T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 21 Oct 2026 17:47:10

Msimsalimu Natembeya, amri kwa polisi kuhusu Ruto yavuta hisia

KAMISHNA wa Kaunti ya Trans Nzoia Hussein Allaso amezua mzozo baada ya kuwaamuru maafisa wa serikali ya kitaifa kuacha kumsalimu Gavana George Natembeya, akimlaumu kwa kumkosea heshima Rais William Ruto. Bw Allaso alitoa agizo hilo wakati wa sherehe za Mashujaa Day katika Shule ya Msingi ya Naminit, wadi ya Chepchoina, eneo bunge la Endebes, akisema maafisa hao hawapaswi kumheshimu gavana ambaye, kwa madai yake, hamheshimu Rais. "Kuanzia leo, hakuna anayeruhusiwa kumsalimu gavana kwa sababu ya kumkosea heshima Rais. Sisi pia tutamkosea heshima," alisema Bw Allaso alipokuwa akiwahutubia machifu. Alisisitiza kuwa maafisa wa serikali ya kitaifa wataendelea kutekeleza majukumu yao bila kutishwa na viongozi wowote. Alisema uzoefu wake wa miaka 30 katika utawala wa mikoa unampa uwezo wa kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa. Agizo hilo limechochea mjadala kuhusu iwapo maafisa wa umma wanapaswa kuonyesha uaminifu kwa Rais binafsi au kuhudumia wananchi kwa kufuata Katiba. Natembeya alijibu vikali, akimtaja Allaso kuwa mtu anayejipendekeza kisiasa na kukosa kuelewa misingi ya utawala wa kikatiba. Gavana huyo alitoa kauli hiyo akiwa nyumbani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri, alipokuwa ameandamana na viongozi wa upinzani. "Uliajiriwa kuhudumu kwa kuzingatia Katiba, si Rais," alisema Natembeya, akimshutumu kamishna kwa kutenda kana kwamba ni mlinzi binafsi wa Rais. Alionya kuwa maafisa wa umma wanapaswa kupanda vyeo kwa kuonyesha weledi na utendaji bora badala ya kujipendekeza kwa viongozi wa kisiasa. Akirejelea Ibara ya 232 ya Katiba, Natembeya alisema watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia maadili ya kazi, uwajibikaji, uwazi na kutopendelea upande wowote wa kisiasa. Mzozo huo umeibuka baada ya ziara ya maendeleo ya Rais Ruto Trans Nzoia, ambako alizindua mradi wa soko la Masinde Muliro. Naibu Gavana Philomena Kapkory aliunga mkono wito wa kuheshimiwa kwa Rais, akisema Trans Nzoia ni kaunti iliyo na jamii mbalimbali ambazo hazipaswi kugawanywa kwa misingi ya siasa. Alisema viongozi wanapaswa kuvumiliana na kudumisha amani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Natembeya alikosa sherehe hizo na badala yake akaandamana na viongozi wa Linda Mwananchi Movement kukutana na Gachagua kujadili uwezekano wa upinzani kuafikiana kuhusu mgombea mmoja wa urais mwaka 2027.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Ripoti yaonya kuhusu hatari ya vipodozi kwa macho

FASHONI  BIDHAA za urembo zinazotumika kila siku na waraibu wa vipodozi, mapambo na mitindo ya urembo ni kiini cha maelfu wanaoishia hospitalini kwa majeraha anuai, utafiti mpya unaonya.  Urembo sasa huenda ukakugharimu uwezo wako wa kuona, wataalam wanatahadharisha wakisisitiza haja ya kuwa makini unapotumia bidhaa mbalimbali za kuboresha mwonekano wako.  Maelfu ya watu hufika hospitalini kila mwaka wakiwa na majeraha ya macho yanayotokana na matumizi ya vifaa vya urembo na vipodozi, kulingana na ripoti mpya.  Ripoti iliwasilishwa katika kongamano la kila mwaka la American Academy of Ophthalmology (AAO).  Ilitaja vifaa hivi kujumuisha vipodozi vya macho, mapambo ya kutia nakshi kucha, bidhaa za nywele, gundi ya kope, spray ya uso na vifaa vinavyotumia moto kupamba nywele.  Vipodozi huenda vikaonekana kuwa na tishio ndogo kwa sababu ni vifaa vinavyotumika nyumbani kila siku.  Hata hivyo, "vinapotagusana na macho, hasa bidhaa zinazosheheni kemikali au vifaa vyenye moto wa kiwango cha juu, vinaweza kusababisha jeraha kubwa," wanaonya wataalam.  Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Missouri, Kansa City walichanganua data kutoka kwenye Mfumo wa Kitaifa wa Kuangazia Majeraha kwenye udadisi uliofanyika kati ya 2005 na 2024.  Walibaini kuwa watu wasiopungua 42,500 waliishia vitengo vya dharura katika hospitalini wakiugua majeraha ya macho yaliyotokana na vipodozi na vifaa vya kujitunza nafsi.  Wanawake na wasichana walijumuisha waathiriwa wanne kwa kila watano (asilimia 82) ya majeraha haya, kulingana na ripoti.  Ingawa umri wa jumla kwa wagonjwa ulikuwa miaka 24, watoto wenye umri wa miaka minne na kwenda chini waliathirika vilevile wakijumuisha karibu robo ya visa vya majeraha kutokana na vipodozi, walisema watafiti.  Mtindo wa majeraha ulitofautiana kutegemea umri wa mgonjwa. Kuchomeka na kemikali kulijumuisha asilimia 46 ya majeraha kwa macho ya wagonjwa wachanga wenye umri chini ya miaka 18, ikilinganishwa na chini ya asilimia moja ya watu wazima, utafiti ulionyesha.  Miongoni mwa majeraha yote ya kuchomeka na kemikali yaliyotibuiwa, asilimia 83 ilihusishwa na mtoto kushika kifaa cha kujipodoa.  Vipodozi hivi vilijumuisha bidhaa za kutunza ngozi na manukato (asilimia 40), bidhaa za kutia nakshi kucha (asilimia 22) spray na shampoo (asilimia 22).  Miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka minne na kwenda chini, asilimia 70 walijeruhiwa walipokuwa wakitumia vifaa au bidhaa za vipodozi wakiwa pekee yao bila uangalizi.  Watu wazima, kwa upande mwingine, aghalabu walipata majeraha ya kukatwa, vidonda au kukwaruzwa kwenye macho yao.  Majeraha kwa watu wazima yalijumuisha majeraha ya macho (asilimia 56) na majeraha ya kuchomeka macho (asilimia 22), kulingana na ripoti hiyo.  Wataalam wanasisitiza umuhimu wa kumakinika kuhusu uhifadhi wa vipodozi na vifaa vya kujitunza binafsi ili kuhakikisha havifikiwi na watoto.  "Kwa watoto, inamaanisha kusisitiza uhifadhi kwa njia salama na kuzuia kufikia bidhaa za urembo bila uangalizi hasa bidhaa majimaji na spray," walisema wataalam.  Vijana chipukizi na watu wazima wanashauriwa kuzingatia mbinu salama za kutumia na mapambo ya moto ili kupunguza tishio la majeraha.   

