T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 09 Jul 2026 08:35:33

Trump aapa kuipiga Iran mpaka isalimu amri

WASHINGTON, Amerika: JESHI la Amerika limesema lilianzisha uvamizi dhidi ya Iran ili kuhakikisha Mkondo-bahari wa Hormuz unafunguliwa kwa usafirishaji wa mafuta na bidhaa nyingine muhimu duniani. Hatua hiyo imesababisha Iran nayo kulipiza kisasi kwa kushambulia kambi za kijeshi za Amerika nchini Kuwait na Bahrain. Vita kati ya mataifa hayo mawili vimechipuka upya huku mazungumzo ya kusitisha vita kati yao yakionekana kutozaa matunda yoyote hivi karibuni. Amerika ilishambulia Iran baada ya nchi hiyo kushambulia meli za kusafirisha mizigo. Rais wa Amerika, Donald Trump tayari amesema kuwa mazungumzo ya kusaka amani na Iran yamekufa na sasa ni wakati wa kurejelea vita. "Wanajeshi wa Amerika wameanza kuendeleza mashambulizi zaidi dhidi ya Iran ili kuwalemaza wasiwe na nguvu tena ya kuzuia usafirishaji wa mafuta na mali kwenye Mlango-bahari wa Hormuz," akasema Kamanda wa jeshi la Amerika katika Ukanda wa Mashariki maarufu kama CENTOM kupitia X. "Amerika inalaumu Iran kwa kushambulia meli ambazo zilikuwa zikipitia mkondo wa Hormuz na kuhatarisha maisha ya manahodha wake," ikaongeza. Mashambulizi ya Amerika yalivuruga miji mingi Kusini mwa Pwani ya Iran huku baadhi ikikosa umeme. Iran nayo ilijibu kwa kushambulia Kuwait na Bahrain ambazo zina makao ya wanajeshi wa Amerika. Wizara ya Ulinzi ya Kuwait ilisema kuwa ilikuwa ikitungua droni na makombora kutoka Iran lakini Qatar nayo ilitoa onyo la kiusalama. Afisa mmoja wa usalama wa Amerika alisema kuwa mashambulizi dhidi ya Iran yataongezeka na kuonya kuwa mara hii wanalenga kulemaza taifa hilo kabisa kijeshi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 09 Jul 2026 07:25:24

Utafiti kuonyesha sababu zinazowafanya wanaume kufa mapema kuliko wanawake.

WANASAYANSI wameibuka na sababu kadhaa ambazo zinasababisha wanaume kufa mapema kuliko wanawake hasa yakiegemea maradhi na mtindo wa maisha. Wanawake huishi kwa miaka mingi kuliko wanaume kwa mujibu wa tafiti ambazo zimefanywa hapo awali. Kwa mfano Amerika, nchi ambayo imeendelea na ina sekta ya afya iliyoimarika ya kiafya, wanaume wengi huishi hadi miaka 76 huku wanawake wakifika miaka 81 na hata zaidi. Kwa muda sasa wanasayansi wamekuwa wakifuatilia nini husababisha hali hiyo na ikabainika kuwa magonjwa ya moyo huwaathiri wanaume wengi kuliko wanawake. Pia wanaume wanaweza kuathiriwa na unene kupita kiasi kuliko wanawake. Awali kulikuwa na dhana kuwa wanaume walikuwa wakiaga japo wana afya imara kuliko wanawake. Hii ni kwa sababu ilidhaniwa kuwa wanawake walikuwa wakifikiriwa walikuwa wakiandamwa na magonjwa yanayotokana na msongo wa mawazo. Hata hivyo, imebainika kuwa huu ni uongo na afya ya wanaume hutegemea sana mtindo wa maisha pamoja na maslahi au maisha ya kijamii. "Ni bayolojia na tabia. Tatizo ni kwamba wanaume wanasubiri ugonjwa uwalemee kabla ya kuenda hospitalini na hawamakinikii matibabu au vipimo vya kugundua maradhi mapema," akasema Mtaalamu wa Afya Dkt David Shusterman akizungumza na jarida New York Post. "Wanasubiri mpaka jambo liende mrama," Tafiti za nyuma zimeonyesha wanaume afadhali waishi kwa kutojua maradhi yanayowasibu kama kansa badala ya kupitia vipimo vinavyogundua maradhi sugu kama hayo. Kwa mujibu wa Shusterman, wanaume ambao wameoa wanaishi kwa miaka miwili zaidi kuliko wasiokuwa kwenye ndoa. "Mke anaweza kugundua mabadiliko ya kiafya ambayo mwanaume huyapuuza. Wanawake mara nyingi huwasukuma wanaume waende wapimwe na hii huwasaidia," akasema Shusterman. "Wanaume ambao hawajaoa wanaweza kufanya vizuri iwapo watamakinikia afya yao. Hoja si ndoa pekee yake bali ni uwajibikaji, kupimwa mara kwa mara na kutosubiri tatizo litokee," Aina mbalimbali za saratani, magonjwa ya moyo na unene kupita kiasi ni baadhi ya magonjwa mwanaume akimakinikia kufahamu hali yake, basi ataishi kwa miaka mingi.

read more