T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 01 Oct 2026 06:55:05

Kaunti zilipa Sh8.3 bilioni kama mishahara bila kufuata kanuni

SERIKALI za kaunti zililipa Sh8.3 bilioni kama mishahara kama pesa taslimu badala ya kutumia mfumo rasmi wa kidijitali, hatua ambayo imeibua hofu kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma. Ripoti mpya ya Mdhibiti wa Bajeti (COB) Margaret Nyakang'o imeonyesha kuwa kaunti ziliendelea kutumia vocha kulipa baadhi ya wafanyakazi, licha ya kuwepo kwa mfumo wa kulipa wa HRIS uliowekwa ili kudhibiti na kuzuia wizi katika malipo ya mishahara. Kaunti zilizoongoza kwa ukiukaji huo ni Nakuru, Wajir, Nairobi, Siaya na Mandera, zikifuatwa na Meru, Elgeyo Marakwet, Kitui, Busia na Lamu. Ripoti hiyo inayohusu mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2026, inaonyesha kuwa malipo ya kawaida ya kutoa pesa taslimu, yalitumika zaidi kuwalipa vibarua, marupurupu ya ziada kwa maafisa wa usalama, wafanyakazi ambao hawakuwa wameingizwa kwenye HRIS na michango ya pensheni. Dkt Nyakang'o alisema mfumo huo unaweka fedha za umma katika hatari ya kutumiwa vibaya na unaweza kuruhusu kuwepo kwa wafanyakazi hewa. "Malipo kwa njia ya kawaida yanaweza kusababisha pesa kupotea. Kaunti ambazo zinatumia njia hii sana ni Nakuru, Wajir, Nairobi, Siaya na Mandera," akasema Dkt Nyakang'o. Kaunti ya Nakuru iliongoza kwa kutumia Sh1.86 bilioni kupitia mfumo wa malipo ya kawaida, kiasi kilichowakilisha asilimia 21.8 ya gharama ya mishahara. Fedha hizo zilijumuisha mishahara ya wafanyakazi 18 ambao hawakuwa kwenye HRIS na vibarua 596. Wajir ilitumia Sh755.35 milioni, huku Nairobi ikitumia Sh496.07 milioni. Siaya ilitumia Sh401.65 milioni, huku Mandera ikitumia Sh362.41 milioni. Kaunti nyingine zilizotumia kiasi kikubwa ni Meru (Sh356.61 milioni), Elgeyo Marakwet (Sh264.11 milioni), Kitui (Sh259.36 milioni), Lamu (Sh236.78 milioni), Garissa (Sh231.53 milioni), Busia (Sh230.93 milioni), Kiambu (Sh207.73 milioni), Kericho (Sh202.3 milioni), Kisii (Sh210.80 milioni), Mombasa (Sh241.26 milioni), Nandi (Sh184.18 milioni), Laikipia (Sh162.57 milioni) na Tharaka Nithi (Sh157.16 milioni). Turkana (Sh141.30 milioni), Machakos (Sh131.26 milioni), Tana River (Sh132.41 milioni), Murang'a (Sh130.09 milioni) Bungoma (Sh80.55 milioni), Kajiado (Sh105.21 milioni), Taita Taveta (Sh108.25 milioni), Baringo (Sh34.87 milioni), Nyamira ((Sh70.6 milioni), Homa Bay (Sh89.73 milioni), Marsabit (Sh79.22 milioni). Nyingine ni Vihiga (Sh59.92 milioni), Uasin Gishu, (Sh42.99 milioni), Makueni (Sh35.85 milioni), Kirinyaga (Sh98.57 milioni), Samburu, Embu (Sh49 milioni), Bomet (Sh19.17 milioni), Pokot Magharibi (Sh31.68 milioni),, Kwale (Sh19 milioni), Nyeri (Sh13.53 milioni), Kakamega (Sh62.7 milioni), Kilifi (Sh31.74 milioni), Isiolo (Sh4.32 milioni) na Kisumu (Sh11.10 milioni) pia ziliripoti malipo ya mishahara nje ya HRIS. Kwa upande mwingine, Narok na Trans Nzoia ni kaunti ambazo hazikutumia njia za kawaida ya wafanyakazi kulipwa kwa kupokezwa fedha. Serikali za kaunti ziliagizwa mnamo Aprili 2024 kuhamishia shughuli zote za malipo ya mishahara kwenye HRIS kufikia Juni 2025. Dkt Nyakang'o alisema sababu zilizotolewa na kaunti ni kuchelewa kutolewa kwa nambari za wafanyakazi, kutokamilika kwa usajili kwenye HRIS, kuwaajiri vibarua, matatizo ya mtandao na ukosefu wa barua za ajira kwa baadhi ya wafanyakazi. Mifumo ya malipo ya kutoa pesa moja kwa moja yanahitaji udhibiti mkali kwa sababu huathiri uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 56 minutes ago

Wakenya walivyotekeleza ulaghai wa Sh25bn pesa za Amerika

MKENYA aliyepata kadi ya kuishi Amerika, Green Card, kupitia bahati nasibu mnamo 2024 anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika ulaghai wa Sh25.8 bilioni uliolenga fedha za serikali za kuwasaidia wanafunzi kugharimia elimu ya juu. Francis Smith Mogambi anadaiwa kushirikiana na washirika wake nchini Kenya kati ya Novemba 2025 na Mei 2026 kuiba taarifa za kibinafsi za raia wa Amerika na kuzitumia kuwaandikisha katika vyuo vya mtandaoni bila wao kujua. Washukiwa walitumia taarifa hizo kuwasilisha maombi ya mikopo na misaada ya elimu kupitia mpango wa serikali wa FAFSA. Baada ya fedha kutolewa, walidaiwa kuzichukua kupitia akaunti za benki na hundi bandia. Mogambi anadaiwa kupokea hundi zilizoandikwa kwa majina ya wanafunzi hewa, kuzitia saini na kuweka fedha hizo katika akaunti zake. Inadaiwa alisalia na asilimia 30 na kisha kutuma nyingine kwa washirika wake Kenya. Polisi walianza kumchunguza baada ya shahidi kusema alijaribu kumshawishi kujiunga na ulaghai huo kwa kumwahidi dola 2,000 (Sh259,000) kila wiki. Mnamo Oktoba 19, Mahakama kuu Nebraska ilimfungulia mashtaka 10, yakiwemo ya kuiba fedha za serikali na kutumia utambulisho wa watu wengine. Uchunguzi huo, uliopewa jina la 'Operation Ghostbusters', pia umehusisha washukiwa katika New Jersey na Virginia. Serikali za Kenya na Amerika zinazuia sarafu za kidijitali zenye thamani ya dola 750,000 (Sh97.4 milioni) zinazohusishwa na ulaghai huo. Ushirikiano huo unahusisha asasi za usalama na haki kama DCI, ARA, ODPP, KRA na FRC. Maafisa wa Amerika pia wamejadiliana na Kenya uwezekano wa kuwarejesha washukiwa nchini Amerika kukabili mashtaka. "Hundi hizo zilitolewa kwa majina ya wanafunzi tofauti, lakini zote zilikuwa na sahihi zilizomlipa Mogambi," polisi walisema katika hati ya kiapo.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Usalama wakazwa KCSE ikianza rasmi

