T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 05 Jul 2026 22:55:44

Aladwa awarai wanachama wa ODM wasusie maandamano Saba Saba

BAADHI ya viongozi wa ODM katika Kaunti ya Nairobi wamewataka wafuasi wao wasishiriki maandamano ya Saba Saba ambayo yanapangwa kufanyika hapo kesho. Wakiongea Nairobi Jumapili, viongozi hao walisema wao ni sehemu ya Serikali Jumuishi na njia ya kusaka suluhu kwa changamoto za nchi ni kupitia mazungumzo badala ya maandamano. Mbunge wa Makadara, George Aladwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi alitoa wito wa umoja kati ya viongozi na akawataka polisi wahakikishe kuwa waandamanaji hawaharibu mali. "Tunasema hakuna mwanachama wetu ambaye atatumika kuzua ghasia jijini na taifa lote. Sote tuko katika Serikali Jumuishi na tunasema kuwa hatutaingia barabarani kwa ajili ya maandamano ya Saba Saba," akasema Bw Aladwa. Kauli yake ilijiri wakati ambapo wanaharakati wa kibinadamu wametoa wito wa kuandaliwa kwa maandamano kupinga kutoweka kwa watu kwa njia tatanishi na pia mauaji ya kiholela mikononi mwa polisi. Mbunge huyo aliwataka Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen na Katibu wa wizara hiyo, Dkt Raymond Omollo kuwalinda Wakenya dhidi ya maandamano yoyote ambayo yanatishia amani ya nchi. Aidha waliwaonya wale ambao wamekuwa wakimshutumu Dkt Omollo kutokana na utendakazi wake, akisema katibu huyo ataendelea kuhudumu serikalini hadi 2027. "Katibu Omollo anafaa aruhusiwe kuendelea na kazi yake bila kuingiliwa. Wale ambao wana malalamishi dhidi yake wayafikishe katika afisi yake jumba la Harambee," akasema. Vilevile Bw Aladwa na viongozi alioandamana nao walisema Kenya ni nchi ambako uhuru wa vyombo vya habari unaheshimiwa katika kutia mizani utendakazi wa upinzani na serikalini. "Ni vyema iwapo vyombo vya habari vitamakinikia amani hata vikishutumu viongozi wa kisiasa. Kama utendakazi wangu ni duni, chombo cha habari kina uhuru wa kunimulika. Tunahitaji amani kuelekea uchaguzi wa 2027," akasema. Kuhusu uongozi wa ODM alipuuza mrengo wa Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna akisema wanaunga mkono ule wa Dkt Oburu Oginga.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Kalonzo: Niko tayari kuwa mgombea mwenza wa Sifuna akiteuliwa

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amesema yuko tayari kuwa mgombea mwenza wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna katika uchaguzi mkuu wa 2027. Hii itafanyika tu iwapo upinzani utamteua Bw Sifuna kuwa mgombea wake wa urais. Akizungumza katika mahojiano na NTV Jumatatu, Bw Musyoka alisema hana tatizo kumuunga mkono Bw Sifuna, mradi tu tiketi hiyo iwe na uwezo wa kumshinda Rais William Ruto katika uchaguzi huo. Makamu huyo wa rais wa zamani alisema pia anaamini Bw Sifuna atarudisha mkono iwapo ndiye atachaguliwa kuwa mgombea wa urais wa upinzani. "Wakati huu hatuachi chochote kwa bahati. Tumekubaliana kwamba tutafanya lolote litakalohitajika. Bila shaka, sina tatizo lolote kumuunga mkono Sifuna," akasema Bw Musyoka. Alisisitiza kuwa yuko tayari kuunga mkono tikiti yoyote ambayo upinzani utaafikiana kwa kauli moja, akitaja pia aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa na Martha Karua kama viongozi anaoweza kuwaunga mkono. "Kwa hivyo, nitaunga mkono hii na nyingine. Nina uhakika Sifuna pia hana tatizo kunisaidia. Sina tatizo kumuunga mkono yeye, Gachagua au mtu mwengine ambaye upinzani utakubaliana naye," akasema. Kauli ya Bw Musyoka inajiri siku chache baada ya kura za maoni kumweka Bw Sifuna mbele ya baadhi ya viongozi wa upinzani wanaotajwa kuwa wapinzani wakuu wa Ruto. Utafiti wa TIFA uliotolewa Julai 24 ulionyesha kuwa asilimia 44 ya wafuasi wa ODM wangemchagua Bw Sifuna kuwa mgombea wa urais wa chama hicho iwapo uchaguzi ungefanyika wakati huo. Rais Ruto alipata asilimia 20, Fred Matiang'i asilimia tisa, Kalonzo asilimia nne na Babu Owino asilimia mbili. Bw Sifuna, ambaye amekuwa akifanya mikutano mbalimbali ya kisiasa kutafuta uungwaji mkono, amesema yuko tayari kumuunga mkono mgombea mmoja wa upinzani ili kumng'oa Rais Ruto mnamo 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Helikopta iliyobeba Wanga, Wandayi yatua ghafla kuepuka ajali

HELIKOPTA iliyokuwa imembeba Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor ililazimika kutua kwa dharura katika Kaunti ya Kericho Jumapili kutokana na hali mbaya ya hewa. Viongozi hao walikuwa wakisafiri kutoka Homa Bay kuelekea Naivasha walipokumbana na mvua na upepo mkali, hali iliyomlazimu rubani kutua kama njia ya kuchukua tahadhari. Helikopta hiyo ilitua katika uwanja wa wazi eneo la Chepngetuny, karibu na Chuo cha Kifundi na Mafunzo cha Belgut ambako ilikaa kwa muda hadi hali ya hewa ilipotulia. Afisi ya Gavana Wanga ilisema watu wote waliokuwa ndani ya helikopta hiyo walikuwa salama na safari iliendelea baada ya hali kuwa nzuri. Afisa mmoja kutoka afisi hiyo alisema helikopta hiyo baadaye ilifika Naivasha salama ambako Gavana Wanga alijiunga na viongozi wengine katika mkutano wa kundi la wabunge la Serikali Jumuishi. Tukio hilo linajiri baada ya ajali ya helikopta katika kijiji cha Chepkiep, Mosop, Kaunti ya Nandi mnamo Februari. Ajali hiyo ilisababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng'eno na watu wengine watano. Kabla ya tukio hilo, Gavana Wanga alikuwa ameandamana na Bw Wandayi na Bi Oduor hadi Kojwach, eneobunge la Kabondo Kasipul, kwa hafla ya malipo ya mahari ya Mbunge wa Nyando Jared Okello. Bi Wanga alichapisha picha za hafla hiyo kwenye ukurasa wake wa Facebook, akiwatakia Bw Okello na mkewe Adhiambo maisha marefu ya ndoa yenye furaha. Mapema Jumapili, Gavana Wanga alikuwa amehudhuria ibada katika kanisa la Faith Community Fellowship Sanctuary, Kochia, ambako alishiriki katika harambee ya maendeleo ya kanisa. Baadaye alihudhuria ibada katika Holy Trinity Catholic Cathedral, Homa Bay Town. Kwa upande wake, Bw Wandayi alihudhuria ibada katika Christian Evangelical Fellowship Church, Atemo, Kabondo Kasipul, kabla ya kujiunga na viongozi hao katika hafla ya mahari. Baada ya kufika Naivasha, Gavana Wanga alishiriki katika mkutano wa Serikali Jumuishi pamoja na Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga na viongozi wengine. Bw Wandayi pia alithibitisha kufika kwake Naivasha, akisema mkutano huo utajadili namna ya kuimarisha umoja wa kitaifa, mwelekeo wa taifa na ajenda ya maendeleo kwa manufaa ya Wakenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 6 hours ago

