T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

UN yaomba Sh1.16b kusaidia Waethiopia 50,000 wanaokimbilia Kenya

MASHIRIKA ya Umoja wa Mataifa yanaomba Sh1.16 bilioni kusaidia takriban watu zaidi ya 50,000 waliokimbilia Kenya kufuatia mapigano katika nchi jirani ya Ethiopia. Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Kenya, Fatima Mohammed-Cole, alisema wanashirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na UNICEF kutafuta fedha za kuwahudumia wakimbizi hao kwa miezi mitatu ijayo. Alisema fedha hizo zitatumika kununua chakula, makazi, maji na vifaa vya usafi, pamoja na kusajili na kulinda wakimbizi. UNHCR pia inakusanya vifaa vya dharura, ikiwemo mahitaji ya nyumbani na vifaa vya kujenga makazi ya muda kwa takriban watu 12,000. Wakati huo huo, wakimbizi zaidi waliendelea kuwasili mjini Moyale huku milio ya risasi ikisikika upande wa Ethiopia. Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo la Upper Eastern, Malik Adan, alisema hali ilitulia kiasi Ijumaa alasiri, ingawa milio ya risasi ilikuwa imesikika asubuhi. Alisema kambi kubwa iliyohamishwa kutoka mjini ina takriban watu 5,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Shirika la Msalaba Mwekundu liliripoti pia kuzaliwa kwa mtoto wa kwanza wa mama mkimbizi katika hospitali moja ya eneo hilo Ijumaa. Kwa upande wake, IOM ilisema serikali ya Kenya na mashirika ya kibinadamu yanaandaa mpango wa kusaidia hadi watu 80,000 iwapo idadi ya wanaowasili itaongezeka.  Mkuu wa IOM nchini Kenya, Nomagugu Ncube, alisema maelfu ya watu wamevuka mpaka kutafuta usalama na wengi wanahifadhiwa na jamii za wenyeji. Alisema mahitaji ya dharura yanajumuisha makazi, vifaa vya nyumbani, matangi ya maji na vidonge vya kusafisha maji. Ncube aliongeza kuwa mashirika hayo yataendelea kutathmini hali na kufuatilia idadi ya wakimbizi ili kuhakikisha wanaohitaji msaada wanapata huduma.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Msidanganywe, hakuna kafyu huku, polisi waambia wakazi wa Likoni

Polisi wamewahakikishia wakazi wa Likoni, Mombasa, kuwa eneo hilo liko salama na hakuna amri ya kutotoka nje usiku iliyotolewa kufuatia tukio la usalama lililosababisha kifo cha afisa wa kaunti na polisi mmoja kujeruhiwa. Katika taarifa aliyotoa Oktoba 30, 2026, Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Pwani Ali Nuno alisema tukio hilo lilitokea Jumatatu, Oktoba 26, maafisa walipokuwa wakitekeleza majukumu yao. Alifichua kuwa bunduki aina ya AK-47 pia ilipotea wakati wa tukio hilo. Bw Nuno alitaja tukio hilo kuwa la uhalifu na kusisitiza kuwa halimaanishi kuwa Likoni au eneo lote la Mombasa halina usalama. Alisema maafisa wa usalama wameimarisha msako wakilenga kuwakamata waliohusika, kurejesha bunduki iliyopotea na kuhakikisha washukiwa wanafikishwa mahakamani. Akijibu uvumi uliokuwa ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuwekwa kwa amri ya kutotoka nje usiku, kamanda huyo alipuuza madai hayo na kusisitiza kuwa hakuna amri kama hiyo iliyotolewa. 'Hakuna marufuku ya kutembea Likoni. Wananchi wanaofuata sheria hawataathiriwa kwa namna yoyote na operesheni za kiusalama zinazoendelea,' alisema. Aliwataka wakazi kuwa watulivu na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa, akionya kuwa habari za kupotosha zinaweza kuzua hofu isiyohitajika. Pia aliwashauri wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu usalama kupitia matangazo rasmi ya Huduma ya Polisi nchini. Wakati huo huo, idara za usalama zimeimarisha operesheni Likoni na maeneo mengine ya Mombasa ili kuwatambua washukiwa na kurejesha utulivu. Kwa mujibu wa Bw Nuno, operesheni hizo zinalenga kuwakamata waliohusika na tukio hilo, kurejesha bunduki iliyopotea na kuimarisha doria katika maeneo yaliyoathiriwa. Alisema maafisa zaidi wa usalama wamepelekwa katika eneo hilo kulinda maisha na mali ya wakazi. Aliwataka wakazi wa Likoni na Mombasa kuendelea na shughuli zao za kawaida bila hofu, huku wakishirikiana na polisi katika kudumisha amani. Pia aliwahimiza wananchi kutoa taarifa za kuaminika zitakazosaidia uchunguzi na kukamatwa kwa washukiwa. 'Naahidi wakazi wa eneo hili kuwa tutatekeleza wajibu wetu kwa haki, bila upendeleo, kwa uthabiti na kwa kuzingatia ukweli,' akaongeza. Polisi wamesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa jamii na kuwafikisha wahusika wa uhalifu Mahakamani

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Saudi Arabia yapiga marufuku safari za Wakenya kutokana na Ebola

