T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 01 Oct 2026 03:55:32

Orengo anaelekea wapi kisiasa? Mdahalo wachacha akikosa mikutano ya upinzani

KUKOSEKANA kwa Gavana wa Siaya James Orengo katika mikutano kadhaa muhimu ya viongozi wa upinzani katika siku za hivi majuzi kumezua mjadala mkubwa kuhusu hatua yake ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Kwa mwanasiasa ambaye amekuwa nguzo muhimu katika siasa za upinzani kwa miongo kadhaa, kila hatua yake au hata kutokuwepo kwake katika hafla muhimu huibua maswali mengi. Hali hiyo imefanya wengi kujiuliza iwapo Orengo anajiandaa kujiunga na muungano mpya wa kisiasa au anapanga kuanzisha mkondo wake mwenyewe. Baada ya kuwa kimya kwa muda, Orengo alijitokeza Septemba 21 wakati wa uzinduzi wa muungano mpya wa The Ukombozi Alliance, uliobadilishwa jina kutoka Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party. Watazamaji wa kisiasa walitafsiri hatua hiyo kama ishara kwamba huenda alikuwa akijipanga kupata nafasi mpya katika upinzani. Hata hivyo, siku chache baadaye alikosekana katika kikao muhimu cha viongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi ambapo Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna aliidhinishwa kuwa mgombea wa urais wa muungano huo katika uchaguzi wa 2027. Kutokuwepo kwake kulionekana kuwa na uzito mkubwa kwa sababu hapo awali jina lake lilikuwa likitajwa miongoni mwa wale waliokuwa wakitazamwa kama viongozi wanaoweza kuwania nafasi ya juu katika muungano huo. Orengo pia hakuhudhuria mkutano wa kisiasa uliofanyika Narok licha ya jina lake kuwekwa kwenye mabango ya viongozi walioalikwa. Viongozi waliokuwepo ni pamoja na kiongozi wa muda wa Jubilee Fred Matiang'i na kiongozi wa People's Party of Kenya Ndindi Nyoro. Katika mahojiano maalum, Orengo aliwataka wafuasi wake kuwa watulivu huku akisema bado anaunga mkono umoja wa upinzani katika mapambano ya kuleta mabadiliko nchini. "Ninaunga mkono mapambano ya mageuzi yanayohitaji umoja na hatua za kisiasa. Wafuasi wangu wawe watulivu. Nitafafanua hatua yangu inayofuata kwa wakati unaofaa," alisema. Ingawa hakufichua mipango yake, taarifa zinaonyesha kuwa Orengo anafikiria kufufua chama cha Liberal Democratic Party (LDP), ambacho zamani kilihusishwa na Raila Odinga na marehemu Dennis Kodhe. Kidokezo kubwa zaidi kilitolewa Jumatano alipoweka ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akisema, "Maadhimisho ya Baba yanakaribia, jiandaeni," akiambatisha picha ya kofia yenye rangi rasmi za LDP, yaani kijani, bluu na nyeupe. Wadadisi wa siasa wanaamini kuwa hatua hiyo huenda ikawa njia ya Orengo kujijengea nafasi mpya ya kujadiliana na makundi mbalimbali ya upinzani, yakiwemo Ukombozi Alliance na Linda Mwananchi. Chanzo cha karibu naye kinasema Orengo anaamini eneo la Nyanza linafaa kuwa na sauti yenye uzito zaidi katika siasa za upinzani. Wafuasi wake wanahisi baadhi ya viongozi ndani ya Linda Mwananchi wanajaribu kupunguza ushawishi wake. Hata hivyo, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amepuuzilia mbali madai ya mzozo mkubwa ndani ya vuguvugu hilo. Amesema tofauti za maoni kati ya Orengo, Sifuna na mbunge Babu Owino ni jambo la kawaida katika mfumo wa vyama vingi. Kwa sasa, hatua anayopanga Orengo bado ni siri. Lakini uchaguzi wa 2027 unapokaribia, kila ishara inaonyesha kuwa gavana huyo wa Siaya anajitayarisha kufanya uamuzi muhimu ambao unaweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za upinzani nchini.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 59 minutes ago

Mivutano yaibuka upya katika upinzani

UPINZANI nchini unakabiliwa na mivutano mipya ya ndani baada ya Kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua kupendekeza muungano wa vyama vitatu, hatua iliyozua malumbano na viongozi wengine wanaolenga kumwondoa Rais William Ruto mamlakani 2027. Bw Gachagua anataka DCP, Linda Mwananchi ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Wiper inayoongozwa na Kalonzo Musyoka ziungane. Katika mahojiano na runinga ya Inooro, Bw Gachagua alisema muungano wa Mlima Kenya, Magharibi na Ukambani unatosha kuushinda utawala wa Rais Ruto. Alidai ana uwezo wa kuleta kura milioni 10, huku Bw Sifuna akileta milioni nne na Bw Musyoka milioni tatu. "Baina yangu, Sifuna, Eugene Wamalwa na Kalonzo Musyoka, uchaguzi utakuwa umekwisha. Hata tusipopata wengine, bado tunaweza kushinda," akasema Bw Gachagua. Hata hivyo, pendekezo hilo limewakera baadhi ya viongozi wa upinzani, wakiwemo kiongozi wa Jubilee Dkt Fred Matiang'i na Kiongozi wa DP Justin Muturi, ambao wamemshutumu Bw Gachagua kwa kiburi na kuwadharau washirika wake. Dkt Matiang'i alisema matamshi ya Bw Gachagua yanahatarisha kuuvunja upinzani kwa kuugawanya kwa misingi ya kikabila. " Kiburi cha walio wengi na majivuno hayo ndiyo yatakayougawanya upinzani na kufanya iwe vigumu kuungana," akasema Aliongeza kuwa uongozi wa nchi haupaswi kuamuliwa kwa misingi ya jamii, bali uwezo wa mtu binafsi. Bw Muturi naye alisema kwamba hakuna jamii moja inayoweza kumwezesha mtu kuwa Rais bila kuungwa mkono na Wakenya kutoka maeneo mengine. "Urais hupatikana kupitia maafikiano ya kitaifa, miungano ya kimkakati na uwezo wa kuwaunganisha Wakenya kutoka jamii na maeneo mbalimbali," alisema. Alionya kuwa mpango wa vyama vitatu si njia ya moja kwa moja ya kuingia Ikulu na akataka muungano ujengwe kwa kuheshimiana, badala ya vitisho na mashindano ya ubabe. Mivutano hiyo inatokana pia na madai ya baadhi ya viongozi kuwa washirika wao ni vibaraka wa serikali. DCP imehusisha madai hayo na Bw Matiang'i na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro wa People's Party of Kenya. Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kuwa mzozo huo unahusu pia udhibiti wa kura za eneo la Mlima Kenya. Aidha, viongozi hao hawajakubaliana kuhusu atakayekuwa mgombea mmoja wa urais wa upinzani. Wengi wana matarajio ya kuwania kiti hicho, huku maswali yakiibuka kuhusu uwezo wao wa kuvutia uungwaji mkono wa kitaifa, fedha na miundo ya kisiasa. Dkt Matiang'i alisema yuko tayari kumuunga mkono mgombea mwingine iwapo atachaguliwa kupitia mchakato wa wazi na unaowashirikisha wote. "Yeyote atakayechaguliwa kupitia mchakato jumuishi na unaokubalika kwetu sote, nitamuunga mkono," akasema. Alisema pia kuwa akichaguliwa Rais, atafuta ushuru wa nyumba, kupambana na ufisadi, kuimarisha usalama na kuhakikisha rasilimali za kaunti zinatumika ipasavyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Masaibu hayaishi, Waititu aongezwa miaka 13 jela

