T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 13 Oct 2026 03:55:17

Ebola: Pigo kampuni ya meli ikisitisha ajira kwa Wakenya

SEKTA ya meli za kitalii za kimataifa imepata pigo nchini kutokana na kisa cha kwanza cha Ebola nchini, huku kampuni ya MSC Cruises ikisitisha kuajiri mabaharia Wakenya kwenye meli zake. MSC Cruises, ambayo huajiri mamia ya Wakenya kwenye meli zake, imesema hatua hiyo ya muda itadumu hadi Oktoba 31, ikitaja hali ya hivi karibuni ya afya ya umma nchini. Katika ujumbe kwa wafanyakazi walioathiriwa, kampuni hiyo ya usafiri wa meli za kitalii,  ilisema uamuzi huo ni wa tahadhari huku ikiendelea kufuatilia na kutathmini hali ilivyo. Kampuni hiyo iliomba radhi kwa kutoa taarifa hiyo katika muda mfupi, lakini ikawahakikishia wafanyakazi walioathiriwa kuwa uamuzi huo hautaathiri ajira zao, mikataba yao ya kazi wala fursa zao za baadaye katika kampuni hiyo. Ilisema wafanyakazi ambao mipango yao ya kusafiri imeahirishwa watapewa kipaumbele katika kupanga upya safari zao kuanzia Novemba 1, isipokuwa kama kutakuwa na matukio mengine yatakayohitaji hatua za ziada. Ingawa MSC Cruises haikutaja Ebola moja kwa moja katika taarifa yake,  hatua hiyo imezua maswali kuhusu uwezekano wa waajiri wengine wa kimataifa kuchukua hatua kama hizo za tahadhari na athari zake kwa Wakenya wanaotafuta ajira nje ya nchi. Mwezi Julai, baadhi ya wafanyakazi Wakenya pia walikwama baada ya kampuni hiyo ya meli za kitalii kuahirisha safari za wafanyakazi kutoka Kenya, ingawa hakuna kisa cha Ebola kilichokuwa kimeripotiwa wakati huo. "Tafadhali fahamuni kuwa kutokana na mlipuko wa Ebola, usimamizi umeamua kuahirisha kuingia kwa wafanyakazi kutoka Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda kwenye meli hadi pale itakapotangazwa vinginevyo," barua pepe kutoka kwa kampuni hiyo ya meli za kitalii ilisema. Duru zilisema baadhi ya wafanyakazi kutoka Diani na Mombasa waliokuwa wanatarajiwa kuabiri meli ya kampuni hiyo walikwama. Mchambuzi wa masuala ya utalii, Bw Mohamed Hersi,  alisema sekta hiyo haijapokea ripoti za watalii waliokatiza safari zao nchini kwa sababu ya Ebola. Hata hivyo, alionya kuwa hali inaweza kubadilika iwapo nchi ambazo Kenya hutegemea sana kwa utalii zitatangaza masharti makali zaidi ya ushauri wa usafiri. "Hatujapokea taarifa za safari zozote zilizoghairiwa. Yote yatategemea ushauri wa usafiri, hasa kutoka kwa serikali za Uingereza, Marekani na Milki za Kiarabu (UAE)," alisema Bw Hersi, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Pollman's Tours and Safaris. Bw Hersi alieleza matumaini kuwa Kenya itaepuka ushauri mkali wa usafiri kwa kuwa kisa cha Ebola kilichoripotiwa kilitoka nje ya nchi na maafisa wa afya wamechukua hatua za kudhibiti hatari. Kwa upande wake, meneja wa kampuni ya Africa Last Minute Ltd, Bw Abraham Guyo, alionya kuwa kisa hicho kinaweza kudhoofisha imani ya wageni kwa Kenya kama kivutio cha watalii, hasa iwapo wasiwasi wa kimataifa utaongezeka. Wizara ya Afya ilithibitisha kisa cha kwanza nchini Kenya cha ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo mnamo Oktoba 6. Mgonjwa huyo, aliyekuwa amesafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia Uganda hadi Nairobi, baadaye alifariki na kuzikwa kwa kuzingatia taratibu za afya ya umma. Serikali imesisitiza kuwa kisa hicho kilitoka nje ya nchi na imewataka Wakenya kuwa watulivu, kufuata mwongozo rasmi wa afya na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa. Serikali imesema inaongeza ufuatiliaji wa magonjwa na kuimarisha hatua nyingine za afya ya umma ili kuzuia maambukizi zaidi.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Waendesha boda boda 300 wapata mafunzo ya usimamizi wa fedha Namanga

Takriban  waendesha boda boda 300 katika mji wa Namanga, Kaunti ya Kajiado, wamepata mafunzo ya usimamizi wa fedha ili kuwasaidia kupanga mapato yao, kulipa mikopo kwa wakati na kuimarisha biashara zao. Mafunzo hayo yaliandaliwa na kampuni ya ufadhili wa mali ya Mogo, yakilenga kuwapa waendeshaji ujuzi wa kukopa kwa uwajibikaji, kuweka akiba na kupanga bajeti kulingana na mapato yao. Washiriki walifundishwa mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua mkopo, kuelewa viwango vya riba na masharti ya ulipaji, kutimiza makataa ya malipo na kutafuta suluhu zinazofaa wanapokumbwa na changamoto za kifedha. Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma katika Mogo, Becky Ngigi, alisema kupata mkopo pekee hakutoshi bila kuwa na maarifa ya kusimamia fedha. "Upatikanaji wa fedha pekee hautoshi. Watu wanahitaji pia maarifa na ujuzi wa kufanya maamuzi mazuri ya kifedha," alisema. Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwapa waendeshaji zana za kusimamia mapato, kutimiza wajibu wa mikopo na kukuza biashara zao kwa njia endelevu. Mwenyekiti wa waendesha boda boda Kaunti ya Kajiado, Alex Gitari, alisema uelewa wa fedha ni muhimu kwa waendeshaji wanaotegemea mikopo kununua pikipiki na kupanua biashara zao. Alisema waendeshaji wanapaswa kupanga mapato yao kwa kuzingatia gharama za uendeshaji, mahitaji ya familia na malipo ya mikopo. Mafunzo hayo yanakuja wakati Kenya ikikabiliwa na changamoto ya kuhakikisha kuwa wananchi wanaopata huduma za kifedha wanazitumia kuboresha maisha yao. Mkakati wa Kitaifa wa Ujumuishaji wa Kifedha wa 2025–2028 unaonyesha kuwa asilimia 84.8 ya watu wazima nchini walipata huduma rasmi za kifedha mwaka 2024, lakini ni asilimia 18.3 pekee waliokuwa na afya nzuri ya kifedha. Sekta ya boda boda inakadiriwa kuzalisha Sh660 bilioni kila mwaka na kusaidia zaidi ya watu milioni 2.5 kupata riziki, kulingana na ripoti ya Viffa Consult kuhusu ukuaji wa sekta hiyo. Mogo imesema itaendelea kuunga mkono mipango inayohamasisha ukopaji wa uwajibikaji, usimamizi bora wa fedha na ukuaji endelevu wa biashara.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 12 hours ago

