T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Watahiniwa waonywa kuhusu udanganyifu katika mitihani ya kitaifa

SERIKALI imewaonya wanafunzi na wasimamizi wa mitihani dhidi ya udanganyifu katika tathmini na mitihani ya kitaifa iliyoanza jana, ikisema watakaopatikana wataadhibiwa, kukiwemo kufutiwa kwa matokeo. Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema wanafunzi 3,634,846 wamejisajili kwa tathmini na mitihani ya mwaka huu, wakiwemo 1,380,463 wa KPSEA, 1,206,028 wa KJSEA na 1,048,355 wa KCSE. "Mwanafunzi yeyote atakayepatikana na hatia atachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufutiwa matokeo," akasema Bw Ogamba, akionya wazazi dhidi ya watu wanaodai kuuza mitihani. Alisema polisi hawajawekwa ndani ya vituo vya KPSEA na KJSEA ili wanafunzi wafanye tathmini katika mazingira tulivu bila vitisho. Serikali pia imeweka mipango ya kukabiliana na mvua, mafuriko, ukosefu wa usalama na maeneo magumu kufikika. Katibu anayesimamia Idara ya Elimu ya Msingi John Ololtuaa alisema walimu na maafisa 342,005 wamepewa jukumu la kusimamia shughuli hiyo, huku watahiniwa 50,873 wakitarajiwa kusahihisha mitihani. Katika kaunti za Kisii na Kisumu, tathmini zilianza bila matatizo makubwa. Mkurugenzi wa Elimu Kisumu Magara Onduso alisema vifaa vilisambazwa kwa wakati na usalama kuimarishwa. "Tumefanya maandalizi ya kutosha. Wasimamizi wamewasili kwa wakati na vifaa vimefikishwa mapema," alisema. Hata hivyo, Wanafunzi Kaunti ya Murang'a wanakabiliwa na wasiwasi wa njaa, huku nyumba 80,000 zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Kaskazini Mashariki, baadhi ya wazazi Garissa walidai shule zilikuwa zikitoza kati ya Sh10,000 na Sh30,000 kwa kila mwanafunzi kwa madai ya kupanga udanganyifu. Mkurugenzi wa Elimu wa eneo hilo Adan Roble alisema ofisi yake haikuwa imepokea taarifa hizo na akaonya watakaohusika kuwa wataadhibiwa. Katika eneo la Bonde la Ufa, wanafunzi katika maeneo ya Turkana yaliyoathiriwa na mashambulizi ya majambazi walisindikizwa hadi vituoni salama. Mvua na mafuriko pia yalilazimu maafisa kutumia boti kufikisha vifaa katika baadhi ya maeneo ya Turkana. Baringo iliripoti changamoto za taarifa za watahiniwa, lakini zilitanzuliwa kwa ushirikiano na KNEC. Trans Nzoia ilisema maandalizi yalikuwa yamekamilika. Nairobi, vifaa vilisambazwa bila matatizo, huku Mombasa na maeneo mengine ya Pwani yakichukua tahadhari dhidi ya mvua na mafuriko. Lamu iliweka boti tayari kusafirisha wasimamizi na maafisa wa usalama kwenye visiwa vya mbali. Katika eneo la Kati, maafisa walisema watawafikishia mitihani watahiniwa watakaougua hospitalini. Serikali imesema itashirikiana na Wizara ya Usalama kukabiliana na changamoto zozote wakati zoezi likiendelea. KPSEA inaendelea hadi Oktoba 28, KJSEA hadi Oktoba 30, huku KCSE ikiendelea hadi Novemba 20, 2026.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 51 minutes ago

Majonzi mtaa ukifiwa na mapasta watatu kupitia ajali Mtito Andei

WAKAZI wa mtaa wa Bangladesh, eneo la Mikindani, Mombasa, wamezama katika majonzi kutokana na vifo vya wachungaji watatu na waumini wengine katika ajali iliyoangamiza watu 24 katika eneo la Kanga, barabara ya Mombasa-Nairobi, Kaunti ya Makueni, Jumapili asubuhi. Wachungaji Joseph Vura wa Campaign for Salvation and Healing Ministry (CASHEM), Fonex Paul wa River of Life na Isaac Juma wa Grace Healing Sanctuary walikuwa kati ya waliokuwa wakirejea kutoka mazishi ya mwenzao katika Kaunti ya Kakamega, basi walimokuwa lilipogonga lori la mizigo lililokuwa limesimama. Katika mtaa wa Bangladesh, familia na marafiki wa marehemu bado wanatatizika kukubali ukweli wa vifo hivyo, huku wengine wakipanga mazishi na kuomboleza wapendwa wao. Bi Judith Awino, ambaye aliishi na shemeji yake Hollon Oduor Waganda kwa miaka 10, alisema alipokea habari za ajali hiyo alipokuwa akiomba katika Kanisa la Lamb of God, Mikindani. "Mume wangu alinipigia simu kuniuliza kuhusu wachungaji waliofariki katika ajali. Hakujua kwamba mdogo wake pia alikuwa ndani ya basi hilo. Tulipojaribu kumpigia simu, hakupokea," alisema. Familia ilimtuma ndugu mwingine wa marehemu aliyekuwa Samburu, kaunti jirani ya Kwale, kwenda Makueni kuthibitisha hali yake. Baadaye aliwapigia simu na kuwathibitishia habari walizokuwa wakihofia. Bi Awino alisema Waganda alikuwa ametembelea nyumbani kwake Jumanne kuazima sanduku la kusafiria. "Waliondoka, lakini sasa wanarejea nyumbani wakiwa wamefariki. Familia yetu imeshtuka," alisema. Mwili wa Waganda ulikuwa ukisubiri kuhamishwa hadi hifadhi ya ya Hospitali ya Coast General kabla ya kusafirishwa Siaya kwa mazishi. Katika Mataa ya Ndege, Jomvu, wakazi wanaomboleza Mchungaji Fonex Paul, aliyehudumu katika kanisa lake kwa zaidi ya miaka 10. Jirani yake Peter Bendi alisema marehemu alikuwa mwenye huruma, mchangamfu na aliyesaidia watoto wa eneo hilo kwa masomo ya ziada. Mchungaji huyo ameacha mkewe Ann Biyaki. Katika Grace Healing Sanctuary, mchungaji msaidizi Fredrick Ochieng Odhiambo alisema kifo cha Juma kimeacha pengo kubwa katika jamii. Juma ameacha mke na watoto wanne. Marehemu Vura, Juma na Fonex walikuwa na makanisa yaliyokuwa umbali mfupi katika mtaa huo wenye wakazi wengi. Wakati huo huo, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir na Mbunge wa Likoni Mishi Mboko Jumatatu walitembelea maaskofu Zachariah Mwagandi na Cosmas Oduor Nyangweso, wanaopokea matibabu katika Hospitali ya Coast General baada ya kunusurika ajali hiyo. Ajali hiyo ilitokea takriban wiki tatu baada ya watu 17 waliokuwa wakisafiri kwenda Subukia Shrine kufariki katika ajali ya Salama, barabara hiyo hiyo, Oktoba 4

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

Jengo la mkasa Eastleigh: nani alilala kazini?