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ameongezewa kifungo cha miaka 13 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya ulanguzi wa fedha zinazohusishwa na zabuni ya ujenzi wa barabara yenye thamani ya Sh588.7 milioni iliyotolewa wakati alipokuwa gavana. Hakimu Mkuu Harrison Barasa wa Mahakama ya Milimani, jana, alimuamuru Waititu kulipa faini ya jumla ya Sh21 milioni au atumikie kifungo cha miaka 13 kutokana na mashtaka matatu ya ulanguzi wa fedha. Hata hivyo, kifungo hicho kitaunganishwa na kile cha miaka 12 ambacho tayari anatumikia kutokana na makosa ya ufisadi. Mkewe, Susan Wangari Ndung'u, alitozwa faini ya Sh18 milioni au kifungo cha miaka miwili iwapo atashindwa kulipa. Mfanyabiashara Charles Mbuthia Chege, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Testimony Enterprises iliyopata zabuni hiyo naye aliangushiwa adhabu ya miaka 13. Mkewe, Beth Wangechi Mburu, walitozwa Sh6 milioni au kifungo cha miaka sita. Hukumu hizo zilitolewa baada ya washtakiwa kufika mahakamani kuomba wapunguziwe adhabu. Waititu na Chege waliiomba mahakama kuwaonea huruma wake zao, wakidai hawakuhusika pakubwa katika mikataba iliyosababisha wapatikane na hatia. Wakili wa Waititu alisema Susan alikuwa mshirika asiyehusika moja kwa moja na shughuli za kampuni hizo. "Mahakama itatambua kuwa Susan alikuwa mshirika wa kimya katika kampuni hizo mbili. Hakuwa mtu wa kutia saini akaunti za benki wala mshiriki katika kufanya maamuzi ya biashara na jukumu lake lilikuwa dogo," akasema wakili huyo. Upande wa Chege ulisema Beth alikuwa na hisa moja pekee katika kampuni na alihusika tu katika kusaini nbarua za awali za usajili. Mawakili pia walidai kuwa kazi za ujenzi wa barabara zilikuwa zimekamilika na ripoti ya ukaguzi haikuonyesha upotevu wa fedha za umma. Walisisitiza kuwa mgogoro ulihusu utaratibu wa kutoa zabuni. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga ombi la kupunguziwa adhabu, ukisema kila mshtakiwa alipaswa kuwajibika binafsi kwa makosa yake. Hakimu Barasa alisema mashtaka ya ulanguzi wa fedha yana sheria maalumu zinazotaka adhabu zinazotolewa zifuate viwango vilivyowekwa. "Kila mtu atawajibika kivyake kwa makosa aliyotenda," akasema. Waititu alitozwa Sh10 milioni au kifungo cha miaka mitano katika shtaka la 10, Sh6 milioni au miaka minne katika shtaka la 11 na Sh5 milioni au miaka minne katika shtaka la 12. Chege alipewa adhabu sawa na hizo, huku Beth akitozwa Sh2 milioni au miaka miwili kwa kila shtaka kati ya matatu. Susan alitozwa jumla ya Sh18 milioni au miaka miwili gerezani. Kampuni zilizohusishwa na mikataba hiyo pia ziliadhibiwa. Testimony Enterprises ilitozwa Sh36 milioni, Saika Two Estate Developers Sh24 milioni na Bienvenue Delta Hotel Sh4 milioni. Kampuni hizo zilipewa siku 14 kulipa faini zao. Kesi hiyo ilitokana na zabuni ya Sh588.7 milioni iliyotolewa na serikali ya Kiambu kwa Testimony kwa ajili ya kuboresha barabara za changarawe na kuziweka lami katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Wakenya walivyotekeleza ulaghai wa Sh25bn pesa za Amerika

MKENYA aliyepata kadi ya kuishi Amerika, Green Card, kupitia bahati nasibu mnamo 2024 anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika ulaghai wa Sh25.8 bilioni uliolenga fedha za serikali za kuwasaidia wanafunzi kugharimia elimu ya juu. Francis Smith Mogambi anadaiwa kushirikiana na washirika wake nchini Kenya kati ya Novemba 2025 na Mei 2026 kuiba taarifa za kibinafsi za raia wa Amerika na kuzitumia kuwaandikisha katika vyuo vya mtandaoni bila wao kujua. Washukiwa walitumia taarifa hizo kuwasilisha maombi ya mikopo na misaada ya elimu kupitia mpango wa serikali wa FAFSA. Baada ya fedha kutolewa, walidaiwa kuzichukua kupitia akaunti za benki na hundi bandia. Mogambi anadaiwa kupokea hundi zilizoandikwa kwa majina ya wanafunzi hewa, kuzitia saini na kuweka fedha hizo katika akaunti zake. Inadaiwa alisalia na asilimia 30 na kisha kutuma nyingine kwa washirika wake Kenya. Polisi walianza kumchunguza baada ya shahidi kusema alijaribu kumshawishi kujiunga na ulaghai huo kwa kumwahidi dola 2,000 (Sh259,000) kila wiki. Mnamo Oktoba 19, Mahakama kuu Nebraska ilimfungulia mashtaka 10, yakiwemo ya kuiba fedha za serikali na kutumia utambulisho wa watu wengine. Uchunguzi huo, uliopewa jina la 'Operation Ghostbusters', pia umehusisha washukiwa katika New Jersey na Virginia. Serikali za Kenya na Amerika zinazuia sarafu za kidijitali zenye thamani ya dola 750,000 (Sh97.4 milioni) zinazohusishwa na ulaghai huo. Ushirikiano huo unahusisha asasi za usalama na haki kama DCI, ARA, ODPP, KRA na FRC. Maafisa wa Amerika pia wamejadiliana na Kenya uwezekano wa kuwarejesha washukiwa nchini Amerika kukabili mashtaka. "Hundi hizo zilitolewa kwa majina ya wanafunzi tofauti, lakini zote zilikuwa na sahihi zilizomlipa Mogambi," polisi walisema katika hati ya kiapo.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Usalama wakazwa KCSE ikianza rasmi