Saudi Arabia imepiga marufuku raia wake kusafiri Kenya na kusitisha utoaji wa visa kwa wasafiri kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki kufuatia kuthibitishwa kwa ugonjwa wa Ebola, hatua inayoongeza wasiwasi kuhusu athari za kimataifa za ugonjwa huo. Hatua hiyo iliyotangazwa Ijumaa, Oktoba 30, inajumuisha pia kuwazuia wasafiri waliotembelea Kenya katika siku 21 zilizotangulia kuingia katika taifa hilo la Mashariki ya Kati. Saudi Arabia imejiunga na El Salvador ambayo tayari imezuia wasafiri kutoka Kenya na mataifa mengine saba ya Afrika. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA), marufuku hiyo inalenga kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo katika taifa hilo. Mamlaka ya afya ya Saudi Arabia, Weqaya, imesema hali ya afya nchini humo ni shwari na inaendelea kufuatiliwa. Hatua hizo zimeibua hofu kuhusu athari zinazoweza kukumba Kenya katika sekta za utalii, biashara na usafiri wa kimataifa. El Salvador ilitangaza kuwa wasafiri waliotoka au kupitia Kenya, Angola, Burundi, Ethiopia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Uganda hawataruhusiwa kuingia nchini humo. Mwanahabari wa CNN Larry Madowo hivi majuzi alifichua kuwa ombi lake la kupata kibali maalumu cha kuingia El Salvador lilikataliwa kutokana na maagizo hayo. Nchi nyingine zimechagua kuimarisha ukaguzi wa afya badala ya kupiga marufuku wasafiri. Korea Kusini iliiongeza Kenya katika orodha ya mataifa ambayo wasafiri wake wanahitaji kufanyiwa uchunguzi mkali wa afya kuanzia Oktoba 20. Wasafiri kutoka Kenya wanatakiwa kutoa taarifa kuhusu hali yao ya afya na wanaweza kufuatiliwa kwa siku 21, ambazo ni kipindi cha kupevuka kwa virusi vya Ebola. Amerika pia iliwaonya raia wake kufikiria upya mipango ya kusafiri Kenya, huku ikiimarisha ukaguzi wa wasafiri kutoka eneo hili. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya dhidi ya mataifa kufunga mipaka au kuzuia biashara kutokana na mlipuko huo. Katika taarifa ya Oktoba 23, WHO ilisema inapendekeza mataifa kuimarisha ushirikiano, ufuatiliaji wa afya, upimaji na kuwafuatilia watu waliokutana na wagonjwa badala ya kuweka vizuizi vya safari. Kenya ilirekodi kisa chake cha kwanza cha Ebola aina ya Bundibugyo baada ya mwanaume aliyekuwa amesafiri kutoka DRC kupitia Uganda kufariki Oktoba 5. Kufikia Oktoba 30, visa tisa vilikuwa vimethibitishwa na watu wawili kufariki. Wagonjwa wengine walikuwa jamaa wa mwathiriwa wa kwanza na wahudumu wa afya waliomhudumia. Katibu katika Idara ya Afya ya Umma, Mary Muthoni, alisema Kenya ilikuwa imepita siku 10 bila kuripoti maambukizi mapya. Alisema serikali ilikuwa imeimarisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo kwa kushirikiana na serikali za kaunti na washirika wa maendeleo. Wizara ya Afya pia ilisema watu waliokuwa wamekutana na wagonjwa na kukamilisha siku 21 za ufuatiliaji bila kuonyesha dalili waliachiliwa hatua kwa hatua. Wengine wanatarajiwa kukamilisha ufuatiliaji kufikia Novemba 11. Ebola ni ugonjwa hatari unaosambazwa kwa kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa. Dalili zake ni pamoja na homa, kutapika na kuharisha, huku wagonjwa mahututi wakikumbwa na kutokwa damu ndani au nje ya mwili.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Watu sita wafariki katika ajali ya matatu katika barabara ya Nakuru-Eldoret

Watu sita, akiwemo dereva wa matatu, walifariki dunia baada ya magari matatu kugongana katika eneo la Koriomat, kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret. Ajali hiyo iliyotokea usiku wa manane ilihusisha lori aina ya Mercedes-Benz Actros, gari aina ya Toyota Succeed na matatu aina  ya Toyota Hiace ya kampuni ya North Rift Sacco iliyokuwa na abiria 10. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Wilberforce Sichirani, alisema lori hilo lilikuwa likitoka Nakuru kuelekea Eldoret lilipokwepa gari jingine lililokuwa mbele yake. Katika kufanya hivyo, dereva wa lori alikata kona kuelekea upande wa kulia na kugonga Toyota Succeed kabla ya kugonga matatu hiyo. Nguvu za mgongano huo zilisababisha matatu na Toyota Succeed kutumbukia kwenye mtaro uliokuwa upande wa kulia wa barabara. Bw Sichirani alisema dereva wa matatu, aliyetambuliwa kama Shabaan Hassan Wanga, na abiria watano wa kike walifariki papo hapo. Abiria wengine ambao idadi yao haijabainishwa walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika hospitali mbalimbali za Kaunti ya Uasin Gishu kwa matibabu. Miili ya waliofariki ilipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret, kusubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti. "Tumeanzisha uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ajali hii ya kusikitisha," alisema Bw Sichirani. Polisi wanaendelea kutambua  waathiriwa wengine na idadi kamili ya waliojeruhiwa. Mabaki ya magari yaliyohusika katika ajali hiyo yanatarajiwa kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Burnt Forest kwa ukaguzi. Ajali hiyo inaongeza idadi ya watu wanaopoteza maisha katika ajali za barabarani nchini, huku mamlaka zikiendelea kuonya kuhusu hatari zinazotokana na makosa ya madereva. Baadhi ya sababu zinazochangia ajali hizo ni pamoja na kupita magari mengine bila tahadhari, mwendo wa kasi na madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Kaunti 47 zinatarajiwa kupata Sh457.28 bilioni katika mgao mpya

KAUNTI 47 zinatarajiwa kupata Sh457.28 bilioni kama mgao wa mapato ya kitaifa katika mwaka wa kifedha wa 2027/2028, ikiwa pendekezo la Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) litapitishwa. Kiasi hicho ni ongezeko la Sh29.28 bilioni ikilinganishwa na Sh428 bilioni ambazo kaunti zilitengewa katika mwaka huu wa kifedha utakaokamilika Juni 30, 2027. CRA, inayoongozwa na Bi Mary Chebukati, inapendekeza Wizara ya Fedha itengee serikali za kaunti fedha hizo katika mwaka unaoanza Julai 2027 na kukamilika Juni 2028. Akizungumza na wanahabari Alhamisi, Bi Chebukati alisema pendekezo hilo linatokana na makadirio ya mapato ya kitaifa ya Sh3.24 trilioni yatakayogawanywa kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti. Kati ya fedha hizo, serikali ya kitaifa inapendekezwa kupata Sh2.78 trilioni, huku kaunti zikitengewa Sh457.28 bilioni. Zaidi ya hayo, Sh10.25 bilioni zinapendekezwa kutolewa kupitia Hazina ya Usawazishaji. Bi Chebukati alisema ongezeko hilo litasaidia kulipia mishahara ya wahudumu wa afya wanaotekeleza mpango wa afya kwa wote (UHC), pamoja na nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali na wafanyakazi wa umma katika awamu ya nne ya mapendekezo ya Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC). Fedha hizo pia zinalenga kutekeleza makubaliano ya mishahara na marupurupu ya wauguzi, na kuongeza kwa asilimia tatu uwezo wa kaunti kutoa huduma kwa wananchi. "Pendekezo hili linalenga kusawazisha mahitaji ya kifedha ya ngazi zote mbili za serikali, kuhakikisha matumizi endelevu, kulipa madeni ya umma na kudumisha utoaji wa huduma kwa Wakenya," alisema. Alisema mgao unaopendekezwa kwa kaunti ni sawa na asilimia 22.3 ya mapato ya kitaifa yaliyokaguliwa na kuidhinishwa hivi majuzi. Kiwango hicho ni zaidi ya kiwango cha chini cha asilimia 15 kinachotakiwa na Katiba. Hata hivyo, pendekezo hilo linatolewa wakati ambapo Baraza la Magavana (CoG) linalalamikia kuchelewa kwa serikali ya kitaifa kutoa Sh8.9 bilioni zilizotengwa kulipia mishahara ya wahudumu wa mpango wa UHC walioajiriwa na kaunti kwa masharti ya kudumu na pensheni. Mwenyekiti wa CoG, Muthomi Njuki, alisema kaunti zimelazimika kutafuta fedha kutoka kwa vyanzo vingine ili kuwalipa wafanyakazi hao. Gavana huyo wa Tharaka Nithi alisema kaunti zimekuwa zikilipa wahudumu hao kwa miezi minne bila kupokea fedha ambazo serikali ya kitaifa iliahidi kutoa. Serikali ya kitaifa kupitia Wizara ya Afya na serikali za kaunti zilikubaliana kuwa wahudumu hao wataajiriwa na kaunti, huku fedha za kugharamia mishahara yao zikifuata kupitia mgao wa ziada kwa serikali za kaunti. Hata hivyo, Bw Njuki alisema fedha hizo bado ziko katika wizara ya fedha kwa sababu taratibu zinazohitajika ili kuzitoa hazijakamilishwa katika Seneti. "Fedha zilizopaswa kutengewa kaunti bado ziko wizara ya fedha kwa sababu taratibu zinazohitajika kuzitoa hazijashughulikiwa katika Seneti," alisema. Alitaka fedha hizo zitolewe mara moja, akionya kuwa kucheleweshwa zaidi kunaweza kudhoofisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Wakati huo huo, CRA imependekeza kuongeza kiwango cha matumizi ya kawaida ya mabunge ya kaunti hadi Sh50.36 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2027/2028, kutoka Sh39.19 bilioni za sasa. Hilo ni ongezeko la Sh11.17 bilioni, ambalo linalenga kugharamia mishahara ya madiwani (MCAs), shughuli za kawaida, magari, mafunzo na ajira za ziada. Kati ya fedha hizo, Sh3.54 bilioni zitatumika kulipa mishahara na marupurupu ya wafanyakazi, Sh1.74 bilioni kwa shughuli na ukarabati, Sh4.81 bilioni kwa magari, Sh474 milioni kwa mafunzo na Sh597 milioni kutekeleza mfumo mpya wa ajira. Kwa upande wa serikali kuu za kaunti, CRA imependekeza matumizi ya kawaida ya Sh25.85 bilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh602 milioni pekee.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

