taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Gachagua ajenga huku akibomoa upinzani
KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP) Rigathi Gachagua anadai analenga kuunganisha viongozi wa upinzani chini ya mgombeaji mmoja wa urais katika uchaguzi wa 2027, lakini matamshi yake makali dhidi ya washirika wake yameibua wasiwasi. Bw Gachagua anaendelea kuwakosoa baadhi ya vinara wa upinzani akiwalaumu kwa kutofanya bidii kujenga umaarufu, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu atakayekabidhiwa urais bila kuungwa mkono na wapigakura. Katika mkutano wake na viongozi nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, Jumanne, kiongozi huyo wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP) alimshambulia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i miongoni mwa wanaomkosoa, akisema baadhi ya washirika wake hawataki kuzungumzia idadi ya kura wanazoweza kuweka mezani Gachagua alimpiga vijembe Muturi, ambaye anatoka eneo la Mbeere, akisema alishindwa hata kuvutia wapigakura katika kituo chake cha kupiga kura wakati wa uchaguzi mdogo wa MCA. "Unasema unataka kutusaidia kumuondoa Kasongo, lakini katika uchaguzi wa MCA kituoni kwako uliweza kupata watu 35 pekee, huku Kasongo akipata 238. Unataka kumfundisha Riggy G nini?" alisema. Aliongeza kuwa hatakubali kufanya kampeni na kuvutia kura ili kuzikabidhi kwa viongozi wengine bila wao kujituma. "Sitasaka kura nikuletee wewe na mke wako," alisema, akiwataka wenzake kutoka kwenye hoteli na kuanza kuwashawishi wananchi. Gachagua pia alifichua kuwa amekuwa akigawa idadi ya kura kwa washirika wake, akisema alimwambia Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alenge kura milioni tano, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka milioni tatu na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa milioni moja. Kauli hizo zimezua mjadala kuhusu nafasi ya viongozi wengine katika mazungumzo ya kuunda muungano wa upinzani, hasa baada ya Muturi kumshutumu Gachagua kwa kutumia vitisho badala ya kujenga ushirikiano wenye kuheshimiana. Matiang'i naye amekosoa pendekezo la Gachagua la kuunganisha maeneo ya Mlima Kenya, Ukambani na Magharibi, akisema siasa zinazotegemea idadi ya watu wa maeneo fulani zinaweza kuvunja umoja wa upinzani na kuua ndoto ya muungano dhidi ya Rais Ruto. Alionya kuhusu kile alichokitaja kama kiburi cha walio wengi kinachoweza kuwatenga viongozi wengine na kufanya mazungumzo ya kupata mgombeaji mmoja kuwa magumu. Hata hivyo, Gachagua amesisitiza kuwa hana kiburi, bali anasema ukweli kuhusu siasa za uchaguzi. "Ninapowaambia tuamke tufanye kazi, wanasema ninawanyanyasa. Mimi si mwenye kiburi, nasema ukweli," alisema. Katika jitihada za kuimarisha muungano huo, jana Gachagua alikutana na aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu nyumbani kwake Wamunyoro. Ngilu alihusika katika kuunda muungano wa NARC uliomuingiza madarakani marehemu Mwai Kibaki mwaka 2002 na kumaliza utawala wa KANU. Gachagua alisema alijifunza kutoka kwa Ngilu kuhusu mikakati iliyotumiwa kuunganisha vyama vya upinzani na kuhakikisha vinaunga mkono mgombeaji mmoja. Haya yanajiri baada ya Gachagua kukutana na Kalonzo na Sifuna katika mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kisiasa. Ameashiria kuwa muungano unaojengwa unaweza kujumuisha viongozi hao pamoja na Eugene Wamalwa. Hata hivyo, hii inaweza kuchukuliwa kwa ishara ya kutokuwa na nia njema na vinara wengine akiwemo Martha Karua, Ndindi Nyoro na Muturi ambao wamekuwa wakihubiri haja ya upinzani kuunga ili kuwa rahisi kumshinda Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao. Kulingana na mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, kauli za Gachagua ni hatari kwa upinzani chini ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Anashangaa kwa nini naibu rais huyo wa zamani anatoa kauli tofauti na msimamo wake wa awali kwamba upinzani unaweza kushinda tu iwapo utaungana na kuteua mmoja wao kuwa mgombea urais wa pamoja. "Kwa maoni yangu, Gachagua anajenga akibomoa. Ukifuatilia kabla ya Sifuna kupata umaarufu, hakuwa akimchangamkia. Sasa kwa vile amevuna, anamleta karibu huku akiwabeza baadhi ya vinara aliokuwa akitangamana nao awali," asema Dkt Gichuki na kuongeza hii ni hatari. "Kwa sasa, upinzani unapaswa kuwa ukihubiri umoja na kutoka mwelekeo kwa wafuasi wao lakini inaonekana Gachagua hayuko tayari kwa hili. Kwa lugha ya mtaa, anachafua bahari wakati ambao yeye na wenzake wanafaa kuwa wakijiandaa kuvua," akasema. Gachagua anasisitiza kuwa tofauti za ndani hazitazuia upinzani kusimamisha mgombeaji mmoja dhidi ya Rais William Ruto mwaka 2027.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 44 minutes ago
Washirika wa Sifuna kuvuliwa nyadhifa muhimu
