taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 18 Nov 2026 04:55:32
Rais Ruto kwenye mizani akihutubia Bunge kuhusu hali ya taifa Alhamisi
RAIS William Ruto anatarajiwa kutoa hotuba yake ya nne kuhusu hali ya taifa kesho mbele ya kikao cha pamoja cha Bunge la Kitaifa na Seneti, huku serikali yake ikikabiliwa na changamoto za deni la taifa, gharama ya maisha na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Hotuba hiyo inajiri siku chache baada ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge (PBO) kuonya kuwa serikali ina nafasi finyu ya kifedha kutekeleza mipango yake kutokana na mzigo mkubwa wa madeni. Ripoti ya PBO kuhusu chaguo za bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2027/28 inaonyesha kuwa bajeti ya kawaida inatarajiwa kuwa Sh5.3 trilioni, huku Sh1.5 trilioni zikitumika kulipa riba ya madeni pekee. Kiasi hicho ni zaidi ya mara mbili ya fedha zinazotengewa miradi ya maendeleo. Deni la taifa limefikia Sh13.1 trilioni, huku serikali ikirekodi upungufu wa mapato wa Sh60.2 bilioni kufikia Juni 2026. Hotuba hiyo pia inatolewa miezi minane kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2027, hivyo Rais Ruto anatarajiwa kueleza mafanikio ya serikali yake na kutoa majibu kuhusu changamoto zinazowakabili wananchi. Mtaalamu wa utawala Barasa Nyukuri, anasema hotuba hiyo itakuwa kipimo cha utendaji wa serikali, hasa ikilinganishwa na ahadi zake za kiuchumi na miradi mikubwa. Anasema Rais anapaswa kueleza jinsi atakavyokabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana, ufadhili wa vyuo vikuu, maandalizi ya uchaguzi, deni la taifa na gharama ya maisha. Masuala mengine yanayotarajiwa kuangaziwa ni mpango wa nyumba za bei nafuu, changamoto za ufadhili wa huduma za afya, usalama kufuatia visa vya utekaji nyara na mageuzi katika sekta mbalimbali. Kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 132(1)(b), Rais anapaswa kuhutubia kikao maalumu cha Bunge mara moja kila mwaka. Pia anatakiwa kuripoti hatua zilizochukuliwa kutekeleza maadili ya kitaifa na maendeleo yaliyopatikana katika kutimiza wajibu wa Kenya kimataifa. Rais pia anatarajiwa kueleza unavyoendelea mpango wake wa mageuzi wa miaka 10 wa thamani ya Sh5 trilioni, aliotangaza katika hotuba yake ya Novemba 20, 2025. Mpango huo ulijumuisha kujenga mabwawa makubwa 50, kupanua kilimo cha unyunyuzaji, kuweka lami kilomita 28,000 za barabara na kupanua kilomita 2,500 za barabara kuu kuwa njia mbili. Pia aliahidi kupanua reli ya kisasa (SGR) hadi Malaba, kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, bandari za Mombasa na Lamu na kuongeza uzalishaji wa umeme hadi megawati 10,000. Hata hivyo, PBO inasema licha ya juhudi za kuimarisha uchumi, ukuaji bado haujafikia kiwango kinachohitajika. Ripoti hiyo inaonya kuwa malipo ya riba yanapunguza fedha zinazoweza kutumiwa kufadhili huduma na miradi mingine. Kwa sababu hiyo, inashauri serikali kuzingatia matumizi yenye ufanisi badala ya kuanzisha miradi mikubwa inayohitaji fedha nyingi. Waziri wa Fedha John Mbadi, anasema serikali imepiga hatua katika kuanzisha Hazina ya Kitaifa ya Miundombinu (NIF), ambayo inalenga kufadhili miradi bila kutegemea mikopo mipya. Serikali inasema hazina hiyo ina mtaji wa awali wa Sh310.6 bilioni, zikiwemo Sh104 bilioni zilizopatikana kupitia uuzaji wa hisa za Kampuni ya Bomba la Mafuta Kenya (KPC) na Sh206 bilioni zilizotarajiwa kutokana na kupunguzwa kwa hisa za serikali katika Safaricom. Hata hivyo, uamuzi wa Mahakama Kuu kubatilisha uuzaji wa asilimia 15 ya hisa za serikali katika Safaricom umeibua mashaka kuhusu sehemu ya fedha hizo. Bw Nyukuri anasema wananchi wanataka majibu ya moja kwa moja kuhusu ajira, ufisadi na ushuru, badala ya ahadi za miradi ya muda mrefu. Anasema changamoto kuu kwa Rais ni kuwashawishi Wakenya kuwa uwekezaji wa serikali unaleta nafuu katika maisha yao ya kila siku kabla ya uchaguzi wa 2027. PBO pia inasema mafanikio ya mpango wa nyumba za bei nafuu yatategemea kasi ya kuuza nyumba zilizokamilika ili fedha hizo zitumike kujenga nyingine.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
Msikose kufanya haya ili ufurahie uhusiano wa kimapenzi
Kudumisha uhusiano wa kimapenzi si jambo rahisi kama wengi wanavyodhani. Wapenzi wanaweza kuanza safari yao wakiwa na furaha, mapenzi na matumaini makubwa, lakini kadiri muda unavyopita, changamoto za maisha, tofauti za tabia na kutoelewana vinaweza kuanza kuwatenganisha. Hata hivyo, uhusiano wenye afya haujengwi kwa bahati. Unahitaji juhudi za watu wawili walio tayari kupendana, kuheshimiana na kutafuta suluhu wanapokumbana na matatizo. Moja ya nguzo muhimu ni kupendana kwa dhati. Mapenzi hayapaswi kuwa maneno matamu pekee, bali yaonekane kupitia matendo ya kila siku, kujali na kuthaminiana. Kila mmoja anapaswa kumfanya mwenzake ajihisi kuwa anathaminiwa. Ukweli pia ni muhimu. Uongo, hata unaposemwa kwa nia ya kuficha jambo dogo, unaweza kuharibu imani ambayo imechukua muda mrefu kujengwa. Wapenzi wanapaswa kuwa wakweli na kuzungumza wazi kuhusu mambo yanayowasumbua. Mawasiliano ni daraja linalowaunganisha watu wawili. Badala ya kunyamaziana au kutegemea mwenzako asome mawazo yako, eleza hisia zako kwa utulivu. Usifiche maumivu kwa kusema kila kitu kiko sawa ilhali moyoni unaumia. Ni bora kueleza kinachokusumbua kuliko kuruhusu kinyongo kikue. Pia, wapenzi wanapaswa kudumisha utamu katika uhusiano wao. Kumtakia mwenzako siku njema, kumpongeza na kumshukuru vinaweza kuleta furaha kubwa. Usisubiri siku ya kuzaliwa au maadhimisho maalumu ndipo uonyeshe kuwa unamjali. Kusamehe ni sehemu nyingine ya safari ya mapenzi. Hakuna binadamu mkamilifu, hivyo makosa yanaweza kutokea. Mtu anapokukosea na kuomba msamaha kwa dhati, ni muhimu kutafuta namna ya kuendelea mbele. Hata hivyo, kusamehe hakumaanishi kuvumilia ukatili, dhuluma au tabia inayojirudia na kuhatarisha usalama wako. Aidha, kiburi kinapaswa kuachwa mlangoni. Wapenzi wanapokosana, kila mmoja akitaka kushinda mabishano, tatizo dogo linaweza kuwa kubwa. Kuomba msamaha hakupunguzi thamani ya mtu. Muhimu ni kuhakikisha kuwa unapotamka samahani, unamaanisha na uko tayari kubadilika. Ni vyema pia kuepuka vitisho vya kuachana kila mara mnapokosana. Kauli kama hizo zinaweza kumfanya mwenzako akose usalama wa kihisia na kuanza kuishi kwa hofu ya kuachwa. Badala yake, jadilianeni kuhusu tatizo na namna ya kulitatua. Usimlinganishe mpenzi wako wa sasa na wapenzi wa zamani. Kila mtu ana tabia na namna yake ya kuonyesha mapenzi. Kuzungumzia wapenzi wa zamani kwa dharau au kumtaka mwenzako afanane nao kunaweza kumuumiza na kumfanya ajione hafai. Uhusiano mzuri pia unahitaji kutoa na kupokea. Si haki mtu mmoja ndiye ajitume kila wakati huku mwingine akifurahia matokeo. Wote wanapaswa kuchangia kwa upendo, muda, heshima na uangalifu. Zaidi ya yote, wapenzi wanapaswa kuheshimu hisia za wenzao. Wanapogombana, ni vizuri kutafuta suluhu mapema badala ya kuruhusu hasira na ukimya vitawale kwa siku nyingi. Na usilazimishe kuwa mpenzi mkamilifu. Jitahidi kuwa mwenzi anayefaa, anayesikiliza, anayejali na aliye tayari kujifunza. Mapenzi imara hayahitaji watu wasiokosea, bali watu wanaokubali kuwajibika na kukua pamoja