Maelfu ya majengo hatarini kuporomoka nchini, uchunguzi wabaini

MAELFU ya Wakenya wanaoishi au kufanya kazi katika majengo mbalimbali nchini wako hatarini baada ya ripoti mpya kufichua kuwa zaidi ya nusu ya majengo yaliyokaguliwa hayakidhi viwango vya ujenzi. Ripoti ya ukaguzi wa ubora kutoka Idara ya Ujenzi wa Umma, iliyowasilishwa bungeni, inaonyesha kuwa asilimia 57 ya majengo yaliyokaguliwa yana kasoro za kimuundo zinazoweza kusababisha mengi kuporomoka. Kati ya majengo 21,282 yaliyokaguliwa kati ya Julai 1, 2025 na Aprili 2, 2026, ni 9,264 pekee, sawa na asilimia 43.53, yaliyopatikana kuwa salama na kukidhi masharti ya ujenzi. Majengo 12,018 hayakufuata viwango vilivyowekwa kisheria. Hali hiyo imezua wasiwasi kuhusu usalama wa wananchi, hasa ikizingatiwa kuwa nchi imeshuhudia majengo 100 yakiporomoka tangu 1996. Mwaka huu pekee, majengo manane yameporomoka, idadi kubwa zaidi kurekodiwa katika mwaka mmoja kulingana na ripoti hiyo. Nairobi, ambayo hivi karibuni ilishuhudia jengo likiporomoka eneo la Eastleigh, ilikuwa na kiwango cha asilimia 57. Kati ya maeneo 3,908 ya ujenzi yaliyokaguliwa, ni 2,261 yaliyokidhi masharti. Uliokuwa mkoa wa magharibi uliongoza kwa usalama, ukiwa na kiwango cha asilimia 77. Kati ya majengo 1,520 yaliyokaguliwa 1,183 yamejengwa kwa kufuata viwango vinavyotakiwa. Kaskazini Mashariki ilikuwa na hali mbaya zaidi, ikiwa na kiwango cha utiifu cha asilimia tano pekee. Kati ya majengo 220 yaliyokaguliwa, ni 11 tu yaliyoruhusiwa kuendelea na ujenzi huku miradi 209 ikisitishwa. Eneo la juu la Mashariki ya nchi lilifuata kwa asilimia 14, huku eneo la Kati ya Bonde la Ufa likiwa na asilimia 18.38, Pwani asilimia 20.25 na Nyanza ya Kati asilimia 20.68. Eneo la Mlima Kenya lilikuwa na kiwango cha asilimia 65. Kati ya maeneo 1,225 yaliyokaguliwa, miradi 807 ilikidhi masharti huku 418 ikisitishwa. Ripoti inasema kuporomoka kwa majengo kunachangiwa zaidi na kasoro katika usanifu, vifaa duni na kazi isiyozingatia viwango. Baadhi ya wajenzi wa majengo wanadaiwa kupunguza gharama kwa kutumia saruji isiyotosha, hasa katika maeneo yenye udongo dhaifu, ili kuongeza faida. "Baadhi ya wasanidi, katika juhudi za kupunguza gharama za ujenzi kwenye maeneo yenye udongo dhaifu, huathiri kiwango na ubora wa saruji, na hivyo kuongeza hatari ya majengo kupata hitilafu za kimuundo na kuporomoka," ripoti inasema. Pia kuna watu wasiohitimu wanaojifanya wahandisi na wasanifu majengo, wanaouza michoro ya ujenzi kwa wawekezaji. Ripoti inasema baadhi ya wakandarasi hutumia wafanyakazi wasio na ujuzi, kupuuza michoro iliyoidhinishwa na kukwepa taratibu muhimu kama kuchanganya saruji kwa vipimo sahihi, kubana na kuimwagilia maji kwa muda unaotakiwa ili ikauke vizuri. Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) ina jukumu la kukagua maeneo ya ujenzi na kuhakikisha yanafuata sheria. Wakaguzi huangalia iwapo mkandarasi amesajiliwa, ana cheti, vibali vimebandikwa kwenye bango la mradi na wataalamu wanaohusika wameidhinishwa. Pia hukagua vifaa vya kujikinga kwa wafanyakazi, mabango ya usalama, uzio wa eneo la ujenzi na iwapo wasimamizi pamoja na wafanyakazi wana vyeti vinavyotambulika. Mradi unapopatikana kukiuka masharti, NCA inaweza kusimamisha ujenzi na kuweka alama nyekundu ya X kuonyesha kuwa kazi hairuhusiwi kuendelea hadi kasoro zirekebishwe. Mwenye jengo hupewa siku 14 kutekeleza masharti yanayotolewa. Akishindwa, anaweza kufunguliwa mashtaka mahakamani. Mtu anayepatikana na hatia ya kukaidi agizo la mkaguzi anaweza kufungwa jela miaka mitatu, kutozwa faini ya Sh1 milioni au adhabu zote mbili. Hata hivyo, ripoti inaonyesha kuwa kufikia Machi 31, 2026, ni kesi 15 pekee zilizokuwa zimefanikiwa katika kaunti mbalimbali. Ripoti inalaumu uchunguzi na mashtaka machache kwa kuchochea hali ya kutowajibika miongoni mwa wawekezaji na wataalamu wasiofuata maadili. Inataka idara za usimamizi na uchunguzi kuimarishwa ili wanaokiuka sheria wawajibishwe. Miradi yote inapaswa pia kufuata Kanuni za Ujenzi za 2024, zinazoweka viwango vya usanifu, ujenzi na utunzaji wa majengo. Kanuni hizo zinataka michoro na usimamizi wa ujenzi kufanywa na wataalamu waliosajiliwa katika taaluma husika. Wanaokiuka masharti hayo wanaweza kutozwa faini ya Sh1 milioni, kufungwa jela au kupokonywa leseni zao za kitaaluma na za kuwa wanakandarasi. Ripoti inasema Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) pia huchunguza kwa kina visa vya majengo kuporomoka ili kubaini iwapo kuna makosa ya jinai yaliyofanyika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 18 hours ago

