T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 19 Jul 2026 21:55:09

Huenda Gachagua akawa debeni 2027 baada ya ushauri uliotolewa na Mwanasheria Mkuu

MAKAHAMA ya Juu imeamuru Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor kutoa ushauri kuhusu mtanziko wa kikatiba unaohusu iwapo maafisa wa serikali waliotimuliwa wanaweza kuwania chaguzi huku wakipinga kufurushwa kwao kortini. Korti Ijumaa iliyopita iliagiza Mwanasheria Mkuu kutoa ushauri katika siku 21. Jopo liliwasilisha suala hilo kwa Mwanasheria Mkuu huku likichelewesha uamuzi muhimu ambao huenda ukaathiri chaguzi kuu zijazo za urais 2027. Kesi hiyo ina umuhimu kwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, aliyekuwa gavana wa Meru, Kawira Mwangaza na aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko, ambao kung'olewa kwao afisini kumezua makabiliano ya muda mrefu kortini. Kiini cha kesi hiyo ni kuhusu iwapo viongozi waliofurushwa kutoa afisi za umma kupitia mchakato wa sheria wanaweza kuwania afisi za uchaguzi kabla ya kesi zao za rufaa kukamilika. Bw Gachagua alitimuliwa na Bunge la Kitaifa 2024 kabla ya kuwasilisha kesi kortini kupinga uhalali wa kumfurusha. Mvutano huo unaendelea katika Mahakama ya Rufaa. Ni miongoni mwa wapeperushaji bendera wanaodhamiria kupinga kuchaguliwa tena kwa Rais William Ruto, katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2027. Bi Mwangaza alitemwa kama gavana wa Meru Agosti 2024 baada ya Seneti kupitisha uamuzi wa bunge la kaunti kumng'atua mamlakani, na kuzua kesi tofauti kortini kuhusu mchakato. Bw Sonko alitimuliwa kama gavana wa Nairobi 2020 na akaendelea kukabiliana kisheria kuhusu ufurushaji wake huku akijihusisha na siasa. Kufuatia kubanduliwa kwao walianzisha vyama tofauti vya kisiasa, huku Bw Gachagua akiwa kinara wa Democracy for the Citizens Party (DCP), Bw Kawira Umoja na Maendeleo Party (UMP) huku Sonko akiongoza National Economic Development Party (NEDP). Kesi iliyo mbele ya Mahakama ya Juu iliwasilishwa na Spika wa Bunge la Kaunti ya Meru, Ayub Bundi Solomon, Aprili 2026 kwa namna ya ushauri wa kurejelewa, akiomba korti hiyo kutafsiri Sura ya Sita ya Katiba pamoja na Vifungu 99 na 193 vinavyosimamia kufuzu na kung'olewa kutoka afisi ya uchaguzi. "Haya ni marejeleo kuhusu ushauri. Marejeleo haya yanatokana na utata ambao haujatatuliwa katika kitovu cha mfumo wa uongozi na uadilifu chini ya Sura ya Sita ya Katiba," anasema. Katika kesi iliyowasilishwa Aprili 10, 2026, Bw Bundi alihoji kuwa amri za korti zinazofutilia mbali ufurushaji zikisubiri rufaa, kimtindo, zimeruhusu maafisa walioondolewa kwa mashtaka ya uadilifu, ikiwemo kutimuliwa, kubaki waliofuzu kwa chaguzi huku kesi zikiendelea. Alifafanua kuwa miaka 15 tangu katiba mpya ilipozinduliwa 2010, "bado hakuna tafsiri thabiti kuhusu ikiwa katiba inabuni kiwango mwafaka kinachoeleweka kuhusu uongozi wa umma hasa kuhusu namna kiwango hicho kinatumika kwa watu waliong'atuliwa afisini." Badala ya kusuluhisha masuala hayo kikatiba papo hapo, jopo la majaji watano wakiongozwa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu waliagiza Spika Bundi kwanza apate ushauri kisheria kutoka kwa Mwanasheria Mkuu kabla ya kesi hiyo kuendelea kusikizwa. "Mlalamishi ameagizwa kutafuta ushauri wa mwanasheria mkuu, na ushauri huo utolewe katika muda wa siku 21 kuanzia tarehe ya uamuzi huu," iliamuru korti. Majaji wengine wa jopo hilo ni Smokin Wanjala, Isaac Lenaola, William Ouko na Mohamed Warsame. Majaji waliagiza kuwa marejeleo na uamuzi uwasilishwe kwa mwanasheria mkuu na kwamba suala hilo lirejeshwe mbele ya Naibu Msajili baada ya kutimiza masharti hayo. Uamuzi huo vilevile uliahirisha kusikiza ombi lililowasilishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka na Tume ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi kujiunga na kesi hiyo. Tume hizo mbili ziliwasilisha ombi kushirikishwa kwa sababu ya majukumu yake kikatiba kuhusu kufuzu kwa mgombea na matakwa ya uadilifu. Spika alihoji kuwa maoni ya Mwanasheria Mkuu kabla ya kuwasilisha marejeleo hayakuwa lazima. Mawakili wake walisisitiza kwamba ushauri tofauti uliotolewa na Korti ya Juu 2024 uliashiria kwamba mchakato si lazima na kwamba muundo wa ugatuzi ulifanya mkondo huo kukosa ustawishaji katika hali hiyo. Majaji walipinga hoja hiyo. "Kanuni 53 ya Sheria za Korti ya Juu 2020, pamoja na orodha ya mamlaka alizonukuu mlalamishi, zinaweka bayana mahitaji ya kutafuta ushauri wa mwanasheria mkuu kabla ya kuwasilisha marejeleo," korti ilisema. Majaji walisema ushauri kama huo, "huenda ukasuluhisha swali lililo mbele yetu kwa namna inayoridhisha mlalamishi, hivyo kuokoa muda muhimu wa korti." Aidha, walihoji kuwa mzozo wa sasa unatofautiana pakubwa na ushauri wa awali kwa sababu mwanasheria mkuu alikuwa mlalamishi katika kesi hiyo na hivyo basi hangetarajiwa kushauri afisi binafsi. Mahakama vilevile ilipuuzilia mbali hoja kuwa mfumo wa ugatuzi unamzuia mwanasheria mkuu kutoa ushauri kuhusu suala hilo. "Mfumo wa ugatuzi jinsi ulivyoundwa kwa sasa haumfungii nje mwanasheria mkuu kutoa ushauri, hasa kwa suala linalohusu umma," majaji walisema. Korti ya juu haikotoa maoni yoyote kuhusu ikiwa maafisa waliong'olewa au kuondolewa mamlakani wanaweza kuwania chaguzi kesi zao za rufaa zikiwa bado hazijakamilika. Badala yake, ilijikita kwenye suala la mchakato lililowasilishwa kwake na kuamuru mwanasheria mkuu kutoa ushauri kwanza kabla ya kikao chochote kuhusu masuala nyeti kikatiba kuendelea. Kesi hiyo imepangiwa kutajwa Agosti

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Vijana waingizwa katika biashara za ngono ajira ikiadimika nchini

