T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 20 Jul 2026 23:55:17

Tangazo la Sifuna kuwa atwania urais latikisa ODM na Upinzani

TANGAZO la Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwa atawania urais mnamo 2027 linaendelea kubadili mwelekeo wa siasa za upinzani na ODM, huku viongozi wengi wakianza kujiunga na mrengo wa Linda Mwananchi anaouongoza. Akizungumza katika mikutano ya kisiasa Kaunti ya Taita Taveta mwishoni mwa wiki, Bw Sifuna alisema licha ya kupokonywa nyadhifa za ukatibu mkuu wa ODM na kiranja wa wachache, anaamini vijana watampa nafasi ya kuwa rais 2027. "Wameninyang'anya kila cheo nilichopewa na Baba, lakini vijana wanasema watanipa cheo cha H.E," akasema. Miongoni mwa viongozi ambao wamebadili msimamo ni Seneta wa Kisii Richard Onyonka, ambaye awali alikuwa mshirika wa karibu wa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i. Bw Onyonka ameonekana mara kadhaa katika mikutano ya Linda Mwananchi na hadharani ameahidi kumuunga mkono Bw Sifuna ikiwa atawania urais. "Mdogo wangu na rais ajaye ni Edwin Sifuna. Ukifika wakati wa kupiga kura nitampigia kura. Nawaona wengine wanatetereka nikisema hivyo lakini sote katika upinzani tuko pamoja," akasema akiwa Voi. Bw Onyonka alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele kumpigia debe Dkt Matiang'i alipozindua azma yake ya urais mnamo 2025. Hata hivyo, hakuhudhuria ziara ya Dkt Matiang'i huko Keumbu, ambako wafuasi wa Linda Mwananchi walivamiwa. Viongozi wengine wa Gusii wanaohusishwa na mrengo huo ni wabunge Clive Gisairo, Anthony Kibagendi na Obadiah Barongo. Ndani ya ODM, mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang' walitumia matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ol Kalou kuikosoa serikali, wakisema viongozi wanapaswa kuwasikiza wananchi na kuheshimu maamuzi yao badala ya kutumia vitisho au rushwa. Kauli zao zimezua hisia kwamba wanaegemea upande wa Linda Mwananchi, ingawa hawajatangaza rasmi msimamo wao. Wakati huo huo, Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata alikosolewa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kumuunga mkono mgombea wa Linda Mwananchi katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Mchanganuzi wa masuala ya siasa Martin Andati anasema hatua hiyo ilionyesha kuwa siasa za eneo la Mlima Kenya zinaendelea kubadilika, huku viongozi wakitafuta miungano mipya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Shinikizo pia zinaongezeka kwa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, huku baadhi ya wabunge wa Ukambani wakihusishwa na shughuli za Linda Mwananchi. Duru hata hivyo zinaashiria kuwa lengo la wabunge hao ni kuhakikisha Mabw Kalonzo na Sifuna wanashirikiana katika uchaguzi wa 2027. Miongoni mwa wabunge wa Wiper wanaohusishwa na mrengo huo ni Joshua Kimilu, Patrick Makau na Danson Mwashako. Katika Magharibi mwa Kenya, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anaendelea kushirikiana na Linda Mwananchi na anapanga mikutano ya kisiasa Trans Nzoia na Bungoma. Ni katika mikutano hiyo ambapo Bw Sifuna anatarajiwa kutawazwa kuwa kigogo wa siasa za Magharibi na kupewa baraka za kuwania urais.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Wataalam watetea kiwanda cha mafuta cha Dangote Lamu

WATAALAMU wa miundomsingi, viwanda na maendeleo ya kimaeneo wameutetea mradi wa Sh2.2 trillioni wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi Lamu. Kiwanda hicho kitafadhiliwa na kampuni ya Dangote Group kutoka nchini Nigeria inayomilikiwa na tajiri wa Afrika, Bw Aliko Dangote. Licha ya kiwanda hicho kutajwa kuwa na manufaa tele endapo kitawekezwa Lamu, Kenya, wenyeji wanasema kwamba lazima watambuliwe, kushirikishwa na matakwa yao kuzingatiwa kwanza kabla ya hatua zozote za kutekeleza mradi huo kuendelezwa maeneo yao. Katika mahojiano na Taifa Jumapili, wataalamu, ikiwemo wafanyakazi wa idara za serikali, waliutaja mradi huo wa kiwanda cha mafuta kuwa suluhu ya pekee itakayobadilisha eneo la Lamu kwa uzuri. Kamishna wa Petroli kwenye Wizara ya Kawi na Petroli nchini, Bw Joseph Otieno, alisema mradi huo utabadilisha eneo hilo kuwa jungu la kiviwanda na maendeleo. Bw Otieno alisema Kenya imekuwa ikinunua na kusafirisha bidhaa za petroli kwa bei ghali kutoka nje, hasa mataifa ya Mashariki ya Kati kupitia bandari ya Mombasa. "Watu wa Lamu waondoe shaka. Mradi utatekelezwa kwa kuwazingatia. Kutakuwa na mikutano na makongamano ya kuwaelimisha wenyeji na umma kwa jumla ili wauelewe vyema mradi. Kutakuwa na vikao vya wadau wa serikali, mwekezaji na wakazi wa mashinani Lamu ambao ndio wenyeji wa mradi," akasema Bw Otieno. Aliongeza, "Lamu itapanuka kimaendeleo. Barabara zitaboreshwa, biashara zitanoga na sekta zote kunufaika. Hata utendakazi wa bandari ya Lamu pia utaboreka na kufanyika kwa njia ya haraka endapo kutakuwepo na kiwanda cha mafuta." Afisa Mtendaji na Mkurugenzi Mkuu wa Zamani wa Mradi wa Bandari ya Lamu, Uchukuzi na Miundomsingi ya Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia (LAPSSET), Dkt Silvester Kasuku alisema kuwekezwa kwa kiwanda cha Sh2.2 trilioni cha kusafisha mafuta kutaleta mwamko na taswira mpya ya Lamu kama eneo ambalo kihistoria lilikuwa limetelekezwa. Dkt Kasuku aliwahakikishia wakazi kwamba serikali itafanya kazi na kushirikiana nao kwa karibu wakati wa kutekelezwa kwa mradi huo. "Tushafanya kazi kwa karibu na jamii ya Lamu wakati tukitekeleza mradi wa Bandari ya Lamu na tukafaulu. Wananchi wa Lamu watambue kuwa tunawazingatia. Masuala ya ajira, utunzi wa mazingira, ufadhili wa kimasomo na mambo mengine, yote tutayajadili kwa pamoja na kuyakidhi katika kila hatua tutakazopiga wakati mradi utakapokuwa ukitekelezwa eneo hilo," akasema Dkt Kasuku. Mwenyekiti wa Zamani wa Muungano wa Save Lamu, Bw Mohamed Athman alitisha kuwa endapo vilio vyao kama jamii kuuhusu mradi vitakaidiwa basi hawatakuwa na budi ila kuelekea mahakamani kuuzuia mradi usifanyike eneo lao. Afisa Mtendaji wa Muungano wa Wanawake wa Lamu, Bi Raya Famau alishikilia haja ya jamii kuhusishwa kwenye vikao mbalimbali vya umma kutoa maoni kuhuuhusu mradi. Alisema wao hawapingi mradi ila furaha yao ni kuona haki zao za kijamii zikiheshimiwa. Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Shee Mbwana alimuomba mwekezaji, Bw Dangote kuweka kikao cha moja kwa moja na wanajamii ili waweze kutoa maoni na vilio vyao kuuhusu mradi. "Hatuna imani na serikali. Imekuwa ikitudhulumu ardhi zetu kila kunapowekezwa miradi mikuu eneo letu. Sasa tunamsihi Dangote afanye kikao cha moja kwa moja na sisi wanajamii ili tumpe vilio na mapendekezo yetu kabla mradi uendelee," akasema Bw Mbwana. Utakapokamilika, mradi huo utakuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku. Kiwanda hicho ambacho ni kikubwa zaidi Afrika Mashariki kinatarajiwa kujengwa kwa muda wa miaka mitatu. Kitasambaza bidhaa za petroli iliyosafishwa Kenya na pia nchi jirani, hivyo kupunguza hali ya ukanda wa Afrika Mashariki kutegemea mafuta yanayonunuliwa kutoka nje. Kiwanda hicho kinalengwa kujengwa eneo la Magogoni karibu na mradi wa Bandari ya Lamu ulioko Kililana, Lamu Magharibi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

