taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 1 hours ago
Wakenya wapatao 4,000 waliangamia barabarani kati ya Januari na Oktoba – NTSA
KENYA imepoteza takriban watu 4,000 katika ajali za barabarani ndani ya miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu, huku Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) ikitaka hali hiyo itangazwe janga la kitaifa. Takwimu za NTSA zinaonyesha kuwa watu 3,995 walifariki kati ya Januari 1 na Oktoba 4, 2026, ongezeko la asilimia 9.2 ikilinganishwa na vifo 3,657 vilivyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana. Watembea kwa miguu ndio walioathirika zaidi, wakifuatwa na waendesha pikipiki. Kati ya waliofariki, watembea kwa miguu walikuwa 1,490, waendesha pikipiki 1,061, abiria 662 na madereva 352. Mamlaka hiyo pia imetambua maeneo zaidi ya 270 hatari kwa ajali nchini, yakiwemo 199 katika Barabara Kuu ya Mombasa-Malaba. Wito huo unafuatia ajali mbaya ya Oktoba 25 eneo la Kanga, karibu na Mtito Andei, ambapo watu 24 walifariki baada ya basi kugongana na lori. Ajali nyingine katika eneo la Salama mnamo Oktoba 3 ilisababisha vifo vya watu 17, wengi wao wakiwa waumini Wakatoliki. Mkurugenzi wa Usalama Barabarani wa NTSA, Andrew Kipalgat, alisema kukabiliana na ajali kunahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa serikali na mashirika husika. Alitaja hali ya magari na barabara, tabia za watumiaji na huduma za dharura kuwa mambo yanayopaswa kuchunguzwa. Ripoti ya Utafiti wa Kiuchumi ya KNBS ya 2026 inaonyesha kuwa watu 5,009 walifariki katika ajali zilizoripotiwa mwaka 2025, ikilinganishwa na 4,748 mwaka 2024. Sababu zinazochangia ajali ni pamoja na mwendo wa kasi, kupita magari kiholela, uchovu wa madereva, ulevi, magari yasiyofaa barabarani na miundombinu duni. NTSA inasema kutangaza usalama barabarani kuwa janga la kitaifa kunaweza kusaidia kuratibu rasilimali na kuimarisha hatua za kupunguza vifo. Hata hivyo, mafanikio yatategemea ufadhili wa kutosha, utekelezaji wa sheria na ukarabati wa maeneo hatari.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 2 hours ago
Ruto awarai wawekezaji wa Urusi na miradi ya Sh5.2 trilioni Kenya
RAIS William Ruto amewaalika wawekezaji wa Urusi kuwekeza katika mpango wa miundomsingi wa Sh5.2 trilioni katika kipindi cha miaka 10, akilenga kuimarisha biashara kati ya mataifa hayo. Akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara wa Kenya na Urusi mjini Moscow, Dkt Ruto alisema uwekezaji huo utasaidia kukuza viwanda, kuunda nafasi za kazi na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini. Alitaja sekta za nishati, uzalishaji wa mbolea, kilimo, usafiri, uchimbaji na uchakataji wa madini pamoja na utengenezaji wa bidhaa kuwa maeneo yanayohitaji uwekezaji. Rais alisema Kenya inataka kuacha kuuza malighafi na kununua bidhaa zilizokamilika, akihimiza wawekezaji kuanzisha viwanda nchini na kutumia Kenya kufikia masoko ya Afrika. Biashara kati ya mataifa hayo ilifikia takriban Sh49.38 bilioni mwaka 2025. Kenya iliuza bidhaa za thamani ya Sh6.76 bilioni, hasa chai, kahawa, maua, matunda na mboga. Dkt Ruto pia alitaja fursa katika kawi ya jotoardhi na magari yanayotumia umeme. Alisema asilimia 93 ya umeme nchini unatokana na vyanzo vinavyoweza kufanywa upya. Alisisitiza kuwa soko la Afrika, la watu bilioni 1.5 kupitia Mkataba wa Biashara Huria wa Bara la Afrika, linaweza kuwapa wawekezaji fursa kubwa ya kupanua biashara zao. Alisema Kenya inataka ushirikiano unaojenga viwanda, kuhamisha teknolojia na kuleta manufaa kwa pande zote.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
Kalonzo kichwa kinauma kuhusu 2027
KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka anakabiliwa na maamuzi magumu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku migawanyiko ndani ya upinzani ikitishia azma yake ya kuwania urais kwa mara ya pili. Ingawa Bw Musyoka angependa kuidhinishwa kuwa mgombea wa urais wa upinzani, huenda akalazimika kuchagua kati ya kuendelea kusisitiza azma hiyo, kukubali kuwa mgombea mwenza wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna au kujiunga na Rais William Ruto. Hata hivyo, hakuna hakikisho kwamba atapata nafasi ya mgombea mwenza iwapo atakubali wito wa kujiunga na Rais Ruto, ambaye tayari anakabiliwa na ushindani wa washirika wake, wakiwemo wanaotaka kuwania nafasi ya Naibu Rais. Kutokuwa na makubaliano kuhusu mgombea mmoja wa upinzani wa kumenyana na Dkt Ruto kunamweka Bw Musyoka, 72, kwenye shinikizo huku baadhi ya wanasiasa wakitilia shaka uwezo wake wa kushinda urais. Jumatatu, Dkt Ruto alitumia ziara yake Tseikuru, nyumbani kwa Bw Musyoka, kumshawishi kiongozi huyo wa Wiper ajiunge naye, akidai amekuwa akidhalilishwa na washirika wake wa kisiasa. "Walimpitisha kwenye mahojiano 2022. Mlimwona akiulizwa kuhusu maelezo yake ya kibinafsi na mafanikio yake. Huko kulikuwa kumdhalilisha. Wale wale walioandaa mahojiano hayo mnamo 2022 wanapanga mengine hivi karibuni. Badala ya Kalonzo kuenda kwenye mahojiano mengine, anapaswa kujiunga nami," akasema Dkt Ruto. Wakati wa ziara hiyo, alimwelekeza mkandarasi anayejenga barabara ya Kandwia-Kyuso-Tseikuru yenye urefu wa kilomita 55 kuiongeza hadi karibu na makazi ya Bw Musyoka, kilomita tatu kutoka mji wa Tseikuru. Bw Musyoka aliwakilisha eneobunge la Mwingi Kaskazini kuanzia 1985 hadi 2013. Aliwania urais 2007 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Mwai Kibaki na Raila Odinga, kabla ya kumuunga mkono Raila katika chaguzi za 2013, 2017 na 2022. Hata hivyo, baadhi ya washirika wake wanaamini