taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 07 Oct 2026 07:55:38
Mke akamatwa baada ya kuripoti mauaji ya mumewe
MWANAMKE mmoja katika Kaunti ya Homa Bay alikamatwa na kuzuiliwa na polisi baada ya uchunguzi kumhusisha na mauaji ya mumewe ambayo awali alikuwa ameenda kuripoti katika kituo cha polisi. Rose Akoth alifika katika Kituo cha Polisi cha Ndiru Jumatatu akidai kuwa mumewe, John Okoko, alikuwa ameuawa na watu wasiojulikana. Hata hivyo, maelezo aliyotoa yaliibua maswali na kuwafanya maafisa wa usalama kuanza kumchunguza kwa kina. Mwili wa Okoko, mwenye umri wa miaka 42, ulipatikana ukiwa umetupwa kwenye kichaka katika Kijiji cha Kadibuoro, Kaunti ya Homa Bay, Jumapili. Polisi wanasema uchunguzi wao ulionyesha kuwa mauaji hayo yalifanyika nyumbani kwake kabla ya mwili kuhamishwa na kutupwa eneo ulikopatikana. Kwa mujibu wa polisi, Okoko aliuawa akiwa amelala ndani ya nyumba yake baada ya kupigwa kwa kifaa kizito. Baada ya mauaji hayo, washukiwa walioshiriki walidaiwa kuusafisha mwili huo bafuni, kumvisha nguo nyingine na baadaye kuubeba umbali wa takriban kilomita moja hadi kichakani. Kamanda wa Polisi wa Rangwe, Magdalene Chebet, alisema Akoth awali alidai kuwa mumewe alikuwa ameenda kukutana na mkulima aliyekuwa amemwahidi miche ya mpunga kabla ya kuuawa na mtu asiyejulikana. Alipoulizwa maswali zaidi na kuombwa kuwaongoza maafisa hadi nyumbani kwake, polisi waligundua ushahidi uliobadilisha mwelekeo wa uchunguzi. Madoa ya damu yalipatikana kwenye kuta za chumba cha kulala na kwenye kitanda cha wanandoa hao. "Ushahidi huo ulitosha kuonyesha kuwa marehemu aliuawa ndani ya nyumba," alisema Chebet. Baada ya kuhojiwa zaidi, Akoth alidaiwa kuwahusisha mwanawe mwenye umri wa miaka 24 na mwanaume mwingine mwenye umri wa miaka 36 kuwa washirika katika mauaji hayo. Habari za kukamatwa kwa washukiwa hao ziliwashtua wakazi wa eneo hilo ambao hapo awali walidhani Okoko alikuwa ameuawa na watu wasiojulikana. Wakazi wenye hasira walimvamia mshukiwa huyo wa miaka 36 kabla ya polisi kuingilia kati na kumuokoa. Polisi wamesema bado hawajabaini sababu ya mauaji hayo. Washukiwa wote watatu wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Ndiru wakisubiri kufikishwa mahakamani, huku mwili wa Okoko ukihifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Homa Bay kwa uchunguzi wa maiti
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
SHERIA: Hauwezi kutunzwa milele na mchumba wako mkitalikiana
Je, mtu aliyepewa posho ya matunzo na mahakama ana haki ya kuendelea kupokea fedha hizo maisha yake yote? Sheria ya Ndoa ya Kenya inaeleza kuwa malipo hayo yanaweza kukoma kutokana na mambo fulani. Chini ya kifungu cha 78, agizo la matunzo ya mwanandoa linaweza kukoma katika hali tofauti, kutegemea namna lilivyowekwa na mazingira ya wahusika. Kwa mfano, ikiwa agizo halikuwekewa dhamana, linaweza kukoma baada ya kifo cha aliyekuwa akipokea matunzo. Ikiwa matunzo yaliwekewa dhamana, agizo hilo hukoma baada ya kifo cha anayelipwa. Sheria pia inasema kuwa agizo la matunzo linaweza kukoma ikiwa mtu anayepokea fedha hizo baadaye ataweza kujikimu mwenyewe. Hii ina maana kuwa hali ya kifedha ya anayelipwa posho ni muhimu katika kuamua iwapo malipo yanapaswa kuendelea. Mtu ambaye awali alihitaji msaada wa kifedha anaweza baadaye kupata uwezo wa kujitegemea. Kifungu cha 79 kinaongeza kuwa agizo la matunzo hukoma anayelipwa anapoingia katika ndoa nyingine. Hata hivyo, sheria haimaanishi kuwa anayelipa anaweza kusitisha malipo kwa uamuzi wake mwenyewe kila anapohisi kuwa hali imebadilika. Kifungu cha 80 kinapatia mahakama mamlaka ya kubadilisha au kufuta agizo lililopo ikiwa imeridhika kuwa lilitokana na taarifa zisizo za kweli au kosa la ukweli, au kumekuwa na mabadiliko makubwa ya hali tangu agizo lilipotolewa. Mahakama pia inaweza kubadilisha masharti ya makubaliano ya matunzo kati ya wanandoa iwapo kutakuwa na mabadiliko makubwa ya mazingira. Kwa upande mwingine, sheria inalinda fedha za matunzo dhidi ya madai ya madeni. Kifungu cha 81 kinasema kuwa fedha hizo haziwezi kuhamishwa kwa mtu mwingine wala kutwaliwa ili kulipia deni la anayelipwa. Kifungu cha 82 kinaweka muda wa miaka mitatu wa kuanzisha kesi ya kudai kila malipo ya matunzo yaliyochelewa. Baada ya muda huo, malipo husika hayawezi kudaiwa kupitia kesi mpya. Sheria pia inaruhusu malimbikizi yanayostahili kudaiwa kuwa deni la kiraia, yakiwemo katika mazingira fulani baada ya kifo cha mhusika. Kwa hivyo, posho ya matunzo si malipo yanayoendelea bila kujali mazingira. Sheria inaweka masharti ya kukomeshwa, kubadilishwa au kufutwa kwa agizo la kuyalipa. Hata hivyo, uamuzi wa kusitisha au kubadilisha agizo kwa sababu ya mabadiliko ya hali unapaswa kufuata utaratibu wa mahakama.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
Jithamini mwanamume, usirudie mwanamke aliyekusaliti
Katika maisha, mwanaume anahitaji kuwa na misimamo, kujithamini na kujua namna ya kushughulika na watu wanaomzunguka. Mafanikio hayaji kwa bahati pekee, bali pia yanahitaji nidhamu, bidii na uwezo wa kufanya maamuzi yanayofaa. Mtaalamu wa masuala ya ustawi wa maisha Nelson Kawei anaorodhesha mambo kadhaa ambayo yanaweza kumsaidia mwanaume kujijenga na kuboresha maisha yake. Usirudie mwanamke aliyekusaliti Mapenzi yanahitaji uaminifu. Ikiwa mtu amekusaliti na kuvunja imani yako, usikimbilie kurudiana naye bila kutathmini kilichotokea na kama uhusiano huo unaweza kujengwa upya. Usikubali kudharauliwa Jithamini na weka mipaka katika mahusiano yako. Heshima inapaswa kuwa ya pande zote, na si lazima uvumilie matusi au unyanyasaji ili kudumisha uhusiano. Simama unapomsalimia mtu kwa mkono Kusimama unapopeana mikono kunaweza kuonyesha adabu na heshima, hasa unapokutana na mtu katika mazingira rasmi. Usiishi kwa kutaka kuwafurahisha watu Usitumie pesa ambazo huna ili kuonekana tajiri au kufurahisha marafiki. Ishi kulingana na uwezo wako na uweke kipaumbele katika mahitaji muhimu. Usile kipande cha mwisho cha chakula ambacho hukununua Zingatia hisia zao. Kutokula kilichobaki ni ishara ya kujali na kushirikiana. Daima jitahidi kuwa bora zaidi Weka malengo ya kuboresha maisha yako kielimu, kikazi, kifedha na kibinafsi. Usiridhike na hali uliyonayo ikiwa unaweza kufanya zaidi. Walinde walio nyuma yako na uwaheshimu walio kando yako Wasaidie wanaokutegemea na uwaheshimu marafiki, wafanyakazi wenzako na watu wanaosafiri nawe katika safari ya maisha. Fikiri kabla ya kujibu swali Unapoulizwa swali, tulia kwa sekunde chache kabla ya kujibu. Hilo linaweza kukusaidia kupanga mawazo na kuepuka kusema jambo kwa pupa. Usilazimishe mahusiano Mapenzi yanahitaji ridhaa na juhudi za pande zote. Usijishushe kwa