T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 05 Oct 2026 02:55:27

Sifuna sasa afyatuka, azindua chama hatimaye

SENETA WA Nairobi Edwin Sifuna jana alizindua rasmi chama cha The Equitable Party (TEP) atakachotumia katika uchaguzi mkuu ujao baada ya juhudi za kusajili Linda Mwananchi Movement (LMM) kukumbwa na vikwazo vingi. Katika hatua kubwa ya kuimarisha azma yake ya kuwania urais, Bw Sifuna alichukua uongozi wa chama hicho akilenga kubadilisha jina lake ili kifahamike kama Linda Mwananchi Movement. Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) mnamo Alhamisi iliidhinisha kuhifadhi jina Linda Mwananchi Movement kwa siku 90, kwa agizo la Jopo la Kutatua Migogoro ya Vyama vya Kisiasa. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na Seneta wa Kisii Richard Onyonka. TEP ilianzishwa mnamo 2022 na Mkenya anayeishi Amerika, Dkt Gilbert Marava Shanga. Viongozi waanzilishi walijiondoa baada ya mazungumzo baina yao na mrengo wa Linda Mwananchi, na kumkabidhi Bw Sifuna uongozi wa chama hicho. Uzinduzi huo ulifanyika wiki moja tu baada ya Linda Mwananchi kwa kauli moja kumwidhinisha Seneta Sifuna kuwa kiongozi wake na mgombea wake wa urais katika uchaguzi ujao. Katika hotuba yake, Bw Sifuna alizungumzia changamoto walizokumbana nazo katika juhudi za kusajili Linda Mwananchi pamoja na kufukuzwa kwao kutoka ODM. Alishutumu ORPP akisema imekuwa ikitumiwa kama chombo cha kuzuia vyama vya upinzani kufanya shughuli zao. "Tunazindua chama chetu leo kwa sababu nyumba ambayo Baba alituachia ilitekwa," akasema Bw Sifuna, akirejelea marehemu Raila Odinga. Bw Sifuna alisema iwapo serikali itaendelea kuzuia kubadilishwa kwa jina la chama hicho, wataendelea kutumia jina la TEP hadi uchaguzi wa 2027. "Chama kitaendelea na utambulisho wake wa sasa hadi kura zipigwe 2027. Ikiwa wataendelea kuweka vikwazo kama walivyofanya awali, tutaendelea na safari yetu kwa sababu sasa tuna chama," akaongeza. Alisema chama hicho kitalenga kurejesha imani ya Wakenya katika Katiba na utawala wa sheria, huku kikihakikisha makundi yote yanatambuliwa na kupewa nafasi sawa katika uongozi na maendeleo ya nchi. "Siwezi pekee yangu kuunda vuguvugu. Vuguvugu hili ni lenu nyote mliochagua njia ya mabadiliko na ambao mapambano na kujitolea kwenu kumetengeneza safari hii," akasema. Bw Sifuna pia alieleza baadhi ya masuala ambayo anatarajia kushughulikia iwapo atapata nafasi ya kuongoza nchi, akitaja mzigo wa kodi unaowakabili wafanyabiashara wadogo na gharama ya juu ya kufanya biashara. Seneta huyo amekuwa akipata uungwaji mkono mkubwa katika kura za maoni, huku utafiti wa Tifa wa mnamo Julai ukionyesha kuwa angepata asilimia 15 ya uungwaji kitaifa iwapo angewania urais. Hii ilimweka nyuma ya Rais William Ruto pekee, ambaye alikuwa na asilimia 24. Bw Sifuna pia aliwaacha nyuma viongozi wengine wa upinzani, akiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka. Wakati wa uzinduzi huo, Sifuna aliwataka Wakenya wenye msimamo kama wake kujiunga na vuguvugu hilo. "Huu ni mwito wa umoja, kufanya kazi pamoja, kukua pamoja na kujenga vuguvugu litakalorejesha matumaini tuliyokuwa nayo mnamo 2010 tulipopitisha Katiba yetu. Vuguvugu hili linaanza na jambo moja rahisi; lazima serikali iwafanyie kazi wananchi," alisema. Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, ambaye ni msemaji wa Linda Mwananchi, alisema mipango inaendelea kubadilisha jina la chama hicho ili liakisi sura ya viongozi na wanachama wake. Gavana Orengo naye alisema yuko tayari kuunga mkono mpango wowote wa kuzuia Rais Ruto kuchaguliwa tena. "Uko mahali panapofaa, uko katika vuguvugu linalofaa na una uongozi unaofaa wa kukupeleka katika nchi ya ahadi. Tunawajibika kwa wananchi wa Kenya," akasema Bw Orengo. Seneta Osotsi alisema walifanikiwa licha ya kile alichodai kuwa ni juhudi za serikali kuwazuia kupata chama. "Tuna jina letu, mliona walivyotutesa lakini tulienda kortini na tukawashinda," alisema. Gavana Natembeya alisema Bw Sifuna na wenzake wanafaa kuingia katika mazungumzo na viongozi wengine wa upinzani na kukubali mgombea mmoja wa urais, akisema seneta huyo wa Nairobi ana uwezo wa kumkabili Rais Ruto. Bw Owino aliwataka viongozi hao kudumisha umoja na kuwashtumu baadhi ya viongozi wa ODM kwa kuwafukuza baada ya kutaka mabadiliko. Pia aliwataka viongozi hao kutumia uzoefu wa Gavana Orengo na kumteua kuwa mmoja wa washauri wakuu wa vuguvugu hilo.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 42 minutes ago

Kalonzo asihi viongozi wa Ukambani walinde ngome yake

KIONGOZI wa chama cha Wiper Patriotic Front (WPF), Kalonzo Musyoka, amewataka washirika wake wa kisiasa kuungana na kulinda ngome yake ya Ukambani dhidi ya juhudi za Rais William Ruto kuongeza ushawishi wake katika eneo hilo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Bw Musyoka, ambaye anapigania tiketi ya urais ya upinzani, amewashutumu viongozi wake kwa kushindwa kukabiliana na washirika wa Rais Ruto wanaofanya kampeni katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni. Akizungumza Jumamosi katika hafla ya ufunguzi wa makazi ya Seneta wa Machakos Agnes Kavindu katika eneo la Mua Hills, Bw Musyoka alisema washirika wake wanapaswa kufanya kazi pamoja badala ya kila mmoja kujipigia debe kivyake. Alitaja kundi la watu watano wanaoendesha kampeni pamoja katika eneo la Machakos, likiongozwa na Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka, na kuwataka viongozi wake kuiga mtindo huo. "Badala ya kuwakabili ilhali wananchi wako nyuma yako, kila mtu anafanya kampeni kivyake. Amkeni na mshirikiane ili mniruhusu kuendeleza kampeni katika maeneo mengine ya nchi," akasema Bw Musyoka. Alisema kutohudhuria kwa wingi kwa washirika wake katika uzinduzi wa sekretarieti ya vuguvugu la Linda Mwananchi jijini Nairobi kumeathiri juhudi zake za kuonyesha kuwa upinzani umeungana kumuunga mkono. Mzozo huo unajiri wakati ambapo Bw Musyoka anakabiliwa na ushindani wa ndani ya Wiper. Machakos, kwa mfano, imekuwa na migawanyiko kati ya Bi Kavindu na Gavana Wavinya Ndeti. Hali imechangiwa na kuingia kwa afisa mkuu wa zamani wa afya wa kaunti hiyo Daniel Yumbya, wakili Musyoka Kala na afisa wa ardhi Nathaniel Nganga katika kinyang'anyiro cha tiketi ya Wiper ya useneta. Kuingia kwa aliyekuwa Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua katika kinyang'anyiro hicho pia kumeongeza ushindani. Mbunge wa Kilome, Thaddeus Nzambia, alisema Machakos imeathiriwa zaidi na juhudi za Rais Ruto kujenga ushawishi Ukambani. Alisema kati ya wabunge wanane wa kaunti hiyo, watano wanaunga mkono Rais, huku wawili pekee wakimuunga mkono Bw Musyoka. Mbunge wa Mavoko Patrick Makau amejitenga na Bw Musyoka na kujiunga na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Bw Nzambia alitaja Makueni pekee kama eneo ambalo viongozi wake bado wako na Bw Musyoka, Kulingana naye, ni mbunge mmoja pekee anayeunga mkono Rais Ruto. Bw Musyoka pia anakabiliwa na ushindani wa tiketi za Wiper katika Kitui, ambako Seneta Enoch Wambua, Mwakilishi wa Wanawake Irene Kasalu na Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu wanawania tiketi ya chama kuwania ugavana. Kuingia kwa aliyekuwa Gavana Charity Ngilu kumeongeza ushindani zaidi japo hatarajii kutumia Wiper. Bw Musyoka amekuwa akiahidi kuwa uteuzi wa Wiper utakuwa huru na wa haki, huku akiwataka washirika wake kutatua tofauti zao na kuimarisha chama.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Ruto afunika ODM