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Wanawake wanavyojichongea, waendeleza itikadi zilezile zinazowakandamiza

FATAKI TAASUBI ya kiume inayolaumiwa kila mara kama moja kati ya visababishi vikuu vya masaibu yanayowaandama mabinti tangu jadi kwa sehemu kubwa inaendelezwa na kuchangiwa na wanawake wenyewe hadi katika kizazi hiki. Japo ni kweli kuwa wanaume wanachangia pakubwa kuhusu ubaguzi wa jinsia ya kike, ukosefu wa usawa na mizigo wanayolazimishwa kubeba wanawake, ni muhimu kukabili ukweli mchungu kwamba mabinti, wakati mwingine, wanapigia debe na kuendeleza mifumo ileile inayowakandamiza.  Ni kinaya kwa hakika na tunaweza kufananisha uhusiano huu na mtumwa aliyezoea mateso ya mmiliki wake kiasi cha kuhiari kuendelea kumtumikia hata anapoamua kumpa uhuru wake!  Taasubi ya kiume haitamalaki kupitia matendo ya wanaume pekee bali hunawiri wakati wanawake huchunguza maamuzi ya wanawake wenzao, kuwadhalilisha mabinti wenzao kwa kukaidi matarajio ya jamii na kuwalaumu kwa majukumu yaleyale yaliyotelekezwa na wanaume.  Video iliyosambazwa sana mitandaoni iliyomwonyesha binti akimkashifu mama yake kwa kumwita 'toxic' eti kwa sababu alikataa kumlelea mtoto wake ili afanye kazi inatoa taswira bayana ya ukinzani huu.  Kwenye video hiyo, binti huyo anasimulia kwa machungu jinsi alivyolazimika kumwacha mtoto wake mchanga na mwanamme aliyemlazimisha baada ya mama yake kukataa katakata kurejelea majukumu ya ulezi kwa mjukuu wake.  Kiburi na matarajio yasiyo ya kirazini ya binti huyo kinastaajaisha mno kwa sababu watu waliofaa zaidi kumlea mtoto huyo basi ni wazazi wake na wala sio nyanya yake.  Hali kwamba alihisi kukomaa na kuwa tayari kujihusisha na shughuli za utu uzima ikiwemo kushiriki tendo la ndoa ni ithbati tosha kwamba alistahili kuwa tayari kwa majukumu ya utu uzima yanayojumuisha kubeba mimba, kuzaa na kumlea mtoto wake.  Badala ya kumkabili baba mtoto wake na kumshurutisha awajibike mwanamke huyu kwa maarifa au kwa kukosa maarifa alihiari kurekodi video chungunzima kumchamba mama yake kwa kutojali na kukataa kumshughulikia alipomhitaji zaidi!  Hata bila kujali kwamba mama yake sasa anastahili muda wa kupumzika baada ya kujitolea mhanga kumlea pamoja na ndugu zake, mwanamke huyu alitarajia bila soni kumtwika mwigo mwingine wa kumlelea mwanawe.   

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Ilani kuhusu baadhi ya vyakula na afya ya akili kwa matineja

UJAUZITO NA UZAZI IWAPO wewe ni mzazi wa vijana barobaro, basi utahitajika kuwa mwangalifu zaidi kuhusu uteuzi wao wa chakula ili kulinda afya yao ya akili.  Wataalam wanatahadharisha kuwa chaguo la vyakula kwa vijana chipukizi linaweza kuwa na madhara zaidi ya afya yao kimwili.  Chaguo la chakula na ulaji wa sukari limehusishwa na kuzuka baadaye kwa matatizo ya afya ya akili hususan wasiwasi uliokithiri na unyogovu, kulingana na utafiti mpya.  Udadisi huo uliashiria kwamba kula kiasi cha ziada cha aina yoyote ya matunda kila siku kunapunguza dalili za unyogovu kwa asilimia 13 na wasiwasi uliokithiri kwa asilimia saba.  Kiasi cha jumla cha ulaji wa matunda kilihusisha kula matunda mara mbili au tatu kwa siku katika kipindi cha utafiti huo ulioshirikisha vijana barobaro 6,537 kutoka shule 71 za sekondari Uingereza na Australia.  Washiriki wenye umri wa miaka 12.5 kwa jumla kutoka Gredi 7- Gredi 10 waliangaziwa kwa miaka minne hadi uchunguzi huo ulipokamilika,  Kunywa vinywaji vilivyoongezwa sukari ikiwemo soda, sharubati na vinywaji vya spoti kulihusishwa na ongezeko la unyogovu na wasiwasi.  Uhusiano kuhusu vinwaji vyenye sukari uligunduliwa miongoni mwa vijana chipukizi wavulana kwa wasichana, japo wavulana walionyesha viwango vya juu zaidi hasa wasiwasi uliokithiri.  "Sekondari ni kipindi ambapo vijana chipukizi huanza kupata uhuru zaidi kuhusu wanachokula na kunywa, wakati huo pia, matatizo mengi ya afya ya akili huanza kuchipuka," walifafanua watafiti.  "Hatusemi kula tufaha kutazuia unyogovu, au kwama kunywa soda kutasababisha wasiwasi – afya ya akili inahusu zaidi ya hayo. Lakini unachokula ni sehemu moja ya maisha ya kijana inayoweza kubadilishwa hivyo kufanya matokeo haya kuwa muhimu kwa mtazamo wa kinga."  Ni rahisi kufikiria chakula na lishebora kama zinazohusu afya ya mwili lakini utafiti huu unaongeza ushahidi kwamba wanachokula vijana ni muhimu vilevile kwa afya yao ya akili, wanasema wataalam.  Wanasisitiza umuhimu wa kuelewa kinachoongoza maamuzi bora ya chakula kwa vijana barobaro na kupatia kipaumbele lishebora kiafya ili kulinda afya yao ya akili.  "Shule, familia na serikali wote wana jukumu la kutekeleza kusaidia tabia inayozingatia afya na afya bora ya akili kwa vijana." 

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

SHERIA: Hauwezi kuoa au kuolewa kabla ya kuvunja ndoa

Sheria ya Ndoa ya Kenya inaweka mipaka kwa mtu aliye kwenye ndoa ya mke mmoja kuingia katika ndoa nyingine, huku ikiorodhesha uhusiano wa kifamilia unaokatazwa kufunga ndoa. Je, mtu anaweza kuoa au kuolewa tena wakati ndoa yake ya kwanza bado ipo kisheria? Jibu linategemea aina ya ndoa aliyo nayo, kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Kenya ya mwaka 2014. Sheria hiyo inaweka wazi kuwa mtu aliye katika ndoa ya mke mmoja haruhusiwi kufunga ndoa nyingine wakati ndoa ya kwanza bado ipo. Hii ina maana kuwa mtu hawezi kuingia katika ndoa nyingine kwa sababu tu ameachana na  mke au mume wake, wameishi kando kwa muda mrefu au hawazungumzi tena. Mambo hayo pekee hayamalizi ndoa kisheria. Kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria ya Ndoa, mtu aliye katika ndoa ya mke mmoja haruhusiwi kufunga ndoa nyingine. Vilevile, mtu aliye katika ndoa ya wake wengi au ndoa inayoweza kuruhusu wake wengi haruhusiwi kuingia katika ndoa nyingine ya mke mmoja. Hata hivyo, kifungu hicho kinaanza kwa kurejelea kifungu cha 8, kinachopaswa kuzingatiwa katika kuelewa masharti yanayotumika kwa aina tofauti za ndoa. Hivyo, mtu anayefikiria kuoa au kuolewa tena anapaswa kwanza kuhakikisha hali ya ndoa yake ya sasa imeamuliwa kisheria badala ya kutegemea hisia au makubaliano ya mdomo pekee. Mbali na kuzuia mtu kuingia katika ndoa nyingine kinyume cha sheria, Sheria ya Ndoa inaeleza pia mahusiano ya kifamilia ambayo watu hawaruhusiwi kufunga ndoa. Kifungu cha 10 kinakataza ndoa kati ya mtu na babu au nyanya yake, mzazi, mtoto, mjukuu, dada, kaka, binamu, shangazi, mjomba, dada au kaka wa mzazi, mpwa na baadhi ya ndugu wengine waliotajwa katika sheria hiyo. Marufuku hiyo pia inahusu uhusiano fulani wa kifamilia kupitia mwenzi wa ndoa au mwenzi wa zamani. Kwa mfano, mtu haruhusiwi kufunga ndoa na babu au nyanya, mzazi, mtoto au mjukuu wa mwenzi wake au mwenzi wa zamani. Sheria hiyo inakataza pia ndoa kati ya mtu na mtu aliyemlea kwa njia ya kuasili, au mtu aliyemuasili, pamoja na mahusiano mengine ambayo mila husika zinakataza ndoa. Muhimu zaidi, kifungu hicho kinaeleza kuwa uhusiano wa damu wa upande mmoja, kama kuwa na mzazi mmoja wa pamoja, pia unaweza kuzuia ndoa. Hata hivyo, sheria inaweka tofauti kuhusu ndoa kati ya binamu kwa watu wanaofuata dini ya Kiislamu. Marufuku ya ndoa kati ya binamu iliyotajwa katika kifungu hicho haiwahusu wanaofuata imani ya Kiislamu. Kwa hivyo, kabla ya kufunga ndoa, ni muhimu kwa wanandoa watarajiwa kuelewa hali ya ndoa zao za awali na uhusiano wao wa kifamilia. Kushauriana na mtaalamu wa sheria kunaweza kusaidia kuzuia migogoro na kuhakikisha ndoa inayokusudiwa inakidhi matakwa ya sheria. Kwa ujumla, Sheria ya Ndoa inalenga kuweka utaratibu unaotambulika kisheria kuhusu ndoa na kuzuia ndoa zinazokatazwa. Mtu anayepanga kuanza maisha mapya ya ndoa anapaswa kuhakikisha kuwa hakuna kizuizi cha kisheria kinachoweza kufanya hatua hiyo iwe batili.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Sifuna anavyopangua hesabu za upinzani kwa fujo 2027 ikikaribia