kuomba mtu akupende au abaki nawe ikiwa hataki kuwa katika uhusiano huo. Fanya mazoezi mara kwa mara Tenga muda wa kufanya mazoezi angalau mara nne kwa wiki, kulingana na afya na uwezo wako. Mazoezi yanaweza kusaidia kuimarisha mwili na kuboresha ustawi wa jumla. Usijilazimishe kwenda mahali ambapo hujaalikwa Ikiwa marafiki wamepanga shughuli bila kukualika, usijilazimishe kujiunga nao. Heshimu mipaka yao na tafuta shughuli zinazokufurahisha. Beba kiasi cha pesa taslimu Ingawa malipo ya simu na kadi yamerahisisha maisha, kuwa na kiasi kidogo cha pesa taslimu kunaweza kukusaidia pale njia hizo zinapokosa kufanya kazi. Vaa vizuri kulingana na shughuli Huhitaji nguo za bei ghali ili uonekane nadhifu. Chagua mavazi safi, yanayokutosha vizuri na yanayofaa tukio husika. Sikiliza kwa makini unapozungumza na watu Tikisa kichwa kuonyesha kuwa unafuatilia mazungumzo na tazama mtu usoni kwa namna inayofaa. Hata hivyo, epuka kumkodolea macho kiasi cha kumfanya akose raha. Tafuta njia mbalimbali za kupata mapato Usitegemee kwa chanzo kimoja cha mapato ikiwa una nafasi ya kufanya zaidi. Unaweza kujifunza ujuzi mpya, kuanzisha biashara ndogo au kufanya kazi ya ziada kulingana na uwezo wako. Kujiheshimu, afafanua Kawei, si kuwadharau wengine au kujifanya mkamilifu. Ni kujua thamani yako, kuheshimu watu, kutumia pesa kwa busara na kujitahidi kuboresha maisha yako kila siku.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Mateso ya kustaafu:Yafichuliwa wastaafu 80,000 wanaishi kwa pensheni ya Sh4,000 kwa mwezi
ZAIDI ya wafanyakazi 80,000 waliostaafu serikalini wanapokea pensheni ya Sh4,000 pekee kwa mwezi, huku wabunge wakishinikiza serikali kuongeza malipo hayo ili kukabiliana na gharama ya maisha inayozidi kupanda. Kamati ya Bunge kuhusu Maombi ya Umma imeitaka Wizara ya Fedha na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kuwasilisha ndani ya miezi miwili ripoti kuhusu fedha zinazohitajika kuongeza pensheni ya wastaafu 319,207. Hatua hiyo inafuatia malalamishi ya wastaafu kuwa wamekuwa wakilipwa viwango vya chini kwa miaka mingi licha ya kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma muhimu. Malalamishi hayo yaliwasilishwa bungeni na Chama cha Kitaifa cha Wastaafu wa Utumishi wa Umma (KNAPS), tawi la Kericho, kinachowakilisha wastaafu kote nchini. Chama hicho kinasema takriban asilimia 25 ya wanachama wake, sawa na watu 80,000, hupokea chini ya Sh4,000 kila mwezi, kiasi ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji yao ya kimsingi. Wastaafu hao wanataka mifumo ya zamani ya pensheni isiyokuwa na michango ya wafanyakazi iunganishwe na mfumo wa sasa wa Public Service Superannuation Scheme (PSSS), ambao wanadai una manufaa bora. Pia wanataka pensheni zao ziongezwe mara kwa mara ili kuendana na kupanda kwa gharama ya maisha, pamoja na sheria kurekebishwa ili kuwalinda wao na familia zao. Katika ripoti iliyowasilishwa Bungeni Septemba 30, kamati ilipendekeza Wizara ya Fedha kushirikiana na SRC kufanya tathmini ya gharama za pensheni kila baada ya miaka mitatu. Tathmini ya kwanza inapaswa kukamilika kufikia Desemba 31, 2026. Hata hivyo, pendekezo la kuunganisha mifumo hiyo limekabiliwa na upinzani kutoka kwa taasisi mbalimbali za serikali kutokana na gharama kubwa inayoweza kuhusika. Mamlaka ya Kusimamia Manufaa ya Wastaafu (RBA) iliambia kamati kuwa kuunganisha mifumo hiyo kutahitaji serikali kwanza kulipa madeni ya pensheni yaliyolimbikiza, yanayokadiriwa kuzidi Sh1 trilioni. Mkurugenzi Mkuu wa RBA Charles Machira alisema tathmini ya Wizarea ya Fedha ya Juni 2024 ilionyesha kuwa madeni hayo yalikuwa yamezidi Sh1 trilioni. Wizara inasema inatumia takriban Sh7.8 bilioni kila mwezi kulipa wastaafu 319,207, sawa na Sh93.7 bilioni kwa mwaka. Mfumo wa zamani haukuwa ukikata michango kutoka mishahara ya wafanyakazi. Badala yake, pensheni ziliamuliwa kwa mujibu wa sheria zilizokuwepo wakati huo. Mfumo mpya ulioanza Januari 2021 unawataka wafanyakazi kuchangia asilimia 7.5 ya mishahara yao kila mwezi, huku serikali ikiongeza kiasi sawa. Kufikia Juni 2026, wafanyakazi 529,635 walikuwa wamejiunga na mfumo huo, wakiwa wameweka akiba ya Sh343.75 bilioni. SRC imesema ongezeko lolote la pensheni lazima lizingatie uwezo wa kifedha wa serikali. Idara ya Utumishi wa Umma pia imeonya kuwa kuongeza pensheni kutaleta mzigo wa muda mrefu kwa serikali, hivyo ni lazima kuhakikisha malipo hayo yanaweza kudumishwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
Sababu za wakazi wa Runda kukataa kanisa la orofa tisa la nabii Owuor
WAKAZI wa mtaa wa kifahari wa Runda, Nairobi, wamepinga mpango wa mhubiri David Owuor wa kujenga kanisa la orofa tisa katika mtaa huo, wakisema mradi huo utazidisha mafuriko, msongamano wa magari na kuvuruga amani yao. Wakazi hao wanataka kanisa la Repentance and Holiness Ministry lijengwe kwa kuzingatia kanuni za eneo hilo, ambazo wanadai zinahitaji majengo ya makazi kuwa na orofa tatu au chini. Wakazi kutoka vyama 13, vinavyowakilisha zaidi ya watu 100 wanaoishi kando ya Barabara ya Kwaheri, wamewasilisha malalamishi rasmi kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu, wakipinga mradi huo unaopanga katika ekari tatu. Wakazi hao wanahofia kuwa jengo hilo refu litavuruga faragha ya majirani, kuzuia mwanga wa jua kuingia katika nyumba zilizo karibu na kubadilisha mandhari ya mtaa huo. Pia wanasema eneo hilo hukumbwa na mafuriko wakati wa mvua na ujenzi wa kanisa hilo unaweza kuzidisha tatizo hilo kutokana na maji ya mvua kutoka kwenye jengo na kumwagika katika makazi jirani. Wakazi hao wanadai kuwa kanisa halijatoa mpango unaokubalika wa mitaro ya maji ya mvua wala wa kushughulikia maji taka, kwa kuwa ardhi hiyo haijaunganishwa na mfumo wa maji taka wa umma. Barabara ya Kwaheri ina upana wa takriban mita tisa, hali ambayo wakazi wanasema haitatosha kuhudumia magari ya wakazi na maelfu ya waumini wanaotarajiwa kuhudhuria ibada. Pia wanahofia kelele zitakazosababishwa na ibada za usiku, maarufu kama kesha, ambazo zinaweza kuwasumbua watoto wa shule na wazee. Kanisa hilo lilinunua ardhi hiyo ya ekari tatu kutoka kwa wamiliki wa shamba la kahawa na mwezi Machi likaomba kubadilisha matumizi yake kutoka kilimo hadi taasisi ya kidini, ofisi na makazi ya wageni. Hata hivyo, kamati ya kiufundi ya Kaunti ya Kiambu ililitaka kanisa kufanya mikutano ya ushirikishaji wa umma na kutoa maelezo kuhusu matumizi ya vyumba vya wageni. Katika mkutano wa Oktoba 22, kanisa liliwasilisha michoro ya usanifu wa jengo hilo kwa wadau. Mshauri wa usanifu aliyeajiriwa na kanisa anasema eneo hilo limetengwa kwa matumizi mseto, hivyo mradi huo unapaswa kuruhusiwa. Lakini wakazi wanasisitiza kuwa eneo hilo limekusudiwa makazi ya watu wachache, na kwamba kuwepo kwa shule na taasisi nyingine zisizo za makazi hakumaanishi kanisa hilo liruhusiwe kujengwa bila kuzingatia kanuni. Waziri wa ardhi wa Kaunti ya Kiambu, Salome Wainaina, amesimamisha shughuli zozote za maendeleo katika ardhi hiyo hadi kanisa na wakazi wafikie makubaliano.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Sababu za wadau wa elimu kupinga mageuzi ya Ruto