bado anafaa kuwania urais, licha ya kuongezeka kwa umaarufu wa Bw Sifuna, hasa miongoni mwa vijana. Seneta wa Kitui Enock Wambua amemshauri Bw Musyoka asikubali kuwa mgombea mwenza wa Bw Sifuna, akisisitiza kuwa anatosha kuwania urais. "Wengine watakapokubaliana kumteua, Ruto anapaswa kuanza kufunganya virago vyake kutoka Ikulu kwa sababu 2027 ndiyo nafasi yake bora zaidi," akasema Bw Wambua katika mahojiano na Taifa Leo. Alipinga madai kuwa Bw Musyoka hakubaliki miongoni mwa vijana, akisema uzoefu wake wa muda mrefu katika siasa unamfaa kuongoza nchi. "Wiper ina vijana, na wanaofanya kazi na Kalonzo ni vijana. Anaelewa masuala yao na anafaa kuwaongoza. Kalonzo anakidhi vigezo vyote, na tutasukuma azma yake ndani ya upinzani," akaongeza. Miezi mitatu iliyopita, kiongozi wa DP Justin Muturi pia alimuunga mkono Bw Musyoka kuwa mgombea wa urais wa upinzani. "Ikiwa haitakuwa mimi, nitamuunga mkono Dkt Stephen Kalonzo Musyoka kuwa mgombea wa urais," akasema Bw Muturi katika ibada ya kanisa Kamulu, Kaunti ya Machakos. Wakati huo huo, uwezekano wa Bw Musyoka kuwa mgombea mwenza wa Bw Sifuna umezua mjadala ndani ya upinzani. Washirika wa kiongozi huyo wa Wiper wamepuuza madai ya aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala kwamba Bw Musyoka anapaswa kukubali nafasi hiyo katika uchaguzi wa 2027. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Bw Malala alidai kuwa kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua alikuwa amekubali kumuunga mkono Bw Sifuna katika mkutano uliofanyika nyumbani kwake Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri. Hata hivyo, Msemaji wa Wiper Ndegwa Njiru alipinga madai hayo, akisema Bw Malala alikuwa akijaribu kuleta mgawanyiko ndani ya upinzani. "Matamshi yanayohusishwa na Seneta Malala yanaweza tu kuelezewa kuwa kazi ya mwandishi wa tamthilia badala ya mwanasiasa makini. Malala anaonekana kuwa na nia ya kuingiza kisu cha migawanyiko ndani ya moyo wa upinzani," akasema. Bw Musyoka alitoa matamshi hayo wakati wa ziara yake kwa Bw Gachagua katika makazi yake ya Wamunyoro. Katika ziara hiyo, Seneta wa Nyandarua John Methu, mshirika wa Bw Gachagua, alisema viongozi wa upinzani wanapaswa kukubaliana kuhusu mikakati ya kumshinda Dkt Ruto. "Kalonzo na Bw Gachagua wamekubaliana kwamba mtoto hatakufa mikononi mwao," akasema Bw Methu, akimaanisha kuwa hawataruhusu juhudi zao za kumwondoa Rais mamlakani zishindwe. Hata hivyo, si viongozi wote wanaounga mkono azma ya Bw Sifuna walio tayari kushirikiana na Bw Musyoka. Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka, mwandani wa Bw Sifuna, hivi majuzi alisema hawako tayari kushirikiana na Bw Musyoka kwa sasa, akisisitiza kuwa wanataka kufanya kazi na eneo la Mlima Kenya na kumuunga mkono mgombea mmoja wa upinzani. "Hatuwezi kushirikiana na Kalonzo kwa sasa kutokana na yale aliyotufanyia kuhusu jina la Ukombozi. Kipaumbele chetu ni kufanya kazi na Mlima Kenya hadi uchaguzi, na njia pekee ya kushirikiana naye ni ikiwa upinzani utatoa mgombea mmoja wa urais, ambaye ni Sifuna," akasema Bw Wamboka. Kwa upande mwingine, kujiunga na Dkt Ruto kunaweza kumfungulia Bw Musyoka njia ya kuwania nafasi ya Naibu Rais. Hata hivyo, nafasi hiyo tayari inatamaniwa na ODM pamoja na washirika wa Naibu Rais Kithure Kindiki, hali inayoweza kuzidisha ushindani ndani ya kambi ya Rais. Mhadhiri wa chuo kikuu Profesa Lumala Masibo alisema mustakabali wa Bw Musyoka utategemea uwezo wa upinzani kufikia makubaliano kuhusu mgombea na mikakati ya pamoja. "Upinzani unahitaji kuwa na mikakati na kila kiongozi anapaswa kuwa tayari kumuunga mkono mwenzake. Ikiwa Kalonzo hatateuliwa kuwa mgombea wa urais, basi huo utakuwa mwisho wake. Akishindana na Ruto akiwa na uungwaji mkono wa upinzani au pekee yake, atashindwa vibaya. Kwa hivyo, ni bora ajiunge na Rais," akasema Profesa Masibo. Aliongeza kuwa Bw Musyoka anaweza kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto ili kuimarisha uungwaji mkono wake Ukambani na kupatanisha mirengo ya ODM na washirika wa Prof Kindiki. Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo pia alisema umri, fedha na mikakati ya Bw Musyoka vinaweza kuwa changamoto, akidai kuwa hajajenga msukumo mkubwa wa kisiasa nje ya Ukambani. "Ni rahisi zaidi kwake kujiunga na Rais, na hapaswi kumshinikiza yeyote kwa masharti magumu kwa sababu anatafuta njia ya kuendelea kuwa na nafasi katika siasa," akasema Bw Bigambo. Aliongeza kuwa kukubali kuwa mgombea mwenza wa Bw Sifuna kunaweza kudhoofisha hadhi ya Bw Musyoka baada ya miaka mingi katika siasa za kitaifa
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 13 hours ago
Mapasta kuchangisha Sh10m kufanikisha mazishi ya waliokufa ajalini Mtito Andei
MUUNGANO wa wachungaji wa kidini Mombasa umeanzisha harambee ya kuchangisha Sh10 milioni kwa ajili ya mazishi ya wenzao watatu waliofariki katika ajali ya Mtito Andei. Haya yanajiri huku shinikizo likiongezeka kwa serikali kujenga barabara ya Mombasa-Nairobi yenye njia mbili kila upande ili kupunguza ajali za barabarani. Watatu hao walikuwa miongoni mwa watu 24 waliofariki Jumapili asubuhi baada ya basi lililokuwa safarini kurudi Mombasa kugongana na lori la mizigo eneo la Kanga, karibu na Mtito Andei. "Mioyo yetu imevunjika. Kanisa liko katika majonzi, na wachungaji wanalia. Tulitumia siku mbili Mtito Andei kuwafariji waathiriwa na kutambua miili ya ndugu zetu," Katibu Mkuu wa muungano huo, Mchungaji Elijah Waini, alisema. Bw Waini alimshukuru Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jr, ambaye utawala wake uliondoa malipo yote ya hospitali na uchunguzi wa maiti, ukahifadhi miili ya marehemu na kutoa magari ya kusafirisha miili hiyo hadi Mombasa kwa ajili ya kuhifadhiwa. Hata hivyo, mwili mmoja wa afisa wa polisi aliyekuwa akihudumu Mikindani, ambaye pia alikuwa mhudumu wa kanisa, bado uko katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Mtito Andei. Duru zilisema kuwa uhamisho wa mwili huo unasubiri maagizo kutoka kwa idara ya kitaifa ya huduma za polisi (NPS), ingawa Taifa Leo haingeweza kuthibitisha kutoka kwa familia ya marehemu.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 18 hours ago
