taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 06:55:25
Ruto afichua dili kali ya kufaidi vijana
RAIS William Ruto amewaonya vijana dhidi ya kuruhusu wanasiasa kuwatumia kama wanablogu au wahuni wa kuvuruga mikutano, akitangaza mpango wa nguzo tano unaolenga kuwapa ajira na kuwawezesha kiuchumi. Akizungumza siku ya pili ya ziara yake katika eneo la Magharibi mwa Kenya Ijumaa, Rais alisema vijana wanapaswa kujikita katika kutafuta fursa za kujipatia riziki badala ya kutumiwa katika mapambano ya kisiasa. Alisema mpango wake unalenga kuwawezesha vijana kupitia elimu, mafunzo ya kazi, mitaji, zabuni za serikali na ajira katika sekta mbalimbali. Nguzo ya kwanza ni mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo vikuu, ambao alisema utahakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo bila kukatizwa na ukosefu wa karo. Pili, serikali inalenga kuwaingiza zaidi ya vijana 100,000 katika mafunzo ya kazi, ambapo kila mmoja atalipwa Sh25,000 kabla ya kupata ajira za kudumu. Kupitia mpango wa Nyota, serikali tayari imetoa Sh50,000 kwa kila mmoja wa vijana zaidi ya 130,000 wenye ujuzi lakini wasio na ajira ili kuanzisha biashara. Ruto alisema serikali inatafuta vijana wengine 200,000 watakaonufaika na mpango huo. Nguzo ya nne ni kuwaunganisha vijana na zabuni za serikali kupitia mpango wa Nyota-AGPO. Vijana watasajiliwa, kupewa mafunzo ya wiki 10 na kusaidiwa kusajili kampuni zao bila malipo. Rais alisema serikali italipa bidhaa zitakazowasilishwa ndani ya siku 60. Nguzo ya tano ni ajira kupitia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, masoko, mabweni, vituo vya teknolojia na ajira za kidijitali. Alisema vijana 700,000 tayari wamepata ajira kupitia usafirishaji wa wafanyakazi nje ya nchi. Ruto pia alishambulia upinzani, akiwataka kuacha kuingilia shughuli za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inapojiandaa kwa uchaguzi wa Agosti 2027. Upinzani unataka mageuzi matano ya uchaguzi yafanywe kabla ya uchaguzi huo, yakiwemo ukaguzi wa sajili ya wapigakura na mabadiliko ya teknolojia ya uchaguzi. Rais alisema IEBC inafaa kupewa nafasi ya kufanya kazi yake na kuwataka wapinzani wajipange kwa uchaguzi badala ya kuamua vifaa vitakavyotumiwa na tume hiyo. Katika ziara hiyo, alikagua miradi ya Sio Port na soko la Sio Port ESP. Alisema serikali imetenga Sh800 milioni kwa ujenzi wa gati hilo na Sh400 milioni kwa upanuzi wake, kabla ya kufunguliwa rasmi Februari mwaka ujao. Alisema pia kituo cha mpaka cha Mulwanda kitakamilika ndani ya miezi minne, huku soko likitarajiwa kukamilika baada ya miezi miwili. Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi alisema serikali imetenga Sh800 bilioni kwa elimu, kutoka Sh400 bilioni mwaka 2022, akitaja hatua hiyo kuwa uwekezaji kwa vijana na vizazi vijavyo.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 52 minutes ago
Upinzani wapatia Ruto silaha kuwaponda
KUONDOKA kwa vinara wakuu wa upinzani katika mkutano na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumempa Rais William Ruto nafasi nyingine ya kuwashambulia kisiasa, akitumia mgogoro huo kuonyesha kuwa wapinzani hawana umoja, mgombeaji wala ajenda ya pamoja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Vinara hao, wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, waliondoka kwenye mkutano wa Novemba 19 baada ya kupinga utaratibu wa majadiliano na mada ambazo IEBC ilikuwa imepanga kuwasilisha. Walioandamana nao ni aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, miongoni mwa wengine. Hata hivyo, hatua hiyo imegeuza mjadala kutoka kwa madai yao kuhusu maandalizi ya uchaguzi na kuuelekeza kwenye uwezo wa upinzani kuendesha mazungumzo na kuunda mkakati mmoja wa kumng'oa Ruto mamlakani. Rais hakupoteza muda kutumia fursa hiyo. Akiwa katika ziara yake ya Magharibi mwa Kenya, aliwashambulia wapinzani akiwataka waache kuilaumu IEBC na badala yake wajipange kushindana naye katika uchaguzi. 'IEBC haina kura, kura ziko kwa wananchi,' alisema Ruto, akiwakosoa viongozi hao kwa kuonekana kuhusisha tume na mizozo yao ya kisiasa. Pia, aliwataka wapinzani waache kuzunguka wakilalamika kuhusu tume hiyo na badala yake waamue watakayemsimamisha kugombea urais, sera watakazotumia na ajenda watakayowasilisha kwa wananchi. Kwa Ruto, kuondoka kwa wapinzani mkutanoni ni fursa ya kuendeleza simulizi kwamba washindani wake hawajajiandaa kwa uchaguzi wa 2027 na huenda wanatafuta mtu wa kulaumu iwapo watashindwa. Lakini Kalonzo na Gachagua walisisitiza kuwa hawakuwa tayari kuhusishwa na mchakato ambao, kwa maoni yao, haukuwa na dhamira ya kushughulikia masuala muhimu ya uchaguzi. Gachagua alisema upinzani ulikuwa umeomba IEBC kuunda timu ya kiufundi Januari 28, 2026 ili kujadili maandalizi ya uchaguzi, lakini madai yao hayakushughulikiwa licha ya kuwasilisha barua na mawasiliano kadhaa. Alisema upinzani hautakubali Wakenya kuingia katika uchaguzi ambao uaminifu wake unatiliwa shaka. 'Tunakataa kuwaruhusu Wakenya kuingia katika mchakato wa uchaguzi uliopangwa kuibiwa bila wao kujua,' alisema. Kalonzo alisema walihudhuria mkutano huo kwa nia njema lakini hawakuridhishwa na namna tume ilivyokuwa ikiendesha mashauriano. 'Tulikuja IEBC leo kwa nia njema na tulitarajia nia hiyo hiyo kutoka kwao. Nia njema huonyeshwa kwa vitendo: tume huru, isiyopendelea upande wowote na iliyojiandaa. Leo hatukupata hayo. Ndiyo maana tumeondoka,' alisema. Kwa upande wake, Maraga alisema hawakutaka kwenda kusikiliza hotuba za maafisa wa IEBC kuhusu mipango yao bila kupata nafasi ya kujadili wasiwasi wao. 'Tunataka kushirikiana na IEBC, hatutaki kwenda kufundishwa. Ndiyo maana tuliondoka,' alisema. Upinzani unataka ukaguzi huru wa sajili ya wapigakura ili kuondoa majina ya watu waliofariki, waliosajiliwa mara mbili na wasiostahili kupiga kura. Pia unataka mabadiliko ya mfumo wa kutuma na kujumlisha matokeo ya urais, ukipendekeza kila eneo bunge kati ya 290 liwe na sava huru za matokeo yanayoweza kufikiwa na vyama, wagombeaji na vyombo vya habari. Unataka pia kuondolewa kwa kituo kikuu cha kujumlishia matokeo ya urais Bomas of Kenya, majaribio ya kupiga kura kwa njia ya kielektroniki kwa Wakenya wanaoishi ughaibuni na kupeperushwa moja kwa moja kwa shughuli za kupiga, kuhesabu na kutangaza kura. Haya ni masuala muhimu yanayohitaji majibu ya wazi kutoka kwa IEBC. Hata hivyo, kuondoka kabla ya kusikiliza maelezo ya tume kumeifanya serikali kupata nafasi ya kuhoji dhamira ya upinzani. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Edung Ethekon alisema ilihuzunisha kuona baadhi ya viongozi wakiondoka kabla ya majadiliano ya kina kuanza. 'Kuondoka kwenye mazungumzo kabla ya majadiliano ya kina kuanza hakusaidii kutatua masuala ya uchaguzi. Kunawanyima wahusika wote nafasi ya kubadilishana mawazo, kufafanua misimamo na kujenga mwafaka,' alisema. Alisema viongozi hao walikosa fursa ya kusikiliza maelezo kuhusu kiwango cha maandalizi ya uchaguzi, hatua zilizopigwa na changamoto zinazokabili tume. Ethekon aliwahimiza viongozi kuwasilisha mapendekezo yao rasmi na kuendelea kushiriki mashauriano badala ya kujiondoa. Gavana wa Kisii Simba Arati pia alikosoa hatua ya upinzani, akisema huenda viongozi hao walitaka kujenga taswira kwamba wametengwa ili watakaposhindwa uchaguzi wawe na sababu ya kupinga matokeo mahakamani. Kwa upande wake, mwenyekiti wa UDA Cecily Mbarire alihoji kwa nini upinzani uliondoka badala ya kuwasilisha hoja zake ndani ya mkutano. Wachambuzi wa siasa wanasema changamoto kubwa kwa Kalonzo, Gachagua, Sifuna, Karua na wenzao sasa ni kuhakikisha madai yao kuhusu uadilifu wa uchaguzi hayafunikwi na mzozo wa kisiasa walioanzisha. 'Wanapaswa pia kuonyesha kuwa wanaweza kukubaliana kuhusu ajenda ya pamoja na mgombeaji wa urais, masuala ambayo Ruto amekuwa akiyatumia kuhoji uwezo wao wa kuunda serikali,' asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki. Vinginevyo, asema, kwa kuondoka mkutanoni, huenda wameingia katika mtego wa kisiasa wa Ruto, wakimpa nafasi ya kuendelea kuwaponda kwa udhaifu wao huku maswali kuhusu maandalizi ya uchaguzi yakisalia bila majibu ya kutosha.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