UKOSEFU wa ajira unaozidi kushuhudiwa nchini umeanza kuwasukuma vijana wengi kuingia katika biashara haramu huku baadhi wakitumbukia kwenye mitandao ya utengenezaji wa filamu za ngono zinazouzwa kwa wateja wa mataifa ya kigeni. Katika mwezi mmoja uliopita pekee, maafisa wa polisi wamevamia nyumba kadhaa katika kaunti za Kiambu, Nairobi, Kajiado na Nakuru na kuwaokoa zaidi ya wanawake 50 waliokuwa wakidaiwa kulazimishwa kutengeneza filamu za ngono. Hii ni baada ya kudanganywa kwa ahadi za ajira zenye mishahara minono. Wiki nne zilizopita, polisi walivamia nyumba moja eneo la Ngoigwa, Thika, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wakazi. Vijana kadhaa wenye umri wa kati ya miaka 18 na 30 walikamatwa wakishukiwa kutengeneza filamu za ngono zilizokusudiwa kuuzwa katika masoko ya nje ya nchi. Polisi walinasa kompyuta, kamera na vifaa vingine vilivyokuwa vikitumiwa kurekodi filamu hizo. Miezi michache kabla ya hapo, maafisa wa Idara ya Upelelezi (DCI) walivunja mtandao mwingine jijini Nakuru baada ya kuvamia sherehe ya ngono katika eneo la Naka Estate. Mfanyabiashara mmoja alikamatwa akishukiwa kuwavutia vijana, wakiwemo wasichana wa shule wenye umri wa miaka 13 hadi 17, kushiriki katika kurekodi filamu ya ngono zilizokuwa zikununuliwa barani Ulaya. Mnamo Julai 21, DCI iliwaokoa wanawake watano waliokuwa wakizuiliwa katika nyumba moja eneo la Mihang'o, Embakasi Mashariki, Nairobi. Uchunguzi ulionyesha kuwa walikuwa wameahidiwa kazi zenye mishahara mizuri lakini badala yake wakalazimishwa kutengeneza filamu ya ngono kwa ajili ya biashara ya mtandaoni. "Waathiriwa walidanganywa kwa ahadi za ajira zenye mapato mazuri lakini wakageuzwa watumwa wa kutengeneza filamu ya ngono kwa manufaa ya biashara," akasema Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin. Siku tatu baadaye, polisi waliwaokoa wanawake wengine 48 katika maeneo ya Ongata Rongai na Kiserian, Kaunti ya Kajiado, walikokuwa wakishikiliwa na magenge mawili yanayoshukiwa kujihusisha na biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu na unyanyasaji wa kingono. Moja ya nyumba hizo ilikuwa imegeuzwa studio ya kisasa ya kamera za mtandaoni yenye kompyuta, kamera na vifaa vya kurusha matangazo ya moja kwa moja kwa wateja wa ng'ambo. Kwa mujibu wa wachunguzi, magenge hayo huwavutia vijana wasiokuwa na ajira kwa matangazo ya kazi kama watayarishaji wa filamu, wapiga picha, wanamitindo, wasaidizi wa masoko ya kidijitali au wafanyakazi wa nyumbani. Wakishakubali kazi hizo, huzuiliwa katika nyumba za kupanga na kulazimishwa kushiriki katika biashara hiyo haramu. "Magenge haya yanatumia ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha kama silaha. Vijana huahidiwa mishahara mikubwa, safari za nje ya nchi na nafasi za kazi, lakini baadaye hulazimishwa kutengeneza filamu za ngono," akasema afisa mmoja mkuu wa DCI aliyeomba kutotajwa. Maafisa wa upelelezi pia wamebaini kuwa baadhi ya washukiwa hutuma fedha kupitia simu au zawadi za thamani ili kujenga uaminifu kwa waathiriwa kabla ya kuwalazimisha kutuma picha na video za ngono. DCI imesema mitandao hiyo sasa inaendesha shughuli zake katika miji ya Nairobi, Nakuru, Kisumu, Eldoret na Thika. Imetoa wito kwa vijana kuwa waangalifu wanapotafuta ajira na kuhakikisha wanathibitisha waajiri kabla ya kukubali ofa yoyote.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Hofu tele mauaji ya usiku yakitanda vijijini Kwale

WAKAZI wa vijiji vinavyopakana na misitu iliyo Mangawani, Kaunti ya Kwale, wanaishi kwa hofu ya mashambulio ya kihalifu ambayo yametanda kwa miaka kadha. Wakazi hao wameeleza hofu kutokana na mfululizo wa mauaji ya kikatili na wizi unaodaiwa kufanywa na genge la wahalifu ambalo hufanya mashambulio usiku na kutoweka katika misitu inayozunguka vijiji hivyo. Kulingana nao, washambuliaji hao hujitokeza kati ya saa mbili na saa tatu usiku, wakiwavamia watu wanaorejea nyumbani kutoka shughuli zao za kila siku. Wakiwa wamejihami kwa mapanga, washambuliaji hao hudaiwa kuwajeruhi au kuwaua waathiriwa kwa haraka kabla ya kutoweka ghafla. Bw Kisilu Mbai, 86, alisema kutokujulikana kwa wahusika wala nia yao ni jambo la kutisha sawa na mauaji yenyewe. "Inashangaza kuwa wahusika hawawezi kupatikana. Tumekuwa tukisihi serikali itusaidie kuwapata, ili angalau tujue ni kina nani," anasema. Katika vijiji 17 vya Mangawani na maeneo jirani, baadhi ya wakazi wanaamini wahalifu hao hujificha katika misitu, huku wengine wakishuku kuwa ni watu kutoka maeneo ya nje wanaoingia vijijini kupanga mashambulizi kabla ya kutoroka. Mauaji hayo pia yamehusishwa na migogoro ya kifamilia, mizozo ya urithi na uhasama wa muda mrefu wa kijamii, ingawa madai hayo hayajathibitishwa. Bw Jacob Mwanzia anasema familia yake ilivunjika moyo baada ya nyanya yake kupatikana ameuawa. "Hatuelewi nia ya washambulizi. Inaonekana wao hunuia tu kuua," akasema. Kulingana na wazee wa vijiji, mashambulizi hayo hujitokeza kwa vipindi vya miezi kadha. Wakati huo, wazazi huwazuia watoto kutoka nje baada ya giza kuingia, makanisa hupunguza shughuli za usiku na waendesha bodaboda hufunga kazi mapema. Mauaji hayo yameambatana na wizi wa mara kwa mara. Makanisa yameripotiwa kuvamiwa na kuibiwa vifaa vya matangazo, vyombo vya muziki, vifaa vya umeme na sadaka. Pia, pikipiki, vifaa vya nyumbani na zana za kilimo zimeibwa. Chifu Msaidizi wa Mangawani, Bw Salim Nzala anasema wamepokea ripoti za mauaji matatu tangu Desemba 2025, huku uchunguzi ukiashiria zaidi migogoro ya kifamilia. "Visa vingi tulivyopokea viliwasilishwa kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu. Kilichosalia kwetu ni kuhakikisha kuna ushirikiano. Kwa hivyo wakazi wasilalamike kwamba serikali haijali, kwa sababu masuala yao yanashughulikiwa," akasema. Serikali imeanzisha kituo cha polisi Mangawani, imeongeza doria na kuandaa mikutano ya umma ili kuwahimiza wakazi kutoa taarifa. Hata hivyo, wakazi wanataka hatua zaidi, wakisema misitu na barabara duni huwapa wahalifu nafasi ya kutoroka. Kamanda wa Polisi wa eneo la Pwani, Bw Ali Nuno anasema hali ya usalama katika eneo zima kwa jumla imeimarika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Ker Odungi Randa atetea uamuzi wa Baraza la Waluo kuimba 'Tutam'