Waendesha boda boda 300 wapata mafunzo ya usimamizi wa fedha Namanga
Takriban waendesha boda boda 300 katika mji wa Namanga, Kaunti ya Kajiado, wamepata mafunzo ya usimamizi wa fedha ili kuwasaidia kupanga mapato yao, kulipa mikopo kwa wakati na kuimarisha biashara zao. Mafunzo hayo yaliandaliwa na kampuni ya ufadhili wa mali ya Mogo, yakilenga kuwapa waendeshaji ujuzi wa kukopa kwa uwajibikaji, kuweka akiba na kupanga bajeti kulingana na mapato yao. Washiriki walifundishwa mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua mkopo, kuelewa viwango vya riba na masharti ya ulipaji, kutimiza makataa ya malipo na kutafuta suluhu zinazofaa wanapokumbwa na changamoto za kifedha. Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma katika Mogo, Becky Ngigi, alisema kupata mkopo pekee hakutoshi bila kuwa na maarifa ya kusimamia fedha. "Upatikanaji wa fedha pekee hautoshi. Watu wanahitaji pia maarifa na ujuzi wa kufanya maamuzi mazuri ya kifedha," alisema. Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwapa waendeshaji zana za kusimamia mapato, kutimiza wajibu wa mikopo na kukuza biashara zao kwa njia endelevu. Mwenyekiti wa waendesha boda boda Kaunti ya Kajiado, Alex Gitari, alisema uelewa wa fedha ni muhimu kwa waendeshaji wanaotegemea mikopo kununua pikipiki na kupanua biashara zao. Alisema waendeshaji wanapaswa kupanga mapato yao kwa kuzingatia gharama za uendeshaji, mahitaji ya familia na malipo ya mikopo. Mafunzo hayo yanakuja wakati Kenya ikikabiliwa na changamoto ya kuhakikisha kuwa wananchi wanaopata huduma za kifedha wanazitumia kuboresha maisha yao. Mkakati wa Kitaifa wa Ujumuishaji wa Kifedha wa 2025–2028 unaonyesha kuwa asilimia 84.8 ya watu wazima nchini walipata huduma rasmi za kifedha mwaka 2024, lakini ni asilimia 18.3 pekee waliokuwa na afya nzuri ya kifedha. Sekta ya boda boda inakadiriwa kuzalisha Sh660 bilioni kila mwaka na kusaidia zaidi ya watu milioni 2.5 kupata riziki, kulingana na ripoti ya Viffa Consult kuhusu ukuaji wa sekta hiyo. Mogo imesema itaendelea kuunga mkono mipango inayohamasisha ukopaji wa uwajibikaji, usimamizi bora wa fedha na ukuaji endelevu wa biashara.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 22 hours ago
Wazee sasa kusaidia familia kutatua mizozo ya urithi
FAMILIA katika eneo la North Rift zimehimizwa kuacha mizozo ya urithi inayodumu kwa miaka mingi na badala yake kutumia upatanishi kutatua tofauti zao kuhusu mali ya wazazi wao. Mahakama imeanza kushirikiana na wazee wa jamii kusaidia familia hizo kufikia makubaliano, kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani na kuwezesha familia kupata mali waliyorithi kwa haraka. Zaidi ya viongozi 60 wa jamii kutoka Baraza la Wazee wa Kalenjin wameidhinishwa na Idara ya Mahakama kuendeleza Mfumo Mbadala wa Kutatua Mizozo (AJS). Wazee hao wanaripotiwa kutatua zaidi ya mizozo 1,200 kupitia upatanishi katika mwaka uliopita, mingi ikihusu migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu. Jaji Charles Yano wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Eldoret alisema kesi za urithi ni miongoni mwa sababu zinazochangia mrundiko wa kesi katika eneo hilo. Akizungumza Jumatatu wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya AJS, jaji huyo alizitaka familia kutumia upatanishi badala ya kusubiri kesi mahakamani kwa miongo kadhaa. "Ninaomba familia kukumbatia mfumo huu na upatanishi unaofanyika kwa ushirikiano na mahakama katika masuala ya urithi, badala ya taratibu za mahakama zinazoweza kuchukua miongo kadhaa," alisema. Aliongeza kuwa kesi za muda mrefu hugharimu familia pesa, huzidisha migawanyiko na kuwanyima warithi fursa ya kufurahia mali yao. Baadhi ya mizozo mikubwa ya urithi inayotajwa katika eneo hilo inahusu mali za mwanasiasa na mkulima mashuhuri Jackson Kibor na John Kiplagat Kibogy. Watoto wao wamekuwa wakizozana mahakamani kwa zaidi ya miaka 10 kuhusu mali inayokadiriwa kuzidi Sh15 bilioni. Chama cha Wanasheria nchini (LSK), tawi la North Rift, kinaunga mkono juhudi hizo na kuendesha kampeni za kuhamasisha wazee, viongozi wa dini na wadau wengine kuhusu umuhimu wa upatanishi. Mwenyekiti wa tawi hilo, Oscar Oduor, alisema mfumo huo unaweza kusaidia familia kutatua mizozo ya urithi kwa kufuata sheria. Mwenyekiti wa upatanishi Uasin Gishu, wakili Daniel Tariko, alisema makubaliano yanayofikiwa kupitia upatanishi unaohusishwa na mahakama yanaweza kupitishwa na mahakama kuwa amri rasmi. Hatua hiyo inaweza kufungua njia kwa warithi kupata mali yao kwa mujibu wa sheria. Kwa familia zinazokumbwa na mizozo, ujumbe ni kutafuta suluhu mapema kabla ya kesi ndefu kuzidisha uhasama na kuchelewesha ugavi wa urithi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 23 hours ago
Uchungu wa familia iliyopoteza jamaa wanne ajalini