Hofu ya Ruto kuhusu usalama wa nchi 2027 ikikaribia
SERIKALI ya Rais William Ruto imeibua wasiwasi kuhusu usalama wa nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, ikionya kuwa kuongezeka kwa magenge ya wahalifu, joto la kisiasa, siasa za kikabila na matamshi ya uchochezi kunaweza kufanya Kenya kuwa katika hatari ya machafuko. Katika ripoti ya hali ya usalama nchini iliyowasilishwa Bungeni na Rais Ruto wakati wa hotuba yake ya Mustakabali wa Taifa, serikali inasema ushindani wa kisiasa unaozidi kupamba moto unaweza kudhoofisha umoja wa kitaifa na kuhatarisha amani kabla ya uchaguzi. Ripoti hiyo inayohusu kipindi cha Septemba 2025 hadi Agosti 31, 2026, inaeleza kuwa mwelekeo wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027 ndio wasiwasi mkubwa zaidi kwa idara za usalama. Serikali inasema mchujo wa vyama, mapitio ya mipaka ya maeneo ya uchaguzi na usajili wa wapigakura ni baadhi ya hatua zinazoweza kuchochea ushindani mkali na hata vurugu. "Safari ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 ndiyo wasiwasi mkuu. Kura za mchujo za vyama, mapitio ya mipaka na usajili wa wapigakura vitaongeza ushindani wa kisiasa, huku hali katika kipindi hiki ikionyesha hatari kubwa ya vurugu zinazochochewa katika hatua hizo," inasema ripoti hiyo. Kwa mujibu wa serikali, kipindi hiki hushuhudia mgawanyiko mkubwa wa kisiasa, kutovumiliana kati ya mirengo hasimu na juhudi za wanasiasa kuchochea wafuasi dhidi ya wapinzani wao. Ripoti hiyo pia inadai kuwa baadhi ya wanasiasa wametumia vurugu katika maeneo mbalimbali kujionyesha kuwa na nguvu na kuwatisha washindani wao. Serikali inaonya kuwa miungano ya kisiasa inayojengwa kwa misingi ya ukabila pamoja na ushindani wa kikanda inaweza kugawa nchi na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa. Matamshi ya chuki nayo yametajwa kuwa tishio kubwa, hasa kutokana na uwezo wake wa kuchochea migawanyiko ya kikabila, ubaguzi na vurugu.Serik ali inakumbusha kuwa matamshi ya uchochezi yalichangia pakubwa machafuko yaliyofuatia uchaguzi wa 2007, yaliyosababisha vifo, watu kuhama makazi yao na mali kuharibiwa. Mwezi uliopita, Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) ilionya kuwa matamshi ya chuki yanaongezeka kuelekea uchaguzi wa 2027, hasa kwenye mitandao ya kijamii. Wiki iliyopita, maaskofu wa Kanisa Katoliki pia waliwataka wanasiasa kudhibiti ndimi zao, wakionya kuwa matamshi ya uchochezi yanaweza kutumbukizwa nchi katika machafuko. Ingawa ripoti inasema hali ya usalama nchini imeendelea kuwa tulivu kwa jumla, inataja changamoto nyingine zinazohitaji kushughulikiwa, zikiwemo ugaidi, itikadi kali za kidini, ulanguzi wa dawa za kulevya, biashara ya silaha haramu, uhalifu wa kimtandao, wizi wa mifugo na biashara ya bidhaa bandia. Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kusambaza taarifa za uongo, kuandikisha vijana katika magenge ya wahalifu na kuratibu maandamano pia kumetajwa kuwa tishio. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, shughuli hizo zilichangia vifo vya watu 17, uharibifu wa mali na kutatiza shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, visa vya uhalifu viliongezeka kutoka 97,366 katika kipindi cha 2024/2025 hadi 97,946 kati ya Septemba 2025 na Agosti 2026, ongezeko la visa 580. Serikali inasema ongezeko la magenge ya wahalifu limekuwa likitatiza juhudi za kudumisha usalama, huku makundi hayo yakitumia vitisho, vurugu na kuwashawishi vijana walio katika mazingira magumu kujiunga na shughuli za uhalifu. Ripoti inasema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, changamoto za kiuchumi na migogoro ya kijamii ni baadhi ya sababu zinazochochea ukuaji wa magenge hayo. Hata hivyo, kinachotia wasiwasi zaidi ni madai kuwa baadhi ya makundi hayo yanatumiwa na wanasiasa kuvuruga mikutano ya wapinzani, kuwatisha wananchi, kuharibu mali na kuchochea mapigano. Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alikabiliwa na maswali magumu kutoka kwa wabunge mwezi huu kuhusu kuongezeka kwa utamaduni wa kutumia wahuni katika shughuli za kisiasa. Bw Murkomen alijibu kuwa baadhi ya magenge hayo yanafadhiliwa na wanasiasa, akidai kuwa viongozi wanaohusika hukalia viti vyao Bungeni na katika nyadhifa za juu za kisiasa huku wakitumia ushawishi wao kuzuia polisi kuchukua hatua. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) nayo imeonya kuwa haitawavumilia wanasiasa watakaohusishwa na kufadhili au kutumia magenge hayo wakati wa uchaguzi. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alisema tume hiyo ina kamati inayosimamia utekelezaji wa kanuni za maadili ya uchaguzi na itachukua hatua dhidi ya wanaokiuka masharti hayo. Alisema wanasiasa watakaopatikana na ushahidi wa kufadhili, kuhifadhi au kuwezesha magenge ya wahalifu wanaweza kutozwa faini au hata kuondolewa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi. Katika kipindi kinachochunguzwa, vyombo vya usalama vilirekodi kukamatwa kwa washukiwa 1,316 wanaohusishwa na magenge hayo, ikilinganishwa na 602 katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia. Ongezeko hilo la watu 714, kwa mujibu wa serikali, linaonyesha kuimarishwa kwa operesheni za usalama lakini pia kuibuka na kupanuka kwa magenge mapya ya uhalifu. Ili kukabiliana na changamoto hizo, serikali inasema imeimarisha operesheni za polisi, ushirikishaji wa wananchi katika masuala ya usalama, matumizi ya teknolojia na mageuzi katika sekta ya usalama. Pia inaandaa miswada sita ya kurekebisha sheria zinazosimamia vyombo vya usalama, ikiwemo Sheria ya Huduma ya Polisi, Sheria ya Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA), Sheria ya Tume ya Huduma za Polisi na Sheria ya Utulivu wa Umma.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 2 hours ago
Sababu za Kuppet kukataa mpango wa shule jumuishi
Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kati (Kuppet) kimepinga mpango wa Rais William Ruto wa kuanzisha mfumo wa shule jumuishi, kikisema hautatatua changamoto za elimu nchini. Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori alisema mpango huo hauna msingi wa kisheria na unaweza kuvuruga usimamizi wa shule, hasa katika Gredi 7, 8 na 9. Kuppet imekuwa ikishinikiza shule za Sekondari Msingi (JS)ziwe na usimamizi wake tofauti na shule za msingi, ikisema walimu wake hawawezi kuongozwa na wakuu wa shule za msingi. "Kuendesha mfumo huu bila marekebisho ya Katiba ni kufanya majaribio," alisema Misori. Alisema Sekondari Msingi hufuata mtaala wa kiwango cha shule za upili, hivyo si vyema kuziweka chini ya wakuu wa shule za msingi ambao wamefunzwa kusimamia elimu ya msingi. Misori alisema kuwa hata kama shule hizo ziko katika eneo moja, zinaweza kuwa na usimamizi tofauti, akitaja shule ya msingi ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambayo huendeshwa kivyake licha ya kuwa ndani ya chuo hicho. Pia alionya kuwa baadhi ya walimu waliofunzwa kufundisha masomo ya msingi wamepewa masomo ya sayansi na kiufundi katika JS bila kuwa na sifa zinazohitajika. Rais Ruto aliagiza Wizara ya Elimu kushirikiana na Chama cha Wakuu wa Shule Jumuishi nchini (Kecsha) kuandaa mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Elimu ya Msingi ndani ya siku 90. Alitoa agizo hilo Novemba 13 wakati wa kufunga mkutano wa Kecsha mjini Mombasa, akisema sheria mpya inapaswa kuweka wazi usimamizi, ajira na ufadhili wa shule hizo. Kecsha imekuwa ikitaka mfumo mpya wa kupandisha vyeo wakuu wa shule ili kuzingatia majukumu yao mapya ya kusimamia wanafunzi kuanzia elimu ya chekechea hadi Gredi 9. Hata hivyo, Kuppet imesema haitakubali JS kuendelea kusimamiwa na wakuu wa shule za msingi. Mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Omboko Milemba alisema viongozi wa Kuppet wamewasilisha mapendekezo yao kwa Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa, wakitaka kuwe na mfumo tofauti wa usimamizi, walimu wa kutosha na mgao unaofaa wa rasilimali. Mzozo huo sasa unatarajiwa kuelekea Bungeni huku muda wa siku 90 uliotolewa na Rais ukianza kuhesabiwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
Biashara ya magendo yasababishia serikali hasara ya Sh1 trilioni kwa mwaka
MKULIMA wa chai kaunti ya Kiambu anapopeleka majani mabichi katika kituo cha kununua chai, huenda mizani ikaonyesha uzito ulio chini kwa asilimia 14 hadi 20 ya alichovuna. Huu ni mfano mmoja tu wa biashara haramu ambayo serikali inasema inaletea Kenya hasara ya zaidi ya Sh800 bilioni kila mwaka. Mitandao hiyo hiyo inayopunguza uzani wa chai ya wakulima pia huuza kemikali bandia, pombe isiyo salama na mbolea feki inayowekwa katika mifuko yenye majina ya bidhaa halisi. Ripoti mpya ya serikali kuhusu biashara haramu nchini, iliyozinduliwa Mombasa Jumatano, inakadiria kuwa shughuli hizo ziligharimu Kenya Sh826 bilioni mwaka 2018, huku hasara hiyo ikivuka Sh1 trilioni katika miaka iliyofuata. Katika mwaka huo, hasara hiyo ilikuwa sawa na asilimia 9.3 ya pato la taifa. Serikali pia ilipoteza mapato ya Sh153.1 bilioni, huku ajira 44,198 zikikosekana na uwekezaji wa Sh123 bilioni kutopatikana. Watengenezaji bidhaa ni miongoni mwa walioathirika zaidi. Ripoti inasema kampuni halali hupoteza wastani wa asilimia 25 ya soko lake, sawa na takriban Sh3.9 milioni kwa mwaka kwa kila kampuni. Pia, ajira katika kampuni hizo hupungua kwa asilimia 25.5. Watumiaji nao wako hatarini. Daktari Robi King'a wa Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Bandia alisema hadi asilimia 60 ya baadhi ya aina za pombe na asilimia 89 ya baadhi ya kemikali za kilimo sokoni huenda ni bandia au vimefungwa upya kinyume cha sheria. Serikali pia hupoteza mapato kupitia ukwepaji wa ushuru. Mwaka wa kifedha wa 2025/26, bidhaa zilizokamatwa kutokana na maafisa wa forodha zilikuwa na thamani ya Sh10.83 bilioni. Ripoti inataja visa kadhaa vinavyoonyesha ukubwa wa tatizo. Katika kituo cha mpakani wa Lwakhakha, maafisa walipata lita 40,971 za ethanol zilizofichwa kwenye magari ya kubeba mafuta yaliyotangazwa kubeba shehena tofauti. Bidhaa hizo zilikuwa na thamani ya Sh26.9 milioni. Katika Bandari ya Mombasa, maafisa walikamata tani 23 za kemikali bandia za kuuwa watoto, huku bidhaa nyingine bandia za thamani ya zaidi ya Sh200 milioni zikiharibiwa Athi River. Maafisa jijini pia walinasa mifuko 190,000 ya mbolea bandia eneo la Kariokor, Ripoti pia ilitaja pombe yenye vibandiko bandia vya ushuru kaunti ya Nyeri na dawa za serikali zikiuzwa katika maduka ya dawa yasiyoidhinishwa Kajiado. Ili kukabili tatizo hilo, ripoti inapendekeza mashirika ya serikali yashirikiane katika operesheni, yaimarishe ufuatiliaji wa bidhaa na kuchunguza watu wanaofadhili mitandao hiyo. King'a alisema hatua za kidijitali zinahitajika pia kwa kuwa bidhaa bandia zinazidi kuuzwa kupitia mitandao ya intaneti. Chama cha Wafanyabiashara wa Rejareja nchini kinataka KRA, Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Bandia, Shirika la Viwango vya ubora nchini na polisi kuunda mpango wa pamoja wa kukabiliana na biashara hiyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
Kiti cha naibu rais chazua ushindani mkali 2027 katika serikali na upinzani
VITA vya kuwania unaibu rais vimeanza kushika kasi katika kambi za Rais William Ruto na upinzani unaoongozwa na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua, huku viongozi mbalimbali wakimezea mate wadhifa huo muhimu katika uchaguzi wa 2027. Katika serikali, Naibu Rais Kithure Kindiki anakabiliwa na ushindani kutoka kwa viongozi wa Mlima Kenya wanaotaka kuchukua nafasi yake. Miongoni mwa wanaotajwa ni Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Mbunge wa Ndia George Kariuki, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung'wah na Mwangi Kiunjuri wa chama cha TSP. Hata hivyo, washirika wa Kindiki, akiwemo Gavana wa Nakuru Susan Kihika na Mbunge wa Nakuru Town East David Gikaria, wanasisitiza kuwa anafaa kuendelea kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto. Kwa upande mwingine, chama cha ODM pia kinataka kushirikishwa katika mazungumzo ya kugawana mamlaka kupitia ushirikiano wake na UDA. Viongozi wanaotajwa kuwa na nafasi ni Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, mawaziri Hassan Joho na Wycliffe Oparanya. Utafiti wa TIFA uliofanywa kati ya Oktoba 26 na Novemba 5 ulionyesha kuwa asilimia 55 ya wafuasi wa Dkt Ruto wanamuunga mkono Profesa Kindiki kuwa mgombea mwenza. Wanga alipata asilimia 12 huku Joho akipata tisa. Hata hivyo, utafiti wa Swiss Poll International uliotolewa Oktoba 28 ulimweka Waiguru mbele kwa asilimia 43, akifuatiwa na Kindiki kwa asilimia 30 na Wanga kwa asilimia 13. Mbunge Kariuki anasema nafasi hiyo haipaswi kuchukuliwa kuwa mali ya Kindiki, akitaka UDA kuruhusu ushindani wa ndani. Anasema mgombea anayevutia kura nyingi ndiye anayefaa kuchaguliwa, akiongeza kuwa Dkt Ruto anapaswa kuwa na uhuru wa kumteua mgombea mwenza atakayemsaidia kushinda uchaguzi. Katika upinzani, mazungumzo yanahusisha viongozi watatu wakuu: Kalonzo Musyoka, Edwin Sifuna na Fred Matiang'i. Hata hivyo, bado hawajakubaliana nani atakuwa mgombea urais na nani atakuwa naibu wake. Washirika wa Gachagua wanasema uchaguzi huo utategemea atakayepata tiketi ya urais na kuzingatia maslahi ya maeneo mbalimbali. Martha Karua, Eugene Wamalwa na Justin Muturi pia wanatajwa katika mazungumzo hayo. Sifuna ameonya kuwa tiketi ya urais haipaswi kutolewa kwa mtu kwa sababu tu amekuwa nje ya serikali kwa muda mrefu. "Hatupaswi kumpa mtu tiketi kwa sababu anasema amekuwa nje ya serikali kwa muda mrefu. Hatuendi serikalini kutafuta starehe," alisema. Wakati huo, Waziri John Mbadi amesema ODM inatarajia makubaliano rasmi na UDA kabla ya Februari 2027. Anasema chama hicho kinataka nafasi kubwa katika ushirikiano huo, ikiwemo ile ya naibu rais. Hata hivyo, Mbunge wa Ugenya David Ochieng' amepinga uwezekano wa Kindiki kubadilishwa na kiongozi wa jamii ya Waluo, akisema anataka Dkt Ruto na Kindiki waendelee pamoja. Hivyo, Dkt Ruto anakabiliwa na changamoto ya kudumisha uhusiano na Kindiki huku akishughulikia madai ya viongozi wa Mlima Kenya Magharibi na ODM. Upinzani nao unapaswa kusawazisha maslahi ya viongozi na maeneo ili kuepusha migawanyiko kabla ya uchaguzi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Hapa ni kuchimbana? Mrengo wa upinzani, ndani ya upinzani waibuka