Afisa wa polisi aliyemuandama barabarani na kumpiga risasi Dkt Mutiso afikishwa kortini

AFISA wa polisi anayetuhumiwa alimpiga risasi Dkt Victoria Mutiso siku 13 zilizopita alifikishwa kortini Jumatatu (Agosti 10, 2026). Konstebo Elijah Kibelion Kimoi kutoka kituo cha Polisi cha Karinde kilichoko eneo la Kikuyu alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Paul Mutai. Konst Kimoi alifikishwa kortini pamoja na Daniel Mwangi Njoroge na Kevin Ngugi Kinuthia. Akiomba washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 30, Koplo Romana Oduor anayechunguza kesi hiyo alisema Njoroge ndiye alikuwa anaendesha gari lililomzuilia Dkt Mutiso kabla ya kutwangwa risasi kichwani na Konst Kimoi. [caption id="attachment_190975" align="alignnone" width="1245"] Washukiwa wa mauaji ya Dkt Victoria Mutiso, Elijah Kimoi (kulia), Daniel Mwangi Njoroge na Kevin Ngugi Kinuthia walipofikishwa kortini Agosti 10, 2026. Picha|Richard Munguti[/caption] Mahakama ilielezwa Kinuthia ni mwendesha piki piki iliyompeleka Konst Kimoi kumuua Dkt Mutiso. Baada ya kukamilisha zoezi la kumwangamiza dakitari huyo wa tiba ya ubongo, Kinuthia alimuhepesha Konst Kimoi. Hakimu alielezwa kuwa baada ya mwili wa Dkt Mutiso kufanyiwa upasuaji kulitolewa risasi iliyofanyiwa utafiti na kubainika ilifyatuliwa kutoka kwa Bastola aina ya Mini Jericho iliyokuwa imepewa afisa mkuu wa polisi ambaye ametoroka. Dkt Mutiso aliuawa kinyama mnamo  Julai 29,2026. Mahakama iliombwa iwazuilie washukiwa hao watatu kwa siku 30 kusaidia polisi kukamilisha zoezi la uchunguzi kubaini kilichopelekea daktari huyo kuuawa. Mahakama ilielezwa mbali na watatu hawa kuna washukiwa wengine wanne waliotiwa nguvuni wiki mbili zilizopita kufuatia mauaji hao. Wengine wanaozuliwa ni pamoja Rose Mbithe Mulwa na watoto wake Chris na Angella ambao ni mawakili. Bi Mulwa alikuwa mke wa Prof David Musyimi Ndetei aliyetalikiwa na ambaye alikuwa anamenyana na Dkt Mutiso kuhusu umiliki wa ardhi ya ekari 20 iliyoko Mlolongo Athi River kaunti ya Machakos. Mwingine ni Nelson Masiga. [caption id="attachment_190976" align="alignnone" width="1245"] Washukiwa wa mauaji ya Dkt Victoria Mutiso wakiwa kortini Agosti 10, 2026. Picha|Richard Munguti[/caption] Mahakama ilifahamishwa polisi wanajaribu kung'amua kitendawili iwapo huenda mzozo wa shamba hiyo ya Mlolongo ulichangia kuuawa kwa Dkt Mutiso aliyezikwa kijiji cha Wanzauni, Kaunti ya Makueni Agosti 8,2026. Kesi ya mzozo huo wa shamba inaendelea katika mahakama kuu Machakos. Konst Kimoi na wenzake wawili watarudishwa kortini Septemba 30, 2026 nao Bi Mulwa na watoto wake watafikishwa kortini Agosti 18, 2026 polisi kueleza ikiwa wamekamilisha ushahidi kubaini mchango wao katika mauaji ya mkurugenzi huyo wa kituo cha utafiti cha tiba ya maradhi ya akili. Angella na Masiga waliagizwa na mahakama ya Mavoko wazuiliwe kwa siku 14 wahojiwe ikiwa walighushi hatimiliki ya shamba hilo iliyoko Mlolongo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Raia walilia ugumu wa maisha Nigeria

ABUJA, Nigeria GRACE Adama huvaa hereni zake katika nyumba yake yenye vyumba viwili jijini Abuja kabla ya kuchukua mkoba na kuelekea kazini. Mwanamke huyo anayefanya kazi katika shirika lisilo la kiserikali la afya hupokea mshahara wa Sh12,870 kwa mwezi, karibu mara mbili ya kiwango cha chini cha mshahara Nigeria. Hata hivyo, Adama anasema maisha yanazidi kuwa magumu kwa sababu mshahara wake hauendani na kupanda kwa gharama ya maisha. "Nikilipwa leo, mshahara wangu hudumu wiki moja tu. Gharama ya maisha, nyumba, umeme, kila kitu kimepanda," akasema Adama. Maisha ya mamilioni ya raia wa Nigeria yamezorota katika miaka mitatu iliyopita tangu serikali ya Rais Bola Tinubu kutekeleza mageuzi makali, yakiwemo kuondoa ruzuku ya mafuta, kushusha thamani ya naira na kupunguza ruzuku ya umeme. Serikali na wawekezaji wanasema hatua hizo zilikuwa muhimu kuiepusha Nigeria na mgogoro mkubwa wa kifedha na hatimaye zingeleta manufaa. Lakini kwa wananchi, gharama zimepanda. Utafiti wa Shirika la SBM Intelligence unaonyesha gharama ya kupika mlo wa wali maarufu jollof rice imeongezeka zaidi ya mara mbili tangu Tinubu aingie madarakani. Bei ya petroli nayo imeongezeka mara sita baada ya ruzuku kuondolewa. Benki ya Dunia inakadiria kuwa zaidi ya nusu ya wananchi wa Nigeria waliishi katika umaskini mwaka jana, ikilinganishwa na karibu asilimia 42 mnamo 2022. Hali hiyo inatofautiana na matumaini ya wawekezaji. Thys Louw, meneja wa uwekezaji katika kampuni ya Ninety One, alisema wawekezaji hawajawahi kuwa na mtazamo mzuri kuhusu Nigeria kwa karibu miongo miwili. Soko la hisa la Nigeria limepanda karibu asilimia 60 mwaka huu, huku uwekezaji wa kigeni ukifikia kiwango cha juu cha miaka sita kwa kiasi cha Sh3 trilioni mwaka jana. Biashara na wananchi pia wanakabiliwa na mikopo ghali, huku kiwango kikuu cha riba kikiwa asilimia 26.5. Bei ya petroli Nigeria sasa ni karibu Sh153 kwa lita, kiwango kinachowalemea wananchi waliokuwa wamezoea mafuta ya bei nafuu. "Suluhisho kwangu ni serikali kupunguza bei ya mafuta," alisema Eji Uchenna, muuzaji wa chakula Lagos. Mnamo Juni, wafanyakazi wa serikali walikataa pendekezo la mshahara wa chini wa Sh9,500, wakitishia kugoma kote nchini. Adama amesema amepunguza matumizi, kuacha nyama na kuhamia nyumba ndogo, lakini bado hulazimika kukopa ili kulipa bili. Wakati huo huo, asilimia 80 ya raia wa Nigeria waliohojiwa na SBM Intelligence walisema nchi inaelekea upande usiofaa. Hata hivyo, upinzani uliogawanyika unaweza kumpa Tinubu nafasi ya kushinda uchaguzi ujao. "Serikali lazima ihakikishe ustawi unawafikia raia wote. Ukosefu wa usawa ukiendelea, hali hiyo huwa hatari," akasema Waziri wa Fedha Taiwo Oyedele.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Makosa katika ukanushaji wa sentensi zenye vitenzi '-ja', '-la', '-fa' na '-nywa'

