T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 8 hours ago

Moto kambi ya Ruto wandani wakivurugana wakisaka ubabe

UBABE wa kisiasa kati ya mawaziri au watumishi wa umma na wanasiasa wanaoumuunga mkono Rais William Ruto unaendelea kutokota, hali inayoweza kuathiri kuchaguliwa kwake tena mnamo 2027. Mivutano hiyo imejitokeza katika maeneo ambayo Rais anatarajiwa kupata kura nyingi huku ikiwa wazi Mlima Kenya iliyokuwa ngome yake ya kisiasa inaendelea kumponyoka. Katika Kaunti ya Kakamega, mvutano kati ya Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na Gavana Fernandes Barasa umetokota na kufikia kilele. Bw Barasa amemtaka Rais Ruto amtimue Bw Oparanya, akidai waziri huyo amekuwa akifanya mikutano ya usiku kupanga njama za kumng'oa 2027. "Namwambia Rais Ruto kwamba tunamheshimu, lakini hapa Kakamega umetuletea mzozo kupitia Waziri Oparanya, ambaye hajui kazi yake wala haelewi majukumu yake. Kazi yake hapa ni kufanya mikutano ya usiku ya kuniondoa madarakani na kunipangia mabaya. Kazi uliyompa haitusaidii. Tafadhali mpe mtu mwingine," akasema Bw Barasa. Gavana huyo pia anadai Bw Oparanya anamuunga mkono Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kakamega Elsie Muhanda kuwania ugavana. Bw Oparanya, aliyekuwa gavana wa Kakamega kati ya 2013 na 2022, amekanusha madai hayo akisema hana mgombea anayemuunga mkono. Alimtaka Bw Barasa kujikita katika kutetea kiti chake. "Anaonekana kupigana vita na nafsi yake kwa sababu yeye si mtu wa hadhi yangu kisiasa. Kwa nini nimfadhili mtu ampinge? Uchaguzi ni wa ushindani na ikiwa anaogopa ushindani basi aachane na siasa," akasema Bw Oparanya kwenye mahojiano na Taifa Leo. Mbunge wa Khwisero Christopher Aseka pia alimkosoa Bw Barasa, akisema rekodi yake ya maendeleo si ya kuridhisha. "Amewahi kufanya nini kuhusiana na masuala ya maendeleo? Amekuwa akiorodheshwa vibaya katika maendeleo na miradi mingi iliyoanzishwa na Oparanya haijakamilika. Rekodi ya Barasa katika maendeleo ni duni na hatutamruhusu kuendeleza siasa za chuki hadi kumtaka Rais amtimue Oparanya," akasema Bw Aseka. Kajiado pia imekuwa uwanja wa mzozo kati ya Msimamzi wa Wafanyakazi Ikulu Katoo ole Metito na Gavana Joseph Ole Lenku, ambao wote waligombea ugavana 2022. Bw Lenku, anayelenga sasa kiti cha useneta, amepinga mpango wa kisiasa wa UDA na ODM unaomuunga mkono Bw Metito kugombea ugavana na Judy Pareno kuwania useneta. Pia ametishia kuondoka ODM na kujiunga na Linda Mwananchi. "Kuna mtu anatudharau mbele yako, lakini hatutavuruga mkutano wako wala kulipiza kisasi. Katoo anadai kuwa msemaji wa Wamaasai ilhali yeye ni msemaji wako. Walisema pia Amboseli haitarejeshwa kwa jamii, lakini neno lako ndilo la mwisho," akasema Bw Lenku wakati wa mkutano wa Rais katika kaunti yake wikendi. Katika Bonde la Ufa, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen anakabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wanaodai anawadhamini wagombeaji ili kuwa na ushawishi eneo hilo baada ya Rais Ruto. Mbunge wa Keiyo Kusini Gideon Kimaiyo mnamo Agosti 5 alikerwa na Bw Murkomen na akasema Kaunti ya Elgeyo-Marakwet si himaya yake kisiasa. "Elgeyo-Marakwet haitakuwa ufalme wa mtu yeyote, wala hatafanikiwa na mipango yake Keiyo Kusini. Ikiwa unataka kuwa kinara, pigana na wanaowania nafasi hiyo pamoja nawe, si Keiyo Kusini," akasema Bw Kimaiyo. Seneta wa Nandi Samson Cherargei pia alimtaka Bw Murkomen kuweka kando ndoto zake za 2032 na kumsaidia Ruto katika uchaguzi wa 2027. "Aweke kando kwa sasa ndoto zake za 2032 na za kuwa kinara, na amsaidie Rais. Hawezi kupigania kuwa msemaji wa jamii wakati tuna Rais Ruto," akasema. Busia nako hali si tofauti, Katibu Mkuu wa Biashara Ndogo Ndogo Susan Mangéni naye akimshambulia aliyekuwa Waziri wa Michezo Ababu Namwamba, akidai anapinga kuchaguliwa kwa Rais Ruto kichinichini. "Ababu Namwamba, unapinga kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto kwa sababu umeumia. Watu wa Budalang'i hawataendelea kuishi katika umaskini wa kudumu kwa sababu ya ubinafsi wako. Wewe si Budalang'i na Budalang'i si wewe," akasema Bi Mangéni. Wawili hao wamekuwa na uhasama mkali kuhusiana na siasa za UDA.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Sifuna awatikisa Mudavadi, Atwoli; waanza ziara Magharibi kumtetea Ruto kwa wananchi