BARAZA la Wazee la Waluo limetetea uamuzi wake wa kushiriki masuala ya kisiasa, likisema hali ya sasa inalazimu wazee kutoa mwongozo kwa jamii badala ya kusalia kimya. Akizungumza katika Ukumbi wa Ofafa jijini Kisumu, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Ker Odungi Randa, alisema wazee walifikia uamuzi huo baada ya mashauriano ya ndani na kubaini kuwa hawawezi tena kunyamaza kuhusu masuala yanayoathiri jamii ya Waluo. "Sisi kama wazee ni alama ya mwongozo. Tunapoona mambo hayaendi sawa, tuna wajibu wa kutoa mwelekeo," akasema huku akisisitiza kuwa baraza linaendelea kuunga mkono Serikali Jumuishi ya Rais William Ruto. Bw Randa pia aliwataka viongozi wa Luo kukoma kushambuliana hadharani akisema migawanyiko ya ndani hupunguza nguvu ya jamii katika majadiliano ya kisiasa na kuwapa nafasi watu wa nje kutumia tofauti hizo kwa manufaa yao. Kauli yake ndiyo utetezi mkubwa zaidi ambao baraza hilo limewahi kutoa kuhusu kuhusika kwake katika siasa. Kwa miaka mingi, baraza lilikuwa likisisitiza kuwa jukumu lake ni kuhifadhi utamaduni wa Waluo, lakini msimamo huo umebadilika kufuatia mabadiliko ya kisiasa ndani ya jamii. Mnamo Julai 2024, baraza liliwahimiza viongozi wa upinzani kufanya mazungumzo yaliyofanikisha kuundwa kwa Serikali Jumuishi. Baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga mnamo 2025, Ker Randa aliwahimiza Waluo kuendeleza mkondo wa kisiasa ulioanzishwa na marehemu. Mnamo Mei mwaka huu, baraza lilimuunga mkono hadharani Rais Ruto kuwania muhula wa pili katika mkutano uliofanyika Kisumu na kuhudhuriwa na viongozi wa ODM. Tamko hilo linakuja wakati ODM inakabiliwa na migawanyiko kufuatia kifo cha Raila. Mrengo unaoongozwa na Seneta wa Siaya Oburu Oginga unaunga mkono ushirikiano na Rais Ruto, huku ule unaoongozwa na Gavana wa Siaya James Orengo ukipinga ushirikiano huo na kudai serikali inaingilia shughuli za chama. Hapo awali, Orengo amesema Baraza la Wazee wa Waluo haliwezi kuwa mpatanishi huru kwa kuwa tayari limeegemea upande mmoja kisiasa. Hata hivyo, baraza limekataa madai kwamba limeacha wajibu wake wa kitamaduni, likisema kutoa mwongozo nyakati za sintofahamu ni sehemu ya jukumu lake kama mlezi wa mila na maadili ya Waluo. Wazee hao pia walidokeza kuwa hivi karibuni watamtangaza mlezi mpya wa baraza hilo baada ya kifo cha Raila Odinga, huku wakithibitisha kuwa tamasha la kitamaduni la Piny Luo litafanyika Kisumu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 6 hours ago

Aladwa: Nitakuwa debeni na ODM lazima iungwe mkono kiti cha ugavana Nairobi

BAADHI ya viongozi wa ODM jijini Nairobi wamekataa wazo la kugawana nyadhifa za kisiasa na UDA kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, wakisisitiza kuwa ODM ndiyo inafaa kutoa mgombeaji wa ugavana wa Nairobi. Wakiongozwa na Mwenyekiti wa ODM Nairobi ambaye pia ni Mbunge wa Makadara, George Aladwa, viongozi hao walisema chama hicho kimekubaliana kumuunga mkono Rais William Ruto na Naibu wake Profesa Kithure Kindiki katika azma yao ya kutetea viti vyao mnamo 2027. Kwa hivyo ODM inastahili kupewa nafasi ya kuwania ugavana wa Nairobi na iungwe mkono na wanasiasa wa vyama vingine tanzu ndani ya Kenya Kwanza. "Kiti cha ugavana wa Nairobi lazima kibaki ODM na hakuna njia ya mkato kuhusu hilo. Tumesema tutamuunga mkono Rais Ruto na Naibu wake katika uchaguzi ujao. Hatutaki siasa za ugavi wa nyadhifa katika ngome za ODM," alisema Bw Aladwa. Mbunge huyo pia alitangaza rasmi nia yake ya kuwania ugavana wa Nairobi. "Nimeijenga na kuihudumia ODM kwa miaka mingi pamoja na marehemu Raila Odinga. Wale wanaopanga kujiunga na chama wawe tayari kwa mchujo. Madiwani na wajumbe wengi wako nyuma yangu, na mchujo utakuwa wa haki na uwazi," akaongeza. Bw Aladwa pia alimtetea Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, akimtuhumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuwashambulia viongozi ambao anajua hawatajibu matamshi yake hadharani. "Kanja alipitia taratibu zote za kuajiriwa na akathibitishwa kisheria. Gachagua aache kusambaza propaganda na amruhusu afanye kazi yake bila kuingiliwa," alisema. Viongozi hao walimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen kuchukua hatua dhidi ya Bw Gachagua wakidai matamshi yake yanayolenga jamii fulani yanaweza kuchochea mvutano wa kisiasa. "Akihitaji kutofautiana na Rais afanye hivyo bila kuwahusisha wananchi wengine. Anapaswa kuheshimu Rais ambaye alichaguliwa na Wakenya," akasema. Aidha, walimtetea Waziri wa Afya Aden Duale, wakisema kauli tata anazodaiwa kutoa zilifasiriwa vibaya na baadhi ya viongozi kwa ajili ya maslahi ya kisiasa. "Hakuna jamii iliyo bora kuliko nyingine nchini Kenya. Wanaomshambulia Duale wanapaswa kwanza kumkosoa Gachagua kwa matamshi yake," akasema Bw Aladwa. Bw Aladwa ndiye mgombeaji pekee wa ODM kutoka mrengo unaoongozwa na Dkt Oburu Oginga ambaye ametangaza analenga ugavana wa Nairobi. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino pia anataka ugavana ila kuna uwezekano finyu atatumia ODM kwa sababu anaegemea mrengo wa Linda Mwananchi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Ruto amwaga miradi ya mamilioni Magharibi, Oparanya akipigiwa debe 2027