USHAWISHI unaoendelea kuongezeka wa Rais William Ruto katika ngome za jadi za ODM na uhasama kati ya viongozi wake unaendelea kulemaza umaarufu wa chama hicho. Haya yanafanyika huku ODM ikijiandaa kushiriki mazungumzo na UDA kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027. Wachanganuzi wa siasa wanasema kosa kubwa la ODM lilikuwa kuwaelekeza wafuasi wake kumuunga mkono Rais Ruto kutafuta muhula wa pili kabla ya kukubaliana kuhusu masharti ya ushirikiano wa kisiasa kati ya vyama hivyo. Wanasema ODM ilipaswa kwanza kujadiliana na UDA na kuweka masharti ya ushirikiano katika makubaliano rasmi kabla ya kuwaomba wafuasi wake kumuunga Rais. Baadhi ya viongozi wa chama hicho pia wamekuwa wakitoa ahadi binafsi zinazodhoofisha msimamo wake rasmi katika mazungumzo. Hali hii imezua hofu kuwa ODM inaweza kukosa nafasi ya kupata maslahi yake katika serikali ijayo. Tangu UDA ianze kushirikiana na marehemu Raila Odinga mnamo 2024, Rais Ruto na washirika wake wamekuwa wakijenga miundo ya kisiasa na kuwavutia viongozi wa mashinani katika maeneo yaliyokuwa ngome za ODM. Miradi ya maendeleo ya serikali pia imeongeza ushawishi wa Ruto katika maeneo hayo. Baadhi ya viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM sasa wanamuunga mkono Rais bila masharti, huku wakipinga msimamo rasmi wa chama. Hali hiyo imeonekana zaidi Nyanza, ambako viongozi kadhaa wa ODM wamekuwa wakifuatana na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, katika hafla za umma na kutangaza kumuunga mkono Rais Ruto. Ndani ya ODM sasa kuna mgawanyiko kuhusu iwapo chama hicho kinapaswa kutia saini makubaliano rasmi na UDA au kuendelea kumuunga Rais kwa nia njema ya kisiasa. Nguvu za chama katika mazungumzo pia zinadhoofishwa na viongozi wake wakuu walio katika Baraza la Mawaziri la Ruto, wakiwemo John Mbadi, Opiyo Wandayi, Wycliffe Oparanya, Beatrice Askul na Hassan Joho. Wachanganuzi wanasema mawaziri hao wana maslahi ya kisiasa katika kuhakikisha serikali ya Kenya Kwanza inaendelea kutawala baada ya 2027. Zaidi ya hayo, baadhi ya viongozi wanapigania nafasi ya mgombea mwenza wa Rais Ruto, huku Bw Mbadi akitangaza azma ya kuwania urais mnamo 2032. Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga amewaonya viongozi wa chama hicho dhidi ya migawanyiko inayoweza kudhoofisha msimamo wao katika mazungumzo. "Ninawaomba viongozi wote wa ODM kuzungumza kwa sauti moja, kama watu wamoja, chini ya uongozi mmoja. Hatuwezi kujiruhusu kugawanywa na maslahi binafsi au matamshi ya kiholela yanayodhoofisha nguvu zetu za pamoja za majadiliano," akasema Dkt Oginga akihutubia mkutano wa Jacaranda Jumamosi. "Nguvu zetu zimekuwa katika umoja wetu, na ni lazima tulinde mshikamano huo kwa kila hali," akaongeza. Dkt Oginga pia alikosoa viongozi wanaojihusisha na mipango ya urithi wa kisiasa wa 2032 badala ya kuangazia uchaguzi wa 2027. "Tuangalie vipaumbele vyetu na ninaona viongozi wengi wakipoteza muda muhimu wakijadili uchaguzi wa 2032. Huo ni usumbufu hatuwezi kumudu. Lazima tuzingatie uchaguzi wa 2027," akasema. Hata hivyo, Bw Mbadi aliwaambia wataalamu kutoka Kano kuwa anajiandaa kuwania urais mnamo 2032, akisema hatapoteza nguvu zake kutafuta nafasi ya Naibu Rais ambayo alidokeza haina mamlaka makubwa katika uendeshaji wa nchi. Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohammed, ni miongoni mwa viongozi wanaosisitiza kuwa ushirikiano wa ODM na UDA lazima uandikwe rasmi. "ODM na UDA zitakuwa na serikali ya muungano iliyoandikwa rasmi, huku vyama viwili vikishirikiana kuunda serikali ijayo. Hakuna kitu kinachoitwa nia njema pekee. Hakuna uungwaji mkono usio na masharti. Lazima makubaliano yaandikwe," akasema Bw Mohamed. Gavana wa Kisii Simba Arati pia alisisitiza kuwa ODM haitakubali kuingia serikalini bila masharti. "Watu wanasema hatupaswi kumwekea masharti Rais William Ruto. Sisi kama ODM tunasema lazima kuwe na makubaliano na masharti yatakayowezesha chama kuingia serikalini," akasema. Lakini baadhi ya viongozi, akiwemo Mbunge wa Nyando Jared Okello, wanapinga msimamo huo. Wanasema ODM inapaswa kumuunga mkono Ruto ili eneo hilo linufaike na miradi ya serikali. "Tunahitaji kufungua mioyo yetu na kuwa pamoja na Rais ili viongozi wengine wa upinzani watakapokuja watukute tayari tuko naye. Kwa sasa tunanufaika na miradi iliyoanzishwa na serikali hii, ilhali hatukumchagua," akasema Bw Okello. Alitilia shaka umuhimu wa mikataba ya kisiasa, akitaja kile alichokiita usaliti wa kisiasa uliowahi kutokea kati ya viongozi wa zamani. Mchangunizi wa siasa na mhadhiri wa chuo kikuu Amerika, Profesa David Monda, alisema timu inayoongozwa na Bw Sifuna imechukua nafasi ya kisiasa iliyokuwa ikihusishwa na kundi la Dkt Oginga. "Ni kama wao ndio wana roho ya Raila kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa wakishabikiwa," akasema Profesa Monda.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Aibu ilioje! Watu wazima kumdhalilisha mtoto anayelilia amani, afya ya akili

FATAKI   SEHEMU kubwa wiki hii midahalo ilizagaa mitandaoni ambapo watu wazima, wanawake kwa wanaume, wengi wao ambao ni wazazi, waliungana kumdhalilisha mtoto.  Endapo wewe ni mraibu wa mitandao ya kijamii, bila shaka ulikumbana na video au kusoma jumbe za watu wakimsawiri vibaya, kunuiza mambo ya soni na hata kumlaani mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14.  Mtoto huyu ambaye kosa la pekee ni ujasiri wa kusimama kidete kutetea amani na afya yake ya akili pamoja na kaka yake mdogo alijipata taabani huku watu wazima wenye akili razini na waliopevuka kiumri wakimmiminia cheche za matusi.  Kisa na maana? Alisisitiza kuendelea kuishi na baba yake wa kambo aliyewalea tangu utotoni pamoja na kaka yake mdogo baada ya wazazi wao kutengana na mama yao mzazi kufa baadaye.  Licha ya kudhalilishwa na watu walioonekana kujawa na machungu ya kushangaza, binti huyo alisema bayana ni heri afe aungane na mama yake jongomeo kuliko kwenda kuishi na baba yake mzazi baada ya kushuhudia aliyompitishia mama yake.  Ilistaajabisha sana kusikia na kusoma jumbe za watu wazima hasa kina mama ambao wangetarajiwa kufahamu uchungu wa mwana wakimuumbua mtoto huyo jinsi alivyopotoka na kubashiri atakavyoishia vibaya maishani.  Wengine bila haya walinuiza kuwa msichana huyo tayari anashiriki unyumba na baba yake mlezi ndiposa hataki kwenda kuishi na baba yake mzazi licha ya kuwa tajiri na kupatiwa usimamizi na korti.  Kanuni za utu, maadili na utamaduni wa Kiafrika unawaasa wazazi kutowasema vibaya watoto wa wenzao wakifahamu fika kwamba wao pia wanalea watoto.  Inavunja moyo kuona jinsi baadhi ya wanajamii wamezoea na kukubali maovu kiasi kwamba mazuri yanapotokea wanayapinga vikali.  Hawaamini mwanamke aliyekandamizwa na mumewe na kuachwa na watoto anaweza kumpata mwanamme atakayempenda pamoja na watoto wake na kumwoa kihalali.   Wanakereketwa maini kuona kuwa inawezekana baba au mama wa kambo kuwapenda na kuwatunza watoto waliokataliwa na kutelekezwa na wazazi wao halisi.  Wanaungulika kuwa baadhi ya watu hawapitii madhila waliyotarajia na wamesitirika kwa neema ya Maulana.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Kufuatanisha watoto kwa karibu kutafanya uzeeke upesi, utafiti

