T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

Man United yazinduka usingizini na kung'ata mtu hatimaye

BAYERN Munich na Paris Saint-Germain (PSG) zimeimarisha matumaini yao ya kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kupata ushindi mnono dhidi ya Atletico Madrid na Villarreal mtawalia Jumanne usiku. Manchester United ilionyesha juhudi za kupambana kwa kurejea kutoka nyuma kwa mabao mawili na kuichapa AS Roma 3-2 katika mechi ya kusisimua kwenye Uwanja wa Old Trafford. Bayern ilipata ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya Atletico Madrid, ambayo iliwasumbua kwa muda mrefu. Lennart Karl aliifungulia Bayern ukurasa wa mabao dakika ya 54 kabla ya Konrad Laimer kuongeza la pili dakika ya 74, akitumia pasi ya Harry Kane. PSG nayo iliweka rekodi kwa kufunga mabao manne ndani ya dakika 17 za mwanzo katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Villarreal. João Neves, Désiré Doué na Senny Mayulu walifunga mabao matatu ndani ya kipindi cha dakika tano kabla ya Fabián Ruiz kuongeza la nne. Ruiz alifunga tena kipindi cha pili kabla ya David Boly, aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza katika mashindano hayo, kukamilisha karamu ya mabao. Katika Uwanja wa Old Trafford, Manchester United ilijipata nyuma kwa mabao mawili baada ya Matías Soulé na Donyell Malen kuifungia Roma. Malen alifunga kupitia penalti. Hata hivyo, Bruno Fernandes aliipatia United bao la kwanza kupitia penalti iliyopigwa upya kabla ya Matheus Cunha kufunga mabao mawili ndani ya dakika nne na kuipa timu hiyo ushindi wa 3-2. Barcelona nayo iliilaza Aston Villa 3-0. Lamine Yamal alifungua ukurasa wa mabao dakika ya saba kabla ya Raphinha kufunga mawili kipindi cha pili, akitumia nafasi iliyotokana na shuti iliyopanguliwa na baadaye pasi ya João Cancelo. Inter Milan iliicharaza Feyenoord 3-0. Yann Bisseck alifungua ukurasa wa mabao kwa shuti ya mbali kabla ya Pio Esposito kuongeza la pili kwa kichwa kutokana na krosi ya Djed Spence. Piotr Zielinski alikamilisha ushindi huo kwa shuti kali ya mbali kipindi cha pili. Katika mechi nyingine, Galatasaray iliilaza Stuttgart 2-0 kupitia mabao mawili ya Aleksei Batrakov. Sporting CP iliishinda Shakhtar Donetsk 1-0 kupitia Issa Doumbia. LASK nayo iliichapa Slovan Bratislava 4-0 ambapo Kasper Jørgensen alifunga mawili, Robert Ljubičić akaongeza la tatu na Samuel Adeniran akafunga la nne. Bodø/Glimt na Lille zilitoka sare ya 0-0. PSG inaongoza msimamo kwa alama 12, huku Barcelona na Aston Villa zikiwa miongoni mwa timu sita zilizo na pointi tisa. Kabla ya mechi hizo, viwanja mbalimbali barani Ulaya vilikaa kimya kwa dakika moja kuomboleza kifo cha mchezaji wa Tenerife, Jesus de Miguel, aliyefariki dunia Jumanne. Ratiba ya Europa League: Milan v Ferencavaros (20.45pm) Palace v Hoffenheim (20.45pm) Sparta Braha v Bournemouth (20.45pm) NEC v Omonio (20.45pm) Anderlecht v RB Salzburg (20.45pm) Real Sociedad v OL (20.45pm) Levski Sofia v Jagiellonia (20.45pm) Torreen v Ararat-Armenia (23.00pm) Celtic v Besikitas (23.00pm) Sturm Graz v Celjie (23.00pm) H-Beersh-Sheva v OFI (23.00pm) AZ v Juventus (23.00pm) Leverkusen v Marsaille (23.00pm) Benfica v Lech Poznari (23.00pm)

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

Wapigakura wampa Trump kipigo kikali kwa kupuuza uchumi, kuzua vita Iran na bei ghali ya bidhaa

WASHINGTON DC, AMERIKA: CHAMA cha Democrats kimefanikiwa kunyakua udhibiti wa mabunge yote mawili ya Marekani, baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Jumanne, Novemba 3, 2026, katika matokeo yanayochukuliwa kuwa pigo kubwa la kisiasa kwa Rais Donald Trump na chama chake cha Republican. Ushindi huo unamaanisha kuwa Wanademocrats watakuwa na udhibiti wa Baraza la Wawakilishi na Seneti kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa pili wa utawala wa Trump, unaotarajiwa kukamilika Januari 2029. [caption id="attachment_193611" align="alignnone" width="2560"] Abdul El-Sayed, aliyechaguliwa kuwa Mwislamu wa kwanza kuingia Seneti Amerika baada ya uchaguzi uliofanyika Jumanne. Picha|Reuters[/caption] Matokeo hayo yanaashiria mabadiliko makubwa katika siasa za Marekani, ambapo wapigakura wameonyesha kutoridhishwa na namna serikali ya Trump inavyoshughulikia masuala muhimu yanayowahusu raia, ikiwemo kupanda kwa gharama ya maisha, vita vya Iran, ushuru wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na madai ya ufisadi serikalini. Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na vyombo vya habari vya Marekani, chama cha Democratic kilipata viti kadhaa vya Seneti kutoka kwa Republican katika majimbo yaliyokuwa yakichukuliwa kuwa ngome za chama hicho tawala. Miongoni mwa majimbo hayo ni Texas, Iowa, Kansas, Ohio, Maine, North Carolina na South Carolina. Katika jimbo la Texas, Wanademocrats walipata ushindi muhimu katika kinyang'anyiro cha Seneti, huku James Talarico akimshinda mgombea wa Republican Ken Paxton. Ushindi huo ni muhimu kwa chama hicho kwa sababu Texas imekuwa ikiegemea Republican katika uchaguzi wa kitaifa kwa muda mrefu. Vilevile, katika jimbo la Maine, mgombea wa Democratic Troy Jackson alimshinda Seneta Susan Collins wa Republican, aliyekuwa akitetea kiti chake baada ya kuhudumu kwa mihula mitano. Huko Kansas, Wanademocrats walipata ushindi wa kihistoria kwa kuchaguliwa kwa seneta wao wa kwanza katika kipindi cha karibu karne moja. Katika Bunge la Wawakilishi, Wanademocrats pia walipata mafanikio makubwa kwa kunyakua zaidi ya viti 24 kutoka kwa Republican. Ushindi huo uliwasaidia kurejesha udhibiti wa asasi hiyo ya kutunga sheria, ambayo ina jukumu muhimu katika kupitisha miswada ya matumizi ya serikali, bajeti na sheria nyingine za kitaifa. Matokeo ya uchaguzi huo pia yalionyesha mabadiliko katika uongozi wa majimbo. Wagombea wa Democratic walishinda nyadhifa za ugavana katika majimbo kadhaa yaliyokuwa yakiongozwa na Republican, yakiwemo Georgia, Ohio, Iowa na Texas. Kwa jumla, chama hicho kinatarajiwa kudhibiti nyadhifa nyingi zaidi za magavana kuliko wapinzani wake, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010. Ushindi wa Wanademokrasia umehusishwa kwa kiasi kikubwa na kutoridhika kwa wapigakura kuhusu hali ya uchumi. Gharama za bidhaa na huduma zimekuwa mojawapo ya masuala makuu katika kampeni, huku wapinzani wa Trump wakilaumu sera za serikali yake kwa kushindwa kupunguza mzigo wa maisha kwa Wamarekani. Vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran pia vilichangia mjadala wa uchaguzi. Baadhi ya wapigakura walionyesha wasiwasi kuhusu gharama za vita hivyo na athari zake kwa usalama wa taifa na uchumi. Suala la ushuru wa bidhaa kutoka nje na madai ya ufisadi katika utawala wa Trump pia lilitajwa miongoni mwa mambo yaliyoathiri maamuzi ya wapigakura. Kwa mujibu wa kura za maoni zilizofanywa na Associated Press, wapigakura wengi walitaka Bunge litumie mamlaka yake kuhakikisha kuwa rais hawajibiki kwa maamuzi yake bila kukaguliwa. Takribani asilimia 70 ya waliohojiwa walisema Bunge halikuwa likifanya vya kutosha kuzuia matumizi mabaya ya mamlaka ya urais. Hata hivyo, Trump amepunguza uzito wa kushindwa kwa chama chake, akisema kuwa yeye mwenyewe hakuwa mgombea katika uchaguzi huo. Pia alilaumu baadhi ya wagombea wa Republican kwa kutofanya kampeni nzuri na kutetea sera zake. Mabadiliko hayo yanatarajiwa kuwa na athari kubwa kwa utawala wa Trump katika miaka miwili iliyosalia ya muhula wake. Kwa kuwa chama cha Democratic kitakuwa na udhibiti wa mabunge yote mawili, kitapata uwezo mkubwa wa kuzuia miswada inayoungwa mkono na rais, kukataa baadhi ya wateule wake katika nyadhifa za serikali na kuanzisha uchunguzi kuhusu shughuli za utawala wake. Hata hivyo, ushindi huo hauondoi mamlaka ya rais kutekeleza baadhi ya sera zake kupitia mamlaka ya kiutendaji. Trump pia ana uwezo wa kupinga miswada inayopitishwa na Bunge kwa kutumia mamlaka yake ya kura ya turufu (veto), hivyo huenda kukazuka mvutano mkubwa kati ya Ikulu ya White House na Bunge. Uchaguzi wa katikati ya muhula hufanyika kila baada ya miaka miwili, katikati ya kipindi cha miaka minne cha rais. Kwa kawaida, uchaguzi huo hutumiwa na wapigakura kutathmini utendaji wa rais na chama chake, huku viti vyote vya Baraza la Wawakilishi na takribani theluthi moja ya Seneti vikiwania. Kwa ushindi huu, Wanademokrasia sasa wana nafasi ya kuimarisha usimamizi wa serikali ya Trump na kuathiri mwelekeo wa sera za Marekani hadi uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka 2028.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Mchango wa siasa katika kueneza Kiswahili kupitia kauli mbiu 'Skiza Wakenya,' 'Usawa ni Sawa,' na 'Linda Mwananchi'

