T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 09 Oct 2026 06:55:18

Wabunge wataka IEBC ijitenge na mchujo vyamani

WABUNGE sasa wanapanga kuondoa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika usimamizi au kusikiliza migogoro inayotokana na mchujo ndani ya vyama vya kisiasa, wakisema hatua hiyo itaongeza uhuru wa vyama hivyo. Wakati wa kujadili Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa mwaka 2024, wabunge walisisitiza kuwa vyama vya kisiasa ni taasisi huru zenye haki ya kusimamia shughuli zao za ndani bila kuingiliwa na IEBC. Wanataka Sheria ya Uchaguzi ifanyiwe marekebisho ili kuondoa mamlaka ya IEBC kushughulikia migogoro ya uteuzi wa wagombea ndani ya vyama na jukumu hilo lihamishiwe Mahakama ya Kutatua Migogoro ya Uchaguzi. Kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 88 inapatia IEBC jukumu la kusimamia au kuendesha kura za maamuzi na uchaguzi. Aidha, Ibara ya 88(4)(e) inaeleza kuwa tume hiyo ina wajibu wa kushughulikia migogoro ya uchaguzi, ikiwemo inayotokana na uteuzi wa wagombea, isipokuwa kesi za uchaguzi na migogoro inayozuka baada ya kutangazwa kwa matokeo. Hata hivyo, wabunge wanasema kuhusika kwa IEBC katika mchujo wa vyama kunadhoofisha uhuru wa vyama vya kisiasa.Kwa mujibu wao, uamuzi wa kumpa mwanasiasa tiketi ya moja kwa moja au kupitia mchujo ni haki ya chama husika pekee. Kwa msingi huo, wanadai IEBC haipaswi kuwa na mamlaka ya kusikiliza malalamishi yanayotokana na maamuzi hayo.Pia walieleza kuwa kushiriki kwa IEBC katika michakato ya vyama ni sawa na kuingilia masuala ya ndani ya vyama vya kisiasa. Hoja nyingine iliyotolewa ni uwezekano wa mgongano wa maslahi. Walisema baadhi ya vyama hupatia IEBC jukumu la kusimamia mchujo kutokana na uwezo wake wa kiteknolojia na kiutawala. Hivyo, si sahihi kwa tume hiyo hiyo kusikiliza migogoro inayotokana na uchaguzi ambao imesimamia. Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria, George Murugara, alisema wabunge wanataka jukumu la IEBC katika kusuluhisha migogoro ya uteuzi lifutwe kabisa. "Tunataka kuondoa jukumu la IEBC katika kushughulikia migogoro inayotokana na uteuzi wa wagombeaji. Migogoro hiyo ishughulikiwe na Mahakama ya Kutatua Migogoro ya Uchaguzi," alisema Murugara. Mbunge wa Ugenya, David Ochieng', alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa inapaswa kuimarisha vyama ili viweze kusimamia shughuli zao kwa uhuru. "IEBC haina kazi katika uteuzi wa ndani ya vyama. Vyama ni kama vilabu. Kama chama kinaamua kunipa tiketi ya moja kwa moja, hilo ni suala lake. Kwa nini IEBC ihusike?" alihoji. Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wanawake wa Baringo, Florence Jematiah, alisema hana tatizo IEBC kusaidia vyama visivyo na uwezo wa kusimamia uchaguzi wa mchujo. Hata hivyo, alionya kuwa matatizo huibuka pale tume hiyo hiyo inapolazimika kusikiliza migogoro inayotokana na mchujo iliyoendesha. Kulingana na Mpango wa Uchaguzi wa 2025-2027 uliozinduliwa Mei, vyama vyote vinavyokusudia kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Agosti 10, 2027, vinapaswa kukamilisha mchujo na kutatua migogoro yote ifikapo Mei 9, 2027. Ratiba hiyo pia inaeleza kuwa wagombea wasioridhika na namna vyama vyao vilivyoshughulikia malalamishi yao watakuwa na hadi Juni 12, 2027 kuwasilisha kesi kwa IEBC, ambayo itatakiwa kutoa uamuzi ndani ya siku 10.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 09 Oct 2026 05:55:38