MTIHANI wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) wa mwaka huu wa 2026 ulianza rasmi jana kote nchini huku maelfu ya watahiniwa wakianza kufanya mitihani yao katika mazingira ya ulinzi mkali na onyo kali dhidi ya udanganyifu. Mwaka huu, watahiniwa, wasimamizi na maafisa wengine wamepigwa marufuku kuingia katika vyumba vya mitihani wakiwa wamevaa saa za mikononi, zikiwemo saa za kawaida na za kisasa. Watahiniwa wanatarajiwa kutumia saa za ukutani zilizowekwa katika vyumba vya mitihani. Katika Moyale, Marsabit, watahiniwa 220 kutoka shule mbili za mpakani walihamishwa hadi shule nyingine baada ya risasi zilizopotea kutoka mapigano upande wa Ethiopia kulenga shule zao. Watahiniwa wa shule za mseto za Sessi na St Mary walihamishiwa shule za msingi zilizo salama zaidi. Jumla ya watahiniwa 1,443 wanafanya mitihani katika vituo 12 vya eneo hilo huku wanajeshi KDF na maafisa wa usalama wa mipaka wakiongeza doria. Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC), Prof Julius Nyabundi, alisema kufikia Jumatatu asubuhi hakukuwa na taarifa za udanganyifu. Alisema huu ni mtihani wa pili kutoka mwisho kusimamiwa na KNEC kabla ya mabadiliko ya mfumo wa mtaala. Uasin Gishu, watahiniwa 22,593 walianza mtihani katika vituo 246. Maafisa walipiga marufuku saa za mikononi, mavazi yasiyo sare za shule na watu wasioidhinishwa kuingia vyumba vya mitihani. Turkana, zaidi ya watahiniwa 7,000 katika vituo 68 walianza mitihani huku wakuu wa shule wakiomba ulinzi zaidi katika maeneo yanayokumbwa na ujangili. Serikali kuu na ile ya kaunti pia inafuatilia uwezekano wa mafuriko kuathiri usafirishaji wa karatasi za mitihani. Baringo ilisajili watahiniwa 16,549 katika vituo zaidi ya 196, huku Trans Nzoia ikiwa na 28,353 katika vituo 253. Maafisa walisema zoezi lilianza bila matatizo makubwa. Nyeri, watahiniwa wanne wanafanyia mitihani hospitalini kutokana na matatizo ya kiafya. Bomet pia ina watahiniwa watatu hospitalini, wakiwemo wawili wenye ujauzito. Murang'a iliwasajili watahiniwa 32,487, lakini kukazuka wasiwasi kuhusu karibu wanafunzi 600 waliodaiwa kuacha shule tangu walipojiunga na Kidato cha Kwanza. Baadhi ya watahiniwa pia walilalamikia kupewa chakula kidogo kutokana na kuchelewa kwa fedha za serikali. Kisumu ilisajili watahiniwa 25,849 katika shule 246, huku Kisii ikiimarisha usalama katika vituo vyake 45. Katika eneo la Pwani, watahiniwa 63,415 walianza mitihani. Kilifi ilikuwa na 25,617, Mombasa 12,187, Kwale 12,171, Taita Taveta 7,994, Tana River 3,082 na Lamu 2,364. Huko Lamu, mitihani ilianza kwa utulivu hata katika maeneo yenye changamoto za kiusalama ya Msiti wa Boni na Kiunga, mpakani mwa Kenya na Somalia. Kwa ujumla, maafisa wa elimu na usalama walisema maandalizi yalikuwa yamekamilika, huku wakiahidi kuhakikisha mitihani inaendeshwa kwa usalama na bila udanganyifu.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

Sakaja atupa Wilbaro, alenga kujinafasi 2027 kupitia ODM

GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja jana alijiunga rasmi na chama cha ODM akilenga kuimarisha nafasi yake ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu ujao. Bw Sakaja, aliyechaguliwa mnamo 2022 kwa chama tawala cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto, alisema yuko tayari kufanya kampeni za muhula wa pili wa Rais akiwa mwanachama wa ODM. ODM na UDA kwa sasa ziko katika Serikali Jumuishi, huku zikiendelea na mchakato wa kutia saini mkataba wa ushirikiano kabla ya uchaguzi mkuu. Hata hivyo, hafla ya kumpokea Bw Sakaja katika makao makuu ya ODM, Chungwa House, ilizua hisia tofauti. Gavana huyo alisisitiza kuwa amekuwa akitekeleza matakwa ya aliyekuwa kiongozi na mwanzilishi wa ODM, marehemu Raila Odinga. "Nilianza safari hii na Baba (Raila Odinga) nilipotwaa ugavana. Na nimekuwa nikishambuliwa kwa kusimama naye na kuwasaidia wanachama wa ODM kuingia katika Baraza la Mawaziri. Nilifanya hivyo kabla ya kuundwa kwa Serikali Jumuishi na Baba ndiye aliyeniambia niingie ODM," akasema Bw Sakaja. Bw Sakaja alipokelewa na Naibu Kiongozi wa ODM aliye pia Gavana wa Kisii, Simba Arati, Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama hicho na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Mbunge wa Suna Mashariki na Mkurugenzi wa Uchaguzi ODM Junet Mohammed, pamoja na Waziri wa Madini Hassan Joho. Gavana huyo alisema anajiunga na chama hicho kwa unyenyekevu, akiwa tayari kuongozwa na ngazi zake za juu na kuanza kampeni za kuvumisha umaarufu wake. "Ninaamini kuwa hatua inayofuata ya siasa zetu haipaswi kupimwa tu kwa uchaguzi tunaoshinda, bali pia kwa maisha tunayobadilisha. Vijana hawapaswi tena kuwa watazamaji katika maamuzi yanayoathiri mustakabali wao bali anapaswa kushiriki, kuwa viongozi na kuwa kiini cha Kenya tunayoijenga," akasema. Bw Sakaja alikumbushwa kuwa Mwenyekiti wa ODM utanzu wa Nairobi ambaye ni Mbunge wa Makadara George Aladwa pia anawania tiketi ya chama hicho kugombea ugavana wa Nairobi. "Tuna mwenyekiti wetu wa chama Nairobi, George Aladwa, ambaye amekuwa akisimama na chama kwa muda mrefu na pia anawania kiti cha ugavana kupitia ODM. Sasa tunaye Gavana Sakaja," akasema Bi Wanga, akiongeza kuwa kila anayetaka kujiunga na chama hicho anakaribishwa. Jana, Bw Aladwa alisema yuko imara ndani ya ODM na kuwataka wafuasi wake wawe watulivu akisisitiza nia yake ya ugavana bado upo hai. "Wafuasi wangu nawaelewa lakini tusipoteze muda kutokana na uvumi unaoendelea. Safari ya kuimarisha Nairobi itaamuliwa na raia kwa usawa na haki na demokrasia. Tuendelee kudumisha amani," akasema Bw Aladwa. Wakati wa kumpokea Bw Sakaja, Bi Wanga alitangaza kuwa uteuzi wa wagombea utafanywa kwa uwazi na bila ubaguzi. Bw Arati pia alifichua kuwa Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri ni miongoni mwa wanaotaka kujiunga na ODM ili kuwania kiti hicho hicho. "Mwenyekiti wetu wa Nairobi, Aladwa, pia anawania ugavana. Atachuana na Gavana Sakaja kuwania tiketi ya chama. Karauri akiamua kujiunga nasi, tutampokea kama tulivyompokea Sakaja. Tunachowaahidi wanachama wetu ni uteuzi huru, wa haki na uwazi," akasema Bw Arati. Kutokana na kutokuwepo kwa Bw Aladwa katika hafla hiyo, Bw Sakaja alisema atamtafuta binafsi ili kuunganisha kura za ODM Nairobi na kuhakikisha chama hicho kinashinda viti vingi. Baadhi ya madiwani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi waliohudhuria hafla hiyo walikuwa wamemuidhinisha Bw Aladwa awali kuwania uongozi wa kaunti hiyo. Polisi nao walilazimika kutumia vitoza machozi kutawanya kundi la wanachama waliokuwa wakijaribu kuvuruga hafla hiyo. Baadhi yao walisikika wakipiga kelele, "Kama hakuna Aladwa, hakuna ODM." Mbali na Gavana Sakaja na Aladwa, ODM inakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea wa makundi mengine ambao wametangaza nia ya kuwania kiti hicho. Wao ni Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino (chama cha Mwananchi), Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya (DCP) na Askofu Margaret Wanjiru . Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua pia ametangaza kuwa chama chake cha DCP kinataka kutawala siasa za Nairobi na inaaminika anamuunga mkono Bw Gakuya.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Joho, Mvurya wapambania kudhibiti Kwale

