T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 19 Jul 2026 12:40:33

Fedha za kilimo zinufaishe wakulima wa mashamba madogo

MASHIRIKA ya kifedha yamehimizwa kubuni upya huduma za ufadhili wa kilimo ili ziambatane na hali halisi ya wakulima, vijana, wanawake wajasiriamali na masoko ya chakula badala ya kuzingatia utoaji wa mikopo pekee. Wito huo ulitolewa wakati wa mkutano wa Financing Agri-Food Systems Sustainably (FINAS) 2026 uliofanyika Nairobi chini ya kaulimbiu "Towards Sustainable Financial Architecture for Africa's Food Systems." Mkutano huo ulileta pamoja serikali, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo na wadau wa kilimo kujadili mbinu za kuwekeza katika mifumo imara ya chakula. Mkurugenzi Mkuu wa Heifer International Kenya, Wairimu Munyinyi-Wahome, alisema huduma za kifedha zinapaswa kuzingatia misimu ya uzalishaji, uwezo wa biashara, fursa za masoko na hatari zinazowakabili wakulima. [caption id="attachment_190271" align="aligncenter" width="300"] Mkurugenzi Mkuu wa Heifer International Kenya, Wairimu Munyinyi-Wahome akizungumza jijini Nairobi. Picha|Sammy Waweru[/caption] "Kwa muda mrefu tumekuwa tukihoji kama wakulima wanafaa kupewa mikopo. Swali muhimu ni kama mifumo yetu ya kifedha iliundwa kuambatana na uhalisia wa kilimo," alisema. Aliongeza kuwa mfumo bora wa kifedha unapaswa kuendana na kilimo, badala ya kulazimisha wakulima kufuata masharti magumu kama dhamana, ratiba zisizobadilika za malipo ya mikopo na historia rasmi ya mikopo. Kwenye kongamano na FINAS 2026, Heifer ilieleza kuwa imejikita katika kuunganisha ufadhili na ujuzi, kuongeza uzalishaji, kuimarisha usawa wa kijinsia katika huduma za kifedha na kusaidia vijana pamoja na wakulima wadogo kupata uwekezaji wa kibiashara. Mkurugenzi Mkuu wa Heifer Rwanda, Verena Ruzibuka, alisema ubunifu mwingi unaoanzishwa na vijana unahitaji msaada zaidi ili kukua na kuwa biashara zinazowanufaisha wakulima. "Mpango wa AYuTe Africa NextGen unaowapa wabunifu wa teknolojia za kilimo ufadhili, mafunzo, ushauri na masoko, umeonyesha jinsi ya kufadhili wakulima," alitaja. [caption id="attachment_190274" align="aligncenter" width="300"] Baadhi ya wakulima walionufaika mwaka huu 2026 kupitia mpango wa AYuTE wa Heifer Kenya ambao hulenga kupiga jeki vijana wenye bunifu mbalimbali za kilimo. Picha|Sammy Waweru[/caption] Mkurugenzi wa Ubunifu wa Fedha wa Heifer Afrika, Wangui Muna, alisema matumizi ya teknolojia na takwimu sahihi yatapunguza hatari za utoaji wa mikopo na kuongeza upatikanaji wa bidhaa za kifedha zinazofaa sekta ya kilimo. Mkutano huo pia ulitumika kuzindua Agricultural Finance Technical Working Group, kundi la kiufundi la fedha litakalosaidia kuimarisha sera na kanuni za ufadhili wa kilimo kwa kutumia ushahidi wa kisayansi. Aidha, kundi hilo linaongozwa na Kenya Bankers Association kwa ushirikiano na GIZ, FSD Kenya, Africa Guarantee Fund, Heifer International na Aceli Africa. Mkurugenzi wa Sera wa Aceli Africa, Titianne Donde, alisema taarifa na takwimu zilizopo zinapaswa kutafsiriwa kuwa sera zitakazochochea uwekezaji katika kilimo. [caption id="attachment_190275" align="aligncenter" width="300"] Heifer Interntanional inahimiza mashirika ya kifedha kubuni upya huduma za ufadhili wa kilimo ili ziambatane na hali halisi ya wakulima, vijana, wanawake wajasiriamali na masoko ya chakula badala ya kuzingatia utoaji wa mikopo pekee. Wengi wa wanaokuza kabichi ni wakulima wa mashamba madogo hivyo basi wanahitaji kupigwa jeki kifedha. Picha|Sammy Waweru[/caption] Kulingana na Wairimu Munyinyi-Wahome, Heifer itaendelea kushirikiana na wadau kubuni mifumo ya kifedha itakayowawezesha wakulima, vyama vya ushirika, wanawake na vijana kujenga biashara imara na endelevu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 19 Jul 2026 09:00:42