KUKANUSHA ni kukataa, kukana, kutokubali au kupinga jambo fulani. Ili mwanafunzi akanushe sentensi kwa usahihi anafaa kuelewa hali na nyakati mbalimbali. Iwapo kukanusha viambishi vya nyakati na hali katika sentensi ni rahisi, baadhi ya wanafunzi huwa na changamoto wanapokanusha vitenzi vya silabi moja - kuja, kula, kufa na kunywa katika wakati uliopita. Aghalabu utapata sentensi kama vile: Watoto wale walikuja kwetu jana, ikiwa imekanushwa hivi: *Watoto wale hawakukuja kwetu jana. Ukanusho wa sentensi hii si sahihi. Silabi ku- imeongezwa katika kukanusha kitenzi walikuja. Ili kuisahihisha sentensi hiyo ifaavyo tunafaa kusema: Watoto wale hawakuja kwetu jana. Kosa hilo pia huwa la kawaida katika kukanusha kitenzi kula. Utapata sentensi: Wageni hao walikula matunda yote imekanushwa hivi: *Wageni hao hawakukula matunda yote. Ukanusho sahihi ni: Wageni hao hawakula matunda yote. Baadhi ya wanafunzi pia hupata changamoto wanapokanusha sentensi zenye vitenzi kufa na kunywa wakati uliopita. Mara kwa mara utapata sentensi kama vile: Wanyama wao walikufa wakati wa kiangazi. Mtoto wangu alikunywa chai, imekanushwa kwa kusema: *Wanyama wao hawakukufa wakati wa kiangazi. *Mtoto wangu hakukunywa chai. Ukanusho sahihi wa sentensi hizo ni: Wanyama wao hawakufa wakati wa kiangazi. Mtoto wangu hakunywa chai. Mwanafunzi mwenye changamoto katika kukanusha sentensi zenye vitenzi kula, kuja, kufa na kunywa katika wakati uliopita, anafaa kufanya mazoezi ya kuvitumia vitenzi hivyo kutunga sentensi katika wakati uliopita na kuzikanusha.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 10 hours ago

IEBC sasa yatoa ratiba ya matukio muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imeweka wazi ratiba muhimu itakayoongoza maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027, huku wanasiasa wakianza mapema kampeni za kutafuta uungwaji mkono. Kwa mujibu wa mpango wa IEBC wa kuendesha uchaguzi wa 2025-2027 mambo kadhaa yamepangwa kabla na baada ya siku ya kupiga kura. Miongoni mwa hatua muhimu ni usajili wa wapigakura ambao IEBC itafanya kwa siku 30 kuanzia Januari 11 hadi Februari 9, 2027. Zoezi hilo linalenga kuwapa vijana na Wakenya wengine ambao hawajasajiliwa nafasi ya kujiandikisha. Baada ya hapo, IEBC itafanya ukaguzi wa sajili ya wapigakura kuanzia Februari 15 hadi Machi 16, 2027 ili kubaini na kuondoa majina yanayojirudia au kasoro nyingine. Maafisa wa serikali wanaotaka kuwania nafasi za kisiasa watatakiwa kujiuzulu ifikapo Februari 9, 2027, miezi sita kabla ya uchaguzi. Vyama vya kisiasa vitatakiwa kuwasilisha orodha za wanachama wao kwa IEBC ifikapo Machi 16, 2027. Kufikia tarehe hiyo, vyama pia vinapaswa kuwa vimewasilisha majina ya watakaoshiriki katika mchujo, pamoja na tarehe na maeneo ya kufanyia kura hizo za mchujo. Vyama vinapaswa kukamilisha chaguzi zao za mchujo na kutatua malalamishi yanayotokana nazo ifikapo Mei 9, 2027. Wagombea huru pia watakuwa na hadi Mei 9 kuwasilisha majina na alama watakazotumia katika uchaguzi. Kufikia wakati huo, hawapaswi kuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa. Kampeni rasmi zitaanza Mei 2027 na kumalizika Agosti 7, siku mbili kabla ya uchaguzi. Hata hivyo, wanasiasa tayari wameanza kampeni licha ya muda rasmi kutokuwa umefika. IEBC pia imepanga wagombea na vyama kuwasilisha majina ya maajenti wa kitaifa, kaunti, maeneobunge na vituo vya kupigia kura ifikapo Julai 27, 2027. Wakenya wataelekea kupiga kura Agosti 10, 2027. Baada ya uchaguzi, IEBC ina siku saba kutangaza matokeo ya urais. Ikiwa hakutakuwa na kesi, rais mteule ataapishwa Jumanne ya kwanza baada ya siku 14 tangu kutangazwa kwa matokeo. Mtu asiyekubali matokeo ya urais atakuwa na hadi Agosti 17 kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Juu. Mahakama hiyo ina siku 14 kuamua kesi hiyo, kumaanisha uamuzi unapaswa kuwa umetolewa kufikia Septemba 7, 2027. Iwapo Mahakama ya Juu itabatilisha uchaguzi wa urais, uchaguzi mpya utafanyika ndani ya siku 60. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon ametoa wito kwa Bunge, Wizara ya Fedha, vyombo vya usalama na wadau wengine kushirikiana na tume kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa amani na wa kuaminika. Kwa IEBC, safari ya kuelekea Agosti 10, 2027 imeanza rasmi na kila hatua itakuwa muhimu katika kuamua ikiwa Kenya itakuwa tayari kwa uchaguzi huru na wa kuaminika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 12 hours ago

