taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
Pengo la Sh33.5b tishio kwa uchaguzi 2027
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) inakabiliwa na pengo la Sh33.5 bilioni katika bajeti inayohitajika kuandaa na kuendesha uchaguzi mkuu wa 2027, huku mabadiliko ya kiteknolojia na upanuzi wa miundombinu yakiongeza gharama. Stakabadhi zilizowasilishwa Bungeni na IEBC, inayoongozwa na Erastus Ethekon, zinaonyesha kuwa tume hiyo imeomba jumla ya Sh74.8 bilioni kwa kipindi cha miaka mitatu ya maandalizi ya uchaguzi. Hata hivyo, serikali imetenga Sh41.3 bilioni pekee, na kuacha pengo la Sh33.5 bilioni ambalo IEBC inasema linaweza kuhatarisha maandalizi ya uchaguzi huru na wa kuaminika. Miongoni mwa maeneo yatakayoathirika ni malipo ya maafisa wa uchaguzi, ambayo yanahitaji Sh7.63 bilioni. Tume pia ina madeni ya Sh5.75 bilioni, mengi yakiwa ada za kisheria zilizotokana na chaguzi zilizopita. "Madeni haya yamekuwa yakijilimbikiza kwa muda na yataathiri vibaya shughuli za tume katika kuendesha uchaguzi mkuu wa 2027," ilisema IEBC. Kamati ya Bunge ya Sheria na Masuala ya Kikatiba (JLAC) imeonya Hazina ya Kitaifa kuwa upungufu huo unaweza kulemaza uwezo wa IEBC kutekeleza majukumu yake ya kikatiba. Hata hivyo, wabunge wameikosoa IEBC kwa baadhi ya vipaumbele vya matumizi, wakisema ni vya "ubadhirifu na visivyo na umuhimu". "Kwa nini IEBC inasisitiza kutumia Sh9.2 bilioni kununua vifaa vipya vya KIEMS wakati wabunge hawajapewa matokeo ya ukaguzi kuthibitisha iwapo vifaa vilivyopo vimepitwa na wakati?" akauliza Mbunge wa Rarieda Dkt Otiende Amollo. IEBC inahitaji zaidi ya Sh10.7 bilioni kununua vifaa vipya vya KIEMS na kubadilisha vile vilivyopitwa na wakati. Tume pia inapanga kuongeza vituo vya kupigia kura kutoka 46,229 vilivyotumika katika uchaguzi wa 2022 hadi 55,393, huku idadi ya wapigakura waliosajiliwa ikitarajiwa kufikia milioni 28.5 mnamo 2027. Wabunge pia wameonyesha wasiwasi kuhusu ongezeko la makadirio ya gharama za uchaguzi, ambayo yamebadilika kutoka Sh57 bilioni hadi Sh61 bilioni, Sh63.9 bilioni na hatimaye Sh74.8 bilioni. Kamati ya Bunge ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Katiba imeitaka Hazina kushughulikia pengo hilo na kutoa ratiba ya wazi ya kutolewa kwa fedha ili shughuli za uchaguzi zitekelezwe kwa wakati. IEBC pia imeonya kuwa kutolipwa kwa madeni ya zamani kunaweza kuathiri uendeshaji wake, ikiwemo kesi za mahakamani na kusababisha wanaotoa zabuni kukataa au kujiondoa katika kutoa huduma. Vifaa vya KIEMS vilinunuliwa 2017 na kwa kuwa teknolojia hubadilishwa baada ya miaka 10, IEBC inasema inalazimika kupata vifaa vipya ili kuhakikisha uchaguzi wa 2027 unaaminika. Mtaalamu wa masuala ya uchaguzi Koki Muli, hata hivyo, amependekeza kupunguza vituo vya kupigia kura kwa nusu na kuruhusu hadi wapigakura 2,000 katika kila kituo ili kupunguza gharama. "Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuruhusu angalau wapigakura 2,000 katika kila kituo. Hili halipaswi kutegemea Bunge kama ilivyo sasa. IEBC inaweza kuamua idadi ya wapigakura kwa kila kituo kiutawala," akasema Bi Muli.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 43 minutes ago
Mahakama yapiga breki ujenzi wa msikiti Treasury Square
MAHAKAMA ya Mazingira na Ardhi mjini Mombasa imesimamisha ujenzi wa msikiti katika Bustani ya Treasury Square eneo la kihistoria na la burudani ya umma, hadi kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria wa Mombasa itakaposikilizwa na kuamuliwa. Chama hicho kinasema Bustani hiyo ni ardhi ya umma inayoshikiliwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Kwa mujibu wa chama hicho, mamlaka haziwezi kubadilisha matumizi ya eneo hilo bila kufuata Katiba pamoja na sheria za mipango miji na mazingira. Mahakama imetoa amri ya muda ya kusimamisha ujenzi katika eneo hilo. "Ombi la mlalamishi limekubaliwa. Ujenzi katika eneo hilo usitishwe hadi kesi hii itakaposikilizwa na kuamuliwa," Mahakama iliamuru. Mahakama pia imewaagiza washtakiwa kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 10 baada ya kupokea hati za kesi. Chama cha Wanasheria wa Mombasa kitapewa siku saba baada ya kupokea majibu hayo kuwasilisha kiapo cha nyongeza pamoja na hoja zake za kisheria. Washtakiwa watakuwa na siku saba zaidi kuwasilisha hoja zao. Washtakiwa ni pamoja na Spika wa Bunge la Kaunti ya Mombasa, Aharub Khatri, Serikali ya Kaunti ya Mombasa, Tume ya Kitaifa ya Ardhi, Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi na taasisi nyingine. Katibu Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Mombasa, Natasha Ali Errey, anasema uchunguzi wa chama hicho umeonyesha kuwa ujenzi ulianza kwenye ardhi ya umma bila idhini muhimu ya kimazingira. "NEMA ilithibitisha kuwa haikuuidhinisha ujenzi huo," Bi Errey anasema katika hati ya kiapo ya kuunga mkono kesi hiyo. Chama hicho kinasema ujenzi wa jengo la kudumu ulianza katika Bustani hiyo Julai 2026. Kwa mujibu wa chama hicho, jengo hilo linajengwa kwa ajili ya msikiti. Chama hicho kinadai kuwa mradi ulianza bila wananchi kushirikishwa kikamilifu. Pia kinasema hakukuwa na mabadiliko rasmi ya matumizi ya ardhi wala vibali vyote vinavyohitajika vya mipango miji na mazingirA. Kwa mujibu wa chama hicho, ujenzi huo umebadilisha kwa kiasi kikubwa matumizi na sura ya eneo hilo la burudani. Pia kinadai kuwa mradi ulianza bila leseni ya tathmini ya athari kwa mazingira. Hali hiyo, kinasema, imewaweka wakazi, wafanyakazi na wageni katika hatari ya kukumbwa na vumbi, uchafu na kelele. Chama hicho pia kinasema ujenzi huo umezuia wananchi kufikia Bustani hiyo. Bustani hiyo ni eneo la wazi la umma lililokuwepo kwa muda mrefu. Lina ukubwa wa takriban mita 300 kwa 200 na linakabili Bunge la Kaunti ya Mombasa. Serikali ya Kaunti ya Mombasa ndilo linalolisimamia. Bustani hiyo ni sehemu ya mandhari ya kihistoria ya Mombasa. Imezungukwa na majengo ya enzi ya ukoloni, yakiwemo Ofisi ya Kamishna wa Kaunti, Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu ya Mombasa. Pia kuna maeneo mengine ya kihistoria katika mazingira yake. Bustani hiyo ina sanamu ya shaba ya mfanyabiashara na mwanzilishi wa shughuli za elimu Allidina Visram. Kwa vizazi vingi, Bustani hiyo imekuwa eneo la burudani, mapumziko na mikusanyiko ya umma. Miti yake mikubwa ya asili na ile iliyoletwa kutoka maeneo mengine hutoa kivuli dhidi ya joto la Mombasa. Pia huhifadhi ndege na viumbe wengine wa mijini. "Hadi hivi karibuni, eneo hilo limetumiwa na kufurahiwa na wananchi, wakazi na wageni wa Jiji la Mombasa kama eneo la burudani, mapumziko na mikusanyiko ya umma ambako shughuli mbalimbali hufanyika," Bi Errey anasema. Chama hicho kinadai kuwa Bw Khatri aliongoza mradi huo akiwa katika nafasi yake binafsi na pia kama Spika wa Bunge la Kaunti. Kinasema alifanya hivyo kwa ushirikiano au kwa msaada wa walalamikiwa wengine. Madai hayo bado hayajathibitishwa mahakamani. Chama hicho kinataka Mahakama itamke kuwa Bustani ni ardhi ya umma inayoshikiliwa kwa niaba ya wananchi wa Mombasa na Kenya. Pia kinataka Mahakama iamuru kuwa eneo hilo haliwezi kuendelezwa bila kufuata sheria. Aidha, kinataka Mahakama ibatilishe vibali au idhini zozote zilizotolewa kuhusiana na mradi huo na kuzuia kabisa ujenzi zaidi. Iwapo Mahakama itaamua kuwa ujenzi huo ni kinyume cha sheria, chama hicho kinataka majengo yote yabomolewe. Pia kinataka Bustani hiyo irejeshwe katika hali yake ya awali.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 2 hours ago