USHINDANI wa kuwania ugavana Kwale kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 unazidi kuonekana kama mchuano wa kisiasa kati ya Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Hassan Joho wa ODM, na mwenzake wa Michezo, Bw Salim Mvurya wa UDA. Bw Mvurya anaongoza juhudi za kuhakikisha kaunti hiyo inasalia chini ya UDA huku Bw Joho akitangaza nia ya ODM kuendeleza ushawishi wake katika eneo la Pwani. "Ni lazima tukifanye ODM kuwa imara tena. Hatuwezi kuruhusu vyama vingine kuchukua maeneo yaliyokuwa ya ODM," alisema Bw Joho wakati wa mkutano wa hivi majuzi wa kisiasa Kwale. Gavana Fatuma Achani, ambaye anatumikia muhula wake wa kwanza, anakabiliwa na ushindani mkali baada ya waliokuwa wakimezea mate tikiti ya ODM, Profesa Hamadi Boga na mfanyabiashara Lungazi Mangale, kuamua kuungana ili kumuunga mkono mmoja wao. Wawili hao, walioibuka wa pili na wa tatu mtawalia katika uchaguzi wa 2022, wamehimizwa na viongozi wa mashinani kudumisha ushirikiano wao hadi uchaguzi utakapofanyika. Viongozi wa ODM wameonya kuwa kuvunjika kwa muungano huo kunaweza kudhoofisha azma ya chama hicho ya kutwaa kiti cha ugavana. Licha ya mikakati hiyo inayoendelea, Waziri Mvurya amewataka wapinzani wa Bi Achani kujiandaa kwa mchuano mkali unaofanana na uchaguzi mdogo wa Msambweni wa mwaka 2020. Uchaguzi huo ulikuwa kipimo kikubwa cha ushawishi wa kisiasa kati yake na Waziri Joho, ambao wakati huo walikuwa magavana wa Kwale na Mombasa mtawalia. Bw Joho aliunga mkono mgombeaji wa ODM Omar Boga, ambaye ni kaka mdogo wa Profesa Boga, huku Mvurya, aliyekuwa mwanachama wa ODM kabla ya kuhamia Jubilee, akiunga mkono mgombeaji huru Feisal Bader. Bw Bader alikuwa akiungwa mkono na wanasiasa waliokuwa washirika wa Naibu Rais wa wakati huo, William Ruto. Hatimaye, Bw Bader alimshinda Omar kwa kupata kura 15,251 dhidi ya 10,444 za mpinzani wake, na hivyo kumpa Mvurya ushindi mkubwa wa kisiasa. "Si siri kwamba rais wetu ni William Samoei Ruto, gavana wetu ni Fatuma Mohamed Achani, na mbunge wa eneo hili ni Feisal Bader. Walimdharau Feisal katika uchaguzi mdogo wa 2020 na wakaja hapa kwa nguvu zao zote, lakini tunawaambia kuwa wanaweza kupanga dhidi ya gavana, lakini atasalia kuwa gavana wa Kwale," alisema Bw Mvurya katika mkutano wa kisiasa Msambweni. Profesa Boga, ambaye aliwahi kuhudumu kama Katibu katika Wizara ya Kilimo wakati wa utawala wa Jubilee, aligombea ugavana mwaka wa 2022 kupitia tiketi ya ODM na kupata kura 53,972, na kushika nafasi ya pili nyuma ya Bi Achani, aliyeibuka mshindi kwa kura 59,674. Bw Mangale, aliyewahi kufanya kazi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Kenya (KPA) kama mhandisi, aligombea kupitia chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kabla ya kujiunga na ODM baada ya chama hicho kusambaratika. Hata hivyo, Gavana Achani ametetea rekodi yake ya uongozi akisema anatarajia kuchaguliwa tena kutokana na miradi ya maendeleo ambayo serikali yake imeanzisha. "Viongozi wanapaswa kutathminiwa na kuchaguliwa tena kwa kuzingatia miradi yao ya maendeleo. Acheni siasa za chuki na uhasama. Kuna baadhi ya watu ambao hawana sera; wanachozungumzia kila mara ni Achani. Nitachaguliwa tena ili kuhudumu mihula yangu miwili," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Majonzi walimu kufa wakielekea harusini

SAFARI ya walimu kutoka Kaunti ndogo ya Matete, Kaunti ya Kakamega, kuenda kusherehekea harusi ya mtoto wa mwenzao iligeuka msiba baada ya watu sita kufariki katika ajali ya barabarani. Ajali hiyo ilitokea usiku wa manane wikendi karibu na Burnt Forest, kwenye barabara kuu ya Eldoret-Nakuru. Miongoni mwa waliofariki ni Janet Andabwa, kaimu mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Chavere, ambaye kifo chake kimeiacha familia yake katika majonzi tele. Mumewe, Geoffrey Besele, ambaye pia ni mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Tande, alisema mkewe aliondoka nyumbani akiwa na furaha baada ya kukamilisha kusimamia na kutathmini mitihani ya KJSEA. Alisema Bi Andabwa aliagana naye na kuanza safari yake kuelekea Nairobi mnamo saa mbili usiku, baada ya kuchukuliwa na walimu wenzake katika kituo cha kibiashara cha Kaburengu. Hata hivyo, furaha hiyo ilikatizwa alfajiri baada ya kupokea simu iliyomfahamisha kuhusu ajali hiyo. "Nilipokea simu ya kuhuzunisha saa kumi alfajiri kwamba alikuwa amepata ajali huko Burnt Forest," akasema Bw Besele huku akishindwa kuzuia machozi katika Kituo cha Polisi cha Tarakwa, ambako mabaki ya magari yaliyohusika kwenye ajali yalikuwa yamepelekwa. Mbali na Bi Andabwa, waliofariki ni mwalimu mwengine kutoka Shule ya St Mikasa Girls, mwalimu wa Chavere, binti wa mwalimu mmoja wa eneo hilo na mfanyabiashara maarufu katika soko la Matete. Walimu na familia zao wameathirika pakubwa kutokana na mkasa huo. Watu wengine watano waliojeruhiwa wanaendelea kupokea matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH), Eldoret. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Wilberforce Sichirani, alisema ajali hiyo ilihusisha lori kubwa lililokuwa likisafirisha saruji na kokoto kuelekea Eldoret. Alisema lori hilo liligongana na gari la abiria la North Rift Shuttle kabla ya kugonga magari mengine matatu. Abiria waliokuwa ndani ya gari aina ya Probox na gari jingine la uchukuzi wa umma pia waliathirika katika ajali hiyo. Mkasa huo umeibua tena wasiwasi kuhusu usalama katika barabara kuu ya Eldoret-Nakuru, miezi michache tu baada ya ajali nyingine katika eneo hatari la Mlima Punda kuua watu saba, wakiwemo wanafunzi wawili waliokuwa wakisafiri kuelekea nyumbani kwa likizo. Mkazi wa Koriomat, Ben Lelei, alisema eneo hilo limekuwa hatari kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva wa malori yanayosafirisha mizigo. Alilalamikia pia watu waliotumia vurugu zilizotokana na ajali hiyo kuwaibia abiria badala ya kuwasaidia manusura. "Ni jambo la kusikitisha kwamba huku baadhi yetu tukijitahidi kuwaokoa manusura, wengine walikuwa wakiiba mali za abiria waliofariki na walionurika," akasema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Winnie njiapanda kisiasa uchaguzi wa 2027 ukijongea