Wito serikali ya Rais Samia ifichue ripoti ya ghasia baada ya uchaguzi Tanzania

WATAALAMU wa Umoja wa Mataifa (UN) wa kutetea haki za binadamu wameitaka serikali ya Tanzania kuchapisha ripoti kamili ya uchunguzi wa ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, wakionya kuwa kuendelea kuificha kunawanyima waathiriwa na familia zao haki ya kujua ukweli na kupata haki. Wataalamu hao wamesema mwaka mmoja baada ya ghasia hizo, hakuna kiongozi wa serikali aliyefunguliwa mashtaka kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu ulioripotiwa, ukiwemo mauaji ya kiholela, watu kutekwa, kukamatwa bila kufuata sheria na kuteswa. "Bado hakuna haki wala uwajibikaji kwa mamia ya waathiriwa. Majibu wanayoyatafuta bado yamefichwa katika ripoti ambazo hazijawekwa wazi," walisema. Ghasia hizo zilifuatia uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, ambapo maandamano yalizuka katika maeneo mbalimbali nchini humo. Vyombo vya usalama vilishutumiwa kutumia nguvu kupita kiasi, ikiwemo risasi, dhidi ya waandamanaji na raia wengine. Wakati huo, huduma za intaneti zilikatizwa kwa siku kadhaa, huku waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu wakiripoti vitisho na unyanyasaji. Tume ya kwanza ya uchunguzi iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwezi Novemba 2025 iliwasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026. Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, alisema tume hiyo ilirekodi vifo vya watu wasiopungua 518 katika maeneo 11, ingawa idadi hiyo huenda ilikuwa kubwa zaidi. Hata hivyo, ripoti hiyo haikuchapishwa kikamilifu. Muhtasari wake haukubainisha watu binafsi waliohusika na ukiukaji wa haki, wala kupendekeza waliohusika wafunguliwe mashtaka. Pia haikufanya tathmini ya kina kuhusu uhalali wa matumizi ya nguvu na vyombo vya usalama. UN imesisitiza kuwa uchunguzi unaofanywa unapaswa kuwa huru, wa haraka, wa kina na usioegemea upande wowote, ili waathiriwa wapate haki ya kujua ukweli, fidia na hatua za kuwawajibisha waliohusika. Mwezi Agosti 2026, serikali ilianzisha tume ya pili ya uchunguzi kuhusu matukio hayo. Hata hivyo, wataalamu wa UN wamesema bado hakuna maelezo ya kutosha kuhusu mamlaka na kazi yake, huku ushirikishwaji wa waathiriwa ukiripotiwa kuwa mdogo. Tume hiyo, inayoongozwa na Jaji mstaafu Shaban Ally Lila, imeanza kukusanya ushahidi kuhusu watu waliopanga, kufadhili, kuratibu au kushiriki katika ghasia hizo. Mwenyekiti wake alisema Oktoba 27 kuwa uchunguzi umeingia katika hatua ya kutambua waliohusika. Wataalamu hao pia wameibua wasiwasi kuhusu madai ya kuwepo kwa makaburi ya halaiki, miili kuondolewa katika vyumba vya kuhifadhia maiti na mamia ya watu kuendelea kuzuiliwa kwa muda mrefu bila kesi zao kusikilizwa. Baadhi ya washukiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya uhaini na makosa yanayohusiana na ugaidi. Aidha, wamesema familia za waathiriwa, mashirika ya kiraia, waandishi wa habari na wanaharakati wanakabiliwa na vitisho, ufuatiliaji na vikwazo vinavyobana uhuru wa kujieleza na kushiriki katika shughuli za kiraia. Historia ya Tanzania ya kuwa na utulivu wa kisiasa katika eneo la Afrika Mashariki imekuwa ikitajwa kama moja ya sifa zake. Hata hivyo, ghasia za uchaguzi wa mwaka jana zimeibua maswali kuhusu uwajibikaji wa vyombo vya usalama, uhuru wa kisiasa na imani ya wananchi katika taasisi za serikali.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 19 hours ago

Korti yaamuru IG Kanja, DCI Amin kufikisha mwanaharakati Mwaipaya kortini

MAHAKAMA Kuu imewaamuru Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin kumfikisha kortini mwanaharakati raia wa Tanzania Twaha Mwaipaya, akiwa hai au maiti, Jaji Alexander Muteti alitoa agizo hilo Oktoba 30, kufuatia madai kwamba Mwaipaya alitekwa nyara eneo la Kamulu, Nairobi, Oktoba 25 na watu wasiojulikana. Jaji pia aliwaagiza Kanja na Amin, au wawakilishi wao, kufika mahakamani Novemba 2 kueleza sababu za kukamatwa na kuzuiliwa kwa Mwaipaya na kwa nini asiachiliwe mara moja. Shirika la Vocal Africa liliwasilisha kesi likitaka Mwaipaya afikishwe mahakamani likidai alipotea akiwa mikononi mwa polisi. Shirika hilo linasema liliripoti kutoweka kwake katika Kituo cha Polisi cha Ruai siku aliyopotea, lakini juhudi za kumtafuta katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Nairobi hazikufua dafu. Mahakama imeagiza polisi na DCI kuwasilisha majibu yao kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo Jumatatu.  Kwa mujibu wa shirika hilo, Mwaipaya ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Tanzania mwenye wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii. Linaonya kuwa maisha yake yako hatarini iwapo atapelekwa kwa nguvu hadi Tanzania, ambako anaweza kuteswa au haki zake kukiukwa. Shirika hilo pia lilieleza kuwa waliomteka walitumia magari yaliyokuwa na nambari bandia na yasiyokuwa na nambari, huku baadhi ya waliokuwa ndani wakiwa wamejifunika nyuso na kubeba bunduki. Lilitaja visa vingine vya watu waliodaiwa kutekwa nchini Kenya, wakiwemo Macmillan Kiarie, Evans Otieno, Michael Oloo na Abdulaziz Duba, ambao hawajulikani waliko. Vocal Africa ilisema inatia wasiwasi kuwa visa hivyo sasa vinahusisha hata raia wa kigeni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Wantam! Sifuna hatimaye azindua kikosi cha Linda Mwananchi