RAIS William Ruto jana alisema serikali yake itaendelea kutekeleza miradi ya mabilioni ya pesa Magharibi mwa nchi huku wabunge wanaounga serikali yake wakiahidi kuwa eneo hilo litaendelea kuunga serikali katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Kiongozi wa nchi jana alikuwa katika Kaunti ya Busia ambapo alipigia debe miradi ambayo serikali yake imetekeleza na inaendelea kutekeleza kuinua eneo hilo kimaendeleo. Kwa upande mwingine, Kiongozi wa Wachache katika Bunge, Junet Mohamed, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na wabunge wa ODM na UDA nao walishiriki mchango eneobunge la Malava ambapo walipuuza umaarufu wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Huku Rais akiwa Busia, kundi la wabunge wa chama cha ODM likiwa Magharibi nalo lilisema kuwa Bw Oparanya ndiye atakuwa mgombeaji mwenza wa Rais 2027. "Watu wakuje polepole na wajue huwezi kuruka laini na wajue kuna watu walikaa na Raila miaka na mikaka. Oparanya ndiye anatosha kutuongoza hapa Magharibi kama kiongozi wa ODM baada ya Oburu Oginga. UDA wakipata rais, sisi ODM lazima tupate naibu rais na huyo ni Oparanya," akasema Bw Mohamed. "Hii pesa yote ambayo inataka kugawanya ODM ni pesa ya Uhuru Kenyatta na ndiyo anatumia kugawa chama chetu lakini hatafaulu. Kama Uhuru alishindwa kufanya baba kuwa rais 2022 sasa ndiye atasaidia mtu yeyote, sisi hatuwezi kuelekea barabara hiyo," akaongeza mbunge huyo wa Suna Mashariki. Mbunge huyo alisisitiza kuwa ODM haitarejelea siasa za maasi na nguvu zao zote sasa ni kuhakikisha kuwa chama kitaendelea kuwa imara. Bw Oparanya alisema amekuwa na uzoefu wa siasa na hatikiswi na wimbi la Bw Sifuna huku akisema kuwa hawezi kusaliti ndoto ya marehemu Raila Odinga. "Mimi mpaka watu wamekuja kuniambia nitengeneze chama kipya lakini nikakataa. Hakuna kiongozi ambaye alikuwa na ufuasi kuliko Raila na wakati huu kama Magharibi tunaingia moja kwa moja kwa serikali ya Rais Ruto," akasema Bw Oparanya. Rais Ruto alisema eneo la Magharibi ni sehemu ya nchi wala haliwezi kuachwa nyuma huku maeneo mengine yakiendelea kupiga hatua kimaendeleo. Alitaja baadhi ya miradi ambayo serikali yake imetekeleza huku akijizuia kuzungumzia suala la umaarufu wa Sifuna. "Tulianzisha barabara ya Mundere kule Seo Port, Matayos na Funyula. Mliniuliza barabara kutoka Butula-Nambale-Amukura-Kocholia, na mwezi ujao nitakuja hapa kuanzisha barabara hiyo ya kilomita 58 kwa sababu nimepata mwanakandarasi," akasema Rais. Alikuwa akihutubu wakati wa kutawazwa kwa Askofu wa nne wa Kanisa la ACK Vitalis Job Ekuru, hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Uganda Jesca Alupe.  "Tuna reli kutoka Narok na tumesema itakuja ifike hapa Malaba ili kurahisisha usafiri. Mimi na Rais wa Uganda Yoweri Museveni tulikubaliana huu ni mradi ambao tufanya pamoja kurahisisha usafiri na kusaidia nchi zetu kuimarisha uchumi," akaongeza Rais Ruto "Kuna barabara itakayofika hapa Malaba kutoka Mau Summit. Nitakuja kuzindua barabara ya Malava-Kimaeti-Bungoma. Barabara nyingine ambazo ziko hapa Busia ambazo ni kilomita 225 zimetengewa Sh5 bilioni na serikali," akasema Rais Ruto. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Gavana Paul Otuoma, mwenzake wa Kakamega Fernandes Barasa na Kenneth Lusaka wa Bungoma miongoni mwa wabunge wengine kutoka Magharibi mwa Nchi. "Tumeweka Sh1.2 bilioni za kuongezea miradi ya stima hapa Busia. Nilikuja kuzindua soko Amagoro na tunaendelea kuwajengea masoko mengine 19 mapya kwa sababu tunataka wafanyabiashara wetu waendelee kufanya biashara mahali safi na kuna umeme," akasema "Tumetoa Sh3.6 bilioni kuwajenga wanafunzi nyumba kupitia mradi wa nyumba ili wasome mahali ambao kuna usafi na panatoshana," "Nimeona wengine wananiambia eti niondoke kwa serikali niunge mtu mwengine mkono (Sifuna) eti ataunda serikali nisiyoijua. Hao viongozi hawajui wanaenda wapi na wao watuheshimu badala ya kututusi ndipo tuwaunge mkono kwa lazima," akaongeza Bw Oparanya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 8 hours ago

Sifuna apokelewa kishujaa Magharibi, Wantam ikitanda hewani

ENEO la Magharibi limegeuka uwanja mkuu wa mapambano ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku Rais William Ruto na viongozi wa upinzani wakilenga zaidi ya milioni 3.3. Magharibi kwa sasa ina jumla ya wapigakura waliosajiliwa milioni 2.92 katika kaunti tano, na inachukuliwa kuwa ngome muhimu inayoweza kuamua mshindi wa urais. Kufikia 2027, eneo hilo lenye kaunti za Bungoma, Kakamega, Trans Nzoia, Vihiga na Busia litakuwa na zaidi ya kura milioni 3.3. Katika uchaguzi wa 2022, Rais Ruto alipata ushindi mkubwa katika Kaunti ya Bungoma kwa kura 255,906, dhidi ya kura 145,280 za aliyekuwa mpinzani wake Raila Odinga. Matokeo hayo yalimsaidia kuingia Ikulu kwa tofauti ndogo ya kura. Sasa, ikiwa zimesalia chini ya miezi 12 kabla ya uchaguzi mkuu, vita vya kuhifadhi au kurejesha kura hizo vimeanza rasmi. umapili, Kiongozi wa kundi la Linda Mwananchi na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alikamilisha ziara ya siku mbili katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia huku Rais Ruto akiwa katika Kaunti ya Busia akizindua na kukagua miradi ya maendeleo. Pande zote mbili zilijitokeza zikisisitiza kuwa zinaungwa mkono na wakazi wa Magharibi. Katika mikutano yake, Bw Sifuna aliendelea kujisawiri kama mgombeaji anayetarajia kupeperusha bendera ya upinzani katika uchaguzi wa urais wa 2027, huku akiwataka wakazi wa Magharibi wasimwache njiani. "Watu wengi wanasema mnanipigia debe tu. Mmenihimiza niende hadi kwenye debe? Msije mkaniacha njiani. Simameni nami ili nikabiliane na Rais William Ruto uso kwa macho," akasema Alisema kundi la Linda Mwananchi limezunguka maeneo mengi nchini na kupokea ahadi za kuungwa mkono. "Nimeunda kikosi imara kutoka Pwani, Mlima Kenya, Nyanza, Magharibi na maeneo mengine. Kwa mapenzi ya Mungu, ndani ya miezi 12 tutakuwa tumekamilisha safari yetu kuelekea Ikulu," akaongeza. Bw Sifuna alisema safari yake ya kisiasa ilianzia Magharibi alipojaribu kuwania ubunge wa Kanduyi kabla ya marehemu Raila Odinga kumlea kisiasa na kumwezesha kuwa Seneta wa Nairobi, Katibu Mkuu wa ODM na Kiranja wa Wachache katika Seneti. Aidha, alidai kuwa viongozi wanaomuunga mkono Rais Ruto wanampotosha kwa kumwambia anaungwa mkono Bungoma. "Kuna watu wanamdanganya Rais kuwa ana kura Bungoma. Ukweli ni kwamba hana kura hapa. Safari ya mabadiliko tayari imeanza," akasema. Ziara hiyo ilihudhuriwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na Waziri wa zamani Musikari Kombo ambaye alihudumu katika utawala wa marehemu Rais Mwai Kibaki. Tangu asubuhi, mamia ya wafuasi walifurika mjini Bungoma wakiwa na mabango yenye picha ya Bw Sifuna huku wakiimba nyimbo za jadi za Bukusu na nyimbo zilizokuwa zikitumika katika kampeni za marehemu Raila Odinga. Msafara huo ulianza kwa ibada katika Kanisa Kuu la St Immaculate mjini Kitale kabla ya kupitia Kiminini, Sikhendu, Kamukuywa, Kimilili, Chwele na Kanduyi. Katika ishara ya kumuunga mkono, wakazi walichangia kati ya Sh50 na Sh1,000 kufanikisha kampeni zake za urais. "Afadhali nidaiwe Sh10 na kila mwananchi wa Bungoma kuliko kudaiwa na tajiri mmoja ambaye baadaye atanitaka nimlipe kwa zabuni nikichaguliwa," akasema Bw Sifuna. Aliahidi kuwa serikali ya upinzani itafuta Ushuru wa Nyumba, ushuru wa mafuta na kodi nyingine alizosema zimekuwa mzigo kwa wananchi. Kwa upande wake, Gavana Natembeya alisema Magharibi imekuwa ikikosa nafasi za kisiasa kutokana na migawanyiko ya viongozi wake, akitoa wito wa kuungwa mkono kwa mgombeaji mmoja wa urais. "Historia yetu imejaa migawanyiko. Watu walidhani mimi na Sifuna tungepambana, lakini tuliketi na kukubaliana. Wenzangu wa upinzani wawe jasiri na waseme wazi, 'Sifuna tosha'," akasema Bw Natembeya. Aliwataka pia viongozi wa Nyanza kuunga mkono mgombeaji kutoka jamii ya Mulembe kama walivyofanya kwa Raila Odinga kwa miaka mingi. Viongozi hao pia waliwashambulia Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, kwa kumpotosha Rais Ruto kuwa Bw Natembeya alisema serikali ya upinzani itafuta Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Ushuru wa Nyumba, Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC) na kodi nyingine alizodai zinawaumiza raia. Gavana Orengo alisema safari ya upinzani kuelekea Ikulu haiwezi kuzuiwa isipokuwa kupitia wizi wa kura, huku Seneta Osotsi akitaka kizazi kipya cha viongozi kupewa nafasi Magharibi. Naye Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alisema Linda Mwananchi tayari imefanya ziara katika kaunti 16 na inalenga kufika kaunti zote 47 kabla ya 2027. Alisema baada ya Magharibi, kundi hilo litaelekea Nyanza, Kisii, Mlima Kenya na Ukambani kukutana na viongozi wa upinzani akiwemo Fred Matiang'i, Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka ili kuunda muungano mmoja utakaompinga Rais Ruto mwakani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Mwanamume apigwa risasi Siaya wakazi wakipinga kiwanda cha nyuklia