VIONGOZI wawili wa Bunge la Kaunti ya Nairobi wanaohusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi Movement (LMM) linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna huenda wakapokonywa nyadhifa zao muhimu katika bunge hilo. Vyanzo vya kuaminika katika City Hall vinasema hatua hiyo inalenga kuwaadhibu madiwani hao kwa kuendelea kumuunga mkono Bw Sifuna licha ya kuchaguliwa na kuteuliwa kupitia chama cha ODM katika uchaguzi mkuu wa 2022. Wanaolengwa ni Kiranja wa Wengi Moses Ogeto na Perpetua Mponjiwa Okello, ambaye aliteuliwa kuwa MCA kupitia ODM. Bw Ogeto anahudumu muhula wake wa tatu kama mwakilishi wa wadi ya Kilimani, eneo bunge la Dagoretti North. Amekuwa akiwakilisha wadi hiyo tangu 2013 na alikuwa mshirika wa karibu wa mwanzilishi wa ODM, marehemu Raila Odinga. Kwa upande wake, Bi Mponjiwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Elimu katika Bunge la Kaunti ya Nairobi. Pia ametangaza nia ya kuwania kiti cha mwakilishi wadi ya Kileleshwa kinachoshikiliwa na MCA wa ODM Robert Alai. "Ni kweli. Hoja imeandaliwa na inaweza kuwasilishwa wakati wowote. Inawalenga viongozi wawili ambao wamekuwa wakiunga mkono chama hasimu huku wakiendelea kunufaika na nafasi walizopewa kupitia ODM," kilisema chanzo kimoja kilichoomba kutotajwa. Akizungumza na Taifa, Bw Ogeto alisema alikuwa amearifiwa kuhusu mpango wa kumuondoa katika wadhifa wake. Hata hivyo, alidai ODM imepoteza misingi iliyowekwa na Raila Odinga, akisema chama hicho sasa kinatanguliza maslahi ya wanasiasa badala ya wananchi. "Watu hawa hawafanyi tena yale Baba alikuwa akifanya, ndio maana tumetengana. Baba alikuwa wa wananchi, lakini wao wanajali pesa. Baba alikuwa akinipa maagizo kuhusu jinsi ya kuwatetea wananchi, lakini leo hakuna anayetaka kuwatetea," alisema. Bw Ogeto alisema kuondolewa kwake hakutakuwa na athari kubwa kwake kwa sababu bunge linakaribia kuingia likizoni hadi Februari kabla ya mapumziko mengine yasiyo na tarehe maalum ya kurejea. Alifichua kuwa anamezea mate kiti cha ubunge cha Dagoretti North kinachoshikiliwa na Beatrice Elachi wa ODM. Alisema hana hofu ya kupoteza wadhifa huo kwa sababu amejijengea uhusiano mzuri na wakazi wa eneo hilo. Iwapo ataondolewa, nafasi yake kama Kiranja wa Wengi inatarajiwa kuchukuliwa na naibu wake Stazo Omung'ala Elija Ang'ila, MCA wa wadi ya Upper Savannah. Jitihada za kumpata Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Peter Imwatok, ili kutoa maoni yake hazikufanikiwa kwani hakujibu simu wala ujumbe.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
Viongozi wa Wiper watishia kujitenga na upinzani kuhusu tiketi ya urais
VIONGOZI wa chama cha Wiper katika eneo la Pwani wametishia kujiondoa katika muungano wa upinzani na kumuunga mkono kiongozi wao Kalonzo Musyoka kuwania urais kivyake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 iwapo hatapewa tiketi ya pamoja ya urais. Viongozi hao wa mashinani wamesisitiza kuwa wakati umefika kwa Bw Musyoka kupewa nafasi ya kuwania urais badala ya kuendelea kuunga mkono wagombeaji wengine au kukubali kuwa mgombea mwenza. Pia walipuuza madai kwamba aliyekuwa makamu wa rais anaweza kushirikiana kisiasa na Rais William Ruto katika uchaguzi ujao, wakisema wawili hao hawana uwezekano wa kuunda muungano. Mwanachama wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya Wiper, Omar Twaha, alidai kuwa Kalonzo amekuwa akidhulumiwa ndani ya upinzani licha ya mchango wake katika juhudi za kuunganisha viongozi wanaopinga utawala wa Rais Ruto. Hata hivyo, Bw Twaha alisema chama hicho hakina nia ya kuvunja muungano wa upinzani, bali kinataka viongozi waheshimiane na kumpa kila mmoja nafasi sawa katika mazungumzo kuhusu mgombeaji wa urais. "Iwapo tutamsimamisha Kalonzo kama chama, tutavunja upinzani, na hilo si lengo letu. Lengo letu ni moja, kumuondoa Rais William Ruto mamlakani. Kwa hivyo, ni lazima tuheshimiane," alisema. Mwenyekiti wa Wiper Pwani, John Chamia, alipuuza madai kwamba Kalonzo anaweza kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto, akisisitiza kuwa wawili hao hawawezi kushirikiana kisiasa. "Anayesema Kalonzo atakuwa naibu wa Ruto anaota. Hatuwezi hata kufanya mazungumzo naye kwa sababu Ruto na Kalonzo hawawezi kuwa pamoja," alisema Bw Chamia. Viongozi hao walisema iwapo Kalonzo atapuuzwa katika mchakato wa kumchagua mgombeaji wa urais wa upinzani, watamlazimisha kuwania kiti hicho nje ya muungano. Walisema Kalonzo alikuwa akimuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga katika chaguzi zilizopita na sasa ni wakati wa viongozi wengine wa upinzani kulipa fadhila hiyo. "Kalonzo hakuzaliwa kuwa mgombea mwenza katika kila uchaguzi. Alimuunga mkono Raila Odinga na sasa ni wakati wa wao kumuunga mkono. Tunamwambia Kalonzo kwamba hatutaki kusikia akiunga mkono mtu mwingine. Tunataka kumuona kwenye karatasi ya kura," alisema mmoja wa viongozi hao. Msimamo huo unajiri huku kukiwa na ushindani mkali ndani ya upinzani kuhusu nani atabeba bendera ya urais katika uchaguzi wa 2027. Miongoni mwa wanaotajwa ni Kalonzo, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i, ambaye pia anaongoza chama cha Jubilee. Naibu kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Cleophas Malala, amekuwa akimhimiza Kalonzo kuachana na azma yake ya urais na kumuunga mkono Sifuna. Bw Malala anasema Sifuna, mwenye umri wa miaka 45, anawakilisha kizazi kipya cha uongozi na anafaa kupewa nafasi ya kuongoza nchi, huku mwanasiasa mkongwe akichaguliwa kuwa mgombea mwenza. "Ninataka Kalonzo kuiga mfumo wa Obama na Biden. Tumuunge mkono Sifuna, mwenye umri wa miaka 45, kuwa mgombeaji wa urais wa upinzani, kisha tutafute mwanasiasa mkongwe awe mgombea mwenza wake," alisema. Hata hivyo, viongozi wa Wiper Pwani walisema Kalonzo ana uzoefu wa kutosha kuongoza nchi na hawatakubali azma yake ya urais kupuuzwa kwa kisingizio cha kudumisha umoja. Pia walidai kuwa baadhi ya watu wanaohusishwa na serikali wanatumia tofauti ndani ya upinzani kujaribu kuudhoofisha kabla ya uchaguzi wa 2027. Walisema umoja wa upinzani ni muhimu, lakini haupaswi kujengwa kwa kumdharau au kumtenga kiongozi yeyote anayetamani kuwania urais.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 2 hours ago
Wataka Mackenzie wa Shakahola anyongwe!