Wazee sasa kusaidia familia kutatua mizozo ya urithi

FAMILIA  katika eneo la North Rift zimehimizwa kuacha mizozo ya urithi inayodumu kwa miaka mingi na badala yake kutumia upatanishi kutatua tofauti zao kuhusu mali ya wazazi wao. Mahakama imeanza kushirikiana na wazee wa jamii kusaidia familia hizo kufikia makubaliano, kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani na kuwezesha familia kupata mali waliyorithi kwa haraka. Zaidi ya viongozi 60 wa jamii kutoka Baraza la Wazee wa Kalenjin wameidhinishwa na Idara ya Mahakama kuendeleza Mfumo Mbadala wa Kutatua Mizozo (AJS). Wazee hao wanaripotiwa kutatua zaidi ya mizozo 1,200 kupitia upatanishi katika mwaka uliopita, mingi ikihusu migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu. Jaji Charles Yano wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Eldoret alisema kesi za urithi ni miongoni mwa sababu zinazochangia mrundiko wa kesi katika eneo hilo. Akizungumza Jumatatu wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya AJS, jaji huyo alizitaka familia kutumia upatanishi badala ya kusubiri kesi mahakamani kwa miongo kadhaa. "Ninaomba familia kukumbatia mfumo huu na upatanishi unaofanyika kwa ushirikiano na mahakama katika masuala ya urithi, badala ya taratibu za mahakama zinazoweza kuchukua miongo kadhaa," alisema. Aliongeza kuwa kesi za muda mrefu hugharimu familia pesa, huzidisha migawanyiko na kuwanyima warithi fursa ya kufurahia mali yao. Baadhi ya mizozo mikubwa ya urithi inayotajwa katika eneo hilo inahusu mali za mwanasiasa na mkulima mashuhuri Jackson Kibor na John Kiplagat Kibogy. Watoto wao wamekuwa wakizozana mahakamani kwa zaidi ya miaka 10 kuhusu mali inayokadiriwa kuzidi Sh15 bilioni. Chama cha Wanasheria nchini (LSK), tawi la North Rift, kinaunga mkono juhudi hizo na kuendesha kampeni za kuhamasisha wazee, viongozi wa dini na wadau wengine kuhusu umuhimu wa upatanishi. Mwenyekiti wa tawi hilo, Oscar Oduor, alisema mfumo huo unaweza kusaidia familia kutatua mizozo ya urithi kwa kufuata sheria. Mwenyekiti wa upatanishi Uasin Gishu, wakili Daniel Tariko, alisema makubaliano yanayofikiwa kupitia upatanishi unaohusishwa na mahakama yanaweza kupitishwa na mahakama kuwa amri rasmi. Hatua hiyo inaweza kufungua njia kwa warithi kupata mali yao kwa mujibu wa sheria. Kwa familia zinazokumbwa na mizozo, ujumbe ni kutafuta suluhu mapema kabla ya kesi ndefu kuzidisha uhasama na kuchelewesha ugavi wa urithi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Uchungu wa familia iliyopoteza jamaa wanne ajalini

FAMILIA katika eneo la Rabai, Kaunti ya Kilifi yaomboleza jamaa wao wanne waliofariki kwenye ajali iliyotokea Jumapili eneo la Kanga lililo Mtito Andei, kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa. Kwenye mahojiano Jumatatu, Bw Mwatsuya Mutsunga alishindwa kuzuia machozi akieleza kuhusu msiba uliokumba familia yake. "Nianze kumwomboleza nani?" aliuliza kwa sauti ya chini iliyotetemeka kwa huzuni. "Mwanangu? Kaka yangu mkubwa? Mke wake? Au mwana wao pia ni damu yangu? Mtu anaanzaje kuomboleza watu wengi namna hii? Na baada ya machozi kukauka, nitawaambia nini waliosalia kama mzee wa familia hii?" aliuliza. Familia yake ni miongoni mwa zilizoathiriwa zaidi na mkasa huo ambao umegusa eneo la Pwani na kitaifa. Basi lililokuwa limebeba karibu abiria 50, wakiwemo zaidi ya wachungaji na waumini 12, liligongana ana kwa ana na lori kubwa la mizigo walipokuwa wakirejea Mombasa kutoka mazishi yaliyofanyika Lugari, Kaunti ya Kakamega. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 24. Miongoni mwa waliofariki ni kaka mkubwa wa Bw Mutsunga, Dkt Patrick Mutsunga; mkewe, Younitta Mutsunga; mtoto wao, Ndune Mutsunga; na mwanawe Mutsunga, Moses Mwadzuya. Bw Mutsunga, alisema jioni ya Jumapili ilikuwa ya uchungu kwake huku taarifa za vifo hivyo zikimfikia moja baada ya nyingine. "Nilipigiwa simu ya kwanza saa moja usiku hivi. Mwanzoni tuliambiwa kuwa kaka yangu mkubwa alikuwa amefariki papo hapo, huku mkewe akifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja Kaunti ya Makueni. Wengine wawili walikuwa bado hawajatambuliwa," alikumbuka. Kabla familia haijapata muda wa kukubali taarifa hizo za kwanza, naibu chifu wa eneo hilo alifika na habari nyingine za kusikitisha kwamba miili ya Ndune na Moses pia ilikuwa imetambuliwa katika eneo la ajali. "Tulivunjika moyo kabisa. Mwezi mmoja tu uliopita, mwanangu Moses aliondoka kijijini na kwenda Mombasa kumsaidia mkewe kutafuta matibabu. Sasa hayupo tena, akiwa ameacha mjane na watoto watatu wanaosoma," akasema. Kaka yake mkubwa, Dkt Patrick, alikuwa nguzo muhimu ya familia. Akiwa mtaalamu wa afya aliyestaafu, aliendesha zahanati ya kibinafsi na shule ya kibinafsi katika Kaunti ya Kwale pamoja na mkewe, Younitta. "Alinipigia simu Jumatano iliyopita kunijulisha kuhusu safari ya kumzika shemeji yake, Askofu Isaiah Giganene," alisema Bw Mutsunga. Alisema alimtakia safari njema. "Sikuwahi kufikiria kwamba hiyo ingekuwa mara ya mwisho kusikia sauti yake. Sasa nimeachiwa jukumu kubwa la kuwatunza wale aliowaacha," aliongeza. Habari za msiba zilipoenea Rabai, wanakijiji waliacha shughuli zao za kila siku na kusaidia kuweka mahema na kukaa pamoja na mzee huyo wa familia aliyekuwa akiomboleza. Waombolezaji walizunguka kutoka hema moja hadi jingine kuwafariji ndugu wa marehemu. Bw Tsuma Kanyonge, mzee wa familia, alisema kupoteza jamaa wanne katika ajali moja ilikuwa pigo kubwa kwa familia na jamii nzima. "Fikiria kupoteza tawi zima la familia kwa wakati mmoja. Tutaendeleaje na maisha?" aliuliza Bw Kanyonge. Alisema walikuwa wamesikia kupitia redio za eneo hilo kwamba kulikuwa na ajali ya magari kugongana ana kwa ana kwenye barabara kuu, lakini hawakujua kuwa jamaa zao walikuwa miongoni mwa waliokuwa ndani ya basi hilo. "Hili ni pigo kubwa, na tunamwomba Rais William Ruto kuingilia kati na kuwasaidia watoto hawa wadogo na wajane," alisema. Msiba huo umeibua tena malalamishi kuhusu hali ya usalama barabarani inayozidi kuzorota katika barabara ya Mombasa–Nairobi. Haya yanajiri wiki chache tu baada ya ajali iliyotokea Salama Oktoba 4 na kusababisha vifo vya mahujaji 17 wa Kanisa Katoliki. "Wiki mbili zilizopita tulipoteza mahujaji 17, na leo tunaomboleza wengine 23. Hali hii itaendelea hadi lini?" aliuliza Bw Kanyonge. Alizitaka mamlaka husika kuwakamata wamiliki wa magari yasiyofaa kutumika barabarani yaliyohusika katika ajali hizo, na kutambua pamoja na kuweka alama katika maeneo yote hatari kwenye barabara hiyo ili kulinda maisha ya watu. Mbunge wa eneo hilo, Bw Kenga Mupe, aliingilia kati Jumatatu asubuhi na kushirikiana na utawala wa eneo hilo kupanga usafirishaji wa miili ya watu hao wanne kutoka Makueni hadi chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Pandya Memorial mjini Mombasa, huku maandalizi ya mazishi yakianza.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Mama akamatwa kwa kuzuia mwanawe kufanya mtihani, adai nambari '666'ni ya kishetani