Mbunge wa Emurua Dikirr aonya Gachagua asikanyage Bonde la Ufa
ZIARA inayopangwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Bonde la Ufa imezua joto la kisiasa baada ya Mbunge wa Emurua Dikirr David Keter kumwonya asithubutu kufika katika eneo hilo. Bw Keter ambaye alichaguliwa na UDA miezi miwili iliyopita, amesema Bw Gachagua si mgeni anayekaribishwa katika eneobunge hilo. Alirithi kiti hicho baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge Johana Ngeno katika ajali ya helikopta Februari 28, 2026. Onyo hilo limekuja wiki moja baada ya Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot kuongoza wabunge kutoka eneo hilo kusema Bw Gachagua ana uhuru wa kutembelea eneo hilo. Hata hivyo, Bw Cheruiyot alimtaka Bw Gachagua asidhani mikutano yake itabadilika kuwa kura za DCP katika uchaguzi wa 2027. Bw Gachagua ametangaza mara kadhaa kuwa ataanza ziara yake Kusini mwa Bonde la Ufa Bomet, Kericho na Narok kabla ya kuelekea Kaskazini mwa Bonde la Ufa ambako atatembelea Nandi, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Baringo, Trans Nzoia na Pokot Magharibi. Baada ya Bonde la Ufa, kiongozi huyo wa DCP anatarajiwa kuelekea Magharibi kutafuta uungwaji mkono huku akilenga kulemaza umaarufu wa UDA na kampeni za Rais William Ruto. "Nataka kumwonya Bw Gachagua asithubutu kufika Emurua Dikirr kwa sababu hakaribishwi hapa. Afadhali aelekeze nguvu zake kwingine kwani hapa ni ngome ya UDA," akasema Bw Keter. Katika uchaguzi mdogo wa Emurua Dikirr, Bw Keter alipata kura 18,266 na kushinda, huku mgombea wa DCP Vincent Kibet Rotich akimaliza wa pili kwa kura 10,760. Hata hivyo, DCP imepata mafanikio katika Narok, jambo ambalo limeongeza matumaini ya Bw Gachagua kupenya ngome ya UDA. Katika uchaguzi mdogo wa udiwani Narok Mjini mnamo Novemba 2025, mgombea wa DCP Douglas Twala Masikonte alimshinda mwaniaji wa UDA Robert Kanyinke Ole Kudate kwa kura 6,007 dhidi ya 4,479. "Hakuna eneo la Bonde la Ufa linaloweza kugawanywa kisiasa kwa sababu watu wameelimika kuhusu haki zao. Wanaojaribu kuwazuia viongozi wa upinzani kufanya kampeni wakumbuke kuwa hawawezi kuzuia azma ya wananchi kufanya maamuzi yao," akasema Bw Rotich. Bw Keter pia amemshutumu Bw Gachagua kwa kuwatusi Wakalenjin huku akitafuta kura zao. "Haikubaliki kwetu kwamba Bw Gachagua amekuwa akimshambulia Rais William Ruto na watu wa jamii yake ya Kalenjin kila siku, akiwaita majina ya kila aina kila anapopata nafasi," akasema. Lakini Bw Cheruiyot alisema Bonde la Ufa haiwezi kuwafungia milango viongozi wa upinzani kwa kuwa wakazi wake ni wakarimu. Seneta huyo alisema wakazi watampokea Bw Gachagua lakini wasitarajie kura. Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago pia alimkaribisha Bw Gachagua lakini akamtaka asichochee migawanyiko. Bonde la Ufa imewahi kukumbwa na ghasia za kisiasa katika chaguzi za 1992, 1997 na 2007, ambapo mamia ya watu waliuawa, wengine kujeruhiwa na maelfu kulazimika kuyahama makazi yao. Bw Gachagua analenga kuvutia jamii ya Kipsigis, akisema inafanana na jamii za Mlima Kenya kwa kuwa ni waaminifu lakini hawasahau viongozi wanaowasaliti.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
Mbadi: Nitaendelea kuvumisha ODM na Tutam!
WAZIRI wa Fedha, John Mbadi amesema hataacha kushiriki siasa za ODM licha ya shinikizo kuwa maafisa wa serikali wajiepushe na siasa za moja kwa moja kuelekea uchaguzi wa 2027. Bw Mbadi alisema atatumia wikendi zake kuimarisha ODM na kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi katika uchaguzi ujao. "Jumamosi na Jumapili zote ni siku zangu za mapumziko. Nitatumia siku hizo kushiriki siasa, hasa siasa za ODM," akasema Bw Mbadi. Waziri huyo, aliwahi kuwa mwenyekiti wa ODM kwa miaka 10 kabla nafasi hiyo kuchukuliwa na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga. Bw Mbadi alisema ODM inaendelea kuwa na umuhimu katika siasa za Kenya licha ya vyama vingine vilivyoanzishwa baadaye kusambaratika. Akizungumza katika hafla ya mchango eneobunge la Ndhiwa, Bw Mbadi alisema hatakaa kimya na kuacha ODM iporomoke. Alimwahidi Bi Wanga msaada wake kuhakikisha ODM inapata zaidi ya wabunge 100 katika uchaguzi wa 2027. "Nitakuunga mkono (Wanga) kuhakikisha ODM inapata zaidi ya wabunge 100 katika Bunge la Kitaifa. Nitatembea nawe," akasema Bw Mbadi. Waziri huyo alisema atashirikiana na viongozi wengine, akiwemo kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga, kuhakikisha chama kinapata magavana wengi na wajumbe wengi wa mabunge ya kaunti. "Nitawapa msaada unaohitajika pamoja na kiongozi wetu wa chama Dkt Oburu Oginga kuhakikisha ODM inapata magavana wengi na madiwani wengi katika mabunge ya kaunti. Tutafanya chochote kinachohitajika kuunga mkono ODM," akaongeza. Bi Wanga alisema ODM inalenga kushinda zaidi ya viti 127 vya ubunge na imeandaa mikakati ya kushinda maeneo ambayo imeyabaini kuwa na nafasi nzuri. "Sisi kama kikosi cha ODM tuko kazini. Tuko imara tunapoelekea mbele na wakati huu tutapata zaidi ya viti 100 vya ubunge," akasema. Gavana huyo pia alisema ODM haitashirikiana na viongozi wanaohusishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akisema chama kinaweza kujadiliana na UDA pekee. "Ndiyo maana hatuwezi kuwa upande moja Gachagua. Anaeneza siasa za ubaguzi, siasa za makabila makubwa na madogo," akasema. Bw Mbadi pia alimshambulia Bw Gachagua akisema siasa za kikabila haziwezi kuwa msingi wa uongozi wa kitaifa. "Huwezi kuwa kiongozi ambaye anaendelea kusema unataka kuwa rais kwa sababu jamii yako ina kura nyingi. Unataka kuongoza jamii yako au nchi nzima? Huyo si kiongozi ambaye tunaweza kushirikiana naye," akasema. Seneta Moses Kajwang alisema ODM bado ina nguvu nyingi Homa Bay na akawahimiza wakazi kujiandikisha kama wapigakura ili kuimarisha chama. "Tunataka kujenga Kenya mpya ambako kila mtu ana haki ya kupata huduma. Ndiyo maana tulimpiga kura ya kumwondoa Gachagua. Alikuwa akisema baadhi ya mambo yamehifadhiwa kwa watu wachache na hilo si sawa," akasema. Seneta huyo pia aliwataka wakazi wa Nyanza kuendelea kumuunga mkono Rais Ruto, akisema serikali imeanzisha miradi ya maendeleo katika eneo hilo baada ya kifo cha Raila Odinga. "Hatutaweza kamwe kumpa kisogo na hatuna nia ya kumfuata James Orengo au Rigathi Gachagua. Viongozi kutoka eneo hili wamekubali kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maendeleo," alisema. Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma aliwataka wafuasi wa Linda Mwananchi kuepuka lugha ya matusi wanapopanga kuandaa mkutano wikendi ijayo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
Wantam!Macho yote kwa Gen Z iwapo watapiga kura 2027