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna ametangaza kikosi cha viongozi anaopendekeza kuongoza chama cha Linda Mwananchi Movement (LMM), akimteua aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi miongoni mwa vigogo watakaokuwa na majukumu makubwa. Sifuna alitangaza mapendekezo hayo jana wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi, huku viongozi wa Linda Mwananchi wakijiandaa kwa mkutano wa kitaifa wa wajumbe utakaopitisha na kuidhinisha uongozi huo. Alisema chama hicho kinapendekeza kuwa na kiongozi mkuu na manaibu wanne, huku nafasi moja ikitengewa mwakilishi kutoka eneo la Pwani. Mwangaza, mbunge wa Mavoko, Patrick Makau na aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) Faith Odhiambo ni miongoni mwa waliopendekezwa kuwa manaibu wa kiongozi wa chama. "Tumekubaliana kuwa na kiongozi wa chama na manaibu wanne. Kwa sasa, tumependekeza kuwa Kawira Mwangaza mmoja wa manaibu hao," alisema Sifuna. Osotsi amependekezwa kuwa mwenyekiti wa chama, akisaidiwa na aliyekuwa Mbunge wa Makadara Reuben Ndolo. Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi amependekezwa kuwa katibu mkuu, huku Pauline Njoroge akitajwa kuwa naibu wake. Seneta wa Kisii Richard Onyonka amependekezwa kuwa mweka hazina wa kitaifa, akisaidiwa na Abigael Gikonyo. Kari Karani amependekezwa kuwa katibu wa masuala ya maandalizi na mipango, huku Francy Kadide akipewa nafasi ya katibu wa masuala ya sheria. Katika uongozi wa wanawake, Caroline Mayuzu amependekezwa kuongoza chama cha wanawake, huku Fredah Onduso akitajwa kuongoza vijana. Torome Nalengoyo, aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa ODM Kaunti ya Narok, amependekezwa kuwa mwakilishi wa makundi madogo katika jamii. Eunice Juma, mmoja wa waanzilishi wa chama hicho, amependekezwa kuwa katibu wa masuala ya Wakenya wanaoishi ughaibuni, huku Gilbert Shanga akitajwa kuwa katibu wa masuala ya kimataifa.  Mbunge wa Trans Nzoia George Natembeya amepewa jukumu la kusimamia kampeni za urais, huku Faith Odhiambo akipendekezwa kuwa naibu mwenyekiti wa kampeni hizo. Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amependekezwa kuwa katibu wa masuala ya kisiasa. Majina hayo yatawasilishwa kwa mkutano wa kitaifa wa wajumbe ili kujadiliwa na kuidhinishwa kabla ya chama hicho kukamilisha kuunda mifumo yake ya uongozi. Akizungumza katika hafla hiyo, Sifuna alisema safari ya kuanzisha chama hicho imekuwa ngumu, akidai kuwa mikutano yao imekuwa ikivurugwa na wahuni. Alitaja vifo vilivyotokea wakati wa mikutano yao Kitengela na Homa Bay, akisema viongozi na wafuasi wao wamepitia changamoto licha ya Kenya kuwa taifa la kidemokrasia. Alisema chama hicho kina azma ya kuweka wananchi mbele na kuunda serikali itakayoheshimu haki za binadamu. Sifuna pia aliahidi kupunguza matumizi ya serikali na kufuta ushuru wa nyumba siku ya kwanza watakapoingia madarakani. Alimkosoa Rais William Ruto, akidai kuwa amekuwa akiiga sera na mawazo ya Linda Mwananchi, huku akiahidi kuwa chama hicho kitamwondoa mamlakani katika uchaguzi ujao. Hafla hiyo ilipambwa na vinara wengine wa upinzani akiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka aliyesisitiza umuhimu wa mashauriano miongoni mwa viongozi wa upinzani kabla ya kuamua mgombea wa urais. Kalonzo alisema katiba ya chama inahitaji NDC itakayofanyika Novemba 13 kabla ya Sifuna kutangazwa rasmi kuwa mgombea wa urais. Alisema lengo lake kuu ni kuhakikisha Rais Ruto anakuwa kiongozi wa muhula mmoja, akionya kuwa upinzani hautafikia azma hiyo bila kuwa na mgombea mmoja. "Kama ni mimi, basi Sifuna lazima aniunge mkono," alisema Kalonzo, akisisitiza kuwa viongozi wanahitaji kuketi pamoja na kukubaliana. Kwa upande wake, aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua aliwataka viongozi wa upinzani kumpa Sifuna nafasi ya kuongoza, akisema ana uwezo wa kufanya hivyo licha ya kuwa na umri wa miaka 44. Osotsi alisema jukumu lake kama mwenyekiti litakuwa kujenga mifumo ya chama kote nchini na kuhakikisha nidhamu inadumishwa. Alionya kuwa chama hicho kinaweza kukumbana na vurugu, lakini akasema atahakikisha wanachama wanafuata taratibu na kufanya kazi kwa umoja. Hafla hiyo inaashiria hatua mpya kwa mrengo wa Linda Mwananchi katika juhudi za kujijenga kama chama na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 30 Oct 2026 10:58:30