KUPAA kwa umaarufu wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kumeanza kutatiza mipango ya viongozi wa upinzani wanaotaka kuungana ili kumng'oa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2027. Miezi michache iliyopita, jina la Sifuna halikuwa likitajwa sana miongoni mwa wanaoweza kuwania urais, ingawa baadhi ya watu walikuwa wakimhusisha na nafasi ya mgombea mwenza. Hata hivyo, umaarufu wake unaoongezeka, hasa miongoni mwa vijana, sasa unamwingiza katika mjadala kuhusu nani anafaa kupeperusha bendera ya upinzani. Mchango wa fedha kutoka kwa kina mama wafanyabiashara maarufu kama mama mboga umeongeza uzito wa kisiasa wa seneta huyo, huku akisema ameguswa na uamuzi wao wa kutumia mapato yao kumsaidia. Alisema hatua hiyo ni ishara ya imani ambayo wananchi wa kawaida wameweka kwake na ambayo hawezi kuichukulia kuwa ya kawaida. Mkutano wake na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, Oktoba 20, umefungua ukurasa mpya katika juhudi za kuunganisha upinzani. Ingawa washirika wa Gachagua walitaja mkutano huo kuwa wa kujuana, wachambuzi wanasema una umuhimu mkubwa katika siasa za kuelekea uchaguzi ujao. Wawili hao waliwahi kuwa pande tofauti wakati wa mchakato wa kumuondoa Gachagua madarakani Oktoba 2024, ambapo Sifuna, akiwa seneta, alishiriki katika mchakato huo. Sasa, wanachunguza uwezekano wa kushirikiana wakati upinzani unapojaribu kukubaliana kuhusu mgombea mmoja wa urais. Chanzo cha ndani ya mazungumzo hayo kiliambia Taifa Jumapili kuwa kuna uwezekano wa kuibuka kwa kile alichokiita "muungano wa milima", unaounganisha Mlima Elgon, eneo la nyumbani kwa Sifuna katika Kaunti ya Bungoma, na Mlima Kenya, ngome ya kisiasa ya Gachagua. Gachagua ametangaza kuwa yuko tayari kuwa mgombea mwenza wa Sifuna iwapo seneta huyo ataonekana kuwa chaguo bora zaidi la upinzani kumkabili Rais Ruto. Hata hivyo, mazungumzo ya ndani yanadaiwa kuhusisha pia jina la Seneta wa Nyandarua John Methu kama mgombea mwenza anayeweza kupendekezwa katika mazungumzo na Sifuna. Hili linaweza kuwa kikwazo katika ushirikiano huo, hasa huku viongozi wakishindania nafasi za juu na kujaribu kuamua nani atakuwa kinara wa tiketi ya urais. Katika mkutano wa Wamunyoro, pande hizo zilikubaliana kuwa na mgombea  moja ya urais na kumuunga mkono atakayechaguliwa kuuongoza. Hata hivyo, bado hawajakubaliana kuhusu utaratibu wa kumteua mgombea huyo. [caption id="attachment_185026" align="aligncenter" width="300"] Viongozi wa kisiasa wanaoegemea vuguvugu la Linda Mwananchi wawasilia mjini Busia kwa mkutano wa kisiasa hivi majuzi. PICHA|ALEX ODHIAMBO[/caption] Ushirikiano unaochipuka unaathiri hesabu za viongozi wengine wa upinzani, wakiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mgombea wa Jubilee Fred Matiang'i, kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua, kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi na wa DAP-K Eugene Wamalwa. Wote wamekuwa wakihusika katika juhudi za kuunganisha upinzani, lakini kuibuka kwa Sifuna na Gachagua kunaweza kubadilisha namna mazungumzo hayo yanavyoendeshwa. Aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama, ambaye sasa ni kamishna wa Tume ya Huduma ya Bunge na mshirika wa Rais Ruto, ameonya kuwa upinzani haupaswi kudharau uzito wa Kalonzo. Muthama anasema uzoefu wa kisiasa wa Kalonzo, uwezo wake wa kufanya mazungumzo na mahusiano aliyojenga kwa miaka mingi vinaweza kuwa muhimu katika uchaguzi ujao. Ametaja kuhudumu kwa Kalonzo chini ya Rais wa zamani Daniel arap Moi, kuteuliwa kuwa makamu wa rais na Mwai Kibaki na kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa 2013 na 2017 kama ushahidi wa uzoefu wake. "Katika siasa za Kenya, uchaguzi hushindwa au kushindwa kwa kutegemea idadi ya wapiga kura, mikakati, uaminifu na mahusiano," alisema Muthama. Alionya kuwa kundi lolote litakalopuuza umuhimu wa Kalonzo litakuwa likifanya kosa kubwa. Umaarufu wa Sifuna umeongezeka kufuatia mzozo wake na chama cha ODM kuhusu ushirikiano wake na chama tawala cha UDA na mwelekeo wa chama hicho baada ya kifo cha Raila Odinga. Akiwa katibu mkuu wa ODM, Sifuna alikuwa miongoni mwa viongozi waliotetea msimamo huru wa chama hicho na kukosoa ushirikiano wa kisiasa kati yake na Rais Ruto. Mvutano huo ulimwelekeza katika mrengo tofauti wa kisiasa, kupitia The Equitable Party, ambayo sasa inabadilisha kuwa Linda Mwananchi. Vuguvugu hilo linajitahidi kujijenga kwa misingi ya kuheshimu Katiba, uwajibikaji wa umma na ajenda ya kiuchumi inayolenga wananchi wa kawaida. Katika mahojiano na wanahabari jijini Nairobi Oktoba 9, Sifuna aliacha wazi uwezekano wa kufanya kazi na viongozi ambao hapo awali walikuwa na misimamo tofauti naye. Alipoulizwa kuhusu ushirikiano na Gachagua, alisema: "Tayari nilipigia kura ya kumuondoa madarakani kwa makosa yake. Kwa hivyo, hauwezi kuniuliza maoni yangu kana kwamba sijachukua hatua tayari." Kauli hiyo ilionyesha kuwa licha ya kushiriki katika mchakato wa kumuondoa Gachagua madarakani, Sifuna haoni kuwa hilo linazuia ushirikiano wao kisiasa. Hata hivyo, amekataa kuingia kwa undani kuhusu azma yake ya urais au namna mgombea mmoja wa upinzani atakavyochaguliwa. "Subirini kwanza. Mazungumzo hayo yatakuja baadaye," aliambia Taifa Leo alipoulizwa kuhusu mipango ya muungano. Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema umaarufu wa Sifuna unaweza kumwezesha kuzungumza na makundi tofauti ya wapiga kura, wakiwemo vijana na wanaopinga serikali jumuishi ya Ruto. Hata hivyo, anasema changamoto yake kubwa ni kubadilisha umaarufu huo kuwa mtandao wa kitaifa wenye uwezo wa kuendesha kampeni, bila kupoteza misingi iliyowavutia wafuasi wake. Kwa Gachagua, ushirikiano huo unatoa nafasi ya kupanua ushawishi wake nje ya Mlima Kenya. Naye Sifuna anaweza kumfungulia mlango kwa vijana na wapiga kura wanaotaka mwelekeo tofauti wa kisiasa. Akiwa ziarani Amerika, Gachagua alisema yuko tayari kuwa mgombea mwenza wa Sifuna iwapo juhudi zake za kumshinda Ruto zitafaulu na washirika wake watamshawishi kuchukua nafasi hiyo. Alisema: "Ninamfahamu Ruto vizuri na mimi ndiye ninayefaa kumpeleka nyumbani. Lakini nikishindwa na wakinishawishi vinginevyo, mimi Riggy G naweza kuwa naibu wa Sifuna." Katika mkutano wa Wamunyoro, alisisitiza kuwa alitaka pande hizo ziwe timu moja na kufanya kazi kwa manufaa ya nchi. Hata hivyo, wakili Chris Omore anasema changamoto kubwa ni iwapo viongozi hao wataweza kuafikiana kuhusu nafasi zao bila kuibua mzozo mwingine wa uongozi. Kwa upande mwingine, Kalonzo amekuwa akihusishwa na juhudi za kuunda upya muungano wa zamani wa Azimio kupitia Ukombozi Alliance, unaolenga kuunganisha vyama nyuma ya mgombea mmoja huku kila chama kikihifadhi utambulisho wake. Lakini Linda Mwananchi na chama cha DCP cha Gachagua vimeonyesha kutochangamkia muungano huo, hali inayoweza kusababisha mazungumzo tofauti ya kuunda muungano. Omore anasema iwapo ushirikiano wa Sifuna na Gachagua utageuka kuwa mpango rasmi wa uchaguzi, Kalonzo atalazimika kujadiliana na kundi lenye viongozi, mitandao na malengo yake. Wakati huo huo, Matiang'i, Karua na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro walikutana Njoro, Kaunti ya Nakuru, Oktoba 21, ambapo walikosoa ahadi za kiuchumi za Ruto na kutaka mwelekeo mpya wa kisiasa. Hali hii inaonyesha kuwa ushindani wa kuamua mgombea wa upinzani hauwahusu Sifuna na Gachagua pekee. Kalonzo, Wamalwa, Muturi na viongozi wengine pia wanajenga ushirikiano wao huku wakijaribu kuathiri uamuzi wa mwisho.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