Salasya sasa adai Sifuna hana umaarufu kisiasa

HUKU viongozi vijana wakichangamkia kuimarika kwa umaarufu wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya amepuuzilia mbali matokeo ya kura ya maoni uliofanywa na kampuni ya TIFA ambao kinara huyo wa Linda Mwananchi aling'aa. Akizungumza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii Julai 24, 2026, mbunge huyo alidai kuwa utafiti huo ulifadhiliwa na Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) kwa lengo la kuzua mgawanyiko ndani ya muungano wa upinzani. Salasya alidai kuwa madhumuni ya utafiti huo yalikuwa kuonyesha kuwa vuguvugu la Linda Mwananchi linaungwa mkono zaidi kuliko muungano wa upinzani, jambo alilosema lilinuia kudhoofisha ushawishi wa viongozi wa upinzani kama kvile Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua. Pia aliubeza utafiti huo kwa kejeli, akisema iwapo mwelekeo huo utaendelea, basi Sifuna atakuwa na asilimia 80 ya umaarufu katika utafiti ujao. Alisisitiza kuwa matokeo hayo hayana uhalali. "NIS wanafanya kazi ya punda kugawanya upinzani kwa kuonyesha Linda Mwananchi inaungwa mkono zaidi kuliko Muungano wa Upinzani. Tiketi ya Sifuna/Matiang'i sasa ndiyo inaongoza, na hivyo kumfanya Kalonzo na Rigathi waonekane si lolote kisiasa. Kwa kweli, wiki ijayo Sifuna atakuwa na asilimia 80 katika kura za maoni kama mgombeaji bora wa urais," alisema Salasya. Kauli za Salasya zilijiri muda mfupi baada ya TIFA kutoa matokeo ya utafiti wake wa hivi punde kuhusu wanaopendelewa kuwania urais, uliomweka Rais William Ruto kileleni kwa asilimia 24 ya uungwaji mkono. Kwa mujibu wa utafiti huo, Sifuna alishika nafasi ya pili kitaifa kwa kupata asilimia 15, na hivyo kuwa mwanasiasa wa upinzani aliyeongoza kwa umaarufu. Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i alifuatia kwa asilimia 14, huku kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akishika nafasi ya nne kwa asilimia 13.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 6 hours ago