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
Sababu zinazoweza kufanya mtu kuagizwa kulipa ex wake posho la matunzo
WATU wengi wanapoachana au kutengana katika ndoa, hudhani kuwa kila mmoja anapaswa kuanza maisha yake bila kuwajibika tena kwa mwenzake. Hata hivyo, sheria inatambua kuwa kuna mazingira ambapo mtu anaweza kuamriwa kuendelea kumtunza mchumba wake, hata baada ya ndoa kuvunjika. Sheria inapatia mahakama mamlaka ya kutoa agizo la matunzo kwa mke, mume au mpenzi wa zamani iwapo kuna sababu zinazohalalisha hatua hiyo. Lengo ni kuhakikisha kuwa mtu ambaye anastahili kupata msaada wa kifedha haachwi bila mahitaji muhimu kutokana na mchumba wake kukwepa wajibu. Moja ya sababu zinazoweza kumfanya mtu aagizwe kulipa matunzo ni kukataa au kupuuza wajibu wa kumtunza mchumba wake kama sheria inavyotaka. Hii ina maana kuwa mtu hawezi kujiondoa katika wajibu wake kwa makusudi na kumwacha mwenzake akihangaika kutafuta mahitaji ya msingi. Pia, mahakama inaweza kutoa agizo hilo pale ambapo mmoja wa wanandoa amemtelekeza mwenzake. Agizo hilo linaweza kuendelea kutumika kwa muda wote ambao hali ya kutelekezwa inaendelea. Hivyo, mtu anayeondoka nyumbani na kuacha mwenzi wake bila msaada anaweza kukabiliwa na hatua za kisheria. Matunzo yanaweza pia kuamriwa wakati kesi za ndoa zinaendelea mahakamani. Hii ni muhimu kwa sababu kesi za kutengana au talaka zinaweza kuchukua muda, huku mmoja wa wanandoa akiwa hana uwezo wa kujikimu bila msaada wa mwenzake. Aidha, mahakama inaweza kuamua kuhusu matunzo wakati wa kutoa uamuzi wa kutengana au kuvunja ndoa, au hata baada ya uamuzi huo kutolewa. Kwa hivyo, kupata talaka hakumaanishi moja kwa moja kwamba wajibu wote wa kifedha kati ya waliokuwa wanandoa unaisha. Sheria pia inazingatia mazingira ya kipekee ambapo mahakama inatoa uamuzi wa kuchukulia kuwa mwenzi amefariki, lakini baadaye anapatikana akiwa hai. Katika hali hiyo, mahakama inaweza kuagiza matunzo kwa mujibu wa mazingira ya kesi. Hata hivyo, agizo la matunzo si jambo linalotolewa kiholela. Mtu anayedai anastahili kusaidiwa anapaswa kuwasilisha ombi mahakamani ili mazingira yake yazingatiwe. Kwa ujumla, sheria inalenga kuzuia hali ambapo mmoja wa wanandoa anaachwa katika mazingira magumu kwa sababu ya kutengana au kuvunjika kwa ndoa. Pia inasisitiza kuwa wajibu wa kifedha haupaswi kupuuzwa kwa sababu tu uhusiano wa kimapenzi umefikia kikomo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Millie akataa kutumiwa kushambulia Uhuru kufaidi Ruto
MBUNGE wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo amesema hana sababu ya kumshambulia rais mstaafu Uhuru Kenyatta ili kupongeza miradi inayotekelezwa na serikali ya sasa inayoongozwa na Rais William Ruto. Millie asema hataki kujiunga na mijadala ya kisiasa inayomtaka kukosoa tawala zilizopita kila anapotambua mafanikio ya utawala wa sasa. Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumatano, Novemba 18, 2026, mbunge huyo alitaja daraja lililojengwa Suba Kaskazini wakati wa utawala wa Uhuru kama mfano wa maendeleo yanayostahili kutambuliwa. "Watu wanataka nimshambulie Uhuru. Lakini Uhuru alijenga daraja Suba Kaskazini. Kwa kweli, kwa nini nimshambulie?" aliuliza. Alisema anaweza kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Ruto bila kumkosoa mtangulizi wake. Millie alisema changamoto za maendeleo nchini haziwezi kulaumiwa kwa serikali moja pekee, akibainisha kuwa tawala zilizopita zimekuwa zikikabiliana na matatizo yanayofanana. Aliongeza kuwa nchi nyingi za Afrika pia zinakabiliwa na changamoto za utawala na maendeleo. Mbunge huyo pia alihoji matumizi ya fedha katika serikali za kaunti, akisema kiasi kikubwa cha fedha kinachotumwa huko hakionekani kuleta maendeleo yanayotoshana nacho. Alisema mjadala kuhusu ufisadi umejikita zaidi katika serikali ya kitaifa huku matumizi mabaya ya fedha katika ugatuzi yakipuuzwa. "Fedha nyingi sana zinatumwa katika kaunti zetu, lakini kuna nini cha kuonyesha?" aliuliza. Alipendekeza mfumo wa usimamizi na ukaguzi wa miradi ya Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) uweze kutoa mafunzo kuhusu kuimarisha uwajibikaji katika kaunti. Millie, ambaye alisema anasomea shahada ya uzamivu katika masuala ya maendeleo, alisema anachunguza sababu zinazofanya Kenya ishindwe kutatua changamoto za muda mrefu za utawala na maendeleo. Katika mahojiano hayo, alikanusha nia ya kuwania ugavana wa Homa Bay, akisema kiti hicho si sehemu ya malengo yake ya kisiasa. Alisema wakazi wa Homa Bay ndio watakaoamua watakayemchagua, akisisitiza kuwa uchaguzi huo hauhusu ushindani kati yake na Gavana Gladys Wanga pekee.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Upinzani wapatia Ruto silaha kuwaponda
KUONDOKA kwa vinara wakuu wa upinzani katika mkutano na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumempa Rais William Ruto nafasi nyingine ya kuwashambulia kisiasa, akitumia mgogoro huo kuonyesha kuwa wapinzani hawana umoja, mgombeaji wala ajenda ya pamoja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Vinara hao, wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, waliondoka kwenye mkutano wa Novemba 19 baada ya kupinga utaratibu wa majadiliano na mada ambazo IEBC ilikuwa imepanga kuwasilisha. Walioandamana nao ni aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, miongoni mwa wengine. Hata hivyo, hatua hiyo imegeuza mjadala kutoka kwa madai yao kuhusu maandalizi ya uchaguzi na kuuelekeza kwenye uwezo wa upinzani kuendesha mazungumzo na kuunda mkakati mmoja wa kumng'oa Ruto mamlakani. Rais hakupoteza muda kutumia fursa hiyo. Akiwa katika ziara yake ya Magharibi mwa Kenya, aliwashambulia wapinzani akiwataka waache kuilaumu IEBC na badala yake wajipange kushindana naye katika uchaguzi. 'IEBC haina kura, kura ziko kwa wananchi,' alisema Ruto, akiwakosoa viongozi hao kwa kuonekana kuhusisha tume na mizozo yao ya kisiasa. Pia, aliwataka wapinzani waache kuzunguka wakilalamika kuhusu tume hiyo na badala yake waamue watakayemsimamisha kugombea urais, sera watakazotumia na ajenda watakayowasilisha kwa wananchi. Kwa Ruto, kuondoka kwa wapinzani mkutanoni ni fursa ya kuendeleza simulizi kwamba washindani wake hawajajiandaa kwa uchaguzi wa 2027 na huenda wanatafuta mtu wa kulaumu iwapo watashindwa. Lakini Kalonzo na Gachagua walisisitiza kuwa hawakuwa tayari kuhusishwa na mchakato ambao, kwa maoni yao, haukuwa na dhamira ya kushughulikia masuala muhimu ya uchaguzi. Gachagua alisema upinzani ulikuwa umeomba IEBC kuunda timu ya kiufundi Januari 28, 2026 ili kujadili maandalizi ya uchaguzi, lakini madai yao hayakushughulikiwa licha ya kuwasilisha barua na mawasiliano kadhaa. Alisema upinzani hautakubali Wakenya kuingia katika uchaguzi ambao uaminifu wake unatiliwa shaka. 'Tunakataa kuwaruhusu Wakenya kuingia katika mchakato wa uchaguzi uliopangwa kuibiwa bila wao kujua,' alisema. Kalonzo alisema walihudhuria mkutano huo kwa nia njema lakini hawakuridhishwa na namna tume ilivyokuwa ikiendesha mashauriano. 