MATUMIZI mbalimbali ya lugha yamethibitisha kwamba katika siasa za Kenya, mbali na mawasiliano, lugha ni nyenzo muhimu ya ushawishi na uhamasishaji. Wanasiasa huitumia kueleza sera zao, kujenga taswira zao na kuwavutia wapigakura. Kiswahili kimekuwa chombo muhimu katika kuendeleza mambo hayo. Kwa mfano, kinatumiwa katika kauli mbiu za vyama vingi, hata pale ambapo majina ya vyama hivyo ni ya Kiingereza. Kwa mfano chama cha The National Alliance (TNA) kilitumia kauli mbiu "Kazi Iendelee", Democratic Citizens Party (DCP) kinatumia "Skiza Wakenya", The Clean Alliance Party of Kenya (CAP-K) nacho kinatumia "Maisha Mapya, Uongozi Mpya", The Equitable Party kina kauli mbiu "Tusawazishe", People's Party of Kenya hutumia "Sauti ya Wakenya", huku Mwongozo Party of Kenya kinatumia "Sote Pamoja". Kauli hizi zinaonyesha jinsi vyama vinatumia Kiswahili kuwasilisha ujumbe kwa wananchi. Aidha, zinadhihirisha kuwa lugha ni sehemu ya mkakati wa kisiasa unaolenga kujenga uhusiano kati ya chama na wapigakura. Uamuzi wa kutumia Kiswahili badala ya Kiingereza au lugha za jamii unaeleweka tunapozingatia nafasi yake nchini. Ni lugha ya taifa na mojawapo ya lugha rasmi inayowaunganisha wananchi wa makabila, maeneo na matabaka mbalimbali. Hivyo basi, mwanasiasa anayekitumia ana nafasi ya kufikisha ujumbe wake kwa hadhira pana zaidi. Hili ni muhimu hasa wakati wa kampeni, ambapo viongozi huwasiliana na watu wenye tofauti za kiisimu na kitamaduni. Faida ya Kiswahili katika siasa haiishii kwenye kura, kwani wanasiasa wanakieneza kila wanapokitumia. Wanakuwa pia mabalozi wa lugha hii wanapoizungumza katika mikutano ya hadhara, mijadala ya kisiasa, mahojiano ya vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali. Wanapozunguka nchini kuuza sera zao, wanakieneza Kiswahili na kukifanya sehemu ya mawasiliano ya kila siku. Kwa njia hii, siasa huipa lugha hii nafasi ya kusikika na kutumiwa na watu wengi katika mazingira tofauti. Uwezo Zaidi ya hayo, Kiswahili kina uwezo wa kisanaa unaowawezesha wanasiasa kubeba mawazo mapana kwa maneno machache. "Kazi Iendelee", "Sote Pamoja" "Mbele Pamoja" na "Maisha Mapya, Uongozi Mpya" ni kauli fupi, rahisi kukumbuka na rahisi kurudiwa zinazosheheni taarifa muhimu kwa umma. Kauli za hivi karibuni kama "Usawa ni Sawa," "Linda Mwananchi" na "Linda Ground" nazo zinaonyesha jinsi maneno ya Kiswahili yanavyoweza kubeba ujumbe wa kijamii na kisiasa kutegemea muktadha. Maneno kama usawa, haki na mwananchi yanagusa hisia na kuibua mijadala kuhusu masuala yanayowahusu raia. Matumizi haya yanakipa Kiswahili nafasi katika mijadala ya kitaifa na kuifanya iwe hai na ambayo inatumika kueleza masuala ya uongozi, uchumi na maendeleo. Pia, yanaondoa lugha hii katika mtazamo ambao unahusu mazungumzo ya kawaida pekee, na kuisawiri kuwa inaweza kubeba hoja nzito za kisiasa na kijamii. Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha matumizi ya lugha na utekelezaji wa sera. Kauli mbiu inaweza kuvutia wananchi, lakini haithibitishi kikamilifu kuwa ahadi zitatekelezwa. Wananchi wanapaswa kuchunguza sera, mipango na matokeo ya viongozi. Kwa hakika, wanasiasa wana nafasi muhimu katika kueneza Kiswahili nchini. Wanapokitumia kuwasilisha sera na kuwasiliana na wananchi, wanakuwa sehemu ya juhudi za kukikuza na kukipa nafasi katika ramani ya kitaifa na kimataifa. Kila jukwaa la kisiasa linalotumia Kiswahili ni fursa ya kukitangaza na kukieneza. Wanasiasa wanabeba bendera ya Kiswahili.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Korti yampa Mbunge wa Mosop Abraham Kirwa siku 5 kueleza kwa nini kiti chake kisitangazwe kuwa wazi