Mahakama yaamuru IG Kanja, DCI Amin kufikisha mwanaharakati Mwaipaya kortini

Mahakama Kuu imewaamuru Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin kumfikisha kortini mwanaharakati  raia wa Tanzania Twaha Mwaipaya, akiwa hai au maiti, Jaji Alexander Muteti alitoa agizo hilo Oktoba 30, kufuatia madai kwamba Mwaipaya alitekwa nyara eneo la Kamulu, Nairobi, Oktoba 25 na watu wasiojulikana. Jaji pia aliwaagiza Kanja na Amin, au wawakilishi wao, kufika mahakamani Novemba 2 kueleza sababu za kukamatwa na kuzuiliwa kwa Mwaipaya na kwa nini asiachiliwe mara moja. Shirika la Vocal Africa liliwasilisha kesi likitaka Mwaipaya afikishwe mahakamani likidai alipotea akiwa mikononi mwa polisi. Shirika hilo linasema liliripoti kutoweka kwake katika Kituo cha Polisi cha Ruai siku aliyopotea, lakini juhudi za kumtafuta katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Nairobi hazikufua dafu. Mahakama imeagiza polisi na DCI kuwasilisha majibu yao kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo Jumatatu. Kwa mujibu wa shirika hilo, Mwaipaya ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Tanzania mwenye wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii. Linaonya kuwa maisha yake yako hatarini iwapo atapelekwa kwa nguvu hadi Tanzania, ambako anaweza kuteswa au haki zake kukiukwa. Shirika hilo pia lilieleza kuwa waliomteka walitumia magari yaliyokuwa na nambari bandia na yasiyokuwa na nambari, huku baadhi ya waliokuwa ndani wakiwa wamejifunika nyuso na kubeba bunduki. Lilitaja visa vingine vya watu waliodaiwa kutekwa nchini Kenya, wakiwemo Macmillan Kiarie, Evans Otieno, Michael Oloo na Abdulaziz Duba, ambao hawajulikani waliko. Vocal Africa ilisema inatia wasiwasi kuwa visa hivyo sasa vinahusisha hata raia wa kigeni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 30 Oct 2026 08:55:40

Wakimbizi kutoka Ethiopia waliopenya Kenya wazidi 50,000 vita vikichacha

IDADI  ya raia wa Ethiopia wanaokimbilia Kenya kupitia Moyale kutokana na mapigano katika nchi hiyo jirani imezidi 50,000, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR). Idadi hiyo imeongezeka kutoka takriban 40,000 mwishoni mwa wiki huku mapigano kati ya vikosi na wanamgambo wa maeneo ya Oromia na Somali nchini Ethiopia yakiingia siku ya nane. UNHCR ilisema wanawake na watoto ndio wengi miongoni mwa waliotoroka makazi yao. Baadhi wamepata hifadhi kwa jamaa na wenyeji, huku wengine wakilala katika shule na makanisa. Shirika hilo lilitaja chakula kuwa hitaji la dharura, likiongeza kuwa wakimbizi wanahitaji maji safi, makazi ya muda, huduma za afya na usafi. Naibu Kamishna wa Kaunti ya Moyale, Benedict Munywoki, alisema idadi ya wanaovuka mpaka inaendelea kuongezeka kutokana na milio ya risasi inayosikika mara kwa mara. Alisema tathmini ilikuwa ikiendelea kubaini idadi kamili ya walioingia nchini, huku mashirika ya kutoa misaada yakishirikiana kuwahudumia. UNHCR inashirikiana na Idara ya Huduma za Wakimbizi nchini, serikali ya Kaunti ya Marsabit, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya na mashirika mengine kuandaa misaada ya dharura kwa karibu watu 12,000. Shirika hilo pia linasema juhudi zinaendelea kuhamisha kambi za wakimbizi kutoka maeneo yaliyo karibu na mpaka ili kuimarisha usalama wao. Kamishna wa Kaunti ya Marsabit, Stanley Kamande, alisema polisi na wanajeshi wa Kenya wameongeza doria mjini Moyale na maeneo ya mpakani kuhakikisha usalama. Wakati huohuo, watu saba wanachunguzwa kwa madai ya kusambaza matamshi ya chuki na kuchochea mizozo ya jamii kupitia mitandao ya kijamii. Bw Kamande aliwataka Wakenya kujiepusha na kauli zinazoweza kuongeza mvutano.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 30 Oct 2026 07:55:42

Kenya yapiga marufuku usafirishaji wa parachichi kwa meli

MAMLAKA ya Kilimo na Chakula (AFA) imepiga marufuku usafirishaji wa parachichi kwa meli kuanzia Ijumaa, Oktoba 30, baada ya kubaini kuwa uzalishaji wa matunda yaliyoiva vya kutosha kwa soko la nje hautoshi. Hatua hiyo inalenga kulinda ubora wa parachichi za Kenya katika masoko ya kimataifa, biashara iliyoingizia nchi takriban Sh20.8 bilioni mwaka 2025. Marufuku hiyo inahusu aina za Hass, Fuerte, Pinkerton na Jumbo. Hata hivyo, wasafirishaji wanaweza kuendelea kusafirisha parachichi kwa ndege baada ya kukaguliwa na kuidhinishwa na Idara ya Mazao ya Kilimo cha Bustani. AFA pia imetangaza kufungwa kwa msimu wa uvunaji wa parachichi kwa viwanda vinavyotengeneza mafuta kutoka matunda hayo. Viwanda vilivyo na akiba ya mafuta ya parachichi vinavyotaka kuyasafirisha nje vinapaswa kuomba ukaguzi kufikia Jumatatu, Novemba 2, 2026. Mamlaka hiyo imesema ni mafuta yatakayokaguliwa na kuthibitishwa mapema pekee yatakayoidhinishwa kusafirishwa nje. Uagizaji wa parachichi kutoka nchi nyingine kwa ajili ya kutengeneza mafuta pia umesitishwa ili kuzuia wafanyabiashara kutumia kisingizio hicho kuvuna matunda mabichi nchini. Kufungwa kwa msimu kunaweza kuwaathiri wakulima wadogo wanaotegemea kampuni za kuuza matunda nje. Baadhi wanaweza kulazimika kutafuta wanunuzi wa ndani, ambao huenda wakatoa bei za chini. Usafirishaji kwa ndege ni ghali zaidi kuliko kwa meli, jambo linaloweza kufanya kampuni kuwa makini zaidi katika kuchagua matunda na kiasi cha kununua kutoka kwa wakulima. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa Kenya iliuza parachichi za thamani ya dola milioni 160.1, sawa na Sh20.8 bilioni, mwaka 2025. Jumla ya tani 120,893 zilisafirishwa, hasa kwa masoko ya Uholanzi, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uhispania na Ufaransa. AFA imesema itaendelea kufuatilia ukomavu wa matunda na uzalishaji kabla ya kutoa mwongozo kuhusu msimu ujao. Aidha, shehena zote za maembe zitakaguliwa kabla ya kupewa vyeti vya kusafirishwa nje, huku vibali vikihakikisha kuwa mizigo hiyo ina maembe pekee.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 30 Oct 2026 06:55:00