UJAUZITO NA UZAZI  KUZAA watoto wakiwa wamefuatana kwa karibu bila muda wa kutosha kabla ya kushika mimba huenda kusababisha kuzeeka haraka, utafiti mpya umefichua.  Kulingana na wataalam, kupachikwa mimba zikifuatana kwa karibu huenda kukazuia mwili kuwa na muda wa kutosha kupata afueni hivyo kusababisha mabadiliko yanayohusiana na kuzeeka kibiolojia kuongezeka.  Utafiti huo ulitathmini mabadiliko kibayolojia yanayotokea mwanamke akiwa mjamzito kwa lengo la kuboresha afya ya ujauzito ulifichua uhusiano uliopo kati ya mimba na kuzeeka.  Muda wa kupata afueni baada ya kujifungua na kubeba mimba nyingine huenda mwishowe ukaathiri afya ya mama ya muda mrefu, wataalam wanasema.  Kutungwa mimba zinazofuatana kwa karibu kunaweza kuzuia kupona kikamilifu hivyo kuruhusu baadhi ya mabadiliko kuongezeka katika mimba zitakazofuata, wanafafanua.  'Utafiti wetu wa awali umebaini kuwa umri kibiolojia huongezeka kwa muda wakati wa ujauzito, na kufikia kilele katika kipindi cha tatu au wakati wa kujifungua," wanafafanua wataalam kutoka Harvard Medical School.  "Tukikubali wazo kuwa mabadiliko haya ya muda mfupi katika umri kibiolojia hutokea, swali ni jinsi tunaweza kuhusisha mabadiliko hayo kwa mkondo wa jumla wa kuzeeka maishani."  Japo kuna uwezekano kwamba huenda mkondo wa kuzeeka kwa jumla ukabadilika, wataalam wanafafanua kuwa hii sio sawa na uharibifu kibiolojia.  "Tunafahamu kuwa sehemu fulani au kubeba mimba hadi miezi tisa ikamilike, kuna manufaa kwa maisha ya mtu binafsi."  Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa sasa linapendekeza kusubiri kwa muda usiopungua miezi 24 baada ya kujifungua salama kabla ya kutungwa mimba nyingine, kama namna ya kupunguza athari za afya kwa mama na mtoto.  "Kuna mshawasha mkubwa kuhusu kutumia nyenzo za kutathmini umri kibiolojia kuelekeza umri wa mtu binafsi kwa kiwango cha kuzuia na kinachowiana na mhusika. Kuchunguza mabadiliko wakati wa ujauzito ni njia mojawapo ya kupata uelewa wa kimsingi kuhusu kuzeeka kwa upana."  Ili kutoa mapendekezo mahsusi kuhusiana na kuzeeka kibiolojia badala ya matokeo ya ujauzito, wataalam wanasema utafiti zaidi utahitajika kupima umri wa kibiolojia kwa mimba kadhaa na kisha kufuatilia kina mama husika kwa miongo kadhaa baadaye. 

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Ilani kuhusu bidhaa za kulainisha ngozi zinazosifiwa sana mitandaoni

FASHONI   KATIKA harakati za kusaka na kudadisi mbinu na bidhaa za vipodozi zinazofaa zaidi kuboresha mwonekano wa ngozi yako, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba umekumbana na aina ya ngozi inayofahamika kama "glass skini."  Glass skin jinsi tafsiri yake inavyoashiria ni ngozi laini inayong'aa na yenye maji ya kutosha inayopigiwa debe mno kwenye mitandao ya kijamii hususan Tiktok na inayohusishwa na mtindo maalum wa kutunza ngozi kutoka Korea.  Hata hivyo, ikiwa umekuwa ukisugua ngozi yako kutwa kucha na kuipaka vipodozi anuai ili kupata Glass Skin, utahitajika kuacha mara moja.  Mtindo wa kutunza ngozi wa Korea na juhudi za kufanikisha glass skin  zimeshika kasi duniani hasa kupitia Tiktok inayofikia mamilioni ya watu.  Hata hivyo, usahihi na usalama wa matini kuhusu mtindo huu wa urembo haujafanyiwa uchunguzi wa kina kulingana na wataalam.  Utafiti mpya sasa umefichua kuwa karibu video zote (asilimia 95)  zinazosambazwa kwenye Tiktok kuhusu mtindo wa kutunza ngozi wa Korea hazina maelezo kuhusu usalama na zinasheheni angalau dai moja la kupotosha.  Watafiti walitathmini video zinazohusu mtindo maarufu wa kutunza ngozi wenye asili ya Korea (Glass skin) Mei 2026 ambapo video 38 zilichunguzwa kuhusu madai ya wataalam wa ngozi, maelezo ya usalama, ubora na uwezo wa kutegemewa kwa kutumia teknolojia maalum.  Asilimia 84 ya video kuhusu glass skin zilifeli kufafanua kuhusu aina mbalimbali ya ngozi huku asilimia 45 zikipigia debe mchanganyiko wa viungo vyenye nguvu bila maelekezo mwafaka ya usalama na asilimia 32 kuahidi matokeo papo hapo.  Video zote hizo ziliorodheshwaa kuwa zisizoweza kutegemewa au zenye kiwango cha chini cha kutegemewa ambapo hakuna yoyote iliyonukuu mrejelewa kutoka nje, kulingana na utafiti huo.  "Matokeo yetu yanaonyesha pengo kubwa kati ya umaarufu wa matini hii na ubora wa maelezo yanayotolewa," walisema wataalam.  "Kufuata mitindo hii bila maelekezo yanayomfaa mtu binafsi huenda kukachangia mwasho, kuchubua ngozi kupita kiasi, chunusi kuchipuka au kuvuruga sehemu ya juu ya ngozi, hasa wakati viungo vyenye nguvu zinapochanganywa."  Ripoti hii iliwasilishwa katika Kongamano la 2026 la European Academy of Dermatology and Venereology, EADV) na iliashiria kuwa sehemu kubwa za video zinazohusu glass skin (asilimia 82) huundwa na wanamitandao mashuhuri (influencers) ambao sio wataalam wa afya.  Nembo za urembo zinajumuisha asilimia 11 huku waundaji matini wengine kuhusu urembo wakichangia asilimia nane na hakuna video yoyote kuhusu ngozi hiyo imeundwa na madaktari wa ngozi, ulisema utafiti.  "Kilichotushangaza zaidi ni jinsi maelezo ya kimsingi kuhusu usalama yalivyozidi kujumuishwa kila wakati," walifafanua wataalam.  "Ni video moja tu miongoni mwa 38 ilitaja tishio la mwasho, na ni mbili pekee ziliangazia kinga ya jua, hakuna yoyote iliyotaja tishio la ugonjwa wa ngozi wala yoyote iliyopendekeza kutafuta ushauri wa daktari wa ngozi."       

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

SHERIA: Hauwezi kutunzwa milele na mchumba wako mkitalikiana

Je, mtu aliyepewa posho ya matunzo na mahakama ana haki ya kuendelea kupokea fedha hizo maisha yake yote? Sheria ya Ndoa ya Kenya inaeleza kuwa malipo hayo yanaweza kukoma kutokana na mambo fulani. Chini ya kifungu cha 78, agizo la matunzo ya mwanandoa linaweza kukoma katika hali tofauti, kutegemea namna lilivyowekwa na mazingira ya wahusika. Kwa mfano, ikiwa agizo halikuwekewa dhamana, linaweza kukoma baada ya kifo cha aliyekuwa akipokea matunzo. Ikiwa matunzo yaliwekewa dhamana, agizo hilo hukoma baada ya kifo cha anayelipwa. Sheria pia inasema kuwa agizo la matunzo linaweza kukoma ikiwa mtu anayepokea fedha hizo baadaye ataweza kujikimu mwenyewe. Hii ina maana kuwa hali ya kifedha ya anayelipwa posho ni muhimu katika kuamua iwapo malipo yanapaswa kuendelea. Mtu ambaye awali alihitaji msaada wa kifedha anaweza baadaye kupata uwezo wa kujitegemea. Kifungu cha 79 kinaongeza kuwa agizo la matunzo hukoma anayelipwa anapoingia katika ndoa nyingine. Hata hivyo, sheria haimaanishi kuwa anayelipa anaweza kusitisha malipo kwa uamuzi wake mwenyewe kila anapohisi kuwa hali imebadilika. Kifungu cha 80 kinapatia mahakama mamlaka ya kubadilisha au kufuta agizo lililopo ikiwa imeridhika kuwa lilitokana na taarifa zisizo za kweli au kosa la ukweli, au kumekuwa na mabadiliko makubwa ya hali tangu agizo lilipotolewa. Mahakama pia inaweza kubadilisha masharti ya makubaliano ya matunzo kati ya wanandoa iwapo kutakuwa na mabadiliko makubwa ya mazingira. Kwa upande mwingine, sheria inalinda fedha za matunzo dhidi ya madai ya madeni. Kifungu cha 81 kinasema kuwa fedha hizo haziwezi kuhamishwa kwa mtu mwingine wala kutwaliwa ili kulipia deni la anayelipwa. Kifungu cha 82 kinaweka muda wa miaka mitatu wa kuanzisha kesi ya kudai kila malipo ya matunzo yaliyochelewa. Baada ya muda huo, malipo husika hayawezi kudaiwa kupitia kesi mpya. Sheria pia inaruhusu malimbikizi yanayostahili kudaiwa kuwa deni la kiraia, yakiwemo katika mazingira fulani baada ya kifo cha mhusika. Kwa hivyo, posho ya matunzo si malipo yanayoendelea bila kujali mazingira. Sheria inaweka masharti ya kukomeshwa, kubadilishwa au kufutwa kwa agizo la kuyalipa. Hata hivyo, uamuzi wa kusitisha au kubadilisha agizo kwa sababu ya mabadiliko ya hali unapaswa kufuata utaratibu wa mahakama.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