WIMBI la kisiasa la Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kupitia vuguvugu la Linda Mwananchi limewafanya baadhi ya viongozi wakuu wa serikali kutoka eneo la Magharibi kuanza kampeni kali kwa Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027. Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambaye amekuwa akijiepusha na shughuli za kisiasa, ameanza ziara za mashinani kuimarisha uungwaji mkono wa chama tawala cha UDA. Mwishoni mwa wiki, Bw Mudavadi alikutana na waliowania tiketi za UDA kutoka Magharibi, huku Katibu Mkuu wa Cotu-K Francis Atwoli akiwa miongoni mwa waliohusika na mikakati ya kupanga mkutano huo. Mnamo Jumatatu, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya pia alikutana na wabunge 25 kutoka Magharibi jijini Kisumu kujadili jinsi ya kumfanyia Rais Ruto kampeni. "Tulikutana kujadili masuala yanayohusu uchaguzi ujao na jinsi tunavyoweza kujiweka vyema kama jamii," akasema Bw Oparanya. Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula nao wamebuni kikosi cha kampeni kinacholenga Magharibi na Nyanza, kwa lengo la kuimarisha uungwaji mkono kwa Rais Ruto. Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema shughuli hizo zinaonekana kulenga kukabili kuongezeka kwa ushawishi wa mrengo wa Linda Mwananchi. Azma ya Bw Sifuna kuwania urais imeibua msisimko katika eneo hilo, huku kukiwa na hofu kwamba vuguvugu hilo linaweza kutokomeza umaarufu wa ODM na pia UDA. Bw Mudavadi alisema uchaguzi wa 2027 utahitaji maandalizi mazuri, akiwataka wagombea wa UDA kuimarisha miundo ya chama mashinani na kuhakikisha usajili wa wapigakura unaongezwa. Alikadiria kuwa kuna wapiga kura milioni 1.5 wenye vitambulisho ambao bado hawajajisajili kutoka eneo la Magharibi. "Njia ya kuelekea 2027 haitashindwa kwa kelele, bali kwa mpangilio, uaminifu na kura," akasema. Bw Atwoli aliwataka wagombea kumuunga mkono Bw Mudavadi kama kinara wa kisiasa wa eneo hilo, akisema Bw Sifuna bado hajatosha mboga. "Yeye atakuwepo baada yetu, lakini wakati wake si sasa," akasema Bw Atwoli. Hata hivyo, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi anayeegemea mrengo wa Linda Mwananchi alipuuzilia mbali mkutano huo, akisema hauwatikisi. Alisema UDA imepoteza umaarufu Magharibi na ndio maana mkutano huo ulifanyika Kisumu badala ya mji wa Magharibi. "Wameingiwa na hofu na unaweza kuona kukata tamaa katika shughuli zao. Eneo hili lina maeneobunge 33, lakini uliuona idadi ya wagombea waliohudhuria mkutano huo," akasema.  Bw Osotsi alidai kuwa baadhi ya viongozi na wagombea kutoka eneo hilo wanasubiri tu chama kipya cha Linda Mwananchi kuanzishwa rasmi ili waondoke UDA na ODM. Hata hivyo, Bw Wandayi na Bw Savula wamesisitiza kuwa wataendelea kuwarai wenyeji wa Magharibi na Nyanza kumuunga mkono Rais Ruto, wakisema uongozi wake ndio utahakikisha maendeleo zaidi katika maeneo hayo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 10 hours ago