MTU mmoja amelazwa hospitalini baada ya kupigwa risasi mguuni vurugu zilizozuka katika mkutano wa uhamasishaji kuhusu mradi wa kujenga kiwanda cha nyuklia cha thamani ya Sh1 trilioni katika eneo la Central Sakwa, Bondo, Kaunti ya Siaya, Ijumaa alasiri. Mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Biashara cha Ka'John ulihudhuriwa na maafisa wa KenGen, Shirika la Nishati na Umeme wa Nyuklia na Mbunge Gideon Ochanda. Waliokuwa wakielezea mradi huo kwa wakazi kabla ya vurugu kuzuka. David Otieno Mboya, mchimbaji mdogo wa madini kutoka kijiji cha Lenya, alisema hakuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo bali alikuwa akirejea nyumbani kutoka kazini alipopigwa risasi. "Nilikuwa napita karibu na eneo la mkutano vurugu zilipoanza. Wakazi walikuwa wakirusha mawe huku polisi wakifyatua risasi. Ghafla nilihisi maumivu makali kwenye mguu wa kushoto na nikagundua nimepigwa risasi," alisema. Alisema hajui iwapo alipigwa risasi na walinzi wa Mbunge Ochanda au maafisa wa polisi waliokuwa eneo hilo. Wasamaria wema walimkimbiza katika Hospitali ya Nango kabla ya kuhamishwa hadi Hospitali ya Bondo. Otieno alisema wakazi wengi wanapinga mradi huo kwa sababu utawalazimu kuhamishwa kutoka makazi yao ya muda mrefu. Mkazi mwingine, Otieno Ombok, alisema NuPEA imepuuza maswali ya jamii kuhusu usalama, fidia na uhamishaji wa wakazi, jambo lililosababisha hasira. Kamanda wa Polisi wa Bondo Peter Leparsare, alisema hakuna aliyekuwa ameripoti rasmi kupigwa risasi kufikia Ijumaa usiku, lakini alithibitisha kuwa polisi walifyatua risasi angani kutawanya umati baada ya mzozo kati ya wakazi na walinzi wa mbunge. Mradi huo ulihamishwa kutoka Kilifi hadi Siaya baada ya kupingwa na wakazi wa Kilifi. Serikali inapanga kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kwa kati ya megawati 3,000 na 6,000 kupitia mradi huo. Gavana wa Siaya James Orengo amesisitiza kuwa mafanikio yake yatategemea ushirikishaji wa wananchi, uwazi na ridhaa kamili ya jamii itakayoathirika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Mtego wa kutoka jadi unaovunja upinzani ufikapo uchaguzi mkuu