Kanuni zinazokwamisha ubunifu wa kilimo Afrika

AFRIKA haina upungufu wa teknolojia za kilimo zinazoweza kusaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuanzia mbegu za mahindi zinazostahimili ukame, ngano inayovumilia joto kali, mifugo bora hadi teknolojia za kidijitali zinazosaidia kufanya maamuzi ya kilimo, watafiti tayari wamebuni suluhu nyingi za kuongeza uzalishaji wa chakula. Hata hivyo, wataalamu wanasema changamoto kubwa si ukosefu wa teknolojia bali ni mifumo ya udhibiti inayochelewesha usambazaji wake kati ya nchi za Afrika, hali inayonyima mamilioni ya wakulima fursa ya kupata kwa wakati ufaao suluhu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Wakizungumza katika mkutano wa DialogueNEXT Africa ulioandaliwa na World Food Prize Foundation jijini Nairobi, wataalamu wa sayansi, watunga sera na viongozi wa sekta ya kilimo walisema kanuni zilizopitwa na wakati zimekuwa kikwazo kikubwa kwa usalama wa chakula na juhudi za kukabiliana na tabianchi. Mshindi wa World Food Prize mwaka 2017 na rais wa zamani wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt Akinwumi Adesina, alisema Afrika haiwezi kuendelea kuchelewesha matumizi ya teknolojia ambazo tayari zimethibitishwa kufanya kazi. "Tatizo si ukosefu wa teknolojia. Tunajua kinachofanya kazi. Changamoto ni ukosefu wa kuungwa mkono na ulingo wa kisiasa ambao hutunga sheria na mifumo ya udhibiti inayochelewesha kuwafikishia wakulima teknolojia hizo," alisema. Alieleza kuwa nchi nyingi hulazimisha aina mpya za mazao kufanyiwa majaribio kwa miaka kadhaa kabla ya kuruhusiwa kulimwa kibiashara. Mara nyingi majaribio hayo hurudiwa katika nchi jirani hata kama zina mazingira yanayofanana. Kulingana na Dkt Adesina, teknolojia zinapaswa kuidhinishwa kulingana na maeneo ya kiikolojia badala ya mipaka ya kisiasa. "Ukame hausafiri kwa pasipoti, wadudu waharibifu hawahitaji visa, na mabadiliko ya tabianchi hayaheshimu mipaka ya nchi. Kanuni zetu zinapaswa kutambua ukweli huo," alisema. [caption id="attachment_190266" align="aligncenter" width="300"] Baadhi ya wadau kutoka sekta ya kilimo wakati wa mkutano wa DialogueNEXT Africa ulioandaliwa na World Food Prize Foundation jijini Nairobi. Picha|Sammy Waweru[/caption] Aliongeza kuwa Afrika hupoteza karibu Dola 7 bilioni (sawa na Sh906 bilioni thamani ya Kenya) kila mwaka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kiwango kinachotarajiwa kuongezeka hadi Dola 50 bilioni (sawa Sh6.47 trilioni thamani ya Kenya) ifikapo mwaka 2050 iwapo hatua za kukabiliana nazo hazitaharakishwa. Alieleza kuwa teknolojia kama vile mbegu zinazostahimili ukame, ngano inayostahimili kiwango cha joto cha juu, mifumo ya kidijitali ya ushauri wa hali ya hewa na bima ya mazao, tayari zinasaidia kupunguza hasara kwa wakulima. Hata hivyo, ukumbatiaji wa matumizi ya bima ya mazao na mifugo nchini Kenya bado uko chini ya asilimia moja. Aidha, alisema soko la kilimo Afrika linatarajiwa kufikia Dola 1 trilioni (sawa Sh129.5 trilioni za Kenya) ifikapo mwaka 2030. "Matajiri wakubwa wa baadaye Afrika watatoka katika sekta ya kilimo kwa sababu kila mtu anahitaji chakula," Dkt Adesina alisema. Naye Profesa Ruth Oniang'o, mtaalamu wa masuala ya kilimo na lishe, alisema teknolojia nyingi haziwafikii wakulima wadogo kwa sababu ya mifumo dhaifu ya usambazaji, uwekezaji mdogo na mawasiliano hafifu kati ya watafiti, maafisa wa nyanjani na wakulima. [caption id="attachment_190267" align="aligncenter" width="300"] Prof Ruth Oniang'o na mwasisi wa African Journal of Food, Agriculture, Nutrition and Development, akizungumza wakati wa DialogueNEXT Africa ulioandaliwa na World Food Prize Foundation jijini Nairobi. Picha|Sammy Waweru[/caption] "Sayansi inapaswa kuelezwa kwa lugha rahisi ili wakulima waweze kuielewa na kuitumia," Prof Ruth alisema, akionya kuwa usalama wa chakula haupaswi kupimwa kwa uzalishaji pekee bali pia kwa ubora, usalama na lishe ya chakula. Alitaja tatizo la sumu kuvu (aflatoxin) kwenye mahindi nchini Kenya kama mfano wa changamoto zinazoweza kudhibitiwa kupitia matumizi ya teknolojia bora. Washiriki wa mkutano huo wa DialogueNEXT Africa walionya kuwa bila kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika kanuni za udhibiti na kukumbatia bioteknolojia pamoja na ubunifu mwingine wa kisayansi, Afrika itapoteza fursa muhimu ya kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kukuza uchumi kupitia kilimo.

read more