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Winnie Odinga, anakabiliwa na utata kuhusu upande wa kisiasa wa kuegemea anapotafuta kiti cha useneta Nairobi katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Winnie ameshindwa kuweka wazi iwapo anaunga mkono uongozi wa ODM au vuguvugu la Linda Mwananchi. Kutokuwepo kwake katika mikutano miwili muhimu Ijumaa na Jumamosi Nairobi kumezidisha maswali kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa. Winnie hakuhudhuria uzinduzi wa makao makuu ya Linda Mwananchi jijini Nairobi wala mkutano wa ODM katika uwanja wa Jacaranda ulioongozwa na viongozi wakuu wa chama hicho. Katika kuwatambulisha viongozi wa Linda Mwananchi uliofanyika Lavington Ijumaa, kiti cha mbele kilikuwa kimetengewa Winnie, lakini hakufika. Hali hiyo inatatanisha zaidi kwa sababu Oktoba 15, wakati wa kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo cha baba yake Raila Odinga, Winnie alitangaza kuwania useneta Nairobi akisema anataka kufanya hivyo pamoja na vijana. "Najua watu wengi wamekuwa wakiuliza nilipo na ninakoelekea. Leo nataka kuwajibu ili kuondoa uvumi," akasema. "Kwa kuwa Edwin Sifuna anawania wadhifa mwingine, nafasi ya useneta Nairobi iko wazi. Ndiyo maana nimeamua kuwania kiti hicho. Siendi pekee yangu, ninaenda na vijana," akaongeza. Matamshi hayo yalifasiriwa kuwa anaegemea Linda Mwananchi, lakini kutohudhuria uzinduzi wake kumezua maswali zaidi. Hata ndani ya vuguvugu hilo, Winnie anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Seneta Maalum, Crystal Asige, ambaye amekuwa akiandamana na Bw Sifuna katika ziara zake za kisiasa. Pia kuna mvutano kuhusu wagombea wa nyadhifa nyingine Nairobi. Bw Sifuna na viongozi wengine wa Linda Mwananchi wameunga mkono Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kuwania ugavana, huku aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo akilenga kiti cha mwakilishi wa kike Nairobi. Profesa Lumala Masibo anasema Winnie anaweza kuwa na nafasi ya kushinda ikiwa atajihusisha na wapigakura na kuzungumza nao badala ya kuonekana kutokuwa na msimamo. "Ikiwa Winnie atacheza karata zake vizuri ndani ya Linda Mwananchi, anaweza kushinda Nairobi. Lakini ikiwa Babu na Faith watawania, itakuwa vigumu. Winnie, Faith na Babu lazima wakae pamoja na mmoja wao ajiondoe," akasema. Katika ODM, Winnie pia anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Bw Jalangó ambaye ameungwa mkono na kaka yake Raila Junior kuwania useneta. Raila Junior amesema atabadilisha msimamo wake tu iwapo dada yake atapata tiketi ya chama. Uhusiano wa Winnie na viongozi wa sasa wa ODM umekuwa na misukosuko tangu kifo cha baba yake. Alipinga kuondolewa kwa Bw Sifuna kama katibu mkuu wa chama Februari mwaka huu. Katika mkutano wa Kamukunji, eneobunge la Kibra Januari 18, 2026, alikosoa viongozi aliowashutumu kwa kutaka kuchukua usukani wa chama baada ya kifo cha Raila. "Katika safari hii, sisi tulikuwa abiria na Baba alikuwa dereva. Siku moja tuliamka na kushtuka. Dereva alikuwa amefariki. Baadhi ya watu wakasogea mbele, wakashika usukani na kuuvuta pande tofauti," alisema. Winnie pia alizua maswali kuhusu ushirikiano wa ODM na UDA, akisisitiza kuwa maamuzi muhimu yanapaswa kuidhinishwa kwenye Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC). Zaidi ya hayo, alikosolewa na baadhi ya viongozi baada ya kumkashifu Waziri wa Fedha John Mbadi kuhusu namna anavyowahutubia viongozi wa chama akidai alikuwa akiwadharau. Changamoto zake zimeongezwa na tofauti za kifamilia. Winnie alitawazwa mrithi wa kisiasa wa Raila katika hafla ya Oktoba 4, lakini Raila Junior hakuhudhuria akisema hakujua kuhusu hafla hiyo. Kwa sasa, Winnie hajapata uungwaji mkono wa wazi kutoka kwa kiongozi mkuu wa ODM wala Linda Mwananchi. Kutohudhuria mikutano ya hivi karibuni kumeacha maswali kuhusu chama atakachotumia, upande atakaoegemea na uwezo wake wa kuunganisha wafuasi kabla ya uchaguzi wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Rekodi ya maendeleo itampa Ruto Tutam 2027 – Kindiki

NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki anatumia mafanikio ya serikali ya Kenya Kwanza katika sekta mbalimbali kuimarisha uungwaji mkono wa Rais William Ruto, huku akiweka msingi wa kusalia katika wadhifa huo kampeni za uchaguzi za 2027 zikichacha. Katika kipindi cha miaka miwili tangu achukue nafasi ya Rigathi Gachagua, Profesa Kindiki amejitahidi kuonyesha mchango wake katika kuleta udhabiti serikalini akiratibu utekelezaji wa miradi muhimu. Juhudi zake pia zinaonekana kulenga kuimarisha uungwaji mkono wa Rais Ruto katika ukanda wa Mlima Kenya, ambao ni muhimu katika mipango ya Rais kutafuta muhula wa pili. Katika tathmini ya utendaji wa serikali, Profesa Kindiki alitetea rekodi ya utawala huo akisema umepiga hatua kubwa licha ya ukosoaji kutoka kwa wapinzani. "Utawala wa Ruto umefanya vizuri zaidi ya matarajio yaliyowekewa, lakini wakosoaji hawatoi tathmini ya haki kuhusu utendakazi wake. Ukosoaji wao una nia mbaya na hauna ukweli," akasema. Alitaja kilimo kama mojawapo ya sekta ambazo serikali imepiga hatua, akisema wakulima milioni 7.9 wa mimea na wafugaji milioni tatu wamesajiliwa ili kurahisisha mipango na utoaji wa huduma. "Leo tunajua tuna wakulima wangapi, mifugo waliyo nayo, wanakoishi, mazao wanayolima na aina ya mbolea wanayohitaji," akasema. Prof Kindiki alisema bei ya gunia la kilo 50 la mbolea imepungua kutoka Sh7,000 mnamo 2022 hadi Sh2,000. Bei ya mbegu bora za mahindi pia imeshuka kutoka Sh300 hadi Sh150 kwa kilo moja. Aliongeza kuwa wakulima wa kahawa sasa wanapata kati ya Sh130 na Sh150 kwa kilo ya matunda ya kahawa, ikilinganishwa na Sh60 mnamo 2022. Katika sekta ya afya, alisema Wakenya milioni 33.3 wamejisajili kupata bima ya afya inayofadhiliwa na serikali, ikilinganishwa na milioni nane mnamo 2022. Kuhusu ajira, alitaja nafasi milioni 1.1 zilizotokana na mpango wa nyumba za gharama nafuu, nafasi 600,000 za ajira nje ya nchi na ajira 350,000 katika sekta ya kidijitali. "Tumeweza kuwasaidia vijana wengi zaidi kupata ajira na fursa za kujipatia mapato," akasema. Pia alitaja kuunganishwa kwa nyumba milioni 1.5 kwenye umeme, kuimarika kwa akiba ya fedha za kigeni na ujenzi wa uwanja wa Talanta wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000. Profesa Kindiki pia amepata sifa kutoka kwa mawaziri wanaosema amekuwa akiratibu vyema mikutano ya kamati za Baraza la Mawaziri na kuondoa vikwazo vinavyochelewesha miradi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 02 Nov 2026 04:55:43