SIASA za upinzani zimepata sura mpya baada ya vigogo wanne, Fred Matiang'i, Ndindi Nyoro, Martha Karua na James Orengo kuonekana wakishirikiana katika juhudi za kuunda mrengo mpya wa kisiasa unaoweza kuathiri mikakati ya kumuondoa Rais William Ruto madarakani mwaka 2027. Muungano unaochipuka wa viongozi hao umeanza kuvutia hisia za kisiasa, hasa baada ya kufanya ziara ya pamoja katika eneo la Gusii, huku wakitarajiwa kuelekea Kirinyaga leo, nyumbani kwa Bi Karua, kwa mikutano mingine ya kisiasa. Ingawa viongozi hao wanasisitiza kuwa lengo lao ni kupanua wigo wa upinzani kote nchini, hatua zao zimeibua maswali kuhusu iwapo wanajenga muungano mpya ndani ya upinzani au wanajiandaa kuwania nafasi kubwa katika mazungumzo yatakayoamua mgombeaji wa urais wa upinzani. Baadhi ya watu wa karibu na viongozi hao wanasema ushirikiano huo umechochewa na kile wanachokitaja kuwa uongozi wa mabavu wa baadhi ya vinara wa upinzani, ambao wanahofia unaweza kudhoofisha juhudi za pamoja za kumkabili Dkt Ruto. Mvutano huo unajiri wakati ambapo upinzani bado unakabiliwa na changamoto ya kuafikiana kuhusu uongozi na mgombeaji mmoja wa urais. Utafiti wa hivi majuzi wa kampuni ya TIFA unaonyesha kuwa asilimia 43 ya waliohojiwa wanamtaja aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuwa kikwazo kikubwa zaidi kwa umoja wa upinzani. Rais Ruto anafuata kwa asilimia 15, huku kiongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi Edwin Sifuna akipata asilimia saba na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka asilimia sita. Hata hivyo, Bw Gachagua amepuuzilia mbali madai kuwa ndiye anayegawanya upinzani, akisisitiza kuwa yeye ndiye anayewaunganisha viongozi hao. Malumbano makali kati yake na Dkt Matiang'i katika siku za hivi majuzi yamezidisha dalili za mgawanyiko kuhusu nani anafaa kuongoza upinzani na jinsi ya kuandaa kampeni za 2027. Msemaji wa Wiper, Bw Ndegwa Njiru ameonya kuwa ushirikiano wa upinzani bado ni dhaifu na viongozi wanapaswa kuheshimiana ili kuepusha migogoro inayoweza kuuvunja. Alisema viongozi wanapaswa kudhibiti wafuasi wao na kuhakikisha hawawadharau wagombeaji wengine wa urais. Tofauti na mirengo mingine, ushirikiano wa Matiang'i, Nyoro, Karua na Orengo unaonekana kuwa na hesabu pana ya kisiasa inayolenga kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi. Dkt Matiang'i, aliyewahi kuhudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani wakati wa utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ndiye anayeonekana kuwa kiini cha ushirikiano huo. Wafuasi wake wanataja uzoefu wake serikalini na kujulikana kitaifa kuwa baadhi ya sifa zinazoweza kumsaidia kumkabili rais anayewania muhula wa pili. Hata hivyo, changamoto yake kubwa ni kupanua ushawishi wake nje ya eneo la Gusii na kupata uungwaji mkono kutoka maeneo mengine. Mchanganuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema kuhusika kwa Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ni muhimu kwa sababu kunapatia ushirikiano huo nafasi katika eneo la Mlima Kenya, ambalo lina ushawishi mkubwa katika siasa za urais. Bw Nyoro amejijengea jina kwa kukosoa sera za serikali na misimamo yake kuhusu masuala ya uchumi. Kwa mujibu wa Bw Mboya, uhusiano wake na Dkt Matiang'i unampa nafasi ya kushiriki katika kuunda mwelekeo wa kisiasa wa kitaifa huku akiendeleza ushawishi wake binafsi. Kwa upande wake, Bi Karua analeta uzoefu wa kupigania mageuzi, utawala bora, Katiba na uwajibikaji. Aliwahi kuwania urais na pia kuwa mgombeaji mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi mkuu uliopita. Katika mkutano wa Gusii, alionyesha kuwa yuko tayari kuweka kando azma yake binafsi ikiwa upinzani utaafikiana kumuunga mkono mgombeaji mwingine. 'Ingawa wengi wetu, akiwemo mimi, tuna azma ya kuwania urais, iwapo itaamuliwa kuwa Dkt Matiang'i ndiye atakuwa mgombeaji, nitajiondoa na kumuunga mkono,' alisema. Alisema yuko tayari pia kumuunga mkono Bw Nyoro iwapo atachaguliwa kuwa mgombeaji wa upinzani. Kauli hiyo inaashiria juhudi za kuzuia azma tofauti za viongozi hao kuwa kikwazo cha kuunda muungano wenye nguvu. Kujiunga kwa Gavana wa Siaya James Orengo nao kumeongeza uzito wa kisiasa kwa kundi hilo, hasa kutokana na uhusiano wake wa muda mrefu na marehemu Raila Odinga na ushawishi wake katika Nyanza. Bw Orengo awali alikuwa amejitambulisha na vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Bw Sifuna. Hata hivyo, hatua zake hivi majuzi, ikiwemo kuhusika katika chama cha Liberal Democratic Party na kumuunga mkono Dkt Matiang'i hadharani Kisii, zimeashiria mwelekeo mpya. Katika mkutano wa Gusii, aliwataka wakazi kumuunga mkono Dkt Matiang'i, akirejelea uhusiano wake na marehemu Raila pamoja na babake, Jaramogi Oginga Odinga. Alisema wakazi wa Gusii wamekuwa wakiunga mkono familia ya Odinga kwa muda mrefu na kwamba kumuunga mkono Dkt Matiang'i kungekuwa njia ya kuendeleza uhusiano huo. Bw Orengo alieleza kuwa Dkt Matiang'i alikuwa na uhusiano wa karibu na Raila, ambaye alimchukulia kama mwanawe. Dkt Matiang'i naye alimtaja Bw Orengo kama mshauri wake wa kisiasa na kumshukuru kwa uongozi na ushauri wake. Ushirikiano huo unaweza kumsaidia Dkt Matiang'i kuimarisha uhusiano na wapigakura wa Nyanza katika kipindi ambacho eneo hilo linajipanga upya kisiasa kufuatia kifo cha Raila. Hata hivyo, kundi hilo si pekee linalotafuta ushawishi ndani ya upinzani. Bw Kalonzo, kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa nao wamekuwa wakifanya kazi pamoja. Wakati huo huo, mirengo inayohusishwa na Bw Gachagua na Bw Sifuna inachunguza uwezekano wa kuunda muungano unaounganisha Mlima Kenya na Mlima Elgon. Wachanganuzi wanaonya kuwa makundi hayo yanaweza kufanya mazungumzo ya kuafikiana kuhusu mgombeaji mmoja kuwa magumu zaidi, hasa kila mmoja akitaka mgombeaji wake apewe nafasi ya kwanza. Dkt Matiang'i amepuuzilia mbali madai kuwa ushirikiano wao ni jaribio la kujitenga na viongozi wengine wa upinzani. Alisema walikubaliana kuwa kila kiongozi anapaswa kuzunguka maeneo tofauti nchini ili kupanua ushawishi wa muungano. 'Tulikubaliana katika upinzani kuwa kila mmoja azunguke nchini. Tunahitaji kuunda timu zitakazofikia maeneo yote ya nchi,' alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 07:55:25
Makanisa yageuza tohara ya wavulana kuwa biashara nono