MHUBIRI aliyepatikana na hatia ya mauaji Shakahola, Paul Nthenge Mackenzie, ameiomba Mahakama imhurumie anaposubiri kuhukumiwa Ijumaa. Hayo yamejiri huku upande wa mashtaka ukitaka apewe hukumu ya kifo, na washtakiwa wenzake wafungwe maisha gerezani. Mahakama Kuu ilimpata na hatia ya mauaji ya watoto 190 na mtu mzima mmoja katika Msitu wa Shakahola, kati ya Januari 2021 na Septemba 2023. Mackenzie sasa amemweleza Jaji Diana Kavedza kuwa yeye na washitakiwa wenzake 28 pia ni waathiriwa wa mkasa huo, ambapo jumla ya watu 429 walifariki dunia wakiamini kuwa walikuwa wakijiandaa kwenda kumwona Yesu. "Kwa namna fulani, tulipoteza mali na watoto wetu. Jambo ambalo tunalijutia, na tunaomba mahakama hii ituhurumie na kulizingatia kabla ya kutupatia adhabu kali," alisema kupitia kwa wakili wake. Washtakiwa hao waliiomba mahakama izingatie hali zao binafsi na mabadiliko ambayo wanasema wamepitia wakiwa kizuizini. Walieleza kuwa vifo hivyo vilikuwa janga kubwa lisilopimika na kusisitiza kuwa hawakuwa na nia ya kupuuza maumivu ya familia zilizowapoteza wapendwa wao. Washtakiwa hao walisema majuto yao yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia mwenendo wao, kutambua makosa yaliyotendeka na utayari wao wa kubadilika. Walisisitiza kuwa adhabu inapaswa kuzingatia uzito wa makosa pamoja na wajibu wa kila mshukiwa na nafasi yake ya kurekebisha mwenendo wake. "Adhabu inayotoa nafasi ya mtu kujirekebisha si ishara ya udhaifu," walisema. Washitakiwa walisema wamekuwa kizuizini tangu 2023, ambapo wameshiriki katika mipango ya kidini na mafunzo mengine. Waliiomba mahakama izingatie pia ushiriki wao katika mipango ya kuwaondoa watu katika misimamo mikali ya kidini iliyofanyika kati ya Agosti 20 na 23, 2025, wakisema hatua hiyo inaonyesha utayari wao wa kubadilika na kurejea katika jamii. Pia, walieleza kuwa mitazamo yao ya kidini imebadilika tangu walipokamatwa, na kuiomba mahakama izingatie mabadiliko hayo pamoja na ripoti za tathmini kabla ya hukumu kutolewa. Waliomba mahakama izingatie huruma, haki na uwiano wa adhabu, huku ikitoa nafasi kwa haki inayolenga kurekebisha madhara yaliyotokea. "Tunapendekeza kifungo kisichozidi miaka 10, huku muda ambao washtakiwa wamekwishatumia kizuizini ukizingatiwa," alisema wakili wao. Hata hivyo, upande wa mashtaka uliomba washtakiwa wote wahukumiwe vifungo vya gerezani na washirikishwe katika mpango maalumu wa kurekebisha mwenendo wao, ukisema hawajaonyesha majuto. Kulingana na upande wa mashtaka, washtakiwa wote isipokuwa Enos Amanya Ngala wameendelea kukana mashtaka. Bw Ngala alikiri kushiriki katika mauaji hayo. "Wameendelea kukana mashtaka, kukataa kuwajibika kwa uhalifu huo na kuyatafsiri mashtaka dhidi yao kwa namna hasi. Kwa hakika, washtakiwa hawakuonyesha majuto wala kujutia matendo yao. Pia inashangaza kwamba bado wanashikilia mafundisho yaliyochangia vifo hivyo," upande wa mashtaka ulisema. Serikali ilipendekeza adhabu zitakazoakisi uzito na ukubwa wa makosa hayo. Kwa Bw Ngala, ilipendekeza kifungo cha miaka 11, muda aliokuwa ametumikia kizuizini tangu Aprili 2023 ukizingatiwa. Pia ilipendekeza afanyiwe mpango wa marekebisho ya tabia akiwa gerezani kwa kipindi cha kati ya miezi 24 na 30, huku ripoti za anavyoendelea zikiwasilishwa mara kwa mara ili kusaidia tathmini ya baadaye ya adhabu yake. Kwa Mackenzie, upande wa mashtaka uliomba mahakama itoe adhabu ya kifo, huku washtakiwa wengine 27 wakihukumiwa kifungo cha maisha gerezani. "Upande wa mashtaka unaunga mkono kutolewa kwa adhabu ya kifo kwa Mackenzie, kwa kuzingatia pia maelezo yake ya kujitetea , majuto yake na uwezekano wa kurekebisha mwenendo wake," alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma, Bw Jami Yamina. Upande wa mashtaka ulisema adhabu inapaswa kuzingatia malengo ya haki ya jinai, yakiwemo kuadhibu, kuzuia uhalifu wa aina hiyo, kulinda umma, kukemea uhalifu, kurekebisha madhara na kuwasaidia wahusika kubadilika. Pia ulipendekeza waathiriwa wagawanywe katika makundi matatu ya umri: watoto wenye umri wa hadi miaka saba, wale wa miaka minane hadi 14, na walio na umri wa miaka 15 hadi 18. Aidha, uliwasilisha pendekezo la Kituo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Ugaidi (NCTC), kilichopendekeza washitakiwa washiriki kwa hiari katika programu za marekebisho ya misimamo mikali na kupewa mafundisho mbadala ili kuwawezesha kurejea katika jamii. Mwezi uliopita, Mahakama Kuu ilimpata Makenzie na wenzake 28 na hatia ya kuwaua watoto 190 na mtu mzima mmoja katika msitu wa Shakahola. Watu hao watapewa kifungo chao Novemba 6.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
Visa vya wahalifu kushambulia polisi, wanajeshi zazua hofu
MATUKIO mawili tofauti ya mapigano kati ya maafisa wa usalama na washukiwa wa uhalifu yamezua wasiwasi kuhusu usalama wa polisi na wanajeshi, huku bunduki zikiendelea kuibwa na magenge ya wahalifu. Katika tukio la kwanza, afisa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) alipigwa risasi na kuuawa na polisi katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, baada ya makabiliano yaliyotokea Jumapili, Novemba 1. Ripoti ya polisi inaonyesha kuwa maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Kahawa Sukari walikuwa kwenye doria mwendo wa saa saba usiku walipopokea taarifa kutoka kwa mwananchi kuhusu wanaume wawili waliokuwa na silaha na kutishia wakazi wa Covo, karibu na Magunas. Polisi waliwafuata washukiwa hao na kuwaamuru wasimame, lakini mmoja wao anadaiwa kutoa bastola na kuwafyatulia risasi maafisa hao, waliolazimika kujibu mashambulizi. "Mshukiwa aliyetoa bunduki alipigwa risasi kifuani na mkono wa kulia. Alikimbizwa katika Hospitali ya Ruiru Level 4 akiwa katika hali mahututi lakini baadaye akafariki akipokea matibabu," ilisema ripoti hiyo. Polisi walipata bastola aina ya Jericho iliyokuwa na risasi 12 pamoja na maganda mawili ya risasi zilizokuwa zimefyatuliwa. Pia walipata kitambulisho cha KDF kilichokuwa na jina la marehemu, Munene Antony, 33. Mshukiwa aliyenusurika anadaiwa kuwaambia wachunguzi kuwa bastola hiyo ilikuwa ya kakake ambaye ni polisi. Uchunguzi unaendelea kubaini umiliki wa silaha hiyo. Wakati huohuo, maafisa wawili wa polisi kutoka Kituo cha Ruai