Jithamini mwanamume, usirudie mwanamke aliyekusaliti

Katika maisha, mwanaume anahitaji kuwa na misimamo, kujithamini na kujua namna ya kushughulika na watu wanaomzunguka. Mafanikio hayaji kwa bahati pekee, bali pia yanahitaji nidhamu, bidii na uwezo wa kufanya maamuzi yanayofaa. Mtaalamu wa masuala ya ustawi wa maisha Nelson Kawei anaorodhesha mambo kadhaa ambayo yanaweza kumsaidia mwanaume kujijenga na kuboresha maisha yake.  Usirudie mwanamke aliyekusaliti Mapenzi yanahitaji uaminifu. Ikiwa mtu amekusaliti na kuvunja imani yako, usikimbilie kurudiana naye bila kutathmini kilichotokea na kama uhusiano huo unaweza kujengwa upya.  Usikubali kudharauliwa Jithamini na weka mipaka katika mahusiano yako. Heshima inapaswa kuwa ya pande zote, na si lazima uvumilie matusi au unyanyasaji ili kudumisha uhusiano.  Simama unapomsalimia mtu kwa mkono Kusimama unapopeana mikono kunaweza kuonyesha adabu na heshima, hasa unapokutana na mtu katika mazingira rasmi.  Usiishi kwa kutaka kuwafurahisha watu Usitumie pesa ambazo huna ili kuonekana tajiri au kufurahisha marafiki. Ishi kulingana na uwezo wako na uweke kipaumbele katika mahitaji muhimu.  Usile kipande cha mwisho cha chakula ambacho hukununua Zingatia hisia zao. Kutokula kilichobaki ni ishara ya kujali na kushirikiana. Daima jitahidi kuwa bora zaidi Weka malengo ya kuboresha maisha yako kielimu, kikazi, kifedha na kibinafsi. Usiridhike na hali uliyonayo ikiwa unaweza kufanya zaidi. Walinde walio nyuma yako na uwaheshimu walio kando yako Wasaidie wanaokutegemea na uwaheshimu marafiki, wafanyakazi wenzako na watu wanaosafiri nawe katika safari ya maisha. Fikiri kabla ya kujibu swali Unapoulizwa swali, tulia kwa sekunde chache kabla ya kujibu. Hilo linaweza kukusaidia kupanga mawazo na kuepuka kusema jambo kwa pupa. Usilazimishe mahusiano Mapenzi yanahitaji ridhaa na juhudi za pande zote. Usijishushe kwa kuomba mtu akupende au abaki nawe ikiwa hataki kuwa katika uhusiano huo. Fanya mazoezi mara kwa mara Tenga muda wa kufanya mazoezi angalau mara nne kwa wiki, kulingana na afya na uwezo wako. Mazoezi yanaweza kusaidia kuimarisha mwili na kuboresha ustawi wa jumla.  Usijilazimishe kwenda mahali ambapo hujaalikwa Ikiwa marafiki wamepanga shughuli bila kukualika, usijilazimishe kujiunga nao. Heshimu mipaka yao na tafuta shughuli zinazokufurahisha.  Beba kiasi cha pesa taslimu Ingawa malipo ya simu na kadi yamerahisisha maisha, kuwa na kiasi kidogo cha pesa taslimu kunaweza kukusaidia pale njia hizo zinapokosa kufanya kazi. Vaa vizuri kulingana na shughuli Huhitaji nguo za bei ghali ili uonekane nadhifu. Chagua mavazi safi, yanayokutosha vizuri na yanayofaa tukio husika. Sikiliza kwa makini unapozungumza na watu Tikisa kichwa kuonyesha kuwa unafuatilia mazungumzo na tazama mtu usoni kwa namna inayofaa. Hata hivyo, epuka kumkodolea macho kiasi cha kumfanya akose raha. Tafuta njia mbalimbali za kupata mapato Usitegemee kwa chanzo kimoja cha mapato ikiwa una nafasi ya kufanya zaidi. Unaweza kujifunza ujuzi mpya, kuanzisha biashara ndogo au kufanya kazi ya ziada kulingana na uwezo wako. Kujiheshimu, afafanua Kawei, si kuwadharau wengine au kujifanya mkamilifu. Ni kujua thamani yako, kuheshimu watu, kutumia pesa kwa busara na kujitahidi kuboresha maisha yako kila siku.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Mateso ya kustaafu:Yafichuliwa wastaafu 80,000 wanaishi kwa pensheni ya Sh4,000 kwa mwezi

ZAIDI ya wafanyakazi 80,000 waliostaafu serikalini wanapokea pensheni ya Sh4,000 pekee kwa mwezi, huku wabunge wakishinikiza serikali kuongeza malipo hayo ili kukabiliana na gharama ya maisha inayozidi kupanda. Kamati ya Bunge kuhusu Maombi ya Umma imeitaka Wizara ya Fedha na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kuwasilisha ndani ya miezi miwili ripoti kuhusu fedha zinazohitajika kuongeza pensheni ya wastaafu 319,207. Hatua hiyo inafuatia malalamishi ya wastaafu kuwa wamekuwa wakilipwa viwango vya chini kwa miaka mingi licha ya kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma muhimu. Malalamishi hayo yaliwasilishwa bungeni na Chama cha Kitaifa cha Wastaafu wa Utumishi wa Umma (KNAPS), tawi la Kericho, kinachowakilisha wastaafu kote nchini. Chama hicho kinasema takriban asilimia 25 ya wanachama wake, sawa na watu 80,000, hupokea chini ya Sh4,000 kila mwezi, kiasi ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji yao ya kimsingi. Wastaafu hao wanataka mifumo ya zamani ya pensheni isiyokuwa na michango ya wafanyakazi iunganishwe na mfumo wa sasa wa Public Service Superannuation Scheme (PSSS), ambao wanadai una manufaa bora. Pia wanataka pensheni zao ziongezwe mara kwa mara ili kuendana na kupanda kwa gharama ya maisha, pamoja na sheria kurekebishwa ili kuwalinda wao na familia zao. Katika ripoti iliyowasilishwa Bungeni Septemba 30, kamati ilipendekeza Wizara ya Fedha kushirikiana na SRC kufanya tathmini ya gharama za pensheni kila baada ya miaka mitatu. Tathmini ya kwanza inapaswa kukamilika kufikia Desemba 31, 2026. Hata hivyo, pendekezo la kuunganisha mifumo hiyo limekabiliwa na upinzani kutoka kwa taasisi mbalimbali za serikali kutokana na gharama kubwa inayoweza kuhusika. Mamlaka ya Kusimamia Manufaa ya Wastaafu (RBA) iliambia kamati kuwa kuunganisha mifumo hiyo kutahitaji serikali kwanza kulipa madeni ya pensheni yaliyolimbikiza, yanayokadiriwa kuzidi Sh1 trilioni. Mkurugenzi Mkuu wa RBA Charles Machira alisema tathmini ya Wizarea ya Fedha ya Juni 2024 ilionyesha kuwa madeni hayo yalikuwa yamezidi Sh1 trilioni. Wizara inasema inatumia takriban Sh7.8 bilioni kila mwezi kulipa wastaafu 319,207, sawa na Sh93.7 bilioni kwa mwaka. Mfumo wa zamani haukuwa ukikata michango kutoka mishahara ya wafanyakazi. Badala yake, pensheni ziliamuliwa kwa mujibu wa sheria zilizokuwepo wakati huo. Mfumo mpya ulioanza Januari 2021 unawataka wafanyakazi kuchangia asilimia 7.5 ya mishahara yao kila mwezi, huku serikali ikiongeza kiasi sawa. Kufikia Juni 2026, wafanyakazi 529,635 walikuwa wamejiunga na mfumo huo, wakiwa wameweka akiba ya Sh343.75 bilioni. SRC imesema ongezeko lolote la pensheni lazima lizingatie uwezo wa kifedha wa serikali. Idara ya Utumishi wa Umma pia imeonya kuwa kuongeza pensheni kutaleta mzigo wa muda mrefu kwa serikali, hivyo ni lazima kuhakikisha malipo hayo yanaweza kudumishwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Sababu za wakazi wa Runda kukataa kanisa la orofa tisa la nabii Owuor