Mahakama yapiga breki ujenzi wa msikiti Treasury Square

MAHAKAMA ya Mazingira na Ardhi mjini Mombasa imesimamisha ujenzi wa msikiti katika Bustani ya Treasury Square eneo la kihistoria na la burudani ya umma, hadi kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria wa Mombasa itakaposikilizwa na kuamuliwa. Chama hicho kinasema Bustani hiyo ni ardhi ya umma inayoshikiliwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Kwa mujibu wa chama hicho, mamlaka haziwezi kubadilisha matumizi ya eneo hilo bila kufuata Katiba pamoja na sheria za mipango miji na mazingira. Mahakama imetoa amri ya muda ya kusimamisha ujenzi katika eneo hilo. "Ombi la mlalamishi limekubaliwa. Ujenzi katika eneo hilo usitishwe hadi kesi hii itakaposikilizwa na kuamuliwa," Mahakama iliamuru. Mahakama pia imewaagiza washtakiwa kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 10 baada ya kupokea hati za kesi. Chama cha Wanasheria wa Mombasa kitapewa siku saba baada ya kupokea majibu hayo kuwasilisha kiapo cha nyongeza pamoja na hoja zake za kisheria. Washtakiwa watakuwa na siku saba zaidi kuwasilisha hoja zao. Washtakiwa ni pamoja na Spika wa Bunge la Kaunti ya Mombasa, Aharub Khatri, Serikali ya Kaunti ya Mombasa, Tume ya Kitaifa ya Ardhi, Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi na taasisi nyingine. Katibu Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Mombasa, Natasha Ali Errey, anasema uchunguzi wa chama hicho umeonyesha kuwa ujenzi ulianza kwenye ardhi ya umma bila idhini muhimu ya kimazingira. "NEMA ilithibitisha kuwa haikuuidhinisha ujenzi huo," Bi Errey anasema katika hati ya kiapo ya kuunga mkono kesi hiyo. Chama hicho kinasema ujenzi wa jengo la kudumu ulianza katika Bustani hiyo Julai 2026. Kwa mujibu wa chama hicho, jengo hilo linajengwa kwa ajili ya msikiti. Chama hicho kinadai kuwa mradi ulianza bila wananchi kushirikishwa kikamilifu. Pia kinasema hakukuwa na mabadiliko rasmi ya matumizi ya ardhi wala vibali vyote vinavyohitajika vya mipango miji na mazingirA. Kwa mujibu wa chama hicho, ujenzi huo umebadilisha kwa kiasi kikubwa matumizi na sura ya eneo hilo la burudani. Pia kinadai kuwa mradi ulianza bila leseni ya tathmini ya athari kwa mazingira. Hali hiyo, kinasema, imewaweka wakazi, wafanyakazi na wageni katika hatari ya kukumbwa na vumbi, uchafu na kelele. Chama hicho pia kinasema ujenzi huo umezuia wananchi kufikia Bustani hiyo. Bustani hiyo ni eneo la wazi la umma lililokuwepo kwa muda mrefu. Lina ukubwa wa takriban mita 300 kwa 200 na linakabili Bunge la Kaunti ya Mombasa. Serikali ya Kaunti ya Mombasa ndilo linalolisimamia. Bustani hiyo ni sehemu ya mandhari ya kihistoria ya Mombasa. Imezungukwa na majengo ya enzi ya ukoloni, yakiwemo Ofisi ya Kamishna wa Kaunti, Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu ya Mombasa. Pia kuna maeneo mengine ya kihistoria katika mazingira yake. Bustani hiyo ina sanamu ya shaba ya mfanyabiashara na mwanzilishi wa shughuli za elimu Allidina Visram. Kwa vizazi vingi, Bustani hiyo imekuwa eneo la burudani, mapumziko na mikusanyiko ya umma. Miti yake mikubwa ya asili na ile iliyoletwa kutoka maeneo mengine hutoa kivuli dhidi ya joto la Mombasa. Pia huhifadhi ndege na viumbe wengine wa mijini. "Hadi hivi karibuni, eneo hilo limetumiwa na kufurahiwa na wananchi, wakazi na wageni wa Jiji la Mombasa kama eneo la burudani, mapumziko na mikusanyiko ya umma ambako shughuli mbalimbali hufanyika," Bi Errey anasema. Chama hicho kinadai kuwa Bw Khatri aliongoza mradi huo akiwa katika nafasi yake binafsi na pia kama Spika wa Bunge la Kaunti. Kinasema alifanya hivyo kwa ushirikiano au kwa msaada wa walalamikiwa wengine. Madai hayo bado hayajathibitishwa mahakamani. Chama hicho kinataka Mahakama itamke kuwa Bustani ni ardhi ya umma inayoshikiliwa kwa niaba ya wananchi wa Mombasa na Kenya. Pia kinataka Mahakama iamuru kuwa eneo hilo haliwezi kuendelezwa bila kufuata sheria. Aidha, kinataka Mahakama ibatilishe vibali au idhini zozote zilizotolewa kuhusiana na mradi huo na kuzuia kabisa ujenzi zaidi. Iwapo Mahakama itaamua kuwa ujenzi huo ni kinyume cha sheria, chama hicho kinataka majengo yote yabomolewe. Pia kinataka Bustani hiyo irejeshwe katika hali yake ya awali.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Pengo la Sh33.5b tishio kwa uchaguzi 2027

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) inakabiliwa na pengo la Sh33.5 bilioni katika bajeti inayohitajika kuandaa na kuendesha uchaguzi mkuu wa 2027, huku mabadiliko ya kiteknolojia na upanuzi wa miundombinu yakiongeza gharama. Stakabadhi zilizowasilishwa Bungeni na IEBC, inayoongozwa na Erastus Ethekon, zinaonyesha kuwa tume hiyo imeomba jumla ya Sh74.8 bilioni kwa kipindi cha miaka mitatu ya maandalizi ya uchaguzi. Hata hivyo, serikali imetenga Sh41.3 bilioni pekee, na kuacha pengo la Sh33.5 bilioni ambalo IEBC inasema linaweza kuhatarisha maandalizi ya uchaguzi huru na wa kuaminika. Miongoni mwa maeneo yatakayoathirika ni malipo ya maafisa wa uchaguzi, ambayo yanahitaji Sh7.63 bilioni. Tume pia ina madeni ya Sh5.75 bilioni, mengi yakiwa ada za kisheria zilizotokana na chaguzi zilizopita. "Madeni haya yamekuwa yakijilimbikiza kwa muda na yataathiri vibaya shughuli za tume katika kuendesha uchaguzi mkuu wa 2027," ilisema IEBC. Kamati ya Bunge ya Sheria na Masuala ya Kikatiba (JLAC) imeonya Hazina ya Kitaifa kuwa upungufu huo unaweza kulemaza uwezo wa IEBC kutekeleza majukumu yake ya kikatiba. Hata hivyo, wabunge wameikosoa IEBC kwa baadhi ya vipaumbele vya matumizi, wakisema ni vya "ubadhirifu na visivyo na umuhimu". "Kwa nini IEBC inasisitiza kutumia Sh9.2 bilioni kununua vifaa vipya vya KIEMS wakati wabunge hawajapewa matokeo ya ukaguzi kuthibitisha iwapo vifaa vilivyopo vimepitwa na wakati?" akauliza Mbunge wa Rarieda Dkt Otiende Amollo. IEBC inahitaji zaidi ya Sh10.7 bilioni kununua vifaa vipya vya KIEMS na kubadilisha vile vilivyopitwa na wakati. Tume pia inapanga kuongeza vituo vya kupigia kura kutoka 46,229 vilivyotumika katika uchaguzi wa 2022 hadi 55,393, huku idadi ya wapigakura waliosajiliwa ikitarajiwa kufikia milioni 28.5 mnamo 2027. Wabunge pia wameonyesha wasiwasi kuhusu ongezeko la makadirio ya gharama za uchaguzi, ambayo yamebadilika kutoka Sh57 bilioni hadi Sh61 bilioni, Sh63.9 bilioni na hatimaye Sh74.8 bilioni. Kamati ya Bunge ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Katiba imeitaka Hazina kushughulikia pengo hilo na kutoa ratiba ya wazi ya kutolewa kwa fedha ili shughuli za uchaguzi zitekelezwe kwa wakati. IEBC pia imeonya kuwa kutolipwa kwa madeni ya zamani kunaweza kuathiri uendeshaji wake, ikiwemo kesi za mahakamani na kusababisha wanaotoa zabuni kukataa au kujiondoa katika kutoa huduma. Vifaa vya KIEMS vilinunuliwa 2017 na kwa kuwa teknolojia hubadilishwa baada ya miaka 10, IEBC inasema inalazimika kupata vifaa vipya ili kuhakikisha uchaguzi wa 2027 unaaminika. Mtaalamu wa masuala ya uchaguzi Koki Muli, hata hivyo, amependekeza kupunguza vituo vya kupigia kura kwa nusu na kuruhusu hadi wapigakura 2,000 katika kila kituo ili kupunguza gharama. "Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuruhusu angalau wapigakura 2,000 katika kila kituo. Hili halipaswi kutegemea Bunge kama ilivyo sasa. IEBC inaweza kuamua idadi ya wapigakura kwa kila kituo kiutawala," akasema Bi Muli.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Mbunge wa Emurua Dikirr aonya Gachagua asikanyage Bonde la Ufa