walijeruhiwa vibaya Jumatatu usiku baada ya kushambuliwa na genge la wanaume waliokuwa wameabiri pikipiki. Washambuliaji hao waliiba bunduki mbili aina ya AK-47, kila moja ikiwa na risasi 30. Maafisa hao, Corporal John Maritim na Corporal Felistus Tuitoek, walipata majeraha kichwani na mikononi baada ya kushambuliwa kwa kitu chenye makali. Walipata matibabu katika Hospitali ya Reale, Utawala, huku polisi wakianzisha msako wa kuwakamata washukiwa na kurejesha silaha hizo. Tukio hilo linaongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa bunduki hizo kutumiwa katika uhalifu mwingine au mashambulizi dhidi ya raia na maafisa wa usalama. Mnamo Oktoba 26, genge lilishambulia maafisa waliokuwa wakilinda kituo cha ukusanyaji ushuru Kaunti ya Mombasa, Likoni, na kumuua afisa mmoja wa kaunti huku wengine watatu wakijeruhiwa. Washambuliaji waliiba bunduki ya AK-47 kutoka kwa afisa wa utawala, ambayo baadaye ilitumika kumpiga risasi afisa huyo wa kaunti. Mnamo Machi, genge jingine lilishambulia polisi aliyekuwa akilinda eneo la viwanda la Bonje, Jomvu, na kumuibia bunduki ya AK-47 pamoja na simu. Matukio hayo yanajiri huku kukiwa na ripoti za mivutano kati ya polisi na wanajeshi. mnamo Septemba, maafisa hao walikabiliana katika kizuizi cha barabarani karibu na Chuo Kikuu cha Turkana, Lodwar, na baadaye katika Kituo cha Polisi cha Lodwar. Tukio jingine la mzozo kati ya polisi na wanajeshi liliripotiwa katika kivuko cha feri cha Likoni, Mombasa, mwezi huohuo. Matukio haya yanaibua maswali kuhusu ushirikiano kati ya idara za usalama, nidhamu kazini na silaha za serikali kuangukia mikononi mwa wahalifu.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
Wanawake Kenya sasa wanataka watoto wawili -utafiti
IDADI ya watoto ambao mwanamke huzaa nchini Kenya inatofautiana pakubwa kulingana na anapoishi, kiwango chake cha elimu na hali yake ya kiuchumi, huku wanawake wengi wakisema wangependa kupata watoto wawili pekee. Ripoti mpya ya Utafiti wa Afya kuhusu Idadi ya Watu Kenya (KDHS) ya mwaka 2025–2026 inaonyesha kuwa mwanamke wa kaunti ya Embu huzaa wastani wa watoto 2.2 katika maisha yake, ikilinganishwa na watoto 6.8 kwa mwanamke wa Mandera. Tofauti hiyo inaonyesha pengo kubwa la uzazi nchini, licha ya Kenya kupiga hatua katika kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na kila mwanamke. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha uzazi nchini kimeshuka hadi watoto 3.1 kwa kila mwanamke, kutoka 3.4 mwaka 2022 na 6.7 mwaka 1988–89. Hata hivyo, idadi ya watoto imeanza kupungua, huku matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi na mahitaji ambayo hayajatimizwa yakiongezeka. Wanawake wengi walisema wangependa kupata watoto wawili, lakini wastani wa kitaifa bado ni 3.1. Hali ni tofauti katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya, ambako wanawake wanapata watoto wengi zaidi na matumizi ya njia za kisasa za kisasa za kupanga uzazi ni madogo mno. Mandera inaongoza kwa kiwango cha juu kwa watoto 6.8 kwa kila mwanamke, ikifuatiwa na Wajir (5.8), Tana River (5.7), Turkana (5.6), Garissa (5.3), West Pokot (5.1) na Samburu (5.0). Kwa upande mwingine, Embu ina kiwango cha chini zaidi cha watoto 2.2, ikifuatiwa na Kiambu na Mombasa zenye 2.3 kila moja. Kericho na Nairobi zina kiwango cha 2.6. Elimu pia inaonekana kuwa na mchango mkubwa katika idadi ya watoto ambao mwanamke huzaa. Wanawake ambao hawajasoma wanapata wastani wa watoto 5.4, ikilinganishwa na 3.6 kwa walio na elimu ya msingi, 3.0 kwa wenye elimu ya sekondari na 2.7 kwa walioendelea na masomo baada ya sekondari. Hali hiyo pia inajitokeza katika hali ya kiuchumi. Wanawake kutoka familia maskini zaidi wana wastani wa watoto 4.5, huku wale kutoka familia tajiri zaidi wakiwa na 2.3. Ripoti inaonyesha pia kuwa wanawake wameanza kupata watoto wakiwa na umri mkubwa zaidi. Hapo awali, wanawake wengi walikuwa wakijifungua zaidi wakiwa na umri wa miaka 20 hadi 24, lakini sasa kundi linaloongoza ni la miaka 25 hadi 29. Vilevile, mimba miongoni mwa wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 zimepungua. Asilimia ya wasichana katika kundi hilo ambao wamewahi kupata mimba imeshuka kutoka 14.8 mwaka 2022 hadi 11.9 sasa. Serikali inalenga kuongeza matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi hadi asilimia 64 ifikapo 2030 na kupunguza mahitaji ambayo hayajatimizwa hadi asilimia 10. Mandera ina kiwango cha chini zaidi cha matumizi, chini ya asilimia moja, huku Wajir ikiwa na asilimia moja na Garissa asilimia tano. Katika kaunti za Nyamira, Nandi na Bomet, wanawake wanapata watoto 1.1 zaidi ya idadi wanayotamani. Hali hiyo inaonyesha kuwa kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa kutahitaji kuboresha upatikanaji wa huduma za kupanga uzazi na elimu kuhusu afya ya uzazi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Mibabe saba kupimana nguvu kuwania ugavana Nairobi
KUTOKA kwa rubani, wafanyabiashara, wabunge hadi viongozi wa kidini, uchaguzi wa ugavana Nairobi mwaka wa 2027 unatarajiwa kuwa na ushindani mkali huku wanasiasa sita wakimezea mate usukani wa kaunti hiyo yenye ushawishi mkubwa kisiasa na kiuchumi. Gavana wa sasa Johnson Sakaja, Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri na Mbunge wa Makadara George Aladwa wanawania tiketi ya chama cha ODM, huku Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya na aliyekuwa Mbunge wa Starehe Margaret Wanjiru wakitafuta tiketi za vyama tofauti. Aliyekuwa Katibu katika Wizara Irungu Nyakera na mfanyabiashara Agnes Kagure, ambao awali walikuwa wameonyesha nia ya kuwania kiti hicho, wameonekana kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho. Mashindano hayo yalipamba moto Jumatatu baada ya Bw Sakaja kuhama chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na kujiunga rasmi na ODM, akitangaza azma ya kuwania muhula wa pili kupitia chama hicho. Hatua hiyo imezua maswali kuhusu hatma ya wagombeaji wengine wa ODM ambao tayari walikuwa wameonyesha nia ya kuwania ugavana. Bw Sakaja alipokelewa katika makao makuu ya ODM, Chungwa House, na viongozi wa chama hicho. Alisema kujiunga kwake hakukuwa mbinu ya kisiasa bali kurejea katika chama alichokuwa akihusishwa nacho. "Baba (Raila