu wa usafi na kama ningekuwa gavana wa Nairobi, tusingekuwa na tatizo la taka. Siwezi kuvumilia kuona kaunti chafu. Tuna kiongozi ambaye haelewi maana ya uongozi. Hata akipewa wadhifa bila malipo, ambao hakufanyia kazi, hajui la kufanya nao," akasema. Pia aliutaka utawala wa Rais William Ruto kushughulikia uhaba wa maji jijini Nairobi, akisema hakutakuwa na maana ya kujenga majumba marefu ya makazi ya gharama nafuu bila kuhakikisha wakazi wanapata maji. Alisema upinzani umeungana na kudokeza kuwa baadhi ya viongozi wake watahudhuria uzinduzi rasmi wa chama hicho utakaofanyika katika wiki zijazo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Pato zuri la karakara za zambarau lamfanya 'kujuta kuhangaikia mahindi' miaka mingi

MUSA Kemei ni mkulima wa matunda ya karakara (passion fruit) eneo la Chai-Moto, Mariashoni, Molo katika Kaunti ya Nakuru. Amekuwa akikuza matunda hayo yenye rangi ya zambarau au 'purple passion' kwa muda wa miaka minane. "Nilikuwa nikilima mahindi kwa zaidi ya miaka 10 kabla ya kuamua kubadilisha na kuanza ukulima huu wa matunda. Hii ilitokana na kupanda kwa gharama za pembejeo za kilimo, kama vile mbolea na mbegu huku nikitumia fedha nyingi kuanzia hatua ya kuandaa shamba hadi kuvuna," anasema. Anasema alikuwa akivuna takriban magunia 15-20 ya mahindi kutoka kwa ekari moja huku akiuza kila gunia la kilo 90 kwa kati ya Sh1,800 na Sh2,500, kulingana na hali ya soko mwishoni mwa mwaka. Katika kila msimu, alikuwa akitumia zaidi ya Sh50,000 kwa shughuli zote kuanzia upanzi hadi kuvuna. Mnamo 2018 alipata motisha kutoka kwa moja wa rafiki zake na pamoja na mkewe walikubaliana kubadilisha matumizi ya sehemu moja ya shamba lao la mahindi ili kupanda matunda hayo. Kwa mtaji wa Sh4,000, aliandaa sehemu ya shamba na kununua miche 150 kutoka kwa rafiki yake, ambaye alikuwa ameiandaa kwenye kitalu, kwa Sh20 kwa kila mche. Fedha zilizobaki alizitumia kwa ajili ya shughuli za upanzi na gharama zingine zikiwepo kulipa wafanyi kazi wa vibarua. Shughuli ya upanzi "Nilichimba mashimo yenye ukubwa wa futi moja, yakiwa na nafasi ya mita moja na nusu kati ya shimo moja hadi jingine katika kila mstari, ili kupata nafasi ya kutosha wakati wa kupulizia dawa, kuweka mbolea, kuvuna, na shughuli nyingine muhimu za usimamizi wa shamba. Wakati wa kupanda, nilichanganya udongo na mbolea ya mifugo niliyokusanya kutoka kwa mifugo wangu," anasema Kemei. Anaongeza kuwa baada ya miezi minne, alipulizia dawa za kuua wadudu, akaweka mbolea ya kukuza mimea huku akipalilia miche yake kwa kuwa mvua ilinyesha ya kutosha. Pia alinunua nguzo za ukubwa wa wastani na kuzitumia kusaidia mimea yake ya matunda ili isidondoke chini wakati matawi yanayobeba matunda yanapokua. Miezi minane baada ya kupanda, Kemei aliweka nyaya kwenye nguzo hizo ambazo zilikuwa zimefikia urefu wa mita mbili hadi tatu kwa kuwa mimea ya karakara hutambaa. Baada ya miezi 10 miti hiyo ilianza kutoa maua. Kemei, 52, alivuna kilo 60 katika mavuno yake ya kwanza baada ya mwaka mmoja na kuziuza kwa Sh100 kwa kilo katika soko la eneo hilo. Wiki mbili baadaye, uzalishaji uliongezeka hadi kilo 150, huku bei ya kila kilo ikipanda hadi Sh120, na katika mavuno ya tatu, kiasi kiliongezeka sana hadi kufikia kilo 200. Alivuna matunda yake kila baada ya wiki mbili na kuona ongezeko la uzalishaji katika kila mzunguko wa mavuno, hasa wakati mvua ilikuwa ya kutosha. Mafanikio hayo katika mauzo yalimpa motisha ya kupanua shamba lake hadi kufikia nusu ekari katika mwaka uliofuata. Anasema kuwa hakuhitaji tena kununua miche kutoka kwa rafiki yake au wakulima wengine wa eneo hilo ili kupanda katika sehemu aliyoongezea ya robo ekari, kwani aliandaa miche yake mwenyewe na kuipanda mwaka wa 2019. Anaeleza kuwa hana majuto yoyote ya kuwekeza katika kilimo cha matunda, kwani mafanikio yake yamemwezesha pia kupanda matunda ya 'tree tomatoes', ambayo kwa sasa yako katika hatua ya kutoa maua na matunda yaliyo katika robo ekari. Kupitia mauzo hayo, ameweza kulipa karo ya shule kwa ajili ya watoto wake na kukidhi mahitaji yake mengine ya kifedha kwa urahisi. Mpango wake ni kupanua shamba lake la matunda ya karakara kutoka nusu ekari hadi ekari moja kufikia mwaka ujao. Hata hivyo, kati ya Novemba na Desemba, mkulima huyo hupata mauzo mazuri na kuvuna zaidi ya kilo 500 kila mwezi, kutokana na mvua ya kutosha inayonyesha katika kipindi hicho. Licha ya uzalishaji mzuri, Kemei anataja uvamizi wa wadudu waharibifu kwenye maua na matunda, kuwa jambo linalosababisha kukauka kwake, hasa wakati wa msimu wa kiangazi kama changamoto kubwa inayowakabili wakulima. "Nimechimba kisima shambani ambacho kinanisaidia kumwagilia matunda yangu maji wakati wa kiangazi. Kwenye kila shina, nimetengeneza mfumo wa chombo ambacho huweka maji, yakisaidia kulisha mmea kwa njia ya matone wakati wa kiangazi," anasema Kemei. Ili kuboresha ujuzi wake wa kilimo, mkulima huyu hushirikiana na maafisa wa kilimo ambao humtembelea mara kwa mara shambani mwake. Kupitia maafisa hao, anajifunza jinsi ya kutengeneza mbolea ya asili kwa kutumia nyasi kavu, majani, na mabua ya mahindi, pamoja na kujifunza kuhusu magonjwa ya mimea na njia za kuyadhibiti. Pia, anajifunza kupitia mtandao na kutembelea wakulima wengine wenye uzoefu katika eneo hilo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