KWA miaka mingi, vijana wamekuwa wakitajwa kuwa kundi kubwa ambalo linaweza kuamua matokeo ya uchaguzi nchini, lakini mara nyingi huwa hawapigi kura. Hali hiyo ilibadilika mnamo 2024 wakati kizazi cha Gen Z kilipoongoza maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha na kubadilisha kabisa ramani ya siasa nchini. Vijana walitumia mitandao ya kijamii kama TikTok, X na Instagram kueleza kwa lugha rahisi vipengele vya Mswada wa Fedha walioamini vingeongeza mzigo wa maisha kwa Wakenya. Kauli mbiu kama #RejectFinanceBill2024 na #OccupyParliament zilisambaa kwa kasi na kugeuza mitandao ya kijamii kuwa kituo kikuu cha kuratibu maandamano yaliyowaleta pamoja vijana kutoka maeneo na makabila mbalimbali. Mnamo Juni 25, 2024, waandamanaji waliingia katika majengo ya Bunge wakati Mswada wa Fedha ulipokuwa ukijadiliwa, katika tukio lililovuta hisia za kimataifa. Kufuatia shinikizo hilo, Rais William Ruto aliuondoa Mswada huo na kukataa kuutia saini kuwa sheria. Tukio hilo liliwapa vijana imani kwamba wanaweza kuathiri maamuzi ya serikali bila kutegemea vyama vya kisiasa au viongozi wa jadi. Sasa, macho yanaelekezwa kwa uchaguzi wa 2027 na iwapo Gen Z itageuza nguvu hiyo ya maandamano kuwa nguvu ya kupiga kura. Charles Mutisya, kijana wa Gen Z kutoka Mombasa, amesema vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuamua viongozi watakaoongoza nchi. Alisema lengo ni kuwaleta pamoja makundi mengine kama waendesha bodaboda na mama mboga ili kuunda nguvu kubwa ya wapigakura. "Tunahitaji kubaki tukiwa na umoja. Tulianzisha vuguvugu la #TukoKadi na ikiwa Gen Z tutasalia kuwa wasiojali, hatutatimiza lengo tuliloweka la kuchagua viongozi wazuri," akasema Bw Mutisya. Aliwataka vijana kupanga upya mikakati yao baada ya kutokea kwa migawanyiko tangu maandamano ya 2024, akisema hali hiyo imewapa wanasiasa nafasi ya kurudisha siasa za kikabila miongoni mwa vijana. "Tunahitaji kufanya maamuzi huru 2027 kwa sababu sasa unaweza kuona wao (wanasiasa) wanatumia siasa za ukabila kutugawanya. Sitarajii Gen Z wafikiri kama mtu wa kijijini, tunahitaji kutenda tofauti na kupinga aina ya siasa tulizo nazo Kenya," akaongeza. Katika kampeni ya kuongeza usajili wa wapigakura iliyokamilika Aprili 2026, wapigakura wapya 2,612,725 walijiandikisha. Kati yao, 2,345,476 waliandikishwa kupitia mpango maalum wa usajili huku 267, 249 wakijiandikisha kupitia usajili wa kawaida. Ingawa IEBC haikutoa takwimu za wapigakura hao kulingana na umri, tume hiyo ilisema vijana wengi walijitokeza, hasa kutokana na vituo vya usajili vilivyowekwa katika vyuo vya elimu ya juu. Mnamo 2022, vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 34 walikuwa wapigakura 8.8 milioni, sawa na karibu asilimia 40 ya wapigakura waliosajiliwa. Gen Z wenye umri wa miaka 18 hadi 29 wanatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa kufikia 2027, baada ya mamilioni ya waliokuwa chini ya miaka 18, 2022 kufikisha umri wa kupiga kura. Mwanaharakati Walid Sketty wa Mombasa alisema vijana wakijitokeza kwa wingi wanaweza kuwa na kura muhimu ya maamuzi. Kwa sasa, kushiriki kwa Gen Z katika siasa hauishii kupiga kura. Vijana wanatumia video fupi, mijadala ya moja kwa moja na mitandao ya kijamii kuelimisha wenzao, kufichua masuala ya uongozi na kuwawajibisha viongozi. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alitambua nguvu hiyo baada ya zoezi la usajili wa wapigakura. "Nyinyi ndio nguvu iliyowasha injini hii. Kupitia nyimbo zenu, lebo zenu za mitandao, dansi zenu na uhamasishaji wa rika kwa rika, mmeonyesha kuwa si viongozi wa kesho pekee, bali washikadau wakuu wa leo, na kwa kweli, mnaweza kuongoza leo," akasema. Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, swali kuu sasa ni iwapo Gen Z itaweza kudumisha umoja wake na kugeuza ushawishi wake wa mitandao na maandamano kuwa kura.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Wantam,tutam! Ni mwaka moja tu kujua mbivu na mbichi
MWAKA mmoja kuanzia leo, Wakenya watamiminika vituo vya kupigia kura kufanya uamuzi kuhusu atakayewatawala hadi 2032. Watachagua ama kumkabidhi Rais William Ruto muda mwingine wa miaka mitano au kumpa nafasi kiongozi mpya kuchukua usukani. Katika uchaguzi huo ambao tayari umepachikwa lakabu ya 'Tutam' dhidi ya 'Wantam', wapigakura watawachagua wabunge 290 wa Bunge la Kitaifa, magavana 47 na manaibu wao 47, wabunge wawakililishi wanawake 47, maseneta na madiwani (MCAs) kutoka wadi. Taifa limegawanywa katika wadi 1,450 za uchaguzi. Huu utakuwa uchaguzi mkuu wa nane tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi 1992. Utakuwa vilevile uchaguzi wa kwanza tangu 1997 ambapo jina la Raila Amolo Odinga halitajitokeza, ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kwenye karatasi za kupiga kura. Bw Odinga aliaga dunia Oktoba mwaka jana na aliwania urais 1997, ubunge wa Langáta 2007, urais 2013, 2017 na 2022. Mnamo 2022, kulikuwepo vituo vya kura 46,229. Kwenye kura ya 2027, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inatarajiwa kuongeza vituo zaidi. Sajili ya IEBC ilikuwa na wapigakura wasiopungua 22.1 milioni 2022, na inatazamiwa kuwa idadi isiyopungua 6.3 milioni itaongezwa kwenye sajili mpya 2027. Tume inapanga shughuli ya usajili Januari mwaka ujao itakayoendeshwa kwa siku 30 kuanzia Januari 11 hadi Februari 9, 2027. amani ya kisiasa inatarajiwa kubadilikabadilika kabla ya siku ya uchaguzi, hasa upande wa upinzani. Hata Rais Ruto ambaye tayari yupo kwenye ushirikiano na ODM inayoongozwa na Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga ndani ya Serikali Jumuishi, angali anavutia vyama zaidi, huku baadhi kutoka upinzani wakitarajiwa kujiunga naye, hasa iwapo watafarakana kuhusu atakayepeperusha bendera ya urais. Ili kupanga kambi yake, Agosti 3, Baraza la muungano wa Azimio linaloongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, lilipitisha mchakato wa mabadiliko na kuwakaribisha wanasiasa wapya. Baraza hilo liliwajumuisha Naibu Kiongozi wa Jubilee Dkt Fred Matiang'i, Kiongozi wa PNU Peter Munya na Seneta wa zamani wa Embu Lenny Kivuti katika kamati kuu ya baraza la Azimio. Lilikaribisha vilevile chama cha Justin Muturi cha Democratic Party, People's Democratic Party na Umoja na Maendeleo Party. Aidha baraza liliafikiana kufanya mageuzi na kumteua mgombea mmoja kumenyana na Rais Ruto. Lilianzisha vilevile mazungumzo na chama cha Rigathi Gachagua cha Democracy for the Citizens Party (DCP) na Linda Mwananchi, vuguvugu linaloendeshwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna. Kabla ya hapo, Bw Kenyatta alimtaja kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, kuwa kiongozi wa chama cha Azimio, nafasi iliyoshikiliwa na Bw Odinga. Ingawa hivyo, mratibu wa haya yote haya ni mtu ambaye hawezi kuwania binafsi. Bw Kenyatta anazuiliwa na kanuni ya hatamu, hashikilii afisi yeyote muhimu katika mpangilio mpya na anafanya kazi pasipo kumulikwa. Kinara wa People's Liberation Party, Martha Karua na wa DAP Eugene Wamalwa ni vinara katika muungano wa upinzani. Huku upinzani ukijadiliana, Rais vilevile anaendelea kusaka uungwaji mkono mashinani kwa kukutana na makundi mbalimbali mashinani. Katika wiki ya kwanza Agosti pekee, Ikulu iliwakaribisha wazee wa kijiji Jumanne, viongozi wa Kiislamu Jumatano na walinzi wa mashirika ya kibinafsi zaidi ya 5,000 Alhamisi. "Mko tayari?" Rais aliuliza katika kikao kimoja. Anaelewa uzito wa kibarua kinachomkabili. "Mtanisaidia kueneza neno hili kwa watu vijijini?" akasema. Matokeo ya utafiti wa TIFA yaliyofanyika kati ya Juni 13 na 22 miongoni mwa wahojiwa 2,048 katika maeneo tisa na kutolewa Julai 24 unamweka rais katika asilimia 24, ambayo haijabadilika kutoka Mei. Hii ni idadi dhaifu kwa rais anayetawala na itabidi Rais Ruto akaze buti ili awe na uungwaji mkono pia maeneo mengine. Seneta Sifuna ni wa pili kwa asilimia 15 akipanda kutoka 10 mnamo Mei na kutoka sufuri mwishoni mwa 2025. Bw Musyoka naye aliporomoka hadi asilimia 13 kutoka kilele cha asilimia 25 Novemba. Wakishajiishwa na uchaguzi mdogo wa Ol Kalou ambapo mwaniaji wa upinzani alimponda wa chama tawala, UDA, muungano wa upinzani unatumai kurudia ushindi huo katika jukwaa la kitaifa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 09 Aug 2026 02:55:09
