T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 09 Jul 2026 07:25:24

Utafiti kuonyesha sababu zinazowafanya wanaume kufa mapema kuliko wanawake.

WANASAYANSI wameibuka na sababu kadhaa ambazo zinasababisha wanaume kufa mapema kuliko wanawake hasa yakiegemea maradhi na mtindo wa maisha. Wanawake huishi kwa miaka mingi kuliko wanaume kwa mujibu wa tafiti ambazo zimefanywa hapo awali. Kwa mfano Amerika, nchi ambayo imeendelea na ina sekta ya afya iliyoimarika ya kiafya, wanaume wengi huishi hadi miaka 76 huku wanawake wakifika miaka 81 na hata zaidi. Kwa muda sasa wanasayansi wamekuwa wakifuatilia nini husababisha hali hiyo na ikabainika kuwa magonjwa ya moyo huwaathiri wanaume wengi kuliko wanawake. Pia wanaume wanaweza kuathiriwa na unene kupita kiasi kuliko wanawake. Awali kulikuwa na dhana kuwa wanaume walikuwa wakiaga japo wana afya imara kuliko wanawake. Hii ni kwa sababu ilidhaniwa kuwa wanawake walikuwa wakifikiriwa walikuwa wakiandamwa na magonjwa yanayotokana na msongo wa mawazo. Hata hivyo, imebainika kuwa huu ni uongo na afya ya wanaume hutegemea sana mtindo wa maisha pamoja na maslahi au maisha ya kijamii. "Ni bayolojia na tabia. Tatizo ni kwamba wanaume wanasubiri ugonjwa uwalemee kabla ya kuenda hospitalini na hawamakinikii matibabu au vipimo vya kugundua maradhi mapema," akasema Mtaalamu wa Afya Dkt David Shusterman akizungumza na jarida New York Post. "Wanasubiri mpaka jambo liende mrama," Tafiti za nyuma zimeonyesha wanaume afadhali waishi kwa kutojua maradhi yanayowasibu kama kansa badala ya kupitia vipimo vinavyogundua maradhi sugu kama hayo. Kwa mujibu wa Shusterman, wanaume ambao wameoa wanaishi kwa miaka miwili zaidi kuliko wasiokuwa kwenye ndoa. "Mke anaweza kugundua mabadiliko ya kiafya ambayo mwanaume huyapuuza. Wanawake mara nyingi huwasukuma wanaume waende wapimwe na hii huwasaidia," akasema Shusterman. "Wanaume ambao hawajaoa wanaweza kufanya vizuri iwapo watamakinikia afya yao. Hoja si ndoa pekee yake bali ni uwajibikaji, kupimwa mara kwa mara na kutosubiri tatizo litokee," Aina mbalimbali za saratani, magonjwa ya moyo na unene kupita kiasi ni baadhi ya magonjwa mwanaume akimakinikia kufahamu hali yake, basi ataishi kwa miaka mingi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 09 Jul 2026 06:35:03

MAONI: Si kazi rahisi kwa Natembeya kuvumisha ajenda ya Sifuna

WAFUASI wake wanamuita 'Comando' jina la utani kuashiria kuwa ni mpambanaji. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anajulikana kwa jina hilo. Ni mwanzilishi wa vuguvugu la "Tawe Movement" ambalo chimbuko lake ni kabila la waluhya kusema kukataa. Akianzisha kauli mbiu hiyo alisema kuwa jamii ya waluhya imekuwa nyuma katika uwakilishi serikalini na maeneo muhimu. Amepiga kelele kuanzia mwaka 2023 na kushika kasi zaidi miaka iliyofuatia hadi wakati huu. Sasa, Natembeya ana kazi kubwa kuuza sera ya seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwa Rais wa Kenya lakini kuu zaidi ni kuhakikisha kuwa ana mbawa nyumbani – yaani kwa jamii ya Mulembe. Katika mazishi ya kakake mbunge wa Bumula Jack Wambuko, ilikubalika kuwa Natembeya aongoze injili ya Sifuna magharibi mwa Kenya. Natembeya akakukabali na kuongoza mkutano nyumbani kwake Milimani, Kitale kuanza mchakato huo. Natembeya ni kiungo muhimu katika mkutano utakaomwidhinisha Sifuna kugombea Urais baadaye mwezi huu. Kiongozi huyo wa zamani wa kanda ya Rift Valley ana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko kutokana na athari zake za magharibi mwa Kenya. Kwanza, amefifisha umaarufu wa spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula. Hatua ya Natembeya kukubali kusimamia ajenda ya Sifuna inamsawiri kuwa mtu wa dhamira kubwa ya kuunganisha waluhya. Kwa umri, anamzidi Sifuna kwa miaka mingi tu lakini ameamua kumshika mkono mdogo wake. Wakosoaji wanashangaa sababu ya mkubwa kuonekana kuacha azma ya kuwa Rais kwa mdogo wake. Pili Natembeya ni gavana na ana eneo kubwa la usimamizi wa kaunti. Magavana huwa na uzito kushinda maseneta. Hivyo, ilitarajiwa na wengi kuwa ni Sifuna angemuunga mkono kwa sababu alikuwa ametangaza kuwa angegombea Urais. Tatu anatakiwa kufahamu kuwa safari ya umoja ya waluhya imekuwa ikikumbwa na changamoto za ubabe kati ya viongozi kutoka maeneo hayo. Safari hii alianza mwanasiasa mkongwe Masinde Muliro lakini aliyefaulu pakubwa alikuwa Michael Wamalwa Kijana katika uchaguzi mkuu wa 2002. Hivyo, Natembeya anatakiwa kuwa na mikakati zaidi ili kuvunja rekodi ya Wamalwa Kijana ambaye aliwaunganisha wenyeji wa magharibi mwa Kenya na kumpigia kura kwa fujo Mwai Kibaki na akawa Rais wa tatu wa Kenya huku Wamalwa akiwa makamu wake. Anapofanya hivyo anatakiwa kukumbuka kuwa Spika Wetangula hayumo katika usingizi, anataka Urais 2032. Mbunge Caleb Amisi amekuja na masharti yake kuhusu Linda Mwananchi. Paul Nabiswa ni mhariri, NTV

read more