Ndoa kati ya Ruto na Oburu ni ya kulazimisha- TIFA

Wakenya wengi wanapinga ushirikiano wa kisiasa kati ya ODM na UDA, hali inayozua maswali kuhusu mustakabali wa mpango huo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Haya ni kwa mujibu wa utafiti mpya wa kampuni ya Trends and Insights for Africa (TIFA) uliofanywa kati ya Juni 13 na 22, 2026, ukihusisha watu 2,048 kutoka kaunti zote 47 nchini na ambao matokeo yake yalitolewa Ijumaa. Utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 52 ya Wakenya wanapinga Serikali Jumuishi, huku asilimia 30 pekee wakiunga mkono mpango huo. Asilimia 15 hawakuwa na maoni huku asilimia nne wakisema hawaufahamu ushirikiano huo. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa licha ya ushirikiano wa karibu miaka miwili kati ya Rais William Ruto na ODM kufuatia maandamano ya Gen Z ya mwaka 2024, bado umma haujaukubalika kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa TIFA, kiwango cha uungwaji mkono kwa ndoa ya vyama hivyo kimeendelea kubaki karibu kilekile kwa mwaka mmoja uliopita. Kilikuwa asilimia 22 Mei 2025, kikaongezeka hadi asilimia 44 Agosti mwaka huo kabla ya kushuka hadi asilimia 30 Novemba 2025. Katika utafiti wa sasa, kimeendelea kusalia asilimia 30. Ripoti hiyo inasema mgawanyiko unaoendelea ndani ya ODM kuhusu iwapo chama hicho kinafaa kuunga mkono azma ya Rais Ruto ya kutetea urais mwaka 2027 umefunga kiwango ambacho ushirikiano huo unaweza kupata uungwaji mkono. Hakuna eneo lolote kati ya kanda tisa za utafiti lililoonyesha wengi wanaounga mkono ushirikiano huo. Eneo la kati la Bonde la Ufa linaongoza kwa asilimia 47 ya wanaounga ushirikiano huo, likifuatiwa na Kaskazini mwa Kenya kwa asilimia 43 na Nyanza kwa asilimia 35. Magharibi ina asilimia 29, Pwani asilimia 31, Kusini mwa Rift Valley asilimia 25, Nairobi asilimia 22, Kusini Mashariki asilimia 30 na Mlima Kenya asilimia 13. TIFA pia imebaini kuwa uungwaji mkono umeshuka kwa kasi zaidi Magharibi mwa Kenya, kutoka asilimia 62 Novemba 2025 hadi asilimia 29 sasa. Nyanza pia imeshuka kutoka asilimia 59 hadi 35, huku Mlima Kenya na Kaskazini mwa Kenya zikisajili kupungua kwa uungwaji mkono. Ripoti hiyo inahusisha hali hiyo na mvutano unaoendelea ndani ya ODM kati ya makundi ya Linda Mwananchi na Linda Ground kuhusu mustakabali wa chama na ushirikiano wake na Kenya Kwanza. Viongozi kama Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi wameendelea kupinga ushirikiano wa karibu na serikali. Wapigakura ambao hawajaamua Wakati huo huo, utafiti huo unaonyesha kuwa uchaguzi wa urais wa 2027 huenda ukaamuliwa katika maeneo yenye wapigakura wengi ambao bado hawajaamua upande wa kuunga mkono. Mlima Kenya, wenye takriban wapiga kura milioni 5.7, umejitokeza kuwa uwanja mkubwa wa kisiasa. Asilimia 25 ya wakazi wa eneo hilo bado hawajaamua mgombea watakayemuunga mkono. Nairobi pia imejitokeza kuwa uwanja muhimu wa kisiasa. Kalonzo anaongoza kwa asilimia 23, akifuatiwa kwa karibu na Sifuna kwa asilimia 22 na Matiang'i kwa asilimia 17. Rais Ruto anaungwa mkono na asilimia sita huku Gachagua akiwa na asilimia nane. Asilimia 21 ya wakazi wa jiji bado hawajaamua. Pwani pia imeonekana kuwa eneo la ushindani mkali. Sifuna anaongoza kwa asilimia 27, Rais Ruto asilimia 21, Kalonzo asilimia 10 na Matiang'i asilimia tisa. Asilimia 21 ya wakazi bado hawajafanya uamuzi. Katika eneo la Kusini Mashariki, Kalonzo ameendelea kutawala ngome yake kwa asilimia 58 dhidi ya asilimia 15 za Rais Ruto. Ni asilimia tisa pekee ambao hawajaamua. Magharibi mwa Kenya pia inaonekana kuwa eneo litakaloamua matokeo ya uchaguzi. Sifuna anaongoza kwa asilimia 28, Rais Ruto asilimia 14 na Matiang'i asilimia 12. Hata hivyo, asilimia 31 ya wakazi bado hawajafanya uamuzi. Kwa upande mwingine, Rais Ruto anaendelea kutawala Kaskazini mwa Kenya kwa asilimia 61 ya uungwaji mkono na bado ana nguvu katika baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa. Nyanza nayo inaendelea kuwa ngome ya upinzani, ingawa ushindani unaongezeka huku Matiang'i akipata asilimia 29 na Rais Ruto asilimia 30. Kwa mujibu wa Katiba, mgombea wa urais lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura halali pamoja na angalau asilimia 25 ya kura katika zaidi ya nusu ya kaunti zote nchini. Kutokana na hali hiyo, TIFA inaeleza kuwa ushindi wa mwaka 2027 hautategemea tu ngome za kisiasa bali pia uwezo wa vyama kuwashawishi mamilioni ya wapiga kura ambao bado hawajaamua katika maeneo kama Mlima Kenya, Nairobi, Magharibi na Pwani. Utafiti huo unatarajiwa kuathiri mikakati ya kampeni za kisiasa, huku Kenya Kwanza na viongozi wa upinzani wakiongeza juhudi za kuvutia wapigakura katika maeneo hayo muhimu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

KCPE, KCSE zafufua kumbukumbu za shule kwa Wakenya wanaoishi Uingereza

KWA Wakenya wengi, kumbukumbu za mitihani ya KCPE na KCSE huibua picha za usiku wa kukesha wakisoma, wasimamizi wakali wa mitihani na shinikizo kubwa la kufaulu. Lakini sasa, kile kilichokuwa chanzo cha hofu kimegeuzwa kuwa burudani inayowaleta pamoja Wakenya nchini na ughaibuni. Nchini Uingereza, jamii ya Wakenya imeanzisha usiku maalum wa maswali na majibu unaotumia maswali ya KCPE na KCSE kama njia ya kuburudika, kukumbushana maisha ya shule na kuimarisha urafiki. Miongoni mwa walioanzisha shughuli hiyo ni Nicholas Njomo Kamau, mtaalamu wa afya anayefanya kazi katika Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza (NHS). Alivutiwa na hafla kama hizo zilizoandaliwa Nairobi na jumuiya ya ubunifu ya Qwani. "Niliona zinafanyika Kenya nikafikiria kwa nini tusizilete hapa, ambako kuna Wakenya wengi. Nimefurahishwa na zilivyopokolewa," alisema. Hafla hizo sasa zimefanyika mara tatu katika ukumbi wa Vaha Lounge mjini Northampton. Washiriki huwekwa katika makundi na kujibu maswali ya Hisabati, Kiingereza, Kiswahili, Sayansi na Masomo ya Jamii bila presha ya kufaulu. Kwa Njomo, uzuri wa wazo hilo ni kwamba karibu kila Mkenya amepitia mfumo wa elimu wa 8-4-4. "Sote tumewahi kupitia mitihani hiyo," alisema. Kilichoanza kama mkutano wa kujiburudisha sasa kimekuwa jukwaa la kujenga urafiki. Washiriki wameunda makundi ya WhatsApp na huendelea kuwasiliana hata baada ya hafla kuisha. Ingawa washindi hupata zawadi kama vile chupa za pombe, wengi husema zawadi kubwa ni kurejea kumbukumbu za utotoni, walimu waliowapenda, ushindani wa shule na maswali magumu yaliyowasumbua. Njomo alisema jambo lililomshangaza zaidi ni kuona hata Wakenya wa umri mkubwa wakijiunga na kufurahia hafla hizo. "Pia tumewaona watu wasiokuwa Wakenya wakija kudadisi. Huondoka wakifurahia muziki, ushindani na mazingira ya Kikenya," alisema huku akicheka. Baada ya maswali na majibu, hafla hubadilika kuwa sherehe ya nyimbo za zamani za Kenya. Wageni hufurahia ugali, nyama choma, pilau na mboga za kienyeji huku nyimbo za Gengetone na nyimbo za zamani zikichezwa. "Tunawaleta ma-DJ wa Kenya kucheza nyimbo zinazotukumbusha enzi za shule," alisema. Mwanafunzi wa uuguzi nchini Uingereza, Lynn Saina, alisema hafla hizo huwasaidia Wakenya kupunguza hamu ya nyumbani. "Kinachonivutia zaidi ni furaha na vicheko. Chumba kilichojaa wageni hubadilika haraka na kuwa familia moja kubwa," alisema. Aliongeza kuwa kati ya vipengele vinavyovutia zaidi ni maswali ya methali za Kiswahili, ambapo washiriki hujaribu kukamilisha methali lakini mara nyingi huishia kubuni methali mpya zinazochekesha kila mtu. Siku ya kwanza, hafla hiyo ilivutia zaidi ya watu 150 uliwathibitishia kuwa Wakenya walikuwa na hamu kubwa ya kumbukumbu zao za shule.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Wanawake pia hutumika kueneza uhuni wa kisiasa-Utafiti