Mataifa yaheshimu mipaka na mamlaka ya kila nchi – Ruto

RAIS William Ruto ametoa wito kwa mataifa yote kuheshimu mamlaka na mipaka ya nchi nyingine bila kujali ukubwa au nguvu zake, akisisitiza kuwa mizozo ya kimataifa inapaswa kutatuliwa kwa njia za amani. Akizungumza Alhamisi, Oktoba 29, katika Mkutano wa Tatu wa Urusi na Afrika mjini Moscow, Urusi, Dkt Ruto alisema uhusiano wa kimataifa unapaswa kujengwa kwa kuheshimiana badala ya mataifa yenye nguvu kutaka kutawala maeneo ya nchi nyingine. Alisema kanuni za usawa wa mataifa, kuheshimu mipaka na kutatua mizozo kwa amani zinapaswa kutumika kwa kila nchi bila ubaguzi. Rais pia alitaka mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisema Afrika yenye watu 1.6 bilioni na mataifa 54 haiwezi kuendelea kukosa uwakilishi wa kudumu katika chombo hicho muhimu. Alisema mfumo wa utawala wa dunia unapaswa kuakisi hali ya sasa badala ya kuendelea kutegemea mipango iliyowekwa mwaka 1945 baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Kenya inaunga mkono msimamo wa pamoja wa Afrika unaotaka bara hilo kupewa viti vya kudumu katika baraza hilo, pamoja na haki inayofurahiwa na wanachama wa sasa. Katika masuala ya uchumi, Dkt Ruto alisema Afrika inapaswa kuacha kutegemea kuuza malighafi na kununua bidhaa zilizokamilika,  na badala yake iwekeze katika viwanda, teknolojia na kuongeza thamani ya bidhaa. Alialika kampuni za Urusi kuwekeza katika viwanda vya Afrika, kuhamisha teknolojia na kutoa mafunzo ya kiufundi yatakayosaidia vijana kupata ajira. Alitaja kilimo, uzalishaji wa mbolea, unyunyuzaji, usindikaji wa mazao, nishati, afya na utengenezaji wa dawa kuwa maeneo muhimu ya ushirikiano. Rais Ruto pia alitaka mataifa tajiri kutoa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa masharti nafuu, akisema Afrika inaathiriwa na ukame, mafuriko na uhaba wa chakula licha ya kuchangia kidogo katika uzalishaji wa gesi chafu. Aidha, alitaka mageuzi katika mifumo ya ufadhili wa kimataifa ili nchi zinazoendelea zipate mikopo nafuu na fedha kwa miundomsingi na viwanda. Alisema mpango wa ushirikiano wa Urusi na Afrika wa 2027–2029 unapaswa kuzaa matokeo yanayopimika, yakiwemo uwekezaji, ajira, tafiti na viwanda vitakavyoboresha maisha ya wananchi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 30 Oct 2026 05:55:56

Bunge lakataa sajili ya wapigakura ikaguliwe kabla ya uchaguzi wa 2027

JUHUDI  za kuhakikisha sajili ya wapigakura inakaguliwa kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 zimepata pigo baada ya Bunge la Kitaifa kuondoa sharti la kisheria lililohitaji zoezi hilo lifanyike. Mnamo Oktoba 22, 2026, wabunge walikataa pendekezo la Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi la kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuajiri kampuni huru na yenye sifa kufanya ukaguzi wa sajili hiyo miezi sita kabla ya uchaguzi. Mbunge wa Homa Bay Town Peter Kaluma aliongoza upinzani dhidi ya pendekezo hilo, akisema lingepandisha gharama bila sababu. Alisema majukumu yaliyopendekezwa tayari yanatekelezwa na IEBC chini ya Kifungu cha 8 cha Sheria ya Uchaguzi. "Kwa nini IEBC iwe na jukumu la kusimamia sajili, kuikagua na kuirekebisha, kisha tutumie pesa za walipa ushuru kulipa kampuni nyingine?" aliuliza Bw Kaluma. Hata hivyo, Bw Omondi alisema ukaguzi huru ni muhimu kwa uwazi na uwajibikaji, hasa katika kuthibitisha idadi ya wapigakura waliofariki na kuhakikisha majina yao yanaondolewa kwenye sajili. Alisema IEBC husajili wapigakura, huku usajili wa vifo ukifanywa na taasisi nyingine huru. Kwa hivyo, kampuni isiyohusishwa na taasisi hizo mbili inapaswa kulinganisha rekodi na kuwaeleza Wakenya ni nani anayestahili kubaki kwenye sajili. "Katiba yetu inahitaji uwazi na inaweka mifumo mbalimbali ya uwajibikaji," alisema Bw Omondi. Pendekezo lake lilitaka kampuni itakayoteuliwa kuwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa IEBC ndani ya siku 30. Tume hiyo pia ingetakiwa kuchapisha ripoti hiyo kwenye tovuti yake na kuiwasilisha kwa Bunge la Kitaifa na Seneti ndani ya siku 14 baada ya kuipokea. Kukataa ukaguzi huo kunazua wasiwasi kutokana na matokeo ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya KPMG kabla ya uchaguzi wa 2022. Ripoti hiyo ilitambua wapigakura 246,465 waliofariki lakini majina yao bado yalikuwa kwenye sajili. Pia ilipata rekodi 481,711 zilizokuwa na nambari za vitambulisho au pasipoti zilizorudiwa au kukosekana kwa taarifa muhimu. Zaidi ya watu 226,000 walikuwa wamesajiliwa kwa kutumia vyeti ambavyo havikulingana na majina yaliyokuwa kwenye sajili. Ukaguzi huo pia ulifichua kuwa wafanyakazi 25 wa zamani wa IEBC walifikia sava za tume hiyo japo hawakuwa wameidhinishwa. Wasiwasi kuhusu wapigakura waliofariki uliongezeka baada ya IEBC kumhoji Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar Hassan kufuatia matamshi yake katika mkutano wa kisiasa Mombasa mnamo Septemba 11, 2026. Bw Omar alisema hata mtu akifa, kidole chake kinaweza kuchukuliwa na kutumika kwenye mfumo wa BVR kupiga kura. Baadaye alieleza tume hiyo kuwa matamshi hayo yalikuwa lugha ya kisiasa iliyolenga kuhamasisha wapigakura, wala hayakuwa na nia ya udanganyifu. Mbunge Aden Mohammed wa Wajir Mashariki, aliyekuwa akiongoza Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa 2024, pia alipinga pendekezo la Bw Omondi akisema lingeongeza majukumu ya IEBC. Bw Kaluma alitaja mapendekezo ya Tume ya Kriegler, iliyoshauri kuepukwa kwa marekebisho makubwa ya sheria za uchaguzi mwaka mmoja kabla ya uchaguzi. Hata hivyo, mswada huo ulifikishwa Bunge la Kitaifa Februari 2025, baada ya kupitishwa na Seneti Desemba 2024. Mswada huo sasa unarejea Seneti kwa kuangaliwa upya, hatua inayotoa nafasi ya sharti la ukaguzi kurejeshwa kupitia maafikiano kati ya mabunge hayo mawili.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 30 Oct 2026 04:55:01