FAMILIA katika eneo la Rabai, Kaunti ya Kilifi yaomboleza jamaa wao wanne waliofariki kwenye ajali iliyotokea Jumapili eneo la Kanga lililo Mtito Andei, kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa. Kwenye mahojiano Jumatatu, Bw Mwatsuya Mutsunga alishindwa kuzuia machozi akieleza kuhusu msiba uliokumba familia yake. "Nianze kumwomboleza nani?" aliuliza kwa sauti ya chini iliyotetemeka kwa huzuni. "Mwanangu? Kaka yangu mkubwa? Mke wake? Au mwana wao pia ni damu yangu? Mtu anaanzaje kuomboleza watu wengi namna hii? Na baada ya machozi kukauka, nitawaambia nini waliosalia kama mzee wa familia hii?" aliuliza. Familia yake ni miongoni mwa zilizoathiriwa zaidi na mkasa huo ambao umegusa eneo la Pwani na kitaifa. Basi lililokuwa limebeba karibu abiria 50, wakiwemo zaidi ya wachungaji na waumini 12, liligongana ana kwa ana na lori kubwa la mizigo walipokuwa wakirejea Mombasa kutoka mazishi yaliyofanyika Lugari, Kaunti ya Kakamega. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 24. Miongoni mwa waliofariki ni kaka mkubwa wa Bw Mutsunga, Dkt Patrick Mutsunga; mkewe, Younitta Mutsunga; mtoto wao, Ndune Mutsunga; na mwanawe Mutsunga, Moses Mwadzuya. Bw Mutsunga, alisema jioni ya Jumapili ilikuwa ya uchungu kwake huku taarifa za vifo hivyo zikimfikia moja baada ya nyingine. "Nilipigiwa simu ya kwanza saa moja usiku hivi. Mwanzoni tuliambiwa kuwa kaka yangu mkubwa alikuwa amefariki papo hapo, huku mkewe akifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja Kaunti ya Makueni. Wengine wawili walikuwa bado hawajatambuliwa," alikumbuka. Kabla familia haijapata muda wa kukubali taarifa hizo za kwanza, naibu chifu wa eneo hilo alifika na habari nyingine za kusikitisha kwamba miili ya Ndune na Moses pia ilikuwa imetambuliwa katika eneo la ajali. "Tulivunjika moyo kabisa. Mwezi mmoja tu uliopita, mwanangu Moses aliondoka kijijini na kwenda Mombasa kumsaidia mkewe kutafuta matibabu. Sasa hayupo tena, akiwa ameacha mjane na watoto watatu wanaosoma," akasema. Kaka yake mkubwa, Dkt Patrick, alikuwa nguzo muhimu ya familia. Akiwa mtaalamu wa afya aliyestaafu, aliendesha zahanati ya kibinafsi na shule ya kibinafsi katika Kaunti ya Kwale pamoja na mkewe, Younitta. "Alinipigia simu Jumatano iliyopita kunijulisha kuhusu safari ya kumzika shemeji yake, Askofu Isaiah Giganene," alisema Bw Mutsunga. Alisema alimtakia safari njema. "Sikuwahi kufikiria kwamba hiyo ingekuwa mara ya mwisho kusikia sauti yake. Sasa nimeachiwa jukumu kubwa la kuwatunza wale aliowaacha," aliongeza. Habari za msiba zilipoenea Rabai, wanakijiji waliacha shughuli zao za kila siku na kusaidia kuweka mahema na kukaa pamoja na mzee huyo wa familia aliyekuwa akiomboleza. Waombolezaji walizunguka kutoka hema moja hadi jingine kuwafariji ndugu wa marehemu. Bw Tsuma Kanyonge, mzee wa familia, alisema kupoteza jamaa wanne katika ajali moja ilikuwa pigo kubwa kwa familia na jamii nzima. "Fikiria kupoteza tawi zima la familia kwa wakati mmoja. Tutaendeleaje na maisha?" aliuliza Bw Kanyonge. Alisema walikuwa wamesikia kupitia redio za eneo hilo kwamba kulikuwa na ajali ya magari kugongana ana kwa ana kwenye barabara kuu, lakini hawakujua kuwa jamaa zao walikuwa miongoni mwa waliokuwa ndani ya basi hilo. "Hili ni pigo kubwa, na tunamwomba Rais William Ruto kuingilia kati na kuwasaidia watoto hawa wadogo na wajane," alisema. Msiba huo umeibua tena malalamishi kuhusu hali ya usalama barabarani inayozidi kuzorota katika barabara ya Mombasa–Nairobi. Haya yanajiri wiki chache tu baada ya ajali iliyotokea Salama Oktoba 4 na kusababisha vifo vya mahujaji 17 wa Kanisa Katoliki. "Wiki mbili zilizopita tulipoteza mahujaji 17, na leo tunaomboleza wengine 23. Hali hii itaendelea hadi lini?" aliuliza Bw Kanyonge. Alizitaka mamlaka husika kuwakamata wamiliki wa magari yasiyofaa kutumika barabarani yaliyohusika katika ajali hizo, na kutambua pamoja na kuweka alama katika maeneo yote hatari kwenye barabara hiyo ili kulinda maisha ya watu. Mbunge wa eneo hilo, Bw Kenga Mupe, aliingilia kati Jumatatu asubuhi na kushirikiana na utawala wa eneo hilo kupanga usafirishaji wa miili ya watu hao wanne kutoka Makueni hadi chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Pandya Memorial mjini Mombasa, huku maandalizi ya mazishi yakianza.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 28 Oct 2026 05:55:32
Mama akamatwa kwa kuzuia mwanawe kufanya mtihani, adai nambari '666'ni ya kishetani
MAMA mmoja mwenye umri wa miaka 38 amekamatwa kaunti ya Mombasa baada ya kumfungia binti yake nyumbani na kumzuia kufanya mtihani wa kitaifa wa KPSEA kwa madai kuwa nambari yake ya mtihani ilikuwa na tarakimu za kishetani, 666. Mama huyo wa watoto watano alikamatwa Jumanne baada ya mwanawe kukosa kufika katika kituo cha mtihani cha shule ya msingi ya Kwa Jomvu. Alidai kuwa uamuzi wake ulitokana na maagizo aliyopokea kutoka kwa Mungu. "Mimi ni mtu ninayemcha Mungu, mtumishi wake na mhubiri. Nilizungumza na Mungu, akanionyesha kuwa nambari ya mtihani wa binti yangu haikuwa sahihi," alisema akiwa katika Kituo cha Polisi cha Jomvu. Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bakari Mwerephe, alisema mwanafunzi huyo alikuwa amefanya mtihani wa siku ya kwanza Jumatatu, lakini mama yake akampigia simu akisema hataruhusiwa kuendelea na mitihani kwa sababu ya nambari hiyo. Shangazi wa msichana huyo aliarifu polisi na maafisa wa Idara ya Watoto, ambao walifika nyumbani saa tatu na nusu asubuhi na kumuokoa mwanafunzi huyo akiwa amevalia sare za shule. Alisindikizwa hadi kituoni na kuruhusiwa kufanya mtihani. Kamanda wa Polisi wa Jomvu, Selina Chirchir, alisema maafisa waliingilia kati ili kuhakikisha haki ya mtoto ya kupata elimu inalindwa. Binamu wa mama huyo, Juliet Ndewa, alisema familia imekuwa ikipambana na kile ilichokitaja kuwa msimamo mkali wa kidini unaoathiri watoto. Mwezi mmoja uliopita, mama huyo alikuwa ameitwa na maafisa wa watoto baada ya kuripotiwa kuwazuia watoto wake kwenda shule na kutafuta matibabu wanapougua. Mama huyo anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa afya ya akili na kuhojiwa zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazohusiana na kupuuza malezi na haki ya mtoto kupata elimu. Katika habari nyingine, wanafunzi watatu wa kike wanafanya mitihani ya KJSEA hospitalini kaunti ya Bomet. Wawili walijifungua siku ya kwanza ya mitihani, huku mwingine akifanya mtihani katika Hospitali ya Tenwek baada ya kujifungua. Huko Nakuru, watahiniwa 27 ambao majina yao hayakuwa kwenye orodha rasmi waliruhusiwa kufanya mitihani maafisa wa Baraza la Mitihani la Kitaifa (KNEC) walipoingilia kati. Walijumuisha watahiniwa 11 wa KPSEA na 16 wa KJSEA. Hata hivyo, mwanafunzi mmoja wa KJSEA katika Shule ya Kionduso PAG, Kisii, alikosa mtihani baada ya kubainika kuwa hakuwa amesajiliwa. Babake, Dickson Asiago, alitaka Wizara ya Elimu ichukue hatua dhidi ya waliohusika. Wakati huohuo, usalama umeimarishwa katika maeneo yanayokumbwa na ujangili katika kaunti za Samburu, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi, Turkana na Baringo ili kuhakikisha watahiniwa wanafanya mitihani bila hofu. KPSEA inatarajiwa kukamilika kesho, huku mitihani ya KJSEA ikiendelea hadi Ijumaa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 28 Oct 2026 04:55:53
Vita kati ya magavana na Ruto kuhusu maendeleo vyatishia ugatuzi
MVUTANO kati ya Rais William Ruto na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kuhusu nani anastahili sifa za miradi ya maendeleo umeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa ugatuzi, huku viongozi wakishindana kudhibiti na kumiliki kisiasa miradi inayolenga kuwahudumia wananchi. Wiki iliyopita, Bw Natembeya alimlaumu Rais kwa kujipa sifa za miradi inayofadhiliwa na serikali ya kaunti, ikiwemo Soko la Masinde Muliro mjini Kitale. Gavana huyo alisema serikali ya kaunti, kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, ilitumia zaidi ya Sh800 milioni kujenga soko hilo, huku serikali ya kitaifa ikichangia Sh56 milioni kukamilisha kazi zilizobaki. Pia alipinga ujenzi wa hospitali ya thamani ya Sh1 bilioni, akisema hakushirikishwa kabla ya mradi huo kuanzishwa. Rais, aliyezindua ujenzi wa hospitali hiyo yenye vitanda 300, alimshutumu gavana kwa kuzuia maendeleo ya huduma muhimu za afya. Hata hivyo, wataalamu wanasema mzozo huo ni sehemu ya vita pana kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuhusu ufadhili, utekelezaji na sifa za miradi. Wakili Ekuru Aukot, aliyeshiriki kuandaa Katiba ya 2010, alisema Ibara ya 6(2) inaeleza kuwa serikali za kitaifa na kaunti ni tofauti lakini zinategemeana, na zinapaswa kushirikiana kupitia mashauriano. Mtaalamu wa utawala Peter Mbae alionya kuwa mashindano hayo yanatishia kudhoofisha ugatuzi na utawala bora. Alisema miradi ya maendeleo ni ya wananchi, wala si viongozi wanaotaka kujipatia umaarufu wa kisiasa. Wakili Steve Kabita pia alisema hakuna serikali inayopaswa kudai kumiliki au kujipa sifa za mradi uliotekelezwa na upande mwingine. Mvutano huo umeenea hadi sekta ya barabara, ambapo magavana wanataka angalau asilimia 15 ya fedha za hazinaya ukarabati wa barabara, huku wengine wakitaka asilimia 42, zitengewe kaunti. Bunge la Kitaifa limependekeza asilimia tano pekee. Magavana pia wamepinga utekelezaji wa mpango wa maeneo ya viwanda katika kaunti, wakisema baadhi ya miradi ilianzishwa bila mashauriano ya kutosha na kabla ya masuala ya umiliki wa ardhi kutatuliwa. Wakati huo huo, serikali ya kitaifa imehusisha Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kukamilisha miradi iliyokwama, ikiwemo hospitali na viwanja vya michezo. Baadhi ya magavana wanahofia kuwa Rais atajipatia sifa za miradi hiyo baada ya kukamilika. Hata hivyo, viongozi wanaounga mkono ushirikiano wanasema serikali zote mbili zina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma. Aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa alisema Katiba inazitaka serikali hizo kushirikiana kwa manufaa ya wananchi. Mzozo huo unaendelea kuibua maswali kuhusu mipaka ya majukumu ya serikali hizo mbili, hasa pale miradi inapohusisha fedha za pamoja. Huku nchi ikielekea uchaguzi mkuu wa 2027, wataalamu wanaonya kuwa ushindani wa kisiasa haupaswi kuchelewesha huduma wala kufuta mafanikio ya ugatuzi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 28 Oct 2026 03:55:10
Bunge lakataa masharti magumu ya kuwaondoa wabunge madarakani
JARIBIO la baadhi ya wabunge kutaka masharti magumu ya kuwaondoa mamlakani wabunge kupitia kura ya wananchi limefeli Bungeni wakati wa kujadili Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi wa 2024. Mbunge wa Suba North Millie Odhiambo aliongoza juhudi za kutaka mbunge aondolewe mamlakani baada ya kupatikana na hatia ya kosa kubwa la jinai, kuhukumiwa na kufungwa jela kwa angalau miezi sita. Alisema masharti yaliyopendekezwa na Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria yalikuwa rahisi mno na yanaweza kutumiwa vibaya kisiasa. Kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati hiyo, hatua ya kumuondoa mbunge ingeanzishwa baada ya thuluthi moja ya wapiga kura waliosajiliwa katika kila wadi ya eneo bunge husika kutia saini ombi hilo. Kwa seneta, thuluthi moja ya wapiga kura katika kila eneo bunge la kaunti ingehitajika. Hata