WANAWAKE wanazidi kuwa sehemu muhimu lakini isiyoonekana ya mitandao ya wahuni wa kisiasa nchini, huku wakitumika kuhamasisha vijana, kusafirisha silaha kwa siri na kukusanya taarifa za kisiri, utafiti mpya umebaini. Kwa miaka mingi, macho ya umma yamekuwa yakielekezwa kwa vijana wanaume wanaovamia mikutano ya kisiasa na maandamano wakiwa na rungu na mawe. Hata hivyo, ripoti mpya inaonyesha kuwa nyuma ya vurugu hizo kuna mtandao uliopangwa vyema unaowahusisha pia wanawake. Kijana mmoja kutoka Mathare, Nairobi, aliyekubali kuzungumza na Taifa Jumapili kwa masharti ya kutotajwa jina kwa hofu ya usalama wake, alisema wanawake wamekuwa sehemu ya mfumo huo. "Bila shaka wapo. Huenda wasiwe mstari wa mbele, lakini wanashiriki kikamilifu," alisema. Kijana huyo, anayejitambulisha kama mmoja wa "vigogo" wa eneo hilo wanaotafutwa na wanasiasa na wafanyabiashara kuwasaka vijana kwa shughuli za kisiasa, alisema hawabagui wanawake wanapofanya uajiri. "Sisi ndio viongozi wanaotafutwa na wanasiasa wanapohitaji watu. Hatujali jinsia. Tunawaajiri wanawake, nao pia huleta wengine," alisema. Kwa mujibu wake, wanawake mara nyingi hawashiriki moja kwa moja katika mashambulizi, bali hujichanganya na umati ili mikutano ionekane kuwa na watu wengi kuliko ilivyo. Pia hukusanya taarifa, huwatetea wenzao wanapokamatwa na wakati mwingine husafirisha mawe au silaha ndogo wanazofichwa kwenye mikoba yao. "Kama hujui utakula nini mchana au jioni, huwezi kuanza kuuliza kama mwanamke anafaa kujiunga na kundi au la," alisema. Hata hivyo, alisema hajawahi kuona mwanamke akifikia kiwango cha kuwa kiongozi mkuu wa mtandao huo, ingawa wengi hutumiwa kuajiri wengine. Ripoti inayoitwa Goonland: Looking Beyond the Money and Violence in the Political Exploitation of Young Men, iliyoandaliwa na shirika la OdipoDev, inaeleza kuwa magenge ya kisiasa si mkusanyiko wa vijana wasio na ajira pekee, bali ni mtandao wenye viongozi, waajiri, wajumbe na waratibu wanaofanya kazi kwa mpangilio maalumu. Utafiti huo ulifanywa kupitia mahojiano na wanachama 40 wa magenge ya wahuni, waajiri watano na maafisa watano wa usalama kutoka Nairobi, Mombasa na Kiambu. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mawasiliano hufanywa kupitia makundi ya WhatsApp na vituo vya mitaani, huku fedha na silaha zikisafirishwa kwa siri kupitia watu wanaoaminika. Wanawake ni miongoni mwa watu hao wanaoaminiwa kusafirisha na kuficha silaha kwa kuwa hawashukiwi kirahisi wakati wa ukaguzi kuhusu usalama. Mzee wa kijiji cha Mathare, Joseph Ouna, alisema akina mama wachanga wanazidi kuvutwa katika shughuli hizo kutokana na ugumu wa maisha. "Akina mama hawa wana watoto, na vijana hawa ni marafiki wao. Wanawapa pesa na kuwasaidia kwa mahitaji mbalimbali, hivyo huwa rahisi kuwashawishi wakubali kazi za kisiasa," alisema. Aidha, alisema baadhi ya wanawake hujitokeza kuwatetea vijana hao wanapokamatwa kwa kuwasawiri kama waathiriwa badala ya wahusika wa vurugu. Mratibu mmoja wa kisiasa kutoka Kayole ambaye hakutaka kutajwa jina alisema aliwahi kuombwa na mwanamke mwenzake amtafutie vijana kwa shughuli za kisiasa lakini alikataa kwa kuhofia kukamatwa au kushambuliwa. Alidai pia kuwa rafiki yake mmoja alipelekwa Ol Kalou kuvuruga uchaguzi mdogo uliofanyika eneo hilo. "Nilimshawishi asiende lakini alikataa. Hadi leo sijui alilipwa kiasi gani," alisema. Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Nyandarua Central, Kenneth Kiprop, alisema hakuna mwanamke aliyekamatwa kufuatia vurugu za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, wala uchunguzi haukubaini wanawake walioshiriki moja kwa moja katika mashambulizi hayo. Utafiti huo unaonyesha kuwa fedha ndizo kichocheo kikuu cha vijana kujiunga na magenge hayo. Kuvuruga mikutano ya kisiasa hulipwa kati ya Sh500 na Sh1,500, shughuli za kuvuruga maandamano hulipa Sh500 hadi Sh2,500, huku migogoro ya ardhi ikilipa kati ya Sh500 na Sh2,000. Hata hivyo, watafiti wanasema si pesa pekee zinazowafanya vijana wabaki kwenye mitandao hiyo. Wengi walieleza kuwa hupata wanatambuliwa, kupata ulinzi, hadhi na hisia ya kuwa sehemu ya kundi. Ripoti hiyo inaonya kuwa kuanzisha nafasi za ajira pekee hakutamaliza tatizo la magenge ya kisiasa, kwa sababu wanaojiunga nayo hujengewa uhusiano unaotokana na hofu na mshikamano wa kijamii ambao si rahisi kuuvunja.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Wantam: Sifuna aoshewa lami, apokelewa kishujaa Bungoma