Sifuna kuzindua makao makuu ya chama na kampeni ya urais

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anatarajiwa leo Ijumaa kuzindua makao makuu ya vuguvugu la Linda Mwananchi na kituo cha kuratibu kampeni zake za urais wa 2027. Ofisi hizo ziko Lavington, Nairobi, na ni sehemu ya juhudi za kuimarisha vuguvugu hilo baada ya kupata chama cha The Equitable Party (TEP), ambacho kinabadilishwa jina kuwa Linda Mwananchi Movement. Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alisema uzinduzi huo pia utahusisha kutangazwa kwa baadhi ya maafisa wa kitaifa wa chama hicho. Alisema orodha kamili itakamilishwa baadaye ili kutoa nafasi kwa wanachama wengine kujiunga. Vuguvugu hilo lilimteua Bw Sifuna kuwa kiongozi wake na mgombea wake wa urais mnamo Septemba. Miongoni mwa wanasiasa wanaotarajiwa kupewa majukumu muhimu ni Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na Gavana wa Siaya James Orengo, ambao walikuwa sehemu ya vuguvugu hilo, wameanzisha vyama vyao tofauti. Bw Owino amepata Muungano Party na kukibadilisha jina kuwa The Mwananchi Party, huku Bw Orengo akizindua Liberal Democratic Party (LDP). Bw Oundo alisema chama hicho kitapanga kongamano la kitaifa la wajumbe (NDC) Novemba 13 ili kukamilisha mabadiliko ya jina na kuthibitisha uongozi mpya. Pia, kinapanga kufungua ofisi katika kaunti zote 47 kufikia Desemba na kuanzisha mfumo wa mtandaoni utakaowawezesha wanaotaka kuwania viti mbalimbali kuwasilisha maombi yao. Baada ya uzinduzi wa Nairobi, vuguvugu hilo linapanga mkutano mkubwa wa kisiasa Kaunti ya Kwale Jumamosi. Hatua hizo zinafuatia kutofautiana kwa Bw Sifuna na chama cha ODM, ambacho alikuwa katibu mkuu wake. Utafiti wa TIFA uliochapishwa Julai ulionyesha kuwa asilimia 15 ya waliohojiwa walimuunga mkono Bw Sifuna iwapo angewania urais. Rais William Ruto alipata asilimia 24 katika utafiti huo. Wakati wa uzinduzi wa TEP, Bw Sifuna alisema vuguvugu hilo linalenga kuangazia matatizo ya wananchi wa kawaida, ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana, changamoto za wakulima, ushuru kwa wafanyabiashara wadogo na gharama ya elimu na matibabu. Alisema chama hicho kinataka vijana na wanawake washirikishwe zaidi katika maamuzi ya kisiasa na kuweka mbele uwajibikaji, huduma kwa wananchi na kuheshimu Katiba. Vuguvugu hilo pia linatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wengine wa upinzani kuhusu uwezekano wa kushirikiana kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 30 Oct 2026 03:55:29

Magavana 17 wapanga mikakati ya kuepuka baridi 2027

HUKU uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 ukikaribia, magavana 17 wanaokamilisha mihula yao miwili wanapanga hatua zao zinazofuata kisiasa, baadhi wakilenga viti vya useneta na wengine wakitaka nyadhifa za juu serikalini au kustaafu siasa za uchaguzi. Hata hivyo, mipango yao huenda ikatatizwa na mswada unaopendekeza magavana wanaoondoka mamlakani wasiruhusiwe kuwania viti vya Seneti au mabunge ya kaunti hadi miaka mitano ipite. Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa 2026, uliowasilishwa na Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango, unalenga kuzuia viongozi hao kuingia mara moja katika taasisi zinazochunguza matumizi ya fedha na utawala wao. Miongoni mwa magavana wanaowania viti vipya ni Ahmed Abdullahi wa Wajir, Muthomi Njuki wa Tharaka Nithi, Anne Waiguru wa Kirinyaga, Joseph ole Lenku wa Kajiado, Mutahi Kahiga wa Nyeri na Julius Malombe wa Kitui. Bw Abdullahi ametangaza azma yake ya kuwania useneta wa Wajir, huku Bw Njuki akitaka kuendea kiti cha Seneta Mwenda Gataya, ambaye anatarajiwa kuwania ubunge. Bi Waiguru, kwa upande wake, ametangaza nia ya kuwa Naibu Rais mwaka 2027. Alisema uzoefu wake kama mtumishi mkuu serikalini, waziri, gavana na mwenyekiti wa Baraza la Magavana unampa uwezo wa kuhudumu katika wadhifa huo. Bw Kahiga anataka kuingia Seneti akisema uzoefu wa kuongoza kaunti kwa miaka kumi utamsaidia kutetea ugatuzi na kupinga serikali ya kitaifa kuingilia majukumu ya kaunti. Gavana wa Kajiado, Bw Lenku anakabiliwa na changamoto baada ya kutofautiana na chama cha ODM kuhusu mipango ya kugawana nyadhifa na UDA. Amesema yuko tayari kuondoka ODM iwapo chama hicho kitaendelea kumtenga. Baadhi ya magavana pia wanapanga kuwaunga mkono washirika wao ili waendelee kuwa na ushawishi baada ya kuondoka mamlakani. Gavana wa Garissa, Gavana Nathif Jama anataka useneta na amemuunga mkono Seneta Abdulkadir Haji kumrithi kama gavana. Mwenzake wa Tana River, Dhadho Godhana anataka useneta na amependekeza Mbunge wa Galole Said Hiribae kumrithi huku Gavana Hillary Barchok  wa Bomet akimuunga mkono aliyekuwa gavana Isaac Ruto kurejea katika wadhifa huo huku akilenga useneta. Hata hivyo, si wote wanaotaka kuendelea na siasa za uchaguzi. Gavana wa Kisumu Anyang' Nyong'o na wa Vihiga Wilber Ottichilo wamesema hawatawania nyadhifa nyingine. Joshua Irungu wa Laikipia bado anashauriana kuhusu kuwania useneta au kushawishi siasa akiwa nje ya Bunge. Mswada wa Bw Murango unataka marekebisho ya Katiba na Sheria ya Uchaguzi ili magavana wanaohudumu au walioondoka mamlakani ndani ya miaka mitano kabla ya uchaguzi wazuiwe kuwania useneta na viti vya wawakilishi wa wadi katika mabunge  ya kaunti. Seneta huyo anasema kipindi hicho kitapatia taasisi muda wa kuchunguza maswali kuhusu uongozi na matumizi ya fedha za umma bila uwezekano wa migongano ya kimaslahi. Lakini Bw Kahiga amepinga pendekezo hilo, akisema linawadhalilisha magavana kwa kuwachukulia kana kwamba wote wameiba. Anasisitiza kuwa kuchaguliwa kuwa seneta hakumpi gavana kinga dhidi ya kujibu maswali kuhusu uongozi wake. Mswada huo unasubiri kusomwa mara ya pili katika Seneti, huku wanaoupinga wakisema unaweza kuwanyima magavana haki ya kushiriki uchaguzi na kuwania nyadhifa za umma.

read more