MTIHANI wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) wa mwaka huu wa 2026 ulianza rasmi jana kote nchini huku maelfu ya watahiniwa wakianza kufanya mitihani yao katika mazingira ya ulinzi mkali na onyo kali dhidi ya udanganyifu. Mwaka huu, watahiniwa, wasimamizi na maafisa wengine wamepigwa marufuku kuingia katika vyumba vya mitihani wakiwa wamevaa saa za mikononi, zikiwemo saa za kawaida na za kisasa. Watahiniwa wanatarajiwa kutumia saa za ukutani zilizowekwa katika vyumba vya mitihani. Katika Moyale, Marsabit, watahiniwa 220 kutoka shule mbili za mpakani walihamishwa hadi shule nyingine baada ya risasi zilizopotea kutoka mapigano upande wa Ethiopia kulenga shule zao. Watahiniwa wa shule za mseto za Sessi na St Mary walihamishiwa shule za msingi zilizo salama zaidi. Jumla ya watahiniwa 1,443 wanafanya mitihani katika vituo 12 vya eneo hilo huku wanajeshi KDF na maafisa wa usalama wa mipaka wakiongeza doria. Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC), Prof Julius Nyabundi, alisema kufikia Jumatatu asubuhi hakukuwa na taarifa za udanganyifu. Alisema huu ni mtihani wa pili kutoka mwisho kusimamiwa na KNEC kabla ya mabadiliko ya mfumo wa mtaala. Uasin Gishu, watahiniwa 22,593 walianza mtihani katika vituo 246. Maafisa walipiga marufuku saa za mikononi, mavazi yasiyo sare za shule na watu wasioidhinishwa kuingia vyumba vya mitihani. Turkana, zaidi ya watahiniwa 7,000 katika vituo 68 walianza mitihani huku wakuu wa shule wakiomba ulinzi zaidi katika maeneo yanayokumbwa na ujangili. Serikali kuu na ile ya kaunti pia inafuatilia uwezekano wa mafuriko kuathiri usafirishaji wa karatasi za mitihani. Baringo ilisajili watahiniwa 16,549 katika vituo zaidi ya 196, huku Trans Nzoia ikiwa na 28,353 katika vituo 253. Maafisa walisema zoezi lilianza bila matatizo makubwa. Nyeri, watahiniwa wanne wanafanyia mitihani hospitalini kutokana na matatizo ya kiafya. Bomet pia ina watahiniwa watatu hospitalini, wakiwemo wawili wenye ujauzito. Murang'a iliwasajili watahiniwa 32,487, lakini kukazuka wasiwasi kuhusu karibu wanafunzi 600 waliodaiwa kuacha shule tangu walipojiunga na Kidato cha Kwanza. Baadhi ya watahiniwa pia walilalamikia kupewa chakula kidogo kutokana na kuchelewa kwa fedha za serikali. Kisumu ilisajili watahiniwa 25,849 katika shule 246, huku Kisii ikiimarisha usalama katika vituo vyake 45. Katika eneo la Pwani, watahiniwa 63,415 walianza mitihani. Kilifi ilikuwa na 25,617, Mombasa 12,187, Kwale 12,171, Taita Taveta 7,994, Tana River 3,082 na Lamu 2,364. Huko Lamu, mitihani ilianza kwa utulivu hata katika maeneo yenye changamoto za kiusalama ya Msiti wa Boni na Kiunga, mpakani mwa Kenya na Somalia. Kwa ujumla, maafisa wa elimu na usalama walisema maandalizi yalikuwa yamekamilika, huku wakiahidi kuhakikisha mitihani inaendeshwa kwa usalama na bila udanganyifu.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Sakaja atupa Wilbaro, alenga kujinafasi 2027 kupitia ODM

GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja jana alijiunga rasmi na chama cha ODM akilenga kuimarisha nafasi yake ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu ujao. Bw Sakaja, aliyechaguliwa mnamo 2022 kwa chama tawala cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto, alisema yuko tayari kufanya kampeni za muhula wa pili wa Rais akiwa mwanachama wa ODM. ODM na UDA kwa sasa ziko katika Serikali Jumuishi, huku zikiendelea na mchakato wa kutia saini mkataba wa ushirikiano kabla ya uchaguzi mkuu. Hata hivyo, hafla ya kumpokea Bw Sakaja katika makao makuu ya ODM, Chungwa House, ilizua hisia tofauti. Gavana huyo alisisitiza kuwa amekuwa akitekeleza matakwa ya aliyekuwa kiongozi na mwanzilishi wa ODM, marehemu Raila Odinga. "Nilianza safari hii na Baba (Raila Odinga) nilipotwaa ugavana. Na nimekuwa nikishambuliwa kwa kusimama naye na kuwasaidia wanachama wa ODM kuingia katika Baraza la Mawaziri. Nilifanya hivyo kabla ya kuundwa kwa Serikali Jumuishi na Baba ndiye aliyeniambia niingie ODM," akasema Bw Sakaja. Bw Sakaja alipokelewa na Naibu Kiongozi wa ODM aliye pia Gavana wa Kisii, Simba Arati, Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama hicho na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Mbunge wa Suna Mashariki na Mkurugenzi wa Uchaguzi ODM Junet Mohammed, pamoja na Waziri wa Madini Hassan Joho. Gavana huyo alisema anajiunga na chama hicho kwa unyenyekevu, akiwa tayari kuongozwa na ngazi zake za juu na kuanza kampeni za kuvumisha umaarufu wake. "Ninaamini kuwa hatua inayofuata ya siasa zetu haipaswi kupimwa tu kwa uchaguzi tunaoshinda, bali pia kwa maisha tunayobadilisha. Vijana hawapaswi tena kuwa watazamaji katika maamuzi yanayoathiri mustakabali wao bali anapaswa kushiriki, kuwa viongozi na kuwa kiini cha Kenya tunayoijenga," akasema. Bw Sakaja alikumbushwa kuwa Mwenyekiti wa ODM utanzu wa Nairobi ambaye ni Mbunge wa Makadara George Aladwa pia anawania tiketi ya chama hicho kugombea ugavana wa Nairobi. "Tuna mwenyekiti wetu wa chama Nairobi, George Aladwa, ambaye amekuwa akisimama na chama kwa muda mrefu na pia anawania kiti cha ugavana kupitia ODM. Sasa tunaye Gavana Sakaja," akasema Bi Wanga, akiongeza kuwa kila anayetaka kujiunga na chama hicho anakaribishwa. Jana, Bw Aladwa alisema yuko imara ndani ya ODM na kuwataka wafuasi wake wawe watulivu akisisitiza nia yake ya ugavana bado upo hai. "Wafuasi wangu nawaelewa lakini tusipoteze muda kutokana na uvumi unaoendelea. Safari ya kuimarisha Nairobi itaamuliwa na raia kwa usawa na haki na demokrasia. Tuendelee kudumisha amani," akasema Bw Aladwa. Wakati wa kumpokea Bw Sakaja, Bi Wanga alitangaza kuwa uteuzi wa wagombea utafanywa kwa uwazi na bila ubaguzi. Bw Arati pia alifichua kuwa Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri ni miongoni mwa wanaotaka kujiunga na ODM ili kuwania kiti hicho hicho. "Mwenyekiti wetu wa Nairobi, Aladwa, pia anawania ugavana. Atachuana na Gavana Sakaja kuwania tiketi ya chama. Karauri akiamua kujiunga nasi, tutampokea kama tulivyompokea Sakaja. Tunachowaahidi wanachama wetu ni uteuzi huru, wa haki na uwazi," akasema Bw Arati. Kutokana na kutokuwepo kwa Bw Aladwa katika hafla hiyo, Bw Sakaja alisema atamtafuta binafsi ili kuunganisha kura za ODM Nairobi na kuhakikisha chama hicho kinashinda viti vingi. Baadhi ya madiwani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi waliohudhuria hafla hiyo walikuwa wamemuidhinisha Bw Aladwa awali kuwania uongozi wa kaunti hiyo. Polisi nao walilazimika kutumia vitoza machozi kutawanya kundi la wanachama waliokuwa wakijaribu kuvuruga hafla hiyo. Baadhi yao walisikika wakipiga kelele, "Kama hakuna Aladwa, hakuna ODM." Mbali na Gavana Sakaja na Aladwa, ODM inakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea wa makundi mengine ambao wametangaza nia ya kuwania kiti hicho. Wao ni Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino (chama cha Mwananchi), Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya (DCP) na Askofu Margaret Wanjiru . Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua pia ametangaza kuwa chama chake cha DCP kinataka kutawala siasa za Nairobi na inaaminika anamuunga mkono Bw Gakuya.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Joho, Mvurya wapambania kudhibiti Kwale