Odinga) ndiye aliyeniambia nijiunge na ODM," alisema, akirejelea uhusiano wake na mwanzilishi wa chama hicho aliyefariki. Alisema anataka muhula mwingine ili kuendeleza huduma kwa wananchi, akisisitiza kuwa uongozi unapaswa kupimwa kwa jinsi maisha yanavyobadilika badala ya ushindi wa uchaguzi pekee. Hata hivyo, Mwenyekiti wa ODM Nairobi George Aladwa amesema hatakubali wageni kupewa tiketi bila kupitia mchujo wa kidemokrasia. "Safari ya kuongoza Nairobi lazima iongozwe na matakwa ya wananchi, haki na misingi ya demokrasia. Nimejizatiti katika maono yetu ya pamoja. Sauti ya wananchi lazima isikike," alisema. Bw Karauri, rubani wa zamani wa Kenya Airways na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa SportPesa, anasema uzoefu wake katika biashara, usafiri wa anga na siasa za eneo bunge unampa uwezo wa kusimamia Nairobi. Alisema alifanya kazi Kenya Airways kwa miaka 11, mitano akiwa nahodha wa ndege, na amejifunza umuhimu wa uwajibikaji na mipango. Ameahidi kuboresha ukusanyaji wa mapato, usafi wa jiji, mabomba ya maji na barabara bila kuongeza ushuru. Pia anataka kukagua majengo ili kubaini yale yasiyo salama na kuhakikisha hospitali za kaunti zina dawa za kutosha. Bw Karauri amemkosoa Sakaja, akisema kuhamia ODM hakutafuta kumbukumbu ya changamoto za uongozi wake, zikiwemo mafuriko, taka na majengo kuporomoka. Kwa upande wake, Bw Gakuya anatumia uungwaji mkono wa kiongozi wa DCP na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuimarisha kampeni zake. Ameahidi kubadilisha jaa la Dandora, kuunda nafasi za ajira na kurejesha hadhi ya Nairobi. Bw Owino amechagua kuwania kupitia Mwananchi Party huku akiendelea kushirikiana na vuguvugu la Linda Mwananchi linalomuunga mkono Seneta Edwin Sifuna kuwania urais. Sifuna tayari amemtaja Owino kama mgombeaji anayempendelea katika ugavana wa Nairobi. Naye Bi Wanjiru, ambaye amepata chama cha Kenya Moja Movement, amesema hatasalimisha azma yake ya ugavana katika mazungumzo ya miungano. Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema ODM inakabiliwa na changamoto ya kuamua kati ya kumpa kipaumbele gavana aliye madarakani, uaminifu wa wanachama wa muda mrefu au mgombeaji anayeweza kushinda. Anasema Sakaja atapimwa kutokana na rekodi ya muhula wake wa kwanza, Aladwa atalazimika kuthibitisha umaarufu wake nje ya chama, huku Karauri akionyesha kuwa uzoefu wa biashara unaweza kutumika kusimamia kaunti. Owino naye atalazimika kuthibitisha kuwa umaarufu wake unaenea nje ya Embakasi Mashariki, huku Gakuya akihitaji kupanua uungwaji mkono wa Gachagua na Wanjiru kujenga mtandao imara katika jiji lote.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 20 hours ago
Aliyekuwa mwanasheria mkuu Paul Kihara Kariuki aaga dunia
ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa Serikali Paul Kihara Kariuki amefariki dunia, akiacha nyuma historia ya zaidi ya miaka 40 katika taaluma ya sheria na utumishi wa umma. Bw Kariuki, ambaye alihudumu kama Mwanasheria Mkuu kati ya 2018 na 2022 chini ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, pia aliwahi kuwa Rais wa Mahakama ya Rufaa kwa miaka mitano. Jaji Mkuu Martha Koome alithibitisha kifo chake Jumanne na kumtaja kama mwanasheria mahiri, kiongozi wa mahakama na mtumishi wa umma aliyechangia pakubwa katika kuimarisha taasisi za sheria nchini. Rais William Ruto alisema mchango wake haukuishia mahakamani, bali pia ulijumuisha kuanzisha Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama (Judiciary Training Institute), iliyosaidia kuwapa majaji na maafisa wengine wa mahakama mafunzo ya kitaalamu. Bw Kenyatta pia alimwomboleza, akisema uongozi wake katika Mahakama ya Rufaa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu uliacha alama muhimu katika taasisi za serikali. Hata hivyo, kipindi chake kama Mwanasheria Mkuu kilikumbwa na mvutano mkubwa kati ya serikali na mahakama kuhusu uteuzi wa majaji 41 waliopendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC). Uhuru alikataa kuwateua wote, akidai alikuwa amepokea taarifa za kijasusi kuhusu masuala ya uadilifu ya baadhi yao. Mzozo huo ulisababisha Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kutishia kumuondoa katika orodha ya mawakili kwa madai ya utovu wa nidhamu wa kitaaluma. Hata hivyo, Kariuki alipata amri ya mahakama iliyozuia hatua hiyo kwa muda. Pia alitetea serikali kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI), ambao hatimaye uliharamishwa na Mahakama ya Juu. Kariuki alizaliwa Kiambu mwaka 1954 na kuhitimu shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka 1977. Aliwahi kuwa jaji wa Mahakama Kuu kuanzia 2003, kabla ya kuwa mkurugenzi wa kwanza wa Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama mwaka 2009. Mwaka 2013 alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Mahakama ya Rufaa chini ya Katiba ya 2010. Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga alimuomboleza kama mwanasheria aliyejitolea katika utumishi wa umma na kuimarisha utawala wa sheria.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 20 hours ago
Majonzi mtahiniwa wa KCSE akifariki ghafla baada ya karatasi mbili
FAMILIA moja katika kijiji cha Kanyaliech, eneo la Koyugi, Kaunti ya Homa Bay, imezama kwenye majonzi baada ya mwanafunzi wa Kidato cha Nne kufariki saa chache tu baada ya kufanya karatasi mbili za kwanza cha mtihani wa KCSE. Congestina Achieng, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Alaro Central, aliaga dunia Jumatatu jioni baada ya kuugua ghafla akilalamikia maumivu makali ya kifua. Kifo chake kiliwashtua wazazi, walimu na wakazi wa eneo hilo, kwani alikuwa ameanza safari ya mtihani wa kitaifa akiwa na matumaini ya kutimiza ndoto zake. Babake, David Ogweno, alisema alipokea simu ya dharura kutoka kwa mkuu wa shule akimtaka afike kumchukua mwanawe baada ya kumaliza karatasi mbili za kwanza. "Afya yake ilizorota haraka. Tulimkimbiza katika Hospitali ya Tamary, lakini kwa bahati mbaya aliaga dunia," alisema Bw Ogweno. Alisema familia imepitia changamoto za kifedha kumwezesha Congestina na watoto wengine kupata elimu. Bw Ogweno, ambaye hufanya kazi za vibarua, alisema mwanawe alikuwa na ndoto ya kuwa wakili ili kusaidia familia kujikwamua kutoka katika umaskini. Mama yake, Pamela Atieno, alisema mwanawe alikuwa akiumwa tangu wiki jana, lakini alitarajia kupata nafuu na kufanya mtihani wa KCSE. "Alilalamikia maumivu ya kifua, nikamnunulia dawa za dukani ili kupunguza maumivu na aweze kufanya mtihani. Baadaye nilipigiwa simu na kuambiwa hangeweza kuendelea," alisema. Walimu wake, Isaiah Opere na Austine Achina, walimtaja kama mwanafunzi mwenye nidhamu, mnyenyekevu na aliyejituma katika masomo. Bw Opere alisema Congestina alikuwa mtulivu na mwenye tabia nzuri, ambaye hakuwahi kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu. Kifo chake kimezima ndoto za msichana aliyetarajia kutumia elimu kujenga maisha bora, na kuacha familia yake ikiwa na majonzi makubwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 03 Nov 2026 08:55:53