BATUK: Wabunge wadai Kenya haijaingia katika makubaliano na Uingereza
Wabunge wamesisitiza kuwa hakuna makubaliano mapya yaliyofikiwa kati ya Kenya na Uingereza kuhusu mkataba wa ushirikiano wa kijeshi na Kenya (BATUK). Kauli hiyo inajiri baada ya Uingereza kusema kuwa kumekuwa na maendeleo makubwa katika kutekeleza baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi. Uingereza ilisema maafisa wake wakuu walikutana na maafisa wa serikali ya Kenya, wabunge na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Masuala ya Kigeni Juni kujadili hatua iliyofikiwa. "Maafisa wakuu wa Uingereza walikutana na maafisa wa Serikali ya Kenya, wabunge na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Masuala ya Kigeni mwezi Juni kujadili maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa," ilisema taarifa hiyo. Uingereza pia ilisema taratibu za pamoja za kushughulikia mabomu na vilipuzi ambavyo havijalipuka zimekamilishwa. Miongoni mwa masuala mengine yaliyoshughulikiwa ni mahitaji ya ulinzi wa mazingira na matumizi ya ardhi, ambayo yamewasilishwa kwa mamlaka husika. Uingereza pia ilisema imeweka hatua mpya za kuzuia unyanyasaji wa kingono. Hata hivyo, Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi iliambia Bunge Jumanne kuwa mkataba huo bado haujaidhinishwa. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Nelson Koech, alisema makubaliano hayo hayawezi kuanza kutumika hadi masharti yaliyowekwa na Kenya yatimizwe. Bunge linataka vifungu vya 6(5) na 23 virekebishwe ili mauaji yawe chini ya mamlaka ya mahakama za Kenya. Wabunge pia wanataka BATUK iwe na mpango wa uwajibikaji kwa jamii unaohusisha maeneo inayofanyia shughuli zake. Bw Koech alisema kamati haitakubali mkataba unaokiuka Katiba au kudhalilisha Wakenya. Alisema kujumuishwa kwa mauaji katika vifungu vinavyopendekezwa kutaimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wahalifu wa makosa hayo makubwa wanawajibishwa nchini. Mbunge wa Laikipia wa Kike Jane Kagiri aliunga mkono msimamo huo, akisema mtu yeyote anayefanya uhalifu nchini Kenya anapaswa kufikishwa mbele ya mahakama za Kenya. Kwa sasa, mkataba huo unaacha makosa kadhaa makubwa chini ya mamlaka ya Kenya, lakini mauaji hayajajumuishwa katika orodha hiyo. Hali hiyo imeibua wasiwasi kwamba Uingereza inaweza kudai mamlaka ya kushughulikia kesi za mauaji yanayohusisha wanajeshi wake. Bw Koech alisema masharti ya kamati bado hayajatimizwa licha ya serikali kutangaza kuanza tena kwa mafunzo ya pamoja ya kijeshi kati ya Kenya na Uingereza katika kituo cha BATUK, Laikipia. Alisema mazungumzo na kubadilishana mawasiliano kumeendelea, lakini Uingereza bado haijatoa ahadi ya kutosha kuhusu madai ya Kenya. BATUK imekuwa ikifanya shughuli nchini Kenya chini ya Mkataba wa Ushirikiano wa Ulinzi kati ya Kenya na Uingereza uliopitishwa mwaka 2016. Mkataba mpya uliwasilishwa Bungeni mwaka 2021 baada ya muda wa mkataba wa awali wa miaka mitano kuisha. Hata hivyo, Bunge la 12 lilimaliza muda wake kabla ya kuidhinisha mkataba huo. Mkataba huo uliwasilishwa tena kwa Bunge la 13 mwezi Novemba 2022. Baada ya kushirikisha wananchi, kamati ilipendekeza uidhinishwe kwa masharti kwamba vifungu vya 6(5) na 23 virekebishwe kabla ya kuanza kutumika.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 08 Aug 2026 22:55:39
Linda Mwananchi ilivyopokonywa jina
VUGUVUGU la Linda Mwananchi limetishia kufanya maandamano ya kila siku nje ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) iwapo ombi lake la kusajiliwa kama chama cha kisiasa halitashughulikiwa. Hatua hiyo inazidisha mvutano kati ya vuguvugu hilo na ofisi ya Msajili wakati Linda Mwananchi ikijaribu kujibadilisha kuwa chama rasmi cha kisiasa kabla uchaguzi mkuu wa 2027. Akizungumza wakati wa ziara ya Linda Mwananchi ya kukutana na wananchi katika Kaunti ya Busia siku ya Ijumaa, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alilaumu watu ambao hakuwataja kwa kujaribu kunyakua jina linalohusishwa na vuguvugu hilo. Osotsi alisema kundi hilo litampa Msajili hadi kesho kutatua suala hilo. Alionya kuwa iwapo suala hilo halitatatuliwa basi wafuasi wa Linda Mwananchi wataanza kufanya mikutano ya kila siku nje ya ofisi za ORPP. "Ruto ametuma wakora kule kwa ofisi ya msajili wa vyama eti wanajaribu kunyakua hii jina yetu. Mimi nataka kuambia William Ruto, Ibara ya 38 inaruhusu Mkenya yeyote kuunda chama," alisema Osotsi. Akaongeza: "Tunaambia huyo msajili kama hutapatiana hiyo jina Jumatatu, tutaandaa mikutano ya kila siku kwa hiyo ofisi." Mzozo huo umejikita katika maombi ya kusajili chama na namna Ofisi ya Msajili inashughulikia jina linalopendekezwa na Linda Mwananchi. Mvutano huo ulipata sura mpya baada ya ORPP kuripotiwa kusajili Liberty National Democratic Alliance, kinachojulikana kama LINDA Party. Hatua hiyo imeibua mvutano mpya na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna pamoja na washirika wake katika Linda Mwananchi. Usajili wa chama kinachotumia jina LINDA umeleta changamoto mpya kwa juhudi zao. Kwa mujibu wa ripoti, chama hicho kipya kinahusishwa na kundi tofauti ambalo pia lilikuwa limejitahidi kupata utambulisho wa kisiasa kwa kutumia jina "Linda". Kundi hilo pinzani limepinga madai ya Linda Mwananchi kwamba ndilo lenye haki ya kutumia jina hilo. Madai hayo yameibua swali kuhusu kundi lenye haki ya kutumia jina na nembo zinazohusishwa na "Linda". Mzozo huo pia umewekea Ofisi ya Msajili shinikizo kutoka pande zote. Viongozi wa Linda Mwananchi wamekuwa wakisisitiza kuwa tayari wamejenga utambulisho wa kisiasa kupitia jina hilo, hivyo wanafaa kupewa nafasi ya kukitumia chama hicho. Hatua ya hivi majuzi inafuatia mikutano kati ya viongozi wa Linda Mwananchi na Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou. Ripoti zinasema kuwa Msajili alikubali kupitia upya uamuzi wa awali wa kukataa jina la Linda Mwananchi baada ya mashauriano na wawakilishi wa vuguvugu hilo. Hatua hiyo ilikuwa imeibua matumaini miongoni mwa viongozi na wafuasi wa Linda Mwananchi kwamba mchakato wa usajili ungeendelea. Hata hivyo, usajili ulioripotiwa wa LINDA Party umeleta changamoto mpya na kugubika Linda Mwananchi na mzozo mwingine kuhusu jina inalotaka kutumia. Wadadisi wanasema haki inayotokana na Kifungu 38 cha Katiba - kinachowapa raia haki ya kuunda au kushiriki katika uundaji wa chama cha kisiasa - inaambatana na masharti ya kisheria yanayosimamia usajili wa vyama vya kisiasa nchini. Ofisi ya Msajili ina jukumu la kusajili na kudhibiti vyama pamoja na kusimamia taratibu za kisheria zinazohusu kuanzishwa kwa vyama. Linda Mwananchi sasa inataka ORPP itatue mzozo huo ili iweze kukamilisha miundo yake kabla ya uchaguzi ujao. Usajili wa chama ni hatua muhimu katika kubadilisha vuguvugu hilo kuwa chombo rasmi cha uchaguzi. Kwa sasa, viongozi wake wameweka Jumatatu kuwa siku ya mwisho kwaMsajili wa Vyama kushughulikia suala hilo kabla kuanza kwa mikutano ya kila siku nje ya ofisi hiyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 08 Aug 2026 23:55:36