MAMA mmoja mwenye umri wa miaka 38 amekamatwa kaunti ya Mombasa baada ya kumfungia binti yake nyumbani na kumzuia kufanya mtihani wa kitaifa wa KPSEA kwa madai kuwa nambari yake ya mtihani ilikuwa na tarakimu za kishetani, 666. Mama huyo wa watoto watano alikamatwa Jumanne baada ya mwanawe kukosa kufika katika kituo cha mtihani cha shule ya msingi ya  Kwa Jomvu. Alidai kuwa uamuzi wake ulitokana na maagizo aliyopokea kutoka kwa Mungu. "Mimi ni mtu ninayemcha Mungu, mtumishi wake na mhubiri. Nilizungumza na Mungu, akanionyesha kuwa nambari ya mtihani wa binti yangu haikuwa sahihi," alisema akiwa katika Kituo cha Polisi cha Jomvu. Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bakari Mwerephe, alisema mwanafunzi huyo alikuwa amefanya mtihani wa siku ya kwanza Jumatatu, lakini mama yake akampigia simu akisema hataruhusiwa kuendelea na mitihani kwa sababu ya nambari hiyo. Shangazi wa msichana huyo aliarifu polisi na maafisa wa Idara ya Watoto, ambao walifika nyumbani saa tatu na nusu asubuhi na kumuokoa mwanafunzi huyo akiwa amevalia sare za shule. Alisindikizwa hadi kituoni na kuruhusiwa kufanya mtihani. Kamanda wa Polisi wa Jomvu, Selina Chirchir, alisema maafisa waliingilia kati ili kuhakikisha haki ya mtoto ya kupata elimu inalindwa. Binamu wa mama huyo, Juliet Ndewa, alisema familia imekuwa ikipambana na kile ilichokitaja kuwa msimamo mkali wa kidini unaoathiri watoto. Mwezi mmoja uliopita, mama huyo alikuwa ameitwa na maafisa wa watoto baada ya kuripotiwa kuwazuia watoto wake kwenda shule na kutafuta matibabu wanapougua. Mama huyo anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa afya ya akili na kuhojiwa zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazohusiana na kupuuza malezi na  haki ya mtoto kupata elimu. Katika habari nyingine, wanafunzi watatu wa kike wanafanya mitihani ya KJSEA hospitalini kaunti ya Bomet. Wawili walijifungua siku ya kwanza ya mitihani, huku mwingine akifanya mtihani katika Hospitali ya Tenwek baada ya kujifungua. Huko Nakuru, watahiniwa 27 ambao majina yao hayakuwa kwenye orodha rasmi waliruhusiwa kufanya mitihani maafisa wa Baraza la Mitihani la Kitaifa (KNEC) walipoingilia kati. Walijumuisha watahiniwa 11 wa KPSEA na 16 wa KJSEA. Hata hivyo, mwanafunzi mmoja wa KJSEA katika Shule ya Kionduso PAG, Kisii, alikosa mtihani baada ya kubainika kuwa hakuwa amesajiliwa. Babake, Dickson Asiago, alitaka Wizara ya Elimu ichukue hatua dhidi ya waliohusika. Wakati huohuo, usalama umeimarishwa katika maeneo yanayokumbwa na ujangili katika kaunti za Samburu, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi, Turkana na Baringo ili kuhakikisha watahiniwa wanafanya mitihani bila hofu. KPSEA inatarajiwa kukamilika kesho, huku mitihani ya KJSEA ikiendelea hadi Ijumaa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