Kaunti 10 zilizopokea kitita kikubwa cha Sh5 trilioni tangu ugatuzi uanze

SERIKALI ya kitaifa itakuwa imetuma jumla ya Sh5 trilioni kwa serikali za kaunti kufikia Juni mwakani, miaka 14 tangu mfumo wa ugatuzi kuanzishwa nchini. Takriban theluthi moja ya fedha hizo zimetengewa kaunti 10 ambazo zimenufaika pakubwa na mfumo huo, zikipokea jumla ya Sh1.6 trilioni kufadhili shughuli za serikali zao na miradi ya maendeleo. Nairobi imepokea kiasi kikubwa zaidi cha fedha hizo, jumla ya Sh240 bilioni, ikiimarisha nafasi yake kama kaunti yenye mgao mkubwa zaidi nchini. Hata hivyo, kwa kuzingatia maeneo ya kijiografia, Kaskazini mwa Kenya ndiyo eneo lililonufaika zaidi, huku kaunti tatu zikiingia katika orodha ya 10 zilizopokea fedha nyingi zaidi. Turkana imepokea Sh167.4 bilioni na kushika nafasi ya pili baada ya Nairobi. Mandera imepokea Sh150.5 bilioni, huku Wajir ikipokea Sh129 bilioni na kushika nafasi ya kumi. Kwa pamoja, kaunti hizo tatu zimepokea Sh447 bilioni, sawa na takriban asilimia tisa ya fedha zote zilizotengewa kaunti. Fedha hizo ni karibu mara mbili ya mgao wa Nairobi, licha ya kaunti hizo tatu kuwa na jumla ya wakazi milioni 2.99 mwaka 2025, ikilinganishwa na milioni 4.9 wa Nairobi, kulingana na takwimu za Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS). Mkoa wa Magharibi pia umefaidika, huku Kakamega ikipokea Sh164 bilioni na Bungoma Sh140 bilioni. Kaunti nyingine zilizoingia kwenye orodha hiyo ni Nakuru iliyopokea Sh165.7 bilioni, Kilifi (Sh157.3 bilioni), Kiambu (Sh157 bilioni) na Kitui (Sh135.4 bilioni). Kwa jumla, Bunge limetenga Sh5.016 trilioni kwa kaunti zote katika kipindi cha miaka 14. Takriban asilimia 60 ya fedha hizo zimetolewa katika miaka saba iliyopita. Wizara ya Fedha ilisema kaunti zilipokea Sh2.5 trilioni katika kipindi cha miaka sita ya kifedha kuanzia 2020/21 hadi 2025/26. Katika mwaka huu wa kifedha, kaunti zimetengewa takriban Sh503 bilioni, zikiwemo Sh428 bilioni kama mgao wa kawaida wa mapato ya kitaifa na Sh75.7 bilioni kama mgao wa masharti. Kaunti pia hukusanya mapato yao wenyewe kufadhili shughuli za kila siku. Kaunti 10 zilizoongoza kwa mgao zinatarajiwa kuwa zimepokea asilimia 32 ya fedha zote kutoka Wizara ya Fedha kufikia Juni 2027. Kaunti hizo zina takriban wakazi milioni 20, sawa na zaidi ya asilimia 37 ya idadi ya watu nchini. Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) imekuwa ikitumia kanuni mbalimbali kuamua kiasi cha fedha kinachopaswa kutolewa kwa kila kaunti. Vigezo vinavyozingatiwa ni pamoja na idadi ya watu, umaskini, afya, kilimo na gharama za kuendesha serikali za kaunti. Katika kipindi cha kwanza, kuanzia 2013/14 hadi 2016/17, idadi ya watu ilikuwa na uzito wa asilimia 45, huku gharama za kuanzisha na kuendesha serikali za kaunti zikiwa na asilimia 25. Katika kipindi hicho, Nairobi ilipokea Sh48 bilioni, Turkana Sh39 bilioni na Mandera Sh33 bilioni. Kanuni ya pili, iliyotumika kati ya 2017/18 na 2019/20, iliendeleza uzito wa idadi ya watu kwa asilimia 45, huku gharama za msingi za kuendesha serikali zikiwa asilimia 26 na umaskini asilimia 18. Kanuni ya tatu, iliyotumika kuanzia 2020/21 hadi 2024/25, ilizingatia vigezo mbalimbali kwa usawa zaidi. Gharama za msingi zilikuwa na asilimia 20, idadi ya watu asilimia 18, afya asilimia 17, umaskini asilimia 14 na kilimo asilimia 10. Kanuni ya nne ilianza kutumika Julai mwaka jana na itaendelea hadi Juni 2030. Imerudisha uzito mkubwa kwa idadi ya watu kwa asilimia 45, huku mgao sawa ukiwa asilimia 22, umaskini asilimia 14 na pengo la mapato asilimia 13. Katika mwaka wa kifedha uliopita, Wizara ya Fedha ilitoa Sh468.9 bilioni chini ya mfumo huo mpya. Kiambu ilinufaika zaidi kwa kupata nyongeza ya Sh1.8 bilioni, huku Kajiado, Kwale, Vihiga na Laikipia kila moja ikipata zaidi ya Sh1 bilioni. Mabadiliko hayo yanaonyesha jinsi kanuni za ugavi wa mapato zinavyoendelea kuathiri uwezo wa kaunti kufadhili huduma na miradi ya maendeleo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 18 hours ago