Gavana akana dai hofu ya uchawi ilimfukuza ofisini
GAVANA wa Tana River, Bw Dhadho Godhana, ameeleza sababu zinazomfanya kutotumia mara kwa mara ofisi yake rasmi mjini Hola, na badala yake kufanyia kazi katika maeneo mengine, yakiwemo afisi za mahusiano ya nje ya kaunti yake zilizo mjini Mombasa na Nairobi. Bw Godhana alipuuzilia mbali madai kwamba hofu ya uchawi ndiyo iliyomlazimu kuachana na ofisi yake ya Hola, akifafanua kuwa kufanya kazi kutoka maeneo mengine ni mkakati wa kudhibiti umati wa watu na kuhakikisha usalama. Alisema amekuwa akipunguza kwa makusudi ziara zake katika jengo kuu la utawala wa kaunti kutokana na uhaba mkubwa wa nafasi na uwezekano wa wananchi kusababisha vurugu. Akizungumzia uvumi ulioibuka kufuatia tukio la mwaka wa 2019 ambapo paka aliyechinjwa alipatikana katika majengo ya Bunge la Kaunti ya Tana River, Bw Godhana alikiri kuwa uchawi ni imani inayoshikiliwa na baadhi ya watu katika jamii, lakini akasisitiza kuwa hauhusiani kwa vyovyote na maamuzi yake kuhusu maeneo anayofanyia kazi. Katika mahojiano na kituo cha runinga cha NTV, alibainisha kuwa hufanyia kazi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo makazi yake binafsi. Hata hivyo, aliongeza kuwa serikali ya kaunti inaendelea kujenga jengo la kisasa la utawala litakalowezesha shughuli zote za serikali ya kaunti kuendeshwa katika eneo moja.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 03 Nov 2026 07:55:36
Mivutano yaibuka upya katika upinzani
UPINZANI nchini unakabiliwa na mivutano mipya ya ndani baada ya Kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua kupendekeza muungano wa vyama vitatu, hatua iliyozua malumbano na viongozi wengine wanaolenga kumwondoa Rais William Ruto mamlakani 2027. Bw Gachagua anataka DCP, Linda Mwananchi ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Wiper inayoongozwa na Kalonzo Musyoka ziungane. Katika mahojiano na runinga ya Inooro, Bw Gachagua alisema muungano wa Mlima Kenya, Magharibi na Ukambani unatosha kuushinda utawala wa Rais Ruto. Alidai ana uwezo wa kuleta kura milioni 10, huku Bw Sifuna akileta milioni nne na Bw Musyoka milioni tatu. "Baina yangu, Sifuna, Eugene Wamalwa na Kalonzo Musyoka, uchaguzi utakuwa umekwisha. Hata tusipopata wengine, bado tunaweza kushinda," akasema Bw Gachagua. Hata hivyo, pendekezo hilo limewakera baadhi ya viongozi wa upinzani, wakiwemo kiongozi wa Jubilee Dkt Fred Matiang'i na Kiongozi wa DP Justin Muturi, ambao wamemshutumu Bw Gachagua kwa kiburi na kuwadharau washirika wake. Dkt Matiang'i alisema matamshi ya Bw Gachagua yanahatarisha kuuvunja upinzani kwa kuugawanya kwa misingi ya kikabila. " Kiburi cha walio wengi na majivuno hayo ndiyo yatakayougawanya upinzani na kufanya iwe vigumu kuungana," akasema Aliongeza kuwa uongozi wa nchi haupaswi kuamuliwa kwa misingi ya jamii, bali uwezo wa mtu binafsi. Bw Muturi naye alisema kwamba hakuna jamii moja inayoweza kumwezesha mtu kuwa Rais bila kuungwa mkono na Wakenya kutoka maeneo mengine. "Urais hupatikana kupitia maafikiano ya kitaifa, miungano ya kimkakati na uwezo wa kuwaunganisha Wakenya kutoka jamii na maeneo mbalimbali," alisema. Alionya kuwa mpango wa vyama vitatu si njia ya moja kwa moja ya kuingia Ikulu na akataka muungano ujengwe kwa kuheshimiana, badala ya vitisho na mashindano ya ubabe. Mivutano hiyo inatokana pia na madai ya baadhi ya viongozi kuwa washirika wao ni vibaraka wa serikali. DCP imehusisha madai hayo na Bw Matiang'i na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro wa People's Party of Kenya. Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kuwa mzozo huo unahusu pia udhibiti wa kura za eneo la Mlima Kenya. Aidha, viongozi hao hawajakubaliana kuhusu atakayekuwa mgombea mmoja wa urais wa upinzani. Wengi wana matarajio ya kuwania kiti hicho, huku maswali yakiibuka kuhusu uwezo wao wa kuvutia uungwaji mkono wa kitaifa, fedha na miundo ya kisiasa. Dkt Matiang'i alisema yuko tayari kumuunga mkono mgombea mwingine iwapo atachaguliwa kupitia mchakato wa wazi na unaowashirikisha wote. "Yeyote atakayechaguliwa kupitia mchakato jumuishi na unaokubalika kwetu sote, nitamuunga mkono," akasema. Alisema pia kuwa akichaguliwa Rais, atafuta ushuru wa nyumba, kupambana na ufisadi, kuimarisha usalama na kuhakikisha rasilimali za kaunti zinatumika ipasavyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 03 Nov 2026 06:55:42
Masaibu hayaishi, Waititu aongezwa miaka 13 jela
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ameongezewa kifungo cha miaka 13 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya ulanguzi wa fedha zinazohusishwa na zabuni ya ujenzi wa barabara yenye thamani ya Sh588.7 milioni iliyotolewa wakati alipokuwa gavana. Hakimu Mkuu Harrison Barasa wa Mahakama ya Milimani, jana, alimuamuru Waititu kulipa faini ya jumla ya Sh21 milioni au atumikie kifungo cha miaka 13 kutokana na mashtaka matatu ya ulanguzi wa fedha. Hata hivyo, kifungo hicho kitaunganishwa na kile cha miaka 12 ambacho tayari anatumikia kutokana na makosa ya ufisadi. Mkewe, Susan Wangari Ndung'u, alitozwa faini ya Sh18 milioni au kifungo cha miaka miwili iwapo atashindwa kulipa. Mfanyabiashara Charles Mbuthia Chege, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Testimony Enterprises iliyopata zabuni hiyo naye aliangushiwa adhabu ya miaka 13. Mkewe, Beth Wangechi Mburu, walitozwa Sh6 milioni au kifungo cha miaka sita. Hukumu hizo zilitolewa baada ya washtakiwa kufika mahakamani kuomba wapunguziwe adhabu. Waititu na Chege waliiomba mahakama kuwaonea huruma wake zao, wakidai hawakuhusika pakubwa katika mikataba iliyosababisha wapatikane na hatia. Wakili wa Waititu alisema Susan alikuwa mshirika asiyehusika moja kwa moja na shughuli za kampuni hizo. "Mahakama itatambua kuwa Susan alikuwa mshirika wa kimya katika kampuni hizo mbili. Hakuwa mtu wa kutia saini akaunti za benki wala mshiriki katika kufanya maamuzi ya biashara na jukumu lake lilikuwa dogo," akasema wakili huyo. Upande wa Chege ulisema Beth alikuwa na hisa moja pekee katika kampuni na alihusika tu katika kusaini nbarua za awali za usajili. Mawakili pia walidai kuwa kazi za ujenzi wa barabara zilikuwa zimekamilika na ripoti ya ukaguzi haikuonyesha upotevu wa fedha za umma. Walisisitiza kuwa mgogoro ulihusu utaratibu wa kutoa zabuni. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga ombi la kupunguziwa adhabu, ukisema kila mshtakiwa alipaswa kuwajibika binafsi kwa makosa yake. Hakimu Barasa alisema mashtaka ya ulanguzi wa fedha yana sheria maalumu zinazotaka adhabu zinazotolewa zifuate viwango vilivyowekwa. "Kila mtu atawajibika kivyake kwa makosa aliyotenda," akasema. Waititu alitozwa Sh10 milioni au kifungo cha miaka mitano katika shtaka la 10, Sh6 milioni au miaka minne katika shtaka la 11 na Sh5 milioni au miaka minne katika shtaka la 12. Chege alipewa adhabu sawa na hizo, huku Beth akitozwa Sh2 milioni au miaka miwili kwa kila shtaka kati ya matatu. Susan alitozwa jumla ya Sh18 milioni au miaka miwili gerezani. Kampuni zilizohusishwa na mikataba hiyo pia ziliadhibiwa. Testimony Enterprises ilitozwa Sh36 milioni, Saika Two Estate Developers Sh24 milioni na Bienvenue Delta Hotel Sh4 milioni. Kampuni hizo zilipewa siku 14 kulipa faini zao. Kesi hiyo ilitokana na zabuni ya Sh588.7 milioni iliyotolewa na serikali ya Kiambu kwa Testimony kwa ajili ya kuboresha barabara za changarawe na kuziweka lami katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 03 Nov 2026 05:55:32
Kesi ya kuandamana hadi ikulu yaambulia patupu
WANAHARAKATI wamepoteza kesi ya kutaka wananchi waruhusiwe kufanya maandamano nje ya Ikulu na ikulu ndogo ya Rais katika maeneo mbalimbali nchini. Mahakama ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na kundi la Operation Linda Jamii, ikisema halikuthibitisha jinsi notisi zilizotangaza makazi hayo kuwa maeneo yaliyolindwa zinavyokiuka Katiba au sheria. Notisi hizo zinajumuisha Ikulu za Nairobi na Mombasa pamoja na ikulu ndogo za Kisumu, Sagana, Nyeri, Eldoret, Nakuru na Kisii. Wanaharakati walidai kuwa marufuku hiyo inakiuka haki ya wananchi kukusanyika, kuandamana na kuwasilisha malalamishi yao kwa Rais William Ruto. Hata hivyo, mahakama ilisema Sheria ya Maeneo Yanayolindwa haizuii watu kuingia kabisa, bali inadhibiti kuingia kwa kutaka kibali kutoka kwa maafisa walioidhinishwa. "Kuingia katika maeneo hayo hakujapigwa marufuku, bali kunadhibitiwa," ikasema mahakama. Iliongeza kuwa wananchi wanaweza kuwasilisha malalamishi yao katika afisi nyingine za serikali, ikiwemo Afisi ya Rais, bila kulazimika kufika ikulu au ikulu ndogo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 03 Nov 2026 04:55:16
Wakenya walivyotekeleza ulaghai wa Sh25bn pesa za Amerika
MKENYA aliyepata kadi ya kuishi Amerika, Green Card, kupitia bahati nasibu mnamo 2024 anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika ulaghai wa Sh25.8 bilioni uliolenga fedha za serikali za kuwasaidia wanafunzi kugharimia elimu ya juu. Francis Smith Mogambi anadaiwa kushirikiana na washirika wake nchini Kenya kati ya Novemba 2025 na Mei 2026 kuiba taarifa za kibinafsi za raia wa Amerika na kuzitumia kuwaandikisha katika vyuo vya mtandaoni bila wao kujua. Washukiwa walitumia taarifa hizo kuwasilisha maombi ya mikopo na misaada ya elimu kupitia mpango wa serikali wa FAFSA. Baada ya fedha kutolewa, walidaiwa kuzichukua kupitia akaunti za benki na hundi bandia. Mogambi anadaiwa kupokea hundi zilizoandikwa kwa majina ya wanafunzi hewa, kuzitia saini na kuweka fedha hizo katika akaunti zake. Inadaiwa alisalia na asilimia 30 na kisha kutuma nyingine kwa washirika wake Kenya. Polisi walianza kumchunguza baada ya shahidi kusema alijaribu kumshawishi kujiunga na ulaghai huo kwa kumwahidi dola 2,000 (Sh259,000) kila wiki. Mnamo Oktoba 19, Mahakama kuu Nebraska ilimfungulia mashtaka 10, yakiwemo ya kuiba fedha za serikali na kutumia utambulisho wa watu wengine. Uchunguzi huo, uliopewa jina la 'Operation Ghostbusters', pia umehusisha washukiwa katika New Jersey na Virginia. Serikali za Kenya na Amerika zinazuia sarafu za kidijitali zenye thamani ya dola 750,000 (Sh97.4 milioni) zinazohusishwa na ulaghai huo. Ushirikiano huo unahusisha asasi za usalama na haki kama DCI, ARA, ODPP, KRA na FRC. Maafisa wa Amerika pia wamejadiliana na Kenya uwezekano wa kuwarejesha washukiwa nchini Amerika kukabili mashtaka. "Hundi hizo zilitolewa kwa majina ya wanafunzi tofauti, lakini zote zilikuwa na sahihi zilizomlipa Mogambi," polisi walisema katika hati ya kiapo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 03 Nov 2026 03:55:39
Usalama wakazwa KCSE ikianza rasmi
MTIHANI wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) wa mwaka huu wa 2026 ulianza rasmi jana kote nchini huku maelfu ya watahiniwa wakianza kufanya mitihani yao katika mazingira ya ulinzi mkali na onyo kali dhidi ya udanganyifu. Mwaka huu, watahiniwa, wasimamizi na maafisa wengine wamepigwa marufuku kuingia katika vyumba vya mitihani wakiwa wamevaa saa za mikononi, zikiwemo saa za kawaida na za kisasa. Watahiniwa wanatarajiwa kutumia saa za ukutani zilizowekwa katika vyumba vya mitihani. Katika Moyale, Marsabit, watahiniwa 220 kutoka shule mbili za mpakani walihamishwa hadi shule nyingine baada ya risasi zilizopotea kutoka mapigano upande wa Ethiopia kulenga shule zao. Watahiniwa wa shule za mseto za Sessi na St Mary walihamishiwa shule za msingi zilizo salama zaidi. Jumla ya watahiniwa 1,443 wanafanya mitihani katika vituo 12 vya eneo hilo huku wanajeshi KDF na maafisa wa usalama wa mipaka wakiongeza doria. Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC), Prof Julius Nyabundi, alisema kufikia Jumatatu asubuhi hakukuwa na taarifa za udanganyifu. Alisema huu ni mtihani wa pili kutoka mwisho kusimamiwa na KNEC kabla ya mabadiliko ya mfumo wa mtaala. Uasin Gishu, watahiniwa 22,593 walianza mtihani katika vituo 246. Maafisa walipiga marufuku saa za mikononi, mavazi yasiyo sare za shule na watu wasioidhinishwa kuingia vyumba vya mitihani. Turkana, zaidi ya watahiniwa 7,000 katika vituo 68 walianza mitihani huku wakuu wa shule wakiomba ulinzi zaidi katika maeneo yanayokumbwa na ujangili. Serikali kuu na ile ya kaunti pia inafuatilia uwezekano wa mafuriko kuathiri usafirishaji wa karatasi za mitihani. Baringo ilisajili watahiniwa 16,549 katika vituo zaidi ya 196, huku Trans Nzoia ikiwa na 28,353 katika vituo 253. Maafisa walisema zoezi lilianza bila matatizo makubwa. Nyeri, watahiniwa wanne wanafanyia mitihani hospitalini kutokana na matatizo ya kiafya. Bomet pia ina watahiniwa watatu hospitalini, wakiwemo wawili wenye ujauzito. Murang'a iliwasajili watahiniwa 32,487, lakini kukazuka wasiwasi kuhusu karibu wanafunzi 600 waliodaiwa kuacha shule tangu walipojiunga na Kidato cha Kwanza. Baadhi ya watahiniwa pia walilalamikia kupewa chakula kidogo kutokana na kuchelewa kwa fedha za serikali. Kisumu ilisajili watahiniwa 25,849 katika shule 246, huku Kisii ikiimarisha usalama katika vituo vyake 45. Katika eneo la Pwani, watahiniwa 63,415 walianza mitihani. Kilifi ilikuwa na 25,617, Mombasa 12,187, Kwale 12,171, Taita Taveta 7,994, Tana River 3,082 na Lamu 2,364. Huko Lamu, mitihani ilianza kwa utulivu hata katika maeneo yenye changamoto za kiusalama ya Msiti wa Boni na Kiunga, mpakani mwa Kenya na Somalia. Kwa ujumla, maafisa wa elimu na usalama walisema maandalizi yalikuwa yamekamilika, huku wakiahidi kuhakikisha mitihani inaendeshwa kwa usalama na bila udanganyifu.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 03 Nov 2026 02:55:45
Sakaja atupa Wilbaro, alenga kujinafasi 2027 kupitia ODM
GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja jana alijiunga rasmi na chama cha ODM akilenga kuimarisha nafasi yake ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu ujao. Bw Sakaja, aliyechaguliwa mnamo 2022 kwa chama tawala cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto, alisema yuko tayari kufanya kampeni za muhula wa pili wa Rais akiwa mwanachama wa ODM. ODM na UDA kwa sasa ziko katika Serikali Jumuishi, huku zikiendelea na mchakato wa kutia saini mkataba wa ushirikiano kabla ya uchaguzi mkuu. Hata hivyo, hafla ya kumpokea Bw Sakaja katika makao makuu ya ODM, Chungwa House, ilizua hisia tofauti. Gavana huyo alisisitiza kuwa amekuwa akitekeleza matakwa ya aliyekuwa kiongozi na mwanzilishi wa ODM, marehemu Raila Odinga. "Nilianza safari hii na Baba (Raila Odinga) nilipotwaa ugavana. Na nimekuwa nikishambuliwa kwa kusimama naye na kuwasaidia wanachama wa ODM kuingia katika Baraza la Mawaziri. Nilifanya hivyo kabla ya kuundwa kwa Serikali Jumuishi na Baba ndiye aliyeniambia niingie ODM," akasema Bw Sakaja. Bw Sakaja alipokelewa na Naibu Kiongozi wa ODM aliye pia Gavana wa Kisii, Simba Arati, Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama hicho na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Mbunge wa Suna Mashariki na Mkurugenzi wa Uchaguzi ODM Junet Mohammed, pamoja na Waziri wa Madini Hassan Joho. Gavana huyo alisema anajiunga na chama hicho kwa unyenyekevu, akiwa tayari kuongozwa na ngazi zake za juu na kuanza kampeni za kuvumisha umaarufu wake. "Ninaamini kuwa hatua inayofuata ya siasa zetu haipaswi kupimwa tu kwa uchaguzi tunaoshinda, bali pia kwa maisha tunayobadilisha. Vijana hawapaswi tena kuwa watazamaji katika maamuzi yanayoathiri mustakabali wao bali anapaswa kushiriki, kuwa viongozi na kuwa kiini cha Kenya tunayoijenga," akasema. Bw Sakaja alikumbushwa kuwa Mwenyekiti wa ODM utanzu wa Nairobi ambaye ni Mbunge wa Makadara George Aladwa pia anawania tiketi ya chama hicho kugombea ugavana wa Nairobi. "Tuna mwenyekiti wetu wa chama Nairobi, George Aladwa, ambaye amekuwa akisimama na chama kwa muda mrefu na pia anawania kiti cha ugavana kupitia ODM. Sasa tunaye Gavana Sakaja," akasema Bi Wanga, akiongeza kuwa kila anayetaka kujiunga na chama hicho anakaribishwa. Jana, Bw Aladwa alisema yuko imara ndani ya ODM na kuwataka wafuasi wake wawe watulivu akisisitiza nia yake ya ugavana bado upo hai. "Wafuasi wangu nawaelewa lakini tusipoteze muda kutokana na uvumi unaoendelea. Safari ya kuimarisha Nairobi itaamuliwa na raia kwa usawa na haki na demokrasia. Tuendelee kudumisha amani," akasema Bw Aladwa. Wakati wa kumpokea Bw Sakaja, Bi Wanga alitangaza kuwa uteuzi wa wagombea utafanywa kwa uwazi na bila ubaguzi. Bw Arati pia alifichua kuwa Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri ni miongoni mwa wanaotaka kujiunga na ODM ili kuwania kiti hicho hicho. "Mwenyekiti wetu wa Nairobi, Aladwa, pia anawania ugavana. Atachuana na Gavana Sakaja kuwania tiketi ya chama. Karauri akiamua kujiunga nasi, tutampokea kama tulivyompokea Sakaja. Tunachowaahidi wanachama wetu ni uteuzi huru, wa haki na uwazi," akasema Bw Arati. Kutokana na kutokuwepo kwa Bw Aladwa katika hafla hiyo, Bw Sakaja alisema atamtafuta binafsi ili kuunganisha kura za ODM Nairobi na kuhakikisha chama hicho kinashinda viti vingi. Baadhi ya madiwani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi waliohudhuria hafla hiyo walikuwa wamemuidhinisha Bw Aladwa awali kuwania uongozi wa kaunti hiyo. Polisi nao walilazimika kutumia vitoza machozi kutawanya kundi la wanachama waliokuwa wakijaribu kuvuruga hafla hiyo. Baadhi yao walisikika wakipiga kelele, "Kama hakuna Aladwa, hakuna ODM." Mbali na Gavana Sakaja na Aladwa, ODM inakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea wa makundi mengine ambao wametangaza nia ya kuwania kiti hicho. Wao ni Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino (chama cha Mwananchi), Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya (DCP) na Askofu Margaret Wanjiru . Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua pia ametangaza kuwa chama chake cha DCP kinataka kutawala siasa za Nairobi na inaaminika anamuunga mkono Bw Gakuya.
read moreRight Column Content