Vita kati ya magavana na Ruto kuhusu maendeleo vyatishia ugatuzi

MVUTANO kati ya Rais William Ruto na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kuhusu nani anastahili sifa za miradi ya maendeleo umeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa ugatuzi, huku viongozi wakishindana kudhibiti na kumiliki kisiasa miradi inayolenga kuwahudumia wananchi. Wiki iliyopita, Bw Natembeya alimlaumu Rais kwa kujipa sifa za miradi inayofadhiliwa na serikali ya kaunti, ikiwemo Soko la Masinde Muliro mjini Kitale. Gavana huyo alisema serikali ya kaunti, kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, ilitumia zaidi ya Sh800 milioni kujenga soko hilo, huku serikali ya kitaifa ikichangia Sh56 milioni kukamilisha kazi zilizobaki. Pia alipinga ujenzi wa hospitali ya thamani ya Sh1 bilioni, akisema hakushirikishwa kabla ya mradi huo kuanzishwa. Rais, aliyezindua ujenzi wa hospitali hiyo yenye vitanda 300, alimshutumu gavana kwa kuzuia maendeleo ya huduma muhimu za afya. Hata hivyo, wataalamu wanasema mzozo huo ni sehemu ya vita pana kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuhusu ufadhili, utekelezaji na sifa za miradi. Wakili Ekuru Aukot, aliyeshiriki kuandaa Katiba ya 2010, alisema Ibara ya 6(2) inaeleza kuwa serikali za kitaifa na kaunti ni tofauti lakini zinategemeana, na zinapaswa kushirikiana kupitia mashauriano. Mtaalamu wa utawala Peter Mbae alionya kuwa mashindano hayo yanatishia kudhoofisha ugatuzi na utawala bora. Alisema miradi ya maendeleo ni ya wananchi, wala si viongozi wanaotaka kujipatia umaarufu wa kisiasa. Wakili Steve Kabita pia alisema hakuna serikali inayopaswa kudai kumiliki au kujipa sifa za mradi uliotekelezwa na upande mwingine. Mvutano huo umeenea hadi sekta ya barabara, ambapo magavana wanataka angalau asilimia 15 ya fedha za hazinaya  ukarabati wa barabara, huku wengine wakitaka asilimia 42, zitengewe kaunti. Bunge la Kitaifa limependekeza asilimia tano pekee. Magavana pia wamepinga utekelezaji wa mpango wa maeneo ya viwanda katika kaunti, wakisema baadhi ya miradi ilianzishwa bila mashauriano ya kutosha na kabla ya masuala ya umiliki wa ardhi kutatuliwa. Wakati huo huo, serikali ya kitaifa imehusisha Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kukamilisha miradi iliyokwama, ikiwemo hospitali na viwanja vya michezo. Baadhi ya magavana wanahofia kuwa Rais atajipatia sifa za miradi hiyo baada ya kukamilika. Hata hivyo, viongozi wanaounga mkono ushirikiano wanasema serikali zote mbili zina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma. Aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa alisema Katiba inazitaka serikali hizo kushirikiana kwa manufaa ya wananchi. Mzozo huo unaendelea kuibua maswali kuhusu mipaka ya majukumu ya serikali hizo mbili, hasa pale miradi inapohusisha fedha za pamoja. Huku  nchi ikielekea uchaguzi mkuu wa 2027, wataalamu wanaonya kuwa ushindani wa kisiasa haupaswi kuchelewesha huduma wala kufuta mafanikio ya ugatuzi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Bunge lakataa masharti magumu ya kuwaondoa wabunge madarakani

JARIBIO la baadhi ya wabunge kutaka masharti magumu ya kuwaondoa mamlakani wabunge kupitia kura ya wananchi limefeli Bungeni wakati wa kujadili Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi wa 2024. Mbunge wa Suba North Millie Odhiambo aliongoza juhudi za kutaka mbunge aondolewe mamlakani baada ya kupatikana na hatia ya kosa kubwa la jinai, kuhukumiwa na kufungwa jela kwa angalau miezi sita. Alisema masharti yaliyopendekezwa na Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria yalikuwa rahisi mno na yanaweza kutumiwa vibaya kisiasa. Kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati hiyo, hatua ya kumuondoa mbunge  ingeanzishwa baada ya thuluthi moja ya wapiga kura waliosajiliwa katika kila wadi ya eneo bunge husika kutia saini ombi hilo. Kwa seneta, thuluthi moja ya wapiga kura katika kila eneo bunge la kaunti ingehitajika. Hata hivyo, uchaguzi mdogo ungeamuliwa kwa kura nyingi zaidi, huku mchakato wa kumwuondoa mbunge ukiruhusiwa kuanzishwa baada ya miaka miwili tangu kuchaguliwa kwake. "Hata kama nitasimama peke yangu, nitasimamia ukweli wangu. Ninapinga marekebisho haya kwa sababu kiwango mnachopendekeza ni cha chini mno," alisema Bi Odhiambo. Mbunge wa Saku, Dido Raso aliunga mkono msimamo huo, akionya kuwa kupata saini za thuluthi moja ya wapiga kura katika kila wadi kunaweza kuwa rahisi na kusababisha mchakato huo kutumiwa vibaya. Lakini Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung'wah na mwenzake wa Wachache Junet Mohamed walipinga masharti magumu, wakisema wananchi hawapaswi kuzuiwa kutumia haki yao ya kuwaondoa viongozi wasiowaridhia. Ichung'wah alisema kuweka kiwango cha asilimia 50 katika kila wadi kungeweza kurudia makosa yaliyofanya mahakama kufutilia mbali sheria za awali. Ibara ya 104 ya Katiba, inaitaka Bunge kuweka sheria zinazoeleza sababu na utaratibu wa kuwaondoa wabunge madarakani. Mnamo 2017, Mahakama Kuu ilitangaza vifungu kadhaa vya sheria kuhusu kuondolewa kwa wabunge kuwa kinyume cha Katiba, ikisema vilikuwa na dosari. Mjadala huo unaendelea huku Bunge likijaribu kuweka mfumo wa kisheria utakaowezesha wananchi kuwawajibisha wawakilishi wao bila mchakato huo kutumiwa vibaya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