Tofauti zaibuka kuhusu tarehe ya kuandaa uchaguzi
INGAWA Katiba ya 2010 iliweka tarehe ya uchaguzi ili iwe wazi na ya kutabirika, suala hilo limefikishwa mahakamani angalau mara tano tangu 2015. Kesi hizo zimehusisha majaji 13 na kuzua tafsiri tofauti kuhusu maana ya kifungu kinachosema uchaguzi ufanyike "Jumanne ya pili ya Agosti katika kila mwaka wa tano". Mzozo huo umeibuka tena baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Malindi Mugure Thande kuamua kuwa uchaguzi mkuu ulipaswa kufanyika Agosti 2026 badala ya 2027. Mwanasheria wa masuala ya Katiba Waikwa Wanyoike anasema mkanganyiko huo unatokana na dhana kwamba Katiba inamhakikishia kila kiongozi aliyechaguliwa kipindi cha miaka mitano. Vita vya kwanza vilianza kabla ya uchaguzi wa 2017 baada ya watu watatu kupinga tarehe iliyokuwa imewekwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC). Walidai kuwa uchaguzi wa madiwani wa kaunti (MCAs) Agosti 8, 2017 ungekatiza kipindi chao cha miaka mitano kwa karibu miezi minane. Jaji Edward Muriithi aliamua Aprili 2017 kuwa kulikuwa na mkanganyiko kati ya vifungu viwili vya Katiba kuhusu muda wa madiwani na tarehe ya uchaguzi. Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa ilibatilisha uamuzi huo Novemba 2017 na kusema tarehe ya uchaguzi iliyowekwa na Katiba haiwezi kubadilishwa. Kesi nyingine iliwasilishwa mwaka 2018 na mwanaharakati Okiya Omtatah na Nyakina Wycliffe Gisebe. Walidai uchaguzi ulipaswa kufanyika Agosti 2021 badala ya 2022. Jaji Weldon Korir alikataa kesi hiyo Novemba 2020, akisema uchaguzi wa viongozi wote unapaswa kufanyika siku moja baada ya kipindi cha miaka mitano. Mwaka 2022, aliyekuwa Seneta mteule Paul Njoroge alipinga tarehe ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9. Jaji Anthony Mrima alikataa hoja hiyo. Mzozo huo ulifika Mahakama ya Juu mwaka 2025 baada ya mwanasheria Dkt Owiso Owiso na wanaharakati Khelef Khalifa na Ashioya Biko kutaka mahakama hiyo ieleze kifungu cha 136(2)(a). Mahakama hiyo ya majaji saba haikugusia kiini cha kesi na ikaiondoa Agosti 15, 2025 kwa misingi ya mamlaka yake. Walalamishi hao walienda Mahakama Kuu ya Malindi, ambako Jaji Thande aliamua kuwa uchaguzi mkuu ulipaswa kufanyika Jumanne, Agosti 11, 2026. Bw Wanyoike anaunga mkono tafsiri hiyo akisema Katiba haimhakikishii Rais, wabunge na maseneta kipindi kamili cha miaka mitano. Hata hivyo, mwanasheria Dudley Ochiel anapinga akisema historia ya kutunga Katiba inaonyesha wazi kuwa Kenya ilikusudia kuwa na mzunguko wa uchaguzi wa miaka mitano. "Historia ya Katiba haiungi mkono nia ya kuanzisha vipindi vya miaka minne kwa viongozi waliochaguliwa," alisema. Mwanasheria Ndung'u Wangenye anasema Mahakama ya Juu ndiyo itakayotoa jibu la mwisho kuhusu suala hilo. "Suluhisho la mwisho litakuwa uamuzi wa Mahakama ya Juu," alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 09 Aug 2026 00:55:57
Malumbano ya ubabe Mlimani kati ya Gachagua, Munya raha kwa Ruto
MALUMBANO yanayoendelea kati ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na baadhi ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya huenda yakawa habari njema kwa Rais William Ruto anapojiandaa kutetea kiti chake katika uchaguzi wa 2027. Kinachoonekana kama mzozo wa kawaida kuhusu vyama kinaweza kuwa na athari kubwa kwa siasa za upinzani, hasa katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya wapigakura. Mzozo huo ulizuka baada ya viongozi wa vyama kadhaa kupinga kauli zinazohusishwa na Gachagua, kwamba vyama vidogo vinafaa kuvunjwa ili vijiunge na Democracy for the Citizens Party (DCP). Miongoni mwa waliopinga wazo hilo ni kinara wa Democratic Party (DP) Justin Muturi, kinara wa Party of National Unity (PNU) Peter Munya na kinara wa Devolution Empowerment Party (DEP) Lenny Kivuti. Viongozi hao walisema umoja wa upinzani haupaswi kujengwa kwa masharti au shinikizo, bali kupitia mashauriano, kuheshimiana na ushirikiano wa hiari. Hata hivyo, malumbano hayo yanaibua swali kubwa kuhusu nani atakuwa na ushawishi mkubwa Mlima Kenya kuelekea 2027. Tangu kuondolewa kwake kama Naibu Rais, Gachagua amekuwa akijaribu kujijenga kama kiongozi mkuu wa kisiasa wa eneo hilo. DCP imekuwa chombo muhimu katika mkakati huo, huku washirika wake wakijaribu kuunganisha wanasiasa wa mlimani chini ya chama kimoja kabla ya mazungumzo ya muungano wa kitaifa. Lakini msimamo wa Muturi, Munya na Kivuti unaonyesha kuwa si viongozi wote wanaompinga Ruto wako tayari kufuata mkondo wa Gachagua. Hilo linaweza kuwa pigo kwa mpango wa Mlima Kenya kuzungumza kwa sauti moja kuelekea 2027. Eneo hilo huwa na nguvu kisiasa linapoungana. Katika chaguzi zilizopita, viongozi walioweza kuunganisha kura za eneo hilo walipata usemi mkubwa katika mazungumzo ya kisiasa kitaifa. Lakini sasa kuna dalili za vituo vingi vya nguvu vita vya ndani vikionekana kuchacha. Jambo linalojitokeza kwenye mzozo huo ni kwamba baadhi ya viongozi wanaompinga Ruto sasa wanatumia nguvu nyingi kumjibu Gachagua, kuliko kueleza namna watakavyompinga Rais katika uchaguzi ujao. Badala ya mjadala kuwa Ruto dhidi ya upinzani, unaanza kuwa Gachagua dhidi ya viongozi wengine wa upinzani na wachambuzi wa siasa wanasema hili linaweza kumfaa Ruto. "Kadiri viongozi hao wanavyobishana kuhusu nani anafaa kuongoza Mlima Kenya, ndivyo wanapoteza muda wa kujenga kampeni moja kubwa ya kitaifa dhidi ya serikali.Kila tofauti ya maoni inaongeza uwezekano wa upinzani kuingia 2027 ukiwa umegawanyika," asema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki. Kiini cha mzozo huo ni: nani ana haki ya kuzungumza kwa niaba ya Mlima Kenya? Washirika wa Gachagua wamemtaja kama kiongozi wa kisiasa wa eneo hilo kufuatia kuondolewa kwake mamlakani. Lakini wapinzani wake wanasema hakuna mtu aliyepewa mamlaka ya kuwa msemaji wa eneo lote. Muturi, Munya na Kivuti wanasisitiza kwamba hakuna mkutano uliowahi kufanyika kumpa Gachagua mamlaka hayo. Pia wanakumbusha kuwa hata marais wa zamani Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta hawakuwahi kudai vyama vingine vivunjwe ili kuonyesha uaminifu kwao. Wanasema Gachagua anaweza kuwa na ushawishi mkubwa, lakini sio eti hana mpinzani. Viongozi hao pia wanaonekana kuhofu kwamba DCP inaweza kuwa chama kikubwa kinachotawala vyama vingine vidogo. Kwao, kulazimisha vyama vidogo kuvunjwa hakutaimarisha demokrasia. Kwa Ruto mzozo huo unaweza kuwa faida kubwa. "Viongozi wanaompinga wanapogawanyika nafasi ya kujenga upinzani mmoja wenye nguvu hupungua. Aidha, mivutano ya hadharani inaweza kuwafanya wapigakura wa Mlima Kenya kutokuwa na uhakika kuhusu upande wa kuunga mkono," asema Dkt Lilian Kimani, mchanganuzi wa siasa. Anasema hii inaweza kumpa Ruto nafasi ya kujaribu kurejesha ushawishi wake katika eneo ambalo wapinzani wameanza kujishindia.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 09 Aug 2026 01:55:18
Hofu kijijini watoto 10 wakijitia kitanzi