KIFO cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kimebadilisha kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa siasa za Kenya, huku Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna akiibuka kama mmoja wa viongozi wanaotikisa hesabu za uchaguzi mkuu wa 2027. Baada ya kuondolewa kama Katibu Mkuu na msemaji wa ODM, Sifuna sasa anaongoza vuguvugu la Linda Mwananchi, ambalo wachambuzi wanasema linaweza kubadili kabisa sura ya siasa za nchi na kutatiza mipango ya serikali pamoja na upinzani. Ndani ya ODM, baadhi ya viongozi wanakiri kuwa kumuondoa Sifuna kutoka uongozi wa chama kulikuwa kosa kubwa. Hata hivyo, sasa anaongoza vuguvugu linalovutia wafuasi wengi, hasa vijana, na ambazo zinazidi kupata nguvu kote nchini. Umaarufu wake umewatia wasiwasi viongozi wa kisiasa wa Magharibi kama Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambao wamekuwa wakijitambulisha kama vinara wa eneo hilo. Jana, Sifuna aliongoza mikutano mikubwa ya kisiasa katika Kaunti ya Trans Nzoia na kutangaza kuwa yuko tayari kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2027. Akizungumza katika mkutano wa mwisho mjini Kitale, Sifuna alimshukuru Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kwa kumuunga mkono na kumhimiza azunguke nchi nzima kutafuta uungwaji mkono. "Nimekubali jukumu hilo. Niko tayari kuzunguka Kenya nzima kutafuta kura na sitawaangusha Wakenya," alisema. Sifuna alidai kuwa upinzani utaungana na kumteua mgombeaji mmoja wa urais atakayemenyana na Rais William Ruto katika uchaguzi ujao. Baada ya mikutano hiyo, msafara wa viongozi hao ulipitia Kaplamai na kusimama katika soko la Sibanga, Cherang'any, kabla ya kurejea Kitale kwa mkutano wa mwisho. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni wa TIFA uliotolewa Ijumaa, Sifuna amempiku kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika umaarufu wa urais kwa mara ya kwanza. Katika utafiti huo, Sifuna alipata asilimia 15 ya uungwaji mkono, akifuatiwa na Naibu Kiongozi wa Jubilee Fred Matiang'i kwa asilimia 14, Kalonzo Musyoka asilimia 13, kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua asilimia saba na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino asilimia mbili. Kwa jumla, viongozi wa upinzani wanaungwa mkono na asilimia 51 ya Wakenya, huku Rais William Ruto akiongoza kivyake kwa asilimia 24. Hata hivyo, kiwango hicho bado hakitoshi kumwezesha kushinda uchaguzi katika duru ya kwanza. Kinachowashangaza wengi si tu umaarufu wa Sifuna bali kasi aliyopanda nayo. Miezi miwili iliyopita hakuwa hata akitajwa katika mazungumzo ya wagombeaji urais. Sasa ameibuka kama mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini. Katika uchaguzi wa Seneti wa Nairobi mwaka 2022, Sifuna alimshinda Askofu Margaret Wanjiru kwa kura 716,876. Leo, umaarufu wake unatajwa kuwa unaweza kubadili mazungumzo ya muungano wa upinzani kuhusu mgombeaji mmoja wa urais. Hata baada ya kuondolewa katika uongozi wa ODM, utafiti unaonyesha karibu nusu ya wafuasi wa chama hicho wangependa awe mgombeaji wao wa urais. Matokeo hayo yanaendana na utafiti wa awali wa Infotrak uliomuonyesha Sifuna akipunguza pengo kati yake na viongozi waliokuwa wakitajwa kama vigogo wa upinzani, jambo linaloashiria kuwa kupanda kwake si bahati bali ni mwelekeo mpya wa kisiasa. Akizungumza baada ya matokeo ya utafiti huo kutolewa, Sifuna alisema jambo muhimu si asilimia aliyopata, bali ni kwamba Rais Ruto anaendelea kushuka chini ya kiwango kinachohitajika kushinda uchaguzi kwa urahisi. Alisema iwapo upinzani utaungana nyuma ya mgombeaji mmoja, utaweza kumshinda Rais Ruto. "Tukijumlisha asilimia za Sifuna, Kalonzo, Matiang'i na viongozi wengine wa upinzani, ziko juu zaidi ya za Rais Ruto. Tunahitaji umoja ili kuwasikiliza Wakenya wanaotaka mabadiliko," alisema. Mchambuzi wa siasa Arnold Maliba alisema wengi wanakosea kuchukulia Linda Mwananchi kama muungano wa kawaida wa kisiasa. Kwa mujibu wake, vuguvugu hilo linalenga kubadili mjadala wa kisiasa kutoka ukabila na makubaliano ya viongozi kuelekea masuala ya utawala bora, uwajibikaji, Katiba na ushiriki wa wananchi. "Linda Mwananchi si chama cha kawaida. Ni vuguvugu linaloweka shinikizo kwa serikali na pia kwa upinzani uliopo," alisema. Kwa Rais Ruto, kupanda kwa Sifuna kunamaanisha hatari ya kupoteza kura za eneo la Magharibi, ambazo ni muhimu katika azma yake ya kutetea urais, hasa baada ya kupoteza uungwaji mkono mkubwa katika Mlima Kenya. Ndani ya upinzani, kuibuka kwa Sifuna kumebadili hesabu zilizoweka Kalonzo Musyoka na Fred Matiang'i kama wagombeaji wakuu wa urais.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 18 hours ago

Kavulani amwonya Asefa, aapa kumlaza mapema kwenye pambano Ndondi

Bondia wa Kenya Jane Kavulani ametuma onyo kali kwa mpinzani wake Roman Asefa Abate wa Ethiopia akiahidi kumwangusha kwa kushinda kwa 'Knockout' yaani KO katika raundi za kwanza, watakapokutana  katika mashindano ya ndondi yatakayofanyika Jumamosi hii kwenye ukumbi wa Edge Convention Centre jijini Nairobi. Kavulani, anayefanya mazoezi katika ukumbi wa Pal Pal Gymnasium uliopo Gikomba jijini Nairobi, alisema amejiandaa vya kutosha na hana shaka ya kuibuka mshindi dhidi ya Methiopia huyo ambaye atakuwa akicheza pambano lake la kwanza la kulipwa. "Nimefanya maandalizi ya kutosha. Lengo langu ni kumaliza pambano mapema kwa KO na kuwapa mashabiki ushindi wa kujivunia," alisema Kavulani. Hata hivyo, Asefa naye ameonyesha kujiamini akisema ananuia kuanza maisha yake ya ndondi za kulipwa kwa ushindi na kurejea Ethiopia akiwa ameshinda pambano lake la kwanza. Zaidi ya mapambano hayo ya wanawake uzani wa featherweight, mashabiki watashuhudia jumla ya mapambano 11 kwenye usiku huo wa ngumi uliofadhiliwa na SportPesa na kuandaliwa na promota Maurice Odera kupitia kampuni ya UFS BXNG. Pambano kuu la usiku litamshuhudia bingwa wa Kenya na Afrika Mashariki Javan Buyu akipambana na Ramadhani Idd wa Tanzania kuwania taji la Universal Boxing Organisation (UBO) Inter-Continental Lightweight katika pambano la raundi 10. Buyu anatarajiwa kutumia uzoefu wake mbele ya mashabiki wa nyumbani huku Idd akinuia kuvuruga mipango ya Mkenya huyo kwa kutwaa taji hilo na kuliondoka nalo Tanzania. Buyu, ambaye ni bingwa wa Kenya na Afrika Mashariki, ana nafasi ya kutwaa taji lake la tatu la kulipwa na kuwa miongoni mwa mabondia wachache wa Kenya kushinda mkanda wa ngazi ya mabara. Bondia huyo amesema yuko tayari kwa mtihani huo baada ya kufanya maandalizi ya miezi mitatu bila kuacha jambo lolote kwa bahati. "Nimekuwa nikifanya mazoezi na kumuomba Mungu kwa ajili ya taji hili. Mimi na timu yangu tumefanya kazi kubwa kujiandaa kwa Julai 25 na tuko tayari. Tumeimarisha kila eneo muhimu litakalotupa ushindi," alisema Buyu. Buyu alitwaa ubingwa wa Kenya Oktoba mwaka jana baada ya kumshinda Christopher Osicho kabla ya kuongeza mkanda wa PST kwa kumcharaza Mtanzania Nasoro Madimba kwa Technical Knockout katika raundi ya tatu mapema mwaka huu. Amesema tayari amemchunguza Ramadhani kupitia video zake. "Ni bondia mzuri, ningempa alama saba kati ya 10, lakini nina kila kitu kinachohitajika kumlazimisha akate tamaa. Namwahidi pambano zuri, lakini aandae moyo wa kukubali kushindwa," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Wetang'ula: Ukabila hauna nafasi katika siasa za Kenya