Itakuwa nusu mkate na UDA 2027,  ODM yaahidi wafuasi

CHAMA cha ODM kimewahakikishia wafuasi wake kuwa hakitapoteza ngome zake za kisiasa licha ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wake Raila Odinga na ushirikiano wake na chama tawala cha UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Viongozi wa chama hicho wamesema wanapania kushinda viti vingi vya magavana, maseneta, wabunge na wawakilishi wadi ili kuimarisha uwezo wao wa kujadiliana kuhusu ugavi wa mamlaka katika serikali ijayo. Akizungumza na wajumbe wa ODM katika Kaunti ya Turkana mjini Lodwar Ijumaa usiku, mwenyekiti wa chama Gladys Wanga alisema chama hicho kimeimarika baada ya kupitia kipindi kigumu kufuatia kifo cha Raila. Alisema ODM na UDA zinatarajiwa kuunda serikali kwa usawa wa asilimia 50 kwa kila chama, huku UDA ikichukua urais na ODM kupewa nafasi ya naibu wa rais. "Ni kawaida kupitia misukosuko tuliyopitia. Sasa tumetulia na tumetambua kuwa wengi wa wafuasi wetu bado wako ndani ya chama. Msitishwe na kulazimishwa kuondoka," alisema Wanga. Aliongeza kuwa ODM italazimika kushinda viti vingi vya uchaguzi ili iwe na nguvu za kudai nafasi muhimu serikalini, zikiwemo nyadhifa 10 za mawaziri. Wanga alisema pia chama hicho kinalenga kuhifadhi nafasi ya Waziri inayoshikiliwa na Beatrice Askul, ambaye aliteuliwa kwa ushawishi wa Raila. Alisema ODM inaendeleza ushirikiano na viongozi wa mashinani ili kuhakikisha kinashinda viti vingi Turkana na kufanya vizuri katika muungano wa serikali jumuishi. Katibu mkuu wa ODM, Catherine Omanyo, aliwataka wajumbe kuepuka migogoro ya ndani, akisisitiza kuwa chama ni kikubwa kuliko mtu mmoja na kinapaswa kuimarishwa ili kuvutia wanachama wapya. Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed alisema Turkana bado ni ngome ya ODM, licha ya Gavana Jeremiah Lomorukai kuondoka katika chama hicho. Alisema chama hicho kinalenga kuhakikisha mmoja wa wabunge wa Turkana Kaskazini, Ekwom Nabuin, au Turkana Kusini, Ariko Namoit, anachukua nafasi ya Lomorukai katika uchaguzi ujao. "Tumekuwa na gavana wa ODM Turkana tangu 2013, na mwaka 2027 gavana atatoka ODM tena," alisema Mohammed. Aliongeza kuwa iwapo UDA itashinda uchaguzi wa 2027, ODM itakuwa na nafasi ya kuwania urais mwaka 2032. Naibu kiongozi wa ODM Simba Arati alisema chama hicho kitafanya uteuzi wa haki na huru ili kumchagua mgombea wake mapema na kuanza kampeni za kurejesha ugavana Turkana. Alisema ODM pia itaimarisha miundo yake ya mashinani ili kukabiliana na ushindani kutoka kwa wagombea wenye uwezo mkubwa wa kifedha. Raila Odinga Junior aliwataka viongozi kubaki pamoja na kuendeleza urithi wa babake wa kutetea maendeleo ya usawa kupitia serikali jumuishi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Jinsi mikutano ya kisiasa yageuka biashara nono Nyanza