KUPOROMOKA kwa jengo la orofa 18 katika Barabara ya 9, Eastleigh, Nairobi, kumeibua lawama kati ya taasisi zilizopaswa kusimamia ujenzi, huku kila upande ukikataa kuwajibika. Gavana Johnson Sakaja alisema kaunti haikuidhinisha mipango ya jengo hilo na kwamba ujenzi ulisimamishwa mara mbili. Alidai baadhi ya vibali vilivyosambazwa mitandaoni vilikuwa bandia. Hata hivyo, Msemaji wa Polisi Muchiri Nyaga alisema utoaji wa vibali na kusimamisha ujenzi ni jukumu la kaunti. Alisema tatizo la vibali haramu linapaswa kushughulikiwa ili kuzuia vifo. "Polisi hawana uhusiano wowote na ujenzi wa majengo ya aina hiyo. Hayo ni majukumu ya serikali za kaunti pekee, na kwa hakika, kaunti zina idara za utekelezaji wa sheria ambazo zina mamlaka ya kusimamisha kabisa kazi yoyote ya ujenzi," akasema Bw Muchiri.  Aliongeza kuwa madai ya gavana yanaonyesha mtu anayezama na kujaribu kushikilia chochote kile ili asizame. Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) Renson Ingonga alisema afisi yake haikuwa imepokea faili ya uchunguzi kutoka kaunti, na akaagiza Idara ya Upelelezi nchini (DCI) ichunguze iwapo maafisa wa kaunti, wajenzi au wataalamu walichangia mkasa huo.  Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) ilisema mradi huo ulisajiliwa Julai 30, 2025, huku kampuni ya 9th Street Plaza Limited ikitajwa kuwa ilihusika nao. Mmiliki Mohamed Khatar Ali Noor alisema jengo lilikuwa na vibali vyote japo mhandisi Joseph Muturi Mugu alijitenga na mradi huo. Mamlaka ya Kitaifa ya Utunzaji wa Mazingira (NEMA) ilikuwa imeiandikia kampuni hiyo Januari 2026 ikiitaka kuwasilisha michoro ya usanifu iliyo wazi kabla ya kushughulikia tathmini ya athari za mazingira. Ripoti ya NCA ya 2015 ilionya kuwa majengo yanaweza kukaliwa bila ukaguzi wa mwisho na cheti cha kuruhusu matumizi. Ukaguzi wa 2018 ulipata majengo 723 kuwa hatari sana na 10,791 kutokuwa salama. Mnamo 2024, Kamati ya Bunge la Kaunti ya Nairobi ilianzishwa kuchunguza madai ya vibali haramu, lakini ikavunjwa kabla ya kupokea barua muhimu. Mwenyekiti wake Nasra Nanda alisema uchunguzi huo ulizimwa licha ya umuhimu wake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Gachagua, Kalonzo wakutana Wamunyoro kujadili urais wa 2027

KINARA wa Wiper, Kalonzo Musyoka na wandani wake jana walisaka uungwaji mkono kutoka kwa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, mirengo hiyo miwili ikiahidi kushirikiana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Hata hivyo, wakati wa mazungumzo kati ya wawili hao, utata wa lini upinzani utatangaza mgombea mmoja wa urais ulitawala mazungumzo kati yao yaliyoandaliwa nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri. Duru ziliarifu kuwa mrengo wa Bw Musyoka ulipendekeza mgombea huyo atangazwe kufikia Desemba mwaka huu ili apate muda wa kutafuta rasilimali na kujenga mitandao ya kampeni ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, Bw Gachagua na washirika wake walitaka mchakato huo uahirishwe hadi miezi michache kabla ya uchaguzi wa Agosti 10, 2027. Wana hofu kuwa Rais William Ruto anaweza kuwashawishi baadhi ya viongozi wa upinzani kujiondoa ikiwa mgombea urais atatajwa mapema. Seneta wa Kitui, Enoch Wambua alisema mkutano huo haukuafikiana kuhusu tarehe kamili, kwa kuwa upinzani unajumuisha washirika wengi. "Hata hivyo, wazungumzaji katika mkutano huo walitambua kuwa Wakenya wanazidi kukosa subira kutokana na kuchelewa kutangazwa kwa mgombea wetu wa urais," akasema Bw Wambua. "Tunapoendelea kujenga muungano imara, huenda zawadi ya Krismasi ikawa kutangazwa kwa mgombea huyo," akaongeza. Hata hivyo, alisema uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa viongozi wakuu wa vyama. Mbunge wa Gatanga Edward Muriu na mwenzake wa Embakasi ya Kati, Benjamin Gathiru, maarufu kama Mejja Donk, walisema upinzani unahitaji muda zaidi kabla ya kumchagua mgombeaji. Bw Muriu alisema wamekubaliana kurasimisha ushirikiano wao kwa kutia saini mkataba, kabla ya kuunda muungano wa kisiasa.Bw Gathiru alionya kuwa kutangaza mgombeaji mapema kunaweza kumpa Rais Ruto nafasi ya kuvuruga upinzani na kuwadhamini wagombeaji miongoni mwao. "Tumekubaliana kuwa vyama tanzu vinapaswa kuheshimiana. Pia tumewapa viongozi wakuu ruhusa ya kuzungumza na kuamua kuhusu mgombea," akasema "Lakini mchakato huo haupaswi kuharakishwa. Tunajua Ruto anaweza kufanya nini. Anaweza kufadhili baadhi ya viongozi wajiondoe na kuwania urais," akaongeza. Kiongozi wa People's Party of Kenya (PPK) , Ndindi Nyoro alisema mazungumzo yanahitaji muda ili kupata mgombea anayefaa kukabiliana na changamoto za nchi. "Tunapaswa kuangalia hali ya nchi, kisha tuamue ni nani katika mrengo wetu ana uwezo zaidi wa kukabiliana na changamoto hizo. Tunatumai mchakato utakuwa wa haki na utazingatia sifa," akasema Bw Nyoro. Alisema chama chake kiko tayari kumuunga mkono mgombeaji atakayechaguliwa kupitia maridhiano. Bw Musyoka aliandamana na Bw Wambua, Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo na mwenzake wa Machakos Wavinya Ndeti, miongoni mwa viongozi wengine. Bw Gachagua alihudhuria akiwa na Bw Muriu, Seneta wa Nyandarua John Methu, Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang'wa. Bw Wambua alisema Musyoka na Gachagua walifanya mazungumzo ya kirafiki kuhusu mustakabali wa nchi. "Viongozi hao wawili wamejitolea kufanya kazi pamoja, kuunganisha wafuasi wao na kuhakikisha azma ya kumfanya Ruto kuwa rais wa muhula mmoja inatimia Agosti 10, 2027," akasema Bw Methu alisema DCP na Wiper zimekubaliana kufanya kazi kama vyama tanzu na kuendelea kutafuta njia ya kumpata mgombea mmoja wa urais. Viongozi hao wanataka kufikia makubaliano yatakayowawezesha kukabiliana na Rais Ruto katika uchaguzi ujao. Mkutano wa jana ulifanyika wiki moja baada ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kumtembelea Gachagua nyumbani kwake pindi alipotoka Amerika. Changamoto zinazokabili upinzani zinafanana na zile zilizokumba muungano wa National Rainbow kabla ya uchaguzi wa 2002. Wakati huo, viongozi wa upinzani walijadiliana kwa muda mrefu kuhusu mgombea wa kumkabili Kanu, chama kilichokuwa madarakani. Katika kitabu chake Seasons of Hope, aliyekuwa Seneta wa Kitui David Musila anakumbuka jinsi Raila Odinga alivyotatua mtanziko huo kupitia kauli maarufu ya "Kibaki Tosha" Septemba 22, 2002, miezi mitatu kabla ya uchaguzi. "Ujumbe ulikuwa wazi; upinzani uliokuwa umeungana dhidi ya Kanu ulikuwa umejipanga. Hata hivyo, hatukuweza kupuuza umuhimu wa kutaka kujua mgombea wetu angekuwa nani. Umati ulikuwa na hamu ya kupata jibu, lakini hakuna aliyekuwa nalo," aliandika Bw Musila. Alisema Raila alipofikia zamu yake ya kuzungumza, alitangaza ghafla kuwa Bw Kibaki ndiye aliyefaa kuwa mgombea. Kauli hiyo ilishangiliwa na umati na kutatua mzozo wa uteuzi. Historia inaonyesha kuwa wagombea wa urais nchini Kenya mara nyingi hutangazwa miezi michache kabla ya uchaguzi. ODM ilimteua Raila Septemba 1, 2007, huku muungano wa Cord ukimuidhinisha Disemba 22, 2012. NASA ilimtangaza Raila Aprili 27, 2017, na Azimio La Umoja ikamuidhinisha Machi 12, 2022. Kwa upande wa Kenya Kwanza, William Ruto aliteuliwa rasmi kuwa mgombea wa UDA Machi 15, 2022.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 26 Oct 2026 05:55:41