Serikali ya Nassir yanusurika kuamriwa kurejeshea wakazi kodi iliyowakata mwaka mzima

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imeponea mzigo wa kuwarejeshea wakazi na wafanyabiashara kodi na ushuru iliyokusanya kwa kipindi cha mwaka mzima chini ya Sheria ya Fedha ambayo Mahakama Kuu imebaini kuwa ilitungwa kinyume na Katiba. Katika hukumu iliyotolewa Novemba 20, Mahakama Kuu mjini Mombasa ilikiri kuwa serikali ya kaunti na Bunge la Kaunti zilikiuka wajibu wao wa kikatiba wa kuwashirikisha wananchi katika utungaji wa sheria. Hata hivyo, mahakama ilisema kubatilisha ukusanyaji wa mapato ya mwaka mzima kungevuruga utoaji wa huduma za umma. Mahakama ilikataa kubatilisha Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 (Na. 6 ya 2024) wala kuamuru kurejeshwa kwa fedha zilizokusanywa, ikisema walalamishi walishindwa kuwataja wasafirishaji au wafanyabiashara waliolipa ushuru uliopingwa na kuwasilisha ushahidi wa malipo hayo. "Kasoro niliyoibaini inahusu utaratibu uliofuatwa. Sijabaini kuwa ada yoyote mahususi ilitozwa nje ya mamlaka ya kaunti," mahakama ilisema. Sheria hiyo ilianza kutekelezwa Januari 1, 2025 na kutumika mwaka mzima. Mahakama ilibainisha kuwa kaunti ilikuwa tayari imetumia mapato hayo kutoa huduma za umma, huku wafanyabiashara wakipata vibali, leseni na huduma nyingine badala ya malipo yao. Mahakama pia iliwakosoa walalamishi kwa kusubiri hadi Aprili 2025 kuwasilisha kesi kupinga sheria ambayo tayari ilikuwa imeanza kutekelezwa, ikisema kuwa kufikia wakati huo wafanyabiashara wengi walikuwa tayari wamelipa. Mashirika mbalimbali ya wafanyabiashara yaliwasilisha kesi hiyo Aprili 2025. Walalamishi walidai kuwa serikali ya kaunti iliwanyima wakazi fursa ya kutosha kuchunguza na kuwasilisha maoni yao kuhusu Mswada wa Fedha kabla ya kupitishwa kuwa sheria. Walisema kaunti ilichapisha tangazo la kuwaalika wananchi kuwasilisha maoni yao Septemba 23, 2024, na kuwapa siku mbili pekee, hadi Septemba 25, kuwasilisha mapendekezo yao. Pia walipinga kikao kimoja cha kusikiliza maoni ya umma kilichofanyika katika Ukumbi wa Jamii wa Tononoka Novemba 14, 2024, wakisema mkutano huo wa saa mbili haukufanyika ipasavyo na haukuweza kuwakilisha kwa njia ya kutosha wakazi wa wadi zote 30 za kaunti. Licha ya zoezi hilo kutofaulu, walisema Bunge la Kaunti liliidhinisha ripoti ya ushirikishwaji wa umma na kupitisha Mswada huo wakati wa kikao maalumu kilichofanyika Desemba 23, 2024. Walalamishi pia walipinga madai kuwa Sheria hiyo ilidumisha viwango vya awali vya ushuru, wakitaja ongezeko la gharama za vibali vya biashara. Walitaja ongezeko la ushuru kwa hadi karibu Sh35,000 kwa baadhi ya biashara. Katibu wa Kaunti, Jeizan Faruk, alipinga kesi hiyo akisisitiza kuwa serikali ya kaunti ilizingatia matakwa ya kisheria kuhusu ushirikishwaji wa umma. Hata hivyo, mahakama ilibaini kuwa washtakiwa walishindwa kuthibitisha kuwa wakazi walipewa fursa ya kutosha kushiriki katika mchakato huo. Mahakama ilikataa hoja kuwa vurugu zilizotokea Tononoka zilihalalisha kusitishwa kwa zoezi hilo, ikisema wakazi ambao hawakuhudhuria mkutano huo hawakupaswa kunyimwa haki yao ya kutoa maoni. Jaji alionya kuwa michakato ya baadaye ya ushirikishwaji wa umma lazima iwe ya maana na yenye kuzingatia maoni ya wananchi, akiongeza kuwa kikao cha kusikiliza maoni kinapovunjika au kushindwa kufanyika, Bunge la Kaunti lazima liitishe kikao kingine.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Serikali yachunguza madai ya udukuzi wa jukwaa la eCitizen