MBUNGE wa Mosop Abraham Kirwa amepewa siku tano kueleza sababu za kutohudhuria vikao vya Bunge kwa zaidi ya miaka miwili, katika kesi inayolenga kiti chake kitangazwe kuwa wazi. Jaji Roselyne Aburili wa Mahakama Kuu aliruhusu Kirwa na Spika wa Bunge la Kitaifa kujibu madai ya mpigakura Timothy Tororey kwamba wakazi wa Mosop wameachwa bila uwakilishi wa kutosha. Jaji aliagiza mbunge huyo na Spika kuwasilisha majibu na hoja zao za maandishi ndani ya siku tano kuanzia Novemba 2, 2026. Tororey naye amepewa siku tano baada ya kupokea majibu hayo kuwasilisha stakabadhi na hoja za ziada. Tororey, mkazi na mpigakura wa Mosop, anadai Kirwa amekuwa nje ya nchi kwa muda mrefu na kukosa vikao na shughuli rasmi za Bunge. Anasema hali hiyo imewanyima wakazi nafasi ya kuwakilishwa katika mijadala, kupiga kura na maamuzi kuhusu matumizi ya rasilimali za taifa. Pia anamlaumu Spika kwa kushindwa kuchukua hatua, akisema sheria inaruhusu kiti cha mbunge kutangazwa wazi iwapo atakosa vikao vinane mfululizo bila ruhusa. Hata hivyo, Spika kupitia Karani wa Bunge Samuel Njoroge alisema Kirwa alipata ruhusa ya kutohudhuria vikao kwa sababu za kiafya ili kupata matibabu nje ya nchi. Kirwa pia alisema alikuwa akisafiri kutafuta matibabu na alikuwa amepata idhini ya Spika. Alidai hakuwahi kupewa rasmi stakabadhi za kesi hiyo, bali aliifahamu kupitia Bunge. Akikubali ombi lao Jaji Aburili alisema suala hilo linaweza kuathiri hatima ya mbunge aliyechaguliwa na wananchi, hivyo ni muhimu asikilizwe kabla ya uamuzi wa mwisho. "Maamuzi yanayoombwa yanaweza kuathiri muda wa kuhudumu kwa mbunge aliyechaguliwa na, kwa upana zaidi, wapigakura anaowawakilisha," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Visa vya wahalifu kushambulia polisi, wanajeshi vyazua hofu

MATUKIO mawili tofauti ya mapigano kati ya maafisa wa usalama na washukiwa wa uhalifu yamezua wasiwasi kuhusu usalama wa polisi na wanajeshi, huku bunduki  zikiendelea kuibwa na magenge ya wahalifu. Katika tukio la kwanza, afisa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) alipigwa risasi na kuuawa na polisi katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, baada ya makabiliano yaliyotokea Jumapili, Novemba 1. Ripoti ya polisi inaonyesha kuwa maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Kahawa Sukari walikuwa kwenye doria mwendo wa saa saba usiku walipopokea taarifa kutoka kwa mwananchi kuhusu wanaume wawili waliokuwa na silaha na kutishia wakazi wa Covo, karibu na Magunas. Polisi waliwafuata washukiwa hao na kuwaamuru wasimame, lakini mmoja wao anadaiwa kutoa bastola na kuwafyatulia risasi maafisa hao, waliolazimika kujibu mashambulizi. "Mshukiwa aliyetoa bunduki alipigwa risasi kifuani na mkono wa kulia. Alikimbizwa katika Hospitali ya Ruiru Level 4 akiwa katika hali mahututi lakini baadaye akafariki akipokea matibabu," ilisema ripoti hiyo. Polisi walipata bastola aina ya Jericho iliyokuwa na risasi 12 pamoja na maganda mawili ya risasi zilizokuwa zimefyatuliwa. Pia walipata kitambulisho cha KDF kilichokuwa na jina la marehemu, Munene Antony, 33. Mshukiwa aliyenusurika anadaiwa kuwaambia wachunguzi kuwa bastola hiyo ilikuwa ya kakake ambaye ni polisi. Uchunguzi unaendelea kubaini umiliki wa silaha hiyo. Wakati huohuo, maafisa wawili wa polisi kutoka Kituo cha Ruai walijeruhiwa vibaya Jumatatu usiku baada ya kushambuliwa na genge la wanaume waliokuwa wameabiri pikipiki. Washambuliaji hao waliiba bunduki mbili aina ya AK-47, kila moja ikiwa na risasi 30. Maafisa hao, Corporal John Maritim na Corporal Felistus Tuitoek, walipata majeraha  kichwani na mikononi baada ya kushambuliwa kwa kitu chenye makali. Walipata matibabu katika Hospitali ya Reale, Utawala, huku polisi wakianzisha msako wa kuwakamata washukiwa na kurejesha silaha hizo. Tukio hilo linaongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa bunduki hizo kutumiwa katika uhalifu mwingine au mashambulizi dhidi ya raia na maafisa wa usalama. Mnamo Oktoba 26, genge lilishambulia maafisa waliokuwa wakilinda kituo cha ukusanyaji ushuru  Kaunti ya Mombasa, Likoni, na kumuua afisa mmoja wa kaunti huku wengine watatu wakijeruhiwa. Washambuliaji waliiba bunduki ya AK-47 kutoka kwa afisa wa utawala, ambayo baadaye ilitumika kumpiga risasi afisa huyo wa kaunti. Mnamo Machi, genge jingine lilishambulia polisi aliyekuwa akilinda eneo la viwanda la Bonje, Jomvu, na kumuibia bunduki ya AK-47 pamoja na simu. Matukio hayo yanajiri huku kukiwa na ripoti za mivutano kati ya polisi na wanajeshi. mnamo Septemba, maafisa hao walikabiliana katika kizuizi cha barabarani karibu na Chuo Kikuu cha Turkana, Lodwar, na baadaye katika Kituo cha Polisi cha Lodwar. Tukio jingine la mzozo kati ya polisi na wanajeshi liliripotiwa katika kivuko cha feri cha Likoni, Mombasa, mwezi huohuo. Matukio haya yanaibua maswali kuhusu ushirikiano kati ya idara za usalama, nidhamu kazini na silaha za serikali kuangukia mikononi mwa wahalifu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 8 hours ago

Washirika wa Sifuna kuvuliwa nyadhifa muhimu

VIONGOZI wawili wa Bunge la Kaunti ya Nairobi wanaohusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi Movement (LMM) linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna huenda wakapokonywa nyadhifa zao muhimu katika bunge hilo. Vyanzo vya kuaminika katika City Hall vinasema hatua hiyo inalenga kuwaadhibu madiwani hao kwa kuendelea kumuunga mkono Bw Sifuna licha ya kuchaguliwa na kuteuliwa kupitia chama cha ODM katika uchaguzi mkuu wa 2022. Wanaolengwa ni Kiranja wa Wengi Moses Ogeto na Perpetua Mponjiwa Okello, ambaye aliteuliwa kuwa MCA kupitia ODM. Bw Ogeto anahudumu muhula wake wa tatu kama mwakilishi wa wadi ya Kilimani, eneo bunge la Dagoretti North. Amekuwa akiwakilisha wadi hiyo tangu 2013 na alikuwa mshirika wa karibu wa mwanzilishi wa ODM, marehemu Raila Odinga. Kwa upande wake, Bi Mponjiwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Elimu katika Bunge la Kaunti ya Nairobi. Pia ametangaza nia ya kuwania kiti cha mwakilishi wadi ya Kileleshwa kinachoshikiliwa na MCA wa ODM Robert Alai. "Ni kweli. Hoja imeandaliwa na inaweza kuwasilishwa wakati wowote. Inawalenga viongozi wawili ambao wamekuwa wakiunga mkono chama hasimu huku wakiendelea kunufaika na nafasi walizopewa kupitia ODM," kilisema chanzo kimoja kilichoomba kutotajwa. Akizungumza na Taifa, Bw Ogeto alisema alikuwa amearifiwa kuhusu mpango wa kumuondoa katika wadhifa wake. Hata hivyo, alidai ODM imepoteza misingi iliyowekwa na Raila Odinga, akisema chama hicho sasa kinatanguliza maslahi ya wanasiasa badala ya wananchi. "Watu hawa hawafanyi tena yale Baba alikuwa akifanya, ndio maana tumetengana. Baba alikuwa wa wananchi, lakini wao wanajali pesa. Baba alikuwa akinipa maagizo kuhusu jinsi ya kuwatetea wananchi, lakini leo hakuna anayetaka kuwatetea," alisema. Bw Ogeto alisema kuondolewa kwake hakutakuwa na athari kubwa kwake kwa sababu bunge linakaribia kuingia likizoni hadi Februari kabla ya mapumziko mengine yasiyo na tarehe maalum ya kurejea. Alifichua kuwa anamezea mate kiti cha ubunge cha Dagoretti North kinachoshikiliwa na Beatrice Elachi wa ODM. Alisema hana hofu ya kupoteza wadhifa huo kwa sababu amejijengea uhusiano mzuri na wakazi wa eneo hilo. Iwapo ataondolewa, nafasi yake kama Kiranja wa Wengi inatarajiwa kuchukuliwa na naibu wake Stazo Omung'ala Elija Ang'ila, MCA wa wadi ya Upper Savannah. Jitihada za kumpata Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Peter Imwatok, ili kutoa maoni yake hazikufanikiwa kwani hakujibu simu wala ujumbe.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Mkenya Phoebe Okowa achaguliwa jaji wa Mahakama ya Kimataifa