hivyo, uchaguzi mdogo ungeamuliwa kwa kura nyingi zaidi, huku mchakato wa kumwuondoa mbunge ukiruhusiwa kuanzishwa baada ya miaka miwili tangu kuchaguliwa kwake. "Hata kama nitasimama peke yangu, nitasimamia ukweli wangu. Ninapinga marekebisho haya kwa sababu kiwango mnachopendekeza ni cha chini mno," alisema Bi Odhiambo. Mbunge wa Saku, Dido Raso aliunga mkono msimamo huo, akionya kuwa kupata saini za thuluthi moja ya wapiga kura katika kila wadi kunaweza kuwa rahisi na kusababisha mchakato huo kutumiwa vibaya. Lakini Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung'wah na mwenzake wa Wachache Junet Mohamed walipinga masharti magumu, wakisema wananchi hawapaswi kuzuiwa kutumia haki yao ya kuwaondoa viongozi wasiowaridhia. Ichung'wah alisema kuweka kiwango cha asilimia 50 katika kila wadi kungeweza kurudia makosa yaliyofanya mahakama kufutilia mbali sheria za awali. Ibara ya 104 ya Katiba, inaitaka Bunge kuweka sheria zinazoeleza sababu na utaratibu wa kuwaondoa wabunge madarakani. Mnamo 2017, Mahakama Kuu ilitangaza vifungu kadhaa vya sheria kuhusu kuondolewa kwa wabunge kuwa kinyume cha Katiba, ikisema vilikuwa na dosari. Mjadala huo unaendelea huku Bunge likijaribu kuweka mfumo wa kisheria utakaowezesha wananchi kuwawajibisha wawakilishi wao bila mchakato huo kutumiwa vibaya.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 28 Oct 2026 02:55:48
Kibarua kizito cha upinzani 2027 ikiwadia
MAZUNGUMZO ya vinara wa upinzani yanaashiria kibarua kizito cha kuunda muungano imara utakaomkabili Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027. Huku uchaguzi ukisalia takriban miezi 10, viongozi hao wanakabiliwa na changamoto ya kukubaliana kuhusu mgombea mmoja wa urais, mgombea mwenza, uwiano wa kikanda na namna ya kuwavutia vijana wa Gen Z. Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, alisema Jumatatu baada ya kukutana na kiongozi wa DCP, Rigathi Gachagua, nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, kwamba upinzani hautakata tamaa katika juhudi za kuungana. "Tuna dhamira ya kuendelea kutafuta umoja," alisema Kalonzo. Gachagua naye alisema njia ya uhakika ya kumshinda Dkt Ruto ni kuafikiana kuhusu mgombea mmoja wa urais. "Tumekubaliana kuwa kumpata mgombea mmoja wa urais ndiyo njia ya uhakika ya kushinda uchaguzi mkuu ujao. Sote tumejitolea kufikia lengo hilo," alisema Gachagua. Aliongeza kuwa viongozi wako tayari kujitolea ili kumpata mtu atakayeongoza juhudi zao za kisiasa. Hata hivyo, kukubaliana kuhusu mgombea huyo kunatarajiwa kuwa kazi ngumu kwa sababu viongozi wengi wana malengo ya kuwania urais. Pia wanahitaji kumpata mtu anayeweza kuvutia wapigakura katika maeneo mbalimbali ya nchi. Utafiti wa Trends and Insights for Africa (Tifa) wa Julai ulionyesha kuwa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alikuwa na uungwaji mkono wa asilimia 15 iwapo angewania urais. Rais Ruto alikuwa na asilimia 24, huku aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i akiwa na asilimia 14 na Kalonzo asilimia 13. Gachagua alikuwa na asilimia saba. Viongozi pia wanapaswa kuzingatia uwezo wa kifedha, mitandao ya kisiasa na miundo ya kampeni ya kila mgombea. Eneo la Mlima Kenya ni muhimu kutokana na idadi yake kubwa ya wapigakura na mchango wake katika ushindi wa Ruto mwaka 2022. Kwa hivyo, nafasi ya mgombea mwenza inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mazungumzo ya upinzani. Tikiti ya Kalonzo na Sifuna imetajwa katika tafiti za hivi karibuni kuwa miongoni mwa zinazovutia. Hata hivyo, viongozi bado wanahitaji kuafikiana kuhusu namna ya kusawazisha maslahi ya maeneo mbalimbali. Seneta wa Kitui Enoch Wambua anasema mgombea wa pamoja anapaswa kutangazwa mapema ili awe na muda wa kutafuta rasilimali na kujenga miundo ya kisiasa. "Wakenya wanahitaji kujua mapema atakayemkabili Ruto kwenye kura. Nasikia kuna makubaliano ya karibu kwamba upinzani utawapa Wakenya zawadi ya Krismasi kwa kutangaza mgombeaji kabla ya mwisho wa mwaka," alisema. Naibu kiongozi wa Jubilee, Jeremiah Kioni, alisema baadhi ya viongozi wana uwezo wa kuvutia wapigakura lakini huenda wasiaminike kuongoza nchi, huku wengine wakiwa na sifa za uongozi lakini wakikosa nguvu za kuvutia kura. Vijana wa Gen Z pia ni sehemu muhimu ya hesabu za upinzani. Wachambuzi wanasema baadhi yao wanaweza kutaka mwelekeo mpya badala ya viongozi ambao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu. Katika eneo la Magharibi, Sifuna na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa wanaonekana kushindania ushawishi. Wamalwa alitembelea Gachagua Jumatatu akiwa na wazee, siku chache baada ya Sifuna kufanya ziara kama hiyo akiwa na wafuasi wa vuguvugu la Linda Mwananchi. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, aliyekuwa mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu na Wafula Wamunyinyi ni miongoni mwa viongozi wa eneo hilo waliounga mkono Sifuna. Mlima Kenya nako, DCP inashindana na Jubilee ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, PPK ya Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na PLP ya Martha Karua. Kaimu Katibu Mkuu wa DCP, John Methu, alisema chama kitachunguza vyama vinavyotaka kujiunga na upinzani ili kuhakikisha havitumiki kusababisha migawanyiko. Kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi alisema licha ya changamoto za kujenga muungano, lengo kuu ni kumuondoa Ruto madarakani kupitia kura na kurejesha utawala bora na kuheshimu Katiba. Rasimu ya mfumo wa kushirikiana inaonyesha kuwa muungano unapanga kuwasilisha makubaliano yake kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kufikia Machi 31, 2027. Makubaliano ya kugawana nyadhifa yanatarajiwa kukamilishwa kufikia wiki ya mwisho ya Machi. Rasimu hiyo pia inapendekeza vyama kugawana maeneo ya kuwania viti, ili kila chama kiweke wagombea katika maeneo ambako kina ushawishi mkubwa. Ramani ya mwisho ya maeneo hayo inapangwa kukamilishwa mwishoni mwa Februari 2027. Hata hivyo, Gachagua amepinga hadharani mpango huo wa kugawana maeneo, akisema ni kiti cha urais pekee kinachopaswa kutokuwa na ushindani wa ndani ya muungano. Mpango huo umekuwa ukizua utata katika miungano ya awali. Mwaka 2022, Raila Odinga alilazimika kuachana nao baada ya vyama vidogo kutishia kujiondoa katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya. Kiongozi wa DAP-K Wamalwa alisema kujenga muungano si tukio la mara moja bali ni mchakato wa mashauriano na mazungumzo endelevu, akitoa mfano wa muungano wa NARC uliomsaidia Mwai Kibaki kushinda uchaguzi wa 2002. Kwa sasa, changamoto kuu kwa upinzani ni kubadilisha matamshi ya umoja kuwa makubaliano kuhusu mgombea, nafasi za uongozi na kugawana maeneo kabla ya muda wa uchaguzi kuwadia.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 15:23:33
"Tuadhibuni sisi, lakini wake muwaache wake zetu," – Waititu
ALIYEKUWA gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na mfanyabiashara Charles Mbuthia Chege wameomba mahakama kuwaachilia huru wake zao katika kesi ya ufujaji wa fedha zinazohusishwa na zabuni ya barabara ya Sh588 milioni. Waititu na Chege, mkurugenzi wa kampuni ya Testimony Enterprises, walitoa ombi hilo Jumanne wakati wa kusikilizwa kwa hoja ya kupunguza adhabu katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Milimani. Kupitia mawakili wao, walisema Susan Wangari Ndung'u na Beth Wangechi Mburu hawakuhusika katika maamuzi ya zabuni hiyo, bali walikuwa washirika katika kampuni. Wakili wa Waititu alisema Susan hakuwa mtiaji saini wa akaunti za kampuni wala hakushiriki katika maamuzi ya biashara. Aliongeza kuwa Beth alikuwa ametia saini tu fomu za kuanzishwa kwa kampuni na hakuwa na jukumu katika shughuli zake. Waititu, ambaye tayari anatumikia kifungo cha miaka 12 kwa makosa yanayohusiana na ufisadi, aliomba mahakama izingatie adhabu ambayo tayari wamepitia. Alisema adhabu inapaswa kurekebisha mkosaji badala ya kuharibu maisha yake, akitaka mahakama iwape nafasi nyingine. Chege naye alisema mkewe alikuwa na hisa moja pekee katika kampuni na hakuwa na mamlaka ya kutia saini akaunti za benki. Alisema alikuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka 11 au kulipa faini ya Sh296 milioni. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga ombi hilo, ukisema kila mshtakiwa anapaswa kuwajibika kwa makosa aliyopatikana nayo na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Jaji wa Mahakama Kuu Rose Ougo alibadilisha uamuzi wa kuwaachilia huru washtakiwa kwa makosa ya ulanguzi wa fedha, akisema mahakama ya awali ilikosea kutathmini ushahidi na sheria. Waititu alipatikana na hatia ya kupokea Sh25 milioni kwa njia ya ufisadi kutoka kwa kampuni iliyopata zabuni ya barabara ya thamani ya Sh588 milioni. Mahakama inatarajiwa kutoa adhabu kwa washtakiwa hao wanne Novemba 2.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 15:00:52
Mutua kulipa Nonini fidia ya Sh3 milioni kwa kumchafulia jina
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Music Copyright Society of Kenya (MCSK) Ezekiel Mutua ameamriwa kumlipa mwanamuziki Nonini fidia ya Sh3 milioni kwa kumchafulia jina kupitia mitandao ya kijamii. Hakimu James Gitau alimwamuru Mutua kumlipa Nonini ambaye majina yake halisi ni Hubert Nakitare, Sh2.5 milioni kama fidia ya kawaida na Sh500,000 kama adhabu ya ziada kutokana na matamshi aliyotoa dhidi yake. Mutua pia ameamriwa kuondoa machapisho hayo kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii. Mzozo huo ulianza Januari 2024, MCSK ilipotangaza kuwa ingesambaza Sh20 milioni za mirahaba kwa wanachama wake 1,600. Nonini, ambaye alikuwa ameondoka katika MCSK Mei 2022, alihoji kiasi hicho baada ya kupata stakabadhi alizoamini zilionyesha kuwa shirika hilo lilikuwa limekusanya mamilioni zaidi ya lililotangazwa. Alisema MCSK ilikuwa imekusanya Sh109 milioni kutokana na mirahaba kati ya Januari na Desemba 2023, huku Sh57 milioni zikitumika kulipa mishahara ya wafanyakazi. Mwanamuziki huyo, anayejulikana kama Godfather wa Genge, alichapisha madai yake mtandaoni akitaka uwazi kuhusu jinsi fedha za wanamuziki zilivyokuwa zikisimamiwa. Hata hivyo, mjadala huo uligeuka kuwa mzozo binafsi baada ya Mutua kumtaja Nonini kuwa mkimbizi wa sheria na kumshutumu kwa kufuja fedha za wanamuziki alipokuwa akihudumu katika mashirika mengine ya hakimiliki. Mutua pia alidai kuwa Nonini alikuwa amesambaza stakabadhi bandia kuhusu hesabu za MCSK na kusema suala hilo lilikuwa limeripotiwa kwa polisi. Nonini aliambia mahakama kuwa madai hayo yalimsawiri kama mhalifu aliyekimbilia Amerika kukwepa mkono wa sheria, hivyo kuharibu sifa yake. Alisema Mutua pia alirudia madai hayo katika mahojiano na kituo cha redio cha Hot 96. Hakimu alisema matamshi hayo yalikuwa na uwezo wa kuharibu sifa ya Nonini kwa kumsawiri kama mtu anayekwepa sheria. Hukumu hiyo ni pigo jingine kwa Mutua, ambaye pia anakabiliwa na kesi ambayo Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), inataka arejeshe Sh27 milioni. Tume hiyo inadai alipandisha mshahara wake na kujilipa marupurupu kinyume cha sheria alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Film Classification Board (KFCB).