SERIKALI imeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya shambulizi kubwa la kimtandao dhidi ya mfumo wa eCitizen, huku kukiwa na hofu kuwa taarifa binafsi za Wakenya na data za serikali huenda ziliibwa. Kundi la wahalifu wa kimtandao linalojiita ByteToBreach linadai kuwa lilidukua mfumo huo na kuiba gigabaiti 600 za stakabadhi za taarifa za wateja, gigabaiti 100 za data na gigabaiti 40 za misimbo ya programu za kompyuta. Taarifa hizo ziliibuliwa Jumatatu na kampuni ya Amerika inayohusika na usalama wa kimtandao, Vecert. Kundi hilo pia linadai kuwa liliweza kuingilia mifumo inayowaunganisha Wakenya na huduma mbalimbali za serikali. Hata hivyo, Wizara ya Usalama wa Ndani ilisema kikosi chake cha kiufundi na usalama kinafanya uchunguzi kubaini ukubwa wa tukio hilo. Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, wizara hiyo ilihakikishia umma kuwa huduma za eCitizen zinaendelea kupatikana kama kawaida. "Tunashirikiana na mashirika husika ya serikali kukabiliana na tukio hili. Huduma za eCitizen zinaendelea kupatikana na umma unaweza kuendelea kuzitumia kama kawaida," ilisema wizara. Kampuni ya Webmasters Kenya Ltd, inayosimamia jukwaa la eCitizen, iliambia 'Taifa Leo' kuwa suala hilo linashughulikiwa na mashirika husika ya serikali. eCitizen ni jukwaa kuu linalowawezesha Wakenya na wakazi wengine kupata huduma za serikali kupitia akaunti moja. Jukwaa hilo linaunganisha zaidi ya huduma 22,000, zikiwemo maombi ya pasipoti, leseni za udereva, vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa na ndoa, vyeti vya tabia njema na usajili wa biashara. Wataalamu wanaonya kuwa iwapo madai ya udukuzi yatathibitishwa, mifumo mingine inayotumia teknolojia ya eCitizen inaweza pia kuwa hatarini. Mtafiti wa usalama wa kimtandao na mkuu wa Cyber Guard Africa, Dkt Bright Gameli, alisema kuingiliwa kwa mfumo mkuu wa habari kama eCitizen kunaweza kuwapa wahalifu njia ya kufikia huduma nyingine zilizounganishwa nao. Kundi hilo limetaja Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Safaricom na Huduma ya Kitaifa ya Polisi kuwa miongoni mwa taasisi zinazoweza kuathirika. Hata hivyo, hakuna taasisi yoyote kati ya hizo iliyothibitisha kudukuliwa. Dkt Gameli alionya kuwa taarifa zilizoibwa zinaweza kutumiwa kufanya wizi wa utambulisho, utapeli na mashambulizi yanayowalenga watu binafsi. Aliwataka Wakenya kuwa waangalifu dhidi ya ujumbe wa ghafla unaodai kuwa nywila zao zimefichuliwa na kuwaelekeza kubofya viunzi ili kuzibadilisha. Kenya imekumbwa na ongezeko la mashambulizi ya kimtandao. Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano nchini zinaonyesha kuwa mashambulizi dhidi ya mifumo ya tovuti yaliongezeka kwa asilimia 163 hadi milioni 27.4 katika miezi mitatu hadi Septemba 2026, kutoka milioni 10.4 katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia. Wataalamu pia wanaonya kuwa matumizi ya Akili Unde (AI) yanarahisisha wahalifu kubaini mianya ya usalama katika mifumo ya kompyuta. ByteToBreach inaripotiwa kuwa kundi linalolenga kuiba taarifa na kuzitumia kutishia taasisi ili zilipwe fedha, la sivyo taarifa hizo zitangazwe au kuuzwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Wanasiasa washangaza kutoa zawadi zisizo za kawaida ikiwemo chupi