MWANASHERIA na msomi wa Kenya Profesa Phoebe Okowa amechaguliwa kuhudumu kwa muhula kamili wa miaka tisa kama jaji wa Mahakama ya Kimataifa kuhusu Haki (ICJ), baada ya kushinda uchaguzi mkali uliohusisha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) na Baraza la Usalama. Profesa Okowa mwenye umri wa miaka 61 alipata ushindi huo katika duru ya tatu ya kupiga kura iliyofanyika katika makao makuu ya UN jijini New York Jumanne. Katika kura ya mwisho, alipata kura 183 kati ya nchi wanachama zilizoshiriki, huku mpinzani wake wa mwisho kutoka Peru, Luz del Carmen Ibáñez Carranza, akipata kura mbili pekee. Nchi sita hazikupiga kura. Pia aliungwa mkono kwa wingi katika Baraza la Usalama la UN, baada ya kukosa kufikia kiwango hicho katika duru ya awali alipopata kura sita pekee kati ya 15. Okowa tayari alikuwa akihudumu katika mahakama hiyo tangu mwaka jana, alipochaguliwa kukamilisha muhula wa jaji kutoka Somalia Abdulqawi Ahmed Yusuf, aliyejiuzulu kabla ya muda wake kumalizika Januari 2027. Ushindani wa wadhifa huo uligeuka kuwa wa Afrika baada ya Muungano wa Afrika kushindwa kuwashawishi Okowa na mwanasheria wa Sierra Leone Charles Chernor Jalloh kujiondoa. Katika duru ya pili, Okowa alipata kura 89 katika Baraza Kuu, lakini hakuchaguliwa kwa sababu hakuwa amepata uungwaji mkono unaohitajika katika Baraza la Usalama. Jalloh alipata kura 30. Baadaye Jalloh na wagombeaji wengine wawili, Paik Jin-Hyun wa Korea Kusini na Marcelo Vázquez-Bermúdez wa Ecuador, walijiondoa, na kuacha mgombeaji wa Peru na Okowa wakipambana katika duru ya mwisho. Uchaguzi wa majaji wa ICJ unahitaji mgombeaji kupata kura nyingi katika Baraza Kuu na Baraza la Usalama kwa wakati mmoja. Okowa ni mtaalamu wa sheria za kimataifa na amewahi pia kuhudumu katika Tume ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Mataifa. Ingawa Kenya ilifanya kampeni kubwa kumuunga mkono, Okowa hatahudumu mahakamani kama mwakilishi wa nchi yake. Atakuwa huru kufanya maamuzi kulingana na sheria na wajibu wake wa mahakama, hata katika kesi zinazohusu Kenya. Katibu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Sing'oei alisema utaalamu wa Okowa utasaidia mahakama hiyo kuendeleza mfumo wa kimataifa unaozingatia sheria. ICJ ina majaji 15 na jukumu lake kuu ni kusikiliza mizozo kati ya mataifa. Pia inaweza kutoa ushauri wa kisheria kwa ombi la Baraza Kuu la UN. Mahakama hiyo ni tofauti na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambayo hushughulikia kesi za watu binafsi wanaotuhumiwa kwa uhalifu mkubwa wa kimataifa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 8 hours ago

Washirika wa Sifuna kuvuliwa nyadhifa muhimu

VIONGOZI wawili wa Bunge la Kaunti ya Nairobi wanaohusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi Movement (LMM) linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna huenda wakapokonywa nyadhifa zao muhimu katika bunge hilo. Vyanzo vya kuaminika katika City Hall vinasema hatua hiyo inalenga kuwaadhibu madiwani hao kwa kuendelea kumuunga mkono Bw Sifuna licha ya kuchaguliwa na kuteuliwa kupitia chama cha ODM katika uchaguzi mkuu wa 2022. Wanaolengwa ni Kiranja wa Wengi Moses Ogeto na Perpetua Mponjiwa Okello, ambaye aliteuliwa kuwa MCA kupitia ODM. Bw Ogeto anahudumu muhula wake wa tatu kama mwakilishi wa wadi ya Kilimani, eneo bunge la Dagoretti North. Amekuwa akiwakilisha wadi hiyo tangu 2013 na alikuwa mshirika wa karibu wa mwanzilishi wa ODM, marehemu Raila Odinga. Kwa upande wake, Bi Mponjiwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Elimu katika Bunge la Kaunti ya Nairobi. Pia ametangaza nia ya kuwania kiti cha mwakilishi wadi ya Kileleshwa kinachoshikiliwa na MCA wa ODM Robert Alai. "Ni kweli. Hoja imeandaliwa na inaweza kuwasilishwa wakati wowote. Inawalenga viongozi wawili ambao wamekuwa wakiunga mkono chama hasimu huku wakiendelea kunufaika na nafasi walizopewa kupitia ODM," kilisema chanzo kimoja kilichoomba kutotajwa. Akizungumza na Taifa, Bw Ogeto alisema alikuwa amearifiwa kuhusu mpango wa kumuondoa katika wadhifa wake. Hata hivyo, alidai ODM imepoteza misingi iliyowekwa na Raila Odinga, akisema chama hicho sasa kinatanguliza maslahi ya wanasiasa badala ya wananchi. "Watu hawa hawafanyi tena yale Baba alikuwa akifanya, ndio maana tumetengana. Baba alikuwa wa wananchi, lakini wao wanajali pesa. Baba alikuwa akinipa maagizo kuhusu jinsi ya kuwatetea wananchi, lakini leo hakuna anayetaka kuwatetea," alisema. Bw Ogeto alisema kuondolewa kwake hakutakuwa na athari kubwa kwake kwa sababu bunge linakaribia kuingia likizoni hadi Februari kabla ya mapumziko mengine yasiyo na tarehe maalum ya kurejea. Alifichua kuwa anamezea mate kiti cha ubunge cha Dagoretti North kinachoshikiliwa na Beatrice Elachi wa ODM. Alisema hana hofu ya kupoteza wadhifa huo kwa sababu amejijengea uhusiano mzuri na wakazi wa eneo hilo. Iwapo ataondolewa, nafasi yake kama Kiranja wa Wengi inatarajiwa kuchukuliwa na naibu wake Stazo Omung'ala Elija Ang'ila, MCA wa wadi ya Upper Savannah. Jitihada za kumpata Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Peter Imwatok, ili kutoa maoni yake hazikufanikiwa kwani hakujibu simu wala ujumbe.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Viongozi wa Wiper watishia kujitenga na upinzani kuhusu tiketi ya urais