SIASA katika eneo la Nyanza zinazidi kuwa ghali huku wanasiasa wakitumia mamilioni ya pesa kurai wananchi kuhudhuria mikutano yao, hali inayofanya ukubwa wa umati kuwa kipimo cha ushawishi wa kisiasa. Nyuma ya mikutano yenye shamrashamra na viwanja vinavyojaa watu kuna biashara inayohusisha kukodisha mabasi, kutoa chakula na kulipa wanaohudhuria. Hali hii inafanya ushindani wa kisiasa kuwa mgumu kwa vijana na wagombea wasio na uwezo mkubwa wa kifedha. Mjadala kuhusu gharama hizo ulizidi kushika kasi baada ya video ya Mwakilishi wa Wanawake wa Homa Bay Joyce Osogo Bensuda kusambaa mitandaoni, akieleza jinsi alivyopanga kutumia mamilioni ya pesa kuleta watu kwenye mkutano. Mnamo Oktoba 2, Bensuda aliandaa Siku ya Wafanyabiashara wa Jua Kali katika Uwanja wa Raila Odinga, Homa Bay. Hafla hiyo iliwaleta pamoja wafanyabiashara kutoka wadi zote 40 za kaunti hiyo kupokea fedha na vifaa vya thamani ya Sh78.1 milioni kupitia  hazina tofauti za serikali. Katika video hiyo, Bensuda anaeleza kuwa alikusudia kutumia zaidi ya Sh1 milioni kuwalipa watu waliohudhuria, huku kila mmoja akitarajiwa kupata Sh1,000. Alisema katika hafla nyingine ya awali alitumia mabasi 56 kusafirisha watu hadi Ndhiwa na kuwalipa waliohudhuria Sh840,000, kila mmoja akipata Sh300. Fedha hizo hazikujumuisha gharama ya kukodi mabasi, fulana na miavuli. Kuhusu mkutano wa uwanja wa Raila Odinga, alisema alikuwa amepanga kutumia mabasi 62 ya shule na Sh1.5 milioni kwa shughuli za kuvutia umati pekee. Bensuda alithibitisha kuwa video hiyo ilikuwa yake, lakini akasisitiza haikuwa na uhusiano na ODM. Hakujibu maswali zaidi baada ya kutumiwa video hiyo na Taifa Jumapili. Uchunguzi wa Taifa Jumapili unaonyesha kuwa mfumo huo unahusisha waratibu wa mashinani, vijana, waendesha bodaboda, vikundi vya wanawake na viongozi wa maoni. Wengine hulipwa fedha taslimu, huku wengine wakipatiwa nauli na chakula. Kwa baadhi ya watu, kuhudhuria mkutano wa kisiasa kumekuwa njia ya kupata mapato ya siku moja badala ya kuonyesha tu uungwaji mkono kwa kiongozi. Emmanuel Sirunda, mwendesha bodaboda kutoka Ugunja, Kaunti ya Siaya, ni mmoja wa wanaofaidika na mfumo huo. Alikuwa miongoni mwa maelfu ya watu waliohudhuria mkutano wa Rais William Ruto katika eneo la Kisumu Shipyard. Sirunda alisema mabasi ya shule yalikodiwa kusafirisha wajumbe kutoka maeneo mbalimbali ya Nyanza. Walipofika, walipewa chakula na kuahidiwa malipo baada ya kusikiliza hotuba ya Rais. "Tulipewa Sh5,000 kila mmoja, bila kujumuisha nauli na chakula cha mchana. Haya ni mapato ambayo singepata kwa siku moja," alisema. Zaidi ya watu 10,000 walipokea Sh5,000 kila mmoja, sawa na takriban Sh50 milioni. Kila mmoja alihitajika kuwasilisha kadi nyekundu aliyokuwa amepewa mwanzoni mwa mkutano ili kulipwa. Shughuli ya kuzindua kaburi la kumbukumbu ya Raila Amolo Odinga mjini Bondo Oktoba 7 pia ilionyesha jinsi wanasiasa wanavyotegemea mitandao ya wahamasishaji kuvuta umati. Sally Akinyi, jina ambalo si lake halisi, alisema amejenga mtandao wa watu anaoweza kuwaita wanasiasa wanapohitaji umati. Anasema hulipwa kuhamasisha wafuasi kwa niaba ya wabunge wawili wa Nyanza wanaotaka kuwania ugavana, mgombea wa ubunge Kisumu ya Kati na, mara nyingine, wasaidizi wa Rais Ruto. Akinyi alisema wanaoitwa kwenye mikutano ndani ya Kisumu hulipwa Sh500 hadi Sh700, huku wanaosafiri nje ya mji wakipata kati ya Sh1,500 na Sh2,500, kutegemea kazi na umbali. Hata hivyo, alisema biashara hiyo si ya uhakika kila wakati, kwani baadhi ya wanasiasa hushindwa kuwalipa wahamasishaji baada ya mikutano. Wakati mwingine, malipo hutolewa kupitia ufadhili wa vikundi au basari badala ya fedha taslimu. Katika eneo la Gusii, linalojumuisha Kisii na Nyamira, viongozi wanaounga mkono serikali jumuishi huandaa hafla za uwezeshaji mara kwa mara. Baadhi ya wakazi hupokea kati ya Sh100 na Sh2,000, huku vikundi vilivyoandaliwa, kama vya wanawake na kwaya, vikivutia fedha zaidi. Wasaidizi wa baadhi ya viongozi wanasema mikutano hii hufadhiliwa na serikali, ikiwemo utoaji wa mchele na maharagwe kwa wafuasi. Vifaa vyenye nembo za kisiasa, kama kofia na fulana, pia hutolewa. Hata hivyo, swali kuu linalosalia ni fedha hizo zinatoka wapi na zinatolewaje.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

Kenya inavyogeuka pango la magenge ya uhalifu

UCHUNGUZI wa miezi kadhaa kuhusu mtandao wa wizi wa simu jijini Nairobi umesababisha kukamatwa kwa MCA wa Ikanga/Kyatune, Cyrus Kisavi Musyoka, na kufichua jinsi magenge ya uhalifu yanavyofanya kazi nchini. Musyoka alikamatwa kuhusiana na visa vya wizi wa simu vilivyoripotiwa Agosti na Septemba 2026. Polisi wanasema picha za kamera za CCTV zilisaidia kumtambua. Simu zilizoibwa zinadaiwa kuuzwa kama mpya kwa wanunuzi wasio na habari, hata nchini Ethiopia. Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Muchiri Nyaga, alisema polisi sasa wanawalenga wafadhili na mitandao inayofadhili uhalifu, badala ya kuwakamata pekee wanaoiba mitaani. Alitaja kukamatwa kwa mshukiwa mmoja jijini Nairobi aliyepatikana na mifuko miwili ya simu zilizokuwa zikisafirishwa kwenda Uganda. "Kuna soko nchini Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nje ya mipaka yetu ya karibu," alisema, akieleza kuwa wezi wanaweza kufadhiliwa, kupewa maeneo ya kufanyia kazi na kuunganishwa na wanunuzi. Takwimu za serikali zinaonyesha ukubwa wa tatizo. Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, alisema mapema Oktoba kuwa serikali ilikuwa imetambua magenge 109 ya uhalifu nchini, kutoka 89 yaliyotangazwa kuwa haramu mwaka 2016. Kati ya Januari 1 na Agosti 31, 2026, washukiwa 1,827 walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa yanayohusiana na magenge na vurugu. Trans Nzoia iliongoza kwa washukiwa 491. Serikali iliripoti hukumu 729, huku kesi 716 zikiendelea mahakamani. Ripoti ya Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu (NCRC) ya mwaka 2025 ilibaini magenge 309 katika kaunti 11. Mombasa ilikuwa na magenge 73, Nairobi 56 na Kilifi 47. Baadhi ya makundi, yakiwemo Gaza Brothers na 42 Brothers, yako katika kaunti kadhaa. Ripoti hiyo ilisema magenge yanahusishwa na wizi, mashambulizi, usambazaji wa dawa za kulevya na kuitisha pesa  kwa vitisho kutoka kwa waendeshaji wa matatu. Pia ilionya kuwa vijana hujiunga na magenge kupitia ushawishi wa marafiki, huku ukosefu wa ajira, ufisadi na ushirikiano dhaifu kati ya polisi na jamii vikichangia tatizo hilo. Ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ya mwaka 2025 ilionya kuwa magenge hutumiwa katika misimu ya uchaguzi kutisha wapinzani, kuvuruga mikutano na kutekeleza malengo ya kisiasa kwa malipo. Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, wachambuzi wanaonya kuwa magenge yanaweza kutumiwa kuendeleza vurugu na vitisho. Ripoti ya Organised Crime Index ya mwaka 2025 iliorodhesha Kenya kuwa nchi iliyoathiriwa zaidi na uhalifu miongoni mwa nchi tisa za Afrika Mashariki, na ya nne kati ya nchi 54 za Afrika. Biashara haramu ya binadamu, usafirishaji wa dawa za kulevya, ulanguzi wa silaha na ulaghai wa kifedha zilitajwa miongoni mwa vitisho. Mchambuzi wa usalama James Chemiati alisema ukosefu wa ajira unawaweka vijana katika hatari ya kuajiriwa na magenge na wanasiasa wanaotaka kutumia vurugu dhidi ya wapinzani. Alisema baadhi ya vijana huishia kujihusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu wa mtandaoni baada ya shughuli za kisiasa kukamilika. Mchambuzi George Musamali alisema magenge yanaweza kuwa na majina, alama, viongozi na maeneo yanayodhibiti. Alitaja Mungiki, Baghdad Boys, Chinkororo na Gaza kama makundi yaliyowahi kutajwa katika miktadha tofauti kuwa walinzi wa jamii au magenge ya uhalifu. Wataalamu wanakubaliana kuwa kukamatwa kwa washukiwa pekee hakutamaliza tatizo. Polisi wanahitaji kuwafuatilia wafadhili, wanunuzi wa bidhaa zinazoibwa na watu wanaotoa ulinzi kwa magenge. Ushirikiano kati ya polisi na jamii, ulinzi wa mashahidi na nafasi za kiuchumi kwa vijana pia ni muhimu. Bila kuwawajibisha wanaofadhili na kunufaika na uhalifu, kukamatwa kwa wahalifu kunaweza kuacha mitandao inayochochea magenge ikiendelea kufanya kazi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 18 hours ago