Kibarua kizito cha upinzani 2027 ikiwadia

MAZUNGUMZO ya vinara wa upinzani yanaashiria  kibarua kizito cha kuunda muungano imara utakaomkabili Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027. Huku uchaguzi ukisalia takriban miezi 10, viongozi hao wanakabiliwa na changamoto ya kukubaliana kuhusu mgombea mmoja wa urais, mgombea mwenza, uwiano wa kikanda na namna ya kuwavutia vijana wa Gen Z. Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, alisema Jumatatu baada ya kukutana na kiongozi wa DCP, Rigathi Gachagua, nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, kwamba upinzani hautakata tamaa katika juhudi za kuungana. "Tuna dhamira ya kuendelea kutafuta umoja," alisema Kalonzo. Gachagua naye alisema njia ya uhakika ya kumshinda Dkt Ruto ni kuafikiana kuhusu mgombea mmoja wa urais. "Tumekubaliana kuwa kumpata mgombea mmoja wa urais ndiyo njia ya uhakika ya kushinda uchaguzi mkuu ujao. Sote tumejitolea kufikia lengo hilo," alisema Gachagua. Aliongeza kuwa viongozi wako tayari kujitolea ili kumpata mtu atakayeongoza juhudi zao za kisiasa. Hata hivyo, kukubaliana kuhusu mgombea huyo kunatarajiwa kuwa kazi ngumu kwa sababu viongozi wengi wana malengo ya kuwania urais. Pia wanahitaji kumpata mtu anayeweza kuvutia wapigakura katika maeneo mbalimbali ya nchi. Utafiti wa Trends and Insights for Africa (Tifa) wa Julai ulionyesha kuwa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alikuwa na uungwaji mkono wa asilimia 15 iwapo angewania urais. Rais Ruto alikuwa na asilimia 24, huku aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i akiwa na asilimia 14 na Kalonzo asilimia 13. Gachagua alikuwa na asilimia saba. Viongozi pia wanapaswa kuzingatia uwezo wa kifedha, mitandao ya kisiasa na miundo ya kampeni ya kila mgombea. Eneo la Mlima Kenya ni muhimu kutokana na idadi yake kubwa ya wapigakura na mchango wake katika ushindi wa Ruto mwaka 2022. Kwa hivyo, nafasi ya mgombea mwenza inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mazungumzo ya upinzani. Tikiti ya Kalonzo na Sifuna imetajwa katika tafiti za hivi karibuni kuwa miongoni mwa zinazovutia. Hata hivyo, viongozi bado wanahitaji kuafikiana kuhusu namna ya kusawazisha maslahi ya maeneo mbalimbali. Seneta wa Kitui Enoch Wambua anasema mgombea wa pamoja anapaswa kutangazwa mapema ili awe na muda wa kutafuta rasilimali na kujenga miundo ya kisiasa. "Wakenya wanahitaji kujua mapema atakayemkabili Ruto kwenye kura. Nasikia kuna makubaliano ya karibu kwamba upinzani utawapa Wakenya zawadi ya Krismasi kwa kutangaza mgombeaji kabla ya mwisho wa mwaka," alisema. Naibu kiongozi wa Jubilee, Jeremiah Kioni, alisema baadhi ya viongozi wana uwezo wa kuvutia wapigakura lakini huenda wasiaminike kuongoza nchi, huku wengine wakiwa na sifa za uongozi lakini wakikosa nguvu za kuvutia kura. Vijana wa Gen Z pia ni sehemu muhimu ya hesabu za upinzani. Wachambuzi wanasema baadhi yao wanaweza kutaka mwelekeo mpya badala ya viongozi ambao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu. Katika eneo la Magharibi, Sifuna na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa wanaonekana kushindania ushawishi. Wamalwa alitembelea Gachagua Jumatatu akiwa na wazee, siku chache baada ya Sifuna kufanya ziara kama hiyo akiwa na wafuasi wa vuguvugu la Linda Mwananchi. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, aliyekuwa mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu na Wafula Wamunyinyi ni miongoni mwa viongozi wa eneo hilo waliounga mkono Sifuna. Mlima Kenya nako, DCP inashindana na Jubilee ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, PPK ya Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na PLP ya Martha Karua. Kaimu Katibu Mkuu wa DCP, John Methu, alisema chama kitachunguza vyama vinavyotaka kujiunga na upinzani ili kuhakikisha havitumiki kusababisha migawanyiko. Kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi alisema licha ya changamoto za kujenga muungano, lengo kuu ni kumuondoa Ruto madarakani kupitia kura na kurejesha utawala bora na kuheshimu Katiba. Rasimu ya mfumo wa kushirikiana inaonyesha kuwa muungano unapanga kuwasilisha makubaliano yake kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kufikia Machi 31, 2027. Makubaliano ya kugawana nyadhifa yanatarajiwa kukamilishwa kufikia wiki ya mwisho ya Machi. Rasimu hiyo pia inapendekeza vyama kugawana maeneo ya kuwania viti, ili kila chama kiweke wagombea katika maeneo ambako kina ushawishi mkubwa. Ramani ya mwisho ya maeneo hayo inapangwa kukamilishwa mwishoni mwa Februari 2027. Hata hivyo, Gachagua amepinga hadharani mpango huo wa kugawana maeneo, akisema ni kiti cha urais pekee kinachopaswa kutokuwa na ushindani wa ndani ya muungano. Mpango huo umekuwa ukizua utata katika miungano ya awali. Mwaka 2022, Raila Odinga alilazimika kuachana nao baada ya vyama vidogo kutishia kujiondoa katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya. Kiongozi wa DAP-K Wamalwa alisema kujenga muungano si tukio la mara moja bali ni mchakato wa mashauriano na mazungumzo endelevu, akitoa mfano wa muungano wa NARC uliomsaidia Mwai Kibaki kushinda uchaguzi wa 2002. Kwa sasa, changamoto kuu kwa upinzani ni kubadilisha matamshi ya umoja kuwa makubaliano kuhusu mgombea, nafasi za uongozi na kugawana maeneo kabla ya muda wa uchaguzi kuwadia.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 15:23:33

"Tuadhibuni sisi, lakini wake muwaache wake zetu," – Waititu

ALIYEKUWA gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na mfanyabiashara Charles Mbuthia Chege wameomba mahakama kuwaachilia huru wake zao katika kesi ya ufujaji wa fedha zinazohusishwa na zabuni ya barabara ya Sh588 milioni. Waititu na Chege, mkurugenzi wa kampuni ya Testimony Enterprises, walitoa ombi hilo Jumanne wakati wa kusikilizwa kwa hoja ya kupunguza adhabu katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Milimani. Kupitia mawakili wao, walisema Susan Wangari Ndung'u na Beth Wangechi Mburu hawakuhusika katika maamuzi ya zabuni hiyo, bali walikuwa washirika katika kampuni. Wakili wa Waititu alisema Susan hakuwa mtiaji saini wa akaunti za kampuni wala hakushiriki katika maamuzi ya biashara. Aliongeza kuwa Beth alikuwa ametia saini tu fomu za kuanzishwa kwa kampuni na hakuwa na jukumu katika shughuli zake. Waititu, ambaye tayari anatumikia kifungo cha miaka 12 kwa makosa yanayohusiana na ufisadi, aliomba mahakama izingatie adhabu ambayo tayari wamepitia. Alisema adhabu inapaswa kurekebisha mkosaji badala ya kuharibu maisha yake, akitaka mahakama iwape nafasi nyingine. Chege naye alisema mkewe alikuwa na hisa moja pekee katika kampuni na hakuwa na mamlaka ya kutia saini akaunti za benki. Alisema alikuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka 11 au kulipa faini ya Sh296 milioni. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga ombi hilo, ukisema kila mshtakiwa anapaswa kuwajibika kwa makosa aliyopatikana nayo na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Jaji wa Mahakama Kuu Rose Ougo alibadilisha uamuzi wa kuwaachilia huru washtakiwa kwa makosa ya ulanguzi wa fedha, akisema mahakama ya awali ilikosea kutathmini ushahidi na sheria. Waititu alipatikana na hatia ya kupokea Sh25 milioni kwa njia ya ufisadi kutoka kwa kampuni iliyopata zabuni ya barabara ya thamani ya Sh588 milioni. Mahakama inatarajiwa kutoa adhabu kwa washtakiwa hao wanne Novemba 2.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 15:00:52