WANASIASA nchini wameanza kutumia mbinu za kipekee kuwavutia wapigakura, huku baadhi ya zawadi wanazotoa zikizua mjadala kuhusu maadili na kampeni za mapema. Ikiwa imesalia chini ya miezi tisa kabla ya uchaguzi huo, wanasiasa hao wanatoa fedha taslimu, vyakula, fulana na kofia zenye majina yao hadi zawadi zisizo za kawaida kama chupi, magodoro na sare za shule, katika harakati zao za kujijenga kisiasa. Ingawa kutoa zawadi kwa wapiga kura si jambo geni nchini, baadhi ya wanasiasa wamevuka mipaka ya kawaida kwa kutoa bidhaa ambazo hazikutarajiwa kuwa sehemu ya kampeni za kisiasa. Tukio la hivi punde lilitokea Novemba 23, wakati mgombeaji wa ugavana wa Kaunti ya Kisii, Kevin Nyamari, alipogawa chupi zenye chapa yake kwa wanawake, hatua iliyozua gumzo kwenye mitandao ya kijamii. Bw Nyamari alitetea hatua hiyo akisema, ilikuwa njia ya kuunga mkono utu na heshima ya wanawake. "Kumpa mtu chupi kunaweza kuonekana kama jambo dogo, lakini hakuna mchango mdogo linapojiri suala la utu. Kujiamini kunakotokana na hilo ni kubwa," alisema. Aliongeza kuwa kujitolea kwake kusaidia watu walio katika mazingira magumu, hasa wasichana na wanawake kumechochewa na huruma na wajibu wa kijamii. Hata hivyo, hatua hiyo ilikosolewa na baadhi ya Wakenya, ambao walitilia shaka ufaafu wa zawadi hizo kwa mwanasiasa anayetarajia kuwania kiti cha ugavana. Mtaalamu wa utawala bora na mwanasiasa, Dkt Peter Mbae, alisema viongozi wanapaswa kuheshimu mipaka ya maadili na badala yake kutoa msaada wenye manufaa ya kudumu. "Wanasiasa wanapaswa kuheshimu mipaka ya maadili na kutoa msaada wa vitendo au kuwawezesha wananchi kiuchumi badala ya kutoa bidhaa za nguo za ndani," alisema. Profesa Tom Nyamache wa Chuo Kikuu cha Turkana, pia alisema wanawake wanahitaji mipango yenye manufaa ya muda mrefu badala ya chupi. Hata hivyo, baadhi ya wakazi walimtetea Bw Nyamari, wakisema kutoa zawadi hizo ni njia bunifu ya kuwafikia wapigakura. Bi Mary Nyanchera, mkazi wa Kisii, alisema hatua hiyo ililenga kuonyesha upendo na kuleta mabadiliko, hata kama mchango huo ulikuwa mdogo. Miezi michache iliyopita, Mbunge wa Ndia, George Kariuki, pia alizua mjadala baada ya kuwagawia wanafunzi sare za shule zilizokuwa na jina lake. Mbunge huyo alisema sare hizo zilinunuliwa kwa pesa zake binafsi baada ya kuguswa na hali ya wanafunzi waliokuwa wamevaa nguo zilizochakaa. Alitetea uamuzi wa kuweka jina lake kwenye sare hizo, akisema hata mashirika ya kimataifa huweka majina yao kwenye misaada wanayotoa. Hata hivyo, wakosoaji walisema hatua hiyo ilikuwa na sura ya kampeni za kisiasa. Mjadala huu unaibua kumbukumbu za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua, ambapo wanasiasa waligawa mitungi ya gesi iliyopakwa rangi ya zambarau, viatu, magodoro na zawadi nyinginezo zenye chapa zao. Maafisa wakuu wa serikali pia walimiminika eneo hilo, huku miradi mbalimbali ya maendeleo ikitekelezwa kabla ya uchaguzi huo. Hata hivyo, mgombeaji wa UDA alishindwa na Sammy Kamau Ngotho wa chama cha DCP. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na wakili, Steve Kabita alisema Wakenya wanapaswa kutarajia mbinu zaidi zisizo za kawaida uchaguzi unapokaribia. "Wanasiasa wanajua kuwa hakuna umaarufu mbaya. Tarajieni mbinu nyingine za kushangaza kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao. Watatumia kila kitu kinachoweza kuwapa manufaa ya kisiasa," alisema. Huku hayo yakijiri, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema zawadi zenye chapa za wanasiasa si haramu, lakini imewaonya viongozi dhidi ya kuanzisha kampeni kabla ya wakati. Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, alisema kipindi rasmi cha kampeni kitaanza Mei 29, 2027. "Shughuli rasmi za kampeni zitaanza Mei 29, 2027. Kushiriki kabla ya kipindi rasmi cha kampeni ni kinyume cha sheria," alisema. Katika warsha ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) mjini Mombasa, Profesa Patrick Lumumba pia alikosoa mikutano ya kisiasa inayoendelea nchini, akisema viongozi tayari wameanza kampeni kinyume na sheria. Mkurugenzi wa EACC anayesimamia maadili na uongozi, Pascal Mweu, naye alionya maafisa wa umma dhidi ya kujihusisha na kampeni za mapema, akisema hatua hiyo inaweza kukiuka Sheria ya Migongano ya Maslahi. Alisema watakaopatikana na hatia watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kushtakiwa mahakamani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 24 Nov 2026 16:19:27