Jukumu nzito la Gachagua akipanga upinzani kuelekea 2027

KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, anaonekana kujipa jukumu la kuunganisha viongozi wa upinzani ili kumkabili Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. Hata hivyo, haijabainika iwapo viongozi wengine wamekubaliana naye kuongoza juhudi hizo au amejipa jukumu hilo mwenyewe. Mafanikio au makosa yake yanaweza kuamua iwapo atakuwa mgombea muhimu, atafanya mwingine kuingia Ikulu au kumsaidia Ruto kupata muhula wa pili kwa ushindi mkubwa. Mchambuzi wa siasa Herman Manyora anasema mpango huo una nafasi ya kufanikiwa, ingawa si rahisi. "Mradi kuna uwezekano hata mdogo wa kufanikiwa, hatuwezi kuupuuza. Siasa ni sanaa ya kufanya yanayowezekana na ndoto zote zina nafasi," alisema. Gachagua anaamini eneo la Mlima Kenya ndilo lenye wapiga kura wengi na kwamba bado ana ushawishi mkubwa miongoni mwao. Anadai kuwa nyumbani kwake Wamunyoro, ambako Ruto alikuwa akitembelea mara kwa mara, kulichangia safari ya kisiasa iliyomfanya rais mwaka 2022. "Naomba ajaribu kukanusha. Alitembelea nyumbani kwangu mara nyingi na mke wangu alimwandalia chakula na kumuombea," alisema Gachagua. Mjadala kuhusu mipango yake ulipamba moto baada ya kurejea kutoka Amerika Oktoba 20, baada ya kukaa huko kwa zaidi ya siku 50, na kukutana na kiongozi wa Linda Mwananchi, Edwin Sifuna, nyumbani kwake Wamunyoro. Washirika wake wanapendekeza kuwa viongozi watatu wenye uwezo mkubwa wa kuvutia wapiga kura ni Gachagua, Sifuna na Kalonzo Musyoka. Mwenyekiti wa DCP anayehusika na wazee mashuhuri, Maina Kamanda, anasema viongozi hao watatu wana uwezo wa kubadilisha mwelekeo wa siasa na kuvutia idadi kubwa ya wapiga kura. Hata hivyo, muungano wa upinzani pia una viongozi wengine, wakiwemo Fred Matiang'i, Martha Karua, Eugene Wamalwa, Justin Muturi, Boniface Mwangi, David Maraga, Jimmi Wanjigi na Okoiti Omtatah. Kwa mujibu wa mkakati unaohusishwa na washirika wa Gachagua, anataka kupunguza kura milioni 7.17 ambazo Ruto alipata mwaka 2022. Gachagua anaamini kuwa anaweza kuvuta takriban kura milioni 3.5 za Mlima Kenya ambazo zilimsaidia Ruto kushinda. Akiondoa kura hizo, anahesabu kuwa Rais atabaki na takriban kura milioni 3.68. Anapojumlisha kura hizo 3.5 milioni na kura milioni 6.94 ambazo Raila Odinga alipata mwaka 2022, anafikia jumla ya takriban kura 10.44  milioni akisema hesabu hizo zinaonyesha Ruto anaweza kushindwa. Lakini Mbunge wa Laikipia Mashariki, Mwangi Kiunjuri, anapinga dhana hiyo. Anasema Gachagua hapaswi kuwania urais wala naibu wa rais. Kiunjuri anaonya kuwa Gachagua akitengwa na viongozi wengine kwa sababu ya kile anachokitaja kuwa tabia ya kutaka kutawala wengine, anaweza kubaki na chama chake na kura za Mlima Kenya, huku Ruto akipata nafasi ya kushinda tena. Anasema Ruto anaweza kuvutia takriban kura milioni nne za wafuasi wa Raila, na kuziunganisha na kura milioni tano anazokadiria anaweza kupata, hivyo kufikisha zaidi ya milioni tisa. Mwanasayansi wa siasa John Okumu pia anaonya kuwa hesabu za upinzani zinaweza kuonekana nzuri hadi pale hatua za Ruto za kuimarisha uungwaji mkono wake zitakapozingatiwa. Okumu anasema Ruto aliposhirikiana na Raila baada ya kumwondoa Gachagua katika wadhifa wa naibu wa rais, alilenga kuvutia sehemu ya kura za Raila kutoka maeneo nje ya Mlima Kenya. Anasema uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kama naibu wa rais pia ulilenga kumtenga Gachagua kisiasa. Mbunge wa Homa Bay, Peter Kaluma, anasema Ruto ana nafasi ya kurithi maeneo yaliyokuwa ngome za Raila. " Kiongozi wetu aliyeaga dunia alituacha katika serikali jumuishi, na mabadiliko ya utawala ni mjadala wa mwaka 2032," alisema. Hata hivyo, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anapinga mtazamo huo. Anasema baadhi ya viongozi waliokuwa na ushawishi katika maeneo ya Raila hawako tayari kuunga mkono Ruto, akitaja Kalonzo, Wamalwa, Babu Owino, James Orengo na Sifuna. Mchambuzi Festus Wangwe anasema kwa sasa hesabu za kisiasa zinaonyesha Gachagua, Sifuna na Kalonzo wana nafasi ya kuvutia wapiga kura. Mkakati wa Wamunyoro unaangazia uwezekano wa tiketi tano za urais na naibu wa rais. Pendekezo la kwanza ni Kalonzo kuwania urais huku Sifuna akiwa mgombea mwenza, mchanganyiko unaolenga kuunganisha uzoefu na nguvu za vijana. Pendekezo la pili ni Sifuna kuwania urais huku Kalonzo akiwa naibu wake. Wanaounga mkono mpango huo wanaamini unaweza kuongeza ushiriki wa vijana katika uchaguzi. Pendekezo la tatu ni Sifuna kuwania urais huku Gachagua akiwa mgombea mwenza. Mchambuzi Malila Munywoki anasema mpango huo unaweza kuvutia kura za Mlima Kenya, lakini ukakumbana na changamoto ya kukubalika kitaifa kutokana na uchovu wa kisiasa kuhusu kubadilishana uongozi kati ya jamii za Wakalenjin na Agikuyu. Pendekezo la nne ni Gachagua kuwania urais huku Kalonzo akiwa naibu wake. Munywoki anasema mpango huo unaweza kukabili changamoto za kukubalika nje ya ngome zao. Chaguo la tano ni Kalonzo kuwania urais huku Gachagua akiwa mgombea mwenza. Wachambuzi wanakubaliana kuwa mafanikio ya upinzani yatategemea iwapo viongozi hao wataafikiana kuhusu mgombea  urais mmoja, kugawana majukumu na kuvutia wapiga kura bila kuruhusu tofauti zao kudhoofisha juhudi za kumkabili Ruto mwaka 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Baraza la wazee laanza msako wa siku 100 wa kubaini wale ambao hawajatahiriwa