ZIARA inayopangwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Bonde la Ufa imezua joto la kisiasa baada ya Mbunge wa Emurua Dikirr David Keter kumwonya asithubutu kufika katika eneo hilo. Bw Keter ambaye alichaguliwa na UDA miezi miwili iliyopita, amesema Bw Gachagua si mgeni anayekaribishwa katika eneobunge hilo. Alirithi kiti hicho baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge Johana Ngeno katika ajali ya helikopta Februari 28, 2026. Onyo hilo limekuja wiki moja baada ya Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot kuongoza wabunge kutoka eneo hilo kusema Bw Gachagua ana uhuru wa kutembelea eneo hilo. Hata hivyo, Bw Cheruiyot alimtaka Bw Gachagua asidhani mikutano yake itabadilika kuwa kura za DCP katika uchaguzi wa 2027. Bw Gachagua ametangaza mara kadhaa kuwa ataanza ziara yake Kusini mwa Bonde la Ufa Bomet, Kericho na Narok kabla ya kuelekea Kaskazini mwa Bonde la Ufa ambako atatembelea Nandi, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Baringo, Trans Nzoia na Pokot Magharibi. Baada ya Bonde la Ufa, kiongozi huyo wa DCP anatarajiwa kuelekea Magharibi kutafuta uungwaji mkono huku akilenga kulemaza umaarufu wa UDA na kampeni za Rais William Ruto. "Nataka kumwonya Bw Gachagua asithubutu kufika Emurua Dikirr kwa sababu hakaribishwi hapa. Afadhali aelekeze nguvu zake kwingine kwani hapa ni ngome ya UDA," akasema Bw Keter. Katika uchaguzi mdogo wa Emurua Dikirr, Bw Keter alipata kura 18,266 na kushinda, huku mgombea wa DCP Vincent Kibet Rotich akimaliza wa pili kwa kura 10,760. Hata hivyo, DCP imepata mafanikio katika Narok, jambo ambalo limeongeza matumaini ya Bw Gachagua kupenya ngome ya UDA. Katika uchaguzi mdogo wa udiwani Narok Mjini mnamo Novemba 2025, mgombea wa DCP Douglas Twala Masikonte alimshinda mwaniaji wa UDA Robert Kanyinke Ole Kudate kwa kura 6,007 dhidi ya 4,479. "Hakuna eneo la Bonde la Ufa linaloweza kugawanywa kisiasa kwa sababu watu wameelimika kuhusu haki zao. Wanaojaribu kuwazuia viongozi wa upinzani kufanya kampeni wakumbuke kuwa hawawezi kuzuia azma ya wananchi kufanya maamuzi yao," akasema Bw Rotich. Bw Keter pia amemshutumu Bw Gachagua kwa kuwatusi Wakalenjin huku akitafuta kura zao. "Haikubaliki kwetu kwamba Bw Gachagua amekuwa akimshambulia Rais William Ruto na watu wa jamii yake ya Kalenjin kila siku, akiwaita majina ya kila aina kila anapopata nafasi," akasema. Lakini Bw Cheruiyot alisema Bonde la Ufa haiwezi kuwafungia milango viongozi wa upinzani kwa kuwa wakazi wake ni wakarimu. Seneta huyo alisema wakazi watampokea Bw Gachagua lakini wasitarajie kura. Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago pia alimkaribisha Bw Gachagua lakini akamtaka asichochee migawanyiko. Bonde la Ufa imewahi kukumbwa na ghasia za kisiasa katika chaguzi za 1992, 1997 na 2007, ambapo mamia ya watu waliuawa, wengine kujeruhiwa na maelfu kulazimika kuyahama makazi yao. Bw Gachagua analenga kuvutia jamii ya Kipsigis, akisema inafanana na jamii za Mlima Kenya kwa kuwa ni waaminifu lakini hawasahau viongozi wanaowasaliti.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

Mbadi: Nitaendelea kuvumisha ODM na Tutam!