WADAU wakuu katika sekta ya elimu wamepinga miswada saba ya mageuzi ya elimu inayosukumwa na Rais William Ruto, wakisema inaweza kufuta mafanikio yaliyopatikana iwapo haitafanyiwa marekebisho. Miswada hiyo, ambayo iko katika hatua ya kukusanya maoni ya umma kupitia Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa, inalenga kubadilisha usimamizi wa shule, mafunzo ya walimu, ufadhili wa wanafunzi na uteuzi wa nafasi katika vyuo vikuu na taasisi za kiufundi. Vyama vya walimu, wahadhiri, wazazi na wamiliki wa shule za kibinafsi wamewasilisha mapendekezo yao, wakishinikiza wabunge kuyazingatia kabla ya kupitisha sheria hizo. Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) kinataka sheria inayopendekezwa kuhusu ufadhili wa elimu ya juu ilinde wanafunzi ambao tayari wanapokea mikopo na ufadhili wa masomo, pamoja na haki za wafanyakazi wa vyuo vikuu. Chama hicho pia kinataka serikali kufanya tathmini ya gharama za utekelezaji wa mfumo huo kabla ya kuanza kutumika. Kinasema mswada huo unaangazia zaidi ufadhili wa wanafunzi huku ukipuuza gharama ya kuendesha vyuo vikuu na kulipa wahadhiri. UASU pia inapinga sharti linalotaka wahitimu kuanza kurejesha mikopo ndani ya mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo. Inataka muda huo uanze tu baada ya mhitimu kupata kazi yenye mapato ya uhakika. Chama hicho kinataka pia kuwakilishwa katika bodi za Mamlaka ya Ufadhili wa Elimu ya Juu na Huduma ya Kitaifa ya Uteuzi wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kiufundi (KUCCPS). Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kati (KUPPET) pia kimepinga muda wa mwaka mmoja wa kuanza kulipa mikopo, kikisema ni mgumu kwa wahitimu katika soko la ajira lenye ushindani. Kinataka ufadhili huo uwe na chanzo cha wazi cha fedha na kiwango kisichozidi asilimia 2.5 ya mapato ya kila mwaka ya ushuru yanayokusanywa na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA). KUPPET pia inataka serikali itoe ufadhili kupitia ruzuku, ufadhili wa masomo na mikopo kulingana na mahitaji ya wanafunzi. Chama cha Wakufunzi wa Vyuo vya Kiufundi na Mafunzo ya Ufundi (KUTVET) kinasema mfumo unaopendekezwa hauzingatii tofauti za gharama za kozi mbalimbali. Kinasema kozi kama uhandisi wa magari, uchomeleaji, umeme na ujenzi zinahitaji vifaa na mafunzo ya vitendo ambayo hayawezi kugharimiwa kwa kiwango sawa na kozi zinazofundishwa darasani pekee. Chama hicho kinataka fedha zitumike pia kununua mashine, vifaa vya usalama, teknolojia za kisasa na kugharamia mafunzo ya vitendo viwandani. Wakati huo huo, Chama cha Walimu wa Shule za Msingi (KNUT) kimepinga pendekezo linalotaka walimu kutoshiriki shughuli nyingine za kujipatia mapato wanapohudumu katika Tume ya Huduma za Walimu (TSC). KNUT kinasema tume hiyo haipaswi kudhibiti shughuli za walimu nje ya saa rasmi za kazi. Kwa upande wake, Chama cha Shule za Kibinafsi nchini kinataka sheria itambue shule za Sekondari Msingi zinazojitegemea, badala ya kuzilazimisha kuwa na sehemu ya shule za msingi za kawaida. Pia kinataka wanafunzi wa shule za kibinafsi waruhusiwe kunufaika na ufadhili wa masomo na basari za serikali bila kubaguliwa kwa sababu tu wanasomea katika taasisi hizo. Chama cha Kitaifa cha Wazazi kinataka wazazi wapewe nafasi kubwa zaidi katika maamuzi ya elimu kupitia marekebisho ya sheria ya elimu ya msingi. Wadau hao wanataka maoni yao yazingatiwe kabla ya miswada hiyo kuwasilishwa bungeni kwa hatua zaidi. Kamati ya Bunge inatarajiwa kukamilisha zoezi la kupokea maoni Alhamisi ijayo, baada ya kusikiliza TSC na Baraza la Magavana.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Vizingiti vinavyokabili ODM ikiendea nusu mkate na UDA
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinaingia katika hatua muhimu ya hesabu zake za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, kikitaka kugawana mamlaka kwa usawa na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) katika muungano unaopendekezwa kumuunga mkono Rais William Ruto. Hata hivyo, huku kiongozi wa ODM Oburu Oginga akisisitiza kuwa chama hicho kinastahili nusu ya mamlaka kwenye makubaliano na UDA, mgawanyiko wa ndani na kutokubaliana kuhusu ushirikiano na Ruto vinatishia kudhoofisha msimamo wake katika mazungumzo. ODM inataka kuwa mshirika sawa na UDA badala ya kuwa chama kidogo katika muungano unaotawaliwa na chama cha rais. Lakini kutaka nusu ya mamlaka na kuhakikisha inapata mgao huo ni mambo mawili tofauti. Oburu alieleza msimamo huo hadharani Juni 2026, akisema makubaliano yoyote ya kabla ya uchaguzi kati ya ODM na UDA lazima yazingatie kanuni ya kugawana mamlaka kwa asilimia 50 kwa kila upande. "Tutakapounda makubaliano ya muungano na UDA, yatategemea mgao wa asilimia 50 kwa kila upande, jambo litakalotufanya kuwa imara zaidi. Hata urais tutaujadili; hatutaacha kiti chochote bila mazungumzo," alisema Oburu. Wakizungumza wakiwa Turkana wiki jana, viongozi wa ODM walioongozwa na Mwenyekiti Gladys Wanga walisisitiza kuwa lazima makubaliano ya UDA yakitwe kwa msingi wa kugawana mamlaka nusu kwa nusu. Kauli hizo zinaashiria kuwa ODM haitaki mazungumzo yahusu nyadhifa za Baraza la Mawaziri pekee, bali pia urais na nafasi nyingine muhimu katika serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi. Hata hivyo, chama hicho kinapaswa kuthibitisha kuwa kina uwezo wa kuhamisha uungwaji mkono wake wa kisiasa hadi kwenye kura, kudumisha umoja na kuhakikisha wafuasi wake wa jadi wanabaki pamoja. Kifo cha Raila Odinga Oktoba 15, 2025, kiliondoa mwanasiasa aliyekuwa mhimili mkuu wa ODM katika mazungumzo ya kisiasa kwa miongo kadhaa. Raila hakuwa tu kiongozi wa chama, bali pia alikuwa mhamasishaji wa wafuasi, mpatanishi wa makundi yaliyokinzana na mtu aliyekuwa na uwezo wa kuunganisha viongozi wenye misimamo tofauti. Ushawishi wake ulitokana na uzoefu wa kushiriki chaguzi kadhaa, mtandao wa kisiasa aliojenga kwa miaka mingi na uwezo wa kujadiliana na washirika akiungwa mkono na maelfu ya wafuasi nyuma yake. Oburu sasa amebeba jukumu la kukiongoza chama katika kipindi hicho cha mpito, lakini changamoto yake ni kuonyesha kuwa nguvu za ODM zinaweza kudumu hata bila mtu aliyeunganisha makundi mbalimbali. ODM bado ina viongozi waliochaguliwa, mitandao ya kisiasa katika maeneo tofauti na utambulisho