BARAZA la Wazee la Jamii za Mlima Kenya, Kiama Kia Ma, limeanzisha msako wa siku 100 wa kubaini wazee wa jamii za Gema ambao hawajatahiriwa, hatua inayozua mjadala kuhusu faragha na mila. Mlezi wa kitaifa wa baraza hilo, Kung'u Muigai, alisema zoezi hilo linawalenga wazee wote 3,674 waliosajiliwa kuendesha shughuli za kitamaduni. Alisema kila mzee atalazimika kuthibitisha kuwa ametahiriwa, huku zoezi hilo likifanywa kwa hiari na kwa faragha katika madhabahu ya kitamaduni. Muigai alisema suala hilo lilijadiliwa katika mkutano wa wazee 63 uliofanyika Kaunti ya Kiambu Septemba 28, baada ya kile alichokitaja kuwa mgogoro wa kitamaduni uliosababishwa na migawanyiko na tamaa. Alisema tangu 2010, visa 340 vya wazee ambao hawajatahiriwa vimeripotiwa, huku 146 vikigunduliwa baada ya vifo vyao. Wazee watakaokataa kushiriki zoezi hilo wataondolewa kwenye sajili ya wanaoruhusiwa kutekeleza majukumu ya kitamaduni. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Wachira Kiago, alisema tohara ni sehemu muhimu ya utambulisho wa jamii, akisisitiza kuwa baraza linapendelea mazungumzo badala ya vurugu. Muigai alisema baadhi ya wazee wamefichuliwa baada ya kugombana na wake zao, huku wengine wakigunduliwa walipolazwa hospitalini. Alifichua kuwa mzee mwenye umri wa miaka 72 kutoka Meru alishawishiwa kutahiriwa miaka miwili iliyopita. Wengine watatu wenye umri wa miaka 65, 68 na 74 kutoka Kiambu wanapona baada ya kufanyiwa tohara mwezi huu. Mwingine mwenye miaka 59 kutoka Murang'a anadaiwa kutoroka baada ya kuripotiwa na mkewe. Kwa mujibu wa Muigai, tangu 2010, visa 340 vya wazee ambao hawajatahiriwa vimeripotiwa, huku 146 vikigunduliwa baada ya vifo vyao. Alisema wazee watakaokataa kushiriki zoezi hilo wataondolewa kwenye sajili ya wanaoruhusiwa kutekeleza majukumu ya kitamaduni. Bw Joseph Kaguthi, mratibu wa baraza linalowakutanisha wazee wa Gema na viongozi wa dini, alisema mwanaume ambaye hajatahiriwa haruhusiwi kushiriki katika mikutano ya wazee, kufanya maamuzi ya kitamaduni au kutekeleza baadhi ya mila. Hata hivyo, mwanahistoria wa tamaduni, John Njue, alisema umuhimu wa kitamaduni wa tohara umepungua kwa miaka mingi, hasa baada ya hospitali na makanisa kuanza kushiriki katika shughuli hiyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Ni matumaini tu uokoaji ukiendelea katika jengo lililoporomoka jijini Nairobi

Familia za watu wanaohofiwa kunaswa chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi, zinaendelea kushikilia matumaini kuwa wapendwa wao watapatikana wakiwa hai, huku shughuli za uokoaji zikiendelea. Jengo hilo lililokuwa likijengwa liliporomoka Ijumaa na watu wasiopungua saba wakahofiwa kunaswa ndani yake. Matumaini yaliongezeka Jumamosi baada ya mwanamume mmoja kuokolewa akiwa hai zaidi ya saa 24 baada ya jengo hilo kuporomoka. Alikimbizwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwa matibabu. Christine Njeri, ambaye dada yake na binamu yake walikuwa wakiendesha duka katika sehemu ya chini ya jengo hilo, alisema hajui waliko tangu tukio hilo. "Tulizungumza jana, lakini sasa simu zao hazipatikani. Walihamia jengo hilo mapema mwaka huu kutoka jengo jingine hapa Eastleigh. Ninachoweza kufanya ni kuomba wapatikane wakiwa hai," alisema alipokuwa akisubiri taarifa kuhusu ndugu zake. Kwa Andrew Bwaio, anayefahamika eneo hilo kama Ojakoya, kusubiri taarifa kuhusu ndugu yake kumekuwa jambo la kuhuzunisha. Alisema kaka yake alikuwa akifanya kazi ya mabomba katika sehemu ya chini ya jengo hilo wakati lilipoporomoka. "Leo asubuhi aliweza kumpigia mama yangu simu nchini Uganda na kumwambia bado alikuwa chini ya vifusi na muda ulikuwa ukiisha. Mama yangu aliniambia nije hapa na nisiende bila yeye au mwili wake," alisema. Bwaio aliongeza kuwa binamu yake mwingine, ambaye pia ni fundi wa mabomba, alishuhudia jengo hilo likiporomoka akiwa katika jengo lililo mkabala. Hata hivyo, alisema tukio hilo lilimwathiri sana kiasi cha kushindwa kufika eneo la mkasa. Jamaa wa watu waliopotea walikusanyika katika hema lililotolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu nchini, wakisubiri taarifa kutoka kwa waokoaji. Kila taarifa mpya iliwapa matumaini, lakini pia iliongeza wasiwasi kuhusu hatima ya wapendwa wao. Shirika hilo lilisema wahudumu wake walishirikiana na mashirika mengine katika juhudi za kumtoa mwanamume huyo kutoka kwenye vifusi baada ya saa kadhaa za kazi ngumu. Katika taarifa Jumamosi alasiri, shirika hilo lilisema wafanyakazi 66 kati ya 67 waliokuwa wakijenga jengo hilo walikuwa wamepatikana na kuthibitishwa kuwa salama. Hata hivyo, msako uliendelea kutafuta mtu yeyote ambaye huenda alikuwa ndani au karibu na jengo hilo lilipoporomoka. Familia zinazotafuta jamaa zao zilitakiwa kutembelea dawati la ufuatiliaji la shirika hilo katika eneo la mkasa au kupiga simu bila malipo kupitia nambari 1199. Wakati huo huo, polisi wameanzisha msako wa kumtafuta mmiliki wa jengo hilo na mkandarasi wake, huku uchunguzi ukilenga kubaini chanzo cha mkasa huo na iwapo sheria zilikiukwa. Msemaji wa polisi Muchiri Nyaga alisema uchunguzi wa kina unaendelea kwa ushirikiano na wataalamu wengine. Alionya kuwa yeyote atakayepatikana na hatia ya uzembe au kukiuka kanuni za ujenzi atachukuliwa hatua kali za kisheria. Polisi pia waliwataka wananchi kuepuka Barabara ya Yusuf Haji na 9th Street ili kuruhusu mashine kubwa, mbwa maalumu wa uokoaji na maafisa kufanya kazi bila usumbufu. Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) ilitaja kampuni ya 9th Street Plaza Limited kuwa msanidi wa mradi huo, huku Stromax Holdings E.A. Limited ikitajwa kuwa mkandarasi. Emmanuel Mwangi Maina aliorodheshwa kama mbunifu na Joseph Muturi Mugu kama mhandisi wa miundo. Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alisema jengo hilo lilikuwa limekiuka miongozo ya ujenzi na kwamba kaunti ilikuwa imewasilisha taarifa kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa uchunguzi zaidi. Huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo, kwa familia zilizokusanyika eneo la mkasa, jambo muhimu zaidi ni kupata wapendwa wao. Kila dakika inayopita inaongeza maswali kuhusu wangapi wataokolewa wakiwa hai na wangapi hawatarejea tena kwa familia zao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 24 Oct 2026 15:19:42

Ruto aponda Kalonzo, akimwaga minofu Ukambani

Rais William Ruto amewataka wakazi wa Ukambani kumwacha kiongozi wa Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, na kuunga mkono azma yake ya kuchaguliwa tena mwaka 2027. Rais alisema serikali yake inalenga kuleta maendeleo katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni, akidai upinzani hauna mpango madhubuti wa kubadilisha maisha ya wakazi. Akizungumza katika mikutano mbalimbali baada ya kuzindua na kukagua miradi ya barabara, maji, nyumba na umeme vijijini, Ruto alisema Ukambani umekuwa nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi. "Hatutaki Ukambani iendelee kubaki nyuma. Tunaunganisha Wakenya wote kupitia serikali jumuishi itakayojumuisha watu wa eneo hili," alisema akiwa Mbiuni, Kaunti ya Machakos. Alionya wakazi dhidi ya viongozi wanaotumia siasa za kikabila na ubaguzi, akisema Wakenya wote ni ndugu na wanafaa kushirikiana kuleta maendeleo. Katika mikutano hiyo, alimkosoa kwa kushindwa kuboresha barabara inayoelekea nyumbani kwake licha ya kuhudumu katika nyadhifa za juu serikalini kwa miaka mingi. Hata hivyo, Ruto alilaumu tawala zilizopita kwa kupuuza eneo hilo katika mipango ya maendeleo, akiahidi kurekebisha hali hiyo. Ujenzi wa barabara ya Kandwia-Kyuso-Tseikuru unatarajiwa kuanza Jumatatu, siku ambayo rais anatarajiwa kuzindua ujenzi wa mabweni katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Tseikuru. Miradi hiyo ni sehemu ya mipango ya miundombinu ya thamani ya zaidi ya Sh150 bilioni iliyotengewa kaunti hizo tatu. Katika Makueni, rais alizindua barabara ya Wote-Kako-Ngoluni na Kyambeke-Kyuasini-Ukia, huku akizindua rasmi barabara iliyokamilika ya Tawa-Itangini. Katika Kaunti ya Kitui, alizindua ujenzi wa barabara ya Kwa Vonza-Kanyangi-Kyandula. Ruto alisema serikali imetenga Sh21 bilioni kuweka lami barabara mpya 10 Machakos na Sh16 bilioni kwa barabara saba Makueni. Aidha, alisema Sh28 bilioni zimetengwa katika mwaka wa kifedha wa 2026/2027 kujenga nyumba 8,000 za gharama nafuu, mabweni 6,000 na masoko 18 Machakos. Katika Mbiuni, alizindua mradi wa maji wa Mwala Cluster wa thamani ya Sh1.47 bilioni, unaolenga kusambaza lita milioni 6.6 za maji kila siku kwa wakazi wa maeneo ya Kangundo na Mwala. Ziara hiyo pia ilishuhudia Mbunge wa Yatta, Robert Basil, akihama Wiper ya Kalonzo na kujiunga na UDA ya Ruto. Basil alimtaja rais kuwa mkombozi wa jamii ya Wakamba, huku Mbunge wa Mwala, Vincent Musyoka, akihimiza wakazi kumuunga mkono katika uchaguzi ujao. Leo, Ruto anatarajiwa kuhudhuria ibada katika Kanisa la AIC Kasina, Mwingi ya Kati, kabla ya kukagua ujenzi wa Daraja la Mto Enziu. Daraja hilo limekuwa suala muhimu tangu Desemba 2021, basi lililokuwa limebeba waumini wa Kanisa Katoliki kwenda harusi liliposombwa na maji na kusababisha vifo vya watu 31. Ruto amesema serikali yake imejitolea kukamilisha mradi huo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 24 Oct 2026 07:55:53