Azma ya Gideon Moi yavuruga hesabu za Ruto 2027

UAMUZI wa Kiongozi wa chama cha Kanu, Gideon Moi kuvunja kimya cha mwaka mmoja na kumshutumu Rais William Ruto kwa kutotekeleza makubaliano ya kisiasa umefungua ushindani mpya wa kudhibiti kura za Bonde la Ufa kuelekea uchaguzi wa 2027. Bw Gideon anadai Rais alisaliti makubaliano yaliyofikiwa Oktoba 10, 2025, katika makazi ya Kabarak ya aliyekuwa Rais Daniel arap Moi. Alisema alikubali kufanya kazi na Dkt Ruto kwa heshima ya urais, licha ya upinzani kutoka kwa baadhi ya wafuasi wake. "Nilifanya hivyo bila kusita, licha ya upinzani kutoka kwa watu wangu," akasema Bw Gideon, akiwataka wakazi wa Baringo wamsamehe kwa kumwamini Rais. Makubaliano hayo yalionekana kuunganisha UDA na Kanu, lakini Gideon lakini aliarifiwa baadaye kuwa kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, Oktoba 15, 2025, kilibadilisha mwelekeo wa makubaliano hayo. Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Moses Kiyiapi alisema kifo cha Raila huenda kilimfanya Rais Ruto kudhani hahitaji tena ushawishi wa Gideon baada ya kuanza kujipenyeza kisiasa Nyanza. "Uamuzi huo sasa unamrudia Rais miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu katika ngome yake ya kisiasa, ambako kila kura ni muhimu," akasema Bw Kiyiapi. Prof Prestone Chitere wa Chuo Kikuu cha Nairobi anasema hatua ya Bw Gideon kumkabili Rais hadharani inaweza kutatiza juhudi za Ruto kuimarisha uungwaji mkono Bonde la Ufa, hasa wakati uungwaji mkono katika maeneo mengine ya nchi haujahakikishwa. Mvutano huo unaweza kuathiri kura katika kaunti za Kimasai, zikiwemo Narok na Kajiado, pamoja na maeneo ya Bonde la Ufa Kaskazini kama Baringo, Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi. Viongozi wa Kanu wameunga mkono msimamo wa Bw Gideon, wakisema Rais lazima aonyeshe kuwa anaweza kutimiza makubaliano ya kisiasa. "Kanu ina mizizi nchini kote, na huwezi kukidharau kuelekea uchaguzi mkuu," alisema aliyekuwa Mbunge wa Tiaty Asman Kamama.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 26 Oct 2026 04:55:38

Wanafunzi 261,000 hawajulikani walipo mitihani ya kitaifa ikianza rasmi

ZAIDI ya wanafunzi 261,000 waliotarajiwa kuendelea na masomo na kufanya mitihani ya kitaifa mwaka huu hawajulikani walipo, hali inayozua maswali kuhusu sera ya serikali ya kuhakikisha wanafunzi wote kutoka shule ya msingi wanajiunga na zile za sekondari. Takwimu za Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) zinaonyesha kuwa watahiniwa 1,233,852 walifanya mtihani wa KCPE mnamo 2022. Hata hivyo, ni wanafunzi 1,048,355 pekee waliojisajili kufanya mtihani wa KCSE mwaka huu, pengo la wanafunzi 185,497. Vilevile, wanafunzi 1,281,210 walifanya tathmini ya KPSEA mnamo 2023, lakini waliojisajili kufanya tathmini ya KJSEA mwaka huu ni 1,206,028. Hii ni tofauti ya wanafunzi 75,182. Kwa jumla, wanafunzi 260,679 hawapo katika makundi yaliyotarajiwa kuendelea hadi mitihani inayofuata. Hata hivyo, tofauti hiyo haimaanishi kwamba wote waliacha shule, kwani huenda baadhi walifariki, wakahamia mifumo mingine ya elimu au kuchelewa kuendelea na masomo. Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema sababu kadhaa zinaweza kueleza tofauti hiyo. "Baadhi ya upungufu huu unatokana na hali za kawaida, ikiwemo wanafunzi waliofariki au ambao hawawezi kuendelea na masomo. Wengine wamehamia mifumo mbadala ya elimu kama shule za kimataifa," akasema. Aliongeza kuwa baadhi ya wanafunzi huacha shule kwa muda kutokana na mimba za mapema au maradhi, lakini huruhusiwa kurejea na kuendelea na masomo. Wakati huo huo, wanafunzi wa Gredi ya Sita na Gredi ya Tisa wanaanza tathmini za kitaifa, huku mitihani ya KCSE ikiendelea kote nchini. Jumla ya watahiniwa 3,634,846 wamejisajili kwa mitihani na tathmini hizo tatu. KNEC imetuma maelfu ya wasimamizi kuhakikisha zoezi hilo linaendeshwa kwa usalama. Mkurugenzi mkuu wa baraza hilo, David Njengere, alisema simu hazitaruhusiwa wakati wa mitihani ya KCSE. "Kukiuka sheria hii kutachukuliwa kuwa udanganyifu wa mtihani kwa mujibu wa sheria na kanuni za KNEC," akasema. Baraza hilo pia zinatumia kufuli zenye nembo ya usalama kwenye kontena za kuhifadhi karatasi za mitihani ili kuimarisha usalama. Hata hivyo, mgogoro kuhusu malipo ya walimu wanaosimamia mitihani bado unaendelea. Muungano wa Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Anuwai (KUPPET) ummewataka wanachama wake kujiepusha na shughuli za KNEC hadi malalamishi yao yatakapotatuliwa. Naibu katibu mkuu wa chama hicho, Moses Nthurima, alisema suala si kulipwa kwa wakati pekee, bali pia kiwango cha malipo. "Tunasisitiza kuwa walimu hawapaswi kujihusisha na shughuli za mitihani kwa sababu hiyo ni aina ya utumwa," akasema. Wakati huo huo, wakuu wa shule wameiomba Bunge kusitisha ukaguzi na ziara za maafisa wa serikali shuleni hadi mitihani imalizike, wakisema shughuli hizo zinawavurugia maandalizi. Hata hivyo, Spika Moses Wetang'ula alisema uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma hauwezi kusitishwa. "Uwajibikaji kuhusu matumizi ya rasilimali za umma si jambo la hiari. Ni wajibu wa kikatiba," akasema.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 26 Oct 2026 03:55:45

Jengo la mauti Eastleigh : Sakaja awalaumu polisi

GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja amelaumu polisi kwa kuwaachilia washukiwa waliohusishwa na ujenzi wa jengo lililoporomoka Eastleigh. Bw Sakaja amewataka maafisa wa usalama waeleze kwa nini watu waliokamatwa kwa kukiuka sheria za mipango ya miji waliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 bila kufikishwa mahakamani. Gavana huyo alisema maafisa wa kaunti walikagua eneo hilo na kubaini kuwa ruhusa ya kubadilisha matumizi ya ardhi ilikuwa imetolewa, lakini mipango ya usanifu iliyohitajika kuidhinisha ujenzi haikuwa imeidhinishwa. Alisema kaunti iliwakamata washukiwa na kuwakabidhi katika Kituo cha Polisi cha Kamukunji, lakini baadaye baadhi yao wakaachiliwa. "Tulitekeleza sheria na kuwakamata waliohusika na kwa kuwa hatuna mamlaka ya kuendesha mashtaka, washukiwa walikabidhiwa polisi. Inaripotiwa kuwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 bila kufikishwa mahakamani," akasema. Rekodi za polisi zinaonyesha washukiwa 14 waliwekwa kizuizini Juni 17, 2026, kwa makosa yanayohusiana na ukiukaji wa sheria za mipango miji. Hata hivyo, rekodi nyingine zinaonyesha washukiwa 10 waliachiliwa kwa dhamana kwa maagizo ya mkuu wa kituo hicho, hali inayozua maswali kuhusu kilichowapata wengine.   Wakati viongozi wakilaumiana, familia za watu waliopotea katika mkasa huo zinaendelea kusubiri habari za wapendwa wao. Kufikia Jumapili adhuhuri, familia 47 zilikuwa zimeripoti ndugu zao kutoweka, ingawa tisa zilikuwa zimeunganishwa tena na jamaa zao, kulingana na Katibu wa Wizara Susan Mang'eni. Dina Mueni amekuwa katika eneo la mkasa tangu Ijumaa akimtafuta dada yake, Eunice Mwikali, 41, aliyekuwa akifanya kazi ya ushonaji katika jengo hilo. "Kama anaweza kupatikana, nitashukuru sana. Si rahisi kumtafuta mtu bila kujua kama yu hai au amefariki," akasema Bi Dina. Hata hivyo, manusura Victor Onyango amewapa familia hizo matumaini. Fundi huyo wa ushonaji alinaswa chini ya vifusi Ijumaa, lakini akaokolewa Jumamosi akiwa na majeraha madogo. "Ninamshukuru Mungu sana," alisema. Hata hivyo, mashine zake tatu za kushona na biashara yake zilibaki chini ya vifusi.      