Mutua kulipa Nonini fidia ya Sh3 milioni kwa kumchafulia jina

ALIYEKUWA  Mkurugenzi Mkuu wa Music Copyright Society of Kenya (MCSK) Ezekiel Mutua ameamriwa kumlipa mwanamuziki Nonini fidia ya Sh3 milioni kwa kumchafulia jina kupitia mitandao ya kijamii. Hakimu James Gitau alimwamuru Mutua kumlipa Nonini ambaye majina yake halisi ni Hubert Nakitare, Sh2.5 milioni kama fidia ya kawaida na Sh500,000 kama adhabu ya ziada kutokana na matamshi aliyotoa dhidi yake. Mutua pia ameamriwa kuondoa machapisho hayo kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii. Mzozo huo ulianza Januari 2024, MCSK ilipotangaza kuwa ingesambaza Sh20 milioni za mirahaba kwa wanachama wake 1,600. Nonini, ambaye alikuwa ameondoka katika MCSK Mei 2022, alihoji kiasi hicho baada ya kupata stakabadhi alizoamini zilionyesha kuwa shirika hilo lilikuwa limekusanya mamilioni zaidi ya lililotangazwa. Alisema MCSK ilikuwa imekusanya Sh109 milioni kutokana na mirahaba kati ya Januari na Desemba 2023, huku Sh57 milioni zikitumika kulipa mishahara ya wafanyakazi. Mwanamuziki huyo, anayejulikana kama Godfather wa Genge, alichapisha madai yake mtandaoni akitaka uwazi kuhusu jinsi fedha za wanamuziki zilivyokuwa zikisimamiwa. Hata hivyo, mjadala huo uligeuka kuwa mzozo binafsi baada ya Mutua kumtaja Nonini kuwa mkimbizi wa sheria na kumshutumu kwa kufuja fedha za wanamuziki alipokuwa akihudumu katika mashirika mengine ya hakimiliki. Mutua pia alidai kuwa Nonini alikuwa amesambaza stakabadhi bandia kuhusu hesabu za MCSK na kusema suala hilo lilikuwa limeripotiwa kwa polisi. Nonini aliambia mahakama kuwa madai hayo yalimsawiri kama mhalifu aliyekimbilia Amerika kukwepa mkono wa sheria, hivyo kuharibu sifa yake. Alisema Mutua pia alirudia madai hayo katika mahojiano na kituo cha redio cha Hot 96. Hakimu alisema matamshi hayo yalikuwa na uwezo wa kuharibu sifa ya Nonini kwa kumsawiri kama mtu anayekwepa sheria. Hukumu hiyo ni pigo jingine kwa Mutua, ambaye pia anakabiliwa na kesi ambayo Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), inataka arejeshe Sh27 milioni. Tume hiyo inadai alipandisha mshahara wake na kujilipa marupurupu kinyume cha sheria alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Film Classification Board (KFCB).

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 05:55:57

Majonzi mtaa ukifiwa na mapasta watatu kupitia ajali Mtito Andei

WAKAZI wa mtaa wa Bangladesh, eneo la Mikindani, Mombasa, wamezama katika majonzi kutokana na vifo vya wachungaji watatu na waumini wengine katika ajali iliyoangamiza watu 24 katika eneo la Kanga, barabara ya Mombasa-Nairobi, Kaunti ya Makueni, Jumapili asubuhi. Wachungaji Joseph Vura wa Campaign for Salvation and Healing Ministry (CASHEM), Fonex Paul wa River of Life na Isaac Juma wa Grace Healing Sanctuary walikuwa kati ya waliokuwa wakirejea kutoka mazishi ya mwenzao katika Kaunti ya Kakamega, basi walimokuwa lilipogonga lori la mizigo lililokuwa limesimama. Katika mtaa wa Bangladesh, familia na marafiki wa marehemu bado wanatatizika kukubali ukweli wa vifo hivyo, huku wengine wakipanga mazishi na kuomboleza wapendwa wao. Bi Judith Awino, ambaye aliishi na shemeji yake Hollon Oduor Waganda kwa miaka 10, alisema alipokea habari za ajali hiyo alipokuwa akiomba katika Kanisa la Lamb of God, Mikindani. "Mume wangu alinipigia simu kuniuliza kuhusu wachungaji waliofariki katika ajali. Hakujua kwamba mdogo wake pia alikuwa ndani ya basi hilo. Tulipojaribu kumpigia simu, hakupokea," alisema. Familia ilimtuma ndugu mwingine wa marehemu aliyekuwa Samburu, kaunti jirani ya Kwale, kwenda Makueni kuthibitisha hali yake. Baadaye aliwapigia simu na kuwathibitishia habari walizokuwa wakihofia. Bi Awino alisema Waganda alikuwa ametembelea nyumbani kwake Jumanne kuazima sanduku la kusafiria. "Waliondoka, lakini sasa wanarejea nyumbani wakiwa wamefariki. Familia yetu imeshtuka," alisema. Mwili wa Waganda ulikuwa ukisubiri kuhamishwa hadi hifadhi ya ya Hospitali ya Coast General kabla ya kusafirishwa Siaya kwa mazishi. Katika Mataa ya Ndege, Jomvu, wakazi wanaomboleza Mchungaji Fonex Paul, aliyehudumu katika kanisa lake kwa zaidi ya miaka 10. Jirani yake Peter Bendi alisema marehemu alikuwa mwenye huruma, mchangamfu na aliyesaidia watoto wa eneo hilo kwa masomo ya ziada. Mchungaji huyo ameacha mkewe Ann Biyaki. Katika Grace Healing Sanctuary, mchungaji msaidizi Fredrick Ochieng Odhiambo alisema kifo cha Juma kimeacha pengo kubwa katika jamii. Juma ameacha mke na watoto wanne. Marehemu Vura, Juma na Fonex walikuwa na makanisa yaliyokuwa umbali mfupi katika mtaa huo wenye wakazi wengi. Wakati huo huo, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir na Mbunge wa Likoni Mishi Mboko Jumatatu walitembelea maaskofu Zachariah Mwagandi na Cosmas Oduor Nyangweso, wanaopokea matibabu katika Hospitali ya Coast General baada ya kunusurika ajali hiyo. Ajali hiyo ilitokea takriban wiki tatu baada ya watu 17 waliokuwa wakisafiri kwenda Subukia Shrine kufariki katika ajali ya Salama, barabara hiyo hiyo, Oktoba 4