'Tulikuja IEBC leo kwa nia njema na tulitarajia nia hiyo hiyo kutoka kwao. Nia njema huonyeshwa kwa vitendo: tume huru, isiyopendelea upande wowote na iliyojiandaa. Leo hatukupata hayo. Ndiyo maana tumeondoka,' alisema. Kwa upande wake, Maraga alisema hawakutaka kwenda kusikiliza hotuba za maafisa wa IEBC kuhusu mipango yao bila kupata nafasi ya kujadili wasiwasi wao. 'Tunataka kushirikiana na IEBC, hatutaki kwenda kufundishwa. Ndiyo maana tuliondoka,' alisema. Upinzani unataka ukaguzi huru wa sajili ya wapigakura ili kuondoa majina ya watu waliofariki, waliosajiliwa mara mbili na wasiostahili kupiga kura. Pia unataka mabadiliko ya mfumo wa kutuma na kujumlisha matokeo ya urais, ukipendekeza kila eneo bunge kati ya 290 liwe na sava huru za matokeo yanayoweza kufikiwa na vyama, wagombeaji na vyombo vya habari. Unataka pia kuondolewa kwa kituo kikuu cha kujumlishia matokeo ya urais Bomas of Kenya, majaribio ya kupiga kura kwa njia ya kielektroniki kwa Wakenya wanaoishi ughaibuni na kupeperushwa moja kwa moja kwa shughuli za kupiga, kuhesabu na kutangaza kura. Haya ni masuala muhimu yanayohitaji majibu ya wazi kutoka kwa IEBC. Hata hivyo, kuondoka kabla ya kusikiliza maelezo ya tume kumeifanya serikali kupata nafasi ya kuhoji dhamira ya upinzani. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Edung Ethekon alisema ilihuzunisha kuona baadhi ya viongozi wakiondoka kabla ya majadiliano ya kina kuanza. 'Kuondoka kwenye mazungumzo kabla ya majadiliano ya kina kuanza hakusaidii kutatua masuala ya uchaguzi. Kunawanyima wahusika wote nafasi ya kubadilishana mawazo, kufafanua misimamo na kujenga mwafaka,' alisema. Alisema viongozi hao walikosa fursa ya kusikiliza maelezo kuhusu kiwango cha maandalizi ya uchaguzi, hatua zilizopigwa na changamoto zinazokabili tume. Ethekon aliwahimiza viongozi kuwasilisha mapendekezo yao rasmi na kuendelea kushiriki mashauriano badala ya kujiondoa. Gavana wa Kisii Simba Arati pia alikosoa hatua ya upinzani, akisema huenda viongozi hao walitaka kujenga taswira kwamba wametengwa ili watakaposhindwa uchaguzi wawe na sababu ya kupinga matokeo mahakamani. Kwa upande wake, mwenyekiti wa UDA Cecily Mbarire alihoji kwa nini upinzani uliondoka badala ya kuwasilisha hoja zake ndani ya mkutano. Wachambuzi wa siasa wanasema changamoto kubwa kwa Kalonzo, Gachagua, Sifuna, Karua na wenzao sasa ni kuhakikisha madai yao kuhusu uadilifu wa uchaguzi hayafunikwi na mzozo wa kisiasa walioanzisha. 'Wanapaswa pia kuonyesha kuwa wanaweza kukubaliana kuhusu ajenda ya pamoja na mgombeaji wa urais, masuala ambayo Ruto amekuwa akiyatumia kuhoji uwezo wao wa kuunda serikali,' asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki. Vinginevyo, asema, kwa kuondoka mkutanoni, huenda wameingia katika mtego wa kisiasa wa Ruto, wakimpa nafasi ya kuendelea kuwaponda kwa udhaifu wao huku maswali kuhusu maandalizi ya uchaguzi yakisalia bila majibu ya kutosha.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
Hofu ya Ruto kuhusu usalama wa nchi 2027 ikikaribia
SERIKALI ya Rais William Ruto imeibua wasiwasi kuhusu usalama wa nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, ikionya kuwa kuongezeka kwa magenge ya wahalifu, joto la kisiasa, siasa za kikabila na matamshi ya uchochezi kunaweza kufanya Kenya kuwa katika hatari ya machafuko. Katika ripoti ya hali ya usalama nchini iliyowasilishwa Bungeni na Rais Ruto wakati wa hotuba yake ya Mustakabali wa Taifa, serikali inasema ushindani wa kisiasa unaozidi kupamba moto unaweza kudhoofisha umoja wa kitaifa na kuhatarisha amani kabla ya uchaguzi. Ripoti hiyo inayohusu kipindi cha Septemba 2025 hadi Agosti 31, 2026, inaeleza kuwa mwelekeo wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027 ndio wasiwasi mkubwa zaidi kwa idara za usalama. Serikali inasema mchujo wa vyama, mapitio ya mipaka ya maeneo ya uchaguzi na usajili wa wapigakura ni baadhi ya hatua zinazoweza kuchochea ushindani mkali na hata vurugu. "Safari ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 ndiyo wasiwasi mkuu. Kura za mchujo za vyama, mapitio ya mipaka na usajili wa wapigakura vitaongeza ushindani wa kisiasa, huku hali katika kipindi hiki ikionyesha hatari kubwa ya vurugu zinazochochewa katika hatua hizo," inasema ripoti hiyo. Kwa mujibu wa serikali, kipindi hiki hushuhudia mgawanyiko mkubwa wa kisiasa, kutovumiliana kati ya mirengo hasimu na juhudi za wanasiasa kuchochea wafuasi dhidi ya wapinzani wao. Ripoti hiyo pia inadai kuwa baadhi ya wanasiasa wametumia vurugu katika maeneo mbalimbali kujionyesha kuwa na nguvu na kuwatisha washindani wao. Serikali inaonya kuwa miungano ya kisiasa inayojengwa kwa misingi ya ukabila pamoja na ushindani wa kikanda inaweza kugawa nchi na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa. Matamshi ya chuki nayo yametajwa kuwa tishio kubwa, hasa kutokana na uwezo wake wa kuchochea migawanyiko ya kikabila, ubaguzi na vurugu.Serik ali inakumbusha kuwa matamshi ya uchochezi yalichangia pakubwa machafuko yaliyofuatia uchaguzi wa 2007, yaliyosababisha vifo, watu kuhama makazi yao na mali kuharibiwa. Mwezi uliopita, Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) ilionya kuwa matamshi ya chuki yanaongezeka kuelekea uchaguzi wa 2027, hasa kwenye mitandao ya kijamii. Wiki iliyopita, maaskofu wa Kanisa Katoliki pia waliwataka wanasiasa kudhibiti ndimi zao, wakionya kuwa matamshi ya uchochezi yanaweza kutumbukizwa nchi katika machafuko. Ingawa ripoti inasema hali ya usalama nchini imeendelea kuwa tulivu kwa jumla, inataja changamoto nyingine zinazohitaji kushughulikiwa, zikiwemo ugaidi, itikadi kali za kidini, ulanguzi wa dawa za kulevya, biashara ya silaha haramu, uhalifu wa kimtandao, wizi wa mifugo na biashara ya bidhaa bandia. Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kusambaza taarifa za uongo, kuandikisha vijana katika magenge ya wahalifu na kuratibu maandamano pia kumetajwa kuwa tishio. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, shughuli hizo zilichangia vifo vya watu 17, uharibifu wa mali na kutatiza shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, visa vya uhalifu viliongezeka kutoka 97,366 katika kipindi cha 2024/2025 hadi 97,946 kati ya Septemba 2025 na Agosti 2026, ongezeko la visa 580. Serikali inasema ongezeko la magenge ya wahalifu limekuwa likitatiza juhudi za kudumisha usalama, huku makundi hayo yakitumia vitisho, vurugu na kuwashawishi vijana walio katika mazingira magumu kujiunga na shughuli za uhalifu. Ripoti inasema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, changamoto za kiuchumi na migogoro ya kijamii ni baadhi ya sababu zinazochochea ukuaji wa magenge hayo. Hata hivyo, kinachotia wasiwasi zaidi ni madai kuwa baadhi ya makundi hayo yanatumiwa na wanasiasa kuvuruga mikutano ya wapinzani, kuwatisha wananchi, kuharibu mali na kuchochea mapigano. Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alikabiliwa na maswali magumu kutoka kwa wabunge mwezi huu kuhusu kuongezeka kwa utamaduni wa kutumia wahuni katika shughuli za kisiasa. Bw Murkomen alijibu kuwa baadhi ya magenge hayo yanafadhiliwa na wanasiasa, akidai kuwa viongozi wanaohusika hukalia viti vyao Bungeni na katika nyadhifa za juu za kisiasa huku wakitumia ushawishi wao kuzuia polisi kuchukua hatua. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) nayo imeonya kuwa haitawavumilia wanasiasa watakaohusishwa na kufadhili au kutumia magenge hayo wakati wa uchaguzi. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alisema tume hiyo ina kamati inayosimamia utekelezaji wa kanuni za maadili ya uchaguzi na itachukua hatua dhidi ya wanaokiuka masharti hayo. Alisema wanasiasa watakaopatikana na ushahidi wa kufadhili, kuhifadhi au kuwezesha magenge ya wahalifu wanaweza kutozwa faini au hata kuondolewa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi. Katika kipindi kinachochunguzwa, vyombo vya usalama vilirekodi kukamatwa kwa washukiwa 1,316 wanaohusishwa na magenge hayo, ikilinganishwa na 602 katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia. Ongezeko hilo la watu 714, kwa mujibu wa serikali, linaonyesha kuimarishwa kwa operesheni za usalama lakini pia kuibuka na kupanuka kwa magenge mapya ya uhalifu. Ili kukabiliana na changamoto hizo, serikali inasema imeimarisha operesheni za polisi, ushirikishaji wa wananchi katika masuala ya usalama, matumizi ya teknolojia na mageuzi katika sekta ya usalama. Pia inaandaa miswada sita ya kurekebisha sheria zinazosimamia vyombo vya usalama, ikiwemo Sheria ya Huduma ya Polisi, Sheria ya Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA), Sheria ya Tume ya Huduma za Polisi na Sheria ya Utulivu wa Umma.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Sababu za Kuppet kukataa mpango wa shule jumuishi
Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kati (Kuppet) kimepinga mpango wa Rais William Ruto wa kuanzisha mfumo wa shule jumuishi, kikisema hautatatua changamoto za elimu nchini. Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori alisema mpango huo hauna msingi wa kisheria na unaweza kuvuruga usimamizi wa shule, hasa katika Gredi 7, 8 na 9. Kuppet imekuwa ikishinikiza shule za Sekondari Msingi (JS)ziwe na usimamizi wake tofauti na shule za msingi, ikisema walimu wake hawawezi kuongozwa na wakuu wa shule za msingi. "Kuendesha mfumo huu bila marekebisho ya Katiba ni kufanya majaribio," alisema Misori. Alisema Sekondari Msingi hufuata mtaala wa kiwango cha shule za upili, hivyo si vyema kuziweka chini ya wakuu wa shule za msingi ambao wamefunzwa kusimamia elimu ya msingi. Misori alisema kuwa hata kama shule hizo ziko katika eneo moja, zinaweza kuwa na usimamizi tofauti, akitaja shule ya msingi ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambayo huendeshwa kivyake licha ya kuwa ndani ya chuo hicho. Pia alionya kuwa baadhi ya walimu waliofunzwa kufundisha masomo ya msingi wamepewa masomo ya sayansi na kiufundi katika JS bila kuwa na sifa zinazohitajika. Rais Ruto aliagiza Wizara ya Elimu kushirikiana na Chama cha Wakuu wa Shule Jumuishi nchini (Kecsha) kuandaa mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Elimu ya Msingi ndani ya siku 90. Alitoa agizo hilo Novemba 13 wakati wa kufunga mkutano wa Kecsha mjini Mombasa, akisema sheria mpya inapaswa kuweka wazi usimamizi, ajira na ufadhili wa shule hizo. Kecsha imekuwa ikitaka mfumo mpya wa kupandisha vyeo wakuu wa shule ili kuzingatia majukumu yao mapya ya kusimamia wanafunzi kuanzia elimu ya chekechea hadi Gredi 9. Hata hivyo, Kuppet imesema haitakubali JS kuendelea kusimamiwa na wakuu wa shule za msingi. Mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Omboko Milemba alisema viongozi wa Kuppet wamewasilisha mapendekezo yao kwa Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa, wakitaka kuwe na mfumo tofauti wa usimamizi, walimu wa kutosha na mgao unaofaa wa rasilimali. Mzozo huo sasa unatarajiwa kuelekea Bungeni huku muda wa siku 90 uliotolewa na Rais ukianza kuhesabiwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Biashara ya magendo yasababishia serikali hasara ya Sh1 trilioni kwa mwaka
MKULIMA wa chai kaunti ya Kiambu anapopeleka majani mabichi katika kituo cha kununua chai, huenda mizani ikaonyesha uzito ulio chini kwa asilimia 14 hadi 20 ya alichovuna. Huu ni mfano mmoja tu wa biashara haramu ambayo serikali inasema inaletea Kenya hasara ya zaidi ya Sh800 bilioni kila mwaka. Mitandao hiyo hiyo inayopunguza uzani wa chai ya wakulima pia huuza kemikali bandia, pombe isiyo salama na mbolea feki inayowekwa katika mifuko yenye majina ya bidhaa halisi. Ripoti mpya ya serikali kuhusu biashara haramu nchini, iliyozinduliwa Mombasa Jumatano, inakadiria kuwa shughuli hizo ziligharimu Kenya Sh826 bilioni mwaka 2018, huku hasara hiyo ikivuka Sh1 trilioni katika miaka iliyofuata. Katika mwaka huo, hasara hiyo ilikuwa sawa na asilimia 9.3 ya pato la taifa. Serikali pia ilipoteza mapato ya Sh153.1 bilioni, huku ajira 44,198 zikikosekana na uwekezaji wa Sh123 bilioni kutopatikana. Watengenezaji bidhaa ni miongoni mwa walioathirika zaidi. Ripoti inasema kampuni halali hupoteza wastani wa asilimia 25 ya soko lake, sawa na takriban Sh3.9 milioni kwa mwaka kwa kila kampuni. Pia, ajira katika kampuni hizo hupungua kwa asilimia 25.5. Watumiaji nao wako hatarini. Daktari Robi King'a wa Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Bandia alisema hadi asilimia 60 ya baadhi ya aina za pombe na asilimia 89 ya baadhi ya kemikali za kilimo sokoni huenda ni bandia au vimefungwa upya kinyume cha sheria. Serikali pia hupoteza mapato kupitia ukwepaji wa ushuru. Mwaka wa kifedha wa 2025/26, bidhaa zilizokamatwa kutokana na maafisa wa forodha zilikuwa na thamani ya Sh10.83 bilioni. Ripoti inataja visa kadhaa vinavyoonyesha ukubwa wa tatizo. Katika kituo cha mpakani wa Lwakhakha, maafisa walipata lita 40,971 za ethanol zilizofichwa kwenye magari ya kubeba mafuta yaliyotangazwa kubeba shehena tofauti. Bidhaa hizo zilikuwa na thamani ya Sh26.9 milioni. Katika Bandari ya Mombasa, maafisa walikamata tani 23 za kemikali bandia za kuuwa watoto, huku bidhaa nyingine bandia za thamani ya zaidi ya Sh200 milioni zikiharibiwa Athi River. Maafisa jijini pia walinasa mifuko 190,000 ya mbolea bandia eneo la Kariokor, Ripoti pia ilitaja pombe yenye vibandiko bandia vya ushuru kaunti ya Nyeri na dawa za serikali zikiuzwa katika maduka ya dawa yasiyoidhinishwa Kajiado. Ili kukabili tatizo hilo, ripoti inapendekeza mashirika ya serikali yashirikiane katika operesheni, yaimarishe ufuatiliaji wa bidhaa na kuchunguza watu wanaofadhili mitandao hiyo. King'a alisema hatua za kidijitali zinahitajika pia kwa kuwa bidhaa bandia zinazidi kuuzwa kupitia mitandao ya intaneti. Chama cha Wafanyabiashara wa Rejareja nchini kinataka KRA, Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Bandia, Shirika la Viwango vya ubora nchini na polisi kuunda mpango wa pamoja wa kukabiliana na biashara hiyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Kiti cha naibu rais chazua ushindani mkali 2027 katika serikali na upinzani