KWA miaka mingi, tohara ilikuwa jukumu la wazee waliokuwa na mamlaka ya kuamua wakati, mahali na jinsi wavulana walivyopaswa kutahiriwa. Lakini sasa makanisa yamechukua nafasi hiyo, yakigeuza utamaduni uliorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kuwa shughuli inayohusisha malipo ya maelfu ya shilingi. Miezi ya Novemba na Desemba, familia katika maeneo ya Bonde la Ufa na Mlima Kenya humiminika katika makanisa kuwaandikisha wana wao katika kambi za tohara zinazochanganya matibabu, mafundisho ya Kikristo na mafunzo ya maisha. Badala ya kwenda msituni au kwenye vituo vya kitamaduni vilivyoendeshwa na wazee, wavulana hukaa katika kumbi za makanisa kwa siku saba hadi 14, wakihudumiwa na madaktari na walezi. Wazazi hulipa kati ya Sh10,000 na Sh50,000 kutegemea kanisa, eneo na muda wa kambi. Kwa hivyo, tohara imegeuka kuwa biashara ya msimu inayozalisha mamilioni ya shilingi kila mwaka. Mlezi wa kitaifa wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Kiama Kia Ma, Kung'u Muigai, anasema wazee wamepokonywa jukumu lao muhimu katika jamii. "Watu hawaliiti biashara, wanaliita huduma ya kanisa," anasema, akiongeza kuwa shughuli hiyo sasa ina thamani ya mamilioni ya pesa kila mwaka. Kwa mujibu wa Joseph Kaguthi, mratibu wa wazee na viongozi wa dini katika Baraza la Pamoja la Wazee wa Mlima Kenya, tohara ilikuwa chini ya usimamizi wa wazee. Wao ndio walioamua nani angefanya tohara, lini na wapi, huku wavulana wakifundishwa majukumu yao katika jamii na kujiunga na rika lililowaongoza maisha yao yote. Familia zililipa kwa kutoa mbuzi, pombe ya kienyeji na heshima kwa wazee. Hata hivyo, kuanzia miaka ya 1920 hadi 1950, wamishenari wa Kanisa la Scotland (PCEA) na Kanisa Katoliki walipinga tohara iliyofanywa misituni, wakihimiza matumizi ya hospitali. "Hospitali zilijengwa na madaktari wakachukua nafasi ya ngariba wa kitamaduni. Wazee walikuwa na maarifa lakini hawakuwa na hospitali. Kanisa lilikuwa nayo," anasema Kaguthi. Baadaye, kuibuka kwa kundi la Mungiki na magenge mengine kulifanya tohara za nyumbani kuwa hatari zaidi. Hali hiyo iliimarisha imani ya wazazi kwamba makanisa yalikuwa maeneo salama zaidi. Mhubiri Charity Kagina wa Murang'a anasema wazazi walikuwa wameanza kushindwa kutambua wazee wa kweli na matapeli. Anasema makanisa yalitoa usalama kupitia walinzi, sajili i na utaratibu wa kufuatilia watoto. Kwa wazazi, hata hivyo, gharama imekuwa mzigo. James Rono wa Eldoret anasema alilipa Sh17,000 kwa mwanawe kuhudhuria kambi ya wiki moja katika kanisa Katoliki. Fedha hizo ziligharamia huduma za daktari, chakula, malazi na mafunzo ya malezi. Anasema gharama hiyo ni kubwa wakati familia zinakabiliwa na mahitaji mengine, ikiwemo karo ya shule. Baadhi ya wazazi hulazimika kutafuta huduma za watu wasio na ujuzi kutokana na gharama hizo. Askofu Joseph Kagunda wa ACK Mlima Kenya Magharibi, ambaye alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa tohara zinazoendeshwa na makanisa, anakiri kuwa ada imeongezeka tangu alipokuwa akitoa huduma hiyo kwa takriban Sh10,000. Anasema awali wavulana hawakupata ushauri wa kutosha, lakini sasa wanapewa mafunzo kuhusu uwajibikaji na maisha ya utu uzima. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa dini wanapinga makanisa kutumia shughuli hiyo kupata faida. Askofu Wilson Kurui wa Jesus Love Ministries, Eldoret, anasema huduma hiyo inapaswa kuwa njia ya kanisa kusaidia jamii badala ya kuwa chanzo cha mapato. Kwa upande mwingine, wazee wanasema makanisa yanapunguza nafasi yao katika utamaduni. Thomas Ingara, mwenye umri wa miaka 91, ambaye ni mtaalamu wa tohara ya kitamaduni kutoka kijiji cha Kalwani, Hamisi, anasema makanisa yanapaswa kuzingatia mahubiri na kuwaachia wazee jukumu la tohara. Kung'u Muigai anasema baadhi ya makanisa huwaalika wazee kwa muda mfupi tu, bila kuwapa nafasi ya kuwafundisha wavulana kikamilifu. Kiama Kia Ma inapendekeza makanisa yatumie wiki moja kuwafundisha wavulana masuala ya kiroho na wazee watumie wiki inayofuata kuwafundisha utamaduni. Hata hivyo, pendekezo hilo halijaungwa mkono na baadhi ya makanisa. Wakati huo huo, usalama wa wavulana unabaki kuwa suala muhimu. Mchungaji Isaac Wanakacha, muuguzi mkuu wa zamani katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi, anashauri wazazi kutumia hospitali za umma na kliniki zilizoidhinishwa, ambazo hutoa huduma kwa gharama nafuu na kuruhusu matumizi ya bima ya SHA. Askofu Edward Khaoya wa Kitale Family House of Hope anasema takriban watoto 10 hufariki kila mwaka kutokana na matatizo yanayohusiana na tohara baada ya kufikishwa katika Moi Hospital. Mtafiti wa utamaduni Mwaura wa Koigi anasema makanisa yalipata umaarufu kwa kutoa maeneo salama na walezi waliokuwa wakiaminika, lakini baadaye huduma hiyo ikageuka kuwa biashara.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 05:55:58
Ripoti: Magenge 309 ya uhalifu yatishia usalama nchini
BONDE la Ufa, Pwani na Nairobi ndiyo maeneo yanayoongoza kwa idadi kubwa ya magenge ya uhalifu yanayotishia usalama wa wananchi, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyowasilishwa bungeni na Rais William Ruto. Ripoti kuhusu hali ya usalama nchini inaonyesha kuwa kuna jumla ya magenge na makundi 309 ya uhalifu kote nchini, ingawa baadhi yake hayafanyi shughuli kwa sasa. Idadi hiyo imeongezeka kwa makundi 200 ikilinganishwa na mwezi uliopita, wakati serikali ilipotangaza kuwa ilikuwa imetambua magenge 109. Mwaka 2016, kupitia Tangazo la Serikali Na. 10427, magenge 89 yalitangazwa kuwa haramu. Ripoti hiyo inayohusu kipindi cha Septemba 2025 hadi Agosti 31, 2026, inaonyesha kuwa Bonde la Ufa linaongoza kwa magenge 20 yanayotekeleza shughuli za uhalifu, likifuatiwa na Pwani iliyo na magenge 17, Nairobi 11, Magharibi 10, Nyanza saba, Mashariki manne na Kati matatu. Baadhi ya magenge yanayofanya shughuli Bonde la Ufa ni Watizedi, Kamiti, Confirm, Barsuliek, Cheptiret Boys, DNA, Answi, Chafua, Exodus na Isilando. Pwani kuna Empire, Military Gang, Wakali Wao, Kitimboni, Zoza Nation, Team Mashamba, Mombasa Republican Council (MRC), Panga Boys na Mawoza. Katika Nairobi kuna magenge kama Team Kazoo, Mujahedeen, Matopeni Mafia, Jeshi ya Allah, Mbogi Genje, Gaza, Tokyo Mafia na Team Mbogi. Magharibi kuna Border Defence Force, Bogi Mawe, Jobless Gang, Marachi Republican Council na Fimbo Movement, huku Nyanza kukiwa na Darfur, China Squad, Sungusungu, Chinkororo na Katalang. Katika eneo la Mashariki kuna G-Unit, Jeshi ya Rasia, Gaza na Nkomori, huku eneo la Kati likiwa na Mungiki, Gaza na Kamagira. Ripoti hiyo inasema magenge hayo yanadhoofisha utawala wa sheria kupitia vurugu, vitisho dhidi ya jamii na kuwashawishi vijana walio katika mazingira magumu kujiunga na uhalifu. Licha ya operesheni za polisi, makundi hayo yanaendelea kujipanga na kuajiri wanachama wapya kutokana na changamoto za kiuchumi, hasa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Kaunti zinazokumbwa na hali ya kutovumiliana kisiasa kutokana na matumizi ya wahuni na magenge hayo ni Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Busia, Murang'a, Kiambu, Nyeri, Mombasa na Nairobi. Ripoti hiyo inasema hali hiyo imechangia ongezeko la ujambazi, mauaji yaliyolengwa, uvamizi wa nyumba, utapeli wa ardhi na ulaghai wa fedha katika sekta za usafiri wa umma na ujenzi. Polisi walikamata washukiwa 1,316 katika kipindi hicho, ikilinganishwa na 602 katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia. Hii ni ongezeko la watu 714. Baadhi ya magenge yanaendesha shughuli katika kaunti kadhaa. Gaza ina mizizi Mombasa, Kwale, Nakuru, Kilifi, Isiolo, Machakos, Nairobi na Kisumu. Mungiki inapatikana Nakuru, Machakos, Nairobi na Kiambu. Panga Boys lina matawi Kilifi, Kwale na Mombasa, huku Wakali Wao likiendesha shughuli Mombasa, Kilifi, Kwale na Nairobi. Serikali imesema inaendesha operesheni ya pamoja inayotegemea taarifa za kijasusi, kuongeza doria na kuimarisha uwepo wa polisi katika maeneo hatari. Hata hivyo, imeonya kuwa baadhi ya wanasiasa wanaowalinda wahalifu wanachangia kuimarisha magenge hayo. Pia, hofu ya kulipiziwa kisasi imewafanya wananchi kusita kuwapa maafisa wa usalama taarifa muhimu kuhusu wanachama wa magenge ya wahalifu.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 04:55:41