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 26 Oct 2026 02:55:26

Pepo la mauti laangamizi waumini wengine 25

SAFARI ya kurudi Mombasa baada ya mazishi ya askofu mwenzao iligeuka kuwa janga kwa wachungaji na familia zao baada ya basi walilokuwa wakisafiria kugongana ana kwa ana na lori katika eneo la Kanga, karibu na Mtito Andei, barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Watu 25 waliaga dunia katika ajali hiyo ya saa mbili kasorobo asubuhi, huku manusura wakisimulia matukio ya mwisho, juhudi za kuokoa wenzao na maumivu ya kutofahamu hatima ya jamaa zao waliokuwa safarini. Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa dereva wa basi hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 52 alikuwa ameliendesha kwa zaidi ya saa 16 bila msaada wa dereva mwingine, jambo lililozua wasiwasi kuhusu uchovu na usalama barabarani. "Dereva aliendesha gari kutoka Lugari, Kaunti ya Kakamega, hadi hapa. Hakuwa na mtu mwengine wa kumsaidia. Lazima alikuwa amechoka," akasema Mchungaji Cosmas Nyangweso, mmoja wa manusura. Alisema aliona basi likianza kuyumba barabarani kabla ya kugongana na lori lililokuwa likitoka upande wa pili. Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, basi hilo lilikuwa likijaribu kuyapita magari mengine lilipopoteza mwelekeo. Kamishna wa Kaunti ya Makueni, Abdullahi Khalif, alisema basi liliteleza na kuingia upande wa pili wa barabara kabla ya kugongana na lori, na kusababisha sehemu kubwa ya paa lake kung'oka. Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) ilisema ripoti za awali zinaashiria kuwa magari hayo yaligongana ana kwa ana na huenda kuyapita magari mengine isivyofaa kulichangia ajali hiyo. Basi hilo lilikuwa likirejea Mombasa baada ya abiria kuhudhuria mazishi ya Askofu Isaiah Kiganane katika kijiji cha Marakusi, Kakamega mnamo Jumamosi. Askofu Zachariah Mwagandi, mkuu wa Kanisa la Glorious River International, alisema wachungaji walijadiliana iwapo warudi Mombasa siku hiyo hiyo baada ya mazishi. Hatimaye waliamua kuondoka saa kumi jioni na kusafiri usiku kucha. "Tulikuwa na furaha tulipoondoka Mtito Andei baada ya kupata kifungua kinywa mwendo wa saa moja asubuhi. Tulikubaliana kuenda moja kwa moja nyumbani kwa askofu marehemu, ambako safari yetu ilianzia Alhamisi," akasema. Hata hivyo, furaha hiyo ilikatizwa na ajali iliyotokea dakika 15 tu baada ya kuondoka Mtito Andei. Mchungaji Spenza Mdave wa Kanisa la Voice of Faith, Malindi, alisema manusura walilazimika kushirikiana na dereva kuwatoa wenzao kwenye mabaki ya basi, huku baadhi ya madereva waliopita wakipuuza kilio chao cha kuomba msaada. "Tulishirikiana na dereva kuwaokoa manusura. Wengi wa waliofariki walikuwa wameketi nyuma ya basi," alisema akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mtito Andei. Hata hivyo, Bw Mdave alikuwa na wasiwasi kuhusu watoto wake wanne waliokuwa safarini. Alisema alianza safari akiwa na watoto wake watano, lakini mmoja alishuka Nairobi huku wengine wakisisitiza kuendelea hadi Malindi kumwona mama yao. Violet Mwandonyi, jamaa wa askofu marehemu, pia hakuwa na taarifa kuhusu watoto wake wawili waliokuwa kwenye basi hilo. Katika Kaunti ya Mombasa, habari za vifo ziliwaacha waumini na familia katika majonzi. Mchungaji Joseph Vura wa Kanisa la Campaign for Salvation and Healing alikuwa amempigia msaidizi wake saa 6:45 asubuhi akimwambia atachelewa kufika kwenye ibada. "Wakati wa simu alikuwa na furaha sana na aliniambia kuhusu safari na wachungaji aliokuwa nao. Sikujua alikuwa akinitumia ujumbe wa mwisho," akasema Mchungaji Andrew Mjomba. Baadaye, Bw Mjomba alipata habari kwamba Vura alikuwa miongoni mwa waliofariki. Mchungaji Isaac Juma wa Kanisa la Grace Healing Centre pia aliaga dunia. Mchungaji Isaac Wangila wa Kanisa la Glory Worship Centre alisema zaidi ya wachungaji 30 waliondoka Mombasa kuenda Kakamega kuhudhuria mazishi hayo. Alisema Mchungaji Stephen Ouma alikuwa amejeruhiwa kifuani na kichwani, huku wachungaji watatu kutoka Bangladesh wakiripotiwa kufariki. Jukwaa la Wahubiri Mombasa limeiomba serikali kuwasafirisha kwa ndege manusura wanaohitaji matibabu maalumu, kuondoa au kulipia bili za hospitali na kusaidia familia kugharamia mazishi. Ajali hiyo imezua tena wito wa kupanuliwa kwa barabara ya Mombasa-Nairobi, wiki tatu tu baada ya mahujaji 17 Wakatoliki kufariki katika ajali nyingine karibu na Salama. Mkurugenzi mkuu wa NTSA, Nashon Kondiwa, alisema ajali za barabarani zimefikia kiwango cha dharura kitaifa, huku watu 5,000 wakipoteza maisha kila mwaka. Alisema kutangaza ajali za barabarani kuwa janga la kitaifa kungewezesha serikali kuunganisha juhudi za usalama, kuongeza ufadhili na kuweka malengo yanayopimika ya kupunguza vifo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 25 Oct 2026 11:50:01

Ripoti yaonya kuhusu hatari ya vipodozi kwa macho

FASHONI  BIDHAA za urembo zinazotumika kila siku na waraibu wa vipodozi, mapambo na mitindo ya urembo ni kiini cha maelfu wanaoishia hospitalini kwa majeraha anuai, utafiti mpya unaonya.  Urembo sasa huenda ukakugharimu uwezo wako wa kuona, wataalam wanatahadharisha wakisisitiza haja ya kuwa makini unapotumia bidhaa mbalimbali za kuboresha mwonekano wako.  Maelfu ya watu hufika hospitalini kila mwaka wakiwa na majeraha ya macho yanayotokana na matumizi ya vifaa vya urembo na vipodozi, kulingana na ripoti mpya.  Ripoti iliwasilishwa katika kongamano la kila mwaka la American Academy of Ophthalmology (AAO).  Ilitaja vifaa hivi kujumuisha vipodozi vya macho, mapambo ya kutia nakshi kucha, bidhaa za nywele, gundi ya kope, spray ya uso na vifaa vinavyotumia moto kupamba nywele.  Vipodozi huenda vikaonekana kuwa na tishio ndogo kwa sababu ni vifaa vinavyotumika nyumbani kila siku.  Hata hivyo, "vinapotagusana na macho, hasa bidhaa zinazosheheni kemikali au vifaa vyenye moto wa kiwango cha juu, vinaweza kusababisha jeraha kubwa," wanaonya wataalam.  Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Missouri, Kansa City walichanganua data kutoka kwenye Mfumo wa Kitaifa wa Kuangazia Majeraha kwenye udadisi uliofanyika kati ya 2005 na 2024.  Walibaini kuwa watu wasiopungua 42,500 waliishia vitengo vya dharura katika hospitalini wakiugua majeraha ya macho yaliyotokana na vipodozi na vifaa vya kujitunza nafsi.  Wanawake na wasichana walijumuisha waathiriwa wanne kwa kila watano (asilimia 82) ya majeraha haya, kulingana na ripoti.  Ingawa umri wa jumla kwa wagonjwa ulikuwa miaka 24, watoto wenye umri wa miaka minne na kwenda chini waliathirika vilevile wakijumuisha karibu robo ya visa vya majeraha kutokana na vipodozi, walisema watafiti.  Mtindo wa majeraha ulitofautiana kutegemea umri wa mgonjwa. Kuchomeka na kemikali kulijumuisha asilimia 46 ya majeraha kwa macho ya wagonjwa wachanga wenye umri chini ya miaka 18, ikilinganishwa na chini ya asilimia moja ya watu wazima, utafiti ulionyesha.  Miongoni mwa majeraha yote ya kuchomeka na kemikali yaliyotibuiwa, asilimia 83 ilihusishwa na mtoto kushika kifaa cha kujipodoa.  Vipodozi hivi vilijumuisha bidhaa za kutunza ngozi na manukato (asilimia 40), bidhaa za kutia nakshi kucha (asilimia 22) spray na shampoo (asilimia 22).  Miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka minne na kwenda chini, asilimia 70 walijeruhiwa walipokuwa wakitumia vifaa au bidhaa za vipodozi wakiwa pekee yao bila uangalizi.  Watu wazima, kwa upande mwingine, aghalabu walipata majeraha ya kukatwa, vidonda au kukwaruzwa kwenye macho yao.  Majeraha kwa watu wazima yalijumuisha majeraha ya macho (asilimia 56) na majeraha ya kuchomeka macho (asilimia 22), kulingana na ripoti hiyo.  Wataalam wanasisitiza umuhimu wa kumakinika kuhusu uhifadhi wa vipodozi na vifaa vya kujitunza binafsi ili kuhakikisha havifikiwi na watoto.  "Kwa watoto, inamaanisha kusisitiza uhifadhi kwa njia salama na kuzuia kufikia bidhaa za urembo bila uangalizi hasa bidhaa majimaji na spray," walisema wataalam.  Vijana chipukizi na watu wazima wanashauriwa kuzingatia mbinu salama za kutumia na mapambo ya moto ili kupunguza tishio la majeraha.   