KUGAWANYIKA kwa upinzani si jambo geni katika siasa za Kenya. Mwaka 1992, chama cha FORD kilichokuwa kimeibuka kama tishio kubwa kwa utawala wa KANU kilisambaratika baada ya viongozi wake Kenneth Matiba na Jaramogi Oginga Odinga kutofautiana kuhusu nani angewania urais. Kutoka kwa mgawanyiko huo vilizaliwa vyama vya FORD-Asili chini ya Matiba na FORD-Kenya chini ya Jaramogi. Badala ya kupambana na Rais Daniel arap Moi, viongozi hao waligeukiana, kila mmoja akidai ndiye aliyekuwa na haki ya kupeperusha bendera ya upinzani. Zaidi ya miaka 30 baadaye, hali kama hiyo inaonekana kujitokeza tena. Viongozi wa upinzani wanakubaliana kuwa Rais William Ruto anapaswa kukabiliwa na mgombea mmoja mwaka 2027. Hata hivyo, bado hawajakubaliana ni nani atakayebeba bendera hiyo. Muungano unaowaleta pamoja Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Fred Matiang'i, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Justin Muturi unasema unataka mgombea mmoja. Lakini kila upande unaonekana kutaka mgombea huyo atoke katika kambi yake. Wakati huo huo, kiongozi wa Safina Jimi Wanjigi ameendelea na mkakati wake tofauti. Kama alivyofanya Mwai Kibaki mwaka 1992, Wanjigi amesema atazingatia ajenda ya uchumi badala ya kujiingiza katika mvutano kuhusu nani anafaa kuongoza muungano. Kwa sasa, wafuasi wa upinzani hawaonekani tu kumpinga Rais Ruto, bali pia wanapambana wao kwa wao. Kila kambi inatumia matokeo ya kura za maoni na nguvu za maeneo yao kama ushahidi wa kwa nini mgombea wao anastahili kupewa tiketi. Historia ya FORD inaonyesha hatari iliyopo. Kwanza, KANU haikuiangusha FORD. FORD ilianguka kwa sababu ya migawanyiko yake yenyewe. Katika harakati za kutafuta mgombea bora, upinzani wa sasa unaweza kujikuta ukijenga migawanyiko itakayompa Ruto nafasi ya kushinda. Wakati FORD ilipoanzishwa, ilionekana kama serikali inayosubiri kuingia madarakani. Mikutano yake ilivutia umati mkubwa na viongozi wake waliheshimiwa kwa mchango wao katika mapambano ya kurejesha mfumo wa vyama vingi. Lakini chama hicho hakikuwahi kuafikiana kuhusu namna ya kumpata mgombea wake wa urais. Matokeo yake yalionekana wazi katika uchaguzi wa mwaka 1992. Upinzani uliingia uchaguzini ukiwa umegawanyika kati ya Matiba, Jaramogi na Kibaki. Moi aliibuka mshindi huku kura za upinzani zikigawanyika. Hilo lilichelewesha kuondolewa kwa KANU madarakani kwa takriban muongo mmoja. Leo, viongozi wa upinzani wanakabiliwa na mtihani kama huo. Gachagua amesema mgombeaji anaweza kutangazwa hata Mei 2027, ilhali Muturi ametaka uamuzi ufanywe mapema na tayari ameonyesha kumuunga mkono Kalonzo. Martha Karua pia amehoji mfumo unaopendekezwa wa kumpata mgombeaji. Wachambuzi wanasema miungano mingi haisambaratiki siku ya uchaguzi. Huvunjika mapema kila upande unapoanza kujijengea mtandao wake, kukusanya fedha na kuwashawishi wafuasi kuwa hakuna mgombeaji mwingine anayefaa. Hapo ndipo kinachoitwa athari ya Matiba huanza. Kila mwanasiasa anakubali umuhimu wa umoja, lakini kwa sharti kwamba umoja huo umuunge mkono yeye. Somo jingine muhimu ni kwamba sheria na taratibu zinapaswa kuwekwa kabla ya majina ya wagombeaji. FORD haikuwahi kukubaliana kuhusu mfumo wa kumpata mgombeaji wake, jambo lililochochea mzozo ulioigawa. Kwa upinzani wa sasa, bado hakuna makubaliano kuhusu sifa za mgombeaji, ratiba ya uteuzi wala mfumo wa kutatua migogoro. Historia pia inaonyesha kuwa umati mkubwa wa watu kwenye mikutano si lazima uwe ishara ya ushindi. Matiba aliporejea nchini mwaka 1992 na kupokelewa na maelfu ya watu, wengi waliamini alikuwa tayari ameshinda. Lakini mvutano kuhusu mgombeaji ndio uliovunja FORD. Aidha, muungano wowote unaotegemea tu kumpinga aliye madarakani huwa katika hatari ya kusambaratika. Swali ambalo Safina amekuwa ikiuliza ni: Baada ya Ruto, nini kitafuata? Kwa mujibu wa Wanjigi, upinzani unapaswa kueleza sera zake kuhusu ushuru, deni la taifa, ukosefu wa ajira, ufisadi, afya, elimu na gharama ya maisha badala ya kutegemea kaulimbiu ya "Wantam" pekee. Somo la mwisho ni kwamba umoja wa kweli huhitaji viongozi wengine kujinyima kwa manufaa ya lengo la pamoja. Hilo lilitokea mwaka 2002, Raila Odinga alipomuunga mkono Mwai Kibaki kwa kauli maarufu ya "Kibaki tosha", hatua iliyosaidia kuondoa KANU madarakani. Historia ya FORD si simulizi ya zamani tu. Ni onyo kwamba upinzani unaweza kuwa na uungwaji mkono mkubwa wa wananchi, lakini ukashindwa ikiwa viongozi wake watashindwa kuweka maslahi ya taifa mbele ya tamaa zao binafsi. Tatizo jingine ambalo lilichangia kusambaratika kwa FORD ni kwamba kila kiongozi aliamini historia yake ya kisiasa ilimpa haki ya kuwania urais. Jaramogi alijiona ndiye aliyekuwa amepigania demokrasia kwa miongo mingi dhidi ya tawala za Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi. Kwa upande wake, Matiba aliamini mateso aliyopitia, ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa bila kesi na kuugua kiharusi akiwa kizuizini, yalikuwa yamemjengea uhalali wa kuongoza upinzani. Kila mmoja alitumia historia yake kama msingi wa kudai tiketi ya urais. Hali kama hiyo inaonekana kujitokeza katika upinzani wa sasa. Baadhi ya viongozi wanategemea ukongwe wao kisiasa, wengine wanajivunia idadi ya wapiga kura kutoka maeneo yao, huku wengine wakisisitiza tajriba yao serikalini, uadilifu wao au mateso wanayodai kuyapata kutokana na kupambana na utawala uliopo. Ingawa hoja hizo zinaweza kuwapa nguvu kisiasa, hazitoshi kuwapa haki ya moja kwa moja ya kupeperusha bendera ya muungano. Kwa mujibu wa historia ya FORD, umoja wa kisiasa haujengwi kwa hoja za nani ameteseka zaidi au nani anaungwa mkono na watu wengi zaidi, bali kwa kuweka utaratibu unaokubalika na wote. Bila makubaliano ya wazi kuhusu namna ya kumpata mgombeaji na jinsi ya kushughulikia malalamishi yatakayojitokeza, tofauti za viongozi zinaweza kugeuka chanzo cha mgawanyiko na kuudhoofisha upinzani kabla hata ya kampeni rasmi kuanza.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 26 Jul 2026 03:55:31