USHINDANI wa kuwania ugavana Kwale kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 unazidi kuonekana kama mchuano wa kisiasa kati ya Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Hassan Joho wa ODM, na mwenzake wa Michezo, Bw Salim Mvurya wa UDA. Bw Mvurya anaongoza juhudi za kuhakikisha kaunti hiyo inasalia chini ya UDA huku Bw Joho akitangaza nia ya ODM kuendeleza ushawishi wake katika eneo la Pwani. "Ni lazima tukifanye ODM kuwa imara tena. Hatuwezi kuruhusu vyama vingine kuchukua maeneo yaliyokuwa ya ODM," alisema Bw Joho wakati wa mkutano wa hivi majuzi wa kisiasa Kwale. Gavana Fatuma Achani, ambaye anatumikia muhula wake wa kwanza, anakabiliwa na ushindani mkali baada ya waliokuwa wakimezea mate tikiti ya ODM, Profesa Hamadi Boga na mfanyabiashara Lungazi Mangale, kuamua kuungana ili kumuunga mkono mmoja wao. Wawili hao, walioibuka wa pili na wa tatu mtawalia katika uchaguzi wa 2022, wamehimizwa na viongozi wa mashinani kudumisha ushirikiano wao hadi uchaguzi utakapofanyika. Viongozi wa ODM wameonya kuwa kuvunjika kwa muungano huo kunaweza kudhoofisha azma ya chama hicho ya kutwaa kiti cha ugavana. Licha ya mikakati hiyo inayoendelea, Waziri Mvurya amewataka wapinzani wa Bi Achani kujiandaa kwa mchuano mkali unaofanana na uchaguzi mdogo wa Msambweni wa mwaka 2020. Uchaguzi huo ulikuwa kipimo kikubwa cha ushawishi wa kisiasa kati yake na Waziri Joho, ambao wakati huo walikuwa magavana wa Kwale na Mombasa mtawalia. Bw Joho aliunga mkono mgombeaji wa ODM Omar Boga, ambaye ni kaka mdogo wa Profesa Boga, huku Mvurya, aliyekuwa mwanachama wa ODM kabla ya kuhamia Jubilee, akiunga mkono mgombeaji huru Feisal Bader. Bw Bader alikuwa akiungwa mkono na wanasiasa waliokuwa washirika wa Naibu Rais wa wakati huo, William Ruto. Hatimaye, Bw Bader alimshinda Omar kwa kupata kura 15,251 dhidi ya 10,444 za mpinzani wake, na hivyo kumpa Mvurya ushindi mkubwa wa kisiasa. "Si siri kwamba rais wetu ni William Samoei Ruto, gavana wetu ni Fatuma Mohamed Achani, na mbunge wa eneo hili ni Feisal Bader. Walimdharau Feisal katika uchaguzi mdogo wa 2020 na wakaja hapa kwa nguvu zao zote, lakini tunawaambia kuwa wanaweza kupanga dhidi ya gavana, lakini atasalia kuwa gavana wa Kwale," alisema Bw Mvurya katika mkutano wa kisiasa Msambweni. Profesa Boga, ambaye aliwahi kuhudumu kama Katibu katika Wizara ya Kilimo wakati wa utawala wa Jubilee, aligombea ugavana mwaka wa 2022 kupitia tiketi ya ODM na kupata kura 53,972, na kushika nafasi ya pili nyuma ya Bi Achani, aliyeibuka mshindi kwa kura 59,674. Bw Mangale, aliyewahi kufanya kazi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Kenya (KPA) kama mhandisi, aligombea kupitia chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kabla ya kujiunga na ODM baada ya chama hicho kusambaratika. Hata hivyo, Gavana Achani ametetea rekodi yake ya uongozi akisema anatarajia kuchaguliwa tena kutokana na miradi ya maendeleo ambayo serikali yake imeanzisha. "Viongozi wanapaswa kutathminiwa na kuchaguliwa tena kwa kuzingatia miradi yao ya maendeleo. Acheni siasa za chuki na uhasama. Kuna baadhi ya watu ambao hawana sera; wanachozungumzia kila mara ni Achani. Nitachaguliwa tena ili kuhudumu mihula yangu miwili," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 02 Nov 2026 07:55:35