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 25 Oct 2026 11:19:48

Wanawake wanavyojichongea, waendeleza itikadi zilezile zinazowakandamiza

FATAKI TAASUBI ya kiume inayolaumiwa kila mara kama moja kati ya visababishi vikuu vya masaibu yanayowaandama mabinti tangu jadi kwa sehemu kubwa inaendelezwa na kuchangiwa na wanawake wenyewe hadi katika kizazi hiki. Japo ni kweli kuwa wanaume wanachangia pakubwa kuhusu ubaguzi wa jinsia ya kike, ukosefu wa usawa na mizigo wanayolazimishwa kubeba wanawake, ni muhimu kukabili ukweli mchungu kwamba mabinti, wakati mwingine, wanapigia debe na kuendeleza mifumo ileile inayowakandamiza.  Ni kinaya kwa hakika na tunaweza kufananisha uhusiano huu na mtumwa aliyezoea mateso ya mmiliki wake kiasi cha kuhiari kuendelea kumtumikia hata anapoamua kumpa uhuru wake!  Taasubi ya kiume haitamalaki kupitia matendo ya wanaume pekee bali hunawiri wakati wanawake huchunguza maamuzi ya wanawake wenzao, kuwadhalilisha mabinti wenzao kwa kukaidi matarajio ya jamii na kuwalaumu kwa majukumu yaleyale yaliyotelekezwa na wanaume.  Video iliyosambazwa sana mitandaoni iliyomwonyesha binti akimkashifu mama yake kwa kumwita 'toxic' eti kwa sababu alikataa kumlelea mtoto wake ili afanye kazi inatoa taswira bayana ya ukinzani huu.  Kwenye video hiyo, binti huyo anasimulia kwa machungu jinsi alivyolazimika kumwacha mtoto wake mchanga na mwanamme aliyemlazimisha baada ya mama yake kukataa katakata kurejelea majukumu ya ulezi kwa mjukuu wake.  Kiburi na matarajio yasiyo ya kirazini ya binti huyo kinastaajaisha mno kwa sababu watu waliofaa zaidi kumlea mtoto huyo basi ni wazazi wake na wala sio nyanya yake.  Hali kwamba alihisi kukomaa na kuwa tayari kujihusisha na shughuli za utu uzima ikiwemo kushiriki tendo la ndoa ni ithbati tosha kwamba alistahili kuwa tayari kwa majukumu ya utu uzima yanayojumuisha kubeba mimba, kuzaa na kumlea mtoto wake.  Badala ya kumkabili baba mtoto wake na kumshurutisha awajibike mwanamke huyu kwa maarifa au kwa kukosa maarifa alihiari kurekodi video chungunzima kumchamba mama yake kwa kutojali na kukataa kumshughulikia alipomhitaji zaidi!  Hata bila kujali kwamba mama yake sasa anastahili muda wa kupumzika baada ya kujitolea mhanga kumlea pamoja na ndugu zake, mwanamke huyu alitarajia bila soni kumtwika mwigo mwingine wa kumlelea mwanawe.   

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 25 Oct 2026 11:35:03

Ilani kuhusu baadhi ya vyakula na afya ya akili kwa matineja

UJAUZITO NA UZAZI IWAPO wewe ni mzazi wa vijana barobaro, basi utahitajika kuwa mwangalifu zaidi kuhusu uteuzi wao wa chakula ili kulinda afya yao ya akili.  Wataalam wanatahadharisha kuwa chaguo la vyakula kwa vijana chipukizi linaweza kuwa na madhara zaidi ya afya yao kimwili.  Chaguo la chakula na ulaji wa sukari limehusishwa na kuzuka baadaye kwa matatizo ya afya ya akili hususan wasiwasi uliokithiri na unyogovu, kulingana na utafiti mpya.  Udadisi huo uliashiria kwamba kula kiasi cha ziada cha aina yoyote ya matunda kila siku kunapunguza dalili za unyogovu kwa asilimia 13 na wasiwasi uliokithiri kwa asilimia saba.  Kiasi cha jumla cha ulaji wa matunda kilihusisha kula matunda mara mbili au tatu kwa siku katika kipindi cha utafiti huo ulioshirikisha vijana barobaro 6,537 kutoka shule 71 za sekondari Uingereza na Australia.  Washiriki wenye umri wa miaka 12.5 kwa jumla kutoka Gredi 7- Gredi 10 waliangaziwa kwa miaka minne hadi uchunguzi huo ulipokamilika,  Kunywa vinywaji vilivyoongezwa sukari ikiwemo soda, sharubati na vinywaji vya spoti kulihusishwa na ongezeko la unyogovu na wasiwasi.  Uhusiano kuhusu vinwaji vyenye sukari uligunduliwa miongoni mwa vijana chipukizi wavulana kwa wasichana, japo wavulana walionyesha viwango vya juu zaidi hasa wasiwasi uliokithiri.  "Sekondari ni kipindi ambapo vijana chipukizi huanza kupata uhuru zaidi kuhusu wanachokula na kunywa, wakati huo pia, matatizo mengi ya afya ya akili huanza kuchipuka," walifafanua watafiti.  "Hatusemi kula tufaha kutazuia unyogovu, au kwama kunywa soda kutasababisha wasiwasi – afya ya akili inahusu zaidi ya hayo. Lakini unachokula ni sehemu moja ya maisha ya kijana inayoweza kubadilishwa hivyo kufanya matokeo haya kuwa muhimu kwa mtazamo wa kinga."  Ni rahisi kufikiria chakula na lishebora kama zinazohusu afya ya mwili lakini utafiti huu unaongeza ushahidi kwamba wanachokula vijana ni muhimu vilevile kwa afya yao ya akili, wanasema wataalam.  Wanasisitiza umuhimu wa kuelewa kinachoongoza maamuzi bora ya chakula kwa vijana barobaro na kupatia kipaumbele lishebora kiafya ili kulinda afya yao ya akili.  "Shule, familia na serikali wote wana jukumu la kutekeleza kusaidia tabia inayozingatia afya na afya bora ya akili kwa vijana." 