WAKAZI wa mtaa wa kifahari wa Runda, Nairobi, wamepinga mpango wa mhubiri David Owuor wa kujenga kanisa la orofa tisa katika mtaa huo, wakisema mradi huo utazidisha mafuriko, msongamano wa magari na kuvuruga amani yao. Wakazi hao wanataka kanisa la Repentance and Holiness Ministry lijengwe kwa kuzingatia kanuni za eneo hilo, ambazo wanadai zinahitaji majengo ya makazi kuwa na orofa tatu au chini. Wakazi kutoka vyama 13, vinavyowakilisha zaidi ya watu 100 wanaoishi kando ya Barabara ya Kwaheri, wamewasilisha malalamishi rasmi kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu, wakipinga mradi huo unaopanga katika ekari tatu. Wakazi hao wanahofia kuwa jengo hilo refu litavuruga faragha ya majirani, kuzuia mwanga wa jua kuingia katika nyumba zilizo karibu na kubadilisha mandhari ya mtaa huo. Pia wanasema eneo hilo hukumbwa na mafuriko wakati wa mvua na ujenzi wa kanisa hilo unaweza kuzidisha tatizo hilo kutokana na maji ya mvua kutoka kwenye jengo na kumwagika katika makazi jirani. Wakazi hao wanadai kuwa kanisa halijatoa mpango unaokubalika wa mitaro ya maji ya mvua wala wa kushughulikia maji taka, kwa kuwa ardhi hiyo haijaunganishwa na mfumo wa maji taka wa umma. Barabara ya Kwaheri ina upana wa takriban mita tisa, hali ambayo wakazi wanasema haitatosha kuhudumia magari ya wakazi na maelfu ya waumini wanaotarajiwa kuhudhuria ibada. Pia wanahofia kelele zitakazosababishwa na ibada za usiku, maarufu kama kesha, ambazo zinaweza kuwasumbua watoto wa shule na wazee. Kanisa hilo lilinunua ardhi hiyo ya ekari tatu kutoka kwa wamiliki wa shamba la kahawa na mwezi Machi likaomba kubadilisha matumizi yake kutoka kilimo hadi taasisi ya kidini, ofisi na makazi ya wageni. Hata hivyo, kamati ya kiufundi ya Kaunti ya Kiambu ililitaka kanisa kufanya mikutano ya ushirikishaji wa umma na kutoa maelezo kuhusu matumizi ya vyumba vya wageni. Katika mkutano wa Oktoba 22, kanisa liliwasilisha michoro ya usanifu wa jengo hilo kwa wadau. Mshauri wa usanifu aliyeajiriwa na kanisa anasema eneo hilo limetengwa kwa matumizi mseto, hivyo mradi huo unapaswa kuruhusiwa. Lakini wakazi wanasisitiza kuwa eneo hilo limekusudiwa makazi ya watu wachache, na kwamba kuwepo kwa shule na taasisi nyingine zisizo za makazi hakumaanishi kanisa hilo liruhusiwe kujengwa bila kuzingatia kanuni. Waziri wa ardhi wa Kaunti ya Kiambu, Salome Wainaina, amesimamisha shughuli zozote za maendeleo katika ardhi hiyo hadi kanisa na wakazi wafikie makubaliano.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Sababu za wadau wa elimu kupinga mageuzi ya Ruto

WADAU wakuu katika sekta ya elimu wamepinga miswada saba ya mageuzi ya elimu inayosukumwa na Rais William Ruto, wakisema inaweza kufuta mafanikio yaliyopatikana iwapo haitafanyiwa marekebisho. Miswada hiyo, ambayo iko katika hatua ya kukusanya maoni ya umma kupitia Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa, inalenga kubadilisha usimamizi wa shule, mafunzo ya walimu, ufadhili wa wanafunzi na uteuzi wa nafasi katika vyuo vikuu na taasisi za kiufundi. Vyama vya walimu, wahadhiri, wazazi na wamiliki wa shule za kibinafsi wamewasilisha mapendekezo yao, wakishinikiza wabunge kuyazingatia kabla ya kupitisha sheria hizo. Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) kinataka sheria inayopendekezwa kuhusu ufadhili wa elimu ya juu ilinde wanafunzi ambao tayari wanapokea mikopo na ufadhili wa masomo, pamoja na haki za wafanyakazi wa vyuo vikuu. Chama hicho pia kinataka serikali kufanya tathmini ya gharama za utekelezaji wa mfumo huo kabla ya kuanza kutumika. Kinasema mswada huo unaangazia zaidi ufadhili wa wanafunzi huku ukipuuza gharama ya kuendesha vyuo vikuu na kulipa wahadhiri. UASU pia inapinga sharti linalotaka wahitimu kuanza kurejesha mikopo ndani ya mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo. Inataka muda huo uanze tu baada ya mhitimu kupata kazi yenye mapato ya uhakika. Chama hicho kinataka pia kuwakilishwa katika bodi za Mamlaka ya Ufadhili wa Elimu ya Juu na Huduma ya Kitaifa ya Uteuzi wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kiufundi (KUCCPS). Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kati (KUPPET) pia kimepinga muda wa mwaka mmoja wa kuanza kulipa mikopo, kikisema ni mgumu kwa wahitimu katika soko la ajira lenye ushindani. Kinataka ufadhili huo uwe na chanzo cha wazi cha fedha na kiwango kisichozidi asilimia 2.5 ya mapato ya kila mwaka ya ushuru yanayokusanywa na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA). KUPPET pia inataka serikali itoe ufadhili kupitia ruzuku, ufadhili wa masomo na mikopo kulingana na mahitaji ya wanafunzi. Chama cha Wakufunzi wa Vyuo vya Kiufundi na Mafunzo ya Ufundi (KUTVET) kinasema mfumo unaopendekezwa hauzingatii tofauti za gharama za kozi mbalimbali. Kinasema kozi kama uhandisi wa magari, uchomeleaji, umeme na ujenzi zinahitaji vifaa na mafunzo ya vitendo ambayo hayawezi kugharimiwa kwa kiwango sawa na kozi zinazofundishwa darasani pekee. Chama hicho kinataka fedha zitumike pia kununua mashine, vifaa vya usalama, teknolojia za kisasa na kugharamia mafunzo ya vitendo viwandani. Wakati huo huo, Chama cha Walimu wa Shule za Msingi (KNUT) kimepinga pendekezo linalotaka walimu kutoshiriki shughuli nyingine za kujipatia mapato wanapohudumu katika Tume ya Huduma za Walimu (TSC). KNUT kinasema tume hiyo haipaswi kudhibiti shughuli za walimu nje ya saa rasmi za kazi. Kwa upande wake, Chama cha Shule za Kibinafsi nchini kinataka sheria itambue shule za Sekondari Msingi zinazojitegemea, badala ya kuzilazimisha kuwa na sehemu ya shule za msingi za kawaida. Pia kinataka wanafunzi wa shule za kibinafsi waruhusiwe kunufaika na ufadhili wa masomo na basari za serikali bila kubaguliwa kwa sababu tu wanasomea katika taasisi hizo. Chama cha Kitaifa cha Wazazi kinataka wazazi wapewe nafasi kubwa zaidi katika maamuzi ya elimu kupitia marekebisho ya sheria ya elimu ya msingi. Wadau hao wanataka maoni yao yazingatiwe kabla ya miswada hiyo kuwasilishwa bungeni kwa hatua zaidi. Kamati ya Bunge inatarajiwa kukamilisha zoezi la kupokea maoni Alhamisi ijayo, baada ya kusikiliza TSC na Baraza la Magavana.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Vizingiti vinavyokabili ODM ikiendea nusu mkate na UDA