Sifuna asubiriwa kwa hamu Amerika ziara ya Kalonzo ikiahirishwa
WAKENYA wanaoishi Amerika wanatazamia kwa hamu ziara ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, ambaye anatarajiwa kuwasili nchini humo huku akijipanga kuimarisha uungwaji mkono wake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Ziara hiyo inatarajiwa kumwezesha Sifuna kukutana na Wakenya wanaoishi ughaibuni, kujadili uongozi wa Kenya na kutafuta michango ya kifedha kwa safari yake ya kisiasa. Ziara hiyo inaanzia New Jersey na inaangazia umuhimu unaoongezeka wa wapiga kura na wafadhili waishio nje ya nchi katika siasa za Kenya. Mwanzilishi mwenza wa The Equitable Party, Dkt Eunice Juma, alisema chama hicho kilikumbana na changamoto nyingi za kiutawala kikitafuta usajili. "Wakati mwingine ilionekana kana kwamba simu kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu zilikuwa zikichelewesha mchakato wa kusajili chama," alisema. Chama hicho baadaye kilisajiliwa na kubadilisha jina kuwa Linda Mwananchi Movement (LMM) baada ya kuidhinishwa kwa kauli moja katika mkutano wa wajumbe Novemba 13, 2026. Profesa Kefa Otiso wa Chuo Kikuu cha Bowling Green State alisema mchango mkubwa wa Wakenya wanaoishi ughaibuni kwa wanasiasa ni kuchangisha fedha na kuwashawishi jamaa na marafiki walio nyumbani kuwaunga mkono wagombeaji. "Fedha kutoka ughaibuni zimekuwa muhimu kwa sababu Wakenya wanaoishi huko wana uwezo wa kuchangia kiasi kikubwa. Nchini Kenya, wanasiasa huwapa wapigakura fedha, lakini ughaibuni Wakenya huchangia wagombeaji," alisema. Mtandao wa LMM nchini Amerika umeunda matawi katika majimbo yote 50. Tamasha la Chakula cha Mulembe-Mashemeji lilichoandaliwa Oktoba 24 lilikuwa sehemu ya maandalizi ya ziara ya Sifuna. Dkt Juma alisema ziara hiyo inalenga kuwakutanisha Wakenya kujadili uongozi, utawala bora, utawala wa sheria na mustakabali wa nchi. Sifuna anatarajiwa kuzindua ofisi za LMM mjini Hackettstown, New Jersey, Novemba 21, kabla ya kuhudhuria ibada ya kanisa Pennsylvania siku inayofuata. Atakutana pia na wafanyabiashara Maryland Novemba 23 na kushiriki mkutano kuhusu siasa za Afrika Mashariki Washington DC Novemba 24. Ratiba yake itaendelea Dallas, Texas, kisha Renton na Oakland ambako atahudhuria mikutano na hafla za kuchangisha fedha. Ziara hiyo itakamilika Silicon Valley Desemba 7. Wakati huo huo, ziara ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka nchini Amerika iliyopangwa kipindi hicho imeahirishwa hadi Februari 2027. Mkurugenzi wake wa mawasiliano David Mutua alisema mabadiliko hayo yamefanywa bila kutoa sababu zaidi. Ziara za wanasiasa wa Kenya nchini Amerika zimekuwa muhimu katika kujenga mitandao ya kisiasa, kuchangisha fedha na kutafuta uhusiano na viongozi wa kimataifa. Amerika ni mshirika muhimu wa Kenya, ambayo ina hadhi ya mshirika mkuu asiye mwanachama wa NATO. Sifuna anatarajia kutumia ziara hiyo kuimarisha uhusiano huo na kuongeza ushawishi wake katika siasa za kitaifa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 03:55:09
Mahakama yafichua majaji na mahakimu walioamua kesi nyingi zaidi mwaka huu
KWA mara ya kwanza, idara ya Mahakama imechapisha takwimu zinazoonyesha idadi ya kesi zilizoamuliwa na kila jaji na hakimu katika mwaka uliotamatika Juni 2026. Ripoti ya kurasa 328 kuhusu hali ya Mahakama na utoaji haki imetaja majina ya maafisa hao pamoja na idadi ya hukumu, maamuzi na maagizo mengine waliyotoa. Hata hivyo, Idara ya Mahakama imesisitiza kuwa takwimu hizo si orodha hiyo haitokani na mashindano ya majaji kazini. Katika Mahakama Kuu, Jaji Reuben Nyakundi aliongoza kwa kuamua kesi 1,791. Alifuatiwa na Alfred Mabeya aliyeshughulikia kesi 968, Teresa Odera (956), Richard Mwongo (913), Teresia Matheka (906) na Kizito Magare (904). Majaji wengine waliokuwa na idadi kubwa ya maamuzi ni Diana Kavedza (824), Mwanaisha Saida (778), Lucy Gitari (745), huku Helene Namisi na Florence Muchemi wakiwa na kesi 744 kila mmoja. Katika Mahakama ya Rufaa, jumla ya kesi 2,394 ziliamuliwa na majopo ya majaji. Jopo la Kisumu lililoongozwa na majaji Hellen Omondi, Luka Kimaru na Milton Makhandia liliongoza kwa kesi 172. Katika Mahakama ya Ajira na Mahusiano Kazini, Jaji Jemima Keli aliongoza kwa maamuzi 499, akifuatwa na Monica Mbaru na Stella Rutto waliokuwa na 484 kila mmoja. Katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi, Emmanuel Washe aliongoza kwa kesi 456, akifuatwa na Fred Nyagaka (455) na David Mugo (442). Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa, mahakama ilipokea kesi mpya 561,580 na kuamua 576,702, kiwango cha utatuzi cha asilimia 103. Kesi zinazosubiri kuamuliwa zimepungua kutoka 405,486 hadi 341,412, lakini bado asilimia 58.9 ya kesi hizo zimekaa mahakamani kwa zaidi ya mwaka mmoja. Mahakama za mahakimu ndizo zilizo na mrundiko mkubwa zaidi wa kesi 274,177, sawa na asilimia 80.3 ya jumla ya kesi zilizochelewa kuamuliwa. Jaji Mkuu Martha Koome alisema licha ya mahakama kuamua kesi nyingi kuliko zilizowasilishwa kwa mwaka wa pili mfululizo, idadi ya kesi za zamani bado ni kubwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 02:55:16
Hofu ya wagonjwa wa saratani kukosa matibabu kufuatia mabadiliko ya SHA
WAGONJWA wa saratani nchini wameibua wasiwasi kuhusu kucheleweshwa kwa matibabu, kukataliwa kwa maombi ya dawa na kupunguzwa kwa kiwango cha fedha wanacholipiwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Wanasema mfumo mpya wa kuidhinisha matibabu umewalazimu kulipa fedha za ziada ili kupata huduma ambazo awali ziligharamiwa kikamilifu na bima ya afya. Katika Hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH), kati ya maombi 30 ya matibabu yaliyowasilishwa kwa SHA Jumatatu, ni 12 pekee yaliidhinishwa. Daktari mmoja mtaalamu wa saratani alisema hata wagonjwa walioidhinishwa walitakiwa kuongeza fedha kutoka mifukoni mwao. Alitaja mgonjwa wa saratani ya utumbo aliyelazimika kulipa Sh20,000 kwa vipimo, licha ya kuwa awali gharama hizo zililipwa na SHA. Daktari alisema hali hiyo imacha wagonjwa wasiojiweza kifedha wakisimamisha matibabu kwa kukosa pesa za kuongeza. Mgonjwa mmoja wa saratani ya matiti alisema kiwango chake cha fedha za kununua dawa ya Letrozole kimepunguzwa hadi Sh5,400, ilhali anahitaji zaidi ya Sh20,000 kwa dawa hiyo inayosaidia kudhibiti ukuaji wa saratani inayochochewa na homoni. "Ninahitaji zaidi ya Sh20,000 kununua dawa zangu. Kiasi hicho kinapopunguzwa nalazimika kuongeza fedha za ziada. Bila dawa hizo huenda nishindwe kudhibiti homoni," akaeleza. Mfumo huo mpya pia umeongeza muda wa kusubiri dawa hospitalini. Maombi ya matibabu sasa yanahitaji kupitishwa na muuguzi, daktari mtaalamu na mfamasia kabla ya kuidhinishwa. Muuguzi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta alisema foleni katika kliniki za saratani zinaongezeka huku wagonjwa wakingoja vibali. Mgonjwa Mary Adhiambo pia alisema kituo cha saratani cha Texas kimeacha kuuza dawa kwa wagonjwa wanaopokea matibabu katika hospitali zingine, na badala yake kuwataka wahamie huko. Mabadiliko hayo yameathiri wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH), ambao awali walinunua baadhi ya dawa katika vituo vingine. Mkurugenzi wa muungano wa mashirika ya kansa Kenya Network for Cancer Organisations, Phoebe Ongadi, alitaka SHA kueleza sababu za mabadiliko hayo na jinsi wagonjwa watakavyolindwa. "Kwa nini mfumo unabadilishwa na kuathiri matibabu? Saratani haisubiri. Hatupaswi kuchezea matibabu ya wagonjwa," alisema Ongadi. Hata hivyo, SHA ilisema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha huduma kwa kuoanisha matibabu na mwongozo wa kitaifa wa saratani pamoja na kuweka viwango sawa vya bei za dawa na huduma.Iliongeza kuwa kiwango cha fedha kinategemea mwongozo wa matibabu, bei zilizoidhinishwa na masharti ya ufadhili. Vile vile, ilisisitiza kuwa wagonjwa hawapaswi kutozwa tena kwa huduma ambazo tayari zimelipiwa na mamlaka hiyo, na gharama zozote za ziada zinapaswa kuelezwa wazi na kuthibitishwa. Mamlaka hiyo ilisema kila mgonjwa anastahili kupata kifurushi cha Sh800,000 cha matibabu ya saratani, kinachojumuisha Sh400,000 kupitia SHIF (Bima ya Afya ya Jamii) na Sh400,000 kutoka kwa hazina ya magonjwa ya dharura, sugu na hatari.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Fri, 20 Nov 2026 17:17:29