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 25 Oct 2026 09:55:47

SHERIA: Hauwezi kuoa au kuolewa kabla ya kuvunja ndoa

Sheria ya Ndoa ya Kenya inaweka mipaka kwa mtu aliye kwenye ndoa ya mke mmoja kuingia katika ndoa nyingine, huku ikiorodhesha uhusiano wa kifamilia unaokatazwa kufunga ndoa. Je, mtu anaweza kuoa au kuolewa tena wakati ndoa yake ya kwanza bado ipo kisheria? Jibu linategemea aina ya ndoa aliyo nayo, kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Kenya ya mwaka 2014. Sheria hiyo inaweka wazi kuwa mtu aliye katika ndoa ya mke mmoja haruhusiwi kufunga ndoa nyingine wakati ndoa ya kwanza bado ipo. Hii ina maana kuwa mtu hawezi kuingia katika ndoa nyingine kwa sababu tu ameachana na  mke au mume wake, wameishi kando kwa muda mrefu au hawazungumzi tena. Mambo hayo pekee hayamalizi ndoa kisheria. Kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria ya Ndoa, mtu aliye katika ndoa ya mke mmoja haruhusiwi kufunga ndoa nyingine. Vilevile, mtu aliye katika ndoa ya wake wengi au ndoa inayoweza kuruhusu wake wengi haruhusiwi kuingia katika ndoa nyingine ya mke mmoja. Hata hivyo, kifungu hicho kinaanza kwa kurejelea kifungu cha 8, kinachopaswa kuzingatiwa katika kuelewa masharti yanayotumika kwa aina tofauti za ndoa. Hivyo, mtu anayefikiria kuoa au kuolewa tena anapaswa kwanza kuhakikisha hali ya ndoa yake ya sasa imeamuliwa kisheria badala ya kutegemea hisia au makubaliano ya mdomo pekee. Mbali na kuzuia mtu kuingia katika ndoa nyingine kinyume cha sheria, Sheria ya Ndoa inaeleza pia mahusiano ya kifamilia ambayo watu hawaruhusiwi kufunga ndoa. Kifungu cha 10 kinakataza ndoa kati ya mtu na babu au nyanya yake, mzazi, mtoto, mjukuu, dada, kaka, binamu, shangazi, mjomba, dada au kaka wa mzazi, mpwa na baadhi ya ndugu wengine waliotajwa katika sheria hiyo. Marufuku hiyo pia inahusu uhusiano fulani wa kifamilia kupitia mwenzi wa ndoa au mwenzi wa zamani. Kwa mfano, mtu haruhusiwi kufunga ndoa na babu au nyanya, mzazi, mtoto au mjukuu wa mwenzi wake au mwenzi wa zamani. Sheria hiyo inakataza pia ndoa kati ya mtu na mtu aliyemlea kwa njia ya kuasili, au mtu aliyemuasili, pamoja na mahusiano mengine ambayo mila husika zinakataza ndoa. Muhimu zaidi, kifungu hicho kinaeleza kuwa uhusiano wa damu wa upande mmoja, kama kuwa na mzazi mmoja wa pamoja, pia unaweza kuzuia ndoa. Hata hivyo, sheria inaweka tofauti kuhusu ndoa kati ya binamu kwa watu wanaofuata dini ya Kiislamu. Marufuku ya ndoa kati ya binamu iliyotajwa katika kifungu hicho haiwahusu wanaofuata imani ya Kiislamu. Kwa hivyo, kabla ya kufunga ndoa, ni muhimu kwa wanandoa watarajiwa kuelewa hali ya ndoa zao za awali na uhusiano wao wa kifamilia. Kushauriana na mtaalamu wa sheria kunaweza kusaidia kuzuia migogoro na kuhakikisha ndoa inayokusudiwa inakidhi matakwa ya sheria. Kwa ujumla, Sheria ya Ndoa inalenga kuweka utaratibu unaotambulika kisheria kuhusu ndoa na kuzuia ndoa zinazokatazwa. Mtu anayepanga kuanza maisha mapya ya ndoa anapaswa kuhakikisha kuwa hakuna kizuizi cha kisheria kinachoweza kufanya hatua hiyo iwe batili.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 25 Oct 2026 08:55:02

Sifuna anavyopangua hesabu za upinzani kwa fujo 2027 ikikaribia

KUPAA kwa umaarufu wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kumeanza kutatiza mipango ya viongozi wa upinzani wanaotaka kuungana ili kumng'oa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2027. Miezi michache iliyopita, jina la Sifuna halikuwa likitajwa sana miongoni mwa wanaoweza kuwania urais, ingawa baadhi ya watu walikuwa wakimhusisha na nafasi ya mgombea mwenza. Hata hivyo, umaarufu wake unaoongezeka, hasa miongoni mwa vijana, sasa unamwingiza katika mjadala kuhusu nani anafaa kupeperusha bendera ya upinzani. Mchango wa fedha kutoka kwa kina mama wafanyabiashara maarufu kama mama mboga umeongeza uzito wa kisiasa wa seneta huyo, huku akisema ameguswa na uamuzi wao wa kutumia mapato yao kumsaidia. Alisema hatua hiyo ni ishara ya imani ambayo wananchi wa kawaida wameweka kwake na ambayo hawezi kuichukulia kuwa ya kawaida. Mkutano wake na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, Oktoba 20, umefungua ukurasa mpya katika juhudi za kuunganisha upinzani. Ingawa washirika wa Gachagua walitaja mkutano huo kuwa wa kujuana, wachambuzi wanasema una umuhimu mkubwa katika siasa za kuelekea uchaguzi ujao. Wawili hao waliwahi kuwa pande tofauti wakati wa mchakato wa kumuondoa Gachagua madarakani Oktoba 2024, ambapo Sifuna, akiwa seneta, alishiriki katika mchakato huo. Sasa, wanachunguza uwezekano wa kushirikiana wakati upinzani unapojaribu kukubaliana kuhusu mgombea mmoja wa urais. Chanzo cha ndani ya mazungumzo hayo kiliambia Taifa Jumapili kuwa kuna uwezekano wa kuibuka kwa kile alichokiita "muungano wa milima", unaounganisha Mlima Elgon, eneo la nyumbani kwa Sifuna katika Kaunti ya Bungoma, na Mlima Kenya, ngome ya kisiasa ya Gachagua. Gachagua ametangaza kuwa yuko tayari kuwa mgombea mwenza wa Sifuna iwapo seneta huyo ataonekana kuwa chaguo bora zaidi la upinzani kumkabili Rais Ruto. Hata hivyo, mazungumzo ya ndani yanadaiwa kuhusisha pia jina la Seneta wa Nyandarua John Methu kama mgombea mwenza anayeweza kupendekezwa katika mazungumzo na Sifuna. Hili linaweza kuwa kikwazo katika ushirikiano huo, hasa huku viongozi wakishindania nafasi za juu na kujaribu kuamua nani atakuwa kinara wa tiketi ya urais. Katika mkutano wa Wamunyoro, pande hizo zilikubaliana kuwa na mgombea  moja ya urais na kumuunga mkono atakayechaguliwa kuuongoza. Hata hivyo, bado hawajakubaliana kuhusu utaratibu wa kumteua mgombea huyo. [caption id="attachment_185026" align="aligncenter" width="300"] Viongozi wa kisiasa wanaoegemea vuguvugu la Linda Mwananchi wawasilia mjini Busia kwa mkutano wa kisiasa hivi majuzi. PICHA|ALEX ODHIAMBO[/caption] Ushirikiano unaochipuka unaathiri hesabu za viongozi wengine wa upinzani, wakiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mgombea wa Jubilee Fred Matiang'i, kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua, kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi na wa DAP-K Eugene Wamalwa. Wote wamekuwa wakihusika katika juhudi za kuunganisha upinzani, lakini kuibuka kwa Sifuna na Gachagua kunaweza kubadilisha namna mazungumzo hayo yanavyoendeshwa. Aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama, ambaye sasa ni kamishna wa Tume ya Huduma ya Bunge na mshirika wa Rais Ruto, ameonya kuwa upinzani haupaswi kudharau uzito wa Kalonzo. Muthama anasema uzoefu wa kisiasa wa Kalonzo, uwezo wake wa kufanya mazungumzo na mahusiano aliyojenga kwa miaka mingi vinaweza kuwa muhimu katika uchaguzi ujao. Ametaja kuhudumu kwa Kalonzo chini ya Rais wa zamani Daniel arap Moi, kuteuliwa kuwa makamu wa rais na Mwai Kibaki na kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa 2013 na 2017 kama ushahidi wa uzoefu wake. "Katika siasa za Kenya, uchaguzi hushindwa au kushindwa kwa kutegemea idadi ya wapiga kura, mikakati, uaminifu na mahusiano," alisema Muthama. Alionya kuwa kundi lolote litakalopuuza umuhimu wa Kalonzo litakuwa likifanya kosa kubwa. Umaarufu wa Sifuna umeongezeka kufuatia mzozo wake na chama cha ODM kuhusu ushirikiano wake na chama tawala cha UDA na mwelekeo wa chama hicho baada ya kifo cha Raila Odinga. Akiwa katibu mkuu wa ODM, Sifuna alikuwa miongoni mwa viongozi waliotetea msimamo huru wa chama hicho na kukosoa ushirikiano wa kisiasa kati yake na Rais Ruto. Mvutano huo ulimwelekeza katika mrengo tofauti wa kisiasa, kupitia The Equitable Party, ambayo sasa inabadilisha kuwa Linda Mwananchi. Vuguvugu hilo linajitahidi kujijenga kwa misingi ya kuheshimu Katiba, uwajibikaji wa umma na ajenda ya kiuchumi inayolenga wananchi wa kawaida. Katika mahojiano na wanahabari jijini Nairobi Oktoba 9, Sifuna aliacha wazi uwezekano wa kufanya kazi na viongozi ambao hapo awali walikuwa na misimamo tofauti naye. Alipoulizwa kuhusu ushirikiano na Gachagua, alisema: "Tayari nilipigia kura ya kumuondoa madarakani kwa makosa yake. Kwa hivyo, hauwezi kuniuliza maoni yangu kana kwamba sijachukua hatua tayari." Kauli hiyo ilionyesha kuwa licha ya kushiriki katika mchakato wa kumuondoa Gachagua madarakani, Sifuna haoni kuwa hilo linazuia ushirikiano wao kisiasa. Hata hivyo, amekataa kuingia kwa undani kuhusu azma yake ya urais au namna mgombea mmoja wa upinzani atakavyochaguliwa. "Subirini kwanza. Mazungumzo hayo yatakuja baadaye," aliambia Taifa Leo alipoulizwa kuhusu mipango ya muungano. Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema umaarufu wa Sifuna unaweza kumwezesha kuzungumza na makundi tofauti ya wapiga kura, wakiwemo vijana na wanaopinga serikali jumuishi ya Ruto. Hata hivyo, anasema changamoto yake kubwa ni kubadilisha umaarufu huo kuwa mtandao wa kitaifa wenye uwezo wa kuendesha kampeni, bila kupoteza misingi iliyowavutia wafuasi wake. Kwa Gachagua, ushirikiano huo unatoa nafasi ya kupanua ushawishi wake nje ya Mlima Kenya. Naye Sifuna anaweza kumfungulia mlango kwa vijana na wapiga kura wanaotaka mwelekeo tofauti wa kisiasa. Akiwa ziarani Amerika, Gachagua alisema yuko tayari kuwa mgombea mwenza wa Sifuna iwapo juhudi zake za kumshinda Ruto zitafaulu na washirika wake watamshawishi kuchukua nafasi hiyo. Alisema: "Ninamfahamu Ruto vizuri na mimi ndiye ninayefaa kumpeleka nyumbani. Lakini nikishindwa na wakinishawishi vinginevyo, mimi Riggy G naweza kuwa naibu wa Sifuna." Katika mkutano wa Wamunyoro, alisisitiza kuwa alitaka pande hizo ziwe timu moja na kufanya kazi kwa manufaa ya nchi. Hata hivyo, wakili Chris Omore anasema changamoto kubwa ni iwapo viongozi hao wataweza kuafikiana kuhusu nafasi zao bila kuibua mzozo mwingine wa uongozi. Kwa upande mwingine, Kalonzo amekuwa akihusishwa na juhudi za kuunda upya muungano wa zamani wa Azimio kupitia Ukombozi Alliance, unaolenga kuunganisha vyama nyuma ya mgombea mmoja huku kila chama kikihifadhi utambulisho wake. Lakini Linda Mwananchi na chama cha DCP cha Gachagua vimeonyesha kutochangamkia muungano huo, hali inayoweza kusababisha mazungumzo tofauti ya kuunda muungano. Omore anasema iwapo ushirikiano wa Sifuna na Gachagua utageuka kuwa mpango rasmi wa uchaguzi, Kalonzo atalazimika kujadiliana na kundi lenye viongozi, mitandao na malengo yake. Wakati huo huo, Matiang'i, Karua na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro walikutana Njoro, Kaunti ya Nakuru, Oktoba 21, ambapo walikosoa ahadi za kiuchumi za Ruto na kutaka mwelekeo mpya wa kisiasa. Hali hii inaonyesha kuwa ushindani wa kuamua mgombea wa upinzani hauwahusu Sifuna na Gachagua pekee. Kalonzo, Wamalwa, Muturi na viongozi wengine pia wanajenga ushirikiano wao huku wakijaribu kuathiri uamuzi wa mwisho.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 25 Oct 2026 07:55:59