VITA vya kuwania unaibu rais vimeanza kushika kasi katika kambi za Rais William Ruto na upinzani unaoongozwa na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua, huku viongozi mbalimbali wakimezea mate wadhifa huo muhimu katika uchaguzi wa 2027. Katika serikali, Naibu Rais Kithure Kindiki anakabiliwa na ushindani kutoka kwa viongozi wa Mlima Kenya wanaotaka kuchukua nafasi yake. Miongoni mwa wanaotajwa ni Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Mbunge wa Ndia George Kariuki, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung'wah na Mwangi Kiunjuri wa chama cha TSP. Hata hivyo, washirika wa Kindiki, akiwemo Gavana wa Nakuru Susan Kihika na Mbunge wa Nakuru Town East David Gikaria, wanasisitiza kuwa anafaa kuendelea kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto. Kwa upande mwingine, chama cha ODM pia kinataka kushirikishwa katika mazungumzo ya kugawana mamlaka kupitia ushirikiano wake na UDA. Viongozi wanaotajwa kuwa na nafasi ni Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, mawaziri Hassan Joho na Wycliffe Oparanya. Utafiti wa TIFA uliofanywa kati ya Oktoba 26 na Novemba 5 ulionyesha kuwa asilimia 55 ya wafuasi wa Dkt Ruto wanamuunga mkono Profesa Kindiki kuwa mgombea mwenza. Wanga alipata asilimia 12 huku Joho akipata tisa. Hata hivyo, utafiti wa Swiss Poll International uliotolewa Oktoba 28 ulimweka Waiguru mbele kwa asilimia 43, akifuatiwa na Kindiki kwa asilimia 30 na Wanga kwa asilimia 13. Mbunge Kariuki anasema nafasi hiyo haipaswi kuchukuliwa kuwa mali ya Kindiki, akitaka UDA kuruhusu ushindani wa ndani. Anasema mgombea anayevutia kura nyingi ndiye anayefaa kuchaguliwa, akiongeza kuwa Dkt Ruto anapaswa kuwa na uhuru wa kumteua mgombea mwenza atakayemsaidia kushinda uchaguzi. Katika upinzani, mazungumzo yanahusisha viongozi watatu wakuu: Kalonzo Musyoka, Edwin Sifuna na Fred Matiang'i. Hata hivyo, bado hawajakubaliana nani atakuwa mgombea urais na nani atakuwa naibu wake. Washirika wa Gachagua wanasema uchaguzi huo utategemea atakayepata tiketi ya urais na kuzingatia maslahi ya maeneo mbalimbali. Martha Karua, Eugene Wamalwa na Justin Muturi pia wanatajwa katika mazungumzo hayo. Sifuna ameonya kuwa tiketi ya urais haipaswi kutolewa kwa mtu kwa sababu tu amekuwa nje ya serikali kwa muda mrefu. "Hatupaswi kumpa mtu tiketi kwa sababu anasema amekuwa nje ya serikali kwa muda mrefu. Hatuendi serikalini kutafuta starehe," alisema. Wakati huo, Waziri John Mbadi amesema ODM inatarajia makubaliano rasmi na UDA kabla ya Februari 2027. Anasema chama hicho kinataka nafasi kubwa katika ushirikiano huo, ikiwemo ile ya naibu rais. Hata hivyo, Mbunge wa Ugenya David Ochieng' amepinga uwezekano wa Kindiki kubadilishwa na kiongozi wa jamii ya Waluo, akisema anataka Dkt Ruto na Kindiki waendelee pamoja. Hivyo, Dkt Ruto anakabiliwa na changamoto ya kudumisha uhusiano na Kindiki huku akishughulikia madai ya viongozi wa Mlima Kenya Magharibi na ODM. Upinzani nao unapaswa kusawazisha maslahi ya viongozi na maeneo ili kuepusha migawanyiko kabla ya uchaguzi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Hapa ni kuchimbana? Mrengo wa upinzani, ndani ya upinzani waibuka
SIASA za upinzani zimepata sura mpya baada ya vigogo wanne, Fred Matiang'i, Ndindi Nyoro, Martha Karua na James Orengo kuonekana wakishirikiana katika juhudi za kuunda mrengo mpya wa kisiasa unaoweza kuathiri mikakati ya kumuondoa Rais William Ruto madarakani mwaka 2027. Muungano unaochipuka wa viongozi hao umeanza kuvutia hisia za kisiasa, hasa baada ya kufanya ziara ya pamoja katika eneo la Gusii, huku wakitarajiwa kuelekea Kirinyaga leo, nyumbani kwa Bi Karua, kwa mikutano mingine ya kisiasa. Ingawa viongozi hao wanasisitiza kuwa lengo lao ni kupanua wigo wa upinzani kote nchini, hatua zao zimeibua maswali kuhusu iwapo wanajenga muungano mpya ndani ya upinzani au wanajiandaa kuwania nafasi kubwa katika mazungumzo yatakayoamua mgombeaji wa urais wa upinzani. Baadhi ya watu wa karibu na viongozi hao wanasema ushirikiano huo umechochewa na kile wanachokitaja kuwa uongozi wa mabavu wa baadhi ya vinara wa upinzani, ambao wanahofia unaweza kudhoofisha juhudi za pamoja za kumkabili Dkt Ruto. Mvutano huo unajiri wakati ambapo upinzani bado unakabiliwa na changamoto ya kuafikiana kuhusu uongozi na mgombeaji mmoja wa urais. Utafiti wa hivi majuzi wa kampuni ya TIFA unaonyesha kuwa asilimia 43 ya waliohojiwa wanamtaja aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuwa kikwazo kikubwa zaidi kwa umoja wa upinzani. Rais Ruto anafuata kwa asilimia 15, huku kiongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi Edwin Sifuna akipata asilimia saba na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka asilimia sita. Hata hivyo, Bw Gachagua amepuuzilia mbali madai kuwa ndiye anayegawanya upinzani, akisisitiza kuwa yeye ndiye anayewaunganisha viongozi hao. Malumbano makali kati yake na Dkt Matiang'i katika siku za hivi majuzi yamezidisha dalili za mgawanyiko kuhusu nani anafaa kuongoza upinzani na jinsi ya kuandaa kampeni za 2027. Msemaji wa Wiper, Bw Ndegwa Njiru ameonya kuwa ushirikiano wa upinzani bado ni dhaifu na viongozi wanapaswa kuheshimiana ili kuepusha migogoro inayoweza kuuvunja. Alisema viongozi wanapaswa kudhibiti wafuasi wao na kuhakikisha hawawadharau wagombeaji wengine wa urais. Tofauti na mirengo mingine, ushirikiano wa Matiang'i, Nyoro, Karua na Orengo unaonekana kuwa na hesabu pana ya kisiasa inayolenga kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi. Dkt Matiang'i, aliyewahi kuhudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani wakati wa utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ndiye anayeonekana kuwa kiini cha ushirikiano huo. Wafuasi wake wanataja uzoefu wake serikalini na kujulikana kitaifa kuwa baadhi ya sifa zinazoweza kumsaidia kumkabili rais anayewania muhula wa pili. Hata hivyo, changamoto yake kubwa ni kupanua ushawishi wake nje ya eneo la Gusii na kupata uungwaji mkono kutoka maeneo mengine. Mchanganuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema kuhusika kwa Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ni muhimu kwa sababu kunapatia ushirikiano huo nafasi katika eneo la Mlima Kenya, ambalo lina ushawishi mkubwa katika siasa za urais. Bw Nyoro amejijengea jina kwa kukosoa sera za serikali na misimamo yake kuhusu masuala ya uchumi. Kwa mujibu wa Bw Mboya, uhusiano wake na Dkt Matiang'i unampa nafasi ya kushiriki katika kuunda mwelekeo wa kisiasa wa kitaifa huku akiendeleza ushawishi wake binafsi. Kwa upande wake, Bi Karua analeta uzoefu wa kupigania mageuzi, utawala bora, Katiba na uwajibikaji. Aliwahi kuwania urais na pia kuwa mgombeaji mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi mkuu uliopita. Katika mkutano wa Gusii, alionyesha kuwa yuko tayari kuweka kando azma yake binafsi ikiwa upinzani utaafikiana kumuunga mkono mgombeaji mwingine. 