HOFU imetanda katika eneo la Ndabibi Central, Naivasha, baada ya watoto wasiopungua 10 kujitia kitanzi katika kipindi cha mwaka mmoja. Wakazi wanasema visa hivyo vimeacha familia zikijiuliza kinachowasukuma watoto wadogo kujiua. Miongoni mwa waliofariki ni Cynthia Muthoni, mwanafunzi wa Gredi ya Sita. Asubuhi ya Juni 6, alionekana kuwa sawa nyumbani kwao. Rachael Wahu Kariuki na binti yake walikuwa wameenda mtoni kufua nguo kabla ya kurejea nyumbani. Mchana, Wahu alimwacha Muthoni akiosha vyombo na kumuagiza apike chakula kabla ya yeye kurejea kazini. Karibu saa tisa alasiri, mama huyo alirudi nyumbani na kumpata binti yake akiwa katika hali nzuri. Aliondoka tena baada ya kuitwa shuleni. Muda mfupi baadaye, majirani wawili walifika kwa pikipiki na kumuomba awafuate. Walimpeleka kwa jirani, ambapo Wahu aliambiwa binti yake alikuwa amefariki baada ya kujitia kitanzi. Dada yake ndiye aliyegundua na kuwaarifu majirani. "Nilimwacha akiwa na furaha. Hakuwa amefanya kosa lolote na hatukuwa tumegombana. Sijui ni nini kilimfanya ajitie kitanzi," alisema Wahu kwa machozi. Mama huyo alisema Muthoni alikuwa amewahi kuugua ugonjwa wa figo. Dawa alizokuwa akitumia zilifanya mwili wake uvimbe na akaanza kuogopa kuchekwa na wanafunzi wenzake. Alikuwa pia amekataa kurejea shuleni na alitaka kujiunga na mafunzo ya ufundi. Kilomita chache kutoka hapo, familia ya Kiragu Mochogua ilikuwa ikiomboleza kifo cha binti yao wa miaka 16, Jane Wanjiru. Jane alikuwa ameenda kutafuta kuni lakini hakurudi nyumbani.Baba yake alimfuata msituni baada ya kuona nyayo zake.Huko ndiko alipompata binti yake akiwa amefariki. Mama yake, Phyllis Wambui, alisema Jane alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya afya na aliacha shule akiwa Darasa la Tano. Dada yake mdogo pia aliacha shule akiwa Darasa la Tatu ili kumhudumia. Familia ilikuwa imeanza kupanga kumrudisha Jane shuleni baada ya afya yake kuimarika. Lakini alifariki kabla ya mpango huo kutimia. Kifo cha Beth Nyaguthie Juma, mwanafunzi wa Gredi ya Sita, pia kimeongeza majonzi katika eneo hilo. Kaka yake, Peter Chege Juma, alisema alipokea simu ya dharura kutoka kwa majirani na kukimbia nyumbani. Alisema kifo cha dada yake kilimvunja moyo kiasi kwamba aliondoka nyumbani kwao na kukodisha nyumba. "Mama yetu alifariki 2024. Dada yangu alikuwa kitindamimba. Kifo chake kilituacha na maumivu makubwa," alisema. Chifu msaidizi wa Ndabibi Central, Aseth Kariuki, alisema visa hivyo vinazidi kuwa vya kutisha. Alisema watoto wenye umri wa kati ya miaka 12 na 15 ndio walioathirika zaidi. "Mwaka huu pekee, tumewazika watoto watano waliofariki baada ya kujitia kitanzi Ndabibi. Tulipofuatilia visa hivyo, wazazi na walimu walisema hawakuona ishara zozote za hatari," alisema. Mercy Wangui Mburu, mwalimu na mhudumu wa kulinda watoto, alisema angalau watoto 10 wamefariki kwa kujitia kitanzi katika eneo hilo tangu Juni mwaka uliopita. Watoto wengine saba wamejaribu kujiua.Wengi wa walioathirika wana umri wa miaka 12 hadi 17. Wangui alisema wahudumu wa jamii wamelemewa na visa hivyo. "Tunahitaji washauri wa kitaalamu. Hata kama watakaa hapa kwa miezi miwili. Tunataka kuelewa watoto hawa wanapitia nini kwa sababu wanateseka kimya kimya," alisema. Alitaka serikali za kitaifa na kaunti kuingilia kati na kuimarisha huduma za afya ya akili katika shule, makanisa na familia. Mtaalamu wa ushauri nasaha Meshack Ondieki alisema wazazi wanapaswa kuwasikiliza watoto wao na kuzingatia mabadiliko katika tabia zao. Alisema ishara za kuangaliwa ni pamoja na kujitenga na familia, kushuka kwa matokeo shuleni, kupoteza hamu ya shughuli walizopenda na kubadilika kwa uhusiano wao na wenzao. Pia alisema kukosa hamu ya kula, uchovu wa mara kwa mara, kupuuza usafi wa kibinafsi na kukataa kushiriki shughuli za kawaida vinaweza kuwa ishara kwamba mtoto anapitia matatizo ya kihisia. Alisema mabadiliko hayo hayafai kupuuzwa kama tabia za kawaida za ujana, hasa yanapotokea kwa pamoja. Kulingana na takwimu za Kaunti ya Nakuru zilizotajwa na wataalamu wa afya ya akili, zaidi ya visa 400 vinavyohusiana na kujiua viliripotiwa kati ya Januari 2020 na Aprili 2025. Takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa changamoto inayokabili watoto na vijana katika eneo hilo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 08 Aug 2026 21:55:04
ODM sasa yamkalia Ruto ngumu kuhusu 2027, yataja matakwa 8
CHAMA cha ODM kimeweka matakwa manane mbele ya Rais William Ruto kabla ya uchaguzi wa 2027, huku viongozi wa chama hicho wakitarajiwa kuyajadili katika mkutano wa siku tatu wa serikali jumuishi unaoanza Naivasha leo Jumapili. Mkutano huo unawakutanisha magavana, manaibu wao na wabunge wa ODM, UDA na vyama vingine vinavyounga mkono serikali jumuishi. Ingawa mkutano huo umeelezwa kuwa wa kuimarisha uhusiano na kujenga mwafaka, ODM inataka serikali itekeleze makubaliano yaliyofikiwa kabla ya chama hicho kuendelea kushirikiana na UDA kuelekea uchaguzi wa 2027. ODM inataka utekelezaji wa ajenda ya vipengele 10 iliyokuwa msingi wa makubaliano ya kisiasa kati ya Rais Ruto na marehemu aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga alisema viongozi watapitia hatua zlizopigwa katika kutekeleza makubaliano hayo. Ajenda hiyo inahusisha masuala yaliyokubaliwa na pande hizo mbili wakati wa mazungumzo yaliyolenga kupunguza mvutano wa kisiasa nchini. ODM pia inataka serikali kutoa mwelekeo kuhusu miswada iliyotokana na Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (Nadco). Baadhi ya mapendekezo ya Nadco yalihusu kuanzishwa kwa afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani na Waziri Mkuu. Chama hicho kinataka kujua hatua ambayo serikali imechukua kutekeleza mapendekezo hayo. ODM inataka hatua zaidi kuchukuliwa kuhusu fidia kwa waathiriwa wa ukatili wa polisi. Bi Wanga alisema suala hilo litakuwa miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo. Hii ni mojawapo ya masuala ambayo chama hicho kinataka serikali ishughulikie kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa. ODM pia inataka kuwe na uwazi kuhusu mustakabali wa ushirikiano wake na UDA kuelekea uchaguzi wa 2027. Chama hicho kinataka kujua jinsi ushirikiano huo utakavyofanya kazi na nafasi ya kila chama katika maandalizi ya uchaguzi. Huku uchaguzi ukikaribia, viongozi wa vyama hivyo wameanza kushindana kuhusu maeneo ya kisiasa na nafasi mbalimbali. ODM inataka ngome zake za jadi za kisiasa zilindwe katika mpango wa ushirikiano wa uchaguzi. Suala la kutengewa maeneo limekuwa chanzo cha mvutano kati ya ODM na UDA. ODM imekuwa ikitaka ngome zake ziheshimiwe, huku UDA ikitaka kila chama kiruhusiwe kuwasilisha wagombea katika maeneo yote isipokuwa kiti cha urais. Gavana wa Mombasa na naibu kiongozi wa ODM Abdullswamad Nassir alisema suala hilo litashughulikiwa na kamati maalum ya vyama hivyo. Suala la nani atakuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto 2027 pia limekuwa nyeti. Baadhi ya viongozi wa ODM tayari wamemuunga mkono Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya kwa wadhifa huo. Hilo limezua ushindani na washirika wa Naibu Rais Kithure Kindiki. ODM inataka ushirikiano huo utoe nafasi ya chama kushiriki katika maamuzi muhimu kuhusu uchaguzi wa 2027. Chama hicho pia kinataka kuwe na mpango wa pamoja wa kuelekea uchaguzi wa 2027. Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohammed alisema mkutano huo utatoa mwelekeo kuhusu uchaguzi ujao. "Kutakuwa na maamuzi mazito yatakayotoa mwelekeo wa kisiasa. Viongozi watatoa mwongozo wa kuelekea 2027," alisema. Mpango huo unatarajiwa kuangazia mikakati ya kampeni, ushirikiano wa vyama na ujumbe wa serikali kwa wapigakura. ODM pia inataka kushiriki katika mjadala kuhusu Ruwaza mpya ya Rais Ruto ya 2060. Rais anatarajiwa kuzindua mpango huo Agosti 12, siku moja baada ya kumalizika kwa mkutano wa Naivasha. Mkutano huo pia unafanyika wakati ODM na UDA zinakabiliwa na ushindani wa kisiasa katika maeneo mbalimbali. Mabadiliko ya uaminifu wa kisiasa, hasa Mlima Kenya, yameongeza presha kwa Rais Ruto. UDA imepoteza baadhi ya washirika wake wakuu, wakiwemo magavana Irungu Kang'ata wa Murang'a na Kiarie Badilisha wa Nyandarua pamoja na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro. Wakati huo huo, vuguvugu la Linda Mwananchi linalohusishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna linaendelea kupanua mbawa zake. ODM ina wasiwasi kuwa vuguvugu hilo linaweza kupunguza nguvu zake katika baadhi ya ngome zake za jadi kuelekea uchaguzi wa 2027.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 08 Aug 2026 02:55:59