VIONGOZI wa chama cha Wiper katika eneo la Pwani wametishia kujiondoa katika muungano wa upinzani na kumuunga mkono kiongozi wao Kalonzo Musyoka kuwania urais kivyake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 iwapo hatapewa tiketi ya pamoja ya urais. Viongozi hao wa mashinani wamesisitiza kuwa wakati umefika kwa Bw Musyoka kupewa nafasi ya kuwania urais badala ya kuendelea kuunga mkono wagombeaji wengine au kukubali kuwa mgombea mwenza. Pia walipuuza madai kwamba aliyekuwa makamu wa rais anaweza kushirikiana kisiasa na Rais William Ruto katika uchaguzi ujao, wakisema wawili hao hawana uwezekano wa kuunda muungano. Mwanachama wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya Wiper, Omar Twaha, alidai kuwa Kalonzo amekuwa akidhulumiwa ndani ya upinzani licha ya mchango wake katika juhudi za kuunganisha viongozi wanaopinga utawala wa Rais Ruto. Hata hivyo, Bw Twaha alisema chama hicho hakina nia ya kuvunja muungano wa upinzani, bali kinataka viongozi waheshimiane na kumpa kila mmoja nafasi sawa katika mazungumzo kuhusu mgombeaji wa urais. "Iwapo tutamsimamisha Kalonzo kama chama, tutavunja upinzani, na hilo si lengo letu. Lengo letu ni moja, kumuondoa Rais William Ruto mamlakani. Kwa hivyo, ni lazima tuheshimiane," alisema. Mwenyekiti wa Wiper Pwani, John Chamia, alipuuza madai kwamba Kalonzo anaweza kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto, akisisitiza kuwa wawili hao hawawezi kushirikiana kisiasa. "Anayesema Kalonzo atakuwa naibu wa Ruto anaota. Hatuwezi hata kufanya mazungumzo naye kwa sababu Ruto na Kalonzo hawawezi kuwa pamoja," alisema Bw Chamia. Viongozi hao walisema iwapo Kalonzo atapuuzwa katika mchakato wa kumchagua mgombeaji wa urais wa upinzani, watamlazimisha kuwania kiti hicho nje ya muungano. Walisema Kalonzo alikuwa akimuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga katika chaguzi zilizopita na sasa ni wakati wa viongozi wengine wa upinzani kulipa fadhila hiyo. "Kalonzo hakuzaliwa kuwa mgombea mwenza katika kila uchaguzi. Alimuunga mkono Raila Odinga na sasa ni wakati wa wao kumuunga mkono. Tunamwambia Kalonzo kwamba hatutaki kusikia akiunga mkono mtu mwingine. Tunataka kumuona kwenye karatasi ya kura," alisema mmoja wa viongozi hao. Msimamo huo unajiri huku kukiwa na ushindani mkali ndani ya upinzani kuhusu nani atabeba bendera ya urais katika uchaguzi wa 2027. Miongoni mwa wanaotajwa ni Kalonzo, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i, ambaye pia anaongoza chama cha Jubilee. Naibu kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Cleophas Malala, amekuwa akimhimiza Kalonzo kuachana na azma yake ya urais na kumuunga mkono Sifuna. Bw Malala anasema Sifuna, mwenye umri wa miaka 45, anawakilisha kizazi kipya cha uongozi na anafaa kupewa nafasi ya kuongoza nchi, huku mwanasiasa mkongwe akichaguliwa kuwa mgombea mwenza. "Ninataka Kalonzo kuiga mfumo wa Obama na Biden. Tumuunge mkono Sifuna, mwenye umri wa miaka 45, kuwa mgombeaji wa urais wa upinzani, kisha tutafute mwanasiasa mkongwe awe mgombea mwenza wake," alisema. Hata hivyo, viongozi wa Wiper Pwani walisema Kalonzo ana uzoefu wa kutosha kuongoza nchi na hawatakubali azma yake ya urais kupuuzwa kwa kisingizio cha kudumisha umoja. Pia walidai kuwa baadhi ya watu wanaohusishwa na serikali wanatumia tofauti ndani ya upinzani kujaribu kuudhoofisha kabla ya uchaguzi wa 2027. Walisema umoja wa upinzani ni muhimu, lakini haupaswi kujengwa kwa kumdharau au kumtenga kiongozi yeyote anayetamani kuwania urais.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 10 hours ago

Wataka Mackenzie wa Shakahola anyongwe!

MHUBIRI aliyepatikana na hatia ya mauaji Shakahola, Paul Nthenge Mackenzie, ameiomba Mahakama imhurumie anaposubiri kuhukumiwa Ijumaa. Hayo yamejiri huku upande wa mashtaka ukitaka apewe hukumu ya kifo, na washtakiwa wenzake wafungwe maisha gerezani. Mahakama Kuu ilimpata na hatia ya mauaji ya watoto 190 na mtu mzima mmoja katika Msitu wa Shakahola, kati ya Januari 2021 na Septemba 2023. Mackenzie sasa amemweleza Jaji Diana Kavedza kuwa yeye na washitakiwa wenzake 28 pia ni waathiriwa wa mkasa huo, ambapo jumla ya watu 429 walifariki dunia wakiamini kuwa walikuwa wakijiandaa kwenda kumwona Yesu. "Kwa namna fulani, tulipoteza mali na watoto wetu. Jambo ambalo tunalijutia, na tunaomba mahakama hii ituhurumie na kulizingatia kabla ya kutupatia adhabu kali," alisema kupitia kwa wakili wake. Washtakiwa hao waliiomba mahakama izingatie hali zao binafsi na mabadiliko ambayo wanasema wamepitia wakiwa kizuizini. Walieleza kuwa vifo hivyo vilikuwa janga kubwa lisilopimika na kusisitiza kuwa hawakuwa na nia ya kupuuza maumivu ya familia zilizowapoteza wapendwa wao. Washtakiwa hao walisema majuto yao yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia mwenendo wao, kutambua makosa yaliyotendeka na utayari wao wa kubadilika. Walisisitiza kuwa adhabu inapaswa kuzingatia uzito wa makosa pamoja na wajibu wa kila mshukiwa na nafasi yake ya kurekebisha mwenendo wake. "Adhabu inayotoa nafasi ya mtu kujirekebisha si ishara ya udhaifu," walisema. Washitakiwa walisema wamekuwa kizuizini tangu 2023, ambapo wameshiriki katika mipango ya kidini na mafunzo mengine. Waliiomba mahakama izingatie pia ushiriki wao katika mipango ya kuwaondoa watu katika misimamo mikali ya kidini iliyofanyika kati ya Agosti 20 na 23, 2025, wakisema hatua hiyo inaonyesha utayari wao wa kubadilika na kurejea katika jamii. Pia, walieleza kuwa mitazamo yao ya kidini imebadilika tangu walipokamatwa, na kuiomba mahakama izingatie mabadiliko hayo pamoja na ripoti za tathmini kabla ya hukumu kutolewa. Waliomba mahakama izingatie huruma, haki na uwiano wa adhabu, huku ikitoa nafasi kwa haki inayolenga kurekebisha madhara yaliyotokea. "Tunapendekeza kifungo kisichozidi miaka 10, huku muda ambao washtakiwa wamekwishatumia kizuizini ukizingatiwa," alisema wakili wao. Hata hivyo, upande wa mashtaka uliomba washtakiwa wote wahukumiwe vifungo vya gerezani na washirikishwe katika mpango maalumu wa kurekebisha mwenendo wao, ukisema hawajaonyesha majuto. Kulingana na upande wa mashtaka, washtakiwa wote isipokuwa Enos Amanya Ngala wameendelea kukana mashtaka. Bw Ngala alikiri kushiriki katika mauaji hayo. "Wameendelea kukana mashtaka, kukataa kuwajibika kwa uhalifu huo na kuyatafsiri mashtaka dhidi yao kwa namna hasi. Kwa hakika, washtakiwa hawakuonyesha majuto wala kujutia matendo yao. Pia inashangaza kwamba bado wanashikilia mafundisho yaliyochangia vifo hivyo," upande wa mashtaka ulisema. Serikali ilipendekeza adhabu zitakazoakisi uzito na ukubwa wa makosa hayo. Kwa Bw Ngala, ilipendekeza kifungo cha miaka 11, muda aliokuwa ametumikia kizuizini tangu Aprili 2023 ukizingatiwa. Pia ilipendekeza afanyiwe mpango wa marekebisho ya tabia akiwa gerezani kwa kipindi cha kati ya miezi 24 na 30, huku ripoti za anavyoendelea zikiwasilishwa mara kwa mara ili kusaidia tathmini ya baadaye ya adhabu yake. Kwa Mackenzie, upande wa mashtaka uliomba mahakama itoe adhabu ya kifo, huku washtakiwa wengine 27 wakihukumiwa kifungo cha maisha gerezani. "Upande wa mashtaka unaunga mkono kutolewa kwa adhabu ya kifo kwa Mackenzie, kwa kuzingatia pia maelezo yake ya kujitetea , majuto yake na uwezekano wa kurekebisha mwenendo wake," alisema  Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma, Bw Jami Yamina. Upande wa mashtaka ulisema adhabu inapaswa kuzingatia malengo ya haki ya jinai, yakiwemo kuadhibu, kuzuia uhalifu wa aina hiyo, kulinda umma, kukemea uhalifu, kurekebisha madhara na kuwasaidia wahusika kubadilika. Pia ulipendekeza waathiriwa wagawanywe katika makundi matatu ya umri: watoto wenye umri wa hadi miaka saba, wale wa miaka minane hadi 14, na walio na umri wa miaka 15 hadi 18. Aidha, uliwasilisha pendekezo la Kituo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Ugaidi (NCTC), kilichopendekeza washitakiwa washiriki kwa hiari katika programu za marekebisho ya misimamo mikali na kupewa mafundisho mbadala ili kuwawezesha kurejea katika jamii. Mwezi uliopita, Mahakama Kuu ilimpata Makenzie na wenzake 28 na hatia ya kuwaua watoto 190 na mtu mzima mmoja katika msitu wa Shakahola. Watu hao watapewa kifungo chao Novemba  6.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Visa vya wahalifu kushambulia polisi, wanajeshi zazua hofu