'Ingawa wengi wetu, akiwemo mimi, tuna azma ya kuwania urais, iwapo itaamuliwa kuwa Dkt Matiang'i ndiye atakuwa mgombeaji, nitajiondoa na kumuunga mkono,' alisema. Alisema yuko tayari pia kumuunga mkono Bw Nyoro iwapo atachaguliwa kuwa mgombeaji wa upinzani. Kauli hiyo inaashiria juhudi za kuzuia azma tofauti za viongozi hao kuwa kikwazo cha kuunda muungano wenye nguvu. Kujiunga kwa Gavana wa Siaya James Orengo nao kumeongeza uzito wa kisiasa kwa kundi hilo, hasa kutokana na uhusiano wake wa muda mrefu na marehemu Raila Odinga na ushawishi wake katika Nyanza. Bw Orengo awali alikuwa amejitambulisha na vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Bw Sifuna. Hata hivyo, hatua zake hivi majuzi, ikiwemo kuhusika katika chama cha Liberal Democratic Party na kumuunga mkono Dkt Matiang'i hadharani Kisii, zimeashiria mwelekeo mpya. Katika mkutano wa Gusii, aliwataka wakazi kumuunga mkono Dkt Matiang'i, akirejelea uhusiano wake na marehemu Raila pamoja na babake, Jaramogi Oginga Odinga. Alisema wakazi wa Gusii wamekuwa wakiunga mkono familia ya Odinga kwa muda mrefu na kwamba kumuunga mkono Dkt Matiang'i kungekuwa njia ya kuendeleza uhusiano huo. Bw Orengo alieleza kuwa Dkt Matiang'i alikuwa na uhusiano wa karibu na Raila, ambaye alimchukulia kama mwanawe. Dkt Matiang'i naye alimtaja Bw Orengo kama mshauri wake wa kisiasa na kumshukuru kwa uongozi na ushauri wake. Ushirikiano huo unaweza kumsaidia Dkt Matiang'i kuimarisha uhusiano na wapigakura wa Nyanza katika kipindi ambacho eneo hilo linajipanga upya kisiasa kufuatia kifo cha Raila. Hata hivyo, kundi hilo si pekee linalotafuta ushawishi ndani ya upinzani. Bw Kalonzo, kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa nao wamekuwa wakifanya kazi pamoja. Wakati huo huo, mirengo inayohusishwa na Bw Gachagua na Bw Sifuna inachunguza uwezekano wa kuunda muungano unaounganisha Mlima Kenya na Mlima Elgon. Wachanganuzi wanaonya kuwa makundi hayo yanaweza kufanya mazungumzo ya kuafikiana kuhusu mgombeaji mmoja kuwa magumu zaidi, hasa kila mmoja akitaka mgombeaji wake apewe nafasi ya kwanza. Dkt Matiang'i amepuuzilia mbali madai kuwa ushirikiano wao ni jaribio la kujitenga na viongozi wengine wa upinzani. Alisema walikubaliana kuwa kila kiongozi anapaswa kuzunguka maeneo tofauti nchini ili kupanua ushawishi wa muungano. 'Tulikubaliana katika upinzani kuwa kila mmoja azunguke nchini. Tunahitaji kuunda timu zitakazofikia maeneo yote ya nchi,' alisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 07:55:25
Makanisa yageuza tohara ya wavulana kuwa biashara nono
KWA miaka mingi, tohara ilikuwa jukumu la wazee waliokuwa na mamlaka ya kuamua wakati, mahali na jinsi wavulana walivyopaswa kutahiriwa. Lakini sasa makanisa yamechukua nafasi hiyo, yakigeuza utamaduni uliorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kuwa shughuli inayohusisha malipo ya maelfu ya shilingi. Miezi ya Novemba na Desemba, familia katika maeneo ya Bonde la Ufa na Mlima Kenya humiminika katika makanisa kuwaandikisha wana wao katika kambi za tohara zinazochanganya matibabu, mafundisho ya Kikristo na mafunzo ya maisha. Badala ya kwenda msituni au kwenye vituo vya kitamaduni vilivyoendeshwa na wazee, wavulana hukaa katika kumbi za makanisa kwa siku saba hadi 14, wakihudumiwa na madaktari na walezi. Wazazi hulipa kati ya Sh10,000 na Sh50,000 kutegemea kanisa, eneo na muda wa kambi. Kwa hivyo, tohara imegeuka kuwa biashara ya msimu inayozalisha mamilioni ya shilingi kila mwaka. Mlezi wa kitaifa wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Kiama Kia Ma, Kung'u Muigai, anasema wazee wamepokonywa jukumu lao muhimu katika jamii. "Watu hawaliiti biashara, wanaliita huduma ya kanisa," anasema, akiongeza kuwa shughuli hiyo sasa ina thamani ya mamilioni ya pesa kila mwaka. Kwa mujibu wa Joseph Kaguthi, mratibu wa wazee na viongozi wa dini katika Baraza la Pamoja la Wazee wa Mlima Kenya, tohara ilikuwa chini ya usimamizi wa wazee. Wao ndio walioamua nani angefanya tohara, lini na wapi, huku wavulana wakifundishwa majukumu yao katika jamii na kujiunga na rika lililowaongoza maisha yao yote. Familia zililipa kwa kutoa mbuzi, pombe ya kienyeji na heshima kwa wazee. Hata hivyo, kuanzia miaka ya 1920 hadi 1950, wamishenari wa Kanisa la Scotland (PCEA) na Kanisa Katoliki walipinga tohara iliyofanywa misituni, wakihimiza matumizi ya hospitali. "Hospitali zilijengwa na madaktari wakachukua nafasi ya ngariba wa kitamaduni. Wazee walikuwa na maarifa lakini hawakuwa na hospitali. Kanisa lilikuwa nayo," anasema Kaguthi. Baadaye, kuibuka kwa kundi la Mungiki na magenge mengine kulifanya tohara za nyumbani kuwa hatari zaidi. Hali hiyo iliimarisha imani ya wazazi kwamba makanisa yalikuwa maeneo salama zaidi. Mhubiri Charity Kagina wa Murang'a anasema wazazi walikuwa wameanza kushindwa kutambua wazee wa kweli na matapeli. Anasema makanisa yalitoa usalama kupitia walinzi, sajili i na utaratibu wa kufuatilia watoto. Kwa wazazi, hata hivyo, gharama imekuwa mzigo. James Rono wa Eldoret anasema alilipa Sh17,000 kwa mwanawe kuhudhuria kambi ya wiki moja katika kanisa Katoliki. Fedha hizo ziligharamia huduma za daktari, chakula, malazi na mafunzo ya malezi. Anasema gharama hiyo ni kubwa wakati familia zinakabiliwa na mahitaji mengine, ikiwemo karo ya shule. Baadhi ya wazazi hulazimika kutafuta huduma za watu wasio na ujuzi kutokana na gharama hizo. Askofu Joseph Kagunda wa ACK Mlima Kenya Magharibi, ambaye alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa tohara zinazoendeshwa na makanisa, anakiri kuwa ada imeongezeka tangu alipokuwa akitoa huduma hiyo kwa takriban Sh10,000. Anasema awali wavulana hawakupata ushauri wa kutosha, lakini sasa wanapewa mafunzo kuhusu uwajibikaji na maisha ya utu uzima. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa dini wanapinga makanisa kutumia shughuli hiyo kupata faida. Askofu Wilson Kurui wa Jesus Love Ministries, Eldoret, anasema huduma hiyo inapaswa kuwa njia ya kanisa kusaidia jamii badala ya kuwa chanzo cha mapato. Kwa upande mwingine, wazee wanasema makanisa yanapunguza nafasi yao katika utamaduni. Thomas Ingara, mwenye umri wa miaka 91, ambaye ni mtaalamu wa tohara ya kitamaduni kutoka kijiji cha Kalwani, Hamisi, anasema makanisa yanapaswa kuzingatia mahubiri na kuwaachia wazee jukumu la tohara. Kung'u Muigai anasema baadhi ya makanisa huwaalika wazee kwa muda mfupi tu, bila kuwapa nafasi ya kuwafundisha wavulana kikamilifu. Kiama Kia Ma inapendekeza makanisa yatumie wiki moja kuwafundisha wavulana masuala ya kiroho na wazee watumie wiki inayofuata kuwafundisha utamaduni. Hata hivyo, pendekezo hilo halijaungwa mkono na baadhi ya makanisa. Wakati huo huo, usalama wa wavulana unabaki kuwa suala muhimu. Mchungaji Isaac Wanakacha, muuguzi mkuu wa zamani katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi, anashauri wazazi kutumia hospitali za umma na kliniki zilizoidhinishwa, ambazo hutoa huduma kwa gharama nafuu na kuruhusu matumizi ya bima ya SHA. Askofu Edward Khaoya wa Kitale Family House of Hope anasema takriban watoto 10 hufariki kila mwaka kutokana na matatizo yanayohusiana na tohara baada ya kufikishwa katika Moi Hospital. Mtafiti wa utamaduni Mwaura wa Koigi anasema makanisa yalipata umaarufu kwa kutoa maeneo salama na walezi waliokuwa wakiaminika, lakini baadaye huduma hiyo ikageuka kuwa biashara.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 06:55:25
Ruto afichua dili kali ya kufaidi vijana