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula amewataka viongozi wa kisiasa kuachana na siasa za ukabila na kuhubiri umoja wa kitaifa, akionya kuwa matamshi ya chuki yanaweza kugawanya taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Akizungumza Jumamosi katika eneo la Oloiborsoito, Kilgoris, Kaunti ya Narok, wakati wa hafla ya kuchangia fedha  Shirika la Wanawake la Olerai, Wetang'ula alisema tofauti za kisiasa hazipaswi kugeuka kuwa chuki, vurugu au uhasama wa kikabila. "Mtu yeyote anayehubiri ukabila ana fikra za zamani. Tunaweza kutofautiana kisiasa, lakini hiyo si sababu ya kutukanana au kuumizana," alisema. Aliwataka wanasiasa kuepuka matamshi ya uchochezi yanayoweza kuwashawishi vijana kuingia katika vurugu, akisisitiza kuwa viongozi wana wajibu wa kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa. "Siasa hazipaswi kuwa sababu ya umwagaji damu. Vijana ni mustakabali wa taifa na hawapaswi kutumiwa katika migogoro ya kisiasa," alisema. Wetang'ula alisema kuwawezesha wanawake na vijana kupitia ujuzi na fursa za kiuchumi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Pia alisifu jamii ya Wamaasai kwa kuhifadhi utamaduni wao, akisema umechangia kukuza utalii nchini. Spika huyo alimkosoa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa madai ya kutoa matamshi yanayoweza kudhoofisha sekta ya utalii, huku akitoa wito wa kutungwa kwa sheria zitakazolinda wachimbaji madini na kuwawezesha kunufaika na rasilimali za taifa. Katika hafla hiyo, mshauri wa Rais William Ruto, Farouk Kibet, aliwataka wakazi wa Kilgoris kuishi kwa amani, huku Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot akilaani siasa za ukabila na kuitaka Wizara ya Usalama kuchukua hatua dhidi ya viongozi wanaotoa matamshi ya uchochezi. Mbunge wa Kitutu Chache North Japheth Nyakundi aliwataka viongozi kuzingatia sera za maendeleo badala ya siasa za kikabila, huku Mbunge wa Kibwezi West Mwengi Mutuse akitetea rekodi ya maendeleo ya serikali ya Rais William Ruto.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 25 Jul 2026 03:55:09

Waziri Duale motoni kwa kauli tata ya kueneza ukabila

WAZIRI wa Afya, Aden Duale analaumiwa kufuatia matamshi yake kuhusu jamii za Kenya kuzua mjadala mkubwa nchini, huku Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ikianzisha uchunguzi kubaini iwapo kauli hizo zilichochea mgawanyiko wa kikabila. Video iliyosambaa kwa kasi mitandaoni ilimuonyesha Bw Duale akizungumza kwa lugha ya Kisomali katika mkutano uliofanyika eneo la Lafey, Kaunti ya Mandera, Julai 20, 2026. Katika hotuba hiyo, alisema utawala wa Rais William Ruto umefanya maendeleo makubwa zaidi katika eneo la Kaskazini Mashariki kuliko tawala za marais waliotangulia, akiwemo Hayati Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta. Pia alieleza kuwa jamii ya Wasomali ina watu takriban milioni 41 duniani na kudai kuwa kwa muda mrefu baadhi ya jamii zimekuwa zikitawala siasa na nafasi muhimu serikalini huku maeneo mengine yakisalia nyuma. Hata hivyo, matamshi hayo yamekosolewa vikali na viongozi wa kisiasa na wananchi walioyataja kuwa ya uchochezi na yanayoweza kuvuruga mshikamano wa kitaifa. Mnamo Ijumaa, NCIC ilisema imeanza uchunguzi kuhusu matamshi hayo. "Timu ya uchunguzi ya Tume inaendelea kufanya uchunguzi bila upendeleo kuhusu matamshi hayo. Tunawahimiza viongozi kujiepusha na kauli zinazoweza kuchochea chuki za kikabila na kuwakumbusha kuwa Kenya ni ya Wakenya wote," alisema mwenyekiti wa NCIC, Askofu Kepha Omae. Aliongeza kuwa tume itaendelea kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mtu yeyote atakayehatarisha umoja wa taifa, hasa wakati nchi inaelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru alisema kauli za Duale zilikuwa za kusikitisha na hatari. "Ni jambo hatari na la kupotosha kueleza changamoto za kisiasa kwa misingi ya ukabila. Kauli kama hizo hazikubaliki kutoka kwa kiongozi mwenye hadhi ya Waziri wa Baraza la Mawaziri," alisema. Suala hilo pia liliibuliwa katika Seneti ambapo Maseneta Enoch Wambua (Kitui), Ledama Ole Kina (Narok) na Abdul Haji (Garissa) walitaka viongozi kuwa waangalifu wanapozungumza kuhusu masuala ya kikabila. Seneta Ole Kina alisema viongozi wana jukumu la kuwaunganisha Wakenya. "Nilimsikia Waziri akilinganisha jamii na kuacha taswira kwamba jamii moja ni bora kuliko nyingine. Kauli kama hizi zinaweza kurudisha taifa kwenye siasa za migawanyiko," alisema. Seneta Wambua alionya kuwa matamshi hayo yanawakumbusha Wakenya hali ilivyokuwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2007. "Tuliona kilichotokea mwaka 2007 baada ya viongozi kuanza kutumia lugha ya chuki. Tunapoelekea uchaguzi wa 2027, viongozi wanapaswa kuhubiri amani badala ya kuwagawa wananchi," alisema. Seneta Abdul Haji alisema iwapo Duale alitoa matamshi hayo kama yalivyosikika kwenye video, basi ilikuwa makosa. Aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando pia alimkosoa Duale, akidai kauli zake zinaakisi msimamo wa utawala wa sasa. Akijibu lawama hizo, Duale alisema kauli zake zilitokana na methali ya jadi ya Kisomali ambayo imetafsiriwa vibaya na kutumiwa kisiasa. Alisema methali hiyo inamrejelea mnyama mwenye tabia ya kujinufaisha na inalenga watu au makundi yaliyozoea kunufaika na mamlaka na rasilimali kiasi kwamba inakuwa ugumu kukubali kugawa nafasi kwa jamii nyingine. Kwa mujibu wa Duale, alichomaanisha ni kwamba tangu uhuru, eneo la Mlima Kenya limekuwa likishikilia nafasi za juu serikalini, ikiwemo urais au makamu wa rais, na kwamba Rais Ruto amejaribu kupanua ushirikishaji kwa kuwapa nafasi Wakenya kutoka jamii mbalimbali. Pia alimshutumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa madai ya kutoa matamshi yaliyolenga Wasomali, ikiwemo kuita Kaskazini Mashariki eneo la ugaidi, kupinga kuondolewa kwa mfumo wa ukaguzi wa vitambulisho kwa Wasomali na kuhoji uteuzi wa Wasomali katika nyadhifa za serikali. Alipoulizwa iwapo angeomba msamaha, Duale alisema taarifa aliyotoa tayari ilifafanua alichomaanisha. "Maneno yangu yanajieleza yenyewe," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 25 Jul 2026 02:55:02