MATUKIO mawili tofauti ya mapigano kati ya maafisa wa usalama na washukiwa wa uhalifu yamezua wasiwasi kuhusu usalama wa polisi na wanajeshi, huku bunduki  zikiendelea kuibwa na magenge ya wahalifu. Katika tukio la kwanza, afisa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) alipigwa risasi na kuuawa na polisi katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, baada ya makabiliano yaliyotokea Jumapili, Novemba 1. Ripoti ya polisi inaonyesha kuwa maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Kahawa Sukari walikuwa kwenye doria mwendo wa saa saba usiku walipopokea taarifa kutoka kwa mwananchi kuhusu wanaume wawili waliokuwa na silaha na kutishia wakazi wa Covo, karibu na Magunas. Polisi waliwafuata washukiwa hao na kuwaamuru wasimame, lakini mmoja wao anadaiwa kutoa bastola na kuwafyatulia risasi maafisa hao, waliolazimika kujibu mashambulizi. "Mshukiwa aliyetoa bunduki alipigwa risasi kifuani na mkono wa kulia. Alikimbizwa katika Hospitali ya Ruiru Level 4 akiwa katika hali mahututi lakini baadaye akafariki akipokea matibabu," ilisema ripoti hiyo. Polisi walipata bastola aina ya Jericho iliyokuwa na risasi 12 pamoja na maganda mawili ya risasi zilizokuwa zimefyatuliwa. Pia walipata kitambulisho cha KDF kilichokuwa na jina la marehemu, Munene Antony, 33. Mshukiwa aliyenusurika anadaiwa kuwaambia wachunguzi kuwa bastola hiyo ilikuwa ya kakake ambaye ni polisi. Uchunguzi unaendelea kubaini umiliki wa silaha hiyo. Wakati huohuo, maafisa wawili wa polisi kutoka Kituo cha Ruai walijeruhiwa vibaya Jumatatu usiku baada ya kushambuliwa na genge la wanaume waliokuwa wameabiri pikipiki. Washambuliaji hao waliiba bunduki mbili aina ya AK-47, kila moja ikiwa na risasi 30. Maafisa hao, Corporal John Maritim na Corporal Felistus Tuitoek, walipata majeraha  kichwani na mikononi baada ya kushambuliwa kwa kitu chenye makali. Walipata matibabu katika Hospitali ya Reale, Utawala, huku polisi wakianzisha msako wa kuwakamata washukiwa na kurejesha silaha hizo. Tukio hilo linaongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa bunduki hizo kutumiwa katika uhalifu mwingine au mashambulizi dhidi ya raia na maafisa wa usalama. Mnamo Oktoba 26, genge lilishambulia maafisa waliokuwa wakilinda kituo cha ukusanyaji ushuru  Kaunti ya Mombasa, Likoni, na kumuua afisa mmoja wa kaunti huku wengine watatu wakijeruhiwa. Washambuliaji waliiba bunduki ya AK-47 kutoka kwa afisa wa utawala, ambayo baadaye ilitumika kumpiga risasi afisa huyo wa kaunti. Mnamo Machi, genge jingine lilishambulia polisi aliyekuwa akilinda eneo la viwanda la Bonje, Jomvu, na kumuibia bunduki ya AK-47 pamoja na simu. Matukio hayo yanajiri huku kukiwa na ripoti za mivutano kati ya polisi na wanajeshi. mnamo Septemba, maafisa hao walikabiliana katika kizuizi cha barabarani karibu na Chuo Kikuu cha Turkana, Lodwar, na baadaye katika Kituo cha Polisi cha Lodwar. Tukio jingine la mzozo kati ya polisi na wanajeshi liliripotiwa katika kivuko cha feri cha Likoni, Mombasa, mwezi huohuo. Matukio haya yanaibua maswali kuhusu ushirikiano kati ya idara za usalama, nidhamu kazini na silaha za serikali kuangukia mikononi mwa wahalifu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 12 hours ago

Wanawake Kenya sasa wanataka watoto wawili -utafiti

IDADI ya watoto ambao mwanamke huzaa nchini Kenya inatofautiana pakubwa kulingana na anapoishi, kiwango chake cha elimu na hali yake ya kiuchumi, huku wanawake wengi wakisema wangependa kupata watoto wawili pekee. Ripoti mpya ya Utafiti wa Afya  kuhusu Idadi ya Watu Kenya (KDHS) ya mwaka 2025–2026 inaonyesha kuwa mwanamke wa kaunti ya Embu huzaa wastani wa watoto 2.2 katika maisha yake, ikilinganishwa na watoto 6.8 kwa mwanamke wa Mandera. Tofauti hiyo inaonyesha pengo kubwa la uzazi nchini, licha ya Kenya kupiga hatua katika kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na kila mwanamke. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha uzazi nchini kimeshuka hadi watoto 3.1 kwa kila mwanamke, kutoka 3.4 mwaka 2022 na 6.7 mwaka 1988–89. Hata hivyo, idadi ya watoto imeanza kupungua, huku matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi na mahitaji ambayo hayajatimizwa yakiongezeka. Wanawake wengi walisema wangependa kupata watoto wawili, lakini wastani wa kitaifa bado ni 3.1. Hali ni tofauti katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya, ambako wanawake wanapata watoto wengi zaidi na matumizi ya njia za kisasa za kisasa za kupanga uzazi ni madogo mno. Mandera inaongoza kwa kiwango cha juu kwa watoto 6.8 kwa kila mwanamke, ikifuatiwa na Wajir (5.8), Tana River (5.7), Turkana (5.6), Garissa (5.3), West Pokot (5.1) na Samburu (5.0). Kwa upande mwingine, Embu ina kiwango cha chini zaidi cha watoto 2.2, ikifuatiwa na Kiambu na Mombasa zenye 2.3 kila moja. Kericho na Nairobi zina kiwango cha 2.6. Elimu pia inaonekana kuwa na mchango mkubwa katika idadi ya watoto ambao mwanamke huzaa. Wanawake ambao hawajasoma wanapata wastani wa watoto 5.4, ikilinganishwa na 3.6 kwa walio na elimu ya msingi, 3.0 kwa wenye elimu ya sekondari na 2.7 kwa walioendelea na masomo baada ya sekondari. Hali hiyo pia inajitokeza katika hali ya kiuchumi. Wanawake kutoka familia maskini zaidi wana wastani wa watoto 4.5, huku wale kutoka familia tajiri zaidi wakiwa na 2.3. Ripoti inaonyesha pia kuwa wanawake wameanza kupata watoto wakiwa na umri mkubwa zaidi. Hapo awali, wanawake wengi walikuwa wakijifungua zaidi wakiwa na umri wa miaka 20 hadi 24, lakini sasa kundi linaloongoza ni la miaka 25 hadi 29. Vilevile, mimba miongoni mwa wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 zimepungua. Asilimia ya wasichana katika kundi hilo ambao wamewahi kupata mimba imeshuka kutoka 14.8 mwaka 2022 hadi 11.9 sasa. Serikali inalenga kuongeza matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi hadi asilimia 64 ifikapo 2030 na kupunguza mahitaji ambayo hayajatimizwa hadi asilimia 10. Mandera ina kiwango cha chini zaidi cha matumizi, chini ya asilimia moja, huku Wajir ikiwa na asilimia moja na Garissa asilimia tano. Katika kaunti za Nyamira, Nandi na Bomet, wanawake wanapata watoto 1.1 zaidi ya idadi wanayotamani. Hali hiyo inaonyesha kuwa kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa kutahitaji kuboresha upatikanaji wa huduma za kupanga uzazi na elimu kuhusu afya ya uzazi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Mibabe saba kupimana nguvu kuwania ugavana Nairobi