RAIS William Ruto amewaonya vijana dhidi ya kuruhusu wanasiasa kuwatumia kama wanablogu au wahuni wa kuvuruga mikutano, akitangaza mpango wa nguzo tano unaolenga kuwapa ajira na kuwawezesha kiuchumi. Akizungumza siku ya pili ya ziara yake katika eneo la Magharibi mwa Kenya Ijumaa, Rais alisema vijana wanapaswa kujikita katika kutafuta fursa za kujipatia riziki badala ya kutumiwa katika mapambano ya kisiasa. Alisema mpango wake unalenga kuwawezesha vijana kupitia elimu, mafunzo ya kazi, mitaji, zabuni za serikali na ajira katika sekta mbalimbali. Nguzo ya kwanza ni mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo vikuu, ambao alisema utahakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo bila kukatizwa na ukosefu wa karo. Pili, serikali inalenga kuwaingiza zaidi ya vijana 100,000 katika mafunzo ya kazi, ambapo kila mmoja atalipwa Sh25,000 kabla ya kupata ajira za kudumu. Kupitia mpango wa Nyota, serikali tayari imetoa Sh50,000 kwa kila mmoja wa vijana zaidi ya 130,000 wenye ujuzi lakini wasio na ajira ili kuanzisha biashara. Ruto alisema serikali inatafuta vijana wengine 200,000 watakaonufaika na mpango huo. Nguzo ya nne ni kuwaunganisha vijana na zabuni za serikali kupitia mpango wa Nyota-AGPO. Vijana watasajiliwa, kupewa mafunzo ya wiki 10 na kusaidiwa kusajili kampuni zao bila malipo. Rais alisema serikali italipa bidhaa zitakazowasilishwa ndani ya siku 60. Nguzo ya tano ni ajira kupitia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, masoko, mabweni, vituo vya teknolojia na ajira za kidijitali. Alisema vijana 700,000 tayari wamepata ajira kupitia usafirishaji wa wafanyakazi nje ya nchi. Ruto pia alishambulia upinzani, akiwataka kuacha kuingilia shughuli za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inapojiandaa kwa uchaguzi wa Agosti 2027. Upinzani unataka mageuzi matano ya uchaguzi yafanywe kabla ya uchaguzi huo, yakiwemo ukaguzi wa sajili ya wapigakura na mabadiliko ya teknolojia ya uchaguzi. Rais alisema IEBC inafaa kupewa nafasi ya kufanya kazi yake na kuwataka wapinzani wajipange kwa uchaguzi badala ya kuamua vifaa vitakavyotumiwa na tume hiyo. Katika ziara hiyo, alikagua miradi ya Sio Port na soko la Sio Port ESP. Alisema serikali imetenga Sh800 milioni kwa ujenzi wa gati hilo na Sh400 milioni kwa upanuzi wake, kabla ya kufunguliwa rasmi Februari mwaka ujao. Alisema pia kituo cha mpaka cha Mulwanda kitakamilika ndani ya miezi minne, huku soko likitarajiwa kukamilika baada ya miezi miwili. Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi alisema serikali imetenga Sh800 bilioni kwa elimu, kutoka Sh400 bilioni mwaka 2022, akitaja hatua hiyo kuwa uwekezaji kwa vijana na vizazi vijavyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 05:55:58
Ripoti: Magenge 309 ya uhalifu yatishia usalama nchini
BONDE la Ufa, Pwani na Nairobi ndiyo maeneo yanayoongoza kwa idadi kubwa ya magenge ya uhalifu yanayotishia usalama wa wananchi, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyowasilishwa bungeni na Rais William Ruto. Ripoti kuhusu hali ya usalama nchini inaonyesha kuwa kuna jumla ya magenge na makundi 309 ya uhalifu kote nchini, ingawa baadhi yake hayafanyi shughuli kwa sasa. Idadi hiyo imeongezeka kwa makundi 200 ikilinganishwa na mwezi uliopita, wakati serikali ilipotangaza kuwa ilikuwa imetambua magenge 109. Mwaka 2016, kupitia Tangazo la Serikali Na. 10427, magenge 89 yalitangazwa kuwa haramu. Ripoti hiyo inayohusu kipindi cha Septemba 2025 hadi Agosti 31, 2026, inaonyesha kuwa Bonde la Ufa linaongoza kwa magenge 20 yanayotekeleza shughuli za uhalifu, likifuatiwa na Pwani iliyo na magenge 17, Nairobi 11, Magharibi 10, Nyanza saba, Mashariki manne na Kati matatu. Baadhi ya magenge yanayofanya shughuli Bonde la Ufa ni Watizedi, Kamiti, Confirm, Barsuliek, Cheptiret Boys, DNA, Answi, Chafua, Exodus na Isilando. Pwani kuna Empire, Military Gang, Wakali Wao, Kitimboni, Zoza Nation, Team Mashamba, Mombasa Republican Council (MRC), Panga Boys na Mawoza. Katika Nairobi kuna magenge kama Team Kazoo, Mujahedeen, Matopeni Mafia, Jeshi ya Allah, Mbogi Genje, Gaza, Tokyo Mafia na Team Mbogi. Magharibi kuna Border Defence Force, Bogi Mawe, Jobless Gang, Marachi Republican Council na Fimbo Movement, huku Nyanza kukiwa na Darfur, China Squad, Sungusungu, Chinkororo na Katalang. Katika eneo la Mashariki kuna G-Unit, Jeshi ya Rasia, Gaza na Nkomori, huku eneo la Kati likiwa na Mungiki, Gaza na Kamagira. Ripoti hiyo inasema magenge hayo yanadhoofisha utawala wa sheria kupitia vurugu, vitisho dhidi ya jamii na kuwashawishi vijana walio katika mazingira magumu kujiunga na uhalifu. Licha ya operesheni za polisi, makundi hayo yanaendelea kujipanga na kuajiri wanachama wapya kutokana na changamoto za kiuchumi, hasa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Kaunti zinazokumbwa na hali ya kutovumiliana kisiasa kutokana na matumizi ya wahuni na magenge hayo ni Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Busia, Murang'a, Kiambu, Nyeri, Mombasa na Nairobi. Ripoti hiyo inasema hali hiyo imechangia ongezeko la ujambazi, mauaji yaliyolengwa, uvamizi wa nyumba, utapeli wa ardhi na ulaghai wa fedha katika sekta za usafiri wa umma na ujenzi. Polisi walikamata washukiwa 1,316 katika kipindi hicho, ikilinganishwa na 602 katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia. Hii ni ongezeko la watu 714. Baadhi ya magenge yanaendesha shughuli katika kaunti kadhaa. Gaza ina mizizi Mombasa, Kwale, Nakuru, Kilifi, Isiolo, Machakos, Nairobi na Kisumu. Mungiki inapatikana Nakuru, Machakos, Nairobi na Kiambu. Panga Boys lina matawi Kilifi, Kwale na Mombasa, huku Wakali Wao likiendesha shughuli Mombasa, Kilifi, Kwale na Nairobi. Serikali imesema inaendesha operesheni ya pamoja inayotegemea taarifa za kijasusi, kuongeza doria na kuimarisha uwepo wa polisi katika maeneo hatari. Hata hivyo, imeonya kuwa baadhi ya wanasiasa wanaowalinda wahalifu wanachangia kuimarisha magenge hayo. Pia, hofu ya kulipiziwa kisasi imewafanya wananchi kusita kuwapa maafisa wa usalama taarifa muhimu kuhusu wanachama wa magenge ya wahalifu.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 04:55:41
Sifuna asubiriwa kwa hamu Amerika ziara ya Kalonzo ikiahirishwa