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 06:55:27
Afisa aliyehepa baada ya mauaji ya wakili kukaa rumande siku 14
AFISA wa Polisi Kenneth Kipkemboi Sang amezuiliwa kwa siku 14 ili kuhojiwa kuhusu mauaji ya wakili Mathew Kyalo Mbobu na mtaalamu wa tiba ya ubongo, Dkt Victoria Nthunya Mutiso. Sang, aliyekamatwa Oktoba 24, 2026, jijini Eldoret alipokuwa akijaribu kuuza gari lake, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Paul Mutai katika Mahakama ya Milimani, Nairobi. Upande wa mashtaka ulisema bastola aliyokabidhiwa afisa huyo ndiyo iliyotumika kumuua Dkt Mutiso Julai 29, 2026. Pia alituhumiwa kutoroka kazi na kukimbilia nje ya nchi baada ya mauaji hayo. Mwendesha mashtaka Virginia Kariuki aliomba mshukiwa azuiliwe bila dhamana, akisema anaweza kutoroka au kuathiri mashahidi. Sang alipinga ombi hilo, akisema uchunguzi tayari umefanyika kwa kina. Hakimu Mutai aliamuru azuiliwe katika Kituo cha Polisi cha Kilimani hadi Novemba 9, 2026, uchunguzi ukiendelea kubaini nafasi yake katika mauaji hayo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 05:55:57
Majonzi mtaa ukifiwa na mapasta watatu kupitia ajali Mtito Andei
WAKAZI wa mtaa wa Bangladesh, eneo la Mikindani, Mombasa, wamezama katika majonzi kutokana na vifo vya wachungaji watatu na waumini wengine katika ajali iliyoangamiza watu 24 katika eneo la Kanga, barabara ya Mombasa-Nairobi, Kaunti ya Makueni, Jumapili asubuhi. Wachungaji Joseph Vura wa Campaign for Salvation and Healing Ministry (CASHEM), Fonex Paul wa River of Life na Isaac Juma wa Grace Healing Sanctuary walikuwa kati ya waliokuwa wakirejea kutoka mazishi ya mwenzao katika Kaunti ya Kakamega, basi walimokuwa lilipogonga lori la mizigo lililokuwa limesimama. Katika mtaa wa Bangladesh, familia na marafiki wa marehemu bado wanatatizika kukubali ukweli wa vifo hivyo, huku wengine wakipanga mazishi na kuomboleza wapendwa wao. Bi Judith Awino, ambaye aliishi na shemeji yake Hollon Oduor Waganda kwa miaka 10, alisema alipokea habari za ajali hiyo alipokuwa akiomba katika Kanisa la Lamb of God, Mikindani. "Mume wangu alinipigia simu kuniuliza kuhusu wachungaji waliofariki katika ajali. Hakujua kwamba mdogo wake pia alikuwa ndani ya basi hilo. Tulipojaribu kumpigia simu, hakupokea," alisema. Familia ilimtuma ndugu mwingine wa marehemu aliyekuwa Samburu, kaunti jirani ya Kwale, kwenda Makueni kuthibitisha hali yake. Baadaye aliwapigia simu na kuwathibitishia habari walizokuwa wakihofia. Bi Awino alisema Waganda alikuwa ametembelea nyumbani kwake Jumanne kuazima sanduku la kusafiria. "Waliondoka, lakini sasa wanarejea nyumbani wakiwa wamefariki. Familia yetu imeshtuka," alisema. Mwili wa Waganda ulikuwa ukisubiri kuhamishwa hadi hifadhi ya ya Hospitali ya Coast General kabla ya kusafirishwa Siaya kwa mazishi. Katika Mataa ya Ndege, Jomvu, wakazi wanaomboleza Mchungaji Fonex Paul, aliyehudumu katika kanisa lake kwa zaidi ya miaka 10. Jirani yake Peter Bendi alisema marehemu alikuwa mwenye huruma, mchangamfu na aliyesaidia watoto wa eneo hilo kwa masomo ya ziada. Mchungaji huyo ameacha mkewe Ann Biyaki. Katika Grace Healing Sanctuary, mchungaji msaidizi Fredrick Ochieng Odhiambo alisema kifo cha Juma kimeacha pengo kubwa katika jamii. Juma ameacha mke na watoto wanne. Marehemu Vura, Juma na Fonex walikuwa na makanisa yaliyokuwa umbali mfupi katika mtaa huo wenye wakazi wengi. Wakati huo huo, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir na Mbunge wa Likoni Mishi Mboko Jumatatu walitembelea maaskofu Zachariah Mwagandi na Cosmas Oduor Nyangweso, wanaopokea matibabu katika Hospitali ya Coast General baada ya kunusurika ajali hiyo. Ajali hiyo ilitokea takriban wiki tatu baada ya watu 17 waliokuwa wakisafiri kwenda Subukia Shrine kufariki katika ajali ya Salama, barabara hiyo hiyo, Oktoba 4
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 27 Oct 2026 04:55:17
Watahiniwa waonywa kuhusu udanganyifu katika mitihani ya kitaifa
SERIKALI imewaonya wanafunzi na wasimamizi wa mitihani dhidi ya udanganyifu katika tathmini na mitihani ya kitaifa iliyoanza jana, ikisema watakaopatikana wataadhibiwa, kukiwemo kufutiwa kwa matokeo. Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema wanafunzi 3,634,846 wamejisajili kwa tathmini na mitihani ya mwaka huu, wakiwemo 1,380,463 wa KPSEA, 1,206,028 wa KJSEA na 1,048,355 wa KCSE. "Mwanafunzi yeyote atakayepatikana na hatia atachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufutiwa matokeo," akasema Bw Ogamba, akionya wazazi dhidi ya watu wanaodai kuuza mitihani. Alisema polisi hawajawekwa ndani ya vituo vya KPSEA na KJSEA ili wanafunzi wafanye tathmini katika mazingira tulivu bila vitisho. Serikali pia imeweka mipango ya kukabiliana na mvua, mafuriko, ukosefu wa usalama na maeneo magumu kufikika. Katibu anayesimamia Idara ya Elimu ya Msingi John Ololtuaa alisema walimu na maafisa 342,005 wamepewa jukumu la kusimamia shughuli hiyo, huku watahiniwa 50,873 wakitarajiwa kusahihisha mitihani. Katika kaunti za Kisii na Kisumu, tathmini zilianza bila matatizo makubwa. Mkurugenzi wa Elimu Kisumu Magara Onduso alisema vifaa vilisambazwa kwa wakati na usalama kuimarishwa. "Tumefanya maandalizi ya kutosha. Wasimamizi wamewasili kwa wakati na vifaa vimefikishwa mapema," alisema. Hata hivyo, Wanafunzi Kaunti ya Murang'a wanakabiliwa na wasiwasi wa njaa, huku nyumba 80,000 zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Kaskazini Mashariki, baadhi ya wazazi Garissa walidai shule zilikuwa zikitoza kati ya Sh10,000 na Sh30,000 kwa kila mwanafunzi kwa madai ya kupanga udanganyifu. Mkurugenzi wa Elimu wa eneo hilo Adan Roble alisema ofisi yake haikuwa imepokea taarifa hizo na akaonya watakaohusika kuwa wataadhibiwa. Katika eneo la Bonde la Ufa, wanafunzi katika maeneo ya Turkana yaliyoathiriwa na mashambulizi ya majambazi walisindikizwa hadi vituoni salama. Mvua na mafuriko pia yalilazimu maafisa kutumia boti kufikisha vifaa katika baadhi ya maeneo ya Turkana. Baringo iliripoti changamoto za taarifa za watahiniwa, lakini zilitanzuliwa kwa ushirikiano na KNEC. Trans Nzoia ilisema maandalizi yalikuwa yamekamilika. Nairobi, vifaa vilisambazwa bila matatizo, huku Mombasa na maeneo mengine ya Pwani yakichukua tahadhari dhidi ya mvua na mafuriko. Lamu iliweka boti tayari kusafirisha wasimamizi na maafisa wa usalama kwenye visiwa vya mbali. Katika eneo la Kati, maafisa walisema watawafikishia mitihani watahiniwa watakaougua hospitalini. Serikali imesema itashirikiana na Wizara ya Usalama kukabiliana na changamoto zozote wakati zoezi likiendelea. KPSEA inaendelea hadi Oktoba 28, KJSEA hadi Oktoba 30, huku KCSE ikiendelea hadi Novemba 20, 2026.
read moreRight Column Content