wa kitaifa uliojengwa kwa miaka mingi. Hata hivyo, rasilimali hizo zitakuwa na thamani katika mazungumzo iwapo chama kitaonyesha kuwa kinaweza kuendelea kuwa na umoja kuelekea 2027. Mazungumzo ya ODM na UDA yalipiga hatua nyingine Agosti 2026, Ruto na Oburu walipotangaza timu za kushughulikia mfumo wa kugawana mamlaka na manifesto ya pamoja ya muungano unaopendekezwa kwa uchaguzi wa 2027. Hatua hiyo ilionyesha kuwa mazungumzo hayahusu tena iwapo vyama hivyo vitashirikiana, bali masharti vitakayokubaliana na namna yatakavyotekelezwa. Kwa ODM, madai ya kugawana serikali kwa asilimia 50 ni msimamo wa mazungumzo, ambao haijulikani ikiwa utakubaliwa na UDA. Kulingana na viongozi wa chama hicho cha chungwa, usawa huo utahusu idadi ya mawaziri, nyadhifa kuu serikalini, uongozi wa Bunge, maeneo ya kuwania viti na kushiriki katika maamuzi muhimu ya serikali. "Masuala hayo yanahitaji kujadiliwa tofauti kwa sababu kupata idadi sawa ya mawaziri hakumaanishi moja kwa moja kuwa vyama vina mamlaka sawa katika kufanya maamuzi," asema mchanganuzi wa siasa Jimmy Opiyo. Suala jingine ni kugawana maeneo ya kisiasa, maarufu kama zoning, ambapo vyama hukubaliana kutosimamisha wagombeaji wanaoshindana katika maeneo fulani. ODM imetaka suala hilo liwe sehemu ya makubaliano, lakini UDA imeonyesha kutokuwa tayari kulikubali, kulingana na taarifa kuhusu mazungumzo ya vyama hivyo. Urais nao ni suala nyeti zaidi. Oburu amesema haupaswi kuachwa nje ya mazungumzo, lakini muungano unaopendekezwa pia unalenga kumuunga mkono Ruto katika uchaguzi wa 2027. Hali hiyo inaibua swali muhimu: Je, ODM inajadili masharti ya kumuunga mkono Ruto au inataka muungano ambao utawezesha kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya uongozi wa nchi? Opiyo anasema jibu litategemea masharti yatakayowekwa katika makubaliano ya mwisho. Anasema kuibuka kwa vuguvugu la Linda Mwananchi kulidhoofisha nguvu za ODM katika majadiliano. "Mgawanyiko huu unaweza kudhoofisha uwezo wa ODM kuwasilisha msimamo mmoja katika mazungumzo na UDA.Changamoto ya ODM si kupata nafasi serikalini pekee, bali kuhakikisha kuwa makubaliano yatakayofikiwa yana manufaa kwa chama na wafuasi wake," asema. Kushiriki katika serikali kunaweza kupatia ODM nafasi ya kushawishi sera, kugawana nyadhifa za uongozi na kushiriki katika maamuzi ya kitaifa. ODM inapaswa pia kutofautisha maslahi ya viongozi binafsi na yale ya wananchi wanaoiunga mkono. Kupata nyadhifa serikalini kunaweza kuwa na thamani kwa viongozi, lakini chama kinahitaji kuwaeleza wananchi namna ushirikiano huo utakavyoboresha maisha yao, utawala na uwakilishi wa kisiasa. "Takwa la kugawana serikali kwa asilimia 50 halitakuwa na nguvu bila ODM kuonyesha kuwa ina uungwaji mkono wa kutosha, inaweza kudumisha wapigakura wake na ina umuhimu wa kisiasa katika uchaguzi ujao," asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki. Anasema mazungumzo hayo yanapatia ODM fursa ya kulinda ushawishi wake katika serikali ya kitaifa, lakini pia yana hatari ya chama kuishia kumuunga mkono Ruto bila kupata dhamana ya kutekelezwa kwa madai yake.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Vigogo wageuza mikakati kuelekea 2027, watua vijijini naTikTok kujipigia debe
CHINI ya mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, wanasiasa wanaowania urais na vyama vyao vya kisiasa wamebadili mbinu zao, wakielekeza nguvu katika vijiji na maeneo ya mashambani kuwafikia wapiga kura. Badala ya kutegemea mikutano mikubwa katika miji na ushawishi wa vigogo wa kisiasa, viongozi wameanza kuingia katika vijiji vidogo, vibanda vya biashara na makazi ya kawaida ili kujenga uhusiano wa karibu na wananchi. Rais William Ruto na viongozi wa upinzani wameongeza ziara za mashinani, wakijitahidi kuwashawishi wapiga kura moja kwa moja kabla ya kampeni rasmi kuanza. Rais Ruto, anayelenga muhula wa pili, ameonekana akila katika vibanda vya kando ya barabara, kuingia manyattani na kutembelea nyumba za kawaida za mashambani. Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, ametembelea zaidi ya kaunti 20 na kuandaa mikutano ya hadhara zaidi ya 50 katika maeneo mbalimbali. Katika ziara zake za Narok na Kajiado Agosti na Septemba 2026, alitembelea maeneo ya mashambani yakiwemo Olokurto, Olpusimoru, Ololulung'a na Ewaso Ng'iro, kabla ya kuelekea Rombo, Loitokitok, Namanga na Kimana. Pia ametembelea maeneo ya mbali ya Pokot Magharibi, yakiwemo Sigor, Kacheliba na Kapenguria, akizindua miradi na kuwahimiza wafuasi wake kujiandikisha kupiga kura kwa wingi. Katika Ukambani, alitembelea Mwingi, Kitui West, Kibwezi, Matuu na Mwala. Mwingi Kaskazini, nyumbani kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, alikagua mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Tseikuru, akazindua barabara na kutoa hati za kumiliki ardhi. Ziara hizo pia zimefika Pwani, Magharibi na Nyanza, maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa ngome za upinzani. Rais ametembelea kaunti za Kisumu, Migori, Siaya na Homa Bay, akitangaza miradi ya masoko, maji, umeme na elimu. Katika ziara ya Pwani iliyochukua siku nane, alitembelea Taita Taveta, Mombasa, Kwale, Kilifi, Lamu na Tana River, ambako alisimamia utoaji wa karibu hati 200,000 za kumiliki ardhi. Upinzani nao haujachelewa. Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ametembelea kaunti 15 katika miezi mitatu, akiandaa mikutano 36 ya mashinani. Vuguvugu la Linda Mwananchi, linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna pamoja na Mbunge Babu Owino na Seneta Godfrey Osotsi, limefanya mikutano sita katika Nyanza, Magharibi na Pwani. Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) cha Rigathi Gachagua kimefanya mikutano 24 katika kaunti mbalimbali, zikiwemo Nakuru, Nyandarua, Laikipia, Kiambu, Kajiado, Nyeri na Murang'a. Mchambuzi wa siasa Profesa XN Iraki anasema mbinu hiyo inaweza kumsaidia Rais Ruto kwa sababu kukutana ana kwa ana na wapiga kura huwafanya wamzoee na kujenga uhusiano naye. Hata hivyo, Dkt Peter Mbae wa DCP anasema ziara hizo huenda zisibadilishe hisia za wananchi wanaokabiliwa na gharama kubwa ya maisha, mzigo wa ushuru na ahadi za kampeni ambazo hazijatekelezwa. Mchambuzi mwingine, Profesa Tom Nyamache, anasema Pwani, Magharibi, jamii ya Maa na Turkana zitasalia kuwa maeneo muhimu katika uchaguzi huo. Wakati huohuo, wataalamu wa utawala wanaonya kuwa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana unaweza kuwafanya washawishike kutumiwa vibaya kisiasa au kuhusishwa na ghasia za uchaguzi. Mbali na mikutano ya mashinani, mitandao ya kijamii kama TikTok, Facebook, X na WhatsApp inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kampeni za 2027. Mwanasheria na mchambuzi wa sera Steve Kabita anasema mitandao hiyo itakuwa jukwaa kuu la kujenga mitazamo ya kisiasa na kushawishi wapiga kura. Mwanaharakati Morara Kebaso anasema wapiga kura wa 2027 watakuwa na uelewa mkubwa zaidi wa masuala ya kisiasa kutokana na elimu ya uraia na matumizi ya teknolojia. Ripoti ya Thomson Reuters Foundation pia inaonyesha kuwa mitandao ya kijamii itakuwa na nafasi kubwa katika uchaguzi ujao, huku kampeni zikielekea zaidi kwenye majukwaa ya kidijitali. Hata hivyo, viongozi wa kijamii na kidini wanawahimiza wananchi kutathmini sera, mipango ya maendeleo na uwezo wa wagombeaji kutatua matatizo yao badala ya kushawishiwa na umaarufu au misimamo ya vyama.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Wabunge walivyokataa mapendekezo ya muafaka wa Ruto na Raila