Walimu kuendelea kufurahia mitandao ya kijamii, TSC yapata pigo

WALIMU chini wataendelea kutoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii bila hofu ya kuadhibiwa baada ya korti kukataa ombi la Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) la kuondoa agizo lililosimamisha utekelezaji wa mwongozo wenye utata kuhusu machapisho yao mtandaoni. Jaji Francis Kyambia alisema barua ya TSC haikufafanua wazi mienendo inayochukuliwa kuwa isiyo ya kitaaluma, hivyo kuwaweka walimu katika hatari ya kuadhibiwa kwa kutoa maoni kuhusu masuala ya umma. "Barua hiyo haifafanui vya kutosha mienendo inayoweza kumfanya mwalimu kuchukuliwa hatua za kinidhamu," akasema jaji huyo. Mgogoro huo unatokana na barua ya Agosti 13, 2026, iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa TSC Evaleen Mitei, iliyowatahadharisha walimu dhidi ya unyanyasaji wa mtandaoni na tabia isiyo ya kitaaluma kwenye mitandao ya kijamii. Mwalimu Fredrick Ochieng aliwasilisha kesi akisema mwongozo huo ulikuwa na lugha tata inayoweza kuingilia uhuru wa walimu kutoa maoni yao kuhusu sera za elimu, utawala na mazingira ya kazi. Pia alilalamikia kutoshirikishwa kwa walimu na wadau wengine kabla ya kutolewa kwa ilani hiyo. TSC ilisema waraka huo haukuanzisha makosa mapya bali uliwakumbusha walimu wajibu wao chini ya sheria na kanuni zilizopo. Ilisema ilichukua hatua hiyo kutokana na kuongezeka kwa matumizi mabaya ya mitandao na kwamba haikulenga kukandamiza uhuru wa kujieleza. Hata hivyo, Jaji Kyambia alisema vikwazo vya uhuru wa kujieleza lazima viwe na msingi wa kisheria na vikidhi masharti ya Katiba. Alisema TSC ilipaswa kushauriana na wadau na kutoa miongozo mahususi badala ya barua ya jumla. Aliongeza kuwa walimu wanaokiuka maadili wanapaswa kushughulikiwa mmoja mmoja chini ya kanuni zilizopo. Agizo la kusimamisha barua hiyo litaendelea kutumika hadi kesi hiyo iamuliwe. Kesi hiyo itatajwa Februari 3, 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 02 Nov 2026 03:55:05

Kalonzo asihi viongozi wa Ukambani walinde ngome yake

KIONGOZI wa chama cha Wiper Patriotic Front (WPF), Kalonzo Musyoka, amewataka washirika wake wa kisiasa kuungana na kulinda ngome yake ya Ukambani dhidi ya juhudi za Rais William Ruto kuongeza ushawishi wake katika eneo hilo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Bw Musyoka, ambaye anapigania tiketi ya urais ya upinzani, amewashutumu viongozi wake kwa kushindwa kukabiliana na washirika wa Rais Ruto wanaofanya kampeni katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni. Akizungumza Jumamosi katika hafla ya ufunguzi wa makazi ya Seneta wa Machakos Agnes Kavindu katika eneo la Mua Hills, Bw Musyoka alisema washirika wake wanapaswa kufanya kazi pamoja badala ya kila mmoja kujipigia debe kivyake. Alitaja kundi la watu watano wanaoendesha kampeni pamoja katika eneo la Machakos, likiongozwa na Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka, na kuwataka viongozi wake kuiga mtindo huo. "Badala ya kuwakabili ilhali wananchi wako nyuma yako, kila mtu anafanya kampeni kivyake. Amkeni na mshirikiane ili mniruhusu kuendeleza kampeni katika maeneo mengine ya nchi," akasema Bw Musyoka. Alisema kutohudhuria kwa wingi kwa washirika wake katika uzinduzi wa sekretarieti ya vuguvugu la Linda Mwananchi jijini Nairobi kumeathiri juhudi zake za kuonyesha kuwa upinzani umeungana kumuunga mkono. Mzozo huo unajiri wakati ambapo Bw Musyoka anakabiliwa na ushindani wa ndani ya Wiper. Machakos, kwa mfano, imekuwa na migawanyiko kati ya Bi Kavindu na Gavana Wavinya Ndeti. Hali imechangiwa na kuingia kwa afisa mkuu wa zamani wa afya wa kaunti hiyo Daniel Yumbya, wakili Musyoka Kala na afisa wa ardhi Nathaniel Nganga katika kinyang'anyiro cha tiketi ya Wiper ya useneta. Kuingia kwa aliyekuwa Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua katika kinyang'anyiro hicho pia kumeongeza ushindani. Mbunge wa Kilome, Thaddeus Nzambia, alisema Machakos imeathiriwa zaidi na juhudi za Rais Ruto kujenga ushawishi Ukambani. Alisema kati ya wabunge wanane wa kaunti hiyo, watano wanaunga mkono Rais, huku wawili pekee wakimuunga mkono Bw Musyoka. Mbunge wa Mavoko Patrick Makau amejitenga na Bw Musyoka na kujiunga na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Bw Nzambia alitaja Makueni pekee kama eneo ambalo viongozi wake bado wako na Bw Musyoka, Kulingana naye, ni mbunge mmoja pekee anayeunga mkono Rais Ruto. Bw Musyoka pia anakabiliwa na ushindani wa tiketi za Wiper katika Kitui, ambako Seneta Enoch Wambua, Mwakilishi wa Wanawake Irene Kasalu na Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu wanawania tiketi ya chama kuwania ugavana. Kuingia kwa aliyekuwa Gavana Charity Ngilu kumeongeza ushindani zaidi japo hatarajii kutumia Wiper. Bw Musyoka amekuwa akiahidi kuwa uteuzi wa Wiper utakuwa huru na wa haki, huku akiwataka washirika wake kutatua tofauti zao na kuimarisha chama.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 02 Nov 2026 02:55:48