Majonzi walimu kufa wakielekea harusini

SAFARI ya walimu kutoka Kaunti ndogo ya Matete, Kaunti ya Kakamega, kuenda kusherehekea harusi ya mtoto wa mwenzao iligeuka msiba baada ya watu sita kufariki katika ajali ya barabarani. Ajali hiyo ilitokea usiku wa manane wikendi karibu na Burnt Forest, kwenye barabara kuu ya Eldoret-Nakuru. Miongoni mwa waliofariki ni Janet Andabwa, kaimu mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Chavere, ambaye kifo chake kimeiacha familia yake katika majonzi tele. Mumewe, Geoffrey Besele, ambaye pia ni mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Tande, alisema mkewe aliondoka nyumbani akiwa na furaha baada ya kukamilisha kusimamia na kutathmini mitihani ya KJSEA. Alisema Bi Andabwa aliagana naye na kuanza safari yake kuelekea Nairobi mnamo saa mbili usiku, baada ya kuchukuliwa na walimu wenzake katika kituo cha kibiashara cha Kaburengu. Hata hivyo, furaha hiyo ilikatizwa alfajiri baada ya kupokea simu iliyomfahamisha kuhusu ajali hiyo. "Nilipokea simu ya kuhuzunisha saa kumi alfajiri kwamba alikuwa amepata ajali huko Burnt Forest," akasema Bw Besele huku akishindwa kuzuia machozi katika Kituo cha Polisi cha Tarakwa, ambako mabaki ya magari yaliyohusika kwenye ajali yalikuwa yamepelekwa. Mbali na Bi Andabwa, waliofariki ni mwalimu mwengine kutoka Shule ya St Mikasa Girls, mwalimu wa Chavere, binti wa mwalimu mmoja wa eneo hilo na mfanyabiashara maarufu katika soko la Matete. Walimu na familia zao wameathirika pakubwa kutokana na mkasa huo. Watu wengine watano waliojeruhiwa wanaendelea kupokea matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH), Eldoret. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Wilberforce Sichirani, alisema ajali hiyo ilihusisha lori kubwa lililokuwa likisafirisha saruji na kokoto kuelekea Eldoret. Alisema lori hilo liligongana na gari la abiria la North Rift Shuttle kabla ya kugonga magari mengine matatu. Abiria waliokuwa ndani ya gari aina ya Probox na gari jingine la uchukuzi wa umma pia waliathirika katika ajali hiyo. Mkasa huo umeibua tena wasiwasi kuhusu usalama katika barabara kuu ya Eldoret-Nakuru, miezi michache tu baada ya ajali nyingine katika eneo hatari la Mlima Punda kuua watu saba, wakiwemo wanafunzi wawili waliokuwa wakisafiri kuelekea nyumbani kwa likizo. Mkazi wa Koriomat, Ben Lelei, alisema eneo hilo limekuwa hatari kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva wa malori yanayosafirisha mizigo. Alilalamikia pia watu waliotumia vurugu zilizotokana na ajali hiyo kuwaibia abiria badala ya kuwasaidia manusura. "Ni jambo la kusikitisha kwamba huku baadhi yetu tukijitahidi kuwaokoa manusura, wengine walikuwa wakiiba mali za abiria waliofariki na walionurika," akasema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 02 Nov 2026 06:55:09

Winnie njiapanda kisiasa uchaguzi wa 2027 ukijongea

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Winnie Odinga, anakabiliwa na utata kuhusu upande wa kisiasa wa kuegemea anapotafuta kiti cha useneta Nairobi katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Winnie ameshindwa kuweka wazi iwapo anaunga mkono uongozi wa ODM au vuguvugu la Linda Mwananchi. Kutokuwepo kwake katika mikutano miwili muhimu Ijumaa na Jumamosi Nairobi kumezidisha maswali kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa. Winnie hakuhudhuria uzinduzi wa makao makuu ya Linda Mwananchi jijini Nairobi wala mkutano wa ODM katika uwanja wa Jacaranda ulioongozwa na viongozi wakuu wa chama hicho. Katika kuwatambulisha viongozi wa Linda Mwananchi uliofanyika Lavington Ijumaa, kiti cha mbele kilikuwa kimetengewa Winnie, lakini hakufika. Hali hiyo inatatanisha zaidi kwa sababu Oktoba 15, wakati wa kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo cha baba yake Raila Odinga, Winnie alitangaza kuwania useneta Nairobi akisema anataka kufanya hivyo pamoja na vijana. "Najua watu wengi wamekuwa wakiuliza nilipo na ninakoelekea. Leo nataka kuwajibu ili kuondoa uvumi," akasema. "Kwa kuwa Edwin Sifuna anawania wadhifa mwingine, nafasi ya useneta Nairobi iko wazi. Ndiyo maana nimeamua kuwania kiti hicho. Siendi pekee yangu, ninaenda na vijana," akaongeza. Matamshi hayo yalifasiriwa kuwa anaegemea Linda Mwananchi, lakini kutohudhuria uzinduzi wake kumezua maswali zaidi. Hata ndani ya vuguvugu hilo, Winnie anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Seneta Maalum, Crystal Asige, ambaye amekuwa akiandamana na Bw Sifuna katika ziara zake za kisiasa. Pia kuna mvutano kuhusu wagombea wa nyadhifa nyingine Nairobi. Bw Sifuna na viongozi wengine wa Linda Mwananchi wameunga mkono Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kuwania ugavana, huku aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo akilenga kiti cha mwakilishi wa kike Nairobi. Profesa Lumala Masibo anasema Winnie anaweza kuwa na nafasi ya kushinda ikiwa atajihusisha na wapigakura na kuzungumza nao badala ya kuonekana kutokuwa na msimamo. "Ikiwa Winnie atacheza karata zake vizuri ndani ya Linda Mwananchi, anaweza kushinda Nairobi. Lakini ikiwa Babu na Faith watawania, itakuwa vigumu. Winnie, Faith na Babu lazima wakae pamoja na mmoja wao ajiondoe," akasema. Katika ODM, Winnie pia anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Bw Jalangó ambaye ameungwa mkono na kaka yake Raila Junior kuwania useneta. Raila Junior amesema atabadilisha msimamo wake tu iwapo dada yake atapata tiketi ya chama. Uhusiano wa Winnie na viongozi wa sasa wa ODM umekuwa na misukosuko tangu kifo cha baba yake. Alipinga kuondolewa kwa Bw Sifuna kama katibu mkuu wa chama Februari mwaka huu. Katika mkutano wa Kamukunji, eneobunge la Kibra Januari 18, 2026, alikosoa viongozi aliowashutumu kwa kutaka kuchukua usukani wa chama baada ya kifo cha Raila. "Katika safari hii, sisi tulikuwa abiria na Baba alikuwa dereva. Siku moja tuliamka na kushtuka. Dereva alikuwa amefariki. Baadhi ya watu wakasogea mbele, wakashika usukani na kuuvuta pande tofauti," alisema. Winnie pia alizua maswali kuhusu ushirikiano wa ODM na UDA, akisisitiza kuwa maamuzi muhimu yanapaswa kuidhinishwa kwenye Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC). Zaidi ya hayo, alikosolewa na baadhi ya viongozi baada ya kumkashifu Waziri wa Fedha John Mbadi kuhusu namna anavyowahutubia viongozi wa chama akidai alikuwa akiwadharau. Changamoto zake zimeongezwa na tofauti za kifamilia. Winnie alitawazwa mrithi wa kisiasa wa Raila katika hafla ya Oktoba 4, lakini Raila Junior hakuhudhuria akisema hakujua kuhusu hafla hiyo. Kwa sasa, Winnie hajapata uungwaji mkono wa wazi kutoka kwa kiongozi mkuu wa ODM wala Linda Mwananchi. Kutohudhuria mikutano ya hivi karibuni kumeacha maswali kuhusu chama atakachotumia, upande atakaoegemea na uwezo wake wa kuunganisha wafuasi kabla ya uchaguzi wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 02 Nov 2026 05:55:17