WABUNGE wa Bunge la Kitaifa wamekataa marekebisho yaliyopendekezwa na Seneti kuhusu kuhesabu na kupeperusha matokeo ya uchaguzi wa urais kwa njia ya kielektroniki, hatua iliyozua malumbano bungeni. Mapendekezo hayo yalitokana na mazungumzo ya kisiasa kati ya timu za Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, yakilenga kuzuia ucheleweshaji wa kutangaza mshindi wa urais na kuimarisha uwazi katika uchaguzi. Seneti ilikuwa imependekeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itume matokeo ya kila kituo cha kupigia kura ndani ya saa mbili baada ya kutangazwa. Matokeo hayo yangetumwa kwa vituo vya kujumlisha kura vya maeneo bunge, kituo cha kitaifa, wagombeaji, maajenti wao na waangalizi wa uchaguzi. Pia, mapendekezo hayo yalitaka IEBC kuanzisha mfumo wa kurusha moja kwa moja matokeo ya urais yanayotangazwa katika vituo vya kujumlisha kura vya maeneo bunge, ikiwemo kura za Wakenya wanaoishi ughaibuni. Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, alikuwa amependekeza matokeo hayo yaonyeshwe moja kwa moja ili wananchi waweze kuyafuatilia na kuyalinganisha na matokeo ya mwisho. Hata hivyo, wakati wa kujadili Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi 2024 ulioanzia Seneti , Mbunge wa Homa Bay Town Peter Kaluma, akiungwa mkono na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung'wah, alifanikiwa kushawishi Bunge kufuta mapendekezo hayo. Hatua hiyo iliwakasirisha baadhi ya wabunge waliotaka sheria ibadilishwe ili kuondoa utata kuhusu uwasilishaji wa matokeo. Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alihoji kwa nini Bunge lilikuwa likifuta mapendekezo yaliyotokana na mazungumzo ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO). Alisema Kenya haipaswi kusubiri siku saba au nane kutangazwa kwa matokeo ya urais wakati teknolojia inaweza kusaidia kuyawasilisha haraka. Mzozo huo unatokana pia na uamuzi wa Mahakama Kuu wa Aprili 6, 2026, ambapo Jaji Chacha Mwita alitangaza kifungu cha sheria kilichoruhusu matokeo kurushwa moja kwa moja kwa madhumuni ya kuwafahamisha wananchi kuwa kinyume cha Katiba. Mahakama ilisema matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura ndiyo msingi wa matokeo ya mwisho na hayawezi kuchukuliwa kuwa taarifa za kuwafahamisha wananchi pekee. Hata hivyo, Bunge lilisema halijapiga marufuku kupeperushwa kwa matokeo moja kwa moja, bali limehifadhi utaratibu uliopo katika Sheria ya Uchaguzi. Wabunge pia walisema mabadiliko makubwa ya sheria za uchaguzi miezi michache kabla ya uchaguzi wa 2027 yanaweza kukiuka mapendekezo ya ripoti ya Kriegler, iliyotaka sheria hizo zisibadilishwe ndani ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 12 hours ago
Wazee wazidisha juhudi kupatanisha Uhuru na Gachagua
JUHUDI mpya za kuunganisha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP), Rigathi Gachagua, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 zinaendelea kushika kasi, huku jina la Naibu Rais Kithure Kindiki likiibuka katika mpango huo. Hii ni mara ya nne tangu 2022 ambapo viongozi hao wawili, waliokuwa washirika wa karibu kabla ya kuwa mahasimu wa kisiasa, wanashinikizwa kuweka tofauti zao kando ili kuunganisha eneo la Mlima Kenya. Kwa mujibu wa taarifa tulizopata, mkutano wa hivi karibuni ulipangwa kufanyika Jumanne lakini Bw Kenyatta hakupatikana. Mlezi wa kitaifa wa baraza la wazee la Kiama Kia Ma, Bw Kung'u Muigai, alithibitisha kuwa maandalizi ya kuwakutanisha viongozi hao yanaendelea. Alisema wanataka pia Prof Kindiki kuhudhuria ili viongozi wakuu wa eneo hilo wajadili mustakabali wake wa kisiasa. "Tunakaribia kufanikiwa. Tunawaomba muwe na subira," alisema, akiongeza kuwa Bw Kenyatta ndiye atakayetoa tarehe ya mkutano huo. Jaribio la kwanza lilifanyika 2022, wakati Bw Gachagua alipotakiwa kushirikiana na Bw Kenyatta, aliyekuwa rais wakati huo, kuunganisha Mlima Kenya nyuma ya mgombea mmoja wa urais. Hata hivyo, Bw Kenyatta aliunga mkono Raila Odinga wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, huku Bw Gachagua akiwa katika kambi ya William Ruto wa Kenya Kwanza. Bw Gachagua alipuuza wito huo na akaungana na Dkt Ruto kushinda uchaguzi. Aliteuliwa naibu rais lakini akatimuliwa mamlakani Oktoba 2024. Kabla ya kuingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2017, Bw Gachagua alikuwa msaidizi binafsi wa Bw Kenyatta kwa miaka 20. Baadaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Mathira na kupanda hadi wadhifa wa naibu rais. Uhusiano wao ulizorota wakati wa kampeni na zaidi baada ya Bw Gachagua kuwa naibu rais. Aliongoza mashambulizi ya kisiasa dhidi ya biashara za familia ya Kenyatta na miradi yake ya urithi. Mzozo ulifikia kilele wakati shamba la Northlands la familia hiyo, Ruiru, lilipovamiwa, mifugo kuibwa na sehemu ya ardhi kuchomwa moto. Bw Gachagua amewahi kuomba msamaha hadharani kwa familia ya Kenyatta kutokana na matukio hayo, lakini Rais huyo mstaafu hajatoa msimamo wa wazi kuhusu uwezekano wa maridhiano. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Bw Wachira Kiago, alisema juhudi za kuunganisha jamii ni endelevu. Alisema jaribio la pili lilikwama baada ya hisia kali kuibuka pande zote mbili, huku siasa za kumuondoa Bw Gachagua madarakani zikitatiza mazungumzo. Jaribio la tatu lilifanyika baada ya kuondolewa kwake, wakati wazee walipoona haja ya kuzuia wapiga kura wa Mlima Kenya kugawanyika bila mwelekeo wa kisiasa. Hata hivyo, juhudi hizo zilikumbwa na changamoto baada ya Rais Ruto pia kuanzisha mazungumzo ya kumkaribia Bw Kenyatta. Mnamo, Bw Gachagua alipuuza madai kuwa kulikuwa na mkutano uliopangwa kati yake na Bw Kenyatta. Katika mahojiano na KTN, alisema hajapanga wala kuomba mkutano huo, lakini hakufunga mlango wa uwezekano wa kukutana naye iwapo kutakuwa na haja. Kauli hiyo ilijiri licha ya Bw Gachagua kutangaza Julai 11 kuwa analenga kukutana na Bw Kenyatta nyumbani kwake Ichaweri ili kumweleza matokeo ya mashauriano ya karibu miezi miwili aliyofanya katika makazi yake ya Wamunyoro. Alisema pia atatafuta ushauri na baraka zake kuelekea uchaguzi wa 2027. Mchambuzi wa siasa Mixson Gitau alisema wapiga kura wanataka viongozi hao waweke kando majivuno yao na kuungana. Alisema tofauti zao zimezua mpasuko mkubwa miongoni mwa wafuasi wao, huku miungano mipya ikiendeleza mgawanyiko huo. Kwa sasa, Bw Gachagua anaendeleza azma yake ya urais huku akijaribu kushawishi Kalonzo Musyoka na Edwin Sifuna kuungana katika upinzani. Wakati huo huo, anamchukulia Dkt Fred Matiang'i kama mradi wa kisiasa wa Bw Kenyatta unaolenga kudhoofisha ushawishi wake Mlima Kenya. Jina la Prof Kindiki linaongeza uzito katika hesabu hizo. Naibu rais amewahi kumuomba aliyekuwa gavana wa Meru, Kiraitu Murungi, amsaidie kumfikia Bw Kenyatta ili aunganishe jamii. Katika hafla moja ya sekta ya maziwa Meru, Prof Kindiki alimuomba Bw Murungi kumshawishi Bw Kenyatta kusaidia kuunganisha jamii ili isije ikapoteza mwelekeo. Bw Joseph Kaguthi, anayeongoza juhudi za kuwakutanisha wazee, wataalamu na viongozi wa dini, alisema ajenda inayopendekezwa ni kuafikiana kuhusu maslahi ya pamoja, ushirikiano na namna ya kuhakikisha kura za eneo hilo zina umuhimu. Alisema mkutano huo unapaswa kufanyika kabla ya Desemba. Bw Muigai alisema mkutano huo pia utajadili nani atakuwa msemaji wa kisiasa wa Mlima Kenya. Alisema Bw Kenyatta anatambuliwa kama mshauri mkuu wa eneo hilo tangu alipostaafu, lakini sasa wanahitaji msemaji atakayewasilisha msimamo wa jamii. Bw Bernard Njue wa mrengo wa kisiasa wa Kiama Kia Ma alisema Bw Kenyatta na Bw Gachagua lazima wapunguze misimamo yao mikali ili mazungumzo yafanikiwe. Alisema Bw Kenyatta anapaswa kumsamehe Bw Gachagua, huku kiongozi huyo wa DCP akionyesha kuwa anaweza kumshirikisha rais huyo wa zamani katika mipango yake ya kisiasa. "Wote wawili lazima watambue kuwa mgawanyiko wao wa sasa hautunufaishi kama jamii. Wasipoungana, tutawagawanya watu wetu," alisema. Wazee wanasema Mlima Kenya hauwezi kumudu kuingia katika uchaguzi wa 2027 ukiwa umegawanyika. Wanataka viongozi hao wakubaliane kuhusu mwelekeo wa kisiasa ili kura za eneo hilo ziwe na nguvu, badala ya kugawanyika katika makundi yanayoshindana.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Ruto sasa arushia Kalonzo ndoano baada ya kuzomwa mkutano wa Linda Mwananchi
KINARA wa chama cha Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kisiasa huku Rais William Ruto akimshawishi kujiunga na serikali yake, wakati ambao washirika wake katika upinzani wanazidi kuwania tiketi kuuwakilisha katika uchaguzi wa urais wa 2027. Kwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 73, uamuzi wa kuendelea na upinzani au kukubali ushirikiano na Rais Ruto unaweza kuamua hatima ya safari yake ya kisiasa ya takriban miaka 40. Bw Kalonzo amekuwa akitamani kuongoza nchi tangu alipowania urais mara ya kwanza mwaka 2007. Baadaye alijitolea kumuunga mkono marehemu Raila Odinga katika chaguzi za 2013, 2017 na 2022, akiwa mgombeaji mwenza wake katika chaguzi mbili za kwanza. Sasa, baada ya miaka mingi ya kumuunga mkono Raila, anataka nafasi ya kuongoza upinzani katika uchaguzi ujao. Hata hivyo, kuibuka kwa viongozi wapya kama Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na kinara wa Democracy for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua kumechanganya hesabu zake. Bw Kalonzo na washirika wake walitaka suala la mgombeaji urais wa upinzani liamuliwe mapema, lakini Bw Sifuna na Bw Gachagua wanataka uamuzi huo uahirishwe wakisema kumtangaza mgombeaji sasa kunaweza kumpa Rais Ruto nafasi ya kugawanya upinzani. Hali hiyo imemweka Kalonzo kwenye njia panda. Akibaki upinzani, anaweza kukosa tiketi ya urais. Akijiunga na serikali, hakuna hakikisho kwamba atapewa nafasi ya mgombeaji mwenza au wadhifa mwingine mkubwa. Huku mjadala huo ukiendelea, viongozi wa serikali wameongeza juhudi za kumshawishi ajiunge na Rais Ruto. Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot na msaidizi wa Rais Farouk Kibet Jumamosi walimhimiza Bw Kalonzo kuondoka upinzani. Bw Murkomen alisema Kalonzo atakaribishwa serikalini na kwamba uzoefu wake wa kisiasa na kidiplomasia utathaminiwa. Bw Cheruiyot, kwa upande wake, alidai viongozi wa upinzani hawana mpangilio wa kumshinda Rais Ruto mwaka 2027 na kumshauri Kalonzo ajiandae kwa uchaguzi wa 2032. Bw Kibet alisema Kalonzo ataheshimiwa zaidi akijiunga na upande wa serikali. Lakini washirika wa Kalonzo wanapinga madai hayo, wakisema Rais Ruto anamtambua kama tishio kubwa zaidi katika uchaguzi ujao. Seneta wa Kitui Enoch Wambua alisema juhudi za kumshawishi Kalonzo ni ishara kwamba Rais anahofia uwezo wake wa kumshinda katika uchaguzi wa Agosti 10, 2027. Alisema Kalonzo ana ushawishi mkubwa katika eneo la Ukambani, ambalo linaweza kuwa na wapiga kura2.2 milioni, kulingana na makadirio ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Wiper pia imesema haitaruhusu Kalonzo kuvurugwa na juhudi za kumshawishi ajiunge na serikali. Seneta wa Makueni Dan Maanzo alisema chama hicho kitaendelea na azma yake ya kuwania urais, akisema kuwa serikali jumuishi ni meli inayozama ambayo Kalonzo hapaswi kupanda. Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi alisema Kalonzo anataka urais ili kuongoza taifa, na azma hiyo haihusishi kushirikiana na Rais Ruto. Hata hivyo, mchambuzi wa siasa Profesa David Monda anasema Kalonzo anaweza kujiunga na serikali iwapo hatapewa tiketi ya upinzani. Profesa Macharia Munene anasema upinzani unakabiliwa na ushindani wa maslahi binafsi, huku kila kiongozi akitaka kuongoza badala ya kujitolea kumuunga mkono mwingine. Rais Ruto amekuwa akimshawishi Kalonzo kwa muda. Mnamo Mei 2025 alisema alimwendea kwanza baada ya uchaguzi wa 2022 kabla ya kumtafuta Raila, lakini Kalonzo akakataa pendekezo lake. Wiki iliyopita, akiwa Tseikuru, nyumbani kwa Kalonzo, Rais alikosoa upinzani kwa kile alichokitaja kuwa kumdhalilisha kiongozi huyo, akimhimiza ajiunge naye badala ya kukabiliwa na mchujo mwingine wa kisiasa. Hata hivyo, Kalonzo aliwahi kusema mwaka 2023 kuwa kuachana na azma yake ya urais kungeashiria kustaafu siasa. Alisema alikuwa tayari kuwania urais mwaka 2002, 2013 na 2022, lakini alijitolea kuwaunga mkono wengine.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 31 Oct 2026 11:31:10
Msidanganywe, hakuna kafyu huku, polisi waambia wakazi wa Likoni