WAZIRI wa Fedha, John Mbadi amesema hataacha kushiriki siasa za ODM licha ya shinikizo kuwa maafisa wa serikali wajiepushe na siasa za moja kwa moja kuelekea uchaguzi wa 2027. Bw Mbadi alisema atatumia wikendi zake kuimarisha ODM na kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi katika uchaguzi ujao. "Jumamosi na Jumapili zote ni siku zangu za mapumziko. Nitatumia siku hizo kushiriki siasa, hasa siasa za ODM," akasema Bw Mbadi. Waziri huyo, aliwahi kuwa mwenyekiti wa ODM kwa miaka 10 kabla nafasi hiyo kuchukuliwa na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga. Bw Mbadi alisema ODM inaendelea kuwa na umuhimu katika siasa za Kenya licha ya vyama vingine vilivyoanzishwa baadaye kusambaratika. Akizungumza katika hafla ya mchango eneobunge la Ndhiwa, Bw Mbadi alisema hatakaa kimya na kuacha ODM iporomoke. Alimwahidi Bi Wanga msaada wake kuhakikisha ODM inapata zaidi ya wabunge 100 katika uchaguzi wa 2027. "Nitakuunga mkono (Wanga) kuhakikisha ODM inapata zaidi ya wabunge 100 katika Bunge la Kitaifa. Nitatembea nawe," akasema Bw Mbadi. Waziri huyo alisema atashirikiana na viongozi wengine, akiwemo kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga, kuhakikisha chama kinapata magavana wengi na wajumbe wengi wa mabunge ya kaunti. "Nitawapa msaada unaohitajika pamoja na kiongozi wetu wa chama Dkt Oburu Oginga kuhakikisha ODM inapata magavana wengi na madiwani wengi katika mabunge ya kaunti. Tutafanya chochote kinachohitajika kuunga mkono ODM," akaongeza. Bi Wanga alisema ODM inalenga kushinda zaidi ya viti 127 vya ubunge na imeandaa mikakati ya kushinda maeneo ambayo imeyabaini kuwa na nafasi nzuri. "Sisi kama kikosi cha ODM tuko kazini. Tuko imara tunapoelekea mbele na wakati huu tutapata zaidi ya viti 100 vya ubunge," akasema. Gavana huyo pia alisema ODM haitashirikiana na viongozi wanaohusishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akisema chama kinaweza kujadiliana na UDA pekee. "Ndiyo maana hatuwezi kuwa upande moja Gachagua. Anaeneza siasa za ubaguzi, siasa za makabila makubwa na madogo," akasema. Bw Mbadi pia alimshambulia Bw Gachagua akisema siasa za kikabila haziwezi kuwa msingi wa uongozi wa kitaifa. "Huwezi kuwa kiongozi ambaye anaendelea kusema unataka kuwa rais kwa sababu jamii yako ina kura nyingi. Unataka kuongoza jamii yako au nchi nzima? Huyo si kiongozi ambaye tunaweza kushirikiana naye," akasema. Seneta Moses Kajwang alisema ODM bado ina nguvu nyingi Homa Bay na akawahimiza wakazi kujiandikisha kama wapigakura ili kuimarisha chama. "Tunataka kujenga Kenya mpya ambako kila mtu ana haki ya kupata huduma. Ndiyo maana tulimpiga kura ya kumwondoa Gachagua. Alikuwa akisema baadhi ya mambo yamehifadhiwa kwa watu wachache na hilo si sawa," akasema. Seneta huyo pia aliwataka wakazi wa Nyanza kuendelea kumuunga mkono Rais Ruto, akisema serikali imeanzisha miradi ya maendeleo katika eneo hilo baada ya kifo cha Raila Odinga. "Hatutaweza kamwe kumpa kisogo na hatuna nia ya kumfuata James Orengo au Rigathi Gachagua. Viongozi kutoka eneo hili wamekubali kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maendeleo," alisema. Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma aliwataka wafuasi wa Linda Mwananchi kuepuka lugha ya matusi wanapopanga kuandaa mkutano wikendi ijayo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Wantam!Macho yote kwa Gen Z iwapo watapiga kura 2027

KWA miaka mingi, vijana wamekuwa wakitajwa kuwa kundi kubwa ambalo linaweza kuamua matokeo ya uchaguzi nchini, lakini mara nyingi huwa hawapigi kura. Hali hiyo ilibadilika mnamo 2024 wakati kizazi cha Gen Z kilipoongoza maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha na kubadilisha kabisa ramani ya siasa nchini. Vijana walitumia mitandao ya kijamii kama TikTok, X na Instagram kueleza kwa lugha rahisi vipengele vya Mswada wa Fedha walioamini vingeongeza mzigo wa maisha kwa Wakenya. Kauli mbiu kama #RejectFinanceBill2024 na #OccupyParliament zilisambaa kwa kasi na kugeuza mitandao ya kijamii kuwa kituo kikuu cha kuratibu maandamano yaliyowaleta pamoja vijana kutoka maeneo na makabila mbalimbali. Mnamo Juni 25, 2024, waandamanaji waliingia katika majengo ya Bunge wakati Mswada wa Fedha ulipokuwa ukijadiliwa, katika tukio lililovuta hisia za kimataifa. Kufuatia shinikizo hilo, Rais William Ruto aliuondoa Mswada huo na kukataa kuutia saini kuwa sheria. Tukio hilo liliwapa vijana imani kwamba wanaweza kuathiri maamuzi ya serikali bila kutegemea vyama vya kisiasa au viongozi wa jadi. Sasa, macho yanaelekezwa kwa uchaguzi wa 2027 na iwapo Gen Z itageuza nguvu hiyo ya maandamano kuwa nguvu ya kupiga kura. Charles Mutisya, kijana wa Gen Z kutoka Mombasa, amesema vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuamua viongozi watakaoongoza nchi. Alisema lengo ni kuwaleta pamoja makundi mengine kama waendesha bodaboda na mama mboga ili kuunda nguvu kubwa ya wapigakura. "Tunahitaji kubaki tukiwa na umoja. Tulianzisha vuguvugu la #TukoKadi na ikiwa Gen Z tutasalia kuwa wasiojali, hatutatimiza lengo tuliloweka la kuchagua viongozi wazuri," akasema Bw Mutisya. Aliwataka vijana kupanga upya mikakati yao baada ya kutokea kwa migawanyiko tangu maandamano ya 2024, akisema hali hiyo imewapa wanasiasa nafasi ya kurudisha siasa za kikabila miongoni mwa vijana.  "Tunahitaji kufanya maamuzi huru 2027 kwa sababu sasa unaweza kuona wao (wanasiasa) wanatumia siasa za ukabila kutugawanya. Sitarajii Gen Z wafikiri kama mtu wa kijijini, tunahitaji kutenda tofauti na kupinga aina ya siasa tulizo nazo Kenya," akaongeza. Katika kampeni ya kuongeza usajili wa wapigakura iliyokamilika Aprili 2026, wapigakura wapya 2,612,725 walijiandikisha. Kati yao, 2,345,476 waliandikishwa kupitia mpango maalum wa usajili huku 267, 249 wakijiandikisha kupitia usajili wa kawaida. Ingawa IEBC haikutoa takwimu za wapigakura hao kulingana na umri, tume hiyo ilisema vijana wengi walijitokeza, hasa kutokana na vituo vya usajili vilivyowekwa katika vyuo vya elimu ya juu. Mnamo 2022, vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 34 walikuwa wapigakura 8.8 milioni, sawa na karibu asilimia 40 ya wapigakura waliosajiliwa. Gen Z wenye umri wa miaka 18 hadi 29 wanatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa kufikia 2027, baada ya mamilioni ya waliokuwa chini ya miaka 18, 2022 kufikisha umri wa kupiga kura. Mwanaharakati Walid Sketty wa Mombasa alisema vijana wakijitokeza kwa wingi wanaweza kuwa na kura muhimu ya maamuzi. Kwa sasa, kushiriki kwa Gen Z katika siasa hauishii kupiga kura. Vijana wanatumia video fupi, mijadala ya moja kwa moja na mitandao ya kijamii kuelimisha wenzao, kufichua masuala ya uongozi na kuwawajibisha viongozi. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alitambua nguvu hiyo baada ya zoezi la usajili wa wapigakura. "Nyinyi ndio nguvu iliyowasha injini hii. Kupitia nyimbo zenu, lebo zenu za mitandao, dansi zenu na uhamasishaji wa rika kwa rika, mmeonyesha kuwa si viongozi wa kesho pekee, bali washikadau wakuu wa leo, na kwa kweli, mnaweza kuongoza leo," akasema. Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, swali kuu sasa ni iwapo Gen Z itaweza kudumisha umoja wake na kugeuza ushawishi wake wa mitandao na maandamano kuwa kura.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