Rekodi ya maendeleo itampa Ruto Tutam 2027 – Kindiki

NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki anatumia mafanikio ya serikali ya Kenya Kwanza katika sekta mbalimbali kuimarisha uungwaji mkono wa Rais William Ruto, huku akiweka msingi wa kusalia katika wadhifa huo kampeni za uchaguzi za 2027 zikichacha. Katika kipindi cha miaka miwili tangu achukue nafasi ya Rigathi Gachagua, Profesa Kindiki amejitahidi kuonyesha mchango wake katika kuleta udhabiti serikalini akiratibu utekelezaji wa miradi muhimu. Juhudi zake pia zinaonekana kulenga kuimarisha uungwaji mkono wa Rais Ruto katika ukanda wa Mlima Kenya, ambao ni muhimu katika mipango ya Rais kutafuta muhula wa pili. Katika tathmini ya utendaji wa serikali, Profesa Kindiki alitetea rekodi ya utawala huo akisema umepiga hatua kubwa licha ya ukosoaji kutoka kwa wapinzani. "Utawala wa Ruto umefanya vizuri zaidi ya matarajio yaliyowekewa, lakini wakosoaji hawatoi tathmini ya haki kuhusu utendakazi wake. Ukosoaji wao una nia mbaya na hauna ukweli," akasema. Alitaja kilimo kama mojawapo ya sekta ambazo serikali imepiga hatua, akisema wakulima milioni 7.9 wa mimea na wafugaji milioni tatu wamesajiliwa ili kurahisisha mipango na utoaji wa huduma. "Leo tunajua tuna wakulima wangapi, mifugo waliyo nayo, wanakoishi, mazao wanayolima na aina ya mbolea wanayohitaji," akasema. Prof Kindiki alisema bei ya gunia la kilo 50 la mbolea imepungua kutoka Sh7,000 mnamo 2022 hadi Sh2,000. Bei ya mbegu bora za mahindi pia imeshuka kutoka Sh300 hadi Sh150 kwa kilo moja. Aliongeza kuwa wakulima wa kahawa sasa wanapata kati ya Sh130 na Sh150 kwa kilo ya matunda ya kahawa, ikilinganishwa na Sh60 mnamo 2022. Katika sekta ya afya, alisema Wakenya milioni 33.3 wamejisajili kupata bima ya afya inayofadhiliwa na serikali, ikilinganishwa na milioni nane mnamo 2022. Kuhusu ajira, alitaja nafasi milioni 1.1 zilizotokana na mpango wa nyumba za gharama nafuu, nafasi 600,000 za ajira nje ya nchi na ajira 350,000 katika sekta ya kidijitali. "Tumeweza kuwasaidia vijana wengi zaidi kupata ajira na fursa za kujipatia mapato," akasema. Pia alitaja kuunganishwa kwa nyumba milioni 1.5 kwenye umeme, kuimarika kwa akiba ya fedha za kigeni na ujenzi wa uwanja wa Talanta wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000. Profesa Kindiki pia amepata sifa kutoka kwa mawaziri wanaosema amekuwa akiratibu vyema mikutano ya kamati za Baraza la Mawaziri na kuondoa vikwazo vinavyochelewesha miradi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 02 Nov 2026 04:55:43

Walimu kuendelea kufurahia mitandao ya kijamii, TSC yapata pigo

WALIMU chini wataendelea kutoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii bila hofu ya kuadhibiwa baada ya korti kukataa ombi la Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) la kuondoa agizo lililosimamisha utekelezaji wa mwongozo wenye utata kuhusu machapisho yao mtandaoni. Jaji Francis Kyambia alisema barua ya TSC haikufafanua wazi mienendo inayochukuliwa kuwa isiyo ya kitaaluma, hivyo kuwaweka walimu katika hatari ya kuadhibiwa kwa kutoa maoni kuhusu masuala ya umma. "Barua hiyo haifafanui vya kutosha mienendo inayoweza kumfanya mwalimu kuchukuliwa hatua za kinidhamu," akasema jaji huyo. Mgogoro huo unatokana na barua ya Agosti 13, 2026, iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa TSC Evaleen Mitei, iliyowatahadharisha walimu dhidi ya unyanyasaji wa mtandaoni na tabia isiyo ya kitaaluma kwenye mitandao ya kijamii. Mwalimu Fredrick Ochieng aliwasilisha kesi akisema mwongozo huo ulikuwa na lugha tata inayoweza kuingilia uhuru wa walimu kutoa maoni yao kuhusu sera za elimu, utawala na mazingira ya kazi. Pia alilalamikia kutoshirikishwa kwa walimu na wadau wengine kabla ya kutolewa kwa ilani hiyo. TSC ilisema waraka huo haukuanzisha makosa mapya bali uliwakumbusha walimu wajibu wao chini ya sheria na kanuni zilizopo. Ilisema ilichukua hatua hiyo kutokana na kuongezeka kwa matumizi mabaya ya mitandao na kwamba haikulenga kukandamiza uhuru wa kujieleza. Hata hivyo, Jaji Kyambia alisema vikwazo vya uhuru wa kujieleza lazima viwe na msingi wa kisheria na vikidhi masharti ya Katiba. Alisema TSC ilipaswa kushauriana na wadau na kutoa miongozo mahususi badala ya barua ya jumla. Aliongeza kuwa walimu wanaokiuka maadili wanapaswa kushughulikiwa mmoja mmoja chini ya kanuni zilizopo. Agizo la kusimamisha barua hiyo litaendelea kutumika hadi kesi hiyo iamuliwe. Kesi hiyo itatajwa Februari 3, 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 02 Nov 2026 03:55:05