Polisi wamewahakikishia wakazi wa Likoni, Mombasa, kuwa eneo hilo liko salama na hakuna amri ya kutotoka nje usiku iliyotolewa kufuatia tukio la usalama lililosababisha kifo cha afisa wa kaunti na polisi mmoja kujeruhiwa. Katika taarifa aliyotoa Oktoba 30, 2026, Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Pwani Ali Nuno alisema tukio hilo lilitokea Jumatatu, Oktoba 26, maafisa walipokuwa wakitekeleza majukumu yao. Alifichua kuwa bunduki aina ya AK-47 pia ilipotea wakati wa tukio hilo. Bw Nuno alitaja tukio hilo kuwa la uhalifu na kusisitiza kuwa halimaanishi kuwa Likoni au eneo lote la Mombasa halina usalama. Alisema maafisa wa usalama wameimarisha msako wakilenga kuwakamata waliohusika, kurejesha bunduki iliyopotea na kuhakikisha washukiwa wanafikishwa mahakamani. Akijibu uvumi uliokuwa ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuwekwa kwa amri ya kutotoka nje usiku, kamanda huyo alipuuza madai hayo na kusisitiza kuwa hakuna amri kama hiyo iliyotolewa. 'Hakuna marufuku ya kutembea Likoni. Wananchi wanaofuata sheria hawataathiriwa kwa namna yoyote na operesheni za kiusalama zinazoendelea,' alisema. Aliwataka wakazi kuwa watulivu na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa, akionya kuwa habari za kupotosha zinaweza kuzua hofu isiyohitajika. Pia aliwashauri wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu usalama kupitia matangazo rasmi ya Huduma ya Polisi nchini. Wakati huo huo, idara za usalama zimeimarisha operesheni Likoni na maeneo mengine ya Mombasa ili kuwatambua washukiwa na kurejesha utulivu. Kwa mujibu wa Bw Nuno, operesheni hizo zinalenga kuwakamata waliohusika na tukio hilo, kurejesha bunduki iliyopotea na kuimarisha doria katika maeneo yaliyoathiriwa. Alisema maafisa zaidi wa usalama wamepelekwa katika eneo hilo kulinda maisha na mali ya wakazi. Aliwataka wakazi wa Likoni na Mombasa kuendelea na shughuli zao za kawaida bila hofu, huku wakishirikiana na polisi katika kudumisha amani. Pia aliwahimiza wananchi kutoa taarifa za kuaminika zitakazosaidia uchunguzi na kukamatwa kwa washukiwa. 'Naahidi wakazi wa eneo hili kuwa tutatekeleza wajibu wetu kwa haki, bila upendeleo, kwa uthabiti na kwa kuzingatia ukweli,' akaongeza. Polisi wamesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa jamii na kuwafikisha wahusika wa uhalifu Mahakamani
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 31 Oct 2026 09:39:30
Saudi Arabia yapiga marufuku safari za Wakenya kutokana na Ebola
Saudi Arabia imepiga marufuku raia wake kusafiri Kenya na kusitisha utoaji wa visa kwa wasafiri kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki kufuatia kuthibitishwa kwa ugonjwa wa Ebola, hatua inayoongeza wasiwasi kuhusu athari za kimataifa za ugonjwa huo. Hatua hiyo iliyotangazwa Ijumaa, Oktoba 30, inajumuisha pia kuwazuia wasafiri waliotembelea Kenya katika siku 21 zilizotangulia kuingia katika taifa hilo la Mashariki ya Kati. Saudi Arabia imejiunga na El Salvador ambayo tayari imezuia wasafiri kutoka Kenya na mataifa mengine saba ya Afrika. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA), marufuku hiyo inalenga kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo katika taifa hilo. Mamlaka ya afya ya Saudi Arabia, Weqaya, imesema hali ya afya nchini humo ni shwari na inaendelea kufuatiliwa. Hatua hizo zimeibua hofu kuhusu athari zinazoweza kukumba Kenya katika sekta za utalii, biashara na usafiri wa kimataifa. El Salvador ilitangaza kuwa wasafiri waliotoka au kupitia Kenya, Angola, Burundi, Ethiopia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Uganda hawataruhusiwa kuingia nchini humo. Mwanahabari wa CNN Larry Madowo hivi majuzi alifichua kuwa ombi lake la kupata kibali maalumu cha kuingia El Salvador lilikataliwa kutokana na maagizo hayo. Nchi nyingine zimechagua kuimarisha ukaguzi wa afya badala ya kupiga marufuku wasafiri. Korea Kusini iliiongeza Kenya katika orodha ya mataifa ambayo wasafiri wake wanahitaji kufanyiwa uchunguzi mkali wa afya kuanzia Oktoba 20. Wasafiri kutoka Kenya wanatakiwa kutoa taarifa kuhusu hali yao ya afya na wanaweza kufuatiliwa kwa siku 21, ambazo ni kipindi cha kupevuka kwa virusi vya Ebola. Amerika pia iliwaonya raia wake kufikiria upya mipango ya kusafiri Kenya, huku ikiimarisha ukaguzi wa wasafiri kutoka eneo hili. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya dhidi ya mataifa kufunga mipaka au kuzuia biashara kutokana na mlipuko huo. Katika taarifa ya Oktoba 23, WHO ilisema inapendekeza mataifa kuimarisha ushirikiano, ufuatiliaji wa afya, upimaji na kuwafuatilia watu waliokutana na wagonjwa badala ya kuweka vizuizi vya safari. Kenya ilirekodi kisa chake cha kwanza cha Ebola aina ya Bundibugyo baada ya mwanaume aliyekuwa amesafiri kutoka DRC kupitia Uganda kufariki Oktoba 5. Kufikia Oktoba 30, visa tisa vilikuwa vimethibitishwa na watu wawili kufariki. Wagonjwa wengine walikuwa jamaa wa mwathiriwa wa kwanza na wahudumu wa afya waliomhudumia. Katibu katika Idara ya Afya ya Umma, Mary Muthoni, alisema Kenya ilikuwa imepita siku 10 bila kuripoti maambukizi mapya. Alisema serikali ilikuwa imeimarisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo kwa kushirikiana na serikali za kaunti na washirika wa maendeleo. Wizara ya Afya pia ilisema watu waliokuwa wamekutana na wagonjwa na kukamilisha siku 21 za ufuatiliaji bila kuonyesha dalili waliachiliwa hatua kwa hatua. Wengine wanatarajiwa kukamilisha ufuatiliaji kufikia Novemba 11. Ebola ni ugonjwa hatari unaosambazwa kwa kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa. Dalili zake ni pamoja na homa, kutapika na kuharisha, huku wagonjwa mahututi wakikumbwa na kutokwa damu ndani au nje ya mwili.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 31 Oct 2026 08:43:44
Watu sita wafariki katika ajali ya matatu katika barabara ya Nakuru-Eldoret
Watu sita, akiwemo dereva wa matatu, walifariki dunia baada ya magari matatu kugongana katika eneo la Koriomat, kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret. Ajali hiyo iliyotokea usiku wa manane ilihusisha lori aina ya Mercedes-Benz Actros, gari aina ya Toyota Succeed na matatu aina ya Toyota Hiace ya kampuni ya North Rift Sacco iliyokuwa na abiria 10. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Wilberforce Sichirani, alisema lori hilo lilikuwa likitoka Nakuru kuelekea Eldoret lilipokwepa gari jingine lililokuwa mbele yake. Katika kufanya hivyo, dereva wa lori alikata kona kuelekea upande wa kulia na kugonga Toyota Succeed kabla ya kugonga matatu hiyo. Nguvu za mgongano huo zilisababisha matatu na Toyota Succeed kutumbukia kwenye mtaro uliokuwa upande wa kulia wa barabara. Bw Sichirani alisema dereva wa matatu, aliyetambuliwa kama Shabaan Hassan Wanga, na abiria watano wa kike walifariki papo hapo. Abiria wengine ambao idadi yao haijabainishwa walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika hospitali mbalimbali za Kaunti ya Uasin Gishu kwa matibabu. Miili ya waliofariki ilipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret, kusubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti. "Tumeanzisha uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ajali hii ya kusikitisha," alisema Bw Sichirani. Polisi wanaendelea kutambua waathiriwa wengine na idadi kamili ya waliojeruhiwa. Mabaki ya magari yaliyohusika katika ajali hiyo yanatarajiwa kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Burnt Forest kwa ukaguzi. Ajali hiyo inaongeza idadi ya watu wanaopoteza maisha katika ajali za barabarani nchini, huku mamlaka zikiendelea kuonya kuhusu hatari zinazotokana na makosa ya madereva. Baadhi ya sababu zinazochangia ajali hizo ni pamoja na kupita magari mengine bila tahadhari, mwendo wa kasi na madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 31 Oct 2026 07:55:43