Wantam,tutam! Ni mwaka moja tu kujua mbivu na mbichi

MWAKA mmoja kuanzia leo, Wakenya watamiminika vituo vya kupigia kura kufanya uamuzi kuhusu atakayewatawala hadi 2032. Watachagua ama kumkabidhi Rais William Ruto muda mwingine wa miaka mitano au kumpa nafasi kiongozi mpya kuchukua usukani. Katika uchaguzi huo ambao tayari umepachikwa lakabu ya 'Tutam' dhidi ya 'Wantam', wapigakura watawachagua wabunge 290 wa Bunge la Kitaifa, magavana 47 na manaibu wao 47, wabunge wawakililishi wanawake 47, maseneta na madiwani (MCAs) kutoka wadi. Taifa limegawanywa katika wadi 1,450 za uchaguzi. Huu utakuwa uchaguzi mkuu wa nane tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi 1992. Utakuwa vilevile uchaguzi wa kwanza tangu 1997 ambapo jina la Raila Amolo Odinga halitajitokeza, ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kwenye karatasi za kupiga kura. Bw Odinga aliaga dunia Oktoba mwaka jana na aliwania urais 1997, ubunge wa Langáta 2007, urais 2013, 2017 na 2022. Mnamo 2022, kulikuwepo vituo vya kura 46,229. Kwenye kura ya 2027, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inatarajiwa kuongeza vituo zaidi. Sajili ya IEBC ilikuwa na wapigakura wasiopungua 22.1 milioni 2022, na inatazamiwa kuwa idadi isiyopungua 6.3 milioni itaongezwa kwenye sajili mpya 2027. Tume inapanga shughuli ya usajili Januari mwaka ujao itakayoendeshwa kwa siku 30 kuanzia Januari 11 hadi Februari 9, 2027. amani ya kisiasa inatarajiwa kubadilikabadilika kabla ya siku ya uchaguzi, hasa upande wa upinzani. Hata Rais Ruto ambaye tayari yupo kwenye ushirikiano na ODM inayoongozwa na Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga ndani ya Serikali Jumuishi, angali anavutia vyama zaidi, huku baadhi kutoka upinzani wakitarajiwa kujiunga naye, hasa iwapo watafarakana kuhusu atakayepeperusha bendera ya urais.  Ili kupanga kambi yake, Agosti 3, Baraza la muungano wa Azimio linaloongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, lilipitisha mchakato wa mabadiliko na kuwakaribisha wanasiasa wapya. Baraza hilo liliwajumuisha Naibu Kiongozi wa Jubilee Dkt Fred Matiang'i, Kiongozi wa PNU Peter Munya na Seneta wa zamani wa Embu Lenny Kivuti katika kamati kuu ya baraza la Azimio. Lilikaribisha vilevile chama cha Justin Muturi cha Democratic Party, People's Democratic Party na Umoja na Maendeleo Party. Aidha baraza liliafikiana kufanya mageuzi na kumteua mgombea mmoja kumenyana na Rais Ruto. Lilianzisha vilevile mazungumzo na chama cha Rigathi Gachagua cha Democracy for the Citizens Party (DCP) na Linda Mwananchi, vuguvugu linaloendeshwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna. Kabla ya hapo, Bw Kenyatta alimtaja kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, kuwa kiongozi wa chama cha Azimio, nafasi iliyoshikiliwa na Bw Odinga. Ingawa hivyo, mratibu wa haya yote haya ni mtu ambaye hawezi kuwania binafsi. Bw Kenyatta anazuiliwa na kanuni ya hatamu, hashikilii afisi yeyote muhimu katika mpangilio mpya na anafanya kazi pasipo kumulikwa. Kinara wa People's Liberation Party, Martha Karua na wa DAP Eugene Wamalwa ni vinara katika muungano wa upinzani. Huku upinzani ukijadiliana, Rais vilevile anaendelea kusaka uungwaji mkono mashinani kwa kukutana na makundi mbalimbali mashinani. Katika wiki ya kwanza Agosti pekee, Ikulu iliwakaribisha wazee wa kijiji Jumanne, viongozi wa Kiislamu Jumatano na walinzi wa mashirika ya kibinafsi zaidi ya 5,000 Alhamisi.  "Mko tayari?" Rais aliuliza katika kikao kimoja. Anaelewa uzito wa kibarua kinachomkabili. "Mtanisaidia kueneza neno hili kwa watu vijijini?" akasema. Matokeo ya utafiti wa TIFA yaliyofanyika kati ya Juni 13 na 22 miongoni mwa wahojiwa 2,048 katika maeneo tisa na kutolewa Julai 24 unamweka rais katika asilimia 24, ambayo haijabadilika kutoka Mei. Hii ni idadi dhaifu kwa rais anayetawala na itabidi Rais Ruto akaze buti ili awe na uungwaji mkono pia maeneo mengine. Seneta Sifuna ni wa pili kwa asilimia 15 akipanda kutoka 10 mnamo Mei na kutoka sufuri mwishoni mwa 2025. Bw Musyoka naye aliporomoka hadi asilimia 13 kutoka kilele cha asilimia 25 Novemba. Wakishajiishwa na uchaguzi mdogo wa Ol Kalou ambapo mwaniaji wa upinzani alimponda wa chama tawala, UDA, muungano wa upinzani unatumai kurudia ushindi huo katika jukwaa la kitaifa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 09 Aug 2026 02:55:09