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinaingia katika hatua muhimu ya hesabu zake za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, kikitaka kugawana mamlaka kwa usawa na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) katika muungano unaopendekezwa kumuunga mkono Rais William Ruto. Hata hivyo, huku kiongozi wa ODM Oburu Oginga akisisitiza kuwa chama hicho kinastahili nusu ya mamlaka  kwenye makubaliano na UDA, mgawanyiko wa ndani na kutokubaliana kuhusu ushirikiano na Ruto vinatishia kudhoofisha msimamo wake katika mazungumzo. ODM inataka kuwa mshirika sawa na UDA badala ya kuwa chama kidogo katika muungano unaotawaliwa na chama cha rais. Lakini kutaka nusu ya mamlaka na kuhakikisha inapata mgao huo ni mambo mawili tofauti. Oburu alieleza msimamo huo hadharani Juni 2026, akisema makubaliano yoyote ya kabla ya uchaguzi kati ya ODM na UDA lazima yazingatie kanuni ya kugawana mamlaka kwa asilimia 50 kwa kila upande. "Tutakapounda makubaliano ya muungano na UDA, yatategemea mgao wa asilimia 50 kwa kila upande, jambo litakalotufanya kuwa imara zaidi. Hata urais tutaujadili; hatutaacha kiti chochote bila mazungumzo," alisema Oburu. Wakizungumza wakiwa Turkana wiki jana, viongozi wa ODM walioongozwa na Mwenyekiti Gladys Wanga walisisitiza kuwa lazima makubaliano ya UDA yakitwe kwa msingi wa kugawana mamlaka  nusu kwa nusu. Kauli hizo zinaashiria kuwa ODM haitaki mazungumzo yahusu nyadhifa za Baraza la Mawaziri pekee, bali pia urais na nafasi nyingine muhimu katika serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi. Hata hivyo, chama hicho kinapaswa kuthibitisha kuwa kina uwezo wa kuhamisha uungwaji mkono wake wa kisiasa hadi kwenye kura, kudumisha umoja na kuhakikisha wafuasi wake wa jadi wanabaki pamoja. Kifo cha Raila Odinga Oktoba 15, 2025, kiliondoa  mwanasiasa aliyekuwa mhimili mkuu wa ODM katika mazungumzo ya kisiasa kwa miongo kadhaa. Raila hakuwa tu kiongozi wa chama, bali pia alikuwa mhamasishaji wa wafuasi, mpatanishi wa makundi yaliyokinzana na mtu aliyekuwa na uwezo wa kuunganisha viongozi wenye misimamo tofauti. Ushawishi wake ulitokana na uzoefu wa kushiriki chaguzi kadhaa, mtandao wa kisiasa aliojenga  kwa miaka mingi na uwezo wa kujadiliana na washirika akiungwa mkono na maelfu ya wafuasi nyuma yake. Oburu sasa amebeba jukumu la kukiongoza chama katika kipindi hicho cha mpito, lakini changamoto yake ni kuonyesha kuwa nguvu za ODM zinaweza kudumu hata bila mtu aliyeunganisha makundi mbalimbali. ODM bado ina viongozi waliochaguliwa, mitandao ya kisiasa katika maeneo tofauti na utambulisho wa kitaifa uliojengwa kwa miaka mingi. Hata hivyo, rasilimali hizo zitakuwa na thamani katika mazungumzo iwapo chama kitaonyesha kuwa kinaweza kuendelea kuwa na umoja kuelekea 2027. Mazungumzo ya ODM na UDA yalipiga hatua nyingine Agosti 2026, Ruto na Oburu walipotangaza timu za kushughulikia mfumo wa kugawana mamlaka na manifesto ya pamoja ya muungano unaopendekezwa kwa uchaguzi wa 2027. Hatua hiyo ilionyesha kuwa mazungumzo hayahusu tena iwapo vyama hivyo vitashirikiana, bali masharti vitakayokubaliana na namna yatakavyotekelezwa. Kwa ODM, madai ya kugawana serikali kwa asilimia 50 ni msimamo wa mazungumzo, ambao haijulikani ikiwa utakubaliwa na UDA. Kulingana na viongozi wa chama hicho cha chungwa, usawa huo utahusu idadi ya mawaziri, nyadhifa kuu serikalini, uongozi wa Bunge, maeneo ya kuwania viti na kushiriki katika maamuzi muhimu ya serikali. "Masuala hayo yanahitaji kujadiliwa tofauti kwa sababu kupata idadi sawa ya mawaziri hakumaanishi moja kwa moja kuwa vyama vina mamlaka sawa katika kufanya maamuzi," asema mchanganuzi wa siasa Jimmy Opiyo. Suala jingine ni kugawana maeneo ya kisiasa, maarufu kama zoning, ambapo vyama hukubaliana kutosimamisha wagombeaji wanaoshindana katika maeneo fulani. ODM imetaka suala hilo liwe sehemu ya makubaliano, lakini UDA imeonyesha kutokuwa tayari kulikubali, kulingana na taarifa kuhusu mazungumzo ya vyama hivyo. Urais nao ni suala nyeti zaidi. Oburu amesema haupaswi kuachwa nje ya mazungumzo, lakini muungano unaopendekezwa pia unalenga kumuunga mkono Ruto katika uchaguzi wa 2027. Hali hiyo inaibua swali muhimu: Je, ODM inajadili masharti ya kumuunga mkono Ruto au inataka muungano ambao utawezesha kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya uongozi wa nchi? Opiyo anasema jibu litategemea masharti yatakayowekwa katika makubaliano ya mwisho. Anasema kuibuka kwa vuguvugu la Linda Mwananchi kulidhoofisha nguvu za ODM katika majadiliano. "Mgawanyiko huu unaweza kudhoofisha uwezo wa ODM kuwasilisha msimamo mmoja katika mazungumzo na UDA.Changamoto ya ODM si kupata nafasi serikalini pekee, bali kuhakikisha kuwa makubaliano yatakayofikiwa yana manufaa kwa chama na wafuasi wake," asema. Kushiriki katika serikali kunaweza kupatia ODM nafasi ya kushawishi sera, kugawana nyadhifa za uongozi na kushiriki katika maamuzi ya kitaifa. ODM inapaswa pia kutofautisha maslahi ya viongozi binafsi na yale ya wananchi wanaoiunga mkono. Kupata nyadhifa serikalini kunaweza kuwa na thamani kwa viongozi, lakini chama kinahitaji kuwaeleza wananchi namna ushirikiano huo utakavyoboresha maisha yao, utawala na uwakilishi wa kisiasa. "Takwa la kugawana serikali kwa asilimia 50 halitakuwa na nguvu bila ODM kuonyesha kuwa ina uungwaji mkono wa kutosha, inaweza kudumisha wapigakura wake na ina umuhimu wa kisiasa katika uchaguzi ujao," asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki. Anasema mazungumzo hayo yanapatia ODM fursa ya kulinda ushawishi wake katika serikali ya kitaifa, lakini pia yana hatari ya chama kuishia kumuunga mkono Ruto bila kupata dhamana ya kutekelezwa kwa madai yake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Vigogo wageuza mikakati kuelekea 2027, watua vijijini naTikTok kujipigia debe