Korti yakataa ombi jipya la kumzuia Sonko kuongoza chama cha NEDP

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Sonko, ataendelea kuhudumu kama kiongozi wa chama cha National Economic Development Party (NEDP) baada ya Mahakama Kuu kukataa kwa mara ya pili ombi la kumzuia kushikilia wadhifa huo. Jaji Roselyne Aburili alikataa ombi jipya lililowasilishwa na wakili Nick Sanare, aliyetaka Sonko azuiwe kutumia mamlaka ya kiongozi wa chama hicho hadi kesi inayopinga ufaafu wake iamuliwe. Wakili huyo pia anataka Msajili wa Vyama vya Kisiasa azuiwe kumtambua au kumchapisha Sonko kwenye Gazeti Rasmi la Serikali kama kiongozi au afisa wa NEDP. Mzozo huo unatokana na swali kuhusu iwapo kuondolewa kwa Sonko katika wadhifa wa ugavana kupitia mchakato wa kumng'oa madarakani kunamnyima kikatiba nafasi ya kuongoza chama cha kisiasa. Bw Sanare anasema kuondolewa kwa Sonko kunamzuia kushikilia wadhifa wowote katika uongozi wa chama chini ya Sura ya Sita ya Katiba na Sheria ya Vyama vya Kisiasa. Anategemea Kifungu cha 75(3) cha Katiba, kinachoweka masharti kuhusu mtu aliyeondolewa madarakani kwa kukiuka maadili ya uongozi kushikilia wadhifa mwingine wa serikali. Pia anataka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) izuiwe kupokea vyeti vya uteuzi, orodha za wagombeaji au stakabadhi nyingine zitakazotiwa saini na Sonko akiwa kiongozi wa NEDP. Katika kesi hiyo, anadai Sonko alianzisha chama hicho kilichosajiliwa Desemba 9, 2025, na ameendelea kutekeleza majukumu ya uongozi, yakiwemo kuwasilisha wagombeaji katika chaguzi ndogo. Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeomba mahakama iondoe jina lake kwenye kesi hiyo, ikisema hakuna ushahidi wa kuonyesha ilikiuka wajibu wake. Msajili wa Vyama vya Kisiasa pia anapinga ombi la Bw Sanare. Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Februari 3, 2027, ambapo itatoa maelekezo kuhusu kuwasilishwa kwa hoja za mwisho na kupanga tarehe ya uamuzi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 24 Nov 2026 15:07:21

Familia za watu wawili waliotekwa nyara zahangaika

FAMILIA za wanaume wawili waliotekwa nyara katika visa tofauti Mombasa na Lamu zimeendelea kukosa majibu kuhusu waliko wapendwa wao baada ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kusema haijawazuilia. Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Mombasa imeagiza maafisa wa usalama kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti kamili ndani ya siku tatu kuhusu kutoweka kwa Ismail Yusuf Mohamed na Ali Kassim. Mohamed alitekwa eneo la Bondeni karibu na Camels Joint usiku wa Oktoba 30 mwaka huu akitafuta chakula. Kwa mujibu wa DCI, kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Central mnamo Oktoba 31 na Fatuma Saidi. Polisi walisema uchunguzi ulianza katika kituo hicho kabla ya kuhamishiwa kwa DCI Urban Police Station, huku taarifa za kutafuta Mohamed zikitumwa katika vituo vya polisi kote nchini. Hata hivyo, DCI ilisema baadhi ya mashahidi wanaohusishwa na tukio hilo hawajapatikana na uchunguzi wa kamera za CCTV bado unaendelea. Shirika la Vocal Africa, ambalo limewasilisha kesi kwa niaba ya Mohamed, linadai kuwa kamera zilirekodi watu waliokuwa wakimfuatilia kwa gari aina ya pickup kabla ya kumteka na kumuingiza katika Toyota Land Cruiser nyeupe. Shirika hilo linataka Inspekta Jenerali wa Polisi amfikishe Mohamed mahakamani akiwa hai au amekufa na kueleza aliko. Mohamed aliwahi kushtakiwa kwa kosa la kuajiri watu kwa ajili ya kundi la kigaidi, lakini aliachiliwa huru na mahakama ya Malindi Agosti 11, 2023 baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi. Katika kisa cha pili, Kassim alitekwa nyumbani kwake katika kijiji cha Tchundwa, Lamu Mashariki, usiku wa Septemba 26, 2026. DCI ilisema takriban watu 10 waliovalia mavazi ya kijeshi na kufunika nyuso zao waliingia nyumbani kwake saa 4.40 usiku na kumchukua. Mkewe, Sauda Mumin, aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi cha Tchundwa siku iliyofuata. Vocal Africa inadai waliomchukua Kassim walijitambulisha kuwa maafisa wa polisi na kumwahidi mkewe kwamba wangemwachilia baada ya kumhoji. Familia zote mbili zinataka maafisa wa usalama kueleza waliko wanaume hao na sababu za kutoweka kwao. Kesi hizo zinatarajiwa kusikilizwa Novemba 23.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 24 Nov 2026 12:48:57