Onyo kali kwa wanaotumia akaunti za M-Pesa za wengine kulangua pesa

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amewaonya Wakenya dhidi ya kuruhusu watu wengine kutumia akaunti zao za benki, laini za M-Pesa na vitambulisho kuhamisha pesa zinazotiliwa shaka, akisema wanaweza kujipata wakichunguzwa kwa uhalifu. Bw Ingonga alisema vijana wako katika hatari zaidi ya kutumiwa na mitandao ya wahalifu kufanikisha ulanguzi wa pesa na uhalifu mwingine wa kifedha. "Msiruhusu akaunti zenu za kifedha, vitambulisho au majukwaa ya kidijitali kutumiwa kwa shughuli za uhalifu," alisema wakati wa mkutano wa mazungumzo na wananchi katika Kanisa la AIC, Riruta, Nairobi. Alisema baadhi ya watu huruhusu marafiki na jamaa kutumia akaunti zao bila kujua chanzo cha pesa zinazopitishwa humo. Alionya kuwa wanaosaidia kuhamisha pesa haramu wanaweza kuwajibishwa kisheria kulingana na ushahidi. Bw Ingonga alikuwa akizungumza katika hafla hiyo kupitia mpango wa Ofisi ya DPP wa Chapa Gumzo na Prosecutor, unaolenga kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu mfumo wa haki za jinai. Pia alionya dhidi ya ulaghai mtandaoni, vitisho vya kidijitali na matumizi mabaya ya Akili Unde kuunda picha, video na sauti bandia. Aliwahimiza vijana kulinda taarifa zao binafsi wanapotumia mitandao, huku akisisitiza kuwa vita dhidi ya uhalifu wa mtandaoni lazima viheshimu haki za kikatiba, zikiwemo faragha na uhuru wa kujieleza. Kamishna wa Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, Jerusah Mwaathime, aliwataka vijana kukataa kujiunga na magenge ya uhalifu na kuepuka kusambaza maudhui yanayochochea vurugu. Onyo hilo linajiri huku ripoti ya Kituo cha Kuripoti Uhalifu wa Kifedha (FRC) ya mwaka 2024 ikionyesha kuwa kilichanganua ripoti 9,571 za shughuli zinazotiliwa shaka. Mamlaka zinaonya kuwa wahalifu hutumia akaunti za watu wengine kuficha chanzo cha pesa. Wakenya wanashauriwa kutokubali kuhamisha pesa wasizojua zilikotoka, kulinda siri zao za M-Pesa na kutotoa taarifa binafsi kwa watu wanaowapigia simu wakijifanya maafisa wa kampuni za huduma za kifedha.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 24 Oct 2026 06:30:48

Watu saba hawajulikani waliko baada ya jengo kuporomoka Eastleigh

Watu saba bado hawajulikani waliko baada ya jengo la ghorofa 18 kuporomoka Eastleigh, Nairobi, huku shughuli za uokoaji zikiendelea kwa tahadhari kutokana na hofu ya kuathiri hewa inayoweza kuwasaidia manusura walio chini ya vifusi. Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alisema wafanyakazi 67 waliokuwa wakijenga jengo hilo kando ya 9th Street kabla ya kuporomoka wamepatikana. Mmoja alijeruhiwa huku wengine 66 wakinusurika bila majeraha. Hata hivyo, watu saba wanaoaminika kuwa walikuwa katika maduka 11 kwenye ghorofa ya chini na sehemu ya chini ya jengo hilo hawakuwa wamepatikana kufikia Ijumaa jioni. "Tuna matumaini kuwa wako salama na shughuli hizi za uokoaji zitahakikisha wanaokolewa wakiwa hai," alisema Bw Murkomen. Shughuli za uokoaji ziliendelea hadi usiku, lakini zilikumbwa na changamoto baada ya kuripotiwa kuwa watu waliokuwa chini ya vifusi walilalamika kuwa mashine za kuchimba zilikuwa zikiathiri upatikanaji wa oksijeni. Waokoaji walisitisha kwa muda matumizi ya mashine hizo ili kushauriana kuhusu njia salama ya kufikia watu hao bila kuhatarisha maisha yao. Bw Murkomen alisema eneo hilo lilihitaji utaalamu wa wahandisi ili kuondoa vifusi bila kusababisha janga zaidi. Timu ya pamoja inayojumuisha Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), polisi, serikali ya kaunti ya Nairobi, Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya inaongoza shughuli hizo. Wakati huohuo, Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) imetaja kampuni na wataalamu walioorodheshwa katika rekodi zake kuhusu mradi huo. Mamlaka hiyo ilisema kampuni ya 9th Street Plaza Limited ndiyo msanidi wa jengo hilo, huku Stromax Holdings E.A Limited ikiwa mkandarasi. Rekodi hizo pia zinamtaja Emmanuel Mwangi Maina kama mbunifu na Joseph Muturi Mugu kama mhandisi wa miundo. NCA ilisema mradi huo ulisajiliwa Julai 30, 2025. Hata hivyo, taarifa hiyo haikubainisha ikiwa jengo hilo lilikaguliwa kabla ya kuporomoka au kama kulikuwa na ukiukaji wa usalama uliokuwa umeripotiwa. Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alisema jengo hilo halikuwa na cheti cha kuruhusu watu kuanza kulitumia. Chanzo cha kuporomoka kwake bado hakijabainika, huku uchunguzi ukitarajiwa kubaini iwapo kulikuwa na uzembe au ukiukaji wa kanuni za ujenzi. Bw Murkomen alionya kuwa wahandisi, wasimamizi wa ujenzi na wataalamu wengine watakaopatikana kuhusika na uzembe wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu. "Njia za mkato hazitatusaidia kama nchi. Ufisadi hautatusaidia. Kutafuta pesa za haraka kunaweza kugharimu maisha," alisema. Aliwataka maafisa wa serikali za kitaifa na kaunti kukagua majengo nchini ili kuhakikisha yanazingatia viwango vya usalama. Waziri huyo alisema tukio la Eastleigh ni la pili la kuporomoka kwa jengo kuripotiwa Nairobi mwaka huu, akitaka wanaohusika na ukiukaji wa sheria wawajibishwe. Kwa sasa, kipaumbele cha mamlaka ni kuwatafuta watu saba ambao hawajapatikana, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha mkasa huo na iwapo kuna mtu au taasisi iliyoshindwa kutekeleza wajibu wake.

read more