Wageni waingiwa na taharuki tele kutokana na agizo la Rais Ruto

MAMIA ya raia wa kigeni wanaofanya biashara nchini jana waligubikwa na taharuki na wasiwasi baada ya Rais William Ruto kuamuru msako dhidi yao hasa wale wanaofanya biashara ndogondogo. Amri hiyo iliyotolewa wiki jana Septemba 2 wakati wa mkutano na wafanyabiashara wadogo (MSME) ilisababisha pilkapilka za kukimbilia stakabadhi za kusafiri, baadhi ya biashara kufungwa na ripoti za vitisho na kuhangaishwa katika sehemu mbalimbali nchini. Mtanziko huo ulitokana na kile wanachosema raia wa kigeni walielewa kama amri ya kuondoka na ufafanuzi uliofuata kutoka kwa serikali kwamba msako huo unalenga wale wanaoendesha shughuli kinyume cha masharti ya uhamiaji, kibali cha kazi na sheria nyinginezo. Jijini Nairobi, raia wa Burundi waliojawa wasiwasi walipanga foleni nje ya ubalozi wao jana, baadhi wakisaka stakabadhi za dharura kusafiri kurejea makwao huku wengine wakitafuta msaada wa kuhalalisha biashara zao na kuendelea kuwepo nchini. Matukio hayo yaliashiria suitafahamu iliyofuatia matamshi ya Rais huku raia wa kigeni wanaofanya biashara wakichanganyikiwa kuhusu iwapo waliagizwa kuondoka nchini au wanahitajika kuhalalisha biashara na hadhi yao ya uhamiaji. Nchini kote, wasiwasi uligeuka hofu ikiripotiwa kuwa raia wa kigeni walichelea kufungua biashara zao, kuacha makao yao na katika baadhi ya maeneo madai ya kuhangaishwa na wizi. Serikali, hata hivyo, inasisitiza msako huo si amri ya kuwafurusha raia wa kigeni nchini. Maafisa wanasema wanaolengwa ni wale wanaoendesha biashara zao bila vibali vya kazi, leseni au hadhi ya uhamiaji inayohitajika, huku raia wa kigeni wafanyabiashara waliosajiliwa wakilindwa. Jijini Nairobi, mamia ya raia wa Burundi walijitokeza katika ubalozi wao wakisaka stakabadhi za usafiri na msaada, huku baadhi wakisema wanajiandaa kurejea makwao kwa sababu hawahisi kuwa salama tena kenya. Foleni ndefu zilipangwa nje ya balozi huku wafanyabiashara waliozongwa na wasiwasi wakiitisha ufafanuzi kuhusu hatima yao. Katika Ubalozi wa Burundi, baadhi ya raia waliozungumza na vyombo vya habari walisema waliondoka nchi yao kusaka nafasi za kitega uchumi na waligeuza Kenya kuwa makao yao ya pili. "Nchi yetu ni ndogo, tunakabiliwa na ukosefu wa ajira na hatuna shughuli nyingi zinazofanyika ndiposa tuling'ang'ana kuja Kenya kuyainua maisha yetu. Tumewajua Wakenya kama watu wa amani na taifa bora Afrika lakini sijakula kwa siku mbili nilipojua tunatimuliwa," akasema Erick Bizimana, aliyekuja Kenya 2022. Mjini Murang'a, Jean Niyonzima, 28, ambaye amechuuza kahawa na mandazi kwa miaka mitano alisema alisimamishwa na maafisa wawili wa polisi Septemba 6 akidai alilazimishwa kusalimisha Sh3,000. Mfanyabiashara mwengine Esperance Ndayishimiye, 24, anayeuza mavazi ya wanawake Murang'a, alisema hali imevurugika. Homa Bay, raia kadhaa wa kigeni waliripoti biashara zao kuvunjwa na mali ikiwemo vifaa vya simu, viatu na nguo kuibiwa. Mfanyabiashara raia wa Rwanda Zarubbabel Rusesabagina alisema alipoteza sehemu kubwa ya mali yake ikiwemo pasipoti, kadi ya ATM, vitambulisho na Sh16,000 pesa taslimu. Mjini Kisii, wafanyabiashara wengi raia wa Uganda, Burundi na Rwanda hawakufungua biashara zao jana wakihofia kukamatwa na mali yao kuporwa. Miji ya Narok, Kericho, na Bomet, raia wa kigeni wachuuzi pia walijiepusha kwenda barabarani huku baadhi wakiripotiwa kusafiri Nairobi kuwasilisha malalamishi kwa serikali. Jijini Mombasa, raia wengi wa kigeni ambao kwa kawaida huchuuza bidhaa au kufanya kazi katika vinyozi, hoteli na vituo vya kuoshea magari hawakuwepo pia. Lakini mjini Nyahururu, baadhi ya wanafanyabiashara waliapa kuwalinda raia wa kigeni ambao wameishi nao kwa miaka mingi. "Tumeishi nao kwa miongo mingi, watoto wetu wanasoma pamoja shuleni. Wengi wao walizaliwa na kulelewa hapa, ni nyumbani ya pekee wanayojua, amri ya rais haina uhalisia," akasema mfanyabiashara Philip Kahome. Waziri wa Biashara Lee Kinyanjui alisema baadhi ya raia wa kigeni wanatumia vibaya hati za kusafiria na mipango ya kuingia nchini kwa kushiriki biashara wakiwa kwenye hadhi ya mwekezaji au mtalii bila vibali vya kazi vinavyohitajika. Bw Kinyanjui alisema raia wa kigeni watakaopatikana wakikiuka masharti ya uhamiaji watapokonywa hati zao kulingana na sheria. Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Abraham Korir Sing'oei vilevile aliwahakikishia raia wa kigeni kwamba matamshi ya Rais hayapaswi kufasiriwa kama amri ya jumla dhidi ya raia wote wa kigeni wafanyabiashara. Alisema wafanyabiashara wadogo na wakubwa na waajiriwa wa mataifa yote walio na stakabadhi zinazohitajika, ikiwemo vibali vya kazi wamelindwa kisheria kuendesha shughuli zao Kenya.

read more