BATUK: Wabunge wadai Kenya haijaingia katika makubaliano na Uingereza

Wabunge wamesisitiza kuwa hakuna makubaliano mapya yaliyofikiwa kati ya Kenya na Uingereza kuhusu mkataba wa ushirikiano wa kijeshi na Kenya (BATUK). Kauli hiyo inajiri baada ya Uingereza kusema kuwa kumekuwa na maendeleo makubwa katika kutekeleza baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi. Uingereza ilisema maafisa wake wakuu walikutana na maafisa wa serikali ya Kenya, wabunge na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Masuala ya Kigeni Juni kujadili hatua iliyofikiwa. "Maafisa wakuu wa Uingereza walikutana na maafisa wa Serikali ya Kenya, wabunge na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Masuala ya Kigeni mwezi Juni kujadili maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa," ilisema taarifa hiyo. Uingereza pia ilisema taratibu za pamoja za kushughulikia mabomu na vilipuzi ambavyo havijalipuka zimekamilishwa. Miongoni mwa masuala mengine yaliyoshughulikiwa ni mahitaji ya ulinzi wa mazingira na matumizi ya ardhi, ambayo yamewasilishwa kwa mamlaka husika. Uingereza pia ilisema imeweka hatua mpya za kuzuia unyanyasaji wa kingono. Hata hivyo, Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi iliambia Bunge Jumanne kuwa mkataba huo bado haujaidhinishwa. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Nelson Koech, alisema makubaliano hayo hayawezi kuanza kutumika hadi masharti yaliyowekwa na Kenya yatimizwe. Bunge linataka vifungu vya 6(5) na 23 virekebishwe ili mauaji yawe chini ya mamlaka ya mahakama za Kenya. Wabunge pia wanataka BATUK iwe na mpango wa uwajibikaji kwa jamii unaohusisha maeneo inayofanyia shughuli zake. Bw Koech alisema kamati haitakubali mkataba unaokiuka Katiba au kudhalilisha Wakenya. Alisema kujumuishwa kwa mauaji katika vifungu vinavyopendekezwa kutaimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wahalifu wa makosa hayo makubwa wanawajibishwa nchini. Mbunge wa Laikipia wa Kike Jane Kagiri aliunga mkono msimamo huo, akisema mtu yeyote anayefanya uhalifu nchini Kenya anapaswa kufikishwa mbele ya mahakama za Kenya. Kwa sasa, mkataba huo unaacha makosa kadhaa makubwa chini ya mamlaka ya Kenya, lakini mauaji hayajajumuishwa katika orodha hiyo. Hali hiyo imeibua wasiwasi kwamba Uingereza inaweza kudai mamlaka ya kushughulikia kesi za mauaji yanayohusisha wanajeshi wake. Bw Koech alisema masharti ya kamati bado hayajatimizwa licha ya serikali kutangaza kuanza tena kwa mafunzo ya pamoja ya kijeshi kati ya Kenya na Uingereza katika kituo cha BATUK, Laikipia. Alisema mazungumzo na kubadilishana mawasiliano kumeendelea, lakini Uingereza bado haijatoa ahadi ya kutosha kuhusu madai ya Kenya. BATUK imekuwa ikifanya shughuli nchini Kenya chini ya Mkataba wa Ushirikiano wa Ulinzi kati ya Kenya na Uingereza uliopitishwa mwaka 2016. Mkataba mpya uliwasilishwa Bungeni mwaka 2021 baada ya muda wa mkataba wa awali wa miaka mitano kuisha. Hata hivyo, Bunge la 12 lilimaliza muda wake kabla ya kuidhinisha mkataba huo. Mkataba huo uliwasilishwa tena kwa Bunge la 13 mwezi Novemba 2022. Baada ya kushirikisha wananchi, kamati ilipendekeza uidhinishwe kwa masharti kwamba vifungu vya 6(5) na 23 virekebishwe kabla ya kuanza kutumika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 08 Aug 2026 22:55:39

Linda Mwananchi ilivyopokonywa jina

VUGUVUGU la Linda Mwananchi limetishia kufanya maandamano ya kila siku nje ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) iwapo ombi lake la kusajiliwa kama chama cha kisiasa halitashughulikiwa. Hatua hiyo inazidisha mvutano kati ya vuguvugu hilo na ofisi ya Msajili wakati Linda Mwananchi ikijaribu kujibadilisha kuwa chama rasmi cha kisiasa kabla uchaguzi mkuu wa 2027. Akizungumza wakati wa ziara ya Linda Mwananchi ya kukutana na wananchi katika Kaunti ya Busia siku ya Ijumaa, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alilaumu watu ambao hakuwataja kwa kujaribu kunyakua jina linalohusishwa na vuguvugu hilo. Osotsi alisema kundi hilo litampa Msajili hadi kesho kutatua suala hilo. Alionya kuwa iwapo suala hilo halitatatuliwa basi wafuasi wa Linda Mwananchi wataanza kufanya mikutano ya kila siku nje ya ofisi za ORPP. "Ruto ametuma wakora kule kwa ofisi ya msajili wa vyama eti wanajaribu kunyakua hii jina yetu. Mimi nataka kuambia William Ruto, Ibara ya 38 inaruhusu Mkenya yeyote kuunda chama," alisema Osotsi. Akaongeza: "Tunaambia huyo msajili kama hutapatiana hiyo jina Jumatatu, tutaandaa mikutano ya kila siku kwa hiyo ofisi." Mzozo huo umejikita katika maombi ya kusajili chama na namna Ofisi ya Msajili inashughulikia jina linalopendekezwa na Linda Mwananchi. Mvutano huo ulipata sura mpya baada ya ORPP kuripotiwa kusajili Liberty National Democratic Alliance, kinachojulikana kama LINDA Party. Hatua hiyo imeibua mvutano mpya na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna pamoja na washirika wake katika Linda Mwananchi. Usajili wa chama kinachotumia jina LINDA umeleta changamoto mpya kwa juhudi zao. Kwa mujibu wa ripoti, chama hicho kipya kinahusishwa na kundi tofauti ambalo pia lilikuwa limejitahidi kupata utambulisho wa kisiasa kwa kutumia jina "Linda". Kundi hilo pinzani limepinga madai ya Linda Mwananchi kwamba ndilo lenye haki ya kutumia jina hilo. Madai hayo yameibua swali kuhusu kundi lenye haki ya kutumia jina na nembo zinazohusishwa na "Linda". Mzozo huo pia umewekea Ofisi ya Msajili shinikizo kutoka pande zote. Viongozi wa Linda Mwananchi wamekuwa wakisisitiza kuwa tayari wamejenga utambulisho wa kisiasa kupitia jina hilo, hivyo wanafaa kupewa nafasi ya kukitumia chama hicho. Hatua ya hivi majuzi inafuatia mikutano kati ya viongozi wa Linda Mwananchi na Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou. Ripoti zinasema kuwa Msajili alikubali kupitia upya uamuzi wa awali wa kukataa jina la Linda Mwananchi baada ya mashauriano na wawakilishi wa vuguvugu hilo. Hatua hiyo ilikuwa imeibua matumaini miongoni mwa viongozi na wafuasi wa Linda Mwananchi kwamba mchakato wa usajili ungeendelea. Hata hivyo, usajili ulioripotiwa wa LINDA Party umeleta changamoto mpya na kugubika Linda Mwananchi na mzozo mwingine kuhusu jina inalotaka kutumia. Wadadisi wanasema haki inayotokana na Kifungu 38 cha Katiba - kinachowapa raia haki ya kuunda au kushiriki katika uundaji wa chama cha kisiasa - inaambatana na masharti ya kisheria yanayosimamia usajili wa vyama vya kisiasa nchini. Ofisi ya Msajili ina jukumu la kusajili na kudhibiti vyama pamoja na kusimamia taratibu za kisheria zinazohusu kuanzishwa kwa vyama. Linda Mwananchi sasa inataka ORPP itatue mzozo huo ili iweze kukamilisha miundo yake kabla ya uchaguzi ujao. Usajili wa chama ni hatua muhimu katika kubadilisha vuguvugu hilo kuwa chombo rasmi cha uchaguzi. Kwa sasa, viongozi wake wameweka Jumatatu kuwa siku ya mwisho kwaMsajili wa Vyama kushughulikia suala hilo kabla kuanza kwa mikutano ya kila siku nje ya ofisi hiyo.

read more