Kalonzo asihi viongozi wa Ukambani walinde ngome yake

KIONGOZI wa chama cha Wiper Patriotic Front (WPF), Kalonzo Musyoka, amewataka washirika wake wa kisiasa kuungana na kulinda ngome yake ya Ukambani dhidi ya juhudi za Rais William Ruto kuongeza ushawishi wake katika eneo hilo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Bw Musyoka, ambaye anapigania tiketi ya urais ya upinzani, amewashutumu viongozi wake kwa kushindwa kukabiliana na washirika wa Rais Ruto wanaofanya kampeni katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni. Akizungumza Jumamosi katika hafla ya ufunguzi wa makazi ya Seneta wa Machakos Agnes Kavindu katika eneo la Mua Hills, Bw Musyoka alisema washirika wake wanapaswa kufanya kazi pamoja badala ya kila mmoja kujipigia debe kivyake. Alitaja kundi la watu watano wanaoendesha kampeni pamoja katika eneo la Machakos, likiongozwa na Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka, na kuwataka viongozi wake kuiga mtindo huo. "Badala ya kuwakabili ilhali wananchi wako nyuma yako, kila mtu anafanya kampeni kivyake. Amkeni na mshirikiane ili mniruhusu kuendeleza kampeni katika maeneo mengine ya nchi," akasema Bw Musyoka. Alisema kutohudhuria kwa wingi kwa washirika wake katika uzinduzi wa sekretarieti ya vuguvugu la Linda Mwananchi jijini Nairobi kumeathiri juhudi zake za kuonyesha kuwa upinzani umeungana kumuunga mkono. Mzozo huo unajiri wakati ambapo Bw Musyoka anakabiliwa na ushindani wa ndani ya Wiper. Machakos, kwa mfano, imekuwa na migawanyiko kati ya Bi Kavindu na Gavana Wavinya Ndeti. Hali imechangiwa na kuingia kwa afisa mkuu wa zamani wa afya wa kaunti hiyo Daniel Yumbya, wakili Musyoka Kala na afisa wa ardhi Nathaniel Nganga katika kinyang'anyiro cha tiketi ya Wiper ya useneta. Kuingia kwa aliyekuwa Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua katika kinyang'anyiro hicho pia kumeongeza ushindani. Mbunge wa Kilome, Thaddeus Nzambia, alisema Machakos imeathiriwa zaidi na juhudi za Rais Ruto kujenga ushawishi Ukambani. Alisema kati ya wabunge wanane wa kaunti hiyo, watano wanaunga mkono Rais, huku wawili pekee wakimuunga mkono Bw Musyoka. Mbunge wa Mavoko Patrick Makau amejitenga na Bw Musyoka na kujiunga na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Bw Nzambia alitaja Makueni pekee kama eneo ambalo viongozi wake bado wako na Bw Musyoka, Kulingana naye, ni mbunge mmoja pekee anayeunga mkono Rais Ruto. Bw Musyoka pia anakabiliwa na ushindani wa tiketi za Wiper katika Kitui, ambako Seneta Enoch Wambua, Mwakilishi wa Wanawake Irene Kasalu na Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu wanawania tiketi ya chama kuwania ugavana. Kuingia kwa aliyekuwa Gavana Charity Ngilu kumeongeza ushindani zaidi japo hatarajii kutumia Wiper. Bw Musyoka amekuwa akiahidi kuwa uteuzi wa Wiper utakuwa huru na wa haki, huku akiwataka washirika wake kutatua tofauti zao na kuimarisha chama.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 02 Nov 2026 02:55:48

Ruto afunika ODM

USHAWISHI unaoendelea kuongezeka wa Rais William Ruto katika ngome za jadi za ODM na uhasama kati ya viongozi wake unaendelea kulemaza umaarufu wa chama hicho. Haya yanafanyika huku ODM ikijiandaa kushiriki mazungumzo na UDA kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027. Wachanganuzi wa siasa wanasema kosa kubwa la ODM lilikuwa kuwaelekeza wafuasi wake kumuunga mkono Rais Ruto kutafuta muhula wa pili kabla ya kukubaliana kuhusu masharti ya ushirikiano wa kisiasa kati ya vyama hivyo. Wanasema ODM ilipaswa kwanza kujadiliana na UDA na kuweka masharti ya ushirikiano katika makubaliano rasmi kabla ya kuwaomba wafuasi wake kumuunga Rais. Baadhi ya viongozi wa chama hicho pia wamekuwa wakitoa ahadi binafsi zinazodhoofisha msimamo wake rasmi katika mazungumzo. Hali hii imezua hofu kuwa ODM inaweza kukosa nafasi ya kupata maslahi yake katika serikali ijayo. Tangu UDA ianze kushirikiana na marehemu Raila Odinga mnamo 2024, Rais Ruto na washirika wake wamekuwa wakijenga miundo ya kisiasa na kuwavutia viongozi wa mashinani katika maeneo yaliyokuwa ngome za ODM. Miradi ya maendeleo ya serikali pia imeongeza ushawishi wa Ruto katika maeneo hayo. Baadhi ya viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM sasa wanamuunga mkono Rais bila masharti, huku wakipinga msimamo rasmi wa chama. Hali hiyo imeonekana zaidi Nyanza, ambako viongozi kadhaa wa ODM wamekuwa wakifuatana na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, katika hafla za umma na kutangaza kumuunga mkono Rais Ruto. Ndani ya ODM sasa kuna mgawanyiko kuhusu iwapo chama hicho kinapaswa kutia saini makubaliano rasmi na UDA au kuendelea kumuunga Rais kwa nia njema ya kisiasa. Nguvu za chama katika mazungumzo pia zinadhoofishwa na viongozi wake wakuu walio katika Baraza la Mawaziri la Ruto, wakiwemo John Mbadi, Opiyo Wandayi, Wycliffe Oparanya, Beatrice Askul na Hassan Joho. Wachanganuzi wanasema mawaziri hao wana maslahi ya kisiasa katika kuhakikisha serikali ya Kenya Kwanza inaendelea kutawala baada ya 2027. Zaidi ya hayo, baadhi ya viongozi wanapigania nafasi ya mgombea mwenza wa Rais Ruto, huku Bw Mbadi akitangaza azma ya kuwania urais mnamo 2032. Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga amewaonya viongozi wa chama hicho dhidi ya migawanyiko inayoweza kudhoofisha msimamo wao katika mazungumzo. "Ninawaomba viongozi wote wa ODM kuzungumza kwa sauti moja, kama watu wamoja, chini ya uongozi mmoja. Hatuwezi kujiruhusu kugawanywa na maslahi binafsi au matamshi ya kiholela yanayodhoofisha nguvu zetu za pamoja za majadiliano," akasema Dkt Oginga akihutubia mkutano wa Jacaranda Jumamosi. "Nguvu zetu zimekuwa katika umoja wetu, na ni lazima tulinde mshikamano huo kwa kila hali," akaongeza. Dkt Oginga pia alikosoa viongozi wanaojihusisha na mipango ya urithi wa kisiasa wa 2032 badala ya kuangazia uchaguzi wa 2027. "Tuangalie vipaumbele vyetu na ninaona viongozi wengi wakipoteza muda muhimu wakijadili uchaguzi wa 2032. Huo ni usumbufu hatuwezi kumudu. Lazima tuzingatie uchaguzi wa 2027," akasema. Hata hivyo, Bw Mbadi aliwaambia wataalamu kutoka Kano kuwa anajiandaa kuwania urais mnamo 2032, akisema hatapoteza nguvu zake kutafuta nafasi ya Naibu Rais ambayo alidokeza haina mamlaka makubwa katika uendeshaji wa nchi. Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohammed, ni miongoni mwa viongozi wanaosisitiza kuwa ushirikiano wa ODM na UDA lazima uandikwe rasmi. "ODM na UDA zitakuwa na serikali ya muungano iliyoandikwa rasmi, huku vyama viwili vikishirikiana kuunda serikali ijayo. Hakuna kitu kinachoitwa nia njema pekee. Hakuna uungwaji mkono usio na masharti. Lazima makubaliano yaandikwe," akasema Bw Mohamed. Gavana wa Kisii Simba Arati pia alisisitiza kuwa ODM haitakubali kuingia serikalini bila masharti. "Watu wanasema hatupaswi kumwekea masharti Rais William Ruto. Sisi kama ODM tunasema lazima kuwe na makubaliano na masharti yatakayowezesha chama kuingia serikalini," akasema. Lakini baadhi ya viongozi, akiwemo Mbunge wa Nyando Jared Okello, wanapinga msimamo huo. Wanasema ODM inapaswa kumuunga mkono Ruto ili eneo hilo linufaike na miradi ya serikali. "Tunahitaji kufungua mioyo yetu na kuwa pamoja na Rais ili viongozi wengine wa upinzani watakapokuja watukute tayari tuko naye. Kwa sasa tunanufaika na miradi iliyoanzishwa na serikali hii, ilhali hatukumchagua," akasema Bw Okello. Alitilia shaka umuhimu wa mikataba ya kisiasa, akitaja kile alichokiita usaliti wa kisiasa uliowahi kutokea kati ya viongozi wa zamani. Mchangunizi wa siasa na mhadhiri wa chuo kikuu Amerika, Profesa David Monda, alisema timu inayoongozwa na Bw Sifuna imechukua nafasi ya kisiasa iliyokuwa ikihusishwa na kundi la Dkt Oginga. "Ni kama wao ndio wana roho ya Raila kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa wakishabikiwa," akasema Profesa Monda.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 01 Nov 2026 15:06:51