Sh1.2 bilioni zimetumika kufidia waathiriwa wa maandamano
JOPO la wataalamu wanaoshughulikia fidia kwa waathiriwa wa maandamano limeshughulikia maombi 1,476 na kulipa zaidi ya Sh1.218 bilioni, huku mwenyekiti Profesa Makau Mutua akitetea uadilifu wa zoezi hilo dhidi ya madai ya hongo. Fidia hiyo ni kwa familia za waliouawa, waliojeruhiwa, manusura wa dhuluma za kingono na waliopata hasara za kiuchumi wakati wa maandamano na ukiukaji wa haki za binadamu tangu 2013. Kiongozi wa kiufundi wa jopo hilo Richard Barno alisema walionufaika ni pamoja na familia za watu 236 waliouawa, 14 waliojeruhiwa vibaya sana, 214 waliojeruhiwa vibaya, 459 waliopata majeraha wastani na 369 waliopata majeraha madogo. Wengine 14 walikuwa waathiriwa wa dhuluma za kingono, huku madai 170 yakihusu hasara za kiuchumi. Barno alisema jopo hilo bado linachunguza zaidi ya faili 3,000 zilizowasilishwa kupitia ofisi zake na njia nyingine rasmi. Mwanachama wa jopo hilo Dkt Duncan Ndeda alisema kiwango cha fidia hutegemea ukubwa wa majeraha na mazingira ya ukiukaji wa haki. Waathiriwa wenye majeraha madogo hupokea Sh50,000, huku walio na majeraha ya wastani wakifidiwa Sh500,000. Waliojeruhiwa vibaya hupata Sh1 milioni nao waliojeruhiwa vibaya sana wakilipwa kati ya Sh1.5 milioni na Sh3 milioni. Familia za waliouawa hupokea angalau Sh3 milioni. Ndeda alisema jopo linatumia njia mbadala kuthibitisha maombi ya waathiriwa ambao hawana ripoti za hospitali, hasa kutokana kuwa baadhi ya matukio yalitokea miaka mingi iliyopita. Katika kesi za vifo, waombaji wanahitaji kuwasilisha vibali vya mazishi na ripoti za upasuaji wa maiti. Taarifa za mashahidi na machifu zinaweza pia kuongeza uzito wa thibitisho la maombi. Wakati huo huo, Profesa Mutua alikanusha madai kwamba baadhi ya wanachama wa jopo wamekuwa wakipokea hongo ili kutoa fidia. Aliwataka wenye ushahidi wa ufisadi kuripoti kwa polisi badala ya kusambaza madai kwenye mitandao ya kijamii. Alisema jopo halina hofu ya kuchunguzwa na kwamba litachapisha orodha ya maombi yaliyoshughulikiwa baada ya kukamilisha kazi yake, lakini taarifa binafsi za waathiriwa zitafichwa kulinda faragha yao. Hata hivyo, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ataruhusiwa kufikia taarifa zote.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Fri, 20 Nov 2026 14:44:26
Tutatengeneza timu yetu vizuuuuri, asema Pochettino akianza kazi Man United
MAURICIO Pochettino jana alianza rasmi majukumu yake kama kocha mpya wa Manchester United baada ya kuwasili katika uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wa Carrington. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 alisema ni heshima na fursa kubwa kuiongoza timu hiyo maarufu ya Uingereza. Pochettino aliondoka kambini mwa timu ya taifa ya Amerika Jumanne usiku baada ya kuiongoza kulaza Haiti 2-0 mchana huo, katika mechi ya marudiano ya robo-fainali ya Ligi ya Mataifa ya Amerika Kaskazini na Kati na Caribbean (CONCACAF Nations League). Alisafiri moja kwa moja hadi Manchester kuanza maandalizi ya kuinoa United, ambayo imempa mkataba wa miaka miwili na nusu baada ya kumruhusu kukamilisha majukumu yake ya kimataifa. "Nina hamu kubwa kuanza kazi hapa. Ni heshima na fursa ya kipekee kuwa katika klabu hii kubwa. Natarajia kuanza kazi vizuri," alisema Pochettino baada ya kuwasili uga wa mazoezi wa Carrington, Jumatano. Kibarua chake cha kwanza ni mechi ngumu dhidi ya Liverpool katika Ligi Kuu Uingereza (EPL) hapo Jumapili. Baada ya hapo watasafiri kuelekea nchini Ureno wiki ijayo kucheza dhidi ya Sporting Lisbon katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Hana muda mwingi wa kuzoea mazingira yake mapya ya kazi kwani wachezaji waliokuwa wakiwajibikia timu zao za taifa walirejea kambini jana. Pochettino aliagana na Amerika kwa ujumbe wa kuatua moyo, akisema anajivunia mafanikio ambayo walipata kipindi akiwa usukani. "Nilipowasili nilitaka timu iamini kuwa inaweza kushindana na yoyote. Natumai imani hiyo sasa imeimarika, si kwa wachezaji pekee bali pia kila mmoja anayeiunga mkono timu hii [ya Amerika]," akasema. Aliongeza kuwa kuondoka kwake katika kikosi cha Amerika haikuwa rahisi, lakini fursa ya kujiunga na Man United ilifanya kuwa vigumu kukataa ofa hiyo. Uzoefu wake katika ukocha unajumuisha vipindi aliponoa klabu za Southampton, Tottenham na Chelsea nchini Uingereza, na PSG nchini Ufaransa. Akiwa kocha wa Amerika alishinda mechi 23, kutoka sare mbili na kupoteza 12 kati ya 37 alizosimamia. Pia aliongoza Amerika kufika hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia 2026 na fainali ya Kombe la CONCACAF Gold Cup 2025.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Fri, 20 Nov 2026 14:08:32
Stars waporomoka hadi nambari 115 katika soka
TIMU ya taifa ya soka Harambee Stars imesawazisha rekodi yake mbovu zaidi katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa zaidi ya miaka minane, baada ya kushuka hadi nafasi ya 115 duniani. Katika viwango vipya vilivyotolewa Jumatano, kikosi cha kocha Benni McCarthy kilishuka nafasi moja kutoka 114 na sasa kimesawazisha matokeo yake ya Julai 2018 kilipokuwa pia katika nafasi ya 115. Kushuka huko kunatokana na matokeo yasiyoridhisha katika mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Afrika (AFCON) 2027 dhidi ya Afrika Kusini. Harambee Stars ilianza kwa sare ya kusisimua ya 2-2 jijini Johannesburg, ambako ililazimika kusawazisha mabao mara mbili baada ya wenyeji kuchukua uongozi. Hata hivyo, ilishindwa kutumia vyema nafasi ya kucheza nyumbani na kupoteza 2-1 dhidi ya Afrika Kusini katika Uwanja wa Nyayo, Nairobi mnamo Jumanne. Sare ya ugenini iliipa Kenya alama 6.50 katika viwango vya FIFA, lakini ikapoteza alama 6.23 kufuatia kichapo cha nyumbani Jumanne usiku. Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Harambee Stars kushuka katika viwango hivyo. Mwezi uliopita ilishuka nafasi tano kutoka 109 hadi 114, baada ya kutoka sare ya 1-1 na Eritrea kabla kufinywa 1-0 na wenyeji Guinea jijini Conakry. Matokeo hayo mabaya yanaifanya Kenya kuendelea kusaka ushindi wake wa kwanza katika Kundi D la kufuzu AFCON. Hata hivyo, tayari imejihakikishia kushiriki fainali hizo za 2027 kwa kuwa itakuwa mwenyeji mwenza wa mashindano hayo. Uganda bado ndiyo timu inayoongoza Afrika Mashariki licha ya kushuka nafasi mbili hadi ya 89 duniani. Tanzania nayo imeipiku Kenya baada ya kupanda nafasi tatu hadi ya 112. Taifa Stars ilicheza mechi mbili dhidi ya Nigeria, ikipoteza 3-1 mjini Uyo kabla ya kutoka sare tasa Zanzibar. Barani Afrika, Morocco imepanda nafasi mbili hadi ya tano duniani, kiwango chake cha juu zaidi katika historia ya viwango hivyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Fri, 20 Nov 2026 11:49:31