Marehemu Papa Francis alinakili kupitia vishawishi vya shetani, shajara zake za siri zafichua

VATICAN, Roma: PAPA Francis, aliyefariki Aprili 2025, alipitia kipindi kigumu cha miaka miwili cha mapambano ya kiroho kuanzia 2021, ambapo alihisi kushawishiwa na Shetani na kuhangaika kuhusu namna ya kutumia mamlaka yake kuliongoza Kanisa Katoliki. Haya yamefichuliwa katika mkusanyiko mpya wa shajara zake za siri zilizochapishwa Jumanne, zikitoa taswira ya changamoto za kiroho alizopitia katika miaka yake ya mwisho. Francis, aliyeliongoza Kanisa Katoliki kwa miaka 12, alisimulia jinsi alivyokuwa na maono ya Shetani na Jehanamu, huku akipambana na hofu ya kuwa kiongozi anayetumia na kuwadhibiti watu kwa manufaa yake. "Yote yalichanganyika na masuala ya uongozi, shinikizo kuhusu maamuzi ya kufanya, pamoja na hali ya ukavu na ukiwa wa kiroho," akasema katika maandishi ya Disemba 2022. Kadinali Victor Fernandez, aliyekuwa mshirika wa karibu wa Francis, ndiye aliyekusanya shajara hizo na kuziandaa katika kitabu chenye kurasa 160 pamoja na maelezo yake. Fernandez alisema marehemu hatimaye alitambua kuwa kipindi hicho kilikuwa jaribio baya zaidi la kiroho alilowahi kupitia. "Alijihisi kuwa katika vita vya kila mara ili asije akaangukia katika kishawishi hicho cha kishetani," akaandikaFernandez. Katika shajara ya Januari 2021, Francis aliorodhesha mara tatu maishani mwake alizohisi kumwona Shetani, ikiwemo wakati alipokuwa papa na kuhudhuria mkutano na maafisa wa Vatican. "Siwezi kusahau ukwaruzo mkubwa wa sauti yake. Bwana alinipa fursa ya kuondoka kwenye mkutano huo na hivyo akaniokoa," aliandika kuhusu tukio hilo. Pia alisimulia maono aliyopata Juni 2018 kuhusu mlango wa kuingia Jehanamu. "Usiku uliopita niliona mlango wa Jehanamu. Nilichungulia ndani kidogo na nikaingiwa na hofu kubwa. Nilishika rozari kama silaha. Namshukuru Bwana kwa msaada huo," akaandika. Fernandez pia alisimulia jinsi Francis alivyokataa kutumia mamlaka yake kuwaadhibu maafisa waliomkosoa hadharani. Alisema papa huyo alihisi Mungu hakutaka awe kiongozi anayewatumia na kuwadhibiti wengine kama vikaragosi. Francis alikuwa mwanamageuzi aliyekumbana na upinzani kutoka kwa makadinali wahafidhina waliokuwa na wasiwasi kuhusu misimamo yake ya kufungua Kanisa kwa mabadiliko. Katika shajara hizo, pia alijutia namna alivyoshughulikia madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya askofu mmoja Chile mnamo 2018. "Nilihuzunika sana kutokana na hali Chile. Ilikuwa vigumu kwangu kukubali kilichotokea; sikufikiri kuwa kilikuwa kibaya kiasi hicho," aliandika. Aidha, alimwelezea mrithi wake, Papa Leo XIV, ambaye wakati huo alikuwa Kadinali Robert Prevost, kama "mchungaji mkuu, mmisionari mkarimu na mtu asiye na dosari." Shajara hizo zinaanzia Disemba 1992 hadi Agosti 2024 na zinatoa mtazamo wa kipekee kuhusu maisha ya kiroho ya papa huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 88.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 24 Nov 2026 11:43:03