Itakuwa nusu mkate na UDA 2027,  ODM yaahidi wafuasi

CHAMA cha ODM kimewahakikishia wafuasi wake kuwa hakitapoteza ngome zake za kisiasa licha ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wake Raila Odinga na ushirikiano wake na chama tawala cha UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Viongozi wa chama hicho wamesema wanapania kushinda viti vingi vya magavana, maseneta, wabunge na wawakilishi wadi ili kuimarisha uwezo wao wa kujadiliana kuhusu ugavi wa mamlaka katika serikali ijayo. Akizungumza na wajumbe wa ODM katika Kaunti ya Turkana mjini Lodwar Ijumaa usiku, mwenyekiti wa chama Gladys Wanga alisema chama hicho kimeimarika baada ya kupitia kipindi kigumu kufuatia kifo cha Raila. Alisema ODM na UDA zinatarajiwa kuunda serikali kwa usawa wa asilimia 50 kwa kila chama, huku UDA ikichukua urais na ODM kupewa nafasi ya naibu wa rais. "Ni kawaida kupitia misukosuko tuliyopitia. Sasa tumetulia na tumetambua kuwa wengi wa wafuasi wetu bado wako ndani ya chama. Msitishwe na kulazimishwa kuondoka," alisema Wanga. Aliongeza kuwa ODM italazimika kushinda viti vingi vya uchaguzi ili iwe na nguvu za kudai nafasi muhimu serikalini, zikiwemo nyadhifa 10 za mawaziri. Wanga alisema pia chama hicho kinalenga kuhifadhi nafasi ya Waziri inayoshikiliwa na Beatrice Askul, ambaye aliteuliwa kwa ushawishi wa Raila. Alisema ODM inaendeleza ushirikiano na viongozi wa mashinani ili kuhakikisha kinashinda viti vingi Turkana na kufanya vizuri katika muungano wa serikali jumuishi. Katibu mkuu wa ODM, Catherine Omanyo, aliwataka wajumbe kuepuka migogoro ya ndani, akisisitiza kuwa chama ni kikubwa kuliko mtu mmoja na kinapaswa kuimarishwa ili kuvutia wanachama wapya. Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed alisema Turkana bado ni ngome ya ODM, licha ya Gavana Jeremiah Lomorukai kuondoka katika chama hicho. Alisema chama hicho kinalenga kuhakikisha mmoja wa wabunge wa Turkana Kaskazini, Ekwom Nabuin, au Turkana Kusini, Ariko Namoit, anachukua nafasi ya Lomorukai katika uchaguzi ujao. "Tumekuwa na gavana wa ODM Turkana tangu 2013, na mwaka 2027 gavana atatoka ODM tena," alisema Mohammed. Aliongeza kuwa iwapo UDA itashinda uchaguzi wa 2027, ODM itakuwa na nafasi ya kuwania urais mwaka 2032. Naibu kiongozi wa ODM Simba Arati alisema chama hicho kitafanya uteuzi wa haki na huru ili kumchagua mgombea wake mapema na kuanza kampeni za kurejesha ugavana Turkana. Alisema ODM pia itaimarisha miundo yake ya mashinani ili kukabiliana na ushindani kutoka kwa wagombea wenye uwezo mkubwa wa kifedha. Raila Odinga Junior aliwataka viongozi kubaki pamoja na kuendeleza urithi wa babake wa kutetea maendeleo ya usawa kupitia serikali jumuishi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 25 Oct 2026 06:55:11