Wimbi jipya la mashambulizi ya Al-Shabaab lafanya wakuu wa usalama kujikuna vichwa
KAUNTI za Mandera, Wajir na Garissa zilishuhudia ongezeko la mashambulizi ya kigaidi mwezi Julai, hali ambayo imewalazimu maafisa wa usalama kutafuta mikakati mipya ya kukabiliana na tishio hilo. Mandera iliongoza kwa kuripoti visa tisa, ikifuatiwa na Garissa ikiwa na visa vinne na Wajir viwili, kwa mujibu wa ripoti ya kijasusi iliyosambazwa kwa maafisa wa usalama katika eneo hilo. Shambulio la hivi majuzi lilitokea Alhamisi usiku ambapo watu 10 walinusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kukanyaga kilipuzi katika barabara ya Takaba-Wargadud-Elwak, Mandera. Tukio hilo lilitokea karibu na kijiji cha Odole saa 12 jioni. Walionusurika walikimbizwa katika Hospitali Ndogo ya Elwak baada ya kujeruhiwa. Mmoja wa manusura alisema walikuwa wakijadili masuala ya siasa za Mandera wakati mlipuko ulipotokea. "Ndani ya sekunde chache kulikuwa kimya. Niligundua damu ikitiririka usoni. Nilikuwa nimekatwa vibaya usoni," alisema. Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mandera Kusini, Tobias Otunga alithibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi umeanzishwa. Afisa mmoja mkuu wa usalama alisema kumekuwa na ongezeko la watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa Al-Shabaab kuingia katika jamii za eneo hilo. "Ujasusi wetu umeonyesha kiwango kikubwa cha wapiganaji hao kupenyeza katika jamii zetu. Hili bado ni tishio kubwa kwa usalama wetu," alisema afisa huyo. Ripoti za kijasusi za Julai 31 zilionyesha kuwa wafugaji wanaoishi karibu na mpaka wa Kenya na Somalia waliona watu waliokuwa wamejihami kwa silaha nzito. Wafugaji hao waliwaambia maafisa wa usalama kuwa wapiganaji hao walikuwa wameanzisha kambi za muda karibu na mpaka na kuwaonya wakazi wasikaribie maeneo hayo. Mnamo Julai 28, washukiwa wa Al-Shabaab waliwavizia maafisa wa usalama waliokuwa katika doria eneo la Quraqura-Wante, Mandera, na kuwaua maafisa watano. Wanne kati ya waliouawa walitoka Kikosi Maalumu cha Operesheni huku mwingine akiwa polisi wa akiba. Kilipuzi kingine kilicholenga kikosi cha maafisa waliokuwa wakija kutoa msaada kililipuka na kuharibu gari la polisi. Shirika la Armed Conflict Location and Event Data (ACLED) limesema ongezeko hilo ni sehemu ya wimbi pana la mashambulizi ya Al-Shabaab katika kaunti za Kaskazini Mashariki na Lamu. ACLED ilirekodi visa 25 vikiwemo vilipuzi viwili vilivyodhibitiwa katika Mandera, Garissa, Wajir na Lamu katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Shirika hilo limesema baadhi ya wapiganaji hao wanakimbilia upande wa Kenya kutokana na operesheni kali za kijeshi nchini Somalia. Maafisa wa usalama pia wamehusisha ongezeko hilo na mpaka usio na ulinzi wa kutosha, uajiri wa vijana katika makundi ya kigaidi na mapigano yanayoendelea upande wa Somalia. MCA wa Garissa Hajir Dahiye ameitaka serikali kupitia upya sera yake kuhusu Jubaland, akisema usalama wa Garissa hauwezi kutenganishwa na hali ya usalama katika eneo hilo la Somalia. Mnamo Julai 26, washukiwa wa Al-Shabaab walivamia kijiji cha Abakaile, Dadaab, na kuharibu mnara wa mawasiliano. Hakuna aliyejeruhiwa katika shambulio hilo. Julai 17, washukiwa hao walifanya mashambulizi yaliyofuatana katika miji ya Fino na Arabia, Mandera, na kusababisha hofu miongoni mwa wakazi. Barabara ya Elwak-Lafey-Mandera imekuwa imefungwa kwa umma tangu 2015 kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara na milipuko ya vilipuzi. Maafisa wa usalama pia wameonya kuhusu ushirikiano wa baadhi ya wenyeji na wanamgambo hao kwa kuwapa taarifa kuhusu mienendo ya maafisa wa usalama na vituo vya polisi. Mkazi wa Wajir Hassan Abdullahi alisema ukosefu wa ajira na ujinga miongoni mwa vijana unawafanya kuwa rahisi kuajiriwa na makundi ya kigaidi. "Tunahitaji mpango wa kuwafikia wananchi kutoka mashinani hadi kitaifa ili kuwaelimisha vijana kuhusu hatari za ugaidi," alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 08 Aug 2026 01:55:24
Lojini za bei nafuu Eldoret zageuka 'mitego ya kifo' baada ya wanawake wawili kuuawa
WANAHARAKATI wa haki za binadamu na wanaotetea wafanyabiashara wa ngono wameonya kuhusu ongezeko la mauaji ya wanawake Eldoret baada ya wanawake wawili kuuawa katika visa viwili tofauti ndani ya siku tano. Visa hivyo vimeibua wasiwasi kuhusu usalama katika nyumba za kulala ambazo wakazi wanasema zimegeuka kuwa maeneo hatari kwa uhalifu. Kisa cha hivi majuzi kilitokea Alhamisi asubuhi katika mtaa wa Kipkaren ambapo mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 26 ulipatikana umefungwa kwenye gunia na kutupwa katika nyumba ya kupanga baada ya waliokuwa wakiishi humo kutoroka. Siku chache kabla ya hapo, mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 38, aliyetambuliwa na wenzake kwa jina la Zeddy, ulipatikana katika nyumba ya gesti eneo la Juakali, kando ya barabara kuu ya Eldoret-Webuye. Mauaji hayo yameongeza hofu miongoni mwa wanawake wanaofanya biashara ya ngono, huku mashirika ya haki yakisema yanaweza kuwa sehemu ya mtindo unaoibuka wa mauaji yanayowalenga wanawake walio katika mazingira hatari. Wakazi wanasema baadhi ya nyumba hizo za kulala wageni hazina rejista za wageni, kamera za usalama wala mifumo madhubuti ya kudhibiti wanaoingia na kutoka. Kiongozi wa Nyumba Kumi eneo hilo, Solomon Musumi, alisema Zeddy alikuwa akiishi katika mojawapo ya vyumba hivyo. Alisema Jumatatu usiku alipokea mwanaume aliyedhaniwa kuwa mteja, kabla ya wanawake waliokuwa katika vyumba vya jirani kugundua mwili wake asubuhi iliyofuata. "Eneo hili haliwezi kuendelea kuwa maficho ya wauaji. Nyumba hizi hazina rejista za wageni wala kamera za usalama, na hivyo kuwa mitego ya kifo," alisema Musumi. Polisi wamethibitisha wameanzisha uchunguzi kuhusu visa hivyo. Kamanda wa Polisi kaunti ndogo ya Kapseret Zaphaniah Kamren alisema washukiwa wawili wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Kipkaren. "Tunaahidi umma kuwa hatutakoma hadi waliohusika na vitendo hivi vya kinyama wakabiliwe na sheria," alisema. Kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi wa Turbo Patrick Wekesa alisema uchunguzi kuhusu kifo cha Zeddy unaendelea.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 08 Aug 2026 00:55:30