Ripoti yafichua changamoto wakulima wa kike wanapitia katika miradi ya kilimo

WAKULIMA wanawake nchini wanazalisha mapato mengi kwa kila hekta kuliko wanaume, lakini wanashindwa kupata faida inayolingana kutokana na ukosefu wa mikopo nafuu na vifaa vya kisasa vya kilimo. Tathmini ya miaka tisa iliyofanywa na Farm to Market Alliance (FtMA), imeonyesha kuwa wanawake hupata wastani wa Sh82,494 kwa hekta wakati wa msimu mkuu wa kilimo, ikilinganishwa na Sh69,833 wanazopata wanaume. Hata hivyo, vituo vya huduma za wakulima vinavyoongozwa na wanawake hupata faida ya wastani wa Sh143,989 kwa mwaka, ikilinganishwa na Sh515,253 kwa vituo vinavyoongozwa na wanaume. Ripoti hiyo inasema tofauti hiyo inachangiwa na changamoto za kupata fedha na vifaa vinavyohitajika kupanua biashara za kilimo. Kwa wastani, vituo vinavyoongozwa na wanawake vina vifaa viwili pekee, ikilinganishwa na 3.2 katika vile vinavyoongozwa na wanaume. Hali hii inapunguza uwezo wao wa kutoa huduma za mashine, kushughulikia mazao mengi na kuyahifadhi baada ya mavuno. Mratibu wa FtMA nchini, George Njoroge, alisema matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanawake na vijana wanaweza kupata mapato zaidi wakipata mbegu bora, mafunzo na masoko ya uhakika. Alisema ni muhimu kuondoa vikwazo vinavyozuia wakulima hao kupanua shughuli zao. Ripoti hiyo pia ilibaini kuwa asilimia 70 ya vituo vya huduma za wakulima havina mikopo kutoka taasisi rasmi, licha ya asilimia 97 kuwa na akaunti za benki. Masharti ya mikopo yanayohitaji wakopaji kutoa ardhi kama dhamana yanatajwa kuwa kikwazo kikuu, na kulazimisha baadhi ya vituo kutegemea mikopo isiyo rasmi. Upungufu wa vifaa pia unasababisha hasara baada ya mavuno. Wanawake wanaweza kupoteza hadi nusu ya mavuno ya maharagwe kwa kuwa wanayakausha kwa mikono kwa kukosa mashine. Changamoto nyingine ni masoko. Ingawa asilimia 88.9 ya wakulima huuza mazao yao, ni asilimia 3.8 pekee walio na mikataba rasmi na wanunuzi. Mpango huo ulioanza 2017 umepanuka kutoka kaunti mbili hadi 13, na kuanzisha vituo 2,126 vilivyofikia wakulima 401,955. Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini, Bai Mankay Sankoh, alisema lengo ni kujenga biashara za vijijini zinazoweza kujiendesha bila kutegemea ufadhili wa miradi. Ripoti inapendekeza mikopo isiyohitaji dhamana ya ardhi, ufadhili wa vifaa kwa vituo vinavyoongozwa na wanawake na kuimarisha mifumo ya masoko.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 24 Nov 2026 11:06:56

Makosa katika utungaji wa sentensi katika ngeli ya mahali ya PA-KU-MU

LUGHA ya Kiswahili ina ngeli mbalimbali. Ngeli ni kundi la nomino zenye upatanisho wa kisarufi wa namna moja. Mifano ya ngeli za Kiswahili ni A-WA, KI-VI, YA-YA, LI-YA, U-U, U-ZI, PA-KU-MU. Ili sentensi iwe sahihi, sharti mtu azingatie upatanisho faafu wa kisarufi. Kuna mazoea ya kuchanganya viashiria na viambishi vya ngeli ya PA-KU-MU katika sentensi moja. Mara kwa mara utapata sentensi kama vile: *Shambani pale kumepandwa miche. *Shimoni mle pameingia panya mkubwa. *Sokoni kule pana bidhaa nyingi. Ujumbe katika sentensi hizi unaeleweka. Hata hivyo, sentensi hizi si sahihi. Hazijazingatia upatanisho unaofaa wa kisarufi. Ngeli ya PA-KU-MU hujumuisha nomino za mahali. Silabi PA- huashiria mahali panapojulikana. Silabi KU- huashiria mahali pasipojulikana na silabi MU – huashiria mahali ndani. Ni kosa kutumia viashiria na viambishi vyote vya PA-KU-MU katika sentensi moja kwani sentensi hiyo itachanganya mahali panapozungumziwa. Ikiwa sentensi inarejelea mahali panapojulikana, sharti vivumishi na viambishi vya vitenzi vianze kwa pa-, Ikiwa ni mahali pasipojulikana kiambishi cha nomino kwenye kitenzi kianze kwa ku-, Iwapo ni mahali ndani sharti kiambishi kitenzi kiwe m-. Ili kukosoa mifano hiyo ya sentensi tunafaa kusema: Shambani pale pamepandwa miche. Shimoni mle mmeingia panya mkubwa. Sokoni kule kuna bidhaa nyingi. Mwanafunzi mwenye changamoto ya kutunga sentensi akitumia nomino za ngeli ya PA-KU-MU anafaa kwanza atambue nomino katika ngeli ya PA-KU-MU kisha afanye mazoezi ya kuandika sentensi sahihi akitumia nomino mbalimbali za ngeli ya PA-KU-MU.

read more