Ruto afunika ODM

USHAWISHI unaoendelea kuongezeka wa Rais William Ruto katika ngome za jadi za ODM na uhasama kati ya viongozi wake unaendelea kulemaza umaarufu wa chama hicho. Haya yanafanyika huku ODM ikijiandaa kushiriki mazungumzo na UDA kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027. Wachanganuzi wa siasa wanasema kosa kubwa la ODM lilikuwa kuwaelekeza wafuasi wake kumuunga mkono Rais Ruto kutafuta muhula wa pili kabla ya kukubaliana kuhusu masharti ya ushirikiano wa kisiasa kati ya vyama hivyo. Wanasema ODM ilipaswa kwanza kujadiliana na UDA na kuweka masharti ya ushirikiano katika makubaliano rasmi kabla ya kuwaomba wafuasi wake kumuunga Rais. Baadhi ya viongozi wa chama hicho pia wamekuwa wakitoa ahadi binafsi zinazodhoofisha msimamo wake rasmi katika mazungumzo. Hali hii imezua hofu kuwa ODM inaweza kukosa nafasi ya kupata maslahi yake katika serikali ijayo. Tangu UDA ianze kushirikiana na marehemu Raila Odinga mnamo 2024, Rais Ruto na washirika wake wamekuwa wakijenga miundo ya kisiasa na kuwavutia viongozi wa mashinani katika maeneo yaliyokuwa ngome za ODM. Miradi ya maendeleo ya serikali pia imeongeza ushawishi wa Ruto katika maeneo hayo. Baadhi ya viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM sasa wanamuunga mkono Rais bila masharti, huku wakipinga msimamo rasmi wa chama. Hali hiyo imeonekana zaidi Nyanza, ambako viongozi kadhaa wa ODM wamekuwa wakifuatana na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, katika hafla za umma na kutangaza kumuunga mkono Rais Ruto. Ndani ya ODM sasa kuna mgawanyiko kuhusu iwapo chama hicho kinapaswa kutia saini makubaliano rasmi na UDA au kuendelea kumuunga Rais kwa nia njema ya kisiasa. Nguvu za chama katika mazungumzo pia zinadhoofishwa na viongozi wake wakuu walio katika Baraza la Mawaziri la Ruto, wakiwemo John Mbadi, Opiyo Wandayi, Wycliffe Oparanya, Beatrice Askul na Hassan Joho. Wachanganuzi wanasema mawaziri hao wana maslahi ya kisiasa katika kuhakikisha serikali ya Kenya Kwanza inaendelea kutawala baada ya 2027. Zaidi ya hayo, baadhi ya viongozi wanapigania nafasi ya mgombea mwenza wa Rais Ruto, huku Bw Mbadi akitangaza azma ya kuwania urais mnamo 2032. Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga amewaonya viongozi wa chama hicho dhidi ya migawanyiko inayoweza kudhoofisha msimamo wao katika mazungumzo. "Ninawaomba viongozi wote wa ODM kuzungumza kwa sauti moja, kama watu wamoja, chini ya uongozi mmoja. Hatuwezi kujiruhusu kugawanywa na maslahi binafsi au matamshi ya kiholela yanayodhoofisha nguvu zetu za pamoja za majadiliano," akasema Dkt Oginga akihutubia mkutano wa Jacaranda Jumamosi. "Nguvu zetu zimekuwa katika umoja wetu, na ni lazima tulinde mshikamano huo kwa kila hali," akaongeza. Dkt Oginga pia alikosoa viongozi wanaojihusisha na mipango ya urithi wa kisiasa wa 2032 badala ya kuangazia uchaguzi wa 2027. "Tuangalie vipaumbele vyetu na ninaona viongozi wengi wakipoteza muda muhimu wakijadili uchaguzi wa 2032. Huo ni usumbufu hatuwezi kumudu. Lazima tuzingatie uchaguzi wa 2027," akasema. Hata hivyo, Bw Mbadi aliwaambia wataalamu kutoka Kano kuwa anajiandaa kuwania urais mnamo 2032, akisema hatapoteza nguvu zake kutafuta nafasi ya Naibu Rais ambayo alidokeza haina mamlaka makubwa katika uendeshaji wa nchi. Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohammed, ni miongoni mwa viongozi wanaosisitiza kuwa ushirikiano wa ODM na UDA lazima uandikwe rasmi. "ODM na UDA zitakuwa na serikali ya muungano iliyoandikwa rasmi, huku vyama viwili vikishirikiana kuunda serikali ijayo. Hakuna kitu kinachoitwa nia njema pekee. Hakuna uungwaji mkono usio na masharti. Lazima makubaliano yaandikwe," akasema Bw Mohamed. Gavana wa Kisii Simba Arati pia alisisitiza kuwa ODM haitakubali kuingia serikalini bila masharti. "Watu wanasema hatupaswi kumwekea masharti Rais William Ruto. Sisi kama ODM tunasema lazima kuwe na makubaliano na masharti yatakayowezesha chama kuingia serikalini," akasema. Lakini baadhi ya viongozi, akiwemo Mbunge wa Nyando Jared Okello, wanapinga msimamo huo. Wanasema ODM inapaswa kumuunga mkono Ruto ili eneo hilo linufaike na miradi ya serikali. "Tunahitaji kufungua mioyo yetu na kuwa pamoja na Rais ili viongozi wengine wa upinzani watakapokuja watukute tayari tuko naye. Kwa sasa tunanufaika na miradi iliyoanzishwa na serikali hii, ilhali hatukumchagua," akasema Bw Okello. Alitilia shaka umuhimu wa mikataba ya kisiasa, akitaja kile alichokiita usaliti wa kisiasa uliowahi kutokea kati ya viongozi wa zamani. Mchangunizi wa siasa na mhadhiri wa chuo kikuu Amerika, Profesa David Monda, alisema timu inayoongozwa na Bw Sifuna imechukua nafasi ya kisiasa iliyokuwa ikihusishwa na kundi la Dkt Oginga. "Ni kama wao ndio wana roho ya Raila kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa wakishabikiwa," akasema Profesa Monda.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 01 Nov 2026 15:06:51

Aibu ilioje! Watu wazima kumdhalilisha mtoto anayelilia amani, afya ya akili

FATAKI   SEHEMU kubwa wiki hii midahalo ilizagaa mitandaoni ambapo watu wazima, wanawake kwa wanaume, wengi wao ambao ni wazazi, waliungana kumdhalilisha mtoto.  Endapo wewe ni mraibu wa mitandao ya kijamii, bila shaka ulikumbana na video au kusoma jumbe za watu wakimsawiri vibaya, kunuiza mambo ya soni na hata kumlaani mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14.  Mtoto huyu ambaye kosa la pekee ni ujasiri wa kusimama kidete kutetea amani na afya yake ya akili pamoja na kaka yake mdogo alijipata taabani huku watu wazima wenye akili razini na waliopevuka kiumri wakimmiminia cheche za matusi.  Kisa na maana? Alisisitiza kuendelea kuishi na baba yake wa kambo aliyewalea tangu utotoni pamoja na kaka yake mdogo baada ya wazazi wao kutengana na mama yao mzazi kufa baadaye.  Licha ya kudhalilishwa na watu walioonekana kujawa na machungu ya kushangaza, binti huyo alisema bayana ni heri afe aungane na mama yake jongomeo kuliko kwenda kuishi na baba yake mzazi baada ya kushuhudia aliyompitishia mama yake.  Ilistaajabisha sana kusikia na kusoma jumbe za watu wazima hasa kina mama ambao wangetarajiwa kufahamu uchungu wa mwana wakimuumbua mtoto huyo jinsi alivyopotoka na kubashiri atakavyoishia vibaya maishani.  Wengine bila haya walinuiza kuwa msichana huyo tayari anashiriki unyumba na baba yake mlezi ndiposa hataki kwenda kuishi na baba yake mzazi licha ya kuwa tajiri na kupatiwa usimamizi na korti.  Kanuni za utu, maadili na utamaduni wa Kiafrika unawaasa wazazi kutowasema vibaya watoto wa wenzao wakifahamu fika kwamba wao pia wanalea watoto.  Inavunja moyo kuona jinsi baadhi ya wanajamii wamezoea na kukubali maovu kiasi kwamba mazuri yanapotokea wanayapinga vikali.  Hawaamini mwanamke aliyekandamizwa na mumewe na kuachwa na watoto anaweza kumpata mwanamme atakayempenda pamoja na watoto wake na kumwoa kihalali.   Wanakereketwa maini kuona kuwa inawezekana baba au mama wa kambo kuwapenda na kuwatunza watoto waliokataliwa na kutelekezwa na wazazi wao halisi.  Wanaungulika kuwa baadhi ya watu hawapitii madhila waliyotarajia na wamesitirika kwa neema ya Maulana.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 01 Nov 2026 15:15:33