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 04:55:17

Watahiniwa waonywa kuhusu udanganyifu katika mitihani ya kitaifa

SERIKALI imewaonya wanafunzi na wasimamizi wa mitihani dhidi ya udanganyifu katika tathmini na mitihani ya kitaifa iliyoanza jana, ikisema watakaopatikana wataadhibiwa, kukiwemo kufutiwa kwa matokeo. Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema wanafunzi 3,634,846 wamejisajili kwa tathmini na mitihani ya mwaka huu, wakiwemo 1,380,463 wa KPSEA, 1,206,028 wa KJSEA na 1,048,355 wa KCSE. "Mwanafunzi yeyote atakayepatikana na hatia atachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufutiwa matokeo," akasema Bw Ogamba, akionya wazazi dhidi ya watu wanaodai kuuza mitihani. Alisema polisi hawajawekwa ndani ya vituo vya KPSEA na KJSEA ili wanafunzi wafanye tathmini katika mazingira tulivu bila vitisho. Serikali pia imeweka mipango ya kukabiliana na mvua, mafuriko, ukosefu wa usalama na maeneo magumu kufikika. Katibu anayesimamia Idara ya Elimu ya Msingi John Ololtuaa alisema walimu na maafisa 342,005 wamepewa jukumu la kusimamia shughuli hiyo, huku watahiniwa 50,873 wakitarajiwa kusahihisha mitihani. Katika kaunti za Kisii na Kisumu, tathmini zilianza bila matatizo makubwa. Mkurugenzi wa Elimu Kisumu Magara Onduso alisema vifaa vilisambazwa kwa wakati na usalama kuimarishwa. "Tumefanya maandalizi ya kutosha. Wasimamizi wamewasili kwa wakati na vifaa vimefikishwa mapema," alisema. Hata hivyo, Wanafunzi Kaunti ya Murang'a wanakabiliwa na wasiwasi wa njaa, huku nyumba 80,000 zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Kaskazini Mashariki, baadhi ya wazazi Garissa walidai shule zilikuwa zikitoza kati ya Sh10,000 na Sh30,000 kwa kila mwanafunzi kwa madai ya kupanga udanganyifu. Mkurugenzi wa Elimu wa eneo hilo Adan Roble alisema ofisi yake haikuwa imepokea taarifa hizo na akaonya watakaohusika kuwa wataadhibiwa. Katika eneo la Bonde la Ufa, wanafunzi katika maeneo ya Turkana yaliyoathiriwa na mashambulizi ya majambazi walisindikizwa hadi vituoni salama. Mvua na mafuriko pia yalilazimu maafisa kutumia boti kufikisha vifaa katika baadhi ya maeneo ya Turkana. Baringo iliripoti changamoto za taarifa za watahiniwa, lakini zilitanzuliwa kwa ushirikiano na KNEC. Trans Nzoia ilisema maandalizi yalikuwa yamekamilika. Nairobi, vifaa vilisambazwa bila matatizo, huku Mombasa na maeneo mengine ya Pwani yakichukua tahadhari dhidi ya mvua na mafuriko. Lamu iliweka boti tayari kusafirisha wasimamizi na maafisa wa usalama kwenye visiwa vya mbali. Katika eneo la Kati, maafisa walisema watawafikishia mitihani watahiniwa watakaougua hospitalini. Serikali imesema itashirikiana na Wizara ya Usalama kukabiliana na changamoto zozote wakati zoezi likiendelea. KPSEA inaendelea hadi Oktoba 28, KJSEA hadi Oktoba 30, huku KCSE ikiendelea hadi Novemba 20, 2026.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 03:55:13

Jengo la mkasa Eastleigh: nani alilala kazini?

KUPOROMOKA kwa jengo la orofa 18 katika Barabara ya 9, Eastleigh, Nairobi, kumeibua lawama kati ya taasisi zilizopaswa kusimamia ujenzi, huku kila upande ukikataa kuwajibika. Gavana Johnson Sakaja alisema kaunti haikuidhinisha mipango ya jengo hilo na kwamba ujenzi ulisimamishwa mara mbili. Alidai baadhi ya vibali vilivyosambazwa mitandaoni vilikuwa bandia. Hata hivyo, Msemaji wa Polisi Muchiri Nyaga alisema utoaji wa vibali na kusimamisha ujenzi ni jukumu la kaunti. Alisema tatizo la vibali haramu linapaswa kushughulikiwa ili kuzuia vifo. "Polisi hawana uhusiano wowote na ujenzi wa majengo ya aina hiyo. Hayo ni majukumu ya serikali za kaunti pekee, na kwa hakika, kaunti zina idara za utekelezaji wa sheria ambazo zina mamlaka ya kusimamisha kabisa kazi yoyote ya ujenzi," akasema Bw Muchiri.  Aliongeza kuwa madai ya gavana yanaonyesha mtu anayezama na kujaribu kushikilia chochote kile ili asizame. Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) Renson Ingonga alisema afisi yake haikuwa imepokea faili ya uchunguzi kutoka kaunti, na akaagiza Idara ya Upelelezi nchini (DCI) ichunguze iwapo maafisa wa kaunti, wajenzi au wataalamu walichangia mkasa huo.  Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) ilisema mradi huo ulisajiliwa Julai 30, 2025, huku kampuni ya 9th Street Plaza Limited ikitajwa kuwa ilihusika nao. Mmiliki Mohamed Khatar Ali Noor alisema jengo lilikuwa na vibali vyote japo mhandisi Joseph Muturi Mugu alijitenga na mradi huo. Mamlaka ya Kitaifa ya Utunzaji wa Mazingira (NEMA) ilikuwa imeiandikia kampuni hiyo Januari 2026 ikiitaka kuwasilisha michoro ya usanifu iliyo wazi kabla ya kushughulikia tathmini ya athari za mazingira. Ripoti ya NCA ya 2015 ilionya kuwa majengo yanaweza kukaliwa bila ukaguzi wa mwisho na cheti cha kuruhusu matumizi. Ukaguzi wa 2018 ulipata majengo 723 kuwa hatari sana na 10,791 kutokuwa salama. Mnamo 2024, Kamati ya Bunge la Kaunti ya Nairobi ilianzishwa kuchunguza madai ya vibali haramu, lakini ikavunjwa kabla ya kupokea barua muhimu. Mwenyekiti wake Nasra Nanda alisema uchunguzi huo ulizimwa licha ya umuhimu wake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 02:55:50