CHINI ya mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, wanasiasa wanaowania urais na vyama vyao vya kisiasa wamebadili mbinu zao, wakielekeza nguvu katika vijiji na maeneo ya mashambani kuwafikia wapiga kura. Badala ya kutegemea mikutano mikubwa katika miji na ushawishi wa vigogo wa kisiasa, viongozi wameanza kuingia katika vijiji vidogo, vibanda vya biashara na makazi ya kawaida ili kujenga uhusiano wa karibu na wananchi. Rais William Ruto na viongozi wa upinzani wameongeza ziara za mashinani, wakijitahidi kuwashawishi wapiga kura moja kwa moja kabla ya kampeni rasmi kuanza. Rais Ruto, anayelenga muhula wa pili, ameonekana akila katika vibanda vya kando ya barabara, kuingia manyattani na kutembelea nyumba za kawaida za mashambani. Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, ametembelea zaidi ya kaunti 20 na kuandaa mikutano ya hadhara zaidi ya 50 katika maeneo mbalimbali. Katika ziara zake za Narok na Kajiado Agosti na Septemba 2026, alitembelea maeneo ya mashambani yakiwemo Olokurto, Olpusimoru, Ololulung'a na Ewaso Ng'iro, kabla ya kuelekea Rombo, Loitokitok, Namanga na Kimana. Pia ametembelea maeneo ya mbali ya Pokot Magharibi, yakiwemo Sigor, Kacheliba na Kapenguria, akizindua miradi na kuwahimiza wafuasi wake kujiandikisha kupiga kura kwa wingi. Katika Ukambani, alitembelea Mwingi, Kitui West, Kibwezi, Matuu na Mwala. Mwingi Kaskazini, nyumbani kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, alikagua mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Tseikuru, akazindua barabara na kutoa hati za kumiliki ardhi. Ziara hizo pia zimefika Pwani, Magharibi na Nyanza, maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa ngome za upinzani. Rais ametembelea kaunti za Kisumu, Migori, Siaya na Homa Bay, akitangaza miradi ya masoko, maji, umeme na elimu. Katika ziara ya Pwani iliyochukua siku nane, alitembelea Taita Taveta, Mombasa, Kwale, Kilifi, Lamu na Tana River, ambako alisimamia utoaji wa karibu hati 200,000 za kumiliki ardhi. Upinzani nao haujachelewa. Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ametembelea kaunti 15 katika miezi mitatu, akiandaa mikutano 36 ya mashinani. Vuguvugu la Linda Mwananchi, linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna pamoja na Mbunge Babu Owino na Seneta Godfrey Osotsi, limefanya mikutano sita katika Nyanza, Magharibi na Pwani. Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) cha Rigathi Gachagua kimefanya mikutano 24 katika kaunti mbalimbali, zikiwemo Nakuru, Nyandarua, Laikipia, Kiambu, Kajiado, Nyeri na Murang'a. Mchambuzi wa siasa Profesa XN Iraki anasema mbinu hiyo inaweza kumsaidia Rais Ruto kwa sababu kukutana ana kwa ana na wapiga kura huwafanya wamzoee na kujenga uhusiano naye. Hata hivyo, Dkt Peter Mbae wa DCP anasema ziara hizo huenda zisibadilishe hisia za wananchi wanaokabiliwa na gharama kubwa ya maisha, mzigo wa ushuru na ahadi za kampeni ambazo hazijatekelezwa. Mchambuzi mwingine, Profesa Tom Nyamache, anasema Pwani, Magharibi, jamii ya Maa na Turkana zitasalia kuwa maeneo muhimu katika uchaguzi huo. Wakati huohuo, wataalamu wa utawala wanaonya kuwa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana unaweza kuwafanya washawishike kutumiwa vibaya kisiasa au kuhusishwa na ghasia za uchaguzi. Mbali na mikutano ya mashinani, mitandao ya kijamii kama TikTok, Facebook, X na WhatsApp inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kampeni za 2027. Mwanasheria na mchambuzi wa sera Steve Kabita anasema mitandao hiyo itakuwa jukwaa kuu la kujenga mitazamo ya kisiasa na kushawishi wapiga kura. Mwanaharakati Morara Kebaso anasema wapiga kura wa 2027 watakuwa na uelewa mkubwa zaidi wa masuala ya kisiasa kutokana na elimu ya uraia na matumizi ya teknolojia. Ripoti ya Thomson Reuters Foundation pia inaonyesha kuwa mitandao ya kijamii itakuwa na nafasi kubwa katika uchaguzi ujao, huku kampeni zikielekea zaidi kwenye majukwaa ya kidijitali. Hata hivyo, viongozi wa kijamii na kidini wanawahimiza wananchi kutathmini sera, mipango ya maendeleo na uwezo wa wagombeaji kutatua matatizo yao badala ya kushawishiwa na umaarufu au misimamo ya vyama.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Wabunge walivyokataa mapendekezo ya muafaka wa Ruto na Raila

WABUNGE wa Bunge la Kitaifa wamekataa marekebisho yaliyopendekezwa na Seneti kuhusu kuhesabu na kupeperusha matokeo ya uchaguzi wa urais kwa njia ya kielektroniki, hatua iliyozua malumbano bungeni. Mapendekezo hayo yalitokana na mazungumzo ya kisiasa kati ya timu za Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, yakilenga kuzuia ucheleweshaji wa kutangaza mshindi wa urais na kuimarisha uwazi katika uchaguzi. Seneti ilikuwa imependekeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itume matokeo ya kila kituo cha kupigia kura ndani ya saa mbili baada ya kutangazwa. Matokeo hayo yangetumwa kwa vituo vya kujumlisha kura vya maeneo bunge, kituo cha kitaifa, wagombeaji, maajenti wao na waangalizi wa uchaguzi. Pia, mapendekezo hayo yalitaka IEBC kuanzisha mfumo wa kurusha moja kwa moja matokeo ya urais yanayotangazwa katika vituo vya kujumlisha kura vya maeneo bunge, ikiwemo kura za Wakenya wanaoishi ughaibuni. Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, alikuwa amependekeza matokeo hayo yaonyeshwe moja kwa moja ili wananchi waweze kuyafuatilia na kuyalinganisha na matokeo ya mwisho. Hata hivyo, wakati wa kujadili Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi 2024 ulioanzia Seneti , Mbunge wa Homa Bay Town Peter Kaluma, akiungwa mkono na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung'wah, alifanikiwa kushawishi Bunge kufuta mapendekezo hayo. Hatua hiyo iliwakasirisha baadhi ya wabunge waliotaka sheria ibadilishwe ili kuondoa utata kuhusu uwasilishaji wa matokeo. Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alihoji kwa nini Bunge lilikuwa likifuta mapendekezo yaliyotokana na mazungumzo ya Kamati ya  Mdahalo wa Kitaifa (NADCO). Alisema Kenya haipaswi kusubiri siku saba au nane kutangazwa kwa matokeo ya urais wakati teknolojia inaweza kusaidia kuyawasilisha haraka. Mzozo huo unatokana pia na uamuzi wa Mahakama Kuu wa Aprili 6, 2026, ambapo Jaji Chacha Mwita alitangaza kifungu cha sheria kilichoruhusu matokeo kurushwa moja kwa moja kwa madhumuni ya kuwafahamisha wananchi kuwa kinyume cha Katiba. Mahakama ilisema matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura ndiyo msingi wa matokeo ya mwisho na hayawezi kuchukuliwa kuwa taarifa za kuwafahamisha wananchi pekee. Hata hivyo, Bunge lilisema halijapiga marufuku kupeperushwa kwa matokeo moja kwa moja, bali limehifadhi utaratibu uliopo katika Sheria ya Uchaguzi. Wabunge pia walisema mabadiliko makubwa ya sheria za uchaguzi miezi michache kabla ya uchaguzi wa 2027 yanaweza kukiuka mapendekezo ya ripoti ya Kriegler, iliyotaka sheria hizo zisibadilishwe ndani ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 01 Nov 2026 02:55:13

