T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 16 Jul 2026 04:54:53

Mzozo: Iran sasa yalenga kufunga Bahari ya Shamu

TEHRAN, Iran: BAADA ya kuzima shughuli katika Mkondo wa Hormuz, Iran sasa inaashiria kuwa inaweza kutumia washirika wake, Wahouthi nchini Yemen kufunga Mkondo wa Bab el-Mandeb ambayo ni ya kuingia Bahari ya Shamu. Ikifaulu, Iran itatatiza biashara ya kimataifa na kusababisha bei ya mafuta kupanda hata zaidi. Wachanganuzi wanasema Iran inalenga kuongeza shinikizo kwa Amerika kwa kudhibiti Mashariki ya Kati na Bahari ya Shamu. Mkondo wa Bab el-Mandeb unaunganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, na ni njia muhimu inayotumiwa na meli nyingi za biashara pamoja na usafirishaji wa mafuta kutoka Saudi Arabia kuenda masoko ya dunia. Jumatatu, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Yemen alionya kuwa majeshi ya nchi hiyo yako tayari kufunga mkondo huo ikiwa Saudi Arabia itaendelea kushambulia Yemen. Alisema hatua hiyo inaweza kusababisha bei ya mafuta duniani kupanda hadi Sh25, 870 kwa pipa. Mohammed al-Farah, mwanachama wa afisi ya kisiasa ya kundi la Ansarullah, maarufu kama Wahouthi, alidai kuwa Amerika inaichochea Saudi Arabia kuendelea na mashambulizi dhidi ya Yemen. Alionya kuwa iwapo hali itaendelea kuwa mbaya, Mkondo wa Hormuz na Bab el-Mandeb zote zitafungwa. Wataalamu wa masuala ya uchumi Mashariki ya Kati wanasema hatua hiyo itaathiri vibaya usafirishaji wa mafuta na bidhaa duniani. Profesa Fawaz Gerges alisema Iran imeonyesha kuwa inaweza kutishia njia zote mbili muhimu za usafirishaji wa mafuta, jambo ambalo litazidisha mzozo wa sasa na kutishia ulimwengu mzima. Wahouthi hapo awali walionyesha uwezo wao wa kuvuruga biashara ya kimataifa. Baada ya vita vya Gaza kuanza mnamo 2023, walishambulia meli katika Bahari ya Shamuwakidai walikuwa wakilenga meli zinazohusishwa na Israel. Mashambulizi hayo yalilazimisha kampuni nyingi za usafirishaji kubadilisha njia na kuzunguka Kusini mwa Afrika, jambo lililoongeza gharama za usafiri. Mtaalamu wa usalama, Andreas Krieg, alisema Iran inaweza kutumia Wahouthi kulemea Amerika iwapo itaendelea kushambuliwa. Naye Abdulaziz Sager wa Kituo cha Utafiti cha Ghuba alisema Wahouthi wana uwezo wa kuvuruga usafiri katika Bab el-Mandeb, lakini huenda wasichukue hatua hiyo bila amri ya Iran. Ingawa hivyo, alionya kuwa jaribio lolote la kufunga njia hiyo linaweza kusababisha Amerika na washirika wake kuanzisha operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya Wahouthi. Vita vinavyoendelea kati ya Amerika-Israel na Iran tayari vimeenea katika sehemu mbalimbali za Mashariki ya Kati, huku maelfu ya watu wakipoteza maisha, wengi wao raia wa Iran na Lebanon.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 16 Jul 2026 02:29:39

TAHARIRI: Amani na uwazi ni muhimu katika kura ya Ol Kalou

UCHAGUZI mdogo wa ubunge wa Ol Kalou leo ni zaidi ya mashindano ya kisiasa kati ya vyama na wagombea wa vyama vikuu nchini. Ni fursa ya kuonyesha kwamba, Kenya imejifunza kutokana na makosa ya chaguzi zilizopita na kwamba, taasisi zake zina uwezo wa kusimamia uchaguzi ulio huru, wa haki na wa kuaminika. Hii ndiyo maana Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) ina wajibu leo wa kuhakikisha kuwa kuna viwango vya juu vya uwazi. Mshindi wa uchaguzi wa leo anastahili kuamuliwa kwa haki wala kusiwe na visa ambavyo vitasababisha kura yenyewe kuzua ghasia au kutiliwa shaka. Maafisa wa IEBC wanapaswa kusimamia zoezi hilo kwa uwazi, uadilifu na kutii sheria. Kila kura itakayoopigwa lazima ihesabiwe kwa uwazi, matokeo ya kila kituo yatangazwe wazi na fomu zote za matokeo zitolewe kwa maajenti na kuwekwa hadharani ili kuondoa mashaka. Wapigakura nao wana jukumu la kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani. Hawapaswi kuruhusu kushawishiwa kwa pesa, vitisho, propaganda au misimamo ya kisiasa inayochochea chuki. Baada ya kupiga kura hakuna haja ya kumiminika vituoni, bali kila mtu aende nyumbani na kuachia IEBC jukumu la kuhesabu kura. Kukusanyika vituoni na kituo cha kujumuisha kura kutazua tu ghasia na makabiliano kati ya wanasiasa pinzani. Aidha, polisi wana wajibu wa kuhakikisha usalama wa kila mtu bila upendeleo. Maafisa wa usalama wanapaswa kuwalinda wapigakura, maajenti wa vyama, maafisa wa uchaguzi na waangalizi wa uchaguzi. Polisi hawapaswi kuegemea upande wowote wala kutumiwa kuvuruga matokeo ya uchaguzi wenyewe. Hatua yoyote ya kukabiliana na ukiukaji wa sheria inapaswa kufanywa kwa kuzingatia sheria. Ni muhimu pia vyama vya kisiasa na wagombea wakubali kuwa ushindi na kushindwa ni sehemu ya demokrasia. Badala ya kutoa matamshi ya uchochezi au kuhamasisha wafuasi wao kufanya vurugu, wanapaswa kutumia njia za kisheria iwapo watakuwa na malalamishi kuhusu matokeo. Ol Kalou imevutia macho ya taifa kwa sababu uchaguzi huu unatazamwa kama kipimo cha nguvu za kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Hata hivyo, umuhimu wake haupaswi kuwa sababu ya kuvuruga amani au kukiuka sheria. Wakenya wanatarajia kuona uchaguzi unaoendeshwa kwa uwazi, usawa na uaminifu.

read more