Serikali ya Sakaja yafyonza Sh125 bilioni miradi ikikwama

GAVANA wa Nairobi, Johnson Sakaja, aliingia ofisini mwaka wa 2022 akiwa na ahadi kubwa ya kuhakikisha kuwa mambo yanaenda sambamba Nairobi lakini miaka minne baadaye takwimu za matumizi ya fedha za umma zinaibua swali iwapo jiji hilo limetimiza lengo hilo. Bw Sakaja alipokuwa akihutubu wakati wa kuapishwa kwake Agosti 2022, alikumbuka maisha yake ya utotoni Ngara na jinsi alivyoshangaa kuona baadhi ya mitaa ikiwa safi, yenye barabara nzuri na iliyopangwa huku mingine ikiwa katika hali mbaya.Alisema akiwa na umri wa miaka saba aliwahamasisha watoto wenzake kuandamana wakitaka mazingira yao yaimarishwe. "Nilijifunza kuwa eneo hilo halikuwa na watu bora zaidi; walikuwa wamejipanga, walikuwa na hisia za jamii, walichagua uongozi mzuri na mambo yakawa sambamba," alisema. Hata hivyo, ripoti za matumizi zinaonyesha Nairobi bado inakabiliwa na changamoto kubwa za maendeleo. Katika miaka minne ya uongozi wa Bw Sakaja, kuanzia Julai 2022 hadi Juni 2026, serikali ya kaunti ilitumia Sh125 bilioni.Kati ya fedha hizo, Sh15.4 bilioni pekee, sawa na asilimia 12.36, zilitumika kwa miradi ya maendeleo huku Sh109.5 bilioni zikitumika katika shughuli za kawaida. Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma inataka angalau asilimia 30 ya matumizi ya kaunti yaelekezwe kwa maendeleo.Hii ina maana kuwa Nairobi ilipaswa kutumia takriban Sh37.5 bilioni kwa maendeleo, tofauti ya zaidi ya Sh22 bilioni ambazo zingetumika kujenga barabara, hospitali, masoko na miradi mingine. Kituo cha Centre for Economic Governance (CEG), kinasema Nairobi ni miongoni mwa kaunti zinazofanya vibaya zaidi katika matumizi ya fedha za maendeleo.Changamoto hiyo pia imeonekana katika miradi iliyokwama. Kufikia Juni, Nairobi ilikuwa na miradi 57 iliyokwama ya thamani ya zaidi ya Sh2 bilioni.Miongoni mwa hiyo ni jengo la matibabu la Sh256 milioni katika Hospitali ya Mbagathi, ukumbi wa kijamii wa Mwiki wa thamani ya Sh76 milioni na wodi ya uzazi ya Sh30 milioni katika Kituo cha Afya cha Umoja 1. Mdhibiti wa Bajeti, Margaret Nyakang'o, alisema miradi hiyo ilikwama kwa sababu mbalimbali, ikiwemo wakandarasi kuondoka kwa kukosa malipo. Wakati huo huo, zaidi ya nusu ya Sh125 bilioni zilizotumiwa na serikali ya Sakaja zilienda kwa mishahara na marupurupu.Takriban Sh63.3 bilioni zilitumika kwa mishahara, sawa na asilimia 50.65 ya matumizi yote. Ukaguzi pia umeibua maswali kuhusu mfumo wa malipo wa kaunti. Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilitaja Sh1.9 bilioni zilizotolewa kutoka akaunti ya mishahara bila kaunti kueleza zilitumika vipi.Aidha, Sh840.4 milioni zilizotajwa kama gharama za wafanyakazi zilikosa stakabadhi muhimu za kuthibitisha waliolipwa.Idadi ya wafanyakazi wa kaunti pia imeongezeka kutoka 13,354 mwaka 2023 hadi 19,258 Juni 2025. Katika sekta ya taka, kaunti ilitumia Sh1.7 bilioni mwaka 2024/25, huku data nyingine ya City Hall ikionyesha matumizi ya Sh3 bilioni. Mkaguzi Mkuu alisema malipo ya Sh361 milioni hayakuwa na stakabadhi za kutosha kuthibitisha huduma zilizotolewa. Nairobi pia ilitumia Sh2.6 bilioni kwa mawakili wa nje mwaka 2024/25, licha ya kuwa na zaidi ya mawakili 100 katika idara yake ya sheria. Ofisi ya Bajeti ya Bunge pia iliorodhesha Nairobi miongoni mwa kaunti zilizofanya vibaya katika matumizi ya rasilimali za umma.Nairobi inachangia karibu theluthi moja ya uchumi wa Kenya, ikiwa na shughuli za kiuchumi zenye thamani ya Sh4.1 trilioni mwaka 2024. Bw Sakaja sasa anaingia mwaka wa mwisho wa muhula wake wa kwanza huku akitakiwa kukabiliana na changamoto za mishahara, miradi iliyokwama, taka na matumizi ya fedha za umma ambazo zinaendelea kuathiri huduma kwa wakazi.

read more