Jinsi mikutano ya kisiasa yageuka biashara nono Nyanza

SIASA katika eneo la Nyanza zinazidi kuwa ghali huku wanasiasa wakitumia mamilioni ya pesa kurai wananchi kuhudhuria mikutano yao, hali inayofanya ukubwa wa umati kuwa kipimo cha ushawishi wa kisiasa. Nyuma ya mikutano yenye shamrashamra na viwanja vinavyojaa watu kuna biashara inayohusisha kukodisha mabasi, kutoa chakula na kulipa wanaohudhuria. Hali hii inafanya ushindani wa kisiasa kuwa mgumu kwa vijana na wagombea wasio na uwezo mkubwa wa kifedha. Mjadala kuhusu gharama hizo ulizidi kushika kasi baada ya video ya Mwakilishi wa Wanawake wa Homa Bay Joyce Osogo Bensuda kusambaa mitandaoni, akieleza jinsi alivyopanga kutumia mamilioni ya pesa kuleta watu kwenye mkutano. Mnamo Oktoba 2, Bensuda aliandaa Siku ya Wafanyabiashara wa Jua Kali katika Uwanja wa Raila Odinga, Homa Bay. Hafla hiyo iliwaleta pamoja wafanyabiashara kutoka wadi zote 40 za kaunti hiyo kupokea fedha na vifaa vya thamani ya Sh78.1 milioni kupitia  hazina tofauti za serikali. Katika video hiyo, Bensuda anaeleza kuwa alikusudia kutumia zaidi ya Sh1 milioni kuwalipa watu waliohudhuria, huku kila mmoja akitarajiwa kupata Sh1,000. Alisema katika hafla nyingine ya awali alitumia mabasi 56 kusafirisha watu hadi Ndhiwa na kuwalipa waliohudhuria Sh840,000, kila mmoja akipata Sh300. Fedha hizo hazikujumuisha gharama ya kukodi mabasi, fulana na miavuli. Kuhusu mkutano wa uwanja wa Raila Odinga, alisema alikuwa amepanga kutumia mabasi 62 ya shule na Sh1.5 milioni kwa shughuli za kuvutia umati pekee. Bensuda alithibitisha kuwa video hiyo ilikuwa yake, lakini akasisitiza haikuwa na uhusiano na ODM. Hakujibu maswali zaidi baada ya kutumiwa video hiyo na Taifa Jumapili. Uchunguzi wa Taifa Jumapili unaonyesha kuwa mfumo huo unahusisha waratibu wa mashinani, vijana, waendesha bodaboda, vikundi vya wanawake na viongozi wa maoni. Wengine hulipwa fedha taslimu, huku wengine wakipatiwa nauli na chakula. Kwa baadhi ya watu, kuhudhuria mkutano wa kisiasa kumekuwa njia ya kupata mapato ya siku moja badala ya kuonyesha tu uungwaji mkono kwa kiongozi. Emmanuel Sirunda, mwendesha bodaboda kutoka Ugunja, Kaunti ya Siaya, ni mmoja wa wanaofaidika na mfumo huo. Alikuwa miongoni mwa maelfu ya watu waliohudhuria mkutano wa Rais William Ruto katika eneo la Kisumu Shipyard. Sirunda alisema mabasi ya shule yalikodiwa kusafirisha wajumbe kutoka maeneo mbalimbali ya Nyanza. Walipofika, walipewa chakula na kuahidiwa malipo baada ya kusikiliza hotuba ya Rais. "Tulipewa Sh5,000 kila mmoja, bila kujumuisha nauli na chakula cha mchana. Haya ni mapato ambayo singepata kwa siku moja," alisema. Zaidi ya watu 10,000 walipokea Sh5,000 kila mmoja, sawa na takriban Sh50 milioni. Kila mmoja alihitajika kuwasilisha kadi nyekundu aliyokuwa amepewa mwanzoni mwa mkutano ili kulipwa. Shughuli ya kuzindua kaburi la kumbukumbu ya Raila Amolo Odinga mjini Bondo Oktoba 7 pia ilionyesha jinsi wanasiasa wanavyotegemea mitandao ya wahamasishaji kuvuta umati. Sally Akinyi, jina ambalo si lake halisi, alisema amejenga mtandao wa watu anaoweza kuwaita wanasiasa wanapohitaji umati. Anasema hulipwa kuhamasisha wafuasi kwa niaba ya wabunge wawili wa Nyanza wanaotaka kuwania ugavana, mgombea wa ubunge Kisumu ya Kati na, mara nyingine, wasaidizi wa Rais Ruto. Akinyi alisema wanaoitwa kwenye mikutano ndani ya Kisumu hulipwa Sh500 hadi Sh700, huku wanaosafiri nje ya mji wakipata kati ya Sh1,500 na Sh2,500, kutegemea kazi na umbali. Hata hivyo, alisema biashara hiyo si ya uhakika kila wakati, kwani baadhi ya wanasiasa hushindwa kuwalipa wahamasishaji baada ya mikutano. Wakati mwingine, malipo hutolewa kupitia ufadhili wa vikundi au basari badala ya fedha taslimu. Katika eneo la Gusii, linalojumuisha Kisii na Nyamira, viongozi wanaounga mkono serikali jumuishi huandaa hafla za uwezeshaji mara kwa mara. Baadhi ya wakazi hupokea kati ya Sh100 na Sh2,000, huku vikundi vilivyoandaliwa, kama vya wanawake na kwaya, vikivutia fedha zaidi. Wasaidizi wa baadhi ya viongozi wanasema mikutano hii hufadhiliwa na serikali, ikiwemo utoaji wa mchele na maharagwe kwa wafuasi. Vifaa vyenye nembo za kisiasa, kama kofia na fulana, pia hutolewa. Hata hivyo, swali kuu linalosalia ni fedha hizo zinatoka wapi na zinatolewaje.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 25 Oct 2026 05:55:41

Kenya inavyogeuka pango la magenge ya uhalifu

UCHUNGUZI wa miezi kadhaa kuhusu mtandao wa wizi wa simu jijini Nairobi umesababisha kukamatwa kwa MCA wa Ikanga/Kyatune, Cyrus Kisavi Musyoka, na kufichua jinsi magenge ya uhalifu yanavyofanya kazi nchini. Musyoka alikamatwa kuhusiana na visa vya wizi wa simu vilivyoripotiwa Agosti na Septemba 2026. Polisi wanasema picha za kamera za CCTV zilisaidia kumtambua. Simu zilizoibwa zinadaiwa kuuzwa kama mpya kwa wanunuzi wasio na habari, hata nchini Ethiopia. Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Muchiri Nyaga, alisema polisi sasa wanawalenga wafadhili na mitandao inayofadhili uhalifu, badala ya kuwakamata pekee wanaoiba mitaani. Alitaja kukamatwa kwa mshukiwa mmoja jijini Nairobi aliyepatikana na mifuko miwili ya simu zilizokuwa zikisafirishwa kwenda Uganda. "Kuna soko nchini Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nje ya mipaka yetu ya karibu," alisema, akieleza kuwa wezi wanaweza kufadhiliwa, kupewa maeneo ya kufanyia kazi na kuunganishwa na wanunuzi. Takwimu za serikali zinaonyesha ukubwa wa tatizo. Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, alisema mapema Oktoba kuwa serikali ilikuwa imetambua magenge 109 ya uhalifu nchini, kutoka 89 yaliyotangazwa kuwa haramu mwaka 2016. Kati ya Januari 1 na Agosti 31, 2026, washukiwa 1,827 walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa yanayohusiana na magenge na vurugu. Trans Nzoia iliongoza kwa washukiwa 491. Serikali iliripoti hukumu 729, huku kesi 716 zikiendelea mahakamani. Ripoti ya Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu (NCRC) ya mwaka 2025 ilibaini magenge 309 katika kaunti 11. Mombasa ilikuwa na magenge 73, Nairobi 56 na Kilifi 47. Baadhi ya makundi, yakiwemo Gaza Brothers na 42 Brothers, yako katika kaunti kadhaa. Ripoti hiyo ilisema magenge yanahusishwa na wizi, mashambulizi, usambazaji wa dawa za kulevya na kuitisha pesa  kwa vitisho kutoka kwa waendeshaji wa matatu. Pia ilionya kuwa vijana hujiunga na magenge kupitia ushawishi wa marafiki, huku ukosefu wa ajira, ufisadi na ushirikiano dhaifu kati ya polisi na jamii vikichangia tatizo hilo. Ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ya mwaka 2025 ilionya kuwa magenge hutumiwa katika misimu ya uchaguzi kutisha wapinzani, kuvuruga mikutano na kutekeleza malengo ya kisiasa kwa malipo. Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, wachambuzi wanaonya kuwa magenge yanaweza kutumiwa kuendeleza vurugu na vitisho. Ripoti ya Organised Crime Index ya mwaka 2025 iliorodhesha Kenya kuwa nchi iliyoathiriwa zaidi na uhalifu miongoni mwa nchi tisa za Afrika Mashariki, na ya nne kati ya nchi 54 za Afrika. Biashara haramu ya binadamu, usafirishaji wa dawa za kulevya, ulanguzi wa silaha na ulaghai wa kifedha zilitajwa miongoni mwa vitisho. Mchambuzi wa usalama James Chemiati alisema ukosefu wa ajira unawaweka vijana katika hatari ya kuajiriwa na magenge na wanasiasa wanaotaka kutumia vurugu dhidi ya wapinzani. Alisema baadhi ya vijana huishia kujihusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu wa mtandaoni baada ya shughuli za kisiasa kukamilika. Mchambuzi George Musamali alisema magenge yanaweza kuwa na majina, alama, viongozi na maeneo yanayodhibiti. Alitaja Mungiki, Baghdad Boys, Chinkororo na Gaza kama makundi yaliyowahi kutajwa katika miktadha tofauti kuwa walinzi wa jamii au magenge ya uhalifu. Wataalamu wanakubaliana kuwa kukamatwa kwa washukiwa pekee hakutamaliza tatizo. Polisi wanahitaji kuwafuatilia wafadhili, wanunuzi wa bidhaa zinazoibwa na watu wanaotoa ulinzi kwa magenge. Ushirikiano kati ya polisi na jamii, ulinzi wa mashahidi na nafasi za kiuchumi kwa vijana pia ni muhimu. Bila kuwawajibisha wanaofadhili na kunufaika na uhalifu, kukamatwa kwa wahalifu kunaweza kuacha mitandao inayochochea magenge ikiendelea kufanya kazi.

read more