Uraibu wa uvutaji sigara na shisha unavyochangia madhara ya muda mrefu
MWENDO wa saa sita usiku mnamo Julai mwaka huu, Mzee Jay Mwashe*, 77 akiwa usingizini, alihisi maumivu fulani kifuani. Lakini muda mfupi baadaye, alihisi kana kwamba anataka kukohoa, kabla ya kuanza kutatizika kupumua. Tukio hilo lilibadilika mara moja na kuwa suala la dharura ambapo juhudi zilifanywa na akafikishwa hospitalini ambapo aliwekwa kwenye oksijeni mara moja kumsaidia kupumua. Baada ya ukaguzi alibainika kuwa na tatizo la moyo lililochangiwa na Ugonjwa Sugu wa Kuziba Mapafu (Chronic Obstructive Pulmonary Disease (COPD). Daktari alimfafanulia kuwa mojawapo ya masuala yanayochangia hali hiyo ni uvutaji sigara licha ya kuwa aliacha kuzivuta takriban miaka 30 iliyopita. "Mimi niliacha kuvuta sigara karibu miaka 30 iliyopita, itakuwaje sasa nielezwe ndio jambo linalochangia hali ninayoshuhudia sasa?" aliuliza huku akijipata hospitali mara kadha baada ya hapo akilazimika kuwekwa kwenye oksijeni. Ingawa mzee huyu sasa anaendelea na matibabu ambayo ni pamoja na kutumia kivuta pumzi(inhaler) kama watu wanaougua pumu, wataalam, wanasema hilo si jambo geni kwani uvutaji sigara una athari za muda mrefu kwa wanaozivuta na hata wale waliopo karibu na mazingira ya watu wanaozivuta. Kulingana na Dkt Joseph Aluoch, tabibu na mtaalam wa kifua, madhara ya muda mrefu ya uvutaji sigara huathiri viungo muhimu vya mwili. "Kuna madhara ya saratani ya mapafu, matatizo ya moyo, mshtuko wa moyo, ugonjwa sugu wa mkamba (bronchitis) miongoni ya mengine," anaeleza. Kwingineko, katika mojawapo ya mitandao, mzazi mmoja alituma picha akitaka kufahamishwa kuhusu kifaa kilichokuwa kwenye picha hiyo. Kulingana naye, kwa muda mrefu mwanae ambaye ni tineja alikuwa amemueleza kuwa ni kichupa cha marashi. Lakini siku hiyo, alikumbana na watu ambao wanaelewa kifaa hicho cha 'vape' ambacho kinatumiwa na vijana wengi kuvuta tumbaku. Wataalam wanaeleza kuwa athari za kiafya za uvutaji sigara si jambo geni. Hata hivyo, licha ya ufahamu huo, bado kuna wengi wanaovuta sigara na hasa vijana na matineja wakiingilia bidhaa kama shisha hasa katika maeneo ya burudani. Pia wapo wanafunzi hata wa shule za msingi na sekondari, ambao wamenaswa wakiwa na 'vape' shuleni. Baadhi ya bidhaa hizi zimewekwa ladha tofauti kwa lengo la kuvutia wateja, bila kuelewa athari zake hasi. Mtaalam wa magonjwa ambaye pia ni mhadhiri katika mojawapo ya vyuo vikuu nchini, Dkt Valentine Budambula, anasema kuwa uvutaji aina yoyote ya tumbaku una madhara yake hata ingawaje kuna wenye fikra kuwa bidhaa kama shisha si mbaya, kutokana na dhana kuwa ni mchanganyiko wa mitishamba. "Unapozungumza kuhusu shisha, unajua kuna watu katika nchi yetu ambao hawajawahi kuiona. Lakini, katika maeneo ya Pwani, iko sana, na watu wanadhania kuwa ni mchanganyiko wa mitishamba.Wanadhania kuwa ni bora zaidi kiafya," anasema Dkt Budambula ambaye pia ni mtafiti mwenza katika utafiti ulioangazia matumizi ya shisha miongoni mwa wanachuo. "Lakini ukweli ni kuwa shisha huwa iliyotiwa ladha, au bila na tumbaku inayoandaliwa kwa njia maalum. Kwa hivyo ni tumbaku, hata tukiita kwa jina lolote lile, ni bidhaa ya tumbaku." Anaeleza kuwa kwa kawaida, huandaliwa kwa njia inayopitia kwa maji au majimaji ya aina nyingine kabla ya kumfikia mvutaji. "Na kwa sababu huwa inapitia kwa maji na majimaji ya aina nyingine, watu wengi hudhania kuwa haina madhara makubwa," anasema akieleza kuwa pia utayarishaji wake hutumia makaa, stima au hata sola, hali inayowafanya baadhi kuamini kuwa ni salama ilhali wakati huo kando na kuvuta hiyo shisha, pia unavuta moshi mwingine, kwa mfano wa makaa ikiwa ndiyo yanayotumika kuiandaa. Dkt Budambula anaeleza kuwa tumbaku si chanzo bali inachochea au kuchangia maradhi ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza. "Kwa maradhi ya kuambukiza tunaweza kusema huchangia Kifua Kikuu. Kwa yale yasiyo ya kuambukiza, ni saratani. Ikiwa unavuta sigara, tumbaku inachangia hatari ya kupata Kifua Kikuu," anaeleza. Hata hivyo, madhara ya tumbaku si kwa wanaovuta pekee, bali pia waliopo karibu na watu wanaovuta sigara kutokana na hali ya kuvuta moshi ule. "Hata tuipatie jina gani, moshi wa tumbaku una zaidi ya kemikali 7,000. Naam, zaidi ya kemikali 7,000. Baadhi yazo zinaweza kusababisha saratani au kuchangia saratani," anasema. Pia kuna zile ambazo mbali na kuchangia kansa husababisha uvimbe ambao unaweza kuwa na kansa au la. "Kisha tunastahili kufahamu kuwa, tofauti na dawa nyingine za kulevya ambapo umaskini huchangia, shisha ni ya watu wanaojiweza. Hata katika utafiti tuliofanya miongoni mwa wanafunzi, wale wenye kipato cha juu walikuwa na uwezekano zaidi wa kuvuta shisha kushinda wa kipato cha chini." Dkt Budambula anaeleza kuwa mapendekezo yake yamekuwa kupunguza mahitaji ya shisha, usambazaji na kuimarisha hamasisho kuhusu shisha, ili watu waweze kufanya maamuzi yao wakiwa na ufahamu kamili. Anasema kuwa ingawaje marufuku imeondolewa, anatumaini kuwa kutakuwa na marufuku mapya, ambayo yatakuwa wazi kuhusu bidhaa za tumbaku hasa wakati huu ambapo sigara za kisasa kama vape zinakuwa changamoto kubwa nchini. "Tunastahili kujua kwamba ni vigumu sana kuacha uvutaji sigara. Hii ni kwa sababu , unapovuta sigara, katika muda wa sekunde zisizodizi 10, dawa hiyo itakuwa kwenye ubongo wako. Ni ikiwa unajidunga ni sekunde tatu. Hii ndio sababu kujidunga na kuvuta sigara ni uraibu mgumu sana kuachana nao," anasema. Pia, anaeleza kuwa tafiti nyingine zimeonyesha kuwa, uvutaji sigara ndio njia inayofungulia utumizi wa aina nyingine ya dawa za kulevya. Dkt Budambula pamoja na dadake, Profesa Nancy Budambula, wamechapisha kitabu 'Chasing the Dragon' kilichotokana na tasnifu yake ya Uzamifu kwa lengo la kuchangia katika afya ya umma. Kitabu hicho kinazungumzia masuala hayo ya dawa za kulevya na athari zake. Katika utafiti wake kuhusu Hali ya Matumizi ya Dawa za Kulevya miongoni mwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Kenya, 2024, Mamlaka ya Kudhibiti Vileo na Dawa za Kulevya (NACADA), ilibainika kuwa mwanafunzi mmoja kwa kila tisa (asilimia 10.9) alikuwa amewahi kutumia shisha maishani mwao, mmoja kwa kila 12 (asilimia 8.6) amewahi kutumia vape, mmoja kwa kila 22 (asilimia 4.6) kutumia 'nicotine pouches', mmoja kwa kila 24 (asilimia 4.1) kunusa au kutafuna tumbaku huku mmoja kwa kila 29 (asilimia 3.3), aliwahi kutumia kuber. Pia utafiti mwingine wa Nacada ulionyesha kuwa baadhi ya watoto walianza uvutaji sigara wakiwa na umri wa chini ya miaka 10. Mnamo 2017, Kenya ilipiga marufuku shisha ambayo ni pamoja na utumizi, uagizaji, uuzaji, utangazaji na usambazaji wake. Hata hivyo, Julai 2026, marufuku hiyo iliondolewa baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu kutokana na hali kwamba kanuni za Afya ya Umma (Kudhibiti Uvutaji Shisha), 2017, zilimalizika muda wake miaka kadha iliyopita baada ya serikali kukosa kuzirasimisha kufuatia agizo la awali la mahakama la 2018. Nchini Kenya, Sheria ya Kudhibiti Tumbaku, 2007 na Kanuni za Kudhibiti Tumbaku, 2014 ndizo zimekuwa zikiendesha masuala ya tumbaku. Hata hivyo Bunge limekuwa likishinikiza marekebisho kupitia Mswada wa Kudhibiti Tumbaku, 2024, unaopendekeza adhabu kali.
read moreRight Column Content