Wataalam watetea kiwanda cha mafuta cha Dangote Lamu

WATAALAMU wa miundomsingi, viwanda na maendeleo ya kimaeneo wameutetea mradi wa Sh2.2 trillioni wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi Lamu. Kiwanda hicho kitafadhiliwa na kampuni ya Dangote Group kutoka nchini Nigeria inayomilikiwa na tajiri wa Afrika, Bw Aliko Dangote. Licha ya kiwanda hicho kutajwa kuwa na manufaa tele endapo kitawekezwa Lamu, Kenya, wenyeji wanasema kwamba lazima watambuliwe, kushirikishwa na matakwa yao kuzingatiwa kwanza kabla ya hatua zozote za kutekeleza mradi huo kuendelezwa maeneo yao. Katika mahojiano na Taifa Jumapili, wataalamu, ikiwemo wafanyakazi wa idara za serikali, waliutaja mradi huo wa kiwanda cha mafuta kuwa suluhu ya pekee itakayobadilisha eneo la Lamu kwa uzuri. Kamishna wa Petroli kwenye Wizara ya Kawi na Petroli nchini, Bw Joseph Otieno, alisema mradi huo utabadilisha eneo hilo kuwa jungu la kiviwanda na maendeleo. Bw Otieno alisema Kenya imekuwa ikinunua na kusafirisha bidhaa za petroli kwa bei ghali kutoka nje, hasa mataifa ya Mashariki ya Kati kupitia bandari ya Mombasa. "Watu wa Lamu waondoe shaka. Mradi utatekelezwa kwa kuwazingatia. Kutakuwa na mikutano na makongamano ya kuwaelimisha wenyeji na umma kwa jumla ili wauelewe vyema mradi. Kutakuwa na vikao vya wadau wa serikali, mwekezaji na wakazi wa mashinani Lamu ambao ndio wenyeji wa mradi," akasema Bw Otieno. Aliongeza, "Lamu itapanuka kimaendeleo. Barabara zitaboreshwa, biashara zitanoga na sekta zote kunufaika. Hata utendakazi wa bandari ya Lamu pia utaboreka na kufanyika kwa njia ya haraka endapo kutakuwepo na kiwanda cha mafuta." Afisa Mtendaji na Mkurugenzi Mkuu wa Zamani wa Mradi wa Bandari ya Lamu, Uchukuzi na Miundomsingi ya Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia (LAPSSET), Dkt Silvester Kasuku alisema kuwekezwa kwa kiwanda cha Sh2.2 trilioni cha kusafisha mafuta kutaleta mwamko na taswira mpya ya Lamu kama eneo ambalo kihistoria lilikuwa limetelekezwa. Dkt Kasuku aliwahakikishia wakazi kwamba serikali itafanya kazi na kushirikiana nao kwa karibu wakati wa kutekelezwa kwa mradi huo. "Tushafanya kazi kwa karibu na jamii ya Lamu wakati tukitekeleza mradi wa Bandari ya Lamu na tukafaulu. Wananchi wa Lamu watambue kuwa tunawazingatia. Masuala ya ajira, utunzi wa mazingira, ufadhili wa kimasomo na mambo mengine, yote tutayajadili kwa pamoja na kuyakidhi katika kila hatua tutakazopiga wakati mradi utakapokuwa ukitekelezwa eneo hilo," akasema Dkt Kasuku. Mwenyekiti wa Zamani wa Muungano wa Save Lamu, Bw Mohamed Athman alitisha kuwa endapo vilio vyao kama jamii kuuhusu mradi vitakaidiwa basi hawatakuwa na budi ila kuelekea mahakamani kuuzuia mradi usifanyike eneo lao. Afisa Mtendaji wa Muungano wa Wanawake wa Lamu, Bi Raya Famau alishikilia haja ya jamii kuhusishwa kwenye vikao mbalimbali vya umma kutoa maoni kuhuuhusu mradi. Alisema wao hawapingi mradi ila furaha yao ni kuona haki zao za kijamii zikiheshimiwa. Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Shee Mbwana alimuomba mwekezaji, Bw Dangote kuweka kikao cha moja kwa moja na wanajamii ili waweze kutoa maoni na vilio vyao kuuhusu mradi. "Hatuna imani na serikali. Imekuwa ikitudhulumu ardhi zetu kila kunapowekezwa miradi mikuu eneo letu. Sasa tunamsihi Dangote afanye kikao cha moja kwa moja na sisi wanajamii ili tumpe vilio na mapendekezo yetu kabla mradi uendelee," akasema Bw Mbwana. Utakapokamilika, mradi huo utakuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku. Kiwanda hicho ambacho ni kikubwa zaidi Afrika Mashariki kinatarajiwa kujengwa kwa muda wa miaka mitatu. Kitasambaza bidhaa za petroli iliyosafishwa Kenya na pia nchi jirani, hivyo kupunguza hali ya ukanda wa Afrika Mashariki kutegemea mafuta yanayonunuliwa kutoka nje. Kiwanda hicho kinalengwa kujengwa eneo la Magogoni karibu na mradi wa Bandari ya Lamu ulioko Kililana, Lamu Magharibi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 26 Jul 2026 05:55:25

Salasya sasa adai Sifuna hana umaarufu kisiasa

HUKU viongozi vijana wakichangamkia kuimarika kwa umaarufu wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya amepuuzilia mbali matokeo ya kura ya maoni uliofanywa na kampuni ya TIFA ambao kinara huyo wa Linda Mwananchi aling'aa. Akizungumza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii Julai 24, 2026, mbunge huyo alidai kuwa utafiti huo ulifadhiliwa na Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) kwa lengo la kuzua mgawanyiko ndani ya muungano wa upinzani. Salasya alidai kuwa madhumuni ya utafiti huo yalikuwa kuonyesha kuwa vuguvugu la Linda Mwananchi linaungwa mkono zaidi kuliko muungano wa upinzani, jambo alilosema lilinuia kudhoofisha ushawishi wa viongozi wa upinzani kama kvile Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua. Pia aliubeza utafiti huo kwa kejeli, akisema iwapo mwelekeo huo utaendelea, basi Sifuna atakuwa na asilimia 80 ya umaarufu katika utafiti ujao. Alisisitiza kuwa matokeo hayo hayana uhalali. "NIS wanafanya kazi ya punda kugawanya upinzani kwa kuonyesha Linda Mwananchi inaungwa mkono zaidi kuliko Muungano wa Upinzani. Tiketi ya Sifuna/Matiang'i sasa ndiyo inaongoza, na hivyo kumfanya Kalonzo na Rigathi waonekane si lolote kisiasa. Kwa kweli, wiki ijayo Sifuna atakuwa na asilimia 80 katika kura za maoni kama mgombeaji bora wa urais," alisema Salasya. Kauli za Salasya zilijiri muda mfupi baada ya TIFA kutoa matokeo ya utafiti wake wa hivi punde kuhusu wanaopendelewa kuwania urais, uliomweka Rais William Ruto kileleni kwa asilimia 24 ya uungwaji mkono. Kwa mujibu wa utafiti huo, Sifuna alishika nafasi ya pili kitaifa kwa kupata asilimia 15, na hivyo kuwa mwanasiasa wa upinzani aliyeongoza kwa umaarufu. Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i alifuatia kwa asilimia 14, huku kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akishika nafasi ya nne kwa asilimia 13.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 26 Jul 2026 01:55:31