WAKENYA wanaoishi Amerika wanatazamia kwa hamu ziara ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, ambaye anatarajiwa kuwasili nchini humo huku akijipanga kuimarisha uungwaji mkono wake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Ziara hiyo inatarajiwa kumwezesha Sifuna kukutana na Wakenya wanaoishi ughaibuni, kujadili uongozi wa Kenya na kutafuta michango ya kifedha kwa safari yake ya kisiasa. Ziara hiyo inaanzia New Jersey na inaangazia umuhimu unaoongezeka wa wapiga kura na wafadhili waishio nje ya nchi katika siasa za Kenya. Mwanzilishi mwenza wa The Equitable Party, Dkt Eunice Juma, alisema chama hicho kilikumbana na changamoto nyingi za kiutawala kikitafuta usajili. "Wakati mwingine ilionekana kana kwamba simu kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu zilikuwa zikichelewesha mchakato wa kusajili chama," alisema. Chama hicho baadaye kilisajiliwa na kubadilisha jina kuwa Linda Mwananchi Movement (LMM) baada ya kuidhinishwa kwa kauli moja katika mkutano wa wajumbe Novemba 13, 2026. Profesa Kefa Otiso wa Chuo Kikuu cha Bowling Green State alisema mchango mkubwa wa Wakenya wanaoishi ughaibuni kwa wanasiasa ni kuchangisha fedha na kuwashawishi jamaa na marafiki walio nyumbani kuwaunga mkono wagombeaji. "Fedha kutoka ughaibuni zimekuwa muhimu kwa sababu Wakenya wanaoishi huko wana uwezo wa kuchangia kiasi kikubwa. Nchini Kenya, wanasiasa huwapa wapigakura fedha, lakini ughaibuni Wakenya huchangia wagombeaji," alisema. Mtandao wa LMM nchini Amerika umeunda matawi katika majimbo yote 50. Tamasha la Chakula cha Mulembe-Mashemeji lilichoandaliwa Oktoba 24 lilikuwa sehemu ya maandalizi ya ziara ya Sifuna. Dkt Juma alisema ziara hiyo inalenga kuwakutanisha Wakenya kujadili uongozi, utawala bora, utawala wa sheria na mustakabali wa nchi. Sifuna anatarajiwa kuzindua ofisi za LMM mjini Hackettstown, New Jersey, Novemba 21, kabla ya kuhudhuria ibada ya kanisa Pennsylvania siku inayofuata. Atakutana pia na wafanyabiashara Maryland Novemba 23 na kushiriki mkutano kuhusu siasa za Afrika Mashariki Washington DC Novemba 24. Ratiba yake itaendelea Dallas, Texas, kisha Renton na Oakland ambako atahudhuria mikutano na hafla za kuchangisha fedha. Ziara hiyo itakamilika Silicon Valley Desemba 7. Wakati huo huo, ziara ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka nchini Amerika iliyopangwa kipindi hicho imeahirishwa hadi Februari 2027. Mkurugenzi wake wa mawasiliano David Mutua alisema mabadiliko hayo yamefanywa bila kutoa sababu zaidi. Ziara za wanasiasa wa Kenya nchini Amerika zimekuwa muhimu katika kujenga mitandao ya kisiasa, kuchangisha fedha na kutafuta uhusiano na viongozi wa kimataifa. Amerika ni mshirika muhimu wa Kenya, ambayo ina hadhi ya mshirika mkuu asiye mwanachama wa NATO. Sifuna anatarajia kutumia ziara hiyo kuimarisha uhusiano huo na kuongeza ushawishi wake katika siasa za kitaifa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 03:55:09
Mahakama yafichua majaji na mahakimu walioamua kesi nyingi zaidi mwaka huu
KWA mara ya kwanza, idara ya Mahakama imechapisha takwimu zinazoonyesha idadi ya kesi zilizoamuliwa na kila jaji na hakimu katika mwaka uliotamatika Juni 2026. Ripoti ya kurasa 328 kuhusu hali ya Mahakama na utoaji haki imetaja majina ya maafisa hao pamoja na idadi ya hukumu, maamuzi na maagizo mengine waliyotoa. Hata hivyo, Idara ya Mahakama imesisitiza kuwa takwimu hizo si orodha hiyo haitokani na mashindano ya majaji kazini. Katika Mahakama Kuu, Jaji Reuben Nyakundi aliongoza kwa kuamua kesi 1,791. Alifuatiwa na Alfred Mabeya aliyeshughulikia kesi 968, Teresa Odera (956), Richard Mwongo (913), Teresia Matheka (906) na Kizito Magare (904). Majaji wengine waliokuwa na idadi kubwa ya maamuzi ni Diana Kavedza (824), Mwanaisha Saida (778), Lucy Gitari (745), huku Helene Namisi na Florence Muchemi wakiwa na kesi 744 kila mmoja. Katika Mahakama ya Rufaa, jumla ya kesi 2,394 ziliamuliwa na majopo ya majaji. Jopo la Kisumu lililoongozwa na majaji Hellen Omondi, Luka Kimaru na Milton Makhandia liliongoza kwa kesi 172. Katika Mahakama ya Ajira na Mahusiano Kazini, Jaji Jemima Keli aliongoza kwa maamuzi 499, akifuatwa na Monica Mbaru na Stella Rutto waliokuwa na 484 kila mmoja. Katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi, Emmanuel Washe aliongoza kwa kesi 456, akifuatwa na Fred Nyagaka (455) na David Mugo (442). Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa, mahakama ilipokea kesi mpya 561,580 na kuamua 576,702, kiwango cha utatuzi cha asilimia 103. Kesi zinazosubiri kuamuliwa zimepungua kutoka 405,486 hadi 341,412, lakini bado asilimia 58.9 ya kesi hizo zimekaa mahakamani kwa zaidi ya mwaka mmoja. Mahakama za mahakimu ndizo zilizo na mrundiko mkubwa zaidi wa kesi 274,177, sawa na asilimia 80.3 ya jumla ya kesi zilizochelewa kuamuliwa. Jaji Mkuu Martha Koome alisema licha ya mahakama kuamua kesi nyingi kuliko zilizowasilishwa kwa mwaka wa pili mfululizo, idadi ya kesi za zamani bado ni kubwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sat, 21 Nov 2026 02:55:16
Hofu ya wagonjwa wa saratani kukosa matibabu kufuatia mabadiliko ya SHA
WAGONJWA wa saratani nchini wameibua wasiwasi kuhusu kucheleweshwa kwa matibabu, kukataliwa kwa maombi ya dawa na kupunguzwa kwa kiwango cha fedha wanacholipiwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Wanasema mfumo mpya wa kuidhinisha matibabu umewalazimu kulipa fedha za ziada ili kupata huduma ambazo awali ziligharamiwa kikamilifu na bima ya afya. Katika Hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH), kati ya maombi 30 ya matibabu yaliyowasilishwa kwa SHA Jumatatu, ni 12 pekee yaliidhinishwa. Daktari mmoja mtaalamu wa saratani alisema hata wagonjwa walioidhinishwa walitakiwa kuongeza fedha kutoka mifukoni mwao. Alitaja mgonjwa wa saratani ya utumbo aliyelazimika kulipa Sh20,000 kwa vipimo, licha ya kuwa awali gharama hizo zililipwa na SHA. Daktari alisema hali hiyo imacha wagonjwa wasiojiweza kifedha wakisimamisha matibabu kwa kukosa pesa za kuongeza. Mgonjwa mmoja wa saratani ya matiti alisema kiwango chake cha fedha za kununua dawa ya Letrozole kimepunguzwa hadi Sh5,400, ilhali anahitaji zaidi ya Sh20,000 kwa dawa hiyo inayosaidia kudhibiti ukuaji wa saratani inayochochewa na homoni. "Ninahitaji zaidi ya Sh20,000 kununua dawa zangu. Kiasi hicho kinapopunguzwa nalazimika kuongeza fedha za ziada. Bila dawa hizo huenda nishindwe kudhibiti homoni," akaeleza. Mfumo huo mpya pia umeongeza muda wa kusubiri dawa hospitalini. Maombi ya matibabu sasa yanahitaji kupitishwa na muuguzi, daktari mtaalamu na mfamasia kabla ya kuidhinishwa. Muuguzi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta alisema foleni katika kliniki za saratani zinaongezeka huku wagonjwa wakingoja vibali. Mgonjwa Mary Adhiambo pia alisema kituo cha saratani cha Texas kimeacha kuuza dawa kwa wagonjwa wanaopokea matibabu katika hospitali zingine, na badala yake kuwataka wahamie huko. Mabadiliko hayo yameathiri wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH), ambao awali walinunua baadhi ya dawa katika vituo vingine. Mkurugenzi wa muungano wa mashirika ya kansa Kenya Network for Cancer Organisations, Phoebe Ongadi, alitaka SHA kueleza sababu za mabadiliko hayo na jinsi wagonjwa watakavyolindwa. "Kwa nini mfumo unabadilishwa na kuathiri matibabu? Saratani haisubiri. Hatupaswi kuchezea matibabu ya wagonjwa," alisema Ongadi. Hata hivyo, SHA ilisema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha huduma kwa kuoanisha matibabu na mwongozo wa kitaifa wa saratani pamoja na kuweka viwango sawa vya bei za dawa na huduma.Iliongeza kuwa kiwango cha fedha kinategemea mwongozo wa matibabu, bei zilizoidhinishwa na masharti ya ufadhili. Vile vile, ilisisitiza kuwa wagonjwa hawapaswi kutozwa tena kwa huduma ambazo tayari zimelipiwa na mamlaka hiyo, na gharama zozote za ziada zinapaswa kuelezwa wazi na kuthibitishwa. Mamlaka hiyo ilisema kila mgonjwa anastahili kupata kifurushi cha Sh800,000 cha matibabu ya saratani, kinachojumuisha Sh400,000 kupitia SHIF (Bima ya Afya ya Jamii) na Sh400,000 kutoka kwa hazina ya magonjwa ya dharura, sugu na hatari.
read moreRight Column Content