Kaunti zadaiwa Sh50b, michango ya pensheni ya wafanyakazi

BARAZA la Magavana (CoG) limetaka maafisa wa kaunti wanaoshindwa kuwasilisha michango ya pensheni iliyokatwa kutoka mishahara ya wafanyakazi wachukuliwe hatua za jinai, huku madeni hayo yakifikia zaidi ya Sh50 bilioni. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Hazina ya Pensheni (RBA), Charles Machira alisema mashirika ya umma, yakiwemo serikali za kaunti, yanadaiwa zaidi ya Sh71.4 bilioni za michango ambayo ilikatwa lakini haikuwasilishwa. Ingawa CPF Group, inayosimamia pensheni za wafanyakazi wa kaunti, imeendelea kuongeza wanachama na mali zake, kutowasilishwa kwa michango hiyo kumetajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa ukuaji wa hazina hiyo. Akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa CPF Group, Mkurugenzi Mkuu, Hosea Kili alisema taasisi hiyo inaendelea na mazungumzo na serikali za kaunti, Baraza la Magavana na Wizara ya Fedha ili kutafuta suluhu ya madeni hayo.  "Hazina ilipata faida ya asilimia 10 mwaka huu, jambo linaloonyesha uthabiti wa uwekezaji wa muda mrefu. Hata hivyo, kutowasilishwa kwa michango na waajiri ni changamoto kubwa. Sielewi kwa nini mshahara unalipwa pamoja na makato ya kisheria lakini fedha hizo haziwasilishwi kwenye hazina husika," alisema Kili. Alisema ukuaji wa mali umeathiriwa na madeni ya zaidi ya Sh50 bilioni ya michango ambayo haijawasilishwa. Naye Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Ahmed Abdullahi alisema kutowasilisha michango iliyokatwa kutoka mishahara ya wafanyakazi ni kosa la jinai. "Ni uhalifu kukata fedha za mfanyakazi halafu ukose kuziwasilisha. Inasikitisha kuwa maafisa wanaohusika, wakiwemo maafisa wa mishahara, wakaguzi wa hesabu, mabunge ya kaunti na Seneti, wameshindwa kuhakikisha sheria inafuatwa. Maafisa wanaosimamia mishahara lakini hawawasilishi makato wanapaswa kukamatwa," alisema. Aliongeza kuwa madeni yanapodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja huwa vigumu kulipwa kutokana na vikwazo vya bajeti. "Wasimamizi wa hazina ya pensheni wahakikishe serikali za sasa za kaunti hazimalizi muhula wao zikiwa na madeni mapya. Madeni ya zamani yashughulikiwe kivyake kupitia mpango maalumu wa malipo," alisema. Wadau pia wamependekeza hatua mbalimbali za kumaliza tatizo hilo, ikiwemo kubadilishana madeni na mali na kukata michango moja kwa moja kabla fedha hazijafika kwa kaunti. Bw Kili alilitaka Baraza la Magavana kushawishi wizara ya fedha kutoa hati za dhamana kwa niaba ya kaunti zote 47 ili kuharakisha ulipaji wa madeni hayo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 25 Jul 2026 00:55:50

Ruto aendeleza juhudi za kuvutia vijana akitafuta Tutam

RAIS William Ruto ameongeza juhudi za kuwavutia vijana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 baada ya kuzindua mpango wa Sh2 bilioni wa kuwawezesha kupata ajira kupitia mafunzo kazini, nafasi za kazi za kidijitali na ushirikiano na sekta ya kibinafsi. Mpango huo wa NextGen Youth Empowerment Programme, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali, Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) na sekta ya kibinafsi, unalenga kuwapa vijana ujuzi na uzoefu unaohitajika katika soko la ajira. Hatua hiyo inajiri huku serikali ya Kenya Kwanza ikijaribu kurejesha imani ya vijana baada ya miezi kadhaa ya malalamiko kuhusu ukosefu wa ajira, ushuru mkubwa na gharama ya juu ya maisha. Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), zaidi ya Wakenya milioni 22.1 walikuwa wamejisajili kupiga kura mwaka 2022, huku walio na umri wa kati ya miaka 18 na 34 wakiwa zaidi ya nusu ya wapigakura wote. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Rais Ruto alisema serikali imeamua kuwekeza katika mipango inayounganisha elimu na ajira. "Mafunzo kazini si kazi za muda tu. Ni daraja kati ya kujifunza na kujipatia kipato, kati ya uwezo na utendaji, na kati ya ndoto na mafanikio. Leo tunajenga daraja hilo kwa vijana wa Kenya kupitia mpango wa NextGen," alisema. Rais alikiri kuwa wahitimu wengi hukumbwa na changamoto ya kupata ajira kwa sababu waajiri wanahitaji uzoefu wa kazi kuliko vyeti vya kitaaluma. "Waajiri wanatafuta uzoefu wa vitendo, nidhamu kazini na ujuzi unaohitajika na sekta mbalimbali. Vipaji vinapokosa nafasi, ndoto huchelewa kutimia na taifa hupoteza uwezo wake wa uzalishaji," alisema. Alisema vijana 100,000 walioajiriwa kama walimu chini ya serikali yake walipitia mafunzo kazini kabla ya kuajiriwa rasmi. Aidha, wahitimu 5,600 wanapata mafunzo chini ya Mpango wa Makazi Nafuu, huku zaidi ya mafundi 2,000 wakipata vyeti kupitia mpango wa kutambua ujuzi. Rais pia alisema zaidi ya vijana 1.9 milioni wamefunzwa ujuzi wa kidijitali, hatua iliyochangia kuundwa kwa nafasi za kazi 350,000 katika sekta hiyo. Aliongeza kuwa zaidi ya Wakenya 580,000 kwa sasa wanafanya kazi nje ya nchi kupitia mpango wa serikali wa ajira majuu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 24 Jul 2026 23:55:39