Kufuatanisha watoto kwa karibu kutafanya uzeeke upesi, utafiti

UJAUZITO NA UZAZI  KUZAA watoto wakiwa wamefuatana kwa karibu bila muda wa kutosha kabla ya kushika mimba huenda kusababisha kuzeeka haraka, utafiti mpya umefichua.  Kulingana na wataalam, kupachikwa mimba zikifuatana kwa karibu huenda kukazuia mwili kuwa na muda wa kutosha kupata afueni hivyo kusababisha mabadiliko yanayohusiana na kuzeeka kibiolojia kuongezeka.  Utafiti huo ulitathmini mabadiliko kibayolojia yanayotokea mwanamke akiwa mjamzito kwa lengo la kuboresha afya ya ujauzito ulifichua uhusiano uliopo kati ya mimba na kuzeeka.  Muda wa kupata afueni baada ya kujifungua na kubeba mimba nyingine huenda mwishowe ukaathiri afya ya mama ya muda mrefu, wataalam wanasema.  Kutungwa mimba zinazofuatana kwa karibu kunaweza kuzuia kupona kikamilifu hivyo kuruhusu baadhi ya mabadiliko kuongezeka katika mimba zitakazofuata, wanafafanua.  'Utafiti wetu wa awali umebaini kuwa umri kibiolojia huongezeka kwa muda wakati wa ujauzito, na kufikia kilele katika kipindi cha tatu au wakati wa kujifungua," wanafafanua wataalam kutoka Harvard Medical School.  "Tukikubali wazo kuwa mabadiliko haya ya muda mfupi katika umri kibiolojia hutokea, swali ni jinsi tunaweza kuhusisha mabadiliko hayo kwa mkondo wa jumla wa kuzeeka maishani."  Japo kuna uwezekano kwamba huenda mkondo wa kuzeeka kwa jumla ukabadilika, wataalam wanafafanua kuwa hii sio sawa na uharibifu kibiolojia.  "Tunafahamu kuwa sehemu fulani au kubeba mimba hadi miezi tisa ikamilike, kuna manufaa kwa maisha ya mtu binafsi."  Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa sasa linapendekeza kusubiri kwa muda usiopungua miezi 24 baada ya kujifungua salama kabla ya kutungwa mimba nyingine, kama namna ya kupunguza athari za afya kwa mama na mtoto.  "Kuna mshawasha mkubwa kuhusu kutumia nyenzo za kutathmini umri kibiolojia kuelekeza umri wa mtu binafsi kwa kiwango cha kuzuia na kinachowiana na mhusika. Kuchunguza mabadiliko wakati wa ujauzito ni njia mojawapo ya kupata uelewa wa kimsingi kuhusu kuzeeka kwa upana."  Ili kutoa mapendekezo mahsusi kuhusiana na kuzeeka kibiolojia badala ya matokeo ya ujauzito, wataalam wanasema utafiti zaidi utahitajika kupima umri wa kibiolojia kwa mimba kadhaa na kisha kufuatilia kina mama husika kwa miongo kadhaa baadaye. 

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 01 Nov 2026 15:30:06

Ilani kuhusu bidhaa za kulainisha ngozi zinazosifiwa sana mitandaoni

FASHONI   KATIKA harakati za kusaka na kudadisi mbinu na bidhaa za vipodozi zinazofaa zaidi kuboresha mwonekano wa ngozi yako, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba umekumbana na aina ya ngozi inayofahamika kama "glass skini."  Glass skin jinsi tafsiri yake inavyoashiria ni ngozi laini inayong'aa na yenye maji ya kutosha inayopigiwa debe mno kwenye mitandao ya kijamii hususan Tiktok na inayohusishwa na mtindo maalum wa kutunza ngozi kutoka Korea.  Hata hivyo, ikiwa umekuwa ukisugua ngozi yako kutwa kucha na kuipaka vipodozi anuai ili kupata Glass Skin, utahitajika kuacha mara moja.  Mtindo wa kutunza ngozi wa Korea na juhudi za kufanikisha glass skin  zimeshika kasi duniani hasa kupitia Tiktok inayofikia mamilioni ya watu.  Hata hivyo, usahihi na usalama wa matini kuhusu mtindo huu wa urembo haujafanyiwa uchunguzi wa kina kulingana na wataalam.  Utafiti mpya sasa umefichua kuwa karibu video zote (asilimia 95)  zinazosambazwa kwenye Tiktok kuhusu mtindo wa kutunza ngozi wa Korea hazina maelezo kuhusu usalama na zinasheheni angalau dai moja la kupotosha.  Watafiti walitathmini video zinazohusu mtindo maarufu wa kutunza ngozi wenye asili ya Korea (Glass skin) Mei 2026 ambapo video 38 zilichunguzwa kuhusu madai ya wataalam wa ngozi, maelezo ya usalama, ubora na uwezo wa kutegemewa kwa kutumia teknolojia maalum.  Asilimia 84 ya video kuhusu glass skin zilifeli kufafanua kuhusu aina mbalimbali ya ngozi huku asilimia 45 zikipigia debe mchanganyiko wa viungo vyenye nguvu bila maelekezo mwafaka ya usalama na asilimia 32 kuahidi matokeo papo hapo.  Video zote hizo ziliorodheshwaa kuwa zisizoweza kutegemewa au zenye kiwango cha chini cha kutegemewa ambapo hakuna yoyote iliyonukuu mrejelewa kutoka nje, kulingana na utafiti huo.  "Matokeo yetu yanaonyesha pengo kubwa kati ya umaarufu wa matini hii na ubora wa maelezo yanayotolewa," walisema wataalam.  "Kufuata mitindo hii bila maelekezo yanayomfaa mtu binafsi huenda kukachangia mwasho, kuchubua ngozi kupita kiasi, chunusi kuchipuka au kuvuruga sehemu ya juu ya ngozi, hasa wakati viungo vyenye nguvu zinapochanganywa."  Ripoti hii iliwasilishwa katika Kongamano la 2026 la European Academy of Dermatology and Venereology, EADV) na iliashiria kuwa sehemu kubwa za video zinazohusu glass skin (asilimia 82) huundwa na wanamitandao mashuhuri (influencers) ambao sio wataalam wa afya.  Nembo za urembo zinajumuisha asilimia 11 huku waundaji matini wengine kuhusu urembo wakichangia asilimia nane na hakuna video yoyote kuhusu ngozi hiyo imeundwa na madaktari wa ngozi, ulisema utafiti.  "Kilichotushangaza zaidi ni jinsi maelezo ya kimsingi kuhusu usalama yalivyozidi kujumuishwa kila wakati," walifafanua wataalam.  "Ni video moja tu miongoni mwa 38 ilitaja tishio la mwasho, na ni mbili pekee ziliangazia kinga ya jua, hakuna yoyote iliyotaja tishio la ugonjwa wa ngozi wala yoyote iliyopendekeza kutafuta ushauri wa daktari wa ngozi."       