DCI imefichua kuwa maafisa walilipwa kumuuwa Dkt Mutiso
WAPELELEZI wametaja Konstebo wa Polisi Elijah Kibelion Kimoi kuwa ndiye aliyempiga risasi na kumuua Daktari Victoria Mutiso katika shambulizi la kikatili lililotokea wiki iliyopita. Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) ilisema Ijumaa kuwa Kimoi, ambaye tayari amekamatwa, alitumia bastola ya polisi kumuua Dkt Mutiso. DCI pia ilimtaja raia Daniel Mwangi Njoroge kuwa mmoja wa waliopanga mauaji hayo. Kulingana na DCI, Njoroge aliajiriwa na mwanasiasa Rose Mbithe Mulwa na mwanawe Christopher Mulwa kwa lengo la kumuua Dkt Mutiso. Inadaiwa mauaji hayo yalitokana na mzozo wa muda mrefu wa kifamilia kuhusu ardhi ya ukubwa wa ekari 20 huko Mlolongo, Machakos. Bi Mulwa amekuwa akizozania ardhi hiyo na aliyekuwa mumewe, Dkt David Musyimi Ndetei, pamoja na mkewe Dkt Mutiso tangu 2001. Mkuu wa DCI Mohamed Amin alisema Njoroge alikodi magari mawili aina ya Toyota Prado kutekeleza mauaji hayo. Alisema Njoroge pia alishirikiana na mhudumu wa bodaboda Kelvin Ngugi Kinuthia, ambaye anadaiwa kumsafirisha Kimoi hadi eneo la tukio na baadaye kumtorosha. Dkt Mutiso alikuwa akisafiri katika teksi ya Uber iliyokuwa ikiendeshwa na Victor Job Chunguli mnamo Julai 29. Walipofika eneo la Mawensi, Upper Hill, Nairobi, Toyota Prado nyeusi ilizuia teksi hiyo.Pikipiki pia ilisimama karibu nao. Mtu aliyekuwa ameketi kiti cha nyuma cha pikipiki alifyatua risasi kadhaa kuelekea Dkt Mutiso kabla ya pikipiki na Prado kutoroka. Bw Chunguli alimpeleka Dkt Mutiso katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, lakini akatangazwa kuwa amefariki alipowasili. Bw Amin alisema baada ya kuwahoji Njoroge na Kinuthia, wawili hao waliwapeleka wapelelezi kwa maafisa watatu wa polisi. Walitajwa kuwa Inspekta Kenneth Kipkemboi Sang, Konstebo Elijah Kibelion Kimoi na Konstebo Collins Kiplangat Bett. Kimoi amekamatwa huku Sang na Bett wakitoroka na wanaendelea kusakwa na polisi . "Kushiriki kwa maafisa hawa ni usaliti mkubwa kwa sare ya polisi na imani ambayo umma umeweka kwao. Lazima wachukuliwe hatua," alisema Bw Amin. Bw Amin pia alisema bastola iliyotumiwa kumuua Dkt Mutiso ilikuwa ya polisi na ilikuwa imewekwa katika kituo kidogo cha polisi cha Nderi, chini ya Kituo cha Polisi cha Kikuyu. Wapelelezi walipokagua sanduku la kuhifadhia silaha katika kituo hicho, walipata bastola aina ya Mini Jericho yenye nambari KP47302127 pamoja na magazini iliyokuwa na risasi 12 za milimita tisa. Ukaguzi wa rejista ya utoaji wa silaha ulionyesha kuwa bastola hiyo ilikuwa imetolewa kwa Inspekta Sang. Silaha hiyo ilipelekwa katika maabara ya uchunguzi wa kisayansi ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa uchunguzi wa risasi. Kulingana na DCI, uchunguzi ulithibitisha kuwa bastola hiyo ndiyo iliyotumiwa katika kumuua Dkt Mutiso. Maganda ya risasi yaliyopatikana eneo la tukio na kichwa cha risasi kilichopatikana mwilini mwa marehemu wakati wa uchunguzi wa mwili vililingana na risasi kutoka kwa bastola hiyo. Bastola hiyo pamoja na pikipiki ya Kinuthia zimechukuliwa na polisi kama ushahidi. Uchunguzi wa mauaji hayo ulihusisha pia kuangalia picha za kamera za usalama, ushahidi wa kisayansi na taarifa nyingine za kijasusi. DCI ilisema ushahidi uliopatikana unaonyesha kuwa baadhi ya washukiwa wa mauaji ya Dkt Mutiso huenda pia walihusika katika mauaji ya wakili Kyalo Mbobu mnamo Septemba 9, 2025. Mbobu alipigwa risasi na mtu aliyekuwa nyuma ya pikipiki akiendesha gari kuelekea nyumbani kando ya Barabara ya Magadi. Mauaji hayo yalifanana na yaliyompata Dkt Mutiso kwa kuwa mshambuliaji alitumia pikipiki. Bw Amin pia alidai kuwa matamshi ya Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kuhusu uchunguzi huo huenda yalifikia Sang na Bett na kuwafanya kutoroka. Alimtaka Bw Gachagua kuwasilisha kwa DCI taarifa yoyote aliyo nayo ambayo inaweza kusaidia uchunguzi wa mauaji hayo. Bw Gachagua alikuwa amedai kuwa maafisa wawili wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Kikuyu walihusika katika mauaji ya Dkt Mutiso. Alisema madai yake yalitokana na "taarifa za kuaminika". "Maafisa hawa wawili katika Kituo cha Polisi cha Kikuyu ndio waliomuua wakili Kyalo Mbobu na pia Dkt Victoria Mutiso," Bw Gachagua alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Fri, 07 Aug 2026 23:55:58
Umoja: Kalonzo ateua washirika wa Gachagua katika uongozi wa Wiper
KIONGOZI wa Wiper Patriotic Front , Kalonzo Musyoka Ijumaa alitangaza mabadiliko katika uongozi wa chama hicho kwa kuwateua washirika wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, huku akilenga kuonyesha umoja wa upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Bw Musyoka alimteua aliyekuwa waziri, Jamleck Kamau kuwa mwenyekiti wa chama, Mbunge wa Nyali, Mohamed Ali kuwa naibu kiongozi wa chama, na wakili wa masuala ya Katiba Ndegwa Njiru kuwa msemaji wa chama. Uteuzi huo ulianza kutekelezwa mara moja na unaashiria upanuzi mkubwa wa uongozi wa Wiper vyama vya upinzani vinapoendelea na mashauriano kuhusu muungano w kukabiliana na Rais William Ruto mwaka 2027. Bw Kamau, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Kigumo, amewahi kuhusishwa kisiasa na Bw Gachagua, huku Bw Njiru akiwa mmoja wa mawakili mashuhuri waliowahi kumtetea kiongozi huyo wa DCP. Bw Musyoka alisema uteuzi huo ulitokana na jukumu alilopewa na wajumbe wa chama wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe la Oktoba 10 mwaka jana. "Jukumu la kwanza nililopewa na wajumbe lilikuwa kutafuta urais wa Jamhuri ya Kenya mnamo Agosti 2027. Jukumu la pili lilikuwa kupanua na kujenga uongozi wa chama hiki hadi kiwe sura ya Kenya," alisema. Alisema mabadiliko hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha Wiper pamoja na muungano mpana wa upinzani kuelekea uchaguzi wa 2027. Bw Musyoka alisema mashauriano yanaendelea kuunganisha vyama vinavyopinga utawala wa Rais Ruto chini ya mwavuli mmoja wa kisiasa. "Huu si uteuzi wa kujipendekeza, bali ni uteuzi wa imani. Kila mmoja wao anafaa kikamilifu katika chama ambacho ajenda yake pekee ni 'Komboa Kenya'," alisema. Kando na mabadiliko hayo ya uongozi, Bw Musyoka alisema hataruhusu tofauti kati ya viongozi wa upinzani kuvuruga juhudi za kuunda muungano mmoja dhidi ya Rais Ruto. Alisema viongozi wa upinzani wanaendelea na mashauriano ya kuleta pamoja Wakenya na akaonya kuwa mgawanyiko utawanufaisha viongozi wa Kenya Kwanza. "Tunapoendelea na kazi hii, mashauriano yanaendelea ili kuleta upinzani chini ya mwavuli mmoja wa kuaminika. Tumekubaliana kuwa mgawanyiko ndiyo mkakati pekee wa utawala huu," alisema. Bw Musyoka pia aliwataka Wakenya kutotafsiri tofauti zinazojitokeza kati ya viongozi wa upinzani kama ishara kwamba mchakato wa kuunda muungano umevunjika. "Hata mkiona tofauti kati ya viongozi wa vyama ndani ya muungano, tafadhali msizichukulie kwa uzito sana. Tumeungana kwa sababu tukigawanya upinzani, William Ruto atapata muhula wa pili," alisema. Alisema mashauriano yataendelea hadi vyama na viongozi wote wanaopinga serikali waungane. "Mashauriano hayo yanaendelea na hayatasitishwa hadi kila chama na kila kiongozi anayepinga serikali awe chini ya paa moja, tayari kuunda serikali moja inayosubiri kuchukua uongozi," alisema.
read moreRight Column Content