UN yaomba Sh1.16b kusaidia Waethiopia 50,000 wanaokimbilia Kenya
MASHIRIKA ya Umoja wa Mataifa yanaomba Sh1.16 bilioni kusaidia takriban watu zaidi ya 50,000 waliokimbilia Kenya kufuatia mapigano katika nchi jirani ya Ethiopia. Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Kenya, Fatima Mohammed-Cole, alisema wanashirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na UNICEF kutafuta fedha za kuwahudumia wakimbizi hao kwa miezi mitatu ijayo. Alisema fedha hizo zitatumika kununua chakula, makazi, maji na vifaa vya usafi, pamoja na kusajili na kulinda wakimbizi. UNHCR pia inakusanya vifaa vya dharura, ikiwemo mahitaji ya nyumbani na vifaa vya kujenga makazi ya muda kwa takriban watu 12,000. Wakati huo huo, wakimbizi zaidi waliendelea kuwasili mjini Moyale huku milio ya risasi ikisikika upande wa Ethiopia. Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo la Upper Eastern, Malik Adan, alisema hali ilitulia kiasi Ijumaa alasiri, ingawa milio ya risasi ilikuwa imesikika asubuhi. Alisema kambi kubwa iliyohamishwa kutoka mjini ina takriban watu 5,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Shirika la Msalaba Mwekundu liliripoti pia kuzaliwa kwa mtoto wa kwanza wa mama mkimbizi katika hospitali moja ya eneo hilo Ijumaa. Kwa upande wake, IOM ilisema serikali ya Kenya na mashirika ya kibinadamu yanaandaa mpango wa kusaidia hadi watu 80,000 iwapo idadi ya wanaowasili itaongezeka. Mkuu wa IOM nchini Kenya, Nomagugu Ncube, alisema maelfu ya watu wamevuka mpaka kutafuta usalama na wengi wanahifadhiwa na jamii za wenyeji. Alisema mahitaji ya dharura yanajumuisha makazi, vifaa vya nyumbani, matangi ya maji na vidonge vya kusafisha maji. Ncube aliongeza kuwa mashirika hayo yataendelea kutathmini hali na kufuatilia idadi ya wakimbizi ili kuhakikisha wanaohitaji msaada wanapata huduma.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 31 Oct 2026 06:55:45
Kaunti 47 zinatarajiwa kupata Sh457.28 bilioni katika mgao mpya
KAUNTI 47 zinatarajiwa kupata Sh457.28 bilioni kama mgao wa mapato ya kitaifa katika mwaka wa kifedha wa 2027/2028, ikiwa pendekezo la Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) litapitishwa. Kiasi hicho ni ongezeko la Sh29.28 bilioni ikilinganishwa na Sh428 bilioni ambazo kaunti zilitengewa katika mwaka huu wa kifedha utakaokamilika Juni 30, 2027. CRA, inayoongozwa na Bi Mary Chebukati, inapendekeza Wizara ya Fedha itengee serikali za kaunti fedha hizo katika mwaka unaoanza Julai 2027 na kukamilika Juni 2028. Akizungumza na wanahabari Alhamisi, Bi Chebukati alisema pendekezo hilo linatokana na makadirio ya mapato ya kitaifa ya Sh3.24 trilioni yatakayogawanywa kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti. Kati ya fedha hizo, serikali ya kitaifa inapendekezwa kupata Sh2.78 trilioni, huku kaunti zikitengewa Sh457.28 bilioni. Zaidi ya hayo, Sh10.25 bilioni zinapendekezwa kutolewa kupitia Hazina ya Usawazishaji. Bi Chebukati alisema ongezeko hilo litasaidia kulipia mishahara ya wahudumu wa afya wanaotekeleza mpango wa afya kwa wote (UHC), pamoja na nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali na wafanyakazi wa umma katika awamu ya nne ya mapendekezo ya Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC). Fedha hizo pia zinalenga kutekeleza makubaliano ya mishahara na marupurupu ya wauguzi, na kuongeza kwa asilimia tatu uwezo wa kaunti kutoa huduma kwa wananchi. "Pendekezo hili linalenga kusawazisha mahitaji ya kifedha ya ngazi zote mbili za serikali, kuhakikisha matumizi endelevu, kulipa madeni ya umma na kudumisha utoaji wa huduma kwa Wakenya," alisema. Alisema mgao unaopendekezwa kwa kaunti ni sawa na asilimia 22.3 ya mapato ya kitaifa yaliyokaguliwa na kuidhinishwa hivi majuzi. Kiwango hicho ni zaidi ya kiwango cha chini cha asilimia 15 kinachotakiwa na Katiba. Hata hivyo, pendekezo hilo linatolewa wakati ambapo Baraza la Magavana (CoG) linalalamikia kuchelewa kwa serikali ya kitaifa kutoa Sh8.9 bilioni zilizotengwa kulipia mishahara ya wahudumu wa mpango wa UHC walioajiriwa na kaunti kwa masharti ya kudumu na pensheni. Mwenyekiti wa CoG, Muthomi Njuki, alisema kaunti zimelazimika kutafuta fedha kutoka kwa vyanzo vingine ili kuwalipa wafanyakazi hao. Gavana huyo wa Tharaka Nithi alisema kaunti zimekuwa zikilipa wahudumu hao kwa miezi minne bila kupokea fedha ambazo serikali ya kitaifa iliahidi kutoa. Serikali ya kitaifa kupitia Wizara ya Afya na serikali za kaunti zilikubaliana kuwa wahudumu hao wataajiriwa na kaunti, huku fedha za kugharamia mishahara yao zikifuata kupitia mgao wa ziada kwa serikali za kaunti. Hata hivyo, Bw Njuki alisema fedha hizo bado ziko katika wizara ya fedha kwa sababu taratibu zinazohitajika ili kuzitoa hazijakamilishwa katika Seneti. "Fedha zilizopaswa kutengewa kaunti bado ziko wizara ya fedha kwa sababu taratibu zinazohitajika kuzitoa hazijashughulikiwa katika Seneti," alisema. Alitaka fedha hizo zitolewe mara moja, akionya kuwa kucheleweshwa zaidi kunaweza kudhoofisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Wakati huo huo, CRA imependekeza kuongeza kiwango cha matumizi ya kawaida ya mabunge ya kaunti hadi Sh50.36 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2027/2028, kutoka Sh39.19 bilioni za sasa. Hilo ni ongezeko la Sh11.17 bilioni, ambalo linalenga kugharamia mishahara ya madiwani (MCAs), shughuli za kawaida, magari, mafunzo na ajira za ziada. Kati ya fedha hizo, Sh3.54 bilioni zitatumika kulipa mishahara na marupurupu ya wafanyakazi, Sh1.74 bilioni kwa shughuli na ukarabati, Sh4.81 bilioni kwa magari, Sh474 milioni kwa mafunzo na Sh597 milioni kutekeleza mfumo mpya wa ajira. Kwa upande wa serikali kuu za kaunti, CRA imependekeza matumizi ya kawaida ya Sh25.85 bilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh602 milioni pekee.
read moreRight Column Content