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 01 Nov 2026 11:55:11

SHERIA: Hauwezi kutunzwa milele na mchumba wako mkitalikiana

Je, mtu aliyepewa posho ya matunzo na mahakama ana haki ya kuendelea kupokea fedha hizo maisha yake yote? Sheria ya Ndoa ya Kenya inaeleza kuwa malipo hayo yanaweza kukoma kutokana na mambo fulani. Chini ya kifungu cha 78, agizo la matunzo ya mwanandoa linaweza kukoma katika hali tofauti, kutegemea namna lilivyowekwa na mazingira ya wahusika. Kwa mfano, ikiwa agizo halikuwekewa dhamana, linaweza kukoma baada ya kifo cha aliyekuwa akipokea matunzo. Ikiwa matunzo yaliwekewa dhamana, agizo hilo hukoma baada ya kifo cha anayelipwa. Sheria pia inasema kuwa agizo la matunzo linaweza kukoma ikiwa mtu anayepokea fedha hizo baadaye ataweza kujikimu mwenyewe. Hii ina maana kuwa hali ya kifedha ya anayelipwa posho ni muhimu katika kuamua iwapo malipo yanapaswa kuendelea. Mtu ambaye awali alihitaji msaada wa kifedha anaweza baadaye kupata uwezo wa kujitegemea. Kifungu cha 79 kinaongeza kuwa agizo la matunzo hukoma anayelipwa anapoingia katika ndoa nyingine. Hata hivyo, sheria haimaanishi kuwa anayelipa anaweza kusitisha malipo kwa uamuzi wake mwenyewe kila anapohisi kuwa hali imebadilika. Kifungu cha 80 kinapatia mahakama mamlaka ya kubadilisha au kufuta agizo lililopo ikiwa imeridhika kuwa lilitokana na taarifa zisizo za kweli au kosa la ukweli, au kumekuwa na mabadiliko makubwa ya hali tangu agizo lilipotolewa. Mahakama pia inaweza kubadilisha masharti ya makubaliano ya matunzo kati ya wanandoa iwapo kutakuwa na mabadiliko makubwa ya mazingira. Kwa upande mwingine, sheria inalinda fedha za matunzo dhidi ya madai ya madeni. Kifungu cha 81 kinasema kuwa fedha hizo haziwezi kuhamishwa kwa mtu mwingine wala kutwaliwa ili kulipia deni la anayelipwa. Kifungu cha 82 kinaweka muda wa miaka mitatu wa kuanzisha kesi ya kudai kila malipo ya matunzo yaliyochelewa. Baada ya muda huo, malipo husika hayawezi kudaiwa kupitia kesi mpya. Sheria pia inaruhusu malimbikizi yanayostahili kudaiwa kuwa deni la kiraia, yakiwemo katika mazingira fulani baada ya kifo cha mhusika. Kwa hivyo, posho ya matunzo si malipo yanayoendelea bila kujali mazingira. Sheria inaweka masharti ya kukomeshwa, kubadilishwa au kufutwa kwa agizo la kuyalipa. Hata hivyo, uamuzi wa kusitisha au kubadilisha agizo kwa sababu ya mabadiliko ya hali unapaswa kufuata utaratibu wa mahakama.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 01 Nov 2026 10:55:58

Jithamini mwanamume, usirudie mwanamke aliyekusaliti

Katika maisha, mwanaume anahitaji kuwa na misimamo, kujithamini na kujua namna ya kushughulika na watu wanaomzunguka. Mafanikio hayaji kwa bahati pekee, bali pia yanahitaji nidhamu, bidii na uwezo wa kufanya maamuzi yanayofaa. Mtaalamu wa masuala ya ustawi wa maisha Nelson Kawei anaorodhesha mambo kadhaa ambayo yanaweza kumsaidia mwanaume kujijenga na kuboresha maisha yake.  Usirudie mwanamke aliyekusaliti Mapenzi yanahitaji uaminifu. Ikiwa mtu amekusaliti na kuvunja imani yako, usikimbilie kurudiana naye bila kutathmini kilichotokea na kama uhusiano huo unaweza kujengwa upya.  Usikubali kudharauliwa Jithamini na weka mipaka katika mahusiano yako. Heshima inapaswa kuwa ya pande zote, na si lazima uvumilie matusi au unyanyasaji ili kudumisha uhusiano.  Simama unapomsalimia mtu kwa mkono Kusimama unapopeana mikono kunaweza kuonyesha adabu na heshima, hasa unapokutana na mtu katika mazingira rasmi.  Usiishi kwa kutaka kuwafurahisha watu Usitumie pesa ambazo huna ili kuonekana tajiri au kufurahisha marafiki. Ishi kulingana na uwezo wako na uweke kipaumbele katika mahitaji muhimu.  Usile kipande cha mwisho cha chakula ambacho hukununua Zingatia hisia zao. Kutokula kilichobaki ni ishara ya kujali na kushirikiana. Daima jitahidi kuwa bora zaidi Weka malengo ya kuboresha maisha yako kielimu, kikazi, kifedha na kibinafsi. Usiridhike na hali uliyonayo ikiwa unaweza kufanya zaidi. Walinde walio nyuma yako na uwaheshimu walio kando yako Wasaidie wanaokutegemea na uwaheshimu marafiki, wafanyakazi wenzako na watu wanaosafiri nawe katika safari ya maisha. Fikiri kabla ya kujibu swali Unapoulizwa swali, tulia kwa sekunde chache kabla ya kujibu. Hilo linaweza kukusaidia kupanga mawazo na kuepuka kusema jambo kwa pupa. Usilazimishe mahusiano Mapenzi yanahitaji ridhaa na juhudi za pande zote. Usijishushe kwa kuomba mtu akupende au abaki nawe ikiwa hataki kuwa katika uhusiano huo. Fanya mazoezi mara kwa mara Tenga muda wa kufanya mazoezi angalau mara nne kwa wiki, kulingana na afya na uwezo wako. Mazoezi yanaweza kusaidia kuimarisha mwili na kuboresha ustawi wa jumla.  Usijilazimishe kwenda mahali ambapo hujaalikwa Ikiwa marafiki wamepanga shughuli bila kukualika, usijilazimishe kujiunga nao. Heshimu mipaka yao na tafuta shughuli zinazokufurahisha.  Beba kiasi cha pesa taslimu Ingawa malipo ya simu na kadi yamerahisisha maisha, kuwa na kiasi kidogo cha pesa taslimu kunaweza kukusaidia pale njia hizo zinapokosa kufanya kazi. Vaa vizuri kulingana na shughuli Huhitaji nguo za bei ghali ili uonekane nadhifu. Chagua mavazi safi, yanayokutosha vizuri na yanayofaa tukio husika. Sikiliza kwa makini unapozungumza na watu Tikisa kichwa kuonyesha kuwa unafuatilia mazungumzo na tazama mtu usoni kwa namna inayofaa. Hata hivyo, epuka kumkodolea macho kiasi cha kumfanya akose raha. Tafuta njia mbalimbali za kupata mapato Usitegemee kwa chanzo kimoja cha mapato ikiwa una nafasi ya kufanya zaidi. Unaweza kujifunza ujuzi mpya, kuanzisha biashara ndogo au kufanya kazi ya ziada kulingana na uwezo wako. Kujiheshimu, afafanua Kawei, si kuwadharau wengine au kujifanya mkamilifu. Ni kujua thamani yako, kuheshimu watu, kutumia pesa kwa busara na kujitahidi kuboresha maisha yako kila siku.

read more