TIFA: Sifuna sasa kifua mbele kupambana na Ruto 2027

TAKRIBAN thuluthi mbili ya wafuasi wa kiongozi wa Democracy for the Citizens (DCP) Rigathi Gachagua wanaompinga Rais William Ruto wanaamini hafai kuwania urais mwaka ujao, bali amuunge mkono mgombeaji mwingine wa upinzani. Haya ni kwa mujibu wa utafiti wa pili wa kitaifa wa kampuni ya Trends and Insights for Africa (TIFA) mwaka 2026, uliofanywa kati ya Juni 13 na 22 na kutolewa Ijumaa. Utafiti huo pia unaonyesha kuwa Rais Ruto bado ndiye mgombeaji anayeungwa mkono zaidi kuwania urais huku uchaguzi mkuu ukisalia chini ya mwaka mmoja. TIFA ilitoa chaguo tatu kuhusu nafasi ya Gachagua katika juhudi zake za kumng'oa Rais Ruto madarakani. Miongoni mwa Wakenya wanaopinga kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto, asilimia 62 walisema Gachagua anafaa kumuunga mkono mgombeaji mwenye nafasi kubwa zaidi ya kushinda kutoka upinzani. Ni asilimia 14 pekee waliotaka awe mgombeaji wa urais wa upinzani iwapo mahakama itamruhusu kugombea. Iwapo mahakama itazuia kugombea, asilimia 29 ya Wakenya wanaamini anafaa kumuunga mkono mgombeaji mwingine wa upinzani. Hata kama ataruhusiwa kugombea, asilimia 33 bado wanaamini anafaa kumuunga mkono mgombeaji mwingine. Asilimia tano pekee wanaamini Rais Ruto hawezi kushindwa bila kujali hatua ambayo Gachagua atachukua, huku asilimia 19 wakisema hawana uhakika. "Matokeo yanaonyesha kuwa wapigakura wanaompinga Rais Ruto wanajali zaidi kuongeza nafasi za upinzani kushinda uchaguzi kuliko kujali nani atakuwa mgombeaji wake," ilisema sehemu ya ripoti ya TIFA. Kwa mujibu wa utafiti huo, Rais Ruto anaongoza kwa asilimia 24 ya uungwaji mkono. Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna anafuatia kwa asilimia 15, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i asilimia 14, kiongozi wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka asilimia 13, Gachagua asilimia saba na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino asilimia mbili. TIFA ilisema ingawa Rais Ruto bado ndiye mgombeaji anayependekezwa zaidi, kiwango chake cha asilimia 24 kinaonyesha upinzani bado una nafasi ya kushindana iwapo utaungana. "Ingawa uungwaji mkono wa upinzani bado umegawanyika, Sifuna ameonyesha ongezeko kubwa zaidi la umaarufu. Umeongezeka kutoka kiwango kisichoweza kupimika mwaka 2025 hadi asilimia 15 mwezi Juni 2026, jambo lililomweka miongoni mwa wagombeaji wakuu wa upinzani," ilisema ripoti hiyo. Ndani ya ODM, Sifuna pia anaungwa mkono na asilimia 44 ya wanachama kama mgombeaji wa urais wa chama, ikilinganishwa na asilimia 20 wanaomuunga mkono Rais Ruto. Kwa upande mwingine, umaarufu wa baadhi ya wanasiasa umeshuka. Matiang'i alishuka kutoka asilimia 32 mwezi Mei 2025 hadi asilimia 14 mwezi Juni 2026. Umaarufu wa Kalonzo nao umeshuka kutoka asilimia 25 mwezi Novemba 2025 hadi asilimia 13. Kwa upande wa Sifuna, kiwango chake cha uungwaji mkono kimeongezeka kwa asilimia 50 tangu Mei, kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15. Umaarufu wa Babu Owino umeshuka kutoka asilimia nane mwezi Novemba mwaka jana hadi asilimia mbili, hali ambayo TIFA inaamini imetokana na baadhi ya wafuasi wake kuhamia kwa Sifuna. Uungwaji mkono wa Gachagua pia umepungua kidogo, jambo ambalo TIFA inalihusisha na kushindwa kwake katika Mahakama Kuu kupinga kuondolewa kwake kama Naibu Rais. Utafiti huo pia unaonyesha kuwa wanachama wa ODM wanaendelea kuunga mkono zaidi msimamo wa Linda Mwananchi huku ule wa Linda Ground ukiendelea kupoteza nguvu. Kwa upande wa vyama vya siasa, ODM imeongeza uungwaji mkono kutoka asilimia 16 hadi 20, huku UDA ikisalia kwa asilimia 17. Hata hivyo, DCP, Wiper, DAP-Kenya na Ford Kenya vimepungua kwa uungwaji mkono. Kwa ujumla, TIFA ilisema ODM na UDA zimepoteza umaarufu tangu uchaguzi wa mwaka 2022, huku DCP ikiibuka kama mshindani mpya na karibu thuluthi moja ya wapigakura bado hawajaamua chama watakachounga mkono. Kuhusu Serikali Jumuishi ya UDA na ODM, asilimia 52 ya Wakenya walisema wanaipinga, huku asilimia 30 wakisema wanaiunga mkono. Asilimia 15 hawakuwa na maoni, huku asilimia nne wakisema hawajui kuhusu ushirikiano huo. Kwa mujibu wa TIFA, kiwango cha uungwaji mkono kwa Serikali Jumuishi kimesalia karibu asilimia 30 tangu Mei mwaka huu. Ripoti hiyo inaeleza kuwa ODM italazimika kuamua ikiwa ushirikiano huo ulikuwa wa muda mfupi wa kutekeleza ajenda ya mageuzi au utageuka kuwa ushirikiano wa muda mrefu.

read more