Wazee wazidisha juhudi kupatanisha Uhuru na Gachagua

JUHUDI mpya za kuunganisha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP), Rigathi Gachagua, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 zinaendelea kushika kasi, huku jina la Naibu Rais Kithure Kindiki likiibuka katika mpango huo. Hii ni mara ya nne tangu 2022 ambapo viongozi hao wawili, waliokuwa washirika wa karibu kabla ya kuwa mahasimu wa kisiasa, wanashinikizwa kuweka tofauti zao kando ili kuunganisha eneo la Mlima Kenya. Kwa mujibu wa taarifa tulizopata, mkutano wa hivi karibuni ulipangwa kufanyika Jumanne lakini Bw Kenyatta hakupatikana. Mlezi wa kitaifa wa baraza la wazee la Kiama Kia Ma, Bw Kung'u Muigai, alithibitisha kuwa maandalizi ya kuwakutanisha viongozi hao yanaendelea. Alisema wanataka pia Prof Kindiki kuhudhuria ili viongozi wakuu wa eneo hilo wajadili mustakabali wake wa kisiasa. "Tunakaribia kufanikiwa. Tunawaomba muwe na subira," alisema, akiongeza kuwa Bw Kenyatta ndiye atakayetoa tarehe ya mkutano huo. Jaribio la kwanza lilifanyika 2022, wakati Bw Gachagua alipotakiwa kushirikiana na Bw Kenyatta, aliyekuwa rais wakati huo, kuunganisha Mlima Kenya nyuma ya mgombea mmoja wa urais. Hata hivyo, Bw Kenyatta aliunga mkono Raila Odinga wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, huku Bw Gachagua akiwa katika kambi ya William Ruto wa Kenya Kwanza. Bw Gachagua alipuuza wito huo na akaungana na  Dkt Ruto kushinda  uchaguzi. Aliteuliwa naibu rais lakini akatimuliwa mamlakani Oktoba 2024. Kabla ya kuingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2017, Bw Gachagua alikuwa msaidizi binafsi wa Bw Kenyatta kwa miaka 20. Baadaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Mathira na kupanda hadi wadhifa wa naibu rais. Uhusiano wao ulizorota wakati wa kampeni na zaidi baada ya Bw Gachagua kuwa naibu rais. Aliongoza mashambulizi ya kisiasa dhidi ya biashara za familia ya Kenyatta na miradi yake ya urithi. Mzozo ulifikia kilele wakati shamba la Northlands la familia hiyo, Ruiru, lilipovamiwa, mifugo kuibwa na sehemu ya ardhi kuchomwa moto. Bw Gachagua amewahi kuomba msamaha hadharani kwa familia ya Kenyatta kutokana na matukio hayo, lakini Rais huyo  mstaafu hajatoa msimamo wa wazi kuhusu uwezekano wa maridhiano. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Bw Wachira Kiago, alisema juhudi za kuunganisha jamii ni endelevu. Alisema jaribio la pili lilikwama baada ya hisia kali kuibuka pande zote mbili, huku siasa za kumuondoa Bw Gachagua madarakani zikitatiza mazungumzo. Jaribio la tatu lilifanyika baada ya kuondolewa kwake, wakati wazee walipoona haja ya kuzuia wapiga kura wa Mlima Kenya kugawanyika bila mwelekeo wa kisiasa. Hata hivyo, juhudi hizo zilikumbwa na changamoto baada ya Rais Ruto pia kuanzisha mazungumzo ya kumkaribia Bw Kenyatta. Mnamo, Bw Gachagua alipuuza madai kuwa kulikuwa na mkutano uliopangwa kati yake na Bw Kenyatta. Katika mahojiano na KTN, alisema hajapanga wala kuomba mkutano huo, lakini hakufunga mlango wa uwezekano wa kukutana naye iwapo kutakuwa na haja. Kauli hiyo ilijiri licha ya Bw Gachagua kutangaza Julai 11 kuwa analenga kukutana na Bw Kenyatta nyumbani kwake Ichaweri ili kumweleza matokeo ya mashauriano ya karibu miezi miwili aliyofanya katika makazi yake ya Wamunyoro. Alisema pia atatafuta ushauri na baraka zake kuelekea uchaguzi wa 2027. Mchambuzi wa siasa Mixson Gitau alisema wapiga kura wanataka viongozi hao waweke kando majivuno yao na kuungana. Alisema tofauti zao zimezua mpasuko mkubwa miongoni mwa wafuasi wao, huku miungano mipya ikiendeleza mgawanyiko huo. Kwa sasa, Bw Gachagua anaendeleza azma yake ya urais huku akijaribu kushawishi Kalonzo Musyoka na Edwin Sifuna kuungana katika upinzani. Wakati huo huo, anamchukulia Dkt Fred Matiang'i kama mradi wa kisiasa wa Bw Kenyatta unaolenga kudhoofisha ushawishi wake Mlima Kenya. Jina la Prof Kindiki linaongeza uzito katika hesabu hizo. Naibu rais amewahi kumuomba aliyekuwa gavana wa Meru, Kiraitu Murungi, amsaidie kumfikia Bw Kenyatta ili aunganishe jamii. Katika hafla moja ya sekta ya maziwa Meru, Prof Kindiki alimuomba Bw Murungi kumshawishi Bw Kenyatta kusaidia kuunganisha jamii ili isije ikapoteza mwelekeo. Bw Joseph Kaguthi, anayeongoza juhudi za kuwakutanisha wazee, wataalamu na viongozi wa dini, alisema ajenda inayopendekezwa ni kuafikiana kuhusu maslahi ya pamoja, ushirikiano na namna ya kuhakikisha kura za eneo hilo zina umuhimu. Alisema mkutano huo unapaswa kufanyika kabla ya Desemba. Bw Muigai alisema mkutano huo pia utajadili nani atakuwa msemaji wa kisiasa wa Mlima Kenya. Alisema Bw Kenyatta anatambuliwa kama mshauri mkuu wa eneo hilo tangu alipostaafu, lakini sasa wanahitaji msemaji atakayewasilisha msimamo wa jamii. Bw Bernard Njue wa mrengo wa kisiasa wa Kiama Kia Ma alisema Bw Kenyatta na Bw Gachagua lazima wapunguze misimamo yao mikali ili mazungumzo yafanikiwe. Alisema Bw Kenyatta anapaswa kumsamehe Bw Gachagua, huku kiongozi huyo wa DCP akionyesha kuwa anaweza kumshirikisha rais huyo wa zamani katika mipango yake ya kisiasa. "Wote wawili lazima watambue kuwa mgawanyiko wao wa sasa hautunufaishi kama jamii. Wasipoungana, tutawagawanya watu wetu," alisema. Wazee wanasema Mlima Kenya hauwezi kumudu kuingia katika uchaguzi wa 2027 ukiwa umegawanyika. Wanataka viongozi hao wakubaliane kuhusu mwelekeo wa kisiasa ili kura za eneo hilo ziwe na nguvu, badala ya kugawanyika katika makundi yanayoshindana.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 01 Nov 2026 03:55:58

Ruto sasa arushia Kalonzo ndoano baada ya kuzomwa mkutano wa Linda Mwananchi

KINARA wa chama cha Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kisiasa huku Rais William Ruto akimshawishi kujiunga na serikali yake, wakati ambao washirika wake katika upinzani wanazidi kuwania tiketi kuuwakilisha katika uchaguzi wa urais wa 2027. Kwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 73, uamuzi wa kuendelea na upinzani au kukubali ushirikiano na Rais Ruto unaweza kuamua hatima ya safari yake ya kisiasa ya takriban miaka 40. Bw Kalonzo amekuwa akitamani kuongoza nchi tangu alipowania urais mara ya kwanza mwaka 2007. Baadaye alijitolea kumuunga mkono marehemu Raila Odinga katika chaguzi za 2013, 2017 na 2022, akiwa mgombeaji mwenza wake katika chaguzi mbili za kwanza. Sasa, baada ya miaka mingi ya kumuunga mkono Raila, anataka nafasi ya kuongoza upinzani katika uchaguzi ujao. Hata hivyo, kuibuka kwa viongozi wapya kama Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na kinara wa Democracy for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua kumechanganya hesabu zake. Bw Kalonzo na washirika wake walitaka suala la mgombeaji urais wa upinzani liamuliwe mapema, lakini Bw Sifuna na Bw Gachagua wanataka uamuzi huo uahirishwe wakisema kumtangaza mgombeaji sasa kunaweza kumpa Rais Ruto nafasi ya kugawanya upinzani. Hali hiyo imemweka Kalonzo kwenye njia panda. Akibaki upinzani, anaweza kukosa tiketi ya urais. Akijiunga na serikali, hakuna hakikisho kwamba atapewa nafasi ya mgombeaji mwenza au wadhifa mwingine mkubwa. Huku mjadala huo ukiendelea, viongozi wa serikali wameongeza juhudi za kumshawishi ajiunge na Rais Ruto. Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot na msaidizi wa Rais Farouk Kibet Jumamosi walimhimiza Bw Kalonzo kuondoka upinzani. Bw Murkomen alisema Kalonzo atakaribishwa serikalini na kwamba uzoefu wake wa kisiasa na kidiplomasia utathaminiwa. Bw Cheruiyot, kwa upande wake, alidai viongozi wa upinzani hawana mpangilio wa kumshinda Rais Ruto mwaka 2027 na kumshauri Kalonzo ajiandae kwa uchaguzi wa 2032. Bw Kibet alisema Kalonzo ataheshimiwa zaidi akijiunga na upande wa serikali. Lakini washirika wa Kalonzo wanapinga madai hayo, wakisema Rais Ruto anamtambua kama tishio kubwa zaidi katika uchaguzi ujao. Seneta wa Kitui Enoch Wambua alisema juhudi za kumshawishi Kalonzo ni ishara kwamba Rais anahofia uwezo wake wa kumshinda katika uchaguzi wa Agosti 10, 2027. Alisema Kalonzo ana ushawishi mkubwa katika eneo la Ukambani, ambalo linaweza kuwa na wapiga kura2.2 milioni, kulingana na makadirio ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Wiper pia imesema haitaruhusu Kalonzo kuvurugwa na juhudi za kumshawishi ajiunge na serikali. Seneta wa Makueni Dan Maanzo alisema chama hicho kitaendelea na azma yake ya kuwania urais, akisema kuwa serikali jumuishi ni meli inayozama ambayo Kalonzo hapaswi kupanda. Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi alisema Kalonzo anataka urais ili kuongoza taifa, na azma hiyo haihusishi kushirikiana na Rais Ruto. Hata hivyo, mchambuzi wa siasa Profesa David Monda anasema Kalonzo anaweza kujiunga na serikali iwapo hatapewa tiketi ya upinzani. Profesa Macharia Munene anasema upinzani unakabiliwa na ushindani wa maslahi binafsi, huku kila kiongozi akitaka kuongoza badala ya kujitolea kumuunga mkono mwingine. Rais Ruto amekuwa akimshawishi Kalonzo kwa muda. Mnamo Mei 2025 alisema alimwendea kwanza baada ya uchaguzi wa 2022 kabla ya kumtafuta Raila, lakini Kalonzo akakataa pendekezo lake. Wiki iliyopita, akiwa Tseikuru, nyumbani kwa Kalonzo, Rais alikosoa upinzani kwa kile alichokitaja kuwa kumdhalilisha kiongozi huyo, akimhimiza ajiunge naye badala ya kukabiliwa na mchujo mwingine wa kisiasa. Hata hivyo, Kalonzo aliwahi kusema mwaka 2023 kuwa kuachana na azma yake ya urais kungeashiria kustaafu siasa. Alisema alikuwa tayari kuwania urais mwaka 2002, 2013 na 2022, lakini alijitolea kuwaunga mkono wengine.

read more