Gachagua, Kalonzo wakutana Wamunyoro kujadili urais wa 2027

KINARA wa Wiper, Kalonzo Musyoka na wandani wake jana walisaka uungwaji mkono kutoka kwa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, mirengo hiyo miwili ikiahidi kushirikiana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Hata hivyo, wakati wa mazungumzo kati ya wawili hao, utata wa lini upinzani utatangaza mgombea mmoja wa urais ulitawala mazungumzo kati yao yaliyoandaliwa nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri. Duru ziliarifu kuwa mrengo wa Bw Musyoka ulipendekeza mgombea huyo atangazwe kufikia Desemba mwaka huu ili apate muda wa kutafuta rasilimali na kujenga mitandao ya kampeni ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, Bw Gachagua na washirika wake walitaka mchakato huo uahirishwe hadi miezi michache kabla ya uchaguzi wa Agosti 10, 2027. Wana hofu kuwa Rais William Ruto anaweza kuwashawishi baadhi ya viongozi wa upinzani kujiondoa ikiwa mgombea urais atatajwa mapema. Seneta wa Kitui, Enoch Wambua alisema mkutano huo haukuafikiana kuhusu tarehe kamili, kwa kuwa upinzani unajumuisha washirika wengi. "Hata hivyo, wazungumzaji katika mkutano huo walitambua kuwa Wakenya wanazidi kukosa subira kutokana na kuchelewa kutangazwa kwa mgombea wetu wa urais," akasema Bw Wambua. "Tunapoendelea kujenga muungano imara, huenda zawadi ya Krismasi ikawa kutangazwa kwa mgombea huyo," akaongeza. Hata hivyo, alisema uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa viongozi wakuu wa vyama. Mbunge wa Gatanga Edward Muriu na mwenzake wa Embakasi ya Kati, Benjamin Gathiru, maarufu kama Mejja Donk, walisema upinzani unahitaji muda zaidi kabla ya kumchagua mgombeaji. Bw Muriu alisema wamekubaliana kurasimisha ushirikiano wao kwa kutia saini mkataba, kabla ya kuunda muungano wa kisiasa.Bw Gathiru alionya kuwa kutangaza mgombeaji mapema kunaweza kumpa Rais Ruto nafasi ya kuvuruga upinzani na kuwadhamini wagombeaji miongoni mwao. "Tumekubaliana kuwa vyama tanzu vinapaswa kuheshimiana. Pia tumewapa viongozi wakuu ruhusa ya kuzungumza na kuamua kuhusu mgombea," akasema "Lakini mchakato huo haupaswi kuharakishwa. Tunajua Ruto anaweza kufanya nini. Anaweza kufadhili baadhi ya viongozi wajiondoe na kuwania urais," akaongeza. Kiongozi wa People's Party of Kenya (PPK) , Ndindi Nyoro alisema mazungumzo yanahitaji muda ili kupata mgombea anayefaa kukabiliana na changamoto za nchi. "Tunapaswa kuangalia hali ya nchi, kisha tuamue ni nani katika mrengo wetu ana uwezo zaidi wa kukabiliana na changamoto hizo. Tunatumai mchakato utakuwa wa haki na utazingatia sifa," akasema Bw Nyoro. Alisema chama chake kiko tayari kumuunga mkono mgombeaji atakayechaguliwa kupitia maridhiano. Bw Musyoka aliandamana na Bw Wambua, Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo na mwenzake wa Machakos Wavinya Ndeti, miongoni mwa viongozi wengine. Bw Gachagua alihudhuria akiwa na Bw Muriu, Seneta wa Nyandarua John Methu, Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang'wa. Bw Wambua alisema Musyoka na Gachagua walifanya mazungumzo ya kirafiki kuhusu mustakabali wa nchi. "Viongozi hao wawili wamejitolea kufanya kazi pamoja, kuunganisha wafuasi wao na kuhakikisha azma ya kumfanya Ruto kuwa rais wa muhula mmoja inatimia Agosti 10, 2027," akasema Bw Methu alisema DCP na Wiper zimekubaliana kufanya kazi kama vyama tanzu na kuendelea kutafuta njia ya kumpata mgombea mmoja wa urais. Viongozi hao wanataka kufikia makubaliano yatakayowawezesha kukabiliana na Rais Ruto katika uchaguzi ujao. Mkutano wa jana ulifanyika wiki moja baada ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kumtembelea Gachagua nyumbani kwake pindi alipotoka Amerika. Changamoto zinazokabili upinzani zinafanana na zile zilizokumba muungano wa National Rainbow kabla ya uchaguzi wa 2002. Wakati huo, viongozi wa upinzani walijadiliana kwa muda mrefu kuhusu mgombea wa kumkabili Kanu, chama kilichokuwa madarakani. Katika kitabu chake Seasons of Hope, aliyekuwa Seneta wa Kitui David Musila anakumbuka jinsi Raila Odinga alivyotatua mtanziko huo kupitia kauli maarufu ya "Kibaki Tosha" Septemba 22, 2002, miezi mitatu kabla ya uchaguzi. "Ujumbe ulikuwa wazi; upinzani uliokuwa umeungana dhidi ya Kanu ulikuwa umejipanga. Hata hivyo, hatukuweza kupuuza umuhimu wa kutaka kujua mgombea wetu angekuwa nani. Umati ulikuwa na hamu ya kupata jibu, lakini hakuna aliyekuwa nalo," aliandika Bw Musila. Alisema Raila alipofikia zamu yake ya kuzungumza, alitangaza ghafla kuwa Bw Kibaki ndiye aliyefaa kuwa mgombea. Kauli hiyo ilishangiliwa na umati na kutatua mzozo wa uteuzi. Historia inaonyesha kuwa wagombea wa urais nchini Kenya mara nyingi hutangazwa miezi michache kabla ya uchaguzi. ODM ilimteua Raila Septemba 1, 2007, huku muungano wa Cord ukimuidhinisha Disemba 22, 2012. NASA ilimtangaza Raila Aprili 27, 2017, na Azimio La Umoja ikamuidhinisha Machi 12, 2022. Kwa upande wa Kenya Kwanza, William Ruto aliteuliwa rasmi kuwa mgombea wa UDA Machi 15, 2022.

read more