KUTOKA kwa rubani, wafanyabiashara, wabunge hadi viongozi wa kidini, uchaguzi wa ugavana Nairobi mwaka wa 2027 unatarajiwa kuwa na ushindani mkali huku wanasiasa sita wakimezea mate  usukani wa kaunti hiyo yenye ushawishi mkubwa kisiasa na kiuchumi. Gavana wa sasa Johnson Sakaja, Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri na Mbunge wa Makadara George Aladwa wanawania tiketi ya chama cha ODM, huku Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya na aliyekuwa Mbunge wa Starehe Margaret Wanjiru wakitafuta tiketi za vyama tofauti. Aliyekuwa Katibu katika Wizara Irungu Nyakera na mfanyabiashara Agnes Kagure, ambao awali walikuwa wameonyesha nia ya kuwania kiti hicho, wameonekana kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho. Mashindano hayo yalipamba moto Jumatatu baada ya Bw Sakaja kuhama chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na kujiunga rasmi na ODM, akitangaza azma ya kuwania muhula wa pili kupitia chama hicho. Hatua hiyo imezua maswali kuhusu hatma ya wagombeaji wengine wa ODM ambao tayari walikuwa wameonyesha nia ya kuwania ugavana. Bw Sakaja alipokelewa katika makao makuu ya ODM, Chungwa House, na viongozi wa chama hicho. Alisema kujiunga kwake hakukuwa mbinu ya kisiasa bali kurejea katika chama alichokuwa akihusishwa nacho. "Baba (Raila Odinga) ndiye aliyeniambia nijiunge na ODM," alisema, akirejelea uhusiano wake na mwanzilishi wa chama hicho aliyefariki. Alisema anataka muhula mwingine ili kuendeleza huduma kwa wananchi, akisisitiza kuwa uongozi unapaswa kupimwa kwa jinsi maisha yanavyobadilika badala ya ushindi wa uchaguzi pekee. Hata hivyo, Mwenyekiti wa ODM Nairobi George Aladwa amesema hatakubali wageni kupewa tiketi bila kupitia mchujo wa kidemokrasia. "Safari ya kuongoza Nairobi lazima iongozwe na matakwa ya wananchi, haki na misingi ya demokrasia. Nimejizatiti katika maono yetu ya pamoja. Sauti ya wananchi lazima isikike," alisema. Bw Karauri, rubani wa zamani wa Kenya Airways na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa SportPesa, anasema uzoefu wake katika biashara, usafiri wa anga na siasa za eneo bunge unampa uwezo wa kusimamia Nairobi. Alisema alifanya kazi Kenya Airways kwa miaka 11, mitano akiwa nahodha wa ndege, na amejifunza umuhimu wa uwajibikaji na mipango. Ameahidi kuboresha ukusanyaji wa mapato, usafi wa jiji, mabomba  ya maji na barabara bila kuongeza ushuru. Pia anataka kukagua majengo ili kubaini yale yasiyo salama na kuhakikisha hospitali za kaunti zina dawa za kutosha. Bw Karauri amemkosoa Sakaja, akisema kuhamia ODM hakutafuta kumbukumbu ya changamoto za uongozi wake, zikiwemo mafuriko, taka na majengo kuporomoka. Kwa upande wake, Bw Gakuya anatumia uungwaji mkono wa kiongozi wa DCP na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuimarisha kampeni zake. Ameahidi kubadilisha jaa la Dandora, kuunda nafasi za ajira na kurejesha hadhi ya Nairobi. Bw Owino amechagua kuwania kupitia Mwananchi Party huku akiendelea kushirikiana na vuguvugu la Linda Mwananchi linalomuunga mkono  Seneta Edwin Sifuna kuwania urais. Sifuna tayari amemtaja Owino kama mgombeaji  anayempendelea katika ugavana wa Nairobi. Naye Bi Wanjiru, ambaye amepata chama cha Kenya Moja Movement, amesema hatasalimisha azma yake ya ugavana katika mazungumzo ya miungano. Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema ODM inakabiliwa na changamoto ya kuamua kati ya kumpa kipaumbele gavana aliye madarakani, uaminifu wa wanachama wa muda mrefu au mgombeaji anayeweza kushinda. Anasema Sakaja atapimwa kutokana na rekodi ya muhula wake wa kwanza, Aladwa atalazimika kuthibitisha umaarufu wake nje ya chama, huku Karauri akionyesha kuwa uzoefu wa biashara unaweza kutumika kusimamia kaunti. Owino naye atalazimika kuthibitisha kuwa umaarufu wake unaenea nje ya Embakasi Mashariki, huku Gakuya akihitaji kupanua uungwaji mkono wa Gachagua na Wanjiru kujenga mtandao imara katika jiji lote.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Gachagua ajenga huku akibomoa upinzani

KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP) Rigathi Gachagua anadai analenga kuunganisha viongozi wa upinzani chini ya mgombeaji mmoja wa urais katika uchaguzi wa 2027, lakini matamshi yake makali dhidi ya washirika wake yameibua wasiwasi. Bw Gachagua anaendelea kuwakosoa baadhi ya vinara wa upinzani akiwalaumu kwa kutofanya bidii kujenga umaarufu, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu atakayekabidhiwa urais bila kuungwa mkono na wapigakura. Katika mkutano wake na viongozi nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, Jumanne, kiongozi huyo wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP) alimshambulia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i miongoni mwa wanaomkosoa, akisema baadhi ya washirika wake hawataki kuzungumzia idadi ya kura wanazoweza kuweka mezani Gachagua alimpiga vijembe Muturi, ambaye anatoka eneo la Mbeere, akisema alishindwa hata kuvutia wapigakura katika kituo chake cha kupiga kura wakati wa uchaguzi mdogo wa MCA. "Unasema unataka kutusaidia kumuondoa Kasongo, lakini katika uchaguzi wa MCA kituoni kwako uliweza kupata watu 35 pekee, huku Kasongo akipata 238. Unataka kumfundisha Riggy G nini?" alisema. Aliongeza kuwa hatakubali kufanya kampeni na kuvutia kura ili kuzikabidhi kwa viongozi wengine bila wao kujituma. "Sitasaka kura nikuletee wewe na mke wako," alisema, akiwataka wenzake kutoka kwenye hoteli na kuanza kuwashawishi wananchi. Gachagua pia alifichua kuwa amekuwa akigawa idadi ya kura kwa washirika wake, akisema alimwambia Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alenge kura milioni tano, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka milioni tatu na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa milioni moja. Kauli hizo zimezua mjadala kuhusu nafasi ya viongozi wengine katika mazungumzo ya kuunda muungano wa upinzani, hasa baada ya Muturi kumshutumu Gachagua kwa kutumia vitisho badala ya kujenga ushirikiano wenye kuheshimiana. Matiang'i naye amekosoa pendekezo la Gachagua la kuunganisha maeneo ya Mlima Kenya, Ukambani na Magharibi, akisema siasa zinazotegemea idadi ya watu wa maeneo fulani zinaweza kuvunja umoja wa upinzani na kuua ndoto ya muungano dhidi ya Rais Ruto. Alionya kuhusu kile alichokitaja kama kiburi cha walio wengi kinachoweza kuwatenga viongozi wengine na kufanya mazungumzo ya kupata mgombeaji mmoja kuwa magumu. Hata hivyo, Gachagua amesisitiza kuwa hana kiburi, bali anasema ukweli kuhusu siasa za uchaguzi. "Ninapowaambia tuamke tufanye kazi, wanasema ninawanyanyasa. Mimi si mwenye kiburi, nasema ukweli," alisema. Katika jitihada za kuimarisha muungano huo, jana Gachagua alikutana na aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu nyumbani kwake Wamunyoro. Ngilu alihusika katika kuunda muungano wa NARC uliomuingiza madarakani marehemu Mwai Kibaki mwaka 2002 na kumaliza utawala wa KANU. Gachagua alisema alijifunza kutoka kwa Ngilu kuhusu mikakati iliyotumiwa kuunganisha vyama vya upinzani na kuhakikisha vinaunga mkono mgombeaji mmoja. Haya yanajiri baada ya Gachagua kukutana na Kalonzo na Sifuna katika mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kisiasa. Ameashiria kuwa muungano unaojengwa unaweza kujumuisha viongozi hao pamoja na Eugene Wamalwa. Hata hivyo, hii inaweza kuchukuliwa kwa ishara ya kutokuwa na nia njema na vinara wengine akiwemo Martha Karua, Ndindi Nyoro na Muturi ambao wamekuwa wakihubiri haja ya upinzani kuunga ili kuwa rahisi kumshinda Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao. Kulingana na mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, kauli za Gachagua ni hatari kwa upinzani chini ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Anashangaa kwa nini naibu rais huyo wa zamani anatoa kauli tofauti na msimamo wake wa awali kwamba upinzani unaweza kushinda tu iwapo utaungana na kuteua mmoja wao kuwa mgombea urais wa pamoja. "Kwa maoni yangu, Gachagua anajenga akibomoa. Ukifuatilia kabla ya Sifuna kupata umaarufu, hakuwa akimchangamkia. Sasa kwa vile amevuna, anamleta karibu huku akiwabeza baadhi ya vinara aliokuwa akitangamana nao awali," asema Dkt Gichuki na kuongeza hii ni hatari. "Kwa sasa, upinzani unapaswa kuwa ukihubiri umoja na kutoka mwelekeo kwa wafuasi wao lakini inaonekana Gachagua hayuko tayari kwa hili. Kwa lugha ya mtaa, anachafua bahari wakati ambao yeye na wenzake wanafaa kuwa wakijiandaa kuvua," akasema. Gachagua anasisitiza kuwa tofauti za ndani hazitazuia upinzani kusimamisha mgombeaji mmoja dhidi ya Rais William Ruto mwaka 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 03 Nov 2026 13:10:23

Aliyekuwa mwanasheria mkuu Paul Kihara Kariuki aaga dunia

ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa Serikali Paul Kihara Kariuki amefariki dunia, akiacha nyuma historia ya zaidi ya miaka 40 katika taaluma ya sheria na utumishi wa umma. Bw Kariuki, ambaye alihudumu kama Mwanasheria Mkuu kati ya 2018 na 2022 chini ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, pia aliwahi kuwa Rais wa Mahakama ya Rufaa kwa miaka mitano. Jaji Mkuu Martha Koome alithibitisha kifo chake Jumanne na kumtaja kama mwanasheria mahiri, kiongozi wa mahakama na mtumishi wa umma aliyechangia pakubwa katika kuimarisha taasisi za sheria nchini. Rais William Ruto alisema mchango wake haukuishia mahakamani, bali pia ulijumuisha kuanzisha Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama (Judiciary Training Institute), iliyosaidia kuwapa majaji na maafisa wengine wa mahakama mafunzo ya kitaalamu. Bw Kenyatta pia alimwomboleza, akisema uongozi wake katika Mahakama ya Rufaa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu uliacha alama muhimu katika taasisi za serikali. Hata hivyo, kipindi chake kama Mwanasheria Mkuu kilikumbwa na mvutano mkubwa kati ya serikali na mahakama kuhusu uteuzi wa majaji 41 waliopendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC). Uhuru alikataa kuwateua wote, akidai alikuwa amepokea taarifa za kijasusi kuhusu masuala ya uadilifu ya baadhi yao. Mzozo huo ulisababisha Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kutishia kumuondoa katika orodha ya mawakili kwa madai ya utovu wa nidhamu wa kitaaluma. Hata hivyo, Kariuki alipata amri ya mahakama iliyozuia hatua hiyo kwa muda. Pia alitetea serikali kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI), ambao hatimaye uliharamishwa na Mahakama ya Juu. Kariuki alizaliwa Kiambu mwaka 1954 na kuhitimu shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka 1977. Aliwahi kuwa jaji wa Mahakama Kuu kuanzia 2003, kabla ya kuwa mkurugenzi wa kwanza wa Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama mwaka 2009. Mwaka 2013 alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Mahakama ya Rufaa chini ya Katiba ya 2010. Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga alimuomboleza kama mwanasheria aliyejitolea katika utumishi wa umma na kuimarisha utawala wa sheria.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 03 Nov 2026 12:57:26

Majonzi mtahiniwa wa KCSE akifariki ghafla baada ya karatasi mbili

FAMILIA  moja katika kijiji cha Kanyaliech, eneo la Koyugi, Kaunti ya Homa Bay, imezama kwenye majonzi baada ya mwanafunzi wa Kidato cha Nne kufariki saa chache tu baada ya kufanya karatasi mbili za kwanza cha mtihani wa KCSE. Congestina Achieng, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Alaro Central, aliaga dunia Jumatatu jioni baada ya kuugua ghafla akilalamikia maumivu makali ya kifua. Kifo chake kiliwashtua wazazi, walimu na wakazi wa eneo hilo, kwani alikuwa ameanza safari ya mtihani wa kitaifa akiwa na matumaini ya kutimiza ndoto zake. Babake, David Ogweno, alisema alipokea simu ya dharura kutoka kwa mkuu wa shule akimtaka afike kumchukua mwanawe baada ya kumaliza karatasi mbili za kwanza. "Afya yake ilizorota haraka. Tulimkimbiza katika Hospitali ya Tamary, lakini kwa bahati mbaya aliaga dunia," alisema Bw Ogweno. Alisema familia imepitia changamoto za kifedha kumwezesha Congestina na watoto wengine kupata elimu. Bw Ogweno, ambaye hufanya kazi za vibarua, alisema mwanawe alikuwa na ndoto ya kuwa wakili ili kusaidia familia kujikwamua kutoka katika umaskini. Mama yake, Pamela Atieno, alisema mwanawe alikuwa akiumwa tangu wiki jana, lakini alitarajia kupata nafuu na kufanya mtihani wa KCSE. "Alilalamikia maumivu ya kifua, nikamnunulia dawa za dukani ili kupunguza maumivu na aweze kufanya mtihani. Baadaye nilipigiwa simu na kuambiwa hangeweza kuendelea," alisema. Walimu wake, Isaiah Opere na Austine Achina, walimtaja kama mwanafunzi mwenye nidhamu, mnyenyekevu na aliyejituma katika masomo. Bw Opere alisema Congestina alikuwa mtulivu na mwenye tabia nzuri, ambaye hakuwahi kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu. Kifo chake kimezima ndoto za msichana aliyetarajia kutumia elimu kujenga maisha bora, na kuacha familia yake ikiwa na majonzi makubwa.

read more