Aibu ilioje! Watu wazima kumdhalilisha mtoto anayelilia amani, afya ya akili

FATAKI   SEHEMU kubwa wiki hii midahalo ilizagaa mitandaoni ambapo watu wazima, wanawake kwa wanaume, wengi wao ambao ni wazazi, waliungana kumdhalilisha mtoto.  Endapo wewe ni mraibu wa mitandao ya kijamii, bila shaka ulikumbana na video au kusoma jumbe za watu wakimsawiri vibaya, kunuiza mambo ya soni na hata kumlaani mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14.  Mtoto huyu ambaye kosa la pekee ni ujasiri wa kusimama kidete kutetea amani na afya yake ya akili pamoja na kaka yake mdogo alijipata taabani huku watu wazima wenye akili razini na waliopevuka kiumri wakimmiminia cheche za matusi.  Kisa na maana? Alisisitiza kuendelea kuishi na baba yake wa kambo aliyewalea tangu utotoni pamoja na kaka yake mdogo baada ya wazazi wao kutengana na mama yao mzazi kufa baadaye.  Licha ya kudhalilishwa na watu walioonekana kujawa na machungu ya kushangaza, binti huyo alisema bayana ni heri afe aungane na mama yake jongomeo kuliko kwenda kuishi na baba yake mzazi baada ya kushuhudia aliyompitishia mama yake.  Ilistaajabisha sana kusikia na kusoma jumbe za watu wazima hasa kina mama ambao wangetarajiwa kufahamu uchungu wa mwana wakimuumbua mtoto huyo jinsi alivyopotoka na kubashiri atakavyoishia vibaya maishani.  Wengine bila haya walinuiza kuwa msichana huyo tayari anashiriki unyumba na baba yake mlezi ndiposa hataki kwenda kuishi na baba yake mzazi licha ya kuwa tajiri na kupatiwa usimamizi na korti.  Kanuni za utu, maadili na utamaduni wa Kiafrika unawaasa wazazi kutowasema vibaya watoto wa wenzao wakifahamu fika kwamba wao pia wanalea watoto.  Inavunja moyo kuona jinsi baadhi ya wanajamii wamezoea na kukubali maovu kiasi kwamba mazuri yanapotokea wanayapinga vikali.  Hawaamini mwanamke aliyekandamizwa na mumewe na kuachwa na watoto anaweza kumpata mwanamme atakayempenda pamoja na watoto wake na kumwoa kihalali.   Wanakereketwa maini kuona kuwa inawezekana baba au mama wa kambo kuwapenda na kuwatunza watoto waliokataliwa na kutelekezwa na wazazi wao halisi.  Wanaungulika kuwa baadhi ya watu hawapitii madhila waliyotarajia na wamesitirika kwa neema ya Maulana.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 01 Nov 2026 15:15:33

Kufuatanisha watoto kwa karibu kutafanya uzeeke upesi, utafiti

UJAUZITO NA UZAZI  KUZAA watoto wakiwa wamefuatana kwa karibu bila muda wa kutosha kabla ya kushika mimba huenda kusababisha kuzeeka haraka, utafiti mpya umefichua.  Kulingana na wataalam, kupachikwa mimba zikifuatana kwa karibu huenda kukazuia mwili kuwa na muda wa kutosha kupata afueni hivyo kusababisha mabadiliko yanayohusiana na kuzeeka kibiolojia kuongezeka.  Utafiti huo ulitathmini mabadiliko kibayolojia yanayotokea mwanamke akiwa mjamzito kwa lengo la kuboresha afya ya ujauzito ulifichua uhusiano uliopo kati ya mimba na kuzeeka.  Muda wa kupata afueni baada ya kujifungua na kubeba mimba nyingine huenda mwishowe ukaathiri afya ya mama ya muda mrefu, wataalam wanasema.  Kutungwa mimba zinazofuatana kwa karibu kunaweza kuzuia kupona kikamilifu hivyo kuruhusu baadhi ya mabadiliko kuongezeka katika mimba zitakazofuata, wanafafanua.  'Utafiti wetu wa awali umebaini kuwa umri kibiolojia huongezeka kwa muda wakati wa ujauzito, na kufikia kilele katika kipindi cha tatu au wakati wa kujifungua," wanafafanua wataalam kutoka Harvard Medical School.  "Tukikubali wazo kuwa mabadiliko haya ya muda mfupi katika umri kibiolojia hutokea, swali ni jinsi tunaweza kuhusisha mabadiliko hayo kwa mkondo wa jumla wa kuzeeka maishani."  Japo kuna uwezekano kwamba huenda mkondo wa kuzeeka kwa jumla ukabadilika, wataalam wanafafanua kuwa hii sio sawa na uharibifu kibiolojia.  "Tunafahamu kuwa sehemu fulani au kubeba mimba hadi miezi tisa ikamilike, kuna manufaa kwa maisha ya mtu binafsi."  Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa sasa linapendekeza kusubiri kwa muda usiopungua miezi 24 baada ya kujifungua salama kabla ya kutungwa mimba nyingine, kama namna ya kupunguza athari za afya kwa mama na mtoto.  "Kuna mshawasha mkubwa kuhusu kutumia nyenzo za kutathmini umri kibiolojia kuelekeza umri wa mtu binafsi kwa kiwango cha kuzuia na kinachowiana na mhusika. Kuchunguza mabadiliko wakati wa ujauzito ni njia mojawapo ya kupata uelewa wa kimsingi kuhusu kuzeeka kwa upana."  Ili kutoa mapendekezo mahsusi kuhusiana na kuzeeka kibiolojia badala ya matokeo ya ujauzito, wataalam wanasema utafiti zaidi utahitajika kupima umri wa kibiolojia kwa mimba kadhaa na kisha kufuatilia kina mama husika kwa miongo kadhaa baadaye. 

read more