Ndoa kati ya Ruto na Oburu ni ya kulazimisha- TIFA

Wakenya wengi wanapinga ushirikiano wa kisiasa kati ya ODM na UDA, hali inayozua maswali kuhusu mustakabali wa mpango huo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Haya ni kwa mujibu wa utafiti mpya wa kampuni ya Trends and Insights for Africa (TIFA) uliofanywa kati ya Juni 13 na 22, 2026, ukihusisha watu 2,048 kutoka kaunti zote 47 nchini na ambao matokeo yake yalitolewa Ijumaa. Utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 52 ya Wakenya wanapinga Serikali Jumuishi, huku asilimia 30 pekee wakiunga mkono mpango huo. Asilimia 15 hawakuwa na maoni huku asilimia nne wakisema hawaufahamu ushirikiano huo. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa licha ya ushirikiano wa karibu miaka miwili kati ya Rais William Ruto na ODM kufuatia maandamano ya Gen Z ya mwaka 2024, bado umma haujaukubalika kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa TIFA, kiwango cha uungwaji mkono kwa ndoa ya vyama hivyo kimeendelea kubaki karibu kilekile kwa mwaka mmoja uliopita. Kilikuwa asilimia 22 Mei 2025, kikaongezeka hadi asilimia 44 Agosti mwaka huo kabla ya kushuka hadi asilimia 30 Novemba 2025. Katika utafiti wa sasa, kimeendelea kusalia asilimia 30. Ripoti hiyo inasema mgawanyiko unaoendelea ndani ya ODM kuhusu iwapo chama hicho kinafaa kuunga mkono azma ya Rais Ruto ya kutetea urais mwaka 2027 umefunga kiwango ambacho ushirikiano huo unaweza kupata uungwaji mkono. Hakuna eneo lolote kati ya kanda tisa za utafiti lililoonyesha wengi wanaounga mkono ushirikiano huo. Eneo la kati la Bonde la Ufa linaongoza kwa asilimia 47 ya wanaounga ushirikiano huo, likifuatiwa na Kaskazini mwa Kenya kwa asilimia 43 na Nyanza kwa asilimia 35. Magharibi ina asilimia 29, Pwani asilimia 31, Kusini mwa Rift Valley asilimia 25, Nairobi asilimia 22, Kusini Mashariki asilimia 30 na Mlima Kenya asilimia 13. TIFA pia imebaini kuwa uungwaji mkono umeshuka kwa kasi zaidi Magharibi mwa Kenya, kutoka asilimia 62 Novemba 2025 hadi asilimia 29 sasa. Nyanza pia imeshuka kutoka asilimia 59 hadi 35, huku Mlima Kenya na Kaskazini mwa Kenya zikisajili kupungua kwa uungwaji mkono. Ripoti hiyo inahusisha hali hiyo na mvutano unaoendelea ndani ya ODM kati ya makundi ya Linda Mwananchi na Linda Ground kuhusu mustakabali wa chama na ushirikiano wake na Kenya Kwanza. Viongozi kama Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi wameendelea kupinga ushirikiano wa karibu na serikali. Wapigakura ambao hawajaamua Wakati huo huo, utafiti huo unaonyesha kuwa uchaguzi wa urais wa 2027 huenda ukaamuliwa katika maeneo yenye wapigakura wengi ambao bado hawajaamua upande wa kuunga mkono. Mlima Kenya, wenye takriban wapiga kura milioni 5.7, umejitokeza kuwa uwanja mkubwa wa kisiasa. Asilimia 25 ya wakazi wa eneo hilo bado hawajaamua mgombea watakayemuunga mkono. Nairobi pia imejitokeza kuwa uwanja muhimu wa kisiasa. Kalonzo anaongoza kwa asilimia 23, akifuatiwa kwa karibu na Sifuna kwa asilimia 22 na Matiang'i kwa asilimia 17. Rais Ruto anaungwa mkono na asilimia sita huku Gachagua akiwa na asilimia nane. Asilimia 21 ya wakazi wa jiji bado hawajaamua. Pwani pia imeonekana kuwa eneo la ushindani mkali. Sifuna anaongoza kwa asilimia 27, Rais Ruto asilimia 21, Kalonzo asilimia 10 na Matiang'i asilimia tisa. Asilimia 21 ya wakazi bado hawajafanya uamuzi. Katika eneo la Kusini Mashariki, Kalonzo ameendelea kutawala ngome yake kwa asilimia 58 dhidi ya asilimia 15 za Rais Ruto. Ni asilimia tisa pekee ambao hawajaamua. Magharibi mwa Kenya pia inaonekana kuwa eneo litakaloamua matokeo ya uchaguzi. Sifuna anaongoza kwa asilimia 28, Rais Ruto asilimia 14 na Matiang'i asilimia 12. Hata hivyo, asilimia 31 ya wakazi bado hawajafanya uamuzi. Kwa upande mwingine, Rais Ruto anaendelea kutawala Kaskazini mwa Kenya kwa asilimia 61 ya uungwaji mkono na bado ana nguvu katika baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa. Nyanza nayo inaendelea kuwa ngome ya upinzani, ingawa ushindani unaongezeka huku Matiang'i akipata asilimia 29 na Rais Ruto asilimia 30. Kwa mujibu wa Katiba, mgombea wa urais lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura halali pamoja na angalau asilimia 25 ya kura katika zaidi ya nusu ya kaunti zote nchini. Kutokana na hali hiyo, TIFA inaeleza kuwa ushindi wa mwaka 2027 hautategemea tu ngome za kisiasa bali pia uwezo wa vyama kuwashawishi mamilioni ya wapiga kura ambao bado hawajaamua katika maeneo kama Mlima Kenya, Nairobi, Magharibi na Pwani. Utafiti huo unatarajiwa kuathiri mikakati ya kampeni za kisiasa, huku Kenya Kwanza na viongozi wa upinzani wakiongeza juhudi za kuvutia wapigakura katika maeneo hayo muhimu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 26 Jul 2026 02:55:13

KCPE, KCSE zafufua kumbukumbu za shule kwa Wakenya wanaoishi Uingereza

KWA Wakenya wengi, kumbukumbu za mitihani ya KCPE na KCSE huibua picha za usiku wa kukesha wakisoma, wasimamizi wakali wa mitihani na shinikizo kubwa la kufaulu. Lakini sasa, kile kilichokuwa chanzo cha hofu kimegeuzwa kuwa burudani inayowaleta pamoja Wakenya nchini na ughaibuni. Nchini Uingereza, jamii ya Wakenya imeanzisha usiku maalum wa maswali na majibu unaotumia maswali ya KCPE na KCSE kama njia ya kuburudika, kukumbushana maisha ya shule na kuimarisha urafiki. Miongoni mwa walioanzisha shughuli hiyo ni Nicholas Njomo Kamau, mtaalamu wa afya anayefanya kazi katika Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza (NHS). Alivutiwa na hafla kama hizo zilizoandaliwa Nairobi na jumuiya ya ubunifu ya Qwani. "Niliona zinafanyika Kenya nikafikiria kwa nini tusizilete hapa, ambako kuna Wakenya wengi. Nimefurahishwa na zilivyopokolewa," alisema. Hafla hizo sasa zimefanyika mara tatu katika ukumbi wa Vaha Lounge mjini Northampton. Washiriki huwekwa katika makundi na kujibu maswali ya Hisabati, Kiingereza, Kiswahili, Sayansi na Masomo ya Jamii bila presha ya kufaulu. Kwa Njomo, uzuri wa wazo hilo ni kwamba karibu kila Mkenya amepitia mfumo wa elimu wa 8-4-4. "Sote tumewahi kupitia mitihani hiyo," alisema. Kilichoanza kama mkutano wa kujiburudisha sasa kimekuwa jukwaa la kujenga urafiki. Washiriki wameunda makundi ya WhatsApp na huendelea kuwasiliana hata baada ya hafla kuisha. Ingawa washindi hupata zawadi kama vile chupa za pombe, wengi husema zawadi kubwa ni kurejea kumbukumbu za utotoni, walimu waliowapenda, ushindani wa shule na maswali magumu yaliyowasumbua. Njomo alisema jambo lililomshangaza zaidi ni kuona hata Wakenya wa umri mkubwa wakijiunga na kufurahia hafla hizo. "Pia tumewaona watu wasiokuwa Wakenya wakija kudadisi. Huondoka wakifurahia muziki, ushindani na mazingira ya Kikenya," alisema huku akicheka. Baada ya maswali na majibu, hafla hubadilika kuwa sherehe ya nyimbo za zamani za Kenya. Wageni hufurahia ugali, nyama choma, pilau na mboga za kienyeji huku nyimbo za Gengetone na nyimbo za zamani zikichezwa. "Tunawaleta ma-DJ wa Kenya kucheza nyimbo zinazotukumbusha enzi za shule," alisema. Mwanafunzi wa uuguzi nchini Uingereza, Lynn Saina, alisema hafla hizo huwasaidia Wakenya kupunguza hamu ya nyumbani. "Kinachonivutia zaidi ni furaha na vicheko. Chumba kilichojaa wageni hubadilika haraka na kuwa familia moja kubwa," alisema. Aliongeza kuwa kati ya vipengele vinavyovutia zaidi ni maswali ya methali za Kiswahili, ambapo washiriki hujaribu kukamilisha methali lakini mara nyingi huishia kubuni methali mpya zinazochekesha kila mtu. Siku ya kwanza, hafla hiyo ilivutia zaidi ya watu 150 uliwathibitishia kuwa Wakenya walikuwa na hamu kubwa ya kumbukumbu zao za shule.

read more